Search This Blog

Tuesday, 14 June 2022

HOFU - 1

 





    IMEANDIKWA NA : GEORGE IRON MOSENYA



    *********************************************************************************



    Simulizi : Hofu

    Sehemu Ya Kwanza (1)





    “OLE!! OLE WAKO KINDO” maneno haya yaliendelea kujirudia katika kichwa chake hata siku ilipobadilika baada ya mshale mfupi wa saa kuielekea namba kumi na mbili na ule mrefu nao ukielekea katika namba moja.

    Ilikuwa saa sita na dakika tano usiku!! Siku ya jumanne.

    Kindo hakuwa amepata usingizi tangu Salome aondoke majira ya saa tatu usiku huku akitoa viapo visivyoeleweka.

    “Aaaargh! Aende zake huko, mimba wampachike watu wengine halafu aniangushie mkasa huu mimi. Hamna kitu kama hicho, maisha ya kulea mtoto mimi nayatoa wapi sasa, chandarua hiki nimeshindwa kukibadili, mama mwenye nyumba ananidai kodi yake hadi leo sijamlipa. Nguo zangu zimetoboka nimeziba na viraka hadi viraka navyo vinazibwa na viraka vingine. Naanza vipi Kindo mimi kupata pesa ya kununua maziwa ya mtoto…. No no!! hata kabla ya mtoto, hilo tumbo nalilea vipi kwa miezi tisa. Mbaya zaidi ni tumbo lisilonihusu kabisa hata kidogo, yeye kama walimlewesha huko wakambaka bila kujua na asubuhi anajidanganya ni mimi nimempachika mimba shauri zake!!” alizungumza peke yake kwa sauti ya juu huku akitupa mikono huku na huku. Kifua kikiwa wazi na jasho likimchuruzika.

    Kindo alikuwa ametaharuki huku akijaribu kuudhibiti mwangwi wa sauti ya Salome. Mwangwi uliompa onyo lisiloeleweka!! Ole wako Kindo….

    Kitanda kilicholegea kikapiga kelele na kuwafanya panya katika dari kucheka katika lugha zao za maudhi.

    Kindo alikuwa ametelemka kwa ajili ya kujifuta jasho lililokuwa linazidi kuchuruzika.

    Joto la leo….!! Alilalamika huku akijipangusa.

    Kisha akarejea kitandani tena, kulilalia godoro lililokuwa katika siku za mwisho za uhai wake.

    Miale ya radi ikawaka huku na kule, kisha ngurumo zikapasua anga.

    “Nd’o maana nikashangaa mbona joto hivi… kumbe mvua inataka kunyesha!!” kauli hii haikumalizika kabla Kindo hajakurupuka na kuanza kuhangaika kuhamisha kitanda kwenda upande mwingine. Maana upande sahihi kilipokuwa palikuwa na tatizo la kuvujia maji, na alikwishaziba matundu hadi akachoka pasi na mafanikio.

    “Salome angekuwepo angenisaidia kuhamisha hiki kitanda….” Kindo akajikuta akisema tena huku akiikaza misuli kwa nguvu zaidi.

    Mvua kubwa sana ikafuatia!!

    Joto likakimbia na sasa Kindo akaanza kulalama kuwa baridi imekuwa kali sana!!

    Mvua haikukoma hata pale usingizi mzito ulipomtwaa Kindo.



    ****



    “Kindooo, yoh! Kindo man, oyaa we Salome muachie mwenzako muda wa kazi huu”

    “We Kindo wewe!!! Kindooo….”

    “Kindo tunakuacha sisi….”

    “Kindo tusilaumiame ohoo shauri zako utamla huyo mwanamke!!!”

    Kindo akajigeuza upande wa kushoto huku akitamani sauti zile ziendelee kuwa ndoto. Lakini haikuwa, sauti zikazidi akalazimika kufunua macho yake.

    “Kwani saa kumi na moja imefika?” aliuliza kwa sauti iliyokuwa inakoroma kwa kulalamika.

    Matusi ya nguoni yaliyofuatia yalimfanya atoke kitandani. Alishawazoea rafiki zake watatu jinsi walivyokuwa mabingwa wa kutukana.

    Alilala na nguo zake zote, alichofanya ni kuvaa viatu na kutoka nje. Huko napo akapokelewa na tusi la nguoni, naye akajibu.

    Usingizi ulikuwa umeenda zake!!

    “Mbona mikono mitupu mwenzetu..” rafiki mmoja akahoji. Kindo akarejea upesi ndani, akainama uvunguni na kutoka na koleo.

    “Salome… shem eeeh pole bwana kwa kukupeperushia ndege wako…” Maulidi mmojawapo wa marafiki alisema huku wakitoweka. Kindo akatikisa kichwa kushoto na kulia.

    Hakuna aliyejua!! Na hakutaka wajue mapema hiyo kabla ya kazi.

    ___________CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    MITALO ilikuwa imesheheni mchanga haswa, na vijana hawa walikuwa wamedamka wakati muafaka kabisa. Walikusanya mchanga vichuguu kwa vichuguu bila kuchoka.

    Kufikia majira ya saa tatu asubuhi walikuwa wamejiridhisha kwa kazi yao ya siku.

    Maulidi akauendea mfuko, akatoa viazi vitamu, John akatoa dumu la maji. Hakuna aliyengoja kukaribishwa.

    Njaa kali iliwafanya wale kwa pupa sana kama kwamba viazi vitaisha, lakini shibe ikawalegeza na kila mmoja akaviona viazi vilivyosalia kama mzigo wa uchafu.

    Kila mmoja alikuwa ameshiba.

    “Wewe Kindo uliyeoa kabla ya muda utabeba hivi vilivyobaki umpelekee Shem Salome.” Masalu, rafiki wa tatu alisema kwa lafudhi yake ya kisukuma. Maulid na John wakacheka lakini Kindo ambaye alikuwa mwepesi wa kucheka siku zote akastaajabisha.

    Hakucheka!!

    “Salome mshenzi sana, ujue mliponiambia wanawake akili zao fupi sikuwahi kuamini kuwa hata Salome naye ni msichana na anaweza kuwa hivyo. Si unakumbuka Maulidi tulitaka kugombana siku moja…” Kindo alitokwa na kauli hiyo akiwa ameinama.

    Kimya kikatanda, hakuna aliyeamini kuwa Kindo anasema vibaya juu ya Salome. Wote walijua ni kiasi gani Kindo alimpenda Salome na hakuwahi kuwa na msichana mwingine zaidi yake, na hata hao marafiki walikiri kuwa Salome pia hakuwa na mwanaume mwingine zaidi ya Kindo.

    “Salome kafanya nini tena…”

    “Ameondoka zake kwenda kwa wanaume zake…” alijibu kwa mkato.

    “Wanaume wake??” wote watatu kwa pamoja waliuliza.

    Kindo akatabasamu kidogo kabla ya kuwaelezea mkasa uliomkumba hatua kwa hatua.

    “Uzuri ni kwamba rafiki zangu wote niliwaeleza kila jambo, siku ile niliowaeleza kuwa nina wasiwasi Salome ana ujauzito kwa sababu haoni siku zake, tena nikawaeleza kuwa ikiwa kweli ana mimba basi ni yangu. Na baada ya hapo ni siku ile nilipowaita na kuwanunulia soda ili kufurahia Salome kuingia siku zake. Wote mlikuwepo, sasa jamani kama aliingia katika siku zake vizuri kabisa hii mimba mimi nahusika nayo vipi? Hebu vaeni viatu vyangu na nyinyi muwe upande wa maamuzi…” Kindo alimaliza, hakuna hata mmoja aliyesema neno zaidi ya kuguna tu.

    Viazi vilizidi kusahaulika na nzi wakajifanyia sherehe.

    “Walah huu mtihani hakiyanani!!” Maulid aliapa huku akisimama asijue kwa nini amesimama. John na Masalu wakabaki kumtazama.

    “Yaani aingie siku zake halafu aseme tena ana mimba yako…. Kindo kaka, kama kweli haujalala na yule mtoto tena baada ya pale kama asemavyo Mau… Walah huu mtihani…” John aliiga lafudhi ya kipemba ya Mau na kusababisha vicheko.

    Kasoro Kindo tu!! Hakucheka. Aghalabu kutabasamu.

    “Kindo, kule kanda ya ziwa, wakurya wanasema hivi ‘Mang’ana ghasalikiree’ yaani mambo yameharibika!!” Masalu alisema kwa kumaanisha lakini sasa kila mmoja hata Kindo naye alicheka.

    “Na alisema anaenda wapi?” John aliuliza.

    “Hakusema yaani aliimba mashairi mengi wee, mara ole wako sijui nini na nini… mwisho akaondoka, yaani akaubamiza ule mlango hadi nikasema ameuvunja. Yule binti yule dah!!” alizungumza huku akijitoa hatiani

    “Kindo nenda nyumbani, Salome ninayemjua mimi walah hawezi kuishi mbali na wewe, mama yake mwenyewe anajua kabisa kuwa yule ni wako. Nenda nyumbani kama hayupo nenda kwa mama yake. Mweleze kilichotokea na usithubutu kusema kuwa ulimfukuza Salome.. usithubutu kabisa.” Maulid alitoa ushauri uliokubaliwa na kila mmoja.

    “Na kitu ambacho nadhani, huenda hata hana mimba yule amefanya kunizingua tu anione msimamo wangu eti eeh!!” Kindo alizungumza huku akiwa na furaha.

    Wakaagana na kumwacha Kindo aende nyumbani na wao wakabaki kungoja wateja wa mchanga waweze kuuza na kujipatia ridhiki.



    ***



    MANENO ya marafiki yakaijenga faraja moyoni mwa Kindo, nguvu zikamjaa tele akatembea upesi upesi akiwa amebeba koleo lake na lile furushi la viazi akakaza mwendo kwenda nyumbani huku akiwa na matumaini tele kuwa anaenda kuonana na Salome tena.

    Mvua iliyokuwa imenyesha ilifanya ardhi isiongope iwapo itakanyagwa.

    Naam!! Alama za kandambili alizokuwa amevaa Kindo wakati wa kutoka alfajiri zilionekana vyema, hata alama za miguu pekupeku ya rafiki zake waliokuja kumgongea asubuhi zilionekana pia.

    Lakini kulikuwa na alama za ziada, zilikwenda mlangoni na kisha kutoweka tena.

    Alama za viatu visivyojulikana kama ni vya kike ama vya kiume.

    “Salo….. Salomeee!!” Kindo alianza kuita kwa sauti ya chini kiasi.

    “Salome mke wangu!!” sasa aliipaza huku akiufuata mlango. Alijua ni kiasi gani Salome alipenda kuitwa mke.

    Akaufungua kwa kuusukuma taratibu akitarajia kukutana na uso wa Salome.

    Mlango ukafunguka, Kindo akaingia ndani lakini alikuwa yeye na kitanda chake ambacho sasa aligundua kuwa kilikuwa kimevunjika upande mmoja. Bila shaka wakati wa kukihamisha.

    Akashusha pumzi kwa nguvu!! Akatamani kuketi kitandani lakini akahofia kitavunjika zaidi. Akakivuta kigoda na kukaa hapo.

    “Kama hayupo, nenda kwa mama yake!!” akaikumbuka sauti ya Maulidi. Akafanya tabasamu hafifu. Akayaendea madumu mawili ya maji, moja lilikuwa tupu na jingine lilikuwa na maji kiasi.

    Akalitwaa ili aweze kwenda kuoga na kisha afanye safari ya kwenda kwa mama mkwe.

    Wakati anatoka nje akamuona mwanaume mgeni kabisa machoni pake akijongea moja kwa moja kuja katika mlango wake.

    Aidha alikuwa anakuja hapo ama la!! Kindo akalazimika kungoja.

    “Habari za asubuhi bwana!!.. bwana Emmanuel kama sijakosea..”

    “Kha!! Hapa… eehm ndio Emmanuel….” Alijiuma uma Kindo, akistaajabu huyu ni nani amjuaye kwa ufasaha namna hiyo.

    “Karibu ndani!!” alimkaribisha yule bwana ambaye hadhi yake haikufanania hata kidogo na muonekano wa mle ndani.

    Kindo akavuruga baadhi ya nguo zake stuli ikabaki wazi akamkaribisha yule bwana ambaye aliingia ndani pasipo kuvua viatu.

    “Emmanuel Kindo….. Kindo Kindo Emmanuel….” Kwa sauti ya chini huku akiipigapiga kalamu yake huku na kule yule bwana aliliimba jina la Kindo.

    “Wewe ni nani samahani bwana!!” Kindo akamkata kauli. Sasa alimkazia macho.

    “Hiki kitanda huwa mnalala vipi watu wawili sasa?” badala ya kujibu aliuliza.

    Kindo akaonekana kukerwa na swali lile. Lakini hakusema neno zaidi ya kuhimiza juu ya utambulisho.

    “Hata kama asingekufa nisingekubali hata kidogo aolewe na mtu wa namna hii… “ aliendelea kusema peke yake. Hali iliyozua wasiwasi kwa Kindo hasahasa baada ya kusikia juu ya kufa na kuoana.

    Bila shaka hapa anamzungumzia msichana!!

    Kindo akaomba kwa kila namna msichana huyo asiwe Salome.

    “Wewe ni nani kaka, nina mashaka kuwa umekosea nyumba….”

    “Weee koma komea hapo hapo nasema shwain wewe!!!” ghafla yule bwana akapaza sauti akimkaripia Kindo, alikuwa amesimama huku akiielekeza fimbo yake ya kutembelea machoni pake Kindo.

    “Nasema kaa kimya kabisa mwanaharamu wewe!!” alizidi kuonya. Kindo akanywea na kukaa kimya.

    “Wewe Emmanuel Kindo, ni kitu gani kilikufanya ukamlaghai mwanangu, akatoroka shuleni na kunidanganya kuwa shule imefungwa sijui anapitia kwa shangazi yake gani huko…… eeh wewe mwanaharamu wewe nakuuliza….” Akasita na kufanya kicheko kidogo kikisindikizwa na kauli nyingine ya kustaajabisha, “ Yaani watoto wa siku hizi, yaani Kindo kiukweli mlijitahidi kuongopa yaani mama yake ujue akadhani kweli kabisa, ila tatizo ni siri haina watu wawili, mwenzako alimshirikisha rafiki yake ndo huyo aliyeniambia…….” Kicheko kikafuata tena. Halafu ghafla tena akabadilika.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    ”We mpumbavu, unanikodolea macho hapa…. Ni kwanini ulimdanganya mwanangu…” kimya kikatanda, Kindo akawa kama zezeta tu asiyeelewa chochote.

    Lazima aduwae!! Maana kama huyu alikuwa mzee wa Salome basi huyo Salome mwenyewe aliishia darasa la saba tu tena miaka mingi ilikuwa imepita tayari.

    “Mzee sikuelewi bado….”

    “Naitwa mzee Gaspari Nshomile mzazi wa Rebeka Nshomile mliyembatiza jina la Rensho…. Yeye ndo Re na mimi ndo Nsho…..RE-NSHO….mimi ni baba yake mzazi na Rensho….” Alijitambulisha yule mzee kwa kujiamini kabisa akitarajia labda Kindo atashtuka lakini ndo kwanza alizidi kushangaa.

    Rensho!! Jina geni kabisa.

    “Mzee!!”

    “Nani mzee wako shenzi wewe…… mimi ni mzazi wa Rensho, mwanafunzi wa kidato cha tano hapo Tabora girls unajifanya humjui eeeh….. hauna redio humu ndani ama….punda kasoro mkia wewe. Umemrubuni msichana halafu amekufa ndo unajifanya humjui… umenichefua tayari na sasa utajua nini maana ya nshomile.” Alipandwa na jazba yule mzee na kuanza kushusha kipigo kwa Kindo, alijaribu kuruka huku na kule lakini hakufua dafu.

    “Huwezi kunikimbia mimi punguani wewe, vita vya Kagera wananijua walioshiriki, mimi nilimkung’uta teke Iddi Amini hakuwahi kunisahau hata leo ukifukua kaburi lake ukamuuliza atakwambia …..” haya yalimtoka huku akimchapa bakora Kindo ambaye muda wote alilalamika kuwa hamjui wala hajawahi kusikia jina la Rensho.

    “Nitarejea baadaye hapa. Shida yangu ni moja tu mkoba wa Rensho uliouchukua. Sijali kama utakuja kumzika ama hautakuja, cha muhimu mkoba halafu mimi na wewe tunayamaliza haya mambo kiume. Vinginevyo nitakukabidhi kwa polisi ukafungwe maisha.” Alitoa onyo, kisha akajiweka sawa kwa kuondoka.

    “Na kabla sijasahau, meseji yako uliyotumiana naye kuwa mnaagana imekutwa katika simu yake… hauna ujanja pumbavu wewe….” Alimaliza akasonya na kutoweka.

    Simu? Aliduwaa Kindo akiwa ardhini akiugulia maumivu.

    Tangu lini mimi nikawa na simu!! Mbona niliiuza huu sasa ni mwezi unapita. Amenifananisha huyu mzee maskini wa Mungu mimi. Alijisemea Kindo huku macho yakimsindikiza yule mzee hadi akatoweka.

    “Mzee Nshomile…..Nshomile kivipi wakati mzee wake Salome anaitwa Wilbard…. Ndio, Salome Wilbard na Rebeca Nshomile wapi na wapi?” sasa alizungumza kwa sauti huku akijikongoja na kusimama akaegemea ukuta wa chumba chake.

    Na hapo Kindo akayakumbuka maneno makali ya mwisho ya Salome. Usiku ule wanakorofishana na kisha Salome kutoweka.

    “Kindo, nazungumza nawe huku natokwa machozi haya yanayoliangukia godoro hili ambalo ni Mungu ajuaye kuwa ni godoro langu la mwisho kufanyia mapenzi. Nazungumza haya huku nikilia na kiumbe kilichopo tumboni kinisikie, nasema nawe Kindo kwa sauti kuu. Sauti ambayo utahitaji kuiskia na hautaisikia kamwe!! Itunze kauli hii Kindo, baba na mama yangu hawawezi kunitunza nikiwa na tumbo hili na sitakuwa jasiri wa kuwaeleza kuhusu jambo hili ambalo ni langu mimi na wewe. Kindo wewe ni mweusi mtanashati una mwanya na ni mrefu, nasema OLE!!! OLE!! KINDO huyu mtoto akikufanana kwa chochote kile na hali amekusikia ukimkana na ukimkana mama yake….KINDO nimevunja viapo vyangu vingi sana, lakini kiapo cha kukusulubisha sitakivunja kamwe!! Lakini usiponiona milele basi ujue nilikusaliti kwa mwanaume mwingine ambaye ni baba wa huyu mtoto” akaubamiza mlango na kutoweka.

    Kindo akasonya akajifunika shuka vizuri akidhani sasa ana amani!!

    LAKINI huo ukawa mwanzo wa hofu!! Hofu kubwa.



    Kindo akaanza kuhisi maneno yale yalikuwa na maana kubwa. Lakini yu wapi wa kuielezea maana ile iwapo Salome hayupo tena!!

    Mtihani!







    “Na kabla sijasahau, meseji yako uliyotumiana naye kuwa mnaagana imekutwa katika simu yake… hauna ujanja pumbavu wewe….” Alimaliza akasonya na kutoweka.

    Simu? Aliduwaa Kindo akiwa ardhini akiugulia maumivu.

    Tangu lini mimi nikawa na simu!! Mbona niliiuza huu sasa ni mwezi unapita. Amenifananisha huyu mzee maskini wa Mungu mimi. Alijisemea Kindo huku macho yakimsindikiza yule mzee hadi akatoweka.

    “Mzee Nshomile…..Nshomile kivipi wakati mzee wake Salome anaitwa Wilbard…. Ndio, Salome Wilbard na Rebeca Nshomile wapi na wapi?” sasa alizungumza kwa sauti huku akijikongoja na kusimama akaegemea ukuta wa chumba chake.



    “Wazee wengine wamechanganyikiwa sijui?” alijiuliza kwa sauti ya juu huku akiamua kukikalia kitanda chake ambacho kimevunjika.

    Lakini!...... amenijuaje kwa jina kamili kabisa la Emmanuel Kindo? Alijiuliza huku akiwa amejiegemeza ukutani na kichwa chake kikipakatwa na mikono yake miwili.

    Swali hili likawa gumu zaidi. Na asingeweza kuendelea kukaa bila kuwa na jibu. Akakumbuka kuwa alitakiwa kwenda kuonana na mama yake Salome ili aweze kupata uhakika kama ni kweli Salome atakuwa yu nyumbani kwao ama la!

    Alitamani kunyanyuka na kuanza safari lakini maumivu kwa mbali kutokana na kipigo alichopokea kutoka kwa mzee Gaspar Nshomile yalimfanya apitishe uamuzi wa kulala kidogo huku akiapa kuwa akiamka tu anaoga kisha anaenda nyumbani kwa mama yake Salome.

    Kindo aliusahau ule usemi wa liwezekanalo leo lisingoje kesho, akafumba macho yake na kuusaka usingizi.

    Wakati yeye akiusaka usingizi na hatimaye kuupata na kuanza kukoroma, mitaa fulani mbali kabisa kutoka alipokuwa amelala yeye liliendelea tukio ambalo laiti kama angeamua kuupuuzia uamuzi wa kulala basi angeweza kulishuhudia na kulipinga kwa nguvu zote. Kidogo imani ingeweza kurejea labda!! Lakini tukio hilo la aina yake lilitokea huko mbali kabisa yeye akiwa amelala kisha tukio lile likahama kwa kasi ya ajabu.

    Mlango ukamshtua kutoka usingizini, ulikuwa umesukumwa kwa nguvu sana. Akayapikicha macho yake na kitu cha kwanza kuona baada ya akili kutulia ni saa ya ukutani.

    Saa kumi na moja na robo!!

    Kindo alikuwa amelala sana!!

    “Mtazame asivyokuwa na aibu!!” sauti ikasema katika namna ya kusuta!! Sauti haikuwa ngeni hata kidogo katika masikio yake. Na kama akili ilivyoishika sauti ile ndivyo macho yalivyoleta uthibitisho.

    Alikuwa ni yeye mwenye ile sauti.

    Mwanamama akiifunga kanga yake kuukuu kiunoni huku akingoja Kindo azungumze.

    “Shkamoo mama!!... karibu mama..yaani…leo nilitaka nije…”

    “Shhhhhhh!! Ishia hapo hapo Kindo, mtoto mbaya wewe. Umejivika ngozi ya kondoo ilhali u chui mkali.” Mama yake Salome alimkatisha Kindo.

    Kindo akastaajabu!! Hakuwahi hata siku moja kuingia katika mtafaruku na mama yake Salome, sasa iweje leo.

    “Kindo, Kindo ni wewe. Kindo ambaye ulikuwa unaugua Salome anakuja kunililia nyumbani, nachukua shilingi zangu kadhaa. Kindo, shilingi pekee zilizopo ndani nakununulia dawa kwa moyo mmoja na kwa ajili ya furaha yako na Salome. Kindo ni mara ngapi Salome amechukua unga wa ugali nyumbani ili usilale njaa wewe, ni mara ngapi Kindo. Mnafiki mkubwa wewe ukachonga mdomo wako kunilaghai kuwa utamuoa mwanangu wewe, na sasa naingia hapa unanirubuni na shkamoo yako hiyo ya kinafiki…. Kindo wewe ni muuaji mkubwa, hufai kuwekwa katika kundi la wanaume. Hufai Kindo…. Yaani…” mama Salome akashindwa kuendelea kuzungumza akabaki kutetemeka na sasa machozi yalikuwa yanamtiririka.

    Kwa mara ya kwanza Kindo anashuhudia uso wa mama huyu maskini ukikosa tabasamu na kutawaliwa na hasira. Kindo akataka kusimama aweze kumnyamazisha akakutana na karipio kali lililomrejesha kuketi kitandani.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Lakini mama, Salome na mimi tulizungumza na kuelewana. Hata ungekuwa wewe mama…. Labda kama Salome amesema vingine tu… unatakiwa kunisikiliza mama..”

    “Mlielewana katika huo upuuzi, ujinga mkubwa mtoto wa kiume unakuwa dhaifu kiasi kile. Salome mwanangu hajasoma hata hilo la saba alifeli lakini narudia Salome sio mjinga hata kidogo wa kuchekelea mahusiano yako sijui ndoa yako na huyo sijui Recho sijui Rensho, kamwe Salome si mjinga. Alikupenda sana ujue, Salome alikupenda sana hujui tu hayawani wewe.

    Kweli Kindo, pesa za ukoo wa mwanamke zinakufanya unamkana mwanangu mimi. Unaamua kumuumiza mwanangu mimi kwa sababu ya mwanamke mwingine mwenye pesa….. hivi unaoa ama unaenda kuolewa Kindo, ona aibu … ona aibu Kindo wewe si wa kufanya ulichofanya kwa Salome.

    Unasimama kabisa kuwaambia rafiki zako akina Mau na John, eti Salome mshenzi sana kupita wasichana wote uliowahi kuona. Mpuuzi mkubwa wewe, unamuita Salome mshenzi kwa sababu umepata mwanamke mwenye pesa, mbingu na ardhi zikuzomee na aibu iwe juu yako.” Alitema cheche mama Salome, machozi hayakuisha kububujika.

    Kindo akabaki kuduwaa asielewe mama Salome anachokizungumza hadi anatokwa na machozi amekitoa wapi.

    “Mama…. Upo sawa kweli?” Kindo aliuliza kwa upole akidhani ataeleweka na kushusha jazba ya mama Salome.

    “Dharau!! Dharau zitakuua maskini wewe, mtazame. Kumpata huyo Rensho sasa kila mtu unamuona mwendawazimu, umemtukana Salome wangu na sasa unanitukana mimi. Wanadamu wanadamu…” alimaliza kwa kicheko cha dharau. Kindo akazidi kuhamanika akihangaika kujiuliza ni kitu gani kinatokea. Baba yake Rensho amekuja kudai mkoba wa marehemu mtoto wake, na sasa mama yake Salome anakuja kumlalamikia kuwa kwa sababu anakaribia kuoana na Rensho basi ameamua kuachana na Salome.

    Hiki nini sasa? Alijiuliza. Wakati huo mama Salome alikuwa anajiandaa kuondoka na hakuonekana kama ataaga.

    “Kindo!!” aliita kisha akamtazama machoni, “ Sijui Salome yupo wapi muda huu baada ya kumweleza hayo maujinga yako, ila napenda tu kukutahadharisha kwamba iwapo Salome atakumbwa na kitu chochote kibaya. Basi itafahamika kama sisi watu wa tabaka la kimaskini tuna haki ama hatuna haki, naapa Kindo. Ole wako Salome aathiriwe na kitendo ulic hofanya, nasema ole wako. Ama zangu ama zako na hiyo ndoa haitafungwa labda wewe na matajiri wenzako mniue kwanza.” Akafanya kiapo kishas akabamiza mlango bila kuaga akatoweka asiijali sauti ya Kindo iliyoendelea kuita mama mama!!

    Siku hii ikawa chungu zaidi kwa Kindo ambaye hakujua ni kitu gani kinatokea na yeye kuandamwa na vitu asivyovijua. Kwanza Rensho katika upande wa baba yake na sasa huyu huyu Rensho anasemwa na mama yake Salome.

    Kizaazaa!! Alikiri Kindo huku akipiga hatua hapa na pale katika chumba chake. Mara akakoma ghafla mlango ulipofunguliwa tena.

    “Mguu huu utarejea tena hapa iwapo tu mwanangu atakumbwa na jambo baya, lakini kama atakuwa salama…. Kindo usitegemee kuniona tena hapa katika kibanda chako na wewe usikanyage nyumbani kwangu!!” mama Salome alikoroma tena kisha akaondoka, wakati huu hakuubamiza mlango.

    Kindo akabaki katika hali isiyoelezeka, hakuwa katika mshtuko wala mshangao, akarejea kitandani kujilaza huku akitafakari ni kitu gani kinatokea katika maisha yake.

    Rensho ni nani?

    Akajaribu kuvuta picha miaka ya nyuma huenda kuna mwanamke waliwahi kupendana naye aliyeenda kwa jina la Rebeka Nshomile, alihangaika sana kufikiri lakini bahati mbaya hakupata kabisa jina linaloendana na hilo hata kwa mbali.

    Wamenifananisha na nani sasa mimi jamani? Swali likapita kichwani mwake



    ****



    WAKATI Kindo akitafakari mambo yanayomtokea na kujiuliza maswali kadhaa, abiria wa basi mojawapo liendalo mkoani wa Mwanza walikuwa katika malalamiko. Kila mmoja na lalamiko lake lakini yote haya yakiwa katika jambo moja tu. Kuharibikiwa gari njiani. Yalikuwa yamepita masaa manne tangu basi liharibike na mbaya zaidi hapakuwa na basi la kampuni hiyo ambalo lingeweza kufika na kuwachukua waendelee na safari.

    Wanaume walikaa katika makundi na wanawake waliunda makundi yao pia. Walikuwa na nyuso za furaha awali wakitarajia kuwa muda si mrefu basi litatengemaa na safari kuendelea lakini baadaye kila mmoja alikuwa amenuna baada ya kugundua kuwa walivyodhani sivyo. Hapakuwa na dalili ya basi hilo kutengemaa mapema.

    Joram alitambua waziwazi kuwa uwezekano wa basi lile kutengemaa ulikuwa mdogo sana, lakini asingeweza kumwambia mtu yeyote yule kasoro tu mafundi wenzake. Ambao kama yeye na wao walishagundua shida hiyo.

    Taarifa ama uhakika huu ulikuwa mbaya sana kwa Joram. Tayari alikuwa amefanikisha alichokuwa anataka na sasa lilibaki hitimisho tu na sasa kinatokea kikwazo kikubwa kiasi kile.

    Joram akaangaza macho yake huku na kule kisha macho yakatua kwa mwanadada Salome ambaye tofauti na abiria wengine yeye alikuwa amejitenga na kukaa peke yake akiwa ameinama, Joram akashikwa na imani akikumbuka kila kitu alivyosimuliwa na Salome usiku uliopita kabla ya kuamua kumchukua na kumsafirisha kinyemela ilimradi tu afike Mwanza

    “Salome yaani hapa sina hata senti!!! Sijui hata tunafanyaje” alijisemea Joram kimoyomoyo huku akimtazama yule binti tena.

    Joram alikuwa katika hisia kuwa Salome huenda anahisi njaa kwani tangu alivyomnunulia soda na keki asubuhi basi hakuwa ameingiza kitu kingine tena tumboni.

    Lakini wakati huo Salome hakuwaza hata kidogo juu ya njaa bali kichwani mwake zilipita kumbukumbu mbaya na nzuri alizowahi kupitia akiwa na mpenzi wake, Kindo. Akazikumbuka ahadi zote walizowahi kupeana kipindi cha nyuma. Akaikumbuka ahadi ya kutosalitiana kamwe, neno usaliti likawa kama linamwandama kichwani mwake na kujihisi mkosefu ajuaye kosa analotaka kufanya. Salome alikuwa katika miadi ya kutoa rushwa ya ngono kwa Joram iwapo tu atamfanikishia safari yake ya Mwanza kwa sababu hakuwa na pesa lakini alitakiwa kuondoka na kuwa mbali kabisa na Kindo aliyeikataa mimba yake. Machozi yakamtiririka Salome na kujiona kama mzigo alionao kichwani ni mkubwa zaidi tena ni kama uonevu uliokithiri.

    Sasa gari lilikuwa limewaharibikia!! Tatizo jingine.

    Kumbukumbu zikaendelea hadi alipoukumbuka usiku usiosahaulika alipoamua kujiweka mbali na Kindo huku akiweka kiapo.

    “Kweli Kindo ni wa…..” kauli hii haikufika mwisho. Mara akahisi kitu kikikimbia kwa kasi kubwa sana katika mwili wake, hali hii huwa inamtokea akiwa katika hali ya kawaida, lakini kwa hali aliyonayo hatakiwi kuwa na hali hiyo.

    Sintofahamu ikamkabili, akadhani hayupo sahihi kufikiria juu ya kinachotaka kumtokea. Muda nao haukumpa nafasi ya kufikiri mara mbili zaidi.

    Damu!!

    Salome alikuwa anavuja damu ya hedhi!!!

    Hana pedi mahali popote pale.

    “Joraaaam…. Joraam….” Aliita huku akipepea mkono, kondakta aliyekuwa akihisi kuwa Salome anaweza kuwa na njaa kali, alitimua mbio akiwa na wazo hilohilo kuwa ni njaa inamsumbua.

    Akamfikia na kukutana na kitu tofauti kabisa.

    Salome alikuwa anavuja damu!!CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Joram akafedheheka katika namna ya pekee, hakutegemea jambo lile kabisa. Si kwamba alimuonea huruma Salome bali alijionea huruma yeye na kujipa pole kwa sababu alichokitaka katika mwili wa Salome kisingeweza kutimia tena akiwa katika hali ile ya kutokwa damu, Salome akamweleza kuwa awaulize wanawake kama wanaweza kuwa na pedi za akiba.

    Joram akaondoka akiwa katika hali ya simanzi, hakujali juu ya wakati mgumu anaopitia Salome bali alijitazama yeye pekee na kujihisi anaonewa kwa kuukosa mwili wa Salome baada ya msaada wake wote ule hadi kumfikisha pale.

    Joram hakurejea tena kwa Salome, badala yake alifika mwanamama mwingine kabisa na kumsaidia Salome, Salome akajisafisha na kuvaa kinga ile.

    Haya yalifanyika kichakani!!

    Ina maana sina mimba ama!! Alijiuliza Salome huku mapigo yake ya moyo yakienda kasi sana. Asingeweza kupata jibu palepale, akajiahidi kuwa akifika Mwanza kwa mwenyeji wake lazima aende hospitali.

    Akiongozana na yule mama waliporejea upande lilipokuwa basi lao walikuta basi jingine limekuja kwa ajili ya kuwachukua abiria baada ya lile jingine kushindikana kutengemaa.

    Utaratibu wa kuingia katika basi hili ambalo lilikuwa la kampuni nyingine sharti uonyeshe tiketi yako mlangoni ndipo unaruhusiwa kuingia.

    Salome akajiweka kando akingoja wenye tiketi zao waweze kuingia na mwisho yeye kwa usimamizi wa Joram aingie na kuketi popote ama kusimama kama basi limejaa.

    Si anasafiri bure!! Atafanyaje?

    Watu waliingia hadi mtu wa mwisho akaingia, Salome alizunguka huku na kule kutazama ni wapi Joram yupo. Hakumuona, akaanza kuulizia wahusika juu ya kijana aitwaye Joram.

    Ajabu! Hakuna hata mmoja aliyetambua jina hilo.

    “Ni mfanyakazi wenu lakini, na nilimuona akiwa hapa anashirikiana nanyi.” Salome alisisitiza lakini kila mmoja alikuwa na haraka.

    “Wewe leta tiketi huyo Joram sio tiketi dada…” alikaripia dereva huku akiungurumisha gari na kupiga honi mara kwa mara.

    “Nimesafiri nanyi kutoka Dar es salaam jamani, nilikuwa na Joram… nisaidieni tafadhali.”

    “Ulikuwa umekaa siti namba ngapi?” kijana mwingine mwenye daftari aliuliza huku akikagua namba kadhaa. Salome akabaki kutumbua macho tu kwa sababu hakuwa amekaa katika siti, bali kujibanabana tu hapa na pale.

    “Joram ndiye anajua….. sikuwa katika siti kaka yangu, lakini nimesafiri nanyi….” Alizidi kujitetea.

    “Duh… ningeweza kukusaidia dada yangu lakini basi letu huwa hatusimamishi abiria hata mmoja, yaani ni ‘level seat’……” wakati anamalizia kauli ile tayari basi lilianza kuondoka, akalirukia na kufunga mlango.

    Likatoweka kwa mbwembwe.



    JIFUNZE: Katika maisha ukijitazama wewe pekee bila kuutazama upande wa pili kila siku utajikuta kuwa mtu wa kulalamika tu na kuhisi unaonewa.

    Iwapo ukifanyiwa jambo tambua kuwa na wewe unaweza kumfanyia mwenzako kwa wakati mwingine. Jifunze kufikiri kabla ya kutenda, ukiiruhusu akili yako kuwa hivyo si kwamba utakuwa mkamilifu la! Bali utaziepusha shari nyingi.









    ****

    Basi lilitimua vumbi Salome asimini kama ni kwelia ameachwa katika safari ile.

    Joram alienda wapi sasa? Alijiuliza asipate jibu na hapo akapatwa na hisia za hatua za mtu nyuma yake. Akageuka na kukutana na sura ya kijana ambaye amechafuliwa na oili na vumbi.

    “Gari limekuacha sista?” aliuliza yule kijana, Salome akatikisa kichwa kuashiria kukubali.

    “Sijui hata nitafanya nini mimi…..” Salome alisema kwa sauti ya chini huku akichuchumaa.

    “Huna la kufanya zaidi ya kulala katika hilo gari bovu halafu kesho utajua la kufanya…” ilijibu ile sauti.

    “Nini? Yaani nilale katika gari…. Hapana kaka yangu, sidhani kama nitakuwa salama.”

    “Kama kulala hapa nje ni salama zaidi waweza kulala pia.” Alijibiwa kisha yule bwana alianza kuondoka, ndipo Salome akagundua kuwa yule mtu alikuwa muhimu kwake kwa muda ule.

    “Samahani kaka yangu.. ni kuchanganyikiwa huku, nisamehe maana sijui hata nimejibu nini….” Salome alimsihi huku akimfuata kwa nyuma. Kijana yule akasimama akiwa karibu na lile basi bovu.

    “Usijali, ingia ndani ya basi wenzangu wameenda kutafuta chakula watarejea baada ya muda.”

    Salome kwa kusuasua akapanda ndani ya lile basi. Akachukua nafasi katika kiti chenye uwezo wa kuchukua watu watatu. Kigiza kilishaanza kuingia na bado waliendelea kuwa wawili tu katika mazingira yale, mmoja akiwa chini na yeye akiwa ndani ya basi.

    Mapigo ya moyo yalikuwa yakiongeza kasi na wakati mwingine yakirejea katika hali ya kawaida. Salome kwa mara ya kwanza katika maisha yake alijikuta akikosa amani kwa kiwango cha juu kabisa na kuziona siku hizo mbili alizopitia kuwa ngumu kupindukia katika maisha yake.

    Dakika zilizidi kusogea na hatimaye likawa giza.

    Wasiwasi nao ukazidi kuwa rafiki yake.

    “Sista….” Sauti ikamkurupua kutoka katika mawazo akaruka kutoa kiti alichokuwa amekaa na kujisogeza pembeni kidogo kabla hajagundua kuwa ilikuwa sauti ya yule kijana asiyemjua jina.

    “Bee… naam!!...” akajiumauma akiwa haamini kuwa yu katika giza nene kama lile yeye na kijana asiyemjua jina.

    “Naona wenzangu wamechelewa hawa sijui nd’o wamepita kwenye vilabu vyao vya pombe huko maana hawa….” Alijibu yule kijana sasa alikuwa ndani ya basi akipiga hatua kuelekea alipokuwa yule dada.

    “Jikinge na baridi….” Kijana akamrushia shuka lililokuwa likitoa harufu kali. Bila shaka liliwahi kufuliwa zamani hizo na halikufuliwa tena.

    “Unaitwa nani ulisema….”

    “Sal…Salome…naitwa Salome…” alijibu kwa sauti iliyojaa uoga.

    “Salome juu ya kaburi lako naliaaa….ule wa Dully Sykes….” Alitania yule kijana. Salome akajilazimisha kutabasamu huku akiikumbuka siku anayomkubalia Kindo kuwa naye penzini, siku hiyo Kindo alimuimbia wimbo huo kuanzia mwanzo hadi mwisho.

    “Mara kwa mara huwa mnalala barabarani kama hivi..”

    “Hapana ni mara moja moja tu kama leo hivi…” alijibiwa.

    “Hamuogopi..”

    “Hata tukiogopa, je tuache kazi na kukaa nyumbani tukisubiri kazi isiyokuwa na changamoto. Salome, kila kitu katika maisha yetu kina changamoto, ukiona kila kitu kimekunyookea basi shtuka utajikuta ukiwa kitandani na kutambua kuwa ulikuwa katika ndoto…basi ili usiishi katika ndoto ni vyema kukabiliana na kila hali. Kama hivi…” alielezea kwa kirefu yule kijana na kisha akajitambulishga kuwa anaitwa Evans.

    Hatimaye mwanga wa ukaonekana na kukatisha mazungumzo yao. Uoga wa Salome ulikuwa umepungua.

    “Wamefika hao na matusi yao… nilijua tu walienda kulewa hao.” Evans alimweleza Salome huku akiinuka na kuelekea nje.

    Salome alibaki pale alipo kungojea nini kitatokea nini. Evans alichelewa kwa takribani nusu saa, na aliporejea alikuwa akiongozana na wenzake wawili. Harufu kali ya pombe za kienyeji ikatawala ndani ya basi.

    “Wanadamu watu wa ajabu sana….” Alisikika mmoja wa wale walevi kisha akaendelea, “yaani unaua wenzako ili upate mali, matajiri wanatafuta mali na sisi maskini hivi ni kitu gani tunatafuta sasa. Wanadamu hawatosheki kabisa……”

    “We Raja nawe umekariri….”

    “Hakuna cha kukariri hapa yaani hii ya leo inakuwa mara ya nne, kila huyu mzee akija kuchukua magari bandarini, basi linachinja tena barabara hii hii….”

    “Yaani kesho ikitokea tena nd’o ntaamini sasa…..” alijibu mlevi wa pili na kisha kimya kikatanda takribani dakika ishirini, kila mmoja akijaribu kuusaka usingizi. Salome na Evans wakila ‘chipsi’ na maji.

    Maneno waliyokuwa wakirushiana wale walevi yalimfikia Salome lakini hakuyatilia maanani sana. Akayapuuzia.

    Simu ya Evans ilikatisha mlo kwa muda kidogo, akajipekua na kupokea.

    “Nini?....acha weeee!!!..Bonta kuwa siriasi bwana….ehee….eheee…. Mungu wanguuu…”

    Salome naye alijikuta amesita kula akabaki kumtazama Evans aliyetaharuki.

    “Ni nini tena…” Salome aliuliza.

    “Ajali, basi limepinduka…”

    “Basi gani?” aliuliza kwa mshangao..

    “Salome mimi huwa siamini mambo ya ushirikina lakini kwa hili sasa naamini..” alisita kisha akaishusha sauti zaidi na kuwa katika mnong’ono, “Si uliwasikia hao jama walichokuwa wanabishana……yaani mwenye haya mabasi kila akija kuchukua mabasi mapya bandarini lazima basi lake moja ama hata lisipokuwa lake ilimradi limebeba abiria wake lazima lipate ajali na kuua watu…. Basi lililokuacha limeua watu Salome. Mungu wako mkubwa!!” alimaliza Vicent, Salome akatamani kuuliza kitu lakini hakujua ni kitu gani alipaswa kuuliza, hofu ilikuwa imemtawala. Yaani ameokoka kutoka katika ajali katika namna ile ya kustaajabisha.

    Ilishangaza!!!

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    ****

    SAA NANE kamili juu ya alama mishumaa iliwashwa na sasa kila mmoja aliuona uso wa mwenzake. Lakini hawakutazamana kwa muda mrefu kabla ya kuanza kunong’ona kila mmoja akimuuliza mwenzake imekuwa vipi hadi wapo eneo hilo ghafla kiasi hicho. Hakuna aliyekuwa na jibu lililonyooka.

    Ikatoka amri ya kuizima mishumaa, kwa pamoja ikazimwa halafu ikafuata amri ya kuwasha tena mishumaa.

    Sasa walikuwa wakitazamana na mshumaa mkubwa zaidi mbele yao.

    “Samahani nyote kwa usumbufu mlioupata ghafla kwa kuwakurupusha majumbani mwenu na kuwaita eneo hili. Lakini nadhani nyote mnajua kuwa hii ni kwa madhumuni yetu sote. Na kama ningewaacha mwendelee kulala basi mngenilaumu kwa nini sikuwaamsha.

    Basi namkaribisha katibu aweze kusema neno kwa ufupi kisha kila mmoja afanye tafakari.” Alimaliza na kumkabidhi rungu katibu ambaye pia sura yake ilizibwa katika mwanga mkubwa.

    “Salaam sana!!”

    “Salaam!!”

    “Kwa masikitiko na majonzi makubwa napenda kuwaeleza kuwa mkakati umeingia doa. Mkakati haujaweza kutimia. Ametutoroka tena bila kutarajia!!! Ametorokea mbali kabisa… na kama tulilala na kujipongeza kuwa tumemaliza basi si kweli ametutoroka na hatujui ni nani amemtorosha.” Aliweka kituo na kuacha wajumbe kumi na wawili waanze kunong’ona wao kwa wao.

    “Kwani bila yeye hatuwezi kuendesha mkakati wetu lakini.” Swali hili lilitoka kwa mjumbe mmoja.

    “Hapana hata kidogo, tunaweza kujipa moyo katika siku za awali lakini baadaye yatazuka mambo magumu sana na tutakuwa tumechelewa sana. Wakati huu…” katibu alijibu kisha akaendelea, “Kwa kifupi mkakati wa mjumbe wa tatu na wenyewe pia ni batili……kazi hii inahamishiwa kwa mjumbe wan ne Yakuza Wenje. Tunahitaji utendaji mapema sana. Na muwe na usiku mwema.” Alimaliza na kisha kila mmoja akazima mshumaa wake, giza likatanda.



    ****



    USIKU ulipita bila kuingiza chakula chochote kinywani, akili yake kwa kiasi kikubwa ilikuwa imevurugwa na watu wawili. Mama yake Salome na mzee Gaspar Nshomile aliyeleta jina la Rensho katika maisha yake.

    Kindo aliamka kivivu vivu akikumbuka kuwa mzee Gaspar na mama yake Salome wote waliahidi kurejea tena.

    Kindo aliutwaa mswaki wake akautia dawa na kutoka nje kusafisha kinywa. Redio yake ndogo ilitangaza habari za ajali mbaya ya gari yeye akiwa nje na hakusikia lolote lile.

    Aliporejea ndani akili yake iliwaza juu ya kula. Tumbo lilikuwa wazi sana, lakini kabla ya kula aliamua kukirekebisha kitanda chake kilichokuwa kimevunjika, zoezi lililomchukua takribani dakika kumi.

    Akiwa tayari kuondoka, anakutana na fadhaa.

    Mama yake Salome akiongozana na binamu yake salome, nyuso zao zikitangaza shari walikuwa wakijongea katika chumba chake. Kindo alitamani kuyakimbia makazi yake, lakini akakumbuka kwamba kuyakimbia makazi yake ni kuufanya uongo kuwa ukweli, Kindo hakutaka kujiharibia zaidi ilikuwa ni heri kupambana kuliko kukimbia.

    “Karibuni, mama shkamoo!!”

    Badala ya kujibu mama Salome alimkazia macho yaliyotangaza chuki.

    “Mama, hebu….. Kindo habari” binamu yake Salome alimsalimia Kindo.

    “Njema shem!!”

    “Kindo, ni kitu gani kimetokea hadi ukafikia hatua hiyo..”

    “Joyce, hakuna kumuuliza uliza huyu….. mwambie kilichotuleta.” Mama mtu aliingilia kati.

    “Nisikilize shem walau kidogo tu nijieleze maana mama hakunipa nafasi ya kujieleza…”

    “Joyce…Joy…usitake kunipandisha hasira zangu tena dakika hii…..hiyo iwe kauli yangu ya mwisho kabla hujabadili mazungumzo hayo na kueleza kilichotuleta…” aling’aka mama Salome. Joyce binamu yake Salome akatii amri.

    “Kindo, mguu wetu huu ni kituo cha polisi, tunaenda kutoa taarifa juu ya kupotea kwa Salome ambaye mara ya mwisho alikuwa kwako. Sijui utajibu nini lakini hiyo ni taarifa tumekuletea. Lakini huna haja ya kuwa na wasiwasi, wakikusumbua sana Rensho na baba yake watakuja kukutoa” Joyce alimaliza kujieleza, mama Salome akamvuta mkono wakaendelea na safari yao.

    Kindo akaisahau njaa aliyokuwanayo, mambo yalikuwa yamezidi kuwa magumu. Neno polisi lilikuwa limemchanganya zaidi Kindo, hakuwahi kuingia katika kosa lolote lililomsukumia katika mkondo huo katika maisha yake yote, sasa anaziona dalili zote za kuingia matatani.

    “Salome rudi nyumbani mpenzi wangu!!!” Kindo alizungumza peke yake huku akijikunakuna hapa na pale pasi na sababu ya msingi.

    Kindo hakutamani tena kuwa karibu na eneo lile akakusudia kutafuta mahali ambapo atayatua mawazo haya.

    Upesi kama anayehofia kupokea ugeni mwingine wa mashaka alifunga mlango wake. Na huku akikimbia akafuata njia ambayo huipita mara moja moja sana. Alianza kwa kutembea upesi upesi, kisha akawa anakimbia kidogokidogo hatimaye mbio zikaongezeka akawa anakimbia kabisa kama anayefukuzwa.

    Alikimbia bila kukoma hadi akakifikia kibanda kimoja akaingia kwa pupa huku akiita jina la ‘mama’.

    “Una nini wewe mtoto, mbona umekuja kwa kasi hivyo. Amekwambiaje huyo mdogo wako kwani.”

    “Nd’o nafika muda huu mama, sijaonana naye.”

    “He! Yeye nd’o nimemuagiza akufuate kwako, hamjazungumza!!” mama aliduwaa.

    Kindo akamweleza kuwa hajafuatwa na mtu bali amejileta mwenyewe hapo kwa mama yake.

    “Hebu pumua kidogo halafu unidanganye sasa ili nishawishike na hii kadi.”

    “Kadi gani mama?”

    “Kwani kadi ulizosambaza wewe huzisomi ama tumepewa za aiana tofautitofauti.” Alisema mama yake na Kindo huku akiendelea kusuka ukili.

    “Mama ujue sikuelewi, kadi.. kadi gani mimi sijatoa kadi.” Alilalamika Kindo huku akijifuta jasho.

    “Hii kadi sio wewe unayetaka kumuoa huyu Rebeca wa Nshomile wewe….. ama kutokwenda kwangu shule unadhani hata majina sijui kusoma. Mtazame aibu zimekushika umeshindwa kuileta mwenyewe unaagiza watu, Salome wa watu amekuvumilia weee!! Msichana wa watu yule mchapakazi kweli. Unakurupuka kwenda kwa huyu Re nani nani sijui…. Watoto wa kisasa bwana…” mama yake Kindo alilalama katika namna ya kumlaumu mwanaye.

    Kindo akashusha pumzi kwa nguvu.

    Alikuwa amechoka!!





    “Kindo mwanangu yaani umeniaibisha ila basi tu… yaani kati ya watoto wangu ambao sikutarajia watanitia aibu basi ni wewe lakini kumbe nilikuwa najidanganya tu. Wewe na baba yako mmefanana akili kabisa….”

    “Mamaaaa…mama!! Unafika mbali mama, ni nani ameleta habari hizo za uzushi uliokithiri, ni nani mama….mimi sijaagiza mtu yeyote kwako na sielewi unaloniambia.” Kindo aligutuka na kumkatisha mama yake.

    Na hapo ghafla akashtukia amenaswa kibao. Akajutia kumsahau mama yake alivyokuwa na mikono myepesi anapokasirishwa na jambo.

    “Pumbavu wewe, unadhani Salome ni muongo kama wewe, unadhani mama yake Salome naye ni mjinga eeh. Hujamfukuza Salome usikuusiku na matusi juu mbwa wewe. Mama yake Salome ametusaidia mambo mangapi, si ningekuwa nimekufa mimi kama asingenipunguzia damu… Kindo mwanangu pesa sio kila kitu katika maisha, pesa ni makaratasi tu zinatafutwa zinapatikana na zinapita. Utu wa mtu hausahauliki kamwe, umemkosea sana heshima mama Salome kwa ulichomfanyia mwanaye. Sio kumkosea mama Salome tu, hata Mungu umemkosea sana Kindo, hivi ndivyo nilivyokufundisha mimi eeh…. Sasa naomba nisimalize kuhesabu hadi tano, uwe umetoweka mbele ya macho yangu.. nadhani nikisema hivyo unajua namaanisha nini.. moja, mbili..” Kindo alimtambua mama yake vyema, si yeye tu hata mtaa ulimtambua mama huyu kwa jinsi alivyokuwa akizitendea haki hasira zake kwa kupigana ama kupiga mtu. Kindo aliijua vyema shughuli hii, na kwa sababu hakutaka kuadhirika akaamua kutimua mbio kama alivyoamriwa ili aweze kurejea tena baadaye mama huyu akiwa ametuliza mzuka wake.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Wakati Michael anatimua mbio kuna mtu alimtazama kisha akafanya tabasamu kisha akanyanyua simu yake na kubofya namba kadhaa na kisha kuzungumza maneno machache tu kuelekea upande wa pili.

    “Kimenuka kwa mama yake!!” kisha akakata simu. Akamtazama tena Kindo alivyokuwa amehamanika.



    ______



    MAPAMBAZUKO yaliivamia anga na kuliondosha giza, Salome akawa wa kwanza kuiona nuru, akayapikicha macho yake na kutazama kushoto na kulia. Akamuona Evans akiwa hoi usingizini akakohoa kuweka koo lake sawa Evans akayafunua macho yake.

    “Mhh!! Asubu…..aah kumekucha..” alijing’atang’ata huku na yeye akiyapikicha macho yake kujiweka sawa.

    Wakapeana salamu, kisha Evans akasimama na kupekua sehemu ya kuhifadhia mizigo.

    “Kaoshe uso dada Salome..” alimweleza huku akimkabidhi kopo la maji. Salome akapokea na kutoka nje.

    Wale walevi wa usiku nao walikuwa wameamka tayari. Wakistaajabu kuwa Salome alilala katika basi moja na wao wasijue, utani wa hapa na pale ukazuka na kisha kupotea baada ya mafundi wakiwa na spea kutoka mjini kuingia pale kulishughulikia basi.



    “Salome sasa hili basi linarudi Dar… itakuwaje kuhusu safari yako wewe.” Evans alimvuta kando Salome na kuzungumza naye.

    “Kitu ambacho naweza kukushauri ni kimoja tu… turejee wote Dar, kwa sababu umesema huna nauli. Tukifika Dar basi mimi nitakufanyia mpango pale staendi ili upate nafasi katika mabasi ambayo kuna rafiki zangu wanahusika nayo….. unaonaje wewe huo utaratibu maana hapa barabarani kupata gari la bure dah sikufichi dadangu itakuwa ngumu na hawa jamaa hawawezi kunisubiri mimi nikupandishe gar indo tuondoke” alieleza kwa ufasaha Evans na Salome akabaki kuwa mwamuzi wa mwisho.

    Hana pesa, hana simu ili ajaribu kufanya mawasiliano na mtu yeyote. Kitu pekee alichokuwanacho ni Evans…..

    “Ulichosema ni sahihi Evans kaka’ngu, lakini huko Dar penyewe ni uhakika wa kufika na kupata gari, na kama si uhakika, mimi nitaishi wapi sasa. Maana…ni stori ndefu sana kuhusu Dar lakini amini kuwa sina mahali sahihi pa kufikia.”

    “Usijali, usijali kuhusu pa kufikia na kuhusu kupata gari hilo la bure hakika tunatakiwa kuvuta subira siku mbili tatu…si unajua cha mtu eeh…”

    “Nimekuelewa sana bro…”

    “Twend’zetu sasa..” alimalizia Evans huku akielekea kwenye basi.

    Safari ya kurejea jijini Dar es salaam!!

    Salome akiwa msichana pekee ndani ya basi lile.



    _______



    “Ndo wenyewe”

    “Sio hao bwana…”

    “Ndio wenyewe aisee….”

    Sauti mbili zilikuwa zikipingana huku zikitilia umakini muungurumo wa gari lililosikika kutokea mbali. Lakini licha ya kupingana hakuna hata mmoja aliyesahau wajibu wake. Umakini ulikuwa wa hali ya juu!!

    Mtego ukanasa!!

    Walikuwa wenyewe waliokuwa wakiwangoja. Upesi gogo kubwa likarushwa barabarani likifuatia na jingine.

    Gari ile ilipofika ikafunga breki za ghafla, na huo ukawa mwisho wa safari ile.

    Mtutu wa bunduki ukalitazama basi lile na kisha amri ya upesi ikatolewa kuwa abiria wote watelemke kutoka katika basi hilo.

    Bunduki haiongopi na haina mjanja!!

    Salome akawa wa kwanza kutelemka huku akitoa kilio cha woga na kitetemeshi cha taharuki.

    Macho yalikuwa yamemtoka pima, nyuma yake alifuata Evans na wenzake.

    Walikuwa wametekwa!!

    Mteka nyara mmoja akasogea kando akaitoa simu yake na kubofya namba kadhaa kisha akasikiliza upande wa pili.

    “T 670 AJZ…..Ok ndo wenyewe….. binti mmoja…..sawa sawa bosi” alimaliza na kurejea kundini. Bila kupoteza muda jumla ya watu watano wakaamuliwa kulala chini, wakatii amri. Kishja kama kipanga anyakuapo vifaranga, mtekaji mmoja mwenye mwili mkubwa akamnyakua abiria mmoja akamziba macho na mdomo na kuanza kutimua naye mbio.

    Abiria waliosalia wakawekewa tego kana kwamba bado wapo chini ya ulinzi, wakabweteka na kuendelea kulala chini bila kujitikisa.

    Walikuja kuteguliwa na raia wengine baadaye kabisa.

    Evans akawa wa kwanza kubaini kuwa Salome hakuwa pamoja nao.

    Salome alikuwa kusudio la watekaji wale.

    “Maskini wee!! Salome weee.. hakuniambia hata kisa chake cha kumkimbiza Dar.. Mungu wangu wee…” aliugulia Evans asieleweke hata kwa mtu mmoja.

    Kila mmoja akaujali uhai wake.

    Hakuna aliyekubali kuendelea kuwa porini kule kwa ajili ya kumsaka msichana wasiyemjua. Kwa shingo upande Evans akaungana nao. Wakatoweka.

    Salome hakujulikana yu wapi tena!!



    ______

    “WELLDONE BOYS!!” Sauti nzito kutoka kwa pande la mtu ilisifia huku akiwagongagonga migongo yao vijana wanne waliokuwa mbele yake.

    “Yaani mmefanya kwa uhakika na kwa muda muafaka!! Nimependa sana.” Alizidi kuwatukuza vijana wake.

    “Lazima watambue mimi ni nani…..” alihamia upande wake na kujisifia. Kisha akanyanyua simu yake ya kiganjani akapiga mahali.

    “Naam!! Yakuza Wenje naongea….Nimeimaliza kazi yako mkuu… sasa tunaweza kuendelea…” Alisema na upande wa pili huku akijisikia fahari sana kwa maneno yaliyokuwa yakimtoka.

    “Don, jioni uje peke yako nikukabidhi halali yenu.” Alimaliza na kuwaaga wale vijana. Tabasamu halikukauka katima uso wake wenye furaha.



    Baada ya Don na wenzake kuondoka. Yakuza alicheka kwa sauti ya juu, alicheka hadi machozi yakamtoka.

    “Watanikoma mwaka huu wajingawajinga wa Sinza Lego…. Yaani lazima wanijue Yakuza kama nimerejea tena kushika usukuni, pumbavu zao. Walidhani nd’o nimeanguka moja kwa moja…..sasa narejea kwa kishindo..” alisema haya kama anayeapiza kwa sauti ya juu. Kisha akajimiminia waini katika glasi na kuimimina kwa mipigo miwili mdomoni, glasi ikawa tupu.



    Yakuza aliitazama saa yake na kuona kama muda hausogei mbele hata kidogo, alikuwa na kiherehere cha kupata alichokitaka baada ya kazi iliyoonekana ngumu halafu yeye akaifanya nyepesi.

    Yalikuwa majira ya saa nane mchana Yakuza alitakiwa kungoja hadi majira ya saa mbili usiku ili aweze kupata uhakika wa ahadi aliyopewa yeye na wenzake iweze kutimia.

    “Mwenyekiti na katibu lazima washangae, nimeweza vipi kufanya upesi kiasi kile.” Aliwaza huku akijitafutia mahali pa kwenda kupoteza muda ili muda wa ahadi ufike.

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    ________



    “Kindoo!!” sauti kali ilimuita kwa mbali, akageuka huku akiwa bado anakimbia. Mtu aliyekuwa anamuita na yeye alikuwa anakimbia. Kindo akapatwa na uoga huenda mtu yule ameagizwa na mama yake aweze kumkamata na kumrudisha nyumbani kitu ambacho Kindo hakuwa tayari. Akalazimika kuendelea kukimbia zaidi na zaidi, lakini yule aliyekuwa anamfukuza alikuwa anakimbia zaidi yake, kadri Kindo alivyoenda mbili ndivyo yeye alivyozidi kumrudisha nyuma katika namna ya kumkaribia zaidi.

    Hatimaye Kindo akasalimu amri, akaamua kutumia mpango mwingine wa kumdhibiti yule bwana. Akaokota jiwe kubwa huku akiwa anahema juu juu.

    “Uki….ukiniso….ukinisogelea nakupasua jiwe…nakupa…” Kindo akiwa anahema alimchimba mkwara yule bwana ambaye walikuwa wakifahamiana lakini hakuwa mtu wake wa karibu kiasi kile.

    “Kindo la!! Ni kitu gani tena kimekusibu unataka kuniponda mawe mimi….Kindo..” alitahamaki yule bwana.

    “Nani amekutuma unikimbize…..nani?” alihoji Kindo akiwa bado amekamata jiwee mkononi.

    “Kindo..sijaagizwa na mtu ujue lakini hii ni kwa usalama wako.”

    “Usalama wangu naujua mwenyewe, nyie watu mbona mnanifuatafuata sana…. Kwanini, si mniache lakini….” Alilalama Kindo, yule bwana akamsogelea na kumfiukia, akaushusha ule mkono wake ulioshika jiwe. Kindo akakubali kuliachia jiwe.

    “Kindo, ni kitu gani kimefanya mpaka utafutwe eeeh!! Mimi ni jiranmi yako, sawa tuliwahi kugombana lakini bado wewe ni jirani yangu. Ugomvi wa kuwania kukinga maji bombani hauwezi kuvunja ujirani, ni kitu gani umekosa Kindo hadi utafutwe…”

    “Nani ananitafuta, mimi sitafutwi na mtu..” alipinga Kindo.

    “Kindo! Difenda imeshuka na kuvamia chumba chako, maaskari wenye sare kabisa wamevamia kwako na sasa unasema hautafutwi, watu wamekuja na picha yako unakataa hawakutafuti wewe….Kindo unachanganyikiwa mdogo wangu. Sikia Kindo kama lipo ulilofanya na sistahili kuambiwa basi mimi nimekupa tu hii taarifa. Kazi ni kwako kusuka ama kunyoa….” Alimaliza kwa kauli hiyo na kisha akaanza kuondoka akimwacha Kindo akiwa anatetemeka.

    “Dula!! Dula…. Nani wananitafuta mimi… dulla wame…” akasita kuzunmgumza baada ya kugundua kuwa Dulla hamsikilizi tena na tayari yupo mbali…..

    Kindo akaketi chini na kuanza kulia.

    Kilio cha mtu mzima!!!!

    Hajui kosa lake lakini anasakamwa kila upande!!!







    Kutokwa machozi? Hii haikuwa namna ya kupata suluhu ya tatizo lilokuwa linamkabili. Kindo alisimama tena na kutazama pande kuu nne za dunia kana kwamba zote zimewekwa miba na hawezi kuvuka hatua moja mbele.

    Alifikiria kusonga mbele, lakini kile kitisho kutoka kwa jirani yake kuwa anasakwa na polisi wenye hasira kilimfanya asifikirie hata kidogo kwenda nyumbani kwake.

    Mama yake mzazi alikuwa amecharuka haswa na asingeweza kukabiliana naye kwa wakati huo.

    Akawakumbuka marafiki zake watatu, ambaye alikuwa jirani zaidi alikuwa ni Maulidi. Kindo akaamua kuchagua eneo hilo kama sahihi zaidi kwa wakati huo.

    Kwa mwendo wa kiaskari alikamata njia moja kwa moja kwenda nyumbani kwao Maulid.

    Mwendo wa dakika kumi na tano alikuwa ameikaribia nyumba ambayo Maulid alikuwa akiishi humo, kufikia hapo alipunguza mwendo huku akiuongoza uso wake usiwe katika uoga aliokuwanao.

    Chumba kimoja cha Maulid kilikuwa wazi, kwa jinsi walivyozoeana Kindo hakuona ajabu kuingia bila kubisha hodi.

    Akamkuta Maulid kitandani akiwa ameuchapa usingizi.

    Kindo akamtikisa kidogo Mau akashtuka.

    “Yalaweeeee!! Yalabi…..” akataharuki huku akiuegemea ukuta kwa mgongo, mikono yake ikimsihi Kindo asimfanyie jambo baya lolote lile kama alikuwa na nia hiyo. Kindo alistaajabu na yeye akaganda vilevile asipige hatua yoyote mbele.

    “Mau…. Umekuwaje wewe…. Mimi nakuja hapa na matatizo yangu na wewe unaanza kupiga makelele tena, kulikoni!!” alihoji Kindo, sasa alipiga hatua mbele na kutaka kuketi kitandani.

    “Weeeee!! Kindo Kindo…. Naomba usiguse kitanda changu nakuomba tafadhali shehe!!” alitoa onyo Mau kisha akaendelea, “Kindo kama wewe ni mzaliwa wa Iringa ukafungwa hirizi za huko basi mimi nitakusulubu kizanziberi yahe… niache Kindo…”

    Macho yakamtoka Kindo baada ya kusikia maneno hayo mapya kabisa.

    “Mau… Mau ujue nina matatizo acha utani wako…” wakati anamalizia kauli hii huku akijilazimisha kutabasamu kama kwamba hajakerwa na lolote Mau alichomoa sime kutoka chini ya godoro lake na kulishikilia kikakamavu.

    “Upige hatua moja mbele niichomoe hiyo shingo yako mara moja!! Upige hatua moja nyuma nisambaratishie mbali huo uti wako wa mgongo mwanga mkubwa weye!!” alibwata Maulid, macho yake akiwa ameyakodoa kumwelekea Kindo. Hakuonyesha dalili hata chembe ya utani, alikuwa anamaanisha anachoamuru.

    Kindo akafadhaika na kubaki akiwa ameachana midomo yake kwa mshangao.

    “Bwan’Kindo sie twakuamini rafikizo, kwamba twapambana pamoja kumbe mwenzetu mwanga mkubwa wewe. Waizuia riziki isikae nasi bali ikufuate weye. Watuongopea Salome mpumbavu kumbe umemtoa kafara mwanaharamu wewe mpenda utajiri, sasa umekuja kunitoa na mimi kafara nasema Kindo hapa umegonga mwamba na iwapo utatoka hai ndani ya nyumba hii basi nisikuone tena mbele ya macho yangu tena na usikumbuke kama mimi Mau nimewahi kuwa rafiki yako walah… na nikikumbwa na madhara yoyote yale Kindo, walah nakutafuta popote ulipo nakuua. Sasa kabla John na Masalu hawajaja kukuulia hapakutokana na ushirikina wako uliokubuhu naomba utoweke mara moja hapa ndani, toweka mshirikina wewe!!” alitoa karipio kali huku jasho likimtoka na mikono ikimtetemeka. Kindo hakuweza kutabasamu tena, akajikaza na kuomba huruma ya Maulid, “Mau rafiki yangu nakuomba tafadhali nisikilize japo…” akiwa hajaimaliza kauli yake Maulid akamkatisha, “Nitaitenganisha shingo yako sasa hivi walah!!” na hapo akaanza kuiburuza panga sakafuni kama anayejaribu kuitia makali zaidi.

    Kindo hakungoja kushuhudia kifo chake. Upesi akaanza kutimua mbio, akijigonga katika ndoo iliyokuwa na maji, akayumba akajikwaa kwenye beseni tupu lililokuwa nje. Kisha akauona uelekeo na kuendelea kukimbia akiwa na hofu kuu juu ya hali inayomkabili.

    Macho yalimchonyota na machozi yakamtoka. Machozi ya uchungu na uoga. Machozi yaliyoziba macho yake asiweze kuliona bonde lililokuwa mbele yake, akaliingia bonde lile na kupiga mweleka chini.

    Kiza kikatanda machoni!!



    ****



    MUZIKI uliwaburudisha wateja wa rika mbalimbali walioamua kuimaliza siku yao katika baa hiyo maarufu sana pembezoni kidogo mwa jiji. Wateja ambao walishaanza kulewa waliinuka na chupa zao mikononi na kuanza kukata mauno huku wakijaribu kwenda sawa na ala za muziki huo.

    “Dennis hivi huwa unapapendea nini hapa?” kijana mmoja alimuuliza mwenzake.

    “Kwani tangu ufike hapa umeboreka, ukimaliza bia moja basi anakuja muhudumu mrembo anakuhudumia, ukianza kunywa mara mlevi mwingine anakata mauno halafu usiku sasa yale mambo yetu.. wanawake na kanga moja iliyolowanishwa maji wanajiweka pale kati, yaani hata kama unajifanya we mlokole vipi kwa wale yale mambo lazima utamani!!!” alijibu Deniss huku akifurahia kila neno analosema.

    “Halafu ukishatamani…”CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Ukishatamani basi pesa yako inazungumza tu… bei zao za kawaida sana!!”

    “Yaani unanunua wanawake tena!!”

    “Yah! Ulidhani watakupa bure tamu yao….” Deniss alijibu huku akimshangaa rafiki yake.

    “Yaani we jamaa kwa wanawake nd’o maana huwa mnagombana na Sam kila siku….”

    “Sikia Don, yule Sam yule atakuwa na matatizo yule si bure atakuwa hanithi..” Deniss akatoa kauli iliyowafanya wacheke kwa pamoja.

    Kicheko walichotoa kilikuwa kicheko cha pesa, naam! Pesa nyingi kwa kazi ndogo kabisa. Na Don alikuwa akihesabu masaa ili aweze kukutana na mzee Yakuza waweze kumalizana.

    Baada ya dakika kadhaa Don aliaga kuwa anaenda msalani. Aliondoka kwa mwendo wa kuyumbayumba huku akipiga mluzi. Deniss akamsindikiza kwa macho nyang’anyi mwenzake hadi alipotokomea.

    “Yaani Don bwana….” Akatokwa na kauli ile kisha akatikisa kichwa kushoto na kulia akaendelea kunywa pombea yake.

    Baada ya dakika kumi na tano Don akarejea, lakini safari hii hakuwa kama alivyoondoka alikuwa amejawa wasiwasi na akili yake haikuwa na nutulivu kabisa jambo ambalo Deniss aliling’amua mapema kabisa.

    “Don! Vipi kaka!!”

    “Aaamh!! Hapana, hakuna kitu….”

    “Hakuna kitu wakati unaonyesha wasiwasi kabisa usoni.”

    “Nimesema hakuna kitu Denny vipi mbona hivyo.” Sasa alijibu kwa jazba.

    “Ushakasirika mtoto wa mama wewe ninaenda msalani akija muhudumu mwambia aongezea bia hapo…” Deniss hakujali jazba za Don, akaaga na kuondoka. Kabla hajafika msalani akambana muhudumu mmoja kwenye kona. Don hakuwa na muda wa kumtafakari Denny maana kuna jambo lilikuwa linapita katika kichwa chake lililoondoka na utulivu wote.

    Dakika kumi baadaye Deniss machachari naye akarejea akiwa ametaharuki zaidi ya Don!! Yeye hakuweza kuhimili wasiwasi wake. Ikaja zamu ya Don kumuuliza mwenzake kulikoni!

    “Don, nimekojoa damu kaka…. Damu nyingi Do…Don nini hiki eeh!!”

    “Whaaat!! Damu?” alishangaa Don

    “Sio damu Don, damu nyingi sana..nimechafua choo huko…halafu nimebanwa tena Don… nini hiki eeeh!!” akiwa amepagawa waziwazi Denis alihoji. Don hakuwa na la kusema akabaki kumtazama Don anavyoropoka kwa sauti yenye kitetemeshi.

    “Denny, tuondoke hapa.. maana usivyojua kuishusha sauti yako basi kila mmoja atajua unakojoa damu…” Don akazungumza huku akisimama, Denny akafuata nyuma. Wakakodi taksi iwapeleke Ilala boma. Nyumbani kwa Don.

    Walipoingia ndani sebuleni kwa Don, Don akafanya jambo lililomuacha Denny mdomo wazi.

    Akaifungua zipu yake upesi upesi akashusha suruali yake chini.

    Denny akatazamana na tupu ya Don iliyotapakaa damu!!

    Na yeye bila kujua nini anafanya akaangusha suruali yake.

    Wote walikuwa wanavuja damu. Lakini kwa Denny kulikuwa na la ziada, damu yake ilichanganyika na usaha!!

    Hakuna aliyeweza kusema neno lolote. Kila mmoja alikuwa anatetemeka!!

    “Denny….nini hiki sasa!!”

    “Damu hiyo Don ama unaona nini wewe!!” alijibu kwa dhihaka huku akizidi kujishangaa.

    Simu ya mkononi ya Don iliita lakini hakunyanyua mkono wake kuipokea, kisha ikaanza kuita simu ya Deniss na yeye alisonya tu bila kufanya jitihada zozote zile za kuipokea!!

    Hali walizokuwanazo zilisikitisha.



    WAKATI Don na Deniss wakihaha juu ya tatizo lililowatokea ghafla. Mwenzao aitwaye Samson ama walivyomzoea kwa jina la Sam alikuwa katika dimbwi loa mawazo akifikiria juu ya jicho la mwanadada likimwaga machozi huku likimsihi msaada. Hakuwahi kulitambua jina lake lakini sura ilikaa vyema katika kichwa chake.

    Kufikia wakati huo alikuwa amebwia chupa kadhaa za ulabu akiwa nyumbani kwake lakini hali ile iliendelea kumweka katika wakati mgumu.

    Aliwahi kushuhudia maiti na amewahi kuua kikatili sana mara kadhaa na akasahau mara moja. Ajabu safari hii ambayo hakuua mtu anastaajabu sura ya mlengwa inasafiri katika kichwa chake kwa kasi ya ajabu.

    Yule ana nini lakini? Eeh yule msichana ni nani kwani? Samson aliiuliza chgupa yake ya bia lakini haikumjibu lolote.

    Akaamua kuinyayua simu yake ili awaulize wenzake kama wanakumbwa na hali hii.

    Akaanza kumpigia Don, simu ikaita kwa muda mrefu bila kupokelewa. Akapiga kite cha ghadhabu kisha akapandisha juu kidogo akakutana na namba ya Deniss na yenyewe ikaita bila kupokelewa.

    “Mabwege wamelewa hadi wamezima kabisa…shenzi kabisa!!” akajipatia majibu yake juu ya wenzake ambao bila yeye kujua kama waliziona simu zake zikiita wakashindwa kupokea.



    “We binti ni nani nakuuliza si unijibu, kama hauna jibu na utoke katika akili yangu. We unadhani ningeweza kukusaidia katika eneo lile, hukuona kama wenzangu walikuwa na bunduki, wangeniua wale ohoo!!” Sam aliendelea kuzungumza peke yake huku akiwa amefumba macho yake akijenga taswira ya binti huyo.

    “Sikia binti ujue unanikosea sana kuendelea kuniandama mimi niliwazuia na wewe ulikuwa shuhuda kabisa. Ningefanya nini sasa baada ya pale eeh niambie sio kukaa unaniandama mimi tu hapa. Ningewakaba mashati ili wanipige risasi eeh ndo ulitaka nife siyo … nakuuliza wewe nijibu….aaaargh!!” hatimaye alipiga kelele na kufumbua macho yake. Hakika alikuwa anaathiriwa na kitu alichokuwa anakiona kichwani mwake.

    Alisimama akatembea kwenda mbele na kurudi nyuma akiwa na bia yake mkononi akiibugia kwa fujo.

    “Hata hivyo unatakiwa kujua kuwa nilikuwa kazini binti sawa eeh!! Nilikuwa nasaka pesa…” alimalizia kwa kauli hii sauti ikiwa chini kabisa kama anayemnong’oneza mtu. Bia ikiwa kando na mikono yote miwili ikikisugua kichwa chake na kukibinyabinya.

    Hatimaye akapitiwa usingizi akiwa palepale katika kochi na mikono yake ikikipakata kichwa chake.

    Alikuja kustuka baadaye akiusikia mlango wake unagongwa kwa nguvu sana. Akapiga mwayo mkubwa huku akisimama na hapo akili yake ikawakumbuka akina Don na Deniss juu ya ahadi ya kugawania pesa yao nyumbani kwake. Akafanya tabasamu dogo kisha akajongea mlangoni.

    Akaufungua mlango pasi na kuitazama saa iliyoonyesha kuwa ilikuwa imetimia saa nane na dakika kadhaa usiku. Yeye alidhani kuwa ni saa mbili bado na ikizidi sana saa tatu.

    Alipotoa komea mara mlango ukasukumwa ndani kwa nguvu, akajirusha kando akiamini ni vurugu za rafiki zake baada ya kupata pesa.

    Lakini macho yakashuhudia kitu tofauti. Kiumbe kisichotambulika sura yake kikivuja damu katika kichwa chake, mikononi na uso usionekana walau kidogo kiliangukia magoti, kisha huku kikikoroma kikatokwa na maneno machache sana.

    “Mmeniu….uua…”CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Kisha mdomo ukatangulia ardhini, na mwili wote ukafuata kwa kishindo. Kiumbe kile kikahema kwa nguvu mara moja kisha kikatulia tuli!!

    Sam akatokwa na yowe la uoga, na alipoitazama saa yake akaingiwa uoga zaidi.

    Ilikuwa saa nane usiku!!!



    **NINI KIMEWATOKEA DON na DENISS

    **KINDO amekataliwa na rafiki zake…. Atakimbilia wapi na ni nani anayezua haya



    ITAENDELEA



0 comments:

Post a Comment

Blog