Simulizi : Hila
Sehemu Ya Pili (2)
TATIZO moja kubwa ambalo huwagharimu wanawake pindi wawapo na ghadhabu ni kuamini kuwa kila kitu wanachofanya wanakuwa sahihi. Na wakiwa katika katika hali hii mara nyingi huwa wakubwa wa siri na wavivu wa kushirikisha mtu juu ya mambo yao. Labda mwanamke mwenzake tena walioshibana.
Ni hiki mkilimsibu mama Tina, akiwa kama mwanamke mwingine tena mwenye mapenzi ya dhati kwa mtoto wake aliyekuwa hajulikani alipo baada ya kukamatwa na polisi.
Alipokea simu ileile ambayo Sam alidai kuwa yawezekana ni Tina atakuwanayo, ajabu hakuzungumza Tina walizungumza wanaume na kumwelekeza mama Tina mahali ambapo Tina yupo, aende na pesa kwa ajili ya kumchukua.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Pesa yenyewe ya kukodi teksi tu! Ajabu.
Bila kuishirikisha akili yake vyema, mama Tina akamshirikisha mdogo wake wa kuishi naye, wakaondoka huku ndani ya teksi wakimnanga Sam kadri walivyoweza, wakafikia hatua ya kumwita mwanaume suruali asiyemjali mchumba wake.
Walipokelewa eneo husika maeneo ya Koko, majira ya usiku.. bado watu walikuwepo katika hoteli wakipata vinywaji na chakula.
Mama Tina akaombwa aingie peke yake ndani na yule mwanamke mwingine akabaki kumsubiri nje!! Akiahidiwa kuwa atarejea na Tina baada ya dakika chache, mama Tina akaingia kichwakichwa!!
Muda mchache ukawa muda mwingi, saa zima likazaa saa la pili na la tatu. Baridi likamzidia yule mwanamke na kujikuta akizidiwa na uvumilivu, akaamua kupiga simu….
Simu ya mama Tina ilikuwa inaita tu bila kupokelewa. Aliendelea kupiga bila mafanikio. Hatimaye akaamua kuingia ndani ya hoteli kumtafuta.
Bado hakufanikiwa kumuona, hadi pale aliposikia kelele za kuhamasishana juu ya jambo Fulani la hatari. Akavutika kwenda kupoteza muda katika tukio hilo wakati huo akimsubiri mama Tina.
Kama alidhani anaenda kupoteza muda haikuwa hivyo…..
Alikuwa anaenda kushuhudia mwili wa mama Tina ukiwa hauna uhai wowote ule.
Mwili ulikuwa sehemu ileile ambayo Sam aliagizwa kwenda kuchukua kadi ya simu na mtu ambaye aliamini kuwa alikuwa ni teja.
Utata ukaendelea!!!
UKUNGU uliyatawala macho yake na kumfanya aone maumbo kadhaa yakiambaa katika ukungu ule katika namna ya kukera, alijaribu kuyapikicha macho yake na hapo akasikia miungurumo ya ajabu ajabu.
Ule ukungu akajiaminisha kuwa ni mawingu na ile miungurumo basi akaona kuna kila dalili ya mvua.
Mvua inataka kunyesha halafu nimekaa nje? Alijiuliza katika nafsi yake, kisha akaulazimisha mwili wake uweze kunyayuka aweze kuondoka eneo lile kujiepusha na mvua kubwa iliyokuwa inataka kumwagika.
“Pumzika Sam, subiri usisimame!” sauti zilizokuwa za miungurumo zikazungumza na akasikia vyema.
“Mungu wangu? Mawingu yameniita jina langu….au malaika?” alijiuliza lakini safari hii kwa sauti ya kukwaruza kidogo. Wakati huohuo akiendelea kunyanyuka….
Mara akaguswa begani, akashtushwa na kitendo kile akajipapasa begani mara akakutana na kiganja cha mkono.
Sam akapagawa na kuanza kupiga kelele!!
Ni katika patashika hiyo alijikuta akiona vyema mbele na wala hapakuwa na mawingu bali umati wa watu ulikuwa umemzunguka.
Sura kadhaa alikuwa akizitambua lakini kuna sura moja aliitambua zaidi.
“Sam mwanangu ulipoteza fahamu hukoo mjini, kuna wasamaria wema wamekuleta hapa….. pole sana” ilikuwa sauti ya Mama Lao!!
“Nini? Nilianguka, hapana hakuna kitu kama hicho mama…hakuna kabisa nasema sijaanguka mimi…” alipinga Sam huku akijisikia fadhaa kuwa amekaa chini huku amezingirwa na umati.
“Dah! Maskini wee! Sijui hata kama ataelewa huyu….” Kijana mwingine alilalamika pembeni huku akimwonea huruma Sam.
Sam aliamua kuituliza akili yake bila kusema lolote, akayafumba macho yake na kujilazimisha kukumbuka mara ya mwisho alikuwa wapi kabla hajarejeshwa nyumbani kwake bila kujitambua. Akili ikafanya kazi yake ipasavyo, akakumbuka kila kitu.
“Nooo! Noooo! Sikuzimia, walinichoma na kitu kama pini hivi eheee! Nimekumbuka ni kitu kama sindano, hapa begani, mh! Hivi ilikuwa begani ama shingoni….. ni..be….aah! ilikuwa shingoni….. wajinga sana wale jamaa wameniteka wale, hata siwajui maskini nimewakosea nini mimi eeh! Nimewakosea nini sasa….wamemchukua Tina wangu….na mama na mama wame…. Whaaaat! Mama amekufa?” Sam alihangaika huku na kule akitoa maelezo ambayo yaliwathibitishia watu kiuhakika kabisa kuwa mtu aliyepoteza fahamu, akirejea katika fikra zake za awali huwa anaweweseka.
Wakadhani kuwa hata Sam alikuwa katika kuweweseka!!
“Anko Sam, ingia ndani upumzike, haupo sawa?”
“Nini? Sipo sawa, sipo sawa natambua kuwa huyu ni mama lao, mama anayelisha mtaa mzima kwa tusiokuwa na familia, huyu hapa mama Khadija na Khadija wake anasoma kidato cha kwanza hapo Makongo, huyu naye sio baba Hamadi, na huyo Hamadi wake si ndiyo yule anayetaka kuwa mtangazaji…. Mnataka nitaje mtaa mzima nd’o mfahamu kuwa nipo katika timamu zangu…..sijachanganyikiwa narudia kusema kuwa nilitekwa baada ya kuchomwa na kitu chenye ncha kali katika bega langu la kuume, na wakati yanatokea haya nilikuwa nimepokea taarifa kuwa mama mkwe wangu amepoteza uhai. Naitwa Samwel Mbaule na nipo katika akili yangu….naomba niaminike!!” Sam aling’aka kwa ghadhabu na kwa kitendo chake cha kutambua watu waliokuwa mbele yake kiliwafanya wote waanze kuamini kile alichokuwa akikisema.
“Simu yako hii hapa… hao wasamaria wema walisema tukupatie ukizinduka…” jirani mmoja alizungumza huku akimkabidhi Sam ile simu.
Sam alicheka kwa kujilazimisha, cheko la karaha….
“Eti wasamaria wema, mabaradhuli wakubwa wale wananionea bure tu…wananionea tu…” alilalama huku akiichukua ile simu, akasimama na kuwashukuru wote waliompokea akiwa amepoteza fahamu, kisha akafungua mlango wake na kuingia ndani ya chumba asichokuwa na imani nacho.
“Mmeweka tena madawa ya kulevya nyie paka shume waonevu wa kukwapua samaki mdogo wa mama mjane maskini…wekeni tena nitavuta na kuzimia tena. Naona mna lengo la kunisababishia niwe na kifafa…endeleeni lakini Mungu aliye hai ananipigania…. Na wakati unakuja hamtaweza kunizimisha tena bastard!!” alikaripia Sam huku akiamini kuwa ujumbe ulikuwa unafika.
*****
Baada ya kujimwagia maji na kuuweka mwili wake katika uchangamfu tena, Sam aliitwaa simu aliyokuwanayo, lengo lake likiwa moja tu. Wazo ambalo alilipata akiwa bafuni, kuwa ukitambua kundi fulani linakushinda basi ungana nao ili wote muwe washindi!
Sam alijiuliza maswali mengi na kuamini kuwa lile kundi linalomwandama lilikuwa likishabihiana na kifo cha Steve Marashi. Hivyo wakimtambua muuaji wa Steve iwe isiwe wataachana naye na hata Tina atarejeshwa mikononi mwake.
“Nyie majamaa…..” alianza kuzungumza kwa sauti akiamini kuwa mle ndani kuna vinasa sauti na lazima watamsikia tu….CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Nyie majamaa mnadhani namjua muuaji ama mimi naweza kumuua rafiki yangu Steve….mnanikosea sana heshima kwa hilo….mnanitesea bure Tina wangu na mama mkwe wangu mmemuua amakweli mmeamua kunionea….sasa sikilizeni humu katika simu kuna mtu alijitambulisha kama muuaji wa Steve na hadi sasa sijajua ni nani…jina lake lilihifadhiwa kwa herufi tatu ‘SLM’….Sikieni sasa hii ni simu ya mchumba wangu….mimi nampigia huyu SLM ili mmsikie wenyewe ni kwanini anasema kuwa anasingiziwa kumuua Steve. Msikie kama atanitaja mimi sasa….” Sam alisita. Akaichukua simu na kuanza kupekua jina lililohifadhiwa kwa herufi zile ambazo zilikuwa zimenasa katika kichwa chake kutokana na zile meseji kadhaa alizotumiwa na kuzifuta.
Sam hakuamini macho yake alipotafuta namba zile pasi na kufanikiwa…alitafuta kwa jitihada zote lakini bado hakufanikiwa!
Jina SLM halikuwepo tena katika simu ile!
Sam akayahisi macho yake yakichonyota, akaamini kuwa wale watekaji walikuwa wanazidi kumwona muongo.
Hatimaye akaanza kulia kama mtoto mdogo!!
“Mmelifuta jina…ni nyie mmelifuta washenzi wakubwa nyie.. mnamjua aliyemuua rafiki yangu…mnamjua na bado mnaniandama…ok! Njooni mniue na mimi..mumuue na Tina..mkamuue kila mtu, wanadhambi wakubwa nyie…” Sam akaporomosha maneno makali makali, kisha akajirusha kitandani kwake.
Hakika alikuwa amepagawa!
Alitamani kulala lakini usingizi ukagoma….
Ili kujinusuru katika utata huu, Sam akaamua kutafuta chcohote cha kuweza kumfariji na kumsahaulisha. Alikuwa amepanga kuwa jioni aelekee katika msiba wa mama mkwe wake huku akijiahidi pia kwenda polisi kupata taarifa juu ya kifo hicho.
Katika kupepesa macho akakutana na kikaratasi cha kuhifadhia santuri ‘CD’… akakitazama kile kikaratasi na hapo akakumbuka kuwa aliyempatia alikuwa ni marehemu Steven Marashi. Alimpatia santuri ile siku moja walipokutana akamweleza kuwa ilikuwa ni filamu yake mpya ambayo anatarajia kuitoa.
Sam akawasha runinga yake, akatia ile santuri ili aweze kujiliwaza na kumuenzi rafiki yake kipenzi.
Kama kawaida alitegemea kukutana na matangazo kadhaa ya filamu kabla ya filamu yenyewe kuanza. Lakini ajabu haya yote yalikuja lakini sio katika mfumo na nembo iliyozoeleka kuwa inasambaza kazi zake Marashi.
“Ah! Alihamia kampuni mpya ama…. Mbona hata siijui hii… Black Entartainment… ya wapi hii….” Alijiuliza Sam….
Mara akatokea Lili.
“Wacha wee alicheza na Lili, si alikuwa anazuga kuwa hataki kucheza naye filamu yoyote….nd’o maana akanipa kama Sapraizi eeh” akakaa vyema aweze kuitazama vyema ile filamu.
Mara ghafla mshangao ukahamia katika mshtuko, Lili alikuwa amevaa katika namna ambayo ni sawasawa na kuwa uchi tu.
“Nd’o maana haya ma Bongo muvi yao siyapendi….sasa nd’o kuvaa gani huku si uchi kabisa yupo?” alihamanika Sam…
Lakini hamaniko hilo halikudumu sana , zaidi likahamia katika kustaajabu. Lili akayageuza makalio yake kuelekea katika kamera na mara likatokea jambo ambalo lilimfanya sam ajikute anaziba macho yake.
Lili alibetua kitufe fulani katika nguo yake ambayo ilikuwa ni sawa tu na mkaa uchi. Lakini baada ya kubetua akawa uchi wa mnyama.
“Mama yangu weee!!....huyu si Lili huyu jamani….” Alijiuliza mwenyewe kisha kaangalia kushoto na kulia kama kuna mtu ambaye anaweza kumjibu.
Hakuwepo!!
Na alipoyarudisha macho yake kwenye runinga akamwona mwanaume akiwa uchi.
Hapa ukawa mwisho wa labda labda sasa ukawa ni uhakika.
Ile ilikuwa ni video ya ngono, muigizaji akiwa ni Lili wa Tanzania, lakini ile sura ya mwanaume haikuwa maarufu na Sam hakumtambua mara moja.
“Ni kitu gani hiki ulinipa Steve Marashi…ulimaanisha nini wewe eeh! Steve ulimaanisha nini, hebu kama haujafa kweli njoo uniambie nini ilikuwa maana yako we rafiki!! Njoo Steve…. Au…aaah! Hapana…” Sam alighafirika kweli.
Lakini hapohapo akasikia sauti ikiwaamuru Lili na mwenzake kulianza tendo.
“Stand by……..ACTION!!!” iliamrisha sauti ile ya kiume.
Kijasho kikaanza kumtoka Sam, masikio yake yalikuwa yameiskia sauti ya STEVEM MARASHI ikitoa amri!!
Amri ya Lili kuanza kucheza ile filamu ya ngono.
Kilichotokea baada ya hapo… Sam alilazimika kuzima runinga yake mara moja!!
Alikuwa amepagawa.
Nafsi moja ilimtuma kuufikisha mkanda ule polisi ikiwa ni kigezo namba moja cha wao kuanza upelelezi juu ya kifo cha Steve Marashi, lakini nafsi nyingine ikamsihi kuwa mkanda ule awapatie wale watu wabaya wanaomsumbua kila kukicha huku wakimmiliki Tina wake.
Hakujua ni wapi angewapata lakini aliamini kuwa wapo karibu naye na wanamsikia!!
Kabla hajapitisha maamuzi yoyote yale, mlango wa sebuleni uligongwa…. Upesi akakimbilia deki na kuitoa mahali ilipokuwa, akaificha chini ya uvungu wa kitanda.
Alipoufungua mlango alikutana ana kwa ana na mwanamke wa kazi, mcheshi na anayemzoea mtu kwa sekunde kadhaa tu.
Alikuwa ni MAMA LAO!!
Hakuwa na tabasamu usoni na ni kama kuna mambo mazito alikuwa ameyabeba na ilikuwa ni lazima ayatue.
“Karibu…” Sam alimkaribisha huku akiachia nafasi mlangoni mama yule akapenya. Sam akaufunga mlango na kisha kumkaribisha mama lao katika mojawapo ya sofa pale sebuleni.
Baada ya salamu na pole za hapa na pale.
Mama lao akamueleza Sam jambo lililobadili kila kitu katika kichwa chake huku likimwacha katika namna ya kukosa maamuzi kabisa!!
Huo ukawa mwendelezo wa utata!!!
Kabla hajapitisha maamuzi yoyote yale, mlango wa sebuleni uligongwa…. Upesi akakimbilia deki na kuitoa mahali ilipokuwa, akaificha chini ya uvungu wa kabati huku akiwa anatetemeka sana na jasho likizidi kumtiririka.
Kisha upesi akachukua kisu kidogo kilichokuwa mezani akakizamisha mfukoni, ili kama kuna hatari yoyote mbele yake akabiliane nayo.
Alipoufungua mlango alikutana ana kwa ana na mwanamke wa kazi, mcheshi na anayemzoea mtu kwa sekunde kadhaa tu baada ya kukutana kwao.
Alikuwa ni MAMA LAO!!
Hakuwa na tabasamu usoni na ni kama kuna mambo mazito alikuwa ameyabeba na ilikuwa ni lazima ayatue.
“Karibu…” Sam alimkaribisha huku akiachia nafasi mlangoni mama yule akapenya. Sam akaufunga mlango na kisha kumkaribisha mama lao katika mojawapo ya sofa pale sebuleni huku akilazimisha tabasamu hafifu midomoni.
Baada ya salamu na pole za hapa na pale. Mama lao akamueleza Sam jambo lililobadili kila kitu katika kichwa chake huku likimwacha katika namna ya kukosa maamuzi kabisa!!
Huo ukawa mwendelezo wa utata!!!
****
Baada ya kudumu kwa dakika takribani dakika mbili bila kuzungumza kilichomleta, hatimaye alishusha pumzi na kumweleza Sam madhumuni ya ujio ule.
“Vipi mama Lao! Na wewe ni mmoja kati ya watu wanaoamini kuwa nimerukwa akili? Umekuja kuhakikisha” Sam aliuliza katika namna ya kusanifu.
“Nilitaka kuamini awali….” Alijibu mama lao kisha akaketi vyema na kumtazama Sam moja kwa moja machoni.
“Ikawaje hata usiamini tena kama nimerukwa na akili mama…”
“Kwa sababu nahisi ni mimi ambaye nimerukwa akili….” Alijibu kwa kifupi mama lao kisha akamalizia, “Nilikutana na watekaji kabla ya tukio”.
Sam akajitoa katika kuegemea kochi na sasa akawa kama nusu anataka kusimama na nusu anataka kuendelea kukaa.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Nini…unamaanisha nini mama lao..”
“Walifika katika mgahawa wangu kununua supu, nilizikariri sura zao kwa sababu walikuwa wanaongea kinyakyusa na walikuwa wakizungumzia jambo ambalo nimeupata mwanga wake sasa baada ya kuhakikisha kuwa haujarukwa na akili….. walikuwa wakikuzungumzia wewe na kwa mbali kama walimzungumzia marehemu Steven Marashi japokuwa hawakumtaja jina lake moja kwa moja….”
“Sijakuelewa mama, wewe uliwaelewaje wakati wewe mzaramo?”
“Wengi sana ukiwamo na wewe mnatambua hivyo lakini mimi ni mnyakyusa, nadhani zaidi ya mama lao hata jina langu haulifahamu naitwa Sekela Ambindwile, lakini mama yangu alizoea kuniita Atuganile. Mbeya wakanifupisha na kuniita Atu….. naitwa Atu. Lakini endelea kuamini kuwa mimi ni mzaramo, napenda iwe hivyo kwa sababu zangu binafsi….” Mama lao alivuta pumzi kisha akazishusha na kuendelea.
“Hivyo, nilielewa kila kitu…. Kumbukumbu zimenikaa sawa baada ya kuwaona leo wakirejea na mwili wako na kudai kuwa wao ni wasamaria wema wamekuokota mbali. Kilichonivuta zaidi ni kauli yao tata kuwa hata eneo lile ni mara yao ya kwanza kufika. Wameelekezwa tu nyumbani kwako kwa sababu wewe unafahamika……. Mashaka yangu yakaanzia hapo.” Mama lao alijiweka sawa, Sam naye akazidisha utulivu zaidi, hakuamini alichokuwa anakisikia.
“Sasa wanataka nini kwangu eeh! Ni nini wanataka… nieleze mama lao nieleze niwapatie”
“Siwezi kusema kuwa nafahamu moja kwa moja lakini kwa maneno niliyoyasikia, nahisi hata wao hawana uhakika kama wewe ni mtu sahihi kwao…. Wanachofanya ni kubashiri tu……na inaonekana wameagizwa” alijibu mama lao. Sam akawa mkimya tu akipokea maneno yale mapya na mazito.
“Kwani wanakudai kitu gani Sam…”
“Sura zao tu sijui, nitajua vipi wanachotaka kwangu mama” Sam alijibu katika namna ya kughafirika. Mama lao akaligundua hilo.
“Lakini ukiachana na hayo ya kutokuwa na uhakika na hicho walichokuwa wakihisia kwako….. wale jamaa ni watu wa serikalini ama la wanafahamiana na mtu serikalini, kupitia mazungumzo yao nilisikia wakimtaja waziri wa ulinzi na waziri mkuu….. bila shaka jambo hili sio dogo.”
“Whaat! Waziri mkuu…. Mungu wee ni kitu gani sasa hiki…”
“Usirukwe na akili Sam, tulia sana kuna jambo hapa. Hivi wewe unaamini kuwa Steve amekufa hivihivi??” mama lao alimuuliza Sam ambaye alikuwa ameanza kuizoea ile hali baada ya taarifa.
“Hivi unaweza kuamini kuwa hadi sasa ninavyozungumza na wewe sijui rafiki yangu amekufa kifo cha namna gani?”
Mama lao alishangaa kwanza kabla ya kumweleza Sam kuwa Steven Marashi anasemekana ameuwawa na sio kuwa tu amekufa kikawaida. Mama lao akamweleza zaidi kwa ushahidi wa magazetini kuwa Steven Marashi alikutwa amekufa katika nyumba ya kulala wageni ambayo inasemekana alikuwa amelala na mpenzi wake ambaye inasemekana ametoweka, awali ikasemekana huyu msichana alikuwa ni Lili, mara vyombo vya usalama vikakanusha na kusema hadi sasa haifahamiki huyo mwanamke alikuwa ni nani.
Sam akaduwaa na kuzidi kuuona utata waziwazi.
“Lili yeye amesemaje juu ya shutuma hizi?”
“Lili hajasema lolote lile, simu yake haipatikani…. Nd’o magazeti yanavyosema. Sijui tu hiyo kesho itakuwaje…”
“Kesho kuna nini?”
“Nd’o anazikwa marehemu….. na raia wanataka kupata mustakabali juu ya kifo hicho cha ghafla cha kipenzi chao. Aliyehusika aadabishwe….” Mama lao alijibu huku akionekana wazi kuingoja siku inayofuata kwa hamu.
Waliendelea kuzungumza mengi juu ya utata huo.
Hatimaye wakaagana kwa makubaliano ya kukutana msibani siku inayofuata!!
Amakweli hakuna aijuaye kesho, hata yule mtunzi wa kalenda!!
Haikuwa nyepesi kama walivyopanga!!
*****
KIKAO kizito kilikuwa kimehitishwa katika ile nyumba ya siri mahali fulani nchini Tanzania.
Mwenyekiti wa kikao hicho alikuwa amewaka kwa hasira kali, kitendo cha jopo lake kushindwa kuambulia lolote lile kulimfanya aone ni uzembe wa hali ya juu japokuwa hata yeye mwenyewe hakujua ni kitu gani wanakitafuta kutoka kwa Sam.
Hiyo ilikuwa ni siku ambayo vijana wake wa kazi walikuwa wameleta mrejesho juu ya walichokuwa wakifuatilia. Na ilikuwa ni siku hiyo ambayo walikuwa wametoa vinasa sauti na kila kitu kilichokuwa kinahusiana na upelelezi wao ndani ya nyumba ya Sam.
Ni kama walivitoa wakati usiokuwa muafaka, hawakufanikiwa kutambua iwapo Sam alipata mkanda wa picha za ngono, na pia hawakuweza kuyanasa maongezi ya mama lao na Sam. Huenda hayo yangeweza kuwaletea mwangaza mkubwa sana na hatimaye na wao wakijue kile wanachokitafuta.
Bahati mbaya hata wao hawakuijua kesho yao!!
Baada ya mwenyekiti wa kikao kile muhimu cha siri kung’aka sana, mwishowe aliwapa nafasi ya mwisho ya kufanya wawezavyo, siku iliyofuata yaani siku ya maziko, wafuatilie hatua kwa hatua kuanzia mwili unavyotolewa mochwari hadi mipangilio ya kuaga na hatimaye kuzika waangalie iwapo wataambulia lolote la kuwasaidia kujua wasichokijua.
Wakaagana huku wakiingoja siku inayofuata, vijana wawili wa kinyakyusa wakalikamata jukumu lile katika mlengo mwingine, safari hii wakataka kubadili mbinu zao.
****
ULIKUWA ni msafara mkubwa sana kuwahi kutokea katika ardhi ya Tanzania. Wananchi walijaa barabarani, wengine wakiushangaa msafara wa kutokea Muhimbili na wengine wakiwa katika sura za majonzi kutokana na tukio la kumpoteza muigizaji wao mahiri.
Barabara ya Bagamoyo ilifungwa kwa muda ili kuruhusu magari yanayokwenda tu Magomeni na kuyazuia yale yanayoelekea Kariakoo yasifanye safari zake.
Ulinzi uliimarishwa pande zote za barabara, vilio vilisikika huku na kule na miale ya kamera ikiwaka bila kupokezana. Kila mmoja alitaka kupata picha ya tukio lile.
Ama kwa hakika lilikuwa tukio la kuteka fikra za yeyote yule!!
Msafara ulienda kwa mwendo wa taratibu huku gari kubwa la muziki likipiga nyimbo za kuwakumbusha wanadamu juu ya kujiweka tayari maana hawaijui siku wala saa.
Katika gari ndogo aina ya Corola, baba wa marehemu akiwa ameyaziba macho yake na miwani alikuwa katika tafakari nzito juu ya wimbi zito lililotanda katika kifo cha mwanaye. Alimini kabisa kuwa hakikuwa kifo cha kawaida bali cha kupangwa, na kuna sababu kadhaa alihisi zinaweza kuwa chanzo cha kifo kile.
Kubwa zaidi aliamini tangu siku ya kwanza ni kuwa kuna hila zimefanyika ili kuondoa uhai wa mwanaye.
Alitamani sana kuwa mkewe angekuwa muelewa tangu awali na kumzuia mtoto wao katika mambo kadhaa waliyodhani anaweza kuwa anajihusisha nayo, lakini mkewe akawa upande wa mtoto wake, akamuunga mkono kwa kila jambo hata yale ambayo yalionekana kuwa ya hatari kabisa.
“Yaani mama Steve ni mbishi huyu mwanamke!! Ona sasa mtoto amekufa anajifanya kugalagala na kuzimia kila mara anawasumbua tu watu, nilimwambia kabisa mapema kuwa tumkanye Steve….” Alilalama mzee Marashi kimyakimya huku akiwa amekamata gazeti mkononi mwake na asilisome.
Alipolitazama lile gazeti na kukutana na picha ya Lili alikumbuka mengi sana, akamkumbuka msichana yule na mengi waliyokuwa wamezungumza awali na hapo akawa amepata wazo la awali kabisa juu ya kifo cha mtoto wake.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Lili lazima kuna mambo kadhaa anayafahamu tu!!
Baada ya maziko nitamtafuta…..
Baada ya kauli ile alitoa miwani yake na kujifuta machozi kiasi machoni pake. Alipotaka kurejesha miwani machoni alishangaa kumuona dereva akiwa anahangaika na usukani, na hapo akasikia makelele mengi kutokea nje. Ile anageuka kutazama ni kitu gani kinatokea katika msafara wao akakutana na mpasuko mkubwa wa kioo ukiambatana na mlio mkubwa sana. Hakuweza kusikia jambo lolote tena.
*****
Edson Mayagi ‘Ninja’, alikuwa akimalizia kipande cha sigara yake wakati macho yake yalipokutana na namba za gari ambazo alielezwa kuwa gari mbili nyuma yake ndipo alipanda baba mzazi wa Steven Marashi. Upesi akakitupa kile kipande cha sigara, akajiweka tayari katika kutimiza alichokuwa ameagizwa kwa malipo makubwa.
Mapigo yake ya moyo yalikuwa juu sana, hakuamini kama ataweza kutoka salama ama ndo atakuwa amefanya kwa ajili ya familia yake ambayo ilikuwa imejazwa pesa nyingi sana kwa ajili yake. Hawakujua ni pesa kwa ajili gani bali walijazwa pesa tu!!
Ni Edson pekee aliyekuwa akilitambua hilo.
Palepale akafanya maombi kwa Mungu wake aweze kufanikisha alichopanga kukifanhya.
Na hapo akaliachia ghafla lori lililokuwa katika mteremko wa kuelekea Kariakoo, moja kwa moja likawa linaelekea katika gari aliyopanda mzee Marashi. Baada ya kuhakikisha kuwa lazima lori lile litajikita katika gari alilopanda Marashi, upesi akaruka na kujichanganya katika umati uliokuwa umetaharuki.
Amakweli Mungu wetu ni wa ajabu sana…. Sala za Edson zikasikilizwa akatoka salama, na mzee Marashi akaupoteza uhai palepale.
Kizaazaa kikaendelea!!
***
KIFO cha mzee Marashi kilizagaa upesi sana hata kabla mwili wa mwanaye haujaingizwa katika nyumba ya milele…… pande kadhaa zikakijadili kifo hiki katika namna wazijuazo. Huku wakisahau kabisa juu ya vifo vya raia wema wengine ndani ya ile gari.
Lakini tabasamu zito kabisa lilikuwa katika midomo ya mzee Matata, tajiri maarufu kabisa nchini Tanzania mwenye asili ya kiasia lakini aliyekifahamu Kiswahili vyema na aliyeijua Tanzania.
Tabasamu lile lilikuwa la mafanikio makubwa mno kutokana na kunyamazishwa kwa mzee Marashi kabla hajaropoka lolote lile.
Amani ikatawala moyo wake!!
Kwa upande wa wale vijana wawili wa kinyakyusa, walipagawa kutokana na tukio lile ambalo halikuhitaji jicho la tatu kutambua kuwa limepangwa maksudi kabisa kwa nia flani.
Nia gani? Hilo likawa swali zito kabisa ambalo lilizua utata mpya!!
UPANDE wa tatu ulikuwa na faida ya ziada, huyu alikuwa ni Sam. Ambaye alikuwa amejichanganya pia katika umati akifuatilia kwa ukaribu zaidi tukio hili ili aweze kupata mwangaza wa kitu gani kinachotokea katika ukungu huu.
Kama ilivyo kawaida ya waandishi, Sam alikuwa na kamera yake akirekodi vitu kadhaa bila kujua ni kwa nini alikuwa anarekodi.
Ni kawaida ya waandishi wa habari!!
Kamera ya sam ilivutika kumrekodi kijana ambaye alikuwa akivuta sigara kwa fujo, mara aimalize mara asiimalize, mara aizime mara aiwashe.
Sam akatambua kuwa mtu yule alikuwa na hofu kuu…..
Ana hofu ya nini sasa? Kuchelewa anapoenda, kukamatwa na trafiki ama? Sam alijiuliza peke yake huku akipendezwa kupata walau picha mbili tatu za yule bwana mfupi mwenye kichwa kikubwa kilichoongezewa ukubwa na nywele zake kichwani.
Macho yake hayakubanduka katika sura ya yule bwana, hata alipopanda garini alimshuhudia….
Awali alikuwa akipiga picha za mnato lakini wakati anabadili na kuamua kurekodi picha zinazotembea ndipo alipomshuhudia yule kijana akiliachia lori lake, Sam akazidisha umakini katika kamera yake akarekodi kila kitu na nzuri zaidi akainasa picha ya yule kijana akijirusha na kujichanganya kagtika umati wa watu.
Sam akaizima kamera yake na papo hapo akauhitaji msaada wa mtu katika kulifuatilia hili, hakutaka kujihangaisha na ile ajali, alitaka kumpata msababishaji wa ile ajali.
Angemuhitaji nani zaidi wa kuweza kumwelewa zaidi ya mama lao.
Kidogo aache klumshirikisha katika hili kwa kuhofia kuwa mama lao hawezi kuwa na msaada wowote ule. Lakini nafsi nyingine ikamweleza kuwa usikihukumu kitabu kwa kulitazama jalada lake tu…..ni heri kuzama ndani na kusoma kilichomo.
Sam akamvuta mama .lao kando na kumweleza kijuu juu kuhusu alichokiona, akamwelekeza mama lao ageuke nyuma aangalie chini ya mti fulani. Akafanya hivyo na kufanikiwa kumwona yule mtu mfupi mwenye kichwa kikubwa akiwa anavuta sigara na ,kupuliza moshi mwingi hewani.
“Una uhakika…..”
“Asilimia zote na nimemrekodi…”
“Twende…” mama lao akamwambia Sam na kwa mwendo wa kawaida kabisa wakalifikia eneo ambalo yule kijana alikuwa pale Sam alitangulia mbele kabisa na mama lao akabaki kwa mbali. Sam akahisi kuwa mama yule ni muoga kwa kitendo chake kile cha kusimama mbali.
Sam hakujua…na hakumjua mama lao….
Wakati akidhani kuwa ni jambo jepesi kufika na kumhoji yule kijana alikumbana na mshtuko baada ya kijana yule kufyatuka ghafla akitimua mbio baada ya Sam kufanya kosa kubwa kwa kujitambulisha kuwa yeye ni mwandishi wa habari.
Bahati ilikuwa mbaya kwa yule kijana kwani alikimbilia upande ambao mama lao alikuwa ametanda.
Ni huko alikutana na shubiri…..
Sam hakuamini macho yake……..
MAMA LAO ni kama alimchezea shere mhanga wake kwa kujifanya kuwa hamtazami na wala hana muda naye hivyo alikuja kwa pupa na alipompita sekunde kadhaa tu upesi Yule mama akafyatuka na kumnasa Ninja mguu wake wa nyuma. Ninja asiyetarajia lile jambo akapepesuka na kisha akatua chini kama mzigo.
Alipojaribu kusimama, Mama lao akawahi kumwamsha vyema kisha akiwa amemkwida shati lake vyema akampa shambulizi la kushtukiza. Akambamiza kichwa chenye uzito wa haja na palepale akapasuka vibaya sana.
Yule bwana akiwa amepagawa alijaribu kujitoa mikononi mwa mama lao lakini haikuwa kwa wepesi kama alivyoweza kudhani.
Mama lao alikuwa imara sana! Akamkata gwala akaanguka chini.
“Wewe ni nani na aliyekutuma ni nani? Jibu mara moja ama napasua makende yako” Mama lao alifoka huku mkono wake ukiwa ukiwa umezikama sehemu za siri za Ninja.
Yule mwanaume hakutegemea kujikuta katika suluba kubwa namna ile tena kutoka kwa mwanamke.
Sam alikuwa amepigwa na bumbuwazi, akili ilikuwa imesimama akishuhudia undava wa yule mwanamke, miguu ilikuwa mizito sana na akili ilikuwa imesimama.
Alikuja kushtushwa na watu ambao walikuwa wakishangilia ugomvi ule na yeye akaanza kupiga hatua kusogea alipokuwa mama lao.
Lakini kabla hajafika likatokea jambo ambalo lilizua kizaazaa kilichoitikisa Magomeni na kufunga barabara kwa muda mrefu sana.
Ukasikika mlio mkali sana wa bunduki, kikasikika kilio cha mama lao. Kisha damu ikatapakaa katika miili miwili iliyokuwa katika ugomvi.
Polisi waliokuwa eneo la ajali walitoa bunduki zao upesi na kuanza kuangaza huku na kule waweze kutambua ni wapi shambulio lile lilitoka. Lakini hawakuambulia kitu chochote…
Sam alipigwa butwaa miguu ikaishiwa nguvu, mwili ukamsisimka alivyotazamana ana kwa ana na lile dimbwi la damu. Huku mama lao na Ninja wakiwa wametulia tuli wakiwa wamekumbatiana.
Kwa jicho la harakaharaka la kibinadamu ungetambua kuwa hawakuwa na chembe ya uhai.
Sam, alitaka kuiruhusu akili yake ipagawe lakini akajionya na kulikumbuka lile angalizo alilopewa na yule bwana ambaye alimuwekea dhamana ya kimaajabu usiku wa manane.
Akakumbuka alielezwa kuwa awe makini!
Sam akajitoa ufahamu na kujifanya hamjui mama lao. Alijisikia vibaya kumsaliti yule mama lakini alitambua kuwa lile halikuwa tukio la kawaida na laiti kama angejiweka mbele lazima angejiingiza matatani, hasahasa akiikumbuka kamera yake ambayo ilikuwa na tukio la bwana Ninja kuunda kwa maksudi kabisa ajali ambayo sasa ilikuwa imeondoka na uhai wa mzee Marashi, baba mzazi wa Steven Marashi.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
***
MAJIRA yaa saa mbili usiku simu ya mkononi ilitoa mwanga kumaanisha kuwa kuna ujumbe ama simu inaingia, bwana Robert Massawe, mkaribu mkuu msaidizi wa jeshi la polisi aliitazama Katina namna ya kuvizia kana kwamba akiitazama upesi itazimika.
Hiyo ilikuwa ni simu yake ya dharula sana ambayo walikuwa wakiifahamu watu wachache mno. Ilikuwa kawaida ya bwana huyu ambaye alikuwa na miaka arobaini na tano kuzima simu zake na kutafakari kwa kina kila linapotokea tukio ambalo linatatanisha.
Alikuwa akiiacha wazi simu yake moja tu kwa ajili ya watu maalumu.
“Goddamn! Shit!!” alifoka baada ya kutambua mpigaji wa ile simu. Alijua kuwa mpigaji alikuwa na kawaida ya usumbufu, na usumbufu huu ulikuwa na chanzo chake. Alitamani sana asiipokee simu yake, lakini ilikuwa lazima aipokee.
“Naam! Mheshimiwa sana Matata…” alizungumza bwana Robert kwa nidhamu na sauti ya chini.
“Pole sana nimekusumbua ulikuwa umelala… niwie radhi bwana…” sauti ya mzee Matata ilizungumza na kisha akashusha pumzi kumsikiliza bwana Robbert.
“Usijali mkuu.. nilikuwa sijalala bado.” Alijibu kwa kuchangamka, changamko la kujilazimisha.
“Pole sana kwa matukio mfululizo yanayolitokea jeshi la polisi, hakika mnapitia kipindi kigumu sana katika hili….” Akavuta pumzi kisha akaendelea.
“Ehe! Nambie vipi nasikia leo kuna ajali imetokea na risasi zimerushwa huku watu wakipoteza uhai…”
Kauli hii ilimkera Robert, lakini ilikuwa lazima ajieleze kitu ambacho alijua wazi kabisa kuwa alikuwa anaukiuka utaratibu
wake wa kazi lakini angefanya nini mbele ya mzee Matata, tajiri ambaye analifadhili jeshi la polisi mara kwa mara.
Robert akamueleza mzee Matata kuwa kijana asiyefahamika jina lake amepigwa risasi kifuani na kufa palepale huku yule mwanamke ambaye alikuwa akipambana naye bila kujulikana chanzo akiwa amepoteza fahamu.
Mzee Matata akakata simu bila kuaga.
Ilikuwa kawaida yake!!
KILE kitendo cha mzee Matata kutawala baadhi ya mazingira katika idara mbalimbali serikalini ilimkwaza sana mzee Robert na kwa namna moja ama nyingine alihisi kuwa si jambo salama kabisa na linaweza kuzua madhara makubwa kwa serikali.
Mzee Robert alitamani sana kurudisha siku nyuma ili arekebishe yaliyotokea hapo zamani kidogo lakini haikuwezekana.
****
Mzee Matata alishusha pumzi zake kwa juhudi huku akiketi katika kiti chake cha kuzunguka. Akafanya mfano wa tabasamu na kisha akampigia kijana aliyeagizwa maalumu kabisa kwa ajili ya kufuatilia nyendo za Ninja aliyeagizwa kumuua mzee Marashi kwa ajali ya kukusudia.
Tabasamu lake lilinoga zaidi alipoifikiria shabaha ambayo kijana yule aliwahi kumfyatua Ninja baada ya kuingia katika mtafaruku usiojulikana. Ni hivyo alikuwa amemuagiza afanye iwapo Ninja atasukwasukwa na jambo lolote.
Mzee Matata alikikuna kipara chake, kisha akatoa cheko la dharau huku akiitazama picha ya mtukufu raisi iliyokuwa imebandikwa katika ofisi yake.
“Congratulation Mr President….” Akaisemesha ile picha iliyokuwa inatabasamu wakati wote.
Hakumkumbuka mama lao…..
Labda kwa sababu hakujua nini kilitokea!!!
****
Samwel Mbaule alitoweka eneo lile akiwa ametaharuki, mapigo ya moyo yalikuwa juu sana na alijihisi yu katika matatizo zaidi. Hakugeuka nyuma licha ya watu kadhaa ambao ambao awali walimuona akiwa na mama lao kumuita.
Sam aliingia katika bajaji na ghafla akajikuta akimwamrisha mwenye Bajaji ampeleke ofisi za gazeti la HAKI, ofisi ambazo alikuwa akifanya kazi pale.
Hakujua ni kwanini alifikiria kwenda huko lakini hakubadili maamuzi. Akaendelea kuamini kuna kitu huko ambacho kinaweza kumpa nafuu ya kimaamuzi.
Majira ya saa sita mchana alikuwa amesimama nje ya ofisi za gazeti lao. Mlinzi ambaye alikuwa amezoeana naye sana leo hii alionekana mwenye wasiwasi. Hata wakati anaandika jina lake kuwa ameingia ndani ya ofisi hizo, mlinzi yule alikuwa mkimya sana.
Hilo hakushtushwa nalo, akaingia mapokezi… ile anaonekana kwa yule dada wa mapokezi, macho yakamtoka pima yule dada na kujikuta akiliita jina la Sam zaidi ya mara mbili hovyohovyo. Sam akawa wa kushangaa tu….
Akamsalimia na kumpita, akafika ofisi kuu.
Wafanyakazi walisimama kufanya kazi wakabaki kumtazama yeye….. alifadhaika sana na kujikuta akishindwa walau kutoa salamu. Alijitazama iwapo alikuwa na mapungufu yoyote lakini hakuambulia kitu chochote kile katika mwili wake.
“Jamani, kwema?” alijikaza akasalimia. Lakini ni wafanyakazi wachache sana waliojibu tena kwa sauti ya chini mno.
Akataka kupuuzia na hapa ili aweze kukiendea kiti chake. Jicho likawa la kwanza kuwa shuhuda, hapakuwa na kompyuta katika meza yake. Kiti kilikuwepo lakini pia lilikosekana koti lake ambalo alikuwa analiacha ofisini kila siku.
Sam akapigwa bumbuwazi asijue ni kitu gani kinaendelea hadi ofisini.
“Jamani mbona… eeh! Mbona kiti changu sikielewielewi ndugu zanguni…” alihoji lakini hakupata jibu.
Kila mmoja alikuwa akimtegea mwenzake aweze kumjibu Sam, lakini hakuna aliyesema kitu. Walionekana kuwa waoga.
Sam, akaona kwamba kuendelea kushangaana haisaidii kitu, akaufungua mlango wa mwanamke wa makamo kabisa ambaye alikuwa akiwazidi wafanyakazi wote wa gazeti la HAKI na hivyo wakazoea kumuita bibi, hata jina lake halisi lilisahaulika.
“Shkamoo bibi…” Sam alimsalimia mwanamke yule ambaye alikuwa amejikita katika kompyuta akifanya kazi yake ya uchapishaji.
“Marahaba….” Alijibu bila kunyanyua uso wake.
“Bibi… ni nini kinatokea hapa… maana sielewi kitu.” Sam alihoji, na mara hiyo yule bibi akanyanyua uso.
“Astakha Firullah” yule mama alibinuka na kiti chake kurudi nyuma huku neno lile likimtoka kwa sauti yenye kitetemeshi. Sam akamsogelea zaidi na kumuuliza nini kinasababisha yote hayo.
Yule mama mtu mzima bado hakuweza kusema bali alikuwa anatetemeka tu.
Wazo la upesi limkamvamia Sam, akauendea mlango na kuufunga kwa funguo, hakutabasamu tena badala yake macho yake makali yakamtazama yule mama.
“Usiniue Sam usiniue” yule mama akajitetea huku hofu ikiwa imetanda waziwazi. Kauli ile ikamshtua Sam, lakini hakutaka kutetereka akaendelea kukazia.
Hatimaye yule mama akatoa maelezo huku akitetemeka. Akamweleza Sam jambo ambalo lilizidi kumshangaza.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Yule mama akamweleza Sam kuwa mkurugenzi wa kampuni yao aliwaeleza kwa kifupi kabisa kuwa wasijiweke karibu na Sam kwa sababu ni muuaji wa kutisha na anajihusisha na watu hatarishi sana. Pia amemuua Steve Marashi.
Sam alibaki mdomo wazi, akarudi kinyumenyume akaufungua mlango na kutoka nje, hatua kwa hatua akaufikia mlango na kutoweka bila kuaga.
Alipofika nje alijikuta asiyekuwa na uelekeo, aliyoyasikia ofisini yalikuwa yamemvuruga kupindukia.
“Sasa kama mimi muuaji mbona sikamatwi tena, mbona hata taarifa zangu sizisikii kwenye vyombo vya habari… hawa watu ni akina nani wanaotaka kunichafulia jina namna hii jamani….” Alijiuliza kisha akajiona yu yatima haswa.
Hatua kadhaa mbele akakutana na Bajaji, akapiga mluzi kumuita dereva mara akasikia mtu akiita jina lake. Akageuka na kumwona mtu akijaribu kumkimbilia, Sam akatambua kuwa atakuwa ni mfanyakazi mwenzake anataka kumuuliza maswali ya kipumbavu ambayo yanaweza kumkoroga zaidi. Akaingia ndani ya Bajaji upesi na kumuamuru dereva aondoe hakutaka kuzungumza na huyo bwana aliyekuwa akimuita, safari hii hakutaka kurejea nyumbani kwake moja kwa moja, bali alienda moja kwa moja nyumba ya kulala wageni. Akachukua chumba na kujipumzisha akiitafakari siku ilivyokuwa na mshikemshike na ni kwa namna gani ilikuwa inamalizika.
Hakumkumbuka mtu aliyekuwa akimuita!!
Amkumbuke ili iweje?
Alibaki kumuwaza Tina wake pamoja na ule mkanda wa ngono ambao hakuwa amemshirikisha mtu yeyote.
***
MAMA LAO ASAKWE AUWAWE!
KOSA kubwa walilolifanya polisi waliowekwa kumlinda Mama lao akiwa hospitali ni ile hali ya kumchukulia kuwa yeye ni mwanamke. Na pia kwa ile hali ya kuchafuka na damu waliamini kuwa alikuwa amejeruhiwa na walikuwa wakitimiza wajibu tu huku wakiamini kuwa yule mwanamke hawezi kuupata uhai wake tena. Hawakujua kuwa hakuwa amejeruhiwa na ile risasi bali ililengwa katika kifua cha yule kijana na kukipasulia mbali.
Kilichomzimisha mama lao ni ule uoga tu!!
Polisi hawakumfunga pingu, walimwacha huru wakati dripu zikipishana katika mishipa yake ya damu.
Majira ya saa nane usiku mama lao alirejewa na fahamu zake. Akatulia kwa muda bila kuweweseka, ikawa kama bahati kumbukumbu zake hazikuwa mbali sana. Akayafumba macho yake! Akabaki katika namna ileile ya kupoteza fahamu lakini akizivuta vyeama pumzi zake.
Alifanya vile ili kupata uhakika wa usalama wa eneo lile.
Ni bila kujua kuwa ile ilikuwa siku yake ya kuingia katika utata mkubwa zaidi maishani mwake. Baada ya takribani dakika thelathini tangu azinduke alisikia hatua za watu zikijongea katika chumba alichokuwa amelazwa.
Aliisikia sauti ikiwaelekeza kwa mbali juu ya kitanda ambacho amelazwa. Walikuwa wanaume wane.
Mama lao akafunua jicho lake kwa upenyo mdogo sana, akatazama kushoto kwa na hatimaye akaziona sura.
Mkojo ukapenya katika nguo yake, tumbo likaanza kumkata.
Alikuwa anaonana moja kwa moja na wanyakyusa ambao walimteka Sam na kisha kumrejesha akiwa amezimia, walikuwa ni walewale walio katika mtandao wa mawaziri kwa jinsi alivyowasikia siku walipoenda kula katika banda lake.
Akiwa hajalifumba jicho lake bado, aliwaona wanyakyusa wale wawili wakisemezana kikabila. Walikuwa wakipanga mpango wa papo kwa hapo na mara kila mmoja akagawana mtu wake, wakawatia kabali wale askari wawili na kisha kuwadunga sindano.
Waliendelea kuwadhibiti hadi walipolainika kabisa. Wakawachukua na kuwasukumia uvunguni mwa vitanda.
Kisha wakasemezana kinyakyusa tena, wakakumbushana juu ya maelekezo ya mkuu wao wa kazi. Kuwa kama yule mama yupo hai aondolewe pale hospitali na kisha auwawe na kama amekufa tayari basi mzoga uachwe hospitali.
Kijana mmoja akainama na kuyasikiliza mapigo ya moyo ya mama lao ambaye alikuwa akiendelea kujikojolea.
“Mzima huyu… si tumdunge na yeye sindano afe hapahapa au?” alimwomba ushauri mwenzake….
Kusikia hivyo mama lao akahisia anazikosa pumzi zake, mapigo ya moyo yakazidi kwenda kasi lakini hakutaka ajulikane kuwa amezinduka, lakini akajiapia kuwa wakitaka kumdunga sindano lazima aanzishe timbwili.
“Kaka eeh! Tufuate tulichoagizwa, hujui bosi ana maana gani aisee… je kama hizi sindano haziui mapema… hebu acha bwana mambo yako….” Mwenzake alimpinga.
Mama lao akaipata nafuu kidogo….
Mara mirija ikatolewa na yeye akabebwa mzegamzega. Akaendelea kujikaza asionyeshe dalili zozote za kuzinduka. Kwa sababu alijua kosa lolote lile litayagharimu maisha yake kabla hajaonana na Sam.
Ndani ya sekunde kadhaa akajikuta hewani kisha akatua katika kitu katika kochi, kwa ule mshtuko akajikuta amefumbua macho, bahati ilikuwa upande wake taa ilikuwa imezimwa katika ile gari ambayo ilionekana kama ya kubebea wagonjwa.
Na mara milango ikafungwa na gari likatoweka kuelekea mahali ambapo mama lao hakujua ni wapi.
Harufu ya kifo ikaziandama pua zake na waziwazi akatambua kuwa yupo katika dakika za mwisho za uhai wake.
Alijaribu kufikiri ni kitu gani atafanya kujiepusha na kikombe hicho lakini akili haikufanya kazi kabisa….
Akaamua kufanya sala zake za mwisho huku akijilaumu kwa kujiingiza katika mchezo asioujua sheria zake!!
****
MAJIRA ya saa mbili na dakika kadhaa Sam alikuwa akitembea kinyonge kuelekea katika nyumba ambayo alikuwa akiichukia. Ilikuwa ni nyumba ambayo aliishi kwa furaha sana wakati akiwa na Tina wake lakini ndani ya juma moja tu ilikuwa imegeuka chungu sana.
Alifika na kufungua mlango, mara akashtuka kuwa mlango ule haukuwa umefungwa na funguo.
Sam akajaribu kukumbuka iwapo wakati anaondoka alifunga mlango, hakulipata jibu, akili yake ilikuwa imechoka haswa na hakujali iwapo ni kweli hakuufunga mlango ama aliufunga kwa kutumia funguo.
Akaingia kichwakichwa akiwa ametawaliwa na uchovu. Akajitupa katika kochi sebuleni, akatazama huku na kule kisha akaingia chumbani. Akaondoa nguo zake kisha akaingia bafuni, akaanza kujimwagia maji.
Maji yale baridi kabisa yakampa uhai kidogo kiakili.
Alipojipaka sabuni akayafumba macho yake, ghafla shingo yake akahisi mlango wa bafuni ukifunguliwa, akataka kufungua macho ilihali ana sabuni usoni sabuni ikapenya machoni, akalazimika kufumba macho.
Na hapo ghafla shingo yake ikakabwa kabla hajapiga kelele za aina yoyote ile.
Sam alitapatapa huku na kule lakini shingo yake haikuachiwa.
“Sam….tulia….” sauti ilimnong’oneza kwa chini sana. Sam hakutulia badala yake alizidisha kutapatapa…. Ule mkono nao ukaendelea kumkamata.
“Sam ni mimi…. Tulia…” ile sauti ikanong’ona tena. Sam akaigundua kuwa amewahi kuisikia mahali.
Akatulia mara akainamishwa chini.
“Nawa!”
Sam akatii akanawa uso, sabuni ikamtoka.
Na hapo akajikuta yu bafuni, ana kwa ana na mama lao.
Sam akapigwa butwaa la mwaka kwa kimbwanga hicho.
“Usiongee…” Mama lao akatoa sauti ya chini sana. Sam akaukumbuka umakini alioonywa na mdhamini mtata wa usiku wa manane.
“Kwani..” akataka kuzungumza, mama lao akamziba mdomo.
Sam akajipa utulivu zaidi!
Mama lao akashusha macho yake chini, Sam naye akayashusha!
Ama! Alikuwa yu uchi wa mnyama… upesi akalirukia taulo lake na kujifunga.
Mama lao akatabasamu!! Kisha akamsogelea Sam na kumnong’oneza.
“Maisha yangu yapo hatarini sana, nimewatoroka wauaji, na walikuja hapa kwako pia…”
“Sielewi Mama lao…” alijibu kwa kunong’ona Sam.
“Wametega vinasa sauti…. Usiruhusu kabisa kuongea sauti ya juu! Wamekuja mara mbili ndani ya chumba chako…”
Mama lao akamsimulia Sam mkasa mzima juu ya tukio la hospitali, na namna ambavyo wauaji walijisahau baada ya kupata wanawake na kwenda kufanya nao uzinzi wakiamini mama lao amezimia.
Mama lao akaitumia nafasi hiyo kukimbia mahali asipopajua, hadi alipopata pikipiki iliyomfikisha nyumbani kwa Sam.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Sam sijui kama nitadumu sana katika kujificha lakini sikiliza kitu kimoja cha msingi, kuna mtu anaitwa BVB huyu ndiye aliyewaagiza wale wanyakyusa kukukamata wewe, na pia ni huyo BVB aliyemwagiza yule mwendawazimu kuiunda ajali na kumuua baba wa Steven Marashi.
Sam, amani na maisha yangu yapo mikononi mwako, mimi nitaenda Mbeya kwetu nitajificha huko lakini ni wewe wa kunifanya niwe huru tena. Tafadhali mtafute huyu BVB mfikishe mbele ya sheria. Simjui hata kwa sura lakini tafadhali kuwa makini kuanzia sasa… una jukumu zito sana nahisi hata Tina watakuwa wanamshikiria wao… halafu nimewasikia wakizungumza juu ya mkanda sijui ni mkanda upi” mama Lao aliongea katika sikio la Sam kwa hisia kali. Kisha akamkumbatia kwa nguvu.
Sam akayasikia mapigo ya moyo ya yule mama jinsi yalivyokuwa juu!!
Vita imeanza rasmi!! Sam akajisemea kisha akamwachia Mama lao na kupiga ngumi ukutani. Hasira ikachemka katika moyo wake, ule uoga akauweka kando na kuuvaa ujasiri.
Mama lao akamtia moyo kuwa ni yeye aliyeushika uhai wa Tina na kubwa zaidi alikuwa mwenye uwezo wa kuifichua siri iliyofichika.
Safari tatanishi ikaanzia pale!!
*****
ALFAJIRI sana Sam akafanikisha kumfikisha mama lao kituo cha mabasi, akapanda na gari na kuliacha jiji la Dar es salaam. Sam alisubiri hadi alipohakikisha basi limeondoka ndipo na yeye taratibu alianza kujivutavuta ili aweze kurejea maskani yake ya Temeke.
Kwa sababu ilikuwa ni asubuhi sana hapakuwa na foleni ambazo huleta kero ya kuishi katika jiji la Dar es salaam, hivyo ndani ya dakika zisizozidi arobaini tayari Sam alikuwa maeneo ya Tandika.
Aliposhuka akavutiwa na muuza magazeti ambaye nd’o kwanza alikuwa anakifungua kibanda chake. Sam akazuga kuwa kuna kitu ama mtu anamngojea pale, lakini nia yake ilikuwa kusoma vichwa vya habari vya magazeti ya siku ile.
Hatimaye yule bwana akaanza kuyatandaza magazeti katika meza yake.
Jicho la Sam likakutana na kichwa cha habari kikubwa kikifuatiwa na vingine vidogovidogo.
“Muuaji wa Steven Marashi aua askari wawili, amlevya daktari na kisha kutoroka mikononi mwa polisi”
Sam hakuwa na subira tena, upesi akamwomba yule bwana ampatie lile gazeti, akafanya malipo na bila kusubiri akafunua na kuisoma ile habari ambayo iliandikwa na mwandishi ambaye jina lake halikuwekwa wazi.
Habari ile ikawa inamzungumzia mama lao….
Kuwa ameua askari wawili na kisha kutoroka mikononi mwa polisi.
Sam akashusha pumzi kubwa sana akalikunja lile gazeti, wakati anaondoka akaliona gazeti jingine na kichwa cha habari, “GAIDI LA KIKE LAUA POLISI NA KUTOROKA”
Sam akafanya tabasamu la karaha na kisha akatoweka.
Akiwa njiani alikumbuka kuwa tayari alikuwa ametangaza vita rasmi tangu alipoambiwa na mama lao juu ya BVB. Japo hakujua hata hilo jina ni la nani lakini aliamini kuwa iwe isiwe atashinda hiyo vita.
Wazo la wapi pa kuanzia kumsaka huyo mtishia amani anayeitwa BVB lilikuja baada ya kutambua wazi kuwa kuna watu wenye nguvu serikali ama popote pale watakuwa nyuma ya kifo cha Steven Marashi, na kama wapo nyuma ya jambo hilo basi lazima kuna kitu watakuwa wanafahamu ama wanakihitaji.
Mkanda wa ngono! Sam akajaribu kuweka hili kama jibu lake sahihi…..
Mkanda huu unahusiana vipi sasa na Tina wangu, na kwanza yupo wapi? Maswali yaliendelea kumiminika katika kichwa chake.
Na alipomkumbuka Tina akazikumbuka siku njema za mapenzi yao, akazikumbuka ahadi tele walizopeana za kulindana. Sam akasimama kando ya barabara na kuegemea mti akayafumba macho yake. Akaikumbuka ile siku walipokutana ndani ya daladala, Sam akiwa anaumwa kichwa na bahati mbaya akawa amekosa siti ndani ya gari, mara akahisi mguso katika bega lake, alipogeuka macho yake yakakutana na sura ya Tina.
“Kaa hapa kaka yangu!” sauti ya Tina ikamweleza Sam wakati huo akimpisha kiti. Sam hakuamini kilichotokea, kupishwa siti na dada tena wa Dar es salaam?
Mara wakajikuta wanashuka kituo kimoja, Tina hakuwa mwenyeji eneo lile hivyo akajikuta akimuuliza Sam.
Ikawa zamu ya Sam kutenda wema, akampeleka hadi mahali alipokuwa anahitaji.
Safari yao ikaanzia hapo, urafiki hatimaye mapenzi. Walipotangaziana ndoa, yakatokea hayo ambayo sasa yamewatenganisha!!!
“Eeh! Mungu wangu mlinde Tina wangu huko alipo…” Sam akafanya dua fupi, kisha akaendelea kutembea huku akiwa amejipanga pa kuanzia.
Naam! Ilikuwa kama alivyopanga na ilikuwa hivyo.
Sam akiwa anatambua vyema kwa ushahidi wa Mama lao kuwa mle ndani kuna vinasa sauti vimetegwa, aliamua kuanza kucheza na akili ya adui yake.
Alipofika akajibwaga kwenye kochi, na baada ya dakika kadhaa akasikika akizungumza kwenye simu.
“Masu eeh! Usiuweke usiku, tukutane Sinza mida ya saa mbili nikupatie ule mzigo. Wao si wamemchukua Tina ngoja na mimi nilipue tu kila mmoja aumie kivyake, wajinga wananichukulia poa. Sasa wewe usipoteze muda tukutane Sinza Hotel, chumba namba kumi na nane….. jitahidi kujali muda, nazima simu.”
Sam akayamaliza mazungumzo hewa huku akitambua wazi kuwa alikuwa ananaswa sauti na wabaya wake.
Simu hii feki ikazua kizaazaa!!
****
WAKATI Sam anapiga simu ile hewa kuna makundi mawili sehemu mbili tofauti yalikuwa yametulia tuli kusikiliza anachokizungumza Sam, kila kundi lilipagawa katika namna ya kipekee.
Kundi moja lilikuwa katika ofisi isiyokuwa rasmi iliyokuwa imejazwa na wanausalama wa taifa wanne. Simu ile iliwapa tumaini na kisha kuwapa swali tena juu ya huyo Tina. Tina ni nani na amechukuliwa na nani, mwanausalama mmoja akamtambua Tina kama mchumba wa Sam. Na pia akazitambua taarifa za kupotea kwake ambazo zilikuwa vituo kadhaa vya polisi.
Hilo wakalipuuzia na kutilia maanani juu ya mzigo ambao Sam alikuwa akitarajia kumpa mtu wa kuitwa Masu, kwa jinsi walivyolinasa jina lake katika vinasa sauti.
Mkuu wa usalama wa taifa akampendekeza kijana wake mahiri kabisa katika kufuatilia kimyakimya, asiyeogopa kufa na asiyetambua nini maana ya kusamehe!
Yakubu Gama akapewa jukumu hili .
Na ni huyu ambaye aliagizwa kutega vinasa sauti katika nyumba ya Sam awali.
Gama alifikishiwa taarifa hii akiwa anajiandaa kuandika barua ya kuomba likizo, hivyo wazo la likizo likaishia palepale.
KUNDI la pili lilikuwa kundi la Mzee Matata, hawa waliipokea taarifa ile kwa shangwe hasahasa baada ya kusikia juu ya mzigo ambao Sam alikuwa akiumiliki.
Ni hili walikuwa wakilitafuta siku zote, na hata uamuzi wa kurudisha vinasa sauti katika nyumba ya Sam ulikuja baada ya kukosekana mtu mwingine wa kumhisi juu ya umiliki wa mzigo ambao walikuwa na mashaka nao tangu awali.
Mzee Matata akafanya tabasamu la ushindi baada ya kupokea taarifa zile, safari hii alikuwa na vijana wapya baada ya wale waliotorokwa na mama lao kuambulia kupigwa risasi na kupoteza maisha.
Akawapendekeza vijana wake wawili aliokuwa akiwaamini sana katika suala zima la kupeleleza.
John na Johnson ama walivyozoea kuitana ‘PACHA’.
Na hakika walikuwa pacha, wote walikuwa na roho mbaya, wote walikuwa wartefu waliojaa miili yao kimazoezi na kubwa zaidi wote walikuwa hawachoki kuua, inapobidi na wakati mwingine hata isipobidi.
Kwao kuua ilikuwa mojawapo ya burudani!!
Na ni hawa waliofyatua risasi kuwasambaratisha wale wanyakyusa wawili baada ya kutorokwa na mwanamke wa shoka MAMA LAO.
****
HAIKUWA saa mbili usiku kama Sam alivyoongea katika simu hewa. Badala yake ilikuwa saa tano asubuhi, akalipia chumba namba kumi na nane, akaingia katika kile chumba kisha akatoka baada ya kufanya alilopanga kufanya kwa umakini.
Alirejea majira ya saa kumi jioni akiwa amevaa miwani na kofia ya pama huku miguuni akiwa amevaa viatu maarufu kwa jina yeboyebo.
Ilikuwa ngumu sana kutambua kuwa yule alikuwa ni Samwel Mbaule.
Akajiweka mahali ambapo angeweza kumwona kila mtu aliyekuwa akiingia na kutoka ndani ya hoteli ile ambayo ilikuwa imejitenga mita kadhaa kutoka barabarani.
Nia yake ikiwa kumtambua adui yake ni nani aweze kuanza vita ya kimyakimya.
Vita ya kumwokoa Tina iwapo yu hai, na pia kumweka huru mama lao dhidi ya hila aliyofanyiwa na kisha kutangazwa kuwa ni muuaji.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Akiwa anakunywa soda yake taratibu, jicho lake liliendelea kuwa makini kabisa kutazama yeyote ambaye ataingia pale na kutoka walau atazame iwapo kuna sura anaweza kuifananisha.
Muda ulizidi kusogea lakini hakuambulia sura yoyote. Akaanza kukata tama huku akihisi mama lao hakuwa na uhakika wowote juu ya watu kuingia katika awamu mbili na kuweka vinasa sauti katika nyumba yake.
“Huenda mama lao alikuwa ameghafirika tu!!” Sam alijisemea huku akiimalizia soda yake ili aweze kuondoka na kuingia katika chumba kile alichokilipia.
Sam alisimama kinyonge kabisa huku kichwa kikimuuma, alijiona kuwa hana mbinu mbadala za kumjua adui yake kama ambavyo mama lao alimpamba kuwa anaweza kuwa.
Taratibu kabisa akafika mapokezi na kuchukua funguo za chumba chake. Akajiondokea huku akili ikimchemka vibaya mno.
Alipoifikia lifti alibaki akijiuliza ni kipi sahihi, kupanda ngazi ili apoteze muda ama apande lifti awahi chumbani bila kuwa na sababu yoyote ya kuwahi?
Wakati anajiuliza mara lifti ikafunguka na mtu mmoja akatoka, Sam akafikia maamuzi ya kuingia ndani ya lifti. Akaiamuru imfikishe ghorofa iliyokuwa na chumba chake.
Ndani ya sekunde kadhaa mlango ukafunguka kumaanisha kuwa alikuwa amefika eneo stahiki.
Taratibu Sam akaanza kuambaa katika korido ili aweze kukifikia chumba chake. Na mara akapatwa mshtuko mkubwa sana baada ya kusikia mlipuko mkubwa, si yeye tu bali wateja takribani wote waliokuwa vyumbani walikurupuka, wengine wakiwa uchi na wengine wakiwa na mavazi ya kulalia. Wanawake kama kawaida yao walikuwa wanalia kwa sauti za bila kujua ni kitu gani kimejiri…..
****
Alikuwa ni Yakubu Gama ambaye alikuwa wa kwanza kuingia katika chumba ambacho Sam alikuwa amekilipia kwa ajili ya kukutana na mtu hewa waliyezungumza naye kwenye simu.
aliingia katika chumba kile hata kabla Sam hajaingia na kutoka baada ya kukilipia. Hivyo wakati Sam anaingia hakuwa peke yake, Gama alikuwa yu ndani tayari.
Waliofuata kuingia katika kile chumba walikuwa ni PACHA kutoka kwa mzee Matata. Alitangulia John kisha Johnson, wakati huo Gama akiwa uvunguni. Nia yake ikiwa ni kutoka katika ficho lile punde baada ya wawili hao walioingia kukabidhiana huo mzigo, aliiweka sawa bastola yake vyema katika kiwambo cha kuzuia sauti. Kisha akaendelea kutulia.
Wawili wale ambao aliamini kuwa ni Sam na mwenzake (Masu) hawakuzungumza lolote badala yake walianza kupekua huku na kule kisha mmoja akaingia bafuni na hakutoka huko.
Gama akiwa uvunguni akabaki katika mshangao lakini hakupoteza umakini wake, akayakaza macho yake vyema bila kuruhusu mtikisiko wa aina yoyote.
Mara yule bwana mmoja aliyebakia akaingiza mikono yake uvunguni na kuanza kupapasa. Gama akawahi kuuondoa mguu wake ambao ungeweza kuguswa na yule bwana…..
Baada ya kupapasa mara yule bwana akainama uvunguni.
Ebwana! Macho kwa macho na Gama. Gama hakumwachia upenyo maana alijua tayari mambo yameharibika. Gama akafyatua teke, lakini kama ilivyo maaajabu… yule bwana akauondoa uso wake ndani ya nukta chache, Gama akajikuta amebutua teke kitanda.
Na palepale akawahi kujitoa uvunguni, lakini kabla hajasimama imara akajikuta akipokea teke kali sana usoni, akayumba lakini hakuanguka akajiweka imara akasimama wima.
Ana kwa ana na kipande cha mtu!!!
Gama hakuonekana kuwa na mwili wa kimazoezi, alikuwa mnene kiasi na anayeonyesha kuwa legelege, jambo hili lilimzubaisha Johnson. Akamchukulia Gama kuwa ni dhaifu, akamsogelea ili amkwide, lakini akakutana na pigo kali la karate katika shingo yake na kisha ngumi kali katika korodani zake.
Yule bwana mkakamavu akajikuta amelainika, hakika alikuwa amekutana na mtu kati ya watu!
“Pachaaa…” akapiga kelele za hofu baada ya kuona amezidiwa, na hizi zilikuwa kelele zake za mwisho kabla Gama hajafyatua ngumi kali iliyojikita katika shingo yake na kumtupa chini ambapo hakuwahi kuamka tena milele.
Wakati akipambana kuvuta pumzi za mwisho mara chumba kikavamiwa na Johnson, yule pacha ambaye alikuwa bafuni, hakuuliza swali akamvamia Gama kwa papara akamnyuka ngumi mbili tatu za harakaharaka. Gama akajituliza kwa umakini zaidi akamuhesabia hatua Johnson alipojisogeza tena Gama naye akafyatuka na kuanguka naye chini mzimamzima.
Akamkaba shingo kwa uimara kisha akamuuliza juu ya wapi ulipo mkanda.
Johnson hakujibu chochote kwa sababu alikuwa amepigwa kabali, Gama akalitambua hilo, upesi akamwachia na katika nukta iliyofuata akampiga ngumi nzito kwenye taya.
Johnson akajiharishia!!
Na hapo akakiri kuwa alikuwa anapambana na kiumbe wa ajabu kupita wote aliowahi kukutana nao katika maisha yake.
“Ni nani alimuua Steven?, Tina ni nani?, na mkanda upo wapi… “
“Sijui lolote mkuu, nimeagizwa tu…” alijibu huku akigumia kwa maumivu makali.
“Jina la aliyekuagiza.. upesi kabla sijainyonga shingo yako bwana mdogo…..” akatoa karipio kali Gama. Macho yake yakiwa mekundu na mikono ikiwa na tamaa kali ya kuua!!
“BVB”
“BVB ni nini maana yake.. upesi….” Alihoji huku akiikaza shingo ya yule bwana.
Hilo likawa swali la mwisho kabisa kuuliza kabla yule bwana hajafanya kitendo cha ajabu, akaanza kujinyonga nyonga kama anayeugulia tumbo. Na mara mlipuko mkubwa ukasikika.
Hapo ndipo kilipozuka kizaazaa!!
Gama akarushwa mbali kabisa na mlipuko ule.
Mlipuko ambao hakuutegemea katika mazingira yale!
Mlipuko ule ukawavuta watu waliokuwa nje na ndani ya hoteli ile akiwamo Sam.
Na hakuwa Sam pekee bali askari kanzu wapatao kumi waliomsindikiza Yakubu Gama wakaingia kazini.
Kwa papara kama kawaida yao!!
Utawajua tu kwa amri zao.
Wakatapakaa huku na kule, raia nao wakakimbilia eneo la tukio, Sam akaongoza mbio hizo akawa mmoja kati ya watu waliowahi kuwasili eneo la tukio.
Macho yake yakakutana na mwili wa Yakubu Gama katika chumba chake.
Sura na umbo havikuwa vigeni kabisa katika macho yake. Sam alijiuliza ni wapi aliwahi kumwona kiumbe yule, akaituliza akili na kujikuta akimkumbuka.
Alikuwa ni yule mwanaume aliyekuja kumwekea dhamana na kisha kumsihi awe makini. Dhamana ya maajabu ya usiku mnene sana.
Inakuwaje bwana huyo katika chumba chake? Ilistaajabisha. Na hapo akajipongeza kwa kujisajili kwa jina lisilokuwa lake wakati anaingia hotelini hapo. Kwani kwa tukio lile tayari ni kizaazaa kipya.
Sam akazidi kutambua kuwa lipo jambo ambalo limetanda katika mkasa wa kifo cha Steven Marashi na hata baba yake mzazi. Kichwani akajiwekea picha kuwa kuna pande zaidi ya moja zinawania mkanda ambao alikuwa anaumiliki!
Pande hizo ni zipi? Alijiuliza bila kupata jawabu!!
Katika purukushani za hapa na pale kabla polisi hawajaweka utando wao wa kuzuia raia kuingia ndani ya kile chumba, Sam alifanikiwa kukitoa kinasa sauti chake ambacho alikiweka baada ya kuingia katika chumba kile na kutoka majira ya saa tano. Kilikuwa kimewekwa katika godoro ambalo alikuwa amelichana na kisha kukitandika kitanda vyema.
Sam alizuga kuwa amesukumwa, akaangukia pale na kwa sekunde chache akaondoka na kile kifaa.
Wakati anaondoka alipishana na yule mwanadada aliyemwandikisha kuingia katika chumba kile. Yule dada bado hakuwa na uhakika kama yu sahihi ama la. Sam mwenye hofu akajikaza akaongeza mwendo.
“We kaka…” yule dada akajaribu kuita. Sam hakugeuka.
“Ni yeye jamani…” sauti ikasikika kama akiwaambia watu fulani.
Sam akawa ameifikia kona, akaanza kukimbia, akakata mitaa hapa na pale hadi akatokea Ubungo.
Jasho lilikuwa linamtoka haswa.
***
Taarifa za vifo vya mapacha wawili tegemeo kabisa katika ngome ya mzee Matata ilipokelewa katika namna ngeni kabisa na mzee yule, alikuwa amepagawa na hakutarajia hata kidogo jambo kama lile lingeweza kutokea.
Hakuamini hata kidogo kama Sam angeweza kukabilia na vijana wale machachari na kisha yeye akaibuka bingwa. Tena sio bingwa wa kawaida tu, bingwa aliyeua.
Upesi akachukua simu yake na kumpigia mzee Robert, mrakibu mkuu wa polisi.
Simu ilipokelewa kwa utulivu! Harakaraka na kwa papara kubwa Matata alianza kumuhoji Robert juu ya tukio lililojitokeza Sinza hotelini.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Kwani kuna tatizo gani mzee Matata ya nini kuuliza kila kitu kinachohusu usalama wa raia na hasahasa siri za jeshi la polisi. Samahani lakini kwa namna moja ama nyingine nashindwa kukuelewa mkuu….”
Bila kujibu chochote mzee Matata akakata simu.
Robert akabaki kutetemeka asijue mzee yule alichukulia vipi maelezo yale aliyompa. Lakini alifanya vile kwa sababu alilazimika kufanya, kwanza alikuwa amevurugwa sana. Matukio yalikuwa yanapangana, kabla hili halijaisha anasikia jingine likipanda juu yake.
Ilikuwa lazima achanganyikiwe na matukio yale yaliyozungukwa na utata.
Akiwa anaanza kusahau juu ya simu aliyozungumza na mzee Matata, mara simu yake ya mkononi ikaita.
Alikuwa ni IGP…..
Robert akaomba dua zote kabla ya kuipokea simu ile kwa sababu alimjua vilivyo mkuu wake wa kazi.
“Robby, hivi ungemjibu mzee Matata vizuri ni kitu gani kingekupungukia labda…… Robby, mzee Matata akiongea na mkuu wan chi ujue utaingia matatani.
Nisikilize Robby, wewe na mimi tunafahamu ni pesa kiasi gani mzee Matata ametoa ili kufadhili kampeni za chama. Unajua ni jinsi gani mzee Matata na raisi ni marafiki, chunga sana mdomo wako Robby, chunga sana inaweza kukugharimu, nimekusihi haya kwa sababu wewe ni mzazi na una familia kubwa… sitaki familia yako iteseke.
Nadhani unanielewa, sasa mpigie simu mzee Matata tena ni muda huu na umwombe msamaha….” Alihitimisha IGP.
“What? Ni nini hiki IGP… Msamaha kwa kuficha siri za jeshi letu mkuu…”
“Nimesema mwombe msamaha. Nimemaliza…” akakata simu IGP.
Robert Massawe akabaki kuitazama simu ile kana kwamba ina lolote la kumshauri ama inaweza kushiriki naye katika mshangao mkubwa aliokuwanao… lakini haikuwa hivyo. Simu nayo iliendelea kumtazama.
“Si bure…..” Robert alijisemea huku akiichukua simu yake na kubofya jina la mzee Matata.
Funika kombe mwanaharamu apite!! Alijisemea huku akiungoja upande wa pili uweze kupokea simu. Simu iliendelea kuita bila kupokelewa!!
*****
WAKATI simu ya mzee Matata ikiita, mzee huyu alikuwa ameenda mahali kujipooza hasira zake. Kitendo cha kukatiwa simu ya Robert alichukulia kama dharau kubwa sana kwake na tena ikiwa imefanywa na mtoto mdogo asiyekuwa na uwezo wa kutoa kauli yoyote mbele yake.
Mzee Matata alikifikia chumba alichokusudia akakifungua na kukabilia na sura iliyokuwa ikisihi huruma. Sura ya kike iliyopauka haswa na kuchubuka kutokana na kipigo.
Macho yake makubwa yalikuwa yamedumbukia ndani na midomo yake ilikuwa mikavu.
“Bitch! Huyo hawara wako anashirikia na watu gani?” Matata alitupa swali. Yule binti aliyezidi kusihi huruma kwa yale macho yake tu alijitahidi aseme lolote lakini akashindwa. Akabaki kulishika koo lake na hapo sauti ya kukoroma ikamtoka.
“Nina kiuuu…”
Hakika alikuwa ana kiu, kiu kikalikausha koo na kuondoka na ile sauti yake nzuri. Sauti iliyompagawisha Sam na kujikuta akiamua kutangaza ndoa kabisa.
Alikuwa ni Christina Elisha Prosper ama alivyozoeleka kwa wengi kama Tina!
Ile hali ya Tina kulalamika kiu badala ya kujibu swali aliloulizwa ilimghafirisha tena mzee Matata, akahisi anazidi kudharauliwa na watu wasiostahili hata kupita njia anayokanyaga yeye.
Mzee Matata akaondoka, sura yake ikiwa nyekundu akaingia bafuni na kutoka na ndoo iliyojaa maji. Akaifikisha katika chumba alichokuwa amehifadhiwa Tina.
“Inama unywe maji kisha unijibu…” mzee Matata akamweleza Tina kwa sauti iliyojaa upole. Tina akajisogeza kwenye ndoo na kuinama kama mbuzi. Akaanza kunywa maji.
Mzee Matata akamvamia pale pale kwenye ndoo na kukishika kisogo chake na kumzamisha kichwa kizima katika ile ndoo.
Tina alitapatapa akirusha miguu huku na kule, alivuta maji kwa pua na midomo. Akazikosa pumzi zake.
Baada ya dakika mbili mzee Matata akamwachia.
Tina akabaki kutapika huku na kule, akizisaka pumzi kwa jitihada kubwa, katika kuruka huku na kule mara akamtapikia mzee Matata katika mguu wake.
Yule mzee asiyekuwa na huruma akamnasa kibao kisha akamfyatua teke kali tumboni huku akimsindikiza na matusi.
Tina akatua katika kingo ya ukuta, uso ukabaki kutambaa sakafuni na maneno yasiyoelewekaeleweka yakimtoka.
“Sam anashirikiana na nani katika kikundi chake cha kijasusi??” alihoji mzee Matata.
“Sijui lolote…. Najua ni mwandishi tu…..” alilalamika Tina.
Mzee Matata akataka kumrushia adhabu nyingine ya teke lakini safari hii akaisikia simu yake ikiita.
Akaufunga mlango na kutoweka.
Akaipokea simu na kuupokea msamaha kutoka kwa Robert. Mrakibu msaidizi wa jeshi la polisi!!
Ile hali ya kuombwa msamaha ikampunguzia ghadhabu kidogo na kujiona mtukufu sana mbele ya watu wenye madaraka.
“Haya kijana…. Ni nani wale waliopambana na kuuana katika hoteli ya Sinza…” akamuhoji Robert kifedhuli.
“Wawili hawajajulikana majina lakini mmoja ni kijana wetu…” alijibu Robert huku akiuma meno yake kwa hasira.
“Na kijana wenu naye amekufa?” aliuliza.
“Haijathibitishwa bado lakini yupo mahututi hospitali ya jeshi Lugalo…”
“Ok! Vizuri ntakupigia baadaye nikihitaji kujua juu ya hali yake. Poleni na muwe na siku njema…” akaaga na kukata simu.
“****!” alifoka Robert huku akiibamiza meza iliyokuwa pale ofisini, akaituliza akili yake na kujiuliza juu ya yule mzee ambaye anatambulika nchini kwa biashara zake kubwa anazomiliki. Sasa kulikoni mambo hayo ya jeshi awe anayafuatilia kwa ukaribu kiasi hicho.
Lazima kuna kitu hapa!! Alijishauri, na kisha akajiapiza kutothubutu kufuatilia nyendo za mzee Matata. Hakutaka kuyapata matata!!
Akakumbuka maneno kadhaa ya IGP alipokumbushwa juu ya familia yake, hapo uoga ukamwingia.
Lakini hakuwa amejitoa katika vita na mzee Matata kama alivyodhania!!
Nd’o kwanza alikuwa anaikaribia.
***
SIMU yake iliyokuwa katika mfumo wa mtetemo iliunguruma mara tatu kabla mkewe hajamgutusha kutoka usingizini.
Robert Masawe alijinyoosha kidogo kabla ya kutazama kwenye kioo na kukutana na namba mpya. Hilo halikumshtua ilikuwa kawaida kupewa taarifa kadha wa kadha kutoka kwa wakuu wake ama wadogo zake kikazi kwa kutumia namba mpya.
“Jambo afande, CW00JT Lugalo hospitali..” alijitambulisha kwa namba yake na Robert akatambua kuwa kuna ujumbe anatakiwa kupokea.
“Endelea afande.”
“Kuna vijana watatu wanahitaji kumwona Inspekta Yakubu Gama….”
“Vijana? Vijana kutoka wapi?”
“Madaktari wameagizwa na mzee Matata!”
“Whaat? Madaktari, madaktari kivipi?”
“Sina nijualo zaidi ya kukupa hii taarifa afande..”
“Usiwaruhusu kwanza!” akaagiza na kukata simu.
Akatulia kitandani kwa sekunde kadhaa, mkewe naye akaketi kitako kuungana na mumewe. Hakutaka kumuuliza lolote, zaidi alibaki kumminyaminya begani kama namna ya kumfariji.
Robert Masawe, mrakibu msaidizi wa polisi aliitwaa tena simu yake wakati anataka kupiga mara ikaingia simu kutoka kwa mzee Matata. Robert akaruka sentimita chache kutoka katika kitanda, ni kama alikuwa ameona mdudu wa hatari.
Hakuipokea simu ile akaiacha iite hadi pale ilipokatika.
Na hapo Robert akampigia IGP.
“Jambo afande!” akasalimia. IGP hakujibu akaendelea kumsikiliza.
“Mkuu, Mzee Matata ameagiza madaktari kwa ajili ya Inspekta Yakubu Gama! Unayo taarifa hiyo?”
“Unawezaje kupata taarifa nzito kama hiyo kabla mimi sijaipata?” IGP akajibu katika mfumo wa swali kwa swali. Jibu ambalo lilimkera Robert lakini hakuwa na la kufanya.
“Lakini mkuu ulipaswa kunieleza kwa sababu vijana walio katika lindo wanatoa taarifa kwangu kama ulivyoagiza mkuu…”
“Kwa hiyo unamaanisha waanze kuripoti kwangu moja kwa moja?”
“Hapana afande!!”
“Waruhusu waingie nimezungumza naye, ametusaidia madaktari kutoka India wanusuru uhai wa Gama…. Wakati mwingine tabia yako ya kupenda kuuliza kila kitu siku ya siku utasababisha tukose misaada….” Akamaliza na kukata simu.
Super retendant Robert Masawe akapagawa!
Na hapo mkewe akaamua kuhoji kulikoni, Robert Masawe alijaribu kumkwepa mkewe lakini mwanamke yule hakukubali kabisa. Akakazia hadi Robert akasalimu amri akaketi kitako na kuanzia kumsimulia mkewe juu ya mkasa mzima unaoendelea.
Mkewe alikuwa makini sana kumsikiliza na baada ya maelezo yale, mkewe akatokwa na kauli ambayo bwana Robert hakuitegemea.
“Ukilala usingizi basi Gama atalala usingizi wa milele leo, pindi utakapoamka utakutana na lile neno kwamba jitihada za madaktari zilishindikana…. Hakuna madaktari hapo mume wangu, hao ni watu wabaya na hapo wanataka kumzimisha Gama ili asiseme ambacho amekigundua huko alipotoka…”
“Heh! Mke wangu umeyajuaje haya yote?”
“Nasoma sana riwaya mume wangu hasahasa za kipelelezi, wewe hupendi riwaya lakini zile za wakongwe zina mambo mengi ya kujifunza, mfano Mhanga wa ikulu ya Beka Mfaume, Mkimbizi ya Hussein Tuwa na Msako wa Hayawani ya Eddie Ganzel…. Naona wanayoyaandika nd’o kisa kama hiki, ukitaka kuamini we lala halafu asubuhi tutasimuliana…. Lakini uhai hautakuwepo tena. Gama atakuwa mfu!!”
Maneno ya mkewe yakamsisimua Robert licha ya kutokuwa na undugu wowote na Gama lakini alitambua kuwa nchi ilikuwa ikimuhitaji sana kijana shupavu kama yeye ili amani iendelee kuwepo huku waovu wakifikishwa mbele ya sheria.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Uzalendo ukajikita katika moyo wake, ujasiri ukajiunga naye upya. Akaona si sawa kumpoteza Gama katika namna nyepesi hivyo.
Alitambua kuwa vijana waliokuwa wameweka ulinzi kwa Gama wasingeweza kuwaruhusu wale madaktari kuingia katika chumba cha mgonjwa bila idhini yake yeye.
Pale pale akachukua simu ya mkewe akabofya namba za mmojawapo wa askari katika lindo la hospitali ya Lugalo ambayo alikuwa amehifadhiwa Gama.
Akamwambia asogee kando kabisa waweze kuzungumza.
“Naomba uende katika chumba alicholazwa Gama, kamtazame hali yake na ukiwa humo chumbani nipigie simu.”
Akamaliza na kukata!!
Yule kijana kama alivyoamrishwa akawapita wale madaktari ambao walikuwa wakingoja ruhusa, akaingia katika chumba alichokuwa amelazwa Gama.
“Hali yake bado si salama amepoteza fahamu bado..”
“Afande! Sina imani hata kidogo na hao madaktari, ni mimi nakueleza wewe tu na ujue wewe tu kwa sababu kanuni za jeshi kumtilia mtu mashaka ni nguzo kuu katika upelelezi. Hivyo nakuomba ufanye kitu kimoja…… ni cha hatari lakini nd’o inaweza kuwa salama yetu…. Wasiliana na daktari mmoja anaitwa Haji. Ni rafiki yangu sana kisha nipe nizungumze naye. Mengineyo nitakujuza.
“Sawa afande!” alijibu yule kijana kisha akatoweka.
Akafanya kama alivyoamriwa!
****CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment