Search This Blog

Tuesday, 14 June 2022

JERAHA LA HISIA - 5

 





    Simulizi : Jeraha La Hisia

    Sehemu Ya Tano (5)









    SAMSON MASHIMI alijiona kuwa amefanya jambo kubwa na la muhimu sana katika maisha yake ya kazi ya ulinzi. Kitendo cha kuonekana muhimu katika jamii alikuwa akikitamani tangu akiwa kijana mdogo. Aliwahi kutegemea kuwa ataonekana muhimu kwa kusoma hadi kidato cha sita badala yake akaaibika kwa kupata matokeo mabaya.

    Akajiona wa muhimu kuingia katika jiji la dare s salaam, kwa lengo la kufanya kazi lakini huku napo akageuka mzigo. Hakuwa na umuhimu wowote ule.

    Hatimaye akapa kazi ya ulinzi ambayo kwa mtazamo wake ilikuwa kazi ya kidhaifu sana. lakini angefanya nini iwapo kazi ambayo anaiona ni ya muhimu kwake hawezi kuipata kwa vigezo vyake.

    Katika kazi hii umuhimu wake ungeweza kuonekana iwapo angekamata majambazi na kuyafikisha katika mkono wa dola. Jambo ambalo hakutaka kukumbana nalo aliamini kuwa angeuwawa hata kabla hajajaribu kupambana.

    Kweli haikutokea mapema kama alivyokuwa akikesha na kuomba.

    Lakini linakuja kutokea hili la utata. Polisi wanamuhadaa na kumpa kipaumbele. Anaamriwa kutoruhusu mtu yeyote kuingia katika nyumba ya Walter bila sababu za msingi. Na kama akiingia basi apige simu polisi waweze kumuuliza ni kipi alikuwa amefuata.

    Lilian akajiingiza katika domo la mamba. Mashimi akaamua kuonyesha kuwa yeye ni nani…aliutafuta umuhimu na kisababu cha kupiga simu polisi.

    Hakujua kuwa Lilian alikuwa mwanasaikolojia na akiolojia alijua mengi kuipita elimu yake ya kidato cha sita ‘failure’ na mikikimikiki ya mgambo hatimaye kuwa mgambo. Wakati anapiga simu Lilian alimuona.

    Wakati akingoja majibu ya simu ile Lilian akafika. Mashimi akajifanya mjuaji akafunga geti, mwisho wa siku akakumbana na dhahama ya kuzamishiwa sindano kali katika mwili wake mara mbili.

    Maumivu makali kupita yote tangu azaliwe. Kibaya zaidi alichomwa na mwanamke. Akaruka huku na kule, mwanamke akatoweka.

    Badala ya kuheshimika akadharaulika tena. Wale askari aliowapigia simu kuwa yule mtu aliyekuwa amemteka Walter na ambaye anaweza kuwa anajua chanzo cha lile varangati alikuwa amerejea, walipowadia upesi upesi walikutana na mada nyingine. Yule mtekaji alikuwa amemsulubu mlinzi.

    “Pumbavu kabisa yaani una rungu halafu mwanamke anakudhalilisha…mshenzi kabisa wewe” askari mmoja alimkoromea yule mlinzi kisha yakafuata matusi mfululizo ya nguoni.

    Askari wale hawakutaka kupoteza muda. Walitoweka huku wakizidi kumwona yule mlinzi ni mpumbavu. Mlinzi hakujua kuwa tayari walikuwa wamekula pesa nyingi sana kutoka kwa wapambe wa Walter ili kufanikisha zoezi lile. Na iwapo wangefanikiwa kumtia mikononi mtu ambaye anahusika na upoteaji wa ghafla wa Dj Walter basi dau lingeongezeka.

    Sasa walikuwa wamekaribia kumpata halafu ghafla uzembe wa mlinzi umesababisha atoweke. Iliwakera.



    ****CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Kigugumizi kilimshika Dokta Suzi akajiuliza tena na tena iwapo aende kuokoa maisha ya Suzi ama atoweke na kujiweka mbali na mkasa huu wa kustaajabisha ambao ulianza kama utani lakini sasa unazua madhara makubwa. Ulianza na watu wawili lakini sasa wachezaji wa mchezo huu walikuwa wanaongezeka. Kila alipoongezeka mchezaji mmoja aliongeza madhara na kuufanya mchezo huu kuwa mgumu.

    Ile hali ya kuwekewa kauzibe na mlinzi huku hapo kabla akionekana kuzungumza na simu na watu ambao Lilian aliamini kuwa walikuwa ni maaskari. Hali hii ikamsababisha Lilian ajione kuwa ni mpuuzi ambaye anataka kulifuata gereza.

    Lilian akakumbuka jinsi alivyokuwa akipata nafasi ya kuwaona wafungwa wakihudumiwa katika hospitali kadha wa kadha. Majeraha yao mengi yalitokana na vipigo.

    Vipigo kutoka kwa wafungwa wababe. Lilian akajiona yu katika orodha ya wasichana dhaifu katika mapambano ya ana kwa ana.

    Kama angepelekwa jela hakika angeteseka sana.

    Uamuzi mgumu ukapita kichwani mwake, hakuwa tayari kufungwa hakuwa tayari kuteseka namna ile.

    Mateso ya ugonjwa wa Ukimwi ambao aliamini kuwa alikuwa akiishi nao yakaonekana kuwa na unafuu zaidi kuliko mateso ya gerezani.

    Lilian akaamua kujiweka mbali na suluba hii.

    Akampatia yule kijana maelezo ya juu juu huku akimuaminisha kuwa baada ya muda atakuwa hapo. Kijana akaridhika na kuondoka zake kwa furaha. Lilian naye akachepuka upande mwingine na kutokomea kuelekea mahali ambapo alipajua yeye mwenyewe. Lengo lake kuu likiwa kuonana na Walter kwanza. Aliamini kuwa ni yeye pekee wa kuweza kutega sikio lake kumsikiliza na kisha kumshauri ama kushauriana juu ya nini cha kufanya.

    Lakini wapi pa kumpatia Walter…nyumbani kwake hayupo na kuna sintofahamu imejitokeza tayari na kamwe hawezi kurejea katika nyumba ile baada ya kuwa amempa suluba yule mlinzi baada ya kumzibia njia.



    ****



    Naomi alipenyeza mitaa miwili na kujikuta yu nyuma ya ile hospitali. Alijipongeza kwa uamuzi wake wa kutoroka ili kukwepa kukutana na uso wa Suzi na mumewe Walter. Naomi hakutaka kukutana na dada yake yule wa damu kwa maovu ambayo alikuwa amemtendea.

    Nafsi yake ilikuwa ikitumaini kuwa Walter ndiye mwanaume sahihi ambaye angeweza kushirikiana naye katika shida na raha pia katika hali ambayo alikuwanayo wakati ule, lakini Walter amemsaliti na kushiriki zinaa na dada yake wa pekee. Dada mwenye virusi vya Ukimwi. Naomi alikuwa anatembea upesi upesi huku akiichukia hali ile ya hofu iliyokuwa inachukua nafasi katika moyo wake.

    Naomi asiyekuwa na aulekeo maalumu ghafla aliijiwa na wazo, wazo ambalo alimini kuwa linaweza kumpa faraja. Wazo la kuhakikisha kuwa anakufa na mtu ama la anashiriki na mtu katika hofu iliyopo.

    Kichwa chake kikawa chepesi katika kufikiri, jeraha la hisia za kufa kwa gonjwa la Ukimwi akaamua kuzihamishia kwa mwingine. Naomi aliamua kutoa adhabu kwa watu kadhaa kabla hajafikia hatma ya aidha kujiua ama kuendelea kuishi kwa matumaini.

    Mtu wa kwanza kabisa katika orodha akawa ni Lilian (Dokta Suzi)…Naomi alijiuliza sana iwapo daktari yule ambaye alikuwa anasimamia afya ya Suzi alitambua kuwa dada yule na mumewe walikuwa wanashiriki zinaa kwa nini hakumshtua ili achue tahadhari mapema. Kwanini alikuwa akizungumza naye huku anatabasamu wakati alikuwa anafahamu fika juu ya mchezo huu.

    Jambo ambalo lilimpa uhakika Naomi juu ya daktari huyu kujua nje ndani juu ya siri iliyojificha ni ile hali ya kulitambua jina la ‘Guda’. Jina ambalo ni Naomi na dada yake pekee walilolitambua.

    Lazima kulikuwa na kitu hapo katikati.

    Safari ya Naomi ikaishia maeneo ya Ubungo,akabahatika kuipata tiketi ya kusafiri kuelekea jijini Mbeya. Nia kuu ikiwa kuonana na Kibwana wa vimwana, ni huyu ambaye alionekana kujua mambo mengi sana juu ya Dokta Lilian.

    Harakati za Naomi zikaanzia kwake.

    Safari ya kuelekea Mbeya.



    ****



    Hali ya hewa ilikuwa tulivu sana. kelele za hapa na pale za watafutaji hazikufanya kero yoyote kwa wapita njia kwani hata wao walikuwa katika kutafuta.

    Mwanadada mrefu wa wastani, haiba yake ya kimjinimjini kutokana na mavazi yake ya kisasa alikuwa mmoja kati ya wapita njia. Aliongeza mwendo na kuwapita wenzake. Kisha akachepuka upande wa pili wa barabara akamwita dereva wa pikipiki.

    Akanong’ona kisha akapanda katika ile pikipiki. Ikaondoka kwa mwendo wa kawaida.

    Makalio yake yaliyojichora vyema katika nguo zake yaliacha gumzo kwa wapita njia wengine. Alijua anatamanisha sana lakini hakujali.

    Pikipiki ilimuacha mita kadhaa kabla ya kuifikia hospitali ya mkoa wa Mbeya. Alimlipa kisha akakaza mwendo kuingia ndani. Akaifuata njia ambayo alipita siku ya mwisho kutembelea ile hospitali akafuata ofisi ambayo alikuwa ameitembelea mara ya mwisho kwa lengo la kuonana na dokta Suzi lakini sasa alihitaji kumuona Kibwana kwanza..lakini hata kama hatakuwepo basi alihitaji kujua ni wapi anaweza kumpata kwa uhakika.

    Simu zote za Kibwana na dokta Suzi hazikuwa zikipatikana. Na hii sasa ilikuwa pata potea.

    Akaifikia ofisi akamkuta mwanamama mkongwe kiasi akiwa na mavazi meupe akiufunga mlango. Akatazama saa yake ilikuwa saa kumi na mbili jioni. Muda wa kufunga ofisi ile.

    “Samahani mama…shkamoo…” Naomi alisalimia. Yule mwanamke akaweka miwani yake sawa kabla ya kujibu… “Marahaba..karibu..” alijibu huku akimdadisi kwa kutumia macho yake binti aliyekuwa mbele yake.

    “Asante namuulizia Dokta Kibwana….” Alitetereka Naomi wakati anazungumza.

    Jina lile lililotajwa likamshtua yule mama, kwa mara nyingine tena akaiweka sawa miwani yake.

    “Nani Kibwana……hebu ngoja…karibu ndani..” alisema mengi upesi upesi. Naomi alipatwa na mashaka lakini mashaka yasokuwa na tija. Kuna jambo alihisi lakini hakujua ni jambo gani. Akaingia katika chumba alichokaribishwa.

    “Ngoja nikamuite….” Yule mwanamke alimuaga Naomi.

    Naomi akatikisa kichwa kukubali.

    Yule mwanamke alipopiga hatua moja nje, ghafla akaufunga ule mlango kama anayejaribu kuurudishia.

    Kuja kugutuka Naomi anajikuta yu ndani ya chumba ambacho kimefungwa kwa nje. Akapagawa. Kuna nini mahali hapa? Akajiuluza.

    Akamuita yule mama lakini hakujibiwa lolote.

    Naomi akatapatapa huku na kule baada ya dakika zipatazo kumi. Mlango ukafunguliwa, Naomi akatumia nguvu kutaka kupenya lakini akakutana na ulinzi madhubuti.

    Walikuwa vijana wawili wakakamavu. Kabla hajauliza lolote alishtukia mikono yake ikitiwa pingu.

    “Nimekuwaje jamani? Mimi mgeni hapa?”

    “Utaeleza kituoni msichana acha kelele.” Alijibiwa. Aliuliza na kulalamika sana lakini hakuna askari aliyenena naye. Akaingizwa garini kisha kituo kikuu cha polisi.

    Naomi akaandikiwa maelezo ya vitu alivyokuwa navyo. Kisu kidogo katika pochi yake.

    “Huyu aliagizwa kumuua jamaa ili wapoteze ushahidi ok….” Askari mmoja alisema kwa sauti ya chini wakati akiendelea kuandika mali za Naomi.

    Baada ya hapo akaingizwa mahabusu.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Balaa lililomkumba Naomi ulikuwa muendelezo wa msako mkali dhidi ya wachunaji ngozi za wanadamu, uasi ambao ulikuwa umetapakaa katika jiji la Mbeya.

    Kati ya watu wote ambao walichunwa ngozi ni mwanaume mmoja tu ambaye aliponea katika tundu la sindano na hatimaye kutoa neno kwa watu wa usalama.

    Huyu alikuwa ni Kibwana wa Vimwana. Baada ya kufanyiwa umafia na Dokta Suzi huku akiminywa na kulegezwa kabisa maungo yake ya uzazi ambayo kamwe yasingeweza kufanya kazi. Akapoteza fahamu kwa masaa zaidi ya kumi na mbili, muhudxumu wa hoteli akaligundua tatizo hilo. Kibwana aliporejewa na fahamu na kujikuta hospitalini alitoa maelezo kuwa kuna mwanamke alimlaghai na kutaka kumchuna ngozi, laiti kama zisingekuwa purukushani za kuruka naye huku na kule basi angekuwa mfu.

    Mlinzi wa hoteli ile maarufu mjini Morogoro aliunga mkono taarifa hii kwa kudai kuwa mwanamama yule alifuta nambari zake za gari katika kijitabu cha orodha ya gari zinazoingia na kutoka.

    Msako ukaanza rasmi wa kulisaka kundi hilo hatari lililosadikiwa kuongozwa na mwanamke. Wakati Kibwana akiwa na siri nzito kifuani alifanya kungoja matokeo iwapo atatakiwa kumtambua Suzi baada ya kukamatwa kwake.

    Kibwana aliusita sana juu ya ushahidi wa Suzi kwani alimini kuwa haitakuwa kazi rahisi kwa jamii kukubali kuwa Suzi anaweza kuwa anahusika katika uchunaji ngozi. Lakini Kibwana aliamua kulipa kisasi kwa namna ile ya kipekee iliyomjia bila kutegemea.

    Ulinzi ukaimarishwa kila mgeni aliyejipeleka hospitali kumuulizia dokta Kibwana alitiwa mahabusu kisha akapigwa maswali kadhaa huku Kibwana akipelekewa baadhi ya picha aweze kutambua iwapo anaweza kuwa yule mwanamke.

    Kibwana alikuwa daktari anayeheshimika sana licha ya tabia zake chafu. Za kubadili wasichana hovyo.

    Siku hii ilikuwa zamu ya Naomi kutiwa hatiani, akiwa katika hekaheka za kumsaka Kibwana kwa sababu nyingine kabisa anajikuta mikononi mwa polisi. Kukamatwa kwa Naomi ni tofauti na wahusika waliopita ambao mahojiano kidogo pekee yaliwaweka huru. Ndugu zao walijitokeza kwa wingi.

    Lakini Naomi anakuwa mwoga mwenye hofu, kile kisu kilichokutwa katika begi lake kinamtia katika matata makubwa. Hakuna ndugu wa karibu ambaye alijitokeza. Hakuna mtu ambaye alikuwa anamtambua Naomi katika jiji la Mbeya.

    Hali hii ikawatia morali askari, wakajiaminisha kuwa Naomi anaweza kuwa mmoja kati ya wachuna ngozi. Na kile kilikuwa kisu cha kazi. Kazi ya uchunaji.

    Hekaheka……Naomi katika tuhuma nzito. Jeraha la hisia limemkimbiza na kumtupia katika domo la sheria.



    ****



    ****



    TAARIFA ya daktari bingwa wa magonjwa ya wanawake kunusurika kuchunwa ngozi na mwanamke kiongozi wa kikundi cha wachuna ngozi jijini Mbeya ambao asili yao ni Zambia ilipokelewa katika namna ya mfadhaiko na mwanadada Suzan ambaye alikuwa katika basi akiwa katika safari ya kuelekea jijini Mbeya. Hakufadhaika kwa sababu daktari mwenzake alikaribia kuchunwa ngozi lakini alistaajabishwa na jinsi taarifa ile ilivyosukwa kisasa na kuleta mvuto katika kuisoma.

    Kibwana alikuwa amedanganya kuwa alikuwa amekabwa na msichana akiwa na kikundi chake cha wachuna ngozi. Ilikuwa poneaponea yake kubakia hai.

    Kamatakamata ilikuwa inaendelea na hadi wakati huo watu ishirini walikuwa wamekamatwa kwa shutuma hizo za uchunaji ngozi.

    Lilian ambaye alikuwa anatabasamu kutokana na uongo ule sasa alikunja ndita na kufedheheka. Cheko likatoweka, fadhaa ikatawala.

    Lilian akatawaliwa na hisia zilizomkera, hisia za kusulubisha roho zisizokuwa na hatia. Hakika alikuwa ana uwezo wa kuzikomboa roho hizo zisizokuwa na hatia. Lilian alikuwa na uwezo wa kuubadilisha uongo wa Dokta Kibwana kisha kuwaweka huru wale wasokuwa na hatia.

    Macho ya Lilian yakarejea katika lile gazeti la kila siku. Akaitazama vyema ile orodha ya waliokamatwa wakihusishwa na tuhuma zile.

    Wanawake (9) na wanaume waliosalia. Roho ikamuuma. Maswali kadhaa yakakivamia kichwa chake. Huenda wale wanawake waliokamatwa walikuwa na watoto nyumbani, ama walikuwa ni wajane familia inawategemea.

    Akajiuliza watakuwa katika hali gani. Hisia zikamnyong’onyesha, akauma meno kwa hasira, uongo wa Kibwana ulikuwa unawatesa wengi.

    “Lazima niuweke ukweli wazi….ukweli ambao utaniweka huru.” Lilian akajiapiza huku akifunika lile gazeti. Kisha akaliweka mbali naye.

    Baada ya muda akasinzia huku akijilaani kwa kuziruhusu hisia zake ziweze kutambaa na kumzidi hatimaye zikasimama wima na kumzidi zaidi kisha zikaanza kumpelekesha huku na kule. Akajikuta yu mtumwa wa mapenzi.

    Akaangukia mikononi mwa Walter na kujikuta wakizini kisha akaukwaa Ukimwi. Usingizi ukapaa akaangaza huku na kule, kila mmoja alikuwa na lake jambo.

    Basi lilikuwa likikwea milima ya Kitonga. Lilian akapiga mbewe kisha akachukua maji katika chupa yake akayagida kwa fujo.

    Kisha akajiegemeza tena katika pembe moja ya kiti. Akasinzia tena.



    ****



    MAJIRA ya saa tano usiku, Walter akiwa na koti zito lililomfunika kuanzia mabegani hadi ugoko wa miguu yake, alitembea kwa kujiamini sana na kufanana na walinzi ambao wamefuzu katika Nyanja hiyo.

    Licha ya kwamba ulikuwa ni usiku wa giza kuu lakini hakuyaruhusu macho yake kutoka nyuma ya miwani nyeusi. Akatembea kwa kasi huku akigeuka nyuma mara kwa mara. Hatimaye akafikia mahali ambapo uoga ulichukua nafasi yake.

    Nyumba iliyokuwa mbele yake iliwashwa taa moja ya nje, huku ndani pakiwa na giza. Eneo lilikuwa tulivu lakini liliamshwa na kelee za mbuzi na ng’ombe wa jirani ambao bila shaka walikuwa wameshtuliwa na kitu chochote kile pale zizini.

    Walter aliyekuwa jasiri muda wote hatimaye akaanza kuingiwa na hofu. Akahofia kukutana na mtu ambaye alitarajia kukutana naye. Lakini hakuwa na budi kukutana naye.

    “Nitamuogopaje msichana?” alijiuliza Walter kimyakimya. Swali hili likampa ujasiri wa kuendelea kusonga mbele. Akakaza mwendo. Nia ya dhati ya kukutana na adui yake ikamkumba na kuamini kuwa uoga wake nd’o utayafanya maisha yake kuwa magumu zaidi.

    Walter alikuwa amefikia maamuzi ambayo kwake aliyaona kuwa sahihi kabisa. Alinuia kukimbilia jijini Kampala nchini Uganda ambapo aliamini kuwa alikuwepo ndugu yake pekee ambaye angeweza kumpa ushauri wa mwisho na kama kuna siri inahitajika kufichwa basi ni huyo pekee angeweza kumfichia.

    Walter alihitaji kuonana na mjomba wake wa Kampala. Anko Muganyizi. Ni huyu ndugu pekee baada ya Frank ambaye angeweza kumsikiliza, kumshauri na ikiwezekana kumsaidia kwa namna yoyote.



    Angefika vipi wakati hana pesa? Huenda si sahihi kusema kuwa Walter, Dj maarufu kabisa kuwa hana pesa. Pesa alikuwanayo lakini ilikuwa katika hifadhi salama. Pesa yote ya Walter ilikuwa imehifadhiwa benki. Na kadi pekee ambayo ingemuwezesha Walter kuchota mamilioni yake katika amana yake.

    Kadi ambayo anakumbuka kwa asilimia zote aliisahau Mbeya katika chumba cha Lilian. Walter hakuwa na ujanja alihitaji pesa ili aweze kuondoka jijini.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/Ni kweli alikuwa na marafiki wengi lakini hakuwa na imani nao kutokana na hisia zake za kusakwa na polisi kwa kosa la kujaribu kujiua. Marafiki haohao wangeweza kugeuka maadui na kisha kumchomesha kwa maaskari kisha ajikute matatani.

    Walter akaamua kujipigania mwenyewe.

    Sasa alikuwa ana kwa ana na nyumba ambayo ndani yake aliamini kuwa palikuwa na kadi yake ya benki.

    Akaanza kugonga mlango taratibu hakupata majibu. Akagonga tena bado kimya.

    Nani alikuwa ameiwasha taa ya nje….na nje palikuwa na viatu vya kike, viatu vya Lilian. Ilistaajabisha. Bila shaka pale ndani aidha palikuwa na mtu ama alikuwepo kisha akatoka.

    Walter akajaribu kuutikisa mlango lakini haukufunguka, sasa akaamini kuwa hapakuwa na mtu. Akashusha pumzi kwa nguvu zote. Kisha mikono ikamlegea kwa kukata tamaa. Jitihada zake hazikuwa na maana hata kidogo.

    Na kadri muda ulivyokuwa unasonga ndivyo wasiwasi wake ukazidi kusogea karibu. Hakuwa na pesa ya kutosha walau kumrejesha jijini Dar es salaam vipi kuhusu pesa ya kwenda nje ya nchi?

    Walter akafadhaika. Akanyanyua kichwa chake kutazamana na anga tulivu isiyo na dalili ya kuhifadhi wingu la mvua.

    Anga ikamzomea, akaona haya akarejesha kichwa chini taratibu mara akakomea juu ya mlango. Macho yakatulia katika sehemu ile. Kuna kitu alikikumbuka. Mara yake ya kwanza kufika nyumbani kwa Lilian alimshuhudia Lily akiutoa funguo wa chumba chake juu ya mlango. Mlango huu huu anaotazamana nao mbele yake.

    Kiherehere kikamshika Walter, akauvamia ule mlango akaupitisha mkono wake juu ya mlango akapapasa huku na kule.

    Lahaula…akaibuka na ufunguo halisi wa chumba kile.

    Huku akitetemeka alijaribu kuufungua ule mlango. Aliingiza funguo mara kadhaa bila mafanikio. Hatimaye akajituliza vyema akaweka hofu kando akaweka umakini zaidi. Mlango ukafunguka.

    Chumba kilikuwa kinanukia utuli wa bei ghali. Bila shaka mtumiaji alikuwa ametoka kuutumia muda mfupi uliopita.

    Lilian alikuwa Mbeya? Kumbe alinitoroka na kuja Mbeya? Walter alijiuliza kwa sauti ya juu kiasi. Macho yake yakiangaza huku na kule kana kwamba muda wowote ule Lilian anaweza kukivamia chumba kile.



    Walter alibaki ameduwaa kwa sekunde kadhaa, akili ikiwa katika mnato bila kukumbuka ni kipi alikuwa amekifuata pale ndani. Baada ya sekunde kadhaa akakumbuka kilichomfanya awe jijini Mbeya. Akakivamia kitanda akaanza kupapasa. Akatupa mikoba ya Lilian huku na kule. Hakuna kitu.

    Akatoa godoro akavuta kitanda kwa fujo, akavamia kabati la nguo la dokta Lilian, akatoa nguo pasi na utaratibu maalumu. Akaangusha viatu kutoka mahali vilipohifadhiwa bado hakukutana na kadi yake ya benki. Mara akafikia koba jingine kubwa jeusi, akakung’uta mara zikatoka chupa ndogondogo na kuvunjika, harufu ya madawa ikatawala, mabomba ya sindano yakasambaa huku na kule.

    Lilian ni muuaji? Walter akapayuka. Hakujua kuwa Lilian alikuwa ni daktari mzoefu na vile vilikuwa vifaa vya kazi.

    Hofu ikajijenga upya katika moyo wake. Sasa akaanza kuogopa waziwazi, akaogopa kuwa katika chumba kile. Hali ilikuwa tete.

    Akiwa katika kushangashangaa mara alisikia vishindo vya harakaharaka kuelekea katika nyumba ya Lilian. Wakati anavuta umakini zaidi mara vishindo vikakoma. Walter akajikuta katika wakati mgumu zaidi kuupitia, alijihisia amezungukwa na watu wabaya ambao muda wowote wanaweza kuondoka na roho yake.

    Walter akanyata katika dirisha ambalo pazia lake lilikuwa limeshushwa na hakukumbuka kulifunua hapo kabla. Akalifunua lile pazia taratibu aweze kutazama ni nani yule aliyekoma kutembea ghafla baada ya kuifikia ile nyumba.



    Jicho lake likakutana na kitu ambacho kilimshtua sana, alishtuka kwa sababu hakutegemea kukutana nacho tena. Ilikuwa ni kadi yake ya benki.

    Walter akaduwaa. Lakini hakudumu katika kuduwaa kwake. Zile hatua zilizokuwa zimekoma zikaanza tena lakini sasa katika namna ya kunyemelea. Walter akaingiwa hofu tena.

    Sasa ilikuwa hofu kuu. Mlango wa kile chumba ukatikisika, Walter hakuwa amejiandaa kukabiliana na shambulizi la ghafla namna hiyo.

    Kadi yake mkononi, macho yakitazama mlangoni alikuwa anangoja lolote litakalotokea………

    Mikono ilikuwa inatetemeka sana na akili ilikuwa imekoma kujishughulisha.





    *****



    LILIAN hakuwa na muda wa kupoteza, baada ya kuwa amefika jijini Mbeya majira ya saa moja usiku. Licha ya kuwa na uchovu wa safari ndefu kutoka jijini Dar es salaam bado hakuweza kustahimili kulala huku akisumbuliwa na hatia moyoni mwake. Lilian alijipumzisha kwa masaa kadhaa huku akiwa ameiweka simu yake katika mlio uliotegeshwa kwa ajili ya kumshtua majira ya saa nne usiku.

    Hewala!!…kama alivyotarajia, simu ilimgutua usingizini. Akajikokota hadi bafuni akajimwagia maji vyema na kisha akajipulizia utuli. Safari ya kuelekea Uyole. Nia kuu ya Lilian ilikuwa kuupata mwangaza juu ya Kibwana na shutuma zake juu ya kukoswa koswa kuchunwa ngozi na msichana hatari.

    Lilian alifahamu fika kuwa si Kibwana wala mdogo wake ambaye anaweza kutegemea ujio wake katika kasri yao ya Uyole. Kasri ambayo awali aliitumia sana kuwa anahifadhi gari yake ambayo kwa wakati huu alikuwa ameiacha jijini Dar es salaam kwa sababu za kiusalama. Lilian akautumia mwanya huo wa giza kumtembelea Kibwana kama atamkuta nyumbani kwake aweze kumpa masharti ya kuusema ukweli ili wale watu wema waliokamatwa bila kosa waweze kuachiwa huru.

    Lilian alichukua taksi ambayo ilimpeleka moja kwa moja hadi nyumbani kwa dokta Kibwana. Akalifikia geti la kuingilia nyumba ya Kibwana. Hapo akashuka upesi katika taksi akafanya malipo na kisha harakaharaka akaelekea katika geti.

    Alipoanza kugonga geti mara akasikia hatua nyuma yake.

    “Wewe ni nani?” sauti nzito ya kiume iliuliza kutokea gizani.

    Lilian alipogeuka akakumbana na kiwiliwili kirefu kilichojaa vyema kimazoezi.

    “Wewe ni nani?” sauti ile ikarudia kuuliza tena.

    “Lili…..” alijibu kwa hofu. Majibizano yao yakakatishwa na geti lililofunguliwa.

    “Dokta…..mweee” aliduwaa mtu aliyefungua geti.

    “Akwino….huyu ni nani?” Lilian aliuliza kwa mshangao lakini walau akiwa na afueni ya kumuona mtu wanayefahamiana.

    “Ni afande…Afande huyu ni wa hapa hapa…” Yule kijana akamtoa hofu yule mwanaume mrefu dhidi ya Lilian.

    Mjinga ameharibu akili za watu huyu…Lilian alijisemea huku akiingia ndani.

    Akwino akaghairi safari yake aliyokuwa amepanga. Kiherehere kikamshika akatamani kusema maneno kadhaa na yule mgeni.

    Wakajiweka sebuleni, yule mnyakyusa akaanza kumsimulia Lilian juu ya hali ya afya ya Kibwana. Alipayuka mambo mengi kana kwamba alikuwepo eneo la tukio, “Huwezi amini dokta yaani ilibaki kidogo tumsahau, alipambana huyo aisee….akawashinda sijui wakamchoma sindano gani lakini kwa sasa ana unafuu. Tumuombee kwa Mungu tu aweze kupona. Kwa sasa nd’o kama hivi ulinzi kama ikulu kila muda….na pale nisingetokea haki ya Mungu wangekufunga pingu wale..yaani hawatanii…” Akwino alimaliza kuimba mashairi yake. Lilian akazuga kusikitika.

    “Kwa hiyo umeenda kumuona tayari na yupo hospitali gani…”

    “Nd’o kesho nasafiri zangu nasikia yupo Morogoro huko hospitali ya mkoa. Hebu ngoja uone….” Alijibu Akwino kipengele ambacho kilikuwa cha muhimu zaidi kwa Lilian. Kisha akasimama na kuliendea kabati. Akatoka na bahasha.

    “Kuna picha tunaenda kuzithibitisha…picha za wachuna ngozi.” Akwino akamwonyesha picha kadhaa Lilian. Picha zote zilionekana kuwa ngeni sana kwa Lilian. Lakini picha ya mwisho ilikuwa na utata kidogo. Akaichukua na kuitazama kwa makini sana. picha ile ilifanana na mtu ambaye amewahi kumwona mahali. Alijaribu kuukaataa uhalisia lakini hali ilibaki kuwa ile picha ilikuwa ile anayoifahamu…..

    Laiti kama picha ingekuwa inasema………….

    Akanyanyua macho yake na kuangaza kona hii na ile kisha akamnong’oneza Akwino maneno kadhaa, Akwino akastaajabu lakini Lilian hakuonyesha kwamba ni utani alisisitiza tena. Akwino akafanya tabasamu hafifu. Lilian akasimama na kuaga.

    Akwino akamsindikiza hadi nje.

    Lilian akatazamana na wale maaskari waliotaka kumtia katika varangati hapo awali, akataka kusema nao neno lakini akahisi kuwa halikuwa na umuhimu wowote. Akaamua kuondoka zake huku akiagana tena na Akwino.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Usisahau nilichokwambia…..” Lilian alisisitiza. Akwino ambaye ni mdogo wake Kibwana akatikisa kichwa kuashiria kuwa ameelewa sana.

    Lilian akatoweka. Kwa mwendo uleule wa taksi.

    Hakutaka Taksi ile impeleke nyumbani, badala yake alikifikia kibanda kilichokuwa kinauza vinywaji baridi akashuka na kuketi katika kiti kimojawapo akaagiza soda. Lilian alifanya hivi ili kuwapoteza wale askari iwapo wangefanya hila yoyote ya kumfuatilia bila yeye kujua.

    Alitumia dakika takribani ishirini bila kuona dalili yoyote ya kufuatiliwa. Akafanya malipo upesi safari hii akachukua pikipiki. Akampa maelekezo na kumpeleka hadi mtaa mmoja kabla ya kuifikia nyumba yake. Hapa akaanza kutembea kwa miguuu lakini kwa mwendo wa kasi. Alipoifikia nyumba yake akashtushwa na vurugu zilizokuwa zinaendelea ndani ya nyumba yake. Kibaya zaidi taa iliyokuwa imezimwa sasa ilikuwa inawaka.

    Maajabu haya!!

    Akasita kwa muda kutembea, alikuwa anatetemeka sana. alidhani wale askari wamemtangulia katika nyumba yake na sasa wanafanya upekuzi. Alitamani kukimbia na kurejea alipotokea lakini miguu ikawa mizito. Aliamini kuwa kama wale ni maaskari katika chumba chake basi bila shaka watakuwepo wengine wametapakaa pande zote za nyumba ile na pale alipokuwa walikuwa wanamuona. Lilian akakaza mwendo japo kwa kukata tamaa akaingia ndani ya nyumba aweze kuwakabili maaskari.

    Lahaula!!

    Ana kwa ana na Walter……wote wakashangaana, nyumba ilikuwa imevurugwa haswa. Hakuna kilichokuwa katika mkao wake, vyote vilikuwa shaghalabaghala. Walter alitegemea kuonana na Lilian lakini sasa alikuwa akimuhofia kama muuaji mkubwa. Hofu yake haikupungua badala yake iliongezeka baada ya Lilian kuanza kumsogelea.

    Harufu ya kifo!!

    Walter akajihami, akanyanyua kinywa chake aweze kusema.

    “Walter jamani…” Lilian akawahi kusema huku akitaka kumkaribia zaidi.

    “Lilian…komea hapo hapo…” Walter akaamuru. Lilian akashangaa, hakutegemea kabisa amri ile. Akasita na kuganda akiwa ameyatumbua macho.

    “Lilian..unataka kuniua..unataka kuniua baada ya kunigombanisha na Naomi wangu..unataka kuniua baada ya kunilaghai nikafanya mapenzi na wewe wakati nina mke wa ndoa Lilian….sasa unataka kuniua, visu vya nini humu ndani Lilian…kumbe wewe ni muuaji…wewe ni mmoja wa wachuna ngozi Lilian…..Lili..Lili kweli ni wewe Lili…haya niue sasa….si ulinidanganya unatoka kidogo kumbe umeharibu umeridhika na sasa unatabasamu tu…muuaji mkubwa wewe…ulidhani ule ujumbe wa Naomi sitauona eeh..” Walter alikomea pale, alikuwa anatetemeka sana hisia zote za usaliti ziliishi naye na kujikuta katika wakati ule mgumu.

    Lilian alikuwa anaduwazwa na maneno ya Walter. Alijaribu kuisoma akili yake lakini alimuona kama aliyechanganyikiwa na ambaye hayupo tayari kubadilishwa kwa lolote lile katika mawazo yake.

    Lilian akajiuliza ni kipi cha kuanza nacho ili kuijenga akili ya Walter upya. Lilian akaingiza mikono yake mifukoni Walter akaanza kutetemeka alidhani Lilian anatoa silaha.

    Lilian akaibuka na kitambulisho. Bila kufanya hatua yoyote mbele akamrushia Walter kile kitambulisho.

    “Soma Walter…” Lilian akatamka kwa shida. Kwa tahadhari kubwa Walter akainama akakichukua na kukitazama. Akakisoa upesiupesi bila kuelewa chochote.

    “Suzi? Suzi ni nani?”

    “Nd’o mimi Walter…naitwa Suzi jina la kazi mimi ni daktari, daktari niliyekuwa namtibu shemeji yako Suzan…..ni simulizi ndefu tafadhali Walter mimi si muuaji……sijawahi kuua. Nisikilize…” Lilian akasihi.

    Walter akajengeka kidogo na kumruhusu Lilian aketi naye akaketi.

    Lilian akaanza kumueleza kwa ufupi sana juu ya maisha yake. Akamgusia kila kitu kilichopaswa kuyafikia masikio ya Walter.

    Akalia na hisia zake za maajabu, hisia ambazo zimewahi kwenda sawa na wanaume wawili tu katika ulimwengu huu. Hisia zilizomtuma kumwekea dawa Walter ili waweze kufanya mapenzi na mwisho wakajikuta penzini.

    Lilian alinena kwa hisia. Walter akaguswa, akalegeza msimamo wake.

    “Walter.....najutia kukuingilia katika mapenzi yako, nimemkosea sana Naomi. Nimekukosea wewe pia. Ni mapenzi tu Walter yaliyoibeba taaluma yangu na kuitupa mbali, ni mapenzi yamenifanya kama mtoto nimefanya mambo yanayostahili kuitwa na kijinga katika maisha yangu…hisia Walter Hisia…..mwenzio nina jeraha la hisia…uwepo wako ulinitonesha nimejikuta nikiwa mtumwa wa kuitafuta tiba lakini badala yake nimejikuta na kidonda kibichi. Nimekukosa Walter nimekukosa na bado natakiwa kuhukumiwa…..Naomi …..nisamehe …….”

    “Naomi yupo wapi?” Walter aliuliza swali lile kana kwamba ndo kitu pekee alichosikia katika mazungumzo ya Lilian yaliyoambatana na kilio cha kwikwi.

    “Naomi yu mikononi mwa polisi kwa kesi ya uchunaji ngozi…..jambo ambalo…”

    “Si nimekwambia Lili wewe ni muuaji tena mchun…”

    “Nooooo Walter…” Lilian akatokwa na ukulele ukiambatana na kilio kikubwa.

    Walter akatulia na kumtazama huku akitetemeka. Lilian hakutaka kumwachia Walter mwanya wa kufanya maamuzi yoyote. Akaamua kuendelea kuzungumza ili Walter aweze kuelewa ni kipi kinaendelea.

    Mkasa wa kutokea Dar hadi kukutana na Kibwana katika hoteli maarufu mji kasoro bahari Morogoro ukayavuta masikio ya Walter akajiweka katika hali ya utulivu sana na kusikiliza. Lilian alisimulia kwa uchungu kisa chote kile cha kufanya mambo nje ya uwezo ilimradi tu aweze kulitetea penzi lake kwa Walter. Harakati za Lilian zilimshangaza sana Walter lakini hakuingilia maongezi hadi pale aliposhikwa na butwaa kwa kitendo cha kijasiri cha Lilian kupambana na Kibwana hadi kufanikiwa kutoka katika chumba kile akiwa salama.

    “Kwa hiyo huyo Kibwana ndo amesema Naomi ni muuaji….”

    “Walter hadi sasa sijui lakini kuna ujumbe nimeutuma huko hospitali nasi tunatakiwa kufanya jambo kuikoa roho ya Naomi…Walter nina hatia kifuani mwangu tafadhali naomba unisamehe tu kwa yote yaliyotokea najua sina muda mrefu wa kukuomba msamaha nawe ukanielewa lakini elewa kuwa Naomi anakupenda sana….tuwe kitu kimoja kwa sasa Walter nitahitaji muda zaidi kukuomba msamaha wewe na Naomi…..Walter pliiiz” Lilian aliangukia katika kifua cha Walter, zile embe bolibo zilizokuwa zikiishi katika kifua kilichochangamka cha Lilian zilimtekenya Walter, machozi yenye uvuguvugu yakatambaa katika mikono yake. Mara zile hisia za huruma zikamtwaa akajihisi yu salama mikononi mwa Lilian tena.

    Mara akaikutanisha mikono yake na kumkumbatia kwa nguvu Lilian, mara wakajikuta wote kwa pamoja wakilia kwa uchungu mkubwa sana. hakuna aliyetaka kumwachia mwenzake…..miili yao ikabadilika kuwa mwili mmoja usiotaka kuishi katika hali tofauti na ile iliyokuwepo.

    Hali ya kimapenzi.



    Walter akasafiri hadi ulimwengu wa hisia kali…Lilian naye akajikita katika safari hiyo pasipokutegemea.

    Ghafla Lilian akatokwa na yowe kubwa sana lililomuogopesha Walter.

    Haraka huku akitetemeka Walter akaitoa mikono yake iliyokuwa imeanza kutamaa katika ncha za matiti ya Lilian.

    Macho yalikuwa yamemtoka Lilian kana kwamba alikuwa anatazamana na yule malaika mtoa roho.

    Lilian alikuwa anatisha kutazama……



    Walter naye alijikuta amekodoa macho huku akiogopa bila kufahamu kwa nini anaogopa. Macho yake yalianza kumsaili Lilian kuanzia usoni, kasha yakashuka chini kwa hatua moja baada ya nyingine. Hatimae macho yakakutana na mfereji mwekundu uliokuwa unazidi kutiririka, wekundu ule ulikuwa wa damu nzito.

    Lilian alikuwa anatokwa na dam nyingi katika unyayo wa mguu wake. Walter alipotambua hili, Lilian naye alikumbuka kutokwa na kilio kilichotangaza maumivu yake makali. Zile chupa za dawa ambazo Walter alizivunja vunja bila kutambua zilikuwa zimezua madhara. Kipande kimoja kilikuwa kimekanyagwa na Lilian ambaye hakuwa na kiatu mguuni.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Badala ya kuendelea kushangaa Walter alichukua kanga na kuwahi kukabiliana na zile damu zilizokuwa zinatiririka. Daktari akawa anatibiwa na mtu asiyekuwa na taaluma.

    Lilian alitoa maelekezo kadha wa kadha kwa Walter. Walter akageuka daktari, mara aelekezwe dawa hii mara ile, mwisho akatakiwa kumchoma sindano ambayo aliambiwa kuwa inazuia tetenesi.

    Walter alifuata maelekezo, akaiondoa nguo ya Lilian, kutokana na maelekezo ya mgonjwa Walter alitakiwa kumchoma sindano matakoni. Walter akiwa anahangaika huku na kule, kila alivyompa mgongo Lilian, daktari huyu alitabasamu kwani maumivu yalikuwa yameisha tayari na alichokuwa anafanya pale ni kumchezea Walter. Hali ya Walter kumjali ilimfurahisha alitamani sana idumu hivyo lakini alikumbuka kuwa kuna kivuli cha Naomi kilikuwa kikilia na kusaga meno juu yake. Hisia hizi zikamweka katika simanzi kuu na kujikuta akitokwa machozi.

    Walter ambaye alikuwa anamchoma ile sindano alimbembeleza akidhani kuwa ni maumivu ya sindano yalikuwa yamemfanya atokwe machozi. Lakini haikuwa hivyo na kamwe asingeweza kujua kuwa Lilian alikuwa katika kilio cha kuyalilia mapenzi. Mapenzi ya dhati.

    Hisia zilikuwa zinamvuruga kichwa chake.



    Alfajiri, Walter alikuwa amemshika mkono Lilian ambaye alikuwa bado anachechemea. Walikuwa wanaelekea kituo kikuu cha mabasi mkoani Mbeya. Wote walikuwa kimya.

    Basi walilopanda kwa pamoja mara ya kwanza nd’o hili likawa bahati yao tena kwa siku hii.

    Wakati mara ya kwanza walijikuta wamekaa siti moja bila kufahamiana, wakafahamiana kupitia vitabu vya mzee Beka Mfaume. Sasa walikuwa wanapanda wakiwa wanafahamiana, tena labda walikuwa ni zaidi ya marafiki.

    Wakafanikiwa kupata siti ya watu wawili, Walter akamkokota Lilian wakaingia ndani ya basi. Kwa jicho la upesi ukiwatazama walifanania kuwa wapenzi na kama hawakuwa wapenzi basi lazima ukaribu wao ungekutia mashaka.

    Baridi ilikuwa kali sana, walipofikia nafasi zao za kukaa Walter alitangulia upande a dirishani. Lilian akafuatia. Hazikupita dakika nyingi, Lilian akaanza kuyumbayumba kasha akamuangukia Walter. Walter akampokea kwa utulivu kichwa chake, akamlaza katika mapaja yake.

    Lilian alikuwa amesinzia.

    Walter alibaki katika tafakari ya aina yake. Alimtazama Lilian kama wanamke wa pekee, anayejua kujali na akikosasi mchoyo wa kujishusha na kuomba msamaha. Kitabia alitofautiana sana na Naomi mkewe wa ndoa ambaye kitu kinaitwa kujishusha kwake ilikuwa ni ndoto ya mchana. Hakuwa tayari walau kujishusha na kumbembeleza hata kama amemkosea.

    Lilian alikuwa na sauti fulani inayoweza kubadili msimamo wa mtu hata kama hakuwa katika mpango huo. Lilian alikuwa na kipaji cha ushawishi. Lilian alikuwa mpiganaji, kimaisha na kimapenzi.

    Au elimu nayo inachangia? Walter alijiuliza huku akiilinganisha elimu ya Lilian nay a mkewe Naomi. Hakika walikuwa watu wawili tofauti.

    “Mh lakini nitachanganuaje kuhusu hili wakati mi myewe sijasoma?” alijiuliza kasha akafanya tabasamu huku akichezea shavu la Lilian ambaye alikuwa amesinzia mapajani kwake.

    Safari ilipoanza Lilian alishtuka kutoka usingizini, labda milio ya honi ama vinginevyo. Kuanzia hapo hakulala tena. Alichangamka na kumchangamsha Walter.

    Safari ya kuelekea Morogoro katika harakati za kumkomboa Naomi na kumtia hatiani Kibwana kwa kupotosha ukweli na hatimaye kuzitia roho nyingi katika kesi wasizohusika nazo.



    *****



    Chumba kikubwa kilichoruhusu hewa mwanana kuingia ndani kilichokuwa kinalindwa masaa yote kilitawaliwa na vichwa kadhaa vilivyokizunguka kitanda.

    Baada ya muda kidogo walibaki watu wawili, mmoja akiwa amelala na mwingine akiwa amekaa katika kitanda, baada ya kuwa wamepeana salamu za hapa na pale hatimaye ukajiri ule muda ambao Yule aliyekuwa amekaa aliungoja. Kwake yeye aliamini kuwa ni jambo ambalo litamfariji sana mgonjwa wake.

    Akampatia simu aweze kuzungumza na mtu. Namba zilikuwa ngeni sana. Na ulikuwa ni usiku wa saa moja.

    Kibwana akaipokea ile simu na kuandika zile namba kwa shauku kubwa sana.

    Kasha akapeleka sikioni aweze kusikiliza ni kipi kinasemwa.

    “Kibwana nazungumza..” alianza kwa kujitambulisha, Akwino alikuwa anatabasamu akingoja kaka yake aweze kufurahia hali ya kuzungumza na yule binti kwani alitambua jinsi kaka huyo alivyokuwa anampenda japo hakupata nafasi ya kuwa naye.

    Hofu iliyojitokeza usoni mwa Kibwana haikuweza kufichika mbele ya Akwino, na hata Kibwana alivyojaribu kujilazimisha kuwa kama awali haikuwezekana.

    “Hebu nenda kule nataka kuongea naye vizuri…” Kibwana alimwondoa Akwino naye akatii.

    Mazungumzo yakaendelea.



    Lilian alikuwa yu pamoja na Walter wakati simu ile inapigwa. Lilian akamwomba Walter akae kimya ili aweze kusema neno.

    “Kibwana….neno ni moja tu..nipo Morogoro na ujinga unaonitangazia nimeusikia japo hujanitaja jina. Sasa ni ombi kwa sasa lakini kisha itageuka kuwa amri….nakuheshimu sana na licha ya kujaribu kunivunjia heshima bado nina masalio ya heshima kwako. Na ili heshima hii kidogo iendelee kubaki nakusihi sana, usimtie yeyote matatani kwa kisingizio cha kutaka kuchunwa ngozi jambo ambalo si kweli….naomba tunga uongo wako mwingine ili uwe huru na raia hao wema wawe huru….najua unamtambua Naomi, amepigwa bila kosa kwa ujinga wowote ambao unaweza kuwa umeufanya wa kumlaghai….nampa kipaumbele. Kama ikifika keshokutwa hajatoka hapo alipo nitausema ukweli wote wa ulichotaka kunifanyia.

    Kumbuka nilirekodi katika simu yangu kila kitu…nina ushahidi wote. Kibwana…..”



    “Naam dokta Suzi” Kibwana aliitika kwa hofu.

    “Nitakufunga usipokuwa makini elimu yako haitakuwa na maana tena baada ya siri hii kuvuja. Kumbuka unaidanganya serikali.” Lilian alisema kiujasiri. Walter aliyekuwa ubavuni mwake alishangazwa na ujasiri huu kutoka kwa mwanamke.

    “Nimekuelewa Dokta tafadhali naomba usifanye upesi nakuahidi nitatekeleza yote.”

    “Maneno dhidi ya vitendo. Uwe na usiku mwema.” Lilian aliaga na kisha akakata simu.

    Uso wake ulikuwa umeiva haswa na alikuwa anatetemeka wakati simu yake ilipoita tena.

    “Kibwana huna ruhusa ya kunipigia simu. Nimesema Vitendo dhidi ya maneno.” Aliweka msisitizo. Hata Walter aliyekuwa pembeni yake aliogopa hasira ile.

    Lakini baada ya kutulia kidogo, Lilian alianza kurejea katika hali ya kawaida akawa yule Lilian mpole lakini ucheshi haukuonekana machoni pake. Taratibu akawa mnyonge, Walter akamkaribia aweze kumuuliza kulikoni, lakini hakuweza kumuwahi kabla chozi halijaanza kumtoka, chozi lile likakikaribisha kilio cha kwikwi. Walter akamkumbatia Lilian.

    “Walter…..nisamehe bure kwa yote yaliyotokea na yanayoendelea kutokea….nakupenda sana.” Lilian alihimili kusema haya huku kilio kikizidi kuchukua nafasi. Kilio hiki kikamchoma Walter. Naomi wake hakuwahi kuyalilia mapenzi kama Lilian anavyofanya, hali hii ilimuathiri sana kichwani na kujiona kama ambaye haziheshimu hisia zake. Alihisi kuwa hata yeye moyo wake ulikuwa penzini tayari, lakini alikuwa katika ndoa na Naomi, na mbaya zaidi aliwahi kuapa kuwa kamwe hatamsaliti ama kumuacha kwa namna yoyote. Hisia hizi zikamsulubu huku zikimweka katika kikaangio na hiari ikibaki kwake, aidha ajikaange ama atoke kikaangioni.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Tafakari ilipokoma na Lilian alikuwa amekoma kulia na sasa alikuwa yu usingizini.

    Walter alimlaza Lilian vyema kitandani kisha akaingia maliwatoni kujisafisha mwili. Wakati anajimwagia maji akawa anakumbuka miaka kadhaa nyuma ambapo mama yake mzazi alikuwa akimsihi mambo kadha wa kadha. Kila alipomnunulia kitu alikuwa akimwambia kuwa ‘ukipendacho kitunze na kukithamini’ neno hili aliwahi kulisikia kwa bibi yake tena wakati alipokuwa akimtetea Naomi wakati wakiwa wadogo.

    ‘wewe unamwambia akipendacho akitunze na kukithamini halafu unamzuia Naomi kucheza hapa wakati anapendana….hebu mwacheni mume wangu..” Walter alijikuta akitokwa na machozi, ni kama alikuwa anaisikia sauti ya marehemu bibi yake. Sauti iliyokuwa inamtetea kila siku.

    Maneno yale yakapata maana katika kipindi hichi cha utata. Walter akahisi huenda Naomi hakuwa chaguo sahihi. Na kama ni hivyo bila shaka chaguo lake limejileta katikati ya safari.

    “Yawezekana akawa ni Lilian?” alijiuliza. Akahofia kujiwekea asilimia zote kwa jibu la ndio.

    Wakati utafika na majibu yatajileta yenyewe……alimaliza kwa kauli ile.

    Wakati alioungoja Walter ni wa Naomi kuwa huru na Lilian kuwa na amani ili aweze kufanya maamuzi sahihi. Maamuzi yatakayomfurahisha nafsi yake na kisha kudumu katika usemi wa ‘ukipendacho kitunze na kukithamini.’



    ****



    HAZIKUWA SIKUMBILI kama Lilian alivyomwagiza Kibwana, alipokea simu kutoka kwa Kibwana ikimsihi kuwa aende kumwekea dhamana Naomi, dhamana ya kizushi aweze kuwa huru.

    Kibwana alikuwa ametetemeshwa hasa na maneno makali kutoka kwa Lilian. Amani ilitoweka na dalili za kupotea uraiani zikamkumba. Hakutaka kufanya mchezo alipotakiwa kuzitambua picha zas husika alipoifikia picha ya Naomi alianza kung’aka akawaka sana kuwa yule ni mgonjwa wake kutoka jijini Dar es salaam. Kibwana akajiweka katika nafasi nzuri ya uigizaji na kulaani kitendo cha polisi kumtia hatiani na kumpiga Naomi.

    Polisi wakamwomba Kibwana awasiliane na ndugu zakewaende kumtoa katika kituo cha polisi. Kibwana akawasiliana na Lilian na kumpa picha nzima.



    Lilian hakuwa mpuuzi wa kujipeleka mwenyewe kituo cha polisi hakutaka kumuamini Kibwana moja kwa moja kutokana na kauli zake. Alihofia kuwa huenda anaweza kuwa anamuuza na alimini kuwa akishakuwa nyuma ya milango ya mahabusu hatakuwa na cha kujitetea tena.

    Lilian akashauriana na Walter wakatafuta mtu wa kuchonga, wakamlipa pesa akajipeka katika kituo kile. Akajitambulisha kama rafiki wa kaka yake na Naomi ameagizwa pale kituoni kwa ajiri ya kumwona na kuondoka na Naomi.

    Haikuchukua muda taratibu zikafanyika. Naomi akaachiwa huru, akapokelewa na mtu ambaye hapo kabla hawajawahi kuonana. Yule mtu wa kuchonga alikuwa zaidi ya muigizaji, alimpokea Naomi kwa masikitiko makubwa, na chozi lilimtoka wakakumbatiana. Naomi alijiuliza yule alikuwa ni nani lakini bahati nzuri hakumuuliza wa sauti ya juu.

    “Twende utajua..” alijibiwa kwa mnong’ono.

    Wakatoweka eneo lile.

    Wakaingia katika taksi na baada ya muda wakashuka kutokana na maelezo ya yule kijana kaka wa kuchonga.

    Akamshika Naomi mkono na kumwongoza hadi mahali tulivu kabisa, migongo miwili ikawa inamtazama. Mara haikuwa migongo tena wakageuka watu anaowafahamu. Wote wakastaajabu kumwona katika hali ile. Alikuwa amevimba uso na kuchanika midomo.

    Walter, Lilian na Naomi macho kwa macho.

    Macho manne yakatazamana na macho mawili ya Naomi.

    Kaka wa kuchonga akabaki kuduwaa. Haikueleweka iwapo watu hawa walikuwa maadui ama walikuwa katika taharuki ama tahamaki.

    Nani aanze kusema neno? Hili lilikuwa swali.

    Lilian akaguswa upya na hisia za usaliti, Walter naye jeraha likatonesheka na kuwa kidonda. Naomi katika kiulizo juu ya mahusiano ya Dokta na mumewe……

    VURUMAI MCHANA KWEUPE…….







    Naomi alikuwa anatetemeka, Walter hakujua nini la kufanya, daktari mwenye ujuzi wa hali ya juu katika kucheza na saikolojia alikumbuka ujuzi wake ambao alikuwa ameutua siku nyingi kutokana na mapenzi ambayo yalikuwa yamemuelemea.

    Lilian akawa wa kwanza kujitoa katika taharuki na kuwaacha mume na mke wakiwa wamehamanika. Lilian akamkaribia Naomi ambaye alikuwa amevimba uso wake kutokana na kipigo aidha kutoka kwa mahabusu wakorofi ama askari waliokuwa wakijaribu kumdhibiti.

    Bila shaka Naomi hakutambua kuwa alikuwa katika hali ile, damu ilikuwa imevilia katika kona moja ya shavu lake. Bila shaka makofi makali ya kitaalamu kutoka kwa askari yalikuwa yamempa athari hizo.

    “Naomiii…..” Lilian alimvamia Naomi na kumkumbatia huku akijaribu kumwondoa hofu na kumweka katika hali ya kuhisi yu salama.

    “Dokta niache nahitaji kuuliza maswali tafadhali.” Naomi alitaka kujitoa katika mikono ya daktari.

    “Naomi maswali yote utauliza mamii pliiz hali yako kiafya si nzuri haitazamiki hata kidogo na ni mbaya zaidi kama utaendelea kukaa bila kupata huduma ya kwanza. Tafadhali Naomi mumeo huyu hapa. Na ataendelea kuwepo kuna watu wabaya wamejaribu kuwatenganisha lakini imeshindikana kabisa…” Lilian alizungumza kwa sauti inayoshawishi, sauti ya ubembelezi sauti ambayo ilikuwa kisu kikali kwa Walter ambayo ilimkata na kumwachia maumivu matamu. Maumivu aliyoyapenda zaidi kuliko kuyachukia.

    Sauti ile ikamshambulia na Naomi. Japo alikuwa mwanamke mwenzake alijikuta akiihusudu sauti ya mwanadada yule. Hasira zikashuka akasahau ni kipi alikuwa akiuliza na kulazimisha ajibiwe.

    Kilio cha kwikwi kikaanza kuchukua nafasi yake taratibu, Lilian akamkumbatia kwa nguvu na upendo zaidi. Kingine cha ajabu kilichomuacha Walter katika mshangao ni ile hali ya Lilian kulia na Naomi badala ya kumbembeleza. Vilio hivi vikampa suluba ya ghafla. Akahisi huruma lakini mara akakumbwa na mshangao. Hakujua ni nani alikuwa anayemuonea huruma.

    Ni Naomi ama ni Lilian? Swali gumu.

    “Walter sorry..naomba uchukue taksi Naomi lazima apelekwe hospitali mapema. She’s real sick……” Lilian akiwa analia alitamka haya kwa ufasaha.

    Walter akakurupuka, safari ya kuelekea barabarani. Akafanikiwa kupata taksi baada ya dakika chache.

    Punde dereva alikuwa makini na maelekezo aliyopewa akawapeleka hospitali ya mtu binafsi. Naomi akapokelewa upesi na kuanza kuhudumiwa. Lilian akiwa na taaluma ya udaktari alitoa maelezo yote kitaalamu. Huduma ikachukua nafasi.

    Hadi wakati huo nafasi ya kuzungumza kinagaubaga na Walter ilikuwa haijapatikana. Na hili lilimfurahisha sana Lilian kwani nia yake ya dhati ilikuwa kufanya mazungumzo wakiwa watatu na kuyaweka mambo sawa. Nafsi ya Lilian ilikuwa ina furaha kwa kufanikisha kumweka Naomi huru tena. Alijipongeza kwa kutoa tabasamu mara kwa mara.

    Walter yeye alikuwa katika mtihani mgumu sana. hadi wakati huo hakuwa na uhakika wa kitu gani ambacho kitatokea baada ya Naomi kupatwa na nafuu kisha kukaa na kuzungumza. Walter alikuwa hajapata jawabu la ‘ukipendacho, kitunze na kukithamini.’….ni nani hasa alikuwa anastahili kutendewa haki na msemo huo?.

    Hakupata jawabu.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Usiku huo ukapita katika namna ya kimya kimya.

    Siku iliyofuata Naomi alikuwa na ahueni japo alikuwa hajaamka bado lakini uso wake ulitangaza faraja kiasi fulani. Majira ya saa mbili asubuhi mkojo mkali uliokuwa umembana uliukatisha usingizi wake uliosababishwa na madawa mbalimbali aliyokuwa amedungwa ili kumuweka sawa kiafya.

    Akiwa na mawenge ya usingizi, aliketi kitandani kisha akapekecha macho yake, akajipigapiga kichwa chake ili kurejesha kumbukumbuku. Hakika akaukumbuka mlango wa choo. Haukuwa mbali sana kutoka katika wodi aliyokuwa amelazwa.

    Akatazama chini akakutana na viatu vya wazi akaviweka miguuni. Akaanza kutembea ili aweze kukidhi haja yake chooni. Naomi akajikongoja akaufungua mlango na kuanza kutembea kuelekea chooni. Masikio makini kabisa yakanasa mawimbi yenye sauti ambayo aliwahi kuisikia mahali. Na haikumchukua mud asana kutambua kuwa aliyekuwa anazungumza ni Lilian.

    Hajui kwanini aliamua kusikiliza mazungumzo yale, labda ni wivu akidhani kuwa Lilian alikuwa anazungumza na mume wake, ama kwa lugha za kigeni hii hali inaitwa ‘spur of time’ yaani unajikuta tu umefanya kitu bila kujua kwa nini unafanya.

    Naye Naomi akajikuta anasikiliza mazungumzo bila kutambua kuwa yalikuwa na umuhimu ama la.

    In a spur of time…..

    “Nyie msimwambie kama kuna tatizo hilo tafadhali maana…..anyway wewe ni daktari na unatambua ugumu wa jambo hili …” sauti ya kiume ilikuwa inasisitiza.

    “Ni kweli dokta yaani ujue nimechanganyikiwa hapa…sijui hata nisemeje lakini I will handle it naamini…” Sauti ya Lilian ilijibu kwa namna ya kujilazimisha kuamini ukweli.

    Naomi alikunja uso wake na kujishika midomo yake asiweze kutokwa na pumzi ambazo zinaweza kusababisha mtu yeyote kuweza kutambua uwepo wake pale. Mapigo ya moyo pekee nd’o hayakuweza kuzuilika kupiga kwa nguvu. Kuna jambo alihisi linaendelea…

    “Kwani dokta huyu ni nani yako maana najua huna ndugu uliniambia nakumbuka.”

    “Yeah…nilikwambia sina ndugu lakini huyu ni zaidi ya ndugu…nitakueleza siku moja ngoja liishe jambo hili kwanza.” Alijibu Lilian kwa mkato kisha zikasikika hatua, Lilian naye akapiga hatua akaingia chooni.

    Ule mkojo uliokuwa unakaribia kumwagika wakati yupo kitandani sasa haukujulikana mahali ulipokuwa umejihifadhi. Lakini haukuwa na dalili ya kutoka tena. Naomi akajikuta anashangaa tu pale chooni. Hakuwa na jipya la kufanya.

    Akafungua bomba na kunawa mikono kisha akatoka nje bila kufanya jambo lolote, hatua kwa hatua akaingia chumbani akaketi katika kitanda. Akairuhusu akili yake kufanya mchanganuo wa kitu gani kinatokea, lakini akili haikutoa ushirikiano wowote badala yake ilikoma kufikiri tena baada ya Walter na Lilian kuingia pale chumbani. Wote walikuwa wanatabasamu, walikuwa pamoja na daktari.

    Naomi alijilazimisha kutabasamu lakini nafsi ikamsuta kuwa hakuwa na furaha hata kidogo. Kuna jambo lilikuwa halijakaa sawa na alikuwa anapakwa mafuta kwa mgongo wa chupa. Alitamani kuzungumza lakini daktari akamsihi awe mtulivu.

    Siku hiyo waliruhusiwa kuondoka. Lilian akasimamia mpango wote jijini Mbeya. Akaongeza pesa katika bili ya chumba ambacho alikuwa analala Walter wakati Naomi yu hospitali.

    Siku hiyo iliwalazimu mke na mume kulalal chumba kimoja. Lilian aliyafanya haya maksudi ilimradi tu kuweza kumfurahisha Naomi na kujitoa katika hatia iliyokuwa inamkabili ya kumsaliti Naomi.

    Hali ilienda kama alivyopanga, japo Walter hakufurahishwa na uamuzi huo wa kulazwa chumba kimoja na Naomi lakini kwa busara za lilian aliamua kufanya hivyo. Kiapo chake kilikuwa kimoja tu kuwa hatakuwa tayari kushiriki jambo lolote na Naomi hadi watakapokaa wote watatu na kuweka mambo sawa.

    Alihitaji kuzungumza na Naomi juu ya kifo cha dada yake mpenzi Maureen, alihitaji maelezo ya kutosha kutoka kwa Naomi kabla hajaamua kusuka ama kunyoa. Iwapo maelezo yatayumba basi Walter alijiapiza kuwa atakuwa tayari kuachana na Naomi kisha kujikita katika penzi la Lilian lakini iwapo mambo yatakuwa kinyume angeweza kujifikiria juu ya kuendelea na mahusiano baina yao wawili.

    Hili likapita katika halmashauri ya kichwa cha Walter.

    ****

    CHUMBANI, eneo hili linabaki kuwa eneo la faragha kupita yote kwa wapenzi, hasahasa wale waliohalalishwa.

    Walter na Naomi walikuwa wapenzi ambao walikuwa wamehalalishwa, ni siku nyingi sana walikuwa hawajapata faragha kama ambayo usiku huu walikuwa wameipata.

    Japokuwa kila mmoja aliingia katika chumba akiwa na lake kichwani. Walter akiwa na chuki dhidi ya Naomi, naye Naomi hakuwa nyuma alikuwa na wasiwasi juu ya mumewe.

    Chumba….chumba kikasema kweli. Kikabadili mitazamo yao. Walter alijikuta akiuvunja ukimya wake baada ya Naomi kufanya jambo ambalo hakulitegemea kwa wakati huo mgumu waliokuwa wanapitia.

    “Walter…” aliita Naomi. Walter akageuka bila kusema neno lolote. Naomi hakujali, “Hivi wewe bado ni mume wangu?” akamuuliza huku akiwa ameinama chini.

    Walter hakutarajia swali jepesi kama lile kutoka kwa Naomi, na vile alilichukulia jepesi hata jibu alilotoa lilikuwa jepesi.

    “Yeah ni mumeo kwani vipi?”

    “Asante,….” Alijibu Naomi. Kisha akasimama wima na kuiendea pembe ya chumba kile, akaanza kuondoa nguo moja baada ya nyingine.

    Naomi hakuwa na utaratibu wa kulala na nguo hata moja pindi anapokuwa chumba kimoja na Walter haijalishi kama ni nyumbani kwao ama popote watakapojikuta wanalala siku hiyo. Utaratibu huu ulijengeka kichwani mwake na kujikuta ukiwa ni utaratibu maalumu. Na sasa alikuwa anautimiza utaratibu ule ule waliojiwekea na Walter kama mtu na mkewe.

    Walter alitaka kumzuia asivue lakini akakumbuka kuwa amekiri kuwa yeye bado ni mume wake. Akiwa kama mume naye alikuwa na utaratibu kuwa Naomi akishavua nguo anambeba na kumpeleka kitandani kisha anambusu shavuni. Baada ya hapo atakayelala sawa na atakayeamua kuendelea na mambo yake sawa vilevile.

    Naomi alibaki wima akiwa mtupu mwilini. Walter alijua ni kipi mkewe alikuwa anangojea. Nafsi ilimsuta kwa uamuzi wake wa kujikausha kana kwamba hamuoni Naomi mpweke katika kona ya nyumba.

    Kosa kubwa ambalo Walter alilifanya ni kugeuka kisha kukutanisha macho yake ana kwa ana na Naomi.

    Macho ya Naomi yalikuwa na mng’aro wa ajabu, mng’aro ambao haukudumu sana. ghafla ukatoweka na kumwagika mashavuni.

    Naomi alikuwa analia, kilio cha upweke. Upweke wa kulikosa penzi la dhati kutoka kwa mume wake wa ndoa.

    “Nivue pete yako kama sina hadhi ya kuwa mkeo Walter. Nenda nayo ukamvalishe Lilian ama yeyote anayekufaa.” Sauti yenye kitetemeshi kutoka kwa Naomi iliungurumisha chumba kile, Walter akajikuta wima bila kutarajia maneno yale machache yalikuwa yamemvuruga.

    Hakika Naomi alikuwa mpweke, uchungu na baridi kali mkoani Mbeya likamfanya atetemeke, Walter akajiona , mkosaji, ile roho yake ya huruma ikamponza kwa mara nyingine. Akajikokota na kumfikia Naomi.

    Walter alikuwa na bukta yake pekee, akamtwaa Naomi akampakata vyema.

    Ajabu…

    Naomi alikuwa amepungua sana uzito. Bila shaka ni kutokana na mawazo. Walter akajikongoja naye hadi akamfikisha kitandani. Naomi alikuwa analia kwa sauti ya chinichini machozi yakitiririka kwa fujo.

    Walter alitamani sana kumuita Lilian katika sakata hili lakini aibu zikamshika na kujioana mjinga. Hadi mambo yake ya chumbani yanahitaji busara za Lilian? Upuuzi mtupu. Walter akaamua kulisimamia jambo hilo kikamilifu.

    Akaanza kumbembeleza Naomi, akamfuta machozi. Kisha akakumbuka kuwa mke wake alikuwa mpenzi mkubwa wa kukumbatiwa kisha kuimbiwa nyimbo za kitoto toto. Walter akajisahaulisha yote anayohisi juu ya Naomi.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Akamkumbatia kisha akaanza kumwimbia wimbo wa ‘maua mazuri yapendeza’…..baada ya hapo akamuimbia wimbo ambao ulimsababisha Naomi atokwe na kicheko, ‘Mabata madogodogo yanaogelea’.

    Naomi akamkumbatia Walter kwa nguvu zote. Alikuwa anacheka huku akiwa anatokwa machozi bado.

    “Nakupenda mume wangu Walter nakupenda sana…nisamehe kama niliwahi kukukosea, nisamehe kama sijawahi kukuonyesha kuwa nakujali…Walter siwezi….siwezi kuishi bila wewe” kicheko kikakatika kilio kikarejea tena.

    Maneno yale yakamtibua Walter, mtu mzima akashindwa kuvumilia zaidi ya pale. Chozi likaanza kutiririka. Hisia za ajabu zikarejea, hisia za mapenzi ya dhati. Penzi la Naomi. Mkewe wa ndoa.

    Nani wa kusimama wima na kuwa juu zaidi ya hisia, hisia hukupeleka pale zinapotaka. Hisia nd’o chanzo cha maovu na mema yote.

    Hisia zako zikisema ndio, akili, mwili navyo husema ndiyo.

    Hisia za Walter zikasema NDIYO.

    Naomi na mumewe wakajikuta katika safari ya kuliwazana.

    Mahaba ya kiutu uzima.

    Si Walter pekee aliyekuwa katika hisia za fungate lao la kipekee baada ya ndoa yao ya kiserikali miezi kadhaa nyuma, Naomi naye alijihisi mpya. Akayapuuzia maneno aliyoyasikia kule hospitali Lilian akisemezana na daktari. Maneno yale licha ya kuwa na ukali fulani lakini mbele ya hisia hayakuwa na madhara yoyote.

    Naomi akayapuuzia, wakaendelea kufarijiana na mumewe.

    Faraja isokifani.



    ****



    LILIAN, alikuwa anaumiza kichwa chake. Baridi lilisahaulika japo kwa muda kidogo. Alikuwa anawaza juu ya kufikisha ujumbe kwa Walter na Naomi kabla hawajaondoka kurejea jijini Dar es salaam kuendelea na maisha yao.

    Lilian alihitaji kusema nao kitabibu juu ya ni namna gani wanaweza kuishi kama mume na mke huku wakiwa wameathirika na virusi vya Ukimwi. Ni haya Lilian aliyaamini na ilikuwalazima ayaseme ili kila mmoja abaki huru.

    Lilian alijua fika kuwa mmoja wao kati ya Naomi ama Walter hajui kama kuna Ukimwi kati yao. Hili lilimpa mashaka sana na alihofia amani kutoweka. Lakini kama mwanamke jasiri aliyeamua kujitoa katika hatia ya usaliti kwa kulipa mema. Hili lilikuwa mojawapo ya tendo jema.

    Lilian akajiweka tayari kwa ajili ya kuchukiwa na mmojawapo kati ya Naomi ama Walter lakin ukweli uwe wazi.

    Liliani akaendelea kuishi na hisia kuwa Walter aliuchukua Ukimwi kwa Suzi (dadake Naomi) kisha kwa kujua ama kutojua akaupandikiza kwake na kwa mkewe mpenzi…huenda mkewe hajui…

    Lilian akaamua kupasua jipu ili ukweli ujitenge mbali na uongo……

    Hiyo siku ya kupasua jipu akaipanga kuwa asubuhi inayofuata…….

    Akajifunika shuka lake kuanza kuutafuta usingizi….

    Wakati Lilian anajifunika shuka, Naomi na Walter walikuwa wamejikita katika kuzifurahisha nafsi zao kimahaba zaidi.

    Usiku wa kukumbukwa kwao..usiku wa kipekee.

    Laiti kama wangejua mawazo ya Lilian juu yao na jinsi alivyokuwa anaingojea asubuhi kwa hamu. Huenda wasingekuwa katika kufarijiana…

    Bali angetafutwa mchawi nani????





    *****



    WALIPOINGIA chumbani hakuna hata mmoja aliyekuwa anamtazama mwenzake. Hakuna aliyefurahia kitendo cha kulazimishwa kulala chumba kimoja. Naomi alikuwa na lake lililomkwaza moyoni na Walter naye alikuwa na hasira zake binafsi na hisia zisizosimulika kiwepesi.

    Hali hii ya wawili hawa kuwa katika chuki ilimpa ujasiri dokta Lilian kuweza kujiaminisha zaidi kuwa hatapata tabu yoyote katika kuufikisha ujumbe wake kwao. Ujumbe juu ya ugonjwa unaoishi katika miili yao, ugonjwa usiokuwa na tiba wala chanjo.

    Ukimwi….

    Majira ya saa nne asubuhi alikiendea chumba chao, nia ikiwa kuwaamsha wajiandae kwa ajili ya kwenda kupata kifungua kinywa.

    Hali hii ya wawili hawa kuchelewa kuamka ilimfanya Lilian aanze kuingiwa na mashaka kuwa huenda wameweza kusemezana na mwisho kupatana.

    Alipougonga mlango, sauti ya kichovu ya Walter ilijibu kutokea ndani. Lilian akasema naye bila kuhitaji kufunguliwa mlango kisha akaondoka.

    Baada ya saa zima Lilian alishuhudia mlango ukifunguliwa. Badala ya watu kutoka ukabaki wazi kwa sekunde kadhaa kisha ikatangulia miguu ya kike iliyokuwa inaelea hewani, baadaye kiwiliwili cha mwanaume akiwa amempakata mkewe.

    Ilivutia kuwatazama Walter na Naomi katika furaha yao ya zama hizo.

    Ushuhuda huu ukamchoma Lilian, akajilazimisha kutabasamu lakini haikuwezekana akabaki katika chuki. Hisia zake juu ya Walter zilikuwa juu sana, alijaribu kujisahaulisha lakini kila mara alikumbwa na pepo la wivu, likamshambulia na kumfanya linavyotaka.

    Ule ujasiri wa kuwaweka kikao wanandoa hawa na kuwaeleza hisia zake juu ya afya zao ulianza kuyoyoma kadri alivyozitazama nyuso zao. Walifanania na wanandoa ambao nd’o kwanza wametoka katika fungate baada ya kuoana kwa shangwe kubwa.

    Lilian akafanya msonyo wa chinichini kabla Walter na Naomi hawajamfikia. Wakati huu tayari Naomi alikuwa anatembea mwenyewe.

    Lilian akalifuta wazo lake la kuzungumza chochote juu ya gonjwa lile na wanandoa hawa. ‘kila mtu aubebe mzigo wake.’ Alijisemea kauli ya kujipa matumaini kutokana na maamuzi yake.

    Siku hiyo waliitumia kuzurura huku na kule katika jiji la Mbeya, katika mizunguko hiyo walikumbuka kukata tiketi kwa ajili ya safari siku inayofuata asubuhi sana.



    *****



    MIOYO ilikuwa inapiga kwa kasi sana, kila mmoja alikuwa akisali kwa nafsi yake ili aondoke pale akiwa na furaha. Mikono yao ilikuwa katika hali ya ubaridi sana, hakuna aliyehisi amemshika mwenzake bali kila mmoja alijihisi kuwa yuko peke yake katika ulimwengu.

    Kwa mara ya kwanza walikuwa wana hofu tangu wafunge ndoa, hofu ya kupima virusi vya Ukimwi. Huu ulikuwa utaratibu waliojiwekea tangu zamani kuwa kila mwezi watakuwa wanapima afya zao. Utaratibu uliowafanya wazoeleke hospitalini na pia kuwa mfano kwa waliowafahamu.

    Hakuna aliyetaka mwenzake agundue kuwa anatetemeka. Kila mmoja alimuona mwenzake msafi kuliko. Hali ilikuwa tete na jasho lilianza kumvuja Walter aliyekumbuka kuwa alifanya uzinzi mara kwa mara na Lilian na hakumbuki kama waliwahi kutumia kinga.

    Naomi hofu yake ilijengwa kihisia, alihisi kuwa Walter aliwahi kufanya uzinifu na dada yake wa kuzaliwa toka nitoke. Kama hisia hizi ni za kweli basi bila shaka Suzi alimuambukiza Walter na Walter naye akavihamishia kwake. Naomi aliamini kuwa iwapo ameathirika basi kwa namna moja au nyingine Walter ndiye atakuwa muhusika na atakuwa na la kujibu kwa dhambi hiyo.

    “Bwana na bibi Walter….” Daktari mwenye ndevu zilizonyolewa siku kadhaa nyuma katika mtindo wa ‘O’ aliwaita majina huku akitabasamu.

    Wote wakashtuka kana kwamba majina yao nd’o majibu ya damu zao. Walter akasimama akamshika mkono Naomi.

    Mara wakajikuta wanatabasamu kwa pamoja, tabasamu la aibu baada ya kugundua kuwa wote walikuwa wanatetemeka.

    Hatua chache zikawafikisha katika viti viwili mbele ya meza ya daktari ambaye kutabasamu kwake ilikuwa jadi.

    “Bwana na bibi Walter.” Aliita daktari. Wanandoa wakamtazama bila kusema chochote.

    Daktari akaanza kujieleza kwa kirefu akipita kona hii na ile, akitoa ushauri huu na ule iwapo wawili hawa watakuwa wameathirika. Hali ikawa inazidi kuwa tete kwa wanandoa. Maneno ya daktari ni kama yalikuwa yanamaanisha kuwa hata wao ni waathirika.

    Ilikuwa ajabu sana, kwanini maneno haya yawashtue kwa siku hii tu. Ni maneno haya haya walizoea kuyasikia kutoka kwa madaktari tofauti, iweje leo yanawatetemesha kila mmoja kwa namna yake ya mapokeo.

    Hali hii ilitisha sana.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Lakini hofu zao zisingeweza kamwe kuuzuia ulimi wa daktari kuyatoa majibu kulinagana na vipimo. Iwe isiwe lazima waondoke na majibu ya afya zao maana walipima kwa hiari bila kulazimishwa hivyo hata majibu waliyachukua kwa hiari.

    “Mpo tayari kupokea majibu yenu.” Daktari aliwauliza huku akiwatazama machoni zamu kwa zamu. Alikuwa anatabasamu kama kawaida. Alishangaza daktari huyu na kama si mtu mwenye subira unaweza kudhani anakucheka kutokana na majibu yako kiafya.

    “Tupo tayari….” Naomi alijibu kwa niaba ya Walter ambaye ulimi ulikuwa mzito.

    Daktari akaweka miwani yake machoni, akasoma kimya kimya maneno fulani katika karatasi. Hatimaye akautema ule ukweli na yueyote mwenye kuumeza aumeze.



    *****



    NYUMBA NZIMA ilikuwa imewaka moto, hakuna aliyejishusha. Baada ya subira na uvumilivu kwa kumuheshimu daktari na kisha dereva wa taksi aliyewarejesha nyumbani sasa uwanja ulikuwa wazi. Geti lilikuwa limefungwa na milango ya sebuleni ilikuwa imefungwa. Mama akageuka mbogo huku baba naye akigeuka faru. Kila mmoja akawa na hasira juu ya mwenzake.

    Naomi alikuwa wa kwanza kuanzisha ‘tifu’ baada ya upenyo kupatikana.

    “Walter..ulinikimbia na kwenda kuniletea Ukimwi…Walter unataka nife kifo kama atakachokufa dada yangu…Walter kwanini umeniua kwanini Walter.” Naomi aliugulia kwa sauti ya juu. Walter hakujishusha na yeye akapanda zaidi ili aonekane mwenye haki.

    Walter akamkaripia Naomi kwa tuhuma anazompatia akampaka zaidi kuwa ni yeye amebakwa na maaskari alivyokuwa rumande na hatimaye ameambukizwa Ukimwi.

    “Nilikuona tu siku ile eti nyoo nibebe sijui nini kunivulia nguo hadharani sijui kitu gani kumbe nia yako unipe maukimwi yako uliyopewa na maaskari huko. Naomi wewe ni muuaji tena muuaji usiyestahili msamaha Malaya mkubwa wewe. Ninajuta kukutana nawe…” Walter akakatishwa ghafla na maneno makali ya Naomi.

    “Walter…Walter unaniambia nimebakwa na polisi Walter….Walter we wa kuniita Malaya, hivi unadhani sijui kama ulikuwa unafanya mapenzi na dada yangu. Walter unaniita mimi Malaya…sikubali nasema hivi Walter sikubali…” Naomi alimalizia kauli hii huku akimvamia Walter. Kijana imara hakutegemea shambulizi lile akayumba huku na kule akasimama tena. Naomi akamrukia tena. Sasa akamkamata shati lake kwa mikono yote miwili akamkunja imara.

    Walter akajaribu kujitoa katika mikono ile lakini hakuweza. Alidhani ni rahisi sana kukabiliana na Naomi, alisahau kuwa huyu ni changudoa wa zamani aliyezoea kukabana na wanaume wababe waliojaribu kumdhulumu baada ya kuwa wamepata penzi lake.



    HASIRA ni jambo la kawaida la kwa binadamu, kuna wanadamu ambao ni wepesi kukasirika kisha hasira zao hupoa upesi vilevile, hawa ni hatari lakini si hatari sana kama ukiwahi kujishusha mbele yao. Dawa ya mtu wa namna hii ni kukaa kimya wakati yeye anapayuka.

    Binadamu wengine kwao hasira ni kitendawili kikubwa. Kuipata ni mara moja kwa mwaka na unakuta ni hasira ya kawaida. Mwanadamu wa namna hii akikumbwa na hasira kali kuishusha kwakwake yahitaji busara za hali ya juu sana, na mara nyingi hasira zao hupunguzwa kwa vitendo mbalimbali ikiwemo kupigana ama kutokwa machozi.

    Walter alikuwa mwanadamu wa aina hiyo. Baada ya kuzidiwa na karaha za Naomi mara akajikuta anamrushia mkono mzito shavuni.

    Kofi likaitika katika mlio wa kustaajabisha. Kimya kikatanda…..walter akamvamia Naomi akamkwida, Naomi akawahi kujitoa katika mikono ya Walter akarudi nyuma hatua tatu kisha akakwapua rimoti ya luninga akairusha, ni kama vile alitaka iwe hivyo, ikampata Walter barabara katika pua yake, damu zikaanza kumtoka. Naomi akiendeleza umbogo wake alitaka kumvamia tena Walter lakini akamkuta yule faru amejanjaruka tayari. Akapokea teke nyoofu katika mbavu zake, akatokwa na kilio cha maumivu huku akimtukania Walter mama yake mzazi ambaye ni marehemu tayari.

    Walter kusikia anatukaniwa mama akazidi kufura kwa hasira akasahau kuwa yule ni mkewe wa ndoa akamvamia akamnyanyua, akajirudisha nyuma sentimeta kadhaa akampiga kichwa kikali. Naomi akashikwa na kizunguzungu akalegea na kujikuta akipiga magoti mbele ya Walter.

    Hali ikazidi kuwa tata baada ya mwanamke aliyedhaniwa kuwa amezimia kumvuta Walter miguu ghafla, Walter ambaye hakuwa amejiandaa alijikuta akituliza mgongo wake katika sofa, Naomi akamuwahi akakaa juu yake na kuanza kumshambulia kwa kucha zake maeneo ya usoni, kifuani na mikononi. Walter alijaribu kupalangana lakini likatokea jingine ambalo hakulitegemea.

    Naomi akapeleka mkono na kisha kumbana katika korodani zake, hapa sasa Walter akatokwa na yowe la hofu. Naomi mwenye hasira na chuki ya waziwazi alimkazia macho Walter.

    “Walter niambie ni kwanini umeniua, kwanini umeniambukiza Ukimwi.” Walter alibaki kimya akiwa amekodoa macho, kila alipojaribu kujitikisa Naomi alikaza zaidi mkono.

    Ni mwanaume gani anao ujasiri mbele ya sehemu hizi nyeti endapo zikikamatwa imara?

    “Walter ulifanya mapenzi na nani baada ya kuondoka Dar?” Naomi akauliza kisharishari. Walter hakuwahi kumwona mkewe katika ghadhabu ya aina ile.

    “Nisamehe Naomi…nisamehe….nilifanya na Dokta….dokta peke yake…”

    “Dokta, unamaanisha dokta Suzi mume wangu…..” Naomi aliuliza.

    “Nisamehe Naomi ni huyo tu hakuna mwingine….” Walter alikuwa amekamatika ujanja mfukoni. Akakiri kumsaliti Naomi kwa kufanya mapenzi na dokta Suzi lakini kuhusu dada yake hakukubaliana na hilo hata kidogo.

    “Kwa hiyo dokta Suzi ameamua kutuua….dokta ametuua mume wangu….nimepigana nawe kisa Dokta……Walter ……Walter ulikosa nini sasa kwangu. Nilikunyima nini. Hukuithamini pete yako ya ndoa kidoleni ukazini na dokta….Walter umeniua……” Naomi alizungumza haya huku akitokwa na machozi, ule uso wenye chuki uligeuka kuwa na majonzi mazito. Walter hakuwa na hasira tena, hatia ikamsulubu. Hatia ikatembea naye.

    Akajihisi ni yeye muuaji na wala si Naomi.

    Machozi yakamtoka, akataka kusema neno lakini Naomi akatokomea kuelekea chumbani. Walter hakulaza damu naye akafuata nyuma, alikuwa anamkimbilia mkewe ili aweze kumlilia na kumbembeleza.

    Alifika chumbani na kumkuta Naomi akiwa analia huku akiwa amejifunika shuka, alijaribu kumbembeleza lakini nd’o kwanza Naomi alizidisha kilio chake. Kilio cha uchungu uliopitiliza.

    “Walter silii kwa ajili yako nalia kwa ajili yetu. Tumeuliwa Walter tumeuliwa na mtu mbaya……naomba kitu kimoja tu mume wangu. Naamini utanikubalia, nahitaji kuonana na Dokta, tukiwa wote nahitaji mbele yetu atubu kwa hili alilolifanya…na kama wewe hautahitaji kuwa name katika hili naomba uniache nikutane na huyo hayawani. Wallah patachimbika…” Naomi alitoa kauli nzito, ikaacha maswali kichwani mwa Walter. Kwa sababu Walter alikuwa muhusika katika kusambaza virusi alimkubalia mkewe. Sio hilo tu kitendo cha Lilian kutumia madawa ya kuongeza nguvu za kiume ili aweze kufanya naye mapenzi kilimuumiza upya. Mara akayumba kimsimamo akamuona Lilian kama mwanamke asiyekuwa na chembe ya huruma , mwenye mapenzi ya wizi mkubwa na mbaya zaidi ni daktari muuaji asiyejali hata kidogo utu wa wenzake.

    “Niahidi kuwa hautafanya fujo Naomi…” walter alisihi.

    “Akisema chanzo cha haya sitaleta fujo..” Naomi akajibu, Walter akaielewa maana yake.

    Hapakuwa na jingine la kuongea. Wakalala huku lao likiwa moja. Kusafiri kimya kimya kurejea Mbeya.

    Bila kumpa taarifa yoyote Lilian. Naomi na Walter walifunga safari ya kimya kimya lengo kuu likiwa kumkabili Lilian. Mwanamke ambaye alionekana kuwa muuaji mbele ya macho ya Walter na Naomi.





    *****

    ULIKUWA umepita mwezi mmoja tangu watoweke katika jiji hili la kijani, tangu waondoke walikuwa na mawasiliano hafifu. Naomi hakuwa msemaji mara kwa mara, na mara nyingi Walter ndiye alikuwa anawasiliana na Lilian.

    Hali ya kuwasiliana iliwasaidia kuwa na uhakika asilimia zote kuwa Lilian alikuwa jijini Mbeya.

    Baada ya kujipatia chumba wawili hawa wanaoamini kuwa ni Lilian aliyewaambukiza Ukimwi. Walter aliwasiliana na Lilian akimdanganya kuwa yupo chumbani katika nyumba yao amelala na Naomi. Lilian aliomba kuzungumza na Naomi. Walter akadanganya kuwa Naomi alikuwa amelala.

    Walter alikuwa ameweka simu yake katika sauti ya juu hivyo Naomi alikuwa anasikiliza kila kitu kilichokuwa kinazungumzwa. Walter akamchimba Lilian maswali ya hapa na pale mwisho wa maongezi ikafahamika kuwa alikuwa nyumbani kwake akijiandaa kwa ajili ya safari ya kuelekea mkoa wa Njombe kikazi siku inayofuatia asubuhi. Naomi alimshurutisha Walter wamtembelee Lilian usiku huohuo, kwa sababu nia yao ilikuwa kumsikia Lilian na nia yake ya kuwaambukiza Ukimwi kwa maksudi walikubaliana wamtembelee.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Baada ya dakika kumi na tano walikuwa nje ya chumba chao. Hawakutumia usafiri wa teksi badala yake walienda kwa mwendo wa miguu. Naomi alitembea upesi upesi kana kwamba anapafahamu nyumbani kwa Lilian, Walter alikuwa anamuogopa Naomi na hakutaka kumkaripia hadi hapo ukweli utakapofahamika. Kadri Naomi alivyokaza mwendo nayeye alikaza mwendo.

    Kwa mujibu wa saa zao tayari ilikuwa imetimia saa moja na nusu usiku. Hali ya hewa haikuwa ya ubaridi mkali sana, lakini Walter na mkewe walivaa makoti mazito kwa tahadhari ya mabadiliko ya hali ya hewa wakati wowote.

    Walter alilazimika kutangulia mbele baada ya kufikia kona ambazo Naomi alikuwa hazifahamu. Mwendo wa kasi vilevile hatimaye wakaifikia nyumba.

    “Nd’o hiyo nyumba mamangu..sasa sijui tunaanzaje?” Walter alimuuliza Naomi huku akielekezea kidole chake katika nyumba ambayo ilikuwa inawaka taa ndani.

    Kama Walter alitegemea Naomi ataanza kujibu swali lake ama kuzua mjadala wa kupanga maneno ya kipi cha kuzungumza na Lilian wakifika pale ndani katika namna ile ya kushtukiza basi alikuwa amekosea sana. Naomi hakungoja sekunde ya ziada baada ya kauli ya Walter, alitimua mbio kama ambaye ameona mnyama wa kutisha. Walter alibaki ameduwaa bila kujua cha kufanya na alipokuja kutanabai Naomi alikuwa anaugonga kwa nguvu mlango wa kuingilia nyumbani kwa Lilian. Hapo ndipo Walter alipogutuka na kuanza kukimbilia kule mlangoni.

    Wakati Walter anakaribia mlangoni, Naomi alikuwa amefanikiwa kuingia ndani bila kufunguliwa na mtu. Mlango ulikuwa umeegeshwa bila komeo.

    Walter naye akaingia ndani. Lilian akiwa na Kanga moja pekee alikuwa amekodoa macho akitazamana na Naomi. Hofu ilitawala machoni pake na alikuwa anahema juu juu.

    “We changudoa mzoefu, malaya wa kimataifa…..daktari usiyekuwa na huruma. Nipo hapa nikiwa na swali moja tu…….namaanisha swali moja tu…si zaidi ya hapo.” Naomi alianza kuunguruma.

    “Lakini Naomi…” Walter aliingilia kati.

    “Koma na unyamaze kimya wakati mnat…….(hakutumia tafsida) si mlikuwa mnafurahi kitandani hapo…kaa kimya Walter kaa kimya tafadhali sihitaji tugombane zaidi.” Naomi akatoa karipio, Walter akabaki kumtazama katika macho yaliyosihi sana suluhu. Kisha akaendelea, “Wewe malaya naomba ujibu maswali yangu…ulitumwa kuingilia ndoa yangu eeeh” alimalizia Naomi, nyumba nzima ni yeye pekee aliyeonekana mbogo kupita wote.

    “Naomi komea hapo hapo mimi sio malaya……kama nimeufanya na wewe huo umalaya basi ulikuwa unaota…umalaya ulioufanya na Kibwana kwani siujui au kwa kuwa nilikaa kimya” Hatimaye Lilian akasema neno, neno lililozua jambo. Naomi hakupenda kujibiwa chochote, na hiki nd’o alikuwa anakisubiri. Lilian aseme neno ili apate sababu ya kumvagaa.

    Hakika ilikuwa hivyo. Akamrukia na kuondoka na kanga yake. Matiti nje, hakuwa na chochote cha ziada. Lilian akabaki uchi wa mnyama.

    Mshikemshike.

    Daktari huyu ambaye hakuwa mzoefu wa mapambano alizidiwa kila kitu, mara moja akaangushwa kitandani.

    “Walter nisaidieee ananiuaaa Walter.” Lilian alilia kwa uchungu baada ya Naomi kumkalia kifuani.

    Kilio cha Lilian kikapenya katika masikio ya Walter, uchungu ukamshika na akahisi kuhanithiwa mbele ya hadhara.

    Lahaula!!……Walter akatazama kushoto na kulia akakutana na mwiko wa kupikia ugali. Akauchukua upesi na kumvamia Naomi, akampiga na ule mwiko mgongoni, Naomi akatokwa na kilio cha maumivu. Walter akaumizwa na jambo hili lakini hakuwa na ujanja zaidi ya kuleta amani kwa njia ile.

    Naomi alimuacha Lilian akiwa anakoroma pale chini huku akiwa ametumbua jicho kwa hofu. Naomi akataka kumvamia Walter lakini akakutana na neno zito ambalo lilimfanya alainike na kuwa mdogo kupita wote pale ndani.

    “Naomi unataka kuua tena…unataka kuua kama ulivyomuua Maureen dada yangu…Naomi roho ile haijakutosha unahitaji kuua tena.”

    Jina Maureen likabadili hali ya hewa pale ndani, Naomi akakosa la kujibu. Kimya kikatanda, hakuna aliyesema na mwenzake. Kwa Lilian hii ilikuwa habari mpya kabisa akabaki kushangaa, Walter na Naomi walimtambua Maureen. Na kifo chake walikitambua. Tatizo jipya tena.

    Simu ya Walter ilitoa mlio ambao ulirejesha uhai wa chumba kile. Simu iliita kwa muda Walter akaitoa na kuipokea bila kutilia maanani kuwa namba ile ilikuwa mpya katika simu yake.

    Naomi na Lilian wakabaki kumtazama.



    ****



    MAZENGO MATHIAS DANDA alikuwa kitandani akipitia mambo kadhaa katika simu yake. Siku hiyo alishindia nyumbani kwake kutokana na afya yake kuzorota kiasi fulani. Mafua na kikohozi vilikuwa vinamsumbua. Akaamua kujipa likizo ya siku kadhaa, likizo kwa usalama wa wagonjwa.

    Hii haswa nd’o ilikuwa kanuni ya madaktari.

    Daktari Danda naye alitii.

    Akiwa kitandani kwake majira ya saa mbili usiku alikuwa hana la kufanya, akajikuta akipitia jumbe tofauti tofauti katika simu yake. Tabasamu likajengeka usoni pake kila alipokuwa anaperuzi, bila shaka kuna mambo kadha wa kadha yalikuwa yanamchekesha.

    “Watu wanatokwa jasho aisee…” alijisemea na mkewe aliyekuwa ameketi katika kochi dogo pale chumbani akasikia.

    “We nawe kwa kuongea na simu yako looh.” Doreen mke wa Danda akampiga kijembe mumewe. Daktari Danda akatokwa na kicheko kidogo kisha akazungumza na mkewe.

    “Yaani ile juzi nimecheka sana ujue, unamfahamu huyu mzee Madati na mkewe….yaani walikuwa wadogo kama nini mh…nilicheka sana yaani hadi wenzangu wakashangaa.”

    “Uliwafanyaje kwani…” aliuliza mkewe.

    Kimya kikatanda na mumewe akaketi kitako, uso wake uliokuwa katika tabasamu ukanywea sana, ukatawaliwa na wasiwasi mkubwa na hofu pia ikachukua nafasi.

    Doreen akagundua hilo.

    “Vipi mwenzangu mgonjwa kazidiwa au…mbona kicheko hakuna tena.”

    “Mh…hivi ina maana wewe….haiwezekani.” alizungumza peke yake. Sasa alikuwa amesimama wima. Kijasho kilikuwa kinamtoka, hakika palikuwa na tatizo. Mkewe naye akaigundua hali ya mumewe, lazima palikuwa na jambo.

    “Hebu ngoja kwanza….sijui itakuwaje aisee…”

    DANDA alikuwa anaelekea kupagawa kuna ujumbe ambao alitegemea kuwa ameutuma lakini badala yake akakutana na taarifa inayomaanisha kuwa ujumbe ule haukupokelewa, ujumbe muhimu kabisa.

    Ujumbe alioutuma siku mbili zilizopita kwa sababu maalum. Ujumbe huu ukamrejesha katika kumbukumbu ya siku hiyo.

    Daktari Danda bila kumshirikisha mtu yeyote yule aliamua kuifanya siku ile kuwa siku ya kipekee sana kwake. Siku ile ilimruhusu kabisa kufanya jambo kama lile.

    Aliamka asubuhi akiwa na uamzi huo kichwani uamuzi wa kucheza na akili za watu. Hakutaka kumshirikisha mtu katika jambo lile na aliamua kulifanya kwa watu ambao ana uhakika kuwa anawafahamu.

    Tangu asubuhi alipata bahati ya kukutana na wagonjwa mbalimbali ambao alikuwa anafahamiana nao. Aliwatumia katika kutekeleza azma yake.

    Walter na mkewe walikuwa wateja wake wa nane kwa siku ile. Kama alivyofanya kwa wagonjwa wengine na kwa hawa alifanya vivyo hivyo. Alitambua fika kuwa ni hatari lakini aliamini kuwa haitadumu sana kwa sababu atasawazisha.

    Daktari Danda akawapa majibu wawili hao kuwa wameathirika na ugonjwa wa UKIMWI….hali iliyozua hofu miongoni mwao. Hakika walitetemeka lakini walionekana kutoshtushwa sana.

    Hawa walikuwa wateja wake wa mara kwa mara na kwa kiasi fulani walikuwa wanafahamiana kwa ukaribu na kuheshimiana pia.

    Baada ya walter na Naomi kutoweka eneo lile. Dokta Danda alichukua namba za simu za Naomi ambazo alikuwa nazo akamtumia ujumbe fulani. Kisha akaachia tabasamu mwanana na kuendelea na kazi nyingine.



    Sasa anashangazwa na taarifa ile kuwa ujumbe haukupokelewa katika simu ya Naomi. Utata.

    Daktari alijaribu kuipiga namba ile ili aweze kuzungumza na Naomi lakini namba ile haikuwa ikipatikana. Naomi alibadilisha namba za simu kitambo tu akiwa katika harakati za hapa na pale.

    Dokta akatafuta jina la Walter na kupiga namba ile. Ikaita akawa anangoja ipokelewe kwa matumaini makubwa kuwa ataeleweka kwa maelezo yake.

    Hatimaye simu ikapokelewa.

    “Walter….” Akaita daktari. Walter akaitika kisha akauliza anayezungumza ni nani.

    “Dokta Danda hapa….”CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Dokta niache nimevurugwa hapa nitakutafuta nikija Dar tafadhali.” Walter alijibu kwa ghadhabu.

    “Hapana Walter naomba niseme nawe dakika mbili tu tafadhali.” Alisihi Danda. Walter akakubali.

    “Unaikumbuka siku ya mwisho tumeonana ni lini.”

    “Hayo nd’o sitaki kusikia daktari.” Aling’aka Walter. Daktari hakuchoka kumsihi hatimaye akajibu.

    “Ni juzi tarehe moja ….” Alijibu Walter.

    “Naomba mnisamehe sana kuna ujumbe nilituma katika simu ya Naomi lakini bahati mbaya haukupokelewa, Walter naomba tu unielewe lakini hakuna hata mmoja kati yenu aliyeathirika na virusi. Naomba unielewe tafadhali.”

    “Unamaanisha nini dokta…kwamba.”

    “Juzi ilikuwa siku ya wajinga duniani…..sijui ilikuwa vipi lakini ujumbe niliokutumieni kwa ajili ya kuwajuza haukufika nisamehe bure kwa lolote baya ambalo limeweza kujitokeza.” Alisihi kwa busara zote daktari.

    Hakika siku ambayo Walter na Naomi wanapima virusi ilikuwa asubuhi ya tarehe moja mwezi wa nne. Siku maarufu kwa jina la ‘siku ya wajinga’ siku ambayo mambo mengi huzushwa, si haba ukisikia umetangaziwa kufa, ama kuambiwa mtu wako wa karibu amepata ajali. Dokta Danda naye aliamua kucheza na wagonjwa wake. Akawapakazia kuwa wana Ukimwi kisha anawatumia ujumbe kuwaeleza kuwa ‘ni siku ya wajinga duniani haujaathirika.’.

    Ujumbe alioutuma kwa Naomi haukupokelewa na sasa kimezuka kizaazaa.

    Walter alibaki amekodoa macho yake bila kujua nini cha kufanya. Alitamani kusema lolote lakini sauti ikakwama, laiti kama angekuwa ni mkorofi huenda angemtusi daktari lakini hasira za Walter zilikuwa mbali sana. akakiri kumuelewa daktari kisha akakata simu.



    NYUMBA ya Lilian ikazidi kuzizima. Mada ya Naomi kumuua Maureen na kutaka kumuua Lilian ikasahaulika, Walter akabaki kuduwaa kama tahira. Lilian akainuka na sasa wakawa wanamshangaa Walter.

    “Naomi….Naomi mke wangu….” Walter aliita kwa furaha, machozi yakiwa yamemlenga lenga.

    Naomi hakutarajia kuitwa kwa upendo kiasi kile, hata Lilian naye hakutarajia.

    “Naomi mke wangu…eti hatuna Ukimwi……sisi ni wazima amini usiamini.”

    Naomi akasimama wima, akasahau tuhuma alizokiuwa amepewa.

    Walter akajielezea kwa ufasaha nini kilichojiri. Ilikuwa ni siku ya wajinga.

    Wote wakabaki midomo wazi.

    “Mungu wangu wa hiyo name sijaathirika.” Lilian alizungumza huku akisimama wima. Macho ya Walter yakawahi kumkwepa maana alikuwa yu uchi. Akajishtukia akajivika kanga yake. Kila mtu alikuwa katika sintofahamu. Ugomvi ulisahaulika, kila mmoja akawaza lake.

    “Nilitaka kujiua Walter…nilitaka kujiua mimi……nilijua umeniambukiza Walter nilijua umewahi kushiriki mapenzi na Suzi…..nisamehe Walter kwa mabaya niliyowaza juu yako nisamehe Naomi nisamehe kwa kukudhulumu penzi lako nisamehe” Lilian akaanza kulia kwa uchungu, Naomi akaungana naye wakaanza kulia, walter naye akajikuta akilia kwa sauti ya juu. Kwa mara ya kwanza.

    Kila mmoja alijiona ni mfu aliyefufuliwa upya. Wakati wakiwa katika hisia kuwa wao ni marehemu watarajiwa sasa wanatambua kuwa wanayo nafasi ya kuishi tena kwa raha zao.

    Dokta Lilian alipekua katika mikoba yake akatoka na mabomba matatu ya Sindano hakutaka kulaza damu, akachukua kifaa kidogo kikiwa na mfano wa kioo.

    “Kesho mbali…mbali sana…tuhakikishe hili hapahapa.” Alisema dokta Suzi bila kujalisha iwapo yupo ambaye atachangia hoja ama vipi.

    Akaiendea meza na kuvipanga vifaa vyake.

    “Tunapima virusi usiku huu huu. Walter…Naomi…lazima iwe hivyo.” Hakuna aliyempinga.

    Walter akachukuliwa damu mkononi. Ikabakishwa katika bomba la sindano.

    Naomi naye akachukuliwa damu.

    Kisha ikafuata zamu ya Walter akapewa sindano kisha maelezo kadhaa akamchukua damu daktari Lilian.

    Yaliyofuata yakabaki mikononi mwa Lilian. Walter na Naomi walikuwa kimya wakimtazama msichana yule akifanya mambo yake.

    Alianza kwa kutumia kipimo cha kawaida cha ‘Determine’ hapo akapata majibu lakini bado hakuridhika akaamua kutumia kipimo cha Unigold ambacho kinahusika katika majibu yote yenye utata…Determine inaweza kutoa majibu kuwa una Ukimwi kumbe hauna lakini Unigold ikisema ndio ni ndio na hapana ni hapana. Lilian alifanya vipimo vyote



    GHAFLA Lilian akatokwa na yowe kubwa akakimbilia kitandani kisha akajirusha kwa nguvu, kitanda kikavunjika. Hakujali akakimbilia vyombo vya kupikia akachukua kikombe, mara chujio, mara sufuria. Kisha akatulia na kugeuka.

    “Tupo hai……tutakuwa hai….Walter, Naomi…..HATUNA VIRUSI.” Hatimaye Lilian alizungumza…….alizungumza akiwa katika mshangao. Hakuamini hata kidogo. Hakuamini kuwa hisia zimewezaje kuishi katika kichwa chake na kumtesa kiasi kile.

    Mbiombio akawakimbilia wawili wale akawakumbatia. Sasa hapa kila mmoja akaielezea furaha yake.

    Walizungumza mengi usiku ule. Naomi akieleza aliyoyapitia, akaelezea habari za Kibwana na mengine mengi alipokuwa rumande. Lilian akasema yake Walter naye akayasema yake yote.

    Wote walizungumzia hisia zao, wote walijikuta kuwa lao lilikuwa moja, Hisia!!....hisia mbaya ….

    Hisia za ajabu kabisa!!

    Yote waliyozungumza yakabaki kuwa simulizi tu na hakuna ambaye alitaka yaendelee kuongelewa siku mpya itakapoanza.

    Hawakupata usingizi maalum usiku huo, kila mmoja alisinzia kwa wakati wake. Asubuhi kila mmoja akaamka kwa muda wake, watatu hawa walikuwa wapya kabisa. Wapya kimawazo na kimtazamo.

    Damu salama katika miili yao nd’o kitu pekee kilichourudisha umoja wao upya. Kila mmoja alitabasamu, tabasamu la kutoka moyoni.

    Damu salama ikayaponya majeraha yao, jeraha la hisia likapotea katika mioyo yao. Jeraha lililopata tiba kwa ukweli pekee kuwekwa wazi. Ni ukweli pekee unaoweza kukuponya katika hisia zako potofu, ukweli wa dhati hilizidi nguvu jeraha. Unaweza kukutonesha lakini ukipona ni uponyaji wa moja kwa moja.

    Kwa nini hisia ziharibu mahusiano yetu, kwanini hisia ichukue nafasi ya kufanya maamuzi katika nafsi zetu. Hisia isilete chuki kati yetu, hisia isilete uhasama kati yetu.

    Jeraha la hisia hutibiwa kwa kuutambua ukweli na kuupa nafasi katika mioyo yetu.



    BASI kubwa lilipiga honi ya mwisho. Lilian akawatazama Walter na Naomi kwa uchungu mkubwa, hatimaye walikuwa wanarejea jijini Dar es salaam baada ya kuwa wameishi kwa kipindi cha juma moja mjini Mbeya kwa furaha kubwa na amani tele bila tofauti kati yao.

    “Naomi..ukifika tu naomba unifikishie ujumbe wangu kwa Suzi..nd’o pekee atakayenipa furaha.” Lilian alimkumbusha Naomi huku akitoweka.

    Safari ikaanza rasmi…….safari ya kwenda kuanza maisha mapya tena kama wanandoa. Wanandoa waliopitia mitafaruku mingi lakini nguvu ya penzi la kweli ikasimama imara kupigana na vizingiti na hatimaye penzi la kweli likathibitika mwishoni.



    Ilikuwa kama Lilian alivyoomba. Suzi dada yake Naomi alisafiri kuelekea Mbeya kwa wajina wake na pia daktari wake.

    Furaha iliyoishi katika nyumba ya Naomi na Walter ikaishi pia katika nyumba ya Lilian na Suzi.

    Lile jeraha likatoweka kwa aibu kuu na kupotelea pasipojulikana……

    Furaha hizi za pekee zikamwondoa mchezoni mwandishi huyu aliyejaribu kwa kila mbinu kulizuia jeraha hili lisipone.

    Mwanzo wa furaha hizo ukaleta mwisho wa simulizi hii ya aina yake katika mapenzi kutoka kwa George Iron Mosenya.



    ***LEO usipite kimyakimya tafadhali  comment chochote kuhusiana na simulizi hii iliyomalizika…….maoni yako yatanijenga

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    **ASANTENI SANA KWA KUWA NAMI TANGU SEHEMU YA KWANZA HADI MWISHO



    MWISHO!!

0 comments:

Post a Comment

Blog