IMEANDIKWA NA : BEKA MFAUME
*********************************************************************************
Simulizi : Msalaba Wa Dhahabu
Sehemu Ya Kwanza (1)
MIAKA 2OO ILIYOPITA
Kisiwa kidogo cha Zebati kilichopo kwenye Bahari ya Hindi chenye wakazi waumini wa dini ya Kikristu wa Kanisa Katoliki, kulikuwa na kanisa kubwa lililokuwa likihudumia wakazi wote wa kisiwa hicho. Ndani ya kanisa hilo, mbele ya altare kulikuwa na msalaba mkubwa wa dhahabu, Msalaba huo ulikuwa wa aina yake na ulipewa heshima ya aina yake! Uliitwa Msalaba Mtakatifu.
Historia ya ujio wa msalaba huo kanisani hapo ilikuwa ni ya kutatanisha. Wakazi wengi waliamini msalaba huo ulifika kwa maajabu ya Mtakatifu Bikira Maria, na ujio wake ulionwa kwa ushuhuda wa mlinzi aliyekuwa akililinda kanisa hilo. Historia ya tukio hilo ambalo haikuwekwa kimaandishi, bali ilikuja kwa maelezo ya wazee walioishi miaka hiyo inaeleza kuwa, ujio wa msalaba huo ulianzia wakati mlinzi huyo alipokuwa akililinda kanisa hilo wakati wa usiku na alikuwa akisinzia, aliposhituliwa na nuru ya mwanga mkali kutoka angani na kumulika eneo alilokuwepo na lile la kanisa. Alipoangalia juu akaona kitu kinachoogopesha kikitoa nuru ya dhahabu mfano wa moto wenye miali kikiwa kinaelea angani na kuwa kama nyota kubwa inayowaka. Kitu hicho kikawa kinateremka kwa kasi kuelekea alipokaa. Tukio hilo likamtia hofu, likamwogopesha, likamchanganya akili na hatimaye akapoteza fahamu.
Alipozinduka, akauona ule mwanga aliouona angani ukiwa upo ndani ya kanisa, akainuka kwa hofu na kuangalia kama kulikuwa na ongezeko la mtu au kiumbe kingine pale alipokuwepo, lakini kabla ya uhakiki wake kutimia, akakurupuka na kukimbia kulitoka eneo hilo! Lakini baada ya kukimbia hatua chache akapata ujasiri wa kugeuka nyuma kuliangalia kanisa. Kitendo hicho kikampa subira ya kutaka kujua kinachoendelea kanisani humo. Akaanza kurudi kwa hatua za kuvizia na kusikilizia. Akiwa ameinama na kukielekeza kichwa chake mbele, sikio lake likiwa tayari kunasa sauti yoyote itakayojitokeza na kujipanga rasmi kutimua mbio kama ikibidi, mlinzi huyo alitembea kwa mwendo wa kunyemelea, wenye dalili zote za woga kurudi kanisani na kuelekea dirishani.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Alipolifikia dirisha, akaanza kuchungulia kimachale kuangalia ndani huku akiwa makini kujiandaa kutoka mbio endapo kutajitokeza kitu kitakachomshitua. Nuru ya mwanga iliyokuwemo humo kanisani ambayo ilikuwa yenye rangi ya dhahabu, ilianza kujibadilisha na kugeuka kuwa ya fedha iliyong’aa kama theluji, ikitokea sehemu ilipo altare. Macho yake yakavutwa kuangalia eneo hilo la altare, akashituka alipouona msalaba, na baadaye akagundua msalaba anaouangalia hapo ndiyo kile kitu mfano wa nyota alichokiona angani.
Ghafla akaisikia sauti nene iliyofanya mwangwi ikimwambia, “Usiogope!”
Akaogopa! Akataka kugeuka kukimbia.
“Usikimbie!” sauti ikaonya.
Mlinzi akapigwa na bumbuazi.
Sauti ikaendelea, “Nenda ukawaambie waenezao neno la Bwana, wazisambaze habari hizi njema zilizokifikia kisiwa chenu kuwa kimebarikiwa. Na huu msalaba unaouona ni Msalaba Mtakatifu, ulioletwa kwa uwezo wa Mtakatifu Bikira Maria. Nguvu zake zilizomo kwenye msalaba huo zitalinda kisiwa chenu kisifikwe na balaa lililokuwa linakaribia kuwafikia!”
Hiyo ndiyo historia iliyoelezea ujio wa msalaba huo hapo kanisani. Lakini pia, ipo historia nyingine inayojaribu kuipinga historia ya tukio hilo ambayo haikukubaliwa na wengi inayoeleza kuwa, msalaba huo wa dhahabu uliletwa na Wamisionari waliokuwa wanasambaza neno la Bwana na waliuacha ili uwe kumbukumbu yao kisiwani hapo.
Yaliyotokea ni haya…
MIAKA 100 BAADAYE
MZEE Robert Mizengwe aliamka kwa kushituka kutoka usingizini, jasho likawa linamtoka. Akainuka na kukaa kitandani, akapepesa macho kwenye kiza cha chumbani huku mkono wake wa kushoto ukigusana na mgongo wa mkewe aliyekuwa akiuendeleza usingizi. Kwa sekunde chache alitulia kimya pale alipokaa na kuamini kilichomwamsha ni ndoto aliyoiota ambayo kwake aliichukulia ni yenye dalili mbaya. Ilikuwa kama ndoto ya aina ya jinamizi. Alipokuwa akijaribu kuikumbuka ndoto hiyo, ghafla akajiwa na tukio lililomshangaza na kumshitua. Akajiona kama aliyekuwa akioteshwa tena ndoto hiyo!
Aliota akimwona mjukuu wake anayeitwa Mathias Deko akilivunja dirisha la kanisa kwa kushirikiana na wenzake, kisha kwa pamoja wakaingia ndani ya kanisa. Akawaona wakielekea kwenye altare ulipo Msalaba Mtakatifu na kuanza kazi ya kuung’oa kwa ajili ya kuuiba…
Tukio hilo likakatika kama sinema iliyojizima ghafla!
“Yesu wangu!” mzee Robert alisema peke yake na kupiga alama ya msalaba. Akajiuliza, je, alikuwa akiota? Hapana, hii siyo ndoto! alijisahihisha. Kukataa huko kwamba hiyo haikuwa ndoto kukawa kama kunamchanganya. Alikuwa na uhakika awali alikuwa ameota ndoto ya aina hiyo na iliyomshitua kutoka usingizini, lakini jinsi ndoto hiyo ilivyorudishwa kwa mara ya pili alikiri haikuwa ndoto, bali ni ushuhuda aliotakiwa aone kwa macho yake! Nimekuwa Mtakatifu? alijiuliza. Aliamini matukio ya aina hiyo huwatokea watakatifu, na huwatokea kama ubashiri wa jambo linalokuja au lililofanyika!
Lakini papohapo akaanza kuikosoa ndoto hiyo. Kwa nini ubashiri umhusishe mjukuu wake? alijiuliza. Na sababu ya kujiuliza hivyo ni kuwa, hakutaka kukubali ubashiri wa mjukuu wake kuhusishwa na wizi! Akajilazimisha kuichukulia ndoto hiyo kama aina ya mzaha aliokuwa ameoteshwa! Na alikuwa na sababu ya kuamini hivyo!
Moja ya sababu ya kuuona huo ni mzaha ni kutokana na Mathias kuwa mhitimu mtarajiwa aliyekuwa akimaliza masomo yake ya shahada inayomhusisha na mafunzo ya kiroho aliyokuwa akiyasoma kwenye chuo kilicho jirani na kanisa hilo. Lakini haikuwa tu kwenye kumaliza mafunzo hayo na kujipatia shahada yake, bali pia, kulikuwa na maandalizi ya sherehe ya Mathias kusimikwa upadri! Kwa mazingira hayo na weledi aliokuwa nao mjukuu wake huyo, mzee Robert akaichukulia ndoto hiyo na yote yaliyojitokeza, kuwa ni mzaha asioukubali!
Akajaribu kulala tena, lakini ghafla bila ya kutarajia na pia kutokuwa na uhakika kama yuko usingizini au yuko macho, mzee Robert akaoteshwa kumwona tena mjukuu wake, safari hii akitoka kanisani akiwa amevaa kanzu ya kiroho huku ameubeba msalaba wa dhahabu juu ya mabega yake akiwa anayumba kutokana na kuelemewa nao kama ilivyokuwa kwa Bwana Yesu alipokuwa akiadhibiwa na Wayahudi wakati akipelekwa kusulubiwa…
Tukio hilo nalo likamalizika bila ya kufika mwisho!
Mzee Robert akashituka, safari hii kwa mshituko mkubwa kuliko wa awali na kutoa yowe dogo la kutaharuki. Akakaa kitandani na kujizuia kwa mhimili wa mikono yake iliyokuwa imeegemea kwenye godoro, akawa anatweta na jasho likimtoka!
Hakulala tena! Ndoto aliyoiota ikaendelea kumpa tabu akilini!
********
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
ASUBUHI kukiwa bado hakujapambazuka, mzee Robert alikwenda kuoga na kisha akaelekea kanisani kama ilivyo ada kwake, lakini asubuhi hii ikawa tofauti na za awali. Safari hii ikawa siyo kwa ajili ya sala pekee, bali pia kuifanyia uhakiki ndoto aliyoiota! Lengo likawa kuangalia kama msalaba huo umeibwa na kujua kama kanisa limevunjwa kama ndoto ilivyokuwa imemwotesha!
Akiwa njiani kuelekea kanisani kwa mwendo wa kasi, tofauti na asubuhi zote za nyuma, sintofahamu ya ndoto aliyoiota ikawa inaendelea kumuweka kwenye wakati mgumu kadri hatua zake zilivyokuwa zikipiga. Nafsini mwake kulikuwa na msukumo uliokuwa ukimtaka aamini ndoto aliyoiota ilikuwa na ukweli fulani na ndiyo hasa iliyompa msukumo wa kutaka kufika haraka kanisani huku hofu yake kubwa ni kuibwa kwa msalaba huo. Ni nafsi yake ndiyo iliyokuwa ikimsumbua ambayo ilikuwa ikiamini, historia ya ujio wa msalaba huo uliopo kanisani uliletwa na Mtakatifu Bikira Maria kwa ajili ya kuzuia mabaya yasikifikie kisiwa hicho! Dhana hiyo ikamuweka kwenye hofu kuu ya kuogopa majanga yaliyobashiriwa yangeweza kutokea kama msalaba huo ungekuwa umeibwa!
Alifika kanisani na kuonana na baadhi ya waumini hasa wazee wenzake wa kanisa ambao walijijengea utaratibu wa kusali kila asubuhi. Mara tu alipoingia kanisani, macho yake yakaangalia moja kwa moja ilipo altare na kujikuta akishusha pumzi na kupiga alama ya msalaba baada ya kuuona Msalaba Mtakatifu upo, haukuibwa! Mzee Robert akawa kwenye faraja wakati akisali na kuamini kuwa, yote aliyoyaona usingizini, zilikuwa ni moja ya ndoto za maruweruwe kama ndoto nyingine za aina hiyo zilivyo!
Pamoja na kuridhishwa na aliyoyaona kanisani, lakini alikiri kulikuwa na kitu kilichokuwa kikimsumbua kwenye ndoto aliyoiota; nako ni kuhusishwa mjukuu wake kwenye ubashiri mbaya uliokuwemo kwenye ndoto hiyo. Hali hiyo ikamfanya awe na mshawasha wa kuonana na Mathias pindi atakapowasili nyumbani. Hakujua angeongea naye nini baada ya kukutana naye, lakini fikra za umuhimu wa kuonana na mjukuu wake huyo zilimtawala njia nzima wakati akirudi nyumbani!
****
USIKU ambao mzee Robert Mizengwe alikuwa akiiota ndoto hiyo, Mathias Deko, mjukuu wa mzee Robert, alikuwa macho chumbani kwake. Muda wote huo wa kuwepo chumbani, Mathias mara kwa mara alikuwa akiangalia saa iliyopo ukutani hadi ikafikia wakati akawa anaiona saa hiyo ikiwa inachelewesha muda aliokuwa akiusubiri ufike. Hisia za kuibeba dhambi zilimtawala ndani ya nafsi yake humo chumbani. Hisia hizo zilikuwa zikisababishwa na shughuli aliyoikusudia kwenda kuifanya muda mchache ujao. Ilikuwa ni hali iliyokuwa ikimpa mkanganyiko wa akili na kuuona muda aliokuwa akiusubiri ukiwa haufiki! Akiwa ndani ya subira, Mathias aliutumia muda huo kujaribu kujiridhisha kwa kujipa moyo kuwa, harakati anazokusudia kuzifanya muda mchache ujao ni kwa ajili ya kujitengenezea maisha yake na si dhambi!
Mawazo hayo yenye mkakati ambao anauona siyo dhambi kutenda, lakini kwa upande pili ungeleta mtazamo wa uasi, yaliasisiwa na yeye mwenyewe na kuyalea kwa miongo kadhaa baada ya kukiri kuchoshwa na maisha ya kidini aliyokuwa akiishi nayo, maisha ambayo kwake yalikuwa kinyume na utashi wake. Maisha ya kiroho! Maisha hayo aliyaona ni maisha yanayojengwa zaidi kisaikolojia ili uepukane na maisha ya anasa ambayo kwake aliyaona ndiyo sahihi binadamu awe nayo. Lazima binadamu ufurahie kwa nini umezaliwa, na furaha hiyo iambatane kwa kuifurahisha nafsi yako pale inapopenda!
Hakupendezwa na maisha ya kiroho, kwake hayakuwa maisha aliyokuwa anayataka, aliyachukulia maisha hayo ni yenye vikwazo vyenye vitisho vya dhambi pale anapotaka kuuburudisha moyo wake. Ni mfumo wa maisha aliouponda na kuuchukulia ni mfumo wa kuishi kwa woga ambako mtu anaishi kwa kuongozwa na kulishwa mawazo na makuhani wanaokutaka ujiandae na maisha ya baadaye yenye falsafa za kuamini kwa kuambiwa yapo, lakini yaliyokosa ushuhuda wa uwepo wake! Mathias aliyachukulia maisha ya aina hiyo humfunga mtu kimawazo kwa kulazimika kulikubali jambo ambalo haliamini kwa sababu tu, kuhani amelitamka!
Mathias alijiona ni mtu anayehitaji kuwa na tabasamu wakati wote badala ya kuishi kwa vitisho vinavyotolewa na makuhani wa dini. Inakuwaje starehe uambiwe ni dhambi? Hakuwa tayari kupokea mapokeo ya aina hiyo! Alihitaji kuwa mtu huru mwenye kuufurahisha moyo wake kwa kufanya starehe pale anapoihitaji. Alihitaji kuwa na tabasamu la kuwa mtu huru asiyefungwa na vipengele vya aya za Biblia. Alitaka kuyafurahia maisha yake kwa kumiliki na kuendesha gari zuri la farasi, atakayeishi kwenye jumba la kifahari, kupumzika na kulala kwenye hoteli za kifahari, kula vyakula vya anasa vyenye kuuzwa bei ya juu na kunywa mivinyo mitamu akiwa amezungukwa na wasichana warembo! Alihitaji maisha ya aina hiyo kabla hajajifunga kwenye maisha ya ndoa, hayo ndiyo maisha anayoyataka, ambayo hayapatikani ukiwa padri!
Akiwa amekaa humo chumbani mwake usiku huo, Mathias alipiga kite cha karaha kuyasikitikia maisha ya kiroho anayotakiwa na babu yake awe nayo. Mimi niwe padri? alijiuliza na swali hilo kulifanyia ni aina ya mzaha wenye kituko. Mathias aliufikiria mkakati ulio mbele yake na kuamini kuwa, mkakati huo ni ukombozi wa maisha yake!
Ghafla akahisi kama kulikuwa na kitu kilichosikika kwa mbali. Akatulia na kuwa makini kusikiliza. Baada ya kimya kifupi, akasikia dirisha la chumba chake likigongwa kwa sauti ya chini kutoka nje. Kukafuatiwa na sauti iliyonong’ona kwa nje ikimwita jina lake, “Mathias!”
“Nakuja!” Mathias alijibu, naye pia kwa sauti ya kunong’ona, kisha akatabasamu peke yake. Muda wa ukombozi umewadia! aliwaza.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Ujio huo wa kuja kuamshwa usiku mwingi aliutarajia. Alifuatwa na wenzake wawili ambao ni wavuvi na wakazi wa hapo kisiwani. Walikuwa ni marafiki zake tokea udogoni waliosoma pamoja kwenye shule ya msingi, walikua na kucheza pamoja na wakawa na tabia ya kutembeleana majumbani mwao. Lakini pasipo na matarajio, Mathias akiwa bado yuko shule ya msingi alijikuta akihamishwa kutoka nyumba aliyokuwa akiishi na wazazi wake na kuhamishiwa kwa babu yake, mzee Robert Mizengwe. Uhamisho huo ukawa umefikisha hatima ya marafiki hao kuwa huru kutembeleana majumbani mwao baada ya Mathias kubanwa na sheria alizozikuta nyumbani kwa babu yake ambako alishinikizwa kujisomea nyumbani kila siku baada ya kutoka shule na kisha kusoma Biblia kabla ya kulala.
Maisha hayo ya kutokuwa huru yalimchukiza Mathias na ukawa mwanzo wa kujikuta akipata fikra mpya za kuhitaji uhuru wake. Pamoja na kuipata adha hiyo ya kukosa uhuru wa kuwatembelea marafiki zake, lakini bado alishindwa kuzizungumza au kuzionyesha hisia hizo kwa familia mpya anayoishi nayo ambayo ina weledi wa dini. Ingawa aliukosa uhuru huo wa kutembeleana na marafiki zake hao, lakini bado aliweza kukutana nao shuleni, na nafasi hiyo kutumika kwa Mathias kuwalalamikia wenzake juu ya aina ya maisha anayoishi na babu yake. Hapo ndipo pakawa pamezaliwa wazo jipya la kuondokana na maisha ya falsafa zilizojaa dhambi na waingie kwenye maisha huru ya kimagharibi kwa kuyafuata huko yaliko. Hata hivyo, kikwazo kwao kikawa pesa za kuwawezesha kuondoka kisiwani hapo.
Dhamira na lengo lao likiwa halijakamilika kutokana na kutokuwa na pesa, Mathias akafaulu kwenda kusoma masomo ya sekondari kwenye shule ya hapohapo kisiwani kwao iliyokuwa ikiongozwa na Kanisa Katoliki. Bahati mbaya wenzake wakaanguka! Matokeo hayo yakawagawa, wenzake wakajishughulisha na biashara ya uvuvi na yeye kuendelea na masomo. Hali hiyo ikawafanya wasipate nafasi ya kuonana mara kwa mara, lakini kila walipoonana, mkakati wao na mazungumzo yao yakawa ni namna gani wataweza kupata pesa za kuwawezesha kuondoka kisiwani humo baada ya kugundua pesa waliyokuwa wakiipata kutokana na biashara ya uvuvi isingewawezesha kuwasafirisha. Wakabakiwa kuwa na usongo uliokuwa ukiwakera kadri siku, miezi hadi miaka ikikatika bila ya malengo yao kufanikiwa.
Ndipo siku moja, Mathias akapata wazo na kulitoa kwa rafiki zake; wazo la kuiba msalaba wa dhahabu uliopo kanisani kwa kuamini kuwa, endapo watafanikiwa kuiba msalaba huo na kuvuka nao bahari, dhahabu iliyopo kwenye msalaba huo itakuwa bidhaa ya kuiuza kwa bei ghali na pato watakalolipata lingewawezesha kuanza maisha mapya ughaibuni tena wakiwa matajiri! Wazo hilo likakubaliwa na wote. Wakajipanga kwa mikakati ya kulitekeleza kwa vitendo wazo la kuiba msalaba huo.
Usiku huo ikawa siku rasmi! Wakapeana muda wa kuamshana, wakakubaliana Mathias awe wa mwisho kuamshwa ifikapo saa tisa usiku!
*******
MATHIAS aliteremka kutoka kitandani, hakusumbuka kuanza kuvaa nguo, alikwishajiandaa kuzivaa mapema kabla ya kuanza kuwasubiri wenzake. Alitoka chumbani kwa kupitia dirisha alilokuwa amegongewa, na kutoka nje. Aliwakuta wenzake wakimsubiri, wote wakiwa wamevaa fulana nzito za kuzuia baridi.
“Vipi, twendeni?” Mathias aliwauliza wenzake kwa sauti ya kunong’ona.
“Twende!” nao wakajibu kwa kupishana kwa sauti ileile ya kunong’ona.
Wakaelekea kanisani!
Walipofika kanisani, wakatembea kwa mwendo wa kuvizia hadi mahali alipokuwepo mlinzi, wakamkuta akiwa amelala na alikuwa akikoroma. Pumzi alizokuwa akizitoa mlinzi, harufu yake ikawajulisha kuwa, alikuwa amekunywa pombe. Wakamwacha, wakaondoka kwa mwendo uleule wa kuvizia na kurudi upande wa pili wa kanisa ambao mara nyingi hautumiwi na watu kupita. Upande huo ndiyo waliopanga wautumie kuweza kuingilia ndani ya kanisa.
Walivyoanza kuvunja dirisha kukaenda sambamba na ndoto ya mzee Robert Mizengwe. Mara baada ya kulivunja dirisha la kanisa na kuingia ndani, Mathias na wenzake wakaenda kwenye altare eneo ulipo msalaba. Kazi ya kuondoa msalaba huo ikawa siyo rahisi kama walivyotarajia. Msalaba huo ulikuwa umeimarishwa uwekwaji wake kwa kuzidishiwa vishikizo vilivyowekwa na nati za kufungia. Wakalazimika kuzifungua nati hizo kwa bisibisi na spana walizokuwa nazo. Iliwachukua muda usiopungua nusu saa hadi kufanikiwa kuufungua huku michirizi ya jasho ikidondoka chini ya videvu vyao. Wakauondoa msalaba, wakautia kwenye gunia walilokuwa wameliandaa, kisha nafasi ile iliyokuwepo msalaba waliouondoa, wakaanza kazi ya kuuweka msalaba bandia walioutengeneza kwa udongo unaonata na kuufunikia kwa bati la shaba walilolipaka rangi ya dhahabu na kulingarisha kwa dawa, ukaonekana hauna tofauti na mwonekano wa Msalaba Mtakatifu wa Bikira Maria!
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
*****
KISIWA cha Zebati kilikuwa na njia nyingi za mkato za miguu zilizokuwa zikiingia na kutoka kwenye kila pembe ya kisiwa. Barabara zilizoonekana kuwa kubwa ni zile zitumikazo kwa kutumiwa na mikokoteni inayovutwa na punda. Mazingira hayo yakawa yamewasaidia Mathias na wenzake kuweza kuzitumia njia za mkato zenye vichochoro vingi usiku huo wakiwa na mzigo wao wa msalaba walioubeba kwa kupokezana pasipo kuonekana au kukutana na mtu. Viumbe pekee walivyopishana navyo ni mbwa na paka waliokuwa wakijitafutia riziki kwenye majalala.
Ingawa mwendo wao haukuwa wa kasi kutokana na kuelemewa na uzito wa msalaba, lakini njia za mkato walizokuwa wakizitumia ziliwawezesha kufika pwani kwa muda mwafaka kabla hakujapamabazuka. Walipofika wakaifuata ngalawa iliyokuwa imeegeshwa kwenye kina kidogo cha maji. Wenzake ndiyo waliotangulia kuingia kwenye ngalawa hiyo wanayoimiliki wakiwa na msalaba wao. Mathias akatumika kuisukuma ngalawa kwenye maji na kisha kuidandia baada ya kuridhika na kina cha maji.
Mawio yalikuwa mbele yao upande wa mashariki ya bahari ambako nuru yenye miali ya rangi ya chungwa, ikiwa imekatiza kwenye mawingi kuashiria jua lilikuwa likichomoza, yaliwakuta wakiwa wamekiacha kisiwa cha Zebati kwa umbali mrefu huku tanga lililojaa upepo likiisukuma ngalawa yao kwa kasi. Hakuna aliyemzungumzisha mwenzake, kila mmoja alionekana kuwa na fikra zake zilizomsukuma kukaa kimya, wakaonekana kama wakiwa waliojawa na simanzi, sura zao zikakita kwenye sintofahamu ya kule wanakoelekea.
Mathias aligeuka nyuma na kukiangalia kisiwa cha Zebati ambacho kilianza kupotea machoni. Aliweza kuviona vijinjia vyembamba vya miguu vikiwa vimetawala kuelekea milimani na kuwa kama nyoka warefu waliojipindapinda. Hisia za kuwa alikuwa akikiangalia kisiwa hicho kwa mara ya mwisho zikamshambulia kwenye moyo wake baada ya kuikumbuka familia ya mzee Robert aliyokuwa akiishinayo, na kisha kuwakumbuka baadhi ya watu aliozoea kuonana nao kila asubuhi wakati akielekea chuoni. Sura zao zikamjia machoni! Ghafla akajikuta amejawa na machozi machoni mwake, akageuka kuangalia mbele na wakati huohuo akameza mate mazito yaliyoinua koromeo lake, kisha aliinama kidogo na kukamata upande wa shati alilovaa na kujifuta machozi.
*******
WAZAZI wake walifariki wakati Mathias akiwa na miaka kumi. Wote walifariki siku moja baada ya kuumwa na nyoka mwenye sumu kali aliyewashambulia walipokuwa shamba wakilima. Kifo cha wazazi wake kilisababisha Mathias achukuliwe na kulelewa na babu yake ambaye ni mmoja wa wazee wa kanisa.
Shule zote alizosoma Mathias kuanzia msingi, sekondari hadi elimu ya juu zilimilikiwa na wamisionari. Baada ya kumaliza masomo yake ya elimu ya juu, alijiunga na chuo cha Kikatoliki kwa elimu ya kiroho ili baadaye awe padri. Kitendo cha kupelekwa kusomea masomo ya kiroho kilimfanya Mathias awe na sura mbili tofauti, moja ikiwa ya utakatifu na nyingine ya kuhusudu mambo ya kimagharibi. Sura ya utakatifu aliimudu vyema kuiweka mbele ya jamii na kuonekana ni kijana mpole, mtulivu mwenye weledi na kuwa tumaini jema kwa wakazi wote wa Zebati waliojaa shauku kijana wao huyo asimikwe upadri.
Lakini upande wa pili sura yake aliificha kwa kificho kikubwa na kutotambuliwa dhamira yake kuanzia babu yake, walimu wake, familia anayoishi nayo hadi jamii yote kwa ujumla. Sura yake halisi iliweza kuonekana nyakati za usiku akiwa amejifungia chumbani baada ya sala ya mwisho ya usiku ambayo familia yote husali pamoja hapo nyumbani kabla ya kutawanyika kwenda kulala. Mara tu anapoingia chumbani mwake na kujifungia, Mathias aliweka kando Biblia na kuanza kusoma vitabu vya riwaya vyenye kuzungumzia uhalifu na mapenzi. Hivyo ndivyo vitabu alivyokuwa akifurahia kuvisoma hadi usiku mwingi na ifikapo asubuhi huvificha vitabu hivyo sehemu ambayo alikuwa na uhakika hakuna mtu yeyote angeweza kuvigundua vilipo, na anapotoka nje ya chumba chake hujigeuza tena kuwa mtu wa kiroho mwenye utukufu wa mbinguni! Na badala ya kubeba jina la Bwana aliye mbinguni, Mathias akawa mwananadharia aliyebeba raha za kimagharibi na kuamini ipo siku, nadharia yake itageuka kuwa vitendo!
Mathias ambaye ni mrefu mwembamba, ni mpole wa kuzaliwa na anazungumza kwa upole, ni mtu mwenye kukiamini kile anachokikubali akilini mwake kwa kuwa kimya kuliko kubishana na mtu. Na siku zote anapozungumza huwa anaongea kwa unyenyekevu kama anayehubiri nasaha kwa mfiwa na kuonekana kama padri aliyekamilika. Kwa aina ya tabia hiyo, Mathias akafanyiwa ubashiri kuwa, angekuwa ni padri mwenye weledi uliotukuka kisiwani hapo.
Wakazi wa kisiwa cha Zebati ni wakulima na wavuvi wenye kipato kinachowatosheleza, lakini pia, walifuga mifugo michache kama kuku, bata, nguruwe, ng’ombe, mbuzi na kondoo. Wote walizungumza lugha moja na ni watu waliopendana. Walijenga ushirikiano wa kazi za maendeleo ya kisiwa chao ambazo walizifanya kwa Harambee huku kanisa likitoa msaada wa vifaa. Amani ilikuwa sehemu kuu ya maisha yao iliyozidisha upendo kwa kila mmoja wao. Maisha yao yakawa ya raha yasiyojua misukosuko ya aina yoyote huku wakiamini Msalaba Mtakatifu uliopo kanisani ndiyo uti wa usalama huo.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
*****
MZEE Robert Mizengwe alirudi nyumbani akitokea kanisani huku akiwa ameridhika kuukuta msalaba ukiwa kanisani. Lakini pamoja na ridhiko hilo, upande wa pili wa ndoto bado uliendelea kumsumbua, nako ni kule kuhusishwa Mathias kwenye ndoto! Usumbufu huo ukawa unamwongezea kasi ya kurudi nyumbani ili aonane na Mathias amweleze kuhusu ndoto aliyoiota, lakini pia alijikuta akiiweka nia ya kutaka kufanya maombi maalumu ya kumwombea mjukuu wake asikaribiwe na mabaya kama yale aliyooteshwa. Akaamini maombi hayo yangepokewa na Yesu ambaye angetoa ubarikio kwa Mathias wa kumwezesha kuishi kwa amani na Shetani kukaa mbali naye.
Alifika nyumbani na kukuta maandalizi ya kifungua kinywa yakiandaliwa. Ilikuwa ni kawaida kwa familia hiyo kupata kifungua kinywa cha pamoja mapema asubuhi kabla ya kila mmoja kuanza kuwa na majukumu yake. Mzee Robert na mkewe wakawa wa kwanza kuwahi kukaa mezani na kisha mmoja baada ya mwingine walifuatia na kujumuika kwenye meza ya chakula. Hatimaye wote wakawa wametimia, lakini kiti kilichozoea kukaliwa na Mathias kikawa kitupu!
Ikaanza kuchukuliwa kwa wepesi kuwa, Mathias angewasili muda wowote wakati wakinywa chai, lakini kadri muda ulivyokuwa ukienda ndivyo hitimisho la kila mtu kumaliza kifungua kinywa chake likawa limetimia, Mathias akiwa hajawasili!
“Mathias yuko wapi?” mzee Robert akawa wa kwanza kuuliza.
Wote waliokuwapo mezani wakaangaliana usoni, kimya cha sekunde chache kikajiunda.
Kijana mdogo wa kiume mwenye umri usiozidi miaka kumi na miwili, aliyekuwa na sare za shule akakivuta nyuma kiti alichokalia na kusimama. “Ngoja nikamwangalie chumbani kwake,” alisema na kuondoka.
Baada ya kijana huyo kuondoka, hakukuwa na yeyote kwenye meza aliyediriki kuhoji kwa nini hadi muda huo Mathias alikuwa hajafika kwenye meza ya chakula. Ilikuwa ni familia iliyojengeka kidhamu iliyozingatia mila, desturi na maadili ya dini ambayo wakati wakiwa wanakula, mazungumzo hayakupewa nafasi kubwa. Waliamini hiyo ilikuwa ni njia ya kukiheshimu chakula.
Kijana aliyekwenda kumwangalia Mathias chumbani kwake alirudi. Wote waliokuwa mezani wakamwangalia kama kwamba ilikuwa ni muhimu kwa kila mmoja kulisikia jibu ambalo angelitoa.
“Hayupo!” yule kijana alijibu. Hakufanya dalili yoyote ya kutaka kurudi kwenye kiti chake, alikuwa kama vile akisubiri kutumwa tena.
“Pengine yuko bafuni anaoga,” mkewe mzee Robert alisema.
“Nilishapitia na huko, lakini pia hayupo!” kijana yule alijibu akiwa bado amesimama.
Wote waliokuwepo mezani wakapigwa na butwaa huku wakiangaliana kwa zamu. Atakuwa amekwenda wapi? kwa pamoja walijiuliza swali hilo kimyakimya.
“Labda amewahi kutoka asubuhi na alishindwa kumuaga yeyote kwa kuamini angewahi kurudi kabla ya kifungua kinywa,” mke wa mzee Robert alisema tena.
“Mimi niliwahi kutoka mapema sana,” mzee Robert alisema. “Na mlango niliufungua mwenyewe, unataka kuniambia alitoka nyuma yangu?”
“Inawezekana,” mkewe alijibu. “Pengine amechelewa mahali.”
Mzee Robert akaonyesha mashaka usoni pake, akashusha pumzi na kulikubali wazo la mkewe. “Tuvute subira,” alisema kwa sauti hafifu.
Kijana aliyekuwa amesimama alirudi kwenye kiti chake na kujiunga na wenzake mezani bila ya kutamka lolote.
Ilipofika mchana, matumaini ya kuwa Mathias angerudi yakaanza kufifia. Juhudi za kumtafuta nje ya nyumbani zikaanza rasmi kwa kuwauliza majirani kama walitokea kumwona Mathias. Lakini baada ya kila aliyeulizwa kukana kumwona, wigo wa mashaka ya kuwa Mathias amepotea ukazidi kwenye familia hiyo!
Hatimaye taarifa za kupotea kwa Mathias zikawasilishwa rasmi kanisani ambako nako walikana kumwona!
Ilipofika alasiri, kengele ya kanisa ikagongwa. Haukuwa ni muda wa kugongwa kengele na linapotokea tukio la aina hiyo huwa ni ishara kwa kila mkazi wa kisiwa hicho kutambua kuna tukio la dharura lililotokea na inapaswa kila mtu aliyeisikia kengele hiyo anapaswa kumwambia mwenzake aliyekuwa hakuisikia na kutakiwa aache shughuli aliyokuwa akiifanya ili aweze kwenda kanisani kusikiliza wito wa kengele hiyo.
Wakazi walianza kuonekana kwenye kila kona ya njia, wengine wakipandisha kwenye miinuko na wengine wakiteremka huku wengine wakiwa kwenye njia tambarare, wote kwa pamoja wakielekea kanisani. Takriban ndani ya saa moja, robo tatu ya wakazi wakawa wamewasili kwenye viwanja vya kanisa. Taarifa rasmi ya kupotea kwa Mathias ikatolewa kwenye jumuiya hiyo na kuleta mshangao kwa wote waliosikia. Likawa ni tukio la kwanza kwa mtu kupotea katika mazingira ya kawaida ukiyaondoa yale ya baharini.
“Tusubiri mpaka usiku, pengine alipata dharura ya safari na hakuwahi kumuaga mtu,” baadhi ya wazee wenzake wa kanisa walimpa moyo mzee Robert.
“Si kawaida ya Mathias kuondoka bila ya kuaga,” mzee Robert alisema. “Inanitia wasiwasi. Nahisi kuna jambo limetokea kwa mjukuu wangu. Nimejaribu kuzungumza na baadhi ya wanafunzi wenzake wa chuoni, lakini hakuna yeyote aliyekiri kumwona kwa siku ya leo wakati jana usiku tulisali naye sala ya usiku na kuagana kabla ya kwenda kulala!
Padri ambaye pia ni paroko wa kanisa hilo na raia wa Italia aliyekuwa amesimama huku mkono mmoja akiwa ameukunja kifuani mwake na mkono mwingine ukiwa umekamata chini ya kidevu, alijaribu kumtuliza mzee Mathias kwa kumwambia, “Ni vyema tukawa watulivu mpaka jioni, lakini endapo hataonekana, itabidi tukaripoti polisi. Na pia naamini kama kuna mabaya yoyote, Bwana Yesu atampa nguvu na kumnusuru.”
Mzee Robert akaikubali rai ya padri.
Kupotea kwa Mathias kukawafanya wakazi wajikusanye vikundi na kuchukua majukumu ya kumtafuta kwa kwenda maeneo tofauti ya kisiwa hicho. Wapo walioambaa na fukwe za bahari kwa matumaini kama angekuwa amekufa maji pengine wangeweza kumwona, wapo waliokwenda nje ya mji kubahatisha upatikanaji wake, ilimradi juhudi za kumtafuta zikawa zimeanzishwa kwa juhudi kubwa. Taarifa za awali na zilizochelewa zote zilipelekwa kanisani. Usiku ulipoingia taarifa za kukatisha tamaa zikawa zimeenea kisiwani kuwa, Mathias hajaonekana.
Taarifa ikapelekwa polisi!
Usiku huo, familia ya mzee Robert ikiwa imekusanyika mezani kwa ajili ya chakula cha jioni, wote walijikuta wakijilazimisha kula huku nyuso zao zikiangalia juu ya meza na kila mmoja akionekana kukwepa kumwangalia mwenzake. Simanzi ilitawala na mzizimo wa huzuni ukajenga kwenye familia yote, kila mmoja akashindwa kuendelea kula.
Sala, maombi ya kumwombea Mathias vikafanyika, wakaomba sana hadi usiku mwingi na kuchelewa kulala kwa matumaini huenda zingekuja habari za kuonekana kwa mpendwa wao. Lakini hadi walipokwenda kulala, hakukuwa na taarifa yoyote iliyoletwa hapo nyumbani inayohusu kuonekana kwa Mathias.
*******
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
KISIWA cha Zebati kilishapotea kwenye upeo wa macho yao, mzunguko wa anga ya buluu ukawa umeangukia kwenye uso wa bahari. kwa pande zote na hakuna kilichoonekana zaidi ya kujiona wao wenyewe na ngalawa yao iliyoonekana kama kifuu kwenye bahari kubwa iliyowazunguka. Wote watatu walikuwa wametulia kwa kujishikiza ndani ya ngalawa na kuisikilizia ilivyokuwa ikipanda mawimbi ya bahari yaliyoonekana kama povu ambayo yalienea sehemu kubwa ya bahari. Hali hiyo ya uwepo wa mawimbi hayo ambayo baadhi yalianza kupiga ubavuni mwa ngalawa na kuipoteza mfumo wa kuelea, ikawalazimu kila baada ya muda wawe wanayakomba maji yaliyokuwa yanaingia kwa kuyatoa nje ingawa tayari yalikwishalowesha gunia lenye msalaba.
“Ukiyaona mawimbi kama haya yenye mapovu ujue bahari inaanza kuchafuka!” mmoja wa wale wavuvi alimwambia Mathias aliyekuwa siyo mzoefu na safari za baharini.
Mathias hakujibu, lakini uso wa wasiwasi ukawa tayari umejijenga.
Hali ya bahari ikaendelea kuchafuka kadri walivyokuwa wakienda na ngalawa ikaanza kupanda milima ya mawimbi kwa kuinuka juu kama inayotaka kubinuka, na kisha kurudi kama inayotua kwa mwelekeo wa kupiga mbizi kama inayotaka kuzama.
“Bahari inazidi kuchafuka!” mmoja kati ya wavuvi wawili alionya.
“Yesu atatusaidia!” mwingine alijibu.
Mathias hakuongea lolote. Mikono yake ilikuwa imejishikiza kwenye ngalawa kwa nguvu zote akihofu asije akatupwa nje, isitoshe, hata woga nao ulikuwa umemtawala. Alikuwa hajawahi kusafiri nje ya kisiwa cha Zebati, lakini pia, alikuwa hajawahi kupanda chombo cha baharini na kusafiri nacho angalau kwa umbali mrefu. Hiyo ilikuwa ndiyo mara yake ya kwanza! Kutokana na kutokuwa na uzoefu na bahari, hali ile ya kuyumbishwa na mawimbi yaliyokuwa yakiongezeka ukubwa kadri muda ulivyozidi kusogea, ikaanza kumtia kichefuchefu. Kinywa chake kikajaa mate yenye chumvi chumvi. Mara ya kwanza aliyameza kama njia ya kutoruhusu kutapika, lakini akagundua kitendo cha kumeza mate kinazidisha kukikuza kichefuchefu. Akaanza kuyatema kila yalivyojijaza mdomoni na kujizuia asitapike. Akili yake ikatekwa kuifikiria hali ya kutotapika, ikawa kama anayepigia upatu kuiruhusu hali ya kutapika imjie kwa kasi!
Mathias akawatazama wenzake ambao nao walikuwa wamejishikiza kwenye ngalawa. Nao walikuwa kimya, hakuna aliyekuwa akitamka lolote japo kulalamika. Nyuso zao zikawa zinaonyesha woga. Kimya hicho cha wenzake ambao ni wazoefu wa bahari kikampa wasiwasi Mathias kuwa, hali ya bahari inaweza ikawa ni ya hatari zaidi kuliko anavyoifikiria.
Ghafla kichefuchefu kikamjia, kinywa chake kikajaa mate yenye ladha ya chumvi, akajaribu kujizuia asitapike kwa kuyameza. Likawa kosa! Alivyoyameza, yakaenda kutibua tumbo. Hali ya kutapika ikamjia kwa nguvu, matapishi yakatoka tumboni na kupanda hadi kinywani. Akayajaza mdomoni kujizuia asitapike! Uvumilivu ukamshinda, akaulengesha uso kando ya bega lake na kuuinamisha. Akachukuliwa na nguvu kubwa iliyokuja na awamu nyingine ya matapishi, mkono wake uliacha kukamata ubavu wa ngalawa na kwenda kuungana na mwingine kuushikilia ubavu wa upande mmoja wa ngalawa, akajizuia asichomoke na kutumbukia baharini. Akafungulia kutapika kwa mfululizo. Akatapika kwa mfululizo hadi nyongo, hatimaye akawa anatapika mate huku msukumo wa kutapika ukiendelea kumsukuma bila ya kutoa chochote kinywani. Akahisi mbavu zikimbana kila msukumo wa kutapika ulivyokuja, ulimwinua kiwiliwili chake, akaonekana kutaka kuiachia ngalawa na dalili za kutumbukia baharini zikawa wazi. Mwenzake aliyekuwa karibu akamdaka, akamzuia kabla hajatumbukia baharini, mwingine naye akaja kumsaidia mwenzake kumwokoa Mathias!
Mathis alitweta akiwa hoi huku viungo vyake vya mwili vikiwa vimelegea. Alihisi kama anayekaribia kukata roho, macho yake yalirembuka na kupata shida kuyafungua. Kila kitu kikawa usoni pake kuonyesha jinsi alivyokata tamaa. Ingawa bahari iliendelea kuchafuka, lakini kile kitendo cha kutapika kikawa kimempa hali ya kujisikia afueni.
Akaliangalia jua kwa macho yaliyokuwa yakipepesa. Taratibu fikra zake zikaanza kurudi Zebati. Muda huo ungekuwa wa mapumziko kwa ajili ya chakula cha mchana. Angekuwa amejipumzisha kwenye bustani ya kanisa iliyo karibu na chuo chao baada ya kula, na angekuwa amejumuika na wanafunzi wenzake wakijadili hiki na kile au angekuwa anasoma moja ya vitabu vya masomo anayoyasoma.
Mathias aliyafikiria mazingira ya bustani aliyoiacha, yenye mandhari ya kupendeza na miinuko ya vichuguu vya hapa na pale, iliyojaa majani aina ya mbudu zilizokolea rangi ya kijani kibichi yaliyofyekwa mara kwa mara na kuwa mafupi wakati wote kiasi cha kuufanya uwanda wa bustani hiyo uonekane kama kiwanja cha kimataifa cha kuchezea mchezo wa gofu. Kwa mara ya kwanza Mathias alijiona akiingiwa na hisia ya kuwa mbali na kitu ambacho angekikosa kwa miongo kadhaa! Wazo hilo likausononesha moyo wake na kujiuliza je, amefanya kosa kuondoka Zebati?
Kujiuliza huko kukamwashiria aina ya majuto ambayo hakukubali kuyakiri, badala yake akajipa matumaini kwa kujipa moyo kuwa, huko anakokwenda kuna maisha mazuri yatakayompa uhuru wa kutenda mambo yake bila ya kuingiliwa!
Mwanzo mgumu! alijipa matumaini.
“Unajisikiaje?” Mathias alihisi kwa mbali kuisikia sauti ikimuuliza hivyo.
“Enhee?” aliitikia kwa kuuliza kuonyesha hakusikia vizuri.
“Unajisikiaje?” safari hii aliisikia vyema sauti ya mwenzake.
“Kwa sasa hivi najisikia afadhali kidogo,” Mathias alisema na kujiweka vizuri. Wenzake wakaacha kuendelea kumshika.
Baada ya kujiweka vizuri, macho yake yakaliangalia gunia lenye msalaba. Ikawa kama vile anasa alizokuwa akiziwazia zimo kwenye gunia hilo. “Msalaba Mtakatifu!” alitamka kwa sauti ndogo ambayo haikusikiwa na wenzake. Kukiri kuwa msalaba huo ni mtakatifu ikaifanya nafsi yake imsute kwa dhambi alizozibeba mikononi mwake! Lakini hapohapo akaliona wazo hilo ni la woga kwa mtu anayekata tamaa na kushindwa. Akajionya, hakutakiwa auangalie msalaba huo kwa jicho la woga, badala yake akiri kuwa, ni kweli Msalaba huo ni mtakatifu na ndio ungeweza kuyabadilisha maisha yake kwa kumletea pesa takatifu zitakazobadilisha maisha yake!
Fikra hizo zikamfanya ayatulize tena macho yake juu ya gunia hilo. Pesa Takatifu iliyo mbele yangu! aliwaza na kutabasamu huku akiendelea kuliangalia gunia lenye msalaba. Kitendo cha kutabasamu peke yake kikamfanya aonekane kama taahira aliyechanganyikiwa. Akajiinua kwa kujizoazoa, akainama kutaka kujifariji angalau kwa kuligusa gunia hilo ili kuonyesha mapenzi yake kwa matumaini yajayo wa mustakabali wa maisha yake kama kwamba Msalaba huo ulikuwa ni kiumbe hai!
Mguso wake ukaenda sambamba na radi iliyopiga kwa nguvu. Akashituka kwa kuruka nyuma, kisha kwa uso uliotaharuki, akapiga alama ya msalaba mbele yake! Wenzake nao wakawa kwenye mshituko uliowafanya waangaliane.
Ghafla Mathias akasema kwa kelele, “Tazameni kule!” huku akinyoosha mkono kuelekeza anakoonyesha.
Wenzake wakaangalia anakoonyesha Mathias. Wote kwa pamoja wakatoa mguno wa hofu baada ya kukiona walichoonyeshwa, kisha kama walioambiana, wakapiga alama ya msalaba kwa pamoja.
“Bwana uwe nasi!” mmoja aliomba.
Lilikuwa wimbi kubwa lililojipinda kama kijiko cha kutengeneza barabara, lenye urefu wa ghorofa zisizopungua saba lililokuwa likija kwa kasi kuelekea upande wao! Wote wakajikunyata na kujipinda migongo wakati wimbi hilo lilipowakaribia. Likaipiga ngalawa yao kwa kishindo, wakafunikwa pamoja na ngalawa yao na kutoa vilio vya hofu!
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
*****
BAADA ya dhoruba ya lile wimbi kupita, nyuma yake kukawaibua wote watatu kutoka kwenye maji, kila mmoja akitikisa uso kukung’uta maji ya usoni na kuanza kuelea huku wakiangaliana kama kila mmoja yupo hai.
“Ngalawa imevunjika!” mmoja kati ya wale wavuvi alisema.
“Unasemaje?” mwenzake aliuliza kwa sauti isiyoamini alichokisikia.
“Ngalawa imevunjika!” safari hii mwenzake alisema kwa sauti kubwa.
Mathias akaiona sura ya yule mvuvi wa pili ikibadilika ghafla baada ya kuangalia upande wa mgongoni kwake alikokuwa yeye. Akageuka kuangalia nyuma na kuiona ngalawa iliyovunjika, naye akatoa sauti ya hofu! Ngalawa ilikuwa imevunjika vipande huku kipande kimoja kikiwa kinaelea na gunia lenye msalaba. Nyuso za kukata tamaa zikawatawala baada ya kuliona tukio hilo. Mathias akaukumbatia upande wa mhimili wa ngalawa uliovunjika kwa madhumuni ya kujiokoa asizame.
Hali ya bahari ikawa imechafuka rasmi, mawimbi yaliyojenga migongo mikubwa yakawa yanawainua kwa kuwapeleka juu na kuwarudisha chini, hali hiyo ikawaletea hofu ya kuzama. Likawa ni suala la kila mmoja kutafuta njia ya kujiokoa! Wenzake Mathias wakaanza kuogelea kuelekea mwelekeo mmoja, wakamwacha Mathias aliyekuwa akijivutavuta kwenye ubao alioulalia huku akipiigisha kwa kuichanganya miguu yake ili kupata kasi ya kuwafuata wenzake walioonekana kuwa na uzoefu wa kuogelea.
Akiwa ameukumbatia ubao wa ngalawa huku taharuki imemwingia, Mathias aliibuka na kuzama sambamba na mawimbi yalivyokuwa yakimchukua, na akiwa kwenye harakati hiyo ya kujiokoa, bila ya kutarajia akauona upande wa ngalawa uliokuwa ukielea na gunia lenye msalaba ukifunikwa na maji. Akaingiwa na mshituko huku akiwa haamini macho yake. Akasahau kama yupo kwenye hatari ya kuzama na kuanza kuwaita wenzake kwa kelele ambao waligeuka na kumwangalia.
“Msalaba unazama!” Mathias aliwaambia wenzake.
Wenzake, wakageuka na kuuangalia msalaba uliokuwa ukizama. Tukio hilo likaonekana kutowashitua kama ilivyokuwa kwa Mathias, kisha kama walioambiana, wote kwa pamoja bila ya kutamka lolote waligeuka na kuanza tena kuogelea kuokoa maisha yao! Mathias akaachwa kwenye mshangao baada ya kutoamini kuwaona wenzake wakikata mawimbi bila ya kuonyesha dalili yoyote ya kuujali msalaba huo. Mathias akageuka kuliangalia tena gunia lenye msalaba, akaliona ndiyo kwanza likiishia kuzama pamoja na ule upande wa ngalawa!
*******
DHORUBA ile haikuishia baharini tu, baada ya kuipiga ngalawa waliyokuwemo Mathias na wenzake na baadaye kuuzamisha msalaba, ikaendelea kupiga kulizunguka eneo hilo huku mawimbi makubwa yakijiinua na kujirudisha. Hali hiyo iliendelea kwa saa kadhaa na baadaye kutulia. Lakini ilipofika usiku kukawa na mabadiliko, hali ile ya dhoruba ikajikusanya tena na kusafiri kuelekea kisiwani Zebati.
Ilipofika saa saba usiku, kisiwa cha Zebati kukawa na upepo ulioanza kuvuma taratibu, lakini hali ikawa inabadilika kadri muda ulivyokuwa ukisogea. Hatimaye upepo wa aina ya kimbunga ukawa unavuma kisiwani pote. Hali hiyo ikawashitusha wakazi waliokuwa wamelala. Wakaamka kwa taharuki, wakajengwa na hofu huenda upepo huo ukaziezua nyumba zao. Upepo ukaendelea kuvuma kwa nguvu, ukatengeneza mlio wa mluzi unaohuzunisha uliosikika ukizunguka kila kona. Minazi iliyopo kwa wingi kisiwani humo na miti mingine kama miembe na mingineyo ikayumbishwa kwa sauti na kulalama kwa kufoka na baadhi ya vishindo vya kuanguka kwa miti vikasikika.
Wanyama nao wakaanza kutoa milio ya hofu; mbwa wakawa wanabweka kwa nguvu, mifugo mingine kama ng’ombe, mbuzi, kondoo, nguruwe hadi bata mzinga na kuku nao walishiriki kutoa vilio vya woga. Kukawa na hali ya sintofahamu iliyokikumba kisiwa hicho!
“Hali hii mbona inatatanisha?” mfugaji mmoja wa kiume mwenye makamo ya utu uzima, mrefu na mwenye maungo yaliyokakamaa alisema kwa sauti ya chini kama aliyekuwa akijizungumzisha peke yake ingawa alikuwa amelala na mkewe.
“Hata mimi nashangaa!” mkewe alijibu kuonyesha na yeye alikuwa macho. “Hali inatisha huko nje!”
Yule mwanamume akashangaa kugundua, kumbe hata mkewe alikuwa yuko macho. Akaamua kutoijibu hoja ya mkewe! Akatulia kimya, akajaribu kuujenga umakini kwa kuusikiliza upepo uliokuwa ukiendelea kuvuma na kubashiri mvua ingenyesha wakati wowote.
“Baba Sai…baba Sai!” ghafla mkewe aliita kwa sauti inayonong’ona na ikiwa na hofu.
“Nakusikia,” baba Sai alijibu, lakini naye alijishangaa kujisikia sauti yake ikiwa na kitetemeshi cha woga. Hakujua kwa nini alifikwa na hali hiyo hasa akizingatia kuwa, kisiwa chao hakikuwa na uhalifu wa wizi au kuwepo kwa wanyama wakali.
“Nenda uani ukaangalie kuna nini!” mkewe alisema kwa suti ileile ya kunong’ona. “Si unaisikia mifugo inavyolia kwa hofu huko uani?”
“Huenda upepo mkali unawaogopesha!” baba Sai alisema na kujaribu kuuficha woga uliokuwa umeanza kumtawala, akairekebisha shuka na kujifunika vizuri. “Watanyamaza wenyewe upepo ukitulia,” alisema na kisha akazuga kulala.
Mkewe hakujibu, akabaki kuusikiliza upepo uliokuwa ukiendelea kuvuma.
Dalili za kubadilika kwa hali iliyopo nje ikawa haipo. Baba Sai aliyekuwa amezuga kulala naye alijikuta akiukosa utulivu. Kulikuwa na kitu kilichokuwa kikimsumbua; nacho ni woga! Hakuwa na jadi ya kuogopa, hata wakazi walikuwa wakimwogopa na wengi wao walimwekea dhana ya kuwa, amechanjia dawa inayompa nguvu. Kwa nini niogope? aliendelea kujiuliza swali hilo bila ya kupata jibu hadi usingizi ukamchukua bila ya kutarajia.
*******
KWENYE fukwe za bahari kisiwani humo usiku huo, ngalawa za uvuvi zilizokuwa zimeegeshwa ziliyumbishwa na mawimbi ya bahari yaliyokuwa yanapiga kwa nguvu na kuzifanya nyingine zikatike kamba zilizofungiwa nanga, zikakotwa hadi kwenye upwa. Ghafla kwenye kiza kinene kilichotanda angani kukapiga mwanga mkali uliofanya mawingu yaliyokuwa yamefukiwa na giza yaonekane kwa uwazi na mwonekano wake uliogopesha. Mwanga huo ulimulika hadi ndani ya nyumba za wakazi wa kisiwani humo. Mlio wa radi wenye nguvu ukafuatia na kuwashitua kwa hofu wakazi wote.
Eneo linaloitwa, ‘Makaburi ya Zamani’ jina lililotokana na kuwepo kwa makaburi yaliyozikiwa wafu miaka mingi iliyopita, ambalo halitumiwi tena kufanyiwa maziko, liligeuka kuwa kichaka cha pori baada ya kuachwa kwa miongo kadhaa bila kufanyiwa huduma yoyote. Eneo hilo ambalo lina mibuyu mingi na linaloonekana kuwa pweke wakati wote, lilikuwa likiogopwa na wakazi kutodiriki kuliingia kutokana na hofu iliyojengwa kuwa, lilikuwa likihifadhi nyoka wengi wakubwa aina ya Chatu. Usiku huo, ule mwanga ulionekana kuzidi kuwaka kwa nguvu kwenye eneo hilo kuliko maeneo mengine.
Moja ya kaburi lililojengwa kwa mawe kwenye eneo hilo likapasuliwa na radi ile na kuacha ufa mkubwa ulioingia hadi ndani. Moshi mdogo ukaanza kujitokeza kwenye eneo lenye ufa na kuelea hewani. Ukaendelea kukua kidogo kidogo, hatimaye ukawa ukungu mzito mweupe, ukajitandaza kwenye makaburi mengine ya jirani na kaburi hilo ambayo yalikuwa tisa. Makaburi hayo nayo yakafanya nyufa baada ya kutandwa na ukungu huo. Nyufa zilizojitengeneza kwenye makaburi yote yaliyozungukwa na ukungu zikaanza kumeguka na kumomonyoa makaburi hayo.
Radi nyingine ikapiga, mlio wake ukapasua anga na kukatiza na kutokomea kama ndege ya kijeshi, kisha ukimya ukajijenga. Ghafla kukasikika mlio kutoka mbali uliofanana na wa mbweha aliyebweka mara moja. Mchanga uliokuwa juu ya makaburi ulianza kujiachia na kutumbukia kufanya mashimo. Viwiliwili mfano wa binadamu vikiwa vimefunikwa na sanda nyeupe vikaanza kujitokeza kutoka kwenye mashimo hayo na kumwaga michanga iliyokuwa imewafunika, vikijiinua kutoka kwenye kulala na kujiweka kitako, kisha vikajiinua na kusimama wima. Walipokuwa wamesimama kukawafanya waonekana kama mazezeta yaliyokuwa yakihaha kwa kuhangaisha nyuso zao kwa kunusanusa kama waliokuwa wakiutafuta mwelekeo wa harufu waliyoinusa.
Ngozi zao za usoni zilikuwa zimesinyaa na kugandana na nyuso zilizokondeana zilizotisha. Nyuso hizo zilikuwa ndefu kama za kunguru lakini mwonekano wake ukiwa wa kibinadamu. Macho yao hayakuwa na mboni, yakawa kama yaliyojigeuza, Hawakuongea wala kutoa sauti ya aina yoyote, wakawa kama magoigoi yasiyojua yanataka kufanya nini. Mmoja akaanza kutembea kigoigoi kuelekea upande yalipo makazi ya watu, wengine nao wakamfuata, na kila walivyotembea, ukungu nao ukawa unawazunguka!
Ikaanza kama mchezo wa kuigiza!
****
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
HALI ya nyumbani kwa baba Sai kukawa si shwari tena, kukurukakara za mifugo inayohangaika uani ikazidi kusikika. Mama Sai ambaye muda wote alikuwa yuko macho akashindwa kuivumilia hali hiyo. Akakiinua kichwa kwa haraka kama mtu aliyesikia kitu, akatulia kwa umakini kusikilizia tena. Ghafla na kwa haraka akamwangalia baba Sai, akamsikia akikoroma!
“Baba Sai…baba Sai,” alimwamsha baba Sai huku akimtingisha.
Baba Sai akashituka kwa nguvu kama aliyepagawa, akageuka kumwangalia mkewe kwa macho yaliyomtoka pima. “Nini?” aliuliza kwa shinikizo kisha akaangalia kandoni mwake kama mtu aliyetarajia kukiona kitu cha kuogopesha.
“Sikiliza!” mama Sai alisema kwa sauti ya kunong’ona na kuganda.
Baba Sai naye akaganda, akatulia kusikiliza. “Ni kitu gani!” aliuliza huku akionyesha kusikia kitu.
“Nahisi kama kuna kitu kinachotembea-tembea uani!” mama Sai alisema kwa kunong’ona. “Nenda kaangalie, labda chatu amevamia mifugo.”
Baba Sai akaamka, akaikaza vizuri saruni yake kiunoni. Akawasha taa ya kandili kisha akachukua panga.
“Mwamshe Sai, mwende pamoja!” mama Sai alishauri kabla ya baba Sai hajatoka chumbani.
Baba Sai hakujibu. Aliufungua mlango wa chumbani na kutoka. Mama Sai aliyekuwa akipigwa kwa nguvu na mapigo ya moyo kutokana na woga, aliinuka kutoka kitandani na kufuata nyuma ya baba Sai, lakini akaishia kwenye kizingiti cha mlango wa chumbani. Akaanza kuita kwa sauti ya chini, “Sai…Sai!” huku akiielekeza sauti yake kwenye chumba mkabala na chumba chao ambacho ndicho chumba cha mtoto wao wa kiume.
Sai mwenye umri wa miaka kumi na tano aliitika kutoka chumbani kwake, wakati huohuo mama Sai akamsikia mumewe akiufungua mlango wa uani.
“Toka nje!” mama Sai alimwamrisha mwanaye kwa sauti isiyo na ukali.
Sai aliufungua mlango wa chumbani kwake, akajitokeza mlangoni.
“Mfuate baba yako uani!” mama Sai alisema kwa sauti iliyoonyesha kiwango cha juu cha woga.
Sai akaangalia upande wa uani akauona mlango wa uani ukiwa wazi. “Kuna nini?” aliuliza.
“Unauliza kuna nini?” mama Sai aliuliza kwa sauti iliyoonyesha kutoridhika na swali la mwanaye. “Nenda, mfuate baba yako!” alikaripia.
Sai akakiruka kizingiti cha mlango wa chumbani kwake na kuanza kumfuata uani baba yake. Lakini akasimama ghafla kuganda baada ya kusikia kukurukakara zenye vishindo kutoka uani. Akaujenga umakini wa kusikilizia. Baada ya sekunde chache akamsikia baba yake akipiga kelele, “Nakufaa!”
Sai aligeuza na kurudi mbio hadi usawa wa milango ya chumba chake na cha wazazi wake ambako mama yake naye alikwishapotea mlangoni baada kurudi mbio chumbani. Akageuka nyuma huku akitweta kwa woga, akauangalia mlango wa uani uliokuwa wazi!
Kukawa kimya!
*******
SAA nne asubuhi Sajini wa Polisi aliwasili nyumbani kwa baba Sai akiwa na baiskeli. Aliiegesha baiskeli ng’ambo ya pili ya barabara kwenye nyumba iliyo mkabala na nyumba ya baba Sai na kuteremka. Nje ya nyumba ya baba Sai na nyumba zilizo jirani na nyumba hiyo kulikuwa na makundi tofauti ya wanaume waliokuwa wamekaa nje ya vibaraza vya nyumba hizo, wote kwa pamoja wakageuka kumwangalia sajini huyo wa polisi alivyokuwa akiiegesha baiskeli yake. Makundi hayo ambayo uwepo wao uliletwa na taarifa za kifo cha baba Sai kilichotokea usiku, yalijikuta yakinong’ona huku yakimwangalia askari huyo.
Baada ya sajini huyo kuiegesha baiskeli, alikatiza barabara kuelekea ng’ambo ya pili ambako ndiko ilipo nyumba ya baba Sai huku akihisi macho ya watu waliokuwepo yakimwangalia. Akiwa ndani ya sare za kazi, alitembea kwa mwendo wa taratibu na kabla hajaifikia nyumba aliyokuwa akiiendea, baadhi ya watu wawili au watatu wakaonekana kwenda kumpokea.
Aliitwa Sebastian, jina ambalo lilikuwa nadra kutamkwa na wakazi wa hapo kwa sababu, wote walimzoea kumuita, ‘Sajini Seba.’ Hakuna ambaye alikuwa hamjui askari huyo hapo kisiwani kutokana na tabia yake ya ucheshi na upole ambayo ilipendwa na kila mtu. Aliweza kujijengea umaarufu mkubwa kutokana na uwezo wake wa kusuluhisha mizozo midogo midogo ya kifamilia na wakati mwingine hata mifarakano ya kindoa.
Sajini Seba ambaye ni mrefu na mpana wa umbo baada ya kupokewa na watu hao walioonekana kuwa na uhusiano wa karibu na baba Sai, aliongozwa kuelekea ndani ya nyumba.
“Ikoje hali ya mama Sai kwa sasa?” Seba aliuliza wakati akiingia ndani ya ukumbi uliojaa wanawake ambao wengine walikuwa wakiendelea kulia.
“Ameanza kupata utulivu,” mmoja kati ya watu waliompokea alijibu.
“Kwa hiyo sasa hivi upo uwezekano wa kuzungumza naye?”
“Nina imani, sasa hivi mtasikilizana.”
“Hali yake ilikuwa mbaya asubuhi nilivyofika,” Sajini Seba alisema.
“Sasa hivi ametulia.”
Wakaingia kwenye chumba alichokuwemo mama Sai. Walimkuta mama Sai akiwa amezungukwa na wanawake wa rika lake, wote wakiwa wamekaa kwenye jamvi.
Mama Sai mwenye mwili mnene uliomfanya aonekane mfupi kuliko urefu wake ulivyo alikuwa akitarajia kufikisha miaka arobaini ndani ya miezi miwili ijayo. Uso wake ni wa duara wenye uzuri wa wastani na uliokaa kitoto, ulitawaliwa na ucheshi wa mara kwa mara na alikuwa akipenda kuongea kwa upole. Wakati Sajini Seba alivyokuwa akiingia chumbani, yeye alikuwa akizungumzia kwa upole wenye simanzi kuhusu tukio la kuuawa kwa baba Sai huku akisikilizwa kwa makini na wanawake wenzake. Mara alipomwona Sajini Seba akiingia, akaacha kuzungumza.
“Karibu baba,” mama Sai alimwambia Seba.
“Ahsante,” Sajini Seba alisema na kupiga goti mbele ya mama Sai na kumpa mkono. “Pole!” aliongezea.
‘Nimeshapoa baba,” mama Sai alisema na kuuangusha chini uso wake, kisha akaguna kwa simanzi.
“Naomba unisamehe kama nitakuwa nakusumbua,” Seba alisema. “Lakini unaonaje endapo mimi na wewe tutaachwa peke yetu kwa muda humu chumbani? Nataka kuzungumza nawe, nataka kupata picha halisi ya jinsi baba Sai alivyokufa.”
“Sawa baba,” mama Sai alijibu bila ya kusita.
Waliokuwemo mle ndani walianza kuondoka kabla hawajatakiwa kufanya hivyo, wakawaacha wao wawili.
“Unaweza kunieleza,” Sajini Seba alisema baada ya kuhakikisha mtu wa mwisho ameshatoka.
Mama Sai alijaza pumzi kifuani na kuzitoa kwa mkupuo. “Nadhani jana usiku uliishuhudia hali ya hewa ilivyokuwa?”
“Ndiyo,” Seba alikubali. “Kulikuwa na upepo mkali.”
“Hali hiyo ndiyo iliyonifanya nimwamshe baba Sai baada ya kuisikia mifugo ikilia kwa hofu uani. Nilihisi wameingiliwa na chatu, nikamwomba baba Sai aende kuangalia kulikoni huko uani.” Mama Sai alinyamaza na kutulia, Sajini Seba naye akaamua kukaa kimya. “Baba Sai akaamka kutoka kitandani,” mama Sai aliendelea na kisa chake. “Alitoka chumbani akiwa ameshika panga na taa ya kandili, nikamuita mwanangu Sai, ili aende akasaidiane na baba yake uani. Lakini kabla ya Sai hajafika uani kuungana na baba yake, tukamsikia baba Sai akipiga kelele kwa kusema, ‘Nakufa!’ Tukapigwa na butwaa mimi na mwanangu, lakini tukajipa moyo wa kwenda uani kuangalia kuna nini hadi baba Sai adai anakufa! Ulikuwa ni uamuzi mgumu, hasa kwa mwanamke akiwa na kijana mdogo wa kiume kuweza kutoka uani kwenye mazingira kama hayo, lakini mimi na mwanangu tulitoka, hatukuogopa! Tulipofika uani tulimkuta baba Sai amelala chini, panga lake likiwa limeanguka karibu na alipolala. Tulijaribu kumwita, akawa hajibu. Lakini tulipomsogelea tukamwona akitokwa na damu za puani na masikioni. Nikapiga kelele za kuita majirani ambao walikuja, baada ya kufika na kumwangalia wakagundua alikwishakata roho! Hivyo ndivyo ilivyokuwa!”
Akiwa ameyaandika maelezo ya mama Sai kwenye daftari dogo, Sajini Seba aliyekuwa amekaa juu ya kigoda, aliing’ata kalamu aliyokuwa akiitumia na kutulia kwa sekunde chache. Akaitoa kalamu mdomoni na kusema, “Nini kingine ulichokiona?”
“Hakuna!” mama Sai alijibu.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Hukusikia hatua au kuona kiwiliwili chochote kilichokuwa kinakimbia baada ya nyie kufika uani?”
“Sikusikia wala kuona.”
“Ulitia mashaka yoyote, pengine kuingiwa na hisia huenda mumeo aliuawa na kitu fulani?”
“Sai na majirani waliokuja walijaribu kulizunguka eneo lote la uani na kutoka nje lakini hawakufanikiwa kuona chochote. Kwa hiyo hata mimi nilibaki kwenye mshangao kama walivyokuwa watu wengine.”
“Eneo aliloangukia baba Sai, kulikuwa na dalili zozote za purukushani, kama vile vitu kusambaa-sambaa na kutibuliwa kwa michanga kuonyesha kulikuwa na patashika?”
“Sikuona!”
“Unamaanisha kulikuwa shwari?”
“Hakukuwa na dalili zozote kuonyesha palikuwa na purukushani.”
“Uani kuna milango mingapi ya kuingilia?”
“Miwili. Mmoja wa kuingilia moja kwa moja uani kutokea nje, na mwingine ni wa kupitia nyumba kubwa.”
“Ilikuwa imefungwa kabla hamjaenda kulala?”
“Na mimi mwenyewe ndiye niliyeifunga yote.”
“Baada ya mumeo kuuawa, milango ilikuwa ipo kwenye hali gani?”
“Yote ilikuwa imefungwa kwa ndani.”
“Una hakika nalo?”
“Niliukuta mlango wa mbele wa nyumba ukiwa umefungwa kwa ndani wakati nilipokwenda kuwafungulia majirani.”
“Na wa uani?”
“Nao ulikuwa umefungwa! Niligundua hilo wakati majirani walipotaka kutoka nje kupitia mlango wa uani kwenda kuangalia kama kungekuwa na kitu cha kukitilia mashaka. Lakini kabla hawajatoka, wakawa wameshangaa kuukuta mlango huo ukiwa umefungwa kwa ndani!”
“Unataka kuniambia, kilichomuua baba Sai hakikupitia kwenye mlango?”
“Sijui!”
“Kabla ya kumwamsha baba Sai, umesema uliisikia mifugo ikilia kwa hofu?”
“Ndiyo.”
“Hali kama hiyo iliwahi kutokea kabla?”
“Hapana.”
“Kwa hiyo ilikushangaza?”
“Na kunishitua pia!”
“Ni kitu gani kilichokufanya ufikirie kuwa ni chatu ndiye aliyewaingilia?”
“Kwa sababu kisiwani kwetu hakuna wanyama wengine wakali.”
“Unadhani kunaweza kukawa na mtu yeyote anayeweza akamfanyia ubaya baba Sai?”
“Baba Sai aliishi kwa amani na kila mtu, sikuwahi kumwona akigombana na mtu ingawa alikuwa akisifiwa kuwa na nguvu.”
“Kwa hiyo mpaka sasa hivi hujui ni kipi kilichomuua baba Sai?”
“Sikijui.”
“Tunaweza tukaenda pamoja uani?”
“Sawa.”
Watu hao wawili wakaondoka chumbani na kusindikizwa na macho ya kinamama hadi uani ambako nako kulikuwa na shughuli za upishi. Seba alivyoiona ile hali ya uani, akatambua kusingekuwa na aina yoyote ya ushahidi kutokana na kupanguliwa kwa mandhari ya uani iliyotokana na maandalizi ya upishi.
“Samahani!” Seba alisema huku akiwaangalia akinamama waliokuwa uani. “Mlipangua-pangua huku uani wakati mkiandaa maeneo ya kupikia?”
Jibu halikutoka papohapo. Akinamama walianza kuangaliana usoni kama vile swali hilo liliwatega. Wakaanza kuulizana, ni nani atakayelijibu swali hilo.
“Ndiyo kulipanguliwa!” mama mmoja mtu mzima alijibu ghafla, tena kwa kujiamini kama vile alishaamua, liwalo na liwe! “Lakini walioifanya kazi hiyo ni wanaume, sijui utataka tukuitie?” alimalizia na kumwangalia Seba usoni.
“Hapana,” Seba alijibu kwa utulivu na kuiangalia hali ya uani ilivyo huku macho yake yakihama kwa utulivu kwa kuangalia kila eneo. Akageuka kutaka kuzungumza na mama Sai, akamwona mama huyo kama aliyeduwaa akiangalia kitu kinachoelea hewani.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment