Simulizi : Muafaka
Sehemu Ya Nne (4)
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Lulu alipofika ofisini siku hiyo, habari zilikwishaenea kuwa Edo ameacha kazi. Habari hizo zilimfanya awaze kwa nini Edo asimsubiri angalau amuage? Tendo la kuacha kazi ghafla limesababishwa na nini? Hakupata jawabu, isipokuwa aliamini kuwa kweli Edo ni laghai. Wiki nzima hiyo ilipita Lulu akiwa hana furaha. Onespot alichukua nafasi hiyo kwa kumpeleka sehemu mbalimbali za starehe kila jioni. Ilipofika Jumamosi, kuliandaliwa karamu ya kujipongeza kwa wafanyakazi wote kwa ajili ya mafanikio ya onesho la mavazi, ni jioni hiyo Lulu ambayo asingeweza kuisahau maishani mwake. Flora na Abraham nao walialikwa kwenye tafrija hiyo. Walipofika ukumbi uliokuwa ikifanyika shughuli hiyo wakiwa pamoja na Lulu, watu walikuwa wamejaa tele wake kwa waume wanameremeta. Alieonekana kumeremeta zaidi alikuwa Vicky, alivaa gauni la gharama iliyompendeza mno. Lulu aliweza kuligundua hilo na kujiuliza moyoni mwake kulikoni?! Na Edo hayupo?! Onespot nae katika wanaume alionekana kama vile mwana wa mfalme. Lulu na dada yake na shemeji yake, walitafuta sehemu wakakaa. Vinywaji na ghasia zote vilikuwepo. Mziki nyororo ukitumbuiza wa moja ya bendi maarufu jijini. Onespot alimuona Lulu, dada yake na shemeji yake. Aliwaendea akawasalimu kisha akawaambia,
“Burudikeni, leo imetokea kuwa ni siku yangu ya kuzaliwa na siku muhimu mno kwangu, mniwie radhi sitaweza kukaa pamoja na nyinyi, lakini…enjoy yourselves…chochote mnachohitaji, wahudumu wapo.” Aliondoka na kujumuika na watu wengine. Baada ya kama saa mbili kupita, MC alinyamazisha muziki na kusema,
“Mabibi na mabwana, tafrija hii leo ni ya aina yake, ninasema ni ya aina yake, sababu inakusudia kusherehekea mambo muhimu matatu, la kwanza ni kujipongeza wafanyakazi wote wa ADFC LTD kwa kufanikisha onesho lao la mavazi lililofanyika wiki iliyopita. Pili ni kusherehekea siku ya kuzaliwa kwa Mkurugenzi Mtendaji bwana Onespot Pato akiwa leo hii anatimiza miaka ishirini na nane. Na la tatu sitalisema mpaka hapo litakapofikia wakati wake, mtaliona wenyewe.” Baada ya MC kusema hivi, keki kubwa ililetwa ikiwa juu ya meza yenye keki hiyo, Onespot aliinamisha uso wake kuzima mishumaa midogo midogo iliyokuwa imepamba keki hiyo kisha
akakabidhiwa kisu cha chakula akaanza kuikata hiyo keki, huku wote waliohudhuria wanaimbishwa na MC wimbo wa “Happy Birthiday to you, happy birthday to you, happy birthday to Onespot.” Jambo la kwanza aliloliona Lulu na kumpa kuwaza, ni mara baada ya Onespot kukata keki hiyo, alichukua kipande kidogo na kumlisha Vicky. Muziki uliendelea, na baada ya kama dakika arobaini na tano hivi MC alinyamazisha muziki na kusema,
“Mabibi na mabwana, na sasa tunaingia katika lile dhumuni letu la tatu na muhimu zaidi, hili sijui niliitaje, labda nitakuwa sikosei nikisema ni dhumuni la wapendanao. Hebu wale wapendanao waje wasimame mbele ya watu waonekane, kisha tuendelee na shughuli.” Kila mtu aligeuza uso wake huku na huku kwa shauku ya kuwaona hao wapendanao, akiwemo Lulu, ambae hakuweza kuamini macho yake wala akili yake alipowaona Onespot na Vicky wakijitokeza kwa madaha na mbwembwe mbele ya umati wa watu. Ilibidi Lulu ajikaze apate kugundua na kuhakikisha zaidi.
MC, baada ya hapo aliwaita watoto wadogo wawili waliovaa nguo nadhifu na za kupendeza. Mmoja alikuwa mvulana wa miaka kama kumi hivi na wa pili msichana mwenye umri wa miaka kama saba. Wote wawili kila mmoja wao alinyanyua sinia ndogo ambayo juu yake palikuwepo kijaluba kidogo chenye pete ya mfuto ya dhahabu. MC aliendelea kusema,
“Wazazi wa bwana Onespot Pato, ninamuomba Onespot achukue pete iliyoshikwa na msichana mdogo amvike Vicky kidoleni mwake.” Onespot alichukua pete, akanyanyua kiganja cha Vicky cha kushoto na kukivika kidole kimoja cha kiganja hicho pete ile ya dhahabu. Vicky nae alichukua pete toka kwa yule mvulana mdogo, akanyanyua kiganja cha Onespot, na kufanya vile vile. MC akaendelea kusema,
“ Sasa ninawatangaza rasmi Onespot na Vicky kama mtu na mchumba wake, official kabisa. Kwao wao pamoja na yote, hii ilikuwa tafrija ya kufunga uchumba…. Engangement party, na kwa kuwatakia heri nasi sote tuione shughuli hii , kuwa ni hivyo. Naomba kila mmoja achukue kinywaji chake chochote kile ambacho anakunywa na kunyanyua juu kinywaji hicho kwa ajili ya maisha marefu na ya furaha kwa Onespot na Vicky mpaka wafikie harusi yao.” Watu wote waliokuwepo hapo, kila mmoja wao, aliyenyanyua bilauri alinyanyua, aliyenyanyua chupa alinyanyua, za bia, za soda, za juisi, ili mradi kila mmoja alifanya hivyo, isipokuwa Lulu. Wote kwa pamoja walisema,CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“CHEERS!”
Lulu alijihisi mwili wote umemfa ganzi. Sio kwa ajili ya Onespot la, bali ni kwa ajili ya Vicky. Hivi sio kweli kuwa Vicky alikuwa msichana wa Edo?! Mwili ulimtetemeka. Flora alimuona mdogo wake kuwa amebadilika. Akamuuliza,
“Vipi! Una nini Lulu?!”
“Ninajisikia homa kali ghafla dada, naomba tuondoke turudi nyumbani!”
Siku iliyofuata ilikuwa siku ya Jumapili. Lulu aliamka akiwa katika hali ya unyonge sana. Kichwa chake alikihisi kizito, kilichochanganyikiwa, moyo wake nao aliuhisi mwepesi unaoelea juu ya maji. Alifikiri, iwapo hajapata mtu angalau wa kumueleza aliyokuwa nayo, ili ayacheuwe kidogo, basi anaweza kuugua. Hakuwa na mtu wa kumuamini na aliyekuwa nae karibu zaidi ya dada yake Flora. Baada ya kupata mlo wa asubuhi, alimuomba Flora, waongee. Hapo ndipo alipomueleza dada yake kila kitu kuhusu yeye, Edo, Onespot na Vicky, kwa kirefu na undani kabisa, bila kuacha kumwambia hisia zake juu ya Edo, kuwa ndie anayempenda. Flora alimsikiliza mdogo wake kwa makini, mwisho akamuuliza,
“Lulu kweli unampenda Edo?!”
“Ni kweli kabisa.”
“Sasa ni kwa nini pale alipokuambia muoane siku ile ile mlipozozana, usikubali?!”
“Dada, ni kweli ninampenda, lakini nilikuwa na uhakika gani na pendo lake juu yangu? Zile picha…zile picha alizopiga akiwa pamoja na Vicky! Mpaka sasa ni kitendawili kwangu. Nilikuwa nina shaka nae, nilipomkatalia ombi lake, nilifanya hivyo kwa kuwa nilikuwa nina hakika nalo kwa wakati ule.”
“Sasa utafanya nini Lulu?!”
“Sijui la kufanya, bali nimekusudia kuonana na Onespot na ikiwezekana na Vicky vile vile, ili niweze kupata japo maelezo kidogo kutoka vinywani mwao. Kama ni kumpoteza, nimekwisha kumpoteza Edo, ambaye nitampenda daima hata kama nitaolewa na mume mwingine.”
“Kibarua chako je?! Vipi utaendelea na kazi ofisini kwa Onespot, Lulu?!” Flora alionesha hofu ya kuwepo kwa mdogo wake ofisini kwa Onespot, baada ya visa vyote hivyo kupita.
“Tazama dada Flora, Onespot hakuwa moyoni mwangu, hayupo na wala hatokuwepo. Sihofii kumkabili Vicky wala yeye. Wao si chochote kwangu. Mshtuko wa moyo wangu ulitokea pale nilipomuwaza Edo, baada ya kugundua kumbe Vicky mwenzake ni Onespot. Kwa hiyo sikimbii ofisi kwa ajili yao. Kesho nitakwenda kumueleza hisia zangu juu yake.”
Asubuhi ya Jumatatu, Lulu alikuwa mmoja wapo katika ya waliofika ofisini mapema mno. Baada ya kuingia ofisini kwake, alitoka kuelekea ofisi ya Onespot, alipofika mlangoni, aligonga kwa kiganja chake cha kulia huku akibisha hodi. Hakukuwa na jibu. Alishika shikio la kitasa cha mlango, akakizungusha taratibu huku akiusukuma mlango. Alipenyeza kichwa chake na kuangalia mezani kwa Onespot, hakuona mtu yeyote. Alirudisha kichwa chake nje na kuusindika mlango huo. Alirudi ofisini kwa Katibu Muhtasi ambae ni Vicky, wa bosi mwenyewe Onespot. Wakati amekaa tuli kwenye kiti hicho, jicho lake ghafla lililenga bahasha kubwa ya rangi ya khaki, iliyokuwepo juu ya meza ya katibu kando kidogo ya computer. Alitulia kidogo na kuikazia macho yake yote mawili bahasha hiyo. Aliwaza kichwani kwake, ‘mbona inaonekana kama vile bahasha hii niliiona mahala kabla ya hapa?!’ Alizidi kuitolea macho, ‘ah, hasa ndio hii … ile bahasha iliyokuwa na picha alizonionesha Onespot.’ Baada ya kukumbuka hivyo, alinyoosha mkono wake wa kulia taratibu na kuichukua bahasha ile. Aliisimamisha juu ya mapaja yake, akatia mkono ndani yake. Humo alitoa bahasha nyingine nyeupe. Taratibu aliifungua bahasha hiyo nayo, ambayo haikuwa imefungwa kwa kugandishwa na gundi. Pia akatia kiganja chake kwenye bahasha hiyo nyeupe, kwa kutumia vidole vikatoka na picha nane. Alizishikilia picha zile na kuziangalia. Nne kati ya hizo, alikwisha wahi kuziona, zilikuwa ni zile zile zikimuonesha Edo na Vicky. Nyingine nne zilizobaki, zilimuacha hoi, zilikuwa ni za yeye na Onespot. Moyo ulianza kumuenda mbio. Alitafakari baada ya kuziangalia vizuri picha zile, zilikuwa katika mkao ambao anaukumbuka vyema sana. Alivuta mawazo ili akumbuke ni mpiga picha gani aliyekuwepo ndani ya chumba cha mazoezi, siku ile Onespot alipomvamia kwa nyuma na kumkumbatia?! Aliweza kumkumbuka mpiga picha aliyekuwa amekaa pamoja na Onespot, kabla ya tukio lile. Alikuwa Halfani Matai, mmoja wa wapiga picha hodari na mashuhuri wa kampuni yao. Pale pale alizirudisha picha zile ndani ya bahasha ile zilizokuwemo, akaichukua bahasha hiyo na kuondoka nayo kutoka ofisini hapo kwa katibu. Lulu akiwa amejaa hasira alikwenda kumsaka Halfani Matai. Moja kwa moja alikwenda kwenye chumba cha wapiga picha za mnato na video, ambacho hicho kilikuwa ni ofisi ya Edo pia. Bahati nzuri alimkuta Halfani amekwishafika, anazungumza na wenzake wengine. Lulu aliwasalimu, kisha akamuomba Halfani waonane faragha. Walitafuta chumba cha ofisi ambacho hakikuwa na mtu wakaketi. Lulu alikuwa amekunja uso, alizitoa picha zote zile nane, akazitapanya juu ya meza iliyokuwa karibu yao, kisha akamuuliza Halfani kwa sauti ya chini iliyojaa huzuni.
“Samahani bwana Halfani, unaweza kuzitambua picha hizi?!” Halfani alikwisha hisi kuwa Lulu amekasirika sana. Alizidondoa moja moja picha zile na kuziangalia. Kisha akajikohoza kidogo na kusema kwa utaratibu,
“Samahani Lulu, picha hizi ni kweli nazitambua na ndie mimi niliyezipiga” Lulu alimtazama Halfani na jicho la kuua, akauliza tena,
“Zote nane?!”
“Ndio Lulu , zote hizi nimezipiga mimi.”
“Kwa nini? Kwa vipi? Kwa sababu zipi? Na imekuwaje ukapiga picha pasipo idhini ya wahusika?! Kwa nini? Niambie Halfani ni kwa nini?” Chozi lilikuwa linamlengalenga Lulu wakati anauliza maswali haya. Halfani alihuzunika sana, halafu akaanza kumueleza Lulu,
“Nakuomba uniwie radhi Lulu na unisikilize ninayokuambia. Ni wiki iliyopita tu, baada ya Edo kuacha kazi, ndipo nilipogundua kuwa nimefanya kosa kubwa katika maisha yangu. Sababu Edo, kabla hajaondoka alimdokeza mmoja wa wapiga picha wenzetu kwa kumuambia kuwa anaamini yupo mmoja wetu aliyesababisha kufarakana kwake yeye na wewe, na pia kusababisha kuacha kazi kwake.” Halfani alitulia kidogo, wakati Lulu anaangalia chini, aliendelea kusema bila kumuangalia usoni Lulu,
“…Edo alisema kwamba ameona picha ambazo ni zako wewe ukiwa pamoja na Onespot, ameoneshwa na Vicky. Picha hizo alisema anayo hakika kabisa ni kazi ya mmoja wetu ingawa hakumjua ni nani.” Lulu wakati huu machozi yalikuwa yanamdondoka aliuliza swali tupu bila kujijua.
“Na kumbe ulikuwa wewe?!” Halfani alikubali kwa kutingisha kichwa, na kuendelea kusema,
“Ndiyo …nilikuwa mimi kama nilivyokubali mwanzo kwa sababu zilizonifanya nifanye hivyo, ni kwamba nimehadaiwa na Onespot. Mimi nilijua uhusiano wako wewe na Edo, na ninaapa kwa dini zote, nisingependa uhusiano wenu uvunjike hata siku moja, lakini masikini wee nimeingia ndani ya mtego wa Onespot bila ya kujua. Yeye bosi Onespot, ninavyojua mimi, msichana wake ni Vicky, pamoja na wasichana wengi alionao, nilijua kuwa Vicky anampenda sana Onespot, na kwa vile wazazi wao ni marafiki wa miaka mingi, nilifahamu kuwa uhusiano wao unayo nafasi kubwa ya kuelekea kwenye ndoa.” Lulu alijipangusa machozi na kukaa vizuri kumuangalia Halfani usoni kwa mtazamo wa “haya endelea”! Nae Halfani aliendelea kusema,
“Vile vile jambo ambalo nililielewa vibaya, nilidhani wewe na Edo, na Vicky na Onespot, ni marafiki wakubwa. Sababu ya kusema hivi, nilikwisha wahi kuja na Onespot nyumbani kwenu siku moja. Mimi nilibaki ndani ya gari yeye aliingia ndani ya nyumba yenu. Alikaa sana humo, alipotoka alinieleza kuwa yeye na nyinyi, yaani wewe, Edo, dada yako na shemeni yako ni marafiki wakubwa. Hapo hapo aliniambia kuwa anataka kuwapa utani halisi yaani practical joke. Ndipo aliponiambia tufanye nini. Picha hizi zako pamoja na yeye. Nilizichukua siku ile pale chumba cha mazoezi . Aliniambia nizipige kitaalamu bila flashi! Siku ile ile baada ya wewe kumkubalia akusindikize, alirudi ofisini akaniambia niwafuate na gari nyingine. Kisha mtakapofika kwenu, kwa mbali nipige picha mbili za mkao mbalimbali. Alipoteremka kwenye gari na kukushika mabega, mimi nilizoom (kuwalenga kwa karibu) na kupiga picha pamoja na hii ya kupungiana.” Lulu alionekana kupungua hasira kidogo. Alimuuliza Halfani.
“…Na hizi za Edo na Vicky?!”CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Hizi zilikuwa rahisi kabisa, sababu Vicky alikuwa anajua kuwa atapigwa picha ambazo anatakiwa aonekane yeye na Edo katika mkao wa kimapenzi. Hii ya zipu, alimuomba Edo amsaidie kufunga zipu. Hii Edo aliyomshika usoni, alikuwa anamuongoza kijana wa kiume katika mkao anaotakiwa aonekane kwenye onesho, pamoja na hii ya Vicky aliyokaa juu ya mapaja ya Edo. Tena ni yeye Vicky ndie aliyekwenda haraka haraka kumkalia Edo na kumwambia kijana anayepaswa kuigiza nae, aangalie mkao unavyotakikana. Na hii ya mwisho ni Vicky tu alipita mbele ya Edo na akatulia kwa kiasi alijua kuwa mimi nitampiga picha. Picha za Edo na Vicky, tumezipiga mbele ya watu wengi tu, kwenye chumba cha zoezi. Na kama utaziangalia vizuri utaona kuwa Vicky katika picha zote yumo ndani ya mavazi ya onesho…ni wakati wa zoezi.” Lulu alirudisha pumzi kwa nguvu na kusema,
“Niziangalie vizuri au niziangalie vibaya, ifae nini?! Maji yamekwisha mwagika. Nakupa hongera bwana Halfani, wewe pamoja na Onespot na Vicky…hongerani!” Halfani alizidi kuonekana anajutia tendo alilolifanya, alimshauri Lulu kwa kumwambia,
“ Lulu, mimi ninajuta kwa nini nimekuwa mjinga wa kuingizwa katika mtego kama huu, wakati ninajua kuwa picha ni kigezo kikubwa cha mtu kuamini jambo. Lakini ni kwa vile niliambiwa ni ‘practical joke’ Naomba unisamehe Lulu. Vile vile nakuomba, mimi na wewe twende pamoja nyumbani kwa Edo, kisha umkubalie muoane.” Lulu alitoa tabasamu la kukata tamaa.
“Kwa sasa hivi sio suala la mimi kumkubalia yeye, ni suala la yeye kunikubalia mimi. Yeye alikwisha hisi uovu wa Onespot na akaniambia hivyo. Ni mimi ndie niliyekuwa mjinga…na...” Lulu hakuweza kumaliza alilokuwa akitaka kulisema, aliangua kilio na kuanza kulia. Halfani alijaribu kumnyamazisha kwa kumpa matumaini kuwa mambo yatakuwa mazuri kati yake na Edo. Alimuahidi kumsaidia mpaka ahakikishe kuwa Edo amekubali kurejeana na Lulu. Lulu alijipangusa machozi na kumwambia Halfani.
“Kabla ya yote haya, ambayo sina matumaini makubwa juu yake, acha nikaonane na Onespot kwanza, ipo haja ya kumpongeza.” Wakati Lulu anaingia ofisini, Onespot alikuwa nyuma ya meza yake anawaka kwa kupendeza na akazidisha kupendeza kwake kwa kutoa tabasamu kubwa la dhati na furaha iliyoonekana wazi juu ya uso wake. Alipomuona Lulu anaisogelea meza yake alitamka,
“Well come, well come beauty queen, karibu sana Malkia wa urembo Lulu Frank.”
“Thank you, thank you King of fools, ahsante sana mfalme wa majuha Onespot Pato, nimeshakaribia.” Lulu aliketi juu ya kiti mbele ya meza ya Onespot kwa kishindo. Onespot alihisi vita. Lakini kama kawaida yake hakujali, alitulia na kumuuliza Lulu,
“Vipi Lulu umekuja kunipongeza au kunitukana?!”
“Nikupongeze kwa lipi mpumbavu kama wewe, kwa hakika nimekuja kukutukana.”
“Kwa kuwa nimekuacha solemba eheh! Haha hahaaah! Mimi ndio Onespot Pato, siachwi bali naacha. Hakuna msichana anayethubutu kusema ‘Hapana” kwangu mimi. Yuko wapi Edo wako sasa?! Ninamuhurumia.” Kwa mshangao wa Onespot, Lulu aliangua kicheko kikubwa kushinda cha kwake yeye Onespot, alicheka kwa nukta kadhaa, kisha akatulia na kumtazama bosi wake huyo usoni.
Akatamka,
“Kama yuko wa kuhurumiwa, basi ni Vicky. Ah! Masikini Vicky, msichana mrembo kama yule kutaka kuolewa na janaume pumbavu kama wewe Onespot! Wewe!! Unamuhurumia Edo kwa lipi? Edo hahitaji huruma zako. Edo anacho kila kitu ambacho wewe unacho, kila kitu ambacho wewe huna jumlisha na pendo langu.” Lulu alitulia kidogo, kisha kwa kujiamini na kuringa aliendelea kusema, “Eti, nimekuacha ‘solemba”, Lulu alisema maneno haya kwa kumuigiza sauti ya Onespot, na mara akarudia sauti yake na kuendelea,
“Unajua maana ya kuacha mtu ‘solemba’ wee! Si ndio maana ninakwambia wewe juha. Licha ya wewe kuwa hujawahi kuwemo moyoni mwangu, pia sijawahi kufanya mapenzi na wewe, hujawahi hata kubusu kiganja changu wala sijawahi
chako. Sasa ‘solemba’ hiyo uliyoniacha ni ipi?! Hivyo kunipeleka hoteli na kuninunulia chakula?! Hivyo kunitembeza kuuona mji?! Jambo ambalo hata watoto wa mitaani wanalifanya kila siku kwa watalii! Hebu fikiria Onespot umjinga kiasi gani?! Kama yupo mwanamme aliyewahi kuniacha ‘solemba’ kwa maana hasa ya kuniacha ‘solemba’. Basi ni Edo, I love him, I love him so much, and I will always do. Wewe..wewe…kitu gani kwangu. Linalonisikitisha ni kukosa nafasi ya kumueleza Edo upumbavu wako, na kuwa amekushinda. Hukuweza kulipata pendo langu. Kila nililolifanya pamoja na wewe, namaanisha huko kutoka nje ni kwa sababu ya kumuudhi Edo kwa kuwa ninampenda, na sio kwa sababu ya kukufurahisha wewe, ambaye si chochote kwangu. Hata baada ya Edo kuacha kazi, nilitoka na wewe kwa kujaribu kumsahau Edo, jambo ambalo nimeshindwa.” Onespot kwa mara ya kwanza katika maisha yake alitulia tuli kumsikiliza Lulu na kutafakari na kuona upo ukweli katika anayoyasema msichana huyo. Lulu alinyanyuka taratibu na kusimama kutaka kutoka nje ya ofisi hiyo, lakini kabla hajatoka, alimuangalia Onespot kwa dharau na huruma na kumwambia.
“Kwa ushauri wa bure Onespot, mwanamme alie barabara na mjanja, siku zote hashindani na wanawake, huwa anashindana na wanaume wenzake. Kwa hiyo vita yako dhidi yangu umedhihirisha upumbavu wako. Na vita yako dhidi ya Edo, amekushinda, hata niolewe na mume mwingine, Edo atakuwa anayo sehemu ndani ya moyo wangu. Mwisho kabisa, Vicky anakupenda sana, nawe jaribu kumuenzi na kumpatiliza, una bahati kupata msichana kama Vicky…lakini kwa upande wako…sijui. …mfanye awe ana bahati nae, kwa heri.” Lulu alitoka ofisi ya Onespot na kuingia ofisi ya Katibu Muhtasi... Vicky, ambae alikuwepo mezani pake. Lulu kabla hajamsalimu, alimtulizia macho na kumuangalia, alimtulizia macho na kumuangalia kiasi cha dakika tatu bila mmoja kusema chochote kwa mwenzake. Mwisho Vicky alishindwa kumtazama Lulu usoni, aliinamisha uso wake kwa huzuni na kuangalia chini. Ndipo Lulu alipotamka kwa kusema,
“Pole sana vicky’’.
“Pole ya nini unipayo Lulu?!’’ Lulu alitabasamu kidogo na kumtulizia macho Vicky.
“Pole kwa yote uliyofanya. ‘’Yapi?!’’
“Hayo ya kuvunja uhusiano wangu mimi na Edo!’’ Vicky aliinamisha uso wake chini kidogo, na kufikiri la kumjibu Lulu. Nae Lulu aliendelea kusema,
“Licha ya hayo, nakupa pole Vicky kwa mwanamme kama Onespot kuwa mumeo mtara-jiwa!”
“Kwani ana nini?’’ Alijibu Vicky haraka haraka kwa sauti ya mshangao.
“Anazo kasoro nyingi ambazo itakubidi ufanye kazi ya ziada ili uzipunguze.’’
“Nitajie kasoro moja tu uijuayo wewe Lulu…kama siyo wivu wako?!” Vicky alimuuliza Lulu kwa sauti ya chini. Lulu aliangua kicheko kusikia hivyo, kisha akatulia kucheka na kusema kwa kuuliza na mshangao,
“Wivu?!... Wivu?!... Nimuonee nani wivu? Kwa lipi? Kwa kuwa u mchumba wa Onespot?! Usijidanganye Vicky, hata wewe unajua sina haja ya Onespot, hata siku moja. Onespot mwana-ume mwenye kasoro chungu nzima mojawapo ikiwa ni msaliti, au hujui hili?! We si ndiye uliyemsaidia katika kulisaliti pendo langu mimi na Edo?!’’ Vicky alishangaa kidogo kutokana na shutuma hizo na kuone-sha kutahayari, lakini alijikaza na kujibu.
“Kila nilichofanya, nilikifanya kwa ajili ya pendo langu kwa Onespot, kama kulikuwa na madhara katika hayo niliyotenda, basi mimi sikuyaona, love is blind mapenzi ni upofu.’’ Vicky alisema haya bila kumuangalia Lulu usoni kisha akaendelea,
“Na wewe Lulu ungekuwa unampenda Edo kweli kweli usingeona kasoro zake ungeendelea kuwa naye labda pendo lake juu yako ni la wasiwasi na ndio
maana ukamtilia shaka.’’ Lulu kidogo alihamaki kwa usemi huu wa Vicky, alitamani ampige kofi, lakini alijizuia na kumwambia Vicky,
“Pendo langu juu ya Edo, halina shaka, lakini si pendo pofu. Upofu wa pendo siku zote unakuja kwa watu dhaifu, na bahati nzuri mimi si mtu dhaifu kama wewe. Mimi siye mtu wa kuambiwa ukitaka nikupende fanya hivi au vile palipo na wasiwasi au shaka, hata kwa mtu nimpendae, nitatia shaka tu.’’ Vicky hakuoneakana kuwa mwenye hisia zozote juu ya sura yake nzuri, alimwambia mrembo mwenzie Lulu.
“Sikuwa na shaka na ahadi ya Onespot ya kuwa nae pamoja, na nashukuru ameitimiza, leo hii mimi ni mchumba wake, na siku za karibuni nitakuwa ni mke wa ndoa.’’ Lulu alidakia na kumjibu Vicky kwa sauti ya mkazo…..
“Lakini kwa gharama ya nani? Ndio, utakuwa mke wa ndoa wa Onespot, lakini huoni kuwa ndoa yako itakuwa inakosa amani kila utakapokumbuka kuwa umeolewa kwa sababu ya kuwatenganisha watu wawili wanaopendana?!…Ndio maana ninakuambia pole sana Vicky, ni dakika chache zilizopita tu, nilikuwa ninamuambia mchumba wako kwamba, ana bahati sana kupata msichana kama wewe kuwa mke wake, sababu nilitambua upofu wa pendo lako juu yake. Vile vile nilimuomba ajirekebishe, na akupende ipasavyo. Nitajitahidi katika sala zangu, nimuombe Mungu amfanye Onespot awe mume bora kwako, si kwa sababu yoyote ile, bali ni kwa ajili yako wewe Vicky… kama mwanamke mwenzangu,…nisingependa Onespot amuumize mwanamke mwingine yeyote yule zaidi ya alivyokwisha kuniumiza mimi, kwa heri …Vicky.’’ Lulu alivuta hatua kutaka kuondoka , alisikia jina lake likiitwa na Vicky, aliitika
“Beeh!”
“Samahani Lulu, nisamehe kwa yote yaliyotokea.”
“Wa kumuomba samahani ni Edo, sio mimi, kwani nimekwisha kusamehe!’’
“Kwa sasa hivi unafikiri ninaweza kukusaidia nini Lulu?!’’
“Ulikuwa wapi nilipokuwa ninahitaji msaada wako Vicky?! Umekwisha chelewa,……….maji yamekwisha mwagika.’’ Kwa wakati huu Lulu alijikaza chozi lisije likamdondoka, na Vicky nae alioneakana mwenye sura ya kujuta na huzuni, waliachana.
* * *
Lulu alimkuta Halfani Matai mpiga picha, anamsubiri. Nae Halfani kumuona Lulu tu, alimuuliza,
“Vipi Lulu uko tayari tuondoke kuelekea kwa Edo?’’
“Ndio, nipo tayari, twende zetu.’’
“Umeonana nae Onespot?!’’
“Wote, pamoja na Vicky pia nimeonana nae”.
“Wamesemaje?”.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Mengi ya kusema nilikuwa nayo mimi, wao waseme nini!’’ Lulu na Halfani walitoka nje ya ofisi yao na kuingia ndani ya gari ndogo iliyokuwa imeegeshwa hapo nje. Ilikuwa ni gari aina ya Toyota Carina ya Halfani, Halfani alikaa nyuma ya usukani na kuanza kuendesha. Baada ya kupita mitaa kadha ya Sinza, mwishowe walisimama mbele ya nyumba aliyokuwa akiishi Edo. Kwa shauku kubwa wote wawili waliteremka kutoka gari hiyo, waliuendea mlango mkubwa wa mbele wa nyumba aliyokuwa akiishi Edo, baada ya kuvuka geti na kuanza kugonga kubisha hodi, mara alitokea mama mmoja wa makamo. Alijitokeza nusu ya kiwiliwili chake sehemu ya juu. Walisalimiana nae vizuri, kisha Halfani alimuuliza mama huyo.
“Samahani shangazi, tumekuja kumuona Edo, sijui yumo au ametoka?’’ Mama yule aliwaangalia vizuri kabla hajawajibu, kisha nae akauliza,
“Kwani nyie wanangu mnatoka wapi? Na… samahani, ni nani zake Edo?!’’ Halfani alikuwa ndiye msemaji mkubwa siku hiyo, alijibu,
“Sisi shangazi tunatokea ofisi aliyokuwa anafanya kazi Edo, sisi ni wafanyakazi wenzake, mimi ni Halfani na huyu mwenzangu ni Lulu.’’
“Lulu?!” Yule mama alirudia jina la Lulu na kulitamka kwa mshangao.
“Ndio mama, huyu ni Lulu, kwani vipi, mbona umeshangaa?”
“Hapana mwanangu sikushangaa, lakini ukweli ni kuwa Edo amekwishahama hapa. Amesema ameacha kazi na anarudi kwao Arusha. Pia ameacha barua hapa, amesema iwapo msichana aitwae Lulu Frank kutoka ofisi aliyokuwa akifanya kazi iwapo atakuja kumuulizia, basi apewe barua hiyo,au apelekewe ofisini. Sasa je, wewe mama ndiye Lulu Frank?..Unafanya kazi pamoja na Edo?’’ Lulu alijibu haraka haraka, hakungoja kujibiwa na Halfani.
“Ndio, ndie mimi Lulu Frank mama!’’
“Basi ngoja nikakuletee hiyo barua, tulikuwa tunataka kuileta ofisini.’’ Mama yule aliingia ndani , akiwaacha Lulu na Halfani wamesimama hapo barazani nje. Baada ya muda mfupi tu yule mama alitoka tena, huku ameshikilia barua kiganjani mwake, alisema,
“Samahani wanangu sikuwakaribisha hata ndani, karibuni mpite ndani.’’ Kwa shauku aliyokuwa nayo Lulu ya kutaka kujua hiyo barua toka kwa Edo imeandikwa nini,aliomba radhi kwa mama huyo na kujidai ana haraka sana. Yule mama alimkabidhi hiyo barua yake.Halfani na Lulu walirudi ndani ya gari na kung’oa kuelekea ofisini kwao. Walipofika,kabla ya kuingia,Lulu aliamua aisome kwanza ile barua, ilikuwa na maneno haya.
Mpenzi wa moyo wangu,
Lulu Frank.
Ninaandika barua hii fupi, nikiwa sina matumaini ya kuonana tena na wewe. Nina matumaini kuwa utakapopata barua hii, utakuwa tayari umekwisha mfahamu Onespot ni mtu wa aina gani, nakutakia maisha mema kama mtaamua kuishi pamoja. Jambo lingine ninapenda kukuambia wakati unasoma barua hii, nadhani nitakuwa tayari nimekwisha oa yule mchumba niliyewekewa na baba yangu, au nitakuwa kwenye matayarisho ya kufanya hivyo. Pamoja na kuwa bado ninakupenda, nimeona ni bora kuafikiana na wazee wangu kwa wanalolitaka. Ndoa ya mapenzi kwa mimi na wewe nikupendaye imeshindikana, heri nifikie muafaka na wazazi wangu katika ndoa ya kupangiwa.
Akupendaye daima,
Edward Oloi (Edo)
Lulu aliangua kilio bila ya kujizuia mbele ya Halfani. Mpiga picha huyo alijaribu kumbembeleza kwa maneno ya kumfarji na kumpa matumaini. Mwishowe Halfani alimwambia Lulu.
“Tafadhali Lulu nyamaza, kilio chako na unisikilize” Lulu alisinasina huku akifuta machozi kwenye macho yake mazuri yalikuwa yamegeuka rangi kidogo kwa sababu ya kilio alimuangalia Halfani.
“Sikia Lulu, mimi binafsi ninajihisi kuwa nina hatia zaidi kuliko mwingine yeyote katika suala hili. Ninaona ndiye mimi niliyevunja uhusiano wako wewe na Edo. Kwani isingekuwa hivyo kama ningekataa kupiga zile picha.’’ Lulu kwa sauti ya chini na ya huzuni naye alijaribu kumwambia Halfani
“Hapana Halfani, huna haja ya kujihisi kuwa una hatia, hii yote ni kazi ya Onespot. Hata kama wewe ungekataa kupiga zile picha, kwa kuwa yeye amekwisha dhamiria ubaya, angemtafuta mpiga picha mwingine… ni bahati mbaya tu kuwa wewe ndiye uliyeingia mtegoni kama nilivyoingia mimi. Edo alikwisha hisi jambo
hili pamoja na kuwa hakuelewa linaendeshwaje, ni mimi tu niliyekuwa mpumbavu.’’ Lulu aliuziba uso wake kwa viganja vyake vyote viwili na kuuinamisha chini baada ya kusema hayo,
“Mimi ninakwenda ofisini kuuliza anwani za Edo za huko Arusha, ambazo nina hakika zitakuwepo ndani ya faili lake. Kisha nifanye safari nimfuate huko kwao. Sitapumzika mpaka nimekutana na Edo. Wacha nikurudishe nyumbani Lulu,ili mimi nianze safari, au utapenda kubaki ofisini?” Halfani alisema habari hizi kumfahamisha Lulu, akiwa na amedhamiria kabisa. Lulu hakutaka kurudi nyumbani kwao kwa wakati ule, alimuomba Halfani amuache hapo hapo ofisini.
* * *
Kuna gari zaidi ya mbili za kifahari zimeegesha nje ya nyumba nzuri aliyokuwa anaiendea Halfani, ni siku mbili baada ya yeye kuagana na Lulu. Nyumba hiyo ilikuwa kando ya mji wa Arusha, ilikuwa ni nyumba ya baba yake Edo, Mzee Oloi. Wakati huo ilikuwa ni majira ya saa kumi alasiri. Halfani alipoikaribia zaidi nyumba hiyo, alitupia macho huku na huku kwa matumaini ya kuona mtu kabla hata hajagonga mlango. Kweli , alimuona kijana mmoja aliyekuwa amevaa kaptula na fulana iliyokuwa haina mikono, nguo zilikuwa zimechafuka kwa udongo. Mvulana huyo mkononi mwake alikuwa amenyanyua reki na jembe, alionekana wazi kuwa alikuwa ndani ya shughuli za bustani inayoizunguka nyumba hiyo. Kijana huyo alimsogelea Halfani, na baada ya kusalimiana alimuuliza amsaidie nini. Nae Halfani alimjibu kwa kumuuliza,
“Samahani kijana, hapa ndipo nyumbani kwa akina Edward…..Edward Oloi?!”
“Eeeh, ndio hapa.”
“Sijui Edward mwenyewe yumo?!’’
“Ndio, yuko ndani.”
“Ahsante kijana, naomba ukaniitie………huyo Edward.’’
“Nimuambie anaitwa na nani?’’
“Muambie Bw. Halfani Matai kutoka Dar es salaam.’’ Kijana aliondoka na kuelekea ndani ya nyumba hiyo, lakini sio kwa kupitia mlango wa mbele, bali alizunguka nyuma ya nyumba. Baada ya dakika chache, kijana yule alirudi akiwa ameongozana na Edo. Halfani alipomuona Edo, alitoa tabasamu kubwa la shukrani. Edo alikuja moja kwa moja mpaka alipokuwa amesimama Halfani, alikunjua mikono yake na kumkumbatia huku nae akitabasamu na kusema
“Siamini macho yangu, karibu sana Bw. Halfani, karibu ndugu yangu, hapa ndio kwetu bwana.” Alimpokea begi ndogo aliyokuwa ameishika Halfani, akampa kijana na kumuashiria aipeleke ndani, kisha Edo alimchukua yule mgeni na kumuingiza ndani ya nyumba kwa kupita njia ileile aliyotokea Edo, nyuma ya nyumba. Edo aliendelea kusema,
“Duh! Its realy a surprise visit, lakini kwema?! Karibu sana nimefurahi….samahani sana rafiki yangu, ninakupitisha kuingia nyumbani kupitia mlango wa nyuma sababu huko mbele, sebuleni, kuna wazee wana kikao chao muhimu.’’ Edo aliyasema haya yote wakati wanaingia ndani ya nyumba. Baada ya mgeni yule kukarimiwa kwa taadhima zote, ilipofika jioni ilibidi akae pamoja na Edo wazungumze. Edo alianza
“Enhe! Lete habari Halfani, kulikoni?!’’ Halfani alionesha kuhuzunika kidogo, alisema kwa sauti ya chini bila kumuangalia Edo usoni.
“Bwana Edo, nimekuja kwako rasmi kwa madhumini mawili, la kwanza ni kuhusu mimi mwenyewe na la pili ni kuhusu Lulu.’’ Alitulia kidogo kumpa nafasi Edo amuelewe anayomueleza, kisha akasema,
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Kuhusu mimi, Bw. Edo, nimekuja kukuomba msamaha, nakuomba ndugu yangu uniwie radhi, kwani nimekukosea. Ni mimi ndiye niliyepiga picha zako wewe ukiwa na Vicky, na nimefanya hivyo kwa miongozo mibaya toka kwa Onespot, kuwa ilikuwa anataka kuwafanyia utani, practical joke. Sikuelewa kamwe kama alikuwa na madhumuni ya kuwatenganisha wewe na Lulu. Nimekuja kufahamu hilo baadae, hivyo naomba kwanza unisamehe Edo”. Edo alitulia tuli kumsikiliza Halfani, wakati anaongea yote haya, baadae aliuliza,
“Bw. Halfani, kuja kwako kutoka Dar es salaam mpaka Arusha kunitafuta nilipo, kumethibitisha wazi kuwa wewe si muhalifu. Muhalifu siku zote hafanyi hivyo, na kwa kuwa nilikuwa ninajua madhumuni ya Onespot tangu awali, kwa hiyo simpi lawama mtu mwingine. Amini kauli yangu Halfani, nimekusamehe……kwa dhati kabisa. Sasa niambie dhumuni lako la pili lililokuleta kwangu.’’ Halfani alionekeana kuwa ana nguvu kidogo na kujiamiani, alisema, “Dhumuni langu la pili ni kuhusu Lulu, ……Edo, Lulu bado anakupenda. Na amekwisha umbuliwa vya kutosha na Onespot, nakuomba umsamehe kama ulivyoweza kunisamehe mimi, na mrudiane, ikiwezekana muoane, kama ulivyokuwa umekusudia.’’ Edo alikutanisha viganja vyake vya mikono na kutengeneza makalio ya kidevu chake ambacho alikiweka juu yake. Akiwa sura yake imebadilika ghafla na kuwa imezama ndani ya mawazo, alimwambia Halfani kwa namna ya kuwa kama anasema peke yake.
“Na mimi pia bado ninampenda Lulu, wala hakuna alilonikosea ambalo ninahitaji nimsamehe. Hana hatia, lakini la kuoana, mbona haliwezekani tena?!’’ Halfani alimuomba Edo kwa kumsihi na kumbembeleza,
“Edo, hakuna lisilowezekana, Lulu yupo anakusubiri wewe, nawe unasema unampenda, na yeye nina hakika anakupenda, sasa nini kinachozuia msioane?!” Edo alionekana kama anayetaka kulia, lakini anajikaza kiume na kumueleza Halfani, alisema,
“Rafiki yangu Halfani, mimi na Lulu tangu siku ya kwanza tulipokutana, tulionekana tuna mambo mengi yanayofanana, kuanzia begi zetu za nguo, ajira yetu, nyoyo zetu katika kupendana, hata maadui wetu pia ni hao hao. Pia lipo jambo ambalo tangu mwanzo, lipo kwa upande wangu, na wake vile vile, nalo ni kuwa tuna wachumba tuliowekewa na wazazi wetu. Mimi nina wangu, na yeye ana wake. Hata hivyo, wazazi wetu, yaani wake yeye na wangu mimi, kila mmoja kwa upande wake alipewa nafasi ya kutoka na kwenda kutafuta mchumba amtakae, na atakaposhindwa arejee kwao, akaoe yule aliyepangiwa,” Edo alipofika hapo, alitulia kidogo na kumuangalia Halfani usoni, halafu akageuza uso kando na kuendelea kusema,
“Kwa hali halisi ilivyo, ni dhahiri kuwa mwisho wetu mimi na Lulu utakuwa huu wa kuoana na wachumba tuliochaguliwa na wazazi wetu. Ninasema hivyo kwa sababu……..nadhani ulipokuja ulikuta gari hapo nje ya nyumba zimeegesha.”
“Ndiyo.’’ Halfani aliitika.
“Na pia nilikuambia kuwa sebuleni kuna wazee wana kikao.”
“Ndiyo ulinifahamisha.’’
“Basi kikao hicho kilikuwa cha kukamilisha masuala ya harusi yangu, yaani mahari, nini, kila kitu wao wenyewe wazee wanajua. Si unajua tena ndoa za kupangiwa, ni kupangiwa kweli.’’
“Kwa hiyo?!’’ Halfani aliuliza.
“Kwa hiyo, mimi nimekwisha wakubalia wazazi wangu, na wao wamo ndani ya mipango ya harusi yangu, hivyo sitaweza wala kuthubutu hata mara moja kurudi tena nikasema simtaki mchumba wa chaguo lao, hata, hili haliwezekani wamekwisha nipa nafasi imeshindikana kuitumia, wacha nioe mchumba wa chaguo lao, ingawa ninampenda Lulu. Atabaki kuwa moyoni mwangu, na nitajifunza kumpenda mke wangu nitakae muoa.” Halfani alirudisha pumzi kwa nguvu kama vile aliyekuwa na
mzigo mzito asioweza kuubeba.
“Kwa hiyo Edo nikamuambie nini Lulu?’’
“Kamwambie kila kitu ninachokueleza, na pia kamuambie nimefurahi mno kwa vile hakuolewa na Onespot, hivyo basi arejee nyumbani kwao, akubaliane na baba yake aozwe yule mchumba wake aliyewekewa. Mwambie aafikiane na wazazi wake kama vile mimi nilivyoafikiana na wangu, wachumba wa kupangiwa kwetu sisi ndio muafaka, ndoa hupangwa mbinguni.’’
* * *
Ilikuwa siku ya Jumatatu Halfani alipofika ofisini kwao asubuhi na mapema siku mbili baada ya kurudi kutoka Arusha.Mtu wa kwanza kukutana naye ndani ya ofisi hiyo alikuwa Vicky. Baada ya kusalimiana, Halfani alionekana ni heri amwambie msichana huyo japo maneno machache kuhusu aonavyo yeye juu ya uhusiano wa Vicky na Onesport, Halfani alianza kwa kuuliza,
“Vicky Harusi yenu wewe na Onespot itakuwa lini?”CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Hivi hujapata kadi yako Halfani? Harusi yetu itakuwa Jumamosi hii.”
“Hapana, bado sijapata…labda nilihitajika katika kutenganisha tu, lakini sio katika kuunganisha.” Vicky alitulia kidogo kama anayefikiria na kuyatafakari aliyoyasema Halfani, kisha akauliza,
“Mbona sikuelewi Halfani?! Ulihitajika kumtenganisha nani! Na huhitajiki kumuunganisha nani?’’
“Wakati Edo na Lulu walipotakiwa watengane, nilionekana mimi Halfani ninafaa,na bila mimi mwenyewe kujua nilitumiwa kutimiza lengo hili. Lakini sasa hivi wewe Vicky na Onespot mnataka kuungana katika ndoa, mimi sionekani hata kuwa wa maana kushuhudia ndoa hiyo, na ndio maana sikukumbukwa hata kwa kadi.’’ Vicky kidogo alihuzunika, alitamka bila kumuangalia Halfani,
“Sio hivyo Halfani, leo ni Jumatatu, mpaka tuifikie Jumamosi, tunazo karibu siku nne katikati hapa, labda kadi yako ipo njiani inaletwa!’’ Vicky alijaribu kujitetea.
“Labda…! Labda…! Katika shauri hili la harusi yenu, nadhani kwa hali ilivyokuwa, nilikuwa mimi niwe wa kwanza kuarifiwa.’’ Aliendelea kusema Halfani kumwambia Vicky, kisha akaendelea,
“;…Lakini sasa hivi ninazidi kutanabahi na kuona kumbe mimi Halfani ni chombo tu katika kutimiza lengo lenu, wewe na Onespot. Kwenu nyinyi, mimi si lolote, si chochote…’’ Vicky alimkatiza Halfani asiendelee na mipasho yake akisema,
“Basi Halfani, basi…nakuomba tafadhali usiendelee. Ungejua ni kiasi gani mimi hivi sasa ninavyojuta kwa suala la Edo na Lulu, usingesema hivyo, lakini sasa nifanye nini na yamekwisha tendeka?! Nimkatae Onespot asinioe? Haiwezekani, nitakuwa ninajidanganya. Nilifanya nilivyofanya kwa sababu ya kutaka jambo hili la kuolewa na Onespot liwe. Nimeyavulia nguo maji, sina budi kuyaoga. Laiti nigelikuwa na uwezo wa kuwafanya Edo na Lulu wawe kama walivyokuwa mwanzoni, na ikiwezekana waoane, ningefanya hivyo, kwani kila ninapowakumbuka, ninakosa amani nafsini mwangu.’’ Vicky alipomaliza kusema haya, alibaki kuduwaa kama sanamu na kuzama katika mawazo. Aligutushwa na swali aliloulizwa na Halfani.
“Je, Onespot anasema nini kuhusu Edo na Lulu?!’’
“Ninashindwa kumjibia, tafadhali Bw. Halfani nenda kamuulize mwenyewe swali hili!’’
“Yuko wapi Onespot?!’’
“Nimemuacha ndani ya ofisi yake.’’
* * *
Baada ya mlango wa ofisi ya Onespot kufunguka, sauti yake ilisikika ikisema,
“Karibu Bw. Halfani!” Halfani aliiendea taratibu meza ya Onespot.
“Have a seat please, tafadhali kaa Halfani enhe, lete habari!!”
“Habari safi tu Bw. Onespot, ninasikia ndoa yenu wewe na Vicky itafungwa Jumamosi hii inayokuja?!’’
“Definitely yes, sawa kabisa Jumamosi,…una kipingamizi au shauri lolote Halfani?!’’
“Hapana, sina shauri wala kipingamizi chochote Onespot nilidhani labda ningealikwa!!” Onespot alikunjua kiganja chake cha kulia na kukigonganisha na paji lake la uso kwa nguvu na kutamka,
“Oh! No! Wajua nimesahau kabisa, na kadi zote zimekwisha. Nimekusahau kabisa rafiki yangu Halfani, Lakini usijali unaweza kuhudhuria kama mmoja wa wapiga picha wa harusi yetu. Kwa vile uliomba likizo ya siku tano, ndio maana hukuwepo wakati kadi za mualiko zilipokuwa zikitolewa.’’ Halfani alimuangalia Onespot usoni, na akaona ndio hapa hapa pa kumuambia alilotaka kumjulisha.
“Bw. Onespot, kumbuka vizuri kuwa sikuwepo wakati unapanga mpango wenu wewe na Vicky wa kuvunja uhusiano wa Edo na Lulu, lakini ulikumbuka kunitumia kama kifaa kwenye kutimiza lengo lako hilo, na kunitia mimi hatiani bila kujijua, lakini kwenye ndoa yenu mmenisahau! Ati unaniambia niwe mmoja wa wapiga picha wa harusi yako! Ahsante sana Onespot, siwezi kuchukua agizo la kupiga picha kutoka kwako wewe kuanzia leo, umenitia katika hatia.’’
“What’s wrong with you man?! Una tatizo gani Halfani?! Enhe! Edo and Lulu is none of your business, hayakuhusu! Achana nao!” Onespot alimwambia Halfani kwa sauti ya juu na ukali kidogo, akionesha kutomuelewa Halfani na malalamiko yake.
“Ya Edo na Lulu,ni kweli hayanihusu, lakini ni wewe uliyenihusisha nayo, au leo unakataa?!”
“Lakini yamekwisha, it’s a closed chapter,finish, enhe! Why should you worry?! Kwa nini ujipe wasiwasi Halfani?”CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Lazima niwe na wasiwasi, sababu nimesababisha watu wawili wapendanao, wasio na hatia, kutengana. Ninajihisi kuwa nina hatia.” Onespot alionesha kudharau kabisa malalamiko ya Halfani na kusisitiza kuwa hakuna cha kukitilia wasiwasi.
“Come on Halfani, don’t feel guilty, iwapo mimi sijihisi kuwa nina hatia sembuse wewe?! Unajiumiza kichwa bure.”
“Ina maana ulilomfanyia Edo na Lulu unaliona ni jambo zuri kabisa Onespot?!”
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment