Simulizi : Msalaba Wa Dhahabu
Sehemu Ya Pili (2)
“Hapana,” Seba alijibu kwa utulivu na kuiangalia hali ya uani ilivyo huku macho yake yakihama kwa utulivu kwa kuangalia kila eneo. Akageuka kutaka kuzungumza na mama Sai, akamwona mama huyo kama aliyeduwaa akiangalia kitu kinachoelea hewani.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Seba akajaribu kuyafuata macho ya mama Sai yanapoangalia, lakini akakumbana na moshi unaoelea uliotokana na shughuli za mapishi. Kutokuona kitu kingine zaidi ya moshi, Seba akahisi mama Sai hana anachokiangalia zaidi ya kuwa mbali kimawazo. “Mama Sai!” aliita.
Mama Sai hakushituka kama afanyavyo mtu mwenye mawazo anavyofanya wakati akishtuliwa. Aligeuka taratibu na kumwangalia Seba. “Bee!” aliitikia kwa upole.
“Nakuona uko mbali kimawazo!”
“Nilikuwa nauangalia huu moshi,” mama Sai alisema, kisha akauangalia tena moshi.
Seba alipomwona mama Sai ametekwa tena na moshi anaouangalia, naye akajikuta akiuangalia moshi huo. Sekunde chache baadaye akalazimika kuhoji. “Sijakuelewa!” alisema.
“Huu moshi unanikumbusha kitu,” mama Sai alisema akiendelea kuuangalia.
“Unakukumbusha nini?” Seba aliuliza kwa sauti ambayo haikutoa uzito wa swali lake.
“Unanikumbusha kuhusu jana usiku nilivyokuwa nimetoka uani nikiwa na Sai.”
Kauli hiyo ikamlazimisha Seba ajenge umakini wa kutaka kusikiliza.
“Kulikuwa na moshi eneo aliloangukia baba Sai, lakini baadaye ukatoweka!” mama Sai aliongea kama vile alikuwa akiongea na nafsi yake.
“Kipi ulichokiona cha ajabu?”
“Mazingira ya moshi wenyewe hayakuwa ya kawaida.”
“Ki-vipi?” Seba aliuliza na kujaribu tena kuujenga umakini.
“Hakukuwa na moto, ulielea kama vile ulikuwa ukijitegemea.”
“Huenda ulikuwa ni moshi uliosambaa kutoka sehemu kulikowashwa moto, ni kawaida kwa usiku moshi kusambaa eneo kubwa.”
“Moshi niliouona ulikuwa kama kiwingu mfano wa ukungu na ulivyotoweka, ulitoweka kwa pamoja kama vile ulikuwa na uhai. Siyo kawaida moshi kutoweka kwa kufanya kiwingu cha pamoja na kupotea ghafla, au wewe unasemaje?”
Seba akawa mwangalifu na swali aliloulizwa baada ya kupata dhana, huenda mama Sai, ameanza kuegemea kwenye imani za kishirikina. “Unataka kuniambia, baba Sai ameuawa kwa nguvu za giza?”
“Huwa namwamini Yesu, siamini nguvu za giza!”
“Kwa nini umesema siyo kawaida moshi kutoweka kwa kufanya kiwingu cha pamoja na kupotea ghafla?”
“Kwa sababu ndicho kitu nilichokiona!”
“Kwa hiyo unataka kuniambia nini?”
“Niliuona moshi wa aina hiyo! Si ulitaka kujua kitu gani nilichokiona baada ya kutoka uani alikokuwepo baba Sai?”
Seba akamwangalia mama Sai, kisha asiseme lolote.
*******
BAHARI ilikuwa shwari na mandhari yake ilionekana kama jangwa kubwa lenye rangi ya buluu lililosambaa hadi upeo wa macho. Ilikuwa imetulia kana kwamba lilikuwa ni zulia lililotandazwa. Kutokea angani, juu ya uso wa bahari kukawa kunaonekana doa jeusi lililokuwa likielea. Kadri lilivyokuwa likionekana, ndivyo likawa linajionyesha kutokuwa na mwelekeo. Lilikuwa likielea kwa kucheza-cheza juu ya mawimbi madogo-madogo kama lililokuwa haliendi mbele wala kurudi nyuma, likicheza hapohapo.
Kilikuwa kichwa cha Mathias!
Alikuwa hoi taabani akiwa ameulalia upande wa ngalawa yao iliyovunjika. Alikwishapoteza fahamu baada ya kushinda na njaa na kupigwa na jua kali la baharini. Mawimbi yaliendelea kuuchezesha mwili wake kama vile kiwiliwili hicho kilikuwa mfu.
Kabla ya kupoteza fahamu, jitihada zake za kuogelea kwa kutumia nguvu zilizoingiwa na taharuki, huku akisaidiwa na ubao aliokuwa akiogelea nao, zikawa zimeingiwa na uchovu uliomwongezea njaa na kiu. Awali kabla ya kupoteza matumaini, alikuwa na hakika ya kukutana na wavuvi ambao wangeweza kumuokoa, lakini kadri muda ulivyokuwa ukienda, ndivyo matumaini yake yakawa yanapotea kwa kasi. Kuchanganyikiwa kukamzidia baada ya kuliona jua la jioni likizama, na kiza cha dunia kikitanda juu ya uso wa bahari huku upeo wake wa macho ukiwa umefikia mwisho bila kuona chochote cha kumtia matumaini. Mazingira hayo yakazidi kumchanganya kiakili na kujiona kama nusu mfu. Hali hiyo ikaanza kumwathiri kisaikolojia, akapoteza kumbukumbu na kushindwa kujua alikuwa na siku ngapi baharini! Vitu asivyovielewa vikaanza kumjia kichwani na kujiona kama aliyekuwa anaweweseka kwenye jinamizi.
Athari za kisaikolojia zikaanza kumshambulia. Akaiona ngalawa iliyokuwa na wavuvi ikipita kwa mbali, akawaita kwa sauti kubwa kuhitaji msaada wao. Wakampungia mkono kumjulisha kuwa alishaonekana. Walikuwa wavuvi wanne waliokaa kwa kujipanga kimsitari huku wakipiga makasia kuelekea alipo. Ngalawa ilipomkaribia, Mathias akaonyesha furaha, lakini dakika hiyohiyo uso wake ukabadilika baada ya kuiona ngalawa hiyo ikimpita kwa mbele umbali wa mita kumi na wavuvi waliomo kwenye ngalawa wakiwa hawaonyeshi dalili yoyote ya kutaka kumpa msaada. Mathias akapiga kelele nyingine za kuwaomba msaada wa kumuokoa, wavuvi hao wakageuka kwa pamoja kama gwaride lililopewa amri, wakamwangalia. Mathias akashituka alipoziona sura za wavuvi hao zikifanana na sura za kunguru weusi! Akiwa haamini alichokiona, akajaribu kutikisa kichwa kukung’uta majimaji yaliyokuwa machoni mwake. Alipoyafumbua macho yake kuangalia tena, wavuvi na ngalawa yao wakawa wamepotea!
Hakuamini! Akayazungusha macho yake kwa hali ya kutaharuki kuangalia eneo lililomzunguka. Yesu wangu! alihamanika peke yake baada ya kuwa na hakika alichokiona, hakionekani tena! Hofu na woga vikamwandama. Akausikia mlio alioshindwa kubuni ni wa kiumbe gani, ukamtoa kwenye jinamizi alilokuwa nalo. Akalazimisha fahamu zake ziweze kurudi, lakini akashindwa kufanya hivyo, badala yake akaingiwa na kiza machoni, kila kitu kikaishia hapo!
Alipoteza fahamu!
****
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
MZEE Robert Mizengwe akiwa chumbani kwake alifahamishwa kuwa chakula cha usiku kipo tayari mezani. Akairuhusu familia yake iendelee kula baada ya yeye kukataa. Kichwani mwake hukukuwa na amani tokea Mathias apotee ghafla, tukio hilo likawa linazidi kumuweka kwenye shinikizo la kujiuliza kama ndoto aliyomuota Mathias akiwa na wenzake wakilivunja dirisha la kanisa na kuiba Msalaba Mtakatifu kunahusiana na kupotea kwake? Alikuwa hajamwambia mtu yeyote kuhusu ndoto hiyo na alijiona kuwa ni mzito wa kuizungumza kwa mtu. Hali hiyo ikaendelea kumwadhibu kwa kumpa shinikizo la mawazo wakati wote, hadi akajikuta akipoteza hamu ya kula.
Mapema siku hiyo, juhudi zilizofanywa na wakazi wa Zebati kukizunguka kisiwa hicho kumtafuta Mathias, zikaishia kuwakatisha tamaa baada ya kuingia giza! Ari ikatoweka na uchovu ukawaingia. Pamoja na kuingiwa uchovu, lakini wengine wao ambao hawakuonyesha kukata tamaa, mzee Robert akiwa ni mmoja wao, waliwatia moyo wenzao ili siku ya pili asubuhi na mapema waendelee tena na msako wao. Wakakubaliana asubuhi na mapema msako wa kumtafuta Mathias uendelee.
Pamoja na kukubaliana huko, lakini matokeo hayo ya awali ya kutoonekana kwa Mathias hadi giza likiwa limeingia, yakawa yamezidi kumchanganya mzee Robert. Uchovu na njaa vikawa sehemu ya mfadhaiko aliokuwa nao hadi aliporudi nyumbani. Ndipo alipoitwa kwa ajili ya chakula cha jioni, akakataa. Akairuhusu familia yake iendelee na mlo huo. Lakini kukataa kwake kula, kukasababisha familia yake hiyo, nayo isusie chakula hicho!
Nyumba nzima ikawa imeingiwa na mfadhaiko!
Asubuhi ya siku ya pili, wakazi wa Zebati walijikuta wakiamka na taarifa nyingine mpya; taarifa ya kifo cha baba Sai! Taarifa za kifo hicho kilichogubikwa na utata zikaanza kuibadili hali halisi iliyotarajiwa kwa wakazi kuamka na ari ya uhamasishaji wa kuendelea kumtafuta Mathias, lakini kwa taarifa za msiba huo, zoezi la kuendelea kumtafuta Mathias likasitishwa. Kisiwa cha Zebati kikafunikwa na msiba wa baba Sai! Simanzi ikatawala kisiwani humo huku kila mkazi akishangazwa na mazingira ya kifo hicho.
Watu pekee waliotaka zoezi la kumtafuta Mathias liendelee ni familia ya mzee Robert Mizengwe, kwao msiba wa kifo cha baba Sai ukaonekana kutowagusa kikamilifu. Lakini fikra hizo za kifamilia zikawa tofauti na mzee Robert mwenyewe aliyekuwa akiendelea kuiweka moyoni siri ya ndoto aliyoota! Kwake yeye, kifo cha utata cha baba Sai ukawa mwanzo wa mashaka kuhusu ndoto hiyo. Lakini si kifo tu, mzee Robert alikumbuka jinsi kisiwa hicho kilivyokumbwa na tufani la upepo mkali uliotokea usiku na kuangusha hadi miti mikubwa. Kwenye kumbukumbu zake hakuwahi kuishuhudia hali kama hiyo ikitokea kisiwani humo ingawa baadhi ya nyakati za nyuma kulishatokea vimbunga vya hapa na pale, lakini haikufanana na hali iliyojitokeza usiku. Hali ilikuwa mbaya mno na ilitisha, na hatimaye ikamalizia na kifo cha baba Sai! Kuna tafsiri gani? alijiuliza. Lakini kwa upande wa pili, hakutaka kuamini tufani lililopita usiku na hatimaye kifo cha utata ndiyo mwanzo wa dalili za maafa yaliyotabiriwa zamani kuwa, yangekifikia kisiwa hicho endapo Msalaba Mtakatifu uliopo kanisani ungeibwa.
Sababu kubwa iliyomfanya asiamini kuwa hizo ni dalili za maafa yaliyotabiriwa ni kule kushuhudia kwa macho yake alipokwenda kanisani na kuuona Msalaba Mtakatifu ukiwa uko palepale kwenye altare. Kwa maana nyingine ni kuwa, Msalaba Mtakatifu ulikuwa haukuibwa kama ndoto yake ilivyotaka aamini! Pamoja na kukiri kuwa, Msalaba Mtakatifu haukuibwa, lakini pia ameuacha ukiwa kanisani, kitendawili cha kupotea ghafla kwa Mathias ukawa ni mtihani mwingine mkubwa kwake. Hakuelewa kwa nini aoteshwe ndoto ya Mathias akiiba Msalaba Mtakatifu kanisani kisha saa chache baadaye, Mathias atoweke! Lakini isitoshe, kisiwa kikakumbwa na tufani la aina yake na baadaye kuingia kwenye msiba wa kifo chenye utata! Sababu ya kuoteshwa ndoto ya aina hii ni nini? alijiuliza. Mzee Mathias akajiona yupo kwenye kuchanganyikiwa zaidi kuliko kupata ufumbuzi wa ndoto yake.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Akiwa amekaa peke yake chumbani, alikiri ndoto aliyoiota ilikuwa na sababu. Siyo bure! alijiambia. Kwa mara nyingine tena, akajaribu kuilazimisha akili yake iweze kupata tafsiri ya ndoto hiyo. Alichokiona ni kwamba, yeye aliota msalaba ukiibwa, lakini siku iliyofuata akashuhudia haukuibwa. Kwake yeye ilimpa jawabu kuwa, hivyo ni vitu viwili tofauti. Lakini ghafla akapata wazo tofauti, inaweza ikawa ni dalili ya Msalaba Mtakatufu upo njiani kuibwa? alijiuliza. Akajiuliza kama ndoto aliyoiota ilikuwa ni hadhari aliyopewa? Kuna kipindi alianza kushawishika na dhana hiyo ya kuwa, ndoto aliyoiota huenda ilikuwa ni hadhari aliyokuwa amepewa kupitia ndotoni, lakini lilipokuja suala la kupotea kwa Mathias, akakiri kuwa kuna walakini uliojificha kwenye ndoto hiyo. Kuna zaidi ya hadhari! alijionya.
Hakutaka kuamini kuwa, mjukuu wake huyo ametoroka hapo nyumbani. Atoroke aende wapi? Na ni kwa sababu gani? alijiuliza. Mzee Robert alijiamini ni mtu pekee aliyekuwa akizijua kwa undani tabia za Mathias kuliko mtu mwingine yeyote hapo kisiwani. Aliamini mjukuu wake siku zote alikuwa akiishi kwa upendo na ndugu zake na hata yeye mwenyewe, aliishi kwa unyenyekevu na kila mtu alimpenda hapo kisiwani. Hakuwa na kiburi na mtu yeyote, hakuwa mbishi wa kupenda kubishana, alipenda zaidi kusikiliza kwa umakini hoja kabla ya kuijibu, na pale alipokuwa akiingiza hoja yake aliamini ni hoja yenye kukubalika kimsingi kulingana na mazungumzo yaliyokuwepo. Lakini pia, mzee Robert alimwona Mathias hakuwa mwenye tamaa ya kimaisha kutokana na kumpokea vizuri Yesu, na ndiyo maana ameweza kuwa mwanafunzi mwenye sifa nzuri chuoni. Kwa nini atoweke? Hapo ndipo palipomchanganya mzee huyo!
*******
JIONI, baba Sai alizikwa kwa mazishi yaliyohudhuriwa na robo tatu ya wakazi wa kisiwa hicho. Muda mfupi kabla mwili wake kwenda kusaliwa kanisani, mlinzi wa kanisa aliwahi kufika kanisani kabla ya mwili wa baba Sai haujawasili. Ingawa naye angekuwa ni mmoja wa watu ambao wangehudhuria mazishi hayo, lakini yeye aliwahi kuondoka mapema msibani ili kwenda kanisani baada ya kupewa taarifa kuwa, alikuwa akitafutwa na Padri Toni ambaye ndiye mkuu wa parokia. Alipofika kanisani, alikwenda moja kwa moja nyumbani kwa Padri Toni, akamkuta msaidizi wa Padri aliyemwambia kuwa, Padri yuko kanisani.
Mlinzi akaaga na kuelekea kanisani alikoelekezwa. Alivyoingia kanisani, akiwa kwenye mwelekeo ilipo picha ya Bikira Maria, alipiga goti na kufuatia kwa kupiga alama ya msalaba kifuani. Alipoinuka, akamwona padri ndiyo kwanza amemaliza kusali, akamfuata.
“Nilikuwa nakutafuta ili nikuulize kama siku mbili hizi ulipata matatizo yoyote kwenye kazi yako?” Padri Toni alisema akiwa anatembea bega kwa bega na mlinzi wakielekea kwenye meza iliyopo kwenye altare.
Kuulizwa swali hilo, moja kwa moja mlinzi akaiwazia gharika ya upepo mkali uliovuma usiku uliopita. “Sikupata matatizo yoyote!” alisema huku mikono yake akiwa ameikunja kwa mbele.
“Una uhakika?”
Kuna tatizo nini limetokea? mlinzi alijiuliza. “Kweli sikupata!” alisema. “Mpaka leo asubuhi nilipoondoka kila kitu kilikuwa kipo shwari pamoja na hali ya hewa ilikuwa mbaya.”
Padre Toni akasema, “Nifuate!”
Wakafuatana. Wakaenda kusimama kwenye dirisha la kanisa lililokuwa limevunjwa kioo na kukongolewa. Kuliona dirisha hilo, mlinzi akapigwa na butwaa.
“Nadhani utakuwa ni upepo uliovuma usiku wa kuamkia leo umekivunja hiki kioo!” mlinzi alianza kujitetea.
“Kabla ya kuondoka ulikagua lindo lako?”
“Asubuhi?” mlinzi aliuliza kipumbavu.
Padre Toni akatabasamu. “Siyo lazima iwe leo asubuhi, linaweza likawa limevunjwa jana au juzi…” alisema.
“Kusema ukweli sikukagua,” mlinzi alikiri.
“Ni muda gani hujakagua?”
“Leo na jana.”
“Jaribu kunisaidia kuangalia vitu vya humu ndani kama vyote viko salama,” alisema.
Ilimchukua mlinzi takriban dakika ishirini kuangalia vitu vyote vya thamani vilivyomo kanisani na wakati mwingine kulazimika kurudia kuangalia upya kuhakiki kama alikagua vizuri, hatimaye alirudi kwa Padri Toni. “Vitu vyote vipo salama,” alisema.
“Hata mimi nilikagua, sikuona upungufu wowote,” Padri Toni alisema. “Lakini najiuliza, aliyelivunja dirisha hili alikuwa na dhamira gani? Sidhani kama ni upepo uliovuma jana ndiyo uliovunja kioo hiki na kulikongoa dirisha, hii inanitia mashaka. Ingawa ndiyo, kulikuwa na upepo mkali, lakini kama ungekuwa ni upepo, ungeweza kupeperusha na hata kuangusha baadhi ya vitu vilivyomo humu ndani.”
Mlinzi akataka kuongea, lakini kabla ya kusema, macho yake yakavutwa mlangoni. Akamwona msaidizi wa Padri Toni akiingia na kuja moja kwa moja pale walipokuwepo.
“Mwili wa baba Sai umewasili,” msaidizi wa Padri Toni alisema huku akionyesha kushangaa na hali ya dirisha.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Waruhusu waingie,” Padri Toni alisema.
Waumini na waombolezaji waliingia na jeneza lililobeba mwili wa baba Sai na kulipeleka mbele. Mmoja kati ya halaiki iliyokuwepo kuuleta mwili wa baba Sai na kuingia kanisani alikuwa ni mzee Robert Mizengwe!
Sala rasmi ya kumwombea baba Sai ikaanza. Padri Toni akaiongoza sala hiyo kwa kutumia maandiko yaliyomo kwenye Biblia. Hatimaye akaanza kutoa nasaha kwa waumini kabla ya kuruhusu jeneza kupelekwa makaburini. Katika busara zake akaligusia suala la dirisha lililovunjwa. “Jioni ya leo nimegundua moja ya dirisha la kanisa letu limevunjwa kioo na kukongolewa,” alisema. “Nilimuuliza mlinzi wetu wa kanisa, naye akakiri kuwa, hakuliona alipokuwa ameondoka asubuhi kwa sababu hakufanya ukaguzi wakati alivyoondoka. Lakini kingine nilichogundua, dirisha hili halikuvunjika lenyewe, bali lilivunjwa. Aliyelivunja, sijui alilivunja kwa bahati mbaya au kwa dhamira ya uovu. Hata hivyo, endapo aliyelivunja alilivunja kwa bahati mbaya na kuogopa kuliripoti tukio hili, ni vyema kwa sasa hivi ajitokeze na kukiri ni yeye ndiye aliyelivunja. Nazungumza hili kwa sababu ya kutaka kujenga tabia njema kwa waumini, kuwa pale wafanyapo jambo bila ya ridhaa yao, lakini jambo hilo likaonekana lina mtazamo hasi machoni kwa watu, ni vyema mtazamo huo ukaondolewa na yeye mwenyewe kwa kukiri kuwa, ilikuwa ni bahati mbaya. Natoa nafasi hii kwa mtu aliyekitenda kitendo hiki ajitokeze hapa mbele, lakini licha ya kusamehewa, pia apate baraka za Bwana Yesu kwa kuwa mkweli.”
Kimya kikajikita, hakuna aliyejitokeza! Waumini wakaanza kujihoji, ni nani angeweza kukitenda kitendo hicho kisha akanyamaza kimya? Kilionekana ni kitendo cha ajabu na cha aina yake kwa mtu kuvunja nyumba ya Mungu kisha asijitokeze akasamehewa! Baada ya ukimya kuendelea bila ya kujitokeza mtu, ikaaminika mtu aliyelivunja dirisha hilo, alikusudia uovu na ndiyo sababu hakujitokeza mbele. Tukio hilo ambalo ni mara ya kwanza kufanyika, ikawa ni habari kubwa, na waumini wakajikuta wakimlaani mhusika na kitendo hicho.
*******
MTU pekee aliyezipokea habari hizo kwa mshituko mkubwa na wa kipekee kuliko waumini wote wakati akiwa kanisani, ni mzee Robert Mizengwe. Dirisha la kanisa limevunjwa! Taarifa hizo kwake zikawa kama kofi lililomchapa usoni. Kuvunjwa kwa dirisha la kanisa ilikuwa ni sehemu ya ndoto aliyoiota! Hofu ikamwingia kuwa, ndoto hiyo imeanza kujidhihirisha kuwa ni ya kweli! Kimbunga kilichokipiga na kuangusha miti na kufuatiwa na kifo cha utata cha baba Sai ni dalili ya mwelekeo wa maafa? Swali hilo likamfanya auangalie Msalaba Mtakatifu ulioko kwenye altare. Maafa yatakujaje ikiwa Msalaba Mtakatifu upo pale?
Ingawa maswali aliyokuwa akijikaba nayo yalimkosesha majibu sahihi, lakini hitimisho la Padre Tino la kudai dirisha la kanisa limevunjwa, ilikuwa taharuki asiyoitarajia na kumshinikiza kuwa, kitendo cha kuvunjwa dirisha la kanisa kunaenda sambamba na ndoto yake! Akakiri kuwa, kitu pekee kilichokuwa kikimchanganya akili ni Msalaba Mtakatifu kuendelea kuwepo kanisani! Laiti msalaba huo usingekuwepo, moja kwa moja angejua umeibwa na dalili hizo zilizojitokeza angezikubali kuwa ni ishara ya maafa yaliyotabiriwa! Ukweli ni upi? alijiuliza.
Lakini kupotea kwa Mathias kutakuwa kunalenga nini? Na atakuwa anahusika vipi na wizi wa msalaba, wakati msalaba upo? Na kwa nini Mathias asionekane? Kuna mtu alimshuhudia akitaka kuiba msalaba Mtakatifu kisha akaamua kuikimbia nchi kwa sababu asingeweza kuikabili aibu hiyo? Na ndiyo sababu ya dirisha la kanisa kuvunjwa lakini kukawa hakukuibwa chochote? Kama mtu huyo alimwona Mathias akivunja dirisha la kanisa na kisha kukimbia, kwa nini mtu huyo hakuliripoti tukio hilo kwa uongozi wa kanisa?
Mzee Robert akakumbuka kuwaona watu wengine wawili kwenye ndoto aliyoota wakiwa na Mathias wakati akivunja dirisha, akajaribu kuvuta kumbukumbu kama sura zao zilionekana kwenye ndoto hiyo. Kumbukumbu ilimkatalia na hatimaye alikiri asingeweza kuzikumbuka sura hizo!
Waumini wakamshitua wakati walipoanza kutoka, akajiunga nao kuelekea makaburini kwa safari ya mwisho ya baba Sai. Tenzi za rohoni zenye maombolezo ziliimbwa kuusindikiza mwili huo!
*****
USIKU baada ya mazishi ya baba Sai, ilipokaribia saa nne, hali ya hewa ilibadilika ghafla kisiwani Zebati. Joto lisilo la kawaida lilirindima na kuwalazimisha wakazi watoe mikeka na virago vingine nje ya nyumba zao kujaribu kuutafuta usingizi kwenye hewa ya wazi. Ilipofika saa tano, hali ilibadilika tena, upepo mkali ukaanza kuvuma, minazi na miti mingine ikaanza kuyumba kwa kelele. Mkazi mmoja ambaye naye alikuwa ametoa mkeka na kulala nje, akaamka kwa hofu. Akaiamsha familia yake na kuitaka irudi ndani. Mbwa nao wakaanza kubweka kwa nguvu huku upepo wenye sauti ya mluzi ukivuma na kuongezeka. Ikawa ni hofu!
Ndani ya chumba kimoja ndani ya nyumba hiyo, msichana aliyeitwa Zebu, aliyekuwa ametangulia kuingia ndani kwa kuihofia hali iliyoko nje, akiwa amekaa kwenye kiti akimwangalia mwenzake aliyekuwa amekaa kitandani, alianza kuilalamikia hali iliyopo nje.
“Hali imeanza kuwa kama ya jana usiku,” alisema.
Mwenzake aliyeitwa Maria, alimuunga mkono kwa kusema, “Na huyo anayebweka nje siyo mbwa wangu?”
Zebu hakujibu. Akili na mawazo yake yalikuwa nje akiusikiliza upepo unaofoka kwa hasira na wakati huohuo akionekana usoni kuwa na aina ya woga.
Ghafla, Maria aliinuka kutoka kitandani na kwenda kulifungua dirisha alilokuwa amelifunga muda mfupi uliopita ili kuuzuia upepo uliokuwa ukiingia na kupeperusha vitu vilivyomo ndani. Akachungulia nje na kumwona mbwa wake akiwa peke yake, akibweka kwa nguvu kuelekea barabarani kama aliyekuwa ameona kitu, akienda mbele na kisha kurudi kinyumenyume. Kugundua kuwa mbwa wake yuko peke yake huku watu wote waliokuwa nje wakiwa wameingia ndani na hata wale wa nyumba za jirani nao wakiwa hawapo na kuufanya mtaa uonekane kuwa mtupu na kimya, hali hiyo ikamfanya Maria apagawe.
“Ndiye yeye!” Maria alisema na kugeuka kumwangalia Zebu kisha, akaurudisha tena uso wake dirishani kuangalia nje. “Jackie! Jackie!” alimwita mbwa wake. “Acha kelele!”
Mbwa akaendelea kubweka huku akisaidiana na wenzake waliokuwa mitaa ya jirani. Maria akaonyesha kuchukizwa na mbwa wake, akalifunga dirisha kwa hasira, akarudi kitandani na kukaa. Akatulia kama vile hakuridhika na mbwa wake kuendelea kuwepo nje. Ghafla akaonekana kuzubaa. Hali hiyo ikamshitua Zebu.
‘Wee Maria, vipi?” Zebu alimuuliza Maria.
“Hivi wewe unajisikia vipi?” Maria aliuliza badala ya kujibu swali aliloulizwa, na sauti yake ikawa imenyongea ghafla!
“Najisikia kawaida, kwani wewe unajisikiaje?” Zebu aliuliza huku akimwangalia Maria kwa umakini.
“Najisikia woga, mwili wangu unazizima na nywele kunisimama!”
Zebu akatoa kicheko kidogo cha kupuuza, “Labda pepo wanataka kukupanda,” alisema kwa dhamira ya utani.
Maria hakujibu. Zebu akajiinua kutoka kitini na kwenda kupanda kitandani, akajilaza na kujifunika shuka, akamwacha Maria bado amezubaa akiwa amekaa. Dakika chache baadaye, Maria alijiinua na kwenda kuiinamia meza iliyokuwa na taa ya kandili, akapunguza utambi wa taa hiyo kiasi cha kukaribia kuzimika, kisha akajiunga na Zebu kitandani kulala.
Wote wakiwa wamefumba macho, walijikuta wakisikilizia hali iliyokuwa ikiendelea nje, milio ya bata na kuku waliokuwa wakilia kwa hofu nayo ikasikika. Maria akauhisi mwili wake umeshikwa na baridi ya woga! Kuna nini Mungu wangu? alijiuliza. Aligeuka na kumwangalia Zebu aliyekuwa amelala, kichwa chake kikiwa upande wa pili wa kitanda.
“Zebu! Zebu,” Maria aliita kwa sauti ya chini kama inayonong’ona kwa woga.
Zebu akaitikia.
Maria akatulia na kuwasikiliza mbwa wabwekao nje, akaukamata mguu wa Zebu na kuutikisa kwa nguvu. “Wee, Zebu amka!” alisema kwa taharuki.
Zebu akajiinua kwa kushtuka na kukaa kitandani, akajaribu kuangalia chumbani kupitia mwanga hafifu wa kandili. “Unasemaje?” aliuliza.
“Unawasikia mbwa wanavyobweka huko nje?” Maria alisema. “Sijui kuna nini?”
“Agh, pengine wanaogopa upepo uvumao!” Zebu alijibu kwa sauti iliyoonyesha alikuwa hataki kuendelea kuizungumzia hoja hiyo zaidi ya ya kutaka kulala.
“Sijui nimwambie Jackie arudi ndani?” Maria alilalama peke yake.
Zebu akampuuza Maria. Akajilaza taratibu kitandani na kujifunika shuka gubigubi.
“Zebu! Zebu!” Maria akamwamsha tena Zebu.
Zebu akaghadhibika. “Unasemaje?” aliuliza kwa hasira isiyotaka karaha.
“Unasikia..? Unasikia?” Maria aliyekuwa amejiinua alisema huku akilitega sikio kusikiliza nje.
Ili kuonyesha kuwa anakerwa, Zebu alijigeuza upande wa pili kuelekea ukutani na kujikunja kama upinde huku akiirekebisha shuka aliyojifunika. Kisha asiseme lolote.
Ghafla, wakaisikia sauti ya mbwa anayenung’unika nje!
“Jackie huyo!” Maria alisema na kukurupuka kutoka kitandani.
Zebu akajigeuza kwa kasi na kuiondoa shuka usoni, akamwangalia Maria aliyekuwa ameshafika mlangoni akihangaika kufanya haraka ya kuufungua mlango.
“Wee Maria unakwenda wapi?” Zebu aliuliza.
“Naenda kumwingiza Jackie!” Maria alisema akiwa amekwishaufungua mlango wa chumbani na kutoka kwa kasi.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Zebu akaugeuza uso wake na kugeukia tena ukutani, akaivuta shuka usoni na kufumba macho. Akamsikia Maria akihangaika kuufungua mlango wa mbele wa nyumba. Maria na mbwa wake! aliwaza. Ghafla hali ya kuendelea kulala ikamwondoka. Akaiondoa shuka maungoni mwake kwa kuiweka pembeni, kisha akajiinua na kujisogea. Akaishusha miguu yake kutoka kitandani na kukanyaga chini. Akatulia palepale alipokaa na kumsikilizia Maria kama angeita kutoka nje.
“Yesu nakufaaa!” sauti kali ya Maria ilisikika ikipiga yowe kutoka nje. Kisha kukawa kimya!
Zebu aliinuka kwa taharuki kutoka kitandani alipokuwa amekaa kama aliyechomwa na sindano kwenye makalio bila ya kutarajia. Aliposimama, akaganda kama sanamu, kisha akarudi tena kukaa, lakini kwa kasi. Akaanza kutetemeka kwa hofu. Ghafla, akaanza kupiga kelele za kuomba msaada.
Wakazi wenzake wa nyumba hiyo waliamka, mmoja akatoka na panga mkononi, wakaenda chumba alichokuwemo Zebu na kumkuta akiwa amekaa kitandani, amejikunyata huku akilia peke yake.
“Vipi?” waliowahi kuingia walimuuliza.
“Mfuateni Maria, yuko nje!” Zebu alisema akiwa ametaharuki.
“Amefanya nini?” mmoja aliuliza.
“Kwani hamkumsikia?” Maria alisema kwa sauti yenye kilio.
“Mimi nimesikia sauti ya mwanamke huko nje, lakini sikujua kama ni ya Maria!” aliyekuwa amekamata panga alisema.
“Umemsikia akisema nini?” mwingine aliuliza.
Kabla ya aliyekamata panga hajajibu, Zebu akasema, “Alikuwa amemfuata mbwa wake…” akashindwa kuendelea kusimulia, akawa analia.
Wanaume wakatoka nje na kuwaacha akinamama chumbani kwa Zebu, wakimbembeleza.
Huko nje, wanaume waliotoka kwenye nyumba hiyo walimkuta Maria amelala ardhini, ingawa kulikuwa na kiza, lakini jinsi alivyokuwa amelala, alionekana kutotikisa sehemu yoyote ya mwili wake. Majirani walioamka, nao wakajiunga kumzunguka Maria huku kila mmoja akitaka kujua kilichotokea.
“Mbebeni mumwingize ndani!” mtu mmoja kutoka nyumba anayoishi Maria alisema.
Wakakubaliana kumwingiza ndani.
‘Mshike vizuri huko kichwani!” sauti za kuhimizana zikawa zinasikika wakati wa kumwinua Maria. “Na nyie inueni kwenye miguu!”
“Haya, wewe wa mbele tangulia kuingia ndani!”
Mwili wa Maria ukaingizwa ndani na kulazwa ukumbini huku wengine wakiagiza taa iletwe haraka kwa ajili ya mwanga. Taa za kandili zaidi ya moja zikaletwa, wakammulika Maria aliyekuwa amelazwa chali.
“Yesu wangu!” mmoja wa waliomwingiza Maria alisema baada ya kumwona vizuri kutokana na mwanga wa taa.
“Haa!” mwingine alishangaa huku akimwangalia Maria. “Anatoka damu puani, mdomoni na masikioni!”
Mwingine aliyemwona vizuri Maria alijikuta akiwa na kigugumizi na kushindwa kuongea lolote. Huku mikono yake ikitetemeka, alipiga alama ya Msalaba kifuani, kisha akawapangua watu waliokuwepo hapo na kutoka nje kwa kasi kama mtu aliyekuwa akisikia kichefuchefu. Alipotoka tu nje, watu waliokuwa nje ambao walishindwa kuingia wakamuuliza, “Tuambie, kuna nini?” baadhi yao wakianza kumzunguka.
Akionekana kama akili yake haijakaa sawa, mtu huyo akawaangalia waliomuuliza kwa mtazamo wa mtu aliyezubaa.
“Tuambie kuna nini?” watu waliomzonga walimsihi awaeleze.
“Maria…Maria..!” mtu huyo alisema na kuonekana kusita.
“Maria amefanya nini?” aliulizwa kwa jazba.
“Amekufa!”
“Eti nini?” sauti za kutaharuki zikajitokeza.
Akionekana kuhema kwa nguvu kwa sababu isiyoeleweka, mtu huyo akasema, “Amekufa kama alivyokufa baba Sai!”
*******
KIFUNIKO kilichokuwa kimefunika kitako cha kalamu, kilianza kuathirika baada ya kutafunwa na meno ya Sajini Seba aliyekuwa amekaa ndani ya ofisi ya kituo cha polisi cha mjini Zebati. Kwa dakika kadhaa alikuwa akijaribu kukariri kwa utulivu mahojiano aliyoyafanya na Zebu asubuhi hiyo baada ya kuarifiwa kifo cha Maria.
“Unasema Maria alianza kushikwa na woga muda mfupi kabla ya kifo chake?” Seba alikumbuka sehemu ya maswali aliyomuuliza Zebu.
“Ndiyo. Lakini pia, alitaka kujua kama na mimi nilikuwa nikihisi hali hiyo ya woga kama aliokuwa nao yeye,” Zebu alijibu. “Alisema anausikia mwili wake ukizizima na nywele kumsimama.”
“Alikwambia ni kitu gani kilichomfanya awe na hali hiyo ya woga?”
“Hakuniambia, lakini ni wazi ilitokana na hali ya upepo mkali uliokuwa ukivuma kwa nguvu usiku. Hata mimi hali hiyo ilinitisha!”
“Na wewe pia mwili ulikuzizima na nywele kukusimama?”
“Hapana. Woga wangu mimi ulihofia paa la nyumba kung’olewa na upepo. Lakini yeye alipatwa na woga baada ya kumsikia mbwa wake akibweka nje.”
“Kwa hiyo woga wake ulikuwa wa kumwonea huruma mbwa wake?”
“Siwezi nikasema hivyo, lakini baada ya kumkemea mbwa wake na kumtaka arudi ndani, ndipo alipotoa madai hayo ya kuogopa.”
“Mbwa wake alirudi ndani baada ya kumkemea?”
“Hakurudi! Na ndiyo sababu alimfuata nje baada ya kumsikia akinung’unika!”
“Alinung’unika?”
“Ndiyo. Alinung’unika.”
“Alipigwa?”
“Sidhani. Alinung’unika kama aliyekuwa akiogopa kitu.”
“Mlitoka pamoja?”
“Alitoka peke yake.”
“Baada ya Maria kukutwa ameanguka huko nje, mbwa wake alipatikana?”
“Hajaonekana mpaka leo!”
Hayo yalikuwa sehemu ya mahojiano yake na Zeba. Lakini pia, Seba alikumbuka baada ya kumhoji Zeba, akaomba aitiwe Marko ambaye ni mwenye nyumba anayoishi Zeba, naye akiwa ni mmoja wa mashuhuda waliotoka nje na kumkuta Maria ameanguka.
“Ulikuwa ni mmoja wa watu waliotangulia kutoka nje?” hiyo nayo ilikuwa ni sehemu ya maswali aliyomhoji Marko.
“Ndiyo,” Marko alijibu.
“Mlipofika nje mkawa mmeona nini?”
“Tulimwona Maria amelala ardhini, tukamfuata. Tukamwingiza ndani na kummulika na taa, tukamwona akitokwa na damu za puani, masikioni na mdomoni akiwa amekwishafariki!”
“Zaidi ya Maria, kipi kingine mlichokiona huko nje?”
“Hatukuona chochote kingine.”
“Kulikuwa na alama zozote kuonyesha palikuwa na vurugu yoyote?”
“Hakukuwa na kitu kama hicho ingawa eneo lenyewe lilikuwa na kiza.”
“Mlivyomkuta nje Maria kabla ya kumuingiza ndani, alikuwa bado hai?”
“Nadhani alikuwa tayari amekufa, kwani tulijaribu kumwita jina lake na kumwinua, lakini hakuonyesha dalili yoyote ya uhai.”
“Mlimkuta na nani?”
“Alikuwa peke yake.”
“Kipi kingine mlichokishuhudia wakati mlipotoka nje?”
“Hakuna.”
“Mazingira ya nje yalikuwaje mlivyomkuta Maria ameanguka?”
“Kulikuwa na upepo mwingi, ingawa ulikuwa umeanza kupungua.”
“Unadhani ni nini kilichomuua Maria?”
“Sijui!”
“Ulikuwa ni mmoja uliyekwenda kumzika baba Sai?”
“Ndiyo.”
“Kifo chake ulisikia kilivyomtokea?”
“Ndiyo.”
“Unadhani kina tofauti na hiki cha Maria?”
“Vinafanana!”
“Unadhani ni kwa nini kumetokea vifo vinavyofanana?”
“Sijui!”
“Wakati mlipotoka nje kwa ajili ya kumwendea Maria, eneo alilokuwa amelala Maria, kulikuwa na dalili yoyote ya kuwepo kwa moshi au ukungu?”
Seba akagundua, swali hilo lilikuwa limemshitua Marko.
Marko hakufanya haraka kujibu. Alionekana kusita na kuwa kama mtu aliyekuwa akijipa hadhari na swali aliloulizwa. “Sidhani…” alianza kusema, lakini akapewa ishara ya mkono kuzuiwa kuendelea kuzungumza.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Nataka uzirudishe vizuri kumbukumbu zako!” Seba alisema huku akionekana kuwa makini.
Marko akajikita kwenye tafakuri huku akiangaliwa na Seba. Akahisi Seba alikuwa akiyasoma mawazo yake.
“Uliuona moshi?” Seba aliuliza ghafla kama aliyekuwa na uhakika kuwa, Marko aliliona tukio hilo. “Au sivyo?”
“Ndiyo niliuona!” Marko alikiri.
“Na ulikuwa ukijua, hata kifo cha baba Sai kulitokea kitu kama hicho?”
“Ndiyo nilikuwa najua!”
“Wenzako uliotoka nao, pia waliuona moshi?”
“Ndiyo waliuona.”
“Nao walisemaje?”
“Hakuna aliyejiingiza kwenye mjadala huo.”
“Ulijuaje kama wameuona halafu hakuna kati yenu aliyelizungumza hilo?”
“Tulinong’onezana kama kupeana hadhari, lakini baada ya hapo hakuna aliyetaka kulizungumza.”
“Kwa nini?”
“Imani imeishaingia kuwa, kulizungumzia tukio la kuona moshi ni sawa na kujitabiria kifo chako!”
“Unaamini vifo hivi vinatokana na nguvu ya giza?”
“Kitu kama hicho!”
Akiwa peke yake ofisini, Sajini Seba aliitoa kalamu mdomoni na kuigonga-gonga juu ya meza. Mzunguko mzima wa mahojiano yake na watu hao ulimuweka kwenye njiapanda. Hakuona mantiki ya uwepo wa moshi au ukungu na kuvihusisha na vifo hivyo. Pamoja na kutoiona mantiki hiyo, lakini alikiri vitu hivyo vimeonekana kwenye matukio ya vifo vyote viwili. Akazivuta fikra zake kujaribu kukumbuka kama ukungu au moshi unaweza kusababisha kifo kwa mtu. Akakumbuka kuwa ipo baadhi ya miti ikichomwa, moshi wake huwa ni sumu na mtu akiivuta hewa hiyo ya moshi kwa muda mrefu anakufa. Lakini si kwa kutokwa na damu puani, mdomoni na masikioni! alijijibu.
Seba aliirudisha kalamu mdomoni na kuanza kukitafuna tena kifuniko cha kalamu. Maeneo yote waliyofia baba Sai na Maria, hakukuwa na moto wowote uliokuwa ukiwaka! aliwaza. Lakini hata kama ungekuwa ni moshi wenye sumu, kwa nini usingewadhuru na hao wengine waliofika pale? Japo kwa kukohoa tu! Kwa hiyo siyo moshi? Sasa ni nini kilichowaua na kuwafanya watokwe damu puani na masikioni? Kuna utata katika vifo hivi!
*******
KUFANANA kwa kifo cha baba Sai na Maria kukazidi kuwashitua wakazi wa Zebati. Likawa ni gumzo kwenye kila kona, hofu ya kuwa kisiwa chao kimeingiliwa na majini ikaanza kutawala kwa kasi. Msafara uliokuwa ukirudi kutoka makaburini kumzika Maria, waliizungumzia hofu hiyo njia nzima hadi majumbani mwao! Hisia zenye woga zikasambaa kwa kasi kwenye kila familia na kila kaya. Minong’ono ya kutafuta kinga ili wasikumbwe na janga hilo ikaanza kusikika. Wengine wakaenda mbali zaidi kutaka tambiko la haraka lifanywe! Baadhi yao wakapanga kwenda kulizungumza hilo wakati wa usiku kwenye kulalia matanga nyumbani kwa akina Maria, lakini pia ikapangwa hata nyumbani kwa baba Sai ambako matanga yanaendelea, nako kukazungumzwe hilo!
Kwa baba Sai ikawa ni matanga ya pili, lakini kwa Maria ikawa ni siku ya kwanza ya matanga. Wingi wa watu ukaegemea kwenda nyumbani kwa akina Maria. Kamati maalumu ikashinikizwa iundwe kwenye matanga hayo ambayo ingehakikisha tambiko na mazindiko yanafanyika baada ya siku tatu za kufunga tanga. Shinikizo hilo likazua mtafaruku usiotarajiwa wa kupingana na kutoelewana. Makundi mawili yakazuka, hoja zenye hisia kali zikawa zinatolewa kwa nguvu zote kwa kila kundi kupinga jingine.
Kundi la kwanza lilikuwa ni la mchanganyiko ambao ni waumini wa kwenda kanisani, wakiungana na wale ambao si waumini wa kanisani lakini wenye imani ya ukristu. Kundi hili ndilo lililokuwa likishinikiza kuamini imani za kishirikina na kutaka matambiko na mazindiko yafanywe kwa haraka kisiwani humo kabla maafa mengine zaidi kuendelea. Kundi la pili, ni la wazee wa kanisa na waumini, wao walizipinga kwa nguvu zote hoja hizo zenye mwelekeo wa kishirikina. Wao walitaka kufanyike sala ya maombi maalumu kupitia kwa Bikira Maria, kuomba kuepusha maafa kwenye kisiwa hicho.
Mzozo huo ukaanza kujengeana chuki kwa makundi hayo mawili na taarifa za mzozo huo zikasambaa hadi kwenye matanga ya baba Sai ambako nako tafrani ya kutoelewana ikaanza ghafla. Hata hivyo, busara zikalazimishwa kuingizwa ili kuepusha ugomvi. Makubaliano yakafanyika kwa sehemu zote mbili zenye matanga kuwa, kila upande ufanye subira hadi asubuhi ifike na kikao maalumu kiitishwe.
Huku hayo yakiendelea, mtu mwingine aliyekuwa akipambana na utata wa vifo hivyo kwa mtazamo wake mwenyewe alikuwa mzee Robert. Yeye alijikuta kwenye shinikizo lililoendelea kumpa wakati mgumu kifikra. Hakuamini kifo cha baba Sai na Maria vilitokana na imani za kishirikina kama wakazi walivyokuwa wakidai, lakini pia alipata wakati mgumu kukiri kuwa, vifo hivyo ni maafa yaliyotabiriwa kwenye ubashiri wa kale ulioelezea ujio wa Msalaba Mtakatifu!
Ndoto aliyoiota ilikuwa ikiendelea kumtesa! Kauli ya Padri Toni kuhusu tukio la kuvunjwa kwa dirisha la kanisa ilidhihirisha kuwa, ndoto aliyoiota ilikuwa na ukweli na alitakiwa akiri mbele ya kasisi huyo kuwa, tukio la kuvunjwa kwa dirisha lilikuwa ni tukio alilooteshwa kabla! Lakini alishindwa kukiri kwa sababu moja tu, ni kuhusishwa kwa Mathias kwenye ndoto hiyo! Laiti ndoto hiyo isingemhusisha mjukuu wake huyo, mzee Robert angeweza kujitokeza mbele mle kanisani wakati wakiusalia mwili wa baba Sai, pale Padri Toni alipoomba mtu aliyelivunja dirisha hilo ajitokeze. Pale ndiyo pangekuwa nafasi yake ya kukiri! Ingekuwa ni nafasi ya kuieleza kadamnasi iliyokuwepo pale kuwa, tukio la kuvunjwa dirisha la kanisa, yeye alikwishaoteshwa kabla, kuwa lingevunjwa! Lakini hakufanya hivyo! Angefanya hivyo angemtia mjukuu wake kwenye aibu ambayo ingeonekana ndiyo sababu ya kutoweka kwake! Ili kumlinda mjukuu, mzee Robert alijikuta akifanya uamuzi wa ubinafsi wa kukaa nayo siri hiyo ili asubiri hadi hapo Mathias atakapoonekana!
Saa chache baada ya kuupitisha uamuzi huo, maafa mengine yakatokea; kifo cha Maria! Kifo chake kikafanana na kile cha baba Sai! Tukio hilo likafanya nafsi yake imsute, kuwa ni yeye pekee aliyekuwa akijua sababu ya maafa hayo, lakini aliendelea kukaa kimya! Pamoja na kukiri ni yeye ndiye mwenye kuijua siri ya maafa yanayotokea, lakini pia, kule kuendelea kwa maafa hayo huku Msalaba Mtakatifu ukiendelea kuwepo kanisani, nako kulimchanganya! Uko wapi uwezo wa Msalaba Mtakatifu kuzuia maafa yaliyotabiriwa? alijiuliza. Ziko wapi nguvu zake? Kwa nini unaendelea kuwepo pale huku dalili za maafa zikianza kujitokeza? Nguvu za Bikira Maria zilizotabiriwa ziko wapi? Utabiri unasema, hadi Msalaba Mtakatifu utakapoibwa ndipo maafa yatakapotokea, vipi leo maafa yanatokea huku Msalaba Mtakatifu ungalipo?
Lakini kwa upande wa pili wa nafsi yake, kulikuwa na kitu kilichokuwa kikimwambia, ‘Kuna siri hujaigundua!’ Na kila alivyokuwa akipanga na kupangua, alijikuta akishindwa kukitegua kitendawili hicho kilichomtega! Kwa nini aote ndoto, akimwona mjukuu wake kwa kushirikiana na wenzake wakivunja dirisha, kisha mjukuu wake huyo atoweke saa chache baada ya kuiota ndoto hiyo? Kwa nini matukio yaliyokuwemo kwenye ndoto yaje yajitokeze, kama vile dirisha la kanisa kuvunjwa, lakini pia ndoto hiyo alipoiota ilimbashiria kuwa, dhamira ya Mathias na wenzake ilikuwa kuiba Msalaba Mtakatifu, tukio ambalo alikwenda kulipeleleza na kuushuhudia Msalaba Mtakatifu ukiwa ungalipo kanisani, vipi tena kuwe na maafa ya vimbunga na watu kuuawa kwa aina moja ya mauaji?
********
ILIKUWA kama ngoma inayomfanyia kelele wakati wote. Mzee Robert alikosa utulivu kichwani mwake, kila wakati alijikuta akiitafakari hali inayoikumba kisiwa hicho, kisiwa kilichosifika kwa amani iliyotokana na usimikwaji wa Msalaba Mtakatifu uliotokana na Mtakatifu Bikira Maria. Aliziwazia siku mbili zilizokuwa na upepo mkali uliokipiga kisiwa hicho. Alishangazwa na hali ya upepo huo ambao kila ukija na kuondoka, lazima uondoke kwa kuua mtu! Aliviwazia vifo vya baba Sai na Maria, vifo vilivyofanana kwa wote kuuawa kwa aina moja ya mauaji yanayosababisha kutokwa na damu puani, masikioni na mdomoni bila ya kuwepo jeraha lolote! Kwa nini wafe vifo vya aina hiyo? Kuna muuaji mmoja? Kwa nini vifo vyao vitanguliwe na upepo mkali? Na kwa nini upepo huo utokee usiku tu? Muuaji hataki kuonekana? Na kwa nini mifugo ilikuwa ikilia kwa hofu kila upepo huo ulipokuwa ukivuma?
Yeye ni mmoja kati ya watu wanaoamini kuwa, baadhi ya wanyama au ndege wana uwezo wa kuona viumbe ambao binadamu hawezi kuwaona kwa macho, lakini pia inakubalika, viumbe wa aina hiyo huwa ni adui kwa binadamu, na anavyoua, uuaji wake lazima uhusishwe na damu! Wazo hilo likamfanya ashawishike kuwa, kule kulia kwa bata nyumbani kwa baba Sai kabla ya kifo chake, na kule kubweka kwa mbwa wa Maria kabla ya kifo cha Maria, huenda mbwa na bata hao waliweza kumwona muuaji aliyetoa roho ya baba Sai na Maria! Majini!CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Mzee Robert aliwafikiria viumbe hao ambao baadhi ya binadamu wanaamini wapo. Akajiuliza, je, hayo ndiyo maafa yaliyotabiriwa enzi za Bikira Maria kukikumba kisiwa hicho? Na kwa nini yawe majini? Alikiri kuwa, viumbe kama majini hukubalika na baadhi ya binadamu kupitia imani zaidi, lakini wapo watu wasioiamini imani hiyo! Kwake yeye hakuwahi kuona sehemu kwenye Biblia inayodai Bikira Maria au nabii yeyote, kwa wakati huo wa manabii kuanzia Yesu na wengine, aliyewahi kupambana kwa shari au kwa amani na viumbe hawa wanaoitwa majini! Pamoja na Biblia kuwataja pepo wabaya kwenye maandiko yake, hata hivyo, mzee Robert alikataa kukiri tafsiri ya pepo wabaya ingekuwa ni majini!
Kwa uelewa wake, ndani ya Biblia maafa hutabirika kuwa, kama vile magonjwa, vimbunga vikali, matetemeko ya ardhi, mafuriko, moto na matufani yatokayo baharini na kadhalika, lakini siyo majini! Ni majanga yanayoonekana kwa macho, ambayo hujeruhi, kutia hasara za mali na kuua! Yote hayo yanaonekana kwa macho! Vipi vifo vya baba Sai na Maria, muuaji asionekane? Vipi huu ubashiri, mbona hauendani na Biblia? Au vifo vya baba Sai na Maria ni kweli vinatokana na imani za kijini zenye unasaba na ushirikina kama baadhi wakazi wanavyodai? Lakini, hata kama ni majini, ndiyo iwe sababu ya nguvu za Msalaba Mtakatifu zishindwe kuyazuia majini hayo? Hapana! mzee Robert alijijibu mwenyewe. Utakatifu wa Bikira Maria una nguvu zaidi ya uchawi! Imani za majini ni sehemu ya ushirikina ambao Kanisa Katoliki inazipinga, kwa sababu kanisa linaamini njia moja ya kumwamini Mungu! Baba Sai na Maria, wote walikuwa waumini wazuri wa kanisa, kwa nini vifo vyao vionekane kishirikina? Nguvu ya Msalaba Mtakatifu imepotelea wapi? Na kwa nini Mathias atoweke?
Lazima niutafute ukweli! mzee Robert alijiambia moyoni.
Akapanga kwenda kumwona mlinzi aliyekuwa akililinda kanisa wakati dirisha lilipovunjwa!
*****
ALIFIKA kanisani na kukutana na Padri Toni, wakatumia dakika kadhaa kuzungumzia mtafaruku wa kiimani uliotokea kwenye matanga ya Maria na baba Sai na kuendelea hadi asubuhi bila kufikiwa mwafaka kuhusu hatima ya kisiwa hicho. Lakini pia, wakazungumzia vifo vya baba Sai na Maria vilivyokwamisha zoezi la kuendelea kumtafuta Mathias.
“Kwa kuwa leo ni tanga la tatu kwa baba Sai na la pili kwa Maria, nadhani kesho baadhi ya wakazi wataanza tena kumtafuta Mathias,” Padri Toni alisema.
Maongezi hayo yakamvutia kumpa ushawishi mzee Robert kutaka kukiri mbele ya Padri Toni kuwa, aliota ndoto yenye utata. Lakini akapata kigugumizi baada ya akili yake kumpa hadhari kuwa, kitendo hicho kingemuingiza Mathias kwenye matatizo na kanisa. Akamuaga Padri kwa kumwambia anataka kuonana na mlinzi wa kanisa kwa shida zake binafsi. Padri Toni akamsindikiza mzee Robert hadi mlangoni, wakapeana mikono ya kuagana.
Alimkuta mlinzi akiwa kwenye lindo lake na kusalimiana naye.
“Nataka kukuuliza kuhusu mjukuu wangu Mathias,” mzee Robert alimwambia mlinzi. “Kabla ya Mathias kupotea, unakumbuka ulimwona lini kwa mara ya mwisho?”
“Tulionana jioni ya siku ya nyuma yake, lakini hatukuzungumza lolote zaidi ya kusalimiana.”
“Baada ya hapo hamkuonana tena?”
“Baada ya hapo si nikasikia amepotea! Sikuamini! Mathias atapotelea wapi hapa kisiwani? Sijui mmefikia wapi hadi sasa?”
Mzee Robert alimwangalia mlinzi alivyokuwa akizungumza bila ya kuonyesha shaka. Akaamini alikuwa hasemi uongo.
“Huenda kesho zoezi la kumtafuta likaanza tena upya,” mzee Robert alisema.
“Nina imani kwa uwezo wa Yesu, atapatikana akiwa salama.”
“Naamini itakuwa hivyo,” mzee Robert alisema kisha alijikuna kichwani. “Vipi aliyevunja dirisha la kanisa, bado hajajitokeza?” aliuliza ghafla.
“Hakuna aliyejitokeza hadi sasa,” mlinzi alijibu kwa utulivu.
“Kwa mtazamo wako, unaamini lilivunjwa na mtu?”
“Kwa jinsi lilivyovunjika, ni dhahiri lilivunjwa na mtu!”
Kama angekuwa amemwona aliyelivunja, kamwe asingesema hivi! mzee Robert aliwaza. Akaamua kuaga.
Mathias atakuwa yuko wapi? mzee Robert alijiuliza wakati akirudi nyumbani. Kwa mara ya kwanza alijikuta akiingiwa na hofu baada ya kuingiwa na wazo jipya asilolitarajia pale alipowaza, huenda upoteaji aliopotea Mathias, nao upo kwenye mazingira ya utata, kama vifo vya baba Sai, Maria!
********
USIKU wa tanga la pili nyumbani kwa akina Maria, kikundi cha kwaya kilichokuwa kikiimba tenzi za rohoni kiliwajumuisha watu waliokuwepo matangani kuimba pamoja kwa sauti ya juu. Ilipofika saa sita, ari ya uimbaji ilianza kupotea baada ya washiriki kujipunguza kwa kuamua kulala. Ilipofika saa nane, kwaya ikashindwa kuendelea kuimba kutokana na upepo ulioanza kuvuma. Hatimaye miti ikaanza kutoa sauti za kuyumbishwa na upepo. Hali hiyo ya hewa ikaanza kuleta hofu kwa kikundi kile cha kwaya ambacho washiriki wake wote walikuwa macho, lakini hata wale waliokuwa wamepitiwa na usingizi walianza kupoteza usingizi na wengine wakaamua kujiinua na kukaa.
Harufu ya bahari ikawa inasikika kwa nguvu, mawimbi yake yakapiga kwa sauti kubwa. Kila mtu aliyekuwepo pale akawa anaisikilizia kwa makini hali hiyo inavyoendelea. Upepo ukazidi kuvuma kwa nguvu na kuonekana ni kimbunga. Hofu iliyoanza kuzoeleka kwa wakazi na baadhi yao wakiwepo hapo matangani, wote wakawa wanajua, hali kama hiyo inapotokea, huwa ni dalili ya mauti kwa mtu!
Mbwa wakawa wa kwanza kubweka, bweko hizo zikaleta hofu miongoni mwao baada ya kuingiwa na kumbukumbu ya vifo vya baba Sai na Maria, kwa kuwa dalili zilianzia kwa mbwa kubweka. Wazo la kufanya sala likawaingia. Sala ya kuomba nguvu za Yesu zitumike kuiangamiza hali hiyo ikaombwa huku baadhi yao wakikamata Biblia mikononi mwao wakati aliyechaguliwa kuiongoza sala hiyo akiendelea kuomba kwa nguvu. Kadri sala ilivyokuwa ikiombwa kwa nguvu, hofu nayo ikazidi kujikita miongoni mwao. Wakaanza kubanana na kuwa karibu kama sehemu yao ya kujikinga.
“Mbwa wamekwishaanza kuwaona!” kijana mmoja aliyekuwa amejibana na wenzake kwenye jamvi aliongea.
“Kuwaona akina nani?” mwingine aliyekuwa karibu alihoji kauli ya kijana huyo.
“Si unajua mbwa ana uwezo wa kuona aina yeyote ya Shetani!” kijana aliyesema mwanzo alijibu.
“Wewe unaamini?” mwingine alidakia kuuliza.
“Kwa nini nisiamini wakati imeandikwa hata kwenye Biblia kuwa Shetani yupo!”
‘Kwa hiyo unaamini kubweka kwa mbwa ni kwa ajili ya kuwaona shetani?”
“Ndiyo.”
“Msalaba Mtakatifu na mbwa unaamini kipi?”
“Nauamini msalaba.”CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Kwa hiyo mbwa wanaweze kuwaona shetani, lakini Msalaba Mtakatifu ukashindwa kuwazuia?”
“Hilo mimi siwezi kukujibu, lakini nataka tuizungumzie hii hali inayoendelea hapa Zebati. Au wewe unaviona vifo vya baba Sai na Maria havina nasaba na upepo wa aina hii?”
“Siamini! Siamini kwa sababu nauamini Msalaba Mtakatifu, laiti mambo unayoyasema kama yangekuwepo, basi yangeshindwa kwa nguvu ya Msalaba Mtakatifu.”
Mwingine akadakia, “Ni bora lifanyike tu, tambiko. Pepo mbaya ameingia kisiwani petu.”
“Wala siyo pepo mbaya,” mwingine akaingilia. “Hapa kisiwani kuna mchawi aliyeingia na anajaribu nguvu ya uchawi wake. Haiwezekani baba Sai na Maria wote wafe kwa aina moja ya kifo…”
“Kanisa linakataza kuamini uchawi,” mmoja alionya.
“Sasa wewe unafikiri ni nini kinachotokea hapa Zebati kama siyo kutupiana majini?”
“Hivi nyie mnabishania nini?” mmoja ambaye muda wote alikuwa kimya akiusikiliza ubishi huo, aliamua kuingilia kati. “Upepo si ndiyo umeanza kuvuma?”
Baadhi yao wakaitikia.
“Na mbwa nao si wameanza kubweka?” baada ya kuitikiwa akaendelea, “Basi tusubiri kama kutatokea mtu mwingine atakayekufa kwa staili hii ya kutokwa na damu puani na masikioni.”
“Na kama ikitokea kuwa hivyo?”
“Hapo tutakuwa tumepata jibu.”
“Kuwa?”
“Kuna ushirikina unaofanyika wa kuua watu!”
Wote wakakubaliana kusubiri upepo unaoendelea kuvuma utaishia na tukio gani.
Wapo walioamua kuendelea na maombi, lakini wengine waliokuwa na hofu iliyopitiliza waliamua kuifuatilia hali hiyo. Baadhi yao wakaiona miali ya radi ikimulika eneo la makaburi ya zamani.
“Mnajua, tokea juzi naiona hali fulani ambayo nashindwa kuielewa,” mmoja alisema.
“Hali gani?” aliyekuwa amekaa naye jirani aliuliza.
“Angalia kule kwenye makaburi ya zamani.”
Walioyasikia mazungumzo yale wakageuza nyuso zao kuangalia upande ulipo makaburi ya zamani.
“Kila hali hii inapoanza,” aliendelea yule mtu. “Eneo la makaburi ya zamani huwa kunapiga radi, lakini mpaka leo hakuna mvua yoyote iliyonyesha!”
“Sasa kipi cha ajabu? Au kwa sababu umeiona radi inapiga kwenye eneo la makaburi ya zamani na tayari umeanza kuwa na imani za kishirikina?”
“Sina maana hiyo, bali najaribu kuizungumzia hali halisi iliyojitokeza.”
“Kwa hiyo unatabiri nini?”
“Ni hali ambayo haijawahi kutokea hapa kisiwani.”
“Una uhakika gani kama haijawahi kutokea?”
“Kwa sababu sijawahi kuiona.”
“Huna cha maana cha kutueleza!”
Mjadala wao ukaishia hapo.
Upepo uliokuwa ukivuma ukaanza kupungua na hatimaye kuacha kabisa, lakini cha ajabu, mbwa waliendelea kubweka. Kuacha kuvuma kwa upepo kukawafanya baadhi ya waliokuwepo pale matangani waanze kuwabeza wale walioonekana kuwa na imani za kishirikina, hata hivyo mjadala huo haukuendelea kwa muda mrefu, kila mmoja akajikunjia upande wake kuutafuta usingizi.
********
WAPO waliokoroma usingizini na wapo waliokuwa hawatulii sehemu moja kutokana na kujigeuzageuza kama waliopatwa na ndoto mbaya. Wapo waliokosa kulala vizuri kutokana na karaha ya mikoromo wanayoisikia. Mmoja wa waliokosa usingizi kutokana na bughudha ya watu kukoroma alijikuta ameshikwa na haja ndogo. Ili kuiondoa karaha ya kuukosa usingizi, aliona aitumie nafasi hiyo kwenda kujisaidia. Akiwa anawasikia mbwa wakiendelea kubweka, aliangaza macho yake kwenye maeneo ya jirani ili kuangalia kama kungekuwepo na kichochoro ambacho kingemfaa kwenda kujisaidia. Akaridhishwa na eneo aliloona linamfaa. Akajiinua, lakini kabla hajasimama, akarudi tena kukaa. Machale yalimcheza! Akausitisha uamuzi wa kwenda kujisaidia baada ya kuyakumbuka mazungumzo ya awali yaliyozungumzia uwezekano wa mtu kufa usiku huo! Wazo hilo likawa limemwingizia woga na kujikuta akifanya uamuzi wa kuendelea kuvumilia kukaa na haja yake hadi asubuhi!
Akajizuia kwa takriban nusu saa, lakini kwa kuwa mara kwa mara akili yake ilikuwa ikitafakari kujizuia kwenda kujisaidia, ikasababisha kadri alivyokuwa akijizuia, ndivyo kibofu chake kikawa kinazidiwa na maumivu. Ukisikia mtu anapasuka kibofu kirahisi ni kutokana na uamuzi wa kijinga kama huu! aliwaza. Hali hiyo ikaendelea kuyafanya mawazo yake yashindwe kuwazia jambo jingine lolote zaidi ya kuyasikilizia maumivu ya kibofu yanayomwendesha. Hatimaye akakiri anajiumiza kwa woga wa kipumbavu, lakini pia akajicheka ujinga. Mwanamume mzima unajitesa kwa ajili ya longolongo za matangani! Ghafla akajipa ujasiri wa kujitambua yeye ni mwanamume, hapaswi kuwa mwoga kama mwanamke! Akafanya uamuzi aliouona unalingana na ujasiri anaojipa. Akaitupa kando shuka aliyojifunika. Liwalo na liwe, siwezi kuvumilia kukaa na mkojo. Nikifa? alijiuliza huku akisimama.
Baada ya kusimama, akaamua kufanya subira ambayo kwake aliiona ni ya kiintelejensia. Akaliangalia kwa makini eneo analotaka kwenda ili kuhakikisha kama usalama upo. Akaiona hali ni tulivu, lakini ukimya uliokuwa umejikita eneo hilo ukamtia mashaka. Akajiona kama anayetaka kuuendekeza woga. Akajilazimisha kuupangua kwa nguvu zote. Akafanya uamuzi wa kuiruka shuka iliyokuwa nyayoni mwa miguu yake. Akaelekea kwenye kichochoro alichokikusudia huku akiuhisi mkojo unataka kumtoka. Kabla ya kuwasili eneo alilopanga kujisaidia, mikono yake ikawahi kuharakisha kufungua vishikizo vya mbele vya suruali. Mara, pasipo kutarajia kabla hata hajamaliza kufungua vifungo, akasikia sauti ya mwanamume ikitokea kichochoro cha ubavuni mwa nyumba ya jirani ikipiga kelele, “Nakufaa!”
Yowe la mtu huyo likamfanya bwana yule agande pale aliposimama, mikono yake iliyokuwa ikiharakia kufungua vishikizo vya suruali ikaishia ilipofikia bila ya kuendelea na zoezi hilo. Mwili ukamnyong’onyea na ubongo wake ukapata shambulizi la dharura la kupooza kutokana na woga, akashindwa kuusikia mkojo wake uliokuwa ukimtoka na kuchirizika ndani ya suruali na kulowanisha miguu yake.
Yowe hilo likawa limewashitua watu waliokuwepo hapo matangani, wakataharuki kwa pamoja huku wengine waliokuwa wamelala, baadhi yao walishituka na kusimama moja kwa moja tayari kwa kukimbia kama ingelazimu kufanya hivyo!
“Kelele zimetokea wapi?” watu walianza kuhoji wakiwa tayari wameamka kikamilifu.
“Kule!” yule bwana aliyejikojolea alisema huku kidole chake kikionyesha kwenye uchochoro ilipotokea sauti. Alikuwa akitetemeka mwili mzima kiasi kwamba miguu yake ilikuwa ikigongana yenyewe huku suruali yake imelowa haja ndogo.
Mkusanyiko wa watu waliojawa na taharuki wakaenda kwenye kichochoro walichoelekezwa, baadhi yao wakiwa wameshika silaha za mawe, magongo na wengine visu. Mwendo wao ukawa wa hadhari kama kwamba walikuwa wakimvizia wanayemfuata. Hatimaye wakamwona mtu aliyekuwa amelala katikati ya kichochoro hicho. Walipomkagua wakamtambua alikuwa ni mwenzao waliyekuwa naye matangani, na baadhi yao wakamtaja kwa jina! Mtu huyo alikuwa akitokwa na damu puani, masikioni na mdomoni huku ukungu uliokuwepo ukipotea taratibu!
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
********
MTU aliyefariki aliitwa Paulo, alikuwa mchuuzi wa samaki, lakini pia alikuwa mnywa pombe mzoefu. Wakazi wengi walimfahamu kwa mambo hayo mawili. Kifo chake kilileta mshituko mwingine kwa wakazi wa Zebati. Kwa mara ya kwanza ikaonekana hakuna jipya la kuelezea kuhusu kifo hicho kilivyotokea. Kila aliyeulizwa alijibu kwa mkato, “Naye amekufa kama alivyokufa baba Sai na Maria!” Lakini pia, kutokuwa na jipya kukaonekana kwa ujio wa Sajini Seba aliyefika hapo mapema asubuhi kwa ajili ya mahojiano na watu walioshuhudia kifo cha Paulo. Akapuuzwa!
“Kuja kwake kutasaidia nini?” watu walihoji kwa kukebehi.
“Kwani tokea alivyoanza kuchunguza vifo vya baba Sai na Maria ni nini cha maana alichogundua?” wengine waliendeleza kebehi. “Anafikiri haya mambo ni ya kipolisi? Inakuwaje baadhi ya watu wanajifanya kutoielewa hali halisi! Wanafikiri bila ya kufanyika mazinguo na makafara, maafa haya polisi watayazuia?”
Sajini akazisikia shutuma hizo, lakini akaendelea kufanya mahojiano na baadhi ya watu waliokuwepo kwenye matanga ya Maria waliokubali kutoa ushahidi. Hata hivyo, sababu ya kifo cha Paulo ilishabihiana na kifo cha baba Sai na Maria kwa kutokwa na damu puani, masikioni na mdomoni! Kisha ukungu!
Kwa mara nyingine akiwa ofisini kwake, Seba hakujikita tena na masuala hayo mawili ya uvujaji wa damu na uwepo wa ukungu. Safari hii alijikuta akigundua kitu kipya ambacho awali hakuwahi kukifikiria. Yalikuwa ni matamshi yaliyotolewa na marehemu wote muda mfupi kabla ya kifo kuwakuta. Wote walitamka kauli moja, ‘Nakufaa!’ Kwa nini wote waitamke kauli hiyo? alijiuliza. Walijua kuwa wanauawa? Ni nini kilichowajulisha hivyo? Kuna kitu walichokiona? Ni kiumbe? Kama siyo kiumbe, ni kipi walichokiona hadi watamke kuwa, wanakufa? Waliuona ukungu unaozungumzwa? Kama waliuona, waliuona kwa mtazamo wa kutisha? Au waliuona kama ukungu wa kawaida? Na kwa nini watishike? Maswali hayo yakamweka pagumu kuyapatia majibu yaliyoridhisha. Alikiri kila swali lilikuwa na uzito uliohitaji mchanganuo wenye mapana. Pamoja na kukosa majibu ambayo yangemwongoza kwenye kutatua kitendawili kilichopo, lakini Seba alikuwa na uhakika, marehemu wote watatu walishuhudia kukiona kitu kilichowatisha kabla ya vifo kuwakuta!
******
BAISKELI ilisimama nje ya Kanisa Kuu Katoliki kisiwani Zebati. Sajini Seba aliteremka akaelekea kwenye nyumba moja kubwa nzuri iliyopo kando ya kanisa na kugonga mlango wa mbao wenye rangi ya kawahia ulionakshiwa kwa dawa ya mbao iliyoung’arisha.
Mlango ulifunguliwa na Padri Toni aliyekuwa kwenye mavazi yake ya kila siku, kanzu na msalaba mkubwa uliokuwa kifuani pake. “Oh, karibu Seba,” alisema huku akitoa nafasi Sajini Seba apite.
“Nashukuru,” Sajini Seba alisema kwa unyenyekevu na kuingia ndani.
Walikwenda kukaa kwenye viti nadhifu vilivyokuwa sebuleni. Ilikuwa ni sebule nadhifu yenye samani za thamani zilizopendezesha kuta zote nne. Picha kubwa ya Yesu aliyesulubiwa msalabani ilikuwa imesimama juu ya meza iliyokuwa na nakshi na kufuatiwa na nyingine ya Bikira Maria ambayo kabla ya Seba kukaa, aliipigia magoti na kupiga alama ya msalaba kifuani pake.
Padri Tino mwenye umri wa miaka sabini na mitano, raia wa Italia, alikuwa ameshaishi kisiwani humo kwa zaidi ya miaka thelathini. Ni mrefu na mwembamba na muda mwingi alivaa miwani ya macho. Alikuwa ni kipenzi kikubwa cha wakazi wa Zebati kutokana na misaada mbalimbali iliyokuwa ikitoka Vatican na kuitawanyisha kwa wakazi wa kisiwa hicho. Pia alikuwa mbunifu wa miradi tofauti aliyoibuni kwa wakazi wa kisiwa hicho iliyowaongezea vipato. Sifa nyingine aliyojiongezea ni uwezo wa kumudu kuzungumza lugha ya wenyeji kwa ufasaha.
“Ipo kahawa na chai, utapendelea kimojawapo?” Padri Toni alimuuliza Seba.
“Nitapenda chai, ahsante,” Sajini alijibu.
Padri Toni akatoa agizo kwa mtumishi ili alete chai ya watu wawili.
“Ujio wako ni wa ghafla,” Padri alisema baada ya mtumishi kuondoka..
“Ni kweli, ujio wangu kwako ni wa ghafla,” Seba alisema huku akimwangalia Padri. “Kilichonileta ni matatizo yanayoendelea kisiwani petu. Hadi leo tumeshatokewa na vifo vitatu vyenye utata. Hali imeanza kuwa mbaya, sijui utata huu wa vifo utaendelea hadi lini?”
Padri Toni alijitikisa kujiweka vizuri kitini. “Hata mimi nipo kwenye mshangao na vifo hivi,” alisema. “Watu wanahamanika na kuingiwa na hofu kuu.”
Chai ikaletwa, wote wakahudumiwa.
“Kuna utata ndani ya vifo vyao,” Seba alisema baada ya kumeza funda la chai. “Mazingira ya vifo yanafanana. Wote wameuawa na kitu kisichojulikana, na wote walikufa kwa aina moja, kuvuja damu masikioni, mdomoni na puani. Isitoshe, sehemu zote ambazo vifo hivyo vimetokea, kulionekana ukungu. Ni tukio la ajabu! Hili jambo linaichanganya sana akili yangu…”
“Siyo wewe peke yako,” Padri Toni alimkatisha Seba. “Nasikia sasa wakazi wanataka kufanya makafara kwa kuomba mizimu yao.”
“Wakazi wamechanganyikiwa na wapo tayari kufanya lolote ambalo wanaliona litawasaidia kuwapa amani. Suluhisho waliloliona ni hilo la kufanya matambiko yatakayoandamana na makafara. Hawataki kusikia lolote jingine zaidi ya hilo!”
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment