Simulizi : My Rose
Sehemu Ya Tano (5)
“Frank usilie mme wangu,hii ni sababu nakupenda sana”.Generose akaongezea maneno yake baada ya lile chozi kumdondokea.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Kama unanipenda kwa nini unanifanyia haya? Kwa nini unataka kufanya haya unayotaka kuyafanya? Umekosa nini? Kisa mapenzi ndiyo unataka kuwaacha wazazi wako na mtu unayempenda? Mama yako utamuacha na nani? Baba yako unataka afanyaje na wakati wewe ndiye mtoto wa pekee? Na huko uendapo utamjibu nini MUNGU akikuuliza haya maswali?”.Nilijikuta namuuliza Generose maswali mfurulizo kama siyo mgonjwa.
“Frank,sina nia mbaya kwa kitu nilichokifanya lakini nimejikuta nakifanya tu! Wewe ungekuwepo na kuwasikia walichokuwa wananiambia Baba na Baba Mdogo, sidhani kama ungevumilia. Mama akijaribu kutetea, wanamtukana na kumuambia yeye ndiyo kaniaribu lakini siyo kweli. Kama kuharibikiwa basi nimejiaribu mwenyewe na hakuna wa kumlaumu. Ni penzi langu kwako ndiyo limefanya nionekane kama nimeharibikiwa, nakupenda sana Frank, narudia tena, NAKUPENDA SANA FRANK”.Bado Generose aliongea ambapo sauti yake sasa ilizidi kupungua na kuwa ya chini sana jambo lililofanya niache kuuliza maswali mengi na kumfariji huku nikiwa na uhakika kuwa yale maziwa yatafanya kazi.
“Frank, sisi wanawake tumeumbwa na moyo mwepesi sana wa kupenda lakini tumeumbwa na moyo mgumu sana katika kufanya maamuzi yetu. Nachokuomba ni kile kile nilichokuambia mwanzo, usije kuzichezea hisia za mwanamke yeyote hapa duniani. Wapende kama ulivyonipenda mimi, sitaki kusikia ukisema utopenda tena. Akijitokeza,mpende na hata akikuumiza usilipe kisasi,sawa?”.Alimaliza kuongea Generose.
“Sawa nimekusikia,haya nyamaza chakula kifanye kazi”.Nilimkubalia kishingo upande ili anyamaze.
“Frank, nakuombe kitu”.Alianza Generose kuongea baada ya kimya kama cha dakika kumi.
“Niambie tu! Rose”. Nilimpa uhuru wa kuzungumza.
“Unajua niliwahi kukwambia nampenda msanii gani”. Aliniuliza Generose.
“Uliniambia unampenda Nameless”.Nikamjibu
“Kumbe unakumbuka, niimbie ule wimbo wake ili nilale”.Aliniomba nimuimbie ule wimbo wa Nameless ambao ndiyo ulikuwa unatamba sana kipindi kile. Unaitwa Sinzia. Nikaanza kumuimbia huku yeye anaitikia.
MIMI:Nasinzia nikikuwaza
ROSE:Oooh
MIMI:Nasinzia nikikuwaza
ROSE:Oooh
MIMI:Miaka rudi,miaka nenda
ROSE:Oooh
MIMI:Kila siku za kalenda
ROSE:Oooh{kwa sauti ya chini sana}
MIMI:Nasinzia nikuwaza.
Safari hii Generose hakujibu kitu zaidi ya shingo yake kulegea na mikono yake kuifungua,huku nayo pia ikilegea. Pia macho yake akayafunga, huku midomo yake ikibakiwa na tabasamu dogo ambalo kamwe halikumtoka alipokuwa na mimi.
“Rose”.Nilianza kuita kwa sauti ya chini baada ya kuona Generose katulia. Nilipoona kakaa kimya zaidi nilianza kumuita huku nikiendelea kuongeza sauti na kuwa ya juu zaidi iliyomshitua hata Mama Generose.
“Rose hamka Rose. Rose usifanye hivyo Mama yangu,nakuomba Rose please”.Nilijikuta nikilia kwa nguvu na kuongea maneno hayo baada ya kuona Generose haamki. Hapo ndipo Mama Generose naye alipoingia kwa hamasa akiwa amejichochea kwa nguvu zote na kufika pale nilipokuwa nimekaa na Generose, bila kuuliza alikuja na kuanza kumtikisa Generose kwa nguvu huku akilia kwa uchungu, uchungu ambao kwa kila mzazi ungemshika.
“Rose mwanangu, hamka hata useme kwa heri mwanangu. Rose,mimi ni mama yako naongea haya, rudi mara moja tu! uniambie kwa heri mwanangu. Rose, Rose, Roseeeeeeee”. Mama Generose alijikuta akitoa maneno kwa sauti ya juu na alipoliita jina la Generose mara ya mwisho,alipoteza fahamu pale pale,kitu kilichofanya niwe jasiri kwa muda na kuanza kuhangaika nje ili nipate msaada. Haikuchukua muda,watu walishajaa pale kwa akina Generose na kuanza kutoa msaada wa kumpepea Mama Generose huku mimi bado nikiwa nimemkamata Generose pale kitandani pake nikiongea naye kana kwamba alikuwa anasikia au ataamka.
“Rose mke wangu, niangalie basi mimi eeh. Niangalie hata mara moja huku ukiendelea kutoa tabasamu lako lililoambatana dimpoz zako nzuri. Rose, usinifanyie hivyo mama yangu,mimi nitaishi vipi sasa? Na mimi nitakufa kama hutoamka. Nakuomba Rose, hamka mama yangu umuone Mama yako anavoteseka mmh. Eti Rose, hivi kweli hutaki kunisikiliza mimi? Rose, ni kweli kabisa umeondoka na kuniacha mimi? Eti Rose, embu nijibu basi mama yangu eeh,naomba unijibu mke wangu,amka mama”. Nilijikuta naongea maneno hayo huku nikiwa na uchungu sana moyoni mwangu,lakini haikusaidia kwani Generose alikuwa kakauka kabisa.
“Rose, Rose, Rose, Rose, Rose, Roseeeeeee”. Niliita jina lake kwa nguvu kama nimechanganyikiwa na baada ya kuita hivyo na mimi nikadondokea kifuani kwa Generose na kupoteza fahamu.
Sijui nilizimia kwa muda gani ila nilipoamka nijilikuta nipo nje, kukiwa tayari kumefungwa maturubai kitu kilichoonesha kuwa Generose hatunaye tena. Watu waliyokuwa wananipepea walitoa taarifa kuwa nimesha amka na kitendo bila kuchelewa niliona askari wawili wakinifuata na kuomba mikono yangu ili wanifunge pingu.
“Kijana tunaomba mikono yako tafadhari, una jambo la kujibu”. Walianza kuongea hayo huku wakionesha hawana utani. Na kwa kuwa walikuwa hawana utani hata kidogo basi na mimi nikawa kama wao.
“Umeshawahi kumuahidi mtu kitu na ukakitekeleza hata kama ni cha hatari?”. Niliwauliza askari wale huku nimewakazia macho.
“Sisi hilo hatujui, tunachotaka ni hiyo mikono yako. Kama hutaki sisi tunatumia nguvu tu!”.Aliongea askari mmoja kijana huku akianza kunishika mikono anifunge pingu. Nilijikuta nampiga ngumi ya jicho na kabla hajakaa sawa nilimsindikiza na teke la tumbo jambo lililofanya yule mwenzake kurudi nyuma na kumshika mwenzake ili asidondoke.
“Mnajua nini nyie wajinga, mmekuja kwenye muda mbaya sana na mtajutia kwa nini mmekuja mida hii”.Niliongea hayo huku tayari watu walishakuja na kuzunguka eneo lile wakishangaa jambo linaloendelea pale msibani.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Unaajidai mjanja si ndiyo eeh, nakuuliza wewe, unajidai mjanja?”.Alikuwa anaongea yule polisi mwingine ambaye kidogo alikuwa ni mkubwa kwangu. Aliongea hayo huku akinifata na kunirushia ngumi nne kwa mfurulizo na kwa nguvu na zote. Sikuwa na mpango wa kuzikwepa hivyo zilinikuta usoni na kusababisha kunipasua sehemu ya shavuni.
“Hapo ndipo ulipoishia kwenye mafunzo yako ya kupiga watu?”.Nilijikuta namuuliza yule askari huku nimeganda kama roboti bila hata kujishika mahali nilipopigwa.
“Nakuuliza wewe mse****, hapo ndiyo umemaliza eeh?”Nilizidi kumuuliza wakati huo nilikuwa namfata huku nimekunja ngumi tayari kwa kulipa alichonifanyia.Kwa uoga mkubwa yule polisi alikuwa anarudi nyuma huku akiwa makini na ujio wangu. Kwa bahati nzuri Baba yake Generose alitokea na kuanza kunifokea kwa matendo niliyokuwa nayafanya na zaidi niligundua kuwa yeye ndiye aliyewaleta wale polisi.
“Nakuambia wewe utaozea jela maisha yako yote, nakuapia haki ya MUNGU ee, utaozea jela wewe. Umemuua mtoto wangu kisa unajidai unampenda,na sasa hivi unaipiga serikali. Nakuambia umeisha wewe mtoto, kama ulichezea wengine hapa ndo mwisho wake leo”. Baba Generose aliongea kwa hasira huku akiwa mbele yangu na kunifanya niwe nazidi kupandisha hasira.
“We Mzee ndiyo umemuua mtoto wako wewe. Rose kafia katika mapaja yangu, wewe ukiwa haupo umeenda huko kuchukua hivi vidudu unavyoviita serikali. Unadhani kama ungekuwepo hapa nyumbani kwako, Rose angekubali kuongea na wewe? Rose anakuchukia kupita maelezo, na huko aendako sidhani kama atakuandalia makao mazuri”.Nilijikuta naongea kwa kujiamini na kwa hasira huku nikifuta damu zilizokuwa zinanitoka.
“Ndiyo Baba Rose, mtoto wa watu kakuambia ukweli mtupu. Hana kosa hata kidogo,muache aende zake,kajitahidi sana kwa alichokifanya. Umeondoka hapa kwa sababu ulikuwa huna uchungu wa mtoto wako, yule mwenye uchungu kabaki hapa halafu unataka umpeleke polisi,ili iweje? Endapo huyu kijana wa watu ataenda polisi basi na mimi utanipoteza kama ulivyompoteza Rose na historia itaandikwa, kuwa Mama na Binti yake wamejiua kwa sababu ya kijana”.Mama Generose aliingilia ugomvi ule kwa kumuambia maneno hayo mme wake ambaye alikuwa katulia na ngozi ya uso kumshuka baada ya kusikia na Mama Generose naye atakufa kama Generose.
“Sitaki kukuona hapa wewe kijana, yaani potea kabla sijabadilisha mawazo yangu. Sitajali kumpoteza yeyote hapa kama utaendelea kuwapo hapa”.Aliongea Baba Generose kwa hasira na kunifanya na mimi nijibishane naye lakini niliwahiwa na wakina Babuu pamoja na Seth na kisha wakaniambia tuondoke pale huku wakinivuta kutoka eneo lile.
“Hivi kweli Rose ameondoka? Ameondoka hata bila kusema kwa heri Frank. Kweli kabisa Rose? Ni kweli mke wangu umeondoka? Nitabaki na nani mimi? Nyie wakina Babuu si ndiyo mtanicheka sasa?”. Nilijikuta naongea hayo wakati nipo njiani narudi pamoja na wakina Babuu.
“Hamna mwanangu, wewe unadhani sisi hatujaumia? Imetuuma sana lakini imeuma zaidi kwako maana alikuwa ni mtu wako muhimu na wa karibu, hivyo hatuwezi kukucheka kwenye tatizo kama hili”.Aliongea Babuu kama kunijibu maswali niliyokuwa najiuliza.
“Kwani nyie mmejuaje na mmefikaje pale kwa akina Rose?”.Niliwauliza wakina Seth.
“Tulipigiwa simu kwa namba yako na kuambiwa kuwa umepoteza fahamu baada ya Rose kufia miguuni mwako”.Alijibu Babuu.
“Kwani mimi nilizimia kwa muda gani?Na kuna taarifa zozote kwa kilichosababisha kifo cha Rose?”. Niliendelea kuuliza.
“Dah! Sijui walisema umezimia tangu saa nne asubuhi hadi ile mida ya saa saba ndo ukazinduka, na wanasema kuwa kanywa sumu ambayo inakuwa inakula utumbo taratibu, unaweza kukaa nayo kwa siku mbili na kama ukichelewa ndani ya siku hizo basi kutibika inakuwa ni ndoto. Na inavyoonekana Rose aliimeza kwa muda mrefu sana”.Alikuwa anajibu maswali yangu Babuu.
“Ujue nyie hamna akili, nani kawaambia Rose kafa?”.Nilibadilika ghafla uso wangu kitu kilichofanya hata wao wakina Babuu kushituka na kuogopa kidogo.
“Mwanangu,embu tuliza kwanza kichwa, utachanganyikiwa hivyo. Twende nyumbani kwanza ili ukatulize kichwa chako”.Aliongea Seth huku akinivuta mkono na kuanza kuteremka barabara iliyokuwa inaelekea nyumbani.
Wakati tunaendelea kushuka ndipo tulisikia sauti nyuma yetu ikituita.Tulipogeuka alikuwa ni Paul akiwa anakuja na baiskeli ile niliyoenda nayo nyumbani kwa akina Generose.
“Mwanangu pole sana. Baiskeli hii mlitaka kuisahau”.Alianza Paul kuongea baada ya kufika pale tulipo kuwepo.
“Haina noma,ila najua kuwa Rose bado yupo”.Niliitikia na Paul alijiunga na msafara wetu ambao uliishia kwa mimi kufikishwa nyumbani na pale nilipoingia tu! Nililakiwa na mama yangu ambaye alikuja kunikumbatia huku akiniliwaza kwa maneno ya kiutu uzima jambo ambalo lilihamsha hisia nyingine kali sana katika moyo wangu.
“Mama, Rose kaondoka mama, Rose kaniacha peke yangu mimi.Nitabaki na sasa?Rose wangu mie,kaondoka hivi hivi”.Nilikuwa naongea hayo huku nikilia kwa uchungu mkubwa na sikuishia hapo.
“Rose mimi nitamfata mama, nilimuahidi nitamfata popote atakapoenda. Rose wangu wee, rudi hata nione tabasamu lako Rose. Siwezi kuishi bila wewe Rose, nitakufa bila wewe Rose”.Nilizidi kulia kwa sauti huku nikimkumbatia mama yangu na baadaye nilianza kumuachia taratibu huku nikiwa nazidi kupoteza nguvu na nilijikuta nikitamka maneno machache kutoka kinywani mwangu.
“My Rose, nitakufata huko uendapo. Nisubiri mama yangu”. Kisha nikadondoka tena na kupoteza fahamu.
Fahamu zilikuja kunirudia tena jioni ya saa kumi mbili tangu saa kumi nilipofika pale nyumbani. Dada zangu walikuwa wananiangalia kwa huruma huku wakionesha wazi kuwa nao walikuwa wanalia kutokana labda na kifo cha Generose au kwa sababu ya hali yangu. Nilipotulia kwa muda kidogo ndipo akili ilikaa sawa na kujikuta naanza kulia tena na kufanya dada zangu nao kufuata nachofanya.
Ilikuwa ni huzuni pale nyumbani hasa kutokana na kutokuwa na wa kumbeleza mwenzake zaidi ya mama ambaye ilifikia muda na yeye aliungana na sisi.
Hivyo ndivyo ilivyokuwa kwa siku ile. Hadi napata usingizi nahisi tayari nilikuwa nimejaza lita tano za machozi kutokana na msiba wa Generose.
Sikuenda kwenye msiba wa Generose kutokana na taarifa zilizokuja kutoka kwa Baba yake Generose ya kuwa nikionekana pale msibani basi polisi watakuwa halali yangu,hivyo nilibaki nyumbani wakati dada zangu walikuwa wanaenda hadi kulala kwa akina Generose. Siku ya tatu baada ya kifo cha Generose ndiyo ilikuwa siku ya mazishi ya Generose. Sikuvumilia hata kidogo na nilijisemea kuwa liwalo na liwe.
Ilikuwa ni tabia yangu hapo zamani kunywa pombe, lakini ni karibu mwaka ulipita tangu niwe na Generose. Niliacha kabisa matumizi ya pombe nilipompata Generose,lakini siku hiyo niliamua kunywa pombe, pombe yenyewe ilikuwa ni konyagi ule mzinga mkubwa.
Nilichukua ile pombe na kuimiminia mdomoni kama maji.
Hiyo kwangu haikunitosha, nilienda hadi kwa wauza bangi wa pale mtaani,kisha nikawaomba wananisokotee misokoto miwili ambayo niliifakamia kwa kasi huku hata yule muuzaji akinishangaa ni nini kimenikuta. Nilipotoka pale nilikuwa kama kichaa au mtu fulani asiye jielewa anachofanya. Nilikuwa napepesuka na huku nikijaribu kuelekea kwa akina Generose.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Hakuna ambaye hakunishangaa kwa ninachofanya na jinsi nilivyoonekana. Nilikuwa nasikitisha sana kiasi kwamba hata wale rafiki zangu wa mtaani walikuwa wananishangaa.
“Oya Kaka Masai vipi kaka? Mbona hivyo leo”. Walionijua hawakusita kuniuliza maswali ya namna hii,lakini mimi sikuwajibu kitu zaidi ya kunyoosha na kuikaza miguu yangu na safari ya kwenda ulipo msiba ndiyo ilikuwa inaendelea.
Nilifika kwa akina Generose na kuambiwa kuwa tayari wameshaenda makaburini kwa ajili ya maziko ya mwili wa Generose wangu. Nilitoka kwa kasi ile ile niliyoijia hadi makaburini ambapo nilikuta wameanza kuufulia mwili wa Generose. Hapo nilichokifanya kilikuwa ni kitu ambacho nisingeweza kukifanya kama ningekuwa mzima.
Niliwasukuma baadhi ya watu pembeni ili nipate upenyo wa kupita. Nilipofika karibu na shimo la kaburi la Generose, nilijikuta najirushia ndani yake na kuanza kulifukua huku nalia kwa nguvu zangu zote na wale wafukiaji nao hawakuacha kumwagia michanga yao.
“Rose… Rose… Rose.. Rose hamka mama yangu unione mara ya mwisho jinsi nilivyo mimi. Rose tafadhari usiniache peke yangu. Rose mama yangu rudi mara moja tu! rudi twende wote huko utakapo, nakuomba Rose urudi, njoo mama yangu. Nakupenda sana mama yangu, usiniache katika hali hii”. Nilikuwa naongea hayo huku naendelea kulifukua kaburi lile ambapo baadaye nguvu ziliniishia kutokana na vilevi nilivyovitumia kunizidi, hivyo nilibaki nimelalia ule mchanga unaolifukia jeneza la Generose na wakati huo na mimi nilikuwa namwagiwa mchanga kwa lengo la kuzikwa na Generose.
Waliokuja kunitoa ni wale wale tena. Wakina Babuu, ambao walinitoa huku tayari nilikuwa nimepoteza fahamu kwa mara nyingine na tena safari hii nilikuwa kama mfu kwani niliposhituka nilijikuta nipo hospitali huku nikiambiwa nilikuwa sina fahamu kwa siku mbili.
Maisha yangu yalianza kubadilika kuanzia ile siku nilipotoka hospitali. Shule niliacha kwenda na nyumbani nilikuwa nachelewa kurudi na nikirudi basi nakuwa nimelewa bangi,mirungi na pombe kali. Baba na Mama walisema hadi walichoka na kubaki wakisubiria na mimi niondoke kama Generose kwani nilikuwa sijulikani wapi nakula wala wapi nashinda kutwa nzima. Nilibadilika kwa kila kitu, ule upole na utani wangu ulipotea na kuwa kinyume na hayo. Nilikuwa mkorofi na mwenye wingi wa kesi chafu pale mtaani kwetu, hakuna ambaye hakuniogopa kuanzia watoto hadi watu wazima. Sikuwa na rafiki tena kama zamani, rafiki zangu walikuwa ni wavuta bangi na walevi. Nilikuwa sina huruma hata kidogo endapo nitachokozwa. Na kamwe sikuogopa kumfanyia mtu kitendo cha ajabu.
Nilishakamatwa na kukaa polisi karibu mwezi mzima ili nibadilike lakini niliporudi mtaani ni kama walikuwa wamenifundisha na kuongeza ukorofi wangu. Sikuwa tena Mr.Bond yule wa mapenzi bali yule wa mapigano, na sikuwa tena Frank wa kucheka na kila mtu,bali Frank kauzu asiye na utani wala tabasamu katika sura yake. Lakini sababu kubwa ni MAPENZI na ubishi wangu kuwa siwezi kupenda mtu nisiyemjua.
Yale majigambo yangu kwa akina Babuu yalititia katika maisha yangu, zile sifa zangu kutoka kwa wasichana kuwa mimi ni HANDSOME, zilipotea kama nyota zilizoona jua linachomoza. Hakuna ambaye hakuamini kuwa mimi ni jambazi au kibaka pale alipoambiwa hivyo japo sikuwahi kufanya matendo kama hayo. Kwa kifupi nilikuwa tayari kwa lolote katika maisha yangu huku nikitaka kutimiza ule msemo wangu nilioupenda kumuambia Generose wa “UKIRUKA nami NITARUKA”.
*************
Siku moja wakati nipo mtaani, nilikuta jamaa mmoja anampiga dada mmoja hivi na kumuaibisha mbele ya umati wa watu uliojaa watoto na vijana wengi, huku wengine wakishangilia baada ya dada yule kupigwa hadi kuvuliwa nguo na yule jamaa. Nilijikuta roho ikiniuma na kukumbuka maneno ya Generose kuhusu kuwaheshimu wanawake na kuwasaidia wawapo na matatizo. Huku nikiwa na baadhi ya rafiki zangu nilimfuata yule jamaa na kumuambia kwa ustaarabu amuache yule dada.
Kwa kuwa alishajiona mbabe akaanza kunitukana na baada ya hapo alianza kumpiga tena yule dada ambaye baadaye nilitambua kuwa ni mdogo wake na alikuwa kamfuma na mvulana ambaye kwa maelezo ya yule dada alikuwa ni mvulana wake,yaani kama mchumba hivi.
Nilimkamata yule jamaa nakumkata mtama mmoja na kisha nikamkalia kwenye kifua na kuanza kumshambulia na ngumi kitu kilichomfanya yule jamaa kupasuka sehemu ya usoni, na sikuishia hapo. Baada ya kumpiga na kumfanya alegee kabisa, nikaanza kumtoa nguo zake na kumbakiza mtupu. Niliporidhika nilimuambia maneno machache kuwa “Awaheshimu wanawake, hao ndiyo mama zetu”. Kisha nikapotea eneo lile.
Baada ya siku tatu nikiwa natembea barabarani nilishitukia nakamatwa na mgambo na kupelekwa polisi ambapo nilituhumiwa kosa la kumpiga yule jamaa na kumsababishia kuvunjika mkono na makovu mengine mwilini mwake bila kusahau kumuaibisha mbele ya watu kwa kumuacha uchi. Sikupinga kosa lile na niliwaambia wale polisi kuwa nikimuona tena namuua kabisa kwa sababu hana heshima kwa wanawake. Niliwekwa rumande huku nikisubiria siku ya kupelekwa mahakamani kwa ajili ya kujibu shitaka lile.
Nakumbuka mama yangu alikuja siku ile baada ya mimi kukamatwa na alinililia sana huku akiomba nibadilike niwe kama zamani.
“Frank mwanangu, rudi nyumbani na uwe kama zamani mwanangu. Nimekukumbuka mwanangu, nakumbuka sana utani wako na siwezi kusahau siku ile nilipokula ugali ulioupika. Nilifurahi sana kula chakula ulichopika mwanangu. Embu rudi tena na anza upya mwanangu, au unataka na mimi nife mwanangu? Embu angalia ulivoisha mwanangu, jionee huruma Frank, utakufa mwanangu na bado tunakuhitaji. Frank rudi nyumbani baba yangu”. Mama alikuwa akiyaongea hayo huku machozi yakimtoka na kusababisha nione kama namuumiza mama yangu kwa matendo yangu. Mawazo hayo yalinipeleka mbali zaidi.
“Usijali mama. Hutohangaika tena, mimi sina umuhimu wowote hapa duniani, nitamfata Rose wangu baada ya kufanikiwa kutoka kwenye mikono hii ya serikali. Usijali mama”.
“Frank, usiseme hivyo mwanangu. Kumbuka siku ile uliponikumbatia, siyo siri mwanangu,nilitaka kukumbatia lakini niliona kama aibu mwanangu. Nakuahidi ukitoka salama humu,nitakukumbatia maisha yangu yote. Usifanye kibaya chochote kuhusu mwili wako. Frank mwanagu, tunakuhitaji sana katika maisha haya. Baba yako hajaenda kazini tangu upatwe na matatizo haya, embu tuonee huruma mwanangu”.Mama alizidi kuongea lakini alikuwa kama anampigia mbuzi gitaa.
Wakati nipo pale naongea na Mama ndipo nilipomuona Baba yake Generose anakuja na askari upande ule tuliokuwepo na mama.Nilipomuona nilijua kuwa mambo yamewiva kwa mzee yule kulipa kisasi chake. Baada ya kufika pale tulipo, Baba Generose alimuoneshea ishara ya kidole yule askari kwa kumuambia mtu mwenyewe ni huyu hapa.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Baada ya kumuonesha yule polisi mahala nilipokuwa nimefungiwa, yule polisi alifungua lile lango la mahabusu na kisha akaniambia niende mapokezi kuchukua vitu vyangu na kupata maelezo mengine. Sikuamini nilichokisikia baada ya kuambiwa ile kesi imefutwa na hivyo mimi ni mtu huru tena. Ila japokuwa nilitolewa mle mahabusu,polisi wale walinisisitiza sana kuhusu matendo yangu, na safari hii walisema kutakuwa hakuna msamaha.
Baada ya kutoka, tulipanda gari ya Baba Generose na kuanza kuelekea nyumbani kwa ajili ya maisha mengine kuendelea. Ndani ya gari kila mtu alikuwa kimya akitegea nani aanze kuongea. Kwangu mimi nilikuwa na maswali kama mawili ya kwa nini Baba Generose alikuwa mwema ghafla vile, na swali lingine nilijiuliza kuhusu mstakabali wa maisha yangu.
Ni vipi nitaishi bila kuvuta bangi na kunywa pombe ambazo kwangu mimi ndizo zilikuwa kama kisogeza maisha yangu, lakini nikivitumia vitu hivyo nakuwa mtu mwingine kabisa ambaye ni katiri. Wakati nipo katika mawazo hayo,ndipo baba Generose alikohoa kidogo na kisha kuanza kuongea.
“Frank, ujue wewe ni kijana mdogo sana. Hayo unayoyafanya hayana faida na vilevile yanawaumiza sana wazazi wako. Tambua kuwa hii ni dunia na ni hadaa, lakini humu tulimo ni ulimwenguni, na ulimwengu ni chuo kikuu. Ulimwengu ni mimi na wewe na watu wote wanao tuzunguka, lakini dunia ni mambo yote uyaonayo na kuyasikia. Mimi kama Baba, nimefunzwa na ulimwengu huu ambao ndiyo chuo kikuu. Na wewe ndiye mwalimu uliyenifundisha”.Baba Generose akaweka koma kidogo kwa kuchungulia nje ya gari baada ya kuona mtoto kavuka barabara huku magari likiwepo na lake likiwa linakuja kwa kasi. Yule mtoto alifanikiwa kukimbia baada ya koswa koswa ile. Baba Generose akaendelea.
“Unamuona huyo mtoto aliyevuka ovyo barabara? Huyo kakosa elimu ya uvukaji wa barabara ndiyo maana kajivukia tu! Mfano ningemgonga na kumuua, unadhani wazazi wake wangenielewa? Lawama zote zingekuja kwangu huku wakisahau wao na walimu wake ndio walipaswa kumpa elimu huyu mtoto jinsi ya kutumia barabara.
Au wangemuona jinsi alivyovuka hivi, unadhani ingekuaje kwa huyu mtoto kama siyo kutukanwa na kutaka hata kupigwa, wakati wao ndiyo walipaswa kufokewa kwa kosa la mtoto huyu. Na nina uhakika kuwa endapo huyu mtoto angekuwa na elimu hiyo angesipo fanya kitendo kile”.Hapo tena Baba Generose akatulia na kuliingiza gari lake sehemu ya maegesho katika Hotel moja ya pale Dodoma na kisha akatuomba mimi na mama tushuke ili tukaongee vizuri mahala pale.
Tulishuka na kuanza kuelekea ndani ya hotel ile huku kila mmoja akiwa kimya na kujiuliza maswali ambayo sidhani kama yalikuwa yana majibu sahihi kwa wakati ule. Baada ya kupata sehemu ya kukaa kila mtu aliagiza anachotaka,huku wao wakiagiza vyakula na mimi niliagiza maji ya kunywa tu!. Japo walinishangaa lakini hawakuwa na la kufanya zaidi ya kujali wafanyacho wao. Baada ya kama dakika tano za kuwapo pale, Baba Generose akafungua mdomo wake tena na kuendelea na maongezi yake ambayo mimi sikuyaelewa yana lenga nini haswa.
“Frank,katika ule mfano wa mtoto yule aliyevuka barabara, naomba niufanye uwe katika hali iliyotokea katika maisha yetu. Hapa na maana kwamba, sikumpa mwanangu elimu ya mahusiano na nini cha kufanya endapo ataingia katika mapenzi,bali nilichofanya ni kumlaumu kama wale wazazi wangelivo mlaumu yule mtoto kwa kuvuka barabara hovyo na kukoswa koswa na magari. Na kibaya zaidi nilikulaumu wewe na kutaka kukufanyia mambo ya ajabu kama wazazi wa yule mtoto mvuka barabara wangelivo nilaumu mimi kwa kumgonga mwana wao.
Frank,najua wajua kuwa hakuna mzazi apendaye au kufurahia mzazi mwingine kupoteza mwana wake. Kama ni hivyo, basi na mimi nadiriki kusema kuwa sipendi wazazi wako wakupoteze wewe kama mimi nilivyompoteza mwanangu. Ni kweli, ulijitahidi sana kumpa furaha Rose, lakini ni upendo wangu kwa Rose ndiyo niliona kama unamharibu mwanangu. Sikutaka mwanangu ajiingize katika mahusiano akiwa na umri ule, na nilimlinda nakumpa malezi yote kama mzazi apaswavyo kufanya kwa mwanawe. Ni mioyo yenu ndiyo iliyovunja kanuni yangu,na ndio maana niligadhabika sana baada ya kugundua mahusiano yenu.
Frank, samahani sana kwa kukukwaza katika maisha yako na ninaomba uniombee msamaha kwa Rose ili anisamehe pia, najua atakusikia wewe kwani wewe ndiye kila kitu kwake. Alikufa huku kachanua tabasamu kitu kilichoonesha alikuwa ana furaha sana awapo na wewe. Lakini endapo angefia miguuni mwangu, kwa yote niliyomfanyia sidhani kama angetoa lile tabasamu.
Baada ya haya machache, naomba nikuombe pia uachane na hayo maisha uliyoyaanza kuishi. Embu muangalie mama yako, katoka huko mbali ili aje akuone wewe, embu muonee huruma kidogo tu!Muache amalize uhai wake hapa duniani akiwa ana furaha moyoni mwake. Fanya hivyo kijana, ila kiukweli, naomba unisamehe sana kwa yote. Nimempoteza mwanangu, sitaki tena mzazi apoteze mwana kwa ajili yangu”.Alimaliza Baba Generose na kunyanyua glasi ya maji na kupiga funda kama nne za maji yale na kuanza kukifakamia chakula alicholetewa.
Moyo wangu ulikuwa kama unanisuta kwa maneno yale ya Baba Generose, yaani alikuwa anaomba msamaha na wakati na yeye kampoteza mtoto kwa ajili ya uhusiano wetu. Nikajiuliza, hivi ingekuaje kama ningesipo bishana na wakina Babuu, au ingekuaje kama ningekuwa siwajui wakina Babuu, haya yote yangetokea? Nilijikuta nikimuomba msamaha Baba Generose na kumuambia kuwa mimi ndiye mwenye makosa na siyo yeye. Lakini Baba Generose alisema kuwa yeye ndiye mwenye makosa, kwani hata kama nisingekuwa mimi, angekuwa mtu mwingine ambaye angekuwa na Generose.
Baada ya maongezi yale, alitupeleka nyumbani na kuahidi kuwa
atakuwa anawasiliana na sisi huku akinisisitizia nirudi kama zamani, na tena aliniambia kuwa adhani kama Generose anafurahia tabia nilizoanzisha.
************
Tayari zilishapita wiki mbili huku nikiwa nimebadilika kiasi, yaani sikuwa mtu wa kutanga tanga tena mtaani hadi usiku japo bangi na pombe sikuacha na ile tabia yangu ya ukauzu pia, haikunitoka. Nilikuwa mtu wa kukaa ndani tu! Nikitoka,basi naenda magengeni kuvuta bangi na nikiridhika narudi zangu nyumbani na kulala. Chakula nilikuwa nakula mara moja kwa siku japo dada zangu nao walikuwa wakijaribu kunipikia vyakula vizuri na vya kurudisha afya.
Siku moja nilijikuta nimemkumbuka sana Generose. Sikuwa na raha tangu asubuhi hivyo niliamua kwenda magengeni na kuchukua misokoto ya bangi na kuivuta ili niyatoe yale mawazo.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Baada ya kuvuta hali ilikuwa ni ile ile, Generose hakunitoka akilini kwa siku ile, yaani alikuja kichwani kuliko siku zote nilizobadilika na kuwa mtu wa ndani. Baada ya kuona hali ile ikinitawala sana, niliamua kutoka kwenye kile kibanda tunachovutia bangi na moja kwa moja safari ikaanza kuelekea makaburini alipozikwa Generose huku nikipitia na mashada ya maua kwa ajili ya kumuenzi mke wangu yule.
Nilipofika nilianza kwa kupalilia kaburi lake na ya jirani kisha nikaweka yale maua na baada ya hapo nikaanza kuongea maneno yangu huku nikiwa na uchungu mwingi moyoni mwangu.
“Rose, unakumbuka kuwa nilikuambia wewe unanishangaza sana? Mwanamke nisiye mjua, leo nimesimama kwenye kaburi lake nikiwa na uchungu sana. Kumbuka nilikuambia,sitakuwa tayari kukupoteza, UKIRUKA na mimi NITARUKA, kumbuka hilo. Nadhani muda wangu wa kuruka umefika”. Baada ya maneno yale nilijikuta nikilia sana huku nalikumbatia kaburi la Generose.
Ukweli nililia sana na kwa kuwa bangi zilishanilevya, nikajikuta nalala pale pale.
Katika maisha yangu nilikuwa siyo mtu wa kuamini sana ndoto. Ila wakati nimelala pale nilikuwa kama naota ile siku ambayo mama yake Generose alitukamata tukiongea usiku na baadaye kumpora simu Generose. Kesho kama unakumbuka nilikutana na Generose na alinipa taarifa za nini kilichotokea. Basi mambo yale yalikuwa kama yanajirudia lakini ni kwa maneno tofauti. Nilimuota Generose vile vile akiwa na mavazi yake ya shule. Katika ndoto ile Generose aliongea mengi sana na zaidi alinisisitiza nibadilike niwe kama zamani.
“Frank, najua nimekuumiza sana kwa kuondoka kwangu, lakini sasa yakupasa kuinuka na kutawanya mabawa yako nakupaa kwa ajili ya kuanza maisha upya bila mimi. Na badala ya kuongelea kifo changu ni heri usherehekee maisha tuliyoishi mimi na wewe”.Generose alikuwa ananiambia maneno hayo usingizini,na mimi nikamjibu.
“Rose unajua siwezi kuwa kama yule bila wewe, naomba nikufuate huko ulipo”. Nilikuwa naongea huku nikitaka kumfuata pale alipo.
“Hapana Frank, mfikilie Mama na ndugu zako kwanza kabla ujaamua kufanya hivyo. Mimi sikufikilia hayo na ndiyo maana roho yangu inatanga tanga sasa hivi. Ni hadi utakapo badilika ndipo na mimi nitapumzika kwa amani, nakuomba Frank, rudi kama zamani”.Alisisitiza Generose.
“Rose, nimekusikiliza mama yangu, sitotaka hata huko ulipo uhangaike. Hakuna watu wenye bahati kama wewe, na ninamshukuru MUNGU kwa kuwa mimi nilipata bahati ya kuwa na wewe.Upumzike kwa amani mke wangu, siku MUNGU akiamua nije nikuone basi tutakutana”.Nilimjibu Generose.
“Asante Frank, sasa naweza kwenda kwa amani. Na muambie baba kuwa nimemsamehe na nina mpenda sana. Na wewe usisahau kuwaheshimu wanawake pamoja na kuufungua moyo wako kwa mtu mwingine. Usichoke kupenda wala kuogopa kupenda, nipo na wewe daima”.Alimaliza Generose na kama siku ile ilivyotokea, Rose alielekea kama shuleni kwao na mimi nikawa narudi nyuma kimgongo mgongo.
“I love you Frank”.Aliongea hayo huku akinipungia mkono.
“I love you too,Rose”.Na mimi nikamjibu na hapo Generose alipotea machoni mwangu baada ya mimi kushituka toka usingizini. Ilikuwa tayari ni jioni.
“Pumzika kwa amani Rose, siku moja tutakutana”.Niliongea hayo huku nikirekebisha mchanga wa kaburi na baada ya hapo safari ya kurudi nyumbani ikaanza. Ila kabla sijafika nyumbani nilipitia kwa akina Generose nakumpa taarifa Baba Generose kama Generose alivyoniambia.
Ghafla hali yangu ya zamani ilirudi na kuanza kukimbia njiani huku nikitabasamu na breki ya kwanza ilikuwa kwa akina Babuu ambapo kama kawaida yao, walikuwepo wote.Nilifika na kuanzisha kelele zangu za zamani kitu kilichofanya kila mmoja kushangilia na kusema “Man’Sai is back”.
“Hilo bwana,limerudi. James Bond,Man’Sai mwenyewe”.Ilikuwa sauti ya Babuu ikinilaki kwa furaha.
“Ha ha haaaa. Nilikuwa kwenye kipindi cha mapito kidogo,ila nimerudi”.Niliwajibu na wote tukacheka huku tukikumbatiana.Ilikuwa ni furaha sana kwa ujio wangu. Baada ya kusalimiana na wakina Babuu, safari ikaanza kwenda nyumbani.
“Oyooooooooo, nimerudi jamani, nimerudi tena”.Ilikuwa ni sauti yangu baada ya kuingia geti la nyumbani. Sauti ile iliwafanya dada zangu, baba na mama kutoka nje na kuona nini kimejiri,isije kuwa nimechanganyikiwa.
“Ni mimi jamani, Frank. Ule muda wa mapito umepita,furaha imerudi tena”.Ghafla dada zangu walinikimbilia na kunirukia kwa furaha huku baba na mama wakiwa kama hawaamini. Baada ya kumalizana na dada zangu nilimfata mama na kumkumbatia kwa nguvu.
“Ulisema utakuwa unanikumbatia kila siku”.Nilimuambia sikioni huku nikiwa bado nimemkumbatia.
“Embu toka hapa, lione likichwa lake kama boga”.
“Haha haaa, huo ndiyo utani wako,bado ujauacha tu!”.Niliongea huku namuachia na kumfuata baba naye nikamkumbatia na kumshukuru sana kwa yote aliyonifanyia kama mzazi.
*************
Baada ya miezi kadhaa walinishauri nianze tena kidato cha sita na dada zangu katika shule ile ile ya Jamhuri. Nilikubali na nilianza japo walikuwa wamefika mbali kidogo kimasomo.
Siku moja wakati naenda shule nilipita ile njia aliyokuwa anapenda kuipita sana Generose,nilipofika pale,niligeuka nyuma kuangalia nilipotoka na kukumbuka siku ile nilivyoenda kwa akina Babuu na kukuta ule ubishani. Na mimi kwa kulazimishwa,nikajiunga na ubishani na mwisho wa siku nikachukua jukumu la mimi kuwa jaribio.
Kisha nikakumbuka siku ile ya kwanza nilipokutana na Generose na yeye kukataa kuwa pale hakuna Generose. Pia nikakumbuka siku ile nilipokutana naye pale Saint John hadi juisi ikampalia kwa sababu ya swali langu. Na baadaye taswira ikaja siku ile mara ya kwanza kuuona mwili wake huku nikimaliza kwa kukumbuka tabasamu lake pamoja na dimpoz ambazo alikuwa nazo.
Nitabasamu baada ya mawazo hayo, kisha nikajisemea.
“Umenibadilisha sana maisha yangu,nitakuenzi daima. You’re MY ROSE, I Miss You and I will still miss you forever”.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Hiyo ndiyo historia ya maisha yangu na Generose,Mamie”. Nilimaliza kumuhadithia Miriam ambaye nilikuwa naye kitandani wakati namsimulia.
“Dah!Pole sana Dadie wangu,kumbe ndiyo ulipitia hayo yote?Dah!ila tumshukuru MUNGU,kwani hayo yote ni maisha tuliyopangiwa kuyapitia”.Aliongea Miriam kwa utaratibu,na mimi nilikubaliana naye.
Nikambusu mdomoni busu la haja,na baada ya hapo tukajikuta katika dunia nyingine ya wapenzi.
…MWISHO..
0 comments:
Post a Comment