Simulizi : Msalaba Wa Dhahabu
Sehemu Ya Tano (5)
Bahati mbaya alichokuwa hakukijua ni mara baada ya kukataa kupigwa sindano, mbinu nyingine ya kuitumia kahawa hiyo ndipo ilipobuniwa na Mganga Mkuu.
Kahawa aliyokuwa akiinywa, ilikuwa imewekwa vidonge vya usingizi! Dakika kumi baadaye, Mathias akawa kwenye usingizi mzito.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Ndoto ile ikamrudia! Akawaona waombolezaji walewale kupitia kwenye dirisha lilelile la wodi aliyolazwa, wakiwa ni wakazi wa Zebati wakitokea tena makaburini wakisema kwa sauti yenye mwangi, “Mathias auawe! Na yeye apelekwe makaburini kama alivyompeleka baba Sai!”
Kurudia kuiota ndoto hiyo tena kukampa Mathias mshituko, akaamua awahi kukimbia kabla hawajamfikia hapo kitandani kama ilivyokuwa awali. Akajaribu kujiinua, mwili ukakataa kuinuka, akajaribu kwa mara nyingine, mwili ukawa umenyong’onyea kabisaa! Akajishangaa kujiona yuko kwenye hali hiyo. Akiwaangalia kwa kihoro, watu hao alioamini ni wafu wakawa wanazidi kumsogelea huku wakitoa sauti zenye jazba za kumtaka auawe. Mathias akapiga kelele, sauti ikakataa kutoka! Akapiga tena kelele, sauti ikawa imebanwa, akawa kama anayenong’ona. Hatimaye akajiona tayari amezungukwa kitandani na watu hao huku kila mmoja akigombea kumkamata. “Safari hii hutuponyoki tena!” walimwambia.
Mathias akajaribu kujinasua kutoka kwenye mikono yao, lakini kila alivyojaribu kufanya hivyo, viungo vhake vya mwili vikawa vinakataa kufanya kazi. Akabebwa mzobemzobe na kutolewa kwenye kitanda alicholalia na kupelekwa kwenye makaburi yaliyopo nyuma ya hospitali hiyo huku umati ule ukimzomea na mmoja wa aliyekuwa akimzomea alikuwa baba Sai! Mathias akaamini yupo kwenye njozi ileile mbaya kama aliyoiota awali, akajaribu kutabasamu kwa matumaini baadaye angezinduka kwa kukurupuka kama alivyozinduka mwanzo na kuwaona tena wauguzi wamemzunguka!
Hakuamka!
Wauguzi waliofika kuwatoa zamu wauguzi wengine waliokuwepo, ndiyo waliomkuta Mathias kitandani akiwa ameshakufa!
*****
MAITI ya Mathias ilishuhudiwa na kikundi cha watu watano cha Kanisa Katoliki kutoka Zebati baada ya Mganga Mkuu kuwafikisha kwenye eneo alikohifadhiwa. Nguvu zikawaishia, matumaini ya kuupata Msalaba Mtakatifu yakatoweka. Wakarudi ofisini kwa Mganga Mkuu vichwa vyao vikiwa vimeinamishwa chini kila mmoja akisikitika kivyake.
“Mtamzikia wapi?” Mganga Mkuu aliuliza baada ya kufika ofisini kwake.
“Tutamsafirisha kumrudisha Zebati. Itabidi mmoja wetu atangulie kurudi Zebati kutoa taarifa hizi.”
“Kama nilivyowaeleza awali, itabidi mfuate taratibu zote za kipolisi.”
“Hilo halina shida tutalitekeleza,” mmoja alijibu. “Isipokuwa tunataka kufahamu jambo moja. Marehemu kabla hajafariki, aliwahi kuwaelezeni au kukueleza jambo lolote ambalo ni geni kwenu?”
Mganga Mkuu akaonyesha mshangao usoni. “Kama lipi?” aliuliza.
“Aliwahi kutamka lolote linalohusu msalaba?”
“Msalaba? Ukiwa na maana gani?”
Kile kikundi cha watu watano wakaangaliana.
“Kama aliwahi kutamka neno linalohusu Msalaba Mtakatifu au kukutwa nao?”
“Hapana, bado sijasikia chochote kuhusu hilo.”
Kimya kidogo kikapita.
“Tunashukuru dokta,” mmoja akakivunja kimya hicho. “Itabidi twende polisi ili kuanza kufuata taratibu zinazotakiwa.”
“Kuna swali nataka kuwauliza,” Mganga Mkuu alisema kabla hajautoa mkono wa kuagana. “Marehemu Mathias alikuwa akionyesha woga wakati wote wa uwepo wake hapa, isitoshe, muda mfupi kabla ya mauti kumkuta, alipiga kelele akiwa usingizini akiomba asamehewe. Kuna chochote alichokifanya Zebati kabla ya kufika huku?”
“Hapana. Hakuna chochote alichokifanya,” mmoja wa kikundi kile alijibu haraka kabla ya kuangaliana machoni na wenzake.
“Kwa nini mmeniuliza kama alikuwa na Msalaba Mtakatifu na wakati huohuo mnasema hakuna chochote?”
Kikundi chote cha watu watano kikapata kigugumizi.
“Msalaba Mtakatifu umeibwa, yeye ni mmoja kati ya watu tunayemtuhumu!” mmoja wa kikundi kile alisema bila ya kutafuna maneno.
Mganga Mkuu akapiga alama ya msalaba kifuani pake. “Asifiwe Yesu Kristu,” alisema.
Watu aliokuwa nao wakaitikia, “Milele amina!”
Kisha akaendelea, “Amewezaje kutenda kitendo kama hicho?”
“Mpaka sasa hivi hatujajua ni nini kilichompata hadi afanye hivi.”
Mganga Mkuu akaishia kukodoa macho.
********
KIFO cha Donna mbele ya macho ya Sajini Seba zilikuwa ni habari nyingine zilizokishitua Kisiwa cha Zebati. Mapokeo ya habari hizo yalilifanya Kanisa Katoliki liwe kwenye wakati mgumu wa kupambana na hali halisi iliyowakumba waumini wake. Nguvu za kishirikina zilianza kuonyesha dalili ya kulimeza kanisa, waganga wa jadi wakachukua nafasi hiyo kujinadi kwa nguvu kuwa, wana uwezo wa kuwapa kinga watu wasiendelee kuuawa na nguvu za giza zinazoaminiwa zimekivamia kisiwa hicho.
Umma wa Zebati ukaziona ni habari njema kwao, safu za watu asubuhi na jioni zikaonekana kwenda kwa waganga hao kwa ajili ya kupewa kinga. Wake kwa waume, vijana na wazee hadi watoto, wakaonekana kuvaa hirizi za kinga wakiwa mitaani, na wale waliokuwa bado kufanyiwa kinga, walihimizwa kwenda kufanyiwa. Imani ya kiroho ikaanza kupuuzwa kwa nguvu na imani ya kishirikina ikajijenga kuichukua nafasi hiyo. Uvaaji wa misalaba na rozari ukapuzwa kwa nguvu kubwa.
Pamoja na kinga hizo kupewa wakazi, majonzi yaliendelea, kila usiku kukawa kunakufa mtu! Vilio vikaanza kutawala kila kona huku waganga wa jadi wakijitetea kwa kusema, wote wanaokufa ni wale ambao hawajepewa kinga, au hawakupokea kinga zao kwa imani! Wimbi la wakazi kuikimbia Zebati likazidi maradufu!CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Hali hiyo ikauweka uongozi wa kanisa kwenye msuguano baada ya kikao kingine cha dharura kuitishwa. Wapo waliotaka wakazi waambiwe ukweli kuwa Mathias na wavuvi wawili ndiyo sababu ya janga linaloikumba Zebati kwa kuiba Msalaba Mtakatifu na kuiondoa kinga iliyokuwa ikiwalinda, upande huo ukawa unaungwa mkono na Padri Toni. Lakini upande wa pili uliokuwa ukiungwa mkono na mzee Robert uliendelea kupinga wazo hilo wakidai kwanza waisubiri Kamati Maalum ya Kanisa iliyomfuatilia Mathias kisiwani Jedani hadi itakaporudi na jibu lenye kueleweka.
“Kuirudisha jamii kwenye imani ya kanisa ni kuwaambia ukweli!” alisema mmoja wa wajumbe wa kikao hicho.”
“Jamii ina haki ya kuupata ukweli!” mwingine alidakia. “Sisi ndiyo wenye kufahamu Msalaba Mtakatifu umeibwa, ni sisi ndiyo tunaofahamu maafa haya yamekuja kutokana na kuibwa kwa msalaba huu, lakini wakati huohuo watu wakiendelea kujiuliza kwa nini Msalaba Mtakatifu umeshindwa kuizuia hali hii? Kwa sababu hawajui chanzo! Matokeo yake wanajua kinyume, kuwa Msalaba Mtakatifu umeshindwa kuzuia majanga! Sasa kanisa linadharauliwa, wakazi na waumini hawana imani nalo tena! Badala yake wamegeuza nyuso na akili zao kuwaabudu waganga wa jadi wanaotumia nafasi hii kuwaaminisha imani za kishirikina! Hali hii hatupaswi kuiachia iendelee! Jamii lazima ifahamishwe ukweli, vinginevyo itapotea kwenye ushirikina!”
“Tuiambie ukweli gani jamii?” mzee Robert aliuliza na kuonekana kama aliyejeruhiwa huku akimwangalia mjumbe aliyetoka kutoa hoja ya mwisho.
“Tuiambie kuwa, Msalaba Mtakatifu umeibwa na huu tulioachiwa ni bandia!” alijibu mtoa hoja wa mwisho huku akijaribu kukabiliana na macho ya mzee Robert. “Jamii inatakiwa ijue sababu za kutokea kwa janga hili!”
“Ni nani atakayetuamini?” mzee Robert aliuliza. Safari hii sauti yake ilikuwa kavu mara mbili ya awali. “Na kwa nini wasituone kuwa tunajikosha baada ya miongo kadhaa kupita, tukiwapa neno la Bwana na kumsifu Bikira Maria kwa kukiteua kisiwa chetu kwa kukipa Msalaba Mtakatifu, huku tukiendelea kuwapa matumaini kuwa, msalaba huu Mtakatifu ndiyo unaotuletea amani na utulivu! Walituamini, lakini pia, wakaendelea kutuamini hadi siku iliyofanyika sala maalum ya kumwomba Bikira Maria kupitia Msalaba wake Mtakatifu, na tukaomba wote kwa pamoja. Siku hiyo ndiyo ilikuwa mwisho wa kuliamini kanisa!
“Kwa nini ilikuwa mwisho? Kwa sababu wameshuhudia Msalaba Mtakatifu ukishindwa kukifanya kile ilichoombwa usiku ule kuwa, kilete amani na kuzuia vifo vya mauzauza vinavyotokea. Majibu yakawa ni kwa kimbunga kuvamia kanisa, kikang’oa msalaba uliokuwa ukipigiwa magoti na waumini. Wakatimka kwa kuliona kanisa siyo mahali pa amani tena! Kinachotokea sasa ni kwamba, watu wanaendelea kufa huku wakihadaiwa na waganga wenye imani za kishirikina! Lakini pia wakazi wakiendelea kukihama kisiwa chetu! Kwa hali kama hii, kwa watu kama hawa waliokata tamaa na kanisa, leo tuwaambie sababu ya matukio haya ni kutokana na Mathias na wenzake wawili kuiba Msalaba Mtakatifu! Na ule waliouona uking’olewa kanisani ulikuwa ni msalaba bandia uliowekwa na Mathias! Kweli watatuelewa? Kwa nini tusijiulize, je kama hawatatuelewa na kauli yetu hii, badala yake wakatuona tunajikosha baada ya kuwaona wakikimbilia kwa waganga wa jadi? Ni hatua gani itakayofuata ambayo tunapaswa kuichukua? Hatua ambayo itasaidia kuwaweka tena sawa baada ya mgongano huo wa kifikra?” Baada ya mzee Robert kumaliza hoja yake hiyo, kimya cha muda kikajikita kwenye ukumbi unaofanyika kikao chao.
“Hoja zako zina maantiki, mzee Robert,” alisema mjumbe mwingine mwenye mrengo wa Padri Toni. “Lakini, pamoja na hayo uliyotueleza, hatuwezi kuiacha hali hii iendelee kwa kuiacha jamii na waumini wetu wazame kwenye ushirikina kama ulivyokiri kuwa wanahadaiwa. Lakini pia, wasiendelee kukikimbia kisiwa kwa hofu iliyowakumba. Jamii inahitaji kuambiwa ukweli! Sisi sote hapa tulipokaa, tunaamini nguvu za Bikira Maria zilikuwepo kwenye Msalaba Mtakatifu ulioibwa, na huu ndiyo ukweli. Lakini kabla hatujaikabili jamii kuiambia ukweli, kuna tukio muhimu ambalo sote tunatakiwa tulifahamu, tukio la kuwepo kwa nguvu za bikira Maria zilizojitokeza baada ya Msalaba Mtakatifu kuibwa! Tukio ninalotaka kuwaambia, ni tukio la kimbunga kilichopiga kanisani. Baada ya tukio lile, wewe mzee Robert na Padri Toni mlijikuta mkiwa mmebaki ndani kanisani, hamkukimbia kama waumini wengine tulivyokimbia. Ninachotaka kuwaelezeni hapa ni kwamba, kile kimbunga kilichotuvuruga kanisani, zilikuwa ni nguvu za Bikira Maria!”
Kauli hiyo ikawafanya wajumbe wote wa kikao wamwangalie mjumbe mwenzao kwa mshangao. Hata wale aliokuwa nao mrengo mmoja wa hoja, nao wakawa wamepigwa na butwaa wa kule mwenzao huyo anakoelekea.
“Pale kanisani kulitokea vurumai kubwa baada ya kimbunga kile kuangusha Msalaba,” mjumbe huyo aliendelea na hoja zake. “Waumini walikanyagana kikatili, kila mtu akitaka kuwahi kutoka nje kuyasalimisha maisha yake. Lilikuwa ni tukio la kutisha na kusikitisha! Lakini, kwa nini tusijiulize, mkanyagano wa hatari kama ule, hakukutokea kifo cha muumini hata mmoja pale kanisani! Matokeo yake, aliyekuja kufa ni yule ambaye hakuja kanisani, ambaye bado ni binti mbichi, Donna! Matukio yote haya yanadhihirisha yalikuwa ni maajabu yake Bikira Maria! Kwa sababu ni yeye ndiye aliyekileta kimbunga kile baada ya kutuona tunaendelea kuabudu msalaba bandia…msalaba wa shetani! Kimbunga kile kilikuwa ni dalili za kukasirika kwake na alitaka kuwaonyesheni wewe mzee Robert na Padri Toni kuwa, tunaoupigia magoti si baraka za nguvu zake, bali tunaoupigia magoti ni nguvu za shetani aliyewatuma Mathias na wenzake kuja kuiba msalaba wake mtakatifu! Na hiyo ndiyo sababu ya kuuangusha kwa hasira msalaba ule wa shetani!
“Kwa hiyo, hata kugundua kwenu kuwa Msalaba Mtakatifu umeibwa na tuliokuwa tunaendelea kuupigia magoti ulikuwa ni wa bandia, hazikuwa akili zenu, bali ni uwezo wa Bikira Maria baada ya kukileta kimbunga kile. Mimi naomba tulikubali hilo, na tukilikubali, basi tukubali kuzitumia nguvu zake Bikira Maria kuwakabili waumini kwa kuwaambia ukweli kuwa, msalaba tuliokuwa tukiupigia magoti haukuwa Msalaba Mtakatifu, bali ulikuwa msalaba wa shetani. Na sababu ya kutokuwepo kwa Msalaba wetu Mtakatifu na kipenzi chetu, kulitokana na kuibwa, na waliouiba ni Mathias na wenzake na ndiyo sababu ya kutoweka kwao! Baada ya hapo ndipo tutakapoutumia mfano wa kimbunga kilicholetwa na Bikira Maria kuiambia jamii. Nadhani kwa hilo watatuelewa! Kama Bikira Maria alishindwa kuvumilia kutuona tukiendelea kumpigia magoti shetani, basi nina imani hata nguvu zake zitatumika kuifanya jamii waelewe tutakayowaambia. Kwa kuwaeleza ukweli, ni imani yangu wataacha kumwamini shetani wanayemwamini sasa, shetani mshirikina!” Baada ya kumaliza hoja yake, mjumbe huyo alikaa na kuwaangalia watu aliokaa nao wameipokeaje hadhari yake.
Wengi wakamuunga mkono.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
********
WIKI moja ikiwa imepita tangu Donna alivyofariki kwenye mikono yake, Sajini Seba alikuwa yupo kwenye wakati mgumu kisaikolojia. Alikosa usingizi, alikosa hamu ya kula na hata kazini akagoma kwenda, lakini hatimaye alikataa kuzungumza na watu. Pole za mara kwa mara alizokuwa akizipokea kila alipokwenda zilimfanya akose uhuru wa kutembea na kumjengea tabia ya kukwepa macho ya watu ambao kila walipomwona walimfanya ni gumzo na kuwa chachu ya mtandao wa imani ya kishirikina kutokana na ushuhuda alioupata wa kuwa mtu wa kwanza kufiwa na mtu mikononi mwake tokea vifo hivyo vya mauzauza vianze kuibuka.
Tukio la kufa Donna mbele ya macho yake lilikuwa kama jinamizi lisiloisha, lakini pia aliliona kama igizo lililotokea kwenye jukwaa. Lilikuwa tukio aliloliona kama aina ya muujiza na kumrejea wakati wote kichwani mwake, na kila lilipojirudia akawa haamini kama ni kweli Donna amekufa! Kwa upande mwingine wa mawazo yake, aliamini kuwa, Donna yupo hai, bali ametoweka kwa muda na angerudi!
Kukataa kuwa Donna amekufa, na kukataa kuonana na watu, na kule kutokwenda kazini, wakuu wake wa kazi wakampa likizo ya lazima ili aweze kuirudisha akili yake kwenye mazingira ya kawaida. Likizo hiyo ikamfanya aanze kujifungia chumbani kwake kutwa nzima huku akijenga matumaini ya kwamba, Donna angetokea na kumgongea mlango! Kwa kuwa hakukuwa na mtu aliyejitolea kumwondoa kwenye hali hiyo ya kuchanganyikiwa, Seba akazidi kujichanganya akili. Akaanza tabia ya kwenda nyumba aliyokuwa akiishi Donna kila usiku kiasi cha mara mbili au tatu na alikuwa akienda muda ambao upepo mbaya unaoua watu ulikuwa ukitokeza na alikuwa hauogopi! Lakini kila alipolifikia eneo lenye nyumba hiyo, akawa haikaribii. Alikuwa akisimama mbali na nyumba hiyo na kuiangalia kwa mbali. Kitendo hicho kikamfanya aonekane kama kivuli kinachotisha ndani ya usiku huo wa giza ambao kutokana na hofu iliyotawala kisiwani humo, hakukuwa na mtu yeyote aliyekuwa akitembea kwa muda huo!
Woga ndiyo uliomfanya asimame kwa mbali. Ulikuwa woga wa endapo angekwenda na kugonga hodi kwenye nyumba hiyo, angeambiwa, ‘Donna hayupo!’ hicho ndicho alichokuwa akiogopa kuambiwa. Ikawa ni hali iliyozidi kumchanganya akili. Watu waliokuwa wakimwona kwa kumchungulia madirishani nyakati hizo za usiku, wakaanza kumwekea wasiwasi kuwa, kijana huyo kipenzi cha wakazi wa Zebati, alikuwa ama angepotea kwa kuvurugikiwa kabisa akili au angepotea kwa kuuawa na upepo mbaya.
Mwito ukafanyika kumwokoa kijana huyo. Watu wakakutana, wakazungumza. Wakakubaliana kuwa, akili ya Seba inahitaji msaada. Pande mbili zikaibuka kubishana, wengine wakitaka Seba apelekwe kuaguliwa kwa waganga wa kienyeji, wengine wakitaka Seba apelekwe kwa Padri Toni akaombewe!
“Vyovyote itakavyokuwa, kama ni kwa mganga wa kienyeji au kwa Padri,” alisema mchangiaji mmoja. “Ni nani atakayemkabili Sajini Seba na kumwambia kuwa eti amechanganyikiwa na anahitajika kwenda kupata tiba?”
Swali lake likaonekana ni suala linalogusa hadithi ya panya ya kumfunga paka kengele. Likawafanya wote waliokuwepo pale wanyamaze kimya.
“Swali jingine,” alisema yule mchangiaji. “Ni yupi kati ya Padri Toni na mganga wa kienyeji anayeweza kwenda nyumbani kwa Sajini Seba na kupokewa bila mshangao kutoka kwa Seba?”
Wote wakaafiki kuwa, ni Padri Toni pekee ndiye mwenye nafasi hiyo ya kukubalika kupokewa kwenye nyumba yoyote kwa sababu ujio wake popote pale huonekana kama nuru yenye neema. Wakakubaliana Padri Toni akapewe taarifa za kuchanganyikiwa akili kwa Sajini Seba.
********
TAARIFA zilifikishwa kwa Padri Toni, naye bila ya kuchelewa, alikwenda nyumbani kwa Seba na kupokewa na Seba mwenyewe aliyemfungulia mlango. Seba akaonekana kuwa mtulivu na mwenye unyenyekevu mbele ya Padri Toni.
“Nikutengenezee chai au kahawa father?” Seba aliuliza baada ya kuingia ndani na mgeni wake na kumkaribisha kiti.
“Hapana, ahsante Seba,” Padri Toni alisema huku akijaribu kumwangalia kwa makini Seba kujaribu kuutafuta kuchanganyikiwa kwake alikoambiwa.
“Naona umeniletea nuru ya neema kwenye nyumba yangu,” Seba alisema kwa unyenyekevu.
“Tumsifu Yesu Kristu,” Padri Toni alisema.
“Milele amina.”
“Sebastian,” Padri Toni alimwita Seba kwa upole.
Kuitwa kwa jina lake kamili, kulimfanya Seba ajisikie tofauti. Kutajwa huko kwa ukamilifu kutoka kwa mtu wa kiroho mwenye kuheshimika kama Padri Toni, Seba aliiona ni baraka iliyomfikia. Akaitikia.
“Unaamini kupitia njia ya Yesu Kristu?” Padri aliuliza huku akimwangalia Seba usoni.
“Ndiyo naamini.”
“Ni faraja kubwa kukusikia ukitamka hivyo,” Padri Toni alisema kwa upole. Akaendelea, “Nadhani wewe Sebastian ni mmoja wa shuhuda wa maafa yanayokikabili kisiwa chetu na ushuhuda wako ndiyo ulionileta kwako. Kama ulivyo wewe, lakini pia wakazi wote wa Zebati wapo kwenye mtafaruku huo wa kuchanganyikiwa kwa kuwapoteza wapendwa wao. Hali hii imetuleta kwenye mgawanyiko ambao haujawahi kutokea hapa kisiwani. Tunawaona wengine wakijiingiza kwenye imani za kishirikina na kumsahau Yesu, na wengine wakikikimbia kisiwa kutokana na hofu iliyowakumba. Lakini ningependa kuwazungumza hawa waliojitumbukiza kwenye imani ya kishirikina.
“Hawa sasa hivi wanakutumia wewe kama mfano wa uliyekumbana na hali halisi ya matukio haya ambayo wanaamini ni ya kishirikina. Wanadai kuwa, kabla ya kuuawa kwa Donna, wewe ulikuwa ukifukuzwa na ukungu unaozungumzwa kuwa ndiyo upepo mbaya, ni uvumi uliozagaa, lakini kutokana na kuaminishwa na imani za kishirikina, najikuta sikubaliani na uvumi huo. Isitoshe hata wewe mwenyewe ulikwisha kunitamkia ya kuwa janga lililopo kisiwani petu limekuja kwa njia za ushirikina. Sasa Sebastian, ujio wangu hapa ni kukurudisha kwenye njia iliyonyooka, njia ya Kristu. Urudi kwenye njia yake yenye matumaini. Nataka uondokane na wazo la kishetani kuwa mwenzako Donna atarudi. Ondoka kwenye imani hiyo kabla waganga hawajakukaribia na kukuongopea kuwa, wanaweza wakamrudisha Donna kwa njia za miujiza. Urudi kwa Yesu, ukubali kuwa, Donna amekufa kwa ahadi yake Mungu na si kitu kingine!”
Wakati wote Padri Toni alivyokuwa akiyazungumza hayo, Seba alikuwa ametulia kimya akiwa ameuinamisha chini uso wake. Baada ya kuwa na uhakika Padri Toni amemaliza alichokuwa akikizungumza, Seba aliuinua uso wake na kumtazama Padri Toni usoni. “Father,” alisema kwa sauti iliyopwaya. “Maisha yangu yote yamekuwa kwa Yesu, na naamini kupitia kwake yeye. Lakini hili la Donna, father linanichanganya. Linanichanganya father…” sauti yake ikabadilika na kuwa kwenye kilio. Akaufudikiza uso wake kwenye viganja na kulia kwa kwikwi.
Padri Toni akainuka, akamshika Seba begani. “Ni shetani anayekuchanganya!” alisema.
“Hapana father!” Seba alisema na kuinua uso wake wenye machozi na kumwangalia Padri Toni. “Nimeyashuhudia kwa macho yangu yaliyonikuta! Uvumi unaozungumzwa dhidi yangu ni wa kweli, ni wa kweli kwa sababu ni kweli nilikuwa nikifukuzwa na viumbe wa ajabu. Nimewashuhudia kwa macho yangu, sikuhadithiwa father, walikuwa ni viumbe hai ambao sijawahi kuwaona kabla, katika maisha yangu. Ndio waliomuua Donna…” kwikwi za kilio zikamkaba na kushindwa kuendelea kuzungumza.
Padri Toni akarudi kitini. Akafumba macho na kupiga alama ya msalaba kifuani. Akasema, “Tumwombe Bwana aliye mbinguni, akurudishie nguvu zako, akupe nguvu ya kauli, unielezee ulichokiona.”
Sala fupi ya Padri Toni ikamwingia Seba. Akaijaza moyoni na kuipokea kwa uadilifu. Nguvu zikamrudia, akapumua mara moja na kuinua uso wake. Akamwangalia Padri Toni.
“Ulikuwa wakati wa usiku nikiwa na Donna tukielelekea kanisani huku tukiwa tumechelewa,” alianza kuuhadithia mkasa uliomkuta. “Ndipo ule upepo mbaya ulipoanza kuvuma, Donna akaniambia amepatwa na woga, kauli ambayo ilitumiwa na wahanga wa janga hili muda mfupi kabla hawajafariki. Nikaingiwa na wasiwasi huenda Donna naye angekuwa mhanga usiku ule. Ndipo yeye alipobadilisha mawazo ya kutaka nimrudishe nyumbani, nikatii matakwa yake. Nikawahi kumrudisha nyumbani, wakati nilipokuwa nikirudi nyumbani kwangu, ndipo nikakutana na ukungu njiani uliokuwa ukinijia kwa mbele…” Seba akayaeleza matukio yote yaliyomkuta usiku ule wa kufukuzwa na kiumbe mwenye miguu yenye kwato lakini mwenye sura iliyofanana na kunguru hadi kifo cha Donna kilivyomtokea mikononi mwake.
Kimya kikajiunda baada ya Seba kumaliza kuyaeleza masaibu yaliyomkuta. Maelezo yake yakaonekana kumgusa Padri Toni ambaye alibaki kimya huku akiwa amejiinamia na kujikita kwenye tafakuri.
“Father,” Seba alisema ghafla na kuuondoa ukimya uliojikita kati yao, lakini pia akamwondoa Padri Toni kutoka kwenye fikra zake. Wakaangaliana. “Kwa nini iwe hivi father?” Seba aliuliza. “Ziko wapi nguvu za Bikira Maria tulizokuwa tukihubiriwa? Uko wapi uwezo wa Msalaba Mtakatifu uliokuwa ukinadiwa? Tulioambiwa ni zawadi kutoka kwake na ungetulinda na majanga yote! Au je, vifo hivi vinavyotokea, siyo janga tuliloambiwa?”
Padri Toni alivuta pumzi na kuiangalia mikono yake iliyojaa vinywelea vyenye mvi. Alikuwa amegundua ni kweli Seba amechanganyikiwa, lakini siyo kuchanganyikiwa kwa hali inayovumishwa, bali amechanganyikiwa na ahadi zilizotokana na kuaminika kuwa, zilikuwa ahadi takatifu zilizokuwa zimemtia matumaini ambazo sasa hazioni zikitimia.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Ni janga tuliloonywa nalo!” Padri Toni alijibu. “Tumemtendea dhambi Bikira Maria, tumemkosea na ndiyo maana janga limetufikia kisiwani kwetu. Janga hili halikuletwa na nguvu za kishirikina zinazovumishwa, bali limeletwa na uroho wa tamaa ya utajiri kwa wale tuliokuwa tukiwaamini. Wameuiba Msalaba Mtakatifu na kutuachia msalaba bandia, ule uliosikia umeangushwa na kimbunga kanisani.”
Seba aliyekuwa ameinama kwa unyenyekevu akimsikiliza Padri Toni kwa makini, aliuinua uso wake na kumwangalia kiongozi huyo wa kiroho kwa mshtuko. “Msalaba Mtakatifu umeibwa?” aliuliza kwa sauti yenye hofu iliyonong’ona.
“Ndiyo umeibwa,” Padri Toni alisema kwa utulivu. “Hilo limegundulika usiku uliofanyika sala maalum ya maombi baada ya Bikira Maria kuonyesha hasira zake wakati tulipokuwa tukiuomba msalaba usio wake. Hasira zake zikaleta kimbunga kikubwa ndani ya kanisa tukiwa katikati ya sala. Nadhani utakuwa umesikia kutoka kwa waumini wenzako jinsi kimbunga hicho kilivyovuma kwa hasira na kuangusha kila kitu mle kanisani. Zilikuwa ni hasira zake zilizolenga kwenye msalaba ule bandia, ukaangushwa na tulipokwenda kuuangalia tukagundua haukuwa Msalaba Mtakatifu! Ulikuwa Msalaba uliotengenezwa kwa bati na kutiwa rangi ya dhahabu! Janga unaloliona la kutuulia wapendwa wetu, Donna akiwa ni mmojawao ni kuwa, ubashiri uliotabiriwa kutoka neno la Bikira Maria umetimia! Neno lilisema, endapo Msalaba Mtakatifu ukiibwa au kupotea, Zebati itafikwa na majanga! Na ndiyo haya yatukutayo sasa!”
“Ni yupi mtenda dhambi hizo?” Seba aliuliza huku uso wake ukiwa umepigwa na butwaa.
“Mathias Mizengwe! Mjukuu wa Robert Mizengwe! Aliyekuwa Padri mtarajiwa, aliyeaminiwa na jamii iliyostarabika kuwa na yeye ni miongoni mwa waliostarabika!”
“Siamini!” Seba alisema kwa sauti ileile inayonong’ona kama yenye hofu. “Siamini kama ni Mathias aliyetuingiza kwenye janga hili!”
“Hakuna aliyeamini, lakini huo ndiyo ukweli!”
“Ndiyo sababu ya kutoweka kwake?”
“Ndiyo hiyo. Alitoweka baada ya kuuiba.”
“Mmekwishapajua alipotorokea?”
“Habari za mwisho zilizopatikana ni kuwa, amelazwa kwenye hospitali ya Jedani baada ya kuopolewa baharini.”
“Amekutwa nao Msalaba Mtakatifu?”
“Bado hatujajua. Tumetuma timu maalum ya kumfuatia Jedani, tunasubiri ituletee taarifa za huko.”
“Lakini kwa nini kulitabiriwa janga kwa kuibwa Msalaba Mtakatifu?” Seba aliuliza akiwa makini usoni.
“Sijui!” Padri alijibu bila ya kusita.
“Kwa nini basi lisiwe janga la kimbunga peke yake, au mafuriko, matetemeko ya ardhi au gonjwa la hatari, majanga yaliyozoeleka na binadamu. Kwa nini iwe viumbe hawa wa ajabu niliowaona? Kwa nini tuadhibiwe kwa kutumiwa viumbe hawa? Kipi kilichofanyika kwa miaka hiyo hadi tuletewe viumbe hawa wa ajabu kama angamizo letu? Na kwa nini Msalaba Mtakatifu uletwe kwa ajili yetu? Kwa nini wasiwe wengine?”
Padri Toni akamwangalia Seba kwa uso wa huzuni. “Hata hilo pia sijui!” alisema. “Ushuhuda wako nami pia unanichanganya na kujiuliza maswali kama hayo. Hata hivyo, nadhani ipo sababu nyuma yake iliyofanya uletwe Msalaba Mtakatifu kwenye kisiwa chetu kwa ajili ya kuwazuia viumbe hao uliowaona ili wasiwepo. Lakini bado nashindwa kuiweka dhana yoyote ya msingi nyuma ya sababu hiyo. Hata mimi inanichanganya!”
“Sasa tutafanyaje?” Seba aliuliza kama vile alikuwa akizungumza peke yake. “Kugunduliwa kuibwa kwa Msalaba Mtakatifu bado hakujawa suluhisho la watu kutoendelea kuuawa, hata usiku wa kuamkia leo nimewasikia watu wakisema kuna mtu mwingine aliyekufa kwa kifo cha aina hiyohiyo! Hali hii itaendelea hadi lini? Hakuna njia nyingine yoyote ya kuizuia hali isiendelee kuwepo? Au ni kweli Majini yanayozungumzwa na watu, yatakuwa yamerudi kwenye mji wao? Na pengine kurudi kwao ni kutokana na kizuizi chao cha Msalaba Mtakatifu kuondolewa?”
Padri Toni alijishika paji lake la uso na kuinamisha chini uso wake. “Haya mambo yananichanganya!” alisema huku akionekana kuchoka. Kisha akauinua tena uso wake.
“Unaamini unaweza ukawa ni ushirikina?” Seba aliuliza na kuyatuliza macho yake machoni mwa Padri Toni.
Padri Toni akayakwepesha macho yake. Kisha akamwangalia Seba kwa macho yaliyokaza, “Usinitie majaribuni!” alisema.
“Sasa utafanya nini wakati jamii imeishangia kwenye imani hiyo?”
“Ni kweli wameingia kwenye imani hiyo, lakini haiwatatulii tatizo lililopo kama mwenyewe unavyosema, tatizo bado lingalipo, watu kila siku wanakufa! Wapo tu kwenye imani ya kijinga!”
“Na unakubali kama kanisa limeshindwa kulitatua au kuliondoa tatizo hili?”
“Maana ya uwepo wa kanisa ni kumwabudu Mungu, kwa hiyo Mungu hashindwi. Tunatakiwa tumwombe huku tukimwogopa kwa maana ya kufunga. Tunatakiwa tufunge na kusali ili atuondolee janga hili.”
“Jamii itakuelewa vipi ukiwapelekea tena imani ya kanisa, kwa kuwaambia washinde huku wakifunga na kusali wakati walishaona kanisa limeshindwa kupitia Msalaba Mtakatifu ulionadiwa, kuwa una uwezo wa kuzuia majanga?”
“Itakuelewa!”
“Itanielewa au kukuelewa?” Seba aliuliza kwa mshangao huku akijionyeshea kidole.
“Nataka wewe uwe mwokozi wa kanisa! Kama jamii ya Zebati iliweza kukutumia kuwa kigezo cha mfano wa ushirikina wanaodhani umekutokea, nataka uutumie ushawishi waliokuona unao, utumike kuwahutubia wakati nitakapoigonga kengele ya dharura ya kuitia watu kanisani.”
“Unataka nizungumze nini nao?”
“Nataka uwaambie nilichokwambia. Jamii inatakiwa ijue Msalaba Mtakatifu umeibwa, ijue kimbunga kile kilichotokea kanisani ni hasira za Bikira Maria hadi kuuangusha ule wa bandia. Jamii inatakiwa imjue ni nani aliyehusika na wizi huo na kisha umalizie kwa kuwataka wawe wanafunga kwa siku arobaini huku wakisali kumwomba Mungu kuliondoa janga lililopo. Nina imani, wale watakaofunga, hawatafikwa na mauti haya ya mauzauza kwani watakuwa wapo kwenye funga ya Mungu!”
Kauli hiyo ikamwingia Seba, akalikubali jukumu alilopewa!
**********
PADRI Toni na Seba waliondoka pamoja kuelekea kanisani. Kuonekana kwao wakiwa pamoja njiani kuliwafanya watu waitane ili kuonyeshana uwepo wao wa pamoja kwa watu hao wawili wakitembea na kuzungumza pamoja huku nyuso zao zikiwa za furaha. Tukio hilo likaonekana kama maajabu yaliyofanywa na Padri Toni kumponyesha Seba. Taarifa hizo zikaenea kwa kasi mitaani kadri Padri Toni na Seba walivyokuwa wakiekelea kanisani.
Padri Toni akiwa na Seba akapokewa na msaidizi wake kabla hajaingia nyumbani kwake.
“Utanisamehe nikikuita pembeni,” msaidizi alimwambia Padri Toni.
“Kuna nini?” Padri Toni aliuliza kwa mshangao.
“Ni taarifa kutoka Jedani!” msaidizi wake alisema huku akionyesha dhahiri, Seba hakutakiwa azijue taarifa hizo.
“Zinasemaje?” Padri Toni aliuliza bila ya kuonyesha kutilia maanani kile alichoambiwa awali kuwa alihitajiwa pembeni.
Msaidizi wake akamwangalia Seba, kisha akamwangalia Padri Toni usoni. Padri Toni akaendelea kukitambua kinachofikiriwa na msaidizi wake huyo.
“Eleza tu, Seba hana tatizo!” Padri alisema.
Akionyesha bado hana imani na uwepo wa Seba, msaidizi wa Padri Toni akasema, “Mathias amefariki!”
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Kitu cha kwanza kilichofanywa na Padri Toni ni kupiga alama ya msalaba kifuani pake. Kisha akauliza, “Ni nani aliyekuletea taarifa hizo?”
Msaidizi wa Padri Toni akalitaja jina la mjumbe mmoja aliyeondoka na timu ya watu watano kwa kumjulisha kuwa, amerudi na taarifa hizo. “Yuko sebuleni kwako anakusubiri,” alimalizia.
“Seba, twende!” Padri Toni alimwambia Seba na wote kwa pamoja wakaelekea nyumbani kwa Padri Toni.
Nusu saa baadaye, kukiwa na taarifa zilizozagaa kuhusu kuonekana kwa Seba akiwa na Padri Toni wakiongozana pamoja kwa amani na furaha iliyohesabiwa imeonekana usoni kwa Seba wakati wakielekea kanisani, ndipo kengele ya mwito wa dharura kutoka kanisani iliposikika. Kengele hiyo ikazifanya hisia za kila mtu ziwaze kuwa, mwito wa kengele hiyo utakuwa unahusiana na kuonekana pamoja kwa Padri Toni na Seba. Dhana ikawaingia, kwa vyovyote vile, watu hao wawili wanataka kuyazungumza yale matukio aliyokumbana nayo Seba wakati wa kifo cha Donna alipomfia mikononi mwake. Kila mtu akawa na hamu ya kumsikia Seba akikizungumza kwa kauli yake mwenyewe kile kilichomkuta!
Muda mfupi baadaye, misururu ya wakazi wa Zebati wakaonekana wakipandisha kilima kutoka pande tofauti za kisiwa hicho, wakielekea kanisani.
****
ILIKUWA siku ya tatu tangu kengele ya dharura ipigwe na wakazi wa Zebati kuhutubiwa na Seba, na ikawa ni siku ya pili tangu wakazi hao waanze kufunga kwa ajili ya maombi baada ya kuukubali ushawishi wa Seba kuwa wanatakiwa wafunge na kusali. Lakini pia, wakashitushwa na habari ya kuibwa kwa Msalaba Mtakatifu na kutoamini masikio yao pale walipoambiwa mhusika na wizi huo ni Mathias!
Siku hiyo ya tatu na ya pili kwa mfungo wa maombi, wakati wa asubuhi, wavuvi wanne kutoka kisiwa cha Zebati wakiwa ndani ya ngalawa wakimalizia kuivuta nyavu yao waliyokuwa wameitegesha baharini, wakaanza kupata faraja baada ya kuiona nyavu hiyo ikiwa na samaki wa kutosha baada ya wiki nzima ya ukame wa samaki kutokana na upepo mkali ulioukumba mwambao wote wa Zebati. Huku wakiwa wanaimba kwa furaha kupeana ari ya nguvu kumalizia kuivuta nyavu hiyo, hatimaye waliwamimina samaki ndani ya ngalawa yao. Lakini wakati wakimalizia kuwamimina samaki, ghafla kitu kingine kisichokuwa samaki kikatoka kwenye nyavu hiyo na kuangukia juu ya samaki. Wote wakapigwa na mshangao. Walipokiangalia kwa makini, wakagundua kuwa ni Msalaba!
Wakiwa wameshangaa, mmoja wao baada ya kuusafisha msalaba huo akasema, “Ni wa dhahabu, halafu unafanana na Msalaba Mtakatifu!”
Kauli ya mvuvi yule ikawavuta wenzake kuuangalia kwa umakini. Wote wakaafiki unafanana na Msalaba Mtakatifu.
“Ina maana misalaba mitakatifu iko mingi?” mmoja aliuliza.
“Pengine,” mwingine alijibu.
“Na huu unaweza ukawa Msalaba Mtakatifu?”
“Ule wa kanisani ulishushwa kwa nguvu za Bikira Maria na huu tumeuvua. Itakuwaje uwe mtakatifu?”
“Halafu si nasikia ule wa kanisani umeibwa na mwanafunzi mmoja aliyekuwa akisomea upadri?”
“Hata mimi nimezisikia taarifa hizo. Pengine huu umeletwa kupitia kwetu, inawezekana tumepata ubarikio tusioujua.”
“Pengine Bikira Maria ametuletea Msalaba mwingine Mtakatifu kupitia kwetu ili uende ukavikabili vifo vinavyotokea.”
“Tupewe kimyakimya hivi bila hata mmoja wetu kuoteshwa japo kwa ndoto ya maruweruwe? Haiwezekani!”
“Sasa tuufanyeje? Tukauuze? Maana hii ni dhahabu!”
“Siyo vibaya tukienda kuuza!”
“Lakini siyo kwa Zebati, Zebati hakuna watu wenye kipato kikubwa cha kumudu kuinunua dhahabu kama hii.”
“Mimi nina ushauri tofauti na nyie,” mvuvi mwingine aliyekuwa hajaingia kwenye mjadala huo alisema.
Wote wakamwangalia. “Haya tuambie,” mmoja wao alisema.
“Kwa nini tusiupeleke kanisani? Nadhani itakuwa baraka kwetu endapo tutafanya uamuzi kama huo hasa tukizingatia hakuna kati yetu mwendaji wa kanisani wa mara kwa mara. Hii itakuwa sehemu ya malipo yetu kwa Mungu.”
Awali walibishana, wawili wakitaka ukauzwe na wengine wawili wakitaka kwanza upelekwe kanisani, na kama utagundulika siyo ule Msalaba Mtakatifu ulioibwa, basi wauuze hata kwa pale kanisani kama watakuwa tayari kuununua. Wakakubaliana na wazo la kuupeleka kanisani kwanza.
********
TAARIFA za kuwasili kwa mwili wa Mathias zikawafikia wakazi wa Zebati ambao walikuwa na siku nne tangu waanze kufunga na kusali. Ndani ya siku hizo nne, kwa maajabu wasiyoyaamini na kwa mara ya kwanza, hakukusikika kwa mtu yeyote kufa kwa kupitiwa na upepo mbaya wala upepo huo kuvuma ndani ya siku hizo. Wakati kukiwa na habari hizo njema, ndipo wakasikia taarifa za kuletwa kwa mwili wa Mathias!
Baadhi ya wakazi wakatishia kutohudhuria mazishi yake kwa madai kuwa, Mathias hakustahili kufanyiwa mazishi yatakayoandamana na sala kwa sababu yeye ndiye aliyesababisha janga la maafa kisiwani hapo. Lakini pia wakahoji, itakuwaje mtu aliyemkaidi Bikira Maria aombewe kwa jina la Yesu kisha aende mbinguni? Sakata hilo likamfikia Padri Toni, naye bila ajizi akaomba kuonana na wakazi kabla ya kufanyika mazishi ya Mathias.
Padri Toni alipata wakati mgumu kuwatuliza wakazi hao ambao walikuwa wakiongea kwa wakati mmoja huku jazba ikiwa imewatawala.
“Hakuna atakayekwenda kumzika mshenzi kama yule!” baadhi yao walibwata.
“Mathias ana tofauti gani na Yuda Iskariote!” wengine walipiga kelele.
“Alaaniwe Mathias!” mayowe yalisikika.
“Jina la Bwana Yesu lisitumike kumwombea!” kelele zikazidi.
Padri Toni aliipunga mikono yake juu kuwatuliza wakazi hao ambao walionekana kama wamepagawa. Baada ya juhudi kubwa kufanywa na wasaidizi wake na Seba kusaidia kuituliza hali hiyo, hatimaye wakazi hao walitulia.
“Tumsifu Yesu Kristu,” Padri Toni alisema baada ya kuwepo utulivu.
“Milele amina,” wakazi wakaitikia kwa sauti zilizofanya mvumo.
Ili asilirudishe zogo ambalo alipata nalo taabu kulituliza, Padri Toni aliamua kutolitaja jina la Mathias kwa kulipa nafasi ya mwanzo. Badala yake, moja kwa moja akaanza kwa kusema, “Turudini kwenye maandiko Matakatifu yanayosema, “Msihukumu, msije mkahukumiwa, kwa kuwa hukumu ile mhukumuyo ndiyo mtakayohukumiwa, na kipimo kile mpimacho ndicho mtakachopimiwa. Je, mnayakubali na kuyaamini maandiko haya?”
Kwanza ilianza kwa wawili watatu kukubali huku wengine wakisita kukubali haraka kwa kuwa walishalijua lengo la Padri Toni kuyatamka maneno hayo. Kimya chao kilivyokuwa kikiendelea, ndivyo wengine walivyojitokeza kwa awamu kuungana na Padri Toni. Hatimaye wote wakajenga umoja kuwa wanayakubali na kuyaamini maandiko hayo.
Baada ya kuona umoja umejirudia miongoni mwa wakazi kulikubali neno lake, Padri Toni alisema, “Kama tunayaamini haya, basi haifai kumbagua mtu kwa tuhuma ya makosa yake kabla hajahukumiwa, si kwa imani yake, wala si kwa jinsia yake au rangi yake. Hukumu zinazomhusu Mwenyezi Mungu anazo Mungu mwenyewe, yeye ndiye mwenye kuhukumu, siyo ninyi. Tuungane pamoja tumpelekeni mwenzetu Mathias kwenye nyumba ya milele na mbele ya hukumu…”
Jioni, wakazi wa kisiwa cha Zebati wakaungana kwenda kumzika Mathias.
*****
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
MAELEZO ya Sajini Seba kuhusu kuwaona viumbe wa ajabu muda mfupi kabla ya Donna kufariki mikononi mwake, yalimsumbua sana Padri Toni. Akawa anajiuliza mara kwa mara, ilikuwaje viumbe wa ajabu wasiokuwepo kwenye uwepo wa binadamu wanatokea? Kuna nasaba gani kati ya viumbe hao na maafa ya kisiwani Zebati? Kuna siri yoyote ihusishayo viumbe hao na eneo hili? Uwepo wa viumbe hao kisiwani hapa ndiyo sababu ya kuteremshiwa Msalaba Mtakatifu kwa ajili ya kukilinda kisiwa hiki na watu wake? Ni kweli kulikuwa na majini yaliyokuwa yakiishi miaka ya zamani kama wenyeji wanavyovumisha? Ni nani mwenye kuijua historia hii kwa undani? Aliifikiria miongo kadhaa aliyoishi kisiwani humo tangu atoke Vatican, lakini kwa miaka yote hiyo ya uwepo wa kuishi kwake hapo kisiwani, alikuwa akisikia tu uvumi huo wa kuwa kulikuwepo na majini yaliyokuwa yakiishi kisiwani hapo kwa miaka mingi ya nyuma yakihusishwa na makaburi ya zamani, lakini taarifa hizo zilikuwa zikielezwa kwa namna tofauti na kuwa kama mkasa wenye visa zaidi ya kimoja, kiasi kwamba aliuchukulia huo ulikuwa ni uvumi tu!
Lakini baada ya janga la kufa kwa watu kisiwani humo na ushuhuda alioutoa Seba, Padri Toni alijikuta akishawishika kutaka kuijua historia ya kisiwa hicho na uvumi huo. Tukio la kuibwa kwa Msalaba Mtakatifu na matokeo ya ubashiri kuendana kwa aina fulani na majini yaliyokuwa yakizungumzwa, kulimfanya aamini kuna uhusiano kati ya uvumi huo unaohusisha uwepo wa Msalaba Mtakatifu.
Muda mfupi baada ya kutoka kwenye mazishi ya Mathias, bado maelezo ya Seba yalikuwa yakimpa usumbufu kwenye akili yake. Akiwa yupo nyumbani, Padri Toni alikwenda kuiosha mikono yake na kuifuta kwa taulo. Baada ya hapo alikwenda kwenye chumba chake cha kujisomea na kuanza kuvisaka vitabu vya zamani vyenye historia tofauti zenye kuelezea maisha ya zama za watawala wa kale ambazo historia zake nyingi zilihusisha matukio ya ajabu ya zama hizo na sehemu zake.
Kwenye kabati alikokuwa akivisaka vitabu anavyovitaka, kulikuwepo na vitabu visivyopungua kumi na vitano vya aina hiyo. Padri Toni alitoa kitabu kimoja baada ya kingine na kuvipitia kwa haraka haraka huku akiwa amesimama mkabala na kabati lenye vitabu hivyo. Hatimaye alipata kitabu kilichomvutia kutokana na historia iliyokuwa imeandikwa humo ambayo ilihusisha kisiwa cha Zebati. Akaondoka na kitabu hicho na kwenda kukaa kwenye kiti cha kivivu kilichokuwa kikiyumba mbele na nyuma. Alizifungua kurasa za kitabu hicho na kuzipitia kwa kuzisoma haraka-haraka huku akionekana kuziruka baadhi. Hatimaye alijikuta akivutiwa na moja ya kurasa aliyokuwa akiisoma. Akatulia na kuisoma kwa umakini, badala ya kufunua kwenda mbele, akaanza kurudi nyuma na kuonekana kutafuta chanzo cha habari aliyokuwa akiisoma. Akaupata ukurasa aliokuwa akiutafuta. Akaisukuma nyuma miwani yake ya kusomea kwa kutumia kidole chake na kuanza kusoma kwa utulivu.
Ilimchukua dakika nyingi kusoma kurasa zilizokuwa zimemvutia na kumtia msisimko pale alipojikuta akisoma historia iliyohusisha kisiwa hicho cha Zebati na enzi za utawala wa Mafarao wa Misri. Uhusiano kati ya watawala hao na kisiwa hicho yalimfanya Padri Toni ashindwe kukiamini alichokuwa akikisoma. Moja ya sehemu ya maandishi hayo yalikielezea kisiwa hicho kilikuwa kikitumika kama eneo kuu la watawala hao kufanyia matambiko kwa kuwachinja binadamu na kutumia damu yao kufanyia makafara na mambo mengi ya kiuchawi ya kumwasi Mungu kwa ajili ya kumwandaa Farao mtarajiwa atakayeiongoza Misri. Uchinjwaji wa binadamu hao wengi wao wakiwa ni watu weusi, damu zao zilitumika kufanyia mazindiko ya kulinda na kuzienzi tawala za Mafarao hao wanapoingia madarakani. Miili ya watu waliowachinja waliwazika kwenye kaburi maalumu ambalo baadaye, wakazi waliliita eneo hilo, ‘Makaburi ya zamani.’
Historia iliendelea kueleza kuwa, wakati hayo yalipokuwa yakifanyika, kisiwa hicho hakikuwa na wakazi waliokuwa wakiishi. Matendo hayo ya kikatili hatimaye yalimchukiza Mungu, hasira zake zikamlazimisha kuwaumba viumbe wenye mwonekano wa ajabu, akawapiga laana katika ujio wao duniani, kwani alikuwa hajawahi kuwaumba viumbe wa aina hiyo wakati alipoiumba dunia na uwepo wa binadamu. Akawatengenezea makazi yao maalum kwenye eneo walikokuwa wakizikiwa watu waliokuwa wakiletwa kuchinjwa. Uwepo wa viumbe hao ukaanza kushambulia kila msafara wa Mafarao watarajiwa wakiwa na wachawi wao na kukumbana na vifo vya ajabu kila walipokuwa wakija kwenye kisiwa hicho cha Zebati.
Baada ya kuonekana kuwa, kila msafara wa Farao mtarajiwa na wachawi wake unaokwenda kwenye kisiwa hicho ukiwa haurudi bila ya mtu hata mmoja, uongozi wa Misri ukaanza kupeleka wapelelezi kuchunguza kutokurudi kwa wenzao, lakini na wapelelezi hao nao baada ya kuonekana hawarudi, misafara hiyo ikasimamishwa. Usimamishwaji wa misafara hiyo ukakiacha kisiwa hicho cha Zebati kiwe hakina binadamu anayeishi wala kufika huko kwa miongo kadhaa.
Utekelezaji wa kuhamia kisiwani hapo ulianzishwa na jamii ya wavuvi kutoka Jedani na Ushelisheli ambao kidogo kidogo wakaanza kuenea kwenye maeneo tofauti ya kisiwa hicho, na ndipo walipoyagundua makaburi hayo na kuyaita, ‘Makaburi ya zamani.’ Ingawa kitabu hicho kiliweza kuelezea historia ya kisiwa hicho, lakini kasoro iliyopatikana kwenye maandishi yake ni kutokuelezea nini kilitokea kati ya wahamiaji baada ya kuhamia kwenye kisiwa hicho na viumbe hao wa ajabu waliohusishwa kuumbwa kwa dharura kutokana na hasira za Mungu. Lakini pia, kitabu hicho hakikueleza jina la ‘Zebati’ lililopewa kisiwa hicho lilitokana na nini.
Akiwa amemaliza kukisoma na kuanza kutafakari upungufu uliomo kwenye kitabu hicho, Padri Tino akausikia mlango wa mbele ukigongwa, akamwona mtumishi wake wa ndani akienda kuufungua mlango na kisha akamsikia akizungumza na watu waliopiga hodi.
Mtumishi alirudi alipokuwa amekaa Padri Toni na kuwaacha wageni kulekule mlangoni. “Kuna wageni wanaomba kuonana nawe,” alimwambia Padri Toni.
“Ni akina nani?” Padri Toni aliuliza.
“Wamejitambulisha kuwa ni wavuvi.”
“Wavuvi?” Padri Toni aliuliza kwa mshangao.
“Ndivyo walivyojitambulisha.”
“Waingize ndani,” Padri Toni alisema bila ya kufikiri mara mbili.
Wavuvi waliingia. Hawakuwa na mavazi ya kivuvi. Wote walionekana wasafi na mmoja wao alikuwa amebeba mzigo kwenye kigunia. Wakasalimiana na Padri Toni na kukaribishwa vizuri.
“Karibuni na niwasaidie nini?” Padri Toni alisema baada ya kukaa.
“Takriban siku nne zilizopita,” mmoja wa wavuvi wale aliyeonekana ni kiongozi wao alisema. “Mimi na wenzangu hawa wakati tukivua kwa kutumia nyavu, tumebahatika na kuuvua Msalaba ambao ni wa dhahabu na unafanana na Msalaba Mtakatifu. Lengo la kuuleta kwako, tunataka uuangalie kama unaweza ukawa ni Msalaba Mtakatifu ulioibwa, lakini kama utakuwa siyo, tutaondoka nao.”
Padri Toni akahisi moyo wake ukimwenda mbio. “Ninaweza nikauona?” aliuliza huku akiuzuia ushawishi uliomjia.
Msalaba ukatolewa kwenye gunia lililokuwa limeuhifadhi, na mara tu Padri Toni alipouona, akajiona akikiangalia kitu alichozoea kukiona. Akajiinua kutoka kitini na kwenda kuugusa ili kuhakikisha mguso wake kama unalingana na dhahabu. Mara baada ya kuugusa, Padri Toni akahisi kizunguzungu kimemjia. Alipokuwa akikaribia kudondoka, wavuvi wale wakawahi kuinuka na kumdaka.
“Unajisikia vibaya?” mmoja alimuuliza Padri Toni huku akiwa amemzuia.
“Oh, nilijisikia kizunguzungu kidogo, lakini sasa hivi nadhani niko vizuri,” Padri Toni alisema.
Wavuvi wakamrudisha kwenye kiti alichokuwa amekalia awali.
“Una hakika unajisikia vizuri?” mmoja aliendelea kumuuliza.
“Nadhani nilikaribia kupata mshituko wa moyo baada ya kuugusa huo msalaba…”
“Kwa nini umejisikia hivyo?”
“Kwa sababu huo ni Msalaba Mtakatifu! Naomba mtoke nje muwatangazie watu mtakaowakuta nje, waambieni Msalaba Mtakatifu umeonekana!” Mara baada ya kusema hivyo, Padri Toni alipiga alama ya msalaba kifuani na kusema, “Mungu ameikubali funga na sala tuliyosali kwa ajili yake!”
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
*********
KENGELE ya kanisa inayotoa mwito wa dharura ilipigwa, ikawashangaza wakazi na kujiuliza ni kitu gani tena kingine kilichojitokeza hadi kengele hiyo ipigwe? Kwa kuwa waliitii kengele hiyo kwa kuelewa haipigwi bila ya sababu ya msingi, wakaacha shughuli zao na kuharakia kwenda kanisani. Waliowahi kufika kanisani wakapata mapema taarifa za kupatikana kwa Msalaba Mtakatifu kabla ya mkusanyiko wa pamoja haujakutana, nao wakarudi mbio kuwawahi watu waliokuwa wakipanda mlimani kuja kanisani. Wakawaambia habari hizo njema za kupatikana kwa Msalaba Mtakatifu. Taarifa hizo zikaanzisha shangwe kwa watu hao waliokuwa wakielekea kanisani, na habari hizo zikazidi kuteremka kwenda kwenye makazi ya watu.
“Haleluya haleluya…” watu walisikika wakiimba kwa furaha kila kona na kuzidi kumiminika kwenda kanisani kuuangalia Msalaba Mtakatifu ulioonekana huku wavuvi walioupata msalaba huo wakibebwa kwa furaha, makofi na vifijo wakipigiwa na kusimikwa ushujaa wa uokozi wa kisiwa cha Zebati.
Kila aliyefika pale alijenga matumaini mapya baada ya kuushuhudia kuuona Msalaba Mtakatifu na kushangilia katika hali ya kupagawa kwa furaha.
“Amani yetu imerudi!” muumini mmoja alipaza sauti iliyosikika eneo hilo lililozungukwa na watu wengi waliohudhuria.
MAAJABU YA MWISHO
USIKU uliokuwa mwingi, uliogubikwa na giza totoro lililokosa mbalamwezi, wakazi wa Zebati wakiwa wamelala usingizi fofofo, moto mkubwa ukazuka kwenye ‘makaburi ya zamani’ na vivuli vya moto vyenye rangi ya dhahabu vikaonekana vikicheza cheza kwenye maeneo ya makazi ya watu. Wakazi wakaamka na taharuki, hofu ikawaingia. Wakaamshana kwa kupigiana kelele na kuonyeshana moto uliokuwa ukiendelea kuwaka kwa hasira ukiunguza miti na majani kwenye eneo hilo la makaburi. Milio ya miti na majani iliyokuwa ikitatarika kwa kuungua ilisikika na kuendelea kuwatia hofu wakazi hao.
Mmoja wa wakazi hao aliyekuwa ameamka na kuutazama moto huo kutoka kwenye dirisha la nyumba yake alikuwa Padri Toni. Yeye pekee ndiye aliyekuwa hakujengwa na hofu yoyote wakati akiuangalia moto huo baada ya fikra zake kurudi kwenye kitabu alichokisoma. Kitabu hicho kikawa ndiyo ufunguo wa kujua chanzo cha moto huo. Aliamini hizo zilikuwa nguvu za Mungu, zilizokuwa zikiwateketeza viumbe wa ajabu aliowaumba na kushuhudiwa na binadamu pekee aliyebahatika kuwaona na kubaki kuwa hai, Sajini Sebastian!
Wakati akiendelea kuuangalia moto huo, Padri Toni akatambua nguvu ya moto unaowaka lazima ungewatia hofu wakazi, wakadhani huenda janga jingine jipya limejitokeza. Akajiandaa akutane nao kuwaondoa hofu hiyo. Akaondoka dirishani na kwenda kusali.
Asubuhi wakazi wa Zebati, baadhi wakiwa tayari wameshafika mashambani na wengine wakijiandaa kwenda kwa ajili ya kilimo huku wengine wakiwa wameanza kuingia kwenye shughuli zao za kila siku, wote kwa pamoja wakashituka na kuangalia mlimani ambako kila mtu aliweza kuliona kwa uwazi kanisa kubwa la Kikatoliki lililozungukwa na miti aina ya mivinje.
Kengele ya mwito wa dharura ilikuwa ikisikika kutoka kwenye kanisa hilo!
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
MWISHO
0 comments:
Post a Comment