Search This Blog

Tuesday, 14 June 2022

ANTI EZEKIEL - 1

 





    IMEANDIKWA NA : GEORGE IRON MOSENYA





    *********************************************************************************



    Simulizi : Anti Ezekiel

    Sehemu Ya Kwanza (1)



    Marashi yaliyopuliziwa na mtu ambaye nilikuwa sijauona uso wake wala kujua yu umbali kiasi gani kutoka katika kiti nilichokuwa nimekaa kwa ajili ya kunyolewa nywele zangu yalinivutia kiuhakika, nikaamua kumshirikisha yule kinyozi aliyekuwa ametingwa katika kuninyoa nywele zangu katika mtindo niliokuwa nimeuchagua.

    “Kausha….” Alinambia na sikuelewa ni kitu gani anamaanisha. Nikahisi hakuwa akizungumza na mimi.

    Marashi yale yakaendelea kutawala na sasa yalisadikika kuwa karibu kabisa na pua zangu. Hapo nikajikuta nanyanyua kichwa changu, kwa lengo la kutazama ufundi ambao kinyozi aliufanya katika kichwa changu.

    Badala ya kutazama kichwa changu nikajikuta natazamana na tabasamu murua la kike. Kichwa chake cha mviringo kilikuwa kimefunikwa na koti lisilokluwa maalumu kwa ajili ya kupambana na baridi bali mojawapo ya kivazi kinachoenda na wakati.

    Nilipoendelea kubung’aa mara yule mmiliki wa sura ile ambaye nilikuwa natazamana naye katika kioo alinikonyeza. Hapo nikakumbwa na aibu na kisha nikajifanya kutazama pembeni.

    “Ana aibu mwenyewe looh!!” ilimtoka sauti fulani yenye mchanganyiko wa besi na nyororo. Nikalazimisha tabasamu lakini sikukitazama kioo.

    Hakujishughulisha na mimki tena badala yake aliendelea kuzungumza na mmiliki wa ile saluni ambaye pia alikuwa kinyozi mkuu na wakati huo alikuwa katika kuzishughulikia nywele zangu. Baada ya hapo akatoweka huku nyuma akiacha harufu kali ya marashi isiyokera pua za mnusaji.

    “Bwege katoka kwa wanaume” yule kinyozi akasema ili nisikie,

    “Nd’o wasichana wa siku hizi hao…” niliunga mkono hoja pasipo kutilia maanani.

    “Wasichana!!! Bora angekuwa msichana basi….yaani mi ananikera sana ujue. Kidume kizima kabisa.” Akatokwa na kauli iliyorindima katika mawimbi ya hasira na kupokelewa na ngoma ya siko langu katika hali ya mshangao na sintofahamu. Nikaamua kuuliza.

    “Mwanaume? Mwanaume kivipi sasa ama umbo lake.” Niliuliza na bado sikutilia maanani mazungumzo yale kama yangeweza kunifikisha popote. Niliamini ni mazungumzo tu ya hapo saluni na yanaishia hapo hapo.

    “Shoga huyu!!! Halafu yupo wazi hata aibu haoni, kuna washkaji wangu washalala naye, mimi siwezi hata kwa bunduki yaani.” Aliongea kwa kunong’ona. Nikamsikia vyema.

    Sasa niliishughulisha akili yangu kuelewa kile alichokuwa ananieleza.

    Kumbe yule dada aliyenikonyeza na kunisia kuwa nimependeza si dada ni mwanaume anayeupenda udada? Niliduwaa hakika. Na hapo nikamuuliza maswali mengi sana yule kinyozi, naye akafurahia kuyajibu.

    Haikuwa mara yangu ya kwanza kusikia kuhusu jina hilo la ‘shoga’ la!! Lakini huyu macho yake ni kama yalitangaza kitu fulani cha ziada, alikuwa kama shoga anayejilazimisha japo yule kinyozi alidai kuwa yeye mwenyewe anajitangaza waziwazi kuwa ni shoga.

    Nilipozidi kuuliza maswali mengi, kinyozi akarusha kijembe.

    “Vipi kaka na wewe unataka kukamatilia?” sikumjibu badala yake tukajikuta tunacheka, na hapo alikuwa anamalizia kunifuta kichwa baada ya kuninyoa.

    “Vipi na ndevu niondoe..” aliniuliza nikakataa. Nikafanya malipo na kisha nikajiondokea huku nikijilazimisha yale mawazo kuhusu yule kijana anayeupenda usichana yanitoke.

    Nilipofika nyumbani sikuwa na mawazo hayo tena na sikutaka hata kumfikiria maana kwa kashfa alizotoa yule kinyozi basi zilitosha kumaanisha kuwa kijana yule alikuwa mdhambi tena asiyestahili hata kupewa salamu.

    Inakuwaje mwanaume anajigeuza kuwa mwanamke??

    Nililala nikiwa na swali hilo kichwani!!!

    Asubuhi hapakuwa na lile swali tena na jibu lake pia halkikufanania kuwepo.

    Siku ikaanza nikiwa nimeyasahau ya jana.

    *****

    SAFARI YA KUKUTANA ANA KWA ANA NA MUHUSIKA.

    UCHAGUZI mdogo wa serikali za mitaa kata ya Makangarawe wilayani Temeke uliambatana na mechi ya kukata na shoka katika mchezo wa soka.

    Timu mbili pinzani zilikuwa zinaumana na mshindi angejiondokea na kitita cha shilingi laki tano.

    Mchezo ule ulivuta mashabiki wengi sana kutokana na upinzani wa wazi wazi baina ya timu hizo. Nikiwa mmoja katika ya wapenzi wa mpira wa miguu niliungana na mashabiki wengine uwanjani.

    Hali ya usalama ilikuwa nzuri kuanzia kipindi cha kwanza hadi ilipokuja kuchafuka kipindi cha pili majira ya saa kumi na mbili ambapo mwamuzi wa mchezo huo alipokataa goli la waziwazi. Walianza wachezaji kumzonga mwamuzi mara mashabiki nao wakaingilia kati, hapo ikazuka vita kubwa ya mashabiki wa kila upande.

    Kikosi cha kutuliza ghasia hakikuwa mbalki, mabomu yalipopigwa ndipo kikazuka kizaazaa cha aina yake, kila mmoja akikimbia kuelekea upande wake. Kipigo kilitolewa haswaa na ungekuwa mwenye mikosi kama ungejikuta katika mikono ile ya maaskari.

    Nilichanja mbuga huku machozi yakinitoka kwa wingi baada ya kuuvuta ule moshi wa bomu. Niliruka matuta hapa na pale.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Kakaaa…” nilisikia sauti ya kike ikiita, sauti iliyotia simanzi, sijui ilikuwaje lakini licha ya hatari ile ya kuishia kulala rumande na kipigo kupokea niligeuka kutazama kulikoni.

    Macho yangu yakakutana na macho yaliyonitia mashaka siku moja nikiwa mahali fulani ambapo sikupakumbuka, nilitaka kuendelea kukimbia lakini nafsi ikasita. Nikiwa bado sijapata maamuzi mara kijana mmoja aliyekuwa katika harakati za kukimbia alipita kwa kasi na kumkanyaga mtu yule, akatokwa na kilio cha maumivu.

    Nikataka kuzuia huruma yangu, lakini nikakumbuka kuwa nimeajiriwa katika kampuni ya kutetea haki za wanadamu na mimi mwenyewe ni mwandishi, mara kwa mara naandika makala zinazosisitiza usawa na pia utu.

    Kwa maana hiyo kama ningekimbia basi ninachokiandika mara kwa mara kisingekuwa na maana. Nisingekuwa na utu.

    Haraka nikakimbia mahali alipokuwa, nikamnyanyua, hakuwa mzito sana nikagundua naweza kumuhimili.

    Nikambeba begani! Nikajikokota hadi aliponielekeza kuwa nyumbani kwake ni jirani tu….nikafuata uelekeo aliokuwa amenielekeza.

    Tukaufikia mlango, nikamshusha. Akajikongoja na kuufungua mlango baada ya kujipekua na kutoka na ufunguo.

    Niliaga na kutaka kuondoka, akanisihi kuwa niingie ndani hadi vurugu zipungue. Naam alikuwa amewaza jambo la maana sana, nikakubaliana naye. Nikaingia ndani.

    Nilipoingia ndani nikakuta picha yake, nikatazamana na ile picha nikakumbuka sasa wapi tulionana.

    Ni huyu kijana tulionana saluni, nikaambiwa kuwa ni shoga!!

    Damu ikachemka nilipofikiria kuwa nipo katika chumba cha shoga.

    Nilifananisha sebule ile na sebule yangu, hakika alikuwa ameniacha kwa kila kitu. Hali hii ya kuniacha kwa kila kitu ikanivuta kuendelea kukaa pale.

    “Unaitwa nani kakangu.” Aliniongelesha kwa sauti ilele ya mchanganyiko.

    “Sam!!” nilimjibu kwa kifupi.

    “Mimi naitwa Ezekiel…asante sana kwa kuniokoa, sijui kama ningelala nyumbani kwangu leo.” Alinijibu huku akiachia tabasamu. Sikusema neno nami nikatabasamu huku nikikwepa kumtazama machoni.

    “Nyumbani kwako pazuri sana!!” nilimsifia.

    “Ah kawaida tu, lakini asante si unajua tena mwanamk…..si unajua tena kujipenda jambo la muhimu.” Akajibu kwa kigugumizi.

    “Unaishi peke yako?” nilimuuliza pasipo na wasiwasi wowote kumtilia.

    “Yah ni nyumbani kwangu naishi peke yangu……khaa! Nimejichubua jamani kucha zangu.” Alijibu kisha akalalamika akizitazama kucha zake zilizopakwa rangi.

    Tofauti na siku niliyomuona pale saluni, siku hii alikuwa amedhoofu sana. Alikuwa amekonda na uso wake ulikuwa umebonyea. Hali hii ilinishangaza, lakini nikalazimika kuuliza baada ya yeye kuanza kukohoa kwa fujo.

    “Unaumwa…”

    “Bora ningekuwa naumwa….mimi naumwa sana.” Alinijibu kwa uchungu. Sasa sauti yake haikuwa mchanganyiko sana, bali ilisikika kama ya kiume waziwazi. Sauti ilikuwa inakoroma.

    “Nini tena maana siku ile tunaonana saluni haukuwa hivi, au kioo kilikuwa kinanidanganya.”

    “Saluni? Saluni gani?” aliniuliza huku akistaajabu. Nikamkumbusha siku ile ambayo ilikuwa miezi miwili iliyopita. Hapo chozi likamtoka sikujua kama ni kwa furaha ama uchungu.

    “Lazima nife lakini basi tu….basi tu nasema. Ipo siku yao na wenyewe” Alilalamika peke yake na sikujua kama alikuwa ananishirikisha ama la.

    “Mbona unasema hivyo bro.” nilihoji. Akanyanyua kichwa akanitazama. Hakusema neno akakohoa tena kikohozi kikavu ambacho kwa kukisikia tu nilitambua kuwa kilikuwa kinamuumiza koo.

    “Wewe ni nani?” aliniuliza…..kabla sijajibu akazungumza tena. “Umesema unaitwa Sam lakini bado sijajua wewe ni nani hadi umeamua kurudi nyuma na kuniokota mimi wakati mama yangu mzazi alishindwa kuniokota.” Alitamka haya huku akiniazia macho.

    Kauli yake ikanitetemesha kidogo, ni kama alikuwa ananikaripia. Sikushtuka sana nikaendelea kumtazama, kwani nilishazoea harakati hizi.

    “Mimi ni Sam, mwanaharakati na pia ni mwajiriwa kwenye kampuni fulani hivi……” nilimjibu.

    “Hivyo tu!” aliuliza na sikujua ana maana gani.

    “Unamaanisha nini.”

    “Ndo hivyo tu kuhusu wewe maana sura yako si ngeni sana kwakweli, licha ya kukuona siku ile saluni bado kuna mahali nadhani tumewahi kuonana ama nimekuona.”

    “Labda gazetini, huwa naandika vihadithi hadithi.” Nilijibu bila kutarajia kuwa anaweza kuwa ananifahamu.

    Akasimama na kujipigia makofi, lakini kikohozi kikaondoka na cheko lake akakaza sura na kuugulia maumivu lakini bado aliweza kuzungumza.

    “Nimesoma hadithi zako kadhaa, wewe si nd’o umeandika ile ya NISAMEHE KABURI…..na nyingine ile ya dada fulani hivi chuoni hana miguu wala mikono na anataka kuwa rubani….yaani napenda hadithi zako hasahasa za kipelelezi, hivi wewe ni mpelelezi eeh….” Alizungumza kwa sauti yake ya kubana pua, bila shaka alikuwa ameizoea. Alionyesha kunifahamu vyema.

    Baada ya koo kukaa sawa aliendelea kuorodhesha makala na hadithi zako ambazo amewahi kuzisoma, na hatimaye tukaagana huku nikiwa sina shauku kubwa sana ya kuendelea kumsikilia Ezekiel, kwani hakuonyesha kama anajitambua vyema. Na mbaya zaidi niliamua kuondoka kwa kuhofia kujitekenezea skendo nikionekana natoka katika nyumba ya yule shoga.

    Mke wangu na wivu wake!! Nilimjua mimi mwenyewe.

    Nikamuaga Ezekiel na kuondoka, huku nikijiapia kuwa hakuna ninalohitaji kujua zaidi kutoka kwa mwanaume qaliyejigeuza mwanamke.

    UTATA MKUU

    Siku iliyofuata nilikuwa na safari ya kuelekea mkoani, hivyo asubuhi na mapema niliwahi kwenda Ubungo. Kiubaridi kilikuwa kinapuliza na nilikuwa nimejiegesha mahali nikipuliza hewani moshi wa sigara kupasha mwili wangu joto.

    Nilijitenga eneo la mbali kabisa na abiria wengine ili nisiweze kuwabughuzi. Mawazo yangu yalikuwa yote juu ya safari yangu kuelekea Singida, niliwaza kuhusu watu wa Singida jinsi walivyo wakarimu na hapo nikajengea picha mara yangu ya mwisho mjini Singida.

    Nikiwa bado pale nilipojiegesha mara nilisikia naguswa begani.

    Nilipogeuka nyuma nilikutana na maajabu.

    Ana kwa ana na yule shoga!!

    Hakuwa anatabasamu ba alionekana kama anayefanya mambo kwa shinikizo. Alinikazia macho kama anayetaka nielewe kitu fulani, nilijitahidi kung’amua jambo nikasafiri na macho yake hadi katika mguu wake, akatabasamu na kisha kutoweka pale katika mguu wake wa kuume akaacha kifurushi kidogo tu cha nguo. Nikataka kumfuata anapoelekea lakini akanionya kwa vitendo. Mwendo wake ulinishangaza sana, alitembea mithili ya ngongoti, alikuwa amenyooka na ni kama hakutaka kupinda, masikioni alikuwa ana vifaa vya kusikilizia, sijui alichokuwa anasikiliza lakini bila shaka walikuwepo watu ambao alikuwa anawasikiliza.

    Ezekiel akatoweka na sikumuona tena.

    Nikarejea hadi pale nilipokuwa nimesimama mwanzo, nikaanza kukitafuta kile kifurushi alichokiacha pale lakini sikukiona, nilihaha sana na kujiuliza nini kimemsibu yule kijana. Na ni kitu gani alikuwa ameniachia katika fundo lile la nguo??

    Lazima kilikuwa kitu cha msingi maana alionyesha kusihi sana.

    Swali gumu jingine likawa, yule bwana amejuaje kama nitakuwa stendi asubuhi ile hadi aniletee ujumbe ule.

    Nikiwa bado katika mtihani mgumu, mara basi nililotakiwa kusafiri nalo likapiga honi kuashiria kuwa dakika yoyote ile linaondoka.

    Ule utata ambao huwa naujenga kwa wahusika katika simulizi sasa ukajijenga katika nafsi yangu na sikujua nautatua vipi?

    Katiba basi tayari begi langu lilikuwa kule, sikukipata kifundo nilichoachiwa na mtu niliyeamini kuwa ni Anti Ezekiel.

    Na ubaya mwingine sikujua hata kitu kilichokuwa kinamsibu Ezekiel.

    Nikayakumbuka maneno yake usiku uliopita “nitakufa …lakini….IPO SIKU YAO NA WENYEWE”

    Hakumalizia, na sikujua alitaka kusema nini.

    Kwanini afe na hao wenyewe ni kina nani??







    Nafsi yangu haikubariki wazo lolote kati ya hayo matatu yaliyokuwa yakinihangaisha kwa wakati ule. Ni kama nilikuwa mbumbumbu wa sekunde kadhaa. Ufahamu ulinirejea baada ya kumuona mtoto mdogo akiwa na mfanowe kile kifundo mikononi mwake akirandaranda maeneo ya pale stendi, nilimwendea mbio mara akageuka na aliponiona akaanza kutimua mbio, sijui ni kipi alikiona kwangu hadi akaanza kutimua mbio kiasi kile, nilitamani sana atambue kuwa sikuwa na ubaya wowote bali nilihitaji kile kifundo, lakini angeanza vipi kunielewa iwapo watoto wadogo wasiokuwa na makazi maalumu maisha yao ni kama kivuli tu hawaishi kukimbia siku zote, na ningejuaje huenda alinifananisha na mgambo wa jiji ambaye husafisha mazingira hadi watoto wasiokuwa na makazi.

    Niliendelea kutimua mbio hadi akafikia lile geti la kutokea nje ambalo magari huytumikia kupita pale, kwa sababu yeye alikuwa mbele alifanikiwa kupenya lakini mimi nikiwa mtu mzima nilizuiliwa, hakuna mtu aliyeruhusiwa kupita pale pasipo na sababu za msingi, nilijitahidi kumweleza yule bwana kuwa nina haja sana na mtoto yule lakini hakuonekana kukaribia kunielewa, akaniomba nimpe tiketi yangu ambayo itaonyesha kuwa nilikuwa ni abiria kweli lakini hata ile tiketi sikuwa nayo kwani niliiacha katika begi langu lililokuwa ndani ya gari. Kitendo cha kurejea ndani ya basi kufuata tiketi kingekuwa cha kizembe tena kisichostahimilika na kile kifundo nisichokijua kingepotea hivihivi mbele ya macho yangu na kila kukicha ningeendelea kuteseka pasi na kujua ni ujumbe gani ulikuwa katika kifundo.

    “Naomba nipite yule mtoto ameniibia!!!!” nilidanganya ili yule jamaa aweze kunielewa lakini aliendelea kuweka ngumu. Hasira zikanipanda na kuamua kufanya maamuzi, nikamsukuma kando kwa nguvu, akajikwaa na kupiga mweleka huko. Hapo sasa nikapenya kwa kasi, nyuma nikasikia filimbi ikipigwa, sikujali nilichohitaji ni kile kifundo, kwani kwa kukipata kile basi ningeweza kuituliza nafsi yangu.

    Niliangaza huku na kule pasi na mafanikio ya kumwona yule mtoto, nilijaribu kuwaulizia watu juu ya mtoto yule lakini hakuna aliyejishughulisha nami, nd’o kwanza kulikuwa kunakucha na kila mtu alikuwa akijipanga kuikabili siku ile.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Sikukata tamaa, niliendelea kuangaza huku na kule, nilijitahidi sana kukumbuka kuwa mtoto yule hakuwa na nywele kichwani na alikuwa na kaptula iliyopasuka pajani, sikuwa nikiijua sura yake.

    Nikajificha mahali na kuendelea kufuatilia nyendop za watu mbalimbali, baada ya dakika zipatazo kumi nikafanikiwa kumuona mtoto yule, mkononi hakuwa na kile kifundo lakini alikuwa ni yeye.

    Nikamnyemelea na kufanikiwa kumkamata, nilimuuliza maswali kadhaa, akakiri kukiokota kifundo kile na alikitupa mahali, niliongozana naye hadi mahali alipodhani amekitupa.

    Tukafanikiwa kukipata, nikampataia pesa ambayo angeweza kunywa chai na kula chakula cha mchana siku hiyo, nikakishindilia mfukoni, na hapo nikachukua pikipiki na hima nikamuamuru dereva alifukuzie gari ambalo lilikuwa na begi langu na tayari lilitoka stendi.

    Wakati tunakubaliana bei na dereva mara niliguswa bega, ni kama alivyonigusa Ezekiel. Nikageuka upesi nikidhani ni Ezekiel tena, lakini sasa sikukutana na sura ya mtu bali ngumi kali katika shavu langu.

    “We mpumbavu umejifanya mjuaji kunikimbia sivyo.” Alikoroma kipande cha mtu ambaye nilimsukuma kule getini ili niweze kukimbilia kile kifundo alichokuwanacho yule mtoto.

    Wakati nataka kujitetea nikamuona yule jamaa akijiandaa kunirushia ngumi nyingine, nikajihami na kuruka kando.

    Mwendesha pikipiki akaona isiwe tabu, akawasha pikipiki yake na kutoweka mbali.

    Akaniachia kizaazaa kinikumbe peke yangu.

    Amakweli mchuma janga hula na wa kwao!!

    Kipande cha mtu kikiwa na hasira, kikanikaba mkono wangu kwa uimara wa hali ya juu. Akaanza kunivuta kuelekea anapotaka yeye. Nikatambua kuwa nikifanya uzembe tu hata lile begi katika gari litapotea, huyu kipande cha mtu lazima angenifikisha katika chombo cha dola na hapo ndipo mlolongo ungeanza, mbaya zaidi hata kitambulisho changu cha kazi sikuwa nacho tena. Vyote vilikuwa katika begi langu.

    Akili yangu ikanituma kufanya tukio la mwisho ambalo litaniweka huru, yule kipande akiwa ameridhika jinsi alivyonikwida nami nilijilainisha na kisha ghafla nikamfyatua mtama, mguu wake wa kushoto ukakutana na ule wa kuume, akaniachia kisha akayumba na kuanguka chini tena.

    Nikatimua na kufanikiwa kuvuka upande wa pili wa barabara, nikakuta pikipiki nyingine, nikakwea na kutoa maelekezo kama yale niliyotoa awali kwa yule aliyenikimbia baada ya kupata msala.

    Tukatoweka!!



    Baada ya dakika thelathini nilikuwa nahema juu juu nikiwa ndani ya basi siti ileile, yaliyotokea yote yalikuwa kama ndoto. Sikuamini kama nimefanikisha mambo yote kwa wakati na sasa nilikuwa katika safari yangu kana kwamba hakuna kilichotokea.

    Bahati nzuri nilikuwa siti ya dirishani hivyo upepo ulipunga vyema na kunirejeshea amani pamoja na usawa katika akili yangu ambayo kidogo ilikuwa imeanza kuvurugika.

    Hapo sasa nilijipekua mahali ambapo nilihifadhi kile kifundo, nilipanga nikifungue mwisho wa safari lakini kihoro kikanisukuma kukifungua kabla hata safari ya kuikaribia Morogoro haijakaribia.

    Nilifungua kwa makini na tahadhari ya hali ya juu huku nikijitahidi nisiiingie katika taharuki kwa kitu ambacho nilikuwa sijakiona bado.

    Kifundo kikawa wazi hatimaye na ndanmi yake kulikuwa na funguo moja ambayo ilikuwa na kutu sana. Haikuonekana kama ilifungua mahali fulani katika siku za karibuni na wala haikuonyesha kama hata siku za usoni itakuwa na manufaa kwa kufungua mahali. Ama la hapo pa kufunguliwa na penyewe pana kutu na pamechakaa kwa kiasi kikubwa.

    Funguo ya nini hii? Nilijiuliza huku nikifadhaika na kujiona kuwa nilihangaika na kukaribia kuiokosa safari yangu kwa sababu ya kitu kisichokuwa na mantiki.

    Nikakifunga kile kifundo na kisha nikakiweka katika mfuko wa suruali yangu!!

    Na hapo nikamkumbuka Ezekiel, hali niliyomshuhudia akiwa nayo maeneo ya Ubungo na hali niliyomshuhudia usiku mmoja kabla baada ya vurugu kumkumba nami nikamwokoa.

    Alikuwa katika muonekano wa tofauti sana hasahasa asubuhi hiyo, alikuwa muoga nma alitembea kikakamavu na ni kama alikuwa akiongozwa na watu!! Kisha akatoweka.

    Akatoweka na asionekane tena!! Ufunguo ule mmoja ni wa nini? Na kwanini alinipa mimi?

    Maswali haya yalinisumbua sana.

    Simu yangu iliita na mlio wake ukayakatisha mawazo yangu yasiyokuwa na dalili ya kufika kikomo.

    Ni namba kutoka ofisini kwetu, nikaipokea na kupewa taarifa kuwa semina iliyotakiwa kufanyika mjini Singida imesogezwa mbele kwa siku mbili kutokana na sababu ambazo nitaelezwa baada ya kufika Singida. Aliyenipigia simu akanieleza kuwa nitapewa posho ya kutosha kuniweka mjini pale hadi siku ya semina.

    Simu hii ikanipa mwongozo mwingine, kama Singida hakuna semina kwa siku hiyo basi ningeweza kurejea jijini Dar na kama kuna lolote kuhusiana na Ezekiel na ule ufunguo basi nitaling’amua.

    Katika maisha yangu hakuna kitu nilikuwa sipendi kama kubaki na majibu nusunusu!!!

    Nilishuka Chalinze na kuchukua usafiri wa kurejea jijini Dar. Bahati nzuri nikapata basi linaloenda Kariakoo moja kwa moja. Nikakwea, na baadaye tulikuwa tunapita Ubungo, nikatabasamu na kukumbuka balaa nililozusha asubuhi ile.



    ****



    Niliujua ukorofi wa mama Eva ambaye ni mke wangu japo si wa ndoa. Hivyo nilimjulisha kuwa narejea jijini Dar baada ya dharula hiyo.

    Nilifika nyumbani na kulitua begi langu kisha nikiwa na ule ufunguo uliochakaa nilienda nyumbani kwa Ezekiel ili kama kuna lolote niweze kutambua na nijue maana ya ufunguo ule uliochakaa tena wenye kutu. Nilishukuru kuwa muda ule nafika nyumbani mama Eva alikuwa ametoka kwenda sokoni maana sikuliona kapu ambalo huwa anabebea mazagazaga mbalimbali.

    Upesi nikatoweka, safari hii sikumpa taarifa kuwa nimefika na kuondoka kwani nilitarajia kurejea upesi.

    Katika safari yangu kwa Ezekiel nilitarajia kukuta lolote lile ambalo lingeweza kunipa mwanga iwapo kuna tukio limemsibu Ezekiel, lakini hapakuwa na lolote la kushangaza kila mmoja alikuwa katika harakati zake.

    Chumba cha Ezekiel kilikuwa kimefungwa, nilijaribu kugonga hodi japo kwa ushahidi tu lakini hapakuwa na majibu.

    Ili kuingia ndani ya nyumba ile nilihitaji kuwa na funguo!!

    Kutaja neno ufunguo nikakumbuka kitu!

    Ni hapo nikaukumbuka ule ufunguo wenye kutu. Nikajipekua na kuibuka na kile kifundo nikakifungua upesi na kuibuka na funguo wenye kutu. Japo sikuwa naamini sana kama yaweza kuwa kweli nililazimika kujiaminisha. Nikatazama kushoto na kulia hakuna hata mtu mmoja aliyejishughulisha na mimi, nikajikoholesha kama yupo ambaye atasema nami bado hakujitokeza mtu yeyote.

    Naam!! Ufunguo ukakifungua kitasa, nikaingia ndani.

    Sasa mbona una kutu huu funguo?? Nilijiuliza huku roho ya kipekuzi ikiniandama, na ni hii roho ilinituma mara kwa mara kufanya upekuzi mara kwa mara. Hata katika ofisi niliyoajiriwa walinitambua kwa tabia hii isiyokera bali kuwashangaza.



    Mara nikakizoea kile chumba, nikaangaza huku na kule sikuona mabadiliko yoyote yale, nikajiuliza kama niliota kuonana na Ezekiel ama tulionana kweli.

    Kama hatukuonana ule funguo ningeutoa wapi? Macho yangu yakavutika na karatasi iliyokuwa mezani, ilikuwa imeandikwa kwa wino mweusi mwandiko wa kuyumbayumba, bila shaka mwandishi aliandika huku akiwa na haraka sana.

    “CHUMBANI USIACHE…PEKUA HATARI OKOA” maandishi yalisomeka vile, mapigo yangu ya moyo yakaenda mbiombio, nikaukumbuka mdomo wa Ezekiel kule Ubungo ulikuwa unachezacheza ukisema maneno haya kwa kurudia na sikuweza kutambua lolote lile.

    Roho ya kidadisi ikazidi kunitawala, nikajiingiza kwa tahadhari kubwa katika chumba cha Ezekiel. Nilipoufikia mlango na wenyewe ulikuwa na tatizo lilelile, haukufunguka hadi ule ufunguo wenye kutu ulipoutekenya!

    “Vitasa vinafanana ama…..” nilijiuliza huku nikiufungua vyema mlango.

    Chumba kilikuwa kikubwa lakini hakikusheheni vitu vingi sana, kabati la nguo na meza ya kujirembea ya wanawake.

    Meza ile ya kisasa ilikuwa na mtoto wa meza, na juu ulikuwa na vipodozi tele, haraka nikauendea mtoto wa meza, nikauvuta na hapo nikakutana na makaratasi mengi yakiwa yameandikwa mambo ambayo sikuyaelewa, nikayatwaa yote na kuyajaza katika mfuko mmoja mweusi, nikapapasa huku na kule sikukutana na kitu kingine ambacho niliona kina maana kwangu.

    Katika hayo makaratasi kuna yaliyokuwa yameandikwa na mengine hayakuandikwa chochote.

    Nikabeba, wakati nataka kutoka nje nikakumbuka karatasi ile ilinisihi kupekua zaidi tena ilisema nisiache.

    Nikaishughulisha akili yangu, nikapekua zaidi na zaidi, mwisho kabisa nikatoa mashuka kitandani.

    Hapa ndipo nilipokutana na jambo la kushangaza na kushtua kuliko yote ambayo hadi kipindi hicho cha utu uzima wangu macho yangu yaliwahi kushuhudia.

    Sura haikuwa ngeni na ilifanana kabisa na ile niliyoonana nayo asubuhi ya siku hiyohiyo maeneo ya Ubungo!!

    Sura ya Ezekiel!!CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Alikuwa ametulia tuli kitandani, bora angekuwa anasema neno lolote ama anatabasamu.

    Haukuhitaji utaalamu wa kidaktari kutambua kuwa mwanadamu yule alikwishapoteza uhai siku nyingi sana, na alikuwa ameanza kuharibika. Ezekiel hakuwa mweupe tena, ngozi yake ilikuwa nyeusi, alikuwa uchi mnyama.

    Kifurushi cha makaratasi kikanitoka mkononi, lakini nilikumbuka kuuzuia mkojo uliotaka kunitoka. Miguu ilikuwa inatetemeka na jasho jembamba lilinitoka.

    Ezekiel aliyenipa funguo, Ezekiel sasa ameozea kitandani!!!

    Tofauti ya masaa matatu tu!!

    Hapana!!

    Nikaanza kurudi kinyumenyume na hapo nikajikwaa kwenye kile kifurushi na nikakumbuka kukiokota, ujasiri ukakaa kando, nikashindwa hata kumfunika Ezekiel pale kitandani.

    Mara mlango wa Ezekiel ukagongwa!!!

    Sikujibu chochote kile!! Mara sauti ya kike ikaita jina lake.

    Hofu ikazidi kutanda, yule ni nani anayemtafuta Ezekiel, na je anamtafuta Ezekiel aliye hai ama huyu anayeozea kitandani!!

    Maswali yakawa lukuki huku nikiwa sina majibu, na sauti kutoka nje ikazidi kuita.









    Upesi nikatoka kule chumbani na kujichanganya sebuleni nikiwa na kifuko changu mkononi nikijiandaa kukabiliana na huyo ambaye alikuwa anabisha hodi.

    Mapigo ya moyo yalikuwa juu sana na sikuweza kujizuia kuitangaza hofu yangu waziwazi.

    Nilipofika sebuleni na Yule mgongaji alikuwa anaingia.

    Haikuwa mara ya kwanza kuonana na yule mwaamke, lakini haikumaanisha kuwa nilikuwa naye karibu sana. Mara kwa mara tulikutana asubuhi katika kituo cha mabasi kila mmoja akienda anapojua mwenyewe.

    “Mambo….mambo kaka” alinisalimia huku akionekana kuusoma uso wangu katika namna ya wasiwasi.

    Labda alidhani najihusisha kimapenzi na yule mwanaume anayesadikika kuwa ni shoga.

    Yule dada lazima alihisia kuwa nina uhusiano na Anti Ezekiel. Nilijilazimisha kutabasamu ili kumwopndoa wasuiwasi na hapo akanishambulia kwa swali moja zito ambalo sikujiandaa kulijibu. Wakati nadhani ataniuliza Ezekiel kama yupo ama la, aliniuliza kama Ezekiel bado amelala.

    Hapo nikajaribu kuzungumza lakini nikashindwa kusema neno lolote. Ina maana Ezekiel alikuwa amelala na kuna baadhi ya watu walikuwa wanafahamu ama. Sasa akama alikuwa amelala na yule aliyenipa funguo kule Ubungo ni nani?

    “Aaah…hayupo Ezekiel hayupo…kwani nani alikwambia alikuwa amelala.” Nilimweleza bila kujipanga. Na hapo nikausoma wasiwasi wake moja kwa moja usoni.

    “Acha utani basi kaka….” Alilaumu huku akionyesha fadhaa waziwazi.

    “Hayupo dadangu…” nilisisitiza.

    Yule dada akaamini kuwa nilijaribu kufanya naye utani wakati hakuwa na utani hata kidogo, na hapo nikatambua kuwa alikuwa na ufahamu mkubwa na uzoefupia katika nyumba ile. Akanipita na kuelekea chumbani kwa Ezekiel huku akiita jina la Ezekiel kwa mikogo.

    Akili ikaniambia kuwa kama ni mtego tayari ulikuwa umefyatuka na ni lazima ningejikuta nimenasika.

    Upesi nikapepea na mfuko wangu mfukoni.

    Nilipotoka nje nikaamua kutimua mbio kabisa, nikiwa na kile kifurushi kuelekea nyumbani, nilijikwaa mara kwa mara lakini sikusimama baada ya dakika tano tayari nilikuwa katika mlango, na nilitanabai kuwa mke wangu naye alikuwa amefika muda si mrefu kutokea sokoni.

    “Na wewe…nini kimekusibu.” Aliniuliza huku akinishangaa, alikuwa ameshika kiuno. Macho yake aliyakazia miguuni mwangu na nilipojitazama nikagundua kuwa sikuwa na viatu mguuni bali nilikuwa nimevaa soksi pekee.

    “Viatu vipo wapi?” alinitupia swali jingine. Bado sikuweza kujibu na niklibaki kubung’aa kama zezeta tu. Mama Eva akanikaribia na kunitikisa na hapo kidogo nikatanmbua kuwa kuna kitu nilitakiwa kufanya, nikaingia ndani huku nikitweta, nikautua ule mfuko kitandani. Mama Eva akanifuata huku akisisitiza kuwa kuna jambo natakiwa kumweleza, sikumjibu kitu chochote kile.

    “Niwekee maji ya kuoga,…ama acha nitaweka mwenyewe maji ya kuoga…hivi yanatoka bombani ama…” nilizungumza bila kituo nikijitahidi kujizuia bila mafanikio.

    “Umekuwaje baba Eva…” alihoji sasa alimaanisha zaidi.

    Sikumjibu na badala yake nikachukua ndoo, nikaenda bombani na kuchota maji, nikamwahidi kuwa nikitoka kuoga nitamsimlia kilichojiri huko nilipotoka, akanikubalia kwa shingo upande.

    Wakati naoga nilizidi kuilazimisha akili yangu ikae sawa. Nilimuwaza yule mwanamke niliyeonana naye wakati natoka katika chumba cha Ezekiel. Swali kubwa lilikuwa ni iwapo yule dada anatambua nyumbani kwangu ni wapi, na swali jingine lilikuwa juu ya maongezi yake. Alidai kuwa Ezekiel alikuwa amelala chumbani wakati mimi nimemuona tena akiwa anaelekea kuoza.

    Haikuwa mara yangu ya kwanza kuona maiti!! Sikuwa na shaka kwa nilichokiona.

    Nilijimwagia maji nisipate walau hisia kama ni ya baridi ama ya moto, manukato yaliyotoka katika ile sabuni hayakuniingia katika hisia hata kidogo. Nilikuwa niponipo tu, nilijua kuwa ninaogopa lakinbi sikujua nafanya nini ili kujitoa katika hali hii.

    Mara katika mawazo yangu ikaniajia sauti ya yule mwanamke, ni kama alikuwa anapiga kelele, anapiga kelele akinitaja, nikajigongagonga kichwa mara sqauti zile zikakatika, lakini tena zikarejea kama mauzauza sasa nilimsikia akiongea na watu, sauti ileile. Baada ya yeye kuzungumza nikasikia sauti ya kiume, baada ya sauti ya kiume nikasikia sauti ya kike. Sauti hii sasa ilikuwa ya mke wangu,mama Eva.

    Bafu letu la nje halikuwa refu sana, nikanyanyua miguu juu nikisimamia kucha ili niweze kuona kama hizo sauti ni kweli ama ni mawazo yangu tu!! Wakati huohuo nikajiapiza kuwa kama nikimaliza kuoga, nitammweleza mke wangu kila kilichotokea naye atanishauri nini cha kufanya, lakini nitaenda na wazo langu kuwa sitakiwi kuwa kimya!! Na kubwa zaiodi sitakiwi kuwa mtaa huo.

    Nilitambua kuwa itakuwa ngumu kwa m,ke wangu kunielewa kutokana na wivu wake, lakini ilikuwa lazima anielewe ili niwe huru na mwenye amani.

    Kichwa kilifanikiwa kutoka nje na hapo nikamuona mke wangu, na wanaume wawili na mwanamke mmoja ambaye sikuhangaika kumtambua kuwa alikuwa ni yule ambaye tulikutana katika nyumba ya Ezekiel na kisha nikatoroka nikimwacha akakabiliane na kimbembe chumbani.

    Kimbembe cha maiti ya Ezekiel.

    Mapigo ya moyo yakaongeza kasi yake na hapo nikasikia joto kwa mbali miguuni. Nilikuwa najikojolea.

    Maaskari!! Niliwaza kitu kile, nikataka kujipa moyo kuwa sasa ningeweza kutoka na kuzungumza nao lakini nilipowatazama kwa makini walikuwa na nywele ndefu.

    Si kwamba hakuna askari mwenye nywele ndefu lakini mmoja alikuwa ni mzungu.

    Wametoka wapi upesi kiasi kile.

    Hatari!! Kengele zikapiga katika kichwa changu.

    Kuendelea kushangaa isingeweza kusaidia, upesi nikakwapua kaptula yangu na kuivaa, nikaachana na taulo, nikapanda juu na kupitia katika dirisha nikaangukia kwa nyuma, sikuishia hapo nikazunguka upesi upande wa pili wa nyumba nikiwa vilevile na bukta yangu, nikawaona wale watui wakiendelea kuhojiana na mke wangu na yule mwaamke akiwahakikishia kitu ambacho sikiweza kukisikia. Mikono ya mama Eva ilielekezea kule bafuni, nikajua anawaambia kuwa nitatoka muda wowote. Nao wakaendelea kusubiria, hadi yule mzungu alipomwambia mwenzake akatazame, yule mtu mweusi akajipapaasa kiunoni na hapo nikaona bastola.

    Wanataka kuniua???

    Kuna nini? Nilijiuliza huku nikitetemeka. Sikuwahi kuingia katika mlolongo mzito kama huu hapo kabla, nilizoea kupambana kwa maneno lakini sasa kuna mtu ananitafuta akiwa na bunduki, nina hatari gani mimi?

    Yule mtu mweusi alirejea akiwa ametaharuki, aliangaza huku na kule kama anayetafuta kitu.

    Mzungu akampokea kwa mfadhaiko, na baada ya chochote walichoweza kuongea nilimwona mzungu akijipekua, akatoka na kitu mfanowe pingu, akamfunga mama Eva na kumuunganisha na yule dada.

    Nilichanganyikiwa, nikataka kujitokeza na kupambana, nafsi ikakubali lakini mwili ukasita, yule mzungu akaingia ndani mwangu na kutoka baada ya muda, hakuwa amebeba chochote. Nikamshuhudia kitoa maneno makali nisiyoweza kuyasikia, kisha wakaongozana wote na kutoka eneo lile. Nikabaki kuwasindikiza kwa macho.

    Punde baada ya wao kutoweka nilitaka kurejea nyumbani lakini nikahisi kuwa patakuwa na mtego wameweka, na kuninasa mimi ingemaanisha kuwa kama ni taarifa kufia hapo basi ni mimi chanzo.

    Nilidumu katika fumbo hilo hadi alipopita Selemani, mtoto mtukutu aliyejulikana mtaa mzima, nilimwita huku nikijifanya kuwa niliamua tu kuwa katika vazi lile la kaptula. Selemani alinishangaa lakini mkubwa mkubwa tu hakuniuliza.

    “Sele, nenda pale ndani kwangu, angaza pale katika kochi kuna mfuko mweusi una makaratasi niletee, nenda sasa hivi.” Nilimsisitiza naye akatoweka huku akiruka huku na kule na kuimba nyimbo za wasanii anaowajua yeye.

    Alipoondoka nilimsindikiza kwa macho hadi alipoingia pale ndani, nil;iangaza kwa makini kama kuna mtu atamvamia lakini hakutokea.

    Hatimaye akatoka na mfuko mkononi, hakika nilikuwa nimecheza pata potea. Maana kama wale watu walihitaji mfuko ule basi ulikuwa umepatikana kirahisi. Mapigo ya moyo yalienda mbio wakati nangojea kukabidhiwa mfuko ule.

    Hakuna lolote lililotokea Selemani akanifikishia mfuko ule wenye makaratasi kama ulivyokuwa. Nikastaajabu kuwa kivipi watu wale hawakuuona mfuko ule pale sebuleni hadi waamue kumchukua mke wangu??

    Ama hawatafuti mfuko?? Nilijiuliza tena.

    Nikamuita Selemani tena, safari hii nikamuagiza suruali yangu na shati.

    “Nikuletee na karatasi lile?”

    “Karatasi gani tena.” nilihoji.

    “Utamfuata mkeo.” Alinambia huku akicheka, yeye alichekeshwa nay ale maandishi lakini mimi yalinistaajabisha.

    “Leta tuone..” nilimwambia naye akatoweka mimi nikabaki na ule mfuko wenye makaratasi ambayo sasa niliamini kuwa hayakuwa na maana tena.

    Safari hii niliamini kuwa hapakuwa na uangalizi wowote wa nyumba yangu, sikuwa katika uoga. Nikamsindikiza kwa macho huku nikiamini atarudi salama.

    Lakini haikuwa hivyo, wakati Selemani anaingia chumbani mwangu, niliwaona anaume wawili. Sio wale wa awali lakini, wakamvamia na kumvuta nje, wakamuuliza kitu nikaona ananyoosha mkono kuelekea upande niliokuwa.

    Na mara wale watu wakaanza kutimua mbio kufuata uelekeo huo huku wakiwasiliana kwa simu zao.

    Swikungoja kuambiwa, nikaanza kutimua mbio na kaptula yangu mfuko mkononi, miiba ilinichoma lakini sikukumbuka kupunguza mwendo. Hali ya hatari ilikuwa nyuma yangu. Nilikaza mwendo zaidi na hatimaye nikaanza kusikia vishindo vikijongea nyuma yangu kwa kasi kubwa!!

    Nimekwisha!!! Nilijisemea!!

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/



    KILICHONISAIDIA ni uenyeji wangu katika mitaa ile, niliongeza kasi na kisha nikapinda mkono wa kushoto ghafla na baada ya hatua mbili nikayumba kulia na hapo nikakutana na kichochoro kingine na kwa mbali ulikuwa ni uwanja wa mpira. Uwanja ambao zilizuka vurugu siku kadhaa nyuma na kunikutanisha na Ezekiel na sasa nipo katika balaa.

    Kulikuwa na wachezaji uwanjani wakiwa katika mazoezi, nikaona hiyo ni nafasi ya kipee ya kupata wasaidizi. Nikaanza kupiga mayowe kwa jitihada zote huku nikipepea mikono juu.

    Kumbuka nilikuwa kifua wazi!! Wanasoka wale wakabaki kunishangaa mimi huku wengine wakisogea nyuma na pembeni kwa tahadhari ya lolote baya ambalo nilikuwa nakabiliwa nalo.

    Walinipokea huku wakisubiri kuona ni kitu gani kinanifanya nirukwe akili vile.

    “Majambaziii majambaziiii…..” nililalamika huku pumzi zikikata na hofu ikitanda zaidi.

    Kusikia neno majambazi, tahadhari kubwa zaidi ikachukuliwa kila mmoja akawa katika mkao wa kujiokoa mwenyewe. Macho yakatazama pande kuu nne za dunia lakini hakuna kilichotokea. Umakini ukaongezeka hadi wa kutazama pande zote kumi na sita, thelathini na mbili na hadi sitini na nne. Hapakuwa na kitu chochote cha hatari kilichojongea pale uwanjani.

    “Huyu chizi huyu labda…” mchezaji mmoja akatoa hoja hiyo. Wenzake wakamkanya na hapo wakamtambulisha kuwa mimi ni mwandishi wa habari katika gazeti fulani. Licha ya yeye kuduwaa, mimi niliduwaa maradufu. Kumbe najulikana sana.

    Yule aliyetoa shutuma za kuwa mimi nina wazimu akagwaya!! Akaungana na wenzake kuendelea kungoja hayo majambazi.

    Bado hayakutokea!!

    Wakaanza kupungua mtu mmoja baada ya mwingine, nikahisi vichwani mwao wamekubaliana na wazo la yule mwenzao kuwa huenda nimepandwa na wazimu.

    Hatimaye nikabaki peke yangu, kifua wazi!! Kifurushiu mkononi. Kila mmoja akaendelea na shughuli zake, hakuna ambaye alikuwa tayari kuniamini. Nikiwa kifua wazi nikalazimika kuendelea kukimbia maana niliamini kuwa wale watu wabaya walikuwa wakinifuatilia.

    Nilitembea kwa tahadhari huku nikiamini kuwa watu kadhaa waliokuwa wananifahamu walikuwa wakinishangaa. Nilipenya nyumba kadhaa hatimaye nikafika nyumbani kwa Enock, rafiki yangu ambaye kabla ya kuhamia kwake ni mimi nilimkaribisha jijini na akaishi nami chumba kimoja kabla sijaamua kuishi na mama Eva.

    Nilimkuta mnkewe yeye alikuwa ametoka kidogo. Mke wake ambaye ni shemeji yangu alishtuka kuniona katika ile hali, nikiwa katika pensi na mkononi kifurushi kikiwa na makaratasi ambayo ni mimi pekee niliamini yalikuwa yana umuhimu.

    Shemeji alinikaribisha ndani huku macho yake yakikwepa mara kwa mara kunitazama.

    “Shem…hebu mwambie Enock akatishe zoezi la kuoga aje kunisikiliza” shemeji akaruka upesi na kuelekea bafuni, hakurejea tena badala yake Enock akiwa amevaa taulo alitokea sebuleni.

    “Kaka nini tena hiki….kimetokea nini…mama Eva ama?? Yaani mmefikia huku.” Alizungumza upesiupesi asinipe nafasi ya kusema lolote, nikaamua kumkatisha, “Noki eeeh!! Hebu nisikilize bwana…..” nilifoka kisha nikamsimulia kwa ufupi kuwa haja yangu ya kwanza ilikuwa nguo. Hilo hapakuwa na utata, miili yetu iliendana hivyo ningeweza kuvaa nguo zake. Akanitimizia hilo mara moja nikavalia palepale sebuleni. Na baada ya pale nikamwomba anipatie kiasi fulani cha pesa, uzuri ulikuwa mwisho wa mwezi na alitambua ni fadhila kiasi gani nimewahi kumtendea. Nikamtajia kiasi akaniahidi kunipa kiasi chote kama nilivyoomba.

    “Mengineyo nitakupigia simu uje mahali tukae tuzungumze, hapa si mahali sahihi hata kidogo. Kuna watu wabaya wasije wakazua lolote la kuzulika.

    Enock hakunielewa kabisa lakini hakuwa na la kufanya, nilikuwa nimefedheheka na akili yangu ilikuwa haijakaa mkao wa kusimulia juu ya Ezekiel kisha mazingaombwe ya kumuona akiwa Ubungo hai na kisha akiwa maiti anayeharibika kitandani baada ya nusu saa, mkasa wa mke wangu kuchukuliwa kisha kuachwa ujumbe, mkasa wa Selemani yule mtoto kukwapuliwa na watu wabaya kisha kuanza kunifukuza mimi. Ningeweza vipi kusimulia tukio lote kwa ufasaha wakati shemeji yangu alikuwa ameniona nikiwa kama tahira tayari aliponikaribisha ndani.

    Hakika sikuweza!!

    “Enock….shemeji yako yupo matatani hadi sasa sijui alipo, tukionana hiyo jioni ama muda wowote ule uje unishauri. Sijui kama yupo mwingine wa kunishauri zaidi yako” nilimnong’oneza Enock kisha nikajivika vyema kofia aliyonipatia, kifurushi changu nikakiweka katika mpangilio mzuri, badala ya ule mfuko mweusi sasa niliyapanga makaratasi yale katika bahasha kubwa ya kaki.

    Dereva wa pikipiki akapigiwa simu, akafika hadi mlangoni. Nikapanda pikipiki na kuagana na Enock mwenye mashaka.

    “Nipeleke Ubungo maji.” Nilimpa maelekezo.

    “Shilingi ngapi?” nilimuhoji.

    “Jamaa amesema atalipia kila kitu cha msingi nikupeleke popote utakapoenda.” Alinijibu. Kisha akavaa ngao ya kichwani na kutokomea.

    Wakati huo ilikuwa tayari saa saba mchana!!!

    Upepo uliovuma wakati pikipiki ikizidi kushika kasi, kidogo ulinipa ahueni ya kufikiri. Nilijiona mtu kati ya watu. Lakini mtu asiyekuwa mkamilifu!!

    Mke wangu alikuwa matatani. Na hawa jamaa hawakusema naenda kumchukua wapi. Baadaye kidogo nikatabasamu baada ya kugundua kuwa kile ninachokiandika kila siku sasa kilikuwa kinanitokea. Maisha ya kwenye simulizi!!

    Tulipofika Ubungo maji nilishuka na kumshukuru yule bwana.

    Baada ya kuondoka nikachukua daladala iliyonipeleka maeneo ya kimara. Nilifanya vile ili kukwepa kupatikana kirahisi iwapo tu mambo yatakuwa makubwa zaidi ya pale.

    Nilichukua chumba maeneo ambayo yalikuwa yamejificha sana. Nikajiandikisha jina la uongo na hatimaye nikawa chumbani huru.

    Nilihisi uchovu lakini sikutaka kulala, nikafungua bahasha yangu. Kitu cha kwanza kukitoa ilikuwa ni picha ndogo ya mtoto wa kiafrika alikuwa anatabasamu. Haikuandikwa chochote kwa mbele lakini nyuma yake iliandikwa ‘MICHIGAN’.

    Jina likanichanganya sana, hii Michigan ya bara la Amerika ama Michigani ni jina la yule mtoto katika picha. Na inahusu nini sasa picha hiyo!!

    Nikabakli na swali kuu la kwanza, nikaiweka kando ile picha nikakutana na makaratasi mengine, moja lilikuwa na maandishi yaliyoandikwa na mtu ambaye anajifunza kuandika ama ni maksudi aliamua kuhadaa kwa namna ile. “THE DON 20 MKAKATI WA KUDUMU” Halikuandikwa neno jingine zaidi.

    Makaratasi yalikuwa mengi sana na pia picha mbalimbali, nyingine nikamuona Ezekiel, alikuwa amekumbatiana na mwanaume wa kizungu, kwa namna walivyokuwa Ezekiel alionekana kama hapendi kushikwa vile lakini ilimlazimu tu. Katika picha ya mzungu paliwekwa alama ya ‘x’….hapakuwa na maelezo kwa nyuma.

    Katika kila karatasi nilijaribu kubashiri majibu yangu lakini hata moja halikuonekana kuendana na ukweli wowote bambao ungeweza kunivusha hatua moja mbele.

    Ina maana Ezekiel alikuwa analazimishwa kuwa alivyokuwa?

    Nani alikuwa anamlazimisha?

    Michigan? Ni kitu gani hiki?

    Picha ya yule mtoto na yule mzungu aliyewekewa alama ‘x’ zinahusika vipi?

    Haya yalikuwa baadhi ya maswali yaliyolundikana katika kichwa changu!!

    Kabla sijamaliza makaratasi mengine, nilihisi njaa kali, hapa ni baada ya kusimama. Nilipoangalia saa ilikuwa saa kumi na mbili na nusu jioni. Nikakumbuka sikuwa nimekula kwa siku nzima.

    Ahadi ya kukutana na Enock nayo ikawa imekufa, kwa sababu simu yangu ya mkononi niliiacha ndani wakati naenda kuoga na sikurudi tena kuichukua.

    Nikajikongoja hadi nje na kufanikiwa kupata chakula. Nikala kwa kadri ya mahitaji yangu na kisha nikalipia na kurejea chumbani ambapo nilioga na kujaribu kujinyoosha kidogo. Usingizi ulipoanza kuninyemelea nikajiahidi kuwa nitalala kidogo na kisha kuamka, nipitie tena makaratasi yaliyosalia ili siku inayofuata niende polisi kisha nifike kazini pia kutafuta watu waelewa ambao wangeshirikiana nami katika mkasa huu wa ajabu ambao hadi wakati huo ulikuwa umenitia matatani.

    Haikuwa kama nilivyojiahidi, nilikuja kushtuka majira ya saa saa kumi na mbili asubuhi. Kitu cha kwanza kusikia zilikuwa ni kelele zilikzokuwa zinapigwa na mwanamke, nilizisikiliza kwa makini nitambue kama kuna hatari yoyote eneo lile lakini nikang’amua kelele zile hazikuwa na wasiwasi wowote na wala hazikuelezea uchungu wowote na badala yake zilikuwa zinaelezea raha fulani na huyo aliyezipiga hakujua kama alikuwa anapiga kelele na kusumbua wengine ambao walikuwa wamelala tena peke yao.

    Nikaghafirika na kuwashangaa wawili hao waliokuwa wakifanya mapenzi kwa raha zao na kutupigia kelel wengine.

    Nikachukua rimoti na kuwasha luninga bila dhumuni lolote ilimradi tu kukwepa kuzisikia kelele za mwanamke yule ambaye kwa lugha moja ningeweza kusema hajastaarabika.

    Nilisimama na kujinyoosha viungo kisha nikauendea mlango wa bafuni, nikaingia kwa ajili ya kujistiri na haja ndogo. Niliacha mlango wazi, sikuwa na shaka kwa sababu nilikuwa mwenyewe.

    Nikiwa maliwatoni, nilisikia vitu ambavyo akili yangu ilinituma kuwa ni muhimu nivisikilize, upesi nikarejea chumbani na kukuta mtangazaji akizungumza juu ya habari fulani ya kuvutia.

    “……mwandishi huyo ambaye alitimua mbio baada ya tukio anasadikiwa kufanya mauaji hayo kwa makusudi. Mwanamke aliyemshuhudia kwa jicho lake akitokea chumbani mwa marehemu anadai mwandishi alitimua mbio baada ya tukio hilo. Uthibitisho zaidi wa suruali yake ambayo ilisheheni simu ya mkononi ambayo imethibitika ni mali yake, pochi iliyokuwa na pesa taslimu laki tatu, katika suruali palikutwa pia na sumu kali ya kuulia wanyama. Jitihada za kumpata yeye na mkewe waliyekuwa wanaishi naye ziligonga mwamba. Hata hivyo mtoto wao mdo aliyejitambulisha kwa jina la Eva amehifadhiwa na jeshi la polisi Tanzania. Huku upelelezi wa kuhakikisha Samson Josephat na mkewe wanaingizwa nguvuni kwa kosa hilo la mauaji.” Alipomaliza kusoma habari hiyo, ilionyeshwa picha kwa ukaribu kabisa, ilikuwa ni suruali yangu, na pochi ilikuwa yangu lakini sumu na zile pesa hazikuwa mali yangu!!!

    Na mbaya zaidi waandishi na maaskari wakaaminishwa kuwa nguo zile zimekutwa katika chumba cha Ezekiel.

    “Mungu wangu..kwani yule dada hakuniona kuwa nilikuwa nimevaa suruali yangu na shati zuri kabisa!!” nilijiuliza kwa sauti kama kwamba kuna yeyote wa kushirikiana nami katika mjadala huu.

    Wakati nawaza juu ya mchezo huu wa ajabu na mchafu kuwahi kunikumba nikaikumbuka kauli ya mwisho ya mtangazaji…”Mtoto wao mdogo aitwaye Eva…..”

    Mapigo ya moyo yakapiga maradufu!!CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Eva alinizoea mimi na mama yake tu!! Hakuna mtu mwingine ambaye angeweza kuishi na Eva.

    Mtoto wangu jamani!! Nilijikuta katika manung’uniko na majuto wakati sijui najutia jambo gani!!

    Mambo yalikuwa yameharibika.

    Wakati nahangaisha kichwa changu kufikiria ni jambo gani sahihi natakiwa kufanya, habari ile ikaendelea, wananchi kadhaa walikuwa wakihojiwa juu ya tukio lile, macho yangu yakamwona yule mchezaji aliyeniita mwehu. Alizungumza kwa hisia kubwa sana akinishutumu kuwa alihisi tu kuna jambo baya nimefanya lakini wenzake wakampinga!!

    Nilitaka kumpiga ngumi lakini nikakumbuka kuwa kile ni kioo, yeye hayupo pale.

    Kwa siku ile sikuiona sura yangu ikirushwa kwenye luninga lakini ningejuaje labda vituo vingine walirusha picha yangu!! Hii ni hatari sana.

    Mke wangu yupo wapi?? Hii ni hila ya watu wabaya kwa sababu nimewakimbia basi wamemuunganisha na mke wangu katika tukio mili kuunda ukweli, maana kwa kumwacha yule angenitetea mpaka tone lake la mwisho la damu.

    Lakini hakuwepo tena!!

    Safari ya kwenda kituo cha polisi kutoa taarifa ikaishia pale na sasa nikawaza mengine, lakini hata yenyewe hayakujiweka katika mkondo mahususi!!!

    Nikapagawa!!!









    Nikiwa na utambuzi fika kuwa mambo yamenikalia vibaya mimi na familia yangu nikaamini kuwa huu ulikuwa wakati muafaka wa kuishughulisha akili yangu mara elfu moja zaidi nilivyojishughulisha kuandika simulizi ya KWAKO MPENDWA, simulizi ambayo ilinipa tunzo katika kampuni yangu.

    Nilitambua kuwa thamani yangu haikuwepo tena na mtu pekee wa kuweza kuirejesha ni mimi pekee. Upesi bila kuoga nikavaa suruali yangu na kisha nikatoweka kutoka katika nyumba ile ya kulala wageni. Wakati natoka nilipishana na muhudumu wa kike ambaye alinipatia chumba siku iliyopita.

    “Shkamoo….habari za asubuhi kaka…” alijing’atang’ata wakati wa kunipa salamu, kivipi binti ambaye tunalandana katika suala la umri anisalimie ‘shkamoo’ tena alionekana kubabaika waziwazi.

    Sikumjibu chochote, badala yake nilitoka nje na kisha kutokomea mbali zaidi na nyumba ile.

    Usafiri wangu kwa mara nyingine ukawa pikipiki. Nikapenya mitaa kadhaa na hatimaye nikafika Kibamba.

    Nikiwa na kofia kichwani, nikafanikiwa kununua na miwani. Nikajipachika usoni. Sasa niliamini kuwa hakuna ambaye angeweza kunona. Ilikuwa mara yangu ya kwanza kuyaficha macho yangu nyuma ya miwani.

    Nilitazama huku na kule hadi nikayafikia magazeti. Gazeti la kwanza kutazama lilikuwa ni Mwangaza. Gazeti ambalo nilikuwa nafanya kazi hapo.



    SAMSON AMESINGIZIWA: ASEMA MATATA.



    Nilijikuta natabasamu kidogo, Alfred Matata; huyu ndiye alikuwa mmiliki wa kampuni inayochapisha gazeti lile na kwa namna ya pili alikuwa bosi wangu. Aliniamini sana kupindukia na mara kwa mara alinishirikisha juu ya mambo yake ya siri.

    Walau mwajiri wangu ameutambua upande wa ukweli, huyu ndiye ambaye angeweza kunisaidia mimi kujua naanzia wapi. Nikalipia lile gazeti nikapatiwa nakala yangu na kisha nikapuuzia vichwa vingine vya habari vilivyosisitiza kuwa mimi ni muarifu na ninasakwa kwa udi na uvumba.



    “MATATA MATATANI KWA KUMTETEA MUUAJI” Kichwa hiki cha habari pia kilinivutia lakini nilipuuza baada ya kugundua kuwa lile ni gazeti la udaku.

    “Pumbavu kabisa…” nilijisemea huku nikitowewka eneo lile na kuambaa upande mwingine wa barabara, nikafikia kwa mama lishe ambaye alikuwa akichochea moto kwa ajili ya kuanza rasmi kuisaka riziki yake, nikachukua nafasi katika dawati lililokuwa pale.

    “Chai bado sana…” nilizungumza huku nikilifunua gazeti.

    “Kidogo tu baba yangu, lakini kitafunwa tayari, maandazi yapo na mihogo hii hapa nageuza.” Alinijibu kwa staha. Nikaendelea kusoma kurasa za gazeti lile.

    Nikaipitia taarifa kuhusu Matata kukanusha juu ya madai kuwa nimeua na kisha kukimbia. Kadri nilivyozidi kusoma moyo wangu ulisuuzika na lile barafu gumu la uchungu na wasiwasi lililokuwa limeniganda nikahisi likiyeyuka. Moyo wangu ukafanya majuto kidogo kwa kitendo changu cha kuwahi kujihusisha kimapenzi na binti wa mzee huyu, lakini cha kushukuru ni kwamba hakuwahi kugundua. Na hata baada ya kuanza kuishi kinyumba na Mama Eva, nikamtupilia mbali binti yule ambaye alidai ataendelea kunipenda kila siku.

    Potelea mbali, sikuwahi kumpa mimba na wala sikuwahi kumfelisha katika masomo yake!!

    Nikaimaliza makala ile huku nikipata mwanga juu ya wapi naenda kuanzia.

    Kwa sababu mama Eva alikuwa amekamatwa kiujanjaujanja basi mzee Matata angeweza kuwa mtu sahihi wa kuanza kuzungumza naye na hata kumkabidhi makaratasi yale ili tusaidiane katika ufumbuzi.

    Nikaanza kuifikiria safari ya kurejea jijini Dar es salaam kwa tahadhari kubwa ili niweze kuonana na mzee mwenye hekima,. Mzee Matata. Tena nilitakiwa kufanya maamuzi haraka sana kabla mambo hayajawa mazito na zile tetesi za kipuuzi kuwa mzee Matata matatani kwa kutetea muuaji hazijawa kweli.

    Nilitambua kuwa kwa mujibu wa muda ingeweza kuwa saa mbili za asubuhi, hata mama muuza naye nilipomuuliza alinijibu kwa uhakika kana kwamba ana saa mkononi, akasema ni saa mbili.

    Wakati huo nilikuwa namalizia pande la muhogo!! Nikagida chai na kufanya malipo kisha nikaambaa kuelekea kona nisizozifahamu, maeneo ambayo hayakuwa karibu sana na barabara.

    Huko nikakutana na kibao kilichoonyesha nyumba ya kulala wageni!!

    Eneo muafaka kabisa kwangu kwa wakati ule.

    Nikaingia pale na kukutana na muhudumu.



    “Vyumba havijafanyiwa usafi kaka hadi saa nne ndo wateja wa mwishomwisho wanatoka.” Balinijibu kichovu huku akijifuta tongotongo machoni.

    Nilijipigia hesabu za kichwa na mara nikakumbuka kuwa wasiwasi wangu wa kurejea mjini, ulikuwa wa bure. Mwanzo nilihisi kuwa mzee Matata atakuwa kazini, lakini nikakumbuka kuwa asubuhi hiyo ilikuwa jumapili. Lazima angekuwa nyumbani kwake. Nikaondoka na kisha nikachukua pikipiki tena, bahasha yangu ikiwa kitu cha muhimu kupita chochote katika mwili wangu!! Nikapepea hadi maeneo ya Shekilango!!

    Nikafanya malipo na kuchepuka kwa hatua kubwa kubwa nikavuka barabara na kuingia vichochoro kadhaa, hatimaye nikatazamana na nyumba ya mzee Matata. Makala yake kuhusu mimi ikaendelea kunijengea uaminifu kwake, nikagonga hodi nikapokelewa na mlinzi ambaye alikuwa akinifahamu, sikutaka kuzungumza naye sana, nikaingia hadi ndani, nikaufikia mlango mkuu wa kuingilia.

    Aliyenipokea alikuwa mke wa mzee Matata, akanikaribisha kwa ukarimu wote kama ilivyo kawaida yake, baada ya salamu akaniuliza kama nitakunywa chochote, nikataka kukubali lakini nikahisia nitapoteza muda wakati mihogo ya mama lishe bado ilikuwa tumboni.

    Nikashukuru na hapo nikamuulizia mzee Matata.

    “Ameenda kanisani.” Akanijibu kwa sauti tulivu huku akihangaika kupunguza sauti katika runinga iliyojiongeza sauti kimakosa.

    Jibu la mwanamke huyu likanistaajabisha lakini nikajificha nisijulikane kama nimestaajabika, mzee Matata na kanisa wapi na wapi? Kila siku ofisini alikuwa akitukashfu sana watu tunaojifanya kuhudhuria kanisa wakati kanisa ni biashara. Mzee Matata hakuwahi kusifia lolote juu ya nyumba za ibada ambazo mkewe alikuwa muhudhuriaji mzuri sana na hata watoto walifuata nyendo za mama yao. Kasoro yeye tu!!

    Iweje leo ameenda kuhudhuria ibada. Tena asubnuhi yote ile.

    Nikaguna lakini sikuuliza kingine nje ya uwezo wa yule mama, badala yake nikaulizia atarudi saa ngapi.

    “Ibada huwa inamalizika saa sita, nadhani unaweza kukadiria.” Alinijibu, sasa alikuwa ananitazama machoni.

    Nikapiga mahesabu yangu upesiupesi nikakutana na jibu la uongo!!

    Ibada ipi ya kumalizika saa sita wakati kwa maelezo ya awali mzee Matata alitoka asubuhi sana.

    Kwanini ananidanganya? Nilijiuliza huku nikijisikia vibaya kudanganywa na mama yule mtu mzima.

    “Haya mimi nipo jikoni mara moja…rimoti hiyo unaweza kubadili chaneli” alitoa kauli hiyo huku akisimama na kujifunga kanga yake vyema kisha akatoweka.

    Hakuelekea jikoni!!! Uongo mwingine. Mzee Matata kama nilivyokwisha elezea alikuwa mzee wangu wa karibu kuna kipindi mkewe akiwa masomoni niliishi nyumbani kwake, kwa siku kadhaa nilizijua kona nyingi sana. Na hata mtoto wake nilimpata kipindi hicho.

    Nililifahamu jiko lilipokuwa, lakini mwanamke huyu hakwenda jikoni!!

    Kwanini?

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Wakati najiuliza na kuumiza kichwa juu ya hayo mara mtu alivamia sebuleni ghafla huku akiweka tahadhari juu ya uwepo wake katika sebule ile.

    Nikashtuka kidogo, nikamtazama na kuwahi kutaka kumsalimia, lakini kabla sijasema lolote akaniziba mdomo. Mikono yake ya uvuguvugu iliyokuwa inanukia marashi haikunikera.



    “Sam….wanasema umeua, umeua jana Sam. Sikia kama ni kweli umeua Sam, hapa si mahali sahihi hata kidogo pa wewe kukaa hata kwa sekunde moja. Baba na mama wametishwa sijui na nani? Wameambiwa wanatambua wewe ulipo Sam, kama mama amekwambia baba ameenda kazini ni uongo mtupu, amepeleka vyeti vyako vyote vya shule polisi amepeleka picha na kila kitu kuhusu wewe, alama yako ya dole gumba, jaribu kunielewa sam. Amepeleka kila kitu!!! Kila kitu sam….Sam pliiiz Sam unajua kuwa nakupenda, na kwa namna yoyote aidha umeua ama hujaua, sam nakutambua kama mwanaume mkarimu kupita wengi katika maisha yangu, sikukosea kukupenda sam, na nilikuahidi kuwa nitakupenda milele, Sam ukiendelea kuwa hapa watakufunga Sam. Sitaki kujua kwa nini uliua lakini sitaki kusikia ukihukumiwa kunyongwa. Mlizni getini aliambiwa ukionekana hapa asikuruhusu kutoka tena. Na makala aliyoiandika upesi upesi alitaka kukujenfea imani naye. Baba anatamani upatikane ili kampuni yake iendelee vizuri Sam….” Alishindwa kuendelea kuzungumza yule binti akaanza kutokwa na machozi. Bado alikuwa ameniziba mdomo. Alikuwa anatetemeka na uso wakle ulimaanisha kila alichokuwa anasema.



    “Anitha…sikia Anitha ukilia si ndo utanipoteza mimi ama…nyamaza nambie nafanya nini, Anitha sijaua hii ni njama tu. Njama ya kuniteteketezaq family yangu kutokana na siri nzito Anitha. Siri ambayo…..yaani aaah…Anitha nisaidie nitoke.” Nilimwambia kwa kunong’ona huku kiganja changu kikiwa kimejikita katika kubadili Chaneli hovyohovyo bila sababu za msingi, nilikaa mfumo wa nusu tako kitini nusu nyingine isieleweke kama ipo hewani ama imefanya mgomo wa kukaa.

    Ni kama nilitaka kusimama.



    “Sam….Sam…mama mama huyooo atajua….” Aliweka tahadhari na kisha akatimua mbio kuelekea vyumbani.

    Na hapo akafika mama mwenye nyumba, nilirudisha miwani usoni asiweze kuisoma hofu yangu!!

    “Anakuja baada ya kama nusu saa hivi, kumbe wametoka tayari. Pole kwa kumsubiri shemeji yangu jamani.” Alinikarimu, lakini sasa sauti yake ilikuwa katika namna ya maigizo na uso wake ukitangaza hasira.

    Nikayaamini maneno ya Anitha, msichana ambaye aliwahi kuwa mpenzi wangu lakini kutokana na heshima kubwa niliyokuwanayo kwa mzee wake nikaamua kuyatupia mapenzi kando.

    Sasa alikuwa amenionyesha maana ya upendo!! Anitha hakuwa ameamini hata kidogo juu ya tetesi za mauaji niliyofanya, na hata kama ni kweli alikuwa amesisitiza kuwa hatajali.

    Mwanamke wa kipekee!!

    Mama aliendelea kupiga porojo zake nami nikaweka tabasamu bandia, alisema anarejea baada ya nusu saa na Anitha alinieleza kuwa mlinzi alizuiwa asiniruhusu nitoke baada ya kuingia.

    Hawa jamaa ni akina nani hawa? Inawezekana wakawa ni polisi kweli wameamini kirahisi hivyo kuwa nimeua?

    Nilijiuliza na dakika kumi na tano zilikuwa zimekatika!!

    Mama alikuwa akiongea maneno mengi tofauti na kawaida yake!! Nikajua hii ni njama nyingine ya kunihadaa, njama ya kunipotezea wakati ili mumewe afike na polisi ama na yeyote yule waweze kunikamata.

    Na kama ni njama walikuwa wamefanikiwa haswa! Ningeaga vipi pale na kuweza kutoroka na kisha kujipanga upya.

    Ghafla wazo likajikita katika ubongo.



    “Hivi mama zile picha za sherehe ya kutimiza miaka hamsini zipo ujue siku ile mama Eva alinighasighasi hata sikuzitazama vyema…”

    “Wacha weee!! Haukuziona kumbe ngoja nikuletee maana zipo katika albamu…nzuri hizo.” Alisifia huku akiondoka, nikaisoma akili yake kuwa yule mama alikuwa amejidanganya kuwa kwa kuangalia albamu ile nitakuwa nimemsaidia katika zoezi la kuuvuta muda maana kama ni maongezi hakika alikuwa ameishiwa.

    Wakati huo zilisalia takribani dakika tisa itimie ile nusu saa aliyoisema mama huyu kuwa mzee Matata atarejea.

    Alipotoka na mimi nikaishika vyema bahasha yangu na kusimama, kumbe Anitha alikuwa akinitazama kupitia alipokuwa amejificha.

    “Anitha, kama wakinikamata usiachie hii bahasha iende kizembe. Humu kuna kila kitu!!” nilimwambia kwa sauti ya kukwaruza kwaruza. Na nikamwona macho yake yakilengwa na machozi. Sikugeuka tena.

    Nikaondoka na kulifikia geti, geti lilikuwa limefungwa kwa kufuli lakini halikuwa limebanwa, nilipojongea nd’o kwanza mlinzi akalibana lile kufuli kisha akaendelea kuvuta sigara huku akipuliza moshi hewani.

    Ametimiza wajibu!! Nilijisemea huku akili ikigoma kabisa kujua ni kipi nafanya kwa wakati huo. Nilijua kuwa Anitha ananitazama kwa huzuni kubwa, nilijua mama amekaribia kufika tena sebuleni akiwa na albamu, na kubwa zaidi nilitambua kuwa mzee Matata si rafiki tena bali adui mkubwa na muda wowote ule anawasili hapo kwa ajili ya kunikamata aidha akiwa na polisi ama akiwa amehadaika na njama za wale watu wabaya waliochanganyikana na wazungu!!!!

    Miguu ilikuwa inatetemeka na bahasha ikaanza kulowa jasho, jasho jepesi kutoka katika kwapa lililokuwa limeibana vyema.

    Nimekamatika!!





    **Rafiki hugeuka adui, usimwamini mtu kwa asilimia mia. Jiamini wewe kwa sababu kamwe huwezi kujidanganya na hata ukijidanganya utatambua kuwa unaponda maji kwenye kinu!!!! Yaani ni kazi bure……

    Lakini moyo wa mwenzako ni kiza kinene!! Huwezi kujua……. JIFUNZE



    AKILI ilikuwa imesimama na si haba nilielekea kuwa mwendawazimu huku nilichokumbuka pekee ni midomo yangu kutetemeka huku nikimtaja Eva na mama yake. Mizimu niliyoiomba haikuniletea muujiza wowote.

    Mlinzi Yule aliendelea kucheka kifedhuli huku akijitahidi kadri ya uwezo wake kuvuta sigara na kupuliza moshi hewani katika namna ya majigambo.

    Nikiwa katika hali ileile niliisikia sautio nyembamba ya kike ikisema name katika namna ya kusihi, nilipata nguvu ya kugeuka huku nikiilazimisha akili yangu isijiruhusu kukutana na mama mwenye nyumba.

    Kha!! Hapakuwa na mtu yeyote, hii nayo ikanistaajabisha. Lakini sauti iliendelea kusihi. Nikajipa ujasiri huku nikijitoa hofu kuwa mimi si mwizi wala sijaua. Na kwa misingi hiyo sitakiwi kuwa muoga.

    Kwa mtazamo huo na masikio yangu yakafunguka. Nikasikia sauti ikisema name kiingereza.

    Maneno yakaniingia na nguvu ziukanijaa tena, ilikuwa ni sauti ya Anitha ikinisihi jambo, macho yangu yakang’ara na kung’amua kuwa Yule mlinzi alikuwa amezeeka na hakuwa na ubavu wa kunizuia kwa lolote lile. Na hapo nikagundua kwa nini nilikuwa na hofu kubwa mwanzoni.

    Kauli ya Anitha ikanisukuma. Nikatoka mbio na kumvamia Yule mzee, nikamjaza kilo kadhaa za ngumi usoni. Tukio ambalo hakulitegemea, akapepesuka huku sigara ikimtoka mdomoni. Akatoa miguno ya maumivu, na hapo nikapata upenyo.

    Kauli ya Anitha ikarudi tena kwa nguvu katika kumbukumbu zangu. Kauli aliyoniambia kwa lugha ya kiingereza.

    “Hilo kufuri ni bovu….”

    Nikalivuta likaachia, nikatoka mbio huku bahasha yangu ikiwa mkononi. Wakati napepea nikaiona gari aina ya difenda ikitimua vumbi kuja katika nyumba yam zee Matata.,

    Walikuwa wamenikamata hawa wajinga!!

    Nilijisemea huku nikijilazimisha kurejea katika hali ya kawaida.

    Nikaingia mitaa miwili ama mitatu na kutokea Sinza kijiweni. Nikajichanganya na umati wa watu wengi, kwa tahadhari kubwa kabisa nikachukua tena pikipiki na kuondoka hadi Mbezi ya Kimara. Huko nikachukua chumba kama kawaida katika nyumba ambayo ni ngumu kufikika katika mazingira ya kawaida.

    Nilipojifungia ndani nilifikiria jambo moja tu!!

    Nilikuwa napambana na nguvu kubwa!! Nilitakiwa kuwa makini.

    Anti Ezekiel!!!!

    Jina hilo likanijia kwa kasi katika namna ya kustukiza, kijana ambaye nilionana naye mara tatu katika maisha yangu huku ile ya nne ikiwa utata. Utata mtupu!!

    Huyu Ezekiel anayesadikika kuwa ni shoga ni nani hasa hadi asababishe yote haya?

    Na nkwanini haya yote yatokee baada ya mimi kufahamiana naye kwa uchache sana?

    Nilijiuliza bila majibu!! Nikabaki kufahamu kuwa jambo pekee nililokuwa nalifahamu kiuhakika kabisa ni kuwa Yule bwana aliitwa Ezekiel. Sikujua jina la baba wala mama yake.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Nikaifungua bahasha yangu tena na kuanza kupekua huku na kule, nilikuwa sijamaliza kupitia zile karatasi ambazo nilizichukua nyumbani kwa Ezekiel. Nikaamua kuzipitia zilizokuwa zimesalia.

    Nikapekua huku na kule, nikakutana na karatasi moja ambayo iliandikwa jina tena, si karatasi hii pekee iliyokuwa imeandikwa jina lakini hili lilikuwa na utofauti katika akili yangu.

    Kindo!!!

    Kindo halikuwa jina geni katika akili yangu, ika karatasi ile chini ya jina iliwekwa tarehe, tarehe ya mbali sana. Takribani miezi tisa iliyopita.

    Cha kushangaza sikutaka lile jina linipite kama mengine kuna mahali nimewahi kulisikia, ama nimewahi kumuita mtu jina lile.

    Nikaigeuza ile karatasi kwa nyuma na hapo nikakutana na neno lililonipa uhai wa kuendelea kutafuta jibu la wapi nimeskia jina lile.

    Sinza.

    Mwandiko ule mbovu uliandika vile. Hivyo nikawa na kazi ya kuunganisha mwezi jina na mahaliu.

    Kwanini kindo, Sinza na mwezi huo.

    Ghafla nikasimama wima na kukibinya kichwa change, kuna kitu kilijileta katika mstari.

    Jina la Kindo nililisikia wakati natafuta pikipiki ya kunibeba na kunifikisha Mbezi. Nilisikia kama si yeye akijitambulisha kwa jina basi alikuwa ameitwa na mwenzake.

    Mtu sahihi wa kunisaidia katika safari ya kuutatua utata huo alikuwa ni Kindo!!

    Lazima kuna kitu alijua juu ya Ezekiel, huenda ni ndugu ama jamaa au vyovyote vile lakini lazima tu!!

    Lazima angefahamu lolote kuhusiana na Ezekiel.

    Nikataka kutoka chumbani muda uleule nikamtafute Kindo lakini nikahofia kujiingiza matatani mapema sana, Sinza na Shekilango hayakuwa maeneo yanayoachana kwa mbali sana.

    Shekilango nilikuwa nimezusha balaa tayari nyumbani kwa Mzee Matata, hapakuwa mahali sahihi hata kidogo kuonekana hata kwa bahati mbaya.

    Muda huo nikataka kujipumzisha lakini nikamkumbuka Enock. Niliahidi kuzungumza naye kwa njia ya simu siku iliyopita lakini nikashindwa kutimiza ahadi. Nilifikiria ugumu ambao atakuwa anapitia katika kichwa chake kutokana na ukimya wangu na pia akilinganisha na vuguvugu hizo zilizosambaa mtaani tayari.

    Nikautambua umuhimu wa simu, nikakifunga chumba change, bahasha nikiiweka chini ya godoro na kuondoka kuingia mitaani, nikapata simu ya bei rahisi, nikanunua na kadi mpya nikaiwekea pesa. Nikaondoka na kurejea chumbani.

    Nikaiandika namba ya simu vyema kutoka katika kumbukumbu ya kichwa change na kisha nikapiga.

    Simu ilinitia matuamini ilivyoanza kuita na baadaye kupokelewa.

    Alikuwa mke wa Enock. Nilitaka kujitambulisha lakini mara Enock akawa ameichukua simu.

    “Noki eeh!!” nilimwita. Na hapo akaitambua sauti yangu!!

    Simu ikakatwa nisijue nini tatizo lakini baada ya dakika zisizozidi kumi na tano alinipigia.

    “Kaka, nini tena hicho umefanya lakini eeh nini kaka, halafu hata hujaniambia. Mimi na wewe tumeanza kufichana mambo yetu tangu lini Sam eeh Sam…” alilaumu Enock.

    “Sikiliza Enock…hivi umeyaamini hayo uliyoyasikia.” Nilimuuliza kwa sauti iliyotulia kabisa.

    “Sijaamini hata moja Sam lakini kama ulijua una msala kwa nini usiniambie. Sikia polisi wamekuja kunisumbua hapa yaani wamepekua kila kona ya nyumba hii kaka. Hivi mbona hata hukuwahi kuniambia kuwa una bunduki Sam eeh Sam ilikuwa nia yako kuniingiza matatani ama?” sasa alisikika kupandwa na hasira.

    Nikastaajabu, ina maana hawa watu wameunda uongo kiasi hicho hadi wamebambika kesi kuwa mimi namiliki bunduki? Nilikaa kimya Enock akaendelea kulalamika, “Sasa mimi hiyo kesho naenda kutoa maelezo gani kituoni eeh naenda kusema nini mimi. Urafiki gani huu sasa?” alizidi kufika mbali na nikaisikia ile kauli yake ya mwisho iliyokuwa katika mtindo wa kujutia urafiki wetu.

    Yaani Enock niliyempokea Dar es salaam maisha yangu magumu lakini nikamtunza, nikamtafutia kazi na mwisho akaweza kujitegemea na kuoa, leo hii anasikitika kuwa rafiki yangu.

    Nilitaka kumweleza mengi kuhusiana na ule mfuko wenye makaratasi lakini sikuona umuhimu wowote ule kwa sababu tayari alikuwa mguu ndani mguu nje. Nusu aliniamini na nusu hakuniamini.

    Hakunifaa hata kidogo katika harakati.

    Nikakata simu na kuizima kabisa, hasira ilinichemka kichwani!!!

    Nilijua kuwa anaweza kunitumia ujumbe wowote ule na pia nilijua kuwa namba yangu ile ipo matatani tayari.

    Sikuiweka tena katika simu!! Nikatoka nje na kwenda kununua kadi nyingine. Zote nilikuwa nazisajiri kwa majina feki.

    Ile namba ya awali nikaitupilia mbali kabisa baada ya kuivunjavunja, sikutaka kumfikiria Enock tena, nikazitazama nguo zilizokuwa katika mwili wangu, zilikuwa mali yake. Nikachukia kujitazama.

    Nikatamani kununua nguo nyingine lakini nikatambua kuwa katika kipindi hicho nilikuwa naihitaji pesa kuliko wakati mwingine.

    Nikarejea chumbani!!

    Nikajitupa kitandani usingizi nao ukasusa kunipitia, nikagalagala huku na kule pasi na mafanikio!! Saa kumi na moja ikanikuta nikiwa bado sijaupata usingizi. Nikaishika simu yangu yenye kadi mpya nisijue ni kitu gani inanisaidia.

    Nikabofya namba nyingine nilizozikariri huenda nitapata msaada wa kimawazo. Sikujua kama nitabonyeza namba zile kwa usahihi, lakini nilifanikiwa kubofya.

    Simu ikaita kwa muda mchache sana na kisha ikapokelewa.

    Alikuwa yeye!!! Sauti yake haikuwahi kupotea masikioni mwangu kamwe!!

    “Nani mwenzangu mbona huongei?” alikaripia nilivyoendelea kuwa kimya.

    “Anitha…..Sam hapa….upo mahali sahihi tuzungumze kidogo.” Nilinong’ona. Kimya kikatanda, na mara Anitha akazungumza name, alikuwa amejifungia chumbani mwake.

    Sikutaka kujua nini kilitokea baada ya mimi kufanikiwa kutoroka lakini nilitaka msaada wake kimawazo kama bado angekuwa radhi kunisaidia. Anitha aliniambia kauli moja nzito ambayo ilinifanya niamini kuwa sasa nimepata wa kunishika mkono.

    “Sam, kwa lolote lile nipo na wewe, najua wewe si muuaji, najua kuna kitu nyuma ya pazia japo sijakijua kitu hicho, nipo tayari kushirikiana na wewe ilimradi tu mimi na wewe tukivumbue kitu hicho.” Kisha akashusha pumzi na kunisikiliza.

    “Anitha wewe ni msichana wa kipekee, nisizungumze sana lakini naomba nikuamini wewe. ….aaahm ni lini unaweza kutoka nyumbani.’

    “Siku yoyote ile, si unajua nipo chuo siku hizi.”

    “Ok kesho naomba ufanye jambo moja la msingi na litakalotuwezesha kujua wapi tunaanzia, hapo Sinza Kijiweni ama Sinza popote pale kuna mtu anaitwa Kindo, simjui kwa sura wala sauti lakini ni huyu anajua kuhusu Ezekiel..”

    “Ezekiel ni nani?” alinikatisha. Nikalazimika kumsimulia upesi kwa ufupi sana juu ya hadithi ya shoga niliyemuona Ubungo akanipa funguo na kisha nikaikuta maiti yake ikioza kitandani Yombo Temeke.

    Maelezo yangu yakamuacha Anitha katika kigugumizi lakini akaahidi kushughulikia jambo hilo.

    “Kwani huwezi kuja chuoni kesho.”

    “Hapana sitakiwi kuonekana kwenye hadhara kubwa namna hiyo ni hatari.”

    “ila kweli, sawa Sam nitakupigia kwa lolote.”

    “Hautanipigia wewe nitakupigia mimi Anitha. Simu haitakuwa ikipatikana mara kwa mara.” Nilimaliza mazungumzo na kisha kukata simu.

    Hapo sasa niliweza kulala na amani kidogo moyo wangu nikiuegemeza kwa Anitha ambaye niliamini anaweza kunisaidia kwa lolote lile, lakini sikujitoa moja kwa moja kwake. Nilikuwa nusu namuamini na nusu nikiishi kwa tahadhari.



    Baada ya kula chakula cha usiku majira ya saa tatu usiku niliiwasha tena simu yangu na kisha nikambipu Anitha.

    Upesi akanipigia.

    Hakunipa nafasi ya kuzungumza na badala yake akachukua usukani kusimulia.



    ANITHA



    SAM najua upo matatani sana, nisingeweza kungoja hata kidogo hiyo kesho ifike ili nianze kumtafuta huyo mtu wa kuitwa Kindo.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Sinza ni kubwa lakini kama una nia ya dhati ni mtaa mdogo sana kuumaliza,. Niliondoka nyumbani nikimuaga baba kuwa naenda chuoni, lakini sikuwa na safari hiyo, safari yangu ikaishia mitaani. Halikuwa jambo jepesi kumpata mtu usiyejua hata kazi yake, lakini nilifanya kwa ajili yako Sam. Nilifanya nikijua kuwa wewe upo upande wa haki, na hakika upo katika haki.

    Mungu hamtupi mwenye nia na anayemtegemea, nilipopiga hatua yangu na kuanza rasmi kumtafuta Kindo nilimtanguliza Mungu, niliulizia kila kona na kila ofisi lakini sikumpata Kindo. Wengine walidai kumfahamu lakini hawakuonyesha ushirikiano kabisa, hadi ilipotimu saa kumi na mbili jioni maeneo ya Sinza kijiweni nikiwa najiandaa kupanda gari nirejee nyumbani pasipo na mafanikio nikasikia jina kama hilo likiitwa. Nilikuwa nimebanwa hasa lakini nguvu za kusukuma abiria wengine zilipatikana nikafanikiwa kupenya na kushuka chini, nikamuuliza mwanafunzi mmoja akaninyooshea kwa kidole huyo mtu wa kuitwa Kindo.

    Ni teja…teja aliyekubuhu, madawa ya kulevya yameweka makazi katika mwili wake, sikuweza hata kusema naye maana alikuwa akitiririkwa na udenda na alikuwa ameuchapa usingizi. Nikapata kigugumizi kuamini kama kweli huyu ndiye Kindo uliyeniagiza kumtafuta ama kuna Kindo mwingine.

    Swali hili nilitamani nije kukuuliza lakini ukadai kuwa hujawahi kumwona Kindo na hata hujui sura yake ilivyo. Kama ungekuwa unamfahamu walau ningekwambia haya Sam. Kuwa kindo ni mweupe wa zamani lakini sasa hajulikani rangi yake, ni mrefu wa wastani na kichwani hana nywele.

    Kwa sababu nisingeweza kusema na mtu asiyesema kwa tahadhari kubwa nilijipiga picha nikiwa usawa wake na katika hiyo picha ameonekana, kama unayo barua pepe nitakutumia uweze kumwona teja huyu wa kuitwa Kindo.

    Na hapo tutajua kama ndiye ama siye!!

    Kesho nitaenda tena kumwona kama akiwa anaongea nitamuuliza juu ya Ezekiel. Tumwombe Mungu atoe jibu zuri, maa sura yake licha ya kumwagika kwa madawa inatangaza chuki kali. Sijui anachukia nini Mungu wangu!!!



    ANITHA akamaliza!!!



    Nilibaki nimekaa hivyohivyo kitako katika kitanda cha futi nne kwa sita, maelezo ya Anitha yalizidi kuzua utata. Japo mwanga ulionekana lakini mwanga huu ulikuwa hafifu sana walau kunipa uwezo wa kupiga hatua moja mbele.

    Ni kweli nilikumbuka kuwa nilisikia jina kindo palepale Sinza kijiweni, lakini katika ile karatasi paliandikwa kuwa ni miezi tisa iliyopita.

    Sasa kilitokea nini miezi tisa iliyopita. Je ni kweli huyu Kindo anayetakiwa ama? Ama Anitha naye anataka kunichezea kamchezo!!!

    No no no!! nililipinga wazo la kumfikiria Anitha vibaya, ni asubugi tu alitoka kuniokoa sasa iweje jioni anikane???

    Hapana ilikuwa mapema sana kumwazia vibaya!!!

    Nikarejesha mawazo yangu kwa Kindo!!

    Kindo teja, kindo mwenye kipara Kindo asiyejitambua, kindo wa miezi tisa iliyopita.

    Kindo ambaye Anti Ezekieli alikuwa amemworodhesha katika karatasi zile.

    Hakuna picha wala neno la ziada!!!

    Utata!!!!



    **JIFUNZE: Katika maisha usipende kumfahamu mtu kwa kuhadithiwa na fulani, ili umfahamu mtu vyema na tabia zake basi akili yako ikupe majibu yenyewe kutokana na vitendo vya huyo mtu. Usimuulize jirani yako ama usitumie tetesi kumfahamu mtu. Je? Utajuaje kama hao wanaokwambia wana chuki naye? Utajuaje kama ni marafiki zake na sasa wanamsifia kwa lolote!!!

    Epuka!! Na hii itakusaidia kujua kuishi na mwanadamu!!

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    *SAM ameamua kumwamini Anitha na anajiepusha kumwazia vibaya ikiwa hajauona ubaya wake, Anitha amekutana na Kindo asiyejitambua, Teja aliyekubuhu!!!

    Je? Ni huyu? Na kama ni huyu anajua nini kilichotokea miezi tisa iliyopita??



    ITAENDELEA



0 comments:

Post a Comment

Blog