IMEANDIKWA NA : IGNAS MKINDI
*********************************************************************************
Simulizi : Mikono Michafu
Sehemu Ya Kwanza (1)
*******
KUNGELE iliita mara ya pili, kwa muda ule na mazingiza ya nyumbani kwangu yalivyo nilijikuta nashtuka kupata mgeni pasipo kuwa na taarifa, nikainuka na kutoka kwa haraka kupitia mlango wa siri ulionifanya nimuone kwa ufasaha mgeni anayegonga bila ya yeye kuniona kisha nikarudi ndani kwa ajili ya kuufungua mlango unaogongwa.
Wakati nilipokuwa namchungulia Yule mgeni, sikuweza kumtambua kuwa ni nani, nilimuona tu kuwa ni mwanamke tena yuko peke yake. Swali lililokuwa limebaki kichwani ni kumjua ni nani na anataka nini. Nikaufungua mlango na kukutana mtu nisiyemtarajia.
Nilibaki nimeduwaa kwa maana ugeni ule nilikuwa siuelewi elewi, nilijiuliza maswali mengi yasiyo na majibu kutokana na namna nnavyofahamiana na kwa jinsi tulivyopoteana na mgeni yule. Nilijiuliza ‘Kutembelewa na Mwajuma! Mwajuma kipaplipapli? Tena nyumbani kwangu?’
Kwa kweli sikumkaribisha kwanza ndani. Sio kwamba niliamua kufanya hivyo bali ni kitendo kilichotokea bila kukifikiria kabla hajanishtua kwa maneno yake.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Hunikaribishi ndani Musa?”
Kwa kweli nilijikuta natetemeka. Sikutetemeka kwa sababu ya kuniuliza hilo swali, bali kwa kuniita jina ambalo kwa muda wote niliokuwa nikifahamiana na Mwajuma, hakuwa akilifahamu jina langu halisi. Nilijikaza kiume na kumkaribisha sehemu ya maongezi yenye viti vyenye vikalio vya kufumwa na ukili. Kwa mara ya kwanza baada ya miaka kadhaa nikakaa karibu na Mwajuma.
Labda kwanza nijitambulishe, naitwa Musa Njiwa, mpelelezi wa kimataifa mwenye rekodi ya mafanikio ya asilimia mia moja kwenye kazi yangu hiyo na kunifanya niwe mmojawapo ya wapelelezi bora hapa nchini pamoja na kuwa na miaka michache katika taasisi ya Usalama wa Taifa nimekuwa nikiaminiwa na kupewa kazi kubwa zenye maslahi kwa taifa.
Japo ninakiri kuwa na kaudhaifu mbele ya kinadada warembo, mimi ni mume wa msichana aitwaye Tausi binti Nurdin ambaye kwangu ni malkia wa warembo aliyeweza kuuteka moyo wangu kiasi cha kuuendesha anavyotaka.
“Niambie Mwajuma” nilipata ujasiri wa kuanza kumuongelesha mgeni wangu.
Mwajuma akatabasamu akiniangalia, kitendo hiki kilinikumbusha mbali sana lakini nilijikaza nikabaki kumwangalia usoni. Mwajuma ana macho ya paka na uso wake umepambwa na pua ya wastani na midomo yenye ‘lips‘ nene. Sio rahisi kuugundua uzuri wake kwa haraka, cha kwanza utakachogundua ni tabia zake za kike ambazo muda zote zinakukumbusha kuwa uko na mtoto wa kike anayehitaji uonyeshe uanamume wako.
Rangi yake asili ya kahawia ilikuwa inaifanya ngozi yake yenye afya ing’ae halafu kwa ujinga wake kavaa vile ambavyo alikuwa ananiacha hoi. Mi nilikuwa napenda sana akivaa kihasara hasara, kwa wasiofumba fumba maneno huwa wanasema kuvaa kimalaya.
Siku hiyo kabla ya kuja Mwajuma ilikuwa ni asubuhi tulivu, nyumba yangu ikionekana kujawa na upweke wa hali ya juu. Mawazoni nilikuwa sehemu tofauti na chumbani nilipokuwepo japo nilikuwa sipajui mahali nilipopelekwa na mawazo hayo. Ndipo ghafla nikashtushwa na kengele ya mlangoni iliyoashiria kuwa kuna mgeni.
Niliuhisi moyo ukinienda mbio mithili ya gari lililofeli breki.
Moja kwa moja akili yangu ilirudi kwenye ugeni nilioupata siku nne kabla ya siku hiyo ambapo nilitembelewa na Mkuu wa usalama wa Taifa, tena bila taarifa yeyote. Kwa cheo chake, mtu huyu anaweza kuonana ama kuwasiliana na mheshimiwa Rais wakati wowote, ni mtu ambaye usalama wote wa nchi hii uko chini ya uongozi wake. Hiyo ilikuwa ni mara ya kwanza maishani kutembelea kwangu, na itakuwa ni mara yake ya mwisho bila shaka yeyote.
Mkuu alinitembelea ghafla akiletwa na usafiri maarufu kama bodaboda. Alikuwa amevaa suruari ya michezo, fulana nyepesi na raba kama aliyekuwa ametoka kwenye mazoezi ya kukimbia. Ni jambo la kustaajabisha sana lakini nilielewa kuwa hakuwa akitaka kujulikana kama anaenda mbali na nyumbani kwake japo kwa jioni ile sikujua ni kwa sababu gani aliamua vile.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Siku hiyo Mkuu alionekana kama ana mzigo mzito sana wa mawazo. Baada ya kubabaika kwa muda, nilimkaribisha ndani lakini hakuchukua muda mrefu kukaa ndani, alitaka tutoke. Aliniambia tunyooshe miguu ufukweni kwa kuwa nyumba yangu haikuwa mbali na bahari ya Hindi.
Wakati tukinyoosha miguu ufukweni, mkuu alinieleza kuhusu hali ya nchi ilivyo. Sikutaka kuamini kuwa alifunga safari toka kwake Oysterbay kuja Boko ninapoishi kwa ajili ya kuniambia habari hizo ila kilichonitatiza zaidi sikujua ni kwa nini alikuwa ananieleza hayo, ila nilidhani kuwa alikuwa akijaribu kupunguza mzigo wa mawazo kichwani.
Uzito wa maneno yake nilikuja kuutambua siku moja baada ya yeye kunitembelea nyumbani kwangu, siku ambayo nilipata taarifa kuwa Mkuu amefariki kukotana na moyo wake kusimama ghafla. Kwa mtindo wa maisha aliyokuwa akiishi mkuu, hata wewe ungeambiwa taarifa hizo ungeishia kucheka kwa kutoamini lakini ndivyo ilivyoamuliwa itangazwe.
Kifo cha Mkuu kiliniuma sana na kujihisi mwenye deni kubwa la kumuenzi na kufanyia kazi maneno yake. Nilikuwa nimefiwa na mlezi wangu katika kazi, mtu ambaye nilimtegemea kwa kila kitu katika kazi yangu. Alikuwa akinichukulia kama mwanaye.
Kwa mara ya kwanza toka nipokee taarifa ya kifo cha mkuu, nilijikuta mawazo yangu yanahamia kwingine japo kwa muda mfupi kutokana na ujio huu wa Mwajuma.
‘Ina maana nilikuwa nampenda Mwajuma kiasi hiki au basi tu uchu umenizidi?’ Nikajikuta nikijiuliza bila jibu.
Katika maisha yangu yote, Mwajuma ndiye msichana pekee aliyeweza kunidanganya na nikaamini kuwa yeye ni mgeni katika ulimwengu wa mapenzi aliyetendwa katika uhusiano wa kwanza na kumfanya asipende kuwa katika mahusiano. Sababu hiyo ilinifanya nizame kwenye penzi lake.
“Eeh baba kikombe hiki kiniepuke, ila ikibidi kukinywa ntakinywa” nilijikuta nikisali ile sala yangu kimoyo moyo nikiwa namwangalia Mwajuma huku udenda ukitaka kunidondoka.
“Mwajuma! Mwenzio nimeoa sasa hivi” nilijikuta nikilalamika kibwege kwa maneno yasiyojulikana yalipotokea.
“Najua umeshangaa mimi kukujua hapa, na zaidi kulijua jina lako halisi. Ukipenda nitakueleza ila kilichonileta ni matatizo, baba yangu amekamatwa huu ni mwaka wa tatu akihusishwa na tukio la ujambazi” alianza kunieleza akipuuza malalamiko yangu ya ‘kiboya’ yasiyo na kichwa wala miguu kuwa nimeoa.
Nilimkazia macho alipotamka neno ‘baba yangu’, akajua namaanisha nini.
“Ni baba yangu kweli Nasibu, ule ulikuwa ni utoto. Mbona we ulinidanganya kuwa unaitwa Nasibu hadi leo likanikaa mdomoni?” alijitetea Mwajuma.
Mwajuma alishawahi kunipeleka kwa wazazi wake nikajitambulishe kumbe hawakuwa wazazi wake wa kweli, walikuwa watoto wa mjini kama yeye. Enzi hizo nilikuwa nimekolea mbaya kwa Mwajuma. “Unadhani kwa kunifuata mimi utapata msaada gani?” nilimuuliza kwa utulivu nikiiga mtindo wake wa kupuuzia baadhi ya hoja.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“We unajuana na watu, pia una upeo mkubwa katika masuala ya sheria. Au na hilo ulikuwa unanidanganya?” alisema akiniangalia usoni.
“Yote ni kweli Mwajuma, unaweza kunieleza kwa ufupi kuhusu kesi yenyewe?”
Mwajuma alinielezea anavyojua yeye. Baada ya maongezi nilimuuliza amepajuaje pale ninapoishi , amefikaje na amejuaje jina langu.
“Usingeniuliza ningedondoka hapa hapa kwa mshangao”
“Na mimi ningekudondokea juu” niliropoka halafu nikaanza kujilaumu kwa kuonyesha uroho usio na tija.
Mwajuma alinielezea alivyoyajua mambo yangu japo sikuridhika na maelezo yake, niliamua kuufuata msemo wa ‘funika kombe mwanaharamu apite’. Alidai kuna siku aliniona maeneo ya Posta mpya nikiwa nasalimiana na mtu, mimi kwenye gari na huyo mtu alikuwa akitembea.
Eti akashuka kumuuliza huyo mtu habari zangu akamweleza. Yaani kwa kifupi hadithi yake haikuwa na mashiko.
Nikaamua kuwa na tahadhari kubwa kwa kila hatua ya utekelezaji jambo lililomleta pale. Japo nilikuwa na uwezo wa kumkatalia, niliona nijifanye mjinga ili nijue kitu halisi alichodhamiria. Ila kuna jambo moja lilikuwa linanikera katika maongezi yale, Mwajuma hakuonyesha dalili za kuwa bado ananipenda.
Unajua hakuna jambo ambalo huwa linanipa mzuka kama msichana akiwa anaonyesha kunipuuzia, huwa najiuliza maswali mengi sana na kutaka kujaribu kuwa ni kweli hahitaji kulala kifuani kwangu au ‘anajishaua’ tu. Kujaribu huko ndiko ambako kulinipelekea kuwa katika mapenzi na wasichana wengi bila sababu za msingi.
“Umekuja na usafiri gani, na una haraka kiasi gani?” nilimuuliza tukiwa tunaelekea ukingoni mwa kikao chetu kisicho rasmi.
“Nilikuja na taxi”alinijibu kwa zile pozi zake zilizokuwa zinanipelekea kuwa nusu mwehu kwake.
“Unaweza kunisubiri kidogo, nijiandae ili nikupeleke japo barabarani?” nilijikuta nikimuuliza kiuchokozi.
“Mkeo akiridhia”
Tulibaki tunaangaliana usoni, kisha nikajikuta nashusha macho yangu, nikashuhudia mapaja yaliyo wazi kwa sehemu kubwa kutokana na sketi yake fupi iliyochanua ambayo ameivaa.
Wakati nainua macho kumtazama tena usoni, nikajikuta macho yangu yanakwamia kifuani kwenye matiti manene wastani yaliyo kwenye blauzi laini ambayo ukiwa na macho makali kama yangu, unaona ‘yaliyomo’.
Mimi huwa ni mgonjwa sana wa matiti, sijui yana siri gani katika ubongo wangu. Huwa nikiyaona tu ubongo wangu unapigwa ganzi, mawasiliano kati ya akili na moyo yanakatika na kuuacha moyo uviamuru viungo vya mwili vishindwe kujikontroo na kuamua vitakavyo.
Mwili ulinisisimka, nikainua macho kumtazama Mwajuma usoni. Tabasamu lilikuwa limefutika kwenye uso wa Mwajuma uso huo ukabaki na kivuli cha huruma kilichojaa ukarimu huku macho yake yakiwa yamelegea. Tukatazamana kwa muda, Mwajuma akashusha pumzi ndefu.
Kwa muda ule mchache niligundua jambo moja kubwa, ‘sijapona ugonjwa wangu’. Mimi ni mdhaifu mbele ya kina dada warembo, lakini nilidhani kuwa baada ya kumuweka mikononi Tausi sitababaishwa tena warembo yaani nitakuwa mgumu kama ‘ukuta wa Berlin’ kumbe wapi ni kama ukuta wa udongo tu, nahitaji kufanya kazi ya ziada.
Nikahisi mambo yanataka kuharibika, nikainuka kwa haraka na kuingia ndani. Kitu cha kwanza kukifanya baada ya kuingia ndani, ni kuinua simu na kumpigia mke wangu Tausi. Tukaongea mambo mengi kuhusu mapenzi yetu na yeye alitumia fursa hiyo kunipa habari kuhusu zoezi aliloenda kulifanya.
Ni kama wiki moja ilikuwa imepita tangu Tausi asafiri kwa ajili ya kukamilisha program zake nchini Ufaransa ambazo alizianza wakati akiwa chini ya baba yake, Mzee Nurdin. Ilikuwa ni siku ambayo nilikutana na jambo ambalo lilinipa utata na shauku kubwa ya kutaka kulijua kwenye uwanja wa ndege wa kimataifa wa Mwalimu Nyerere, Dar es Salaam.
Ndege moja ya abiria iliwasili, abiria wa kwanza kuteremka alikuwa kijana mmoja mtanashati ambaye alitembea haraka haraka na kukamilisha taratibu zote za kutoka kisha akaingia kwenye gari moja la kifahari lililoegeshwa nje ya uwanja.
Kilichonitia mashaka ni kuwa baada ya kutoka tu yule kijana ndipo mbwa wa kugundua dawa za kulevya akaletwa na ukaguzi kuanza kama kawaida kwa abiria waliosalia. Nikanakili namba za lile gari bila kujali kama nitakuwa na kazi nazo ama lah kisha nikaendelea na shughuli yangu ya kumsindikiza Tausi.
Baada ya kumaliza kilichonipeleka pale, yaani kumsindikiza Tausi nikapata shauku ya kufuatilia taarifa za kuhusu gari lile. Nilishtushwa zaidi na ukweli kuwa namba za lile gari hazikuwa zikiendana na gari lile, na mmliki wa gari halisi lenye namba zile ana ubini wa mmojawapo ya majina matatu ya kiongozi mmoja wa kisiasa.
Nilipofuatilia zaidi nikapata taarifa kuwa mmiliki huyo aliwahi kuripoti kupotelewa na hilo gari lake lakini hakuwahi kufuatilia kama kuna taarifa yeyote iliyopatikana kuhusiana na gari lake alilodai limepotea. Cha kushangaza zaidi, baada ya kufuatilia nikalikuta ndani ya eneo lake la kuhifadhia magari likiwa limeegeshwa kwa mtindo wa kufichwa huku likiwa halina kibao cha namba.
Kwa jinsi tukio lilivyoenda pale uwanja wa ndege na huu muendelezo wake nikajiridhisha kuwa mheshimiwa anahusika na ile ni biashara haramu. Nikabaki na swali moja tu, kwanini ajihusishe na mambo haramu wakati kwa nafasi yake anaweza kupata mahitaji yote muhimu? Huo ndiyo ukawa mtihani wangu mkubwa.
Kwa siku mbili nilizofanya kazi ile nilijikuta nikipata maswali mengi zaidi kuliko majibu niliyoyategemea. Nilipata muunganiko wa ajabu sana uliotengeneza mtandao fulani ambao binafsi nilivutiwa kuujua mfungamano wao au kwa lugha nyepesi, japo linalowaunganisha hadi watengeneze mtandao huo. Ndipo nilipotatizwa na suala la Mkuu.
Mwajuma alikuwa nje ananisubiri wakati naongea na Tausi. Nilipomaliza kuongea na mpenzi wangu nikajiandaa na kutoka nikiwa mpya kabisa kumsindikiza Mwajuma kwa gari yangu kisha tukakubaliana kuwa tuonane kesho yake ambayo itakuwa ndiyo siku ya kesi ya baba yake kuendelea mahakamani.
Nilipotoka chumbani nilikuwa mpya kabisa tofauti na yule aliyekuwa akimtamani Mwajuma. Nadhani hata Mwajuma alishangaa kwa namna nilivyotoka na swaga tofauti na nilivyoingia chumbani.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
******
Ngoja nikujuze kidogo kuhusu kisa cha Mwajuma ‘kipaplipapli’…..
Miaka kadhaa iliyopita nilipewa kazi maalum kuipeleleza taasisi fulani ya fedha kama inatekeleza sera yao ya kuwawezesha kina mama wa kipato cha chini, sera ambayo iliifanya serikali kuipa ruzuku kubwa.
Ili kuifanikisha kazi hiyo ilinibidi nikapange chumba eneo ya uswahilini ambalo ni mojawapo ya maeneo yaliyotajwa katika mipango yao ya utekelezaji. Huko ndiko nilikutana na Mwajuma.
Hiyo ilikuwa ni kazi yangu ya kwanza toka nihitimu mafunzo ya upelelezi na ndiyo ilinifanya niamininike zaidi na kupewa majukumu makubwa ya ndani na nje ya nchi.
Nilipokuwa maeneo yale nilikuwa nina kawaida ya kula kwa dada Salome, huyu ni mama lishe wa jirani ya pale nilipokuwa nakaa. Alikuwa akipika chakula kizuri sana na kwa usafi mkubwa hivyo wengi tulikuwa tunapenda kwenda kula pale. Na mara nyingi baada ya kula nilipenda kukaa na kupiga stori mbili tatu na dada Salome ambazo zilinisaidia katika kazi yangu.
Siku moja wakati nakula, akaja Mwajuma ambaye alionekana amekwazwa na jambo fulani kubwa sana. Akaongea kwa muda na dada Salome kisha akataka kuondoka kabla dada Salome hajamwambia kwa sauti kubwa kuwa amsubiri amalize kazi waondoke wote.
Sikuonekana kumtilia maanani sana Mwajuma, lakini alianza kugusa hisia zangu alipomsaidia dada Salome kazi ya kuninawisha mikono. Mtoto alipiga goti kwa heshima, nikakumbuka mabinti wa kisukuma nilivyoenda Sengerema kumtembelea rafiki yangu mmoja.
Si kawaida ya mabinti wa uswahilini kuwa na heshima ya vile, nikawa nanawa mikono huku namkagua kitendo kilichomshtua dada Salome kiasi cha kunitupia maneno ya utani.
“Nasibu vipi, kisu kimegusa mfupa?”
Nikajikuta natabasamu bila kujibu neno, ila cha ajabu Mwajuma hakuonyesha kama aliyajali yale maneno. Sikujua kama alielewa akajikausha au hakujua dada Salome anaongelea nini.
Jina la Nasibu ndilo nililokuwa nikilitumia katika kazi yangu ile na wengi walijua kuwa nafanya kazi kwenye ofisi ya wakili mmoja katikati ya jiji kama karani.
Baada ya kunawa nikaendelea kuwepo pale kama kawaida yangu kupiga stori lakini siku hiyo dada Salome hakuonyesha kama anahitaji stori kutokana na ule ugeni wa Mwajuma, nikaamua kuaga.
“Mbona husubiri nikutambulishe? Huyu anaitwa Mwajuma au tumezoea kumuita kipaplipapli”
Mwajuma akamwangalia dada Salome kwa jicho la kumkataza. Dada Salome akamgeukia Mwajuma.
“Huyu anaitwa Nasibu, anatusaidia saidia mambo ya kisheria. Anafanya kazi ofisi ya mawakili mjini.”
“Nashukuru kukufahamu Mwajuma” nilijibu nikimpa mkono ambao Mwajuma aliupokea akibonyea kwa heshima huku akinitupia jicho la wizi.
“Usije kummezea mate bwana ‘angu” sauti moja mbaya ilisikika ikitokea upande wa jikoni kisha akatokea dada mmoja aliyebarikiwa kuwa na sura mbaya na umbile ambalo sio rahisi kujua mbele wapi, au nyuma wapi endapo angevaa nguo kubwa ya moja kwa moja halafu akasimama gizani.
Kitu kilichokuwa kikinikera pale kwa dada Salome, ni Zaituni, huyu dada alikuwa anajifanya kumsaidia dada Salome lakini nadhani alikuwa akitafuta mabwana kwa maana alikuwa akinisumbua kila siku akitaka kulazimisha mapenzi au watoto wa mjini wanasema ‘kujiweka’.
“Namimi nafurahi kukufahamu shemeji” alijibu Mwajuma na kumfanya dada Salome alipuke kicheko na kunifanya nizidi kukereka.
“Njoo basi unichumu Nasibu wangu” aliniambia Zaituni akinisogelea na kusababisha harufu ya viungo vya mchuzi vilivyochanganyikana na jasho kutawala kwenye pua yangu.
“Sipendi!” nilijikuta nikisema kwa hasira kiasi cha kumshangaza Zaituni mwenyewe na dada Salome kwa sababu mara zote akinitania huwa naishia kucheka tu na kuondoka.
“Mnh! Leo?” aliguna dada Salome kisha akaendelea “ Zaituni, usije kunifukuzia mteja wangu. Kama hapendi huo utani ni bora ukauacha”
Wakati wote Mwajuma alikuwa kama anaangalia sinema. Mi nikajifanya kutaka kuondoka kwa hasira.
“Basi nisamehe Nasibu, sikujua kama hupendi utani huu” alijisemesha Zaituni kwa aibu.
“Usijali, ili mradi ushaelewa kuwa sipendi hamna tabu” nilijikakamua kuongea.
Ni kweli kuwa nilikasirika lakini kwa wakati ule sikuwa najua kama nilikasirika kwa vile alikuwa akihatarisha uwezekano wa kumng’oa mtoto Mwajuma. Kimsingi hata mwenyewe nilijishangaa kuwa hasira zile zilikuwa zimetokea wapi usiku ule.
Inaelekea dada Salome alishajua kinachoendelea kichwani mwangu japo hata mimi mwenyewe nilikuwa bado sijakijua kwa kuwa alikuwa akiniangalia kama mtu anayenisoma mawazo yangu.
Baada ya siku mbili tatu za kutomwona Mwajuma nilijikuta nikivunja ukimya kwa dada Salome na kumuulizia.
“Ingepita wiki bila kumuulizia ningetembea bila nguo toka hapa hadi nyumbani” dada Salome alianza kujibu kwa maneno yake ‘mbofu mbofu’.
“Hata yeye alikuulizia kutaka kujua habari zako, basi acha nikupambe mdogo wangu, yaani ungesikia maneno niliyomwambia ungeninunulia soda. Mwajuma kipaplipapli yupo nikupe namba yake?” aliendelea dada Salome na kuuliza swali la kizushi.
“Kwanini mnamuita kipaplipapli?” nilimuuliza kuzuga kabla sijaichukua namba yake ya simu.
“Sasa ukimpigia si ndio utamuuliza mwenyewe?” alinijibu dada Salome huku akinisogezea simu yake kunipa namba ya simu.
Kama alijua kuwa nisingeweza kutamka kuwa naitaka namba yake, niliipokea simu ya dada Salome nikijifanya kuinakili namba ya Mwajuma kwa shingo upande kumbe moyo wangu ulikuwa ukinidunda kwa shauku ya kuipata namba yake.
Kwa jinsi Mwajuma anavyoonekana, ni kama anamstahili mwanamme anayejua kulea mpenzi wake, mwanamme anayeweza kudekeza. Yaani nilijihisi kama ni mimi peke yangu mwenye sifa zinazostahili kuwa karibu na Mwajuma kutokana na huruma yangu kwa watoto wa kike. Ukimwona tu jinsi alivyo utatamani umkumbatie akulalie mabegani akuelezee mahitaji yake ili umtimizie.
Kama Mwajuma anakuja na tatizo nawe mfukoni una hela ya kodi ya nyumba tu, lazima utampa. Anavutia kutatuliwa matatizo yake yote ili aishi kwa raha duniani. Nikamkumbuka mzee mmoja aliyewahi kunihadithia safari yake ya Tanga enzi hizo.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Aliniambia kuwa kutokana na wema aliotendewa na mtoto wa kitanga aliyekuwa mwenyeji wake, alijikuta kila alichowaza kumpa dada yule anakiona kidogo, mwishowe akaamua kumtoroka alfajiri tena kwa kulisukuma gari kwa umbali mrefu ili asije kumshtua usingizini.
Baada ya kutoka kwa dada Salome, nikajiandaa kabisa kulala na kujilaza kitandani ndipo nikampigia simu Mwajuma. Ndugu yangu, Mwajuma kajaliwa sauti ya kike! Yaani kama ndiyo hivyo una siku nyingi, unaweza kujikuta unajichafua. Tuliongea mengi ya kawaida hadi tukahamia idhaa ya hadithi za mapenzi.
Tuliongea mengi na kimsingi aliniaminisha kuwa hayuko katika uhusiano wa kimapenzi kutokana na kuumizwa na mpenzi wake wa kwanza. Nilijikuta nikimshangaa mwanamme mwenzangu aliyeshindwa kumtunza binti mwenye mvuto wa kipekee kama Mwajuma.
Nikikumbuka nilivyosumbuka siku ya kwanza kufanya mapenzi na Mwajuma akijifanya hajazoea, huwa najikuta nikijicheka mwenyewe. Ila aliweza kujikontroo na kuonyesha kuwa anazoea pole pole hadi akawa fundi kabisa. Nikajiona bonge la shababi kumbe ye alikuwa ananiona boya tu.
Huo ndiyo ulikuwa mwanzo wa uhusiano wangu na Mwajuma. Kwa kweli nilikamatika kiasi cha kutangaza kuwa nataka ndoa na Mwajuma. Hapo ndipo nilipopelekwa kwa Mzee mmoja wa mjini maarufu kama Anko Kidevu, Mwajuma akidai kuwa ndiye baba yake.
Kutokana na mapenzi yetu kuyaendesha kwa siri, nilichelewa sana kupata stori kuhusu Mwajuma. Na mwenyewe alikuwa anajitahidi sana kuniganda ili nisipate muda wa kongea ongea na watu na kweli alifanikiwa. Lakini mchezo mzima ulikuja kuwekwa wazi na Zaituni baada ya kutibuana na Mwajuma.
Siku hiyo sitaisahau maishani mwangu kwa maana Zaituni alikuja nyumba niliyopanga akiwa ameongozana na mashoga zake na matarumbeta kuja kusutana na Mwajuma, ndiyo hapo siri zote zikafichuka na Mwajuma akanitoroka kabla sijamuona tena alipokuja nyumbani.
Kumbe hilo jina la kipaplipali alikuwa alipewa na wenzake kwa kuwa kila mwanamme anayemjaribu huwa hamuachi hadi Mwajuma mwenyewe aamue kuvunja uhusiano wakawa wanamtania kuwa ana utamu wa ‘Fanta kipaplipapli’
*******
Tatizo la macho huwa hayana mipaka halafu tabia haina dawa, wakati naingia na gari langu katika viwanja vya mahakama ya Hakimu mkazi wa Kisutu, macho yangu yalitua moja kwa moja kwa binti mmoja aliyekuwa kanipa mgongo. Ili kupata figa kama ya binti huyo akinadada wengi hujikuta wakihudhuria kwenye ‘gym’ karibu kila jioni.
Kwa kusema ukweli starehe yangu kubwa huwa ni kuwaangalia mabinti warembo, nakumbuka toka wakati nasoma sekondari nilikuwa kila nikitoka shule jioni hukaa pale Posta mpya na kuanza kuangalia wasichana warembo wakienda na kurudi. Nafsi yangu ikishiba napanda daladala kurudi nyumbani. Basi nimejikuta hata sasa napenda kukodolea macho warembo kisha nawaacha waende zao bila kuwasemesha.
Baada ya kuegesha tu gari nikaanza juhudi za kuiona sura yake ili nione kama kuna uwiano kati ya sura na umbile lile, niliona kuwa ni vyema niitendee haki nafsi yangu kabla ya kuingia ndani kusikiliza kesi niliyoifuata. Nikajifanya natoa simu kuongea na mtu huku nikielekea upande aliopo mlimbwende yule aliyekuwa akionekana anamsubiri mtu.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment