Simulizi : Msalaba Wa Dhahabu
Sehemu Ya Nne (4)
“Huwezi kujua, pengine ni mwanzo wa upepo mbaya. Wacha nikurudishe nyumbani!”
Wakageuza bila ya kuongeza neno la kubishana.
“Tufanye haraka!” Donna alisisitiza wakati wakitembea., hali fulani ya woga ilionekana kumwingia.
“Lakini mimi sitaingia nyumbani, nitageuzia kibarazani ili na mimi niwahi kurudi nyumbani,” Seba alisema kukubaliana na takwa la Donna.
“Kwa nini usilale kwangu?” Donna aliuliza.
“Wacha tu nirudi nyumbani.”
“Mji wote hauna watu, wote wako kanisani. Nahofia kutembea peke yako. Ni afadhali kama ingekuwa watu hawakwenda kwenye sala, tatizo lolote lingekutokea kungekuwepo na watu wa kuwa nao. Lakini angalia jinsi mji ulivyokuwa mtupu halafu uko ukimya, ukipata tatizo ni nani atakayekuona? Ni bora leo ulale kwangu, Seba.”
“Usiwe na wasiwasi Donna,” Seba alisema na kumshika Donna begani. “Niache tu nirudi nyumbani, nitafika salama.”
“Nahisi kama vile naogopa!” Donna alisema na kumwangalia Seba. “We unajisikiaje?”
Seba akaonekana kuzubaishwa na kauli hiyo. Kisha kabla hajajibu, Donna akaonekana kama anayesikilizia kitu kwa kukigandisha kichwa kama anayetega sikio. “Unausikia upepo unaovuma? Na mbwa nao hao wameanza kubweka.”
Kauli hiyo ikamfanya Seba apigwe na butwaa na kumwangalia Donna kwa kumuiba. Ni kweli vitu alivyovizungumza Donna vilikuwa vikisikika kwa wakati huo, lakini Seba hakuwa huko kimawazo. Mawazo yake yalikuwa kwengine, alikuwa akiiwazia kauli ya Donna ambayo ilimrejesha kwenye kumbukumbu ya mahojiano aliyoyafanya na Zebu saa chache baada ya Maria kufariki. Zebu alitoa madai kama hayo kuwa, muda mfupi kabla ya Maria hajakufa, Maria alilalamika kuwa, alikuwa akijisikia woga na akataka kujua kutoka kwa Zebu kama naye alikuwa akijisikia hivyo. Akiwa hapo, Seba alishangaa kumwona Donna naye akiitoa kauli kama hiyo! Inaashiria nini? alijiuliza.
“Vipi?” Donna aliuliza baada ya kumwona Seba hayupo kimawazo.
Seba akakurupuka na kujifanya kupuuza. Akasema, “Hakuna chochote!”
“Kwa hiyo utalala?” Donna aliuliza na kumwangalia Seba machoni.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Seba alishusha pumzi na kutumia sekunde chache kabla hajajibu. Hakuelewa kwa nini alikuwa akikazania kurudi nyumbani kwake. “Leo niache tu nikalale nyumbani, lakini nakuahidi, kesho nitakuja kulala kwako.”
Kabla ya Donna hajajibu pendekezo la Seba, macho yake yakaangalia mlango wa mbele wa nyumba yao iliyokuwa hatua chache kutoka walipo ambao ulikuwa umefungwa. Akageuka na kumwangalia Seba. “Kwa hiyo umeamua kutolala kwangu?” alisema.
“Unajua Donna,” Seba alisema na kusimama huku akiashiria wataagania hapo aliposimama. “Si kwamba nina sababu yoyote ya kung’ang’ania kwenda kulala kwangu, hapana! Bali kuna kitu kimeng’ang’ania kwenye nafsi yangu kikiniambia nirudi nyumbani.” Baada ya kusema hivyo akageuka kuiangalia nyumba anayoishi Donna. “Kuna mtu yeyote aliyebakia nyumbani kwenu zaidi ya Costa?” aliuliza.
“Yupo Costa na mdogo wake. Hata Maiko yupo!” Donna alijibu.
“Hee, hata Maiko hakwenda kwenye sala ya maombi?” Seba alishangaa. “Mimi nadhani nyumbani kwangu kutakuwa hakuna mtu aliyebaki. Kabla ya kuja huku, nyumba nzima niliisikia wakihimizana kwenda kanisani. Labda ni sababu hiyo ya nyumba kubaki peke yake ndiyo inayonifanya niwaze kurudi nyumbani.”
“Haya, kesho!” Donna alisema kwa sauti iliyoonyesha kushindwa kuendelea kumshawishi Seba.
“Utamgongea Costa kukufungulia mlango?”
“Nitakwenda kumgongea yeye!” Donna alijibu na papohapo kuiangalia nyumba yao kwa mara moja na kisha kumwangalia tena Seba.
“Haya, ni hapo kesho!” Seba aliaga na kuukamata mkono wa Donna, kisha alijipinda na kukibusu kiganja cha Donna.
“Moyo wangu ni mzito kukuacha ukienda peke yako Seba,” Donna alilalamika.
Seba akaunda tabasamu la kujiamini, “Unadhani nitakuwa mhanga wa upepo mbaya usiku huu?” aliuliza. “Nitafika nyumbani salama, usijali wangu.” Baada ya kusema hivyo, akainama tena. Safari hii akambusu Donna shavuni. “Lala salama wangu,” alisema.
Donna akafanya tabasamu fupi. “Wacha nikusindikize mpaka mtaa wa pili,” alisema.
“Aaa Donna, sasa huo utakuwa utoto!” Seba alilalamika.
“Nataka nikusindikize hadi mtaa wa pili, baada ya hapo nageuza narudi zangu.”
Seba akamwangalia Donna. Macho ya Donna yalikuwa yaking’ara kimapenzi. Hali hiyo ikamfanya Seba alainike. “Lakini hadi mtaa wa pili!” aliweka sharti. “Zaidi ya hapo sitakuruhusu uendelee, sawa?”
“Sawa!” Donna alijibu.
Donna akamsindikiza Seba hadi kwenye kona inayoingia mtaa wa pili.
“Rudia hapa!” Seba alimwambia Donna na kusimama.
Donna akatoa kicheko kidogo na kumwangalia Seba. “Haya narudi,” alisema huku akimwangalia Seba kwa jicho la mahaba.
Seba akawa kama amezubaa huku akimwangalia Donna.
“Mbona hauendi?” Donna alimuuliza Seba.
“Nataka kwanza nikuone ukirudi hadi ukaribie nyumbani kwenu, kisha ndiyo mimi nitaondoka.”
“Shauri yako, sisi kwetu karibu, wewe kwenu mbali!” Donna alisema huku akielekea kwao.
Seba alisubiri hadi Donna alipobakiza nyumba kama nne kuweza kufika nyumbani kwao ndipo naye alipogeuka na kuondoka, lakini hakukata kwenye kona hiyo waliyokuwa wamesimama, badala yake aliamua kunyoosha kwa lengo la kutaka kuhakikisha kumwona Donna hadi anaingia nyumbani kwao. Akiwa anatembea kwa mwendo wa kasi kidogo, Seba aligeuka nyuma kumwangalia tena Donna akitarajia kumwona amebakiza hatua chache kufika kwao. Hakumwona! Akashangaa, ilikuwa kama Donna amepotea ghafla machoni pake! Hakuamini kuwa angekuwa amekwishaingia kwao kwa haraka hivyo. Kisha akakumbuka kuwa, Donna angelazimika kwenda dirishani kwa Costa kumgongea ili amfungulie mlango. Wazo hilo likamfariji, akaamini kuwa, Donna atakuwa ameingia kwenye kichochoro cha nyumba yao kwa ajili kumgongea Costa. Akapata ushawishi wa kumsubiri hadi amwone akitoka kwenye uchochoro alioingia akiwa anaelekea kwenye mlango wa mbele kwa ajili ya kufunguliwa.
Akiwa anasubiri amwone Donna akitoka kwenye uchochoro aliohisi ameingia, Seba alianza kuingiwa na wasiwasi baada ya kuona Donna anachelewa kujitokeza. Wazo la kumfuata kwenda kumwangalia likamjia. Lakini kabla ya kuinua mguu kwa ajili ya kuitimiza azma yake hiyo, akageuka kuangalia upande aliokuwa akielekea awali. Hakujua ni nini kilichomgeuza kuangalia huko, lakini mara alipogeuka na kuangalia akapata mshituko. Mbele yake kulikuwa na ukungu mweupe uliokuwa upo katikati ya barabara ukija kama moshi kuelekea kule aliko!
*****
PADRI Toni alikubali matokeo. Alikubali kushindwa, uwezo wa kuwazuia waumini waliotaharuki kwa sala aliyokuwa akiiendesha ukafikia tamati. Akawaangalia kwa macho yaliyojaa fadhaa walivyokuwa wakikanyagana mlangoni kila mmoja akitumia nguvu zake kulazimisha kutoka nje ya kanisa huku vilio vya hofu na maumivu vikisikika. Kimbunga kilikuwa kikiendelea kupiga humo kanisani na kanzu aliyokuwa nayo ilikuwa ikipeperushwa na kuwa kama bendera. Alikuwa akipingana na upepo uliokuwa ukitaka kumwangusha huku yeye mwenyewe akiwa amekumbatia nguzo kujizuia kuzolewa na kimbunga hicho.
Pamoja na hali hiyo kumtia kwenye fadhaa, lakini pia alikuwa akishuhudia maajabu ambayo alikuwa haamini kama yanatokea mbele ya macho yake. Mishumaa iliyoangushwa na waumini waliotaharuki iliendelea kuwaka ingawa kimbunga kikali kiliendelea kuangusha vitu kadhaa vingi vikiwa vya dhahabu vilivyotundikwa kwenye madhabahu.
Padri Toni hatimaye alimwona mtu wa mwisho akitoka kwa kujizoa zoa kwenye lango la kanisa na mara mtu huyo alipotoka na mishumaa nayo ikasinzia na kuanza kuzimika mmoja baada ya mwingine! Yalikuwa ni maajabu kwake, lakini kwa moyo wa chuma aliokuwa nao, mara baada ya kimbunga kutulia humo kanisani, Padri Toni badala ya kutoka nje na kukimbia kama walivyofanya wengine, yeye alijikokota na kwenda kuwasha mshumaa ambao aliutumia kwenda kuwashia mingine iliyokuwa juu ya altare.
Akiwa amezungukwa na vitu kadhaa vilivyoangushwa na kimbunga na kuzagaa sakafuni, huku vingine vikiwa vitu vilivyoachwa nyuma na waumini kama, viatu, hereni, kofia, vitambaa vya kichwani na vinginevyo, Padri Toni aliviangalia vitu hivyo kwa masikitiko na kutingisha kichwa. Tukio lililotokea lilikuwa bado limemuweka njia panda, alishindwa kuamini kwa nini nguvu za sala zilishindwa kuizuia hali hiyo wakati Msalaba Mtakatifu ambao uliaminika kuwa na uwezo wa kuzuia gharika yoyote ulikuwemo mle kanisani. Wazo hilo likamfanya auinue uso wake juu kuuangalia Msalaba Mtakatifu pale ulipo ili iwe kama ushuhuda wa jinsi ulivyoshindwa. Haukuwepo! Akashituka na kutoa macho baada ya kugundua hivyo! Yesu Kristu! alihamanika peke yake.
Akaanza kubabaika huku akijaribu kuutafuta kwa kuangaza macho kama aliyepotelewa na kitu kilichotoka maungoni mwake, akauona umelala chini ukiwa umedondoka kutoka mahali ulipokuwa. Nao, ulikuwa ni moja ya vitu vilivyoangushwa na kimbunga hicho! Kwa mwendo wa taratibu, Padri Toni aliuendea msalaba huo ulipoanguka na alipoinama kutaka kuugusa, ghafla akasikia sauti ya kikohozi kutoka nyuma yake! Akaganda kwa mshituko na kubaki vilevile akiwa ameinama, akatulia kama sananu iliyotengenezwa kuwa hivyo. Aliuhisi mwili wake ukiwa umeingiwa na ubaridi wa woga. Awali, aliamini kusingekuwa na mtu yeyote aliyekuwa amebakia humo kanisani. Ufahamu wa kuwepo kwa mtu mwingine kukamsumbua kiakili. Atakuwa nani? alijiuliza huku akijaribu kuidhibiti taharuki iliyomjia. Akajaribu kuangalia nyuma kwa kuchungulia kupitia katikati ya miguu yake. Chini ya kanzu yake akaiona miguu ya mtu aliyemsimamia kwa nyuma. Hakuwa na uhakika kama alikuwa ni binadamu halisi au ni mmoja wa viumbe wanaozungumzwa na wakazi waliowapa jina kwa kuwaita upepo mbaya. Akahisi mauti yamemjia!
Padri Toni alijiinua taratibu bila ya kugeuka nyuma, akasali kimya-kimya ili awe na uwezo wa kukabiliana na kiumbe aliyekuwa nyuma yake. Mapigo ya moyo yakimwenda kasi, akageuka taratibu kuangalia nyuma, akapigwa na butwaa la ghafla baada ya kukutana na kiumbe asiyemtarajia!
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
*********
SAJINI Seba akiwa kama aliyepigwa ganzi baada ya kuuona ukungu, akatulia kuuangalia. Kumbukumbu ikiwa inamrudia vyema kuhusu maelezo aliyopewa na mashuhuda walioshuhudia kuziona maiti za baba Sai, Maria na Paulo kwenye eneo walilofia, wakielezea kuhusu ukungu waliouona, hisia za kuwa zamu yake imefika kukumbana na mauti hayo zikachukua nafasi yake! Seba kama anayenyata, alianza taratibu kurudi kinyumenyume bila ya kugeuka huku akiuangalia ukungu uliokuwa mbele yake ukizidi kusogea.
Ghafla akapepesa kwa kasi macho yake baada ya kuona aina fulani ya kiumbe ndani ya ukungu huo aliyefanana na kitu alichohisi ni farasi. Akajiuliza, ni kiza ndicho kinachoifanya akili yake itengeneze kiumbe wa aina hiyo kwa ajili ya woga? Au ni kweli amekiona kiumbe anayefanana na farasi? Akashindwa kupata jibu lenye uhakika. Lakini akili yake ikamlazimisha aamini kuna kitu alichokiona kikiandamana na ukungu huo. Hatimaye macho yake yakadhihirisha kuwa, alikuwa akiona aina ya viumbe ndani ya ukungu huo ambao alikuwa na uhakika hawakuwa binadamu! Sajini Seba hakufikiri tena mara mbili, aligeuka na kuangalia alikotoka na kuanza kutoka mkuku. Mwelekeo wake ukawa mmoja, nyumbani kwa Donna!
Mbele yake akamwona Donna akitoka kwenye kichochoro cha nyumba yao alikokwenda kumgongea dirisha Costa! Kutokana na woga uliomwingia, Seba aliita kwa kelele huku akimtaka Donna afanye haraka kuingia ndani!
Akiwa anakimbia kwa kutumia nguvu zake zote, Seba akaanza kuzisikia hatua kutoka nyuma yake zikiwa zinamkaribia, lakini hazikuwa hatua za binadamu au mnyama mwingine kama vile mbwa, badala yake akawa anasikia milio ya hatua za kwato! Akatambua kuwa, kuna mnyama anayemfukuza!
“Donna!” aliita tena akiwa hatua chache kuifikia nyumba anayoishi Donna huku akiuona mlango ukifunguliwa. “Usifunge mlango!” na kurudia kuitamka kauli hiyo.
Akili yake ikahamanika baada ya kumwona Donna amesimama mlangoni badala ya kuingia! Donna akaonekana kama aliyezubaishwa na kelele za Seba.
“Ingia ndani Donna, upepo mbaya unakuja!” Seba alipiga kelele.
Seba akageuka nyuma kuangalia umbali uliopo kati yake na kiumbe anayemfukuza. Akamwona amemkaribia! Kumwona kwake kwa karibu kukawa kumemfanya amwone vizuri kiumbe huyo! Uso wa Seba ukazidisha taharuki!
“Nakufa!” Seba alipiga kelele.
**********
“ROBERT!” Padri Toni aliita kwa mshangao na kushusha pumzi za afueni zilizosheheni woga. Mwili wake ukalegea kutokana na tahfif iliyomjia. “Nilidhani hakuna mtu mwingine aliyebakia humu ndani!” alisema.
Mzee Robert akionekana kuwa mtulivu lakini mwenye uso uliojaa uchovu, alimwangalia Padri Toni kivivu-vivu. “Hata mimi nilidhani nimebaki peke yangu!” alisema. “Nilikuwa nimejificha chini ya mabenchi hadi gharika ilivyoisha. Nikawa na uhakika hakutakuwa na mtu ambaye angebaki humu ndani, lakini nilivyoinuka nikatambua kumbe sikuwa peke yangu baada ya kukuona!”
Padri Toni akamwangalia mzee Robert. “Huonekani kupata hata mchubuko! Umeepuka vipi ndani ya mkanyagano kama ule?” aliuliza.
“Nilitaharuki, nikawahi kujificha mapema kwenye mabenchi. Nilijua nisingeweza kukanyagana kugombania kutoka nje,” mzee Robert alisema. “Lakini kingine hasa kilichonifanya nizidi kuendelea kubaki humu ndani ni kuhusu huu Msalaba Mtakatifu, niliuona ukianguka na nadhani ndiyo sababu kuu iliyowafanya waumini wachanganyikiwe! Nikaapa, kama nitasalimika basi lazima niukague huu msalaba!” mzee Robert alisema huku akiuangalia msalaba uliokuwa chini ya miguu ya Padri Toni.
Padri Toni akafanya mshangao usoni. “Lazima uukague? Una maana gani ukisema hivyo?” alisema. “Mimi nilidhani ungesema labda ni kwa ajili kuulinda usije ukaibwa!”
Kauli ya Padri Toni ikamshitua mzee Robert. Kwa nini azungumzie tishio la kuibwa kwa msalaba? alijiuliza. Inawezekana na yeye ana hofu kama yangu ya kuuona msalaba umeshindwa kuyakabili majanga yanayokikumba kisiwa hiki? “Hilo nalo pia lilikuwepo kichwani mwangu,” alisema kwa utulivu. “Kitendo cha Msalaba Mtakatifu kuangushwa na kimbunga ni ishara isiyopendeza. Ni ishara inayoonyesha, neno limetimia! Na ndiyo sababu ya kutaka kuhakikisha, je, ni kweli neno limetimia?”
“Kwa kuukagua?” Padri Toni aliuliza na kuonyesha hajamwelewa vizuri mzee Robert.
“Ndiyo hasa lengo langu!”
“Ukidhamiria nini?”
“Kuna uwezekano tukawa tunasali kwenye msalaba ambao siyo!”
Padri Toni akayatuliza macho yake usoni kwa mzee Robert, kisha akauangalia msalaba uliopo chini ya miguu yake.
“Ilikwishatabiriwa, utakapoibwa msalaba huu, ndipo majanga yatakapotokea,” mzee Robert alisema wakati macho ya Padri Toni yakiwa bado yanauangalia msalaba.
“Kwa maana nyingine, ungekuwa na nguvu usingeangushwa na kimbunga?”
“Swadakta! Kimbunga ni moja ya majanga, na neno lilisema, Msalaba Mtakatifu umeletwa kwa ajili ya kukabiliana na majanga, vipi majanga yaonekane kujitokeza kisiwani kwetu huku Msalaba Mtakatifu ukiwepo? Hapo lazima kuwe na walakini!”
Bila ya kutamka neno jungine, Padri Toni aliinama na kuushika msalaba uliokuwa chini. Akatulia kama aliyehisi jambo. Kisha akatumia nguvu kidogo kuusogeza, ukasogea! Kwa kuwa hakutarajia kukutana na wepesi kwenye kuusukuma msalaba huo, nguvu aliyokuwa ameitumia ikamyumbisha kidogo. Lakini pia, wakati msalaba huo uliposogezwa ulitoa mlio wa bati wa kuburuzika.
“Hili ni bati?” Padri Toni alisema kama vile alikuwa akijiuliza mwenyewe. Kisha kwa sauti iliyopanda akahitimisha kwa kusema, “Robert, hili ni bati, siyo dhahabu!”
Kauli hiyo ikamfanya mzee Robert agande vilevile alivyosimama, kauli ikampotea ghafla.
Mathias! aliwaza.
*********
MZEE Robert alijumuika na Padri Toni kuushika msalaba huo na kuuinua. Ulikuwa mwepesi tofauti na jinsi ulivyokuwa ukionekana.
“Ni bati lililopakwa rangi ya dhahabu. Nadhani uliibwa siku dirisha lilipovunjwa, walioiba ndiyo waliouweka msalaba huu ili tuendelee kuuamini huku wao wakiondoka na Msalaba Mtakatifu!” Padri Toni alisema akiwa amesimama wima.
Mzee Robert hakujibu. Moyoni alikuwa na fadhaiko na akilini alikuwa akijituhumu fedheha inayomwandama kwa kutoliweka wazi suala la ndoto alizoota zinazomhusu Mathias. Hofu ilikuwa imemjia kuwa, baada saa chache taarifa za kuibwa kwa Msalaba Mtakatifu zitaenea kisiwani pote! Taarifa hizo zingewafanya wakazi wajiulize ni nani aliyethubutu kukifanya kitendo hicho? Fikra za kumtafuta mwizi zingeanzishwa kwa watu kuliweka tukio la wizi huo na kupotea kwa Mathias, jibu la hesabu hizo kwa haraka zingemtuhumu moja kwa moja Mathias! Nyumba yangu itakuwa na tuhuma za wizi huo! mzee Robert alifadhaika nafsini mwake huku akiendelea kuuangalia msalaba bandia lakini akiwa hauoni!
*********
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
SEBA alikiingia kibaraza cha mbele kwa kasi na kumvamia Donna, akaingia naye ndani kwa nguvu kubwa, akakosa mhimili wa kujizuia, yeye na Donna wakamkokota Costa aliyekuwa hatua chache kutoka mlangoni na kuanguka naye pamoja ukumbini. Seba akamsikia Donna akitamka neno, lakini kutokana na purukushani hiyo akawa hakuelewa kilichosemwa na Donna!
Seba alionekana kuchanganyikiwa, taharuki na ushujaa vyote akaviweka pamoja. Akausukuma kwa nguvu mlango kwa kupiga teke, mlango ukajipiga bila ya kujifunga, ukaacha uwazi. Tukio hilo likamfanya Seba ainuke kwa kukurupuka, akaufuata mlango na kuufunga huku akiwaambia wenzake, “Kimbilieni vyumbani!”
Costa akakurupuka na kukimbilia chumbani kwake, lakini Donna akabaki palepale alipoangushwa na Seba. Seba akarudi alipokuwa amelala Donna, akakikirika naye kumbeba na kuingia naye chumbani kwa Donna na kumlaza kitandani, kisha akawasha taa. Ghafla akajiona akiishiwa nguvu baada ya kumwangalia Donna pale kitandani. Donna alikuwa akitokwa na damu mdomoni, puani na masikioni!
Seba alizubaa akiwa haamini anachokiona mbele yake, ghafla akili zikamrejea, akakumbuka Donna alikuwa na tabia ya kuhifadhi panga uvunguni mwa kitanda. Bila ya kufikiri mara mbili, Seba alikurupuka, akapiga magoti na kuchungulia chini ya kitandani, akaliona panga! Akatia mkono uvunguni na kulitoa, akaifuata taa, akaichukua na kutoka ukumbini huku akiapa kwa sauti, “Nataka na mimi mniue!”
Alipofika ukumbini akapigwa na butwaa baada ya kuuona ukungu ukitoweka kupitia kwenye penyo za mlango kutoka sehemu alipokuwa ameangukia Donna. Hali hiyo ikamchanganya zaidi, akili ikawa siyo yake tena, ghafla alianza kucharanga panga kwenye ukungu ule huku akipiga kelele zenye hasira. Panga likawa linapungwa huku na kule kama anayefyeka, hatimaye pumzi zikamwishia na kuanguka!
*****
ASUBUHI baada ya taarifa za kifo cha Donna kusambaa kisiwani kote na matukio yaliyotokea kanisani wakati wa sala maalum ya maombi, hofu ikatawala kisiwani humo, kila aliyemwona mwenzake, mazungumzo yakawa ni hayo. Siku hiyohiyo kamati ya wazee na kikundi cha waganga wa jadi wakakaa kikao cha pamoja kuandaa mkakati wa kupambana na gharika inayokikumba kisiwa chao.
Mazungumzo yao yakajikita kuuangalia mwanzo wa matukio yalivyoanza. Wakahesabu kwa kuanza na Mathias ambaye alipotea ghafla, lakini pia ikagundulika kuwa, siku aliyopotea Mathias ndiyo siku ambayo wavuvi wawili walipopotea. Ingawa awali ilidhaniwa kwamba wavuvi hao walikwenda visiwa vya jirani kwa ajili ya shughuli zao za kiuvuvi, lakini baada ya taarifa zilizoletwa na wavuvi wengine ambao ni wazoefu wa kwenda kwenye visiwa hivyo vya jirani kwa ajili ya uvuvi kusema kuwa hawajawaona wavuvi hao wakifika huko, ndipo ikaanza kukubalika kuwa, nao walikuwa wamepotea kama alivyopotea Mathias! Hofu ikakitwa kwenye kikao hicho kuwa, huenda kupotea kwa Mathias pamoja na wavuvi hao ulikuwa mwendelezo wa yale yanayokikumba kisiwa hicho!
Ingawa kamati hiyo ya wazee iliwaweka baadhi ya wakazi kusubiri wangetoka na jibu gani kwenye kikao chao na waganga hao huku wengi wakishurutisha lazima kufanyike matambiko kisiwani humo, lakini baadhi ya wakazi hofu zao zikakosa subira. Msururu wa akinamama waliobeba mizigo kichwani, watoto migongoni na wengine wakiwakamatia mikononi na baadhi ya wanaume waliokuwa katika hali kama hiyo, walionekana wakielekea pwani kwa ajili ya kukwea vyombo kukikimbia kisiwa hicho ambacho ilishaaminika kimevamiwa na majini yanayopoteza na kuua watu! Huo ukawa mwanzo wa wakazi kuzitenga rozari na misalaba, imani za kishirikina zikaanza kuchukua nafasi yake!
Uvumi huo wa kuwepo majini, wengi waliukubali. Waliukubali kwa sababu waliuhusisha na hadithi za zama za nyuma zilizokuwa zikihadithiwa kuwa, enzi hizo kisiwa cha Zebati kilikuwa kikikaliwa na majini ambao walilazimika kuhama baada ya binadamu kuingia kisiwani humo! Ingawa hadithi hiyo ilikubalika miongoni mwa wakazi, lakini hatimaye ikaanza kupotea masikioni mwa watu. Lakini baada ya kisiwa hicho kuingiliwa na hali tata ya watu kufa na kupotea kimiujiza, hadithi ya majini hayo ikarudishwa upya. Habari zikaenea kwa kasi kuwa, wale majini waliokimbia binadamu, wameamua kurudi tena kwenye mji wao! Na vifo vinavyotokea na watu kupotea ni ulipizaji wa kisasi unaofanywa na majini hao ili kuhakikisha binadamu hakai tena! Na ili kukabiliana na hali hiyo, ndipo baadhi ya watu walipodai kafara na matambiko yafanywe haraka kisiwani humo. Hoja hiyo ikatekwa na waganga wa jadi, wakaiendeleza kuwa, bila ya makafara kufanyika, watu wote wanaoishi kisiwani humo watapotea kimiujiza au kuuawa!
Ilipofika mchana, kamati ya wazee ikakubaliana na hoja ya waganga wa jadi kuwa, kafara na matambiko yafanywe! Taarifa ikasambazwa, na watu wenye mifugo wakatakiwa waiandae mifugo yao myeusi kwa ajili ya kuchinjwa!
*********
WAKATI taarifa za waumini kupoteza imani na kanisa zikiwa zimesambaa kisiwani pote, mzee Robert Mizengwe alikuwa akizunguka ndani ya ofisi ya Padri Toni iliyomo kanisani akienda huku na kule huku Padri Toni mwenyewe akiwa amekaa kwenye kiti cha ofisini, kidevu chake akiwa amekipakata kwenye viganja vyake vya mikono na wakati mwingine macho yake yalikuwa yakihama kuufuatia mwelekeo aliokuwa akiuelekea mzee Robert, wote wawili walionekana kuchanganyikiwa na taarifa hizo!
Kwa takriban ndani ya muda wa saa moja watu hao walikuwa wakijaribu kutafuta ufumbuzi wa suala hilo hasa wakizingatia ni wao wawili peke yao ndiyo waliokuwa wakiijua siri ya janga linaloikumba kisiwa chao baada ya kutambua kuwa, Msalaba Mtakatifu ulikuwa umeibwa, na ule uliokuwa ukitumika ulikuwa ni bandia! Ubashiri wa kale ulikuwa umetimia!
Lakini pia, tukio hilo la kutambua Msalaba Mtakatifu ulikuwa umeibwa lilimfanya mzee Robert kwa mara ya kwanza akiri mbele ya Padri Toni kuuelezea wasiwasi wake dhidi ya mjukuu wake Mathias kuwa, kutoweka kwake kuna unasaba na wizi huo! Kwa maelezo hayo, ikamlazimu aeleze sababu za kumtuhumu mjukuu wake huyo. Ndipo akazielezea ndoto alizokuwa akiziota ambazo ziliendana na matukio yaliyotokea hadi lile la kuvunjwa kwa dirisha la kanisa!
Maelezo ya mzee Robert yalimshangaza Padri Toni. Aliyachukulia ni kama mifano iliyowatokea manabii ambao walioteshwa ndoto na kuwa ubashiri wa kweli.
“Huenda Mungu anataka kukupa Utakatifu!” Padri Toni alisema.
“Nafsi yangu bado ina ubinafsi, huwezi kuupata Utakatifu ndani ya ubinafsi!” mzee Robert alisema huku akitikisa kichwa.
“Kwa nini unasema hivyo?”
“Nilistahili kukwambia ndoto hizi mapema, lakini sikufanya hivyo hadi madhara yametokea, na hii imetokana na sababu ya kutaka kumlinda mjukuu wangu. Mtu wa aina yangu aliyepata ubarikio wa kuoteshwa ndoto zenye ubashiri wa kweli, halafu akawa kimya kwa ajili ya ubinafsi wake, katu hawezi kuupata Utakatifu. Nadhani Mungu amenipa mtihani ambao umenishinda!”
“Itabidi uje kutubu dhambi zako!”
“Unadhani kutaniondoa kwenye ubinafsi wangu?” mzee Robert alisema kwa sauti iliyokata tamaa huku akionyesha kukataa kwa kutikisa kichwa. Akaifuata meza ya Padri Toni, akajiinua na kuikalia ncha ya meza hiyo kwa upande mmoja wa makalio yake. “Nadhani tujadili suala la janga hili litakavyoondoka hapa kisiwani wakati Msalaba Mtakatifu umeishaibwa, kuliko kuendelea kuuzungumza Utakatifu wangu ulioshindikana!” aliendelea. “Watu bado wanaendelea kufa, hatujui ni nani usiku wa leo atafikwa na mauti, lakini pia hatujui gharika ya kimbunga inachopiga takriban kila siku, usiku wa leo kitafanya uharibifu gani. Kama kimbunga kimeweza kuliparaganyisha kanisa na waumini kutawanyika kwa kukimbia kwa hofu, ni wazi imani ya waumini kwa kanisa imeshaanza kupotea!”
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Ili kuwarudishia imani, itabidi tuwaeleze kuwa, ni Mathias ndiye aliyeiba Msalaba Mtakatifu, na ndiye chanzo cha majanga yanayoikumba Zebati!” Padri Tino alisema.
“Hapana!” mzee Robert alisema kwa sauti iliyoonyesha moja kwa moja kutopendezewa na rai hiyo. Akateremka kutoka mezani na kumwangalia Padri Toni. “Waumini watatuona ni wanafiki!” alisema kwa sauti yenye ukali kidogo. “Hakuna atakayetuamini wala kutuelewa! Matukio ya vifo vya kimiujiza vinavyoendelea na gharika ya kimbunga kupiga hadi kanisani huku kanisa likitumika kuwa ni eneo pekee ambalo lingeweza kukabiliana na janga hili kwa kufanya maombi maalum limeshindwa kuonyesha uwezo wake! Kila usiku unakuwa ni usiku wa kifo cha mtu, ulioaminika kuwa ni Msalaba Mtakatifu umeshindwa kuizuia gharika ya kimbunga kilichopiga kanisani na baadaye kufuatiwa na kifo kingine cha Donna! Lakini pia, imani ya waumini na wakazi wote wa Zebati wameanza kuamini, ni janga lililopo ndilo lililowapoteza kimiujiza Mathias na wavuvi wawili kwa kuamini wamechukuliwa na majini! Hiyo ndiyo imani yao kwa sasa hivi!
“Ni mimi na wewe ndiyo tunaoujua ukweli wa uwepo wa janga hili, ni mimi na wewe ndiyo tunaojua kisiwa chetu hakina tena kinga ya Msalaba Mtakatifu, na ni mimi na wewe ndiyo tunaoamini hivyo, lakini waumini hawataamini tutakapowaambia, kisiwa kimeingia kwenye janga kwa sababu Mathias na wenzake wawili wameuiba Msalaba Mtakatifu! Kwa vyovyote watadhani tunajikosha kwa kuwasingizia watu waliopotea kuwafanya kafara wa janga hili. Hapana Padri! Tutafute njia nyingine. Waumini walishuhudia kanisani Msalaba Mtakatifu ulioaminika ni ulinzi wao ukisombwa na kimbunga, halafu leo tuwaambie kuwa, Mathias na wenzake ndiyo waliouiba Msalaba Mtakatifu na kutuachia msalaba bandia? Hawatatuelewa!”
“Tutawaonyesha msalaba bandia waliotuwekea.”
“Bado hatutafanikiwa kuwaondoa fikra za kuwa tunawasingizia akina Mathias. Wanaweza hata kufikiria kuwa ni sisi ndiyo tulioutengeneza msalaba huu wa bandia. Ni vyema kutafuta njia nyingine mbadala ya kukabiliana na janga hili.”
Padri Toni aliyekuwa ameiegemea meza, alijiinua na kuegemea kiti. Akamwangalia Mzee Robert. “Kwa hiyo unanitaka niwaambie uongo waumini wangu?” aliuliza kwa sauti ya upole.
“Si kila ukweli hauna madhara!” mzee Robert alisema. “Kuna wakati ukweli una madhara. Njia pekee ya kufanya ni kutosema lolote kwa waumini, lakini wakati huohuo tunatafuta njia ya kuwarudisha kwenye imani ya kanisa!”
“Ipi?”
“Bado sijaijua, lakini itapatikana!”
Padri Toni akaonekana kuchoka na kauli hiyo, akajishika kwenye paji la uso na kisha uso wake kuuinamisha chini. Akasikitika. Akauinua uso wake. “Lakini Robert,” alisema. “Una hakika Mathias na wenzake ndiyo walioiba Msalaba Mtakatifu?”
“Kusema nina uhakika nitakosea,” alisema mzee Robert. “Lakini endapo njozi nilizooteshwa nitakuwa nimeoteshwa kwa miujiza ya Mwenyezi Mungu, basi hatuna budi tulikubali hilo kuwa, Mathias anahusika na wizi huu!”
“Sasa unataka nidanganye wakati ukweli ndiyo huo? Au bado unataka kumlinda mjukuu wako?”
Mzee Robert akakivuta kiti kilichokuwa mbele ya meza na kukikalia. “Nina wazo,” alisema. “Lakini ni langu binafsi. Tuitishe Kamati ya Kanisa, hawa ndiyo tuwaambie ukweli na siyo waumini. Tuwafahamishe hali halisi na tuwaombe habari hizi zibakie kuwa siri. Dhumuni la kuwaambia hivyo, tuweze kuunda kamati maalum ambayo itahusika kumtafuta Mathias na wenzake. Endapo tutafanikiwa kumkamata mmoja wao, utakuwa mwanzo wa kupatikana kwa Msalaba Mtakatifu hata kama watakuwa wameuuza, pengine inaweza kutusaidia kuufuatilia na tunaweza kubahatika tukaupata kabla haujayeyushwa!”
“Wazo langu kwa waumini bado liko palepale, Robert!” Padri Toni alisema kwa sauti ya ubishi. “Kwa nini tusiwaeleze ukweli ili nao wasaidie kuingia kwenye msako wa kumtafuta Mathias na wenzake?”
Sura ya ubishi ikajiunda usoni kwa mzee Robert. “Kuwaeleza waumini haina maana itazuia vifo au gharika,” alisema kwa sauti ya kulazimisha aeleweke. Kinachotakiwa ni uwezekano wa kupatikana na kurudishwa kwa Msalaba Mtakatifu, kupatikana kwake ndiyo kutazuia vifo na gharika kisiwani hapa. Lakini pia uelewe, endapo tutawaambia ukweli waumini, uwezekano wa habari hizo kusambaa kwa haraka ni mkubwa mno na hatari ya kusambaa kwa habari hizo kunawezesha zikawafikia Mathias na hao wenzake wawili. Je, huoni kuwa zinaweza zikawashawishi kukimbilia mbali zaidi? Na kukimbilia mbali zaidi ndiyo uwezekano wa kuupata Msalaba Mtakatifu unavyopotea zaidi. Lipi ni bora kwako? Habari ziwe nyeti ili kutuwezesha kuwapata kirahisi na kuupata Msalaba Mtakatifu au ziwe wazi na upatikanaji wao uwe wa tabu kama itakavyokuwa kwa Msalaba Mtakatifu?”
Padri Toni akainuka kutoka kwenye kiti, akatoka mezani na kuanza kuizunguka ofisi huku mikono yake akiwa ameiweka mgongoni, mmoja akiwa ameunyoosha na mwingine ukiwa umekamata ule ulionyooka. Kimya kati yao kikajitokeza, mzee Robert akawa na kazi ya kumwangalia Padri Toni kila kona aliyokuwa akienda.
“Nakubaliana na mawazo yako!” Padri Toni alisema ghafla.
Saa chache baadaye, Kamati ya Kanisa ikakutanishwa, kikao kikafanyika, makubaliano yakafikiwa habari hizo ziendelee kuwa siri. Wapelelezi wakachaguliwa kwa ajili ya kufanya msako maalum wa kumtafuta Mathias na wavuvi wawili!
********
HOSPITALI Kuu ya kisiwani Jedani ni moja ya hospitali kongwe zilizojengwa na wakoloni wa Kijerumani ambayo mjengo wake kwa kiasi fulani ulifanana na makazi ya mtawala wa kisiwa hicho. Jengo la hospitali hiyo lilikuwa na rangi nyeupe na sehemu yake ya mbele ya mapokezi ambayo ndiyo iliyofanana kwa kiasi kikubwa na makazi ya mtawala, iliezekwa vigae. Wodi zake zilijengwa kama mabweni ya shule na kuwa mfano wa misitari mitatu iliyonyooka, zilikuwa tatu na zote ziliezekwa kwa makuti. Wodi namba moja ilijengwa karibu na makaburi ya wakazi wa eneo hilo, na madirisha yake yote yalikuwa mkabala na makaburi hayo. Wodi hiyo ndiyo aliyolazwa Mathias.
Akiwa amerejewa na fahamu na kujikuta amelala kwenye hospitali asiyoijua, lakini pia, akagundua haipo kisiwani Zebati, Mathias alihojiwa na Mganga Mkuu wa Hospitali hiyo pamoja na mpelelezi wa polisi kisiwani hapo.
“Jina lako?” mpelelezi alimuuliza Mathias baada ya kuruhusiwa na Mganga Mkuu kufanya mahojiano naye.
“Mathias,” Mathias alijibu huku sura zote mbili zikiwa ngeni kwake, ya daktari na yule anayemhoji. “Mathias Mizengwe,” alimalizia.
“Makazi yako ni wapi?”
“Zebati.”
“Uliopolewa ukiwa unaelea baharini huku umezirai, ilikuwaje?”
Mathias akionekana dhaifu, hatia ilimjenga usoni pake na majuto ya kuingia kwenye majaribu ya shetani ya jaribio lake la kuiba Msalaba Mtakatifu ukiisulubu akili yake. Akawa tayari kuueleza mkasa wote wa baharini ulivyokuwa, lakini hakuwa tayari kueleza lolote lililohusu Msalaba Mtakatifu. “Tulikuwa tukisafiri na wenzangu kwenye ngalawa,” alisema. “Dhoruba ikatupiga na kuivunja ngalawa yetu, kila mmoja akitupwa upande wake. Nikajitahidi kuogelea hadi nikaishiwa nguvu, baada ya hapo sikujua kilichoendelea!”
“Kwa hiyo ulikuwa na wenzako?”
“Ndiyo.”CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Mlikuwa mkisafiri kuelekea wapi?”
“Shelisheli,” Mathias alijibu kwa sauti dhaifu, akajiinua na kujigeuza ubavu mmoja. “Wenzangu nao wamepatikana?” aliuliza.
“Hapana, umepatikana peke yako. Una ndugu yeyote au jamaa hapa Jedani?”
Mathias akapigwa na mshangao, akaangalia pande zote kama vile kungemhakikishia kuwa ni kweli yuko ugenini. “Ina maana nipo Jedani?” aliuliza.
“Ndiyo. Unaye ndugu au jamaa yako yeyote hapa Jedani?” mpelelezi alirudia tena swali lake.
“Hapana.”
Kachero yule akamwangalia daktari. “Una lolote la kumuuliza ambalo utapenda nisikie?” aliuliza.
Daktari alimwangalia Mathias, kisha alisema, “Hapana.”
Kachero akamwangalia Mathias na kusema “Usiwe na wasiwasi, wakati tukiendelea kukupa huduma nataka ujisikie uko nyumbani.”
“Nashukuru,” Mathias alisema.
Wakaondoka.
Walipokuwa njiani wakirudi ofisini, kachero akamwambia daktari, “Kitakachofuata wakati Mathias akiendelea kuwepo hapa, ni kufanya utaratibu wa kuwatangazia wenyeji wa Jedani kuja kumtambua huyu bwana. Pengine inawezekana akapatikana mtu anayemjua vizuri na kutupa taarifa zake. Endapo hakutatokea mtu wa kumtambua, basi utaratibu utakaofuata ni kufanya mpango wa kumrudisha Zebati.”
*********
TAARIFA za kuopolewa mtu baharini zilizagaa kwenye kisiwa chote cha Jedani. Wito ukatolewa kwa wakazi wote kisiwani hapo waende Hospitali Kuu ya Jedani kumtambua mtu huyo. Endapo atapatikana yeyote mwenye kumfahamu basi atoe taarifa kwa Mganga Mkuu. Pamoja na kutokwenda kwa wakazi wote, lakini wale waliokwenda kumwona, hakuna hata mmoja aliyeweza kumjua.
Kutokana na taarifa hizo za kupatikana kwa mtu aliyeopolewa baharini kuzagaa kila kona ya kisiwa hicho, wavuvi wakasaidia kuzisambaza zaidi taarifa hizo kwa wavuvi wenzao wenye kusafiri visiwa vya jirani. Kuzagaa kwa taarifa hizo, hatimaye ziliwafikia wanakamati walioteuliwa na Kanisa Katoliki la Zebati waliopewa kazi ya kumtafuta Mathias na wenzake wawili. Mara baada ya kuzipata, wakafuatilia zaidi na baadaye kupata habari kamili. Mipango na maandalizi ya kwenda kisiwani Jedani ikafanywa. Lakini safari hiyo ikafanywa kuwa wa siri
Wanakamati hao ambao wako watano wenye elimu nzuri ya kiroho waliwasili kisiwani Jedani na kwenda moja kwa moja hadi kwenye Hospitali Kuu ya Jedani.
Baada ya kufika na kujitambulisha kwa walinzi wa hospitali hiyo kuwa ni ugeni kutoka Kanisa Katoliki kisiwani Zebati, walinzi waliwachukua na kuwapeleka hadi ofisini kwa Mganga Mkuu na kukaribishwa na mhusika mwenyewe.
“Karibuni,” Mganga Mkuu alisema huku akijaribu kuwaangalia kwa shauku watu hao.
“Ni wageni wako,” mlinzi alimwambia Mganga Mkuu.
Baada ya mlinzi kuondoka, kikundi hicho cha watu watano kikajitambulisha kwa Mganga Mkuu kwa mmoja wao kusema, “Sisi ni watumishi wa Mungu kutoka Kanisa Katoliki kisiwani Zebati. Kilichotuleta hapa ni habari tulizosikia za kuopolewa kwa mtu baharini ambaye amelazwa kwenye hospitali yako. Sijui kama habari hizo ni kweli?”
Mganga Mkuu hakujibu kwa haraka. “Kwa hiyo mmesafiri kutoka Zebati kwa ajili ya mtu huyu?” aliuliza.
“Ndiyo.”
“Mmepotelewa na mtu yeyote Zebati hadi kuwafanya mfunge safari ya kuja huku?”
“Ndiyo.”
“Wangapi?”
“Walikuwa watatu, lakini tunasikia mmempata mmoja?”
“Wa jinsia gani?”
“Mwanamume.”
“Anaitwaje?”
“Mathias Mizengwe.”
“Ni kweli ninaye mtu huyo,” Mganga Mkuu alisema na mwili wake kuonyesha amani. “Karibuni.”
Hali ya ushirikiano ikaanza kujengeka.
“Kwa hiyo lengo lenu ni kutaka kumwona na kumtambua?” Mganga Mkuu aliuliza.
“Ndiyo. Kumtambua na kumchukua kama atakuwa ni mmoja kati ya watatu waliopotea.”
“Nadhani hilo halina tatizo, lakini kwa kuwa suala hili lilipitia katika taratibu za kipolisi, nitakachokifanya ni kuwaruhusu kwenda kumtambua kama ni mmoja wa watu wenu waliowapotea. Lakini suala la kumchukua na kuondoka naye, itabidi mfuate taratibu za polisi.”
“Sawa, tupo tayari kwa yote hayo.”
“Vyema. Twendeni mkamwone.”
Wakiwa njiani kuelekea wodi aliyolazwa Mathias, mmoja wa kundi hilo kutoka Zebati alisema, “Endapo tutamkuta akiwa amelala, tutakuomba utuamshie. Tuna maswali mawili, matatu ya kumuuliza kabla hatujaanza taratibu za kipolisi za kuondoka naye.”
“Hilo halitawezekana kutokana…” Mganga Mkuu alianza kujibu.
“Usiwe na wasiwasi na sisi daktari,” mmoja alimkatisha Mganga Mkuu. “Tupo hapa kwa nia njema kabisa.”
“Nafahamu. Lakini hali halisi ndiyo inayonifanya nishindwe kulifanya hilo mnalotaka.”
“Kama ipi?”
“Mathias amefariki saa mbili zilizopita!”
*****
SAA chache kabla ya kifo chake, Mathias alikuwa njozini akiota. Aliota akimwona Padri Toni akiendesha sala ya mazishi akiwa amezungukwa na waombolezaji, wote wakiwa ni wakazi wa Zebati. Padri Toni alikuwa akiuachia mchanga kutoka kwenye kiganja chake na kuangukia ndani ya kaburi huku akisema, “Umekuja kwa udongo, utarudi kwa udongo…”
Tukio hilo likiwa linaendelea, ghafla mmoja wa waombolezaji ambaye sura yake ilifahamika na Mathias, akasema, “Padri, mbona Mathias unayemwombea hayumo humo kaburini?”
Umati wa waombolezaji uliokuwepo pale ukapigwa na butwaa na minong’ono ya fadhaa ikazuka. Lakini mtu mmoja kutoka kwenye umati ule akajitokeza, akapaza sauti yake huku akiuelekeza mkono wake upande ilipo hospitali, “Jamani ee, tunamtafuta Mathias yupi zaidi ya yule kule aliyelala hospitali?”
Waombolezaji kwa pamoja wakageuka kuiangalia hospitali hiyo, kisha wote kwa mkupuo wakapandwa na jazba na kuanza kuelekea hospitalini. Mathias aliyekuwa amelala kwenye wodi namba moja, ileile aliyolazwa hospitalini Jedani, akiwa analiona tukio hilo kupitia kwenye dirisha lililopo kando ya kitanda chake ambalo lilikuwa mkabala na makaburi, akaanza kuingiwa na woga baada ya kuliona kundi hilo la waombolezaji likimjia kwa hasira huku wakipiga kelele zinazofanya mwangi, “Ndiyo aadhibiwe! Aadhibiwe! Aadhibiwe!”
Umati ule ukafika kwenye dirisha alipokuwa amelala, wakamvamia.
“Wewe ndiye uliyemuua baba Sai! Na wewe uende kule alipolala baba Sai na wenzake!” huku wengine wakidai, “Aende alikompeleka Maria na akamwone Paulo na Donna…ndiyo, Forlan na Simoni watakuwa wakimsubiri…ndiyo auawe!”
“Nisameheni jamani, jamani nisameheni!” Mathias alipiga kelele na kujaribu kujinasua kutoka kwenye mikono ya waombolezaji hao. Watu hao wakamng’ang’ania kila alivyotaka kuchopoka. Hatimaye akajivuta kwa nguvu na kujinasua, nguvu aliyoitumia ikasababisha shati lake lichanike upande mmoja…
Akazinduka kutoka usingizini. Mapigo ya moyo wake yakawa yanapiga kwa kasi huku jasho likimtoka kwa wingi. Akawa anatweta na kutoa macho huku akishangaa kujiona amezungukwa kitandani na wauguzi waliokuwa wamemdhibiti kwa kumkamata mikono na maeneo mengine ya maungo yake, wakati huohuo Mganga Mkuu alikuwa amesimama kando ya kitanda chake akimwangalia.
“Ulikuwa ukiota njozi mbaya,” Mganga Mkuu alimwambia kwa sauti ya upole. “Ulikuwa ukipiga kelele, uliota nini?”CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Akili ya Mathias ilikuwa bado imetekwa na woga wa ndoto aliyoiota, alikuwa akiendelea kutweta na macho yake akiwa ameyatoa kama aliyefikwa na matatizo ya akili. Aliwaangalia watu waliomzunguka kama vile angechomoka na kukimbia muda wowote. Kwa sekunde kadhaa akaonekana bado yupo kwenye butwaa, akameza sehemu kubwa ya mate, kisha alisema, “Watu walikuwa wakinifuata kutaka kuniua!”
Moja kwa moja kauli hiyo ikawaingizia hisia watu waliomzunguka, wamwone amechanganyikiwa na akili. Mganga Mkuu akataka kuzungumza jambo kwa Mathias, akasita. Akawaangalia wale wauguzi na kusema, “Mnaweza mkamwachia!” Kisha akamwangalia muuguzi wa kike kati ya waliokuwepo na kusema, “Utamchoma sindano ya usingizi, anahitaji kupumzika.” Baada ya kusema hivyo aliondoka.
Muuguzi wa kike ndiye aliyekwenda kuiandaa sindano hiyo.
Akiwa amebaki peke yake kitandani, Mathias akapata nafasi ya kuifikiria ndoto aliyoiota. Ikawa kila alivyokuwa akiikumbuka, ndivyo woga nao ukawa unaongezeka. Hakujua kwa nini alihusishwa kwa kutajiwa majina ya watu anaowajua. Akayakumbuka majina hayo kama vile baba Sai, Maria, Forlan.., kisha akajiuliza, kwa nini walitaka kumuua? Akajaribu kuitafuta tafsiri ya kuota hivyo, hakuipata maana yake! Walikuwa wakitaka kuniua ili niende walikokuwa watu walionitajia! Wapi? Makaburini? Ndoto hiyo ikawa imemuweka kwenye hofu kubwa kila alipojaribu kuitafsiri na kuhisi mwelekeo wake unahusiana na aina ya kifo! Akiwa kwenye taharuki ya ndoto hiyo aliyoiota, ghafla macho yake yakakumbana na kitu ambacho hakukitarajia kukishuhudia. Kukishuhudia kwake kukamfanya ataharuki kwa kutoa sauti ya woga.
Alikuwa ameuona upande wa shati lake uliochanika! Huku akionekana kutoamini kilichotokea, kihoro cha woga kikazidi kumwandama na kumchanganya akili. Alikumbuka ni muda mfupi uliopita alitoka kuota ndoto inayohusiana na kuchanwa kwa shati lake akiwa kwenye purukushani ya kujiokoa na watu waliomvamia. Iweje liwe limechanika kweli? alijiuliza. Ina maana sikuwa ndotoni, bali yalikuwa matukio yaliyokuwa yakifanyika kweli? Akajaribu kuivuta kumbukumbu wakati akiwa kitandani hapo kabla ya kupitiwa na usingizi, akakumbuka shati lake lilikuwa zima!
Uhakika huo ukamwingizia hofu mpya kuwa, watu aliowaota walidhamiria kumuua kweli! Mungu wangu! alihamanika. Akageuka upande uliko makaburi na kuyaangalia. Papohapo akapata tafsiri ya ndoto hiyo! Akachukulia kuwa, ingawa alioteshwa kuwaona watu anaowafahamu ambao wote ni wakazi wa Zebati, lakini uoteshwaji huo haukuwalenga wao, bali ulimaanisha ni wafu waliozikwa kwenye makaburi hayo yaliyopo jirani na hospitali hiyo aliyolazwa! Kuyaamini mawazo hayo, kukamfanya awashukuru wauguzi kimoyomoyo kuwa ndiyo waliomwezesha kuzinduka usingizini, akiamini wakati alipokuwa akihangaika kitandani akipambana na wafu waliomjia, wauguzi hao wakasaidia kumwamsha, akazinduka na kukiepuka kifo!
Wazo hilo likamfanya aingiwe na hadhari kuwa, eneo hilo ni la hatari! Na endapo usingizi utampitia kwa mara nyingine, kuna uwezekano wafu hao wakamrudia tena na pengine akashindwa kuzinduka kutoka usingizi kama alivyomudu mara ya kwanza na wafu hao wakamuua kweli!
Wazo la kutoroka hospitali likamjia! Eneo hilo la makaburi alilokuwa mkabala nalo likawa sehemu inayohatarisha maisha yake, asingekuwa na utayari wa kulala tena kwenye wodi hiyo inayotazamana na makaburi hayo! Lazima niitoroke hospitali hii! alijiapiza.
Akiwa bado yuko kwenye bumbuwazi huku akiiangalia sehemu ya shati iliyochanika, Mathias alijikuta akiupata mshituko mwingine asioutarajia. Muuguzi aliyeambiwa aje kumchoma sindano ya usingizi akamwona anakuja huku akiwa ameshika sinia ndogo yenye rangi ya fedha iliyobeba sindano!
“Hapana, usinichome!” Mathias alimwambia muuguzi aliyekuwa amejiandaa kuitoa sindano kutoka kwenye sinia. “Tafadhali usinichome!” aliomba kwa unyenyekevu na macho yake kulengwa na machozi.
Muuguzi akaonekana kushangaa. “Kwa nini hutaki nikuchome sindano?” aliuliza.
“Ukinichoma nitakufa!”
“Utakufa?” muuguzi aliuliza kimzaha.
“Ni kweli nitakufa.”
“Ki-vipi?”
“Watu waliotaka kuniua watanifuata tena!”
Muuguzi akamwangalia Mathias kwa umakini na kushawishika kuwa, mgonjwa wake huyo bado yupo kwenye kurukwa na akili. “Kama hutaki haya, mimi naondoka!” alisema kwa upole.
“Ahsante kwa kunielewa, Yesu akubariki!” Mathias alisema na kuvikutanisha pamoja viganja vyake na kuviweka kifuani kama anayefanya maombi.
Muuguzi akaondoka na sinia yenye sindano, akamwendea Mganga Mkuu na kumweleza yaliyotokea.
“Basi niachie mimi,” Mganga Mkuu alimwambia muuguzi.
Dakika chache baadaye Mganga Mkuu alimwendea Mathias kitandani kwake.
“Unajisikiaje?” Mganga Mkuu alimuuliza Mathias.
“Sasa hivi najisikia vizuri na nahisi sina matatizo yoyote, unaweza ukaniruhusu nitembee-tembee kunyoosha miguu?” Mathias alisema kwa lengo la kutaka kutoroka.
“Ni vyema kwanza ukapata kitu cha moto tumboni kama kahawa, iweze kukurudishia nguvu ya kuweza kutembea-tembea. Ni muda mrefu bado hujala kitu. Baada ya kunywa unaweza ukatembea-tembea hapa na pale.”
“Wapi nitaipata hiyo kahawa?”
“Nitamwagiza muuguzi akuletee sasa hivi,” Mganga Mkuu alisema na kuondoka.
Dakika zisizozidi tano, muuguzi mwingine wa kike alikuja kitandani kwa Mathias akiwa na kikombe cha kahawa mkononi, akafanya tabasamu la ukarimu na kusema, “Karibu!” huku akimpa Mathias kikombe chenye kahawa. “Daktari ameniagiza nikuletee kahawa.”
Mathias akapokea. “Ahsante,” alishukuru.
Muuguzi akaondoka.
Wakati muuguzi akiondoka, Mathias alikunywa funda dogo la kahawa na kuuhisi mdomo wake ukichangamka. Akapiga funda jingine, kisha akajiweka vizuri kitandani na kuanza kuinywa huku akili yake ikizama kwenye kutoroka baada ya kuimaliza kahawa hiyo. Bahati mbaya alichokuwa hakukijua ni mara baada ya kukataa kupigwa sindano, mbinu nyingine ya kuitumia kahawa hiyo ndipo ilipobuniwa na Mganga Mkuu.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment