IMEANDIKWA NA : GLOBAL PUBLISHERS
*********************************************************************************
Simulizi : Familia Tata
Sehemu Ya Kwanza (1)
NI saa moja na nusu usiku!
Nyumbani kwa mzee Linus, Nakasangwe, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam, ndani ya ua mkubwa wa nyumba yake, mapambo yamepambwa vya kutosha na wageni waalikwa wakianza kuingia.
.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/-
Katika meza kubwa, pamoja na watu wengine, mzee Komba, jirani na rafiki yake wa muda mrefu, amekaa. Juddy mwenye umri wa miaka 23, mtoto wa pili wa mzee Linus alikuwa anafanyiwa sherehe ya kuagwa.
Kesho yake asubuhi, alitarajiwa kupanda ndege kuelekea Uingereza masomoni baada ya kufanya vizuri katika miaka yake mitatu ya kusomea Uhandisi katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Familia ya Linus na Komba ni marafiki wa muda mrefu, urafiki wao una historia ndefu. Walifahamiana shuleni, walipokutana katika michezo ya umisseta miaka ya sabini, lakini walijikuta wakiwa karibu zaidi walipokutana Dar es Salaam kikazi, mwanzoni mwa miaka ya themanini.
Ingawa walifanya kazi ofisi tofauti, lakini walifanikiwa kupanga sehemu moja, Kigogo. Baadaye, Linus katika pitapita zake, akasikia kuhusu kuuzwa kwa viwanja eneo la Nakasangwe, pembezoni mwa Kiwanda cha saruji cha Wazo, Tegeta, Dar. Viliuzwa kwa bei rahisi, akamshawishi rafiki yake, wakanunua jirani na mara moja wakaanza kujenga!
Ingawa wote sasa ni wastaafu, lakini wamejenga makazi bora na familia zao zinaendelea vizuri, wote wakibarikiwa kuwa na watoto wanne kila mmoja. Familia zao ni zaidi ya marafiki, shughuli ya kila mmoja wao, ni shughuli ya wote. Ndiyo maana leo mzee Komba ni mgeni rasmi, mke wake, ndiye anawaongoza akina mama katika masuala ya mapishi na vijana wa pande zote mbili, ndiyo wasimamizi wakuu wa mambo ya muziki, burudani na usafiri.
Shamrashamra ni nyingi kweli katika mtaa huu, muziki unasikika kwa sauti ya chini lakini ya kupendeza, majirani na wageni wengine kutoka mbali wanaendelea kumiminika katika nyumba hii yenye eneo kubwa kwa ndani.
Katika eneo la jukwaa, lililotayarishwa rasmi kwa ajili ya watu kucheza wakati wa burudani ukifika, mafundi walikuwa wanamalizia kufunga vyombo, huyu akijaribu kile na huyu akijaribu kile.
Juddy, licha ya kwamba ilikuwa ndiyo siku yake, naye alikuwepo uani hapo kuwapokea ndugu, jamaa na marafiki waliojitokeza kwenye shughuli hiyo.
Hadi ilipofika saa mbili na nusu za usiku, ukumbi ulionekana kujaa, kwani maeneo machache tu ndiyo yaliyoonekana kuhitaji watu. Juddy alishaingia ndani kubadili nguo na tayari alisharejea akiwa amekaa meza kuu.
Antony, kijana mwenye umri wa miaka 14, mtoto wa tatu wa mzee Komba, alionekana akiingia ndani ya nyumba ya mzee Linus akiwa amebeba mfuko mweusi wa rambo, ndani yake kukionekana kuwa na kitu kisichofahamika. Mama yake Juddy, aliyekuwa akitokea jikoni alimuona.
“Nini hicho Tonny?” alimuuliza Antony, ambaye alifahamika zaidi kifupi kama Tonny, kijana wa jirani yao.
“Mama, wee subiri, kuna sapraizi nataka kuifanya hapa,” alisema Tonny huku akielekea chooni.
Mama yake Juddy akaguna na kutikisa kichwa, kisha akasema: “Mambo ya watoto bwana…” huyoo akaenda zake uani kuungana na wageni wengine!
Tonny akaingia chooni, akaufungua mfuko wake wa rambo. Akatoa sanamu ya kishetani sehemu ya kichwa, akaitazama, akatabasamu. Akaijaribu kuivaa na kwenda kujiangalia kwenye kioo. Yes, alifanana na shetani kabisa!
“Sasa subiri uone moto wake hapo uani,” alijisemea kimoyomoyo, akafungua mlango na kutoka nje ya choo, akaanza kutembea taratibu kuelekea uani…!!!!
Tonny alikuwa amevaa kinyago cha kishetani akiwa chooni katika nyumba ya mzee Linus, swahiba mkubwa wa familia yao nyumba ya pili. Akionekana kama shetani, alitoka na kuanza kutembea taratibu kuelekea uani kulikokuwa na shamrashamra za sherehe za kumuaga Juddy…
sasa Endelea...UDDY aliondoka meza kuu na kwenda katika jukwaa lililotayarishwa tayari kwa sherehe. Pale alipokaa, alisikia kama vile kuna mkwaruzo kwenye kipaza sauti, akasogea ili kumwelekeza fundi mitambo arekebishe kasoro hiyo.
Wageni wengine wote walikuwa tayari kwenye viti vyao na wahudumu waliifanya vizuri kazi yao, vinywaji mfululizo viliendelea kutolewa na stori za hapa na pale zikipamba moto miongoni mwa wageni.
Watoto wadogo waliokuwa wakicheza muziki wa msanii Mr Nice, uitwao Kidali Poo, ndiyo waliokuwa wa kwanza kumuona Tonny katika mavazi yake ya kishetani. Walipiga kelele kubwa na kukimbilia upande wa watu. Kelele zile ziliwashtua watu wote akiwemo Juddy aliyekuwa akizungumza na fundi mitambo, alipotazama mlangoni, akamuona mtu aliyeamini ni shetani…!
.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Mamamaaaaaa,” Juddy alipiga kelele na kuanza kukimbia jukwaani. Akitafuta sehemu salama ya kukimbilia, kwa bahati mbaya akakanyaga waya, akaanguka na bila kutarajia, kichwa chake kikaenda kuangukia kwenye maungio ya nyaya za umeme!
Waya mmoja ukachomoka, ukaishia kwenye shingo yake. Ndani ya sekunde chache, mwili wake ukabadilika rangi….
Kelele za kukimbia kwa watoto na vijana wengine zilidumu kwa muda kadhaa kabla Tonny hajavua kinyago kile na kuanza kucheka. Shughuli ilishaharibika. Wakati watu wanaanza kurejea katika hali ya kawaida, wakagundua mtu aliyelala kimya ametulia chini, pembeni ya jukwaa.
Ni Juddy!
Haraka watu wakakusanyika, wakaogopa kumsogelea. Fundi mitambo alijua kilichotokea. Akazima umeme wa jukwaani, akamsogelea na kumgusa, akawatazama watu kwa huzuni.
“Jamani tumbebe, mambo yameshaharibika,” alisema fundi mitambo.
“Hebu subiri, nini?” Mzee Komba aliuliza baada ya kubaini utulivu aliokuwa nao Juddy, moyoni mwake akajua mambo hayako sawa.
“Hebu watoto tokeni hapa, sogeeni kule,” alisema mzee huyo na watoto, wakiwa kimya, wakasogea pembeni. Mzee Linus akasogea, mama Juddy alikuwa amesimama mbali, mwili ukimtetemeka!
Mmoja kati ya wageni waalikwa alikuwa daktari, Dr Junior. Akasogea na kwenda kumgeuza Juddy, akamshika moyo, akaonyesha uso wa huzuni pia. Akatoa ishara ya kumbeba msichana huyo. Akabebwa na kupelekwa kwenye gari kwa safari ya kuelekea hospitalini.
Wakati magari yanafuatana kuelekea hospitali ili kupata uhakika wa nini kimetokea, wageni waliokuwa hapo wakaonekana wamejipanga makundi makundi, mama Juddy alikimbilia chumbani kwake kujifungia, akilia kwa uchungu.
“Sijui kama atapona, ”fundi mitambo aliwaambia watu waliomzunguka kutaka kujua nini kimetokea. “Alikanyaga waya wakati anakimbia, bahati mbaya alipoanguka akaangukia hapa, hizi nyaya zikachomoka moja ikamgusa mwilini na bahati mbaya akailalia,” alisema fundi huyo na kusababisha vilio kutoka kwa watu waliokusanyika eneo hilo.
Mzee Linus, Komba, Dr Junior na majirani wengine kadhaa walikuwa nje ya Hospitali ya IMTU, eneo la Mbezi jijini Dar es Salaam wakisubiri ripoti ya daktari, ingawa wote walitambua kwamba Juddy alishafariki. Hakuna aliyekuwa akisema chochote, wote walionekana kujiinamia kwa huzuni. Aliyekuwa na hali mbaya zaidi, alikuwa ni mzee Komba. Kijana wake ndiye aliyesababisha tafaruku yote, hakuelewa nini hatima yake.
Baada ya nusu saa, daktari wa hospitali hiyo aliyetambulika kwa jina la Rama, alitokea kwenye ukumbi waliokuwa wamejazana watu, akaomba wahusika wa karibu kumfuata ofisini kwake.
“Poleni sana, mpendwa wetu amefariki dunia. Inaonekana ameunguzwa vibaya na umeme, poleni sana,” Dk. Rama aliwaambia mzee Linus na mzee Komba waliokuwa wamekumbatia mikono vifuani mwao!
Juddy aliyeangukia katika nyaya za umeme wakati akikimbia kumuogopa mtu aliyekuwa amevaa kinyago.
Wakiwa hospitali, waliitwa ofisini kwa daktari kupewa matokeo ya uchunguzi wa Juddy na kuambiwa kuwa alikuwa amefariki dunia.
Sasa Endelea...
Taarifa rasmi ya kifo cha Juddy ikatolewa kwa watu waliokuwepo pale uani nyumbani kwa mzee Linus. Vilio vikaongezeka na ghafla sherehe ikageuka na kuwa msiba mkubwa. Hata hivyo, vinywaji vilivyokuwa vimetayarishwa kwa ajili ya mnuso huo, vikaendelea kuteketea.
Mzee Linus, Komba na majirani wengine wakaingia ndani kuuchukua mwili wa Juddy hospitalini IMTU na safari ya kuupeleka katika Chumba cha kuhifadhia maiti kwenye Hospitali ya Mwananyamala ilianza.
Hospitalini Mwananyamala, mtu wa chumba cha maiti aliwapokea. Taratibu zikaanza kufanywa ili mwili huo uhifadhiwe.
“Poleni sana, marehemu amefariki katika mazingira gani?” aliwauliza. Dr. Junior akajitokeza na kumwelezea kwa kifupi kilichotokea.
“Aisee, sasa hii ni lazima tupate karatasi kutoka polisi kwa sababu hili ni tukio linaloweza kufananishwa na jinai,” mtu yule aliwaambia.
Walitakiwa kwenda kutoa taarifa katika kituo cha polisi kilichopo karibu na eneo la tukio, jambo lililomaanisha walitakiwa kwenda kituo cha Wazo au Kawe.
Mzee Komba akachukua simu yake ya kiganjani, akabonyeza namba kadhaa na kuiweka sikioni. Upande wa pili ulipokea, naye akatoa maelezo mafupi ya tukio lao.
Akatoa ishara ya kumtaka mhudumu wa chumba cha maiti kusubiri. Dakika mbili baadaye, simu ya mezani ya chumba cha maiti iliita, mhudumu aliipokea. Alionekana akipewa maelekezo kwani muda wote alikuwa akiitikia ‘ndiyo’ huku akitikisa kichwa.
“Nimeambiwa niipokee maiti lakini nyinyi lazima muende mkapate karatasi ya Polisi na muilete hapa ili tuweze kuandikisha maelezo yake kama ulivyo utaratibu,” aliwaambia baada ya kumaliza kuzungumza na simu, iliyotoka kwa mganga mkuu wa hospitali hiyo.
Wote waliitikia na kusaidia kuihifadhi maiti katika jokofu. Kisha wakaondoka kuelekea Kawe ambako baada ya maelezo, walipewa askari mmoja na kuambiwa watakutana na wenzao wa Wazo tayari kwa safari ya kwenda eneo la tukio.
Saa nane za usiku msafara wa watu waliokwenda hospitalini uliwasili nyumbani kwa mzee Linus, wakiwa wameongozana na gari mbili za polisi aina ya Difenda.
Baada ya kuzungumza na wenyeji na kupata maelezo ya jinsi tukio hilo lilivyotokea, askari aliyeonekana kuwa kiongozi wao alisema.
“Yuko wapi kijana aliyesababisha hali hii?”
Kwa mara ya kwanza watu wakamkumbuka Tonny, hakukuwa na yeyote aliyemfikiria.
“Tonny, Tonny…..” watu wakaanza kuliita jina lake, lakini hakuonekana.
.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Ni lazima apatikane,” askari huyo alisema, hali iliyoanza kuzua hofu miongoni mwa waombelezaji waliojazana ndani ya nyumba hiyo.
Akatafutwa nyumba nzima hakuonekana, nyumbani kwa mzee Komba pia hakuwepo.
“Anaweza kuwa amekimbia?” askari huyo aliuliza tena na mzee Komba akasema hadhani kama kijana huyo anaweza kukimbia, hasa kutokana na udogo wa umri wake, haonekani kuelewa lolote.
Polisi wakaagiza kufunguliwa kwa vyumba vyote ndani ya nyumba ya mzee Komba. Wakaanza chumba cha wazazi, kisha watoto, stoo, jikoni na kila mahali, Tonny hakupatikana.
Wakafikia vyoo vya ndani, mlango ulionekana umefungwa kwa ndani. Wakagonga, wakaita haukufunguliwa wala kusikika sauti yoyote.
“Antony, Antony, fungua mlango, Antony!!!” Mzee Komba aliita kwa sauti huku akigonga kwa nguvu mlango, hakukuwa na majibu.
“Inabidi uvunjwe,” askari alisema. Mzee Komba akatikisa kichwa kukubali. Kazi hiyo ikafanyika, kitasa kikavunjwa na mara mlango ukawa wazi.
Tonny alionekana akiwa amelala sakafuni!!!!!!
ASKARI alimsogelea Tonny, akamwangalia vizuri usoni mwake, mwili ulionekana kuloa maji. Mzee Komba naye akaingia chooni na kumtazama mwanaye. Askari akamgeuza uso ukatazama juu.
Dr Junior, jirani yao ambaye kwa muda wote amekuwa karibu na tukio hili, akawaomba wambebe kijana huyo na kumtoa nje, kwa sababu ya nafasi ndogo ndani ya choo.
Tonny akatolewa na kulazwa kwenye korido. Dr Junior alimtazama, akamshika kifuani kupima mapigo ya moyo wake.
“Amepoteza fahamu, nadhani ataamka baada ya muda mfupi,” aliwaambia watu ambao sasa walishakuwa wengi ndani ya nyumba ya mzee Komba.
“Apepewe,” askari aliamuru na mara moja, ndugu zake Tonny wakaanza kumpepea kwa khanga na vitenge.
Baada ya dakika chache za kupepewa, Tonny alijitingisha, dalili kuwa fahamu zinaanza kumrejea, kisha akafunua macho, akainuka na kukaa. Wote walimtazama kwa hofu.
“Unajua nini kimetokea?” Baba yake alimuuliza mwanaye huku ameingiza mikono kwenye mifukoni ya suruali yake.
“Ndiyo baba,” Tonny alijibu, machozi yakimlengalenga machoni mwake.
“Nini kimetokea?,” mzee Komba alimuuliza tena.
“Kule kwa kina Juddy baba….,” Tonny akashindwa kumalizia, akaanza kulia kwa sauti.
“Mbadilishieni nguo,” askari alisema, akachukuliwa na kuingizwa ndani, akabadilishwa nguo.
“Mzee, poleni kwa matatizo, inauma sana. Hata hivyo, huyu kijana itabidi twende naye kituoni kwa mahojiano zaidi. Mambo mengine nadhani mtayajua huko,” askari alimweleza mzee Komba aliyetingisha kichwa kukubaliana naye!!!
***
Baada ya gari la polisi kuondoka alfajiri ile, huzuni ilirejea upya. Mama yake Tonny alikuwa akilia pamoja na mama Juddy, ni tukio ambalo halikutarajiwa na liliwagusa wote kwa pamoja.
“Dada hata sijui nikuambie nini, naumia sana yaani..,” mama yake Tonny alimwambia mama Juddy, akimfuta machozi wakati yeye mwenyewe akiwa analia.
“Usijali dada, mipango ya Mungu, ni bahati mbaya, sote nafsi zetu zitaonja mauti,” naye alimjibu mwenzie, kitu ambacho kilimfariji sana.
Siku hiyo ilitumika kusambaza habari kwa ndugu jamaa na marafiki sehemu zote duniani. Msiba huo uliwashtua watu wengi. Aliyeumia zaidi alikuwa ni Asfat, dada yake Tonny aliyekuwa swahiba mkubwa wa Juddy.
Alikuwa Birmingham nchini Uingereza anakosoma, akisubiri kupanda treni kuelekea London kumpokea shosti wake alipopokea simu ya kaka yake, Amani. Ilikuwa ni saa moja na nusu asubuhi kwa saa za huko.
“Usiniambie ameshapanda ndege tayari kaka,” Asfat alimwambia Amani mara tu alipoweka simu yake sikioni.
“Si bora hata angepanda baadaye, hatapanda tena,” Amani aliongea kwa sauti ndogo, yenye majonzi, iliyomshtua sana dada yake.
“Heee, imekuaje tena kaka Amani mbona unanishtua, baba amegoma kwani…,” aliuliza kwa hamaki.
“Dah, dada wee acha tu, Juddy amefariki,”
“Ni...ni...ni...?!!
Amani alimtuliza dada yake, akamwelezea kisa kizima kilivyokuwa, habari ambazo zilimsikitisha na kumliza sana. Aliyekufa ni rafiki yake wa kufa na kuzikana na aliyeua ni mdogo wake wa damu!
Shughuli za msiba zikaendelea, ukapangwa kufanyika siku nne baadaye ili kuweza kuwakusanya ndugu na marafiki waliokuwa mbali.
Kama ilivyo kawaida ya siku zote, licha ya msiba ule kusababishwa na wao, lakini walishiriki kwenye shughuli kama kawaida, wote wakionyesha kuwa na uchungu. Katika hali ya kawaida, hakuna mtu aliyetegemea yaliyokuwa yakitokea.
Mzee Komba na familia yake walishiriki kila hatua ya tukio lile na mzee Linus na familia yake nao hawakuonyesha kinyongo chochote, wote waliamini kilichotokea ilikuwa ni mipango ya Mungu.
Juddy alizikwa siku nne baada ya kufariki katika tukio lililokusanya umati mkubwa wa watu, kwenye makaburi ya Nakasangwe!
Watoto wa familia zote mbili walishiriki kikamilifu shughuli ile ya msiba na walikaa nyumbani kwa mzee Linus kwa siku zote, hadi ya saba, wakati walipokaa kikao cha pamoja kujadili kilichotokea na mzee Komba ndiye alikuwa mwenyekiti wa kikao kile.
“Rafiki, kaka yangu, shemeji yangu na wanangu wote wa nyumba hii, kwa niaba ya familia yangu, tunaomba kuwaomba radhi kwa yote yaliyotokea, lakini tunaamini ni kazi ya Mungu ambayo siku zote haina makosa,” Mzee Komba alisema huku akijifuta machozi, kitendo ambacho pia kilifanywa na watu wote, hasa Asfat, aliyesafiri kutoka Ulaya kuja kuhudhuria mazishi ya rafiki yake mkubwa!
.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Usijali kaka, rafiki, jirani na wanangu wote. Kama ulivyosema, hili ni tukio ambalo hakuna aliyelitegemea, huu msiba ni wetu wote kama ambavyo tumeshuhudia, wote mmeshiriki kikamilifu tokea mwanzo hadi sasa. Nyinyi ni sisi na sisi ni nyinyi, haya yamepita, sasa tujitahidi kumnusuru Tonny, ni kijana mdogo aliyetaka kuwachekesha wenzake lakini matatizo yakatokea,” Mzee Linus naye alisema, huku watu wote wakiendelea kujifuta machozi!
Walijadili mambo mengi sana kama familia marafiki na hatimaye baadaye wakakubaliana kuondoa aina yoyote ya chuki baina yao. Wakasimama na kushikana mikono. Wakati wa tendo hili, wote waliendelea kutokwa na machozi.
Tonny alikaa polisi kwa siku tatu, baadaye akapelekwa katika mahakama ya watoto Kisutu jijini Dar es Salaam ambako alisomewa shtaka la mauaji ya bila kukusudia. Na baada ya kusomewa mashtaka yake ambapo hakutakiwa kujibu chochote kwa kuwa mahakama ile haikuwa na uwezo wa kusikiliza kesi hiyo, akapelekwa Segerea.
Wazazi walimtafuta mwanasheria aliyekuwa akitamba sana jijini Dar es Salaam, Bennedict ili aweze kumsimamia Tonny. Kazi hiyo hata hivyo haikuwa ngumu sana kutokana na wazazi wa marehemu nao kupigana kwa nguvu zote kuhakikisha kijana huyo anaachiwa!
Tonny aliachiliwa huru baada ya miezi mitatu tu na alipotoka mahakamani, alikwenda moja kwa moja nyumbani kwa akina Juddy akiwa analia!
Kilio chake kiliashiria majuto aliyokuwa nayo. Hata hivyo, wote walionyesha moyo wa huruma dhidi yake na akaomba apelekwe kaburini kwa Juddy ili akaweke shada la maua.
Ombi hilo likakubaliwa na familia zote zikapanga kitendo hicho kifanyike kesho yake ambayo ilikuwa ni Jumapili ili wengine pia wahudhurie.
Makaburini, Tonny alipiga magoti katikati ya kaburi la Juddy, akachukua mshumaa na kuuwasha, akalibusu shada lake la maua na kuliweka, kisha machozi yakaanza kumtoka. Wanafamilia wengine waliomsindikiza nao waliweka mashada yao na kupiga magoti. Mwishowe wote kwa pamoja walisali na kuondoka!
Asfat akarejea zake shuleni Ulaya na ndugu wa familia zingine wakaendelea na maisha yao ya kila siku. Hakukuwa na tofauti yoyote kati ya familia hizi kwa kipindi kirefu.
Mwaka mmoja na miezi sita baada ya kifo cha Juddy, maisha yalikuwa katika mtindo wake wa kawaida kabisa kwa familia hizi rafiki.
Baptist, ambaye alimuachia ziwa Juddy, alikuwa akitoka mjini kutengeneza gari lao lililokuwa limeharibika mfumo wake wa umeme eneo moja la Gerezani, jijini Dar es Salaam. Wakati akirejea nyumbani alikuwa na mawazo mengi.
Katika umri wake wa miaka 25, alikuwa mtu wa kujirusha sana katika maeneo ya starehe. Ilikuwa ni lazima aende klabu kila mwisho wa wiki na hii ilimfanya kuwa na marafiki wengi wa kike na kiume.
Lakini sifa yake kubwa ilikuwa ni tabia yake ya kuendesha gari kwa mwendo kasi. Hata kama alikuwa akienda sehemu ya karibu, alipenda kulikimbiza...
Mama yake Tonny alikuwa uani kwake akifua nguo za mtoto wake wa mwisho, Subby wakati akitaniana na kaka yake Tonny aliyeitwa Santo. Santo alikuwa akisoma darasa la saba katika Shule ya Msingi Bunge na siku hiyo ya Jumamosi, hakwenda shule.
Mama Tonny alikuwa akimpenda sana Santo na mara nyingi walikuwa wakitaniana. Leo, wakiwa hapa, mama alikuwa akimshambulia Tonny kwamba ni lazima atafeli kwa sababu ya kupenda sana filamu. Na kweli, Santo alikuwa shabiki mkubwa wa filamu, hasa za Kizungu, ingawa pia alivutiwa na zile za Kihindi na Kibongo.
Baada ya kuzidiwa utani na mama yake, Santo akaamua kuondoka lakini akamvizia akiwa amejisahau, akamtekenya kwenye mbavu. Mama alipata mshtuko mkubwa na akiwa na hasira, aliinuka na kuanza kumfukuza kijana wake aliyekuwa anakimbilia nje ya geti!
***
Baptist alikuwa anakata kona maarufu mtaani kwao iitwayo Kwa Kipira, akiwa katika mwendo wa kasi kama kawaida yake. Mtaa ulikuwa kimya na hakukuwa na mtu barabarani. Akiwa anakaribia kwenye geti la nyumba ya Mzee Komba, ghafla akamuona mtu akitokeza kwa kasi na kuingia barabarani.
Hakuweza kujizuia, hakuweza kulizuia gari, kishindo kikubwa kikasikika na mtu mmoja alionekana akirushwa juu na alipoanguka chini, akabakia kuwa mtulivu pale chini alipofikia.
Alikuwa ni Santo!
Kishindo kile kilileta kelele kubwa mtaani na mara moja, kila mtu aliyekuwepo alitoka nje ya nyumba ili kushuhudia kilichotokea. Bap alifanikiwa kusimamisha gari mita chache mbele, akatoka nje ya gari na kumkimbilia mtu aliyemgonga!
Kishindo kile kilikuwa kama nyundo iliyopiga katika kichwa cha mama yake Tonny, alitambua kabisa kwamba aliyegongwa ni mtoto wake. Naye pasipo kutarajia alianguka na kupoteza fahamu muda uleule mwanaye alipogongwa.
Ndani ya dakika moja, watu wengi walijazana pale alipokuwa amelala Santo, mwili wake ulijaa damu na watu wakawa kama waliochanganyikiwa. Kwa muda wakawa hawajui wafanye nini hadi akili zilipowarejea.
Baptist alikuwa wa kwanza kumshika Santo, akamgeuza vizuri na kumtazama, akatoa ishara kwa wenzake wambebe, wakampakia kwenye gari alilomgonga nalo. Watu wengine wawili wakaingia ndani ya gari lile, kwa kasi ya ajabu, likaondoka kuelekea hospitalini!
Watu wengine nao mtaani wakawasha magari yao na kulifuatilia gari lililombeba Santo. Baptist aliendesha gari kwa kasi hadi alipofika katika Hospitali ya Mico iliyopo Tegeta Basihaya. Madaktari wakampokea haraka mgonjwa na moja kwa moja akapelekwa chumba cha upasuaji!
Nyumbani kwa akina Santo, baadhi ya majirani walishtuka baada ya kumuona mama yake Santo akiwa amelala chini, tena kwa namna ya kutisha. Walipomchunguza, wakagundua kwamba alikuwa amepoteza fahamu.
Wakamfanyia huduma ya kwanza, kisha wakambeba na kumwingiza ndani kwake. Alirejewa na fahamu baada ya nusu saa, akashangaa kuona watu wamemzunguka sebuleni alipolala kwenye kochi.
.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Vipi?” aliwauliza wanawake wawili waliokuwa karibu yake, akiwemo mama yake Juddy.
“Tulia, tuliza akili kwanza, upo salama?” mama Juddy alimwambia mwenzake huku akimtengeneza vizuri kanga zake alizojifunga.
“Kuna nini kimetokea dada, niambie haraka,” mama yake Santo alimwambia mama Juddy huku akimshika mikono yake kwa nguvu kubwa.
“Tumekukuta umeanguka pale mlangoni kwako, ndiyo tukakubeba na kukuingiza ndani,” alijibiwa!
“Mnenikuta nimeanguka?” aliuliza tena na kuanza kuvuta kumbukumbu.
Baada ya kumfikisha hospitalini alikopokelewa, Baptist akachukua simu yake na kumpigia baba yake mzazi, mzee Linus.
“Shikamoo baba,” Baptist aliongea mara tu ilipopokelewa.
“Marahaba, tunakaribia hapa hospitali, vipi hali yake,” mzee Linus alijibu, kauli ambayo ilimshangaza sana Baptist, hakutegemea kama mzee wake alishataarifiwa. Ukweli ni kwamba mama yake, alimpigia simu na kumweleza kilichotokea mara tu walipoondoka nyumbani kuelekea hospitali.
Naye mzee Linus aliwasiliana na rafiki yake. Bahati nzuri, mzee Komba alikuwa Bahari Beach Hotel alikokuwa na kikao cha kikazi na washirika wake kibiashara, wakati mzee Linus alikuwa akirejea kutoka shambani kwake Mapinga, alikuwa akikaribia Bunju, njia ya kuelekea Bagamoyo!
Wakakubaliana kukutana hospitali.
***
Mama Tonny alivuta kumbukumbu zake vizuri akiwa amejiinamia chini. Kwa mbali akakumbuka kuhusu kilichotokea. Kishindo cha kugongwa na gari mtoto wake kikajirudia tena akilini mwake, akapiga ukulele..
“Mamaaaaaa!”
Watu wote waliokuwa sebuleni hapo wakashtuka, mama yake Juddy akawahi kumshika mkono na kumtuliza.
“Vipi mwenzangu?” aliuliza
“Santoo, Santooo, mwanangu Santooo jamani,” mama Tonny alianza kuangua kilio, Mama Juddy akamshika vizuri na kumtuliza, akazidi kupiga kelele na kuuliza alipo mwanae.
“Amepelekwa hospitali.”
“Wamempeleka yeye au maiti yake?” aliuliza huku akiuma meno kwa uchungu, hakuamini kama mwanae alikuwa mzima.
“Mzima kabisa dada, wala usiogope,” mama Juddy alijitahidi kumfariji.
“Nataka kwenda, nataka kwenda, sasa hivi,” alisema na kuinuka, wanawake wenzake walijaribu kumzuia, lakini akawashinda nguvu, asijue hospitali waliyokwenda, akatoka nje ya geti na kuanza kutimua mbio akiwa pekupeku bila viatu.
Bahati nzuri kulikuwa na vijana wa kiume mtaani hapo ambao bado walikuwa katika vikundi wakijadili tukio hilo, wakaambiwa wamkamate asije kupata madhara zaidi.
Zoezi lile halikuwa kubwa, vijana kadhaa wenye ubavu walimkimbiza mama kidogo, na kumkamata na kumsihi atulie, kwani tayari akina baba walikuwa wameshafika hospitalini, na taarifa zilizoletwa muda huo zilisema Santo alikuwa bado chumba cha upasuaji.
Kwa unyonge mama akakubali kurudi nyumbani, lakini akiwa anatoa kilio kikubwa. Vijana wale walimuongoza nyumbani wakijaribu kumpa matumaini.
***
Baptist aliwafuata mzee Komba na baba yake waliokuwa wamekaa kwenye benchi wakizungumza kwa huzuni.
“Inabidi niende polisi kutoa taarifa za ajali,” aliwaambia huku naye akionekana kuwa mwenye huzuni kubwa.
“Sawa, nenda kituo cha Wazo, halafu kitakachotokea utatuambia,” alisema mzee Linus.
Baptist akaendesha gari kwa kasi kama kawaida yake hadi Kituo Kidogo cha Polisi Wazo. Alijua haitakuwa rahisi kutoka wakati ule, akatafuta sehemu nzuri na kuegesha, akasogea kaunta ya polisi na kueleza tatizo lake kwa askari aliyekuwa zamu.
“Zunguka, vua viatu, saa, mkanda, afande, mfungulie mlango huyu, kaua,” askari aliyekuwepo kaunta alisema kwa sauti kubwa, hali iliyosababisha watu wote waliokuwa jirani kumtazama Baptist aliyekuwa sasa anazunguka kuingia kaunta.
“Kwani imekuaje?” alisema askari mwingine aliyekuwa ndani, ambaye alionekana kama ndiye mkubwa, kuliko yule aliyekaa kaunta. Akataka kijana yule aingie ofisini kwake.
Baptist akaingia, akakisogelea kiti kilichokuwa kinatazamana na kile cha ofisa wa polisi, akakaa. Ofisa huyo akataka kupata maelezo ya nini hasa kimetokea.
Baptist akamuelezea kuanzia mwanzo hadi mwisho. Askari akatingisha kichwa. Akachukua mkono wa simu ya mezani, akabonyeza namba kadhaa kisha akauweka sikioni.
“Hebu askari watatu waje ofisini mara moja, wanatakiwa kwenda kupima ajali Nakasangwe na halafu kuangalia maendeleo ya majeruhi hospitalini haraka..,” ofisa yule wa polisi aliongea kwenye simu na kisha kurudisha mkonga sehemu yake.
Dakika moja baadaye, askari watatu, akiwemo mwanamke mmoja walikuwa ofisini hapo, wakapewa maelekezo, kisha wakainuka pamoja na Baptist na kuelekea kwenye gari la Polisi aina ya Toyota Land Cruiser, maarufu kama Difenda. Wakakanyaga moto hadi eneo la tukio. Wakachukua vipimo pamoja na kupata vidokezo kutoka kwa majirani ambao sasa walikuwa wengi wamejikusanya ilipotokea ajali na nyumbani kwao mzee Komba, wengi wakiulizia maendeleo ya majeruhi.
Baada ya kumaliza shughuli hiyo, wakawasha gari wakiwa na Baptist na kuondoka kuelekea hospitali alikolazwa majeruhi. Wakaomba kukutana na daktari aliyempokea mgonjwa na kutaka kujua hali yake.
“Ana hali mbaya sana afande, sidhani kama atapona,” daktari aliyempokea na kumshughulikia Santo aliwaambia askari wale alipowakaribisha ofisini kwake na wao kujitambulisha.
.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Ameumia kwa kiasi gani,?” askari kiongozi wa msafara aliuliza. Kabla daktari huyo hajajibu chochote, simu yake ya mezani ikaita. Akatoa ishara ya kumtaka radhi, akainua mkonga wa kuongelea na kuuweka sikioni, alisikiliza kwa sekunde chache kabla ya kuurudisha mahali pale.
“He is dead (amefariki),” alisema huku akitoa miwani yake na kuifuta kwa kitambaa chake cheupe!
***
Vilio viliripuka nyumbani kwa mzee Komba mara tu taarifa za kifo hicho zilipopelekwa. Alikuwa ni mzee huyo aliyempigia simu mtoto wake mkubwa wa kiume, akimfahamisha tukio hilo la kusikitisha. Mama yake Tonny alipoteza fahamu mara tu alipofuatwa na mtoto wake na kumweleza kuwa kule hospitalini, Santo amefariki dunia!
Taarifa za kifo hicho zilisambaa kwa kasi kubwa, ndugu mbalimbali wa ndani na nje ya nchi waliarifiwa na zilipomfikia Asfat, ambaye sasa alikuwa ameshamaliza masomo na akijiandaa kwa safari ya kurejea nyumbani Tanzania, hakuamini.
“What?” aliuliza wakati alipopokea simu ya kaka yake, Amani, aliyemtaarifu juu ya msiba huo.
“Ndiyo hivyo sista, bahati mbaya,” Amani alisema kwa upole.
Asfat hakutaka kuamini kirahisi kama kifo kile kilikuwa bahati mbaya, akilini mwake aliona huenda kilikuwa ni kisasi, hivyo akataka maelezo ya kutosha kutoka kwa kaka yake.
“Kaka Amani, slowly please (taratibu tafadhali), hebu niambie vizuri, una uhakika kaka Baptist kamgonga Santo kwa bahati mbaya? Sitaki kuamini, naona kama kisasi fulani hivi, wewe unaonaje?” Asfat aliongea huku akiwa ameuma meno.
“Hapana dada Asfat, ni ajali. Santo alikuwa na mama uani, wanataniana, si unawajua walivyo, sijui ilikuwaje wakaanza kufukuzana, Santo akakimbilia nje, sasa ile anatokeza tu mlangoni na Baptist anapita, si unajua anavyoendeshaga, hakujua, hakumuona, hakuna hata mtu mmoja anayemlaumu Bap, ni ajali dada, amini ninachokuambia, ambacho najua hata mama atakuambia hicho hicho,” Amani alijaribu kumtuliza dada yake.
Asfat akakubali, lakini hakuridhika!!!!…
...Baptist akaondoka na askari wale kurejea kituoni Wazo, ambako aliwekwa mahabusu na baadaye kufunguliwa jalada la ajali iliyosababisha kifo.
Pale hospitalini, mzee Komba na mzee Linus wakaanza taratibu za kuutoa mwili ili uende kuhifadhiwa hospitali yenye majokofu ya kuhifadhia maiti. Majirani wengine kadhaa nao walikuwa wameshawasili hospitalini hapo kwa msaada wowote unaoweza kuhitajika.
Mzee Komba akashauriwa kurejea nyumbani ili aweze kupumzisha akili sambamba na kupokea wageni, kazi ile ya kushughulika na mwili wa marehemu ikaachwa mikononi mwa mzee Linus, akishirikiana na vijana wa familia zote mbili.
Nyumbani kwa mzee Komba, watu walishaanza kujaa, kila mmoja akizungumza kwa jinsi alivyoona kuhusiana na ajali ile. Mama yake Juddy, alikuwa muda wote akimtuliza shoga yake, dada yake na jirani yake wa miaka mingi, mama Tonny.
Uani, walikuwepo majirani wawili, mama Rama na mama Sabina, wamekaa chini ya muarobaini kujikinga na jua wakizungumza.
“Mimi nina wasiwasi,” Mama Rama alianza
“Wa nini na wewe shosti, umeanza,” alijibu Mama Sabina.
“Hii ajali, hivi unafikiri ni bahati mbaya kweli?”
“Jamani hebu acha uchuro, sasa wewe unadhani ni makusudi?”
“Kabisa, akili yangu hainipi kabisa, unakumbuka kifo cha Juddy?”
“Jamani, kwani vipi mama Rama?”
“Naona kama Bap kafanya makusudi, hivi unaendeshaje mwendo mkali vile wakati umeshafika nyumbani?”
“Usiseme hivyo, kwani wewe ni mgeni na Bap, si kila siku ndiyo mwendo wake jamani?”
“Hata kama, naona kama alikuwa anatafuta nafasi alipize kisasi kwa kifo cha dada yake, hivi unadhani walifurahi kwa jinsi Tonny alivyofanya?”
“Mmh, mi sidhani bwana, naona ni ajali tu, mbona Salum naye anaendeshaga mwendo mkali, ingekuwa yeye ndiyo kamgonga ungesemaje,” Mama Sabina alimwambia shoga yake, akimzungumzia jirani yao mwingine, Salum ambaye pia anasifika kwa kuendesha gari kwa mwendo kasi, hata akiwa hatua mbili kutoka nyumbani kwake…
***
Mzee Komba na vijana wake walifanikiwa kuufikisha mwili wa Santo katika hospitali ya serikali ya Mwananyamala, baada ya kumaliza taratibu zote wakarejea nyumbani kujiunga na waombolezaji wengine. Watu sasa walishakuwa wengi.
Kila mmoja alizungumza lake, lakini wengi wakilaumu tabia ya uendeshaji wa mwendokasi wa Bap, wakisema kama isingekuwa vile, angeweza kunusuru maisha ya Santo. Hata hivyo, hali ilikuwa tofauti sana kwa mama yake marehemu, mama Tonny.
Akiwa amejikunyata chini alipolala kwenye mkeka akifarijiwa na mama Juddy, picha ya tukio lile ilijirudia. Alimuona mtoto wake akimtekenya, akajiona mwenyewe akiinuka kwa hasira na kuanza kumfukuza mwanaye.
“Mwanangu nimemuua mwenyewe dada,” alijikuta akimwambia mama Juddy, aliyekuwa na majirani wengine wawili sebuleni kwake, ambao nao walishtushwa na kauli ile.
“Kivipi shoga,” Mama Juddy alimuuliza mwenzake kwa namna ya kushangaa kidogo, maana alijua ni mtoto wake ndiye alimuua Santo kwa kumgonga na gari.
“Bila mimi asingeweza kugongwa na gari. Tulikuwa tunataniana na mwanangu hapa ndani, nisingeinuka na kuanza kumfukuza wala haya yasingetokea. Hivi ni gari ya nani imemgonga?” alisema na kumalizia na swali!
Mama Juddy alisita kidogo kujibu swali hilo, akawatazama majirani zake kuwaashiria wamjibu. Wote walionekana kusita kujibu hali iliyomfanya mama Tonny kurudia kuuliza.
“Ni nani aliyemgonga Santo?”
“Kagongwa na kaka yake, Bap!” mama Juddy hatimaye alisema, huku akimshika mkono mfiwa katika namna ya kumtuliza.
“Nani? Bap? No!” Mama Tonny alijikuta akisema kwa sauti iliyowashtua wote waliokuwepo sebuleni.
Ghafla akainuka, akakaa katika mkeka, akamtazama shoga yake mama Juddy, akamuegemea na kujikuta akiangua kilio kwa sauti huku akizungumza maneno yasiyoeleweka!
.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
***
Nje, chini ya mti, watu kadhaa walikuwa wamekaa wakizungumza taratibu. Kila mmoja alikuwa na majonzi, wakiomboleza msiba wa ghafla wa Santo, kijana mdogo aliyekuwa na umri wa miaka tisa tu!
Mzee Linus alikuwa amejiinamia, kichwani mwake akiwaza mambo mengi, kifo kile cha kijana wake kilimuumiza sana, lakini alimshukuru Mungu kwa kila jambo. Kama aliyekumbuka kitu, akamshika mkono mzee Komba na kumnong’oneza jambo!
Mzee Linus alikuwa amejiinamia, kichwani mwake akiwaza mambo mengi, kifo kile cha kijana wake kilimuumiza sana, lakini alimshukuru Mungu kwa kila jambo. Kama aliyekumbuka kitu, akamshika mkono mzee Komba na kumnong’oneza jambo!
SASA ENDELEA…
“Kaka!”
“Niambie,” Mzee Komba alimuitikia rafiki yake, kichwa chake kikiwa na mawazo mengi.
“Hivi nini kitatokea kwa Bap?” aliuliza tena
“Kivipi?” naye akajikuta akiuliza.
“Hii kwake itakuwa ni kesi ya mauaji au kitu gani,?”
“Sidhani, ni traffic case,” alisema mzee Komba.
“Ila itabidi lazima tumwambie Bap, tabia yake ya kuendesha gari kwa kasi si nzuri, atamgonga mtu sehemu wasiyomfahamu, wanaweza kumfanyia kitu kibaya sana,” alisema mzee Linus.
“Kila siku ninamkataza, lakini hasikii. Kuna wakati niliamua hata kumzuia kuendesha gari, lakini nikashindwa, hebu tumuache, tuamini kwamba atabadilika mwenyewe, hasa baada ya tukio hili.”
“Lakini hatujafuatilia Polisi, nini kimemtokea?”
“Amewekwa mahabusu, katika jambo kama hili, hatuna sababu ya kuhangaika hivi sasa, hebu hili tulijadili kesho, mwache alale leo,”
Watu wakaendelea kujaa pale nyumbani kwa mzee Komba, msiba ulikuwa wa ghafla sana. Mama yake Tonny baada ya kuambiwa aliyemgonga na kumuua mwanawe ni Bap, akili yake ikachanganyikiwa. Mambo mengi yalipita kichwani mwake, akajikuta akihusisha tukio hilo na kile kilichotokea mwaka mmoja na nusu uliopita!
“Atakuwa amefanya makusudi?” alijiuliza, lakini sauti asiyoifahamu, ikamtaarifu kuwa ni bahati mbaya, naye kwa moyo mkunjufu kabisa, akainua mikono yake juu akimshukuru Mungu na kumuombea Baptist!
Baada ya kuwasiliana na ndugu zake wa karibu ambao walikuja msibani pale siku ile ile, mzee Komba akawatangazia majirani na waombolezaji wengine kuwa mazishi ya mtoto wake yatafanyika siku tatu baadaye, wakisubiri watu wengine waliokuwa nje ya Dar es Salaam wafike. Hakutaka kwenda kumzika mtoto wake nyumbani kwao Mbinga, alitaka azikwe Dar kwa kuwa ndipo yalipo maisha yake!
Asfat aliwasili Dar es Salaam saa tano na nusu asubuhi, akakodi teksi iliyomtoa uwanja wa ndege wa Julius Nyerere na kumfikisha Nakasagwe saa saba mchana. Alipokelewa kwa vilio kutoka kwa ndugu, jamaa na marafiki. Baada ya kuingiza begi lake chumbani kwake, akaingia bafuni na alipomaliza kuoga, akamfuata mama yake na kumuomba waongee kidogo.
Wakatoka nje kabisa ya nyumba, ambako watu walikuwa wametapakaa. Wakatafuta eneo la peke yao, wakakaa chini ya matofali na kuanza kuzungumza. Asfat akamtaka mama yake amueleze ukweli juu ya tukio lile, kwa sababu alimwambia wazi kuwa yeye binafsi, haamini kama ile ilikuwa ni ajali kama ajali zingine.
Mama akamtazama, macho yake yakaanza kujaa machozi, akajifuta kwa khanga aliyokuwa amejifunga na baadaye akamwambia;
“Hata mimi mwanzo nilikuwa na mawazo kama yako, sikuamini mara moja, lakini kadiri nikirejea tukio zima, sioni ni wapi Bap alikusudia. Kama kuna mtu wa kumlaumu, nilaumuni mimi, nisingemfukuza, asingetoka nje.”
Kwa mara nyingine, Asfat akakubali, lakini hakuridhika!
Baada ya kumaliza mazungumzo hayo, akarejea chumbani kwake, akaikumbuka albamu yake ya picha, akaichukua na kuanza kuziangalia picha zake, zikiwemo za zamani enzi za utoto hadi ukubwani.
Akakutana na picha aliyoipenda sana, alikuwa amepiga na marehemu Juddy, wakati flani wa sikukuu ya Krismas, miaka kadhaa iliyopita, aliipenda picha hiyo kwa vile ilimkumbusha mambo ya siku hiyo, ambayo hawezi kusahau.
…
Ni siku ambayo alimjua mwanaume kwa mara ya kwanza. Alifanya tendo hilo katika vyoo vya ukumbi wa disco, katika ufukwe wa Coco, jijini Dar es Salaam.
“Ninahitaji kuongea na Festo,” alijisemea mwenyewe, akimkumbuka mvulana ambaye alifanya naye kitendo hicho, ambaye walikuwa bado wakiwasiliana, ingawa urafiki wao wa kimapenzi ulikuwa umefifia sana!
Festo baada ya kumaliza shule, alienda India kusomea udaktari, mara ya mwisho walipowasiliana, ni wakati alipompigia simu akiwa Mumbai, akimtaka ampokee uwanja wa ndege wa Heathrow, jijini London alipokwenda kwa shughuli zake. Hiyo ilikuwa mara yake ya kwanza kufika Uingereza na hakutaka kuhangaika. Alimpokea na kumwelekeza sehemu anayoweza kufikia.
Baada ya hapo waliwasiliana tu kwa simu hadi Festo aliporejea Dar es Salaam na kuajiriwa katika hospitali ya Taifa Muhimbili. Asfat akaitoa simu yake ya mkononi, akatafuta jina alilolihitaji, alipolipata akabonyeza kupiga.
“Mambo?” Asfat alizungumza mara baada ya upande wa pili kupokea.
“Poa, umekuja lini mbona kimya kimya,” upande wa pili nao ukajibu.
“Nimepata msiba ghafla, mdogo wangu Santo amefariki juzi kwa kugongwa na gari,”
“Dah, pole sana aisee, mipango ikoje,”
“Tunategemea kuzika keshokutwa hapa hapa Dar,” alisema Asfat.
Baada ya kimya kidogo kupita, Asfat akarudi tena simuni.
“Festo, nina shida sana ya kuonana na wewe, ni muhimu sana katika maisha yangu kwa kweli,”
“Nitakuja msibani kesho, tutaongea.”
.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Hapana, sitaki tuzungumzie huku, iwe sehemu nyingine,” Asfat alisema na kumfanya Festo ahamishe hisia zake, akadhani mwenzake alihitaji mazungumzo ya kimapenzi.
“Wapi sasa, hoteli?” akajikuta akiuliza.
“Hapana, sehemu tu tulivu, ninahitaji kuongea na wewe, nina ishu ya muhimu sana kwangu,”
Baada ya kujibishana kwa muda wakakubaliana siku na muda wa kuonana!
Shughuli ya msiba iliendelea, maneno ya hapa na pale yaliendelea kama kawaida ya misiba ya uswahilini. Kwa muda wote, mama Juddy hakubanduka karibu na mama Tonny, alikaa naye na kumfariji kwa kila kilichoendelea. Hali kama hiyo pia ilikuwa kwa mzee Linus na rafiki yake mzee Komba.
Watoto wa familia zote nao walikuwa kitu kimoja, hakuna mtu aliyeonyesha tofauti. Walishirikiana kama kawaida hadi msiba ule ukaonekana wa familia zote.
Hatimaye mazishi yakafanyika katika makaburi ya Nakasangwe, karibu kabisa na sehemu aliyozikwa Juddy, mwaka mmoja na nusu uliopita. Wiki mbili baada ya mazishi hayo, maisha yaliendelea kama kawaida.
***
“Ndiyo hivyo Festo, nataka kulipiza kisasi, nisaidie jinsi ya kuipata hiyo sumu,” Asfat alimalizia kwa kumwambia mpenzi wake wa zamani, baada ya kumweleza mkasa wa familia zao na jinsi ambavyo hakuridhishwa na kifo cha mdogo wake, akiamini Baptist alifanya makusudi.
Walikuwa wamekaa pembeni katika ufukwe wa Kawe, wakiwaangalia watu mbalimbali wakipunga upepo na kuogelea.
Asfat alitaka kulipiza kisasi kwa kumuua ye yote katika familia ya mzee Linus, ilimuuma sana.
“Hapana Asfat, siwezi kukusaidia kutimiza lengo lako, sisi tumeapa kumsaidia mgonjwa na siyo kummaliza, isitoshe, kwa jinsi watu walivyokuwa wakizungumza siku ile pale msibani, inaonekana kabisa ni ajali,” Festo alimwambia Asfat, aliyetoa macho kwa mshangao.
.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment