Search This Blog

Wednesday, 1 June 2022

MAWIO NA MACHWEO - 1

 











    IMEANDIKWA NA : FRANK MASAI



    *********************************************************************************



    Simulizi : Mawio Na Machweo

    Sehemu Ya Kwanza (1)



    MWAKA 2005.

    CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/



    Naweza kusema ndio mwaka uliokuwa na mafanikio na furaha kubwa katika familia ya Bwana na Bibi Masai, kwani ndio mwaka ambao watoto wao tisa kila mmoja kwa uwezo wake aliitikia wito wa wazee wale ambao ndio wazazi wetu.



    Wazee wangu nilikuwa naishi nao Dodoma kipindi chote wakati nasoma kidato cha sita.

    Pia sikuwepo nyumbani peke yangu kama mtoto. Nilikuwa na dada zangu ambao pia tulimaliza wote kidato cha sita,hao ni Angel na Vene au Veneranda.



    Siku hiyo wazazi wangu waliwaita kaka na dada zangu wote ambao tayari walikuwa na makazi yao.Wengine mikoani na wengine palepale Dodoma. Waliitwa kwa nia moja tu!.



    Waliitwa kwaajili ya tafrija ya pongezi,kwa wengine kupata watoto,kazi,kufunga ndoa,kumaliza chuo na wengne kama mimi na dada zangu ni kwa ajili ya kupongezwa kwa kuchaguliwa kujiunga vyuoni. Kwangu mimi nilipata nafasi ya kuendelea na chuo cha biashara pale Dodoma{CBE}. Dada zangu wao walichaguliwa mmoja kwenda Mzumbe Morogoro kusomea Sheria na mwingine Tumaini kusomea uandishi wa habari, hiyo ni baada ya kufaulu vizuri sana katika masomo yetu.

    *****************



    Ilikuwa ni Jumapili moja yenye amani sana katika familia yetu. Kaka na dada zangu wote walijumuika nasi na kuleta mvuto wa kipekee pale mtaani. Mimi na dada zangu wale wawili, tukiwa kama waenyeji kwa siku ile, tulikuwa tunaangaika kuandaa mazingira mazuri kwa ajili ya ugeni ule.



    Purukushani za wajukuu na vicheko vya wake wa kaka zangu pamoja na dada zangu,vilifanya nyumba ipendeze na kuchangamka sana. Na kwa upande wa kiume huku kwetu, kila mtu alijaribu kuonesha umahiri wake wa kufuraisha na kupendezesha nyumba ile.



    Sikuwa nyuma katika hilo.Ghafla nilianza kuchana {kurap} kwa mitindo huru{freestyle},huku mistari yangu ikitoa pongezi nyingi kwa wazazi na kuwashukuru familia yangu kwa kufikishana pale. Mistari ile ilifanya wafurahi kana kwamba wamemuona Eminem au Kanye West akiwa jukwaani. Waliomba nitulie kwani tayari mizuka ilishapanda hivyo ningendelea zaidi, ningemaliza uhondo kabla ya muda ujafika maana nlishaanza pia "kuvunjika"{kucheza kwa kushirikisha viungo vyote vya mwili} jambo lililofanya wale ambao hawajawahi kuona vile, hasa wajukuu na shemeji zangu kuacha kazi zao na kuja kushangaa nifanyacho.

    Yalitoka makofi na shangwe nyingi baada ya tendo lile,huku nikiwapa ahadi ya mazuri nitakayoyafanya usiku ule wa furaha.

    *************



    Nilisifika pale mtaani kwetu kwa kurap{HIP HOP} na kucheza, na hata shule nilizosoma nilipata umaarufu kwa sababu hiyo.Nilikuwa naweza sana kucheza, yaani toka kitambo,ila niliongeza zaidi ujuzi ule baada ya matatizo yaliyonitokea baina yangu na Generose {Hii ni ile simulizi ya My Rose,kwa waliyoisoma}.

    Matatizo yale yalisababisha Baba na Baba yake Generose kunipa muda wa kutoa yale mawazo kwa kunipeleka Chuo Cha Sanaa Cha Bagamoyo, ambapo huku ndipo nilijifunza zaidi kucheza na kuimba.

    Nilijenga urafiki na watu wengi sana pale mtaani na sehemu nyingine nilizokuwa nazitembelea. Hiyo ni kwa sababu nilikuwa sina majivuno wala kisirani.Sifa hizo ndizo zililofanya siku ile ya tafrija wajae rafiki zangu wengi kwa ajili ya kusaidia kazi mbalimbali pale nyumbani.



    Hatukua matajiri sana, wala masikini sana na ndiyo maana tuliweza kumudu kuandaa tafrija ile. Wazazi wetu kwa uwezo wao waliweza kutusomesha kadiri ya kiwango tunachohitaji. Na uzuri pale nyumbani,wote tuliweza kugusa elimu ya kidato cha nne, sifa zikaenda kwa wazee wangu.

    ************



    Muda wa saa mbili usiku,tafrija ilipamba moto. Waalikwa walikuwa wamekaa sehemu zao na waenyeji walikua panapo husika. Kila mtu pale nyumbani alipewa nafasi ya kuwaalika watu wake kwa idadi aijuayo.

    CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Baada ya kila kitu kuwa sawa,Baba na Mama yangu walianza kwa kutoa utambulisho wao na baadaye walifuata kaka na dada zangu kujitambulisha na kuutambulisha ugeni walio ualika.

    Ilipofika zamu yangu kujitambulisha,waalikwa na wana tafrija ile, hawakusita kutoa shangwe zao baada ya mimi kushika kipaza sauti.

    Ukumbi ulilipuka kwa shangwe.Sio ndugu wala jamaa, wote kwa pamoja walikua wanapiga makofi kwani mimi ndiye niliyefanya tafrija iende kama ilivyopangwa. Yaani kazi nyingi zilifanywa na rafiki zangu. Hiyo ni sababu ya kuwa na mahusiano mazuri na watu wote pale mtaani kwetu na kujiheshimu kwa familia yetu kwa ujumla, hasa dada zangu.



    "Tupe mistari Man'Sai". Ilisikika sauti ya kijana mmoja kutoka nyuma kabisa baada ya mimi kushika kipaza sauti kile.

    Nilitabasamu na kushindwa kuongea lolote zaidi ya kutoa machozi ya furaha kwa sababu si rahisi katika maisha ya binaadamu kukubalika na kila mtu hasa kwa matendo niliyoyafanya baada ya yaliyotokea kwa Generose.

    Ila kwa kitendo kilichotokea pale, kilifanya niamini kuwa siku nikifa basi nitazikwa labda kama Mwalimu Nyerere. Lakini pia sikuacha kujionya kuwa "POPOTE UNAPOKUBARIKA,LAZIMA APATIKANE WA KUKUPINGA".





    "Ninyi nyote mliyokuja hapa nimewaalika mimi,sina sababu ya kutaja jina la kila mtu. Ndugu yangu yeyote aleyewaita hapa leo,basi na mimi nahusika katika kuita huko, kwani midomo yao na mwili wao ni mwili wangu pia,sisi sote ni watoto wa baba mmoja.

    Wale niliyo waalika kwa mdomo na maandishi yangu,kaeni mkitambua kuwa nyie ni watu muhimu sana katika familia yangu,nawapendeni sana nyote mliokuja". Hayo yalikua maneno yangu ya ukaribisho.



    Na baada ya hapo wageni wote walisimama hata wale ambao mara ya kwanza walikua hawajui kwa nini nashangiliwa sana, sasa kwa pamoja walikuwa wakipiga makofi na kushangilia. Niliamini kuwa sauti yangu ilizama kwa kila sikio la mtu pale ukumbini.



    Tafrija iliendelea,zawadi zikatolewa na pongezi nyingi zikaenda kwa wazazi wangu kwa kutufikisha pale.

    Baadae wazazi na watu wengine wa makamo waliondoka na kuwaachia ukumbi vijana na wapenda burudani.Hapo na mimi nikaenda jukwaani na kukamata kipaza sauti kisha nikaanza kazi yangu ya kisanii.



    Mwanzo nilianza kurap bila midundo{Accapela} lakini baadaye DJ aliweka mdundo ambao nilienda nao kama kawaida ya wasanii wenye uwezo.

    Nilitumia muda mwingi kufokafoka jambo lililofanya wengine kuchoka kwa nifanyacho hasa wakina dada.



    DJ alitambua hali ile ivyo badala ya kuzidi kutoa midundo ya hip hop akabadilisha na kuweka "beat" ya wimbo wa Michael Jackson ile ya Bilie Jean. Nilitabasamu kwani niligundua nia ya DJ na kiukweli alifanikiwa.



    Niliendelea kufoka foka ndani ya mdundo ule lakini ilipofika katikati niliweka kipaza sauti chini na kisha nkaanza kucheza na kuvunjika mwili wangu kitu kilicho amsha mayowe na shangwe nyingi ukumbini mle.

    Ilikuwa ni kelele na fujo pale jukwaani japo zilikuwa hazina madhara kwangu. Kila mtu alitaka kunitunza,na wengine walitaka japo wanishike tu!



    Huku nikiendelea kuvunjika, DJ aliweka wimbo mwingine wa Michael Jackson uitwao Thriller. Hapo ndipo hali ikazidi kuwa tete na kubadilika kwani baadhi ya rafiki zangu walivamia jukwaa na kuanza kucheza na mimi.



    Kama umewahi kuona video ya wimbo huu nadhani utatambua nini kilichoendelea jukwaani kwa muda ule.

    Tulicheza kama yale mazombi. Na hapo kila mmoja alipanda jukwaani na kuanza kucheza na sisi hasa wale waliyoelewa kucheza wimbo ule. Ilikua ni furaha tosha pale jukwaani hasa kwa wapenda burudani za vile.





    Hadi saa nane za usiku bado watu waliendelea kufurahia tafrija ile,lakini kwangu mimi niliona ndio muda muafaka wa kwenda kupumzisha ubongo wangu.

    *************

    Nilifika chumbani na kujitupa kitandani na bila kusita usingizi nao ukanitembelea na kunichukua hadi dunia nyingine iitwayo ndoto.

    Ndoto ni mawazo uliyowaza kwa muda mrefu sana.Au yaweza kuwa ni matukio ambayo unayafanya sana katika maisha yako, na pale ulalapo, ndipo yanakuwa marudio.Yaani kwa kifupi ndoto ni matendo uyafanyayo kwa wingi au mambo uyawazayo.

    Lakini vilevile kuna muda ndoto huja tu! Si lazima uwe umewaza au umeyafanya ndio uote.



    Nlipelekwa mbali sana katika usingizi ule.

    Nilimuota Generose ambaye ndiye msichana aliyejua thamani yangu katika mapenzi. Generose huyu ndiye aliyefanya nijisikie mwenye amani maishani mwangu na nisiyeishiwa na tabasamu katika uso wangu. Lakini kilichotokea,namshukuru Mungu.





    Nilikuwa sijaongea na Generose karibu wiki mbili. Iwe kwenye simu au kwa kuonana uso kwa uso.

    Siku hiyo nikiwa katika mawazo mengi juu ya Generose, ghafla niliona simu yangu ikionesha namba na jina la Rose ikimaanisha kuwa alikuwa anapiga. Lakini nilipo pokea,hakuwa Generose bali mama yake na alinitaka niende kumuona Generose.



    Nilipofika kwa akina Generose kama mama yake alivyotaka, nilikutana na Generose aliyeisha mwili na kunyong’onyea huku midomo yake ikiwa imemkauka. Nilikuwa nampenda sana Generose hivyo nilimpa moyo sana kwa yote yanayoendelea kumkuta.



    Wakati nipo naye pale chumbani kwake,Generose aliniomba nimuimbie wimbo wa Sinzia uliyoimbwa na Nameless. Tuliimba kwa pamoja kwa sekunde kadhaa,ila baadaye Generose alilegea mwili wote na hata nilipomuita hakuitika. Nilipoanza kulia huku nikiomba msaada,ghafla nilihisi naguswa mwilini mwangu na mikono iliyokuwa ya baridi sana.Ndipo nilishituka toka ndotoni na kukuta ni kaka yangu akinigusa huku akinihamsha na kuniambia nisogee kidogo na yeye alale.



    Ilikuwa yapata saa kumi alfajiri, na kitendo cha kaka yangu kunishitua kilifanya nikae macho hadi saa kumi na mbili huku nikiendelea kutafakari ile ndoto na kusababisha nimkumbuke sana Rose wangu





    Ugeni ule ulidumu kwa siku tatu pale nyumbani. Hadi siku ya tano inatimia, tayari nyumba ilirudi kama zamani.

    Baadaye Dada yangu yule mdogo, naye alienda Morogoro kwenda kuanza masomo yake ya Sheria huko Mzumbe na yule mwingine,alienda Dar es Salaam kwa ajili ya kusomea uandishi wa habari katika chuo cha Tumaini.

    CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Sasa nyumba ikabaki na mimi kama mtoto, ambapo pia wiki iliyofuata, nilitakiwa kwenda kuanza masomo pale CBE ya Dodoma. Pia alikuwapo Shangazi yangu mkubwa kwa upande wa baba, pamoja na wazazi wangu yaani baba na mama..

    ***********





    Ikawa siku nyingine tena ya huzuni sana katika nyumba yetu ile niliyoishi kwa muda mrefu. Japo nilienda chuo cha pale pale Dodoma lakini ikaonekana kama naenda mbali na Dodoma.

    Mtaa ukapoa, nyumbani pakawa huzuni tupu. Huku nikijaribu kutoa ahadi ya kuwatembelea kila nikipata muda lakini ilionekana kuwa wananihitaji sana nyumbani.Lakini kulikuwa hakuna jinsi,nilitakiwa kwenda kuanza masomo yangu ya shahada ya Ugavi CBE Dodoma.

    ***********************



    Kwa ufasaha mkubwa wa baba yangu, alifikisha safari yangu kwenye lango la Chuo kwa kutumia gari aina ya Nissan Patrol ambayo ilikuwa ni zawadi ya familia iliyotolewa siku ile ya tafrija..



    Baba yangu kama kawaida ya wazazi wengne, japo alishaongea na kunihasa sana ,lakini ni kama hakumaliza wosia wake ,hivyo kabla sijashuka garini alinisihi sana kuhusu mapenzi kwani alifahamu chanzo cha mimi kupata daraja la tatu katika kidato cha sita na dada zangu kupata daraja la kwanza kwa yule waMzumbe na la pili kwa yule aliyeenda Tumaini,na wakati mimi nilikua mkali kuliko wao.



    Kikweli sababu ya mimi kupata matokeo mabovu kuliko dada zangu,ni kwa sababu nilichanganyikiwa sana na yaliyotukia kwa Generose. Hivyo baba hakutaka niingie tena kwenye mapenzi wakati nipo masomoni.



    Siwezi kuyasahau maneno ya siku ile hata kidogo. Japo kuna kipindi nilijidai nayasahau na kujitosa mapenzini tena, kitu ambacho kimefanya usome mkasa huu kama burudani kwa sasa. Lakini ni usahaurifu wangu ndiyo umesabisha haya yote.

    Kwa sasa siwezi kusahau, maana yamenifunza. Hakuacha kuniambia kuwa pale ni chuo,ndipo sehemu ya kuanza safari yangu ya kuelekea kuanza maisha ya kujitegemea, hivyo mambo ya usanii niyaweke pembeni na kujali zaidi masomo japo alijua mi kuacha hilo ni vigumu..

    **************





    Kulikuwa hakuna mtu anayefuatilia mambo ya mwingine pale chuoni. Mimi nikiwa na begi langu la nguo,niliamua kuweka earphone na kuanza kusikiliza muziki kutoka kwenye Ipod niliyopewa na shemeji yangu{mke wa kaka}baada ya kuvutiwa na uchezaji wangu siku ile ya tafrija.

    Sauti ikawa juu masikioni pangu hivyo sikusikia chochote cha duniani. Nikaanza safari yangu ya kwenda ofisini ambapo niliishia kwenye kupanga mstari uelekeao huko ofisini.



    Nikiwa nimesimama kwa muda mrefu sana kwenye mstari ule wa kuelekea ofisi ya usajili wa wanachuo, nilihisi kama naguswa begani, lakini nilipuuzia kwa kujua ni bahati mbaya mtu kanigusa.

    Akili yangu ikarudi kwenye ule mziki kutoka kwenye Ipod. Ghafla zile earphone zilitolewa masikioni mwangu na hapo ikafata sauti nzuri na tamu lakini ilikuwa ya msisitizo na maonyo juu yake.



    “Kaka haya madude yatakupeleka Muhimbili kutibiwa masikio,yaani husikii unachoambiwa wala hujui kinachoendelea duniani, na mbaya zaidi huhisi hata kama unaguswa. Kaka utaharibika masikio angali tunakuhitaji". Ni sauti ya mwanadada iliyopenya vyema masikioni mwangu baada ya kutoa zile earphone.

    Hakunipa nafasi ya kujitetea, moja kwa moja akaenda kwenye sababu iliyomleta.



    "Anyway, tuyaache hayo. Nakuomba kaka yangu unisaidie nisimame hapo mbele yako ili niende ofisini. Naumwa sana malaria kaka yangu. Nahitaji kufanya usajili nipate chumba ili nikajipumzishe maana hizi dawa zinavyonipelekesha, naweza kudondoka hapa. Nakuomba kaka yangu". Ilimaliza sauti ile nyororo na tamu, ambapo kwa muda wote aliokuwa anaongea niliutazama uso wake nadhifu, pamoja na midomo yake iliyotengenezwa kiustadi na Mheshimiwa MUNGU, ikipambwa kwa kutanuka na tabasamu ambalo kwangu lilikuwa kama ugonjwa uliovamia mishipa ya moyo wangu na kusababisha damu yangu itapakae tabasam lile la haja.

    Sikuacha kumsifu MUNGU kimoyo moyo kwa kuumba kiumbe kama kile ambacho kwangu kilikuwa kama pambo katika ubongo wangu.



    "Mambo vipi dada yangu.Naona umekuja moto kidogo,hadi umenitisha.Na usijali kuhusu haya madude,ni kwa leo tu!.Si wajua bado sijafahamiana na watu hapa chuo? Basi lazima nijiliwaze kwa hii kitu bwana". Ilinitoka sauti hiyo bila kikomo huku nikirudi nyuma kuacha upenyo wa yeye kuingia ili aelekee ofisini.

    Kabla hata hajasema chochote kwa msaada wangu, nikaanza kusikia kelele za kejeri na matusi zikitoka nyuma yangu.



    Kejeri zilikua nyingi sana kiukweli.Wengine waliniita mdhaifu kwa wanawake,eti nimelainika kwa sauti ya kike, na wengine walidiriki kusema najipendekeza.

    Kwangu ilikua si kitu juu ya maneno hayo.Nilichofanya ni kuzirudisha zile earphone mahala pake na kuendelea kufurahia mdundo wa muziki.



    Hilo likawa kosa hasa kwa wale wababe. Hawakusita kunifata na kuzitoa zile earphone masikioni na kuanza kufanya anayoyawaza.



    "We fala sisi tunakuambia ulichofanya siyo kizuri,wewe unajidai unafunga vioo si ndio eeh. Tupo hapa tangu asubuhi,we kirahisi rahisi unamuweka mtu asiyejua ata uchungu wa kusimama hapa. Unajidai msamalia mwema saana,si ndiyo eeh". Sauti ya mkeletwa mmoja iliingia sawia masikioni mwangu bila mikwaruzo wala uoga.

    Nilimuangalia vizuri jamaa yule na kugundua kuwa anapenda ubabe na fujo lakini siyo mwenye akili wala kujua thamani ya utu.



    "Hivi wewe, huyu kusimama hapa kakupunguzia nini? Dada wa watu anaumwa,licha ya kuumwa huyu hastaili kusimama kwa muda mrefu hapa,huyu mi ni kama mama yangu. Kaja na shida ndogo kama hii, acha nimsaidie. Hata kama na wewe unataka,unaweza kukaa mbele yangu". Nilimjibu jamaa yule huku nikijivuta tena nyuma ili aingie.



    Wanafunzi wana akili mbovu sana, hasa kwenye kutafasiri kauli za watu..



    "We fala umeniambiaje!? Una maana gani kuniambia nikae mbele yako? Unajidai unajua kiswahili sana si ndiyo eeh. Nitakuzingua halafu hii siku utaikumbuka hadi utapofukiwa ardhini". Jamaa alikuwa kagadhibika na kauli zangu na sasa macho yakamtoka na kutengeneza vibwawa vya hasira za machozi hali iliyosababisha macho kuwa mekundu kama salu la nyanya.



    "Kaka usimjibu,we muache au ngoja nitoke msije mkapigana bure kwa kitu kidogo tu!". Aliongea binti yule niliyempa nafasi asimame mbele yangu huku akianza kuchomoka kwenye ile nafasi.



    Nimvuta mkono na kumrudisha tena pale na kumwambia atulie na asijali, hakuna ugomvi utaotokea. Kisha nikamgeukia yule jamaa nikiwa na tabasamu la kizushi la kumuonesha siogopi kauli zake.

    Lakini kwa kuwa nimestarabika, sikutaka maneno mengi juu yake.



    "Poa bwana.Mi sitaki hii siku uifanye iwe sintosahau maishani mwangu. Kama umekerwa na nilichofanya,samahani sana. Natoka nafasi hii namuachia dada hapo. Mi naenda kuanza upya kule nyuma maana sioni kama nitapoteza kitu.

    Ila tafadhari, usiniongeleshe tena kwa sababu nitagairi na hutonifanya kitu". Kauli ikamuingia vyema yule jamaa na hapo nikawa natoka ile nafasi huku namuacha yule jamaa bila kauli nyingine kumtoka.



    "Mwanangu umetengeneza bonge la CV kwa mtoto,yaani bonge la CV ambalo sidhani kama wewe mwenyewe umegundua hilo. Yaani ningekuwa mimi pale,ningeacha hata anipige vibao ili CV yangu ikae vyema zaidi.Ujue kupigwa sababu ya mtoto mzuri kama yule ni bonge la sifa hilo,tena kwa kisa cha kipumbavu kama kile, yaani ni bonge la sifa".



    "Dah! Mwanangu wewe ni jasiri kinoma, yaani kusimama na jitu limeenda hewani vile kama kamba ya kujinyongea.Mh! Aisee, mimi ningetoa haja zote pale pale. Wewe kwanza licheki (huku anamuoneshea kidole yule jamaa), jeusii kama sijui limefukuliwa kwa mafuriko ya mkaa, yaani dah!,ngoja niache". Yalikuwa maneno ya wanachuo wawili niliokutana nao kule nyuma baada kutoka pale mbele nilipo kuwepo.

    Maneno yalionyesha kuwa walikubali kwa nilichokifanya lakini walikerwa na yule jamaa hasa kwa tabia zake alizo onesha.



    "Sikiliza mwanangu,ngoja nikupe picha lilivyoenda.” Jamaa wa kwanza aliongea huku akinishika bega kuonesha msisitizo. Akaendelea, “Yule manzi kaja hapa na kutuuliza sisi, eti ni nani tuna muona ana roho nzuri na anaweza kumuachia nafasi ili aingie ofisini maana yeye anaumwa malaria, na pale kameza vidonge,hivyo miguu yake haina nguvu pale. Ujue sisi tulimuambiaje?” Jamaa akatulia kama kusikilizia jibu, na bila kupata jibu akazidi kutirirka alichokiona.

    CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Tukamwambia yeye aanze mmoja-mmoja kwenye mstari hadi apate mtu mwenye moyo hiyo ampe nafasi". Akawa anaongea yule jamaa ambaye mimi nilimtungia jina kwa kumuita mzee wa CV.

    Mzee wa CV huku anaonesha vitendo vingi kwa mikono yake,akazidi kuendelea na huku mimi nikiwa nimepambwa na tabasamu kubwa usoni kwa sababu ya uchangamfu wa mzee wa CV na habari zake zenye wingi wa bashasha.



    "Basi yule manzi akaanza kwa lile Jangiri lililokutoa mstarini”.Hapo baada ya kusema hivyo nilishindwa kuzuia cheko yangu iliyomfanya Mzee wa CV kutulia kidogo akisubiri nimalize cheko yangu iliyotokana na jina alilomuita yule jamaa.

    Baada ya kuhakikisha nimemaliza kucheka, akaendelea.



    “Lile jamaa likamcheki tu usoni halafu likafyonza na kubetua midomo kwa dharau. Basi Manzi hakuchoka, akasonga hadi kwa kile pale kimbau-mbau.

    Si wajua videmu sura mbaya vinavojishaua vikiona mtoto mzuri anaomba msaada?. Basi kile kikarefusha lile domo likawa kubwa kuliko kichwa, vimacho vikamtoka kama kabanwa na haja kubwa. Basi na ndio kikaweka tege zaidi na vimiguu vyake vyenye makovu kama ndege iliyotoka vitani". Mzee wa CV aliendelea kushusha makombora kwa wale walio mnyima yule binti nafasi kiasi cha kutufanya wote tuliomzunguka kucheka tu! Na hakuishia hapo, akaendelea,



    "Kile kidada kifupi kama soksi zangu,akakipita.Na yule dada aliyerefusha kisogo kwa nywele,naye akapitwa. Akaenda kwa yule mchizi aliyekuwa nyuma yako.Mchizi nikaona anatabasamu halafu akamuoneshea Manzi ishara kuwa aje kwako.Wakati huo bado sisi tunacheki movie tu!.

    Mara akakugusa begani. Na wewe sijui hukusikia au sijui vipi, mwenyewe unajua. Basi manzi kwa aibu akacheki nyuma alipotoka, macho yote yanamuangalia yeye. Akicheki mbele,bado watu watatu halafu wote wanaonekana watata balaa. Ghafla akakutoa hizo earphone”. Hapo Mzee wa CV akagota na kuhamishia maneno kwangu kuhusu zile earphone.



    “Halafu wewe hayo sijui unavaa ya nini,yatakuua masikio ujue, yaani hayo yanakuharibu kabisaaa, bora uachane nayo". Niliitikia kwa kukubali ushauri wake na baadaye akaendelea na hadithi yake isiyo na jina.



    "Basi manzi sijui akawa anakuambia nini, wewe ukawa unamuangalia tu usoni. Sisi tukajisema leo mtoto mzuri kapatikana. Ila cha kushangaza, mzee sijui ulikuwa na wewe unamuambia nini huku unarudi nyuma kumpa nafasi manzi asimame.

    Hapo ndipo niliamini kuna watu wa ajabu duniani. Kwa mfano yule jamaa aliyekuwa nyuma yako, alimpokea kwa bonge la tabasamu lakini akamtosa. Ila wewe ulimcheki kikaudhu lakini ukampa nafasi, yaani hapo ndiyo nathibitisha kuwa uzuri wa mtu haupo nje bali ndani". Mzee wa CV alikuwa anaongea bila kutoa nafasi hata ya kujitetea.Kwangu kukawa tabasamu ndo limetawala muda wote wakati anaongea





    "Nilipokuona wewe ni mtata halafu disminder, ni pale ulipoweka earphone zako ili usisikie wanachosema. Aisee kaka,wewe ni mdudu wa sayari nyingine kabisa.

    Sasa kuna lile jamaa palee, lile jeupe kama papai. Lile ndilo lililokuwa chochezi halafu lina matusi hatari. Likawa linamchochea Jangiri ili akufuate na kukutemea mbovu.Nilikasirika kinoma, yaani mijitu mingine sijui vipi, UJINGA TU!". Mzee wa CV akamaliza maneno yake kwa sauti ya juu na ya hasira na kufanya wanachuo wengine wageuke kwa hamaniko la kutaka kujua kuna nini.



    "Mbona easy tu! wazee. Mimi sina kinyongo na mtu kwa sababu sijui leo kama itaisha au kesho kama nitainusa. Sasa kama nitamind vitu vidogo kama vile, vipi na mimi nikishikwa na jambo wakati huo yeye ndiye awezaye kunisaidia, embu fikiria itakuwaje? Jaribuni kufikilia nyie wenyewe.

    Haya maisha tu! Hayana ishu katika utu ambao nd’o kila kitu katika maisha ya mwanadamu. Dada wa watu anaumwa, yaani nimuache anaugulia maumivu hapa mstarini kwa sababu mimi nimekuja kabla yake? Hilo halipo wazee, yaani halipo hata kidogo".Niliongea hayo nikiwa na hasira kwa kitendo walichotufanyia wale watu pamoja na yule dada niliyempa nafasi.



    "Poa mwanangu, wewe tusubiri tuone maana manzi ndo kazama ofisini hivyo. Ila sikufichi mwanangu, pale umetengeneza bonge la CV mzee. Labda asiwe anajua thamani ya utu uliomfanyia ndiyo anaweza kukuzingua. Halafu nimekumbuka”.Mzee wa CV akawa kama amekumbuka jambo na kusababisha soga yake iendelee.

    “Pale manzi akawa anataka atoke mstarini,sijui alikuwa anataka aepushe shari au vipi. Mzee mwenyewe nikakuona umemkamatia mkono halafu ukamrudisha pale alipokuwepo. Daah! Yaani pale umechukua point zote tatu, yaani kama Man U vile.Bro wewe ni noma, nakuambia tena, wewe ni noma". Hakuchoka kuongea Mzee wa CV,wakati huo yule dada alikuwa kaenda ofisini kufanya yaliyomleta na baada kama ya dakika tano akawa anatoka..



    "Ehee mwana, manzi huyoo anatoka. Cheki mtoto anavyo kuangalia usoni na jinsi anavyotabasamu. Dah! yaani kama haumwi. Cheki mwanangu sura hiyo ilivyo “baby face”, kama Boyonce. Au ni Beyonce nini huyu sisi hatumjui?”.Mzee wa CV akawa anaongea hayo huku ananiuliza mimi swali ambalo hata sijui jibu lake.

    “Ee bwana ee,mtoto anakuja kwako.Yuwii mama yangu wee, dah! ngoja nikae kimya". Maneno yalikuwa yanamtoka mzee wa CV kwa kunong'ona wakati huo namuona yule dada anakuja kwangu kwa tabasamu pana usoni pake kana kwamba kweli alikuwa haumwi.



    "Dah!Aisee kaka sina cha kukupa zaidi ya kukwambia asante sana, yaani asante sana kaka". Alimaliza dada yule kutoa shukurani zake huku kanishika mikono yangu miwili kwa upendo au msisitizo, (hapo chagua mwenyewe,kati ya upendo au msisitizo, mi sijui nitumie neno gani kati ya hayo).



    "Aaah dada,huyu ndugu yetu tayari. Yaani kwa wema wote ule aliyokufanyia, kupambana na Jangiri hadi akaamua kuachia nafasi yake. Kweli unamshukuru kwa kumshika mikono tu!? Embu kuwa mzungu bwana". Mzee wa CV akaweka chombezo lake wakati huo mimi nikadhani mzee wa CV anataka yule dada anipe hela.

    CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Nikamgeukia yule dada na kutaka kumwambia aache,asinipe hela. Kumbe mzee wa CV anamuonesha matendo ya kufanya pale nilipompa kisogo. Bila kusita dada yule akazungusha mikono shingoni mwangu na kunibusu mdomoni.

    Nikawa nimeganda sijui cha kufanya baada ya tendo lile la ghafla. Huku pembeni likaamka shangwe kubwa lililoambatana na kelele, wengi wao wakifurahia lile tendo la dada yule kunibusu.

    Mzee wa CV akaenda mbali zaidi,akawa anashangilia huku anataja jina la msanii maarufu duniani jina ambalo wenzake walipolisikia na wao wakalifuata kwa kulitamka kwa zogo zaidi.

    Wakati huo nilimuona dada yule akitokomea kweye kundi la watu na baadaye kupotea kabisa sehemu ile. Huku akaacha yowe linaendelea kunisakama kwa kuitwa jina la msanii yule nguri wa Marekani.

    "Jay Z, Jay Z, Jay Z, Jay Z, Jay Z, Jay Z, Jay Z". Hilo ndilo jina lililokuwa linatajwa pale wakati huo,wakimaanisha mimi ni Jay Z na yule dada ni Beyonce.



    "Heee nyie, mmeshafanya hapa ni kilabu cha pombe, si ndiyo eeh. Embu waone kwanza, kama siyo wasomi wanaoenda kuanza degree,mshakuwa watu wazima nyie".Lile shangwe lilikatishwa hivyo na sekretari wa ofisi ile ya chuo.



    "Waambie hao dada maana tungeongea sisi wangesema ni wakorofi". Jangiri akawa kachangia mada kama mkereketwa wa kelele zile.



    "Tulia wewe, we si upo mbele na sisi tupo nyuma yako,tunachokufanya hutakiwi kulalamika wala kujua. Kama we ni mbabe basi hapa umekwama, tulikustahi ulipo mtukana mwana ila sasa hivi hatukuachi. Kuku wewe". Aliongea jamaa mwingine ambaye tangu nakuja pale ndiyo mara yangu ya kwanza namsikia, lakini alikuwepo kwenye kushangilia jina la Jay Z.

    Nikamuona Jangiri katulia kama mtoto aliyetoka kuogeshwa. Akakaa kimya akimsubiri sekretari aingie na huduma iendelee.



    "We kaka mwenye shati jekundu na jinzi la bluu,njoo huku ofisini". Sekretari aliniita na mimi bila kipingamizi nikaitikia wito.

    Ndani ya dakika tano nikatoka na risiti pamoja na funguo nne ambazo nilipewa kwa ajili ya kuwapa na wenzangu nitakao enda nao. Niligawa zile risiti na funguo kwa jamaa zangu wale watatu akiwemo Mzee Wa CV. Wengine nao wa kule nyuma, waliitwa ofisini kama mimi na kupewa funguo, hapo ule usemi wa nyuma aende mbele, ukatimia.



    Kilikuwa ni chumba pekee pale cha wanafunzi pale CBE chenye AC. Hivyo tulikuwa kama watu maalumu sana kukaa kwenye chumba kama kile. Jamaa zangu wale walifurahi sana, lakini shukurani nyingi zikaja kwangu kwa sababu wema wangu uliwapelekea kukaa chumba kile chenye hadhi yake pale chuoni. Wengi walinikubali kwa muda mfupi tu, sababu ya wema wangu.



    "Sasa Jigga,sisi sote humu tunajifahamu, ni wewe tu! uliye mgeni kwetu.Hapa wote tumetoka shule moja. Huyo jamaa aliyempiga mkwara Jangiri anaitwa Saint Justine Kinala au Saint JK, namkubali sana kwa kupiga Kung Fu,ila yeye atakuwa anasomea Marketing au Masoko kwa Kiswahili.

    Mkubwa hapo anaitwa Stephano Sungura, yeye atakuwa anasomea Uhasibu na mimi mwenyewe niite Christopher Jengo au usiumie sana mdomo,niite Chris, mi nitakuwa mambo ya Ugavi". Alimaliza mzee wa CV kutambulisha. Na sasa ataitwa Chris na siyo Mzee wa CV tena.



    "Mi' niiteni Frank Masai au Man'Sai ukipenda. Na mimi nipo na wewe Chris kwenye Ugavi na Manunuzi. Nashukuruni sana kuwafahamu wazee, na nadhani tutakuwa pamoja katika kuendeleza gurudumu hili la Elimu". Na mimi nikajitambulisha kwao.

    Kilichofata tukapeana namba za simu. Japo niliwaambia majina yangu,lakini hakuna aliyenakiri majina hayo zaidi ya Jay Z. Sikupinga,maana halikuwa jina baya sana.



    ******

    Mwezi ukapita na masomo yakaendelea huku jina la Jay Z nalo likawa ndiyo jina langu rasmi japo najua jina hilo halikuendana na mimi hata kidogo. Kisura Jay Z nilimuacha mbali sana. Licha ya hilo pia nilikuwa sijawahi kumuonesha mtu kuwa naweza kurap jambo lililowafanya watu wasiojua chanzo cha jina lile kushangaa na kujiuliza maswali mengi ya kwa nini mimi ni Jay Z.

    Tangu siku ile pale mstarini, sikupata kumuona tena yule dada ambaye sisi tulimuita Beyonce. Chris aliendelea kuwa rafiki yangu wa karibu sana, na yeye ndiye alikuwa analisambaza jina lile la Jay Z pale chuoni.

    *****************



    Nakumbuka ilikuwa Jumamosi moja moto sana pale chuoni.Watu walikuwa katika harakati zao binafsi,jambo lililofanya wanachuo wapishane kama wapo sokoni. Siku hiyo ndio ilikuwa siku maalumu ya kuwakaribisha wanachuo wapya pale CBE maarufu kama ‘WELCOME FIRST YEAR’.

    Shamra shamra zikikuwa zimepamba moto kila mahali nilipoweka uso wangu. Mapulizo na marembo mbalimbali vilirushwa angani kuonesha ishara ya amani inaendelea pale chuoni.



    Mida ya mchana wanachuo wengi walikuwa kwenye ukumbi maalumu wa Chuo wakimsikiliza Mkuu Wa Chuo akitoa mawaidha yake pamoja na sheria za pale chuoni na zaidi alisisitiza tujikaze sana kwenye Elimu zaidi ya mambo mengine hasa ya kidunia.

    Wengi walikuwa wanamsikiliza lakini wengi hao hao walikuwa wanatamani usiku uingie ili waende ukumbini ambapo sherehe ilipelekwa kule kwa ajili ya wanafunzi kuburudika kwa pamoja. Ukumbi wa KILIMANI ndiyo uliyo chaguliwa kwa ajili ya kufanya burudani hiyo huku wasanii kama TID na AY wakialikwa kwa ajili ya kutumbuiza.



    Kila mtu ana kichwa na akili zake na mawazo yake.

    Japokuwa wengi walikuwa wanajiandaa kwa ajili ya usiku ule mzuri, kwangu mimi ilikuwa tofauti sana. Nilikuwa sina haja wala hamu yoyote ya kwenda ukumbini. Akili yangu yote niliiweka kwenye somo la Uchumi ambalo kiukweli lilikuwa ni somo lililotesa wanachuo wengi sana pale CBE, ndio maana akili yangu siku ile ikajaa pale.

    Nilikuwa bize sana tangu saa kumi hadi muda ule wa saa moja jioni, na nilikuwa na mpango wa kuendelea hadi pale litakapoeleweka kwenye akili yangu.Chris aliliona hilo,kipindi mimi nasoma yeye alikuwa anajipanga kwa usiku huo hasa kimavazi.



    “Oya Jay Z,vipi mkubwa? We leo hauibuki nini pande za Kilimani”.Aliuliza Chris baada ya kuona sina habari kabisa na usiku hule..



    “Aaah, nyie nendeni tu, mi niacheni kwanza nimalize hili dude na nikimaliza nitalala,mtanisimulia ilikuwaje huko au siyo Jet Li?”. Nilimaliza hivyo kumjibu Chris huku nikimtania Saint Justine ambaye tulimuita Jet Li kutokana na sifa zake za kupigana na kuruka sarakasi huku nikikumbuka tukio moja lililotukuta mitaa ya Chako ni Chako huko Airport.

    Wakati tunatoka huko kupata chakula mida ya saa tatu na dakika kadhaa, usiku ghafla walitokea vibaka kama sita hivi lakini walikuwa wakiongezeka kadiri hali ilivyokuwa inawazidia.

    Saint Justine ndiye aliyekuwa anawadhibiti kwa kuwapiga mapigo ya nguvu, kisha baada ya kulegea vibaka wale alikuwa anawatupa kwetu na sisi tunaanza kuneemeka na kuwapora vitu vyao hasa hela na simu. Kiukweli sisi ndiyo tukawa kama wahuni lakini kiundani zaidi,wao ndiyo walituanza.

    Mapigano yale yalimalizika pale tuliposikia sauti za watu pamoja na gari za polisi zikija,na sisi tukaacha mapigano na kupotea eneo lile,wakati huo vibaka wote walikuwa hoi kwa kipigo chetu.



    “Dah! Jigga, hapo sasa unazingua kamanda wetu. Ujue kusoma ni haki ya kila mwanachuo hapa, lakini linapofika suala la muunganiko kama hili la leo, yatupasa nasi tufurahi pamoja kama ndugu wapya katika familia ya wanafunzi. Sasa kama kusoma kutakufanya usifurahie hata kidogo uwepo wa wanafunzi wenzako katika siku ya leo tu! Nitakuona wa ajabu Jigga”.Aliongea Saint maneno hayo ambayo kidogo yaliniingia akilini.

    CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Kweli kitu nilichotaka kufanya siku ile moja tu!, hakikuwa kizuri hasa kwa sababu ilikuwa ni siku moja na tena ni usiku. Lakini kama ningekuwa naona nitapoteza nini siku ile,nisinge thubutu kwenda kwani kwa usiku ule tu! Unaweza ukameza hata vitu vingi na kukusaidia kupata alama fulani katika masomo ya pale chuoni.



    “Dah!Mwanangu, unaongea hadi moyo wangu unataka kulia! Umeshinda kwa hilo, lakini si bado muda? Au ndiyo tunaenda saa mbili kama watoto wadogo kumuangalia AY na TID?”. Nilikubaliana nao kwenda lakini si kwa muda ule, mimi nilitaka zaidi twende saa nne na kuendelea. Na wale rafiki zangu walikubaliana na hilo na kunifanya niendelee kusoma hadi mida ya saa tatu na nusu nilipoenda kuoga.



    Nilipotoka nikavaa fulana yangu nyekundu imechorwa nyota moja halafu kwa chini yake kuna neno Converse lenye rangi nyeupe.

    Chini nikaweka raba nyeupe aina ya K.Swiss na jinzi ya bluu chapa ya Roca Wear.

    Siku hiyo kila mtu alitoka kivyake upande wa mavazi, lakini wote tulipendeza sana,yaani kama ni watu maarufu basi ungetuita G.Unit lile kundi la kina 50 Cent.





    Tuliingia Kilimani mida ya saa nne na nusu na tulikuta TID alishamaliza kufanya yake na AY ndiyo akawa anapagawisha mida ile wanafunzi wa CBE na wananchi wa kawaida waliyolipia mlangoni ili waingie.



    Sikuwa mpenzi sana wa kucheza muziki kwenye kumbi kama zile,yaani kifupi nilikuwa sijazoea na vilevile maonenesho ya wasanii wetu huwa na vurugu sana hasa msanii anapokuwa jukwaani.

    Hata AY alivyokuwa jukwaani watu walikuwa wamemzonga na wengine kushika kipaza sauti ili waimbe wao. Jambo lile lilitufanya tukae kaunta na kuangalia watu na mizuka yao.

    Japo ilikuwa kama vurugu lakini ilikuwa inaleta raha ndani yake, na utamu uliongezeka zaidi pale AY alipoanza kuimba wimbo wa USIJARIBU.

    Kila mtu hata wale jamaa zangu wote walinyanyuka na kuanza kucheza. Hapo ndipo nikaamini kutohudhuria matamasha, nilikuwa nakosa mengi.

    Baada ya kuucheza wimbo hule nikatoka nje kwenda kupata upepo maana joto nililokuwa nalo, halisimuliki.





    Zikiwa zimepita kama dakika ishirini tangu nitoke nje kupunga upepo,ndipo simu yangu ikawa inaita. Kuangalia alikuwa ni Chris. Nikabonyeza kitufe cha kupokelea na kuweka sikioni..



    “Oya Jay upo wapi?Njoo hapa kaunta mwanangu, kuna bonge la tukio linaendelea humu ndani, fasta mwanangu usije kujilaumu”.Alimaliza kuongea Chris huku sauti yake ikija na kelele za ukumbini mle.

    Nikanyanyuka pale nilipokuwa nimekaa na kuelekea ukumbini na moja kwa moja nikaelekea kaunta na kuwakuta wakina Chris wakiwa hawaamini kinachoendelea pale ukumbini.



    “Eee bwana Jigga, ona jamaa anavyochukua maujiko pale jukwaani”.Aliongea Stephano,yule jamaa mwingine tunayekaa naye chumba kimoja.

    Watu walikuwa chini ya jukwaa wakishangilia huku pale jukwaani alikuwepo yule jamaa aliyenitoa kwenye mstari mwezi mmoja uliopita,sisi tulikuwa tunamuita Jangiri.

    Jamaa alikuwa anavunjika na kucheza mwili mzima kama hana mifupa kitu kilichoonesha kuwa pale ukumbini hakuna kama yeye.



    Ilikuwa ni kweli, pale ukumbini kulikuwa hakuna awezaye kufanya vile kwa wakati ule ambao mimi nilikuwa nje na ndiyo maana hata jamaa zangu walikuwa wanashangaa yale yanayoendelea kujili.

    Niliwashangaa sana jinsi walivyokuwa wana hamaki jamaa anavyoranda pale jukwaani,lakini nilijua ni kwa sababu walikuwa hawajui kuwa mimi mwenyewe ni mkali wa mambo yale,tena yule aliyeyasomea sehemu maaalum (Bagamoyo).



    “Yaani Chris unanitoa nje kwenye upepo wangu mwanana ili nije kumuona Jangiri anavyojigonga gonga jukwaani?. Ha ha haa, embu ona anavyo jikakamaza kama mwana-mazingaombwe anasubiri gari lipite juu yake”.Nilikuwa naongea huku nimebetua midomo yangu kwa juu, na kuonesha chuki na dharau kwa akifanyacho Jangiri pale jukwaani.



    “Aaa Jay, tuache chuki na bifu za kijinga bwana. Mshikaji anaweza,hiyo usibishe Jay. Ni halali yake kuvuta mashabiki namna ile. Jamaa anafanya mambo ambayo hata Michael Jackson akimuona atamchukua. Embu ona mikono anavyocheza nayo,kama nyoka vile”.Stephano akawa anampamba Jangiri kwa kupinga kauli niliyoongea.



    Tukiwa bado tunaendelea kujadili anachofanya Jangiri,ghafla mshereheshaji (MC) aliongea kwenye kipaza sauti ya kuwa yeyote awezaye kwenda kupambana na Zaganda Mrwanda aende pale jukwaani huku akitangaza dau la shilingi laki moja kwa atakayekuwa mshindi.



    Kauli ile ya MC ilifanya ukumbi mzima kutulia kwa muda na kusubiri mpinzani wa Jangiri ambaye sasa tulimtambua kuwa anaitwa Zaganda Mrwanda aende kupambana naye.

    Zaganda akiwa pale juu alikuwa anajipiga piga kifuani kwa kujigamba huku akionesha kidole cha shahada hewani akimaanisha ni yeye pekee,yaani hana mpinzani pale ukumbini.



    Kwa jinsi nilivyokuwa namchukia Zaganda kwa aliyonifanyia mwezi ule uliopita,nilijikuta nachomoka bila kuwapa taarifa wakina Chris ambao walibaki midomo wazi na maswali mengi vichwani huku majibu yake wakidhani naenda kumfanyia vurugu Zaganda.

    Bila kutegemea kwenye masikio ya wengi walisikia MC anatangaza mpinzani wa Zaganda ni Man’Sai au maarufu pale chuoni kama Jay Z,hiyo ni baada ya mimi kwenda na kumwambia afanye hivyo.

    CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Hatimaye Zaganda kapata mpinzani bila kutegemea. Anaitwa Jay Z, mwana Ugavi huyu na ni kijana wangu pia,yaani mimi ndiye CR wake”.Tangazo lilitoka na mimi macho yangu yote nilimuelekezea Zaganda Jangiri ambaye alikuwa amebinjua midomo yake kwa kuiweka upande, yaani alikuwa ananidharau kwa kuwa alidhani siwezi kumfanya lolote pale jukwaani.



    “DJ weka mambo tuone kati ya Ugavi na Uhasibu nani ataondoka na huu mshiko kwenye bahasha”.MC alitoa ruhusa ya mpambano kuanza kati yangu na Zaganda,ambaye muda wote alikuwa haishi tambo pale jukwaani.

    ***

    DJ alianza kwa kusugua CD kama kachanganyikiwa. Na hapo hapo bila kulaza damu huku nikionesha dhamira ya kuua ufalme wa muda mfupi aliouchukua Zaganda, nilianza kucheza huku nafuata ile misuguo ya CD. Ukumbi ulikuwa hauamini tangu nilipopanda pale jukwaani hivyo hadi naanza kucheza ukumbi bado ulikuwa kimya wengi wao wakidhani sitoweza.



    Acha kabisa,sijui lile yowe nani alilipiga,yaani hadi sasa hivi mpenzi msomaji,sijajua nani aliongea vile.Ukumbi ulikuwa kimya kabisa wakiangalia uwezo wangu,ndipo ilitoka sauti moja kali sana huku ikipiga kelele yenye maneno ya chuki.



    “Jay Z muue huyo Mnyarwanda mweusi kama moshi wa tairi”.Maneno hayo sasa ndiyo kama yakawaamsha wananchi wote waliokuwa ukumbini na kuanza kushangilia kwa nguvu zote. Na mimi sikuwa nyuma baada ya hamasa ile,huku napo kwa DJ misuguo ikazidi kuongezeka.

    Nilizidi kucheza kwa kuvunjika bila kumpa nafasi Zaganda ambaye alikuwa anakuna kidevu chake ambacho kilikuwa hakina hata malaika wa ndevu,alikuwa ananishangaa mambo niliyokuwa namfanyia.



    Muziki ni kama uchawi,kuna hali fulani unakuwa nayo wakati wimbo uupendao unapokuwa unaingia masikioni. Na kama unapenda mziki,basi utapenda vyote vilivyokuwamo katika wimbo huo.



    Bila kusita, DJ akaweka wimbo fulani wa Usher Raymond unaitwa My Way.

    Hapo nilimuona Zaganda akiingia kwa mbwembwe za kuruka sarakasi ambazo alikuwa hasogei mbele wala nyuma,yaani alikuwa anatua hapo wakati anaziruka sarakasi hizo.Na pale alipoamua kuacha kuruka sarakasi hizo, aliruka hewani na alipotua chini, alitua huku kapiga msamba mmoja ambao sidhani kama ukiwa hauna mazoezi, utaupiga. Hapo ukumbi mzima ulibadilisha muelekeo wa kushangilia, na jina lililotajwa midomoni mwao lilikuwa ni Zaganda.



    Huku bado midomo ya mashabiki ikitaja jina la Zaganda na mimi nikaingilia wimbo ule ule wa Usher lakini mimi niliingia kwa sarakasi ya kutembelea mikono. Nikaenda hadi katikati ya jukwaa kisha nikatua kichwa changu chini,hivyo nikawa kichwa juu miguu chini.

    Nikatanua miguu yangu na kuonekana kama nimepiga msamba juu kwa juu. Kisha kwa kasi nilianza kuzunguka kwa kichwa (Spin) na kufanya nionekane kama feni pale jukwaani.



    Ukiwa msanii ukae ukijua kuwa washabiki siyo watu wazuri hasa wakiwa kwenye burudani. Lakini ubaya wao hauna madhara katika kazi ufanyazo.

    Nasema haya kwani baada ya tendo lile la mimi kucheza pale jukwaani, lilihamisha jina Zaganda midomoni mwao na kisha jina Jay Z likatawala tena vinywa vyao.



    Nikiwa bado nazunguka kwa kichwa pale jukwaani huku DJ akiwa makini kabisa na kazi yake.

    Niliposimama kuzunguka, basi nao mziki ukasimama huku nikibaki nimesimamia kichwa.

    Nilikutanisha miguu yangu na kunyooka kabisa,kisha nikaanza kuipeleka miguu ile kulia na kushoto huku kazi hiyo nikiacha kiuno changu iifanye.

    DJ naye hakuwa nyuma, alikuwa anaweka makorombwezo fulani ya kusindikiza lile tendo.



    Nilipoona nimeridhika kwa tendo lile, niliachia mikono yangu yote na kubaki nimesimamia kichwa peke yake,hiyo ilifanya kichwa kikose balansi. Hapo nilijiachia mzima mzima na kujidondosha pale jukwaani na wakati huo nadondoka,DJ aliweka mlio kama wa bomu kwenye makorombwezo yake, hivyo kuufanya ule mdondoko wangu kwenda sawa na mlio ule wa bomu.



    Hapo ukumbi mzima ulilipuka kwa yowe kubwa na la kutishia amani kwa yule ambaye hajui ni nini kinaendelea wakati ule mle ukumbini. Ilikuwa ni furaha tosha na burudani kwa yeyote aliyekuwa anashuhudia mambo yanayoendelea.



    Ni kama dakika mbili ilifanya nifanye hayo yote,na niliposimama kumuangalia Zaganda nilimuona katoa macho yake huku akiwa kama haamini yanayoendelea kujiri kwa wakati ule.



    Huku kila mtu akiwa anaamini nishammaliza Zaganda,DJ akaweka wimbo mwingine ambao nao ulikuwa na mahadhi ya kucheza. Bila kutegemea,nilimuona Zaganda akiingia kwa ari mpya ambayo kila mtazamaji alipendezwa sana na ujio ule.



    Alikuwa anaingia jukwaani huku anaterezesha viatu vyake kama Michael Jackson na wakati huo alikuwa anatunisha kifua chake mbele na kukirudisha nyuma hasa upande wa kushoto na kuufanya ule upande uonekane kama moyo ndiyo unaodunda,na wakati huo mdundo wa wimbo ule uliowekwa ulizidi kuongeza upendezaji wa mtindo ule aliyoingia nao Zaganda



    Zaganda alipoacha kucheza na wimbo nao ulisimama,kisha Zaganda akaniangalia pale nilipo,akatabasamu na kuanza kunifuata huku DJ nilisikia akiweka wimbo wa Hoi uliyoimbwa na WAKILISHA lile kundi la akina Langa au kwa jina lingine wanaitwa ‘Coca Cola Pop Stars’.

    Kwa ule mtindo aliokuja nao hata mimi nilimpigia makofi, kwa sababu alikuwa anakuja huku shingo yake anaizamisha ndani na kuivuta kwa juu tena. Na wakati mwingine alikuwa anairefusha na kusababisha aonekane kama mdudu fulani ambaye siwezi hata kumtaja.

    CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Ukumbi mzima ulikuwa umelipuka kwa shangwe na furaha kwa kitendo kile. Zaganda alipojua kavuta wengi kwa mtindo ule, akaubadilisha kwa kuuboresha zaidi.

    Alikuwa anajivuta huku kainama na kuupandisha mgongo wake juu na kuushusha chini. Yaani ukimuona hivi,unaweza kusema ni ngamia lakini akirudisha ule mgongo,waweza sema ni nyoka jinsi alivyokuwa anajivuta. Basi hapo ni ukumbi mzima unatoa mayowe na mbwembwe za DJ ndizo hasa zilizokuwa zinafanya Zaganda azidi kupata kichwa.



    Kwa mwendo uleule wa ngamia na nyoka,Zaganda akanifikia kisha akasimama wima wakati huo na DJ naye akasimamisha wimbo.

    Zaganda akawa kama ananikagua,alipomaliza akageuka nyuma kama wafanyavyo wanajeshi.Akapiga kwata la mguu pande na mguu sawa, kisha akaanza kurudi alipotoka kwa mwendo ule wa haraka wa kijeshi lakini kwake ulipendeza zaidi. DJ naye alikuwa ameweka nyimbo ya kijeshi iliyomfanya Zaganda aongeze mbwembwe kwenye ule mtindo wake anaoufanya.



    Alipofika mwisho akasimama tena na kuwageukia washabiki na kuwapigia saluti, na baada ya kufanya hivyo alinigeukia mimi. Akaigeuza mikono yake na kuwa kama ameshika bunduki.

    Akafanya kama anakoki risasi kwenye bunduki ,wakati huo DJ naye alikuwa anatoa milio ya kukoki bunduki.Baada ya ule mlio wa kuikoki bunduki,nilisikia milio ya risasi zilizokuwa zinatoka kwenye spika za ukumbi ule, yaani ilikuwa ni kama vitani. Nilipomuangalia Zaganda alikuwa kama ananitupia mimi zile risasi kwa kutumia mikono yake ambayo aliigeuza na kuwa bunduki. Hakika alikuwa anavutia kwa mtindo ule.



    Nilitabasamu tu!Huku natikisa kichwa kushoto na kulia kama nasikitika vile.



    “Yo yo yo,tumeona muvu za kutosha sana usiku huu wa leo na ninaona tayari kuna mmoja kama kakubali vile.Lakini siyo mbaya endapo nitawauliza wenyewe kama wanataka kuendelea au mpambano uishie hapa”.MC alianza kuongea baada ya Zaganda kumaliza ile kazi yake. Akamfata Zaganda na kuanza kuongea naye.



    “Ehee,Zaganda Soldier,nimeona jinsi ulivyomteketeza adui wako hapa mwishoni. Unasemaje au unamwambiaje mpinzani wako?”.Aliulizwa Zaganda.



    “We mwenyewe si unaona? Mpinzani kishakufa hadi sasa hivi. Cha msingi wachimba makaburi wafanye kazi yao na wachonga majeneza waalikwe kwenye tenda ya kumtengenezea jeneza huyu marehem akapumzike kwa amani”.Aliongea Zaganda na kufuatiwa na shangwe kubwa sana kutoka kwa washabiki.



    “Oiy,oiy. Mi sisemi chochote hapo. Ngoja niende kwa Jay Z”.Aliongea MC huku anakuja kwangu.



    “Ehee,Jay Z kaka,nimeona muvu zako mkubwa,lakini yaonekana kama umekubali vile Zaganda Soldier kukubwaga”.Aliongea MC baada ya kufika pale nilipokuwepo.

    Nikiwa na tabasamu pana usoni kwangu,nikafungua kinywa changu na kuanza kuongea.



    “MC siyo kila pongezi zina maanisha mtu kakubali kushindwa.Jamaa kafanya vizuri hilo sikatai na kwa kuwa kadhamiria kunishinda, basi na mimi nitamuonesha jinsi navyopambana kiume. Yote aliyoyaona nyuma,ni ya kitoto tu! Sasa namfundisha adabu na kila akiniona aseme shikamoo baba”.Kelele zilizotoka hapo baada ya kauli ile,sidhani kama Rais angekuwepo kungesikika kelele kama zile kutoka kwenye umati ule.

    Watu walikuwa kama wamepagawa baada ya kauli ile,wakati huo nilimuona Zaganda akiwa anaruka ruka kama bondia asubiriaye mpambano kuanza.



    Nikiwa bado karibu na MC, DJ akaweka mambo kwenye mitambo yake. Sikufahamu ilikuwa ni kitu gani alichoweka lakini ulikuwa ni mdundo wa muziki ukiwa tupu yaani beat (Instrumental) kwa kiingereza.



    Ilikuwa inachezeka sana ile beat,na hapo Zaganda aliniwahi kwa fujo na manjonjo mengi kama kawaida yake. Safari hii alikuwa anaranda kwa mgongo na saa nyingine alikuwa anatembelea tumbo.



    Kwa kuwa MC hakuwa mbali na mimi,nilimpora kipaza sauti na kisha nikaanza kurap au kufoka-foka kupitia biti ile huku nikiimba juu ya kile kinachotokea pale. Hapo ukumbi ulibadilika na kuwa kama uwanja wa mpira baada ya goli kuingia. Mimi nilikuwa nafoka-foka halafu Zaganda yeye alikuwa anavunja anavyojua.



    Nilizidi kumpa mizuka au hamasa Zaganda ya kuendelea kufanya yake pale jukwaani. Ilifika kipindi nilikuwa nataja jina lake kwa fujo sana kama wale waimba Ragga,na yeye ndiyo kama alichanganyikiwa baada ya kusikia sauti yangu ikilitaja jina lake kwa fujo. Alizidi kujinyonga na kujinyongorota pale jukwaani kwa dakika kama saba hivi,halafu DJ alikata ile beat.



    Hapo ukumbi mzima ulikuwa unasikika jina la Jay Z kana kwamba alikuwapo pale. Na bila uchoyo,Zaganda aliniangalia na kunioneshea dole gumba na kutikisa kichwa chini na juu kuonesha kuwa alikubali kazi niliyoifanya muda mchache uliopita.



    Nilipoangalia kwenye vyumba vya wageni,niliwaona AY na TID wakiwa kama hawaamini jambo ambalo lilikuwa limejiri wakati ule.

    Wakati bado naendelea kupepesa macho yangu hasa kwa mashabiki,niliweza kuona sura kama ya yule dada ambaye nilimpa nafasi kwenye mstari mwezi mmoja uliopita.Lakini fikra zile zilikatishwa na wimbo wa Rihanna uitwao Pon De Replay. Hiyo ilikuwa inamaanisha ni zamu yangu kuingia na kutoa burudani.

    CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Muziki ni kitu kingine ambacho ukikielewa na kikakukaa mwilini na akilini, basi chochote utakachokifanya, kitakuwa unakifanya kwa sababu ya muziki.



    Wakati ule wimbo unaendelea kwenye spika za ukumbini,na mimi niliingia kati kwa kutembea kama roboti huku bado nikiwa nimeshika kile kipaza sauti na viungo vyangu vya mwili,vilionekana kama havina nyama yaani vimebaki mifupa tu!.

    Mtindo ule wa kucheza unahitaji pumzi kubwa wakati unaucheza,na vilevile unahitaji mwili wa mazoezi kwani wakati unafanya yale mambo ya kiroboti,ni lazima muda mwingi uwe umebana pumzi na kuukakamaza mwili.



    Nilienda hadi kwa Zaganda kwa mtindo uleule wa kiroboti,kisha nikaanza kumfanyia vitendo vya ajabu-ajabu kwa mtindo ule. Baada ya kuridhika,niliwageukia mashabiki na kuanza kuwaonesha jinsi gani nimepewa kipaji maalum cha kucheza hasa kama roboti.

    Nilipomaliza kwa washabiki niliamua kumpa pigo la mwisho Zaganda,pigo ambalo kwa kila mshindani aliyepambana na mimi hapo kabla,nikimpa pigo lile ni lazima akubali kuwa kashindwa.



    Nilimgeukia Zaganda na kisha nilikaa chini na kuikunja miguu yangu na kuwa kama nasubiria chakula. Baada ya kukaa hivyo,nilijipindua kiustadi na kusimamia kichwa changu kisha nikaachia mikono yote na kugeuka kwa kumpa mgongo Zaganda.



    Halafu nikaanza kurudi nilipotokea kwa kutembelea kichwa vilevile. Nilidunda dunda kwa kichwa kama hatua tatu,kisha nilinyoosha miguu yangu na kuuacha mwili udondoke mzima mzima.

    Baada ya kudondoka niliinukia mikono kwa mtindo kama wa kupiga “push up” na bila kuchelewesha nilijikunja miguu yangu na kuonekana kama vile nge, wakati huo nilikuwa nimeweka kidevu kama msaada kwangu ili nisiharibu ule mtindo wangu.



    Baada ya kuridhika na mtindo ule,niliinuka na kusimama wima na kuanza kuruka sarakasi nyingi na zisizo na idadi na baadae nilijiachia kwa kuruka juu zaidi angani ambapo huko niliranda kama mara tatu na nilipotua chini, nilikuwa nimetua huku nimesimama nimechana msamba wa hatari.



    Baada ya hapo nilimuoneshea ishara ya bastola kwa kutumia vidole vyangu nikiimaanisha nimemuua Zaganda.

    Nilikuja kushtuka nikiwa nimebebwa juu-juu na wahuzuriaji waliofika mle siku ile, wengi wao wakiwa wanachuo. Jina lililotajwa vinywani mwao lilikuwa ni Jay Z.

    Walikuwa wananirusha juu juu na kunidaka kama vile nilikuwa tayari nimeshinda.

    “Zaganda umeona Ugavi ilivyonyanyuliwa juu?Vipi? Una cha kusema hadi hapo”.MC aliingia kwa maneno hayo kumuelekezea Zaganda.

    Zaganda huku akitabasamu na kutoamini kilichotokea,akajibu swali la MC.



    “Kaka mpe chake tu! Sina ujanja hadi hapo.Alichofanya leo ni zaidi ya Usher Raymond au Chris Brown. Mpe laki yake akajipongeze. Hongera Jay, nimekukubali”.Baada ya maneno yale ya Zaganda lilitoka shangwe la kufa mtu,na kwa kuonesha kuwa kulikuwa hakuna kokoro kwa ushindi ule,Zaganda alipewa kiasi kile cha hela na kuja kunikabidhi ambapo pia alinikumbatia kuonesha upendo baina yetu.



    AY na TID nao walijichanga na kunipa laki mbili,na Zaganda wakampa laki moja kama kifuta jasho huku wakituahidi kutuita katika kazi zao za kisanii ili twende kurembesha jukwaa kwa kucheza kwetu.



    “Umemuua Jangiri Zaganda, Jay. Umemuua kaka.Amekufa yule,hana jipya,ha ha haaa”.Yalikuwa maneno ya wale jamaa zangu hasa Chris baada ya mimi kushuka jukwaani.



    Lilikuwa ni tendo kama la saa moja na nusu pale jukwaani,lakini burudani iliyotoka pale,sidhani kama imesahaulika pale chuoni.Na hapo ndipo jina la Jay Z likawa juu zaidi ya mara ya kwanza kwani sasa walishajua kuwa naweza kufanya hata muziki wa kufoka foka au rap kwa kiingereza.

    ***

    Nikawa najiongezea umaarufu pale chuoni kwa kufanya mitindo huru (freestyle) . Na mara kwa mara nilikuwa nahamasisha wanachuo wenzangu kwa kupitia muziki niliokuwa naufanya. Halikadharika,nilikuwa napata mialiko mbalimbali kwa ajili ya kusherehesha au kutoa ujumbe kupitia kazi zile za kisanii.



    Pia niliweza kufanya kampeni ya Rais wa chuo ambaye alitoka kwenye mwaka wetu.Na alipopata madaraka aliweza kunifanya kuwa Spika wa chuo huku Zaganda yeye akipewa uwaziri mkuu.

    Hayo ndiyo yakawa maisha yangu ya chuo kwa mwaka wa kwanza, huku nikijipatia umaarufu kwa muda mfupi kwa kupewa jina la Jay Z.



    MWAKA WA PILI CHUONI.



    NILIENDELEA kuwa maarufu pale chuoni hadi mwaka wa pili ulipoingia.Mwaka wa kwanza sikufanya vizuri sana katika masomo yangu jambo ambalo nilihisi ni sababu ya kujihusisha zaidi na mambo ya kisanii zaidi ya mambo ya kitaaluma ya pale chuoni hasa kusoma.

    Fikra hizo zilinifanya niachane na yale mambo ya kisanii na sasa nikajikita zaidi kwenye masomo ya pale chuoni ambapo kila rafiki yangu aliunga mkono suala hilo na kuliona ndilo la muhimu zaidi.



    Mwaka ule wa pili nilitoka katika makazi ya chuo (HOSTEL) na nikaenda kupanga chumba maeneno ya Makole tukiwa mimi na Chris. Tukaanza maisha kama watu wa kawaida huku tukiwa pamoja na bega kwa bega na wale rafiki zetu wengine.

    CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Maisha yalikuwa mazuri huku jina Jay Z ndilo lilikuwa vinywani mwa kila mwanachuo pale chuoni. Sikuweza kuonana na dada yule niliyempisha kwenye mstari wa kuingilia ofisini mwaka uliopita hadi kipindi hicho japokuwa nilikuwa maarufu sana pale chuoni.

    Tangu lile busu alilonibusu na kuunda jina la Jay Z,dada yule hakuweza kunitafuta wala mimi sikuwa na mpango huo.



    *****



    Katika harakati zangu za kusoma,tulifanikiwa kuunda kundi la majadiliano ya masomo lililokuwa na watu sita. Kundi lile lilitishia sana amani ya masomo katika mwaka wetu kwa sababu kila somo katika mwaka ule lilipata mtaalam wake,huku mtaalam huyo aliweza kutufundisha na sisi tukamuelewa zaidi ya tulivyomuelewa mkufunzi wa somo lile.



    Tukawa moto wa kuotea mbali katika masomo ya pale chuoni,na kila somo sasa kwangu mimi lilikaa kichwani vizuri sana.



    Katika vikundi vingi sana vya kujisomea,iwe chuoni au sekondari ni lazima kutakuwa na hadithi za maisha baada ya kumaliza kusoma. Lakini kiundani zaidi ukifuatilia hadithi hizo huwa ni za mapenzi. Basi hata kwenye kundi letu hayo mambo yalikuwepo.



    Mara nyingi huwa nikisikia hadithi hizo, basi naaga kwa kusingizia kitu fulani kwa sababu nilikuwa sipendi sana kuzungumzia habari za mapenzi, na zaidi nilikuwa nakwepa maswali yao ili wasiniulize historia yangu ya nyuma ya mapenzi ambayo kiukweli ilikuwa inaniumiza sana hasa pale nilipokuwa naikumbuka.



    Nilifanikiwa kukwepa hilo suala kwa muda,lakini siku moja baada ya kumaliza kujisomea Chris Mcharuko kama wengi walivyomuita pale chuuoni,alianzisha hadithi hizo na kabla sijaaga aliniwahi na kuniulizia juu ya mahusiano yangu ya mapenzi.



    “Hivi Jay,mbona tangu tumeanza hapa chuoni kusoma,sijawahi kuona wala kusikia kama una demu?”Chris alianza kuongea huku anacheka cheka,akaendelea.



    “Yaani hata usiku,mimi naongea na demu wangu lakini wewe sijawahi kukusikia hata mara moja ukiongelea mapenzi kwenye simu. Mara nyingi huwa nakusikia unasema msalimie mama,sijui shangazi mara unasema asante baba,yaani sikuelewi mshikaji wangu.Embu leo tupe undani wa historia yako ya mapenzi”.Yalikuwa ni maneno ya Chris ambayo yalinifanya nikae tena huku kundi zima likiwa kama lina hamu ya kutaka kusikia kitu kutoka kwangu baada ya ombi lile la Chris.



    “Hayo mambo yana wakati wake jamani.Mapenzi na masomo ni kama petrol na moto.Mara nyingi huwa ni dhoruba na majanga pale vinapokutana.Kifupi napenda sana kuwa peke yangu na sihitaji mtu wala mwanamke katika maisha yangu. Na kama hamjui,nitakufa nikiwa single, hayo ndiyo maisha niliyoyachagua”.Niliongea hayo huku nikiwa sina hata chembe moja ya utani kama walivyonizoea.



    “Masai sikiliza. Haya maisha tu mdogo wangu na usije ukaweka rehani na kiapo kuwa hutokuja kupenda tena,kwa sababu ukisema hayo siku moja utakuja kujutia kauli yako hasa pale utakapokuja penda tena”.Hapo aliongea kaka mmoja aitwaye Solomon Maganga ambaye alikuwa ni mtu wa makamo mwenye miaka kama ishirini na nane au thelathini.



    Solomon alikuwa hapendi sana kuniita jina la Jay Z kutokana na umri wake kuwa mkubwa na mambo ya ujana yalishampa mkono,hivyo alipenda sana kuniita jina langu halisi hasa la ubini wangu(MASAI). Hakuishia hapo,akaendelea.



    “Mapenzi hayana muda hata siku moja.Mapenzi naweza kuyafananisha na maji kwangu mimi,hata usipokunywa utayaoga,na usipoyaoga utayapikia tu!.Cha msingi Masai ni kujipanga jinsi ya kucheza nayo. Ukijikita sana kwenye hayo mapenzi kuliko masomo,ni kweli itakuwa ni moto kukutana na petrol,ni lazima upotee”.Aliongea Solo huku maneno hayo yakiungwa na karibu kundi zima.

    Nilimuheshimu sana Solomon kwa sababu kila alipokuwa anafumbua mdomo wake kuongea,alikuwa anaongea kitu cha maana na chenye mguso.



    “Labda nilikosea kuongea kuwa sitopenda tena. Kaka Solo,pale naposema kuwa nitakufa single nina maana yangu.Mapenzi mimi yameniumiza sana,mimi nilikuwa siyo mtu wa kupata three ya mwanzoni bali one ya kwanza. Lakini haya yote ya kupata three yalitokea kwa sababu ya mapenzi. Mpenzi wangu niliyempenda aliondoka mikononi mwangu wakati grafu ya upendo kwangu ilishagusa juu kabisa”.Nilikaa kimya kidogo na kuugulia maumivu baada ya kukumbuka yaliyonitokea nyuma. Nikameza fundo la mate lililokuwa kooni mwangu na kuendelea kuongea.



    “Sababu ya mapenzi,mimi nikawa kama kichaa,mimi nikawa mlevi wa vinywaji vikali zaidi ya mwili wangu.Bangi zikawa na mimi,fujo na maovu yote mtaani na mimi nilikuwepo.Haikuwa hadithi ya kushtua pale taarifa ilipotoka kuwa nipo polisi. Leo hii mnaniambia mapenzi sijui ni kama maji,hiyo hamna kaka.Upendo kwa wazazi wangu,ndugu zangu na nyie rafiki zangu wanitosha sana”.Niliongea kwa hisia maneno hayo na kuna kipindi nilikuwa nagonga kifua kuonesha ni kiasi gani mapenzi kwangu yaliniumiza.



    “Masai kaka.Unatakiwa kusahau ya nyuma na kuangalia yaliyo mbele yako kwa sasa. Unapoumia moyoni ndipo pia unapopata elimu ya maumivu. Kamwe usipende kupata furaha pekee katika maisha yako,karibisha na maumivu pia ambayo ndiyo hasa yanayoweza kukupa ujasiri wa kukubali ufanyacho. Hapa namaanisha jifunze kupokea furaha na huzuni katika mzunguko wako wa maisha”.Alikuwa anaendelea Solo kutoa ushauri kwangu.

    CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Mimi mwenyewe nimeumizwa sana kwenye haya mapenzi,lakini sikuchoka kupenda bali kuzidi kumuomba MUNGU ili anipatie mtu bora na atakayenifaa katika maisha yangu. Na sasa nipo na Silvia wangu{Akamgeukia Silvia na kumbusu shavuni}. Namshukuru MUNGU ananipenda,ananithamini na ananiamini sana. Na kwa uwezo wake MUNGU,tutajenga familia iliyobora kabisa”.Solomon aliendelea kusisitiza kauli yake huku akitolea mfano maisha yake.





    Itaendelea

0 comments:

Post a Comment

Blog