Search This Blog

Wednesday, 1 June 2022

MUAFAKA - 3

 







    Simulizi : Muafaka

    Sehemu Ya Tatu (3)



    “Ni kwa sababu nina kupenda Lulu… I love you…I really do …dear!” Lulu aligeuka na kutaka kuondoka, bali Onespot alimshika mkono na kumgeuza amuangalie yeye.

    “Unataka nini?!” Lulu alisema kwa ukali.

    “Sema wewe unataka nini, nifanye, hata kama ni kukupigia magoti mbele ya watu mimi niko tayari.” Lulu alikuwa karibu chozi limtoke, alisema kwa taratibu kwa sauti ya kubembeleza.

    “Tafadhali Onespot niache usinibughudhi…ndilo ninalolitaka, please, leave me alone… Hebu niache niwe huru.” Onespot nae alijifanya mnyonge ajabu na kumuulizia Lulu pasipo kumuangalia usoni, kwa sauti ya masikitiko.

    “Ina maana… Lulu… Wewe ni mtumwa kwangu?!”

    “La hasha… Mimi si mtumwa kwako, bali vitendo vyako kwangu, vinanifanya nikose uhuru ninaostahiki.”

    “Ni vitendo gani hivyo Lulu? Unaweza kuniambia?!” Lulu alisimama hapa aliposimama huku akihema hema kwa chuki, kichwani mwake alifikiri aondoke au amuambie, mwisho aliona dawa ni kumwambia, alimtamka kwa haraka haraka,CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Vitendo vyako, kama ulinyofanya muda mchache uliopita vya kunikumbatia mbele za watu… ulikuwa una maana gani? Mimi ni nani wako? Ni mwanamke wako? Unafikiri watu watanielewa vipi? Usifikiri kuwa mimi ni msichana rahisi tu wa kukumbatiwa na kila mwanamme anaejihisi kufanya hivyo. Mwisho kabisa tendo la kuja nyumbani kwetu bila ya kualikwa. Kwa nini ufanye hivyo?!” Muda wote huu Onespot alimtulizia macho Lulu kwa kumuangalia na kumsikiliza kwa makini na huzuni usoni, baadae akajibu kwa sauti ya upole,

    “Ni kwa sababu ya upendo Lulu, nakupenda. Naomba unisamehe kwa kila nililokukosea, si dhamira yangu kukudhalilisha. Love is blind you know, mapenzi ni

    upofu. Apendae huwa anafanya mambo bila kuyaona kuwa ni mabaya. Niwie radhi Lulu, na ukubali kuwa yote niliyotenda ni kwasababu nakupenda mno.” Lulu alitulia na kumuangalia Onespot, kisha akatamka kwa sauti ya chini kumuuliza mvulana huyo,

    “Lakini Onespot si nilikuambia kuwa sikupendi!”

    “Pia uliniashiria kuwa unampenda Edward!”

    “Kumbe unajua, Sasa?!”

    “Ninatambua kwamba kukutaka kwangu hapo awali hakukuwa na mfuato mwema Lulu, my approach was not good. Nilijitapa mno, lakini baadae nilijua kuwa ninakupenda kweli, na kukuhurumia kuhusu huyo Edo wako!” Lulu alitoa macho kumsikiliza Onespot ambae alipofika hapo alisita kusema na kumuangalia Lulu.

    “Mbona sikuelewi Onespot?”

    “Edo ni ndumilakuwili”

    “Eeeh, eti unasemaje?!!” Lulu alizidi kumkazia macho Onespot kwa shauku ya kutaka jibu.

    “Ndio, Edo kakughilibu, wewe pamoja na Vicky.”

    “Vicky?!”

    “Vicky Kapate, katibu muhtasi wangu ni girlfriend wa Edo Oloi, na kila mfanyakazi hapa kwenye kampuni hii, analijua jambo hili isipokuwa wewe.” Onespot alimpa muda Lulu aimeze taarifa hiyo kwanza kabla ya kuendelea kusema,

    “Kwa kuwa sasa hivi, Vicky nae ni mwanamitindo basi subiri utaona mwenyewe. Mimi ninakuambia hili tu sababu nakupenda. Nitasikitika sana nitakapokuona huna pakuegemea wakati Edo na Vicky watakapoamua kuwa wazi juu ya pendo lao jambo ambalo litakuwa hivi karibuni hali ya kuwa mimi nipo na ninakupenda kweli.” Lulu hakujua asema nini alibaki amesimama huku damu ikimwenda mbio ndani ya mwili wake. Onespot aliongeza kusema,

    “Ninakuomba Lulu uniruhusu nikusindikize nyumbani japo kuwa mpaka nnje ya nyumba yenu tu, sawa?” Lulu bila kujijua alijisikia akitikisa kichwa kukubali na kutoa sauti ndogo ya chini.

    “Sawa… Onespot.”

    “Basi nisubiri hapo nnje ya ofisi” Onespot alimwendea yule mpiga picha aliekuwa amekaa nae. Kama kawaida yao wakaongea kidogo bila kusikika walichoongea, kisha akatoka na kumfuata Lulu aliekuwa nnje ya ofisi amesimama, anamsubiri. Alikata mitaa ya jiji la Dar es salaam taratibu, Onespot akiwa kimya nyuma ya usukani na Lulu nae akionekana ana mawazo kibao aliketi kwenye kiti cha kushoto mbele ya gari. Walipofika mbele ya nyumba aishio Lulu, Onespot aliliegesha gari mbele ya nyumba, akateremka haraka haraka, akazunguka na akaenda kumfungulia Lulu mlango wa gari. Baada ya Lulu kushuka, alimsimamisha mbele ya mlango huo wa gari, akamshika mabega yote mawili kwa mikono yake na kusema taratibu,

    “Sikiliza Lulu, nakuomba usiamini maneno yangu moja kwa moja. Tumia macho yako vizuri utaona. Tumia masikio yako vizuri.. utasikia. Tumia kauli yako vizuri katika kuuliza utagundua na zaidi ya yote tumia akili yako katika kufikiri, lakini utambue kwamba hakuna mwizi anaeiba kisha akasema… hata mahakamani licha ya kuulizwa na mtu uraiani… kwa heri Lulu, nenda kapumzike tutaonana kesho.” Onespot alimuacha Lulu akivuta hatua kidogo kidogo kuelekea mlango wa mbele wa nyumba, alipoufikia karibu, nae aliingia ndani ya gari lake na kuondoka.



    * * *



    Kadri mazoezi yalivyoendelea kupamba moto ndivyo wakati wa kukutana Lulu na Edo ulivyokuwa mdogo au haupo. Kuonana kwao kulikuwa ni kwa

    kusalimiana na kila mmoja kuelekea chumba chake cha kufanyia mazoezi. Edo yeye alikuwa akijipa matumaini kuwa baada ya onesho tu atamuuliza Lulu iwapo tayari amekwisha fikiria suala la ndoa na ikiwezekana wapange mipango yao. Edo alikuwa anampenda sana Lulu kwa wakati huu alijihisi. Lulu nae pamoja na hisia za pendo kubwa juu ya Edo, lakini tayari alianza kutia shaka ya kughilibiwa na wasiwasi juu ya uhusiano wa Vicky na Edo. Alianza kufarijika na maneno ya Onespot juu ya kuwa hakuamini kikamilifu, kwani wakati mwingi wa Onespot ulipotezwa kwenye mazoezi alipokuwemo Lulu. Ipo siku Edo alipatwa na udhuru wa kufiwa na jirani yao mtaa anaoishi. Habari hii alimueleza Vicky wakati wapo katika mazoezi.

    “Samahani Vicky, leo itanibidi niondoke mapema ili nikawahi maziko ya jirani yetu.” Vicky hapo hapo aliwaza mbinu za kuitumia nafasi hiyo kufanikisha azimio lao. Alijidai kumshauri Edo kwa kusema,

    “Unaonaje ukaenda kumfahamisha Onespot habari hii? Sababu akinikuta mimi nimekaa bure, itakuwa kero.” Edo alifikiri, kisha akaona si ushauri mbaya.

    “Sasa sijui nitamuona wapi saa hizi!” Vicky alianza kucheka kwa nguvu kiasi cha kumfanya Edo ashangae.

    “Mbona unanicheka Vicky?!”

    “Hapana Edo sikucheki wewe, namcheka huyo Onespot!”

    “Ana nini?!”

    “Ah! Kwani siku hizi anabanduka chumba cha mazoezi cha Lulu! Nina hakika utamkuta huko huko!” Edo baada ya shughuli zake, alienda chumba alichokuwepo Lulu, kweli alimkua Onespot amekaa, na baada ya yeye Onespot kumuona Edo tu, alijifanya hakumuona na akawa anamwita Lulu.

    “Lulu, Lulu?”

    “Bee.”

    “Hebu njoo mara moja.” Wakati Lulu anamwendea Onespot na Edo nae akamwendea huyo huyo. Kwa pamoja walifika mbele ya Onespot.



    “Samahani Onespot?” Edo alianza kusema.

    “Bila samahani Bwana Edo.” Onespot alimjibu.

    “Leo nitakuwa na udhuru kidogo huko ninakoishi kwa hiyo napenda kukutaarifu kuwa nitaondoka mapema,” Edo alisema kwa heshima.

    “Hapana wasiwasi bwana Edo unaweza kwenda tu, Lakini mazoezi yanaendeleaje na Vicky?!” Onespot alimruhusu na kuongeza kwa kumuuliza Edo.

    “Yanaendelea vizuri tu, Vicky is ok!” Edo alimgeukia Lulu na kumueleza kuwa siku hiyo atakuwa msibani, Lulu alimuitikia vizuri tu, Edo akatoka kwenda zake. Baada ya muda si mrefu Vicky alingia chumbani alipokuwepo Onespot na Lulu. Alimuonesha ishara Onespot ambayo ilimfanya asiondoke alipokuwa Lulu. Nae Vicky alimwendea palepale na alipohakikisha kuwa atakalolisema Lulu anaweza kulisikia, alifunua kinywa chake kwa sauti ya kubembeleza.

    “Bosi Onespot, ninaomba ruksa ya kuondoka mapema leo nina udhuru kidogo ninataka Edo anipeleke…nadhani na yeye amekwisha kujulisha pia.” Lulu alisikia kila neno alilolitamka Vicky pasipo shida. Alizungusha shingo yake kuhakikisha kama ni kweli Vicky ndie anayetamka maneno hayo. Vicky nae alijifanya kama vile ndio kwanza anamuona Lulu nae akagutuka kidogo na kusema:

    “Ah! Vipi Lulu…mambo?!”

    “Safi tu, sijui wewe Vicky!” Lulu alijibu bila wasiwasi.

    “Mimi ni mzima tu, ninaendelea na zoezi.”

    “Na hilo zoezi nalo linaendeleaje?!” Lulu aliuliza swali hili moja lakini akiwa na maana ya zaidi ya moja.

    “Nina shukuru kutokana na juhudi za Edo, nimekwisha zowea…nadhani sitapata tabu siku ya onesho ikifika.”

    “Ninakutakia mafanikio katika shughuli yako Vicky.” Vicky alipoambiwa hivi

    kidogo alishtuka kimoyomoyo na kuwaza vipi Lulu amekwishaelewa lengo lao nini?!’ Onespot alimfariji aliposema yafuatayo kurudia ombi lake.

    “Vicky usiwe na hofu…ruksa, unaweza kwenda unapotaka wewe na Edo, kwani hata Edo mwenyewe amekwisha kuja kunijulisha juu ya udhuru wenu. Nendeni mnapotaka mradi tu shughuli za kampuni ziende vizuri.” Lulu alijisikia miguu ikimtetemeka. Aliwaza kichwani kwake na kuona kuwa ni kweli upo uhusiano wa karibu zaidi kati ya Edo na Vicky. Edo…Edo anayempenda kwa moyo wake wote, kwa nini amdanganye?! Anajidai kuna msiba, kumbe vile ana ahadi na Vicky? Hapo hapo alihisi chozi linamjia machoni mwake. Aliomba radhi ya kutaka kwenda kujisaidia kidogo. Alipoingia chooni la kwanza kulifanya aliangua kilio cha kimya kimya. Alitumia zaidi ya dakika tano chooni humo. Mwisho aliosha uso wake, akajaliza vipodozi usoni mwake. Alipojiangalia kiooni na kujiona yupo sawa, alitoka chooni kuja kuukabili ukweli aliofikiria yeye kwamba ni sawa.

    Wakati Lulu anaingia chumba chake cha mazoezi kutoka kujisaidia, Onespot na Vicky walikuwa bado wamesimama pamoja. Walipomuona Lulu anaelekea walipokuwa wamesimama Vicky alipaza sauti na kusema kumwambia Onespot,

    “Na mimi ni mwanamke vilevile kama wanawake wengine na Edo ni mseja, si mume wa mtu, kwa hiyo sioni ubaya wowote nilioufanya.” Kisha akaanza kuondoka na kuzidi kusema kwa nguvu kumpasha Onespot,

    “…Babu weee! Ulivyoshindwa kuvila usivitie ila eeh.” Huku akigusana mabega na Lulu wakipishana. Lulu aligeuza shingo kumuangalia Vicky ambae amekwishafika mlangoni. Onespot alikuwa anatikisa kichwa wakati Lulu amegeuka tena kumuangalia kwa sura ya mshangao. Lulu ilimbidi amuulize Onespot kwa sauti ya kuchanganyikiwa,CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Kwani vipi?! Mbona siwaelewi?!” Onespot alijiinamia kidogo, kwa sauti ya chini na bila kumuangalia Lulu usoni alisema,

    “Ni hayo hayo niliyokwisha kukueleza!”

    “Yapi Onespot?!”

    “Ah, si hayo ya Vicky na Edo!”

    “Eeh, wana nini?!!” Onespot alinyanyua uso wake sasa kumuangalia Lulu na kumueleza.

    “Nilikuwa ninajaribu kumwambia Vicky kwamba anavyofanya sio vizuri… kutembea na Edo, wakati anafahamu kuwa Edo ni boyfriend wako! Basi hayo majibu aliyonipa, wacha, sikutegemea, nadhani mengine umeyasikia ulipokuwa unaingia. Anasema yeye hajali, maadamu Edo si mume wa mtu, bado ni mseja, atakwenda nae tu. Na ananishutumu mimi kuwa labda ninamuonea wivu. Nimeshindwa kumtongoza basi niwaachie walioweza kufanya hivyo, nisimtie ila.” Lulu alijiona amezidi kuchoka kutokana na maneno hayo. Alijikaza kidogo na kusema,

    “Sio peke yake mwenye makosa, siku zote mwanamke yeye huwa anaanzwa kutakiwa. Ikiwa yeye Edo anajua kuwa ana girlfriend kwanini atafute mwingine?! Usimlaumu sana Vicky!” Onespot kusikia hivi, moyo wake ulifurahi ajabu na akajipongeza kimoyomoyo. Aliona sasa amekwishampata Lulu. Alijaribu kuangusha turufu yake nyingine.

    “Hakuna ambalo haliwezi kutokea kwa sisi binadamu ulimwenguni humu. Na wala hakuna la ajabu. Nakuomba Lulu ujaribu kusahau yaliyopo na kutia bidii zaidi katika kazi yako. Sahau habari za Vicky na ….Edo. Kwa kukusaidia zaidi unaonaje kesho nikakupeleka pahali ambapo ungepoteza mawazo kidogo?!” Lulu alitulia tuli akiangalia chini, wakati huu walikuwa wamekaa juu ya viti chumbani humo. Alinyanyua uso wake na kusema,

    “ Ninaweza kusahau habari za Vicky, lakini siwezi kusahau habari za Edo…Onespot. Kwa sababu ninampenda mno, kiasi cha kutoamini kuwa huyo Edo ninayemjua mimi, ndie huyu tunayemzungumzia hapa sasa hivi!” Alitulia kidogo

    kuvuta fikra kisha akaendelea kusema,

    “Unajua Onespot kuwa Edo amekwishanitaka tuoane?!”

    “Hapana.” Onespot alijibu kwa mkato.

    “Basi ni kweli ninakuambia, alinitaka tuoane, na hivi sasa anasubiri jibu langu tu…Sasa nashangaa kuona mambo yako hivi!!” Lulu alishika tama na kukodoa macho kuangalia pasipo kuona anachokiangalia. Onespot mara moja alitambua kuwa asipoucheza mchezo huo kwa uangalifu hataambua kitu kama anavyotaraji. Sababu aligundua kuwa ni kweli Lulu anampenda Edo. Alitamka pasipo kujiamini,

    “Lakini Lulu si nilikuambia kuwa Edo kwa suala la wanawake, sivyo kama anavyoonekana? Mtu akimuona anamuona ni mkimya na muaminifu, lakini bwana yule mbele ya wasichana….mhuu sikuambii kitu. Na sisi wanaume tunajuana tulivyo.”

    Lulu alimuambia Onespot kuwa ni lazima amuone Edo. Kwa kuwa kwa siku hiyo haiwezekani sababu amekwishaaga kuwa ana udhuru, basi atamsubiri siku ya pili, amuombe wakutane jioni yake. Onespot alisisitiza kwamba haina maana kwa wakati ule, angesubiri kidogo kwanza, angalau mpaka onesho litakapofanyika na kumalizika. Lakini Lulu kwa kiasi alichosikia na kuona, basi itakuwa ni bora zaidi wakutane yeye Lulu na Edo, ili walizungumze suala la uhusiano wao. Hapo ndipo Onespot akaangusha turufu tena na kusema,

    “Kama ni suala la kuona, basi Lulu bado hujaona. Unaonaje ukinikubalia tukutane pahali kesho ili nikuoneshe cha kuzungumza zaidi na Edo? Si kwamba ninajaribu kuwa fitina, la hasha, bali ninajaribu kukusaidia wewe kwa unalolitaka mwenyewe. Na ninafanya hivi kwa sababu ninakupenda.” Onespot aliamuangalia Lulu amuone atasemaje kwa hayo aliyomuambia. Lulu aliwaza ni kitu gani hicho ambacho ataoneshwa yeye kiwe ni kigezo cha mazungumzo yake na Edo, hakuficha shauku yake aliuliza,

    “Ni kitu gani unachotaka kunionesha Onespot?!”

    “Ni mpaka hapo kesho tutakapokutana, tusiandikie mate wakati wino upo!” Lulu hakuwa na jinsi wala hila ya kukataa, bali ni kukubali tu kukutana na Onespot siku inayofuata. Si kwa sababu alitakiwa iwe hivyo, bali alikuwa anahamu kubwa ya kuona hicho ambacho anataka kuoneshwa na Onespot.

    * * *



    Siku iliyofuata, asubuhi katika ofisi za kampuni ya ADFC, shughuli ziliendelea kama kawaida, lakini kabla hazijaanza, Edo kama kawaida yake, alimtafuta Lulu amsalimu kwanza.. Walipokutana, Lulu hakuwa mwenye furaha kabisa, baada ya kusalimiana Lulu alimuuliza Edo,

    “Vipi Edo…habari za mazikoni?” Edo bila kuonesha shaka wala wasiwasi alijibu,

    “Salama tu, tulizika salama. Lakini maiti ilikwenda kuzikwa kijijini kwao kupita Mbagala. Sijui kunaitwa Kongowe…mbali kweli. Nilirudi usiku nikiwa hoi!.” Lulu alimuangalia kwa jicho lisiloeleweka kiasi ya kuwa Edo ilibidi amuulize,

    “Vipi Lulu?! Mbona unaniangalia hivyo?!”

    “Hapana sina neno?!”

    “Ndio, lipo jambo, ni lazima liwepo, kwani umebadilika mno Lulu!!”

    “Mbona na wewe unaonekana unashuku sana kuwa kuna jambo lililonikera?!” Edo alipomuona tayari amekasirika sana, alihisi lipo tatizo. Kwa hiyo hakutaka waliongelee hapo walipokuwa kwa wakati huo. Alimuomba kwa sauti ya utaratibu,

    “ Tafadhali Lulu, ninakuomba tukutane leo, baada ya saa za kazi, tafadhali sana. Inaonekana kuna ulazima wa mazungumzo kati yetu.” Lulu alikumbuka kuwa siku hiyo alikuwa na ahadi na Onespot ili akaoneshwe kitu ambacho hakijui ni nini,

    kwahiyo hapo hapo alisema kumwambia Edo,

    “Leo haitowezekana.” Lulu akiwa bado amenuna alifikiria sijui amwambie ukweli. Mwisho akaona kuna dhara gani kusema ukweli, na kwa vile hana uhusiano wowote wa kimapenzi na Onespot, aliamua amwambie ukweli tu Edo, alitamka,

    “Kwa sababu nina ahadi ya kukutana na Onespot leo.”

    “Eheeeh!!! Ati nini?!” Edo aliuliza kwa sauti ya juu na mshangao mkubwa.

    “Tunakutana na Onespot leo.” Lulu alirudia kusema kwa msisitizo.

    “Kwa shughuli ipi? Na wapi mtakutania?!”

    “Wewe unadhani ni kwa shughuli gani? Edo, mbona unapokutana na Vicky sikuulizi kwa shughuli gani?!” Edo aliposika hivyo, aliona haina maana kubishana, alijikaza asihamaki na kumuuliza tena kwa sauti ya chini na taratibu,

    “Sawa…sawa Lulu, sasa panga wewe ni lini tukutane nje ya ofisi hizi?” Lulu haraka aliwaza na kuona baada ya siku hiyo atakuwa tayari ameoneshwa alichooneshwa na atakuwa tayari kumkabili Edo. Alimjibu na kumwambia,

    “Tukutane kesho baada ya kazi Edo.”

    “Vema, ni mpaka hapo kesho Mungu akipenda.”



    * * *



    Taa zenye muangaza mdogo zilikuwa zikiwaka ndani ya ukumbi wa kulia chakula wa hotel kubwa wenye meza nyingi zilizotandikwa kwa unadhifu kwa vitambaa safi na vizuri vya meza. Baadhi ya meza zilikuwa na viti sita, baadhi viti vinne, baadhi viti vinane na nyingine zilikuwepo zenye viti viwili tu. Kati ya hizi, moja wapo waliketi Lulu na Onespot juu ya viti na kuiweka kati meza hiyo. Onespot alimuuliza Lulu,

    “Ungependelea chakula gani?” Kabla Lulu hajajibu alimsogezea menu na kuendelea na kusema, “…hebu angalia vilivyopo!” Lulu hakuwa na hamu kabisa ya kula chochote, kilichomleta hapo ilikuwa ni hicho alichokusudiwa kuoneshwa.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Samahani Onespot, sijisikii hamu ya kula kabisa…. Nitakunywa kinywaji baridi tu”

    “Una uhakika huhitaji chakula?”

    “Kabisa …nina hakika kabisa, asante.”

    “Basi na mimi pia sitakula, nitakunywa tu.” Waliagiza vinywaji walivyohitaji, na vitafunwa kidogo, kisha wakaanza kuzungumza. Onespot alimwambia Lulu,

    “Kwanza kabisa nataka unielewe Lulu kwamba nitakachokuonesha hapa, utakiona tu, lakini huondoki nacho, hilo ni mosi. Pili narudia tena, sifanyi hivi kwa ufitina bali ni kwa pendo langu juu yako.”

    “Sawa Onespot nimekusikia na kukuelewa pia.” Onespot alinyanyua briefcase aliyokuja nayo, akaiweka juu ya meza na kuifungua.. Alitoa bahasha kubwa ya kaki akaiweka mezani. Kisha akaifunga ile briefcase na kuirudisha chini karibu na miguu yake, akasema,

    “Ninakuambia utakachokiona hapa huondoki nacho, kwa sababu, mimi nimekichukua kutoka ndani ya dawati la meza ya Vicky, pasipo mwenyewe kujua. Sasa ningependa nikirudishe pale pale.” Wakati anasema hivi alifunua ile bahasha akatia mkono wake ndani yake, akatoa picha nne zenye ukubwa wa inchi nne kwa sita na kuzitandaza juu ya meza huku akiendelea kusema,

    “Funua macho yako uweze kuona vizuri ninachokuonesha. Angalia hizi picha hapa za Edo akiwa na Vicky.” Huku moyo ukimwenda mbio, Lulu alinyoosha mkono wake na kuinyanyua moja ya picha zile nne. Ilikuwa kweli ni Edo akimfunga zipu ya mgongoni Vicky. Lulu hakuamini macho yake, aliikodolea macho akaiangalia kwa sekunde chache, bila kutamka chochote. Kisha akaiweka na kuchukua nyingine ya pili, hii ilionekana kama vile Vicky yupo juu ya kifua cha Edo, wamesimama, lakini

    kichwa chake amekiegemeza kifuani pa Edo, nayo aliiangalia kwa makini, kisha akaitua na kuchukua nyingine ya tatu. Hii Edo alikuwa amemshika Vicky shavuni kwa kiganja chake cha kulia huku akimuangalia machoni. Nayo pia aliiangalia akaiweka na kuchukua ya nne na ya mwisho. Hii Edo alikuwa amekaa juu ya kiti, Vicky nae amekaa juu ya mapaja ya Edo, akiwa mikono yake ameizungusha kwenye shingo ya Edo huku yeye Vicky akitoa tabasamu kubwa. Alitulia na picha hiyo mikononi mwake kwa muda usiopungua dakika tatu.



     Wakati huu wote Onespot alitulia kimya akinywa kinywaji chake taratibu huku akimuangalia Lulu usoni. Lulu kabla hajaiweka juu ya meza picha hiyo ya nne, bila kujijuwa alisikia chozi likimchirizika juu ya mashavu yake. Kuona vile Onespot alitoa kihanjifu toka mfuko wake wa koti na kunyoosha mkono wake kumpa Lulu. Nae alikipokea na kupangusa machozi yake. Onespot alisema,

    “Pole sana Lulu…I am sorry.”

    “Ahsante sana Onespot!”

    “Je, umeonaje picha hizo?!”

    “We acha tu.”

    “Je, unamfikiriaje Edo?”

    “Nampenda sana!” Onespot ambae wakati akiuliza maswali haya yote alikuwa ameegemea kiti, aliposika hivi alikaa wima na kwa ghafla na kutamka,

    “Enhee, unasema unampenda sana Edo?!”

    “Lakini…sijui niseme nini!!” Onespot alikuwa hakuelewa, lakini sasa akaanza kumuelewa Lulu.

    “Usiseme kitu Lulu, fikiri kwanza. Si ulisema ulitaka mkutane na Edo?”

    “Ndio, nilipenda nikutane nae… na yeye pia ameniambia leo, kuwa anataka kukutana na mimi.” Onespot alionekana kufikiri kidogo, kisha akasema,

    “Lakini Lulu, pamoja na yote haya, ukumbuke tuna kazi kubwa inayotusubiri siku tatu tu mbele yetu… ya onesho la mavazi. Tafadhali naomba utakapokutana na Edo…msije mkakasirishana kiasi cha kususia jukumu hili, kwa hapa lilipofikia.” Lulu hakuwa makini kwa chochote, aliwaza kukutana na Edo tu ili apate ufumbuzi wa picha zile, alimuhakikishia Onespot kuwa asiwe na wasiwasi na suala la onesho, litafanikiwa tu, na kuongeza,

    “Kwa sasa. Onespot nakuomba unisindikize nyumbani, kwani ninahitaji muda mrefu wa kufikiri kabla ya kesho…na ahsante kwa kunionesha picha hizi.”

    Jioni ile, wakati Lulu ametoka na Onespot, Vicky nae kabla ya kuondoka ofisini mwao, alitafuta kila njia ya kuzungumza na Edo, ambae kwa siku hiyo nzima hakuonekana kuwa ni mwenye furaha kutokana na kauli ya Lulu kwamba anakwenda kukutana na Onespot. Kwa kuwa Vicky alilijua jambo hilo, basi alianza kumkera Edo kwa kumuuliza maswali madogo madogo. Edo nae aliyajibu kwa mkato pasipo kuendeleza. Ndipo Vicky alipomsumbua zaidi Edo kwa kumuuliza,

    “Leo una nini Edo?!”

    “Hapana sina neno, kwani unanionaje Vicky?!”

    “Nakuona huna furaha umekasirika, ambavyo sio kawaida yako!”

    “Mbona nipo kama nilivyo siku zote!” Vicky alitoa tabasamu kubwa lililoambatana na mguno, huku akimtazama Edo usoni, kisha akamwambia

    “Kama ungekuwa kama ulivyo siku zote nisingekuuliza. Ninajua umekasirika, au tusema ndio umegundua baada ya muda mrefu kupita?” Edo kusikia hivi alitulia kidogo, kisha akamkazia macho Vicky nakumuuliza,

    “Nimegundua?! Nimegundua kitu gani?!”

    “Eeh, lakini usinitangaze Edo nisije nikamwaga unga!” Edo kwa shauku na kusisitiza alimuuliza tena Vicky.

    “Sema Vicky, kitu gani mbona sikuelewi?!”

    “Nilifikiri…labda umekwishajua kuwa Onespot anatembea na Lulu siku hizi.”

    Kabla hata Edo hajasema kitu, Vicky aliendelea kusema kwa haraka haraka.

    “…Lakini tafadhali usije ukamwambia mtu kuwa mimi ndiye niliyekuambia, sababu Onespot mwenyewe hufanya ni siri kubwa… hata leo hii wanatoka nje pamoja.” Edo alifikiri kidogo kwa kuinamisha kichwa, kisha akanyanyua uso wake kumuangalia Vicky na kusema,

    “Hilo jambo la kutoka nje pamoja leo ninalielewa, ameniambia Lulu mwenyewe… na hilo la Lulu kutembea na Onespot siliamini, sio kweli.”

    “Una maana huniamini Edo?”

    “Ninakuamini lakini siamini uniambialo.”

    “Sasaa…unaweza kunisubiri kiasi cha dakika chache nikachukue kitu nje nikuoneshe ambacho kimenifanya nikwambie hivyo, licha ya kuwa ni mengi yanayosemwa kuhusu Onespot na Lulu…nisubiri kidogo.” Vicky alitoka haraka haraka baada ya kusema haya, bila kusubiri jibu la Edo. Alikwenda moja kwa moja mpaka ndani ya ofisi ya Onespot, wakati huu wafanyakazi wengi tayari walikuwa wamekwisha ondoka. Baada ya muda mfupi alikuja chumbani alimokuwemo Edo, akiwa ameshika bahasha kubwa nyeupe mkononi mwake: Alimsogelea Edo na kumwambia,

    “Njoo uone mwenyewe kwa macho yako, nadhani baada ya hapo utaamini ninayokuambia.” Edo alimsogelea Vicky pale aliposimama. Vicky alitia kiganja ndani ya bahasha hiyo na kutoa picha zenye ukubwa wa inchi sita kwa inchi nne, kama zile alizooneshwa Lulu na Onespot, zilikuwa nne, lakini hizi zilikuwa zimemuonesha Lulu na Onespot. Vicky alisema,

    “Tazama, tazama!” Huku akizikunjua kunjua picha hizo zilizokuwemo viganjani mwake, kama vile karata. Edo alizipokea picha hizo zote kwa kiganja chake cha kulia na kuanza kuziangalia kwa kutumia viganja viwili, kama vile ameshika karata na yeye, picha ya kwanza ilionesha Onespot amemkumbatia Lulu kwa nyuma. Picha ya pili ilionesha Onespot amemshika mabega Lulu kwa kupitisha mkono mgongoni wakiwa wanatoka chumbani. Picha ya tatu ilionesha Lulu na Onespot wamesimama mbele ya mlango wa gari ya Onespot wakiwa yeye Onespot ameweka viganja vyake vyote viwili juu ya mabega ya Lulu na picha ya nne na ya mwisho inaonesha Lulu yupo nje ya nyumba yao akipungiana mkono na Onespot ambae yupo karibu na gari yake. Edo alizitulizia macho picha hizo kisha akamuuliza Vicky,

    “Samahani Vicky, picha hizi umezipata wapi?!”

    “Ofisini kwa Onespot, juu ya meza.”CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Je, unaweza kuniachia picha hizi angalau kwa leo tu?…kesho nitazirudisha!”

    “Hata, kwa hili siwezi Edo. Unataka nifukuzwe kazi?! Tena ninakuambia usimwambie mtu tafadhili, hata huyo Lulu mwenyewe…kwa usalama wangu.” Wakati Edo ameshangaa kumsikiliza Vicky, akiwa amezishika picha hizo, Vicky alizipora ghafla na kuziweka sawa kisha akazirudisha ndani ya bahasha aliyokuwa ameishikilia, Edo alimtazama Vicky, bila kusema neno aliondoka.



    * * *



    Usiku ule Edo hakupata usingizi sawasawa mawazo yake yote yalitawaliwa na Lulu, aliwaza hivi kweli Lulu anaweza kukubali kuchotwa na ghiliba za Onespot! Kwani alifahamu wazi kuwa Onespot bado anapigana vita vya kumpata Lulu, lakini jinsi gani anapigana vita hiyo, ndio hakulitambua. Kilichomsikitisha Edo ni kuwa Lulu amekwishanaswa na mtego wa Onespot. Picha zile aliwaza Edo ni za Lulu akiwa na Onespot mpaka nyumbani kwa akina Lulu, hivyo ni dhahiri kuwa upo uhusiano mkubwa, ukiongezea na kukumbatiana. Usiku ulionekana ni mrefu mno kwa Edo, aliomba kuche haraka. Wakati huo huo, Lulu nae hali ilikuwa hiyo hiyo kama ya Edo,

    baada ya kuziona picha zile za Edo na Vicky, alipofika nyumbani, alishindwa hata kula chakula. Aliamini kuwa ni kweli Edo ni mvulana wa Vicky na kwamba yeye Lulu anadanganywa tu. Alifahamu kuwa hakuna neno lolote lile ambalo anaweza kuambiwa na Edo akaamini tena, picha zimekwisha maliza kila kitu.



    * * *



    Wakati Edo na Lulu, kila mmoja yupo kwake juu ya kitanda anawaza hili na lile na kuomba usiku umalizike, hali haikuwa hivyo kwa upande wa Onespot na Vicky, wao waliomba usiku usimalizike. Vicky na Onespot walikutana siku hiyo, usiku mwingi baada ya Onespot kumpeleka Lulu kwao. Waliagana hivyo, kuwa wakutane ili wabadilishane habari. Mara baada ya Vicky kuachana na Edo, alirudi nyumbani kwao, akala chakula, kisha akajitayarisha kwa kutoka. Baada ya muda kupita, Onespot alifika kwa akina Vicky na kumchukua kuondoka nae. Walitafuta sehemu nzuri wakaketi na kuongea. Onespot ndie aliyeanza kwa kuuliza,

    ’’Vipi Vicky! Hebu nipe habari za picha zile, Edo alipoziona alisema nini?”

    “Hakusema kitu bali alitaka azichukue na kuzirudisha kesho, nami sikumkubalia.”

    “Very good, angezichukua, kwa ninavyomjua Edo angezichunguza na si ajabu angepata ufafanuzi wa jinsi zilivyochukuliwa na mpiga picha.” Onespot alimpongeza Vicky kwa furaha nae Vicky alitaka kujua na Lulu nae alipoziona picha zake akiwa na Edo alisema nini.

    “Aseme nini! Hakuwa na la kusema bali chozi lilimtoka. Sasa ujanja wao wote kwisha. Tumekwisha gonga gogo tusikilize mlio sasa.” Vicky na Onespot waliongea huku wanapata chakula cha jioni, walipanga mipango yao inayofuata na jinsi ya kuitekeleza, Vicky akiwa moyo wake umefurahi mno. Hakuhisi wala kufahamu kuwa analolitenda kwa Edo na Lulu ni baya. Lengo lake ni kumridhisha Onespot ambae anampenda sana, basi, jingine lolote kwake yeye si muhimu.



    * * *



    Siku iliyofuata Edo alifika mapema zaidi ofisini kwao, kuliko ilivyokuwa kawaida yake. Kabla ya kwenda kwenye chumba cha mazoezi ya onesho, alikaa kimya hapo juu ya kiti akiwa amekunja mikono yake juu ya meza iliyokuwepo mbele yake. Ofisi hiyo wakati huo ilikuwa tupu kwa maana ya kuwa hapakuwa na mtu mwingine zaidi ya yeye Edo. Wakati akiwa katika hali hiyo ya utulivu na ukimya aliisikia sauti ya soli ngumu za viatu vya kike vikitembea sakafuni ikizidi kusikika kuelekea chumba cha ofisi alichokuwemo, alibaki kama alivyokuwa akisubiri mwenye hatua hizo aidha apite nje ya chumba hicho au aingie chumbani humo mlango ulikuwa wazi, mara uso wa Lulu ukiwa hauna furaha kabisa ulijitokeza na kubisha hodi. Edo aliitika, na baada ya kusalimiana alimkaribisha Lulu aketi juu ya kiti kingine kilichokuwepo karibu na meza hiyo. Baada ya kukaa, Lulu alimwambia Edo kuwa anashukuru kumkuta yeye Edo yupo peke yake, kwani alipenda iwe hivi. Edo naye akamwambia Lulu naye pia anashukuru, kwani alikuwa anamuwaza yeye na jinsi ya kumpata akiwa peke yake hapo kazini. Baada ya salam fupi na shukrani hizo walizopeana, Edo alitangulia kumuuliza Lulu,

    “Vipi mkutano wenu wewe na Onespot ulikwendaje?”

    “Mbona unatanguliza kuniuliza habari za Onespot haraka haraka Edo?!”

    “Kwa sababu mara ya mwisho tulipokutana jana uliniambia unakwenda kumuona au kukutana na Onespot.” Lulu aliguna na kutoa tabasamu la chini chini lisiloeleweka, aligeuza uso wake kando, kisha kwa ghafla akamuangalia Edo na kumjibu, “Afadhali ya mimi nilipokwenda kukutana na Onespot angalau nilikutaarifu

    na kukuambia kweli kuliko wewe ulipokwenda kukutana na Vicky ukaniambia uongo kuwa unakwenda mazikoni, kudanganyana ni kwanini?!!” Edo kidogo aliduwaa kwa kusikia habari hizo na kumjibu Lulu,

    “ Mimi sijawahi kukutana na Vicky nje ya ofisi hii kama nilivyosema, na ni kweli kabisa juzi tulifiwa na jirani yetu na nilikwenda Kongowe kuzika, sasa lipi nililodanganya?!” Lulu kwa sauti ya ukali kidogo alimgeukia Edo na kusema,

    “Sikiliza Edo, nimesikia mengi, na nimeona vya kutosha kabisa kuthibitisha kuwa wewe girlfriend wako ni Vicky, kwa hiyo usinibabaishe.” Edo alitaka kupandisha jazba lakini akajikaza na akasema kwa sauti ya chini,

    “Lulu unaonekana umekwisha nasa ndani ya mtego wa Onespot na kwa hiyo unatengeneza visababu vya kunisingizia mimi. Mimi na Vicky hatuna uhusiano wa kimapenzi kabisa, isipokuwa nikuulize wewe, ni kitu gani kilichopo kati yako wewe na Onespot?!” Lulu nae hasira zilimpanda, hasira za kike. Mwanamke ni rahisi kumuonea wivu mwanamke mwenziwe kuliko ilivyo kwa mwanamme. Ni wanaume wachache wanaopandisha wivu kwa wanaume wenzao haraka. Lulu alisema kwa hasira kumwambia Edo.

    “Mimi na Onespot hakuna jambo lolote la kimapenzi, isipokuwa wewe na Vicky lipo, nasema tena lipo. Sasa wewe unanitafutia visababu ili uweze kuendeleza uhusiano wako na Vicky. Unafikiri ningekuwa na uhusiano kama huo unaodhani, ningekuambia kuwa ninakwenda kukutana na Onespot?!” Edo alifikiri na kuona kuwa Lulu amekwisha shawishika alikumbuka zile picha, alijisikia anamuambia Lulu,

    “ Inawezekana uliniambia hivyo Lulu ili nikate tamaa juu yako. Lakini ninalokuambia mimi bado ninakupenda sana. Na kukuthibitishia hili, nijibu swali langu, iwapo umekubali kuolewa na mimi, na ukisema ndio, basi na tuondoke sasa hivi tukatafute padre atuoze.” Lulu aliangua kicheko cha dharau na cha kusikitika.

    “Ni kweli ninayoambiwa sikujua kama Edo kumbe wewe ni ndumilakuwili. Hivi ni kweli unanitaka tuoane?! Siwezi kuolewa na mwanamme nilie na wasiwasi nae. Ni kweli nami pia ninakupenda, lakini pendo langu linazibwa na shaka niliyonayo juu yako!” Edo alichanganyikiwa, hakujua ni kitu gani kilichomsibu Lulu, lakini kwa vyovyote vile alikuwa na uhakika wa mkono wa Onespot lazima uwepo, kama alivyoona katika picha. Alimwambia Lulu kwa sauti ya masikitiko,

    “Lulu hivi kwa nini unitilie shaka?! Unajua sikuelewi kabisa! Sielewi sababu za shaka yako juu yangu, sina ovu lolote nililolifanya ndani ya uhusiano wetu.” Lulu alimuangalia Edo kwa jicho kali huku akimuwazia Edo vinginevyo, aliwaza ni kweli Edo ni langhai, sumu ya Onespot ilikwisha anza kufanya kazi, alisema kwa sauti ndogo,

    “Unakifahamu vizuri ulichokifanya na ndio maana ninakutilia shaka.” Edo alikuwa hajui amwambie nini Lulu, wakati anafahamu ni yeye aliyekosewa kwa sababu ya Lulu kumkubali Onespot kwa kiasi alichokiona kwenye picha. Aliamua asiwe na haja ya kuendeleza kubishana. Jambo moja ambalo halikuwekwa wazi kati yao ni lile la kuwa kila mmoja wao aliona picha za mwenzie, hilo waliliachia katika mazungumzo yao lakini hawakulitaja. Mwisho Edo alisema,CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Ninaona hapa tutabishana mpaka kesho, kila mmoja kati yetu anajiona yeye si muhalifu kama anavyoonekana na mwenzie. La kuthibitisha pendo langu kwako nimekuambia tufunge ndoa leo hii; Hilo pia umekataa kwa shaka uliyonayo hii itakuwa ni kazi ya Onespot. Ipo siku utakuja jua ukweli uko wapi.” Lulu alidakia na kusema,

    “ Mpaka hivi sasa nimekwishajua ukweli uko wapi kwa kujifariji, nitamkubalia Onespot kwa analolitaka la kuwa mimi girlfriend wake, huenda ikanisaidia kukusahau wewe.”

    “Fanya hivyo tafadhali, huenda ikakusaidia kuujuwa ukweli. Nami

    nitakusaidia kwa njia niijuayo.”





    Siku ya tatu baadaa ya Lulu kukabiliana na Edo na kuambiana kila mmoja alilolitaka kumuambia mwenzie, ilikuwa siku ya onesho la mavazi. Lulu alifanya kila aina ya vishindo vya kumuonesha Edo kuwa yuko karibu zaidi na Onespot. Edo yeye alifanya kazi zake kama kawaida, bila kujali kitu chochote, pamoja na kuwa kero la Vicky la kumfuata huku na kule kila alipokwenda au aliposimama, ilizidi hasa kila Vicky alipoona kuwa Lulu anawaangalia. Onespot alizidi kujishaua kwa kumfuata fuata Lulu, mara kwa kumuuliza hiki, mara kwa kumrekebisha kile katika kila vazi alilovaa. Onesho lilifana sana kwa kuhudhuriwa na watu wengi ambao hawafahamu kabisa ni kitu gani kinaendelea kati ya Lulu, Onespot, Vicky, na Edo. Baada ya onesho hilo kumalizika, watu walitawanyika kila mmoja akashika njia kurudi kwake. Onespot alihakikisha kuwa anamsindikiza Lulu kwa kumchukua ndani ya gari yake wakati Edo yupo anaangalia. Siku ile Edo alipokuwa nyumbani kwake alitafakari na kuona kuwa ameshindwa na Onespot. Japokuwa pendo lake lilikuwa limezidi juu ya Lulu, lakini hakuwa na njia zaidi ya kufanya kushinda ile aliyomuambia Lulu akubali mara moja waoane. Pia aliwaza hivi ni kweli Onespot anampenda Lulu?! Kwani alifahamu wazi kwamba anachofanya Onespot ni kushindana na yeye Edo, ingawa Lulu hakutaka kulielewa hilo. Vile vile alikuwa na mashaka na wasiwasi mkubwa juu ya zile picha alizoziona, hakuziamini sawasawa. Maadamu Lulu hakutaka kumuelewa anazidi kudumisha uhusiano wake na Onespot, Edo aliamua siku atakayokwenda kazini aende akamkabili bosi wake huyo Onespot, amueleze ukweli na kisha aache kazi. Alifikia uamuzi afanye hivyo na arudi nyumbani kwao Arusha akamuombe msamaha baba yake kisha aoe mke aliyechaguliwa na wazazi wake kabla hajaingia mapenzini na msichana mwingine. Hakuona maana ya kutafuta msichana mwingine wakati moyo wake ukiwa kwa Lulu.

    Alipoteza imani juu ya ndoa za mapenzi, aliona ni heri ndoa za kupangiwa.



    * * *



    Siku iliyofuata ilikuwa Jumapili, siku ya mapumziko kwa wote baada ya kazi ngumu. Onespot aliitumia siku hiyo kwa kukamilisha lengo lake. Alienda nyumbani kwa kina Lulu saa za mchana. Alipokelewa kwa furaha sana na Flora pamoja na mumewe Abraham. Kwa ucheshi na uchangamfu, Onespot alipoombwa ajiunge na familia hiyo hapo nyumbani kwa chakula cha mchana, haraka alikubali; Lulu, pamoja na kuwa alimuambia Edo atamkubali Onespot ombi lake la kutaka awe msichana wake, moyo wake ulikuwa mzito sana kwa analotaka huyo Onespot. Alionesha vituko vya kumsogelea na kuwa nae karibu Onespot pale ambapo alijua Edo yupo karibu na anaona, vinginevyo hakuwa na hamu kubwa ya kuwa msichana wa Onespot. Kwa hiyo bwana huyo alipokuja nyumbani kwao, nafsini mwake hakufurahiwa, alijikaza tu. Wakati wote wanne, Flora, Abraham, Lulu na Onespot wapo mezani wanakula, Onespot alianza kusema,

    “Pole sana Lulu kwa uchovu wa shughuli za jana.”

    “Ahsante sana Onespot, nimekwishapoa.” Waliendelea kula huku wanazungumza hili na lile katika mazungumzo yao. Mara Onespot alitamka na kuomba,

    “Samahani Lulu, nimekuja kwa makusudi ya kukuomba na kuwafahamisha Flora na Abraham kuwa ninataka kukutoa nje leo kwa ajili ya chakula cha jioni. Huu ni mualiko maalum wa mimi na wewe kwa ajili ya kujipongeza kwa mafanikio ya onesho.” Flora na Abraham walitoa tabasamu la kukubaliana na Onespot. Lulu yeye aliinama na kuwaza kidogo, kisha akaona iwapo atakataa mualiko huo, hataeleweka na yeyote kati ya hao watatu aliokuwa nao,alikubali

    “ Sawa Onespot, njoo jioni unichukue.” Onespot alitabasamu kichini chini

    huku akiwaza sasa robo tatu ya kazi yake imekamilika.



    * * *



    Siku ya Jumatatu, saa moja asubuhi, Edo alikwishajitayarisha kwa kila kitu, yaani ki-safari ya kurudi kwao Arusha. Hata nyumba anayoishi alikwisha kabidhi funguo kwa mwenye nyumba, na alikwisha kata tiketi ya basi la saa tano, akiamini kwa saa chache za katikati hapo zitamtosha kumalizia aliyoyakusudia kuyafanya, lakini jambo la safari siku hiyo, lilikuwa ni la uhakika na hakuna kipingamizi kinachoweza kumzuia isipokuwa rehema za Mungu… na Lulu ambaye alikwisha kata tamaa kumpata. Saa mbili na nusu Edo alikuwa uso kwa uso na Onespot ndani ya ofisi ya bosi huyo. Onespot akiwa amekaa juu ya kiti kikubwa cha kuyumba nyuma ya meza kubwa ya ofisi, na Edo nae akiwa ameketi juu ya kiti cha ofisi cha kawaida kilichokuwepo mbele ya meza hiyo. Akiwa na kalamu kiganjani akiichezea chezea, kwa kuipeleka kiganja cha kushoto na kuirudisha kiganja cha kulia, Onespot alimuuliza Edo kwa tabasamu la dharau. “Ndio…Edo unasemaje?!” Edo nae alimuangalia Onespot kwa nukta chache kabla hajamjibu huku nae akitabasamu.

    “Hongera sana Onespot.”

    “Kwa lipi Edo?”

    “Unafahamu vizuri ni kwa lipi…nililokupia hongera”

    “Ni mengi niliyoshinda na kufanikiwa, ingekuwa bora ukafafanua.”

    “Ni kuhusuu… Lulu.” Onespot alirudi nyuma kidogo, akaegemea kiti alichokalia na kuangua kicheko kikubwa, kisha akanyamaza ghafla. “ Kumbe umekwisha fahamu hilo eeh, ahsante kwa kunipongeza, thank you very much Edo. Ni jana tu, nilikuwa pamoja na Lulu jioni, mambo yetu sio mabaya.” Alitulia kidogo Onespot baada ya kusema haya, kisha akaendelea kusema kwa kumkodolea macho Edo.

    “…Lakini si nilikuambia?! Wakati wote mimi ni mshindi, na hakuna vita ninayoitaka nishinde, halafu nikashindwa…never…it will never happen. Umeamini sasa kama mimi ni mpiganaji Edo?!” Edo alitoa tabasamu kubwa na kumtazama usoni Onespot ambaye alionekana kuwa na shauku ya kutaka kusikia Edo atasema nini. Edo alimuambia Onespot,

    “Bado ninaamini kuwa vipo vita ambavyo huwezi kuvishinda. Sikiliza, nakupa hongera kwa kufanikiwa kuuvunja uhusiano wangu mimi na Lulu, nakupa hongera kwa kufanikiwa kutoka nje pamoja na Lulu. Lakini hebu tuwe wakweli, bado haujafanikiwa kulivunja pendo langu juu ya Lulu, bado hujafanikiwa kulivunja pendo la Lulu juu yangu. Lulu ananipenda, na mimi nampenda. Lulu hakupendi, anakwenda na wewe ili kujaribu kunikomoa mimi kwa ajili ya sumu na mbinu ulizoweza kuzitumia, na hizo ndizo ninazokupia hongera, japokuwa sizijui ni zipi lakini umeshinda. Vita vingine huviwezi Onespot, pendo letu mimi na Lulu bado hujaweza kulivunja.” Onespot hakuonesha kuyajali hayo yote aliyoambiwa na Edo. Alitikisa kichwa chake na kutamka,

    “Wewe Edo u hodari wa maneno. Mimi Onespot ni Hodari wa maneno na vitendo. Ikiwa unakubali kuwa nimevunja uhusiano wenu, sasa ni pendo gani unalolizungumzia?! Maadam uhusiano haupo, na pendo vilevile litapotea. Kuvunjika kwa uhusiano, ndio mwanzo wa kuvunjika kwa pendo lenu. Niambie jingine muheshimiwa, kwa hilo nimekushinda…Lulu nimempata mimi.” Edo nae alizidi kutabasamu kwa kumuona jinsi Onespot anavyojinaki.

    “ Kama upo ukweli kwa uyasemayo Onespot, basi labda, nasema labda kwa upande wangu, kuvunja pendo lake juu yangu kwa kuwa hatupo pamoja. Lakini kwa upande wangu mimi, nitampenda Lulu daima hata kama sinae. Hivyo basi

    iwapo utafanikiwa kumpata, nakuomba umtunze, umpende na umfanyie kama yale ambayo unapenda kujifanyia mwenyewe.” Onespot alitoa mguno wa dharau na kujigeuza hapo kitini alipokaa.

    “Nitakalolifanya kwa Lulu ninajua mwenyewe, sipendi kufundishwa. Kwa kuwa nimekwisha mpata we bwana niachie tu.”CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Bado hujampata…kumbuka ulivyoniambia! Wasiwasi wangu ni kuwa ulilolidhamiria juu yake sio zuri, ndio maana leo hii ninaacha kazi na kurudi kwetu Arusha, ili nisilishuhudie utakalofanya juu yake, na pia kumpa nafasi atambue lengo lako na kama anaweza kukupenda. Kwa heri Onespot, iko siku tutakutana ili nije kukupa hongera ya ukamilifu, kama kweli umezaliwa mshindi…goodbye.” Edo alinyanyuka akaweka barua ya kuacha kazi juu ya meza ya Onespot na kuanza kuondoka.

    “Hebu subiri kidogo Edo!” Onespot alimsimamisha Edo. Edo alisimama na kugeuza shingo yake kumuangalia Onespot ambae aliendelea kusema,

    “Yapo masuala ya kazi Edo, bado hatujayazungumza mfano mafao yako! Mshahara wako! Mbona hukuvitaja?!”

    “Nilikwisha kukuambia kuwa sifanyi kazi kwa ajili ya shida ya fedha. Kwa hizo pesa zangu chukua wewe zitakusaidia kutilia petrol garini mwako wakati ukimtembeza Lulu katika jiji hili la Dar es salaam. Kwa heri!” Edo alitoka akaenda zake akamuacha Onespot ametulia mezani kwake.



    * * *



    ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog