Simulizi :
Sehemu Ya Tatu (3)
“Wakazi wamechanganyikiwa na wapo tayari kufanya lolote ambalo wanaliona litawasaidia kuwapa amani. Suluhisho waliloliona ni hilo la kufanya matambiko yatakayoandamana na makafara. Hawataki kusikia lolote jingine zaidi ya hilo!”CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Siwalaumu, najua wamepatwa na kiwewe dhidi ya vifo vinavyoendelea. Watu wamepagawa, lakini wanahitaji watulizwe kwa kupewa neno la Bwana ili imani yao irudi kwenye kanisa, badala ya kuomba mizimu na kufanya makafara. Kunahitajika kufanywe maombi maalumu ya sala, kumwomba Bikira Maria kupitia Msalaba Mtakatifu atunusuru na balaa hili!” Padri Toni alinyamaza na kuangalia chini, akaonekana kama anayesali ingawa alikuwa hafanyi hivyo.
Kimya cha sekunde chache kikapita kati yao.
“Kilichonileta hapa baba ni kukwambia mawazo yangu,” Sajini Seba alikivunja kimya hicho. Akaendelea, “Inanipa wakati mgumu kuamini, wakazi watakubaliana na wazo la kufanya sala ya maombi. Nasema hivyo kutokana na ukweli kuwa, hata mimi ambaye nachunguza vifo hivi nimefikia mahali nimekiri, kuna utata kwenye vifo vyote vitatu! Ni vifo vinavyoonyesha kuna muuaji anayeua, lakini haonekani na wala hajulikani! Kuna mauzauza yanayoandamana na dalili za kishirikina ambayo yameshuhudiwa na wakazi wakati vifo hivyo vikitokea. Inaogopesha, imefikia mahali hakuna anayejua ni nani atakayefuata kufa!” Seba akasita na kukiinamisha kichwa chake chini. Alipokiinua, akamwangalia Padri Toni usoni, akasema, “Kuna ulazima wa kufanya makafara na matambiko kuiokoa hali hii!”
Padri Toni alihisi kama aliyechapwa kofi usoni. “Unapotea mwanangu kuamini hivyo,” alisema kwa utulivu. “Yesu ametukataza kuamini ushirikina. Ukiamini ushirikina ni sawa na kutomwamini Mungu, unakuwa kama uliyefanya uchaguzi kati ya Mungu na ushirikina, nawe ukachagua ushirikina ndiyo ukuongoze. Usipotee huko mwanangu, muweke Mungu mbele, yeye ndiye mwokozi wa kila jambo. Ukimwamini yeye, kila jambo litapata nuru yake na kila nuru yake ndiyo amani yako.”
“Baba,” Seba alisema kwa unyenyekevu. “Umesahau kwamba, baba Sai na Maria walikuwa ni kondoo wako? Walikuwa wamelibeba jina la Yesu wakati wote, walikuwa watiifu katika sala, popote walipokwenda walikuwa naye. Je, hiyo haikutosha kwa Yesu kuwalinda na kuwaokoa na balaa lililowakuta?”
Padri Toni alifumba macho na kuwa kimya kwa sekunde chache. Kisha akatangulia kusema kabla ya kufumbua macho, “Mlaani shetani, Seba! Yesu hashindwi na kitu.” Kisha akafumbua macho, akamwangalia Seba. “Yaliyowakuta baba Sai na Maria ni mapenzi yake Mungu aliyetwaa chake. Yeye aliwapenda sana.”
“Nadhani hata familia zao ziliwapenda sana na ndiyo maana walilia na kugaragara chini kwa uchungu huku wakiomboleza, lakini kibaya zaidi hawaamini kama wapendwa wao walikufa kwa mapenzi ya Mungu kwa sababu Mungu haui kwa mauzauza!”
“Shetani hana nguvu mbele ya Yesu, Seba. Usihadaike na mauzauza uliyoyasikia.”
“Yesu alikuwa wapi wakati mauzauza yalipomtokea baba Sai hadi kuuawa? Lakini kama vile haikutosha, mauzauza hayo yakajirudia tena na kuja kumuua Maria, Yesu alikuwa wapi asiyazuie na hayo ya pili? Kibaya zaidi na Paulo naye akauawa kwa aina hiyohiyo ya mauzauza! Halafu baba unawataka wakazi wakuelewe kuwa hayo hayakuwa mauzauza, bali yalikuwa mapenzi ya Mungu yaliyotimizwa?” Seba akatoa kicheko kidogo cha kukata tamaa. “Hakuna atakayekuelewa!” alisema. “Kunahitajika ushawishi wa ziada ufanywe na kanisa ili waamini hayo unayoniambia, lakini si kwa kutegemea misalaba tuivaayo shingoni na rozari tushikazo mikononi kuwa zitatuokoa! Imani hiyo imekwishaanza kumeguka kwenye mioyo yetu. Ili kuwarudisha watu kwa Yesu, kunatakiwa juhudi ya makusudi itakayowathibitishia kuwa hakuna kifo kingine cha aina hii kitakachotokea. Vinginevyo, watu wote pamoja na mimi mwenyewe, tutatafuta njia mbadala isiyokuwa ya Yesu, ili mradi njia hiyo itahakikisha inayalinda maisha yetu hata kama ni kwa kuamini ushirikina!”
*********
MZEE Robert Mizengwe alitoka bafuni na kurudi chumbani ambako alivaa nguo kisha, akaenda kujumuika na familia yake mezani kwa ajili ya kupata kifungua kinywa. Alikuwa ameamka na mtafaruku wa mawazo asubuhi hiyo na alijikuta akiinywa chai hiyo bila ya vitafunwa. Hakujisikia kuwa na hamu ya kutafuna chochote kwa sababu hata njaa ilipotea!
Hali hiyo ikamshangaza mkewe. “Mbona huchukui vitafunwa?” alimuuliza.
“Sijisikii kula,” mzee Robert alijibu kivivu. Akakiinua kikombe cha chai na kukiweka mdomoni, kisha bila ya kuinywa chai akakirudisha mezani.
Mkewe akamwangalia kwa makini usoni kisha, asiseme lolote.
Mzee Robert akaviegesha viwiko vya mikono juu ya meza na kukiegesha kidevu kwenye vidole alivyovishikisha pamoja na kuwa kama ngumi. Macho yake yakaangalia katikati ya meza. “Nimeota ndoto nyingine!” alisema ghafla na sauti yake ilikuwa ndogo kama aliyezungumza na nafsi yake, akanyamaza. Akaendelea kuiangalia meza.
Wote waliokuwepo mezani wakaganda kumsikiliza. Badala ya kuendelea, mzee Robert akaendelea kuangalia juu ya meza.
“Inayomhusu tena Mathias?” mkewe alimuuliza. Swali hilo likawafanya wote waliokuwepo pale mezani washikwe na ubaridi, wakaganda kama sanamu huku mshawasha wa kutaka kujua mzee Robert atajibu nini ukiwapata.
Mzee Robert akaubaini umakini uliokuwepo pale mezani wa kusubiriwa jibu lake. Ndoto aliyoiota mara ya kwanza ni mkewe tu ndiye aliyekuwa amemhadithia. Akashangaa na kujiuliza, iweje mkewe aulize swali kama hilo mbele ya wengine? Lakini akatambua kuwa ni yeye ndiye aliyelianzisha suala hilo hapo mezani. Ghafla akabadili mada. “Natarajia kwenda kumwona Sajini Seba nijue amefikia wapi kuhusu suala la Mathias!” alisema.
Mkewe akaielewa akili ya mumewe iliposimamia. Akaamua kuendeleza hoja hiyo ya mumewe bila ya kushangaa. “Pengine anaweza akawa amepata taarifa zake,” alisema.
“Pengine,” mzee Robert alijibu. “Vifo vya baba Sai na huyu msichana Maria vimemfanya asiwe na muda wa kufuatilia suala lake kwa ukamilifu.”
“Watu nao wameanza kuamini vifo vyao vina mkono wa nguvu za giza.”
“Hizo ni imani za kishirikina!” mzee Robert alisema kwa ukali na sauti yake ilikuwa ya kukebehi.
“Sina maana ya kutaka kuamini,” mkewe alijitetea. “Lakini mazingira ya vifo vyenyewe ndiyo yanamtatanisha kila mtu!”
“Kutoka damu puani na masikioni haina maana ni vifo vya kutatanisha!” mzee Robert aliendelea kuzungumza kwa sauti ileile yenye kebehi. “Watu wengi wamekwishakufa vifo vya aina hiyo, hata mgandamizo wa damu ukizidi unaweza ukapatwa na hali kama hiyo!”
“Hata hivyo, kabla ya vifo vyao kulitokea mambo ya ajabu kama kimbunga kilichopiga. Hakujawahi kutokea kimbunga cha aina hii hapa Zebati. Kimbunga kilichoogopesha hata mifugo! Ndiyo maana watu wanavihusisha vifo vya baba Sai na Maria ni nguvu za giza.”
“Jambo lolote ambalo halijatokea kwa muda mrefu, pindi likitokea, basi kila mtu atasema lake!” mzee Robert alisema kiubishi.
“Lini ilishatokea watu wakafa kimauzauza kama hivi?” mkewe naye akajikita kwenye ubishi. “Ni lini Zebati kulitokea kimbunga cha aina hii? Halafu inakuwaje kwenye eneo la kifo kuonekane ukungu usiojulikana ulikotokea?”CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/Swali hilo likamfanya mzee Robert ashindwe kulijibu haraka kama alivyokuwa akiyajibu maswali ya awali. Hata hivyo hakukubali kushindwa. “Pamoja na hilo, lakini suala la ushirikina halipo!” alisema kiubishi na kila mmoja aliyekuwepo pale mezani alitambua kuwa, alikuwa akitaka kuonyesha msimamo wa kanisa kupinga kwa nguvu zote masuala ya kiushirikina kupewa nafasi.
“Lakini…” mkewe alianza kusema, akanyamaza ghafla baada ya kuusikia mlango ukigongwa na kufuatiwa na sauti iliyosema, “Hodi.”
“Karibu,” mzee Robert aliitikia na kuangalia mlangoni.
Kijana aliyekuwepo mezani alitoka kwenye meza ya chakula na kwenda kuufungua mlango wa mbele. Akasikika akisema, “Karibu!”
“Mzee Robert yupo?” sauti ya kiume kutoka nje ya mlango ilisikika ikiuliza.
“Yupo,” kijana alijibu. Akageuka nyuma kumwangalia mzee Robert aliyekuwa bado yuko mezani. Kisha, akatoa nafasi kwa mgeni huyo aingie ndani.
Mtu wa makamo aliyekadirika kuwa na miaka isiyopungua arobaini na mitano akaingia. Mara alipoingia watu wote waliokuwepo mezani walisimama na kusalimiana naye.
“Tukuandalie chai au kahawa?” mzee Robert alimuuliza mgeni huyo ambaye alikuwa akifahamika na familia hiyo.
“Hapana, ahsante,” alijibu mgeni huyo aliyeitwa Yogo. “Kwa kweli sina muda wa kukaa, nimekuja kwa ajili kukuona mara moja.”
“Unanihitaji faragha?” mzee Robert aliuliza.
“Nimeleta habari za msiba!” Yogo alisema na kujaribu kuziangalia nyuso za wote hapo mezani.
Kimya cha ghafla kikajiunda humo ndani, wote waliokuwepo pale akili zikawagonga kwa hofu huenda ni habari za kifo cha Mathias.
“Nani amefariki?” mzee Robert aliuliza kwa sauti iliyopwaya na kujaribu kujilazimisha kuwa mtulivu.
“Mtu mwingine ameuawa usiku wa kuamkia leo!” alisema Yogo. “Ameuawa palepale msibani pa Maria!”
Taarifa hiyo ikaleta ukimya wa ghafla pale mezani, na wengine wao wakapiga alama ya msalaba kimyakimya. Wakaduwaa kwa hofu, mke wa mzee Robert akauziba mdomo wake kwa kiganja chake kuonyesha mshituko alioupata.
“Ni nani aliyeuawa?” mzee Robert aliuliza.
“Paulo!” Yogo alijibu.
“Paulo yupi?”
“Yule kijana mchuuzi wa samaki, mlevi-mlevi hivi!”
“Maskini Paulo!” mke wa mzee Robert alisema ghafla kwa sauti ya juu. “Huyu kijana nilimwona juzi akiuza samaki hapo nyumba ya jirani.., amekufa?”
“Ilikuwaje?” mzee Robert aliuliza huku akiomba isiwe aina ya vifo vilivyowatokea baba Sai na Maria.
“Amekufa kama walivyokufa baba Sai na Maria!” Yogo alisema kwa sauti iliyoonyesha kuhofia hali inavyoendelea hapo kisiwani. “Naye amekutwa akitoka damu za puani, machoni na mdomoni!”
Macho ya mzee Robert yakakutana na ya mkewe aliyekuwa akimwangalia kwa mwonekano wa kumsuta kama vile akimwambia, ‘je, unayaamini maneno yangu?’
Wote kasoro mzee Robert, wakashusha pumzi za hofu huku wakionekana kuchanganyikiwa. Wakamwangalia Yogo usoni kama vile angekuwa na la ziada la kueleza!
Mzee Robert akaanza kujiuliza tena kuhusu ndoto aliyoiota!
****
WAVUVI wanne, wakazi wa kisiwa kinachoitwa Jebaiduni kilichopo Kaskazini Magharibi mwa kisiwa cha Zebati, wakirudi kutoka kuvua wakiwa kwenye mtumbwi, wakaona kitu kinachoelea baharini. Wakapata udadisi wa kutaka kukijua. Awali walifikiri ni kipande cha gogo la mti, lakini walipokaribia wakagundua kuwa ni binadamu. Hekaheka za kumuopoa kumtia kwenye mtumbwi zikaanza. Mara baada ya kumlaza kwenye mtumbwi, wakaanza kumkagua. Wakagundua alikuwa bado yuko hai, lakini wakaihofia hali yake iliyokosa dhamana ya uhai kutokana na kuwa mbaya. Ili kuyaokoa maisha yake yasije yakaishia mikononi mwao, jitihada za kupiga makasia zikafanywa na wavuvi wale angalau waweze kufika Jebaiduni kabla mtu huyo hajakata roho!
Waliwasili Jebaiduni wakati wa alasiri katika eneo la dagoni lenye kufanyiwa mnada wa samaki ambako watu wengi hufika kwa ajili ya ununuzi wa kitoweo hicho. Kama ilivyo kawaida ya maeneo hayo, chombo kinachotoka baharini kinapowasili, baadhi ya watu hukifuata majini kwa ajili ya kuangalia kilichopatikana kwa siku hiyo. Na ndivyo ilivyokuwa kwa chombo cha wavuvi hao, mara kilipowasili na kutupa nanga kwenye maji yaliyokupwa, baadhi ya watu walikifuata. Watu wengine waliokuwa ufukweni kwa matumaini ya kuwaona watu waliokifuata chombo hicho wakirudi na habari njema ya samaki waliopatikana, wakashangaa kuwaona hawarudi kwa muda waliotarajia kuwa wangerudi. Badala yake wakawaona kama kuna kitu wanachokishangaa kikiwa ndani ya mtumbwi. Nao wakavutika na kitendo hicho kwa kuanza kuulizana; kulikoni?
Ndani ya muda mfupi taarifa zikasambaa eneo lote la dagoni, wapiga mnada au madalali, wachuuzi na wanunuzi wengine wa samaki wakaacha shughuli zilizowapeleka huko, wakatanda ufukweni kuwaangalia watu waliokuwa wameubeba mwili wa mtu uliotolewa kwenye mtumbwi huku minong’ono ikizagaa kuvuka eneo hilo kuwa, kuna mtu ameopolewa baharini akiwa amekufa. Maofisa na polisi wa forodha nao wakawa ni miongoni mwa wa watu waliokuwa wakiisubiri maiti hiyo ifike ufukweni.
Mara baada ya mtu huyo kufikishwa ufukweni ndipo ukweli ukajulikana kuwa, alikuwa hajafa! Watu wakatakiwa wasimzonge ili aweze kupata hewa safi. Polisi wa forodha na maofisa wao wakafanya juhudi za haraka ili mtu huyo afikishwe hospitali. Ukapatikana usafiri wa mkokoteni wa punda na mtu huyo akawahishwa kupelekwa Hospitali Kuu ya Kisiwa cha Jebaiduni!
Alikuwa Mathias!
*********
AKIWA bado amepoteza fahamu, Mathias aliwekwa kwenye chumba maalumu cha uangalizi wa karibu na wakati huohuo akaanza kufuatiliwa afya yake.
“Yuko hai, lakini mapigo ya moyo wake ni dhaifu sana,” daktari alisema huku akikiondoa kipima mapigo ya moyo kutoka masikioni na kukitegesha shingoni mwake.
“Ni habari njema,” alisema mmoja wa askari aliyekuwa kwenye msafara wa watu waliompeleka Mathias hospitali. Kisha akamwangalia Mathias aliyekuwa amelala kitandani. “Atakaporejewa na fahamu na kuwa kwenye hali nzuri, nadhani ataweza kujieleza yeye ni nani na ilikuwaje mpaka akaopolewa baharini.”
********
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
KENGELE ya Kanisa ilisikika ikipigwa kisiwani Zebati, haukuwa muda uliozoeleka wa kusikika kengele. Hali hiyo ikawa ishara tosha kwa wakazi kutambua kuwa, ni kengele ya tukio muhimu la dharura inayowataka wakazi wote kuacha shughuli zao na kuitikia mwito wa kengele hiyo kuelekea kanisani. Muda mfupi baada ya kengele hiyo kusikika, misururu ya wakazi, wanawake kwa wanaume wenye umri uliotofautiana walionekana wakipandisha mlimani ambako ndiko liliko Kanisa Kuu la Katoliki. Dakika arobaini baadaye, uwanja wa kanisa ukawa umefurika watu kusikiliza walichoitiwa.
Wakiwa wapo kwenye kusubiri, vikundi vilivyokuwa vimejianzisha hapo, vilianza kubashiri kile walichoitiwa kuwa, ni kuzungumzia hali ya utata iliyojitokeza kisiwani hapo na huku wengine wakinadi kuwa, Mathias ameonekana! Zogo la minong’ono hiyo iliyokuwa imetawala ikaanza kufifia taratibu pale Padri Tino aliyekuwa kwenye vazi la kanzu alipojitokeza na kwenda kusimama kwenye jukwaa maalum lililopo uwanjani hapo.
Mara baada ya kusimama kwenye jukwaa, Padri Toni aliwaangalia waumini kwa utulivu. “Tumsifu Yesu Kristu!” alisema.
Umati uliokuwepo pale ukaitikia kwa sauti iliyovuma, “Milele amina!”
“Naanza kwa kuwashukuru wote mliofika hapa kwa kuacha shughuli zenu muhimu,” Padri Toni aliendelea. “Naamini kuwa, uwezo wake Bwana ndiye aliyewapeni nguvu za kufika hapa. Tumsifu Yesu Kristu…”
Umati ukaitikia tena, “Milele amina!”
“Ndugu zangu, nyote mnajua kuwa, hivi karibuni kisiwa chetu kimeingia kwenye msiba mkubwa wa matukio ya kusikitisha ya vifo vya mfululizo vilivyojaa utata. Tumewazika wapendwa wetu tuliokuwa tukiwapenda, lakini Mungu amewapenda zaidi! Najua, mkanganyiko mkubwa wa akili na mifadhaiko imetupata kwa matukio haya ya kushangaza, lakini pia ningependa kuichukua fursa hii kuwapeni pole mliofiwa na wapendwa wenu, pia shukrani kwa wakazi wote mliojitolea kwa hali na mali kujumuika na wafiwa na kuonyesha ukarimu wa kukaa pamoja nao wakati wote wa machungu.
“Lakini, pamoja na ushiriki wetu kwenye misiba ya wenzetu hawa na ambayo pia ni misiba yetu, kumejitokeza hali ya kutofautiana miongoni mwetu. Moja ya tofauti hizo, ni kwa miongoni mwenu kuvihusisha vifo hivi na imani ya kishirikina! Nakiri haya ni maafa yaliyokikumba kisiwa chetu, lakini haya pia ni majaribu ya shetani anayetaka kututawala. Woga na udhaifu ulio miongoni mwenu mmeanza kuzungumza maneno ya kumuasi Bwana wetu Yesu Kristu kwa kutaka kuacha kuifuata njia yake yenye mwanga na matumaini, badala yake mnataka kuifuata njia anayopita shetani. Huu ni usaliti mkubwa mnaotaka kuutenda kwenye kanisa! Katika neno lake Bwana, Biblia inatuambia, ‘Mwamini Yesu Kristu katika shida, yeye ndiye mwokozi wako wa raha na shida zako. Tujikumbushe Luka 8:47. Akasema, yule mwanamke alipoona kwamba hawezi kusitirika, akaja akitetemeka, akaanguka mbele yake, akamweleza mbele ya watu wote sababu yake ya kumgusa na jinsi alivyoponywa. Mara akaambiwa, binti imani yako imekuponya!” Padri Toni akanyamaza kidogo na kuiangalia kadamnasi iliyokuwepo pale. Kisha akaendelea, “Aliambiwaje yule binti?”
“Imani yako imekuponya!” umati ulijibu kwa sauti moja.
“Ni imani yako kwa Yesu Kristu, ndiyo itakayokuponya katika shida zako, na wala si mizimu na makafara. Kufanya hivyo ni kumwacha Bwana wetu Yesu Kristu na kumfuata shetani! Hivyo ndugu zangu kutokewa na vifo vyenye utata, vimbunga visivyoeleweka, najua ni janga zito na ni mtihani wa imani zetu. Wale wenye mioyo yenye kutaharuki na iliyojaa woga, hawa ni wepesi wa kupoteza imani yao mbele ya Bwana, wao hukimbia ovyo na kupiga mayowe barabarani huku wakimnadi shetani awasaidie. Wanadhani shetani ataleta miujiza. Kumwamini shetani ni kumuudhi Mungu, lakini pia ni kumpoteza Yesu!
“Ninatoa nafasi kwa wale wote ambao nafsi zao zilianza kutekwa na shetani, huu ni wakati wao wa kurudi kwa Yesu Kristu. Imani yako uiweke kwake yeye kwa sababu wokovu upo kwake. Leo wote tuko hapa kwa ajili ya kumwamini yeye. Chini ya jina lake, maafa haya yatatoweka! Tumsifu Yesu Kristu!”
“Milele amina!” umati ukajibu.
“Kengele mliyoisikia, nimewaita kwa ajili ya kuwapeni ujumbe huu, lakini pia nataka kuwaarifu kuwa, ili kutoa nafasi kwa maziko ya kijana wetu Paulo yafanyike jioni ya leo, usiku ifikapo saa tatu, kutakuwa na sala maalum ya maombi itakayofanyika hapa kanisani. Lengo la sala hii ni kufanya maombi maalum, tuondokane na janga hili lililokifikia kisiwa chetu. Tutasali chini ya Msalaba Mtakatifu kumwomba mama yetu Bikira Maria atuondoe kwenye hali hii ya kutatanisha. Uwepo wenu ndiyo utakaofanikisha maombi yetu kumfikia mama yetu, Bikira Maria.” Baada ya kusema hivyo, Padri Toni alitulia kwa sekunde chache huku ameuinamisha chini uso wake. Ukimya wake ukagubika eneo lote la hapo.
“Tusali!” Padri Toni alisema ghafla na kuuvunja ukimya uliokuwepo. “Baba yetu uliye mbinguni…” aliomba.
Ngurumo za sauti za waumini zikawa zinaenda sambamba na maneno ya sala yatamkwayo na Padri na kufanya mwangwi uliotawala uwanjani hapo.
Mara baada ya sala hiyo, waumini wote walitawanyika huku kila mtu akiwa ameuitikia mwito wa sala itakayofanyika usiku. Tumaini jipya likawa limewaingia, kanisa likawa limewaunganisha tena!
Mtu pekee aliyekuwa tofauti na mawazo hayo, alikuwa ni mzee Robert Mizengwe. Yeye hakuamini sala hiyo ingeleta ushwari wa mambo kisiwani hapo!
********
SAA chache kabla ya kengele iliyowakusanya wakazi wa Zebati kupigwa kanisani, mzee Robert alikuwa yupo kwenye shinikizo jipya lililozidi kumpa jinamizi lililoendelea kumchanganya kichwa. Jinamizi hilo alikuwa ameamka nalo asubuhi ya siku hiyo baada ya kuota ndoto nyingine. Ilikuwa ndoto iliyozidi kumtundika kwenye njiapanda! Alimwota Mathias akiwa na taji la miba kichwani huku ameubeba Msalaba Mtakatifu mgongoni mwake mithili ya siku ambayo Yesu Kristu alibebeshwa msalaba kwenda kusulubiwa. Nguo aliyokuwa ameivaa ilikuwa imefanana na ile aliyokuwa ameivaa Yesu ambayo ilionekana kumsitiri zaidi kuliko kumhifadhi. Nyuma yake Mathias, kulikuwa na kundi kubwa la watu, lililokuwa likimfuata huku likimzomea na kumtupia vitu vilivyofanana na mawe, lakini watu waliokuwa wakimzomea hawakuwa Wayahudi wa Nazareth, bali walikuwa ni wakazi wa Zebati na baadhi yao ni majirani anaowafahamu!
Mzee Robert alikumbuka jinsi alivyoshituka kutoka usingizini baada ya ndoto hiyo kumkatikia. Moyo wake ulipiga kwa kasi na jasho lilimtoka kwa wingi. Akajaribu kuirudisha kwenye kumbukumbu ndoto aliyoiota, akaikumbuka vizuri! Akajiuliza, nini maana ya kuota ndoto hiyo? Na ilikuwa ikimpa tafsiri gani? Kwa nini aoteshwe Mathias kwa mfano wa Yesu? Akalikumbuka kundi la watu lililokuwa likimzomea na kumtupia mawe Mathias. Kwa nini kuwepo na kitendo hicho? Na kwa nini wawe watu wa Zebati? Na kwa nini ndoto zote zimhusishe Mathias?
Akiwa njiani pamoja na wakazi wengine akitokea kanisani kuitikia mwito wa kengele, mzee Robert alijitahidi kutembea akiwa peke yake. Hakutaka kuzungumza na muumini yeyote na wala hakuwa mshiriki wa maongezi yaliyokuwa yakiongewa na wakazi hao waliokuwa wakiijadili hotuba ya Padri waliyoipokea kwenye mioyo yao na kuwarudisha kwenye umoja. Kichwa chake kilikuwa kwenye fukuto la kuitafuta tafsiri ya ndoto hiyo nyingine aliyoiota na tukio lililojitokeza kanisani la kuvunjwa kwa dirisha!
Akiwa ndani ya fikra hizo, alijikuta akilifikiria tukio jingine bila ya kutarajia. Tukio lililotokea asubuhi ya siku hiyo alipokuwa akibishana na mkewe kwenye meza ya chakula wakati wakistafutahi. Ubishi ambao ulikatishwa na ujio wa Yogo aliyekuwa ameleta habari za msiba wa Paulo!
Taarifa hiyo ya Yogo ilimbwagisha moyo, ikamwogopesha! Mzee Robert akajaribu kuzihusisha ndoto hizo na vifo hivyo. Ni kweli ndoto hizo zinambashiria janga linalosababishwa na Mathias? Na ndiyo sababu ya kumwota Mathias kwenye ndoto zake? Na ndiyo sababu inayosababisha vifo vyote viwe vinafanana? Na kwa nini kutokee kimbunga kabla ya kifo? Na kama ni janga, kwa nini ndoto nilizoota zisinioteshe ubashiri wa kimbunga na mauaji, badala yake zinioteshe Mathias pekee?
Mzee Robert akaikumbuka hotuba ya Padri Toni aliyekiri kuwa, ni kweli kuna janga na kuwataka waumini wote waende kusali sala maalumu ya maombi kupitia Msalaba Mtakatifu. Janga hili linasababishwa na nini? alijiuliza.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Akiwa anatembea taratibu kuelekea nyumbani kwake huku akiwa amekiinamisha kichwa chake chini na kuonekana kuchoka, mzee Robert aliumiza kichwa kuitafuta nasaba iliyopo kati ya ndoto anazoota na matukio yanayotokea. Kwa mara ya kwanza alianza kuingiwa na hofu baada ya kuilinganisha ndoto ya kwanza iliyomwotesha kumwona Mathias na wenzake wawili wakivunja dirisha la kanisa kwa lengo la kuiba Msalaba Mtakatifu na kauli aliyotoka kuizungumza Padri Toni ya kuvunjwa dirisha la kanisa. Kauli hiyo imeonyesha kuwepo kwa dalili za ukweli na alichokiota, na kibaya zaidi, dirisha lilelile la kanisa lililozungumzwa na Padri ndilo alilokuwa ameliota! Njia nzima alijikuta akisumbuliwa na kauli hiyo ya Padri Toni. Ilikuwa kauli iliyodhihirisha ubashiri wa ndoto aliyoota!
Ingawa tukio la kuvunjwa dirisha limetokea kuwa la kweli na kumdhihirishia uwepo wa nasaba wa ndoto aliyoiota na tukio hilo, lakini bado aliona kuna upungufu; upungufu wa kutoonyesha Msalaba Mtakatifu kuwa umeibwa! Kusudio la ndoto hiyo lilikuwa ni ubashiri aliooteshwa kuwa Msalaba Mtakatifu ungeibwa! Sasa iweje tena kutokee majanga? alijiuliza. Lakini pia akajiuliza, ni unasaba gani uliopo na kutoweka kwa Mathias? Kutoyapata majibu hayo kukawa kunampa pingamizi hata yeye mwenyewe la kumwendea Padri Toni kumwelezea kuhusu ndoto alizoota. Akaamua kwanza autafute ukweli wa ndoto zake hadi ajue maana ya kuoteshwa ndoto za aina hizo kabla hajamwendea Padri Toni.
Akiwa hajakivuka kizingiti cha mlango wa nyumbani kwake kuingia ndani, akajiwa na wazo la ghafla ambalo aliliona lingeweza kumtegulia kitendawili kinachomtega. Akaipanga siku inayofuata, mapema asubuhi, atakapokwenda kanisani, aukague Msalaba Mtakatifu uliopo kwenye altare ili athibitishe kama ndiyo wenyewe!
Hakujua kwa nini alijiwa na wazo la aina hiyo, lakini alilikubali kuwa, lilikuwa wazo la busara.
*****
MAZISHI ya Paulo yalimalizika jua likiwa limeshazama. watu wakagawanyika kurudi majumbani kwao na wengine kwenda maeneo tofauti waliyopanga na baadhi yao walirudi msibani. Kitendo cha kumzika Paulo kilikuwa kimewapa uhakika wakazi wa kisiwa hicho kuwa amani ilikuwa imepotea kisiwani humo! Maonyo yakawa yametolewa kwa watu wanaopenda kutembea usiku, hasa wale wanaopenda kupoteza muda kwenye vilabu vya pombe, kuwa wabaki majumbani kwao kwa usalama wao hadi muda wa kwenda kanisani kwa ajili ya sala ya maombi maalum utakapowadia.
Hali ilikuwa tete kwenye mji wote, ukimya ukatawala kila mahali. Woga na hofu ya kuuawa kimaajabu ikawa inatawala kwa kila mtu. Usiku ulipoingia, hofu ikazidi. Watu wakawa wanaongea kwa sauti za chini na wengine walifikia hadi kuzungumza kwa kunong’ona kutokana na hofu kuwa, kama wangezungumza kwa sauti ya juu, sauti zao zingeifikia miujiza inayoua na kuwafanya kuwa chambo cha kuuawa! Watu walihimizana kukaa pamoja kwa vikundi kwenye kila kaya na kushauriwa kutokuwa peke yao kwa muda mrefu. Baadhi yao woga uliwapanda kwa kiwango cha juu kiasi kwamba, hata utaratibu wa kwenda kujisaidia chooni, iliwabidi waombe msaada wa kusindikizwa huku wakiomba wanaowasindikiza japo wawe wakisubiri nje ya mlango wa choo hadi watakapomaliza haja zao.
********
KIZA cha usiku kikiwa kimetawala kwenye anga ya kisiwa cha Zebati, muda wa kwenda kwenye sala ya maombi maalumu nao ukawa unakaribia. Shime za kuhimizana kwenda kwa vikundi kuelekea kwenye sala hiyo ukawa unahimizwa kwa msisitizo. Hatimaye makundi ya waumini wanawake kwa wanaume, huku wanawake wengi wakionekana wamejifunga vitambaa vichwani waliokuwa wakiimba nyimbo za utukufu wa kumsifu Yesu, walitembea kwa makundi yenye umri tofauti kwa mwendo wa kasi wakitokea pande tofauti za mji wakipandisha kwenye njia zinazoelekea kanisani ambako kanisa lilionekana kileleni mwa mlima uliokaa kama kichuguu huku miali ya moto ikionekana ikiwaka kulizunguka kanisa hilo.
Kanisani kwenyewe ambako mienge iliyokuwa ikiwaka moto iliyotumika kama taa za kutoa mwanga ilionekana kandoni mwa ukuta uliozunguka kanisa huku miali hiyo ya moto ikifanya vivuli-vivuli vya rangi ya dhahabu. Wasaidizi wa Padri Toni walikuwa wamesimama kwenye lango kuu la kuingilia kanisani wakigawa mshumaa kwa kila muumini na kuwashwa kabla hajaingia ndani. Hali hiyo ilianza taratibu huku neno la kumtukuza Yesu likiwa linatajwa mara kwa mara kutoka vinywani mwao kwa sauti zilizoonyesha hali fulani ya woga. Watu wakawa wanaongezeka kadri muda ulivyokuwa ukienda na hatimaye waumini waliowahi kuingia kanisani wakawa wamejaa hadi nafasi kukosekana. Waumini waliochelewa wakalazimka kusimama nje kwa kujazana kwenye lango kuu la kuingilia kanisani huku kila mmoja akijaribu kupata nafasi ya kuona ndani.
Sala maalum ikaanzishwa na Padri Toni. Mwendelezo wa nyimbo za kumsifu Mungu na Yesu ziliimbwa kila zilipohitajika huku sauti nyororo za wanawake zikisikika kupanda na kushuka na vifungu maalum vinavyowataja Mitume waliomo kwenye Biblia vikihusishwa na uendeshaji wa sala hiyo. Akiwa kwenye maombi hayo maalum, Padre Toni aliwaasa waumini waondokane na fikra za ushirikina na waendelee kumwomba Yesu Kristu awatoe kwenye janga linalokikabili kisiwa hicho.
Wakati sala ya maombi ikiendelea, nje ya kanisa hali ya hewa ilianza kubadilika. Upepo ulianza kusukuma matawi ya miti iliyozunguka kanisa, ukasambaa na kuingia baharini ambako mawimbi ya bahari yalianza kujikusanya na kupiga kwa nguvu kwenye fukwe kama yenye hasira. Hali hiyo ikaanza kuchukuliwa kama ashirio baya na waumini waliokuwa wamesimama nje ya kanisa.
Taratibu, kadri muda ulivyokuwa ukienda ndivyo mabadiliko ya hali ya hewa yalivyozidi kubadilika. Upepo ukawa unavuma kwa hasira na kuanza kutoa mruzi ambao kwa mazoea ya wakazi tangu hali hiyo ianze, ashirio la kuwa mtu atakufa likaanza kuwatia hofu waumini walioko nje ya kanisa, kwa kuamini kuwa, wao ndiyo waliokuwa kwenye mazingira ya kuwa wahanga wa kwanza kuuawa, kuliko wale walioko ndani!
Moto uliokuwemo kwenye mienge iliyosimikwa ukutani ilianza kupeperushwa kwa nguvu na upepo. Waumini waliokuwa nje ya kanisa wakaanza kutoka ya nje ya sala, kihere cha woga kikawaingia baada ya macho yao kuvutwa kuiangalia ile mienge. Moto wa kwenye mienge ulikuwa ukitoa sauti za kufokafoka kutokana na kusukumwa na upepo na kuanza kupoteza nuru kuonyesha ingezimika wakati wowote. Ghafla, baadhi ikaanza kuzimika. Sauti za hofu zikasikika kutoka kwa waumini baada ya kuiona hali hiyo, wengine wakakumbuka kupiga alama ya msalaba mbele ya vifua vyao huku sura za hofu zilizotaharuki zikionyesha kuchanganyikiwa.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Kama ilivyoanza kuzoeleka, hali hiyo inapozidi dalili za kwanza huwa ni mbwa kubweka. Wakasikika! Walisikika kutoka umbali mrefu, bweko zao zikafanya mwangi, mbwa wengine wakapokea. Hali ya kupokezana kutoka eneo moja kwenda jingine ikashamiri, hatimaye mbwa wanaofugwa na Padri Toni waliopo kwenye eneo hilo la kanisani nao wakawaitikia wenzao na kuanza kubweka kwa nguvu. Tukio la aina hiyo la kusikika mbwa kubweka lilishaanza kutafsiriwa na wakazi kuwa ni ishara mbaya, ishara ya kuwa, uhai wa mtu upo njiani kutolewa! Ni ishara iliyoanza kuogopwa, ikawajengea hadhari iliyowafanya waonyane kuwa, hali hiyo inapojitokeza, watu wasikae nje ya nyumba zao na wale ambao huwakuta wakiwa nje ya nyumba zao, walitakiwa kuchukua hatua za haraka za kujiokoa kwa kuingia kwenye nyumba yoyote itakayokuwa jirani. Na wale wote wanaofanikiwa kukimbilia ndani, wahakikishe milango na madirisha vinafungwa ili upepo ambao umeanza kuaminika ndiyo unaoua, usiingie ndani!
Waumini waliokuwa wamekosa nafasi ya kuingia kanisani, bweko za mbwa walizokuwa wakiendelea kuzisikika, zikawakumbusha maonyo hayo! Lakini pia, wakatambua kuwa, maeneo yenye nyumba zilizopo jirani na kanisa zilikuwa hatua kadhaa hadi kuzifikia kutokana na eneo la kanisa kutengwa peke yake. Hofu yao ikawa imejengeka kuwa, wasingeweza kuzifikia kwa kukimbia kabla ya kukutana na upepo huo mbaya ambao waliamini ulikuwa ukijiimarisha kwenye viunga vya kisiwa hicho. Amani yao wakaiona iko sehemu moja tu; kuingia kanisani! Lakini pia, kwa imani iliyotawala kwenye nyoyo zao, wakiamini, kanisa ni nyumba ya Mungu na isingewezekana kwa upepo huo mbaya uwe na uwezo wa kuingia humo! Ikaanza kwa wale waliokuwa nyuma zaidi kuanza kuwasukuma waliokuwa mbele yao ili waingie kanisani kujiokoa!
Vilio vikaanzia hapo! Sauti za akinamama na watoto zikasikika kuugulia kwa mayowe ya maumivu yaliyotokana na kukanyagana. Umakini uliokuwepo kwa waumini wa ndani wa kuifuata sala ukaanza kupotea baada ya vurugu hiyo ya mlangoni kupamba moto. Nyuso za waumini walio ndani zikaanza kuonyesha hofu na woga. Miongozo ya Biblia ikawekwa pembeni, waumini wakaanza kufikiria namna ya kujiokoa na hali hiyo!
Wakati hali ya tafrani ikiwa imeshawagusa, ubaridi mithili ya ule wa jokofu linapofunguliwa uliingia ghafla kanisani. Mguso wa ubaridi huo kwenye miili yao ukawafanya watoe sauti za mshituko na wengine kufanya kilio cha woga. Mshituko huo ukawa kama ni ishara ya kupitishiana ujumbe kuwa, mambo humo kanisani si shwari tena!
Padri Toni alikwishaiona taharuki iliyowaingia waumini wake, akazidi kuwapa moyo kwa kuomba kwa juhudi huku akiwasihi, Yesu yuko pamoja nao. Wakati Padri Toni akiwa kwenye juhudi za kuomba, ghafla kukazuka upepo kanisani, ukiwa haujulikani ulivyoingia! Ukaanza kuzungukia aliposimama Padri Toni, na kuwa kama kimbunga cha Kinyamkela. Kikafanya mduara uliojitengeneza kutoka sakafuni jirani na ilipo altare. Mzunguko wake ukasomba baadhi ya karatasi zilizokuwa kwenye meza ya Padri na vitu vingine vidogo-vidogo vyenye kupepea, vikazungushwa kwa kasi kuelekea juu, likaonekana kama umbo la mnyama asiyeeleweka anayejaribu kujiunda kwa kujirefusha kwenda juu kuufuata mwelekeo wa kimbunga hicho. Biblia kubwa iliyokuwa mezani kwa Padri Toni ikafunguka! Kurasa zake zikajifungua bila ya mpangilio, zikatoa mlio wa karatasi zinazogongana. Wakati hayo yakitokea, waumini walikuwa wameganda kwa mshangao, wakitoa macho ya woga wakiliangalia tukio wasiloliamini kuwa lingeweza kutokea ndani ya kanisa.
Mtu pekee aliyeonekana kutokutishwa na hali hiyo au kukata tamaa ni Padri Toni. Ingawa alianza kuyumbishwa na upepo wa kimbunga hicho huku kanzu yake nzito ikipeperushwa kwa nguvu na kujitahidi kujizuia kwa nguzo iliyokuwa jirani yake ili asianguke, aliendelea kuomba kwa nguvu na kuonekana kupoteza mhimili wa akili baada ya kusikika akiomba kwa sauti kubwa kama aliyeingiwa na pepo! Waumini waliokuwa wanaliangalia tukio hilo kwa macho yaliyowatoka pima kwa woga, waliendelea kuishikilia mishumaa inayowaka mikononi mwao huku wengine mikono yao ikitetemeka!
Ghafla upepo ukabadilisha mwelekeo, ukajisambaza na kuanza kupuliza kwenye mishumaa waliyoishikilia. Moto wa mishumaa ukaanza kufokafoka kwa kupeperushwa na kufifisha nuru kama unaotaka kuzimika. Cha ajabu haukuzimika, moto iliokuwa ukiwaka ukaonekana kama iliokuwa ukibishana na upepo huo, ukajiinua kwa pamoja kurudisha nuru na kuendelea kuwaka kama kawaida. Hali hiyo haikuchukua muda, upepo ukapuliza tena! Ikafifia tena! Lakini kama ilivyokuwa mwanzo, haukuzimika! Ukaibuka kama vile ulikuwa ukishindana na nguvu ya upepo.
Mparaganyiko wa sauti ukawa unasikika kwa nguvu kutoka kwa waumini, ikawa kila mmoja anajiombea mwenyewe kwa maneno yoyote yaliyokuwa yakimjia bila ya kujali kama yalitokana na Biblia au na nafsi yake mwenyewe. Wapo waliosema, “Yesu tuokoe!” Lakini pia, wapo waliolalamika, “Majini yametuingilia!” Ikawa ni zogo la watu waliopagawa! Ghafla sanamu ya Bikira Maria ikaangushwa na upepo kutoka ukutani ilipokuwa imetundikwa! Waumini wakatoa kwa pamoja sauti ya kushangaa baada ya tukio hilo wakiwa hawaamini kilichotokea! Uvumilivu uliokuwepo kwao ukaonekana kuanza kupotea, kila mmoja akaonekana kuwa tayari kukimbia. Ikawa kama vile inasubiriwa mmoja aanze!
Kundi la watu waliokuwa mlangoni wakaonekana kusukumana kutoka nje, na wale waliokuwa ndani baada ya kuwaona wenzao wakigombana kutoka nje, nao wakajiunga ili watoke. Kanisa kwao likawa siyo tena sehemu ya amani! Ukawa mvurugano wa aina yake, wote kwa pamoja kugombania kutoka kwenye mlango mmoja!
*********
MAPEMA usiku wa siku hiyo, Sajini Seba alikuwa hakwenda kuhudhuria sala hiyo ya maombi maalum. Mwito wa sala hiyo kwake aliona ni kitu kilichokuja ghafla kulingana na mipango yake. Mara baada ya wito wa sala hiyo maalum kutangazwa na kuenea kisiwani humo, Seba alimfuata rafiki yake wa kike anayeitwa Donna jioni hiyo na kumuuliza kama angekwenda kanisani kuhudhuria sala hiyo maalum.
“Wewe utakwenda?” Donna alirudisha swali badala ya jibu.
“Sidhani kama nitakwenda,” Seba alijibu.
“Kwa nini?”
“Kuna kitu kinachoniambia, vifo vinavyotokea havitasimamishwa na sala ya maombi. Nahisi kuna nguvu inayotekeleza mauaji haya ambayo sala haina uwezo wa kuzuia!”
“Seba! Kwa nini unasema hivyo?” Donna aliuliza kwa mshangao na kumwangalia Seba machoni.
Seba ambaye mikono yake yote miwili ilikuwa ndani ya mifuko ya suruali, alikwepesha macho na kuangalia chini. Akayainua mabega yake juu na kusema, “Sidhani kama ninaweza nikajieleza kwa hilo.”
Donna alivuta pumzi na kuzishusha. “Nguvu za giza haziwezi kushindana na nguvu za Yesu, au unahisi kuna muuaji anayeua watu?” aliuliza.
“Kuna mauzauza yanayoua!”
“Unadhani yana uwezo mkubwa kuliko wa Yesu?”
“Sijui, lakini siyo vibaya wakijaribu kuomba.”
“Unazungumza kama vile watu wanachokwenda kukifanya ni sawa na kupoteza muda?”
“Siwezi nikalithibitisha hilo.”
“Unajua kinachonishangaza ni nini?”
“Sijui!”CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Nakujua vizuri Seba kuwa, ni muumini mzuri wa kanisa na imani yako siku zote ipo kwa Yesu. Lakini kwa haya unayoyazungumza leo, hakika unanishangaza! Wewe leo ni wa kutomwamini Yesu?”
“Sijasema kama simwamini Yesu,” Seba aliikana tuhuma hiyo. “Bali ninachosema ni kuwa, tatizo lililoingia kisiwani kwetu halitaweza kutatuliwa kwa nguvu ya maombi.”
Donna akafanya tabasamu fupi lenye taswira ya kumshangaa Seba. “Unadhani kungefanyika nini?” aliuliza.
“Sijui!”
Safari hii Donna akaonyesha mshangao wa wazi. “Sasa kwa nini unapingana na suluhisho la watu kwenda kufanya maombi?”
“Sijapingana nalo, nilichomaanisha ni kwamba, sidhani kama hilo litakuwa suluhisho.”
Donna akashusha pumzi za kusalimu amri. “Kwa hiyo huendi kwenye maombi?” aliuliza.
Kwa sekunde chache Seba alikaa kimya na kuonekana kufikiri jinsi ya kumjibu Donna. “Siendi!” hatimaye alisema. Alipomwona Donna akiukunja uso wake, akaendelea kusema, “Sababu ya kutokwenda ni kwamba, nadhani umesahau kama nina ahadi ya kula chakula cha jioni hapa kwako nyumbani.”
“Seba! Huwezi ukakataa kwenda kwa ajili ya sababu hiyo! Kwa nini isiwe kesho? Eeh? Ahirisha mpaka kesho! Kwanza chakula chenyewe nilikuwa bado sijajiandaa kukipika mpaka sasa!”
Seba akauonyesha uso wa mshangao. “Kwa nini wakati unajua kuwa leo jioni nitakula hapa?” aliuliza.
“Nilijua na wewe ungeenda kwenye sala maalum, nikaona hakukuwa na sababu ya kukiandaa.”
“Ahadi ya kuja kula kwako, kwangu mimi ni sababu ya maana sana kuliko kuhudhuria sala hiyo.”
“Yesu wangu!” Donna alisema huku viganja vyake vya mikono akiwa amevikinga kwenye kinywa chake.
“Kwa hiyo na wewe nakuomba usiende!” Seba alimwambia Donna. “Baki nyumbani ili unipikie, sawa?”
Donna alisita kwa sekunde kadhaa. Hakutaka kutoa majibu ya papo kwa hapo kwa sababu alikuwa akimpenda Seba. Kisha kwa sauti iliyopwaya alijitetea kwa kusema, “Nadhani haitakuwa vizuri kama sitakwenda, Seba.”
“Unajihisi utapata dhambi kama hutakwenda?”
“Hii ni sala ya dharura ya maombezi kwa ajili ya shida maalum, karibu kila mtu atakwenda. Kwa nini nami nisiende?”
“Siyo kila mtu atakayekwenda! Wapo wataokuwa na sababu kama zako ambao hawatakwenda!”
Donna akajiwa na hisia kuwa, uamuzi mwingine wowote atakaouchukua kinyume na Seba anavyotaka unaweza ukaleta kutoelewana kati yao. Akaamua kuliepusha hilo. “Kwa hiyo unanitaka nisiende?” aliuliza.
“Nataka unipikie. Tutakuwa pamoja wakati wote wa kupika, kwa hiyo usiende!” Seba alisema.
“Sawa,” Donna alisema kwa sauti iliyopwaya.
Wakaagana.
*********
USIKU ulipoingia, Seba alikwenda nyumbani kwa Donna mapema kabla ya watu kuanza kwenda kwenye sala maalum ya maombi. Akiwa na Donna chumbani, aliwasikia wakazi wenzake wanaoishi nyumba moja na Donna wakiagana kwenda kanisani kwenye maombi.
“Umewaambiaje wenzako?” Seba alimuuliza Donna. “Kuwa hutakwenda?”
Donna aligeuka na kumwangalia Seba bila ya kumjibu. Donna akatoka kuelekea uani lilipo jiko. Seba akagwaya peke yake chumbani baada ya kujiwa na hisia za kuwa, kitendo cha kumzuia Donna kutokwenda kwenye sala maalum hakikuwa cha haki. Akajiuliza kama aitumie nafasi hiyo kumshauri Donna atakaporudi tena chumbani amwambie kuwa, wangeweza kwenda kanisani baada ya kula.
Donna akarudi chumbani, lakini hakuonyesha kuwa angetulia, bado alionekana kuwepo kwenye hekaheka za kupika.
“Kuna kitu nataka kukwambia,” Seba alimwambia Donna.
Donna akasimama na kumwangalia Seba machoni bila ya kutamka lolote.
“Baada ya kula, twende kanisani!” Seba alisema.
“Kwenda kufanya nini wakati umeshaona kwenda huko ni kupoteza muda?” Donna alisema huku akionyesha kutaka kutoka chumbani.
“Watu hawatatuelewa wakijua hatukushiriki sala.”
“Kwani mwanzoni hukuwa na mawazo hayo?”
“Lengo langu ni kutaka kukupeleka wewe, kwangu siyo tatizo hata kama sitakwenda. Leo asubuhi nimeonana na Padri Toni na kumweleza msimamo wangu kuwa, tatizo lililopo halitatatuliwa na maombi.”
Uso wa Donna ukaingiwa na mshituko wa kutoamini alichokisikia kutoka kwa Seba. “Eti nini Seba?” aliuliza.
“Nimemwambia Padri Toni!” Seba alisisitiza.
“Kwa nini ulimwambia hivyo?”
“Ni sababu za kiupelelezi, nimegundua kuna walakini kwenye hivi vifo. Kuna nguvu fulani ambayo bado sijaijua, inatumika kufanya mauaji haya. Nina hakika nguvu hiyo si ya kusimamishwa na maombi!”
“Seba!” Donna alisema kuonyesha ameishiwa na la kuzungumza. Akataka kuondoka.
“Kwa hiyo baada ya kula upo tayari nikupeleke?” Seba alisema kabla ya Donna hajatoka.
“Muda utakuwa umekwenda.”
“Unadhani sala ya maombi huchukua muda mfupi? Inaweza ikachukua zaidi ya saa tatu.”
“Tutaangalia!” Donna alisema na kutoka.
Kilikuwa chakula alichokipenda Seba wakati walipokuwa wakila. Donna alikuwa ameandaa wali wa samli kwa kitoweo cha samaki aina ya Pweza aliyekaangwa kwa vitunguu swaum, mchuzi wa chukuchuku wa pweza ulioungwa kwa embe mbichi, ngogwe, bamia na nyanya na nyongeza ya kachumbari iliyotiwa pilipili mbuzi. Walikula pamoja na kuzungumzia kwa kifupi hali tete inayokikumba kisiwa chao huku Seba akisisitiza imani yake kuhusu hali hiyo, lakini pia wakazungumzia kuhusu mipango yao ya kufunga ndoa. Kwa kuwa walikubaliana baada ya chakula waende kanisani kujiunga na sala ya maombi, waliamua kuyafupisha mazungumzo yao ili wawahi kwenda huko.
Baada ya kumaliza kula, Donna ambaye alioga mapema mara tu baada ya kupika, alibadilisha nguo na kuwa tayari kutoka. Wakatoka! Hali ya mji ilikuwa kimya wakati wakitembea kwenye barabara za mji huo. Nyumba zote zilikuwa kwenye utulivu na kukosa uhai kutokana na kutokuwepo watu. Walijihisi kama wako peke yao kwenye mji wote walipokuwa wakitembea na giza lilionekana kukomaa kutokana na kutokuwepo kwa mbalamwezi, hali hiyo ikawaletea aina ya simanzi waliyoshindwa kuijadili. Mtu mmoja au wawili walionekana wakikatiza kwa nadra na kuwa kama vivuli vya binadamu visivyo rasmi.
Walikuwa wakitembea bega kwa bega, ingawa hali ya ukimya uliokuwepo haikuwaridhisha sana, lakini kitendo cha kutembea wawili peke yao kiliwafanya kwa sehemu fulani wajisikie huru kwa kupitisha mikono yao kushikana, mara viganja kwa viganja au wakati mwingine wapitishiane kwenye viuno na kukumbatiana kwa kulalishiana vichwa vyao.
Wakiwa kwenye hali hiyo, wakaanza kukabiliana na hali ya hewa iliyobadilika ghafla. Kukawa na ka-upepo kanakoonyesha dalili ya kungekuwepo mvua. Lakini kadri walivyokuwa wakitembea, hali hiyo ikaendelea kubadilika, upepo ukaanza kidogo kidogo kuwa mkali na kuanza kutikisa miti.
“Bwana, miye siendi tena kanisani!” Donna alisema ghafla.
“Kwa nini?” Seba aliuliza na kuonekana kushitushwa na kauli ya Donna.
“Si unaiona hali ya hewa imeanza kubadilika, bora unirudishe tu, nyumbani!”
Seba hakujibu kwa haraka. Alijikita kwenye tafakuri na kuonekana kukielewa kilichomaanishwa na Donna. “Unachoongea ni kweli,” alisema. “Huwezi kujua, pengine ni mwanzo wa upepo mbaya. Wacha nikurudishe nyumbani!”
Wakageuza bila ya kuongeza neno la kubishana.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment