Search This Blog

Tuesday, 14 June 2022

HILA - 3

 





    Simulizi : Hila

    Sehemu Ya Tatu (3)



    JOPO la madaktari wenye asili ya kihindi liliingia katika chumba cha ambacho Yakubu Gama alikuwa amelazwa. Walikuwa wameng’ara katika sare zao rangi ya bluu. Waliweza kuongea maneno machache tu ya kiingereza, asili yao ilikuwa uhindini.

    Baada ya kuingia katika kile chumba milango ilifungwa huku wakitoa agizo kuwa haruhusiwi mtu yeyote kuingia katika chumba kile.

    Askari wakabaki kufanya ulinzi!

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Baada ya milango kufungwa, daktari mmoja alitwaa simu yake na kupiga namba kadhaa, sekunde chache mbele simu ikapokelewa.

    “Tupo ndani ya chumba tayari!” alizungumza kwa kiingereza kibovu.

    “Kumbuka kufanya upesi na kwa usahihi kama nilivyowaeleza….”

    “Hakuna mashaka!”

    Akakata simu na kuwafanyia wale wenzake kama ishara!

    Wakakizunguka kitanda kama wakizungukavyo kitanda cha mgonjwa mahututi.

    Mgonjwa alikuwa ana majeraha makubwa ya kuunguzwa na moto na pia alikuwa amevunjika mkono na mguu.

    Naam! Gama aliyejeruhiwa katika mlipuko wa bomu.

    Wakamtundika mipira mingine katika mishipa yake na kisha kuruhusu dawa zimwingie kwa kasi. Wakati huohuo daktari mwingine akiuamsha moyo wa mgonjwa kwa kutumia mashine.

    Hatimaye akakohoa, wakaendelea na jitihada zao hadi fahamu zikamrejea.

    Wale madaktari wakafanya kama walivyoagizwa wakaanza kumuhoji mgonjwa kitandani. Maswali yao yote yalikuwa juu ya tukio lililopita na kumfanya awe pale kitandani hoi.

    Walimuuliza alichokuwa anakumbuka lakini hapakuwa na majibu, yule bwana hakuonekana kukumbuka jambo lolote lile. Walimuuliza jina lake akajitambulisha kuwa yeye ni Hasani Hasani.

    Madaktari waliyarekodi majibu yote hayo, kama walivyoagizwa kuwa kwa majibu yoyote atakayoyatoa yule bwana ambaye walimtambua kwa jina la Gama Yakubu.

    Baada ya kurekodi kilichokuwa kinafuata ni kuuondoa uhai wa mtu yule aliyesadikika kuwa na lolote ajualo kuhusiana na mkakati mahususi wa siri!!

    Naam! Wakamwondoa uhai wake kwa kumchoma sindano yenye sumu kali.

    Kisha wakatoka ndani ya kile chumba huku wakitikisa vichwa vyao.

    Wakasikitika na kutoa majibu kuwa haikuwezekana kuokoa uhai wa Gama kwani damu ilivilia katika ubongo wake.

    Pia wakasisitiza zaidi kuwa mwili wa marehemu umeharibika vibaya hivyo ni vyema uzikwe mapema.

    Taarifa za Yakubu Gama kupoteza uhai zikamfikia IGP na mrakibu msaidizi Robert.

    Kila mmoja akaipokea katika namna aijuayo mwenyewe.

    IGP akampigia simu mzee Matata na kumshukuru kwa jitihada kubwa alizoonyesha, akamsifu kwa uzalendo wake katika nchi isiyokuwa yake. Lakini hakusahau kumkandia bwana Robert kuwa kwa kuchelewa kwake kuwaruhusu madaktari basi amechangia kifo cha Yakubu Gama. Mwisho akamweleza Mzee Matata kuwa raisi atasimamia safari nzima ya madaktari wale kurejea nchini India.

    Mzee Matata akashukuru na kisha simu ikakatwa.

    Gama akahesabika kuwa kijana wa pili muhimu kabisa katika usalama wa taifa kupoteza uhai katika kipindi cha mwezi mmoja..



    Mzee Robert alipewa taarifa ile ya kifo na mkewe kama ushuhuda juu ya alichomweleza usiku juu ya madaktari hao feki.

    Bwana Robert alimkumbatia mkewe na kumshukuru kwa ushauri wake lakini akabaki kusikitika kuwa yeye hakuwa juu ya IGP hivyo asingeweza kuwazuia madaktari wale kuingia katika kile chumba alichokuwa amelazwa Gama.

    Mke akatoa pole na kumtia moyo mume wake.

    Mzee Robert akashukuru! Na baada ya hapo akamuaga mkewe na kuelekea hospitali ya Lugalo.

    Huko akaenda kukutana na Daktari Macho.

    Bwana ambaye walisoma naye shule moja ya msingi hadi chuo kikuu, na hapo wakatengana mmoja akisomea udaktari na mwingine akisomea uhasibu!

    Taaluma zikawatenganisha lakini baadaye zikawakutanisha tena, Dokta Macho akiwa anafanya kazi katika hospitali ya jeshi na Robert akiwa na cheo cha Mrakibu mkuu wa polisi.

    Usiku ule thamani ya urafiki wao iliendelea kuonekana huku wakiwa wanaaminiana kwa silimia kubwa.

    Dokta Macho aliyasikiliza mashaka ya Robert na kuamua kutii alichosisitizwa, akamuhamisha chumba Yakubu Gama kisha katika kile kitanda akawekwa bwana aliyeshukiwa kuwa ni mwizi, wananchi wakachukua sheria mikononi na kumchoma moto. Lakini kabla mambo hayajawa mabaya sana akaponea chupuchupu na kuwahishwa hospitali.

    Majeraha katika mwili wake na yale ya Yakubu Gama baada ya mlipuko yalifanana sana maana yote yalikuwa majeraha ya moto.

    Wale madaktari kutoka India wakakutana na mchezo ndani ya mchezo waliopanga kuucheza. Wakachezewa shere na mwisho wa siku wakaumalizia uhai wa yule kibaka.

    Wakajisifu kuwa wamemuua Yakubu Gama.

    ***

    Kwa kitendo kile cha kuwarubuni madaktari, bwana Robert alitambua vyema kuwa amejiingiza katika vita na IGP pamoja na mkuu wan chi maana hawa walikuwa hawaambiliki kwa lolote juu ya mtu wa kuitwa mzee Matata.

    Hofu kubwa aliyokuwanayo Robert ni juu ya usalama wake na daktari aliyeshiriki katika tukio lile.

    Na hapo akatambua kuwa hatakiwi kulala kitandani na kupeleka mambo taratibu taratibu.

    Badala yake alitakiwa kufanya mambo kwa kasi ya ajabu ili hata siku wakimlaza usingizi wa milele basi neno lake liendelee kuishi huku likiwaumbua wote waliokuwa wakijificha huku kiuhalisia walikuwa wauaji.

    Kwa kufikiria ni namna gani anaweza kuchakarika kwa kasi bila uoga. Robert akaamua kuyahamishia mambo yaliyokuwa katika kichwa chake akayaweka katika maandishi.

    Neno kwa neno kuanzia mashaka yake juu ya mzee Matata, pia lawama zake juu ya IGP na kisha akagusa mamlaka kuu ndani ya nchi akapagusa Ikulu. Akapataja kuwa panahusika kumficha mzee Matata.

    Baada ya kuandika kurasa nyingi sana akautuma ujumbe ule mahali ambapo aliamini kuwa ni sahihi kabisa na wala hatakuwa amepotea kufanya vile.

    Hakujitambulisha yeye ni nani wala cheo chake katika uongozi wa jeshi la polisi.

    Harakati zikazidi kupamba moto!!



    *****



    MOROGORO MJINI



    AKILI za kuzaliwa za Atuganile ama maarufu kama mama lao zilimfaa mara nyingi sana. Hata katika maisha yake ambapo alikuwa ameishia darasa la saba hakubabaika na kuyaogopa maisha. Alipambana kwa mafanikio jijini Mbeya na kisha kuingia jijini Dar es salaam huku akiwa hana mwenyeji hata mmoja. Lakini licha ya hayo bado aliweza kupambana bila kuwa ombaomba.

    Kilichokuwa kinambeba katika maisha yake ni siri zake kwa jambo ambalo anatarajia kulifanya. Kila wakati alikuwa akihofia kuwaambia watu mipango yake kwa kuhofia kukatishwa tama. Hivyo aliiongoza serikali ya maisha yake kwa kutumia kichwa chake mwenyewe.

    Tabia hiyo iliendelea hata siku ile ambapo alipandishwa gari na Sam kwa ajili ya kwenda Mbeya.

    Naam! Alihitaji Sam atambue kuwa yupo Mbeya, ili ikitokea siku moja Sam amekamatwa na kubananishwa ipasavyo ajikute akiisaidia ;polisi upelelezi wa kumtafuta mama lao Mbeya.

    Msako ambao ungewachukua miaka zaidi ya kumi bila mafanikio yoyote.

    Wangedumu wakimsaka mama lao jijini Mbeya wakati mipango yake ilikuwa tofauti kabisa.

    Mama lao kwa utashi wake mkubwa gari lilipofika Morogoro akashuka, bila kutoa taarifa.

    Gari likaondoka huku siti yake ikibaki wazi, kondakta akajisikia vibaya sana kuwa amemuacha abiria wa kwenda Mbeya stendi ya Msamvu Morogoro.

    Wakati kondakta akifadhaika na kumuuliza jirani yake juu ya yule abiria wa Mbeya aliyeachwa njiani. Mama lao alikuwa ameshikilia gazeti ambalo lilikuwa likimtangaza kuwa anasakwa kwa mauaji.

    Alitabasamu kisha akacheka kwa nguvu!

    Hakuwa na wasiwasi hata kidogo.

    Hakika alikuwa na jina kubwa lakini bahati nzuri iliyoje hakuwa na kumbukumbu ya kuwahi kupiga picha jijini Dar es salaam. Mazingira aliyofanyia kazi hayakuwa mepesi kupiga picha, alikuwa ni mtu wa kutingwa masaa yote.

    Nani angekuja kumpiga picha!!

    Ungekuwa mgahawa wa watu wa kifahari walau wangepata huo muda wa kuchukua kumbukumbu. Lakini waliohudhuria mgahawa ule wengi wao walikuwa mafukara tu ambao msongo wa mawazo ni kipande kimoja katika maisha yao ya kila siku.

    “Wali nyama, niwekee wa kushiba!” hizi nd’o zilikuwa lugha zao. Baada ya hapo ni malipo na kukutana tena ni kesho yake.

    Magazeti yakabaki kuandika jina la mama lao tu!

    Bila picha wala jina halisi hawakulijua.

    Tanzania nzima kuna akina mama lao wangapi??

    Bahati iliyoje kwa mama lao Atuganile kuonyesha makucha yake pasipo kujulikana.



    *****



    KATIKA Mji ambao aliishi mama lao kwa wakati ule, ulikuwa ni mji wa maficho pia kwa kijana Yakubu Gama ambaye alikuwa amehifadhiwa kwa ajili ya matibabu.

    Fahamu zilikuwa zimerejea tayari na damu yake ilikuwa inachemka haswa kwa ajili ya mapambano. Alikuwa na kiu ya kujua kunani hadi mambo haya yote yanatokea.

    Na kubwa zaidi alitamani kumjua muuaji wa Steven Marashi ambaye alikuwa pacha wake katika kazi kabla hajahamishiwa kazi maalumu ya upelelezi, kazi ambayo ilimfanya ajikute katika sanaa ya maigizo na hatimaye kuanza kucheza katika filamu.

    Hakuna hata muigizaji mmoja aliyetambua kuwa Steven Marashi alikuwa kijana wa usalama wa taifa.

    Kwa tukio lile la kulipukiwa na bomu ambalo lilikuwa katika mwili wa kijana aliyeagizwa na BVB kulizidi kumtamanisha kutambua kuwa ni kitu gani ambacho kinafichwa.

    Hisia zake kubwa zikajijenga juu ya upelelezi ambao Steven Marashi alikuwa akiufanya kimyakimya dhidi ya kigogo wa serikali. Upelelezi alioubatiza jina oparesheni tokomeza. Alichotaka kukitokomeza alifahamu yeye mwenyewe.. jambo la muhimu alimsihi Gama kuwa mtulivu ayangoje majibu.

    Hivyo kama Steve ameuwawa bila shaka ule upepelezi wake ambao alikuwa hajaukabidhi ofisi kuu ulikuwa katika mikono ya mtu mwingine ambaye amezing’amua siri nzito za usalama wa taifa.

    Kitendo cha kutaka kuuwawa akiwa hospitali kilimsababisha apigie mstari mashaka yake na kuamini kuwa anatakiwa apambane upesi ili kuupata ukweli.

    Na aliamini hilo linawezekana sana kwa sababu tayari alitambulika kuwa amekufa. Na vile mwili wake haukuagwa kwa sababu kuwa ulikuwa umeharibika sana.

    Akabaki kujulikana yu hai kwa watu wasiozidi wanne!

    Hakuna hata mmoja kutoka katika familia yake aliyetambua kama yu hai mjini Morogoro.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Gama alijaribu kutembea kwa kujivutavuta hadi akakifikia kioo. Akajitazama!

    Lahaula! Hakuwa yeye, sura yake iliunda mfano wa mapunye na ngozi yake ilikuwa imechubuliwa vibaya sana na lile bomu. Akajaribu tena na tena kujitazama hakuwa yeye!

    Hasira zikamjaa kifuani akaubamiza ukuta kwa ngumi nzito!

    Na hapo mwenyeji wake ambaye ni daktari akaingia na kumsihi ajipumzishe kwani hakutakiwa kujihangaisha kwa lolote hadi pale atakapopona!

    Gama alirejea kitandani akajilaza lakini ni kwa kupumzisha mwili tu na sio akili. Akili ilikuwa inapanga mikakati kabambe!

    Akamfikiria sana hayati Steven Marashi, akakifikiria kifo chake kilivyokuwa cha upesi, na tetesi zake ambazo hazikuwa zinaeleweka. Mara ameuliwa kishirikia na mpenzi wake, mara amejiua.

    Gama akaufikiria ukakamavu wa Steve, akafikiria ni jinsi gani alikuwa na uwezo wa kupambana na maadui zake, akaitambua misimamo yake.

    Hapa zile tetesi za kujiua akazifutilia mbali.

    Akamkumbuka tena namna alivyokuwa bingwa wa mapambano ya ana kwa ana. Pia alivyoweza kupambana na mtu mwenye silaha…. Hakika Steven alikuwa mwiba!

    Kuhusu mtu yeyote kuweza kumuua kirahisi vile labda kwa kumnyonga ama kumpa sumu. Hili nalo akalifutilia mbali!

    Angeweza kufa mtu mwingine kizembe namna ile lakini sio Steve!!

    Gama alipingana kabisa na hisia za Steve kuuwawa kizembe.



    Mara ghafla akayafikiria MAPENZI.

    Na hapo akaketi kitako. Akajenga picha ya mfanyakazi mwenzake huyo ambaye tayari ni marehemu.

    Akamkumbuka jinsi alivyokuwa anakosa raha pale anapokerwa ama anapomkosea mpenzi wake. Alikuwa anashindwa kufanya kazi kabisa na wakati mwingine hata kufanya chini ya kiwango!

    Yawezekana mapenzi yamemuua Steven!! Gama alijisemea huku akitikisa kichwa chake kuuunga mkono hoja ile.

    “Lakini mapenzi kivipi?” akajiuliza….

    Akawafikiria baadhi ya wasichana ambao walikuwa wakijihusisha kimapenzi na Steve.

    Mariam, Subira, Recho…..

    Akayamaliza majina yote yale aliyokuwa akiyafahamu, akampa kipaumbele Mariam. Huyu ndiye alikuwa akitumia naye muda mwingi mara kwa mara kwa sababu Subira na Recho hawa walikuwa wake za watu hivyo ndoa zao ziliwakosesha muda wa kuwa na Steve mara kwa mara.

    Lakini Mariam hakuwa ameolewa na mpenzi pekee aliyekuwanaye kiuwazi alikuwa ni Steve, penzi lilianza kwa kasi kubwa lakini baadaye penzi likashuka thamani, ikawa linapita hadi juma moja bila Steve kutoka na kwenda mahali na Mariam, lawama zikaanza na mwisho zikapoa. Mariam akawa hawezi tena kumwendesha Steve!

    Sasa nani alikuwa akimwendesha?? Akajiuliza!

    Huyu nd’o anayetakikana nijue nini kimemuua Steven Marashi!

    Hapa kama si mapenzi basi kuna HILA zimefanyika, aidha Mariam alimuua kulipiza kisasi ama.. ama…..

    Gama akakosa lolote la kutabiri!

    Akajipa siku tatu za ziada mbele ili aweze kuanza rasmi kazi nzito kupita zote alizowahi kufanya. Kujua ni kipi kimemuua rafiki yake na kuna njama gani zinaendelea asizozijua!!

    Kubwa zaidi kuhusu ripoti ya hujuma ambayo anaamini Steve alikuwa ama ameikamilisha ama alikuwa amekaribia kuikamilisha.

    Gama akatabasamu kisha akajilaza tena. Wakati huu ni mwili na akili.

    Akasinzia huku fikra ya mwisho kabisa akiwa amemfikiria mtu wa kufanya naye hiyo kazi.



    *****



    MIAKA MINNE ILIYOPITA



    ILIKUWA imebaki miaka minne kabla ya uchaguzi mkuu kufanyika tena. Chama tawala kilitarajiwa kusimamisha mgombea mpya baada ya yule wa awali kuwa anaelekea kumaliza miaka yake kumi kama katiba isemavyo hawezi tena kugombea. Anatakiwa kuwaachia wenzake.

    Tofauti na miaka mingine ambapo mgombea anaandaliwa mapema kabisa. Lakini hii ya wakati huu ilikuwa kinyume kabisa. Wagombea wenye sifa walionekana kuwa wawili na wote walikuwa wenye nguvu sana hivyo likawa ni jukumu la chama tawala kufanya uchaguzi sahihi ili nchi iendelee kuwa chini ya utawala wao.

    John Masele, waziri wa mambo ya ndani na nje ya Tanzania alikuwa ameitangaza nia yake mapema kabisa kuwa anataka kuingia ikulu. Wafuasi wake wakaanza kumuita raisi mtarajiwa, jina likazoeleka huku akionekana kukosa kabisa dosari yoyote ya kupata nafasi hiyo.

    John Masele alikuwa akikubalika hata kwa wapinzani, alikuwa na sera za peke yake ambazo zililenga katika kumkomboa mtanzania kiuchumi, kiutamaduni na kifikra.

    Raisi aliyekuwa madarakani hakufanana misimamo na Masele, hivyo alitambua wazi kuwa hataishi kwa raha tena wakati akiitwa raisi mstaafu. Alihofia bwana Masele anaweza kutumia utawala wake kumsababisha yeye aonekane hakuna lolote alilofanya wakati akiwa ikulu. Jambo ambalo kwake lilikuwa fedheha kuu.

    Raisi akamshawishi, Mathias Obhare, waziri wa nishati na madini atangaze nia ya kugombea pia. Huku akimsisitiza kuwa asimuhofie Masele na siasa zake kwani yeye ana watu wenye ushawishi mkubwa na pia wenye pesa nyingi, hivyo watashinda.

    Na hapo akamwambia kuwa mzee Matata atakuwa nyuma yake kuanzia hatua ya kwanza hadi ya mwisho watakapokuwa wakipongezana wakiwa ikulu huku yeye akiwa ni raisi.

    Kumsikia mzee Matata pekee haikutosha kumshawishi Mathias kukubaliana na wazo la raisi. Kitu kikubwa kilichokuwa kinamkwamisha katika hilo ni ukaribu aliokuwanao kwa John Masele kuanzia chuo kikuu walipokutana, John akawa raisi wa chuo huku Mathias akiwa makamu wake. Ukaribu huu ukaunda kama undugu, na hatimaye wakajiunga na chama tawala.

    Sasa John ni waziri wa mambo ya ndani na nje wakati yeye ni waziri wa nishati na madini.

    Raisi anataka kuwafanya maadui kwa mara ya kwanza!!!

    Mathias hatimaye anashawishika, waandishi wa habari wanaitwa katika mkutano.

    Mathias Obhare anatangaza nia ya kuwania nafasi ambayo John Masele alikuwa anawania.

    Kujitangaza kwa Mathias Obhare kulimshtua sana Masele, akajiuliza ni lini Obhare akawaza upinzani kama ule. Kwanza ni yeye alikuwa wa kwanza kumshawishi atangaze nia, in akuwaje sasa na yeye atangaze nia.

    Si bure kuna kitu hapa! akajisemea

    Na hapo akatambua wazi kuwa kuna hila imefanyika dhidi yake ili asiweze kuleta mapinduzi kwani alikuwa na misimamo tofauti kabisa na chama tawala japo naye alikuwa ndani yake.

    Kwa utulivu kabisa akaamua kukutana na Obhare na kumshawishi asigombee nafasi ile kwa sababu kwa namna moja ama nyingine ingeweza kuwaingiza katika malumbano makubwa na kuutia doa urafiki wao. Akamsihi kuwa iwapo ataachia nafasi ile basi atamchagua kuwa makamu wa raisi kama walivyofanya wakati wakiwa chuo kikuu

    Obhare hakutoa jibu palepale, akayafikisha yale yote kwa raisi.

    Mtukufu Raisi akatumia huo mwanya kuanza kumchafua Masele mbele ya wananchi.

    Akasambaza maneno makali kwa wajumbe juu ya uoga wa kushindwa alionao Masele pia akaelezea juu ya tamaa ya madaraka aliyokuwa nayo bwana yule.

    Na hapo baraza la chama tawala likatangaza rasmi kuliondoa jina la waziri wa mambo ya ndani na nje katika kinyang’anyiro kile.

    Fukuto likaanzia hapo!



    Baada ya juma moja, jambo jingine kubwa likazuka.

    Mathias Obhare akatekwa na kuibiwa gari lake kisha akapigwa sana. Kipigo kilichosababisha akimbizwe Afrika kusini upesi kwa ajili ya matibabu.

    Zikasemekana ni hila za Masele baada ya kuzidiwa kete na mpinzani wake kisiasa.

    Baraza likaketi tena na kumweka kitimoto Masele ambaye alikataa kata kata kujihusisha na tukio lile, huku akisisitiza kuwa amebariki bwana Obhare kuwania kiti kile.

    Lakini maneno yake hayakutosha kutengua kilichokuwa kimepangwa tayari.

    Akiwa ameketi nyumbani na familia yake, mara akaisikia taarifa ya habari kuwa Raisi amemvua nyadhifa za uwaziri wa mambo ya ndani na nje….. huku sababu kuu ya kufanya vile ikisemekana ni kwa maslahi ya wananchi na sio chama.

    Jina la Masele likazidi kuchafuka huku Mathias Obhare akianza kukaa katika damu za raia wema.

    Wachache wenye kujitambua walihisi kuna jambo linatokea hapo katikakati. Lakini hawakuwa na pa kusemea.

    Lakini mtanzania mmoja ambaye alikuwa masomoni nchini uingereza alitamani sana amalize masomo yake ili aweze kuingia katika upelelezi juu ya kipi kinachotokea maana naye alitilia mashaka matukio yale mfululizo.

    Huyu alikuwa ni Steven Marashi, mwanausalama wa taifa aliyekuwa ameenda kuongeza elimu yake nchini uingereza.

    Akiwa huko akajiunga katika vikundi vya kiafrika vya kucheza ngoma na kufanya michezo ya majukwaani, fani aliyokuwa akiipenda tangu utoto wake alipokuwa shuleni.

    Fani ikanoga na kung’ara zaidi katika ukubwa wake.

    Aliporejea nchini Tanzania, akaingia rasmi katika sanaa ya maigizo.

    Ungeanza vipi kujua yule bwana alikuwa mwanausalama wa taifa na mpelelezi aliyekubuhu?

    Safari ikaanzia hapo!!!

    Alipojiunga na sanaa mtu mmoja tu ndiye aliyejua ni kwanini anajiunga katika sanaa, huyu alikuwa ni rafiki yake kikazi na hatimaye hadi mtaani wakawa marafiki na kushirikishana mambo yao mengine.

    Alikuwa ni Yakubu Gama, zao la usalama wa taifa lenye asili ya Naijeria lakini mwenye uraia halisi kabisa wa Tanzania kwa kuzaliwa.

    Na baada ya miaka minne Steven anakufa katika mazingira ya kutatanisha!!!

    Na baada ya kifo chake mambo mengi yanajitokeza hapo katikati, Gama hakupata hata fursa ya kuonana na Sam yule mwandishi ambaye alikuwa rafiki wa karibu sana wa Steve!

    Hadi usiku ule aliokwenda kumwekea dhamana.

    Dhamana iliyotoka wa mtukufu raisi moja kwa moja, kupitia amri ya IGP.

    Dhamana iliyokuwa na makusudi ndani yake!

    Kuna kitu kilikuwa kinatafutwa na Sam alidhaniwa kuwa anaweza kuwanacho ama kuwezesha kupatikana kwacho!

    Ni kitu gani hicho?

    Hili swali linabaki katika kichwa cha Yakubu Gama ambaye yu hai sasa lakini akiwa amejeruhiwa!

    Yakubu Gama anaapa kuwa atapeleleza hatua kwa hatua hadi ajue ni kitu gani kilimuua Steve! Huenda katika utafiti huo akatambua pia ni nani anayeitwa BVB.



    ****CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/



    YAKUBU Gama alijisikia kuwa yupo fiti kiasi cha kuanza rasmi harakati zake za kuusaka ukweli. Lakini mwili haukuwa imara, miguu bado ilikuwa dhaifu na alitakiwa kutembea hatua chache na kisha kupumzika. Sumu iliyokuwa katika bomu lililolipuka ilikuwa imemuathiri.

    Gama hakutaka kupumzika zaidi, hivyo akaamua harakati hizi azifanye huku akiwa na wasaidizi. Alihitaji watu wa kufanya kazi kwa niaba yake. Alihitaji watu wachache na ikiwezekana hata mmoja tu mwenye roho ya paka isiyoogopa kifo na kifua cha chuma cha kutunza siri.

    Ni wapi atawapata? Hili nd’o lilikuwa swali alilojiuliza kabla hajaamua kuwasiliana na mrakibu msaidizi Robert Masawe ambaye nd’o alifanikisha mipango ya kuokoa uhai wake. Huku akitilia mkazo suala la mwili feki wa Gama kuzikwa bila kuagwa kwa sababu ulikuwa umeharibika.

    Mpango huo ukahitimishwa na ripoti ya daktari Macho ambaye lake lilikuwa moja na bwana Robert Masawe.

    Robert Masawe, akitumia gari ya mkewe aliendesha usiku mnene, hadi Morogoro ambapo alikutana na Gama.

    Baada ya salamu Gama alimweleza mambo kadhaa na kisha kumwomba amtafutie mwanamke mwaminifu mwenye kifua cha chuma na roho ya paka ambaye anaweza kushirikiana naye kwa ukaribu zaidi.

    “Gama… huhofii kwamba mwanamke anaweza kutuharibia”

    “Mwanamke mwenye kifua cha chuma ni zaidi ya mwanaume jasiri….” Alijibu Gama huku akiwa amemkazia macho Robert.

    “Basi nipe siku ya leo nifikirie kwa kina maana hili jambo tunaloshiriki lina matokeo mawili…”

    “Ni ama kufa kwa mateso ama kupona na majina yetu kudumu katika vitabu milele na milele” Gama alimalizia ile sentensi kabla hata Robert hajamalizia.

    Robert akatabasamu na kujisikia fahari kuzungumza na kuwa katika mpango ule madhubuti na kijana machachari kama Gama.

    “Laiti kama usingekuwa umejeruhiwa naamini hili jambo ungelimaliza mwenyewe tena upesi sana.” Robert alisema huku akisikitika.

    Maongezi yao yakamalizika kwa ahadi ya kupata muafaka ndani ya masaa machache yajayo.



    Njia nzima akiwa anaendesha gari bwana Masawe alijiuliza ni kwanini Gama alikuwa akihitaji mwanamke katika shughuli ile.. lakini hakutaka kuumiza kichwa sana kwani alikuwa na mtihani wa kumtafuta huyo mwanamke anayeweza kushirikiana na Gama.

    Alifikiria sana juu ya watumishi wa jeshi la polisi ambao anaweza kuwaamini lakini nafsi haikutulia kwa yeyote. Akafikiria kwa kina sana hata watu kadhaa aliowahi kukutana nao maishani. Akafikiria na kukosa jibu.

    Hapakuwa na yeyote wa kuweza kuaminika katika hili!

    Hofu ya kuyakoroga mambo na mwisho kuishia kitanzini ilikuwa imemtawala Robert. Lakini maji alikuwa ameyavulia nguo, hivyo iwe isiwe sharti lilikuwa lazima ayaoge tu.

    Alipofika mzani wa Mikese kuondoka kutoka Morogoro, mara kama radi vile akili yake ikawaka na kukumbuka kitu. Akamkumbuka dada yake lakini kutoka tumbo la mama mwingine.

    Ilikuwa ni miaka mingi imepita bila kuonana naye. Lakini moyo ukajiachia kabisa kuwa iwapo hakubadili tabia zake basi ni yule alikuwa akimfaa kwa kazi iliyokuwa mbele yake.

    Alikuwa na kifua cha chuma, jasiri asiyeyaogopa maisha.

    Alikuwa na uwezo wa kuitunza siri kadri awezavyo, alikuwa muongeaji sana lakini bahati mbaya alikuwa hayasemi yaliyo siri kwake.

    Hili jambo lilimfanya Robert amshauri dada yake aende jeshini. Lakini hilo likagonga mwamba, dada alikuwa na siri zake lukuki. Hatimaye akaondoka nyumbani pasi na kuaga.

    Robert akaingia jeshini na ikapita miaka mingi sana bila kuonana.

    Ssa alikuwa akiuhitaji msaada wake ndugu huyo!

    Wapi pa kumpata? Alijiuliza.

    Jibu lilikuwa jepesi tu, ni mtu mmoja tu ambaye angeweza kujua.

    Huyu alikuwa ni mdogo wao wa mwisho ambaye alitokea kuivana sana na dada yao. Lakini na yeye alikuwa na tabia zilezile.

    Roho ya paka na kifua cha chuma! Huenda nd’o maana wakapendana.



    Akaitazama saa yake, ilikuwa ni saa nane usiku. Hakutaka kusubiri zaidi akaegesha gari pembeni, akaichukua simu yake na kubofya namba za mama yake mzazi.

    Bahati nzuri mama hakuwa amelala, alikuwa kwenye sherehe fulani na nd’o ilikuwa inaisha.

    “Haujambo…” aliuliza.

    Mama tayari amelewa looh! Robert alijisemea baada ya kumsikia mama yake. Alimjua vyema alivyo rafiki wa pombe. Lakini uzuri ni kwamba hakuwa mtu wa kupoteza kumbukumbu hata akilewa.

    “Mama unayo namba ya Subira… ninahitaji sana namba yake sasa hivi.”

    “Amefanyaje mwanangu tena mnataka kumfunga”

    “Aaah! Mama hapana….”

    “Hana simu… nikifika nyumbani nipigie nitampa simu yangu mzungumze.”



    Kweli baada ya nusu saa Robert akapiga simu, mama alikuwa nyumbani tayari na simu ikapokelewa na Subira. Mdogo wao wa mwisho.

    “Shkamoo kaka.”

    “Marahaba, Subira hivi mmefunga shule ama?”

    “Ndio tumefunga.”

    “Nahitaji kesho uje Dar…”

    “Mbona ghafla kaka, mi nataka kusoma twisheni…”

    “Ndio ni ghafla lakini nahitaji uje, unakuja na kuondoka baada ya siku chache tu…”

    “Aaah! Mi na wifi hazipandi kaka, sitaki tugombane.”

    “Hautafikia nyumbani kwangu, nitakupokea tutazungumza na utalala mahali na kisha kuondoka. Nakutumia pesa kwenye simu ya mama, usije ukamwacha akatoa yeye ataenda kunywa pombe pesa yote. Nenda ukatoe mwenyewe halafu asijue kama unakuja huku, si unamjua mama tena.?”

    “Sawa kaka! Kama usemavyo itakuwa hivyo” alijibu kwa ufupi. Robert akakiri kuwa hakika alikuwa anazungumza na roho ya paka.



    ****

    DAR-ES-SALAAM, Tanzania saa tano usiku!



    Katika mgahawa mdogo ambapo chipsi huuzwa hadi majira ya saa tisa usiku. Robert alikuwa ameketi na mdogo wake wa mwisho, Subira ambaye alikuwa ametokea jijini Mbeya siku hiyohiyo. Na kuingia jijini Dar majira ya saa kumi na mbili jioni. Lakini waliamua kukutana majira hayo ya saa tano usiku kwa sababu za kiusalama zaidi. Alikuwa ni Robert aliyetoa ushauri ule.

    Mgahawa ulikuwa na watu wachache sana, licha ya hayo walijitenga mbali kabisa na mwanga.

    Kwa kuwatazama upesi ungeweza kudhania kuwa yule likuwa ni mtu mzima amechepuka katika ndoa yake na hapo yupo na mwanafunzi wanayeishi naye katika mapenzi ya siri. Na kule kukaa kwao gizani ni kuendelea kuipalilia siri yao kwa maua ya miiba.

    Robert alikuwa mtulivu, lakini Subira alikuwa mtulivu na makini sana. Alipiga funda moja la soda yake kisha akamtazama kaka yake machoni, ikiwa ni ishara ya kumtaka aanze kuzungumza.

    “Subira mdogo wangu, nia yangu ya kuonana na wewe ni kwa ajili moja tu. Kwa ajili ya kukomboa mamia ya watanzania kutoka katika maisha magumu wanayoishi.”

    “Lakini mimi bado mwanafunzi! Unataka nijiunge na siasa ama” alijibu huku akimkazia macho.

    “Natambua na nd’o maana nikaamua kuonana na wewe. Wanafunzi nd’o mzizi wa ukombozi” Akasita kisha akaendelea, “Hivi shuleni kwenu kuna waalimu wangapi?”

    “Sidhani kama umeniita Dar ili kujua maendeleo yangu shuleni…” Subira alimkatiza.

    “No! anyway, tuachane na hayo lakini nimekuita hapa nahitaji msaada wako mkubwa kupita yote.”

    “Upi kaka..”

    “Nahitaji kuonana na Sekela.”

    “Dada Sekela?” Subira akahoji. Robert akatikisa kichwa kukubaliana na mdogo wake.

    “Unafahamu alipo ama, maana ni miaka sasa hajarudi nyumbani. Naamini yupo Dar!” Subira alitoa jibu ambalo Robert alilitarajia.

    Hivyo ikamlazimu kusimulia kila kitu kilivyo na ni kwa jinsi gani msaada wa Subira ulikuwa unahitajika ili Sekela aweze kupatikana. Alitambua wazi kuwa licha ya umri mdogo wa binti yule hakuwa akitekwa kirahisi kwa maswali ya mitego.

    Robert akasimulia mkasa juu ya serikali inavyoendeshwa kihuni huku wenye haki wengi wakiishi kama digidigi katika nchi yao ambayo inajitamba kuwa ni nchi huru kwa watu huru.

    Alipomaliza kusimulia juu ya ugumu anaokutana nao hasahasa imani ya IGP na raisi juu ya mtu mbaya mzee Matata machozi yalikuwa yanamlenga Subira.

    “Mzee Matata.. sura yake siku ambayo ameleta msaada wa vitabu shuleni kwetu haikunivutia kabisa kuamini kuwa eti amefanya vile kwa sababu ya huruma kwa watanzania. Walinibishia sana wenzangu lakini sasa naanza kupata imani na kila nilichokuwa nawaza siku ile…” Subira alizungumza kwa sauti ya chini huku akitikisa kichwa juu na chini.

    Maelezo ya kaka yake yalikuwa yamemgusa haswa na kuamua kumuamini na kumfungukia kile akijuacho.

    “Kaka, kumbuka yule ni dada yako, hata kama baba zenu ni tofauti anabaki kuwa dada yako tu. Nakumbuka uliwahi kusema kuwa polisi hana ndugu, kama umeamua usemi huo uzidi ule wa damu nzito kuliko maji basi amini kuwa mateso atakayopata dada yatakuwa juu yako na laana ya mama itakuangukia kwa sababu nitamweleza iwapo mambo yataenda kinyume. Mimi nitakukutanisha na Sekela, ila uyashike hayo niliyokueleza….”

    “Subira, niamini mimi siwezi kufanya ujinga kama huo hata siku moja….”

    “Sekela yupo Morogoro, nitawasiliana naye na kukutanisha naye. Kesho usiku… naomba unipeleke nikalale sasa…” alimaliza Subira na kusimama, Robert naye akasimama.

    Wakaondoka hadi nyumba ya kulala wageni ambayo Robert alikuwa amemuandalia mdogo wake.

    Usiku ule ukapita!!

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    ****

    MOROGORO, Saa mbili usiku.



    Subira alikuwa katika nyumba ya wageni tayari alikuwa amewasiliana na dada yake juu ya kuonana kwao.

    Hakumweleza kabisa juu ya ujio wa bwana Robert. Hivyo Sekela hakutilia mashaka yoyote na majira hayo alikuwa amekaribia katika chumba kile.

    Walipeana mambo kedekede ya hapa na pale huku mdogo mtu akiwa mwingi wa maswali ya hapa na pale huku akihitaji kujua nini hatma ya dada yake katika kuusaka uhuru wake tena.

    Kabla hii mada haijafika mbali mlango wa chumba kile ukagongwa. Subira alijua nini kinaendelea, mapigo yake ya moyo yalikuwa juu sana lakini alijikaza asionekane mwoga. Akauendea mlango na kuufungua. Na hapo akaingia Robert Masawe.

    Ana kwa ana na Sekela ama maarufu kwa jina la mama lao. Dada yake kutoka kwa baba mwingine lakini mama yao akiwa ni mmoja.

    Mama lao hakuonyesha mshtuko wa aina yoyote lakini jicho lake liliwaka haswa kumaanisha kuwa yu katika hasira kali mno.

    Moyoni alijua tayari amekamatika, alitaka kumvamia Robert ili akabiliane naye lakini akashangazwa na upole wa yule bwana.

    “Dada nisamehe bure, lakini amini kuwa hautajutia litakalozungumzwa maana hata wewe linakuhusu… kaka kama ulikuwa hujafahamu huyu hapa anaitwa mama lao, sahau kuhusu Atuganile au sekela. Bila shaka kila mmoja anamuhitaji mwenzake iwapo uliyonieleza ni ya ukweli”

    “Sijabadili chochote katika maelezo yangu ya awali…”

    “Basi mimi nawapisha!” Subira akasimama na kutoweka.

    Mama lao akazungumza kwa kina na Robert, hatimaye akaondoka naye wakati huohuo wa usiku.

    Akaenda kukabidhiwa kwa Yakubu Gama!

    Naam! Kikosi kazi kikaanza kujengeka!

    Baada ya kumwona mama lao na umbile lake, Yakubu alitaka kumpuuzia lakini walipoanza kuzungumza tu. Ile hali ya kujiamini ya mama lao ikamfanya aanze kuamini anazungumza na mwanamke wea shoka.

    Mama lao akamueleza Gama juu ya kutekwa kwake na kuponea chupuchupu kufa mbele ya mikono ya wanaume wa kinyakyusa, Gama naye akamweleza mkasa wake uliotaka kuondoka na uhai wake.

    Katika maelezo yao, kila mmoja akajikuta katika fumbo la nani ni BVB.

    Yakubu Gama akawa kiongozi wa huu mchezo, mama lao akawa mtekelezaji. Kikosi kazi kikawa kinamkosa jemedari mmoja tu, huyu alikuwa ni Sam. Alikuwa akihitajika sana ili kuweza kukamilisha huu mchezo. Mchezo ambao Yakubu Gama aliubatiza jina la Kombolera

    Mama lao alihoji nini maana ya Kombolera katika jambo hili zito. Lakini Gama akamwambia aelewe kuwa hiyo ni kombolera tu na mwishowe hatauliza tena kwa nini yaitwa kombolera. Bali atajiona mwenyewe akicheza kombolera

    “Haya kombolera yetu inaanzia jijini Dar es salaam.” Gama akaagiza kisha usiku ukawa mwingi wote wakalala.



    MAMA lao alichepuka mitaa kadhaa ya Kinondoni, akiwa amejitanda juba jeusi. Ilikuwa ni siku ya Ijumaa. Na alipanga iwe hivyo ili aweze kujichanganya na waumini wa dini ya kiislamu hata likitokea lolote baya dhidi yake.

    Alitembea hadi uwanja wa Biafra, akakitazama kikaratasi mkononi mwake akaisoma ramani kama ilivyochorwa na Gama.

    Akaifuata na kuielewa, akahesabu nyumba nne nyuma ya jingo la ghorofa ambapo zamani ilikuwa shule ya Biafra.

    Nyumba ilikuwa pweke sana lakini kwa mbali ulisikika mziki wa mwambao ukikata mawimbi.

    Mama lao mwenye roho ya paka akafika mlango na kubisha hodi. Aliita mara kadhaa, lakini hakupata majibu. Lakini wakati anataka kuondoka zake akasikia hatua nyuma yake.

    “Karibu dada!”

    “Asalaam aleykum..” mama lao akasalimia. Yule dada akamjibu vyema na kumkaribisha.

    “Samahani sijui nimepotea ama nipo sahihi, hapa nd’o kwa Mariam…” aliuliza mama yao ilihali akiwa amemtambua yule dada kuwa ndiye Mariam.

    “Ni hapa kulikoni…”

    “Ooh! Asante… kumbe sijapotea…” mama lao akaketi kwenye kibaraza. Kisha hakumpa nafasi ya kuuliza yule binti.

    “Kwanza pole sana kwa msiba japo ni wetu wote! Naitwa Sekela..” alijitambulisha. Mariam akatambua yule dada alikuwa akizungumzia msiba wa Steven Marashi lakini alilazimika kuuliza ili kupata uhakika.

    Mama lao akajieleza kuwa yeye ni mama yake mdogo na Steven Marashi.. hayati Steven Marashi. Na alikuwa na ujumbe mzito wa kuzungumza na Mariam.

    Yule binti aliikunja sura yake kumaanisha kuwa amekerwa na taarifa ile.

    “Ni kitu gani hicho… na kwanini asiende kuulizwa Lili mnakaa tu kuniumiza mimi kichwa…” Mariam akaanza kuongea kwa hasira.

    Mama yao akacheka kimoyomoyo, huku akitambua kuwa yule binti alikuwa haujui ule usemi wa usizungumze iwapo una hasira.

    “Familia yetu.. ama niseme mimi hapa nakutambua wewe kuwa ni wifi yangu, sijui lolote kuhusu Lili, kwanza Lili ni nani?

    “Mpenzi wake!” alijibu kwa kiburi huku akibetua midomo yake.

    “Mariam!” mama lao aliita kiutu uzima kisha akamsihi Mariam aketi chini.

    “Nani mwingine amekuja kukuuliza juu ya Steve sasa. Jamani kaka yangu mimi….” Aliuliza kwa kulalamika.

    “Kuna mwingine amejifanya sijui askari sijui mwandishi nani ameniuliza maswali kedekede mwisho wa siku wamekuja maaskari wa kweli wamemsomba hapa….. bora akome maana alikuwa na maswali huyo!” Mariam akazidi kufunguka.

    Mama lao akaguswa na pointi ya mwandishi wa habari, akahoji zaidi. Akaelezewa juu ya muonekano wa mwandishi huyo.

    Alipoelezewa akatambua kuwa hakuwa Sam.

    Mama yao akaendelea kumuuliza Mariam na hatimaye akafikia lengo. Alitaka kujua iwapo Mariam angeweza kujua chochote juu ya kifo cha Steve.

    Mariam alikataa kata kata na mwisho akazirusha lawama zote kwa Lili. Mbaya zaidi hata alipokuwa akikaa hakuweza kupajua.

    Alichojua ni kwamba Lili ni muigizaji wa filamu na walikutana na Steve hukohuko kwenye filamu.

    Mamalao akafikiria kwa kina kisha akaichezea akili ya Mariam.

    “Ujue wifi, tuna mashaka kuwa kaka yetu alinyweshwa sumu, madaktari hawajasema lolote lakini alinyweshwa sumu kisha akaporwa vifaa vyake vya kazi.”

    “Nini.. au ule mkanda aliokuwa akitembea nao mara kwa mara… halafu hata sikuwa najua kazi yake ni nini….” Mariam akaropoka.

    Mama lao akamsifu Yakubu Gama kimya kimya kwa sababu alimwelezea Mariam kama alivyo na tabia zake za kuropoka bila kujua lipi jema na lipi sio jema.

    “Ndio huo mkanda na vifaa vingine……”

    “Mh! Labda Lili wake alitaka ajiachie vyema na waziri nd’o maana akamwekea sumu tutajuaje sie tulioachwa!!” akaongea kifedhuli kama anayeshushua!

    “Waziri? Ina maana Lili hakuwa mwaminifu kwa kaka yangu ama..”

    “Wanajua wenyewe.. mi sijui kwakweli, basi tu marehemu hasemwi vibaya, ila Steve hajui tu nilimpenda kiasi gani… akaenda kwa hicho ki Lili chake… haya yapo wapi laana tupu…” aliendelea kuropoka mambo mazuri Mariam. Mama lao akayahifadhi katika kichwa chake.

    Baada ya mazungumzo marefu akaaga!

    Huku akikiri kweli ile ilikuwa komborela.

    Wakati anaondoka akajisemea kimoyomoyo, KOMBOLERA Mariam!!

    Kisha akatabasamu!!



    ****

    Wakati mama lao akitabasamu baada kuanza kucheza komborela vizuri. Tina mchumba wa Sam alikuwa katika kilio kikubwa.

    Kwa mara nyingine alikuwa akikabiliana ana kwa ana na mzee Matata, mzee ambaye kabla ya matatizo hayo aliwahi kuwa mtu wake wa karibu sana. Ukaribu huu ulikuwa wa sababu maalumu sana ambayo sasa ilikuwa imegeuka shubiri!

    Ukaribu huu ulianzia kwa Lilian ambaye alikuwa rafiki wa Tina wa muda mrefu kudhaminiwa akafanya filamu, msimamizi wa kila kitu akawa ni mzee Matata na kampuni yake.

    Kama hili halitoshi filamu ikasambazwa na mzee Matata. Kisha akamnunulia gari ya kutembelea Lilian.

    Magazeti yakamtaja Lilian kama msanii wa filamu mwenye umri mdogo lakini mafanikio makubwa, hawakujua ambacho kilikuwa kinaendelea.

    Tina aliingiwa na wivu lakini hakuuweka wazi kwa sababu Lili alikuwa akimpatia pesa mara kwa mara na kumsaidia mambo mengi yaliyohitaji pesa kutatuliwa.

    Raha ziliendelea na Tina akazidi kuwa karibu na Lilian na mzee Matata. Wakicheka kunywa na kufurahi pamoja.



    Siku moja Lilian alimwomba ushauri Tina juu ya jambo ambalo alikuwa ameshirikishwa na mzee Matata. Lilikuwa likihusiana na mambo ya filamu. Hakika lilikuwa dili kubwa ambalo Lilian hakuwahi kulipata tangu aanze kucheza filamu.

    Lilian alitakiwa kucheza filamu na wazungu lakini atatakiwa kufanya busu la mdomo kwa mdomo ambalo kitanzania waigizaji wake hawaruhusiwi kufanya vile.

    Kwa kucheza filamu ile angelipwa kiasi cha dola za kimarekani laki moja ambazo ni zaidi ya milioni mia moja za kitanzania.

    Tina aliposikia juu ya dau lile, mate yakamtoka kwa tamaa akatamani mchumba wake Sam angemruhusu na yeye kujiingiza katika masuala ya filamu. Lakini Sam hakutaka kabisa mambo hayo!!

    Tina kwa kutambua kuwa Lilian atampatia kiasi fulani cha pesa baada ya kulipwa, akajikuta akimpa ushauri wa kukubali.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Kwani kubusu nd’o nini, mbona kina Angelina Jolie wanafanya makubwa zaidi ya hayo. Cha msingi filamu sio ya bongo basi… huo nd’o uigizaji bwana watu wanapata pesa kama hivyo. Shoga!! Usiache” Tina akamshauri Lili

    Umri wa Lilian ulikuwa mdogo na uwezo wake wa kufikiri ulikuwa mdogo vilevile. Akasahau ule usemi wa akili za kushikiwa changanya na za kwako.

    Akajipeleka kuusaini huo mkataba huku akitabasamu na kujitapa katika vyombo vya habari kuwa muda si mrefu atakuwa kama nyota wa ‘Hollywood’.

    Kilichokuja kutokea pale ikabaki kuwa siri ya watu watatu!

    Lilian muhusika mkuu, Tina mshauri na Mzee Matata mzalishaji wa hiyo filamu.

    Liliani akaleweshwa madawa asiyoyajua na kisha kuchezeshwa filamu ya ngono!!

    Filamu ambayo ilikuwa na maana kubwa sana katika kubomoa na si kujenga. Filamu ambayo mkono wa mtu mzito serikalini ulisimamia ifanyike ili kulisulubu tabaka fulani.

    Baada ya filamu ile, Lilian akaanza kuishi kama mtumwa!

    Kila aliloambiwa alitakiwa kulitii, kwa nje alionekana mrembo na mwenye tabasamu muda wote lakini ndani ya moyo wake alikuwa katika kifungo kibaya mno.

    Alikuwa anateketea.



    Angefanya nini wakati kuna mkanda ambao ameigiza filamu ya ngono, alitishiwa kuwa akikataa jambo lolote lile mwisho wa siku mkanda ule utasambazwa Tanzania nzima.

    Onyo lile likamtetemesha Lili na kuondoka na uhuru na amani yake. Hakutaka hata kidogo kuchafuliwa jina lake, alitamani kurudisha siku nyuma ili akatae dili lile lakini neno ninge huja mwisho wa safari.

    Lili alikuwa mwishoni!

    Tina aliijua ile siri, akapewa onyo na Lilian kuwa ajitahidi mtu asijue juu ya jambo lile.

    Wasichana na siri wapi na wapi?

    Tina naye akamshirikisha mama yake juu ya jambo lile!!

    Wakadhani siri inaweza kutunzwa na watu wawili.

    Baada ya Lilian kutambua kuwa yu kifungoni basi akaamua kuwa mtumwa safi. Kila alichotakiwa kufanya alitii ilimradi kuwafurahisha wanaoshikiria mkanda ule.

    Safari hii akatakiwa kumshawishi muigizaji mwenza Steven Marashi hadi ajikute katika penzi lake. Hakujua ni kwa nini anatakiwa kuanzisha mahusiano na kijana yule ambaye alikuwa akimzidi miaka mingi.

    “Lakini jamani ananizidi sana mbona mnanionea…” alilalamika Lili baada ya kupewa mtihani ule.

    “Anakuzidi, wewe umelala na mababa wangapi leo hii unasema Steve mkubwa kwako…”

    “Noo Matata sio kama unavyodhani lakini naheshimiana naye kama kaka yangu tena kaka mkubwa…”

    “Ok! Kwa hiyo umekataa…” Mzee Matata akamuhoji huku akitabasamu.

    Lili akajua mzee Matata amekasirika tayari. Akampooza na kukubali kuwa atayaanzisha mahusiano.

    Utumwa ukaendelea!!!



    Hatua kwa hatua, mara ikaundwa filamu wakacheza pamoja. Mara ghafla wakatakiwa na kampuni moja nchini Ghana, Lili kaambatana na Steven marashi wakiwa wasanii pekee kutoka Tanzania.

    Ni huko ambapo uvumilivu ulimshinda Steve na kujikuta akiibanjua amri ya sita na kisha kuyaanzisha mahusiano ya siri na Lili ambaye kiumri alikuwa mdogo wake sana.

    Mapenzi kikohozi hayafichiki hata kwa dawa!

    Hatimaye uhusiano ukawa wazi, Steve na Lili. Lili na Steve.

    Steve Marashi naye akasahau kuwa mapenzi kitovu cha uzembe. Akajisahau ni kwa nini alijiingiza katika uigizaji, akajisahau kuwa yeye ni mwanausalama wa taifa na katika filamu alikuwa chini ya mwamvuli ule ili aweze kuyafanya mambo yake vyema.

    Penzi la Lili likamkolea, hakujua kuwa Lili alikuwa akitumiwa ili aweze kumpeleleza.

    Mpelelezi yule akaanza kupelelezwa!!

    Lilian akawa anategea wakiwa chumbani, anamuandalia mambo ambayo hakuwahi kufanyiwa na wasichana wake wa huko nyuma. Kisha kumchimba hapa na pale.

    Yale mambo yakasababisha Steve aachane na Mariam, msichana aliyedumu naye penzini kwa muda mrefu kiasi. Ikawa Lili na Steve, Steve na Lili. Magazeti ya udaku yakabaki kuwaandika kila kukicha.

    Shambulio baya ambalo Steve hakujua kama ni shambulio lilifanyika nchini Uganda. Kama kawaida Steve na Lili waliitwa kwa ajili ya kufanya filamu.

    Shambulio lenyewe nalo liliandaliwa kama filamu ya pili isiyokuwa na mpiga picha wala muongozaji.

    Kwanza ilianza shughuli iliyowapeleka Kampala, kutwa nzima wakashinda mbele ya kamera wakitengeneza filamu. Kazi ikakamilika.

    Usiku wakakutana wasanii wote pamoja na wawezeshaji wa filamu ile kukamilika. Walikutana kwa ajili ya kupata chakula.

    Pia wakacheza mziki kidogo.

    Lili alimuona msichana mmoja akimkumbatia Steve wakawa wanacheza mziki. Lili akaipata sababu.

    Ni hapo ambapo Lili aliianzisha filamu ya pili. Filamu isiyokuwa na wahusika wengi sana, bali wawili tu. Akaacha kunywa kinywaji chake, akatafuta meza nyingine akahamia hapo na kujiinamia.

    Mwanamke akauvuta mdomo!

    Steve alipomuona akagundua tayari Lili wake amekerwa na jambo. Alipoenda kumsemesha Lili hakujibu kitu zaidi ya kuzidi kuuvuta mdomo. Kisha ili kuifikisha ile filamu sehemu nzuri zaidi, Lili akamponyoka Steve na kukimbilia chumbani.

    Hakujua kuwa Lili alikuwa kazini.

    Akamfuata huko na kuanza kumbembeleza. Lili akaanza kumlalamikia Steve kuwa amemuacha yeye amekaa halafu akaenda kucheza na watu wengine.

    Steve ndani ya moyo wake alilipuuzia jambo lile lakini kwa nje alilazimika kumbembeleza Lili. Alitambua kuwa hata umri nao ulichangia.

    Katika kubembeleza mara amguse hapa mara kule.

    Lili akaanza kuyajibu mashambulizi!

    Alimfinyafinya Steve mgongo wake kabla ya kuanza kumshambulia kwa ulimi mkali katika kona mbalimbali za mwili wake huku machozi yakimtoka na kilio cha kwikwi kikisindikiza.

    Kila Steve alivyojaribu kujibu mapigo alikutana na pigo jingine jipya kabisa kutoka kwa Lili.

    “Ni kitu gani unataka nikufanyie Steve mpenzi wangu.. unaitaka roho yangu eeh!” alilalamika Lilian.

    Ama! Wanawake ni sumu kali hakika!

    Steve akalegea kabisa, akaanza kuweweseka na kujibu kila kitu ambacho Lilian alikuwa akimuuliza.

    “Baby… kwani we ulisomea filamu ulipokuwa uingereza… niambie ukweli mpenzi wangu. Mbona mimi wanijua kwa kila kitu…”

    “Hapana mpenzi sema nikikwambia kazi yangu mi utaniacha… lakini huwezi amini Honey mimi mtu safi kabisa.”

    “Mh! Kazi gani sasa hiyo hadi isababishe kuondoka na penzi langu kwako…” Lilian alinong’ona katika masikio ya Steve, kisha akauingiza ulimi katika sikio la Steve.

    Wacha wee!! Steve akasisimka mwili mzima. Na palepale Lili akaupenyeza mkono wake na kuzikamata ikulu za Steve.

    Naam! Mwanaume akasalimu amri na hapo mpelelezi yule akageuka chiriku. Akajieleza hata ambavyo hajaulizwa.

    Steve akaelezea hadi nia yake ya kujiingiza katika filamu na hapo akayasema mashaka aliyonayo dhidi ya raisi mtarajiwa bwana Mathias Obhare.

    “Yaani mpenzi wanguu… oooh! Huyu Mathias huyu naamini kabisa amemfanyia mtimanyongo Msele na ile kesi ya kutekwa ni ya kuundwa tu… ninachohisi raisi na Mathias Obhare wanao mpango fulani wa kubebana, na lazima kuna kitu wanaficha nd’o maana…..aaah!” hakuweza kuendelea Lili alikuwa ameshalipata jibu alilokuwa ameagizwa na mzee Matata. Na palepale akamrukia kifuani kwake wakiwa uchi wa mnyama kisha…. Kisha………..mkono ukazikamata ikulu…………

    Asubuhi kila mmoja alikuwa hoi!!

    Mpelelezi akawa amepepelezwa!

    Baada ya tukio hili mambo yakaanza kubadilika kwa kasi ya ajabu.

    Naam hata kabla ya mwezi kumalizika, sasa Tina shahidi wa tukio lote hili ni adui mkubwa wa mzee Matata, hajui Lili alipo, hajui nini kilimuua Steve, hajui Sam wake kama yu hai ama amekufa.

    Alichojua ni kwamba yeye ni mateka wa mzee Matata na hajui hatma yake.



    SASA mzee Matata alikuwa amesimama mbele ya Tina, hapakuwa na urafiki tena bali uadui mkubwa mno.

    Tina alikuwa amekonda sana kutokana na mateso. Alitakiwa aseme ni wapi ambapo ule mkanda wa ngono aliocheza Lilian ulikuwa ukipatikana.

    Tina alikataa katakata kuwa hajui lolote juu ya uwepo wa mkanda ule na alipinga vikali kuwa Sam alikuwa na mkanda ule.

    “Baada ya masaa arobaini na nane nitaigawanya shingo yako mbali kabisa na kichwa chako iwapo utaendelea kuficha siri juu ya wapi ulipo mkanda…. Ni aidha uuseme ukweli ama ufe.” Mzee Matata alimfokea Tina kisha kumzaba kofi kali mgongoni na kuubamiza mlango kisha akaufunga kwa nje.

    Tina alibaki kuikumbuka siku ya kwanza kukutana na mzee Matata akatamani siku zirudi nyuma siku hiyo isijitokeze maishani mwake.

    Akaijutia na siku ambayo aliruhusu kinywa chake kumshauri Lili juu ya dili lile haramu.



    *****



    KIJIJI CHA MAFISA, HANDENI TANGA.



    Mwanaume ambaye umri wake ulikaribia miaka hamsini alikuwa amejikita katika kulima bustani ya wastani ambayo ilikuwa jirani na nyumba ndogo ya tofali za kuchoma.

    Mwili wake ulikuwa umenawiri na alikuwa akitokwa jasho hivyo kusababisha kipara chake kiweze kuonekana vyema.

    Kila alivyokuwa akinyanyua jembe na kulikita katika ardhi alikuwa akisindikiza na wimbo wa kabila lake.

    Alionekana kufurahia wimbo ule na hivyo kasi yake katika kulima ikaongezeka maradufu.

    Hatua zilizosikika nyuma yake zilimsimamisha kulima, akageuka na kukutana na sura ambayo haikuwa ngeni sana machoni pake, lakini hakujua ni wapi walikwahi kukutana ama bwana yule alimuona wapi hapo kabla.

    “Habari kiongozi..shkamoo” kijana alimsalimia yule mzee kwa nidhamu ya hali ya juu.

    “Marahaba bwana.. wewe si mgeni machoni pangu lakini sidhani kama ni kijana wa hapa kijijini kwetu….” Alijibu yule mwanaume mtu mzima.

    “Mheshimiwa tumeonana kama mara tatu hivi, niliwahi kukutembelea ofisini kwako… nilikuwa nikiandika makala miaka minne sasa imepita…”

    “Ahaaa ni Samweli ama ni Samson…. Kama sijakosea…”

    “Samwel Mbaule mheshimiwa…..” alijibu yule kijana huku akifurahia kutambulika mapema tofauti na alivyodhania

    Mbele yake alikuwa ni John Masele, waziri wa zamani wa mambo ya ndani na nje ambaye kipindi cha miaka mitatu iliyopita alitangaza nia ya kugombe uraisi lakini yakatokea mambo ya ghafla na hatimaye kuvuliwa vyeo vyote alivyokuwanavyo, mwishowe akaamua kulikimbia jiji na kurejea kijijini kulima.

    “Sura yako haibadiliki Sam…. Ni kipi kimekuleta huku kijijini kwetu ambapo hatujui hata Tanzania inaendaje.”

    “Ni wewe mzee nimekuja kwako…. Nimehangaika sana lakini kupitia ile makala nliyofanya na wewe nimeweza kukumbuka ulisema juu ya kijiji cha Mafisa kuwa ukistaafu utakuja kulima huku. Naam! Nimefanikiwa kukupata…nimejaribu tu kama pata potea kwa sababu bila kukuona wewe mambo yanaweza kuendelea kuniwia magumu”

    “Sam, mbona unahatarisha maisha yako sana…. Hapa si mahali salama hata kidogo. Ni watu wachache sana wanaoweza kuonana na mimi kisha wakaendelea kuishi kwa amani…. Wewe si mwandishi wa kwanza kufika huku… waandishi wangapi umewasikia wamekufa kwa ajali za gari, wangapi umewasikia wamepigwa risasi na jeshi la polisi kwa kisingizio kuwa ni bahati mbaya… hao wote wamekufa na siri zao Sam”

    “Natambua sana mzee wangu lakini tayari nipo hatarini sitakiwi kurudi nyuma mzee. Hata nikisema nikomee hapa nilipoishia sanasana nitaishia kumpoteza mchumba wangu ambaye yu mikononi mwa watu wabaya”

    “Sam ondoka sasa hivi kama hujaonana na mimi kisha saa mbili na nusu usiku njoo tukutane eneo hilihili, na baada ya kukutana huko naomba uishi na kauli moja kichwani mwako ya kwamba hujawahi kukutana na mimi popote pale. Sahau kabisa kama tulionana…. Hata ukibanwa vipi nakusihi jibu lako liwe hujawahi kuonana name, na mimi nikiulizwa nitasema sijawahi kukutana na kiumbe kama wewe maishani”

    Sam akatii na kuaga!!

    Majira ya saa mbili na nusu ndani ya giza kali wakakutana shambani kuzungumza!!

    Walizungumza kwa utulivu wa hali ya juu wakiamini kuwa walikuwa wao peke yao.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    ****



    BAADA ya mazungumzo mafupi lakini mazito na John Masele waziri wa zamani wa mambo ya ndani na nje. Sam alichukua pikipiki ambayo ilimfikisha Handeni Tanga.

    Ulikuwa mwendo mrefu lakini kwa ushauri aliopewa na John kuwa eneo lile halikuwa salama basi ilimlazimu kufanya vile.

    Saa nne usiku alikuwa akitetemeka kutokana na baridi kali maeneo ya Handeni kwa kipindi kile.

    Alikuwa amejifunika shuka zito katika nyumba ya kulala wageni ambayo ilikuwa pembeni kidogo na mji.

    Akiwa ndani ya blangeti, Sam alitoa faili alilokabidhiwa na John Masele, kisha akakitoa na kile kinasa sauti chake ambacho alikuwa amekitega katika kile chumba ambacho Gama alilipukiwa na bomu.

    Alianza kwa kusikiliza tena upya harakati zote zilizofanyika katika chumba kile tangu alipokitega kinasa sauti kile.

    Ukimya ulidumu kwa muda mrefu hadi pale alipoyasikia mapigano makali ndani ya chumba huku matusi yakitawala ugomvi ule.

    Baadaye akaisikia sauti ikihoji kwa ghadhabu juu ya nani aliyewaagiza na amewaagiza nini katika kile chumba.

    “BVB” akalisikia lile jibu.

    Na hapo akakumbuka maongezi yake na mama lao. Mama yule alimweleza kuwa aliyepo nyuma ya mambo hayo alikuwa ni BVB.

    Sam akakizima kinasa sauti kisha akalifungua faili na kuanza kusoma. Kadri alivyozidi kusoma ndivyo baridi lilivyouacha mwili wake na kisha kutawaliwa na joto kali.

    Hii ni baada ya kukutana na jina la mtu ambaye alidhamini kampeni za chama tawala wakati raisi aliyepo madarakani alipokuwa akiwania kiti hicho.

    Ndugu Benson Van Bronchost raia wa uholanzi.

    Sam akarejea kulisoma mara mbilimbili lile jina na kujikuta akizinasa herufi B.V.B.

    Naam! Hatua moja mbele katika kulitafuta jibu.

    Kisha akayakumbuka mazungumzo mafupi na John Masele juu ya hila alizofanyiwa ilimradi tu asiingie ikulu.

    John Masele alimweleza Sam kuwa ni maslahi binafsi yaliyosababisha awekewe zengwe na kubwa zaidi ni uswahiba kati ya raisi aliyepo na mtarajiwa raisi.

    “Uliwahi kumfahamu hayati Steven Marashi…” lilikuwa swali kutoka kwa John Masele.

    Sam akakubali kuwa anamfahamu kama muigizaji wa filamu.

    “Alikuwa zaidi ya hapo, na laiti angeendelea kuwa hai mambo yangekuwa mengine wakati huu. Yule kijana alikuwa mpinga maovu sana, na hata wenzake katika jopo la vijana wa usalama wa taifa walikuwa wakimchukia. Tatizo alikuwa makini sana, hivyo hawakuweza kuzigundua nyendo zake. Steven alikuwa amefikia hatua nzuri sana alikuwa na picha za video za watu hawa wabaya. Huu ushahidi ungekufaa sana katika kufanya ukombozi…”

    Mzee Masele akasita kidogo kisha akawa mwenye kuzungumza mwenyewe, “Tatizo mapenzi, haya mapenzi haya nilitamani sana kumkanya lakini hakuwa mtu wangu wa karibu sana hasahasa katika mambo binafsi”

    Sam akayakumbuka mazungumzo hayo na kutambua kuwa bado safari ilikuwa ndefu hadi kuupata ukweli. Lakini kitendo cha kutambua kirefu cha BvB basi alijua ni hapo anapoweza kuanzia.

    Akaendelea kuyafungua yale mafaili akakutana na baadhi ya picha zilizochongwa kutoka kwenye magazeti kadha wa kadha, baadhi ya picha zilimwonyesha John Masele enzi zake za uwaziri akiwa pamoja na raisi na waziri wa nishati na madini bwana Mathias Obhare.

    Picha nyingine zilimwonyesha raisi akiwa ikulu pamoja na wazungu watatu wote wakiwa katika tabasamu zito.

    Picha nyingine, hii ilikuwa picha ya rangi kabisa na haikunokena kuwa ya kukatwa kutoka katika gazeti. Hii ilimwonyesha raisi akiwa hoteli ambayo kwa mtazamo tu wa kijografia ilionekana si ya afrika. Alikuwa na wazungu wawili wakitabasamu Picha zote hazikuwa na maelezo yoyote yale.

    Mara akakutana na picha nyingine, hii sura haikuwa ngeni hata kidogo machoni pake.

    Alifumba macho na kukigongagonga kichwa chake ili aweze kukumbuka ni wapi aliwahi kuiona sura ile kwa mara ya kwanza.

    Akavutia picha mikutano kadhaa aliyowahi kuhudhuria, hakuipata sura ile. Akawakumbuka baadhi ya wanasiasa bado haikuja ile sura.

    Labda sijawahi kuiona! Alijisemea… lakini mara jicho lake likatua katika mkoba wake, akakumbuka kuwa ndani ya kile kimkoba palikuwa na filamu ya ngono.

    Hapohapo akaikumbuka sura ile…. Ile sura ilikuwa miongoni mwa walioshiriki kufanya ngono na Lili huku wakirekodiwa.

    “Ni nani mtu huyu.. eeh ni nani wewe mwanaharamu usiyekuwa na haya wewe… ni nani wewe ukaenda kucheza ile filamu bila aibu.

    Tazama upo ikulu, hukujua kama ikulu ni sehemu takatifu we uliyelaaniwa… “

    Akaigeuza ile picha kwa nyuma kutazama kama kuna maelezo yoyote lakini hakuambulia kitu.

    “Mzee Masele nawe mbona wataka kunitia uchizi sasa eeh! Mbona mtihani unazidi kuwa mgumu, halafu hata namba ya simu hukunipatia we mzee… hivi unataka nije tena huko kijijini ama?” Sama alizungumza peke yake, kichwa kikiwa kinamuuma haswa.

    Akapekua kibegi chake na kutoka na tembe maalumu kwa maumivu ya kichwa akameza!!

    Akalala huku akijipangia ratiba kuwa asubuhi na mapema atatafuta kibanda chenye huduma za internet aweze kumchimba huyo BvB na atambue ni wapi pa kupiga hatua nyingine.

    Pia aliamini kuwa akiwa kwenye mtandao atatafuta muafaka wa zile picha nyingine.



    ****



    MAJIRA ya saa nne asubuhi Sam alikuwa katika kibanda chenye huduma za internet jirani na kituo kidogo cha mabasi Handeni, alilipia huduma ile kwa saa zima ili aweze kufanya mambo yake kwa utulivu. Akatwaa nafasi yake, dada mfupi muhudumu wa pale akafika na kutazama saa na dakika ambayo Sam alikuwa ameanza kutumia huduma ile.

    “CD Rom inafanya kazi eeh” Sam akamuuliza yule dada.

    “Nini?” akauliza badala ya kujibu.

    “Huu mlango wa kompyuta unafanya kazi…” Sam akalainisha lugha kidogo.

    “Yes of course..” alijibu yule dada kwa madoido, kisha akatoweka na kwenda kwa mteja mwingine.

    Alianza kwa kuliandika jina la Benson van Bronchost kwenye GOOGLE. Yakatokea majibu mengi sana, majina ya wacheza soka, wanamuziki wa kiholanzi na mengineyo mengi.

    Akaghairi na kuandika ‘Benson van Bronchost Tanzania’

    Alipolitafuta jina lile akaambulia majibu kuwa ‘no match found’. Akatazama huenda amekosea herufi japo moja lakini hakuwa amekosea chochote.

    Hapakuwa na kitu kama hicho nchini Tanzania!!

    Sam akashusha pumzi kwa nguvu na kulegea mwili. Matumaini yakaanza kufifia tena.

    Iwapo mtandao umeshindwa kumng’amua BvB yeye ataanzia wapi kufanikisha hilo kwa kutumia akili yake ya kawaida.

    Alibaki akiikodolea macho kompyuta, alipotazama dakika aligundua kuwa alikuwa ametumia dakika kumi tu na alikuwa na dakika hamsini za ziada. Kichwani akakiri kuwa huyo wa kuitwa BVB alikuwa makini sana na mambo aliyokuwa anayafanya. Na kile kitendo cha mtandao kushindwa kumtambua maana yakea likuwa akiyafanya mambo yake kwa uangalifu.

    Baada ya hapo akaingiza tena jina la raisi wa Tanzania, kisha akachagua kuona picha za raisi akiwa na wawekezaji wan je.

    Zikatokeza picha nyingi sana, akapekua kibegi chake na kuanza kufananisha picha alizonazo na zile za kwenye mtandao.

    Picha moja tu nd’o ilipata ufanano wake. Sam akategemea kukutana na maelezo juu ya picha ile lakini akakutana na hali kama ile ya picha aliyokuwa ameishikilia.

    Duh! Sam akaguna!! Kisha akajilazimisha kucheka ilihali macho yalitaka kumtoka kwa hasira.

    Sam akatamani kuomba arudishiwe pesa yake lakini aliamini kuwa hataeleweka.

    Akaamua kutumia muda ule kufanya mambo ambayo hakupanga kuyafanya. Kwanza alitaka kuitazama ile CD ya ngono ili aweze kuitambua ile sura iwapo ni yenyewe ama la akaitoa cd yake, mara akasita. Wingi wa watu katika kibanda kile Sam akajisikia aibu kuitazama na pia kujulikana sana la Lili kungezua maswali kwa wale ambao wangetupia jicho na kutambua kinachoendelea.

    Heri nusu shari kuliko shari kamili! Sam akajiepusha na hilo.

    Moja kwa moja akaona ule haukuwa wakati muafaka kufanya vile.

    Sam akaingia katika anuani yake ya barua pepe. Yote hii ni kupoteza muda ilimradi tu asiondoke huku nafsi yake ikimuuma sana, kutokamilisha lengo na pia kupoteza pesa bure.

    Alikuta akiwa na takribani barua pepe tisa ambazo hazijasomwa.

    Alitaka kuzipuuzia na kufanya mambo mengine lakini akavutiwa na moja iliyoandikwa.

    ‘MUHIMU SANA SOMA’

    Haikumshtua sana barua pepe ile, kwani hilo lilikuwa neno la kawaida tu la kusisitiza. Ni vile tu muda ulikuwa unaruhusu nd’o maana Sam akaisoma.

    Kwa sababu muda uliruhusu alijikuta akiifungua ile barua, akakutana na maelezo marefu kiasi lakini ambayo yalikuwa yanasisimua.

    “SAM, bila shaka utaipata barua hii ukiwa katika harakati zako za kizalendo.

    Nimekuandikia wewe haya ili ubaki na ushahidi huu hata nikiuwawa ama nikifungwa maisha jamii ibaki na shuhuda wewe wa kuwaeleza ukweli. Nimekuandikia wewe kwa sababu sijawahi kukuona ukiogopa, na kubwa zaidi u mtetezi wa wanyonge.

    Sam, nchi hii imegawanwa, sio ya kwetu watanzania. Tunatawaliwa upya kisirisiri, uhuru wetu ni wa bendera tu!

    Raisi, makamu wake, mkuu wa majeshi na wengineo wote wakubwa wamekuwa vibaraka. Wanawalamba miguu wazungu, wanawasikiliza kwa kila jambo hata kama ni kuhusu kuua watanzania wenzetu. Waone wanavyopendeza na suti zao kwa nje lakini ni watumwa walioozea katika utumwa. Wanatabasamu mbele yetu weusi, wanalia kwa weupe.

    Kisa wanawalamba miguu weupe basi wanataka na sisi tuwalambe wao! Hali inatisha kijana wangu.

    Mzee Matata nd’o raisi wako Sam, huyo raisi jina anamtetemekea mno na hana la kusema dhidi yake.

    Ninakuambatanishia ushahidi wa simu nilizozungumza na IGP najua ni hatari lakini nakuamini wewe, sikiliza anavyomnyenyekea mzee Matata. Halafu ujiulize je hii nchi imeuzwa?

    Mzee Matata ni nani katika nchi hii hadi atutawale, kuna HILA hapa Sam si bure. Wewe ni mwandishi kijana na mwanamapinduzi amka sasa!

    Steven Marashi ana roho kama yako, ya kiukombozi. Tazama wamemuua, Yakubu Gama alivyojaribu kufuatilia na yeye wamemuua. Kuna nini hapo unadhani.

    Sam ni wewe unayesadikiwa kuwa una nyaraka za marehemu Steven Marashi, kama ni hakika basi zifanyie kazi sasa kabla nchi haijamezwa na wakoloni wenye roho mbaya za kiuaji kuliko wale wakoloni wa kijerumani.

    Nakutakia utendaji mwema!!

    Usijihangaishe kujibu barua hii maana haitasomwa!”

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Sam alisisimka mno, damu ikachemka na akili ikachangamka upya.

    Upesi akanunua ‘flash disk’ akaipachika katika tundu la kompyuta na kupakua ile barua pamoja na zile sauti ambazo zilikuwa zimerekodiwa na mtu ambaye hakujitambulisha jina.

    Sam alitumia akili ya ziada sana maana hakutaka kumuamini mtu kwa asilimia zote. Hata hii barua hakutaka kuamini kwa asilimia zote inatoka kwa mtu mwema.

    Baada ya kupakua (download) na kuweka katika flash disk yake alitoweka na kuchukua chumba katika nyumba ya kulala wageni nyingine kabisa. Aliingia nyumba isiyokuwa na hadhi ya juu.

    Alikuwa na maana yake!

    Alikumbuka kumuuliza yule dada iwapo mida ya jioni ofisi yake itakuwa wazi, yule dada akajibu kuwa atakuwepo.

    Sam akaondoka!!!



    *****



    ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog