IMEANDIKWA NA : IGNAS MKINDI
*********************************************************************************
Sehemu Ya Kwanza (1)
.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“SIJAMUUA Adrian Zayumba lakini siwezi kuwa mnafiki kusema kuwa nimehuzunishwa na kifo chake, kusema kweli kuuawa kwake ni jambo lililonifurahisha mno” alijibu Alice Kwigema akiwaangalia maaskari watatu, wawili wa kiume na mmoja wa kike waliokuwa wamemsimamia mbele.
“Unaweza kutuambia ni nani aliyemuua?” aliuliza askari mmojawapo.
“Ningemjua ningeshampa zawadi yake, kama ni mwanamme hata penzi ningempa tena usiku kucha, mchana kutwa” alisema Alice akirembua jicho lake kuonyesha kuwa hakuwa na wasiwasi na kile alichokisema.
Kauli hiyo ilimfanya askari mmojawapo ambaye ndiye alikuwa kiongozi wa mahojiano hayo kuanza kumwangalia Alice kama anayemkagua uzuri wake kisha akameza funda kubwa la mate.
Alice, msichana mrembo aliyevalia kifulana na kipensi kidogo laini vya maua maua juu yake akiwa amejifunga mtandio mwepesi huku nywele zake ndefu kiasi akiwa kaziachia alionekana akiwa ametulia kwenye kiti katika chumba cha mahojiano.
Ukimya ulikuwa umetawala kwa sekunde kadhaa kisha ghafla yule askari wa kike akamchapa kofi kali sana Alice kiasi cha kutoa ukelele halafu akakikusanya kifulana chake kilichoacha sehemu kubwa ya mwili wake wazi na kumvutia Alice karibu na uso wake, wakawa wanatazamana huku nyuso zao zikiwa zimekaribiana sana akaanza kumwambia kwa msisitizo…
“Umalaya wako huko huko, hapa tunataka majibu ya uhakika kutokana na kila tunachokuuliza” kisha akamuachia Alice akidondokea kwenye kiti huku akijishika shika shavu kuugulia maumivu.
“Narudia tena kukuuliza, unamjua aliyemuua Adrian Zayumba?” aliuliza yule askari wa kike kwa ukali huku akimwangalia Alice kwa jicho la chuki.
“Utanipiga utaniumiza bure dada, mimi sijui chochote ila kama unataka maoni yangu kuhusu kifo cha huyo mtu, narudia tena kusema kwamba nimefurahi mno na Mungu atanisamehe kwa hilo” Alice alijibu kwa sauti ndogo akiugulia maumivu.
Yule askari wa kike aliyeonekana kujawa na jazba akamvamia tena na kumkaba kwa nguvu. Wale askari wengine wawili wakamvamia askari mwenzao kumzuia asije akamdhuru Alice.
Kitendo cha wale askari wa kiume kutaka kumnasua askari wa kike kilizua purukushani kiasi cha askari waliokuwa nje ya chumba cha mahojiano kuingia ndani kwa kasi.
Baada ya dakika kadhaa walifanikiwa kuwaachanisha huku yule askari wa kike akihemea juu juu kwa hasira wakati huo Alice alikuwa ameshavurugwa vya kutosha.
“Huo uzuri wako peleka huko huko, hapa hatumaindi urembo” maneno yaliendelea kumtoka yule askari wa kike mwenye sura ya kiume na umbile la kukomaa.
“Koplo, tatizo ni uzuri wake au tunafanya mahojiano tupate mambo yatakayotusaidia katika upelelezi?” aliuliza yule askari aliyemmezea mate Alice.
“Na wewe asiyekujua kama mgonjwa wa wanawake ni nani?” aliongea yule askari wa kike kwa hasira huku akitolewa katika chumba cha mahojiano na kusababisha kicheko cha chini chini kwa maaskari waliobakia.
“Askari kaa sawa!” alisema kwa sauti kubwa yule askari aliyeshutumiwa kuwa ni mgonjwa kwa warembo, wote wakasimama kwa ukakamavu. Akaingia mzee mmoja mrefu, mweusi anayeonekana mkakamavu akiwa amevaa Kaunda suti, ACP Maswe.
“Kuna nini Inspekta Ndilana?” aliuliza ACP Maswe
“Hakuna tatizo afande, tulikuwa tunafanya mahojiano na mtuhumiwa katika kesi ya mauaji ya Adrian Zayumba, bi Alice Kwigema” alijibu yule askari aliyemmezea mate Alice anayejulikana kama Inspekta Ndilana.
Afande Maswe aliangaza huku na kule akiwa kama anawakagua askari mmoja baada ya mwingine kisha macho yake yakatua kwa Alice aliyeonekana kuvurugika. Afande Maswe akamwangalia kwa muda kisha akaamuru Alice arudishwe rumande hadi kesho yake asubuhi apelekwe ofisini kwake. Kisha akamuagiza Inspeka Ndilana amfuate ofisini kwake.
Amri hizo zilitekelezwa mara moja na baada ya dakika kadhaa Inspekta Ndilana alikuwa ofisini kwa Afande Maswe akitoa maelezo kuhusu mahojiano waliyoyafanya na Alice...
.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Hakutujibu vile tulivyotarajia na haonekani kama anaweza kujibu chochote ambacho kitasaidia katika kesi au katika kumhusisha moja kwa moja na mauaji ya Adrian Zayumba.” Alijieleza Ispekta Ndilana.
“Kwa nini unafikiria hivyo?” alihoji Afande Maswe
“Maswali mengi tuliyomuuliza alionekana kuyashangaa na kuanza yeye kutuuliza sisi.”
“Ndipo mkaamua kumpiga, sivyo?”
“Hapana afande, koplo Asha alikuwa anajaribu kumtisha ili tupate ukweli wake”
“Una kitu chochote ulichogundua kutokana na mahojiano mliyoyafanya na mtuhumiwa?”
“Inaonekana ana chuki kubwa sana na marehemu kiasi cha kutuambia kuwa yuko tayari kumpa zawadi muuaji endapo atamjua” Inspekta Ndilana akakaa kimya kidogo kisha akaendelea kwa sauti ya kukwama kwama “tena zawadi ya kulala naye kama akiwa mwanamume.”
Afande Maswe alimwangalia kwa muda Ispekta Ndilana kisha akamwamuru aondoke.
********
NI miezi takribani mitatu toka mwili wa Adrian Zayumba uokotwe nje, hatua chache toka nyumbani kwake ukiwa na majeraha kadhaa yanayosemekana yametokana na kuchomwa vitu vyenye ncha kali. Upelelezi wa polisi ulikuwa unaegemea moja kwa moja katika matukio kadhaa yaliyotokea siku chache kabla ya kifo chake na mtuhumiwa wa kwanza akiwa Alice ambaye hakuwa akijulikana alipo.
Adrian Zayumba alikuwa maaarufu kwa jina la Anko Zayumba kutokana na makala zake mbalimbali alizokuwa akizitoa katika magazeti kuhusiana na masuala ya mapenzi na mahusiano. Ukurasa uliompatia umaarufu sana ni ule wa ‘Muulize Anko Zayumba’ ambapo alikuwa akijibu na kutatua masuala mbalimbali kuhusiana na mahusiano ya kimapenzi.
Siku chache kabla ya kifo cha Anko Zayumba kulikuwa na hukumu ya kesi moja ambayo ilivuta hisia za watu wengi kutokana na kesi hiyo kupewa nafasi ya kipekee katika vyombo vya habari. Kesi hiyo ilikuwa inahusiana na madai ya Anko Zayumba kutaka apewe mtoto aliyezaa na Alice Kwigema miaka mitatu iliyopita wakati wana mahusiano ya kimapenzi.
Baada ya kesi kurindima kwa muda mrefu hatimaye siku hiyo mahakama iliamuru kuwa mtoto aliyekuwa akiishi na Alice akabidhiwe kwa Anko Zayumba ila mama yake, Alice aliruhusiwa kwenda kumuona kila alipojisikia. Baada ya hukumu hiyo mtoto Catherine alikabidhiwa kwa Anko Zayumba akiwa anamlilia mama yake kitu kilichomfanya Alice naye aanze kulia kwa uchungu huku Anko Zayumba akitabasamu.
Wakati wakitoka kwenye chumba cha mahakama Alice alianzisha vurugu kubwa akimuapia Anko Zayumba kwa sauti kuwa ni lazima atamuua kwa njia yeyote ile kauli ambayo ilisababisha askari wamuweke chini ya ulinzi Alice na hatimaye kumfungulia shitaka ya kutishia kuua.
Ndugu wa Alice kwa kushirikiana na wakili wake, Hamis Mzee Pembe walifanikiwa kumtoa Alice kwa dhamana na kurudi naye nyumbani na kisha kufanya mchakato wa kuimaliza kesi kibinaadam kwa kujenga hoja kuwa aliropoka tu kutokana na uchungu wa kumkosa mwanaye.
Siku hiyo baada ya hukumu, Alice alikuwa kama ambaye amefiwa na mwanaye aliyempenda mno, Catherine. Akawekewa uangalizi wa kutosha ili asije akafanya jambo lolote la kujidhuru. Alice aliishi hivyo kwa siku chache kabla ya siku ambayo kilitokea kifo cha Anko Zayumba.
Siku ambayo Anko Zayumba aliuawa, Alice alitoweka nyumbani kwao saa kumi na moja alfajiri na hakurudi tena hadi baada ya miezi mitatu alipotiwa nguvuni na polisi kwa mahojiano. Siku aliyokamatwa Alice alikutwa ufukweni mwa bahari ya Hindi, maeneo ya Kilwa Masoko akiwa na mwanamke mwenzake aliyejulikana kama Hadija Mashushu.
********
SIKU iliyofuatia asubuhi, Alice alipelekwa na askari mmoja wa kike akiwa ameongozana na Ispekta Ndilana moja kwa moja ofisini kwa Afande Maswe akiwa kafungwa pingu mikononi. Alipoingizwa Afande Maswe akaamuru afunguliwe pingu kisha akamwambia askari aliyemleta na Inspekta Ndilana wawapishe.
Yule askari wa kike akatoka haraka haraka lakini Inspekta Ndilana akawa anatoka kwa kujivuta vuta huku mawazo yakiwa yanazunguka kichwani mwake ‘afande anataka kula mzigo au?’. Baadaye akajikuta anaongea kwa sauti ndogo “sikubali”.
“Unasema?” aliuliza afande Maswe
“Ah hapana afande,” Inspekta ndilana alishtuka na kujibu huku akitaka kutoka kwa haraka.
“Subiri”
Inspekta Ndilana akawa anasubiri huku akionekana mwenye wasiwasi. Afande Maswe akamgeukia Alice
“Utakunywa chai, kahawa au soda?”
Alice alikaa kimya kwa muda akionekana kama asiyeamini anachoulizwa.
“Nakuuliza wewe Alice” Afande Maswe alikazia swali lake
“Chai” alijibu kwa sauti ya chini.
Afande Maswe akamgeukia Inspekta Ndilana
“Watuwekee vikombe viwili vya chai”
“Sawa afande” Inspekta Ndilana akatoa heshima na kugeuka kuondoka na kuwaacha Afande Maswe na mrembo Alice peke yao.
Afande Maswe akabaki akimwangalia Alice kwa muda, Alice akawa akimwangalia Afande Maswe kwa macho ya wizi.
“Alice, mimi naitwa Maswe, Steven Maswe” Afande Maswe alianza kwa kujitambulisha kwa Alice ambaye hadi muda huo alikuwa kama haelewi elewi kinachoendelea.
Kabla Afande Maswe hajaendelea wala Alice kusema chochote, Mhudumu aligonga mlango na kuwapa vikombe viwili vikubwa vya chai na kutoka.
“Pole kwa kilichotokea jana”
“Ahsante” alijibu Alice kwa mara ya kwanza.
“Mimi nimekuita ili tuongee kirafiki ili ifikie mahali ukaendelee na shughuli zako na sisi tuendelee na uchunguzi wetu, sawa mama?”
“Sawa”.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Kwanza unajua ni kwa sababu gani uko hapa?” aliuliza Afande Maswe kwa upole
“Natuhumiwa kumuua Zayumba” alijibu Alice kwa kifupi
“Mimi nina mtazamo tofauti Alice, mimi nadhani umehusishwa na mauaji ya Adrian Zayumba kwa sababu uliwahi kusema ungemuua kwa namna yeyote na pia siku ambayo marehemu anauawa haukujulikana ulikuwa wapi na ukatoweka hadi ulipokamatwa miezi mitatu baadaye. Sasa ili tujue ni kundi gani tukuweke, unatakiwa kwanza utuondolee utata wa sehemu uliyokuwepo siku ambayo Zayumba aliuawa na sehemu uliyokuwepo kwa miezi mitatu na ni kwa sababu gani? Unieleze ukweli na sitaandika popote wala kukusainisha” alijieleza Afande Maswe kwa utaratibu.
Alice alikaa kimya kidogo wakati Afande Maswe anamkodolea macho kusubiri majibu. Alice alipiga funda moja la chai na kujikohoza kidogo.
“Kwa chuki niliyokuwa nayo kwa Zayumba, sikuiona adhabu yeyote aliyostahili kutoka kwangu zaidi ya kumchukulia uhai wake na kweli nilipanga kufanya hivyo katika siku niliyotoroka nyumbani. Sikutaka kwenda asubuhi asubuhi vile ila ndiyo muda ambao niliweza kutoroka pale nyumbani nilipokuwa naishi kwa kuwa niliwekewe mtu wa kuniangalia na mara nyingi alikuwa akipitiwa na usingizi alfajiri. Baada ya kutoka pale nyumbani nikajihisi kupoteza ujasiri wa kwenda kumdhuru Zayumba na kadiri nilivyokuwa nikiendelea na safari ndivyo moyo wangu ulivyozidi kukosa ujasiri. Nikaamua kuahirisha kwanza safari nikaenda kwa rafiki yangu Salome. Wakati niko kwa Salome ndipo nikapata habari kuwa Zayumba ameuawa. Nikaenda Kilwa kumsindikiza dada yake Salome aliyekuwa anaenda mapumzikoni na ndiko nilipokuwa muda wote” alimaliza kujielezea Alice.
“Wewe ulikuwa unaishi wapi?”
“Kigamboni”
“Unajua alipokuwa akiishi marehemu Zayumba?”
“Ndiyo alikuwa akiishi Kinondoni Moroko” alijibu Alice bila kusita
“Salome anaishi wapi?”
“Magomeni Mikumi”
“Wapi uliamua kutokwenda kwa Zayumba na kwenda kwa Salome”
“Wakati nimeshavuka na pantone nikiwa nasubiri gari za Mwenge badala yake nikapanda daladala la Ubungo nikateremkia Magomeni Usalama”
“Alice”
“Abee!”
“Ulipataje habari za kifo cha Zayumba na ilikuwa muda gani?”
“Nilitumiwa ujumbe na aliyekuwa wakili wangu katika kesi ya kudaiwa mtoto na Zayumba, ilikuwa inakaribia saa sita mchana kuanzia hapo tukawa tunajibizana ”
“Majibizano yalihusu nini?”
“Alikuwa ananiuliza ni kwanini niliamua kwenda kumuua Zayumba, nikamwambia kuwa sijaenda niko kwa rafiki yangu. Akaniuliza kama nina habari kuwa Zayumba kauawa, nikamwambia sina habari. Ndipo akaniambia kuwa Zayumba ameuawa na akanishauri nitafute sehemu ya kupumzika kwa muda akili yangu itulie ili nikirudi tuanze kumdai mtoto. Sasa wakati niko pale kwa Salome dada yake alikuwa kwenye maandalizi ya kuondoka kwenda mapumzikoni Kilwa, akataka kwenda na Salome ila Salome hakukubali kwa vile alikuwa na mambo yake hivyo nikachukua hiyo fursa, nikamuomba niende naye”
“Wakili wako anaitwa nani?”
“Hamisi Mzee Pembe”
“Anajua kama umekamatwa?”
“Nadhani atakuwa anajua kwa kuwa dada Hadija aliyekuwepo wakati nakamatwa atakuwa alimpa taarifa Salome na sidhani kama Salome anaweza kuacha kutoa taarifa nyumbani. Na kama amefanya hivyo ni lazima nyumbani watakuwa wamemwambia wakili Pembe”
“Sawa Alice. Hebu nijibu jambo moja kwanza”
“Jambo gani?”
“Kwanini ulikuwa unamchukia sana Zayumba, ni kwa ajili tu ya kukunyang’anya mtoto au kuna mengine?” aliuliza Afande Maswe kwa sauti ya upole
Ukimya unatawala kwa dakika kadhaa, Alice anajiinamia chini kwa muda kisha anainua uso kumtazama Afande Maswe na kuanza kumuelezea….
*****************
Ni mambo binafsi sana lakini kwa hatua iliyofikia sina budi kukueleza ukweli wote ili nawe uweze kunielewa. Sidhani kama nitaweza kukuelezea kiasi cha kukufanya uelewe hisia zangu lakini nadhani unaweza japo kwa uchache ukagundua ni kwa nini nadhani hakustahili kuishi. Adrian Zayumba ni muuaji, ana roho ya mnyama tofauti na watu walivyomjua.
Chanzo cha mimi kumchukia Adrian ni mapenzi. Hadi namaliza kidato cha sita sikuwahi kufurahia mapenzi japo tayari niliwahi kuwa na rafiki wa kiume ambaye ndiye alinitoa usichana wangu. Baada ya kukaa kwa muda nikaanzisha uhusiano na mwanamme mwingine lakini sikuwahi kufurahia uhusiano huo nikaamua kuachana na mambo ya mapenzi.
Baada ya takribani miaka mitatu, wakati nakaribia kumaliza digrii yangu nikawa nasoma makala za Adrian Zayumba kwenye magazeti, nikavutiwa kumueleza matatizo yangu kuwa sifurahii uhusiano wa kimapenzi kwa kuwa nilikuwa nikiumia kila wakati wa kufanya tendo. Na niliamua kuuliza kwa kuwa nilikuwa nikishangaa kuona wasichana wenzangu wakifurahia lakini kila mimi nikijaribu sioni hicho wanachofurahia.
Hali hiyo ilinifanya niogope kujiingiza katika mahusiano kwa kuwa sikupenda kufanya mapenzi mara kwa mara kwa sababu sikuwahi kuyafurahia. Hali hiyo ilipekekea wapenzi wangu kutonielewa na kusababisha mizozo ya hapa na pale katika mahusiano hayo na ndipo mwishowe nikaamua kuachana kabisa na mambo ya mapenzi na nikaishi bila kuwa na rafiki yeyote wa kiume.
Adrian alikuwa ni mwanamme wa tofauti sana, alikuwa akinisikiliza na kunipa moyo kuwa kuna siku nitampata mwanamme atakayenielewa na kila kitu kitakaa sawa. Tukawa na mazoea ya kuwasiliana na Adrian na kutoka wote mara kwa mara na mwishowe nikajikuta natokea kumpenda kimapenzi. Nilijiuliza ni kwanini nisubiri atokee atakayenielewa wakati tayari kuna mtu mbele yangu anayenielewa…
Nikajitosa mzima mzima kwa Adrian, tukaanzisha uhusiano wa kimapenzi. Na kweli kwa mara ya kwanza nikawa nafurahia uhusiano wa kimapenzi, na Adrian Zayumba alikuwa ndiyo kila kitu kwangu katika masuala ya kuhusu mapenzi na mwishowe akanitambulisha kwa ndugu zake nami nikamtambulisha kwetu na kila mtu alijua kuwa penzi letu ni la kweli na siku moja tutakuja kufunga ndoa.
Ndugu wa pande zote mbili walionekana kuufurahia uhusiano wetu na tulichukuliwa kama mfano wa wapendanao kiasi ikafikia nikajiona ni mwanamke mwenye bahati kuliko wote duniani. Ila kuna jambo ambalo lilikuwa likinitia mashaka kwa Zayumba. Kazi yake…
Kwa kuwa tulianzisha uhusiano kutokana na kazi yake, sikuwa na amani kabisa, nilijua kuwa kuna uwezekano akatokea mwanamke mwingine akazama katika mapenzi na Zayumba, hivyo nikawa najitahidi kumshawishi kuwa aachane na hiyo kazi yake ya ushauri wa masuala ya mapenzi. Na mara nyingi wanawake walikuwa wakimpigia simu kutaka ushauri wakati mimi nipo, jambo ambalo lilikuwa linaniuma sana.
.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Wakati kwangu mapenzi yalikuwa yakitoka moyoni, nilihisi kuwa kwa Adrian, mapenzi kwake ni kazi na kila nilipojitahidi kuyapuuzia mawazo hayo bado yalikuwa yanazunguka akilini mwangu. Na Adrian alionekana kuipenda sana kazi ya mapenzi na kiukweli aliijua haswa. Hakuna siku ambayo iliniuma kama siku moja alipokuwa anamuelekeza mwanamke namna ya kufanya ili afurahie ngono.
Baada ya kuelekezwa huyo mwanamke akawa anapiga kila siku kutaka kuonana na Adrian eti kuna mambo alikuwa anataka kumuuliza uso kwa uso. Siku hiyo Adrian aliamua kukutana naye ila alimwambia kuwa ataenda na mimi, yule mwanamke hakuonyesha kusita. Alikubali moja kwa moja jambo ambalo lilinipa matumaini kuwa huenda hana nia mbaya.
Siku ambayo tulipanga kukutana na huyo mwanamke, nilijipigilia haswa ili aone kuwa Adrian anamiliki mrembo na hata kama anataka kumtega akate tamaa. Tukatoka na Adrian majira ya saa nne za asubuhi kuelekea ambapo tulikubaliana kuonana naye, ilikuwa ni kwenye hoteli moja iliyojificha maeneo ya Mnazi Mmoja.
Kwa mujibu wa maelezo yake ya simu, huyo mama alikuwa ana uhusiano na mtu mwenye uwezo kwa hiyo alikuwa anafanya mambo hayo kwa tahadhari sana ila asigundulike na mpenzi wake japo ilikuwa ni katika kuboresha mapenzi yao.
Tukafika hotelini hapo na kukutana na huyo mwanamke baada ya mawasiliano ya simu kutambulishana namna kujua nani ni nani. Kwa kweli huyo mwanamke hakuonekana kupania kama nilivyopania mimi, alikuwa amevaa kigauni cha kawaida tu kilichoshonwa kwa khanga. Mkononi alikuwa na simu ya bei mbaya na funguo za gari. Nywele zake alikuwa kaziachia tu kama ambaye yuko maeneo ya nyumbani kwake.
Kwa jinsi alivyokuwa anajiamini, mwenyewe nilijihisi napwaya pamoja na ‘kuuramba’ vya kutosha. Akawa anamuuliza Adrian mambo mazito mazito ya kuhusu ngono tena bila kumung’unya hata neno moja kiasi hata Adrian mwenyewe akawa anajibu kwa aibu wakati huo nilikuwa nimeukumbatia mkono wa Adrian.
Baada ya takribani dakika arobaini, tuliagana na yule dada aliomba atupe lifti hadi tuendapo kwa kuwa wakati ule Adrian hakuwa na usafiri, tulikuwa tunatumia taxi. Tukakubali akatupeleka hadi Kinondoni Moroko anapoishi Adrian. Lakini kuna kitu nilikihisi toka kwa Adrian, alionekana kuzama sana kwenye mawazo kwa ile kutwa nzima.
Baada ya kuwa katika mahusiano kwa muda na Adrian, nilipata ujauzito kwa bahati mbaya. Japo hatukuwa tumepanga, sikuwa na wasiwasi kuhusiana na mapokeo ya Zayumba kwa vile tayari tuna mwelekeo wa kuanzisha familia. Ingawa sio kwa muda ule ila sikudhani kama lingekuwa tatizo. Nikamueleza Adrian.
Kwa mshangao mkubwa Adrian aliniambia nikaitoe ile mimba kwa kuwa hakuwa tayari kuwa na mtoto kwa kipindi kile. Nilishangaa kwa vile yeye alikuwa na kazi na mimi nilikuwa natarajia kuajiriwa na serikalini kwa hiyo kusengekuwa na kizuizi chochote katika kuendesha maisha hususan kumlea mtoto ambaye angepatikana. Sikuamini nikarudi nyumbani nikiwa na mawazo kibao japo sikuwa najua nawaza nini.
Baada ya siku kama tatu hivi nikarudi tena kwa Adrian kumweleza kuhusu ule ujauzito, Adrian alikuwa mkali sana akanichapa na vibao kwa mara ya kwanza toka tuanze uhusiano wetu. Na akaniambia kuwa kama sitaki kuitoa hiyo mimba nisimtafute tena, akadiriki kuniambia kuwa ile mimba siyo yake ndiyo maana namng’ang’anizia.
Nikaendelea kukaa na ile mimba huku nikiwa naendelea kumtafuta ili nijaribu kumwelewesha madhara ya utoaji wa mimba nan i kwa nini nataka tusiitoe ile mimba lakini hakuwa tayari kunisikiliza na akawa kakata mguu kwetu na hata nikienda kwake alikuwa akiniacha nje na kuondoka. Baada ya miezi michache hata ndugu wakaanza kugundua kuwa mapenzi yetu hayako sawa. Lakini hadi wakati huo hawakuwa wakijua kama nina ujauzito.
Ikatokea siku ambayo sitaisahau katika maisha yangu yote, ni siku iliyoniuma sana. Siku hiyo nilienda kwake katika zile zile jitihada za kumshawishi akubali tuzae, nilikuta mlango uko wazi ila umerudishiwa. Nilipoingia, sikumkuta Adrian ila nilimkuta mwanamke mwingine chumbani kwake tena akiwa kavaa khanga moja tu. Alikuwa ni yule tuliyeenda kumwona wote.
Nilijihisi kutetemeka kwa uchungu na hasira ila yeye hakushtuka wala kunisemesha chochote na kabla sijatamka neon au kufanya chochote, Adrian aliingia akiwa na mfuko wenye vitu mbalimbali kama ambaye katoka kufanya manunuzi, halafu cha ajabu Adrian hakuonyesha kuujali ujio wangu pale. Nilijiona mjinga sana kumuamini Adrian na kumkabidhi moyo wangu wote.
Uvumilivu ukawa umenishinda rasmi, nikawa nakaa tu nyumbani peke yangu nalia huku ndugu zangu wakijaribu kunifariji bila mafanikio na miezi ilipokuwa ikisonga na dalili za mimba zikaanza kuonekana mwishowe nyumbani wakajua, nikakalishwa chini kuulizwa kuwa mzigo ni wa nani. Nikamtaja Adrian, nikabebwa msobe msobe hadi kwao.
Adrian aliniruka mbele ya ndugu zangu na ndugu zake na kuwaacha watu wote midomo wazi. Kwa kweli hakuna siku ambayo nilijisikia vibaya mwenye maisha yangu kama siku hiyo, nilitamani ardhi inimeze ili nijisitiri na aibu ile.
Baada ya kikao kile nikaamua rasmi kuitoa mimba ile ili nianze maisha mapya lakini mpango wangu uligundulika. Ndugu waliniwekea uangalizi na kunionya kuwa endapo ningetoa ule ujauzito wasingekuwa na radhi na mimi. Nikautunza ule ujauzito hadi muda wa kujifungua ukafika.
Siku ya kujifungua nikapelekwa hospitali ya Amana lakini ikashindikana, nikachukuliwa na gari la wagonjwa kupelekwa Muhimbili nikafanikiwa kujifungua kwa operesheni lakini nilipoteza fahamu kwa takribani siku mbili. Siku ya tatu nikazinduka na kwa mara ya kwanza nikamuona mwanangu Catherine.
Baada ya kumpata Catherine, Adrian na ndugu zake wakafanya majaribio kadhaa ya kutaka kurudisha uhusiano lakini sikuwapa nafasi ndipo wakaanza vitisho na kutumia umaarufu wake hatimaye akafungua kesi na kuninyang’anya mwanangu mpenzi na hatimaye akafanikiwa azma yake. Kwa hili sitamsamehe kamwe duniani hadi ahera.
*******.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Alimaliza kuhadithia Alice akibubujikwa na machozi na kumfanya Afande Maswe abaki kaduwaa akimwangalia Alice kisha akatoa kitambaa cheupe na kumkabidhi Alice.
“Unajua alipo mwanao”
“Hapana ila nahisi atakuwa Masaki kwa dada yake mkubwa Adrian” alijibu Alice huku akijifuta machozi kwa kitambaa alichopewa na Afande Maswe.
“Unadhani ni kwa nini atakuwa huko?”
“Najua tu kwa kuwa huyo dada yake ndiye alikuwa anang’ang’ania sana Adrian amchukue mwanangu. Lakini nitampata tu mwanangu” Alice alisema kwa hasira.
“Hivi Alice, huyo mwanamke uliyemkuta kwa marehemu alikuwa naye hadi wakati umauti unamfika?” aliuliza Afande Maswe
“Nasikia walishaachana ila sijui vizuri mambo yao kwa kuwa sikuwa nafuatilia”
“Uliwahi kulijua jina lake?”
“Ndiyo. Anaitwa Salma”
“Alice, utarudi rumande kwa sababu tukikuachia upelelezi unaweza kuvurugika, lakini nakuahidi kuwa tutachunguza jambo hili kwa haraka ili haki itendeke.” alisema Afande Maswe kwa sauti ya kukwaruza kama aliyebanwa na kikohozi.
Afande Maswe alimuita askari aliyekuwa anasubiri nje na kumwamuru amrudishe Alice mahabusu hadi atakapohitajiwa tena na kuagiza kuitiwa Inspekta Ndilana.
Alice akachukuliwa kurudishwa rumande. Na baada ya dakika kadhaa Afande Maswe alikuwa uso kwa uso na Inspekta Ndilana aliyeonekana kujawa wa donge moyoni.
“Kuna mambo ambayo nataka uyafanyie uchunguzi” alianza kuongea afande Maswe akimtazama usoni Inspekta Ndilana aliyekaa kimya kama anayesubiri kusomewa hukumu.
Afande Maswe akachomoa kifaa cha kurekodia sauti chini ya meza yake na kukibonyeza, yakaanza kusikika mahojiano kati ya Afande Maswe na Alice kuanzia mwanzo hadi mwisho kisha afande Maswe akakizima na kumtazama Inspekta Ndilana usoni.
“Kutokana na mahojiano uliyosikia wewe unafikiria nini?” Afande Maswe alimuuliza Inspekta Ndilana akimwangalia usoni.
“Inawezekana aliwahi asubuhi, akamuua kisha akakimbilia kwa huyo Salome” alijibu Inspekta Ndilana.
“Ripoti ya uchunguzi wa mwili wa marehemu inasema kuwa marehemu aliuawa kati ya saa mbili na saa tatu asubuhi, na inavyoonekana marehemu alishambuliwa toka mbele. Unadhani Alice peke yake anaweza kumshambulia toka mbele na kufanikiwa kumuua Adrian Zayumba? Kama alikodi mtu, unadhani toka saa kumi na moja alfajiri aliyotoroka kwao hadi saa mbili asubuhi angeweza kupata mtu wa kuifanya kazi hiyo na alimlipaje?” Afande Maswe alimimina maswali mfululizo kutokana na jibu la Inspekta Ndilana.
“Daah! Hapo lazima kutakuwa na mtu wa tatu, swali ni nani?” alijishangaza Inspekta Ndilana.
“Nataka kwanza kujua kama kweli siku ya tukio Alice alikuwa kwa Salome, pili nataka kujua kama nyumbani kwa kina Alice wanajua kama Alice amekamatwa na walichukua hatua gani. Fanya mahojiano na Salome na watu wa nyumbani kwa kina Alice. Nataka taarifa kamili kesho asubuhi” Afande Maswe alitoa maelekezo kwa Inspekta Ndilana kisha akamruhusu aondoke.
Afande Maswe aliamua kukaa nalo mwenyewe faili la kesi hiyo na hakuna aliyejua sababu ya kamanda wa polisi kuamua kuishikilia kesi yeye mwenyewe wakati ana wasaidizi lukuki wenye ujuzi wa kutosha kuifanya kazi hiyo kwa ufanisi.
Alipotoka pale Inspekta Ndilana alienda moja kwa moja nyumbani kwa kina Alice, akakutana na wanafamilia na kufanya mahojiano ya kina na kila mmojawao. Kikubwa alichopata ni kuwa wanazo taarifa kuwa Alice anashikiliwa na polisi na wanachokifanya ni kuchangishana wamlipe Wakili Hamisi Mzee Pembe ili aweze kusimamia kesi.
Alipoenda kwa Salome hakuambiwa mambo tofauti sana na aliyoyasema Alice, kulikuwa na tofauti ndogo ndogo tu ambazo hazikuwa na athari katika suala zima.
Kesho yake asubuhi, Inspekta Ndilana akarudisha ripoti kwa Afande Maswe.
“Umefikiria nini baada ya kupata majibu hayo?” aliulizwa Inspekta Ndilana akabaki anatumbua macho kama fundi saa aliyepoteza nati kisha akakurupuka kama aliyetoka usingizini
“Naam afande”
“Nimekuuliza, nijibu”
“Mimi naona kama hahusiki na hayo mauaji ya Adrian Zayumba” Inspekta Ndilana alijibu kwa kujiamini
“Kama sio yeye, muuaji atakuwa nani?” aliuliza Afande Maswe
Inspekta Ndilana alikaa kimya kwa muda mrefu akijifanya kuwaza na kuwazua huku Afande Maswe akiwa katulia anamwangalia.
“Au unafikiria tuendelee kuchunguza jambo gani ili tumpate muuaji?” Afande Maswe alimuongeza swali Inspekta Ndilana.
“Nadhani tukim’bana zaidi Alice, anaweza kutuambia mambo mengine yatakayotuongoza kujua muaji” alijifutua Inspekta Ndilana kutoa mawazo.
“Hali inaonyesha kuwa uliubana uchunguzi wako kwa kujihakikishia kuwa Allice ndiyo muuaji, sivyo?” Afande Maswe aliuliza swali akiujua kabisa kuwa ndiyo ukweli wenyewe.
“Mazingira yote yalikuwa yakionyesha kuwa Alice ndiyo muuaji afande”
“Katika hali kama hizi ndipo huwa mnalazimishia watu kushitakiwa kwa mauaji kwa kuwa mnakuwa mmejifunga katika uchunguzi wenu na matokeo yake mnampeleka mahakamani mtu ambaye hahusiki na hata kama anahusika kunakuwa hakuna ushahidi wa kutosha kumtia hatiani. Sisemi kuwa Alice hahusiki ama anahusika ila ninachotaka kukwambia ni kuwa nataka kujua kama cheo chako unastahili kuwa nacho” aliongea Afande Maswe kwa sauti ya chini lakini iliyoonyesha kuwa anamaanisha anachokiongea.
“Sawa afande” alijibu Inspekta Ndilana kwa woga.
“Nakupa siku tatu za kufanya uchunguzi kuthibitisha kama Alice anahusika kwa namna yeyote. Ukishindwa kunishawishi namuachia na ntakupa siku tatu nyingine umtafute muuaji. Napo ukishindwa, cheo chako kitakuwa hatarini” Afande Maswe alimalizia kuongea na kuamuru Inspekta Ndilana atoke ofisini kwake. Inspekta Ndilana alitoka mule ofisini akiwa kama aliyemwagiwa maji ya baridi
Yalipita masaa kadhaa Inspekta Ndilana akiwa ametulia ofisini kwake akiwaza bila kujua anachokiwaza, hakuwa akijua aanzie wapi na amalizie wapi katika uchunguzi wa tukio la mauaji ya Adrian Zayumba. Yalipofikia masaa mawili kabla ya muda wake wa kuondoka, akapata jambo la kufanya ili japo amuonyeshe afande wake kuwa ameanza kazi.
Alijikusanya nguvu na kuingia ofisini kwa Afande Maswe..
“Vipi?”
“Afande, nahitaji faili la kesi na mahojiano uliyofanya na mtuhumiwa” alijikaza Inspekta Ndilana ili aongee kijasiri..CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Afande Maswe aliinamisha kichwa na kucheka kidogo kisha akainua uso kumtazama Inspekta Ndilana aliyekuwa akijikaza asipoteze ujasiri.
“Nilikuwa najiuliza unafanyaje kazi bila kuwa na vitu hivi ulivyokuja kuviomba, nikapita ofisini kwako nikakuona umetulia kimya nikaona nipite nisikusemeshe”
“Unajua afande, tayari nilikuwa na mtazamo tofauti na hali ya uchunguzi inavyoenda kwa hiyo nilikuwa naiweka sawa akili yangu kabla ya kuanza kufanyia kazi changamoto mpya” alijibu bila kufikiria na kumuacha afande Maswe akimwangalia kwa umakini kisha akatoa faili na kifaa alichomrekodia Alice na kumkabidhi Inspekta Ndilana.
Inspekta Ndilana akavipokea na kutaka kuondoka haraka haraka kabla hajasimamishwa na Afande Maswe, akageuka na kumtazama Afande Maswe kwa wasiwasi.
“Unatumia akili zako kwa uchache sana, sasa huu mtihani ndiyo utakaonifanya nijue kuwa umeamua kuziweka akili zako katika kazi au bado unacheza? Na nimeshakwambia nitakachofanya endapo utashindwa” aliongea Afande Maswe akimalizia na maneno yaliyokuwa yakimnyima raha Inspekta Ndilana.
Usiku wa siku hiyo ulitumika na Inspekta Ndilana kumlaani afande wake hasa kila akikumbuka maneno ya bosi wake ambayo kwake ni kama vitisho. Alijikuta akimaliza kila aina ya matusi anayoyajua kumtukana afande Maswe ili mradi tu atoe msongo wake wa mawazo.
Alfajiri yake, Inspecta Ndilana aliamua kuanza kulipitia upya faili la kesi ya mauaji ya Adrian Zayumba, alipitia taarifa za hospitali baada ya uchunguzi wa mwili wa marehemu, na taarifa za majirani pamoja taarifa za watu kadhaa waliohojiwa wakiwemo wafanyakazi wenziye.
Alilipitia faili mara tatu lakini hakupata jambo lolote lililompa mwanga kwamba aanzie wapi katika kuthibitisha tuhuma za Alice kuhusika na mauaji, akataka kukubaliana na hali halisi kwamba hakuna ushahidi wa nguvu wa kumtia hatiani Alice ila sasa nafsi yake ikawa inasita akijiuliza, “Alice akiachiwa hawezi kweli kuniharibia upelelezi wangu?”
Ilipofika majira ya saa sita mchana, Inspekta Ndilana alipata wazo, akaenda moja kwa moja makao makuu ya jeshi la polisi na kupitiliza ofisi ya Kamishna Zebedayo ambaye ndiye aliyemuingiza kwenye jeshi la polisi. Akamuelezea kila kitu na kumuomba ampigie Afande Maswe ili amuondolee jukumu la kupepeleza hiyo kesi.
“Unadhani ni nini kazi ya polisi?” aliulizwa kwa utaratibu akikaziwa macho.
Inspekta Ndilana alibaki kimya bila kusema neno lolote.
“Ninazo taarifa kuwa umepewa kazi hiyo, na nimemwambia ACP Maswe kuwa endapo ukishindwa siyo tu akushushe cheo bali ufutwe kazi mara moja kwa maana hii siyo mara ya kwanza unakabidhiwa kazi unatupa taarifa matokeo yake tunapeleka watu mahakamani na mwishowe wanaishia kuachiwa tu kwa kukosekana ushahidi wa kutosha” alikazia Kamishna Zebedayo.
Inspekta Ndilana alitoka pale kimya kimya na kuishilia.
******
Jina kamili la Inspekta Ndilana ni Jackson Ndilana ambaye baada ya kumaliza chuo kikuu akafanyiwa mpango na Kamishna Zebedayo kuingia katika jeshi la polisi baada ya kusota mtaani kwa zaidi ya mwaka akitafuta ajira.
Kutokana na elimu yake aliweza kupanda vyeo haraka haraka na mara nyingi amekuwa akifanya kazi za ofisini pamoja na kuwa alipelekwa kwenye kozi maalum ya upelelezi wa makosa ya jinai na kufanya vizuri. Alianzia kufanya kazi makao makuu kisha akahamishiwa kwenye chuo cha polisi Moshi kama Mkufunzi na sehemu zote alifanya vizuri sana hadi wakubwa wake wakawa wakimfikiria kumpandisha zaidi cheo.
Wakati wakiwaza hayo, likatoka wazo kuwa ni lazima kwanza apate uzoefu wa vituoni kabla ya kumpandisha cheo na wazo hilo likaungwa mkono na viongozi wote ndipo akapelekwa kwanza mkoa wa Mtwara.
Ndani ya miezi nane aliyokaa Mtwara, Ndilana hakuonesha ufanisi katika majukumu yake bila kujua kama alikuwa anaangaliwa na taarifa zake zilikuwa zikifikishwa makao makuu kila siku sana sana tu alikuwa akipata skendo za uzinzi. Ikabidi aondolewe na kurudishwa kanda maalum ya Dar es Salaam chini ya Kamishna Msaidizi Steven Maswe.
Akiwa pale, alipewa kazi tatu za matukio tofauti lakini zote ziliisha kwa watuhumiwa kuachiwa huru kutokana na kukosekana kwa ushahidi wa kujitosheleza kuwatia watuhumiwa hatiani na hii ilikuwa ni kesi ya nne kukabidhiwa.
Majibu ya Kamishna Zebedayo yalifanya kengele ya hatari ilie kichwani kwa Inspekta Ndilana na mara moja kumbukumbu za mwenendo wake wote toka apelekwe kufanya kazi kwenye vituo zikaanza kuzunguka kwenye kichwa chake na mwishowe akajiridhisha kwamba haitendei haki kazi yake na tayari amekwishawaumiza watu wengi sana kutokana na uzembe wake.
******
Baada ya kutoka pale makao makuu, Ndilana aliamua kwenda kukaa sehemu yenye utulivu ili kuiweka sawa akili yake kichwani alikuwa akiwaza ataishije bila posho na mshahara wa polisi. Alikuwa akifikiria ugumu wa kupata kazi kutokana na kozi ya sayansi za jamii aliyoichukua chuo kikuu, mwisho akaamua apige pombe aitie akili ujinga.
Akawasha gari yake akaenda nyumbani kwake Magomeni kubadilisha sare za kazi kisha moja kwa moja hadi baa moja iliyojificha maeneo ya Kinondoni, akaegesha gari na kuanza kupata bia mbili tatu. Pamoja na kufuata pombe lakini maeneo hayo anaishi askari mwenzie mmoja wa kike ambaye alikuwa akimfukuzia kwa muda mrefu.
Alijua fika kuwa hata angemuita asingefika pale kujumuika naye ila huwa anapenda tu kwenda baa ile kwa kuwa hata huyo askari akitoka ama kuingia nyumbani kwake kutokana na majukumu yake angeweza kumuona na kustarehesha nafsi yake. Baada ya kuchapa bia takribani sita alitokea dada mmoja na kukaa jirani yake..CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Unanikumbuka afande?” aliuliza dada yule na kumfanya Ndilana amwangalie kwa umakini.
“Kusema kweli sikukumbuki, naomba unikumbushe tafandhali”
“Mi naitwa Hadija, ni rafiki yake Alice”
Ndilana alikuwa anapeleka glasi ya bia mdomoni, akashtuka na kuirudisha chini. Akamtazama tena upya Hadija.
“Hadija Mashushu?”
“Ndiyo”
Hadija Mashushu ndiye dada yake Salome aliyekuwa na Alice mapumzikoni Kilwa wakati Alice anakamatwa. Na siku ambayo Ndilana alienda kumhoji Salome kutokana na maagizo ya Afande Maswe, Hadija hakuwepo ila walionana siku ya kwanza Alice aliyofikishwa mahakamani.
“Nashukuru kwa kuikumbuka sura yangu na kunikumbusha, sikuwa nakukumbuka hata kidogo. Huwa unakaa sana hapa au umekuja mara moja tu?” alijieleza Ndilana kabla ya kumalizia kwa swali
“Nimekuja kukutana na wakili kuangalia uwezekano wa kumtoa Alice. Au utatusaidia afande?” aliongea Hadija kwa sauti ya kuomba msaada.
Ndilana akajiweka vizuri na kumkodolea macho Hadija, akakutana na macho ya shangingi lililokubuhu yakiwa yamelegea mithili ya komba aliyekunywa pombe ya mnazi. Akajikuta akisisimkwa mwili na kubaki akimkodolea kwa dakika kadhaa. Hadija kwa uzoefu wake akawa amekwisha kuusoma mchezo, akatabasamu.
“Kila kitu kiko ndani ya uwezo wako afande, ni kuamua tu” Hadija alimwambia maneno ambayo yalimfanya Ndilana badala ya akili yake kuhamia kwenye mapenzi akakumbuka kauli ya Afande Maswe “Unatumia akili zako kwa uchache sana, sasa huu mtihani ndiyo utakaonifanya nijue kuwa umeamua kuziweka akili zako katika kazi au bado unacheza”
Ndilana alishusha pumzi ndefu kisha akamwangalia tena Hadija aliyekuwa bado akimwangalia kwa tabasamu, Ndilana naye akatabasamu kisha akamuonyesha ishara Hadija asogeza sikio. Hadija akawa akisogeza sikio huku akiwa kama anayeogopa kutekenywa.
“Malizana kwanza na wakili wenu kisha nipigie leo leo tuonane, mimi hapa namalizia bia yangu naondoka.”
“Naomba namba yako” Hadija alimwambia Ndilana kwa sauti iliyojaa pumzi
Ndilana akaichukua simu ya Hadija na kuandika namba yake kisha akajibipu. Ghafla akaingia jamaa mmoja aliyevalia suti nadhifu akawa anaangaza angaza kabla ya kutoa simu yake na kuanza kubonyeza namba ili apige. Hadija akainua haraka haraka na kumuwahi kisha wakaelekea kukaa sehemu nyingine.
Muda huo ilikuwa yakaribia saa kumi na mbili za jioni.
Ndilana aliondoka pale akiwa na kama bia tano kichwani ila hakuwa amelewa japo stimu zilikuwa zishaanza kumwingia, akawasha gari lake na moja kwa moja akarudi ofisini ambako aliacha kifaa kilichorekodi mahojiano kati ya Afande Maswa na Alice.
Ndilana akachukua kijitabu kidogo na kalamu akaanza kusikiliza mahojiano, akayasikiliza mwanzo hadi mwisho na kuyarudia kwa takribani mara nne kisha akaanza tena kuyasikiliza huku akiandika baadhi ya vitu kwenye kijitabu chake, mwisho akayasikiliza tena mwanzo hadi mwisho. Akakiridisha sehemu aliyotumia kukihifadhia na kutoka.
Ilikuwa yakaribia saa tatu usiku wakati Ndilana anatoka ofisini kwake na ilikuwa imebakia siku moja kabla Afande Maswe hajamuachia Alice na kumtaka Inspekta Ndilana amtafute muuaji ndani ya siku tatu nyingine. Inspekta akawa anaendesha kuelekea nyumbani kwake, mara simu yake ikaita.
Akatoa kuiangalia, ilikuwa ni simu ya Hadija Mashushu akaipokea.
“Uko wapi nije?” aliuliza Hadija kwa sauti ya mapozi
Inspekta Ndilana akamuelekeza sehemu atakayomkuta, ni baa moja ambayo ina vyumba vya kulala. Baada ya kuelekezwa, Hadija alitabasamu kisha akakata simu.
Ilimchukua Ndilana kama dakika nane tu hadi kufika sehemu aliyomuaelekeza Hadija, akaagiza bia yake moja akimsubiri. Zilipita dakika arobaini bila Hadija kufika, Ndilana akaitoa simu yake mfukoni na kumpigia lakini simu iliita bila kupokelewa.
“Huyu mwanamke kaamua kunichezea sinema leo” alijikuta akiongea mwenyewe kisha akainuka na kuelekea kwenye gari lake, mara simu yake ikaita. Kuiangalia ni namba ya Hadija. Akasimama na kuipokea.
“Mimi ni Salome, Hadija amekamatwa na muda huu anapelekwa kituo cha Urafiki” iliongea sauti ya upande wa pili kisha simu ikakatwa.
Inspekta Ndilana akabaki ameduwaa kwa muda kisha akakata shauri aende akasikilize kilichojiri. Akawasha gari na kuwahi kituo cha polisi cha Urafiki. Alipofika hakujitambulisha kwanza kama na yeye ni askari, alijifanya kama raia anayeulizia kuhusu ndugu yake akaambiwa kuwa amekamatwa kwa tuhuma za kufanya biashara ya dawa za kulevya.
“Amekamatwa nayo?”
“Hapana” alijibu askari wa zamu.
“Sasa imekuwaje?”
“Acha kusumbua na maswali yako, sema una shida gani” alijibu yule askari
“Sawa, naomba nionane naye”
Zikapita longolongo za hapa na pale mwisho akakutanishwa na Hadija anayeonekana alikamatwa wakati akijiandaa kwa mtoko.
“Imekuaje?”
“Hata mimi sielewi hadi hivi sasa. Baada ya wewe kuondoka pale, niliongea na yule wakili na tukafikia muafaka. Nikarudi nyumbani kujiandaa kwa ajili ya kuja kuonana na wewe, wakati natoka nikawakuta askari nje ya nyumba yangu. Wakaniambia kuwa wamepata taarifa kuwa nafanya biashara ya dawa za kulevya, wakapekua nyumba yangu lakini hawakukuta kitu ndipo wakanichukua kunileta hapa kwa madai kuwa wanasubiri taarifa nyingine ila wameshaniambia wazi kuwa wanataka hela ndiyo waniachie” alijieleza Hadija.
.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
*****ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment