Simulizi : Changudoa
Sehemu Ya Tatu (3)
Bi Faudhia alizama akaibuka tena.
"Nakufaa!!" Akazama akanywa vikombe akaibuka tena. "Niokoeni"
Akazama kimya akaibuka tena kimya, kisha akazama moja kwa moja. Hakuibuka tena na wala hazikusikika kelele zake.
Dakika kumi na tano baadaye, walibaki wale manahodha wa chombo waliojitahidi walau kushika mabaki ya mbao za ngalawa yao na kuelea juu kwa juu. Walijitahidi kushikilia mbao zile na kusogea nazo taratibu.
Usiku ulikuwa mkubwa, hawakuweza kuona chochote lakini kwa msaada wa mwanga wa mbalamwezi, waliweza kuonana wao kwa wao. Walipotazama kwa mbali, waliweza kuona taa za majumba na bandari ya zanzibar. Hayakuwa karibu kiasi cha walivyoona wao. Ilibidi upite Makoba, Fujoni, mdogo kisha bububu ndio uingie Zanzibar.
Wakaendelea kusubiri zaidi muujiza.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Siku mbili baadaye miili miwili ilikutwa ufukoni mwa bahari karibu na ufuko wa mji wa Mkokotoni jirani na Ngalawa iliyozama huko Kiongwa. Ikapelekwa katika hospitali ya serikali katika kisiwa hicho kisha picha za maiti hizo zikitangazwa katika vituo vyote vya runinga. Mmoja kati ya watu waliokuwa wakitazama taarifa ya habari, alikuwa Salim. Ni wakati huo akiwa Mazizini kwa mama yake mdogo sebuleni akipata chakula cha usiku.
Sehemu ya taarifa hiyo ya habari ilisomeka hivi. "Miili miwili ya watu ambao hawajatambulika mpaka sasa imekutwa ufukweni mwa bahari ya hindi mmoja ukiwa ni wa kike mwingine wa mwanaume ikionekana chombo walichopanda kuzama. Mwili huo wa mwanaume umeharibika vibaya sana na sura yake kutojulikana kabisa huku wa mwanamke huyo ukiwa umeharibika sehemu ndogo ya mgongoni"
Kisha ikafuatiwa na picha ya Bi Faudhia. Salim akapaaliwa mara alipotazamana na uso wa mama yake. Kijiko kikamdondoka na kupiga ukunga wa nguvu.
"Antiii!!!"
Mama yake mdogo aliyekuwa anamalizia kuvaa chumbani kwake, alitoka mbio na kuja sebuleni alipo Salim.
"Kuna nini?"
Salim hakuzungumza chochote huku machozi yakimbubujika, alimuonesha mama yake mdogo runinga. Mama yake mdogo alipotazama akakuta taarifa ile ikiisha lakini sura ya dada yake aliiona.
"Faudhia dada yangu jamani"
Alikuwa mwepesi kweli wa kulia. Machozi yakamtoka, Salim akazungumza.
"Si Mama peke yake" akikaa chini huku chakula akikisogeza pembeni "Alikuwa na mwanaume ambaye uso wake umeharibiwa vibaya na samaki, unadhani atakuwa ni nani?"
"Unataka kusema ni.."
Hakumalizia kwa kukamatwa na kitu kama donge zito la uchungu kooni mwake na kumpa Salim nafasi ya kuzungumza
"Ni Rashid"
Salim akanyanyuka na kwenda chumbani kuvaa shati lake.
...
Rashid alipofika katika kitengo cha ukaguzi, akiwa na watu wake wasiopungua tisa; hila zao zikakamatika.
"Piteni huku"
Askari walizungumza kwa lugha ngeni akiwaelekeza katika chumba cha mahojiano zaidi. maiti zao mbili zilikaguliwa kwa mashine maalumu baada ya kutambulikana kulikuwa na ulakini katika pasi zao za kusafiria. Ndipo kile kitu kilichowaumiza askari wale kuwakagua muda wote, kikawa wazi.
Madawa ya kulevya.
Rashid hakuamini kile alichokiona. Madaktari wawili waliletwa ndani ya chumba kile huku wale waombolezaji wakiwa wamenyamaza kulia wakitetemeka kwa hofu. Milioni mbili mbili na safari ya kwenda south bila malipo zikiwatokea puani. Ama hakika walikamatika.
Madaktari wale wakafanyia upasuaji zile maiti na kutoa kete nyingi sana za madawa ya kulenya. Maiti za watoto wa kike zilitolewa utumbo na kile kitu hivyo kuweka nafasi nzuri ya kuhifadhi madawa yale.
"Mpo chini ya ulinzi kuanzia sasa"
Ilikuwa ni kauli ya mwisho aliyopata kuisikia Rashid mara baada ya hapo kila sehemu ya kiungo chake cha fahamu hakikufanya kazi. Kwa kweli alitumia pesa nyingi kuratibu mpango huo lakini ulionekana kwenda tofauti na hiyo ikawa sababu ya kuona anaurudia umasikini.
Hakutaka iwe hivyo.
...
Mzee Kumba hakusubiri kumpa Tony taarifa kuwa anampeleka Nadia katika nyumba ya kulelea watoto wasio na uwezo. Alijua Tony ni lazima angekataa. Alijua fika Tony anafahamu mipango michafu waliyokuwa wakiifanya katika nyumba ile. Kuwauza mabinti kwa mabwana wakizungu, kuwatumia watoto hao hao kuuza madawa ya kulevya na pia hata kuwapiga picha kwa ajili ya kujipatia msaada katika mashirika mbalimbali ya kimataifa.
Ikawa sababu ya kutomwambia kabisa hata Nadia alipomwomba Mzee Kumba amsubiri Tony amuage. Mzee Kumba akampeleka Nadia katika makazi hayo rasmi huku kila mmoja akishangaa sababu ya mwanamke huyo mrembo kuingizwa ndani ya nyumba hiyo. Hakuna aliyethubutu kumueleza Nadia ubaya wa mahali hapo kwa kuwa alionekana kupafurahia sana.
Akawa amejiingiza jehanamu bila kujua.
Wiki ya kwanza tu, ikamuonesha taswira ya mambo yaliyojificha mahali hapo. Kama ufuska ulifanywa mbele ya macho yake. Wasichana wadogo wenye umri chini yake, wasiopungua miaka kumi na miwili, walivaa vinguo ambavyo yeye mwenyewe alikiri kuwa asingeweza kuvivaa. Vibukta vifupi kama nguo zao za ndani pamoja na vinguo vya juu vilivyoacha vitovu vyao wazi, vikawa vichocheo vya mambo ya ngono. Usiku wa manane ndio walikuwa wakitoka wamejipara haswa na hawakuulizwa walipokuwa wanaenda.
Hiyo ikamshangaza sana Nadia.
Hiyo ikamfanya Nadia kuchunguza nini kilikuwa kinaendeea mahali hapo. Akamfuata mlinzi wa eneo hilo.
"Ka' Sele, mi n'na swali" alipokuwa na Sele Getini "Hivi mbona huwazuii hawa watoto kutoka usiku? Wakipata matatizo je?"
Sele alicheka sana. Akapaaliwa lakini hakucha kucheka. "Hivi nikuulize Nadia" akaendelea kucheka huku akijitahidi kujizuia asicheke "Wewe unaona wale wana utoto gani? Wale na viguo vile usiku huu, bado unawaona watoto?"
"Sa' ka' Sele, unataka kusema wale watu wazima? Wana utu uzima gani wale?" Akiuliza kwa wahka na mshangao alipomuona Sele akiwaita wale mabinti ni watoto. "Sikia Nadia" akiwa ameacha kucheka na sasa akiongea kwa umakini "Najua una haki na sababu ya kushangaa lakini ukiingia hapa hakuna mtoto na kila kinachofanyika humu ni siri labda hukuelezwa hapo mwanzo. Acha nikueleze ili usije ukafanywa kitu kibaya na mkuu"
"Mkuu!?"
"Ndiyo" macho yakiwa yamemtoka Sele na yaliyong'ara "ka' Rashid"
Haikuwa rahisi kwa Nadia kutambua Rashid huyo ni yule kaka yake aliyembaka. Nadia akauliza "Ina maana mwenye hii sehemu sio Mzee Kumba?"
"Mzee Kumba!?" Sele akacheka kwa dharau kisha akamwambia "Yule ni kama kibaraka au niseme msaidizi wa huyo Rashid. Rashid ndiye bosi wa hii sehemu"
"Mnhh!!" Nadia akabaki akiwa ameduwaa na kushangazwa na mambo aliyoelezwa. "Sasa yuko wapi huyo bosi?"
"Yupo bondeni" Sele akazungumza kwa lugha ya mtaani akimaanisha afrika ya kusini.
"South?" Nadia akauliza, Sele akaitikia kwa utingisha kichwa.
Nadia aliporudi bwenini kwake hakukaa kimya. Akawauliza wenzake aliobaki nao. "Hivi hiki ni kituo cha msaada ama danguro?"
"He! Nadia?" Mmoja alishangaa akauliza "kwanini umesema hivyo?"
"Kuruthum, ina maana unashangaa huelewi kinachoendelea?" Kuruthum akakaa kimya. "Ukimya una maanisha unaelewa ndio maana umeamua kukaa kimya" Bado kuruthum akakaa kimya. Kuruthum hakutaka kujihusisha na maongezi ambayo Nadia ameyaanzisha kwa kuwa yalielekea kule ambapo walikatazwa na Kaka Rashid kama walivyopenda kumuita.
Ni kweli yalikuwa mambo machafu na mabaya yaliyoumiza nafsi zao lakini hawakuwa na njia nyingine ya kuyaepuka kwa kuwa hawakuwa na sehemu ya kwenda. Wengi wao waliokotwa mitaani wakivuta chupa ya gundi na petroli. Wengi wao walitolewa katika mabar ya vichochoroni wakiuza miili yao kwa bei rahisi. Wengi wao walikuwa vibaka wa mifukoni hivyo kupata sehemu ya kulala ilikuwa ahueni kwao. Ilikuwa afadhali kwao kupata chakula, sehemu nzuri ya kulala na mahitaji yao mengine waliyoyahitaji. Wakayaficha mambo hayo japo yaliwaumiza lakini hwakuona sababu ya kuyaeleza kwa mtu mwingine. Kuruthum akawa mmoja wa kuyaficha kwa Nadia na kutoka nje alipomuona Nadia aking'ang'ania kuambiwa ukweli.
Mzee kumba alishangazwa na maswali ya ghafla kutoka kwa Nadia. Hakuelewa kwanini alipomuona tu, bila salamu akamvamia na maswali hayo. "Umeyatoa wapi hayo mambo?"
"Anha an'aaa, mi nauliza kuna nini kinaendelea humu ndani?"
"Nadia wewe bado mgeni sana unanishangaza sana unapouliza mambo ambayo hayaeleweki. Hakuna kitu kama hicho na kama umeshachoka ustaarabu unaweza kutoka" Si kwamba Mzee Kumba alimaanisha alichozungumza. Alitamani sana aendelee kumuona Nadia. Alitamani atimize lile lililopo moyoni mwake. Alimtisha kuona msimamo wa Nadia.
Alifanikiwa, Nadia pia akanywea.
Nadia alifikiria maisha ya zanzibar kwa nduguze wa mke mdogo wa baba yake. Hakutamani kurudi kule kibaha alipookoka mikononi mwa wabakaji. Hapana asingependa kwenda mtaani kwa kuogopa kufanywa kitoweo cha wabakaji wengine. Akaomba msamaha. "Kama sivyo, basi nisamehe Mzee Kumba" Mzee Kumba akatabasamu kifedhuli na kuondoka bila kuzungumza chochote.
...
Tony zilipita siku kadhaa bila kumuona Nadia akirudi nyumbani. Kwa kuwa hakuagwa, hakuweza kung'amua kama angekuwa katika ile nyumba ya ufuska. Hakuwa na sababu ya kwenda kumtafuta huko kwa kuwa alipaona mbali.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
"Baba ina maana Nadia harudi tena"
"Kwanini unamtafuta hivyo?" Alimuuliza bila kumtazama akiwa anashughulikia kiko chake cha kuvutia tumbaku.
"Maana sina uhakika kama huko alipo Nadia kutakuwa salama kama ameenda kwao Zanzibar. Inabidi nimfuate"
"Sawa" Mzee Kumba akamjibu kikawaida akipuliza moshi mzito hewani akijaribu kuvuta tafakuri mbali mbali za mambo yake aliyokuwa akiyafikiria. Katika mawazo yake aliwaza uzuri wa Nadia. Kuanzia kwenye nyonga mpaka kwenye miguu yake. Ni hapo alipotafakari kuhusu kifua chake mpaka juu ya uso wake. Uso uliosadifu umalaika. Akacheka. Tony akachukia alipoona Mzee Kumba, babaye alipokuwa akimuongelesha anacheka mwenyewe. Hakuwa akimjibu hiyo ikawa sababu ya kumuona baba yake anamdharau. Tony akasonya.
Siku chache baadaye kabla Tony hajaelekea Zanzibar, aliamua kwenda kwenye ile nyumba. Sababu ya kuamua kwenda huko ilikuwa ni mara alipokumbuka kuwa baba yake alimuahidi Nadia atampeleka katika nyumba yake ya kulea yatima. Si sababu hiyo tu. Aliwahi kumsikia baba yake akiongea katika simu na mtu asiyemfahamu huku akilitaja jina la Nadia.
"Nadia! Hapana Sele inabidi umtafute huyo msichana na uhakikishe unampata.. Anajua siri zetu nyingi sasa usipomkamata basi kaa ukijua Rashid akirudi hatakuwa na msamaha na wewe" Maongezi hayo yakampa mwanga kuwa Nadia yupo katika nyumba ile. "Lazima nifanye kitu" Kule akajibiwa Nadia katoroka kwenye nyumba.
Si mlinzi Sele aliyekubali Nadia alikuwepo hapo bali mmoja kati ya wasichana waliokuwa na Nadia. Alimueleza mambo mengi ya kushangaza ambayo Nadia alikuwa akiyafanya alipoingia katika nyumba hiyo. Mambo ambayo Tony alikuwa na hakika Nadia aliyafanya kwa kutopenda ila shida zilimghiribu. "Sawa ahsante dada yangu" Tony akaachana na yule msichana asipate mwanga wa kumsaildia wapi pa kumpata Nadia. Alijisikia uchungu sana kwa ukatili wa baba yake lakini hakuwa na jinsi. Baba yake alichangia kuyaharibu maisha ya Nadia. Akajilaumu yeye mwenyewe kumleta Nadia kwa baba yake.
Siku ile ambayo Mzee Kumba alikumbana na maswali ya Nadia na kuyapangua yote, alirudi tena usiku wake. Mfuko wa viazi vikavu na nyama ya kuku.
"Vyako hivi Nadia"
"Kwanini mmewatoa wenzangu vyumbani?"
"Usiwajali endelea kula"
Mzee Kumba alikuwa akicheka bila haya usoni mwake. Nadia alikuwa akitafuna paja la kuku, mara akashitushwa na mguso mapajani mwake.
"He! Mzee Kumba?"Akaishusha nyama ya kuku kwenye mfuko ule laini na kumtolea macho ya mshangao uliojaa hasira. "Yaani we mzee huna haya? Umekuja hapa kunihonga mimi na vijichipsi vyako vikavu unanishika shika mimi kama changudoa?"
Nadia akanaswa kibao cha uso. Kikamuingia. Alijishika shavu lake alilopigwa kibao kile. Alimuangalia tena kwa hasira na kuudhika na jambo lile.
"Kwa nini umenipiga? Kwanini umenipiga kibao nakuuliza?"
"Wewe huna ujanja wa kunikataa, mshenzi wewe" mzee kumba akageuka mlangoni na kuita "Abdullah" sauti ya kiume ikasikika "Muite na Sele tumalize yetu"
Aliingia kijana aliyezoeana sana na Nadia kisha nyuma akafuata Sele. Macho yalimtoka pima Nadia hakuamini kama hao aliowaamini wote wangeshiriki na mpango mchafu wa mzee Kumba.
"Sele hata wewe?"
"Hata mimi nini kimya wewe"
"Siamini Abdully"
Abdully akacheka kwa kebehi. Sele na Abdully wakamvamia Nadia wakambana ili kumpa urahisi Mzee Kumba kufanya analotaka. Kumba akamuingilia Nadia aliyebanwa mikono na Sele huku miguu ikibanwa na Abdully. Alijitahidi kujijitetea lakini haikuwezekana. Alijawa na uchungu mkubwa moyoni mwake.
Kitendo hicho cha kubakwa tena na mtu aliyemuamini angeweza kumsaidia, kikamuumiza na kumkera sana. Alibaki peke yake usiku kucha akilia. Siku ya pili hakuweza kumtazama Sele wala Abdully kutokana na hasira aliyokuwa nayo.
Wiki tatu baadaye akatumwa kufanya jambo lililomuingiza katika matatizo makubwa. Alitumwa kusafirisha mzigo fulani. Huko akakutana na vitu vya ajabu vilivyomfanya aghairi kurudi tena kwenye nyumba ya yatima
______
Nadia aliigiza kuelekea chooni. Mwendo ulikuwa wa haraka na wenye tahadhari kubwa. Alikuwa akigeuka nyuma mara kwa mara akijaribu kumfuatilia yeyote aliyekuwa akimfuatilia yeye. Hakuingia chooni kama wale waliokuwa wakimfuatilia walivyodhani. Alipitiliza moja kwa moja katikati ya upenyo wa kikundi fulani cha wasichana waliokuwa wakitokea chooni. Yeye akaelekea moja kwa moja nyuma ya jengo lile na kutoka nje ya viunga vile bila kuona kama kuna yeyote alikuwa akimfuatilia.
"Ametupotea" Mmoja kati ya vijana wa Mzee kumba alizungumza kwa wahka. "Haiwezekani"
Mwingine hofu ikamfanya akimbilie kule alipokuwa mwenzake. Walikuwa wakizungumza katika vifaa maalumu vilivyounganishwa moja kwa moja kwenye simu zao bila waya unaonekana.
Mmoja aliyegundua kwanza Nadia amewapotea yeye alikuwa chooni huku mwingine akiwa amesimama pale aliposimama mwanzo na mwenzake. "Vipi?"
Aliyefika akauliza kwa pupa, aliyekuwa akimuwinda Nadia alikuwa hana jibu zaidi ya kuyatoa macho pima sanjari na pumzi ndefu zilizokuwa zikipishana katika pua zake. Alikuwa akitembea tembea na kuzunguka kila kona bila mpangilio maalumu akimpa shida mwenzake aliyemfuata kugeuka geuka.
"Hoya vipi wewe!?" Akawa amechoka kuvumilia akauliza kwa jazba. "Demu mjanja" Akawa anatembea kuelekea ule upenyo aliupita Nadia, yule mwingine akamfuata. "Amekutorokaje?"
"Da! Sielewi yaani" Huku akiangaza huku na kule kama anayeweza kumuona akisusua njiani. "Tumwambie mzee" Yule wa pili akatoa wazo ambalo yule aliyempoteza Nadia akalipinga. "Turudi kwenye mzigo tusitishe safari"
"Kweli"
Wakarudi mbio mbio mpaka kule ilipo maiti yenye madawa ya kulevya. Wakawa wamechelewa.
Mizigo ya Nadia pamoja na maiti ndani ya jeneza lake nadhifu ikapakiwa ndani ya ndege ya kukodi. Wao wakiwa wanatoka eneo lile la mizigo kwa hali ya kuhamanika na kutaka kusimamisha safari ya ndege ile, gurudumu za ndege ile zikawa zinaacha ardhi ya uwanja wa ndege wa mwalimu nyerere na kupaa juu.
"Shenzi"
"Kwanini waondoke bila mtu wakati sio ya abiria"
yule wa pili akiwa anatumbulia macho akiona ndege ile ikiyoyoma angani
"Haiwezekani wafanye hivi kwanini waondoke bila abiria wao"
Yule mwingine aliyeonekana kama mratibu wa mpango huo wa kusafirisha maiti ile akawa amekikumbatia kichwa chake kwa hali ya kukosa matumaini na kuchutuma akiwa amesawajika usoni.
"Mpigie mzee"
Hatimaye akakubali. Jambo aliloelezwa Mzee Kumba likamchanganya sana. Hakuweza kukubali kirahisi mzigo wenye thamani kama ule kupotelea uwanja wa ndege. Hakukubali msichana aliyemdharau kama Nadia kuwatoroka walinzi wake makini aliowaamini.
"Msirudi bila Nadia kama na mtajua jinsi ya kuupata mzigo wangu" Alifoka kwa hasira.
Kazi ikaingia shubiri kwao, wao pia wakatamani wakimbie. Ama hakika yule aliyetorokwa na Nadia alikuwa na roho ngumu, pamoja na matumaini ya kushangaza.
"Tumtafute Nadia" Akiwa amekunja sura macho yamemtoka pima na pumzi zikiendelea kupishana huku makwapani amelowa jasho.
Nadia alipofika kituo cha kipawa, hakuchagua gari. Akalipanda la pugu kajiungeni na kwenda popote pa afadhali kuyakimbia makazi ya Mzee Kumba. Bila kujua kuwa aliwakimbia maadui zake wawili wakubwa huku mmoja akiwa hajui kama amemkimbia. Ndani ya gari akadaiwa nauli, hakuwa nayo. Konda alikuwa mtata sana haswa alipouona uzuri wa Nadia. Alijua ni lazima angepata kitu. Akaendelea kukomaa kumdai huku akimtisha kuosha gari mwisho wa safari yao. Nadia alikuwa akilia sana. Hata m'mama mmoja alipotaka kumlipia Nadia nauli, yule konda alikataa na kudai kuwa ni lazima Nadia ndio alipe. Akasingizia kuwa huo ndiyo mchezo wa huyo msichana.
"Kazoea sana kila siku anapanda hili gari ka' la babake" Watu wakashindwa kumsikiliza hata Nadia alipojaribu kujitetea "We konda wewe! Lini mi nimelipanda hili gari" akajifuta chozi kwa upande wa dira lake pana "Muogope Mungu kakaangu"
"Nyoo muogope kwanza wewe unayetaka kudhurumu wenzako" akasonya kisha akapiga bodi kumuashiria dereva ashushe abiria pale Mombasa "Leo nakuambia unaosha gari" Nadia hakuendelea kubishana. Hakuelewa ni vipi aliidondosha ile pochi yake pale nje kidogo ya geti la kutokea uwanja wa ndege. Hakujua kuwa ilimsaidia zaidi kuwapa ugumu wale watu wawili waliokuwa wakimfuatilia. Ndani ya pochi alipewa simu. Simu ambayo iliwekwa kifaa maalumu cha kumfuatilia popote atakapoenda. "Pumbavu" Yule kiongozi akatusi. "Nini?" Kibaraka akahoji"
Yule ambaye ni kama kiongozi, alipoinama kama anayeokota kitu aliinuka nacho na kumuonesha yule mwenzake. Yeye akachekaCHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
"Huyu demu mjanja"
"Amejuaje?"
Yule ambaye ni kibaraka akahoji huku naye akicheka. Wakafungua zipu ya pochi ile ndogo ya kubeba mkononi, wakashangazwa.
"Ameacha pesa zote?"
Yule kibaraka akatoa macho pima yaliyotangaza uchu wa kuziona zile pesa zilizokumbatiana kwa msaada wa mpira maalumu(Rubberband)
"Hapana"
yule ambaye ni kiongozi akaropoka, kibaraka akamtazama. "Huyu mwanamke alikuwa hafahamu chochote kwa kuwa asingeacha simu" akaitoa ile simu yenye chombo cha kuwaongoza popote alipo kwenye saa zao na kuendelea kueleza hisia zake "Angeiacha simu akachukua pesa" Zilikuwa pesa nyingi. Pesa za kigeni na za Tanzania. Yule kiongozi akazitia mfukoni. Wakasonga mbele zaidi.
Nadia alikuwa ameacha kulia na gari likapita mbuyuni, Gongo la mboto na shule ya Pugu sekondari kisha likaishia Kona.
"Njoo huku wewe"
Ni hapo Nadia alipokumbuka maneno ya kebehi aliyokuwa akiyarudia rudia yule kondakta ambaye alisema kuwa ni lazima aoshe gari kwa siku hiyo.
"Nisamehe kaka yangu"
"Njoo sasa" kondakta huyo hakuwa mkali kama hapo awali "kwanza umekula?" Masikio yakamzibuka na kuona ilikuwa heri yake.
"Hapana sijala"
"Njoo sasa"
Hayo yalikuwa ni majira ya alasiri, jua kali la saa tisa lilikomesha tumbo la Nadia ambaye hakula tangu jana mchana. Akapelekwa kwa mama ntilie, akaagiza wali na samaki chakula akipendacho.
"Sasa itakuwaje mwanangu?" Ambaye alionekana ni dereva wa gari ile alimuuliza yule konda aliyekuwa akinywa maji.
"Vipi suka?"
"Kuhusu huyu sungura tope unatafuna peke yako?"
"Acha uboya wewe, kama mtungo mi naanza"
"Poa tu"
Kisha yule ambaye ni kondakta akamgeukia Nadia na kumwambia. "Sikia dada mimi nataka tukalale pamoja"
Nadia alitoa macho na kupaaliwa na maji aliyokunywa. Akawa anakataa kwa kutingisha kichwa. "Hapana usiogope, nitakupa pesa nzuri" Pesa, pesa ikamlaghai Nadia akaitamani pesa. Akakubali kwenda na yule kondakta aliyemuachia deiwaka mlangoni kwake kuelekea tena kariakoo. Kondakta akatembea na Nadia kisha akamlipa shilingi elfu kumi kama ujira wake wa kutoa penzi.
"Na yule dereva wangu anahitaji naye atakupa yake"
Nadia akatabasamu kwa raha japo aliumia kwa kitendo alichokifanya. Angefanya nini kama hakuwa na hakika ya kula usiku? Hali ya uchangudoa ikaanza kumnyemelea na kuihalalisha hiyo ni kazi ambayo Mungu amempangia kuja kuishi nayo duniani.
Dereva akatembea naye aliporudi kule pugu kajiungeni na kumlipa pia shilingi elfu kumi jumla Nadia akawa na shilingi elfu ishirini mfukoni mwake.
_______
Simu yake Mzee Kumba iliita wakati ambao amejilaza kwenye kochi, sebuleni kwake mawazo tele yakimsumbua kichwa. Juu ya kioo cha simu yake, ilikuwa namba ngeni. Kilichomfanya agune si mlio wa simu uliomkatisha usingizi wake aliuona kama unambuguzi, bali ni aina ya namba iliyoingia kwenye simu yake wakati huo. Ilikuwa ni namba ya nje ya nchi.
"Rashid"
Sauti ilinong'ona moyoni mwake. Akaipokea kwa unyonge na hofu ikawa imemtawala.
"Habari yako Rashid"
"Unataka nife we mzee"
Kweli Rashid alikuwa na haki ya kushikwa na hasira na iliyojaa jazba. Siku zilipita na kila alipopiga simu haikupokelewa. Aliona Mzee Kumba anamdharau.
"Ah.. Hap.. Aan.. Aaa Rashid" Mzee Kumba alipatwa na uoga kutoka na sauti iliyotangaza hasira kutoka kwa Rashid.
"Sasa nini wewe mzee? Ni siku ya ngapi leo ninasubiri ujio wa huo mzigo? Ni kiasi gani cha fedha ulichochukua kwenye akaunti kuratibu huu mpango? We mzee usin'changanye"
"Rashid kuna tatizo"
"Tatizo?"
Rashid akang'aka kiasi cha kumfanya Mzee Kumba kutoa simu sikioni mwake kutokana na ukali wa sauti ya Rashid.
"Mzigo umekuja lakini umepotea kwa kuwa msindikizaji ametupotea uwanjani"
Rashid alitukana matusi mazito ambayo kama Mzee Kumba asingekuwa mshirika wake wa biashara haramu angemuachia laana nzito ya kuokota makopo.
Mzee Kumba akabaki akiomba radhi na kuahidi kuwa atamtafuta huyo msichana kwa udi na uvumba na kumfanya kitu kibaya sana. Haikusaidia. Rashid akang'aka kuuliza kuhusu msindikizaji kwanini awe mwanamke katika jambo zito kama hilo. Msichana huyo ni yupi?
"Anaitwa Nadia ni mgeni ndio maana amekuwa mzembe"
Mzee Kumba akajitetea. Rashid akamkatisha kwa wahka.
"Nadia?"
"Ndiyo alikuja wakati wewe upo safarini ni koko koko wa huko kwenu pwani huko" Majibu hayo yakazidi kumchanganya Rashid.
"Naomba mumtafute huyo msichana usiku na mchana mpaka mumpate mkimkosa andaeni makaburi yenu"
Kisha mawasiliano baina yao yakakatika. Rashid aliporudishwa ndani, alibaki mwenye mawazo sana. Aliwaza Nadia anayezungumziwa ni yupi? Hakumsahau Nadia dada yake ndio maana aliwaza sana juu ya Nadia aliyemsikia kutoka kwa Mzee Kumba.
"Lazima nitoke humu ndani, lazima"
Usiku wa siku hiyo, Rashid ndio alikuwa kwenye mawazo mazito. Fikra zake ziliwaza juu ya kisasi. Alihisi lazima Nadia amerudi kulipa kisasi. Hakuwa na shaka kuwa inawezekana Nadia anafahamu kuwa yeye ndiye muhusika wa mauaji ya wazazi wake, lakini ni lazima atalipiza kisasi cha kubakwa. Uoga ukapungua pale alipokumbuka Nadia na si mwingine yeyote alifahamu kama ni yeye alikuwa na kopi halali za hati ya mali za Mzee Mansoor, baba yao. Lakini bado kitendo cha kubakwa, Nadia angekuwa na kila sababu ya kulipiza kisasi.
Aliwaza.
"Lakini Nadia amepafahamu vipi pale? Ni vipi amejua mimi ni muhusika wa ile sehemu?" Akiwa amesimama mara akakaa akijaribu kufikiria zaidi "Mimi ni mtu mwenye jina kubwa mjini, labda alipotoka zanzibar alikuwa akiuliza kwa watu jina langu na kufanikiwa kupata sehemu ninayokaa"
Akaendelea kujiwazia na wazo hilo la mwisho akaliona ndio lina mashiko.
"Nitaondoka usiku huu huu"
Akanyanyuka na kwenda mpaka katika dirisha la mahabusu hiyo la juu sana. Akalitazama kwa makini huku akiwa ameshika kiuno, mwanga hafifu wa jua lililokuwa linaelekea kuangukia magharibi likionesha rangi ya udongo iliyokumbatia mawingu ulijipenyeza.
"Yes!" Akaropoka.
Akasubiri kwa dakika ishirini zaidi karibu na muda wa chakula. Si muda wa chakula peke yake, alisubiri pia giza lizidi kuathiri nchi. Muda wa chakula yeye hakwenda. Huko kwenye mstari wa chakula yule askari muuza madawa ya kulevya, akawa anamtafuta na asimuone. Hisia zikamtekenya na kumsisimua nywele zake.
Rashid alikwisha vunja nondo za dirisha lile. Nondo zilikuwa dhaifu zilizoliwa na kutu, hivyo ilikuwa rahisi kutokana na wahusika kusahau kuhusu ulinzi huo. Shuka la kitandani, likamsaidia kushuka ghorofa moja mpaka chini kwa kufunga mafundo kadhaa. Ikawa zamu ya kutafuta njia ya kuruka uzio. Uzio ulikuwa ni mrefu na wenye ulinzi mkali. Uzio ulikuwa ukimulikwa muda wote na taa kubwa yenye mwanga mkali. Askari wenye mitutu ya bunduki na mbwa mkali walililinda eneo la chini la uzio. Moyo ukamlipuka alipotafakari jinsi ya njama zake za kutoroka zinapozidi kufifia.
Wakati ambao Rashid amejificha gizani akijaribu kucheza karata yake ya mwisho, yule askari mnoko akashitukia mchezo. Alitoka kule bwaloni mpaka katika chumba cha mahabusu cha Rashid.
Patupu!!
Macho yakamtoka pima alipoona mlango wa chuma umefungwa. Akatazama dirisha akaliona limeachama.
"Shenzi" Akabwata.
Alirudi mpaka kule ofisini kwenye ulinzi wa gereza zima lililounganishwa na mahabusu ambao walikuwa wanasubiri kusomewa kesi zao. Kwa english mbovu alibwata.
"Kuna mahabusu ametoroka, na wewe unakunywa kahawa guu juu!"
Akamtoa yule askari mwenzie mguu wake uliyokuwa ukining'inia hewani juu ya meza na aliyepaliwa na kahawa ya moto.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
"Chumba namba ngapi?"
Aliweka kikombe cha kahawa pembeni akaiinamia kompyuta yake yenye video zote za kila kona ya gereza hilo kubwa.
"Namba 26"
"Mbona geti limefungwa?"
Yeye akatazama kwa kamera za ndani. Hakuwa na hofu sana kwa kuwa mageti yote ya mahabusu na gereza, aliyafungua yeye kwa kompyuta zake. Yule askari aliyemjua Rashid, akampiga konzi yule askari mlinzi.
"Angalia kwa kamera za nje, zinazopiga ukuta"
"Pumbavu"
Akamaka kwa ghadhabu aliposhuhudia dirisha likiachama mithiri ya kumzomea. Jasho la kwapa likamtoka. Kwa macho yaliyomtoka pima alimtazama yule askari mwenye ghadhabu na kumuuliza kwa unyenyekevu.
"Sasa tunafanyaje"
"Tangaza kwa askari wanaolinda kuta zote kuwa kuna mmoja ametoroka hivyo waimarishe ulinzi wao"
Kisha akatoka na kuelekea nje. Alifungua kasha la risasi kwenye bunduki yake na kutazama kama zilitosha. Zinatosha, Akaenda nje kumtafuta Rashid peke yake, moyoni akiamini Rashid ni mtu mwenye uwezo wa kufanya lolote pale pasipo na uangalifu thabiti. Hilo lilitokana na asili ya kiarabu aliyonayo Rashid. Alizani huenda ametoka katika nchi mojawapo hatari za kiarabu zinazoogopwa.
Rashid alimtazama yule askari wa upande wa kusini, akamuona amezubaa wala hana shughuli naye pale chini. Akageuka upande wa pili yule wa mbele yake alikuwa akitembea tembea na mtutu wake kifuani mwake. Mwanga mkali ukapita kwenye eneo alipojificha licha ya mwanga hafifu wa taa zilizopachikwa ukutani, akajidumbukiza kwenye shimo la maji machafu pembeni yake, wala asionekane.
Alipoingia huko akapishana na mikojo na vinyesi vya wafungwa wenzake, kiasi cha kumkera. Kule chini kulikuwa na mwanga kiasi uliomuwezesha kuona mbele. Mbele maji yalikuwa yakiporomokea korongoni. Macho yalimtoka pima kwa furaha kwa kuiona njia ya kutoka nje. Hakutaka kuchelewa wala kupoteza muda tena alianza kukimbia ndani ya maji yaliyomfunika ugoko wote mpaka kwenye magoti yake. Hakujali tena kunuka kwa yale maji wala uchafu wake akakimbia mpaka pale lilipo lile geti, mara king'ora kikali kikapiga mbinja.
"Mungu wangu" alijisemea kwa hofu
Kilikuwa ni king'ora cha kuashiria wito Kengele ya hatari. Askari walikusanyika wote walikwishataarifiwa juu ya kutoroka kwa mmoja wa mahabusu ambaye hukumu yake ilikuwa siku chache mbele, mara baada ya ushahidi kukamilika. Msako ulikuwa mkali. Mbwa walifunguliwa na kuzunguka kila kona wakisaidiwa na polisi waliowashika pamoja na bunduki zao kubwa. Kote kukawa kweupe kutokana na na mwanga wa taa za dharula kuwashwa na kuwa kama mchana.
Kizaazaa.
Wafungwa walikuwa wakijiuliza lakini baadhi ya mahabusu wakawa wameshaingiwa na udadisi wa mwenzao kutoroka. Hivyo kutokana na umbali wa selo za mahabusu na wafungwa na hata kutoshirikiana nao kwa ukaribu kwa mambo kadhaa, wafungwa hawakuweza kutambua nini kinaendelea. Rashid baada ya kusikia king'ora kile, alisimama. Mapigo ya moyo yalimuenda mbio na kutazama pale kwenye lile eneo la shimo lilipomsaidia kuingia na aliona vivuli vya mbwa wa polisi pamoja na vishindo vya miguu ya polisi ikikimbia.
Wasiwasi wa kukamatwa ukamuingia.
...
"Kuna shida na tunapaswa kukutana sasa hivi"
Mzee kumba alikuwa akiongea na wenzake kwenye simu. Wale washirika wa madawa ya kulevya waliokuwa wakishirikiana na Rashid siku zote, Mzee Kumba akiwa kama msaidizi wa Rashid
"Kuna nini?"
"Mzigo umepotea na mjumbe ametoweka?" Mzee Kumba alikuwa akizungumza kwa sauti iliyojaa hofu kiasi. Hiyo ilikuwa ni kwenye simu na kitambo kidogo wajumbe wale pamoja na Kumba walikutana mahala Fulani kulizungumzia jambo zito waliloelezwa.
"Unasemaje Kumba?" Mfanyabiashara mwenye mwili mnene na upara unaong'aa, alifoka. "This is not serious"
"Hatuna haja ya kulaumiana" Mzee Kumba akasema "Sasa ni wakati wa kuangalia jinsi ya kumsaidia Rashid"
"Pumbavu sana wewe mzee " Mwenye upara unaong'aa hakuzuia hasira zake, akaziachia wazi. "Tumeshaweka pesa nyingi kwenye mzigo wa kwanza, huna sababu ya kutueleza huu upuuzi zaidi ya kutueleza ni vipi tutapata pesa zetu"
"Ndiyo"
Yule mwingine alionekana kama muoga, hivyo alidakia kilichoanza kuulizwa.
"Sikilizeni" Mzee Kumba akaipata sauti yake. Wajumbe walipoanza kusimama, wakavirudia viti
vyao na mwenye upara akayatoa macho yake kwa hasira.
"Unataka kutueleza nini?" Yule muoga naye akaipata hasira kupitia sauti yake isiyotetemesha.
"Najaribu kutafuta njia kwanza ya kumkomboa ndugu yetu kisha tujue kama tutashindwa ndio tuanze kulaumiana. Kwa kuwa mimi sioni sababu ya nyinyi kunilaumu wakati nyinyi mlinituma na nimetekeleza sasa hakuna ubaya tukakaa kama tuliopoteza tujaribu kutafuta njia ya kutatua tatizo linalotukabili"
Alijaribu kutafuta maneno mazuri ya kuwalaghai wenzake kwa kuwa aliona lawama ni lazima zote zimuangukie yeye.
"No way" mwenye upara akapandisha hasira zaidi "Naona wewe na Rashid kuna mchezo mnataka kutuchezea sasa mimi sio mtoto mdogo wa kuniibia milioni hamsini zangu nawaambia mtazilipa" Akaondoka mara baada ya kuipiga meza waliyokalia na kudondosha glass za vinywaji walivyokuwa wakinywa.
"Bwana Reinhard, Reinhard"
Mzee Kumba alijaribu kumuita yule mwenye upara lakini hakugeuka. Yule aliyebaki alikuwa akiangaliana na Mzee Kumba kwa macho ya hasira. Mzee Kumba akazungumza alipoweka mikono yote juu ya meza.
"Sasa tunafanyaje ndugu yangu?"
"Mwanaharamu, mshenzi mkubwa wewe" Naye alinyanyuka na kupiga hatua kadhaa za kuondoka. Kisha akarudi "Kesho jioni kabla jua halijatua nahitaji pesa zangu"
hakuwa na mzaha tena wala hakuwa yule bwege aliyekuwa akimfuatisha yule mwenye upara Reinhard, alikuwa anatisha kimaneno na hata sura yake. "Ama zako ama zangu..." Heri hakumalizia neno lake, akaondoka.
Siku iliyofuata ndiyo siku ambayo Mzee Kumba alikutana na wale vijana wawili kabla ya jua kuzama kama alivyoambiwa na yule mjumbe wa mwisho kuvunja kikao kwa kitisho.
"Nadia yuko wapi?"
Mzee Kumba alikuwa akitetemeka mashavu, mikono na kila kiungo katia mwili wake.
"Mzee kazi imekuwa kubwa"
"Unamueleza nani?"
Mzee Kumba akamnasa kibao yule kibaraka aliyejitia kujitetea kisha akatoa tusi zito la kuwatukania mama zao hao vijana na kumgeukia yule kiongozi wa kundi lake.
"Yuko wapi Nadia?"
"Kama alivyokueleza Hashimu mzee, Nadia ni mjanja sana" naye akanaswa kibao kabla hata hajamaliza kuongea, lakini akaendelea huku akilia "Mzee ulitupa hiki kifaa kinachotujulisha alipo Nadia lakini yeye aliitupa hii pochi na pesa zote alichukua pasipo kuchukua simu"
Uongo!!
Lakini Mzee Kumba aling'amua na kuwacheka kwa kebehi. Alikuwa akiwaoneshea kidole chake cha shahada huku akicheka kwa kuonesha kuwa amewadharau kwa uongo wao.
"Hivi nyinyi"
huku akikirudisha kidole chake kwa Hashimu kisha kwa yule kiongozi
"Wewe Gaston, unaniona mimi ni mpumbavu?" Alimuuliza yule kiongozi ambaye jina lake ni Gaston.
"Hapana"
"Sasa kwanini unifundishe kuhusu Nadia wakati ni mimi nimemleta kwenu? Namjua yeye hana ujanja huo unaousema. Kama angetamani pesa angeondoka nazo zote pamoja na simu. Asingeweza kuchukua simu aache pesa au achukue pesa aache simu sasa mimi shida yangu Nadia na sio moja kati ya hivyo vitu"
Alikuwa ameshasimama na kuzungukazunguka. Haikuwa rahisi kukadiria umri kamili wa Mzee Kumba. Haikuwa rahisi pia kuamini kama Mzee Kumba alikuwa mzee. Ujasiri na nguvu alizonazo zikamnawirisha na kumfanya aonekane bado kijana.
"Ni kweli mzee"
"Gaston Gaston, Gaston" alisimama alipo Gaston na kumshika mabegani kisha akasema "Ninapenda kuwaambia kuwa mzigo unahitajika haswa Nadia pia, sijawaita kutupiana lawama na nyinyi au kuhesabu vingapi vimepotea"
"Sawa Mzee"
Hashimu akajibu haraka akidhani ndio mwisho wa mchezo.
Mzee Kumba aliwachukua mpaka katika chumba fulani ndani ya nyumba ile walichokikuta Gaston na Hashimu, hawakukiamini. Nani ambaye angekuwa tayari kumuona mke wake na watoto wakiwawamefungwa kamba na wakivuja damukwenye vidonda vilivyochubua ngozizao? Nani angebaki akiwa amesimama alipomuona mama yake akilia kwa uchungu naye akiwa anavuja damu huku nguo yake imechanika? Hakika Gaston na Hashimu walikutana na mtihani mzito.
Hashimu akakosa ujasiri wa kumtazama mama yake.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Mama yake alikwisha mueleza mara nyingi aachane na mambo ya watoto watukutu, yeye hakusikia. Mama yake ambaye ameathiriwa na umri kumtupa mkono, alilia alipomuona kijana wake na mzee ambaye alimkamata akiwa anaelekea bombani, Mzee Kumba. Ilikuwa ni majira ya jana jioni baada ya mzee Kumba alipotoka kuachana na wale wafanyabiashara,
Mzee Kumba alipanga kufanya jambo. Alizijua familia zote za vijana wake na hivyo ikawa rahisi kupanga mipango yake. Alifika maeneo ya jirani na anapoishi Bi Asha, mama yake Hashimu.
"Oh baba huyo!"Akapokelewa vizuri na yeye Kumba akakenua meno kama alikuwa mwema."Hashimu cha utembezi hata hujamkuta mjukuu wako"
"Hapana Bi Asha mi nimekufuata wewe"
Mzee Kumba alikuwa na gari ndogo yenye mazingira mazuri. Usiulize wapi Mzee huyo ameipata. Yeye ni mzee wa mjini, alijua pa kuzipata gari za kukodisha zilizoitwa za Magumashi hivyo haikumpa shida kujua wamiliki wake. Yote ilikuwa ni kuwapoteza watakaojifanya kumfuatilia. Namba za gari alizoenda nazo hazikuwa halali na zile zilizosajiriwa. Na kama ungetazama kwa makini, basi ungeona kuwa namba za mbele na za nyuma hazikufanana. Mzee Kumba akamchukua Bi Asha kwa ulaghai wa kwenda kuzungumza naye sehemu nzuri kuhusu mienendo ya Hashimu. Alipoingia ndani ya gari, Mzee Kumba hakuwa peke yake. Vijana wengine wawili walikuwa wamejificha kwenye giza ni hapo mikono yao iliyokomaa ilipojipenyeza katikati ya shingo yake hata akagundua kuwa ametegwa. Bi Asha alipotaka kupiga kelele, kitambaa chenye dawa kikakumbatia midomo yake, usingiziukampokea.
Usingizi ulipomuisha akajikuta yupo katika chumba chenye giza huku akisikia vilio kutoka chumba chapili. vilikuwa ni vilio vya watoto kwa mbali vikichanganyika na vilio vyamwanamke mtu mzima. "Nisaidie tunauwawa"
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment