Search This Blog

Wednesday, 1 June 2022

MAWIO NA MACHWEO - 2

 







    Simulizi : Mawio Na Machweo

    Sehemu Ya Pili (2)

    CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/



    “Kifupi Kaka Masai,wewe jipe moyo na kuacha akili yako ili relax na iwe tayari kumfikiria mtu mwingine.Handsome kama wewe huwezi kukaa single maisha yako yote. Kumbuka kuwa baba na mama yako watapenda kuitwa bibi na babu kutoka kwenye mwili wako. Wakati huo dada,kaka na rafiki zako kama sisi, tutataka kumjua wifi au shemeji yetu na kuwanunulia watoto wako pipi na mapulizo.Embu ona thamani ya haya yote Kaka Masai.Achana na mambo ya kujikatisha tamaa”.Aliongea Silvia ambaye alikuwa ni mchumba wa Solomoni ambaye naye alikuwa ana umri kuanzia miaka ishirini na saba hadi ishirini na tisa.



    Silvia na Solomon walikuwa wana hekima sana katika maongezi na mambo yao kitu kilichonifanya niwapende sana na kuwa nawashilikisha hadi mambo yangu ya ndani ambayo hata Chris nilikuwa simwambii japo ndiye alikuwa rafiki yangu mkubwa na wa karibu sana.



    “Mimi hapo Jay siingilii hata kidogo.Nadhani unapata mengi sana kutoka kwa wakubwa zetu.Lakini mimi na swali,maana umeongea jambo moja kwa hisia sana kitu kilichoamsha viulizo kichwani kwa yaliyokukuta.Embu tumalizie kutuambia ni nini hasa kilichofanya uyachukie mapenzi kiasi hicho,maana hizo mambo za kugonga hadi kifua,zimenipa mshawasha sana wa kujua nini kilitokea”.Chris aliongea hayo.



    “Aaah Chris tulia bwana. Ndiyo maana sisi hatukutaka kuongelea hayo kwa kuwa inaonekana aliumia sana na mapenzi. Kama tutamuomba atusimulie yaliyomsibu ni kama tutakuwa tunasokomeza kijinga cha mkaa kwenye kovu lililoanza kupoa maumivu kama siyo kupona kabisa.

    Nachotaka kusema ni kuwa, siyo vizuri kumkumbusha mwenzako jambo ambalo kwake hakulipenda na akaona bora lipite. Tunachotakiwa kwa sasa ni kumfanya aone mambo yaliyomkuta ni ya kawaida na yampasa kusahau kisha kufungua moyo wake kwa mtu mwingine”.Aliongea Solo kama kupinga kauli ya Chris ya mimi kutaka kuhadithia yaliyonikuta.Hakuishia hapo Solomon.



    “Ila pia ni swali zuri endapo yeye mwenyewe ataamua kutujibu, kwa sababu hata mimi japo natetea asiseme,ila nina hamu sana ya kujua ni nini kilimtokea Bwana Masai”.Alimaliza kuongea Solo huku akiniangalia usoni akisubiri neno kutoka kwangu.

    Kiukweli sikupenda sana kusimulia yaliyopita kwa sababu ya maumivu niliyoyapata katika maisha yale. Niliamua kuwaambia tusahau habari hizo huku nikiwaahidi kufanyia kazi ushauri waliyonipa.

    ****

    Tayari tulishamaliza muhula wa kwanza wa masomo katika ule mwaka wa pili. Na sasa tuliingia muhula wa pili na wa mwisho kabisa kabla hatujaukaribisha mwaka wa tatu wa masomo pale CBE.



    Muhula ule walituhamisha madarasa kutoka pale chuoni na kutupeleka madarasa mengine tofauti na ya pale chuo.

    CBE waliweza kukodisha madarasa ya VETA pamoja na jengo fulani la ghorofa nne lililopo katikati ya mji wa Dodoma ambalo ndilo sisi tulilopelekwa. Nakumbuka darasa tulilohamishiwa lilikuwa ndilo darasa la mwisho kabisa,yaani ndilo darasa lililokuwa juu katika ghorofa lile.Lilikuwa kwenye ghorofa la nne.

    Kutokana na madarasa yale kuwa makubwa sana,basi tuliweza kuchanganywa na kuwa mikondo miwili yaani A na B. Tulienea vizuri sana.Marafiki nao wakaongezeka kadiri siku zilivyo yoyoma.



    Kundi letu la kujisomea pia,halikuvurugika zaidi ya kuongezeka na kufikia watu kumi. Tukauwasha moto rasmi katika masomo kwani sasa hata wale waliyokuwa wanachukua masomo tofauti na sisi waliingia. Rafiki yangu Saint Justin au Jet Li kama tulivyozoea kumuita, na yeye alikuwa mmoja wa kikundi japo alichukua masomo ya masoko.



    Masomo ya Masoko au Marketing kwa kiingereza na masomo ya Ugavi au Procurement, kwa kifupi yaliendana sana. Masomo yale sisi tuliyaita mapacha na ndiyo maana hata Saint Justin aliweza kutumudu na kuwa mmoja wa kundi kwa muda mrefu.



    Huku tukiwa tunachagizwa na matokeo yetu mazuri ya mhula uliyopita,tukawa wenye kupenda sifa sana katika masomo. Yaani kila somo likawa halitupiti kizembe.Majaribio na mazoezi ya chuo,tulikuwa tunayafanya na tulikuwa tunafaulu vizuri kuliko mwanachuo yeyote pale CBE hasa katika darasa letu.



    Kila ilipofika siku ya kufanya majaribio pale chuoni,kila mtu alikuwa anataka kukaa na sisi ili tuwe tunamsaidia sehemu pale anapokwama. Na sisi tulikuwa hatuna hiyana na mtu,pale tulipopata nafasi ya kumsaidia mtu wa hivyo,tulimsaidia kwa moyo mmoja.Hiyo nayo ikawa ndiyo siri ya kupendwa na kila mwanachuo pale chuoni.

    ****

    Nakumbuka siku moja nilichelewa sana kwenda darasani,nadhani ni kwa sababu ya mvua zilizokuwa zinaendelea kunyesha kwa wakati ule. Siku hiyo Chris alikataa kwenda darasani kwa sababu alikuwa anategemea mpenzi wake kwenda pale nyumbani tulipokuwa tunakaa,hivyo alinisihi sana nisiwahi kurudi ili yeye afurahi na mpenzi wake huyo. Sikuwa na tatizo kuhusu ombi hilo.



    Nikatoka mbiombio na kwenda kituo cha daladala ambapo nilipanda ya Jamatini/Nkuhungu, ilinipeleka hadi yalipo madarasa yetu mapya.Kiukweli nilikuwa nimechelewa sana,lakini namshukuru MUNGU kwani kuchelewa kwangu kulinipa furaha ya macho.

    CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Niliposhuka kwenye ile daladala,moja kwa moja nilielekea kwenye geti kubwa la jengo lile na kuanza kulisukuma kwa ajili ya kutaka kuingia. Lakini kabla sijafanikiwa kupiga hata hatua moja ya kuingia ndani mwa jengo lile,nilisikia kelele za wanaume na miruzi mingi ikiwatoka midomoni mwao.



    Ilikuwa ni miruzi na kelele za kihuni ambazo mara nyingi ilitoka kutokana hasa baada ya kuona msichana au wasichana warembo wakipita mbele yao. Kwa kuwa na mimi nilishapitia mambo hayo,nilihamasika kugeuka na kutaka kujua ni nini kinaendelea.



    Mawazo yangu hayakuwa na makosa.Yalikuwa sawa sawia,lakini watu waliokuwa wanapigiwa kelele nilikuwa nawafahamu vizuri sana, hasa mmoja wao aliyekuwa katikati ya wengine aliyekuwa anaonekana kama kiongozi wao.



    Walikuwa ni wasichana watatu ambao wawili walivaa sare sare na mmoja alikuwa kavaa tofauti na wale wengine,huyo ndiye nilihisi kuwa ni kiongozi wao,na hakuwa mwingine,bali ni yule aliyefanya niitwe Jay Z.Ndiye yule yule msichana wa kwanza kunipiga busu pale chuoni,tena la mdomoni ambalo hadi muda ule kulikuwa hakuna mwanachuo mwingine aliyefanikiwa kufanya vile.



    Kiukweli yule binti alikuwa ana kila sifa ya kuitwa mrembo sema yeye hakufaa kugombania mashindano kama Miss Tanzania kutokana na umbo lake la Kibantu.

    Namaanisha yule binti kwa huku nyuma alikuwa kajaza sana mithili ya punda milia yule aliyenona kabisa. Wakati huo anatembea, ule mzigo wa nyuma ulikamatwa vyema na kiuno kilichotumbukia kwa ndani kiasi halafu kikapanda kidogo na kukutana na tumbo ambalo lilikuwa halijatokeza hata kidogo.

    Kwa juu ya tumbo kuna kifua kilichokuwa na matiti madogo lakini yaliyochongoka ambayo yanaweza kusababisha mihemko fulani katika mwili wowote wa mwanaume.



    Nilipomtazama usoni,hapo ndipo nikaimba haleluya haleluya ule wimbo wa kumsifu MUNGU. Kama binadamu ni wawili wawili,basi ile ilikuwa ni kiboko,maana kuanzia sura hadi nywele huwezi kusita kumuita Beyonce.



    Huku sasa akiwa karibu kabisa kunifikia pale getini nilipokuwa nimesimama nikishangaa ujio wao, nikagundua alikuwa siyo mtu wa shida wala mshamba. Mavazi yaliyowekwa mwilini mwake huwezi kuyaona Tanzania na hata kama ukiyaona,utaambulia kuulizia bei na kuondoka bila kununua. Hata jinsi alivyokuwa anatembea,ni kama hataki lakini ndiyo alikuwa anakuja hivyo mbele yangu.



    Cha ajabu aliponifikia pale mlangoni,alinipita bila hata salaam na mbaya zaidi wale wenzake wawili walinifyonza kwa kitendo cha kuwaangalia na kuwazibia njia ya kupita. Nikaanza kujiuliza maswali ambayo sidhani kama yangepata majibu kwa wakati ule.



    “Ina maana kanisahau au ndiyo kujishaua tu! kwa sababu kina vijihela.Na hivi vingine navyo kama vimechomekwa kwenye vinguo vyao.Eti vinasema nimeviangalia sana,pumbavu kabisa”.Nilijikuta najiongelea peke yangu huku nikimaliza na tusi dogo lililoambatana na msonyo wa haja.

    Ghafla nilishituka na kugundua kuwa nazidi kuchelewa darasani kutokana na kuwafikiria wale wasichana ambao wao tayari walikuwa wameshapanda juu.



    Bila kupoteza tena muda,nilivamia lile geti la jengo lile na kuanza kuelekea yalipo madarasa yetu kwa kupanda ngazi kwa kasi kidogo huku nikiwaza yaliyokuwa yametokea muda mchache uliyopita.

    Nilipofika ghorofa ya tatu macho yangu yakapata mshituko mwingine wa haja,jambo ambalo lilifanya nipunguze mwendo kidogo wakati napanda zile ngazi. Macho nilishindwa kuyafumba na nikayaacha yamebaki yanashangaa kile kilicho mbele yangu.



    Alikuwa ni yuleyule binti ambaye sikumfahamu jina zaidi ya kumuita Beyonce kutokana na sura yake aliyokuwa kaibeba. Alikuwa amesimama huku akiangalia upande niliyokuwa natokea na aliponiona alitoa tabasamu tamu na la kuvutia usoni mwake.



    Midomo yake ilitengenezwa na ‘Lips’ ambazo kwa kila mwanaume rijali angetaka kuzibusu au hata kuzinyonya kama akipewa nafasi hiyo. Wakati bado natathimini midomo yake,macho yangu yakaelekea kwenye macho yake madogo na ya kurembuka kiasi,huku yamebebwa na uso mwembamba kiasi na kufanya macho yale yawe karibu karibu huku yakitenganishwa na pua yake ndefu na ya kuvutia sana.

    Akili yangu ilihama sana kwa sababu ya binti yule ambapo sasa zilibaki hatua kama tano niweze kufika mahali alipo. Hapo mawazo yangu ya kumsifia yakahama na kuja kwenye mawazo ya kulipa kisasi cha yeye kunipita bila hata salaam pale nje. Nilijisemea moyoni kuwa nitampita bila kusema chochote na yeye.



    Na ndivyo ilivyokuwa.



    Niliongeza kasi ya kutembea na nikaweka nyongeza ya mruzi ambao sikujua hata nilikuwa nautoa sababu gani na wala haukuwa wimbo bali kelele tu!. Kwa kasi ya ajabu nilimpita pale alipo huku nimeangalia juu kana kwamba sijamuona wala nini.

    Baada ya kumpita nilianza kujipongeza kwa kitu cha kijasiri kama kile huku nikijisemea moyoni kuwa wao ndiyo walianza tangu pale getini kwa vijitabia walivyoonesha wale rafiki zake wenye mbwembwe nyingi na kejeri.



    Nikiwa nimeshatangulia kama hatua tatu tangu nimpite,ndipo nikasikia sauti nyororo na yenye kila sababu ya kuitwa tamu na nzuri. Ni sauti iliyojipanga kusema neno, ni sauti iliyokuwa na uhakika ikifanyacho.



    “Kaka jamani,si na kuita?”.Aliongeza maneno hayo baada ya kuona sijaitika wala kugeuka zaidi ya kwenda mbele na kuendelea kupiga ule mruzi uchwara.

    Ndipo niligeuka na kushindwa kujitetea kwa kile nilichaofanya jambo lililonifanya nikodoe macho yangu kama zezeta kwa binti yule.



    “Mambo vipi kaka. Mbona ukanipita bila hata salaam wala ishara yoyote?.Au ndo’ unalipa ya pale nje? Hatuendi hivyo kaka”.Yalikuja maswali mfululizo yakiishia na ushauri ambao ulikuwa kama laumu kutokana na sura yake kuwa katika masikitiko kwa kile nilichokifanya.



    “Hamna dada,lazima nijishtukie bwana. Si wajua pale ulinipita na wale rafiki zako walitoa vimaneno vya mashauzi na kunitusi pia. Basi mimi nikajua ndivyo mlivyoamua kufanya. Na ndio maana nilivyokuona hapa,nikajua bado upo kwenye hali yako ile ile ya mashauzi”.Nilimjibu hivyo yule binti huku nikionesha wazi kuwa sikufurahia kitendo walichofanya pale nje.



    “Achana na hisia hizo kaka yangu. Mimi siyo wa hivyo unavyowaza,ni mambo fulani yalifanya nifanye vile pale getini. Ila kwa kweli halikuwa kusudio langu na wale wadada wawili nimewaonya kwa kile walichofanya. ‘By the way’ naitwa Miriam Mendrovic,nasoma Procurement na leo ndiyo siku yangu ya kwanza kuja kusomea huku”.Alijitetea yule dada na kujitambulisha baada ya kuona nimeridhika na utetezi wake. Akaendelea,



    “Nasikia darasa letu lipo juu kabisa,wanasema ni ‘flow’ ya nne sijui”.Alimaliza binti yule ambaye tayari nilimjua kama Miriam. Na kizuri niligundua kuwa nasoma naye darasa moja na ‘course’ moja ya Ugavi.CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Kitu kingine nilichokigundua kutoka kwa Miriam ni kupenda kuweka maneno ya kiingereza pale alipokuwa anaongea lugha yetu adimu na adhimu ya Kiswahili. Hilo nikaliweka kichwani huku nikiahidi kulifanyia kazi kadiri urafiki wetu utakapoenda mbele.



    Nilitabasamu na kushika kidevu changu ambacho kama niliotea, siku hiyo nilikiondoa ndevu ambazo nilikuwa nazifuga kwa wingi hadi watu wakawa wananiita Jay Z nyani. Wengi walionipenda na kunijali,walikuwa kila siku wananisema kuhusu zile ndevu, lakini mimi nilikuwa kama siwasikii huku nikiwapa msemo mmoja tu! wa kiingereza,



    “THIS IS MY REALITY(Hii ni asili yangu)”. Ndio msemo niliowaambia.Wakati huo nawaambia nilikuwa nazishika zile ndevu kuanzia kwenye ‘TIMBA’ hadi kwenye mzuzu wa ndevu zile.

    Lakini siku hiyo nilikuwa nimenyoa kuanzia kichwani hadi hizo ndevu,hivyo kuufanya ule u HB wangu uonekane vyema.

    Huku bado naendelea kumtazama Miriam kwa macho ya kumsifu, nikaanza kuongea.



    “Ahaa,kumbe na wewe ni Afisa Ugavi?. Mimi mwenyewe nipo hukohuko na hapa ndiyo nawahi kipindi kwenye hilohilo darasa. Kama vipi tuongozane kwenda huko”.Nilimjibu kwa kumchangamkia na kuanza kupanda zile ngazi zilizobaki.



    “Pia naitwa Frank….. Frank Masai au Man’Sai ,sema hapa chuo wengi wamezoea kuniita Jay Z.(Hapo kwenye kutaja jina la Jay Z tulitamka kwa pamoja hivyo kuzifanya sauti zetu mbili ziweze kuelewana na kutengeneza ara nzuri kama zile ‘ara za roho’)”.Tulicheka kwa pamoja baada ya ule mgongano wa sauti huku tunazidi kuishurutisha miguu yetu kwa kupanda zile ngazi.

    Tulikuwa tunapanda huku tukiendelea kupiga soga za hapa na pale tena kwa furaha kama tulikuwa tunajuana kwa miaka sitini.



    “Yaani hizi ngazi kaka yangu,we acha tu. Ningekuwa na uwezo ningemwambia ‘Uncle’ aweke lift”.Aliongea Miriam huku kasimama akiwa amechoka kumalizia ngazi kama tatu zilizobaki.



    “Uncle ndio nini”.Nilimuuliza Miriam kwa lengo la kuanza kumrekebisha lugha yake anayoichanganya na Kiswahili.



    “Uncle ni mjomba,kwani hujui au unataka unizuge tu hapa”.Aliongea huku anatabasamu.



    “Siyo kama sijui,ila nakushangaa unapochanganya lugha mbili kwa wakati mmoja na wakati huo unajua tafsiri ya neno hilo. Nimekusikia kitambo sana,mara ‘by the way’ sijui ‘flow’. Kwani hayana Kiswahili hayo”.Nilitimiza ahadi yangu ya kumrekebisha lugha yake.



    “Mh! Upo makini wewe, I start to like you. Oh sorry……”Akashindwa kuendelea na kubaki kaweka mkono wake mdomoni kuonesha hakudhamiria kuzidi kuongea maneno ya lugha nyingine.



    “Embu nyanyuka twende maana hapa tutamaliza lisaa lizima tunaongea”.Nilimwambia anyanyuke baada ya kuona tunazidi kuchelewa kipindi.



    “Tushachelewa bwana. Twende kwa pozi.Halafu nimelipenda sana jina lako la Masai. Kwani wewe Mmasai”.Alizidi kuongea Miriam huku akinyanyuka.



    “Hamna Miriam. Ni jina tu!Mimi ni mtu wa Kusini mwa nchi bwana. Kwetu ni Sumbawanga, kule wachawi wanapotokea kwa wingi kama mnavyosemaga”.Nilimjibu huku tunazimalizia zile ngazi na kuanza kuukaribia mlango wa lile darasa.



    “Mimi ni Mfipa asilia kabisa. Vipi wewe wa wapi? Maana hilo jina Mendrovic ni kama jina la Waziri wa Ulinzi wa Urusi aitwaye Ludovic Mendrovic. Isije ikawa ndiye baba yako yule,ha ha haaa naweza nikazimia hapa”.Nilizidi kuongea huku nikiingiza na utani kidogo kwa Miriam aliyeonekana mwenye tabasamu kwa kila nukta ya maongezi yangu niliyoiweka.Wakati huo nilishaushika mlango kwa ajili ya kuusukuma na kuingia,ila nilisubiri kwanza anijibu swali langu.



    “We mcheshi na mjuzi wa mambo sana. Wengine hata huyo Waziri wa Ulinzi wa Urusi hawamjui na wala hawajawahi kumuona,yaani hata ukiwauliza Rais wa Urusi sidhani kama watakutajia jina lake. Lakini wewe ulivolitaja hilo jina,ni kama una undugu naye. Ni kweli yule ndiye baba yangu”.Hatimaye Miriam alinijibu jibu ambalo lilifanya niachie ule mlango na kumvutia pembeni Miriam na kuomba anipe japo kidogo historia yake ya yeye kuwa hapa badala ya Urusi.



    “Marehem Mama yangu alikuwa ni Mtanzania na alifariki wakati ananileta mimi duniani. Baba alikutana na mama enzi zile Tanzania imetapakaa sana sera ya ujamaa. Na wakati huo Baba na watu wengine ndiyo walikuwa mstari wa mbele kuwahamasisha vijana wenzao katika kusambaza sera za ujamaa.

    Mwaka 1987 baba na mama wakabahatika kunileta mimi duniani ila ndiyo ukawa mwisho wa mama yangu”.Hadi anamaliza kuongea hayo nilikuwa nimebung’aa kama mtu anayesubiria hela zake alizoshinda kwenye bahati nasibu.

    Nilikuwa siamini kama naongea na mtoto wa waziri wa ulinzi wa Urusi ambaye alikuwa anapewa nafasi kubwa sana ya kushiriki uchaguzi wa Rais mwaka unaofuata kama mgombea wa chama tawala.



    Nikawa kama najiuliza maswali ambayo tayari yalikuwa yana majibu. Lakini nikazidi kujiumiza kwa maswali mengine ya kumchimba zaidi. Kama ni mtoto wa Waziri wa Urusi ,ni kwa nini yupo Tanzania kwa sasa? Kwa nini anasoma CBE,tena ya Dodoma? Na kwa nini baba yake kaamua kumuacha Tanzania,nchi yenye amani lakini yenye shida nyingi kwa wananchi?.Yakawa maswali mfululizo yaliyopita kichwani mwangu kwa sekunde chache.



    “Aisee Miriam umeamsha maswali mengi sana kwenye kichwa changu,ila ngoja tusome hata kwa huu muda uliobakia,na kama baadae tutakuwa pamoja nadhani nitapata majibu ya maswali yangu”.Nilimwambia Miriam na kuufuata mlango wa darasa na kuuvuta kimya kimya ili nisiwashitue wengine.

    Tulipoingia darasani hatukuonekana na watu wengi kwa sababu tuliingilia mlango wa nyuma hivyo wanachuo wote walikuwa wametupa mgongo.Ni mkufunzi pekee ndiye alikuwa anatuona wakati tunaingia,na yeye wala hakujali kuingia kwetu kule, jambo lililofanya wanachuo nao wawe katika harakati zao bila kuangalia nyuma.



    Nilivuta kiti kistaarabu ili nisiwapigie kelele waliokuwa katika mawazo ya kusoma lile somo.Nilipofanikiwa kukivuta nikakinyanyua kwa ajili ya kukipeleka upande wa pembeni,upande ambao nilipenda sana kukaa.Na tena nilipenda sana kukaa nyuma ambapo kulikuwa na dirisha.



    Wakati nafanya hayo,Miriam alikuwa ananiangalia huku kasimama pembeni asijue nataka kufanya nini. Alipoona nimenyanyua kiti na kuanza kuelekea pembeni,ndipo alinishika mkono na kunivuta kana kwamba alikuwa hapendi niende kule. Na mimi nikawa mgumu kukubali kufanya atakayo yeye kwa hiyo ikawa vuta nikuvute kati yetu. Mwisho aliamua kuanza kusogeza midomo yake karibu na sikio langu kwa lengo la kuninong’oneza.



    Kumbe matendo yetu yote tuliyokuwa tunayafanya,mkufunzi wetu alikuwa anayaona.Lakini kitendo cha Miriam kuanza kusogeza midomo yake karibu na uso wangu,mkufunzi yule alikitafsiri vibaya jambo lililofanya atushitue tutoke kwenye hisia zile.

    CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Aisee nyie wapenzi wawili,kwanza mmechelewa,halafu mmeingia darasani mmeanza kuvutana vutana kama mnacheza mchezo wa kuvuta kamba. Mkaona haitoshi,sasa mnataka kubusiana si ndiyo eeh!. Huko kuliko wafanya mchelewe hamkuridhika kabisa hadi mnaleta mapenzi ya njiwa darasani?”. Maneno hayo yalifanya darasa zima kugeuka na kukuta Miriam kanishika mkono wangu na mimi nimebeba kiti huku wote tukiwa tumeganda kama tulikuwa hatujasikia maneno ya Mkufunzi.



    “Oyooo,Jay Z na Beyonce wanataka kutoa ‘single’”.



    “Wazee wa Crazy In Love hao bwana”.Zilisikika sauti za wanachuo wenzangu baada ya kugeuka na kukuta hali yetu ile. Wengine walisema tunataka kutoa wimbo pamoja na wengine waliutaja ule wimbo wa Beyonce aliyomshilikisha Jay Z,Crazy In Love.

    Hapo Miriam aliniachia mkono wangu na kuvuta kiti kilicho karibu yake na kukaa huku akiwa na uso wa hira. Na mimi ili kuvunja zogo lililoanza mle darasani,nilipeleka kile kiti changu mahala nilipopanga tangu mwanzo. Darasa likatulia na yule Mkufunzi wetu akaendelea kufundisha.



    Macho ya Miriam hayakukwama kuniangalia. Kila mara alikuwa ananiangalia nachofanya na kuna kipindi macho yetu yaligongana na kuamsha hali fulani ya uelewano. Mara nyingi nikikutanisha naye macho, nilikuwa namzomea huku natoa ulimi wangu nje jambo lililofanya awe anatabsamu kila dakika akiniona.



    Kwangu mimi niliona kawaida sana kwa mambo yalivyokuwa yanaendelea kati yetu,hivyo wala sikuwa na wasiwasi na chochote wakati hali ile inaendelea.



    Baina yetu,yaani mimi na Miriam,hakuna aliyeelewa lile somo kwa siku ile. Hiyo ni kwa sababu kila mmoja wetu alikuwa anahamu ya kujua mwenzake ana nini.



    Baada ya kipindi kuisha, Miriam alisogeza kiti chake mahali nilipo na kuanza kuongea na mimi huku akinilaumu kwa nilichokifanya pale mwanzo.



    “Yaani wewe bwana,sasa kwa nini unapenda kukaa nyuma peke yako?Mimi nakukataza usiende,wewe unakuwa mbishi hadi mwalim akatuona”.Alianza kuongea Miriam baada ya kufanikiwa kuweka kiti chake karibu na mimi. Wakati huo wote, wale wanachuo wa mle darasani walikuwa wanatuangalia huku wakitabasamu kwa kufurahia nyuso zetu zilivyokuwa zinatazamana.



    “Ha ha haa,yaani mimi huwezi kunikalisha katikati wala mbele. Nishajizoelea huku nyuma kabisa. Hayo masuala ya kukaa mbele,ni kutaka kuwa mfano kwa mwalimu”.Nilimjibu Miriam hivyo,wakati huo macho yake yalikuwa yananitazama moja kwa moja huku yakishindwa kuangalia pembeni kutokana na uwezo wangu mzuri wa kuongea bila kusababisha kero kwa mtu mwingine.

    Kuna watu hawajui kuongea na hata akiongea basi ni kero kwa msikilizaji. Mtu anaongea kwa sauti kama spika za ukumbini,au anaongea huku anarusha rusha mate kama mashine ya kumwagilia bustani. Hizo mimi sikuwa nazo hata kidogo. Wengi waliniambia kwa kiingereza kuwa ‘I TALK LIKE A GENTLEMAN’, yaani naongea kama mwanaume rijali.



    “Ujue mimi sikuelewi kabisa. Sasa ukikaa huku nyuma,unaonaje? Halafu mbona kundi lako lote linakaa mbele tena sehemu moja?”.Miriam akazidi kuongea maneno ambayo yakaanza kunishangaza. Kumbe alikuwa anajua hadi kundi langu la kusomea,nikajisemea kimoyomoyo huku nikiamini kuwa atakuwa anajua mengi sana kuhusu mimi.



    “Yaani Miriam,mimi nikikaa mbele huwa sielewi hata kidogo. Huku nyuma ndiyo nampata vizuri sana mwalimu. Na pia nalishukuru sana lile kundi kwa sababu huwa wananakiri anachitoa mwalimu,kwa hiyo na mimi napata kitu kutoka kwao”.Nikaendelea kuongea na Miriam ambaye alikuwa haridhiki na mimi kukaa nyuma.



    “Yaani wewe hapo mimi hata sikuelewi. Huna sababu za msingi za kukaa nyuma hata kidogo.Huwezi kusema ukikaa mbele eti humwelewi mwalim na wakati ukikaa huku nyuma sauti hata haiji vizuri. Sasa sijui hapo utaniambiaje tena”.Miriam alizidi kunisomea risala ambayo kwangu sikujua hasa ni nini nia yake na ningekuwa siyo mtu mstaarabu,ningeanza kumjibu hovyo tu!.

    Maneno kama ‘Wewe inakuhusu nini mimi kukaa nyuma’ au ‘Achana na mimi,jali mambo yako’,sikuyapa nafasi katika kinywa changu. Si kwa Miriam pekee,bali ni kwa kila mtu niliyekuwa naongea naye.

    Miriam alizidi kuongea huku tukijibishana hasa kuhusu mimi kukaa kule nyuma hadi pale nilipoamua kukubaliana naye kuhusu kukaa mbele.



    “Haya poa bwana,umeshinda. Kuanzia kesho anza kuniwekea nafasi sehemu ya mbele”.Nilikubaliana naye baada ya mabishano marefu sana yasiyo na kichwa wala miguu.



    “Siyo kesho.Hivi vipindi viwili vilivyobaki vyote tunaenda kukaa mbele”.Miriam aliongea huku mimi nikiwa namshangaa kwa afanyacho.

    Kwa kifupi hata kama hiyo kesho angewahi na kuniwekea sehemu ya kukaa wala nisingeenda. Lakini hilo suala la kuniambia niende mbele muda ule,ndilo lililofanya nizidi kumshangaa.



    “Sasa mbele tutaenda kukaa wapi? Si unaona tayari kumeisha jaa? Kama vipi we tutulie tu! huku huku”.Nilijitetea ili nisiende.

    Kwangu mimi tangu nianze pale CBE ndio ingekuwa mara yangu ya kwanza kwenda kukaa mbele,tena kwa kupelekwa na msichana. Rafiki zangu walishanilazimisha sana kwenda kukaa nao,lakini walinishindwa.



    “Hilo ondoa shaka. Wale wadada wawili nitawatoa halafu tutakaa sisi”.Alijibu Miriam huku akimaanisha wale rafiki zake wawili aliyonipita nao nje,ndiyo watatuachia nafasi ya kukaa.



    “Haaa, wewe vipi?Yaani uwatoe wenzako ili ukae wewe wakati umechelewa mwenyewe?”.Nilimuuliza kwa kumshangaa.



    “Wale siyo wanafunzi,ni rafiki zangu tu! Wananisindikizaga.Kwa hiyo wala usitie shaka”.Alijibu.



    “Sasa kama siyo wanafunzi,wanakusindikiza wewe ili iweje?Na kwa nini uje na mabeki tatu wako chuoni?”.Nilimuuliza tena huku nikiwakandia wale wadada.



    “Ha ha haa,eti mabeki tatu. We hayo tuyaache,siyo muhimu sana kuyajua. Kwa sasa twende tukakae pale mbele”.Alinikatalia kuniambia.

    Nilikubali kufanya atakacho ili nisimuudhi na kukosa majibu ya maswali yangu niliyojiuliza.



    Baada ya kukubali,alitoa simu yake na kuandika ujumbe mfupi na baada ya dakika kama tatu wale wadada walikuja mahala tulipo,kisha wakaamriwa kunisalimia na kunitaka radhi kwa kile walichofanya pale nje. Hawakuwa na hiyana kuhusu hilo,walikubali na kisha sisi tukanyanyuka na kuelekea pale walipotoka wao.



    “Ayaaa,Jigga leo anaenda kukaa mbele. Kweli Beyonce leo kafanya kibogoyo kuutafuna mfupa,ha haaa”.Yalikuwa baadhi ya maneno ya wanachuo wa mle darasani baada ya kuniona naenda kukaa mbele. Hawakuishia hapo.

    CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Aisee,mnapendeza kichizi mkikaa pamoja. Yaani mnafaa sana kuwa bibi na bwana”. Yalikuwa maneno mengine kutoka kwao.



    “Unadhani mchezo nini,mtu hadi kachelewa kuja class unadhani ni kazi ndogo. Hapo kapelekwa hadi saluni kutolewa Osama zake”.Alikuwa jamaa mwingine akiongea,jambo lililofanya darasa zima liangue kicheko.

    Kwetu sisi lilikuwa ni tabasamu tu! Ndiyo limetawala kwenye nyuso zetu.



    “Mbona uwajibu? We si muongeaji wewe?”.Aliniuliza Miriam baada ya kukaa.



    “Mimi siyo muongeaji bwana,labda unamsemea Chris”.Nikamjibu.



    “Hivi nani asiyekuja hapa chuo kwa uongeaji wako? Yaani ni kama umefungiwa karedio mdomoni”.Aliongea tena.



    “Jay Z leo utaota. Nahisi hizo nguo utazivaa wiki nzima kwa sababu zinanukia mtoto mzuri”.Aliongea jamaa mwingine kutoka nyuma yetu.



    “Nimjibu huyo?”.Nilimuuliza Miriam.



    “Embu mjibu nisikie kama nachokisikiaga kwa watu ni kweli”.Aliniruhusu Miriam.



    “Najua ni ushamba ndiyo unakusumbua,na hizo ni tabia za watu wa Chang’ombe. We unadhani mimi ndo wewe wa kuvaa matambala ya deki wiki nzima. Kwanza hapo ulipo uja……..”.Miriam alinikatisha kwa kuniwekea mkono wake mdomoni huku akiwa hoi kwa kucheka.



    “Nini sasa,mbona unanikata stimu?”.Nilimuuliza Miriam.



    “Kwa hiyo Jigga umepata moto? Utani tu kaka”.Aliongea yule jamaa kwa kubembeleza.

    Kwa kipindi kile nilichokuwa nasoma pale chuoni,mtaa wa Chang’ombe ulikuwa ukisifika sana kwa uchafu na mpangilio mbaya wa makazi ya watu. Hivyo endapo utamtania mtu kuwa anakaa Chang’ombe,basi huwa mpole.



    “Sipo moto wala nini.Ila ishu nyingine ni kuzinguana kaka.Ila usikonde tupo pamoja”.Nilijikuta nikijilaumu kwa kufuata maneno ya Miriam ambayo yalitaka kama kutuchonganisha mimi na yule jamaa.

    Jamaa alikubali yaishe,na sasa darasa likawa limemaliza utani na kuanza kumsubiria mkufunzi wa kipindi kilichokuwa kinafata ambacho kilikuwa ni cha Ujasiliamali.



    Baada ya kama nusu saa,mkufunzi wa somo linalofata alikuja. Wakati huo mimi na Miriam tulikuwa tupo bize sana kwenye kunakiri alichofundisha mkufunzi aliyetoka.

    Ni kama na yeye alistaajabu baada ya kuona siku ile nimekaa mbele,lakini alinyamaza na kufanya kilichomleta darasani mle.Alifundisha kwa uwezo wake wote,na baada ya kumaliza aliondoka na kutuachia zoezi la kufanya.



    “Vipi Kaka Masai, zoezi linaeleweka lile?”.Alikuwa ni Solomon,yule kaka mkubwa aliyekuwepo kwenye kundi letu. Aliniuliza hayo baada ya kumsalimia Miriam.



    “Hilo halina tatizo kabisa, hapo tunakimbia tu! Dakika mbili,tayari kitu kimeisha”.Nilimjibu Solomon kwa uhakika swali aliloniuliza.



    “Kwani pale mwalim anataka nini?”.Aliniuliza Solomon tena.



    “Kile kipengele cha kwanza,pale anataka umwambie sifa za mjasiriamali,ambazo ndizo zile zisemazo kuwa,si lazima awe msomi, kinachotakiwa ni fedha ili uwe mjasiriamali,awe mbunifu na zile nyingine. Halafu kile kipengele cha pili ambacho ndicho kama kinachanganya watu wengi,kile kina maswali mawili ndani yake.



    Kwanza pale unatakiwa uelezee ni njia gani ambazo zitakufanya uongeze mapato katika ujasiriamali wako. Hapo utataja mambo Kama, kuchukua mikopo yenye riba ndogo, kuna ile nyingine ya kushare biashara zako au hisa Na makampuni au watu wengine, pia kuna ile njia ya kuwa ‘partners’ na nyingine nyingi”. Nikawa namuelezea Solomon yale maswali yanajibika vipi. Sikuishia hapo,



    “Kitu kingine kwenye kipengele cha pili, anataka umuelezee jinsi ya kupanga biashara yako kabla ujaianzisha (BUSINESS PLAN).Pale utamtajia zile njia kumi za kuzifuata katika mtiririko.Usizichanganye, ziandike kama yeye alivozifundisha. Halafu kumbuka na kuzielezea”.Nikawa nimemaliza kumsaidia Solomon, ambaye alishukuru na kutuaga kwa kwenda alipokuwa amekaa mwanzo.

    “Ujue siamini”. Alianza Miriam.



    “Uamini nini sasa? Mbona unanitisha”.Nikajibu.

    “Yaani mimi pale nilikuwa naona chenga tu! Kumbe ni rahisi vile”.

    “Ha ha haaa,ni rahisi ukiwa na mimi hivi,subiri uwe peke yako kwenye chumba cha mtihani,ndo utaona ugumu wake”.Nikamjibu tena.

    Naweza kusema kuwa,mimi nilikuwa ndiye mkali wa somo la ujasiriamali katika kundi letu. Hivyo hakuna aliyebabaika kama tatizo likitokea hasa katika maswali kama yale.

    “Nimekukubali sana. Yaani umemuelekeza mtu mzima kama yule na kakuelewa bila hata ubishi. Mi sina neno hadi hapo”.Alinisifia Miriam.

    “Asante mama.Ila mbona hata yeye unielekeza sana somo la‘BUSINESS MATHEMATICS’”.

    “Ina maana huyu mzee ni mkali wa ‘Math’”.

    “Huyo ni noma kwenye hesabu. Ule mhula uliyopita aliua A kwenye ‘STATISTICS’.

    “Aisee,itabidi na mimi nije m’we mnanisaidia”.

    “Karibu sana bibie”.



    Tuliongea mengi na Miriam hadi pale aliposema anahisi njaa hivyo aliniomba aende kula kwanza.Kwa kuwa na mimi nilikuwa hivyo hivyo, niliomba tuongozane ili tukajumuike pamoja.

    “Mh!Hapana Frank,kila mtu aende kivyake”.Alikataa Miriam baada ya mimi kumuomba ombi langu.

    “Sasa kwa nini hutaki?”.Nilimuuliza.

    “Basi tu! Au nipe namba yako ya simu,nikifika nitakupigia ili uje”.Aliniambia hivyo lakini bado mimi nikawa na maswali lukuki kwa afanyacho.

    Nilimpa namba yangu na yeye akatoka sehemu ile na kwenda alipotaka kupatia chakula.



    Baada ya Miriam kuondoka na wale wenzake na kukaa nje kama dakika kumi,ndipo simu yangu ilipoanza kuita na pale nilipoipokea alikuwa ni Miriam akiniomba nishuke na kuelekea sehemu moja iitwayo Zunie,ambayo ilikuwa maarufu sana pale Dodoma kwa kutengeneza juisi mbalimbali na vitafunwa kama vile keki,karanga na vingine kama hivyo.

    Nilianza kushuka haraka ngazi za ghorofa lile na baada ya dakika kama ishirini,tayari nilikuwa mbele ya Miriam na pembeni yangu walikuwa wale rafiki zake ,ambao baadae waliondoka na kwenda kukaa sehemu nyingine.

    CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Hivi unaweza kuniambia nini kinaendelea katika mambo ufanyayo?”.Nilianza kumuuliza baada ya kuletewa glasi yangu yenye juisi ya ukwaju.

    “Kwani kuna nini kimetokea jamani”.Na yeye akajidai hajui alichofanya.



    “Ina maana hujui au umeamua kuzingua tu!”



    “Masai bwana. We hayo yasikuumize kichwa kwa sasa ila baadae utakuja kuelewa ni kwa nini nafanya hivi”.



    “Kwa hiyo kwa sasa hivi sipaswi kufahamu, si ndiyo ee”.



    “Yeah, we tufurahi tukiwa hivi tu! Mbona yatosha”.



    “Mh! Haya bwana, ngoja mi niache, isijekuwa nakuchimba sana”.Nilikubali yaishe huku nanyanyua gilasi yangu ya juisi na kunywa kimiminika kilichomo mle.



    “Nashukuru kuwa wewe ni muelewa. Mwingine angesipokubali”.



    “Kawaida tu. Haya embu niambie kwa nini upo Tanzania badala ya Urusi?”Nilianzisha soga nyingine.



    “Mh! Na wewe usahau tu!”



    “Aisee nilikuwa na usongo wewe wa kujua hilo na mengine mengi kuhusu wewe”.



    “Ok. Nitakwambia, ila na wewe niahidi kuwa nikikuuliza kitu utanijibu”.



    “Hilo ondoa shaka kabisa”.Nilikubaliana naye.



    “Huku Tanzania kuna usalama sana kwa sasa kuliko kule Urusi. Kule kama unavyojua, baba kateuliwa kugombea Urais kwa tiketi ya chama Tawala.Hivyo hata maisha yake yapo hatarini kidogo hasa kwa majambazi na wale wasiopenda sera za Ujamaa, ambazo ni sera bado zinatumiwa sana kule Urusi.

    Kwa kuwa nina asili ya Uafrika na tena ni Mtanzania,niliamua kumwambia baba anitafutie uraia wa Tanzania kwa miaka kadhaa ili niepukane na yatakayotokea huko Urusi,hasa kutekwa”.Aliongea Miriam kwa umakini huku akiendelea kunywa kinywaji chake.



    “Baba hakuwa na tatizo kuhusu hilo, kwa kuwa alielewa mpangilio mzima Urusi.Hivyo alichofanya ni kuwasiliana na kaka yake,ambaye ni Mjomba wangu aliyoko huku Tanzania, na kumwambia anishughulikie suala hilo.Haikuchukua muda,nikawa nimeletwa Tanzania.Lakini suala kubwa la mimi kuwa huku ni usalama”.Alimaliza Miriam huku akinikaribisha kama na swali lingine niweze kuuliza.



    “Sasa kwa nini umechagua kuja kuishi Dodoma na siyo Mwanza, Arusha au Dar es Salaam?”Nilimuuliza.



    “Mjomba wangu ana kampuni moja kubwa sana hapa Tanzania.Kampuni hiyo ina matawi karibu kila kanda hapa Tanzania, ambapo mwaka juzi ndipo ilipofunguliwa kampuni nyingine kanda ya kati ambayo imewekwa hapa Dodoma.

    Sijui umewahi kuisikia kampuni inaitwa MENDRO FAMILY LIMITED COMPANY?”



    “Ahaaa, ile ya uingizaji wa bidhaa kutoka nje ya nchi kwa kupitia bahari na barabara?”Nilimjibu huku nikionesha naifahamu kampuni anayoizungumzia.



    “Siyo kuingiza bidhaa kwa njia hizo tu! Pia inajishughulisha na uchimbaji wa madini na mafuta ya hapa Tanzania, ambapo inachukua asilimia chache sana kuliko serikali ambayo wanachukua karibu asilimia sabini ya uchimbaji huo.

    Sasa baada ya kufungua tawi hapa Dodoma, waliona mimi ndiyo niwe mmiliki wa tawi hilo lakini kwanza waliona nisomee mambo ya biashara ndiyo niweze kuiendeleza kampuni hiyo vizuri. Nilichagua CBE ya huku ili iwe rahisi kwangu kuwa naifatilia kampuni hiyo vizuri.

    Pia mjomba ana majengo mengi sana ambayo anayafanyia biashara zake, hata hilo tunalosomea pia ni lake”.Miriam alikuwa ananijibu majibu yangu vizuri kabisa kitu kilichonifanya niishiwe maswali ya kuuliza na kubaki najibaraguza.



    “Duh! Kwa hiyo na huo ni mjengo tunaosomea ni wenu? Dah! Mpo matawi ya juu. Kwani wewe huna ndugu wengine kama kaka au dada hivi”.



    “Kwa upande wa baba nipo peke yangu, lakini mjomba ana mtoto wake wa kiume anaitwa Yuri, ambaye yeye anasimamia kanda ya kaskazini katika mkoa wa Arusha”.Alijibu Miriam



    “Aisee hapo sina swali tena”.Nilimwambia baada ya kuridhika na maelezo yake.



    “Ok. Sasa zamu yangu kukuuliza”.Aliamishia kibao kwangu huku mimi nikishusha pumzi ndefu na nikiomba kwa hudi na uvumba asiulizie masuala ya mapenzi.



    “Nakusikiliza”.Nilimpa ruhusa huku moyo ukiwa hauna amani.



    “Naweza kuijua familia yako?”Alianza kwa swali hilo.



    “Kuijua kivipi yaani, nikupeleke ukaione au nikuhadithie”.Niliuliza kwa sababu sikujua anataka nini kwa mujibu wa swali lake.



    “Hapana. Nataka uniambie labda mpo wangapi, mnafanya kazi gani, mnaishi wapi. Na vitu kama hivyo”. Nilitabasamu kidogo baada ya kukumbuka idadi ya familia yetu huku nikilinganisha na ya kwao. Lakini sikuwa na wasiwasi wa kumjibu kwa sababu nilijivunia kuwa kila mtoto katika familia yetu alisoma na ana kazi.



    “Sisi kama watoto tupo kumi”.Nilisimama kidogo baada ya kuanza hivyo huku nikisubiria atapokeaje idadi hiyo. Ni kama nilivyotegemea, aliipokea kwa hamaki sana.



    “Khaa! Mbona wengi hivyo? Wote baba mmoja na mama mmoja au?”.



    “Hamna, siyo baba mmoja na mama mmoja. Wanne ni baba yetu mmoja na mama yao alishafariki, halafu sita wengine ndiyo mimi nimo humo,na mama yetu yupo. Kwa hiyo wale wanne walikuwa na mama yao na sisi tuna mama yetu lakini baba ni yule yule”.Nilimjibu.



    “Ahaa.Ila hata hivyo bado mpo wengi sana”.



    “Huo ndio Uafrika asilia, siyo nyie katoto kamoja tu!”

    CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Ha ha haa. Tuache hayo, kwa hiyo wako wapi hao tisa wote? Maana wewe ndiyo wa kumi”.



    “Umejuaje kama mimi ndiyo wa kumi? Una akili wewe”.



    “Aaah! Si ninajua kuwa wewe upo hapa, lakini hao wengine sijui walipo”.



    “Ha ha haa, haya bwana. Kaka yangu wa kwanza, yeye yupo Morogoro na ni mwalimu wa Shule ya Msingi.



    Wa pili ni kaka pia, yeye yupo Arusha ni Mtangazaji.

    Wa tatu yupo Dar, ni Mwanajeshi.

    Wa nne ni dada yangu, upande wa mama mwingine.Yeye ni muuguzi wa hospitali hapa hapa Dodoma.

    Wa tano pia,ni dada yangu upande wa mama mwingine,ni askari magereza huko Mbeya.

    Wa sita ni kaka yangu kwa upande wa mama mwingine, yeye ni afisa masoko huko Mwanza.

    Wa saba ni kaka yangu wa tumbo moja yeye ni mwalimu wa sekondari huko Singida.

    Wa nane ni dada yangu, upande wa mama mwingine, yeye yupo anasomea utangazaji Chuo cha Tumaini tawi la Dar.

    Wa tisa,ni dada yangu wa tumbo moja,yeye yupo chuo cha Mzumbe anachukua Sheria.

    Na wa kumi ndiyo mimi sasa, nadhani wajua wapi nilipo”.Nilimaliza kumpa orodha ndefu ambayo hadi naimaliza, ilikuwa inamshangaza sana Miriam.



    “Duh! Aisee nimsifu sana baba yako kwa jitahada za kuwasomesha ninyi nyote hivyo. Yaani kwa kuwa wewe ndiyo toto la mwisho hapo, basi una raha balaa. Yaani ukitaka kurudi shule ya msingi, yupo kaka atakufundisha.Ukiugua, yupo dada atakutibu. Ukipotea, kaka na dada yako watakutangaza redioni. Ukienda sekondari una kaka, ukifungwa una dada askari magereza, atakulinda gerezani. Ukiwa na kesi, dada yupo mwanasheria.Sijui jeshini mara sokoni, aisee hongera sana”.Alisifia Miriam huku akiwa ana tabasamu pana usoni pake.

    Aliangalia saa yake na kugundua kuwa muda wa kipindi cha mwisho umewadia, hivyo kama kawaida, aliomba aanze yeye kuondoka ndiyo mimi nifate. Wakati huo pale tulipokaa kulikuwa kumejificha sana.



    Nilikubaliana naye kuhusu hilo kwa kuwa sikutaka mabishano wala kumuhudhi.Alipoondoka na mimi nikakaa kama dakika tano ndipo nikanyanyuka na kuanza kurudi darasani, ambapo sikwenda kukaa karibu yake tena kama mwanzo, bali nilikaa zangu nyuma kama zamani.



    Nilisoma nikiwa na amani sana siku ile, yaani ilikuwa ni kushinda siku zote. Nilifurahi kila muda nilipokumbuka sura ya Miriam pamoja na uchangamfu wake.

    Nilijikuta nasahau kauli zangu nilizowaambia rafiki zangu kuhusu mimi na wanawake, na kujikuta nikisahau kabisa hata machungu ya nyuma.



    Siku hiyo sikuwahi hata kurudi nyumbani kwa sababu ya Chris, ambaye aliniambia kuwa atakuwepo na mpenzi wake. Hivyo nilibaki eneo lile hadi mida ya saa moja, wakati huo wanachuo wote hadi Miriam walikuwa wameshaondoka. Mimi nikabaki kujisomea tu pale.



    “We kijana muda wa kukaa humu umeisha, utaendelea kesho”.Ilikuwa ni sauti ya mwanaume mmoja wa makamo ambaye nilipomuangalia vizuri, niligundua kuwa alikuwa ni mlinzi.



    “Sasa mzee kwani kuna kiwango cha muda kwa watu kukaa humu?”Nilimuuliza.



    “Hili ni jengo la kibiashara kijana, acha biashara nyingine zifanyike”.Aliniambia yule mzee na kunifanya nianze kukusanya kilichokuwa changu kwa ajili ya kuondoka.



    “Kwani kijana unaitwa nani?”Aliniuliza yule mzee wakati nampita kuelekea mlango wa darasa lile ili niondoke.



    “Naitwa Frank Masai”.Huku nampa mkono.



    “Ohoo, Frank Masai. Na mimi naitwa Mzee Said Soji”.



    “Nafurahi kukufahamu mzee”.Nilimshukuru na kuanza kuondoka.



    “Kijana”.Aliniita Mzee Said.



    “Kuwa makini na urafiki uliouanzisha,usije ukajutia”.Mzee Said aliniambia kama kunionya na kuanza kupanga meza za darasa lile huku akiniacha mimi na maswali kibao kichwani na sikuwa na uwezo wa kumuuliza kwa kuwa niliona hana mpango na mimi tena.





    Nilirudi zangu nyumbani napokaa na kumkuta Chris yupo katulia muda mrefu kama ananisubiria mimi.

    “Oyooo, Jay Z.Nasikia leo live live na Beyonce kaka, ha ha haaa. Embu niambie”.Alianza Chris huku akinikumbatia na kugongesha mabega yetu kama salamu.



    “Mh! Ha ha haa, kweli sasa hivi dunia ni kijiji. Yaani habari unazo!!?”Nilikuwa nashangaa kufika kwa taarifa hizo kwa Chris.



    “Ha ha haa, usipime kaka.Ni kweli au? Maana kwa jinsi ulivyokuwa mgumu na kwa niliyoyasikia, aisee sikutaka kuamini. Eti mtoto akakukalisha mbele, kweli hiyo Jigga? ”.Aliongea Chris huku akitabasamu. Na mimi nilianza kumuhadithia kuanzia mwanzo ilivyokuwa hadi mwisho. Lakini sikumwambia maneno ya mwisho aliyoniambia Mzee Said.



    “Hilo zali kaka. Yaani hapo ubugi mwenyewe tu.Kakupa na namba zake za simu?”



    “Hiyo tena, kanipa na tena wakati nipo kwenye daladala alinitumia ujumbe wa kuniuliza kama nipo nyumbani. Sijamjibu, si wajua sina salio”.



    “Oyooo, Jay Z na Beyonce haoo, kama utani vile”.Alikuwa Chris akiongea kwa utani mwingi na kelele ambazo ziliwafanya hadi wapangaji wengine wakasirike.

    Hatukujali hilo, sisi tuliendelea kupiga soga zetu hadi pale tuliporidhika nakuanza kujisomea huku nikiwa kiongozi mkuu kwa kumfundisha Chris masomo ambayo alikuwa hayawezi na zaidi kumuelekeza yale tuliyoyasoma siku ile.

    ****



    Urafiki wangu na Miriam ulishika kasi zaidi baada ya kuamia kundi letu. Ule ukaribu wetu ukawa mkubwa sana tena sana, lakini ile tabia ya yeye kutangulia kwenda kupata chakula ndiyo mimi nifuate haikuisha kwa wakati ule.

    CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Baada ya mwezi mmoja, hatimaye nilianza kuhisi hali fulani hivi katika moyo wangu. Hali ambayo kwa wale wataalam wa saikolojia ya moyo, wangesema tayari nipo kwenye dimbwi la mapenzi.



    Ni kweli. Nilianza kumpenda Miriam,na hilo lilidhihirika pale siku moja ambapo hakuja chuo karibu wiki nzima. Nilijaribu kumpigia simu, lakini haikupatikana.

    Wale rafiki zake nao, wakawa hawaji tena chuoni. Moyo wangu ukashikwa na mashaka pamoja na joto la maumivu ya kutomuona Miriam. Nilipoa sana na kuwa mpole huku muda mwingi nikikaa namfikiria sana Miriam.

    Nilishindwa kuvumilia hali ile. Moja kwa moja nilienda kwa watu ambao nawaamini sana katika ushauri wao ili niwape yanayonisibu. Walikuwa ni Solomon pamoja na Silvia.



    Ilikuwa ni kawaida sana kwa Silvia na Solomon kuwakuta wakiwa wamekaa pamoja. Hiyo ndiyo hali niliyoikuta pia pale nilipoenda kuwapa yanayonisibu katika moyo na kichwa changu.



    Sikuwa na cha kuwaficha kwa sababu niliwaona ni kama kaka na dada zangu wa kwanza pale chuoni. Na niliwapenda kwa sababu walikuwa na uwezo wa kumshauri mtu bila hata ya kumsengenya, na walikuwa ni wasiri sana katika mambo waliyoelezwa na watu wengine, hata uwaudhi vipi, hawawezi kuropoka mambo yako hadharani. Hivyo ndivyo ilivyokuwa hata pale siku ile nilipowafuata.



    “Kaka Masai. Ile siku wakati unaenda kukaa pale mbele na dada Miriam, tayari nilijua lazima kutakuwa kuna zao la upendo baina yenu. Hivyo ndivyo mapenzi yalivyo. Yule aliyekuita Jay Z kisa Miriam, hakukosea hata kidogo. Alishayaona mapenzi yenu kabla ya nyie hamjayaona.”Alianza kuongea Silvia baada ya mimi kuwaelezea hisia zangu juu ya Miriam.



    “Mimi kabla ya kukushauri, kwanza napenda kusema kuwa namshukuru MUNGU kwani sasa umependa na utakuwa na mpenzi hivi karibuni, tena mpenzi mwenye kila sifa za kuitwa mpenzi, kuanzia mavazi tabia na hata maongezi yake.”Aliongea Solomon huku akionesha tabasam la ahueni katika uso wake na lenye wingi wa matumaini katika kile alichokiongea.



    “Sasa kaka, nashindwa kuelewa ni vipi Miriam atakuwa mpenzi wangu. Kwanza sisi ni marafiki wakubwa sana ambapo itakuwa ni ajabu kubwa kwa mimi kumwambia kuwa nataka awe mpenzi wangu. Na isitoshe, yule ni mtu mwingine hapa duniani, yaani siendani naye kwa kila kitu. Yeye ni mwenye hela na mimi ni wa kawaida tu! yeye mavazi yake ni Urusi na Marekani, mimi ni Saba Saba na nikijitutumua sana labda Peter Fashion.

    Baba yake ni Waziri huko nchi za watu, mimi baba yangu mstaafu wa zamani huko. Hatuendani hata kidogo.” Nilijikuta naongea vitu ambavyo kwa muelewa kama Solomon na Silvia, hawawezi kuvikubali hata kidogo.



    “Masai unanifurahisha sana. Nani kakuambia kuwa mapenzi ni muonekano wa nje au wewe ni nani? Nani kakuambia hayo Kaka Masai? Nani kakuambia mapenzi ni fedha au mavazi? Niambie sasa hivi nimfuate na nimpige hata vibao.”Aliongea Solomon huku akiwa kanikazia uso akisubiria jibu.

    Ilibidi niiname chini kuonesha kuwa sina uhakika na nisemacho. Akaendelea,



    “Kaka Masai ngoja nikuambie kitu kimoja kuhusu mapenzi.

    Hakuna ajuaye nini maana ya mapenzi hadi sasa. Kila mtu huyaelezea kwa jinsi alivyo yashuhudia. Kama ulimshuhudia mtu anakufa kwa sababu ya mapenzi, ni lazima useme mapenzi ni kifo. Kama ulishuhudia wapenzi wawili wanapendana hadi kufa, ni lazima useme mapenzi ni matamu.

    Kaka Masai, hujawahi kusikia msemo usemao kuwa mapenzi ni hisia ambazo kila moyo huzielewa?”Aliongea Solomon huku akimaliza na swali ambalo nililijibu kwa kutikisa kichwa kuonesha kuwa sijawahi kuhusikia.



    “Basi kama hujawahi kusikia hilo, mimi leo nakwambia kuwa, mapenzi ni hisia ambazo kila moyo huzielewa. Hakuna moyo ambao hutoelewa hisia za mapenzi katika dunia ya leo. Mapenzi huja tu. Mapenzi hayakwepeki Kaka Masai.

    Najua hunielewi na unaona sikujibu swali lako la ni vipi Miriam atakuwa wako. Ngoja nikuambie.

    Unajua Miriam kuwa na yeye ana hisia kama zako?”Alipoongea hivyo Solomon nilishtuka na kuuliza kivipi aseme hivyo? Akajibu



    “Hapo ndipo narudi kwenye hisia sasa. Yaani nyie, mkikutana hivi, macho yenu yanaonesha kuwa kila mmoja anampenda mwenzake sana tu. Miriam anakupenda sana Masai, niamini mimi nikuambiayo.

    Jinsi anavyokuangalia, na jinsi anavyoongea na wewe ni tofauti na anavyoongea na Chris, Saint au sisi hapa. Hizo ndizo naziita hisia za upendo. Hujiulizi kwa nini anakuomba wewe uende kupata naye chakula na siyo sisi?”Alizidi kuchombeza maneno yaliyoanza kunivuta na kuamini asemacho.



    Kiukweli tangu Generose apotee machoni mwangu, sikuwahi kufikiria kuwa ipo siku na mimi nitapenda tena kama zamani nilivyompenda Generose. Lakini hadi hapo tayari nilishaamini kuwa mapenzi ni maji kama alivyowahi kusema Solomon.



    “Kaka Masai. Hivi ushawahi kumuuliza Miriam alikuwa wapi kabla hajaingia huku Ugavi?”Aliniuliza Silvia.



    “Hapana.Sijui kiukweli. Ila nachojua ni kwamba Miriam alikuwa darasa tofauti na sisi lakini wote tunasomea Ugavi”.Nilimjibu.



    “Siyo kweli kaka Masai. Kama angekuwa anachukua masomo ambayo sisi tunayachukua, tungekuwa naye darasa moja”.Aliongea Silvia na kuniacha na swali.



    “Kwa nini unasema tungekuwa naye darasa moja?”Nikauliza.



    “Katika usajili wa wanafunzi, yule alikuwa ni wa kwanza kabla yetu. Hivyo jina lake lingekuwa katika mkondo wetu wa A. Kwa sababu gani ujue nasema hivyo. Wale wanachuo mia moja waliyosajiliwa mwanzo, wote wapo darasani kwetu. Hivyo na kama yeye angekuwa Ugavi, basi tungekuwa naye”.Alimaliza Silvia.



    “Sasa hapo unataka useme nini dada”.Nikimuuliza Silvia.



    “Hapa nataka nikuhakikishie kuwa Miriam anakupenda wewe. Mwanzoni Miriam alikuwa anasomea mambo ya Utawala wa Biashara (Business Administration-BA). Baada ya kupata sifa za kundi letu, ndiyo akaamua kuamia Ugavi ila lengo kubwa ilikuwa ni kutaka kuwa karibu na wewe”. Silvia aliongea maneno ambayo nilianza kuyaamini hasa nilipokumbuka maneno yake ya nyuma, kuwa alisikia mimi muongeaji sana na kuhusu kundi langu lote kukaa mbele halafu mimi nipo nyuma.

    Nilitabasam kidogo huku naangalia chini kama naona aibu, kisha nikaendelea.

    “Sasa Dada Silvia, haya yote uliyajuaje?”Nikamuuliza tena.

    CHANZO : http://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Ha ha haaa. Masai sisi ni watu wazima, tunaelewa. Mwanzoni niliona kuwa kuhama kwake darasa labda ni kimasomo tu! Lakini baada ya kuhamia kundini kwetu, kila muda akawa anataka kusoma na wewe, mara akiwa hajaelewa anakutaja wewe umsaidie. Hapo watu wazima tukajua sababu ya Miriam kuwepo pale”.Silvia aliniacha bila swali kuhusu Miriam kuhama darasa. Na niliamini kahama kwa ajili ya kutaka kuwa karibu na mimi.



    Itaendelea

0 comments:

Post a Comment

Blog