IMEANDIKWA NA : AMRI BAWJI
*********************************************************************************
Sehemu Ya Kwanza (1)
Wakati Edward anafika kwenye kituo cha mabasi yanayotoka Arusha kwenda Dar es Salaam, basi lililokuwepo tayari kwa safari ni moja, mengine yote yalikwishaondoka. Hakuwa na wasiwasi, kwani alikuwa tayari amekwishakata tiketi yake tangu siku iliyopita. Wapiga debe walimzogoma kwa kuwahi wamkatie tiketi. Aliwajulisha kuwa yeye tayari amekwisha kata. Mkononi mwake alinyanyua sanduku la wastani lenye mabaka mabaka. Aliingia ndani ya gari taratibu na kutafuta nafasi iliyokuwa tupu kwenye sehemu za kuwekea mizigo na kupandisha sanduku lake, Kisha akatia mkono kwenye mfuko wa shati, akatoa tiketi yake na kuiangalia.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Kiti chake kilikuwa na nambari 30 upande wa dirishani. Gari hili lilikuwa aina ya viti viwili viwili kila pande. Akaangaza macho huku na huko, kwa madhumuni ya kukiona kiti nambari 30, na tegemeo ni kukiona kiti hicho kitupu, hakikukaliwa na mtu sababu kiti chenye nambari hiyo ni chake yeye. Lakini badala yake tayari kiti hicho kilikuwa kimekaliwa na msichana mmoja mrembo.Aliangalia tena tiketi yake aliyokuwa nayo mkononi kuhakikisha kuwa nambari 30 ni yake kweli. Akaona ni kweli yake. Alimwendea yule msichana na kumuomba radhi ampishe kwenye kiti chake.
“Samahani dada, naona kiti hiki ni changu.” Edward aliomba kwa heshima na unyenyekevu.
“Kiti hiki ni changu kaka, angalia vizuri tiketi yako” Msichana yule alijibu bila wasiwasi na kuendelea kujiweka vizuri juu ya kiti. Edward aliangalia tena tiketi yake na kwa hilo hakuwa na shaka yeyote kuwa tiketi nambari 30 na kiti chenye nambari hiyo ni chake. Kwa hiyo, aliitoa ile tiketi yake na kumkabidhi yule msichana huku akisema: “Hebu tafadhali dada nisaidie kuisoma hii tiketi, huenda nimekosea. Hiyo siyo nambari 30?” Msichana yule aliipokea na kuisoma, kisha naye akatoa yake na kumkabidhi Edward huku naye akisema:
“Hebu na mimi isome hii yangu kama sikukosea ni nambari 30 nayo pia…Mimi ndio nimekwishakaa hivi, sasa wewe ni bora umtafute kondakta akutafutie kiti cha kukaa kabla gari halijaondoka” Yule msichana alimshauri Edward. Edward alimtafuta kondakta na kumueleza hali halisi ilivyo kati ya yeye na yule msichana, na kuhusu kukatiwa tiketi nambari ya kiti kimoja. Kondakta yule alikuja mpaka pale karibu na viti alipokaa yule msichana. Akaomba aoneshwe tiketi zote mbili. Baada ya kuzikagua na kulinganisha na karatasi ya orodha ya majina ya abiria aliyokuwa nayo, aligundua kuwa tiketi nambari 30 ni ya Edward, na yule msichana alikatiwa tiketi nambari hiyo kwa makosa. Baada ya mjadala mrefu, Edward alikubali kumwachia yule msichana kiti na yeye atafutiwe kingine. Edward alipatiwa kiti nambari 31, ambacho ni ubavuni mwa yule msichana. Kwa hiyo walikaa pamoja, lakini kila mtu na kiti chake.
* * *
Edward ni mtoto pekee wa Bwana na Bibi Jonathan Oloi. Ni kijana mrefu wa kimo, maji ya kunde na mwenye sura jamali. Ni mcheshi sana pale panapo stahili na ni mkimya mno pale ambapo hastahili kusema. Ana umri wa miaka 27. amemaliza elimu ya sekondari kidato cha sita, na baada ya hapo alipata nafasi ya kwenda Australia. Huko alijiunga na chuo cha taaluma ya upigaji picha, Utengenezaji na uhariri wa filamu fupi za matangazo ya biashara.Alichukua taaluma hiyo kwa muda wa miaka mitatu. Baada ya kurudi, aliajiriwa na shirika la kigeni kwa muda wa miaka minne.
Mkataba wa shirika hili ulikwisha na baada ya kukaa bila kazi kwa takribani
miezi sita. Sasa amepata ajira nyingine ambayo makao yake makuu ni Dar es Salaam. Kwa hiyo siku hiyo alikuwa anasafiri kutoka Arusha ambako ndio kwao, na kuelekea Dar es Salaam kwa ajili ya ajira hiyo.
Mzee Jonathan Oloi, baba yake Edward hakuwa mchache wa fedha. Alikuwa anazo biashara zake ndogo ndogo. Anayo mashamba makubwa ya kahawa, na mifugo ya kutosha. Kwa kuwa mtoto wake alikuwa ni huyo huyo mmoja tu, hivyo (Edward au Edo) walikuwa naye karibu wakati wote. Mzee Oloi hakupendelea suala la kijana wake kufanya kazi za kuajiriwa. Lakini Edo mwenyewe alikuwa anapenda mno kazi yake ya kupiga picha za filamu fupi za matangazo ya biashara. Zaidi ya yote hayo, Bwana Jonathan Oloi na mkewe walikuwa wanataka mno mtoto wao wa pekee aoe, waliweza kumtafutia mchumba ambaye waliona kuwa atafaa. Kwa kuwa wazazi wa binti huyo hawakuwa na uhusiano wa mbali na familia ya marehemu baba yake Mzee Oloi, mazungumzo yalifanywa na wazazi wa pande zote mbili, tangu Edo alipokuwa Australia na walikubaliana. Baada ya Edo kurudi toka ngámbo, kabla hata hajaanza kazi, alijulishwa habari hizo. Edo alikataa na kutaka afanye kazi kwanza.
Ajira yake ya kwanza ilipokwisha alikaa nyumbani kwa muda wa miezi sita. Suala la yeye kuoa lilizungumzwa tena na akatakiwa na wazazi wake akubali mchumba aliyechaguliwa na afunge ndoa. Lakini Edo alikataa kabisa na kusema,
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Sikilizeni wazee wangu, mimi bado sijawa mkubwa wa kukimbilia kufunga ndoa hilo mosi. Pili, hata kama naamua kuoa basi nitaoa mke niliye mchagua mimi mwenyewe niliye mpenda. Sintaoa mwanamke ambae hata hatujajuana, ni wazazi tu wamekaa na kupanga. Nitatafuta mwenyewe mke wa kuoa.” Kwa vile ni mtoto pekee, Edo alikuwa na sauti sana kwa wazazi wake, isitoshe walimlea ki ujukuu. Baba yake Edo alimwambia mwanae,
“Edo mwanangu, ingawa wewe mwenyewe unajiona u mdogo, bado hujawa wa kuoa, lakini sisi wazazi wako tunajiona kuwa tu wakubwa sasa, tuna hamu na wajukuu. Kwa kuwa mtoto wetu ni wewe tu, basi ndio maana tungependa uoe kabla Mungu hajamchukua hata mmoja wetu.”
Mama yake Edo naye alimrai mwanae pia kwa kusema,
“Edward fahamu sisi ni wazazi wako, isitoshe wewe uko pekee yako, hivyo pendo letu lote lipo kwako. Unadhani sisi tunaweza kukupa chochote kilicho kibaya kwako.Haiwezekani hivyo basi mchumba tulie kutafutia, tunaamini atakufaa na anatoka katika familia inayofanana na yako. Ukoo huo kwa mbali unahusiana na babu zako. Mwanangu fikiri sana jambo hili.” Edo aliwasikiliza wazazi wake kwa makini kisha naye akatoa rai zake pamoja na maombi kwa kusema.
“Baba na mama wapendwa, kwa kuwa furaha yenu ni kuniona mimi nimo ndani ya furaha, hilo ninalikubali wala sina shaka nalo. Na mchumba mlie mtafuta kwa ajili yangu naamini mmefikiria sana mpaka kumpata. Na ninyi na wazazi wake mkaamua mpange mpango wa mimi na huyu binti tuoane, vema. Lakini je mmepata kusikia kauli yeyote ya huyo binti kuhusu mpango huu?”.
“Hapana” Walijibu kwa pamoja.
“Kwa hiyo hamuoni wazazi wangu kuwa ninaweza nisiwe na furaha katika ndoa yangu endapo huyu binti atakubali tu kuolewa kwa kuwaridhisha wazee wake? Huenda asinipende kama mnavyotaka ninyi. Kwa nini nisipewe nafasi ya kuchagua mchumba mimi mwenyewe? Iwapo furaha yenu ndio yangu, basi tafadhali naomba mnipe muda, angalau wa miezi michache nitafute mchumba mimi mwenyewe.”
“Ina maana ukatafute huko Dar es Salaam uliko pata kazi?” Baba yake aliuliza.
“Popote pale katika ulimwengu huu baba, mradi tu mwanamke huyo aniridhi nafsi yangu”
Wazazi wake Edo walitulia kimya, baadaye kidogo mzee Oloi alimwambia mwanawe,
“Kama hivi tunavyosema, tulikwisha panga na tunajua linalokufaa ni nini. Hivyo basi tunakupa nafasi hiyo ya kuchagua mchumba atakae kufaa mwenyewe, lakini itakapotimu miezi sita, kama bado hujapata wa kumuoa, basi rudi uje uoe huyu tuliye kuchagulia, sababu sintavunja uchumba huu mpaka wewe umeoa.”
“Sawasawa baba nimesikia.”
Hayo yalikuwa ni mazungumzo ya mwisho kati ya Edward na baba yake na mama yake, kabla ya kuondoka Arusha kuelekea Dar es Salaam.
* * *
Gari lilianza kuondoshwa taratibu kutoka stendi ya mabasi ya Arusha. Kilometa chache baada ya kutoka hapo, walifika Usa River. Edo baada ya kuhakikisha kuwa sasa hana wasiwasi hapo alipokaa aligeuza kcihwa chake kumuangalia msichana aliyekaa naye karibu.
Kwa mara ya kwanza alitambua kuwa ni mzuri, kwa hali halisi ya uzuri utakikanavyo, hasa wa kisasa. Pamoja na kuwa msichana huyu alikuwa amekaa juu ya kiti cha basi, alionyesha dhahiri kuwa ni mrefu, alikuwa mwembamba, mweusi wa wastani na nywele zake zilizotengenezwa ki unadhifu zilikuwa zimeteremka hadi mabegani kwake. Edo alishikwa na hamu ya kutaka kumjua zaidi. Msichana huyo aliyekuwa kiti cha dirishani, alionekana kupendezewa zaidi na yanayopitwa na gari huko nje, kuliko mvulana aliyekaa naye karibu. Edo alijikohoza kidogo na kusema,
“Samahani dada, ni vizuri tukafahamiana, kwa vile tunasafiri pamoja. Mimi jina langu ni Edo Oloi, ni mwenyeji wa Arusha, na ninaelekea Dar es Salaam.” Alitoa tabasamu kubwa wakati akisema hivi, na yule msichana aligeuza uso kumtazama, alitabasamu naye pia, akajibu,
“Mimi jina langu ninaitwa Lulu Frank, naelekea Dar”
“Vizuri sana, inaonekana tutakuwa pamoja safari yote”
“Mungu akipenda”alijibu Lulu kwa ufupi.
Baada ya hapo walikaa kimya kipindi kirefu, gari ikiwa inakata mbuga tu. Waliwasili Moshi. Baada ya muda mchache safari ilianza tena.
“Bi Lulu, Dar es Salaam ndiko unakoishi?”
“Ndio, ninafanya kazi, au tuseme ninakwenda kuanza kazi.”
“Ahaa, hali kadhalika na mimi, ninakwenda kuanza kazi.” Walinyamaza tena kimya, baadae kidogo, Edo alianza kusema kwa hamu kubwa ya kutaka kumfahamu zaidi Lulu, kwa kumwambia,
“Lulu naomba unisamehe tafadhali, kabla sijakuuliza swali ambalo ni la kibinafsi kabisa.”
Lulu alimtazama Edo kwa sura iliyojaa wasiwasi baada ya kusikia hivyo ilibidi amuulize Edo,
“Ni swali gani hilo? Mbona unanitisha!!”
“Hapana, usiogope kabisa, swali lenyewe ni la kawaida sana, lakini ni kwa watu wanaojuana, kwa wasiojuana kama hivi mimi na wewe, ni lazima tuombane radhi kwanza.”
“ Sawa, Bwana Edward, niko radhi, niulize tu.” Edo kusikia hivyo alitulia kidogo na kuinamisha uso wake chini kama vile amesahau swali alilokuwa anataka kumuuliza Lulu, kIsha kwa ghafla alimtazama usoni na kumuuliza,
“Hivi Lulu umekwisha olewa? Au tusemee… una mume? Au mchumba?.” Lulu alitoa tabasamu kubwa lililomfanya aonekane mrembo zaidi na kujibu,
“Hapana, bado sijaolewa. Sina mume wala mwanaume na… pia sina mchumba.”
“Je una umri gani?”
“Miaka ishirini na mbili, kwa nini? Mbona unaniuliza umri wangu?”
“Sababu, jinsi ulivyo. Nina maana umbo lako zuri, sura yako nzuri, haiyumkini msichana kama wewe kuwa huna mume, mwanaume wala mchumba mpaka wakati huu.”
“Basi nisemayo ni yakini, sina uhusiano wa kimapenzi na mwanamume yeyote.”
“Kwa kukosa au kwa kupenda?”
“Kukosa ni vipi na kupenda ni vipi?” Lulu aliuliza swali hili huku akicheka cheka.
“Kukosa ni kuwa hakuna mtu aliyewahi kukutaka kama rafiki yake, nina maana hakuna mwanamme. Kupenda nako ni kuwa unatakiwa na wavulana lakini wewe hutaki…huwataki kwa urafiki, mapenzi na wala kuoana nao.” Lulu aliangua kicheko akacheka sana, kiasi cha kumpa tamaa Edo hata akaona sasa amekwisha upata mwanzo wa uzoefu na Lulu, jambo ambalo amelidhamiria. Lulu alimtazama Edo na kusema,
“Unasikia Edo, ni kweli sina mvulana yeyote kwa kukosa.”
“Siyo kweli! Una maana hujawahi kutakiwa na mvulana yeyote maishani mwako!!”
“Ndiyo ninatakiwa takriban kila siku ya maisha yangu, tangu nipate fahamu, lakini hao wavulana wanaonitaka sio kwa dhati ya urafiki au kunioa, bali dhamira zao kwangu ni kuchezeana tu, jambo ambalo siko tayari nalo…Mmoja kati ya walionitaka, alikuwa na dhamira ya kunioa, lakini kwa kupitia kwa wazazi wake yaani ndoa ya kupangiwa; na mimi ningependa kuolewa na mvulana ambaye ninampenda. Bahati mbaya sijawahi kupenda mvulana yeyote kimapenzi hasa kama msichana na mvulana. Nadhani nimejieleza vya kutosha!” Lulu alimalizia kwa kutabasamu huku akimuangalia Edward ambaye wakati huu alikuwa ametulia na kumsikiliza Lulu kwa makini sana kama vile mjukuu anayesikiliza hadithi aipendayo toka kwa bibi yake.
“Kiasi umejieleza. Hujawahi kupenda… kama mimi. Hupendi ndoa za kupangiwa… pia kama mimi, na umepewa nambari ya kiti cha gari nambari 30, vilevile kama mimi! Sijui ni lipi jingine?” Edo alisema maneno haya kwa sauti ya uchovu na kujaribu kumfanya Lulu aamini kuwa mambo yao mengi yanafanana.
“Ina maana wewe pia Edo hujawahi kupenda?”
“Hapana, kabisa… sijapenda mtu.”CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Na… pia hupendi ndoa za kupangiwa!!” Sauti ya chini ilisikika iliyokuwa na mchanganyiko wa maelezo na swali.
“Hivi nisemavyo, nimetoka kumkatalia baba yangu na mama yangu walionizaa kunioza mke waliyemchagua wao.”
“Na kwa nini katika umri ulio nao bado hujapenda msichana tu.”
“Kwa sababu bado sijakutana na msichana ambaye… tunapendana.”
“Mungu atakupa.”
“Aamen.”
* * ** * *
Saa kumi na mbili na dakika thelathini na saba jioni, gari walilokuwa wakisafiria Edward na Lulu, liliwasili kituo cha mabasi cha Kisutu jijini Dar es Salaam. Waliagana, kila mmoja akaelekea sehemu yake aliyokuwa amepanga kufikia. Ingawa Edo alikuwa na shauku ya kutaka kukutana na Lulu tena, lakini hakuweza kuielezea hali yake hiyo. Alisitasita kisha akachukua begi lake na kuondoka. Lulu alifikia eneo la Upanga ambako wanaishi dada yake na shemeji yake. Wakati anaingia nyumbani humo, ilikuwa tayari giza limekwisha ingia. Alipokelewa vizuri na dada yake. Alioneshwa chumba cha wageni ambacho aliambiwa kwa sasa kitakuwa chake. Chumba hicho kilikuwa cha kujitegemea, choo kilikuwemo humo humo.
Kwa hiyo Lulu alitupa begi juu ya kitanda na kuanza kulifungua kwa minajili ya kutoa nguo za kubadilisha kabla hajaingia bafuni kuoga. Alianza kugundua tofauti wakati ameanza kufungua begi hiyo. Ujazo wake haukuwa kama anavyokumbuka begi lake lilivyokuwa. Hili kidogo limepojaa… limepungua kidogo.
Alianza kuingiwa na wasiwasi. Alifungua begi hilo taratibu. Kweli aligundua kuwa hilo begi silo lake, amechukua begi la abiria mwingine ambalo limefanana na lake kwa makosa. Tena la abiria wa kiume, kutokana na vitu vilivyokuwemo humo ndani ya begi hilo ni vya kiume na nguo za kiume. Lulu alitoka mbio chumbani na kwenda kumueleza dada yake. Baada ya hapo walitoka pamoja na shemeji yake kuelekea kituo cha mabasi ya Arusha, Kisutu. Gari walilokuwa wamesafiria walilikuta lipo, lakini hakukuwa na begi yeyote. Walipojaribu kuwauliza wahudumu wahusika, walijibiwa kuwa hakuna begi yoyote iliyokuwa imebaki ndani ya basi, wala hakuna mtu aliyekuja kulalamika kuhusu begi. Lulu aliamini kuwa yeyote yule aliyechukua begi lake, alichukua kwa makosa ni kuwa mabegi yamefanana; sababu hata yeye aliamini kabisa kuwa begi alilokuwa nalo ni lake mpaka alipolifungua. Wasiwasi wake ulikuwa ni siku inayofuata ilikuwa siku ya kwenda kuanza kazi kwenye ofisi mpya iliyomuajiri, na nguo zake zote zilikuwa ndani ya begi lake, pamoja na hati zake na vyeti vyake vyote vya shule. Dada yake alimpoza kwa kumhakikishia kuwa suala la nguo atapata, walijiliwaza kuwa huenda huyo aliyechukua begi la Lulu atalirejesha kwenye ofisi ya mabasi hapo Kisutu.
* * *
Kijana wa umri wa miaka 28, maji ya kunde, si mrefu wala si mfupi, kimo chake wastani, sura yake nzuri ya kiasi, bali inayoonekana kuvutia sana kutokana na hali ya umaridadi aliokuwa nao na kila dalili za kuonekana kuwa yeye ni tajiri, hali ambayo ni kweli, alikuwa amesimama nyuma ya meza kubwa ya ofisi na kufanya umbo lake la urefu wa futi tano na inchi saba hivi lionekane vizuri. Alikuwa amevaa suti nadhifu ya rangi ya samawati, shati jeupe na tai pana yenye rangi za mchanganyiko wa kufanana na suti hiyo. Kwa jina kijana huyo anaitwa Onespot Pato, Mkurugenzi Mtendaji wa ADFC Ltd, kampuni inayoshughulika na mambo ya mitindo ya nguo na matangazo ya biashara ambayo Edward Oloi amekuja kuanza kazi kwa siku ya kwanza. Onespot Pato alinyoosha mkono wake wa kulia na kufungua kiganja chake kumpa Edward Oloi aliyekuwa amesimama mbele ya meza hiyo ya ofisi iliyokuwa kati yao. Kwa tabasamu kubwa lenye kujiamini Bwana Pato alijitambulisha,
“Karibu sana ndugu, mimi ninaitwa Onespot Pato, ndiye Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hii.” Edward nae alitoa mkono na kupokea kiganja cha Onespot huku naye akitabasamu na kusema,
“Asante sana Mr. Pato nimefurahi kukuona. Mimi naitwa Edward Oloi, natokea Arusha, nimekuja kuripoti kwa ajili ya kuanza kazi katika kampuni yako.”
“OK, yes, karibu sana ukae, ndio, nilikuwa ninategemea watu wawili kutoka Arusha. Mmoja wapo ukiwa wewe, mwingine bado hajawasili.” Edward alikaa haraka haraka, kwani alijihisi ipo tofauti kubwa kati yake na Onespot kwa wakati ule, sababu ya namna walivyokuwa wamevaa. Licha ya kuwa nguo alizokuwa amevaa Edward ni za kawaida, pia zilikuwa si safi sana, sababu zilikuwa ni zilezile alizokuwa amevaa siku iliyopita akiwa safarini toka Arusha, hakubadili.
“Habari za Arusha Bw. Oloi? “
“Nzuri tu Mr. Pato.”
Wakati huu Onespot alikuwa ameketi juu ya kiti chake kikubwa kilichopo nyuma ya ile meza kubwa ya ofisi, huku akichombezwa chombezwa na kiti hicho kilichokuwa kinaweza kuzungukazunguka.
“Sasa bwana Oloi kabla hujasaini mikataba ya kuanza kazi katika ofisi hii,
tunaweza kuona ile barua tuliyokutumia… ya kuajiriwa?” Kabla Edward hajajibu, mlango wa ofisi hiyo uligongwa kwa nje, Onespot alijibu kwa kiingereza,
“Come in.” Uso wa katibu muhtasi wa Onespot ulijitokeza na kuuliza,
“Boss kuna mgeni mwingine anasema naye pia anatokea Arusha, aingie au asubiri?”
“Muache aingie tafadhali.” Mara mlango uligongwa tena kwa taratibu, nae Onespot akajibu kwa kuvuta sauti.
“Tafadhali… ingia, karibuni.” Naye Edward aligeuza shingo yake kwa shauku ya kutaka kumuona huyo mgeni anaetoka Arusha kama yeye. Hakuamini macho yake, alikuwa ni Lulu Frank. Onespot alisimama kutoka alipokaa akitoa tabasamu la furaha kubwa na akamkaribisha.
“Karibu sana mama, have a seat please!”Alimuelekeza kukaa juu ya kiti kingine kilichokuwa mbele ya meza yake kinachoelekezana na alicho kikalia Edward. Lulu alikaa taratibu huku akimuangalia Edward kwa mtazamo unaoashiria kusema “na wewe umefuata nini hapa?”
“Eeeh, mimi ninaitwa Onespot Pato… na huyu bwana hapa, yeye anaitwa Edward Oloi.” Onespot alitamka haya kumtoa Lulu kwenye mshangao na kuendelea kusema,
“Mimi ndie mmiliki wa kampuni ya ADFC Ltd na pia ni mtendaji… Mkurugenzi Mtendaji.” Lulu alimtazama Onespot kisha akamwangalia Edward huku akitoa tabasamu la chini chini na kutamka,
“Nimefurahi kuwafahamu bwana Onespot Pato na bwana Edward Oloi… mimi jina langu ninaitwa Lulu Frank nimekuja kuripoti kuitikia barua ya wito wa kuajiriwa na ADFC Ltd hapa Dar es Salaam.” Onespot alionekana kupendezwa na kila kitu kuhusu Lulu, sura yake, umbo lake, sauti yake na hata jinsi anavyozungumza.
“Hapana shaka Lulu… sasa naomba nione zile barua zenu… samahani Lulu, huyu Bw. Oloi pia, ndio kwanza amefika kuripoti kwa ajili ya ajira vilevile.” Alinyamaza kidogo akatoa faili kubwa toka dawati ya meza yake, akaliweka juu ya meza hiyo, akafunuafunua kurasa za faili hiyo, kisha akanyanyua uso wake kuwaangalia Lulu na Edward na kusema tena,
“Naomba nione barua zenu tafadhali.” Lulu alimuangalia Edward ambaye alibaki kimya bila kuonesha dalili zozote za kutoa barua aliyotakiwa aitoe. Wote wawili walionekana kama vile wanashangazwa na ombi la Onespot jambo ambalo lilimfanya yeye Onespot nae ashangae na kuuliza, “Vipi waungwana?! Majina yenu yapo hapa ndani ya faili hili, ninachoomba ni barua zenu tu au mmeziacha mlikofikizia?” Lulu alijiweka sawa kwenye kiti alichokuwa kaketi na kusema,
“Samahani Mr. Pato, mimi kwa upande wangu, nimetokewa na tatizo kubwa jana nilipowasili hapa Dar es Salaam.”Aliinamisha uso wake chini Onespot akamuuliza,
“Ni tatizo gani hilo Lulu?”CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Wakati tunateremka kutoka ndani ya basi tulilosafiria nilichukua begi ambalo sio langu nikifikiri kuwa ni langu. Kwani limefanana kila kitu na langu. Niligundua hilo baada ya kufika nyumbani na kufungua begi hilo. Nguo zilizomo zilikuwa sio zangu ni za mtu mwingine tena za kiume. Nguo zangu na vitu vyangu vimo kwenye sanduku langu ambalo nina hakika limefanana na hili nililochukua.” Onespot alicheka kidogo baada ya kusikia habari hizo akakunja mikono yake mbele ya kifua chake na kurudi nyuma kuegemea kiti alichokikalia.
“Enhe na wewe Bwana Oloi nawe?” Edward kwa wakati wote huu alikuwa kamkodolea macho Lulu wakati anazungumza mpaka amenyamaza.
“Mimi Bw. Pato ni hivyo hivyo!”
“Ni hivyo hivyo vipi?!...Bwana Oloi, hebu kuwa serious, usilete utani!”
“Na wala sithubutu kukutania wewe wala Lulu bwana Pato. Ni kweli kabisa
nami pia nilipofika nilipofikizia, kufungua begi nakuta nguo za kike, sikutaka kuchakua tena, nilijua begi hiyo nimeichukua kimakosa, imefanana na yangu lakini sio yangu. Hebu nitazame hivi nilivyo, nimekosa hata nguo za kubadili!” Lulu alimuangalia Edward kwa kumtuliza macho kisha akasema kwa sauti ya chini,
“Inawezekana tumebadilishana mabegi wakati wa kuteremka.” Onespot alimuangalia Lulu kisha akamuangalia Edward.
“Hivi ni kitu gani kinachoendelea hapa?! Mbona siwaelewi mnazungumza nini?!”
“Tunachozungumza ni kweli bwana Pato, mimi na huyu bwana Edward tulisafiri gari moja kutoka Arusha kuja hapa Dar es Salaam.”
“Na vilevile mlikuwa na mabegi yanayofanana au sio?!” Onespot aliwauliza kwa mshangao.
“Ni kweli kabisa,” Edward alijibu kwa sauti ya chini lakini ya msisitizo wa kutaka waaminiwe wanayoyasema. Akaendelea,
“Hii habari kubwa Bwana Pato, kwani hata nambari za viti vyetu katika basi hilo hapo awali tulikatiwa nambari moja, zote nambari 30! La ajabu zaidi ni kwamba kazi tulizozijia pia mwajiri wetu ni mmoja!!.”
“Sasa hebu niwaulize, baada ya kila mmoja wenu kufungua begi ambalo si lake, hakuweza kuona nyaraka au hati zozote ambazo labda zingeweza kumtambulisha jina mwingine?!”
“Kusema kweli bwana Pato, mimi baada ya kulifungua begi na kuona nguo za kike, niligundua sio langu basi sikutaka kulipekua tena, nikiwa na imani kuwa mwenye begi hili atarudisha langu na kuulizia lake kwenye ofisi ya basi hilo tulilosafiria. Na kazi hiyo nilikuwa niifanye leo baada ya kutoka hapa, na sikujua kamwe kama ni la Lulu.” Edward alisema haya kwa utaratibu na kutaka akubaliwe.
“Hali kadhalika nami pia sikulipekua begi hilo, ila mimi nilienda ofisi ya basi hiyo hiyo jana, lakini sikukuta begi lililoachwa kwa hiyo niliamini kuwa begi langu limechukuliwa kimakosa, nami pia nilipanga leo niende tena huko ofisi ya mabasi nikaulizie.” Onespot aliangua kicheko akacheka sana kiasi akawafanya Lulu na Edward nao wacheke, kicheko cha wasiwasi,
“It is a good story, any way, mtafanya nini?!… lakini… Lulu inaonekana wewe umefanikiwa kupata nguo za kubadili. Haiyumkini kuwa nguo ulizovaa nawe pia ndizo ulizosafiri nazo tangu jana, kama anavyoonekana bwana Oloi hapa.” Lulu alimuangalia Edward kwa jicho la huruma kidogo,
“Nashukuru mimi nimefikizia kwa dada yangu ambaye tunafanana sana kimaumbile na ndiye aliyeniazima nguo hizi nilizovaa.” Edward alimwomba Onespot Pato wasitiliwe shaka na kuwa waliloeleza ni la kweli.
“Ingawa hamuonekani kuwa mnaweza kusema uongo, lakini hadithi yenu ni miujiza kweli iwapo ni kweli nyinyi hamkupanga kufanya hivyo. Nina maana kama ni kweli wewe ndie hasa Edward Oloi mwenyewe na huyu naye ndiye Lulu Frank halisi walioitwa kwa ajili ya kuajiriwa na ADFC Ltd. Pia, hivi ni kwa nini nilipokuwa ninawajulisha kwa kila mmoja wenu Lulu alipoingia hamkusema kuwa mnafahamiana?!” Onespot alirudia kuwauliza kwa sauti ya chini,
“Mbona nilipowajulisha kwa kila mmoja wenu hamkuniambia kuwa mnafahamiana, maana yake nini, ni kunicheza shere sio?’’
“Hapana ,’’ walijibu kwa pamoja Lulu na Edo.
“Kwa hali tuliyokuwa nayo Bwana Pato, hatukupendelea kuuvuruga mtiririko mzima wa utambulisho. Tulionelea hakukuwa na ubaya kwa wewe kututambulisha tena,’’ Edward alijibu kwa sauti ya kuomba radhi.
“Na hata hivyo,’’ Lulu naye aliendelea kusema, “Ni kwa mara ya kwanza mimi na Edward kuonana jana ndani ya basi, na bado hatujatambulishwa rasmi na mtu yeyote, hivyo sioni kosa katika kukubali kutambulishwa tena nawe Bwana Pato, hasa
tukitilia maanani kuwa kwa hivi sasa wewe ni mwajiri wetu sisi sote wawili.Tusamehe iwapo hilo limekuudhi, lakini nina hakika si mimi wala Edo, hatukuwa na dhamira yeyote mbaya.’’ Kwa mastaajabu ya wote, Onespot alipiga kofi kugonganisha viganja vyake, taratibu zaidi ya mara mbili, jambo lililomfanya aonekane jamali zaidi, na kusema,
“Sawa sawa Edward na Lulu, sijui ni wapi tena mtapata utambulisho na kujifanya hamjuani………any way………nadhani sasa hivi la kufanya ni kukuruhusu wewe Bwana Oloi uende ukabadilishe nguo zako, ma’nake unaonekana valuvalu kwelikweli, you look shabby. Na wewe Lulu labda tungeanza na kukupa maelezo juu ya kazi yako na nini unatakiwa kufanya.’’
“Maelezo hayo ni sasa hivi bosi?’’ Lulu alimuuliza Onespot.
“Ndiyo, leo hii, a’fu kesho utaweza kuleta ile barua yako ya ajira.’’
“Samahani bosi,’’ Edward alimuomba Onespot,”Je, nami nahitajika leo, au ni mpaka hapo kesho?’’
“Enhee! Unaweza kwenda zako na kuripoti kesho Mr. Oloi.’’
“Sawa bosi, lakini itabidi nimsubiri Bi Lulu.’’
“Kwanini, unahitaji kufanyiwa utambulisho kwake tena?’’
“Hapana bosi, ninahitaji begi langu kutoka kwake, ili nipate nguo za kubadili.’’
“Ooh! My God, nadhani ni vema niwaruhusu nyote mwende zenu leo mkabadilishane hayo mabegi yenu na kesho mje rasmi na barua zenu tayari kwa kuanza kazi. Inaelekea ninyi wawili hamtenganishwi, sijui itakuwaje, tutaona.”
* * *
Wakati Edward Oloi amejipumzisha katika chumba cha hoteli alikofikia, na baada ya kumpatia Lulu begi lake naye kuchukua lake kutoka kwa Lulu, mawazo yalianza kumjia na kuanza kumfikiria sana msichana huyo. Vile vile alikumbuka maneno ya mwisho ya Onespot aliyotamka, ‘NINYI WAWILI HAMTENGANISHWI, SIJUI ITAKUWAJE, TUTAONA’………….. “Sijui itakuwaje, tutaona!” Alijisikia akirudia maneno hayo peke yake kwa sauti.
Alikuwa amelala chali juu ya kitanda kikubwa, alinyoosha mkono wake wa kulia akanyanyua mto wa pili, wa kwanza akiwa ameuwekea kichwa chake, akauvuta mto huo wa pili na kuuweka juu ya kifua chake, kisha akaukumbatia kwa kutumia mikono yake yote miwili. Alibaki katika hali hiyo kwa muda usiopungua dakika tano huku akiitolea macho dari ya chumba kile pasipo kuitambua akilini mwake. Alirudisha pumzi kwa nguvu na kutamka, “Aaah! Lulu……’’
* * *
Wakati huo Lulu Frank alikuwa mezani akila chakula pamoja na dada yake aitwaye Flora Frank na mumewe Abraham Loito. Abraham alimuuliza shemejie Lulu wakati wakiendelea kula,
“Vipi Lulu, nasikia umefanikiwa kupata begi lako!?’’ Lulu alitoa kicheko kidogo kilichoambatana na mguno,
“Mhnn! Shemeji, ni miujiza mitupu!’’
“Kwa vipi?’’
“Aliyechukua begi langu kimakosa hatukukutana tena stendi ya mabasi, bali tumekutana ofisini nilikokwenda kuripoti.’’ Lulu alimweleza shemeji yake habari zote zilizotokea kati ya yeye, Edwar na Onespot, vilevile alimhadithia kuwa Edward na yeye walisafiri pamoja, na hakuacha kumjulisha mkasa wa nambari za viti.
“Inaelekea jamaa huyo……….huyo…….Edward na wewe mna mengi ya
kufanana,’’ Abraham alimwambia Lulu.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Ndivyo, inavyoelekea, na ndio maana nikakwambia ni miujiza……’’
Kwa sababu siku iliyopita Lulu alikuwa amechoka kwa safari, pamoja na kubadilishiwa begi lake na asubuhi aliamkia kwenda kuripoti hivyo hakupata nafasi ya kuulizana habari vizuri na dada yake, kwa hiyo Flora alitumia nafasi hii ya kutaka kujua habari za nyumbani kwao Arusha na za wazazi wao.
“Enhee, hebu nieleze Lulu, nililetewa habari kuwa umepatiwa mchumba na unataka kuolewa, sijakaa vizuri mara baada ya siku chache napata simu yako kuwa unakuja huku Dar es salaam kuanza kazi, imekuwaje? Nilikuwa nakusubiri kwa hamu kubwa uje unipashe za huko nyumbani.’’ Lulu alichukua dakika chache kwanza kwa kutafuna na kumeza kilichokuwa kinywani mwake kabla ya kumjibu dada yake,
“Dada Flora, we acha tu, hiyo kasheshe iliyokuwepo kati yangu na baba, si ya kusema, hivi nikwambiavyo nimekuja kwa masharti.’’
“Hebu nifafanulie basi, mbona unazidi kunipa wasiwasi? Ni kasheshe gani, na ni masharti gani hayo?’’ Wakati huo Flora alikuwa amekwishamaliza kula, aligeuka kidogo pale kitini alipokuwa amekaa na kumwangalia Lulu, ambaye alinyanyua bilauri ya maji na kuikutanisha na midomo yake, kisha kugugumia robo tatu nzima ya maji yaliyokuwemo. Alivuta kitambaa cha kukaushia mikono akapangusa midomo yake kisha naye akageuka kidogo kumwangalia Flora.
“Mwenzangu, baba alitaka niolewe na mume huyo. Nikwamwambia sitaki ndoa za kupangiwa. Pia, nikamwambia kuwa sikuwa tayari kuolewa, bado sijatimiza hata miaka ishirini na tano, haraka ya nini? Mnh, sikwambii dada, baba alifoka na radhi mkononi…Niliposema mbona wewe da’ Flora umeolewa na mtu uliyemchagua mwenyewe, niliambiwa ninyamaze nifunge mdomo wangu, nisikutaje, kwani wewe pamoja na kuwa umechagua mwenyewe mume wa kukuoa, lakini ulichagua tangu ukiwa na umri mdogo kwa hiyo uchumba wenu wewe na Abraham ulijulikana tangu awali, je mimi yuko wapi huyo mchumba niliempata mpaka sasa? Na kwa vile sikuwa naye niliyemchagua, basi, ni lazima niolewe na huyo bwana waliyenichagulia. Wiki nzima dada, kila siku vikao na suala ni hilo hilo la kuolewa na niliyepangiwa. Na mimi siku zote hizi nilikataa.’’ Shemeji yake ambaye kwa muda wote huo alikuwa akisikiliza maelezo yake wakati akimweleza dada yake, alimtania Lulu kwa kumwambia,
“Lakini na wewe Lulu, kwa nini usikubali tu? Unajua wakati mwingine ndoa za kupangiwa huwa zinadumu zaidi, we kubali tu usijivunge……….’’
“Yaani na wewe shemeji unawaunga mkono hao wakwe zako huko nyumbani?’’
“Kwa jambo kama hilo la heri bwana kwa nini nisiwaunge mkono?’’
“Kumbe hunitakii mema shemeji.’’
“Una maana hao wazazi wako pia hawakutakii mema?’’
Flora alimgeukia mumewe na kumwambia,
“Abraham, hebu muache kwanza amalize maelezo yake.’’ Na kwa Lulu nae akamuuliza, “Lulu, endelea, ilikuwa ni masharti gani uliyopewa?’’ Abraham alimuangalia Lulu kwa tabasamu kubwa na kusema,
“Masharti gani kama si kuambiwa aje afanye kazi na kisha arudi kuolewa na huyo bwana shemeji aliyowekewa?!” Lulu alicheka kidogo kisha akasema,
“Shemeji bwana, ni hivi kuna ukweli kwa uliyosema. Baba nilipomweleza kuwa nimepata kazi huku Dar es salaam, aliniambia kuwa haniruhusu mpaka nikubali kuwa nitafikiria suala la mchumba yule niliyechaguliwa. Nije nifanye kazi, na baada ya miezi sita, kama sikupata niliye mchagua mwenyewe, basi nirudi nikaolewe na yule niliyechaguliwa.’’ Abraham alidakia kwa kusema,
“Kwa hiyo una kazi mbili za kufanya Lulu, una kazi ya kutafuta mchumba.’’
“Nitazifanya zote.’’
“Utaweza Lulu?’’ Dada yake alimuuliza.
“Nitaweza, nitatumia kichwa kwa kufikiria zaidi kuliko nitakavyotumia moyo kwa kuhisi.’’
“Tafadhali fanya hivyo Lulu,’’ dada yake alisisitiza.
* * *
Wakati Lulu anaingia alimkuta tayari Edward yupo nje ya ofisi ya Onespot James Pato amekaa juu ya kiti kilichokuwepo mbele ya meza ya Ofisi ya Katibu Muhtasi wa Bwana Pato. Lulu alitoa salamu na Edward pamoja na Victoria, waliitikia kwa uchangamfu. Kisha Lulu akakaribishwa kukaa juu ya kiti kingine karibu na Edward.
Victoria Kapate, Katibu Muhtasi wa Bwana Onespot James Pato, ni msichana wa miaka 23 mrefu kiasi, maji ya kunde, maridadi sana. Ana sura nzuri, macho makubwa maangavu, midomo ya kuvutia ambayo saa zote inatabasamu. Vicky kama wanavyomuita watu wengi, kwa ujumla ni mrembo hasa wa sifa ukichanganya na umbo lake lililo umbwa likaumbika na kufuatia na kutunzwa.
Mzee Kapate, baba yake Vicky na Mzee Pato, baba yake Onespot ni marafiki wa siku nyingi. Walikuwa ni watafutaji hodari tangu wakati wa ujana wao. Kwa hivi sasa wote wana hali nzuri sana ya kifedha. Mzee Pato amejaliwa kupata mtoto mmoja tu wa kiume nae ndiye Onespot. Mtoto ambaye amemlea kijukuu, kiasi ya kuwa ametokea kuwa na majivuno na kujiamini mno.
Pamoja na kuwa si mtu muovu wa tabia, lakini kuringa kwake kunamfanya aonekane si mtu mwema, uhusiano wa Onespot na wasichana ni kuwa hakubali kukataliwa. Hakuna msichana anaethubutu kusema ‘Hapana’ anapotakiwa na Onespot, kwa vile anacho kila kitu msichana anachohitaji mvulana kuwa nacho. Tajiri, mtanashati; anavutia, mcheshi na anao moyo wa kutoa chochote kwa msichana bila kufikiria mara mbili. Hali ambayo ilimfanya Vicky awe mmoja wa wasichana waathirika mbele ya Onespot.
Vicky Kapate ni mtoto wa pili na wa mwisho wa Mzee Kapate,, wa kwanza akiwa wa kike vilevile. Mzee Kapate hakujaaliwa kupata mtoto mwingine zaidi ya hao wasichana wawili, ambao mkubwa alikwisha olewa. Pamoja na kuwa Vicky anamhusudu sana Onespot, lakini pia wazazi wao walikuwa wanauguza hamu kubwa ya kutaka watoto wao hao wawili waoane. Tatizo ni kuwa Mzeee Pato hawezi kumlazimisha kijana wake kuoa kama mwenyewe hajataka. Jambo ambalo wazee hao wawili Pato na Kapate wameweza kulifanya ni kumuomba Onespot amchukue mwenzie Vicky awe Katibu Muhtasi wake. Tamaa yao ni kuwa kuwepo karibu sana, kwa mvulana na msichana huyo kunaweza kuzaa matunda ya mapenzi kati yao. Kwa upande wa Vicky nae, hiyo ilikuwa ni nafasi aliyokuwa anaiota.
* * *
Onespot, kama kawaida yake aliingia kwa vishindo ofisini kwa Vicky ambako ndiko kulipokuwa na mlango wa kuingia ofisini kwake. Alipofika pale aliwakuta Edward na Lulu wapo pamoja na Vicky.
Aliwasalimu,
“Good morning everybody.’’
“Morning Sir,’’ Kwa pamoja waliitikia. Alimtulizia macho Lulu na pasipo hofu alimsifia uzuri wake hapo hapo.
“Wah! You look so beautiful Lulu, hivi umepata kuambiwa na mtu yeyote kuwa u mrembo kiasi gani Lulu?!’’ Lulu alihuzunika kidogo na kuinamisha uso wake chini. Vicky nae aling’ata mdomo wake wa chini kwa kuuingiza kinywani kwake na kukunja uso. Aliyemudu kutoa tabasamu la chini chini ni Edward peke yake.
Sijui kwa kukubaliana na Onespot kuwa Lulu kweli mrembo ama kwa kumuweka Onespot katika fungu la waropokaji ovyo. Pasipo kumpa nafasi mtu mwingine ya kusema chochote Onespot aliendelea.
“Eeeh, wacha niwafanyie utambulisho kwanza, Bwana Edward Oloi,’’ alinyoosha mkono wake kumuelekeza Edward,
“….Huyu ni Bi Lulu Frank… na huyu mumuonae hapa ni Katibu Muhtasi wangu kwa jina ni Victoria Kapate au Vicky kwa wote na mimi… samahani ninapenda kuitwa Onespot, sitaki kusikia ‘Sir’ au ‘Boss’ ondoa hii yote. Onespot , basi, mmenielewa?… hasa ninyi wageni’’
Edward na Lulu walitabasamu kidogo kwa pamoja wakaitikia,
“Ndio tumekuelewa… Onespot.”
“Na mimi vile vile huwa wananiiita Edo tu,’’ Edward alijieleza na yeye kuwafahamisha wote.
“All right, all right, Lulu, Onespot, Vicky na Edo…that’s good’’ Onespot alirudia majina yao wote pamoja na lake kwa haraka na kuchanganya lugha ya kiswahili na kingereza kama kawaida yake.
* * *CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Edo na Lulu walianza kazi pamoja katika kampuni ya ADFC Ltd inayoshughulika na matanganzo ya biashara na mitindo ya nguo, kutengeneza filamu ndogo ndogo za biashara za bidhaa mbalimbali na kuendesha maonyesho ya mavazi ya mitindo mbalimbali Lulu alikuwa ni mwana mitindo (model) pamoja na wasichana wengine wengi warembo walioajiriwa kwa ajili ya shughuli hizo. Edo nae alikuwa mpiga picha za kawaida na za video pamoja na kutengeneza hizo filamu za matangazo. Nae pia hakuwa peke yake walikuwepo wavulana wachache waliokuwa na kazi kama yeye.
Shughuli zote hizo Mkurugenzi mtendaji wake alikuwa ni Onespot akisaidiana na Katibu Muhtasi wake Vicky. Kwa upande wa kazi, hivyo ndivyo ilivyokuwa, na shughuli zote zilikwenda vizuri kila mmoja akitimiza wajibu wake ipasavyo. Lakini hali ya kila mmoja haikuwa hivyo ki-ubinafsi. Kwani Onespot alionesha kila dalili za kutaka kuwa karibu zaidi na Lulu. Vicky nae alinyenyekea na kutii kila amri inayotolewa na Onespot kwa matumaini kuwa huyo Onespot atalitambua pendo la Vicky juu yake. Edo nae, kila siku zilivyozidi kusonga alijihisi moyo wake umejaa hisia za Lulu kuliko msichana mwingine yeyote hapo kazini. Kwa upande wa Lulu, yeye alikuwa kila mara anakumbuka hali ilivyo huko nyumbani kwao atokako na kwamba ana kazi mbili za kufanya, kazi ambayo ni ajira yake, na kazi ya kumtafuta mwanamume ambae angempenda kiasi cha kutosha kumuingiza yeye ndani ya ndoa. Vinginevyo arudi akaolewe na mume aliyechaguliwa na wazazi wake. Kutokana na kazi aliyokuwa nayo, nafasi ya kuonana na wanaume zaidi ya wafanyakazi wenzake, ilikuwa ndogo. Kwa hiyo moyo wake ulikuwa saa zote unafanya kazi ya kutafuta ni yupi mume bora kwake kati ya hao waliokuwa na yeye karibu, bali kichwa chake pia alikitumia katika kupima, kuchuja na kuchambua. Kutokana na ujana na urembo aliokuwa nao, vishawishi vingi vya wanaume havikuwacha kumuandama Lulu hapo kazini pake, lakini zaidi vilitoka kwa boss, Onespot.
“Unaonekana una mawazo mengi sana leo Lulu, unaonaje jioni ya leo ukatoka kupata chakula katika hoteli yeyote ya kifahari kama vile Sheraton na ubavuni pako ukiwa na ‘Handsome young man’ kama mimi Onespot for a company?’’ Onespot alimshawishi Lulu kwa majivuno.
“Asante sana Onespot, kusema kweli nisingependa kutoka nje ya nyumbani kwetu jioni ya leo’’ Lulu alijibu kwa sauti ya unyonge, wakati moyoni mwake alichukia
namna ya Onespot anayomtaka msichana kwa kujifaharisha na mali alizonazo pamoja na kujiona kuwa yeye ni mzuri mno.
“Basi hamna neno, siku nyingine, tunaweza tukaenda hata Zanzibar for a week-end… you know?’’ Onespot alisema haya huku kamkazia macho Lulu. Mtu mwingine alikuwa Edo ambae alionesha kumjali sana Lulu.
“Samahani Lulu, unaoneakana umo ndani ya mawazo mengi mno leo.Unaonaje tukaahirisha upigaji wa picha zinazokuhusu wewe leo, ili uweze kuenda nyumbani mapema na kupata muda mrefu wa kupumzika, kufikiri na kesho tutaendelea na upigaji wa picha wakati ukiwa fresh’’.Edo alimuambia Lulu kwa upole na taratibu na kuonyesha kuwa anamjali na kuheshimu hisia zake.
“Asante sana Edo, tunaweza tuendelee tu na upigaji picha wetu. Nakuahidi mawazo yote nitayaweka kando, kwani ni ya kawaida tu, usijali’’.
“Natamani ningejua mawazo yako ili nami kama nitaweza, nisaidie kufikiri.’’ Lulu alicheka kidogo na kujiona kidogo amepungukiwa na alichokuwa akifikiri,
“Asante kwa wema wako Edo, lakini linalonihusu mimi ni langu mimi tu.’’
“Kweli?!!’’
“Ni kweli kabisa.’’
“Sawa iwapo unadhani hivyo. Lakini watu wanasema ‘vichwa viwili ni bora kuliko kimoja.’’
“Kama ni hivyo basi niwache nifikirie peke yangu, nitakapojiona ninahitaji msaada wa mtu mwengine nitakwambia wewe Edo unisaidie.”
“Tafadhali usiwache kufanya hivyo Lulu. Pale unapoona ninaweza kusaidia, basi wakati wowote, saa yeyote, pahali popote nieleze nitakuwa tayari kusaidia.’’
“Natanguliza shukrani, Ahsante Edo.’’ Lulu alianza kupendezewa na mazungumzo kati yake na Edo. Yalikuwa yakimfarijii na kumliwaza. Mazungumzo kati yao yalikuwa rahisi yasiyokuwa na majivuno wala kujitapa. Hali kama hiyo iliendelea kwa muda kiasi kumfanya Lulu aanze kuvutika taratibu kwa Edo.
* * *
* * *
Hisia za Vicky juu ya Onespot zilifika kiwango ambacho alishindwa kujikaza kwa kukaa kimya na kuonesha ishara kuwa anampenda kijana huyo. Aliamua asema kwa namna moja au nyingine huku damu ikimwenda mbio mwilini mwake Vicky alitamka kumuuliza Onespot aliekuwa amekaa juu ya kiti kikubwa nyuma ya meza yake ya ofisi.
“Onespot , leo jioni unakwenda wapi?’’
Onespot alinyanyua uso wake kumuangalia Vicky kwa sura ya kushangaa.
“Siendi popote Vicky, kwani vipi unataka kunialika?!’’
“Hapana, ninataka wewe unialike mimi…Onespot.’’
“Hapana shaka Vicky, why not?! Sema ungependa kwenda wapi? Ni nani ambaye asingependa kutoka na msichana mrembo kama wewe mtoto wa mzee Kapate?!’’ Kama kawaida yake Onespot ni mtu wa maneno mengi na majisifu aliendelea kusema,
“Lakini utani mbali Vicky, mimi na wewe tukiwa pamoja! We make a good pair au sio?” Kwa Onespot ilikuwa faghari, kwa wasichana wengi waliowahi kuanza hata kumtongoza yeye kwanza, kabla hajawaambia lolote, na kwa Vicky ingawa upo wakati alitamani amtoe nje kwa matembezi, lakini pia zilikuwa zinakuja hisia za u-dada dada, kwa vile baba zao ni marafiki wakubwa.
Vicky moyo ulizidi kumwenda mbio akajiona kama yupo kwenye ndoto, aliitikia swali la mwisho la Onespot kwa kutamka.
“Ndio…ndio…we make a good pair.’’
“Nadhani watu wakituona watazimia,…kama tunatoka sayari nyingine vile. Sio utani Vicky mimi na wewe wazuri bwanaa!’’CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Jioni ile Onespot alimtoa Vicky nje, walipata chakula cha jioni ndani ya hoteli moja kubwa na maarufu jijini Dar es salaam. Kisha wakatembelea majumba ya starehe kwa muziki na vinywaji Vicky alivuta hatua ya kwanza aliyokuwa anaiwania.
Uhusiano wa Lulu na Edo uliweza kuzaa penzi. Zipo baadhi ya siku waliweza hata kutembelea maeneo mbalimbali ya jiji la Dar es Salaam pamoja, baada ya saa za kazi. Edo alijikuta kuwa hawezi kupitisha siku pasipo kumuona Lulu. Mapenzi hayajifichi, kwa namna walivyokuwa, kila mmoja hapo kazini alijua kuwa Edo na Lulu wapo mapenzini, habari ambayo iliweza kumfikia Onespot ambae hakuipokea kwa furaha. Vile vile baada ya kufanya uchunguzi wake, aliona wazi kuwa Edo na Lulu wanapendana.
* * *
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment