Simulizi : Msafara Wa Mamba
Sehemu Ya Tano (5)
ILIPOISHIA:
Kauli ile ilinishtua na kunifanya nikae vizuri kwenye kochi kutaka kujua niangamie kwa sababu gani.
"Mai una maanisha nini?"
"Hivi wewe na Joel mmejuana muda gani?"
"Mbona unaniuliza hivyo?"
"Herena jibu swali sio kuuliza swali juu ya swali."
"Muda mrefu."
"Unamjua vizuri?"
SASA ENDELEA…
"Kivipi?"
"Maisha yake kwa ujumla."
"Ndiyo," nilimjibu kwa mkato.
"Si kweli humjui vizuri Mr Joel," Mai alinikatalia bila kumwelewa.
Maneno ya Mai yalizidi kuniweka njia panda na kushindwa kumwelewa alikuwa akimaanisha nini.
"Mai mbona kama sikuelewi?"
"Ni vigumu kunielewa ila utanielewa muda si mrefu."
"Ehe una maana gani?"
"Herena mimi namfahamu vizuri Mr Joel kwani ile ndiyo hospital yake na siri zake naweza kusema nazijua mimi kati ya wafanyakazi wote."
"Unataka kuniambia ulikuwa mwanamke wake?" niliona Mai alitaka kunirusha roho.
"Sivyo ufikiliavyo, unajua Mr Joel ni rafiki mkubwa wa mchumba wangu hivyo ana siri zake nyingi ambazo aliniambia kama mchumba wake pale Mr Joel alipokuwa akija na wasichana kupima afya zao."
"Sasa Mai umekuja kunirusha roho ili niachane na mpenzi wangu, Mai unajua japo ni rafiki yangu naweza kukubadilikia sasa hivi naomba uzungumze mengine yaliyokuleta kuhusu mpenzi wangu hakuna cha kututenganisha.
“Walianza ooh ameathirika yote ili kunitilia mchanga chakula changu. Lakini leo umewaumbua watu , hilo halijaisha nawe unakuja na yako kujuana imekuwa nongwa au nawe ni mmoja wa wake wenzangu?"
"Herena kila unalofikiria sivyo la muhimu ni kuwa msikivu, mimi simtamani Mr Joel ila kilicho nileta hapa ni umuhimu wa ukaribu wangu na wewe. Sipo tayari kukuona ukiangamia nikikuona wakati bado una nafasi ya kuokoka."
"Mai kuwa muwazi ulikuwa ukitaka kusema nini juu ya Mr Joel?"
"Japo hili ni siri kati mume wangu na Mr Joel lakini kisu kimegusa mfupa. Herena ndio maana mwanzo nilisema wenye pesa wanatumaliza, kubali usikubali Mr Joel ni muuaji mkubwa."
Kauli ile ilifanya nihisi kama kuna kitu kimechoma katikati ya moyo wangu.
"Mungu wangu Mai una maana gani kumwita mpenzi wangu muuaji mkubwa?"
"Herena ndugu yangu yule mzee ni hatari anatumia pesa zake kueneza virusi vya ukimwi kwa wasichana na mwanamke yoyote mzuri. Ni wasichana wengi amewaumiza ambao ninaowafahamu ni zaidi ya wane."
"Mai ni maneno gani hayo ya uongo unayoyaleta nilikuona tokea mwanzo ukimtolea macho mpenzi wangu tangu nilipokutambulisha. Kwa hiyo naomba utoke taratibu kabla sijakasirika," nilimbadilikia.
"Herena hebu punguza munkali ninacho kizungumza ni kwa faida yako leo na kesho tusije nyoosheana vidole au kulaumiana kwa kujua jambo na kukaa kimya."CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
"Nimesema tokaaa...kama hutaki nitakumwagia maji ya moto unajifanya rafiki kumbe mnafiki...tokaaa."
Nilijikuta nimepandisha jazba na kumfukuza Maimuna kwa sauti ya juu kitu kilichomfanya mama atoke chumbani baada ya kutuacha tuzungumze. Alipotoka alinikuta nikimnyanyua Mai kwa nguvu ili nimtoe nje japo Mai aling'ang'ania kama shetani wa kutumwa.
"Herena vipi tena mbona hivyo?"
"Mama huyu ni mmoja wa maadui zangu."
"Maadui zako kwani tatizo nini? Hebu muache kwanza."
"Kila kukicha maadui wanaongezeka juu ya penzi langu na Anko wananiona nafaidi naye huyu kaja na mapya. Mama leo mwenyewe umeamini kuwa Anko afya yake ni salama yeye analeta umbea kuwa Anko ni mmuaji kamuua nani kama alikataliwa si yeye."
"Hebu punguza jazba eti mwanangu tatizo nini?" mama alimuuliza Mai.
"Mama sikiliza mimi na Herena ni marafiki wa muda mrefu sana sema tulipoteana. Kwa kweli leo nilipomuona nilifurahi sana ila furaha yangu ilitumbukia nyongo baada ya kujua rafiki ya shoga yangu ni yule muuaji mkubwa."
"Una maana gani kusema ni muuaji?" mama alimuuliza.
"Mama Mr Joel ni muathirika wa kipindi kirefu zaidi ya miaka saba sasa ila amekuwa akitumia madawa ya kuongeza nguvu. Hata mkewe mama Jose ni muathirika ila mkewe amekuwa akifuata ushauri wa daktari. Ila mumewe amekuwa kiwembe kwa kuusambaza ugonjwa kwa wasichana wadogo hasa wanafunzi na wanawake wazuri.
“Kwa vile hammjui vizuri ule sasa hivi si mwili wake alikuwa ana mwili mkubwa sana ila kutofuata ushauri kila kukicha akija hospital anapungua uzito."
Yalikuwa maneno mapya yaliyonifanya nirudi hadi kwenye kochi na kukaa nikifikilia kauli ya Maimuna ilikuwa na ukweli gani.
"Kwa nini unasema hivyo wakati leo tu tumetoka kupima na kukutwa wote wapo sawa?" Mama alimuuliza.
"Ni kweli majibu yameonyesha sawa ila ukweli unabakia palepale kuwa Herena yupo sawa ila Mr Joel ameathirika."
"Mbona hapo sikuelewi mwanangu aathirike kivipi majibu yameonyesha yupo sawa?" mama alishangaa.
"Mama ile ni siri nzito ambayo ameibeba mchumba wangu na baadhi ya madaktari wa ile hospitali ambao hupewa pesa kupindisha ukweli."
"Unasema?" Nilijikuta nimeropoka na kukaa kitako.
"Ukweli ndio huo kila siku anapobanwa na wasichana kupima hawezi kupima sehemu nyingine zaidi ya hospital yetu. Kama mnaona mimi muongo mwambie mwende hospitali nyingine kama atakubali."
Tulijikuta tukitazamana na mama kila mmoja alikosa jibu Mai aliendelea kuzungumza:
"Kwa kweli nimekuwa nikiumia kitendo cha Mr Joel kuwadanganya wasichana. Lakini leo kisu kimegusa mfupa sikuwa radhi kukuona ndugu yangu mtu niliyemuona kama taa yangu ukiumia nakuona lakini ukweli ndio huo."
"Mmh! Kweli naamini maneno yako mwanangu lazima nami niseme ukweli mimi mama yako nimeathirika na mtu aliyeniambukiza nilijua ni yeye lakini mwanangu alikuwa mbishi nina imani ukweli umeujua."
Nilikuwa kama nipo ndotoni nisipate jibu juu ya kuathirika kwa Anko iweje aathirike mimi niwe mzima. Japo niliamini kwa upande mmoja lakini kwa upande wa pili bado moyo ulikuwa mzito.
Kwa ushahidi Maimuna alitotolea vyeti vya Anko vilivyoonyesha ameathirika na jinsi maendeleo yake ya chembe za CD4 mwili. Baada ya wote kuvitazama nilijikuta nikitokwa na machozi na kunyanyuka hadi kwa Mai na kumpigia magoti kumuomba msamaha.
******************
Siku ya pili nilikwenda hadi kwenye kituo cha kupima na kutoa ushauri juu ya ugonjwa wa ukimwi. Baada ya kufika nilikutana na mshauri ambaye sikuwa mgeni kwake. Aliponiona alinikaribisha pamoja na kunikumbuka lakini jina langu hakulikumbuka.
"Karibu mdogo wangu."
"Asante dada yangu."
"Kama sikosei ni jana tu ulikuwa hapa?"
"Ni kweli dada yangu."
"Mm’hu ulikuwa na tatizo gani?"
"Nilikuwa na swali moja juu ya maambukizi ya ukimwi."
"Uliza tu."
"Hivi kuna uwezekano mtu mwenye ukimwi kutembea na mtu asiye na ukimwi na asipate?" .
"Ndiyo."CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
"Kwa nini?"
"Inategemeana na damu ambayo uliyonayo ambayo hairuhusu virusi kuingia mwilini."
"Mmh! Ina maana mtu kama huyo kama ni mwanamke anaweza kuwa na mwanaume mwenye virusi na kuweza kuzaa nae?"
"Si vizuri kiafya hasa unapomgundua mwenzio ameathirika ni muhimu kutumia kinga muda wote."
"Kwa nini wakati siwezi kuupata huo ukimwi?"
"Sikiliza mdogo wangu mwenzio anapokuwa ameathirika na wewe kuwa salama unatakiwa kuishi naye kwa taadhari kubwa hasa katika jambo la kukutana kimwili. Huwezi kujua nguvu ya chembe zako hai zinaweza kukosa nguvu kama kila siku utazipiganisha na maradhi.
“Hivyo inaweza kuwa rahisi hata magonjwa mengine kukuingia na kukusababishia mwili wako kukosa kinga na kukufanya ufe kwa urahisi."
"Na mwenye ukimwi wa muda mrefu huweza kupoteza nguvu kwa muda gani?"
"Inategemea usikivu wake kwa kufuatilia ushauri wa wataalamu, kama atakuwa mfuatiliaji wa masharti ataishi kwa muda mrefu huku afya yake ikiwa nzuri. Lakini akienda kinyume na hapo lazima mwili wake utapoteza nguvu na kufa haraka au kuandamwa na maradhi ambayo yatamtesa mpaka kifo chake."
"Mbona kuna mtu ambaye anaonekana ni muathirika wa muda mrefu lakini bado anaendelea kuishi na hali yake nzuri japo afuatilii matibabu?"
"Si kweli kama hafuatilii masharti lazima kuna mabadiliko mwilini mwake na atakapopatwa na ugonjwa wowote ni rahisi kufa. Pia wapo wanaofanya mtindo wa kubadili damu kwa wenye pesa lakini huwa hawajui kila wanapokwenda kinyume na mashriti huuchosha mwili na siku moja hufa kama mdhaha na afya zao.
“Wengi huwa hawajui mwili unapopoteza kinga hutakiwa kufuata masharti ili kuuweka salama muda wote. Usifikili kubadili damu au kula madawa makali na kwenda kinyume na masharti yake mwili huchoka na kufika kipindi hushindwa kufanya kazi na mtu kufa ghafla." "Kwa hiyo unataka kuniambia hata mtu mwenye afya asiyefuata masharti hukumu yake ni hiyo?"
"Ni kweli kabisa."
"Sasa dada yangu nilikuwa na tatizo moja lililonirudisha kwako leo, ni hivi nina rafiki wa kiume mtu mzima ambaye ana mke. Lakini kila kona wanasema kuwa ni muathirika, lakini jana tulipopima alionekana yupo salama."
"Sasa tatizo nini?"
"Bado kuna watu wamenihakikishia kuwa ni muathirika kwa ushahidi wa vyeti, sasa utanisaidia vipi?"
"Mimi nakushauri usisikilize maneno ya watu kwa vile mmepima mmeonekana wote mpo salama, subiri miezi mitatu mkapime tena ili kujua ukweli wa mambo."
"Kuna mtu amesema kuwa Anko ananunua vyeti hapo kuna ukweli gani?"
"Mmh! Hapo pagumu kidogo..sasa ni hivi kwa vile vipimo vya hapa naviamini mwite aje hapa ili tuchukue vipimo vyetu kwa mara nyingine ukweli utajulikana tu."
"Sidhani kama atakuja vituo hivi vidogo haviamini."
'Tatizo si udogo wa kituo, cha muhimu ni mitambo ya kisasa yenye kuona vizuri bila ubabaishaji."
"Mmh ngoja nimjaribu."
"Sikiliza mdogo wangu nipe hiyo simu nitampigia mimi kumwita kuwa wewe nimekuokota hapo nje akiwa ameanguka akifika tutalazimisha akibisha mweleze ukweli. Kama kweli yupo salama atakubali."
Nilimpa simu yule dada ambaye alimpigia simu ambayo Anko aliipokea na kuahidi angefika muda si mrefu. Haikuchukua muda Anko alifika na kunikuta nimekaa mbele ya meza ya mshauri, alipofika mshauri alimkaribisha.
"Karibu mzee wangu."
"Asante" alikaa kitini huku akinishangaa.
"Vipi dear kuna tatizo gani?"
"Mmh! Afadhari umekuja, dada huyu ndiye bwana yangu naomba utupime wote," nilisema huku nikimkazia macho.
"Tupime nini tena?" aliuliza kwa mshtuko.
"Afya zetu."
"Herena sasa utakuwa mchezo si jana tu tumepima sasa vipimo vya leo vya nini, labda miezi mitatu ingekuwa imefika."
"Sikiliza Sweet siku zote ili kupata ukweli wa kitu lazima upime sehemu zaidi ya tatu ili tuwe na uhakika wa afya zetu."
"Siku zote vituo vidogo kama hivi vipimo vyake si vya kweli unaweza kukajikuta upo salama kumbe umeathirika au ujikute umeathirika kumbe upo salama."
"Kwani tatizo nini kama bado huamini vipimo vya jana ruksa twende tukarudie sasa hivi."
"Sawa lakini tuanzie hapa."
"Hapa siwezi kupima kituo hiki ni chini ya hadhi yangu."
"Wanakuja hapa hata mawaziri wenye nyadhifa serikalini itakuwa wewe, nasema hivi hapa tunapima tena," nilisisitiza baada ya kuona kama anataka kukwepa.
"Siwezi kama ndicho ulichoniitia sina muda wa kuwepo hapa tutaonana baadaye."
"Mr Joel kwa taarifa yako nakujua vizuri kuwa vyeti vyote unanunua, umemuua mama yangu na mimi unataka kuniua siyo," mtoto wa kike yalinitoka.
"Ni maneno gani hayo Herena mimi nimemuuaje mama yako?"
"Unajua vizuri sasa kama hutaki kupima siwezi kukulazimisha, ninacho kuomba kuanzia leo mimi na wewe inatosha bado nayahitaji maisha."
"Lakini kwa nini umefikia huko ni jambo la kuelewana."
"Na kuelewana ni kukubali kupima tena mimi mbona najitolea iweje wewe ukatae."
"Siviamini vipimo vya hapa."
"Aaaha kumbe unavikubali vile vya kule ambavyo umewahonga madaktari ili upate kutuua vizuri."
"Hivi Herena na maneno yako machafu nikipima na kukutwa salama utaniambia nini?" Anko alizungumza huku akitetemeka.
"Nikuambie nini zaidi ya kuongeza upendo kwako."CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
"Basi nipo tayari kupima," Anko alisema kwa jazba.
"Hilo ndilo lililobakia mengine hayakuwa na muhimu," nilimwambia huku mshauri akiangalia marumbano yetu.
Anko alikaa huku jasho likimtoka, mshauri alimtuliza kwa kumuuliza
"Mr nani vile?"
"Joel," Anko alijibu kwa mkato.
"Samahani Mr Joel japo kupima ni hiyari ya mtu lakini suala la kujua hali za wanamahsiano si vizuri mmoja kupima na mwenzake kutopima bado mtakuwa hamjatatua tatizo. La muhimu ni wote kujua afya zenu ili mjue muishi vipi katika kutimiza malengo yenu.
“ Kutokana na maelezo ya mwenzio kusikiliza habari za pembeni kuwa wewe ni muathirika japo mwanzo aliziba macho lakini imefikia kikomo sasa kwa hiyo una unafasi nyingine ya kudhigilisha ukweli."
"Lakini daktari si jana tu tumepima wote na kukutwa tupo salama sasa nashangaa tatizo nini?"
"Sikiliza mzee Joel kuna taarifa ambazo nina imani leo zitapata ukweli kuwa wewe una urafiki na madaktari wa hospital unayotibiwa hivyo kukufichia siri zako kwa kutoa majibu ya uongo."
"Nani kasema habari hizi za uuaji?" Anko macho yalimtoka pima.
"Si wakati wa kutafuta mchawi vipimo ndivyo vitakavyo waonyesha wachawi wenu."
"Haya tupime."
Mshauri baada ya kuandika majina yetu tulikwenda chumba cha kupimia vipimo kisha tulirudi kwenye kiti tusubiri majibu ambayo yalichukua robo saa. Baada ya majibu kufika mbele ya meza nilishangaa kumuona Anko akijipekua kama amepoteza kitu. Alitoa pochi yake na kutoa noti ya elfu kumi na kunipa
"Herena niletee vocha ya simu mara moja."
"Mwache tu nitamtuma mtu afuate," mshauri aliingilia kati mzungumzo.
"Hapana, kwenye pesa huwa simuamini mtu, wacha tu my daring afuate."
Sikutaka mabishano nilinyanyuka na kutoka nje ya kituo kwani maduka hayakuwa mbali. Nilinunua haraka na kurudi ndani, nilishangaa mjomba alinyamaza ghafla baada ya kuniona na kuniuliza.
"Vipi umepata?"
"Ndiyo."
"Vizuri, samahani mpenzi nilisahau kukuagiza ya elfu 20 naomba umenilee nyingine."
"Dear hebu kwanza tusikilize majibu mara moja nyingine tutanunua tukitoka."
"Mwache tu kwanza si unajua kuna wateja wengine tumewagandisha kwa kipindi kirefu kwa ajili ya kuwapa upendeleo kutokana na uzito wa tatizo lenu."
"Okay daktari lakini iwe hivyohivyo."
Nilijiuliza iwe hivyo hivyo nini, sikutaka kuhoji nilikaa kitini kusikiliza majibu yetu.
Baada ya utulivu wa dakika moja mshauri alituita majina yetu.
"Herena."
"Abee."
"Mzee Joel."
"Naam."
"Majibu yenu majibu yake kama ifuatavyo ila kwa yoyote ambaye hatakubaliana na majibu haya bado ana nafasi ya kwenda mbele zaidi kupata ukweli. Lakini kipimo chetu ni cha uhakika na kutoa majibu ya kweli yasiyo na utata hata kidogo," mshauri alitulia kumeza mate na kupitisha jicho lake kwa kila mmoja kisha alisema:
"Ila kabla sijatoa majibu nini malengo yenu?"
"Ni kuwa mke wa pili wa mzee Joel," nilijibu.
"Kwa mfano mzee joel ameathirika na wewe mzima utayapokeaje majibu yako?"
“Nitayapokea kama yalivyo lakini sitaendelea na mwenzangu kwa vile hakuwa mkweli kwangu," nilijibu.
"Hapana Herena hapo utakuwa hujamtendelea haki mwenzako, ina maana wewe ukikutwa unao na yeye hana utachukua uamuzi gani?"
"Nitamsikiliza mwenyewe ana semaje, uamuzi wowote atakaoutoa itakuwa sawa kwa upande wangu."
"Eti mzee Joel vipi ukikutwa wewe upo sawa na mwenzako ameathirika utachukua hatua gani?"
"Kwa upande wangu kwa vile nina mapenzi ya dhati kwa mwenzangu sitamtenga nitakuwa naye bega kwa bega hadi mwisho wa maisha yake kwa muda wote kuwa karibu yake ili kumtoa mawazo potofu kuwa mwenye virusi hana rafiki au rafiki wa mwenye virusi ni mwenye virusi."
"Asante sana mzee Joel kuonyesha ukomavu kwenye janga hili ambalo wengi huwatelekeza wenzi wao. Je, kama wote umejikuta mpo salama mtafanyaje? Nitaanza ni Herena."
"Mmh mimi nitamshukuru Mungu kwa kunilinda pili nitazidisha mapenzi yangu kwa mwenzangu na tatu nitaendelea kuwa muaminifu kwake."
"Vizuri Herena, na mzee wangu?"
"Mimi nitamshukuru Mungu na kuendelea kuwa muaminifu na mwenye mapenzi ya vitendo yenye kutoka chini ya uvungu wa moyo wangu na kumtimizia vyote nilivyo muahidi."
"Nashukuru kuwasikieni ni watu mnaoonyesha mapenzi ya kweli kwa kila mtu kwa mwenzake. Mwisho vipi kama wote mjikute mmeathirika mtachukua uamuzi gani?" swali lile kidogo lilinitisha kwa kuonyesha ukweli fulani, lakini nilijikaza ili kupata ukweli.
"Mm’hu Herena naona kama upo mbali kidogo?" aliniuliza baada ya kuhama kimawazo.
"Aaah, nipo sawa," nilijibu huku nikijiweka sawa kitini.
"Ehe, utachukua uamuzi gani?"
"Kwa vile mimi nipo chini ya mtu nitamsikiliza mwenzangu ana semaje."
"Sawa, lakini nataka maoni yako mwenyewe."
"Nitaendelea kuwa karibu na mwanzangu na kuwa mshauri mwema katika kuafuata yote tulishauriwa na daktari na kufuata kila nilichoelezwa kulinda afya zetu."
"Mmh vizuri sana Herena na mzee wangu?"
"Mimi kama mimi naamini ukimwi si kifo bali ni ugonjwa unaotakiwa kufuata masharti yake ambayo humfanya mtu aishi maisha marefu bila tatizo, hivyo basi nami nitakuwa bega kwa bega na mwenzangu kuhakikisha hatuendi nje ya masharti ya kuishi kwa usalama."CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
"Nashukuru kwa uelewa wenu mkubwa ambao utanisaidia kuyasema majibu yangu bila hofu," alitulia kwa kuzichukua kalatasi za majibu juu ya meza na kuzipitia kwa mara ya mwisho kisha alituuliza swali:
"Mmesema mahusiano yenu yana muda gani?"
"Mmh ni mwaka wa tatu sasa," nilijibu kwa niaba ya wote.
"Na katika mahusiano yenu huwa mnatumia kinga au bila kinga?"
"Hutumia siku moja moja hasa kipindi cha hatari ya mimba zaidi ya hapo huwa hatutumii."
"Mmh....sawa," alivuta pumzi kwa ndani na kuzitoa kisha alisema kwa sauti ya chini iliyosikika.
" Majibu yenu yanaonyesha kama ifuatavyo nitaanza na Herena, majibu yako yanaonyesha damu yako ni salama."
Nilipiga magoti kwa mara nyingine na kunyanyua mikono juu kwa kusema:
"Asante Mungu."
Baada ya kushukuru nilirudi kitini kusikiliza majibu ya Anko yalikuwa yakisemaje, lakini niliamini yote yaliyokuja juu ya Anko ni uongo ili kututenganishe. Nilitulia tuli kusikiliza majibu ya Anko:
"Majibu ya pili ya Mr Joel yanaonyesha damu yake ni cha..."
Hakumalizia Anko alimkata kauli.
"Muongo mkubwa ndio maana nilikataa kupima vipimo vya uchochoroni."
Nilimshika Anko na kumkalisha kitini huku nikimuomba awe mtulivu.
"Mpenzi tatizo nini hebu tumsikilize kwanza nawe utazungumza nakuomba uwe mpole."
"Hapana Herena huyu binti anataka kunivunjia heshima yangu tu," Anko alisema huku jasho zikumtoka kwa wingi kwenye paji la uso.
Baada ya kutulia huku akitweta nilimruhusu mshauri aendelee
"Kwanza kabla ya kumalizia kutoa majibu kuna kitu nataka nikiweke wazi. Mr Joel kwa tabia yako utaendelea kuueneza ukimwi kwa kutumia pesa zako kuwahonga washauri na madaktari wasiojua thamini ya maisha ya watu.
“Hivi hiyo laki tano yako inalingana na uhai wa Herena? Kama kweli ulikuwa ukimpenda Helena kwa nini usimwambie ukweli kuwa wewe ni muathirika ili mjue mjikinge vipi kuliko kuueneza bila woga.
“ Ni kweli nina shida na hela lakini si kwa mtindo huu, nimejitolea kufanya kazi hii kwa ajili ya kuokoa maisha wa watu na si kuangamiza maisha ya watu. Kwa nini unaonekana ni mwelewa lakini si kwa vitendo zaidi ya kuzungumza mdomoni lakini moyoni una dhamira mbaya.
“Mr Joel kuwa na virusi vya ukimwi si aibu siku hizi watu wameelimika. Kujitangaza ni kujikinga na kujiingiza kwenye vishawishi vya kufanya ngono na watu wasio kujua. Hivi ni wangapi katika dunia hii wenye mawazo wa kiuuaji kwa kuusambaza ukimwi kwa watu wasio na hatia.
“Si kwa wanaume hata wanawake wengi wamekuwa na tabia hiyo wanapojijua wameathirika na wana pesa hutumia pesa zao kufanya mapenzi na vijana wadogo kwa kuwapa pesa nyingi na kufanya nao mapenzi bila kinga.
Huo si ujanja bali kuliangamiza taifa ambalo nguvu kazi yake ni vijana.
“ Hivyo nakuombeni kama tulivyo zungumza awali, bado mna nafasi ya kuendelea kuwa pamoja kwa kutumia kinga na kupunguza kukutana kila wakati ili kuupa mwili nafasi ya kujenga uwezo wa kujilinda.
“Namalizia kwa kutoa ushauri kwa wote waliojitolea kuokoa maisha ya watu juu ya janga lolote si ukimwi tu. Wajitoe kwa ajili ya kuokoa si kuangamiza, pesa utakayopewa ili upindeshe ukweli hujui ni bomu ambalo hata wewe linaweza kukulipukia.
“Hivyo basi tuwe wakweli na wawazi kwa yoyote atakayetaka kuangamiza wenzake kwa ajili ya pesa zake ili wafe wengi. Ni nani aliyekuambia ukimwi ni kifo, ukimwi ni ugonjwa kama ugonjwa wowote unaweza kufa na ugonjwa mwingine tofauti na ukimwi na mwenye ukimwi akaendelea kuwepo.
“Ndugu zangu kama majibu yanavyo onyesha mmoja yupo safi na mmoja ameathirika. Ni wazi Mr Joel uliisha pata ushauri juu ya ukimwi mara ya kwanza ulipokutwa nao. Nakuomba ufuate ushauri wa washauri ili uishi muda mrefu.
“Mwisho nakuombeni muondoke salama na kuendelea kuwa karibu na mwenzako katika kupeana moyo na kufarijiana."
"Siwezi kuendelea kuwa na muuaji mzoefu kumbe umenituma vocha ili uniue....Asante dada yangu Tanzania tukiwa na moyo kama wako ile kauli mbiu ya Rais Tanzania bila ukimwi unawezekana.
“Lakini kwa walio tanguliza masrahi yao binafsi ambayo hayainufaishi nchi kauli hiyo itakuwa sawa na kumpigia mbuzi gitaa," nilijikuta nikizungumza kwa uchungu baada ya kugundua Anko kila siku alikuwa akinizunguka na kuitafuta roho yangu kama Zilairi mtoa roho.
"Nooo sivyo hivyo dada huyu bwana hafai lazima nimfungulie kesi kwa kosa la mauaji."
"Hapana usifanye hivyo watu hawa ni kuwaelimisha tu."CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
"Hivi ni wangapi amewaambukiza akiwemo mama yangu mzazi hakulidhika aliitaka na roho yangu."
"Herena ni shetani lakini bado nakupenda na nina mipango mingi juu yako," Anko alinipigia magoti mbele yangu kuniomba msamaha.
"Mipango mingi ya kuniondoa duniani kwa kuwahonga wote wanajihusisha na upimaji wa maambukizi ya ukimwi."
"Samahani mzee Joel pesa yako hii hapa," yule mshauri alitoa laki tano na kumpa Anko lakini niliziwahi na kuzichukua kisha nilimrudishia yule mshauri.
"Asante yako kwa kuokoa maisha yangu."
"Hapana, nashukuru," mshauri alizikataa.
"Si kweli ulichokifanya ni ujasiri wa ajabu hii hela nakupa mimi naomba upokee."
Alipokea zile hela kisha nilimuaga na kuondoka huku Anko akinifuata kwa nyuma. Nilipofika kwenye gari langu niliingia ndani na kung'oa nanga japo aliniita na kulikimbilia gari langu.
Nilikwenda hadi nyumbani ambako nilimkuta mama na kumweleza hali halisi juu ya hali ya Anko na ujanja aliousema Mai juu ya kuhonga watoa majibu.
"Nina imani ukweli umeupata sasa unasemaje?"
"Siwezi kumtenga ila nitakuwa naye karibu kama sehemu ya familia si mpenzi na nina mpango wa kutafuta mchumba wa kweli ili anioe."
"Nina amani sasa utaamini kinywa cha mkubwa kinanuka lakini maneno yake hayanuki."
"Ni kweli mzazi wangu hili limekuwa kusudio la Mungu ili liwe fundisho kwa wengine."
"Nina imani ukijiunga na kikundi cha kutoa ushauri utakuwa mwalimu mwema."
"Mmh nitaweza?"
"Kwani hao wameweza vipi ushinde wewe unayejua ABC ya maambukizi ya ukimwi."
"Nitajaribu."
Tukiwa katikati ya mazungumzo tulishangaa kumuona Anko amesimama mbele yetu kama mwanga aliyekamatwa mchana. Nilijikuta nikipandwa na hasira na kunyanyuka kitini na kumfukuza.
"Nakuomba utoke muuaji mkubwa."
"Hapana Herena hebu msikilize anataka kusema nini," mama aliingilia kati.
"Hapana mama siwezi kumsikiliza kwa lolote muuaji."
"Herena nasema rudi nyuma na ukae chini, hata kama ungeambukizwa nisinge mlaumu, ni wewe uliyeanza kununua vyeti kuficha ukweli leo ndio umejua athari zake," kauli ya mama ilinifanya niwe mpole ghafla na kumuacha Anko aseme kilicho mleta:
"Ndiyo baba unasemaje?" mama alimuuliza kwa sauti ya chini.
"Leo nimekuja kuomba msamaha kwako na kwa Herena kwa kitendo nilichokitenda ambacho si cha kibinadamu. Naweza kusema umejua nimeathirika baada ya mke wangu kupima wakati wa ujauzito.
“Na wakati huo nimeisha achana na wewe, lakini kwa Herena nilimpenda niliogopa kumwambia ukweli kutokana na kumpenda sana. Ninachokuombeni mnisamehe nami nitalipa fidia pia kuanzisha kitengo cha ushauri nasaha juu ya ukimwi ikiwa pamoja kukupeleka kusoma zaidi."
Hatukuwa na muda wa kumtafuta mchawi kwa kila mmoja wetu alikuwa na makosa. Hivyo tulikubaliana kwa pamoja kushirikiana kuanzisha NGOS kwa ajili ya kutoa matangazo juu ya kujikinga na maambukizi ya ukimwi.
****
Baada ya muda nilikwenda kusomea mambo ya ushauri nikiwa kama mkurugenzi wa shirika la NI KWELI, likiwa na maana Ni kweli ukimwi upo tuache ubishi.
Baada ya kumaliza tuliaji watu wengi, tulianza na mashule hasa kwa kutoa elimu kwa walimu kwa tabia zao chafu za kutembea na wanafunzi. Kisha tulimalizia kwa wanafunzi kwa kuelewa nini kilicho wapeleka pale shuleni ni elimu na si mapenzi.
Pia shirika letu liliandaa kongamano kubwa la vituo vyote vya ushauri nasaha na kupima virusi kwa kuwa wakweli ili kuokoa nafsi za watu. Nilitumia matukio yangu kama somo kwa wote ili tuwe wakweli na wawazi kwa kuweka masrahi ya taifa mbele kuliko kuwema maslahi binafsi.
Shirika letu kwa muda mfupi liliweka kupata misaada mingi kutoka kwa wahisani na kuweza kupanuka na kuzunguka Tanzania nzima kwa kutoa elimu ya ukimwi kwa mafanikio makubwa. Mfano wangu ndio nilioutumia kwa kutoa elimu ya kweli.
Tuligawa vipeperushi na vitabu bure mashuleni juu ya umuhimu wa elimu na kujilinda na ukimwi. Anko na mkewe walikuwa walezi ambao waliongeza nguvu kwenye kampuni yetu.
Namalizia kwa kusema Ukimwi upo na unaua, kila mmoja asimpime mwenzie kwa macho bali mkapime wote ili kujua afya zenu. Vile vile usichukulia kipimo cha mwenzako kujua afya yako bali kupewa mwenyewe.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Pia kwa wote ulijitolea kuokoa maisha ya Watanzania ili tuendane ya kauli mbinu ya mkuu wa nchi Tanzania bila ukimwi inawezekana. Kama kutanguliza maslahi ya taifa mbele na si masilahi binafsi itawezeakana.
Mwisho ni maofisini na mashuleni tusipo kuwa makini ukimwi utatumaliza hasa wanaopenda rushwa ngono ambao ndio hatari mkubwa katika kueneza virusi vya ukimwi. Namazia kwa kufuata yote tuliyozungumza tokea mwanzo wa mkasa huu Tanzania bila Ukimwi inawezekana.
MWISHO
0 comments:
Post a Comment