Search This Blog

Sunday, 19 June 2022

MJI TULIVU ULIONIPA UGONJWA WA MILELE - 1

 





    IMEANDIKWA NA : GEORGE IRON MOSENYA






    *********************************************************************************



    Simulizi : Mji Tulivu Ulionipa Ugonjwa Wa Milele


    Sehemu Ya Kwanza (1)





    Maisha wakati mwingine si jitihada pekee zinazoweza kukutoa sehemu moja kwenda nyingine, kuna wakati bahati inahusika katika maisha.

    Si kwa wote lakini mimi nilibahatika kuwa mtoto kutoka familia ya kimasikini ambaye baadaye nilienda kusoma na kisha kupata kazi nzuri ambayo ilinitoa katika umasikini na kunitupa katika daraja la kati na baadaye nikawa tajiri.

    Nikayabadili maisha ya kizazi changu na kuwaweka katika mirija ya kujiendesha wenyewe.

    Hadi ninafikisha miaka thelathini tayari nilikuwa nimeyaweka maisha yangu sawa, nikiwa nimesaidia ndugu zangu kwa kiwango cha uwezo wangu pamoja na marafiki pia.

    Baada ya kutimiza ndoto hizi ndipo kwa mara ya kwanza nikafikiria juu ya utulivu wa hali ya juu niliokuwa nauhitaji na niliwahi kuuota tangu nikiwa nasoma, nilijiahidi kuwa nitakapomaliza kuinyanyua familia yangu sasa nitaangalia vyema maisha yangu.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Niliwahi kuwa na marafiki wa kike lakini sikuwahi kunyanyua kinywa changu na kuwatamkia kuwa nina nia ya kuingia nao katika ndoa.

    Nilikuwa nina deni, sikutaka nijiongezee majukumu mengi yatakayosababisha nishindwe kutimiza vile nilivyopanga kutimiza.

    Katika mkesha wa mwaka mpya nilimpigia mama yangu simu na kumweleza bayana kuwa ndoto mojawapo katika mwaka unaoanza ni kuyabadili maisha yangu kwa kujihifadhi katika mji tulivu.

    Akaniuliza iwapo nataka kuhama Tanzania, nikacheka na kumweleza kuwa sina wazo la kuhama Tanzania bali nahitaji kuingia katika mji tulivu.

    “Unataka kuoa?” mama aliniuliza.

    Nikacheka bila kumjibu chochote, naye akacheka kisha akanitakia kila la heri. Nikampongeza kwa kuelewa maana yangu upesi sana!
    _____
    Mwaka ulianza vyema na shughuli zikiendelea kama kawaida huku lile wazo likiwa kapuni kusubiri utekelezaji wake.

    Naomba niweke wazi kuwa nilikuwa aina fulani ya mwanadamu ambaye napenda sana kufanya jambo kadri ya wakati, maana niliwahi kufanya mambo mengi kwa wakati mmoja na kujikuta nikiharibu ama kutoyafanya kwa ufanisi mambo mengine.

    Hivyo sikuwahi kupanga siku ya kuusaka mji ule tulivu!!

    Siku hii ikiwa ni miezi miwili baada ya mwaka kuanza pale ofisini kwetu palikuwa na nafasi za kazi zilikuwa zimetangazwa na watu wengi sana walikuwa wameomba nafasi. Katika ile hatua ya awali ya usahili walifika wasahiliwa mia moja na hamsini.

    Nafasi zilikuwa tano tu zilizokuwa wazi. Katika ngazi ya mwisho kabisa nd’o ambayo mimi na wakurugenzi wenzangu tulikuwa tunahusishwa lakini hatua za awali walisimamia wenzetu waliokuwa na vyeo vya chini.

    Baada ya hatua za awali hii siku ndiyo ilikuwa ile ya kupata mbivu na mbichi.

    Wasahiliwa ishirini wa mwisho.
    Katika usahili nilikuwa natazamwa sana, hakika sikuwa mtu wa mchezo, ukifanya vibaya usitarajie kuwa nitakubeba kisa tu u msichana ama umeonyesha huruma ya aina yoyote.

    Sikuwa mtu wa aina hiyo kabisa, na kilichokuwa kinanifanya niwe hivi ni njia ambazo nilikuwa nimepitia, hakuna njia ya panya yoyote niliyopitia katika safari yangu ya kimasomo hadi kutafuta kazi.

    Na pia nilikuwa nina hofu na Mungu!

    Kitendo cha kumpitisha mtu asiyekuwa na vigezo na kumwacha mwenye vigezo kungeisononesha nafsi yangu sana.

    Katika usahili nilikuwa naogopwa sana.

    Hata siku hiyo nilikuwa yuleyule, maswali yangu yalikuwa si magumu lakini yenye mitego. Maswali yangu yakiwa na nia moja tu, kuupima uelewa halisi wa msailiwa.

    Walipita wasahiliwa wote katika hatua ya kwanza, niliwanukuu majina yao.

    Baada ya hatua zote za usahili kumalizika hatimaye tuliwaeleza kuwa baada ya majuma mawili tutawapigia simu katika nambari walizotuachia.

    Tukawaaga wakaondoka!!

    Masuala ya usahili yakaishia hapo…..
    Nikaendelea na shughuli nyingine hadi majira ya saa tatu usiku ndipo niliifunga ofisi yangu na kutoka nje kuelekea katika gari langu.

    Nilifungua mlango na kuiwasha gari nikaiacha ikiunguruma kwa muda huku nikiwa nimewasha kiyoyozi ili kuleta hewa safi, mara nikasikia hatua zikijongea nilipokuwa. Nikatambua huyo atakuwa aidha mlinzi ama kijana mwingine tu amekuja kuniomba shilingi mia tano.

    Nikaandaa hiyo pesa ili tusizungumze sana.

    Sikuwa napendelea sana kusikiliza maelezo yao kwa sababu huwa wanadanganya wana njaa kisha ukiwape pesa wanaenda kujidunga madawa ya kulevya.

    “Samahani kaka…” nikaisikia sauti ya kike.

    Nikageuka upesi kumkabili anayeniita, sikuitarajia kabisa sauti ya kike muda ule. Sikuwa na mazoea na watoto wa kike kabisa. Mazoea ya kikazi yalitosha kabisa!

    “Nikusaidie nini?” nilimuuliza bila kuijibu salamu yake.

    “Naitwa Nyambura…. Naitwa Nyambura Kone…” alijitambulisha jina lake.

    “Samahani sidhani kama nakufahamu..” nilimjibu huku nikijiandaa kuingia garini ili niondoke.

    Akajieleza kuwa siku hiyo alishiriki usahili katika kampuni ninayofanyia kazi.

    Aliposema vile jina likanikaa sawa kichwani.

    Anataka kutoa rushwa!! Nilijiwazia huku nikimsikiliza aendelee kuzungumza na hapo nikamwomba ajieleze kwa haraka kidogo, kichwani tayari nikiwa nimepanga shambulizi kubwa na kumpa ili nimuaibishe ikiwa atanishawishi kunipa rushwa ya aina yoyote, tena bora angezungumzia pesa ila akithubutu kunieleza rushwa ya ngono hata vibao nitamchapa hadharani.

    Akajikohoza kisha akazungumza.

    “Naitwa Nyambura..” nikamzuia kwa mkono na kumsihi aendelee kwani jina lake tayari alilitaja awali. Na huku niliona ni kupoteza muda anakoelekea.

    Yule binti aliyejitambulisha kwa jina la Nyambura Kone akajieleza.

    “Mimi ni mtoto wa tatu katika familia yangu… nimetoka Musoma vijijini kuja jijini Dar es salaam kwa ajili ya usahili huu, usahili ambao naamini kuwa kwa leo hakika sijafanya vizuri, lakini hiyo sio tafsiri ya jinsi nilivyo, ninauguliwa mama yangu na sijui hata kama nitamkuta akiwa hai, sijala tangu nilipokula jana mchana, zaidi ya yale maji mliyotupatia sijala chochote….. nimekuja kwa miguu katika usahili na nitarejea kwa miguu kama unavyoniona…. Nakusihi sana na sijui kwanini nimekusudia kuonana na wewe lakini nakuomba utakapofanya maamuzi basi nipe nafasi ya upendeleo. Sipo kama nilivyojaribu kujieleza katika usahili…. Nina matatizo makubwa sana yananikabili… ni matatizo yangu na si ya kampuni yenu lakini nakuomba kwa maelezo yangu haya mafupi unisaidie uwezavyo. Mama yangu anakufa, lakini wadogo zangu wanahitaji kula, achana na kusoma maana imeshindikana tayari… mimi ni kila kitu kwao.” Aliweka kituo yule binti. Akabaki kunitazama

    Maneno yake hayakunishawishi sana, kwa sababu ninaamini katika ushawishi wa katikati ya chumba cha usahili na si vinginevyo.

    Nikaitoa pochi yangu na kutoa noti tatu za shilingi elfu tano nikampatia kama nauli na nikamweleza kuwa nimesikia ombi lake.

    Nilimweleza ilimradi tu kuyamaliza yale mazungumzo, aondoke na mimi niondoke.

    “Namba ya simu si yangu ni ya huyo aliyenipokea, ikiwa nitapata nafasi ya kupigiwa simu utamwambia anifikishie ujumbe.”

    Akamaliza kunisihi huku akishindwa walau kutoa shukrani kwa kiasi cha pesa nilichompatia.

    Hakika jambo lile liliniudhi sana, nikahisi huyu ni changudoa aliyebobea na kwangu mimi alitaka pesa nyingi ili niununue mwili wake, sasa sijaununua na nimempatia kiasi kidogo cha pesa.

    Pesa zangu ziliniuma sana!
    Niliondoka pale lakini sikwenda nyumbani moja kwa moja, sikuwa nimeoa niliishi peke yangu. Hivyo ilinilazimu kupita hotelini kupata chakula.

    Kitendo cha kuondoka eneo lile nikamsahau na kumpuuzia yule dada aliyejitambulisha kwangu kwa jina la Nyambura!

    Nilipomaliza kupata chakula, wakati nalipia bili ndo nikamkumbuka tena Nyambura na kujisemea kuwa laiti kama nisingempatia ile pesa basi ndo ningeitumia kulipa ile bili ya chakula.
    Niliondoka pale, sasa nilikuwa naelekea nyumbani.

    Tofauti na siku zote, nilishangazwa na ile foleni katika barabara ya Morogoro kutokea Kariakoo nilipopitia, nilitazama saa yangu na ilikuwa saa nne usiku. Foleni ilikuwa kubwa kiasi kwamba gari zilikuwa hazitembei kabisa.

    Taratibu taratibu hadi gari ikafikia kile chanzo cha foleni, kuna ajali ilikuwa imetokea.

    Nilipotambua kuwa ni ajali nikapandisha vioo vya gari langu, kwani mazingira kama hayo kwa jiji la Dar es salaam huwa vibaka nao wanaingia kazini.

    Lakini nilibaki kutazama nione hiyo ajali kupitia kioo kwenye kioo.

    Hapo sasa gari zilikuwa hazitembei kabisa, nikashusha vioo na kujaribu kuwauliza madereva waliokuwa wameshuka.

    Wakanieleza kuwa njia imefungwa kwa mbele, raia wamegomea gari zisiondoke kwa sababu katika hii foleni ipo gari iliyogonga!

    Niliishiawa nguvu nikaamua kushuka na mimi garini.

    Nilidadisi na kuelekezwa majeruhi alipokuwa.

    Nilifika na kujikuta natazamana na mwanamke aliyejivika mavazi mafupi sana yaliyouacha mwili wake wazi, vijana wa pembeni wakawa wanamteta wakisema kuwa ni changudoa alikuwa kazini. Mwil wake ulikuwa umetokwa na fahamu na hakuonekana kujeruhiwa sana…..

    Maneno yale yakapenya na kunifikia, nami nikakiri kuwa huenda kweli ni changudoa.

    “Unasema changudoa… unamaanisha changudoa ana haki ya kugongwa na gari akiwa upande wake sahihi…. Sharia ya wapi uliyoisoma wewe inayoruhusu mtu kugongwa na gari kwa sababu tu ya shughuli zake…. Sikiliza kaka usipokuwa na uhakika na kitu ni heri ukakaa kimya! Angekuwa dada yako ungesema sawa afe kwa sababu ni changudoa!!!” ilisikika sauti kali ya kike ikijibu mapigo kwa jazba.

    Nikaguswa na maneno yake, kwa sababu nami na elimu yangu nilikuwa nimekiri kuuwa ni sawa tu agongwe kwa sababu ni changudoa.

    Nikageuka kutazama ni nani anayetokwa na maneno yale makali.

    Nyambura!! Mungu wangu, nilishtuka sana.

    Sijui ni kwanini nilishtuka vile, lakini kuna kitu kama hofu kiliniingia.

    Nikachelewa kubandua macho yangu kwake, mwishowe nikajikuta natazamana naye.
    NAKUSIHI!!
    Usimuhukumu mtu yeyote kwa sababu ya muonekano wake, kwa sababu ya kipato chake, kwa sababu ya kabila ama imani yake kidini.

    FIKIRI KABLA HUJATENDA!!
    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
    **************
    Ndugu msomaji, nilikusihi usimuhukumu mtu kwa sababu ya kile unachofikiri wewe juu yake.

    Na sasa Nakusihi tena JIPIME MARA mbili zaidi kabla hujapata wasaa wa kumpima mwenzako


    Baada ya yule dada kutonitambua sikupoteza wakati zaidi eneo lile, nilihisi kuwa na yeye ni walewale.

    Nikazikumbuka pesa zangu, na hapa nikakiri kuwa yule binti alikuwa ananitaka kimapenzi hakuwa na lolote la ziada, sasa Mungu kawapa pigo.

    Nikajiondokea nikaingia kwenye gari na hapo foleni ilikuwa inaanza kusogea. Bila shaka huko mbele palikuwa pamesuluhishwa tayari.

    Nilifika nyumbani kwangu nikiwa nimechoka sana nikajitupa kitandani, kwanza nikapitiwa na usingizi nikaja kuamka baadaye sana nikaoga na kulala tena.

    Asubuhi nilikuwa nimemsahau yule dada na vimbwanga vyake.
    _____
    BAADA YA JUMA MOJA, majina yalikuwa yametoka tayari. Sikukumbuka wala sikujali juu ya yule dada ambaye alihitaji nimsaidie aweze kuchomoza na kwa jinsi nilivyompa alama chache katika ule usahili basi ilikuwa lazima tu aanguke.

    Kweli hakuwemo!
    Nilikuwa ofisini kwangu nikapokea simu kutoka kwa Hadija ambaye ni katibu muhtasi wangu, nikaipokea upesi na kumsikiliza huku nikimsihi kuwa nitapenda zaidi kama atazungumza kwa muda mfupi. Alinieleza kuwa yupo mtu anahitaji kuonana na mimi na amesihi sana kuwa ni muhimu.

    Nikamruhusu aingie.

    Zikapita sekunde kadhaa kabla mlango wangu haujasukumwa.

    Alisimama mbele yangu yuleyule binti, Nyambura!

    “Shkamoo..” alinisalimia.

    Nilisita kuitikia kwa sababu nilitambua wazi kuwa umri wake haukuwa wa kuniambia mimi shkamoo.

    Alisalimia tu kwa sababu ya nidhamu ya uoga.

    “Habari yako…” nikamsabahi.

    “Jina langu halipo katika orodha,” alisema kisha akaendelea, “Ni kwa sababu haukuweza kunisaidia…..” akajaribu kuzungumza lakini akakosa cha kusema. Akabaki kutupatupa mikono hewani.

    “Kuna jingine labda naweza kukusaidia…” nilimuuliza huku nikipambana kuizuia hasira yangu isichukue nafasi kubwa.

    Maana niloiona yule binti ananichukulia mimi dhaifu kama wanaume wengine….

    Akazungumza huku akiwa amesimama, akanieleza kuwa mama yake alikuwa amepoteza maisha tayari. Akanisihi kama ninao msaada wowote ili aweze kufika Musoma basi nimsaidie.

    “Ujue ile siku ya kwanza nilipokusaidia sio kwamba nilikuwa boya sana, naomba uondoke na kamwe usirudi hapa….” Nilimkaripia huku nikisimama.

    Akanikazia macho yake kisha akazungumza.

    “Unaweza kunipiga kama utahitaji… mwili huu umezoea suluba tayari.” Alinijibu kiujasiri.

    Kisha akaendelea kuzungumza, alisema mengi sana ambayo labda yangemgusa mwanaume wa kawaida, lakini mimi yalionekana kama maigizo tu na hakuna alichokuwa anamaanisha.

    Hakika sikumsaidia kitu chochote.

    “Naitwa Nyambura! Asante sana kaka kwa moyo wako….” Alimaliza kisha akaondoka.

    Alipoondoka nikatazama fungu la pesa lililosheheni katika meza yangu pale ofisini, pesa ambayo niliipata kwa kazi isiyokuwa ya kutoa jasho.

    Kwani ningempa hata laki ningepungukiwa nini! Nilijiuliza.

    Nikanyanyua simu ya ofisini, nikampigia Hadija na kumuuliza kama yule binti anaonekana pale amwite.

    Akanambia kuwa amepita kasi huku akiwa analia sana.

    “Kwani umemfanyaje?” aliniuliza.

    Moyo ukaniuma, nikakata simu na kujikuta najuta.

    Hivi ninakuwaje mimi! Sasa najuta nini? Si ni ukweli ni malaya yule na ananiongopea tu hapa au!!

    Nilijifariji lakini bado moyo wangu ulikuwa hauna amani.

    Ilikuwa kawaida yangu nikiwa naikosa amani ya nafsi basi huwa nampigia mama yangu mzazi na ananishauri ama kunitia moyo.

    Hata siku hii nilimpigia pia.

    Nikamweleza juu ya hali ile, ilimsikitisha pia lakini mwisho alisema kuwa mjini pana mengi.

    Huenda hata huyo ananiongopea tu!

    Akanisihi niwe na amani.

    Kweli amani ikatawala.

    Nikaachana na Nyambura.
    _____
    Baada ya miezi miwili kupita afisa habari wa kampuni alipoteza maisha kwa kile kilichosemekana alikula ama kulishwa chakula chenye sumu, hivyo baada ya muda fulani nafasi ya kazi ikatangazwa.

    Na kitendo cha kuwa na afisa habari mmoja kilisababisha wakurugenzi na bodi nzima wapendekeze kupatikana kwa maafisa habari wawili yaani mtu na msaidizi wake.

    Nafasi za kazi zikatangazwa magazetini. Kama kawaida wasahiliwa kutoka kila kona wakafika na bahasha zao za kaki siku ya usahili.

    Kwa sababu afisa habari alihitajika upesi sana usaili huu ulifanyika siku mfululizo.

    Hatimaye yakabaki majina sita ya mwisho.

    Hawa walipangiwa siku yao, wanawake watatu na wanaume watatu.

    Ikafika siku yao ya usahili wa ziada kama ulivyo utaratibu wa kampuni.

    Wasahiliwa wakaingia mmoja baada ya mwingine.

    Hatimaye wakalifikia jina la Neema Wilson.

    Akaingia binti ambaye kimavazi alipangilia kama ilivyostahili, nikatazama katika karatasi zangu, binti yule alikuwa vizuri katika lugha tatu… kifaransa, Kiswahili na kiingereza.

    Nikaamua kuwa mchokozi nikachagua kuzungumza naye kifaransa katika usahili wake.

    Kwa sababu wenzangu walikuwa hawajui lugha hii wakaniachia mimi mwenyewe.

    Nikanyanyua uso wangu ili nimtupie swali la kwanza.

    Mungu wangu! Nilikuwa natazamana ana kwa ana na Nyambura, yule binti kutoka Musoma ambaye aliwahi kufanya usahili katika kampuni yetu.

    Swali nililopanga kuuliza likayeyuka nikajikuta natokwa na swali ambalo sikutarajia.

    “Wewe ni Neema ama Nyambura….” Nilimuuliza. Akanitazama kwa sekunde chache akiwa hana mashaka hata kidogo akanieleza kuwa yeye ni Neema.

    Nikajaribu kujiweka sawa nikauliza maswali ya msingi kwa kifaransa, akanijibu vyema.

    Nikamruhusu atoke.

    Lakini nikimweleza kwa kifaransa kuwa aningoje nje!

    Akatii!

    Baada ya usahili nikaonana naye na kumuuliza kwa mara ya pili jina lake ni nani.

    “Naitwa Nyambura!” alinijibu bila wasiwasi.

    “Na kwa nini umejitambulisha kama Neema.” Nilimuuliza kitafiti.

    “Neema ni jina langu pia. Unaweza kunitambua kwa yote ukihitaji….” Alinijibu kisha akaniaga na kuondoka.

    Lakini kabla hajafika mbali aligeuka.

    “Hauamini kama mimi ni Nyambura…. Ulinipa elfu kumi na tano mara ya mwisho na sasa sijakuomba hata kunisaidia ili nipate nafasi katika kampuni yako…” alinieleza kisha akaondoka zake, akianiacha nisijue kuna kitu gani kinaendelea.
    Upesi nkatika ofisi yangu nikapekua nyaraka kadhaa za wasahiliwa wa wakati ule wa Nyambura. Nikakutana na nyaraka zinazoelezea wasifu wa Nyambura… nikabahatika kuona viambatanishi.

    Cheti chake cha kidato cha nne kiliandikwa jina NYAMBURA na cha kidato cha sita pia.

    Nikaviweka kando na kutazama hivi vya sasa.

    Jina lilikuwa NEEMA…..
    Ni kitu gani anaficha huyu binti? Nilijiuliza huku nikizidi kushangaa ile kasi ya kuingia katika akili yangu ilivyokuwa inaongezeka.
    NAKUSIHI!

    Sio kila ukionacho kinang’ara basi ni dhahabu hiyo, kuna ming’aro mingine inatengenezwa ing’ae kuliko dhahabu. Ilimradi tu kukuchanganya wewe unayetaka dhahabu halisi……


    *******************


    WAKATI mwingine katika maisha sio kila kitu ukionacho ukubali kuwaza kukimiliki.

    Kile kitendo cha kuiruhusu akili yako kuwaza juu ya kumiliki kitu fulani, unajiwekea deni katika akili yako na hapo akili inaanza kukulazimisha ulilipe.

    Na uombe sana deni hilo lisiwe mahusiano ya kimapenzi


    KWA jinsi Nyambura alivyojieleza katika usahili basi lingekuwa jambo la ajabu kumnyima nafasi ya uafisa habari katika kampuni yetu.

    Niliunga mkono nafasi ile akabidhiwe binti yule.

    Katibu muhtasi akapiga simu, Nyambura akaanza kazi rasmi.

    Uchapaji kazi wa Nyambura ulinifanya nijisikie hatia sana nilipoyakumbuka maneno yake siku alipokuwa ananisihi sana nimsaidie apate kazi kwa sababu anao ndugu wanamtegemea kwa dhati sana.

    Nakumbuka kuwa nilimpuuza na kumwona kuwa na yeye ni walewale.

    Wasichana wa kileo

    Kwa sababu yeye alikuwa ni afisa habari wa kampuni na mimi nikiwa katika bodi ya wakurugenzi, hatukuweza kuonana mara kwa mara kwa sababu kama ni habari angeweza kuzikuta kwa katibu muhtasi wetu!

    Habari ikiwa nyeti sana ndo angeweza kuonana na mkurugenzi moja kwa moja.

    Waswahili wanasema kizuri chajiuza, kibaya chajitembeza.

    Sifa za Nyambura zilisambaa upesi sana, alikuwa ni mfanyakazi makini sana anayeijali ofisi yake na asiyekuwa na mazoea kama ya wafanyakazi wengine ya kuanza kutegea kazi pindi wanapoizoea ofisi. Nyambura hakuwa hivyo!

    Haikushangaza pale alipopewa zawadi na kampuni kutokana na utendaji kazi wake.

    Kuajiriwa kwa Nyambura kukaifanya kampuni yetu ya kusambaa kwa kasi sana mkoa kwa mkoa.

    Nyambura hakuchoka wala kuonyesha dalili ya kuchoka, alizidi kuchapa kazi.

    Nyambura alikuwa zaidi ya afisa habari!
    Miezi mitatu baadaye Nyambura alikuwa amejenga ushawishi hadi kampuni yetu ikafungua tawi kubwa jijini Arusha. Ni katika ufunguzi huu wa tawi nilichaguliwa kwenda kukata utepe nikiwa kama mkurugenzi mtendaji.

    Na hapa nikatakiwa kuongozana na afisa habari wa kampuni!

    Nyambura!!

    Ndugu msikilizaji, licha ya kwamba nilikuwa nina pesa za kutosha lakini sikuwa mpenzi wa kusafiri kwa njia ya ndege. Safari kama hizo nilikuwa natumia gari yangu binafsi, aidha ninaendesha mwenyewe ama namchukua dereva wa kuniendesha.

    Safari hii pia niliamua tusafiri kwa kutumia gari langu.

    Niliketi na Nyambura kwa dakika kadhaa kuzungumzia kitu ambacho tunapaswa kwenda kufanya kule, hasahasa wakati wa kuzungumza na watu wa Arusha juu ya kampuni yetu iliyokuwa inahusika na mambo ya usafirishaji wa mizigo ndani na nje ya nchi.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Ni hapa ndipo nilipokiri kuwa Nyambura alikuwa anajua jinsi ya kuzipanga karata na kumfunga mpinzani wake, alizungumza hadi nikatamani hiyo siku yeye ndo asungumze na wakazi wa Arusha mimi niwe kando.

    Yule binti alikuwa na akili halafu na kipaji cha ziada…

    Alikuwa anajiamini na hatoi neno lisilokuwa na maana mdomoni mwake.

    Safari ya Arusha ikaiva!

    Tukaondoka na dereva, mimi na Nyambura tukaketi nyuma tukiendelea kupanga mikakati ya hapa na pale.

    Mikakati ilipomalizika tukaanza kupeana stori za hapa na pale kuhusu maisha.

    Kisha utani kidogo, nikakumbuka kumwomba msamaha kwa kumcheleweshea kazi alipokuja katika usaili siku ya kwanza.

    Nyambura akacheka kidogo! Kisha akanitazama na kuzungumza huku akiwa anatabasamu.

    “Mama yangu alikufa… na wadogo zangu wawili wakamfuata nyuma. Lakini mimi nipo hai na ananiona ninavyopambana huko alipo…” alizungumza huku lile tabasamu likitoweka katika uso wake.

    Sikutaka tuendelee kuzungumza sana juu ya jambo lile, kwa sababu niliona waziwazi kuwa nilikuwa upande wa hatia kwa sababu alinieleza awali na bado sikutaka kumtetea ili aweze kuipata ajira.

    Nikabadili mada!

    ______
    SHUGHULI za kikazi Arusha zilienda vyema kabisa huku Nyambura akizidi kunidhihirishia kuwa yeye ni moto wa kuotea mbali.

    Siku ya mwisho ya kuwa Arusha nilimwalika Nyambura chakula cha usiku katika hoteli niliyokuwa nimefikia.

    Tukakubaliana muda wa kukutana.

    Nilifika majira ya saa mbili, yeye akafika nusu saa baadaye….

    Nilimuona kuanzia mbali alivyokuwa anatembea kimadaha, vazi lake la usiku lilikuwa limeukamata mwili wake na kuufanya urembo wake kuonekana bayana. Hata kabla hajanifikia niliweza kutambua kuwa manukato yake yalikuwa yanatoa harufu mwanana sana.

    Nikajiskia fadhaa sana kwa sababu nilikuwa nimevaa kawaida sana.

    Wakati Nyambura alikuwa amejipanga vyema.

    Alifika na kunisalimia katika namna ya kunikumbatia.

    Kwa mara ya kwanza katika maisha yangu nikajikuta natamani mwanamke aendelee kunikumbatia kwa muda mrefu zaidi!

    Nyambura akaketi tukaagiza chakula na vinywaji huku tukivunja kanuni ya chakula, tulikuwa tunazungumza tena mazungumzo yalikuwa mengi kuliko mwendo wa kula chakula.

    Usingeweza kumdhania hata kidogo kuwa huyu Nyambura ndo yule afisa habari machachari wa kampuni yetu.

    Kila sekunde zilivyozidi kusogea mbele nami nikajikuta nazidi kutamani kuendelea kuwa pamoja na Nyambura.

    Nikapiga moyo konde na kumsihi twende chumbani kwangu ili tunywe pombe kwa tani yetu!

    Awali alijaribu kupinga lakini nikasihi sana hadi akanikubalia ombi langu.

    Tukaingia chumbani, tulikunywa sana.

    Nyambura akawa wa kwanza kulewa, lakini alikuwa anajitambua.

    Pombe zikamualika shetani katikati yetu, zaidi kwangu mimi akanisukuma kumuhimiza Nyambura tuvunje amri ya sita.

    Nyambura akanikatalia huku akilia kilevilevi, nikasikia kama anasema kuwa kamwe hajawahi kufanya kitendo hicho.

    Nikadhani zile ni pombe tu zinamsukuma kusema vile. Nami mashetani yalikuwa yamenipanda na sikuweza kujizuia.

    La! Haula! yalikuwa maajabu makubwa sana kupata kuyashuhudia!!

    Nyambura alikuwa yu salama bado, alikuwa na usichana wake!!

    Alipambana sana na siku ile sikuweza kumfanya jambo lolote lile.

    Pombe zilipotutoka kichwani nikajikuta namtamkia Nyambura kuwa ninampenda sana.

    Hakuzungusha maneno sana badala yake alinijibu.

    “Sina wazazi lakini nina baadhi ya ndugu, kama unanipenda kanitolee mahari unioe!!” alijibu huku amenikazia macho.

    Jibu lile la Nyambura likanifanya nizidi kumtazama kwa jicho la tatu kama msichana wa tofauti sana.

    Na hapo rasmi nikajikuta naingia katika matamanio ya kumuoa hasimu wangu wa zamani, Nyambura!!

    Haikuwa safari nyepesi hata kidogo.

    Na sikujua safari ile kama ingenifikisha pale iliponifikisha!!!!


    ********************
    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
    Kujaribu kumsahau mtu unayempenda ni jambo gumu sana, ni sawa kabisa na kujaribu kumkumbuka mtu ambaye hata hujawahi kumuona.

    Tazama jinsi ambavyo haiwezekani!!


    ILIANZA kama masihara, mara nikajikuta nazama katika uhitaji wa kuwa karibu kabisa na Nyambura.

    Walisema penzi ni kikohozi!

    Ilikuwa hivi hata kwangu, wafanyakazi wakaanza kutubadilisha majina hatua kwa hatua hatimaye nikafungua kinywa na kuwaeleza kuwa ni kweli tupo katika mahusiano na tunataka kuyabadili yawe ndoa mapema sana.

    Wengi walitupongeza na kututakia heri!

    Kasoro rafiki yangu mmoja ambaye alikuwa yu katika ndoa tayari, yeye aliniuliza ninamfahamu Nyambura kiasi gani.

    Sikutaka kujishughulisha na swali lake nikamweleza kuwa tunafahamiana sana!

    Akatabasamu kisha akanipongeza, nilijua wazi kuwa hakuwa akimaanisha.

    Siku mbili baadaye alinifuata ofisini, aliniomba nimsikilize kwa dakika chache, akanielezea mashaka yake juu ya uhusiano wa ghafla sana kati yangu na Nyambura. Akanisihi sana nijipime upya tena kama ni kweli nahitaji kuwa na yule binti kama mke wangu.

    “Sikiliza Joshua, sikatai kuwa Nyambura ni mchapakazi na kila mtu anampenda, kuhusu hilo sina swali kabisa lakini je ana utayari wa kuwa mke kaka… au ndo furaha uliyopata Arusha imekusukuma huko?” aliniuliza yule rafiki yangu na mkurugenzi mwenzangu pia kwa pale ofisini.

    Niliyasikiliza vizuri sana maneno yake. Kuna namna alimchambua Nyambura kwa ajinsi alivyomuona yeye, sikuipenda ile hali na nikawa namjibu tu ilimradi aondoke zake.

    Mapenzi, yasikie tu mapenzi na uombe lisiwe penzi la kwanza… penzi la kwanza maishani huwa lina kila aina ya ubora. Kuaminiana kwa hali ya juu, hapa hujajua maana ya kutendwa!

    Nilimwalika Nyambura chakula cha jioni katika hoteli moja ya kifahari, huko nikamweleza jinsi gani Revokatus yule mkurugenzi mwenzangu anavyosema kuhusu yeye.

    Nilitarajia kuwa Nyambura atakasirika lakini haikuwa hivyo, alinijibu kikarimu sana.

    “Yule ni mwanandoa mzoefu tayari, unapaswa kumsikiliza na usimkasirikie, hawezi kuwa na chuki yoyote juu yetu…. Ni vyema kumsikiliza halafu kwa vitendo sisi tutamwonyesha kuwa alivyowaza juu yetu si sawa…”

    Majibu ya Nyambura yalizidi kunifanya nimpuuzie Revo na badala yake nikapiga hatua mbele siku ile nikamtamkie tena Nyambura kuwa ninataka kumuoa na ninahitaji kwenda rasmi kumtolea mahari, akanielekeza kwa ndugu zake waliopo Musoma.

    Kwa sababu mimi nilikuwa mkurugenzi, jambo la ruhusa kwangu lilikuwa dogo sana.

    Nisingeweza kukosa.

    Nikazungumza na Revo aweze kunisindikiza akanieleza kuwa mkewe anaumwa hivyo hataweza kwenda, nikapata marafiki wawili wa kwenda nao pamoja na mjomba wangu ambaye nilimtumia kama mshenga!!!

    Baada ya siku nne mambo yalikuwa tayari, tukafanya safari.

    Tulipokelewa vizuri sana na ndugu zake Nyambura, nilistaajabu kabisa jinsi mkoa wa Mara unavyozungumzwa jijini Dar es salaam ni tofauti kabisa na uhalisia tuliokutana nao.

    Walitufanyia ukarimu sana, na sisi tukajishusha mno ili tupate Baraka na kuachiwa mke.

    Ile siku ya tatu wilayani Musoma mkoani Mara, tukapokea simu kutoka jijini Dar es salaam.

    Revo, yule rafiki na mkurugenzi mwenzangu alikuwa hoi hospitali baada ya kula chakula kilichosadikika kuwa kimewekewa sumu.

    Tuliendelea kuwajulia hali mara kwa mara jijini Dar es salaam hadi tulipopewa taarifa kuwa hali yake inaendelea vizuri, hapo nasi tukapata ahueni.

    Masuala ya Musoma yakamalizika hatimaye tukarejea jijini Dar es salaam.

    Ile nafika tu nikakutana na barua ofisini, Revo alikuwa amenuia kuuza hisa zake na kuachana na kampuni ile tuliyoianzisha wote kwa jasho sana!!

    Hii ilinishtua sana, maelezo yake hayakuwa yamenyooka sana, nilipatwa na ukakasi sana kuweza kuelewa chanzo cha haya….

    Nikampigia simu, akapokea na kunisisitiza kuwa anahitaji kupumzika na mkewe waweze kulea watoto wao mapacha.

    Sababu ambayo sikuipima katika ujazo wa kusema yawezekana ikawa ni sababu kuu.

    Kama kawaida nikamtafuta Nyambura faragha na kuzungumza naye.

    Akanijibu kwa hekima kabisa kuwa ni heri nikazinunua hisa za Revo ili niweze kuwa na umiliki mkubwa zaidi wa ile kampuni inayotanuka.

    “Wewe zinunue lakini ili kuboresha urafiki wenu mweleze kuwa wakati wowote akihitaji kurejea katika kampuni basi anakaribishwa!”

    Nikayapokea vyema manenoya kinywa cha mwanamke, nikayafanyia kazi.

    Mwezi mmoja baadaye nikazinunua zile hisa na kisha nikatangaza tarehe rasmi ya kufunga ndoa na Nyambura!!

    Nilipanga iwe ndoa ya kanisani.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Revo akasahaulika nami nikawa mmiliki mkubwa zaidi wa kampuni ile, hapo nhikiwa na asilimia 90 ya umiliki.

    Nilikuwa na sauti kubwa zaidi katika vikao vya kampuni.

    Katika kikao kimoja nikampandisha cheo Nyambura kutoka kuwa msemaji mkuu wa kampuni hadi kuwa msimamizi wa ofisi zote za kampuni yetu zilizoko mikoani!!

    Sikuwa najua ninachofanya kinaweza kuwa na madhara yoyote, nilichotazama ni kwamba nafsi yangu inafurahi huku ya Nyambura ikifurahi zaidi.

    Baada ya maamuzi hayo, nikampigia mama simu na kumfahamisha kuwa ule mji tulivu nilioapa kuwa ninahitaji kuupata basi nimebakiza hatua chake kabla 

0 comments:

Post a Comment

Blog