Search This Blog

Wednesday, 1 June 2022

MUAFAKA - 5

 







    Simulizi : Muafaka

    Sehemu Ya Tano (5)



    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Well… ninasikitika… yaani ninawasikitikia, lakini sijuti, I don’t regret. Nilitaka kumthibitishia Edo kuwa ninaweza kupigana vita ya aina yoyote ile, na nimeshinda, basi.” Halfani alimuangalia Onespot halafu kwa sauti ya chini akamuambia,



    “Lakini ufahamu kuwa ushindi wako unaathari kubwa katika ndoa yako unayotaka kuifunga?”



    “Kwa vipi Halfani?!”



    “Kwa vile umemshirikisha Vicky, mke unayetaka kumuoa katika vita hivyo. Sumu ya baadhi ya silaha ulizotumia katika vita hiyo itabaki kuwepo ndani ya ndoa yenu.”



    “Kwa nini?!”



    “Kwa sababu nyoyo za binadamu zimeumbwa na udhaifu ndani yake, hasa hasa za wanawake. Anapomtendea mtu kosa, basi huwa hawezi kulisahau kosa lile, hata kama atajidai hana dosari mbele ya watu wengi au wote, lakini nafsini mwake ataikosa amani, vile vile kumbuka kuna na Mungu, shahidi wa vitendo vyetu vyote. Hata siku moja hatakuwa upande wa msaliti, anayesaliti binadamu wenzake waonekane hawafai kwa manufaa yake. Hivyo basi amani haitakuwepo ndani



    ya ndoa yenu. Ingawa wewe utajifanya kichwa ngumu, hujali wala hujuti, lakini muongo siku zote utawakumbuka Edo na Lulu, na huyo mkeo mtarajiwa, hivi sasa tayari amekwisha anza kujuta na kukosa amani.” Onespot baada ya kuyasikia haya kutoka kwa Halfani, alirudisha pumzi kwa nguvu na kusema,



    “ Look here Halfani, tazama bwana, ni kweli uliyoyasema yote lakini ikiwa nitajiingiza katika hali ya kujuta na kumuwaza Edo na Lulu, sasa nitakuwa ninafanya nini?! Kwa sasa hivi wacha niendelee na mipango yangu. Na huyo Vicky, ni kwa muda tu hayo majuto yake, baadae atayawacha na kusahau.” Halfani alitikisa kichwa chake kwa masikitiko na huzuni kwa kuona ni jinsi gani Onespot ni mtu wa kujipenda na kujipendelea, akamuambia,



    “Amani katika ndoa yako itakuja pale tu utakapokubali kumuona Edo na Lulu na kuwaomba radhi, kwa vile umekwishafanikiwa kuwatenganisha, vinginevyo vyovyote vile unajidanganya. Kiburi si uungwana, utakuwa muungwana zaidi ukiweza kufanya hivi ninavyokuambia, na amani itakuwepo ndani ya ndoa yako. Kwa heri.” Halfani alisimama kutaka kuondoka, lakini Onespot alimzuia kwa kusema,



    “Hebu subiri kwanza Halfani.” Halfani aliketi tena juu ya kiti na kumuangalia Onespot kwa jicho la unasemaje.



    “Kwa hiyo utakuja kupiga picha harusini kwetu au sio?!” Onespot alimuuliza Halfani.



    “Nadhani nilikwisha kukupa jawabu la swali hilo, ambalo ni kuwa, sitapiga picha yoyote kuanzia sasa, ambayo ninaagizwa na wewe, hii ni pamoja na kuacha kazi katika kampuni yako.”



    “Kwa nini ufanye hivyo Halfani?!”



    “Kwa sababu ndio njia pekee ya kuonesha kuwa sikuwa pamoja nawe katika nia yako ya usaliti nilipopiga zile picha za Edo na Lulu.” Onespot alibaki kushangaa na kuduwaa wakati Halfani anatoka ofisini kwake.



    * * *

    * * *



    Halfani alikuwa bado hajaonana na Lulu tangu arejee kutoka Arusha. Aliahirisha kuonana nae kwanza kwa kutaka aonane na Onespot na Vicky kwanza, pili ni kuwa alikuwa anajishauri namna ya kumkabili Lulu na jinsi ya kumpa ujumbe utokao kwa Edo. Kwa kuwa hilo, la kwanza amekwisha lifanya, kwa hiyo jioni ya siku hiyo aliamua aende nyumbani kwa akina Lulu. Alipofika alikaribishwa vizuri na dada yake Lulu, Flora, baada ya kusalimiana na kujitambulisha, aliombwa akae sebuleni asubiri akaitiwe Lulu. Baada ya dakika chache, Lulu alitokea akiwa anaoneakana mpole na aliyependeza asiye hatia kama malaika. Alitoa tabasamu kubwa alipomuaona Halfani na kusema,



    “Karibu sana Halfani, jisikie upo nyumbani.” Ahsante sana Lulu, tayari najihisi nipo nyumbani.”



    “Kabla hatujaulizana habari Halfani, sijui ungependelea kinywaji gani?!”



    “Soda tu inatosha.”



    “Soda gani unapendelea”



    “Sprite tafadhali, nataka nikate kiu.” Wote walicheka halafu Lulu alitoweka kidogo na baada ya muda wa dakika chache alikuja tena akiwa amenyanyua kisinia kilichokuwa na chupa ya soda ya sprite juu yake. Aliiweka juu ya meza ya kahawa iliyokuwa mbele ya Halfani na kuifungua ile soda. Wakati Halfani anakunywa soda taratibu, walianza mazungumzo yao. Halfani alimueleza habari zote Lulu. Alimueleza habari za makutano yake na Edo na akatoa ujumbe aliopewa ampe Lulu, kuhusu muafaka wa Edo na wazaai wake. Lulu alimsikiliza Halfani kwa utulivu na makini na alipokwisha maliza, Lulu alimuuliza tena ili afahamu zaidi kuhusu suala hilo.



    “Kwa hiyo Edo anaoa mchumba aliyewekewa na wazazi wake?!”



    “Ndio hivyo Lulu, nasikitika nimejitahidi kadri ya uwezo wangu. Na ni kweli niliwakuta hao wazee wakijadili suala lake la harusi.” Lulu alikaa kimya kwa muda pasipo kusema wala kumuangalia Halfani, alionekana amepotea katika msitu wa mawazo. Ilibidi Halfani amtoe katika mawazo hayo kwa kumuuliza,

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Vipi Lulu, unafikiria nini ?!....Mbona kimya mno?!”



    “Unajua Halfani siamini kama haya yote yaliyotokea kuwa ni kweli! Ninaona kama vile nilikuwa ndani ya usingizi. Edo ni ndoto ambayo nimeipenda na kuithamini. Onespot nae ni njozi iliyokuwa inanitishia, Vicky ni ndoto isiyoeleweka. Sasa hivi najiona nimetoka usingizini, na wewe Halfani ulie hapa mbele ya macho yangu ndie uliye halisi na unajaribu kuitafsiri ndoto na njozi yangu. Ninashukuru sana sana Bw. Halfani, utabaki kuwa kama kaka yangu. Sasa hivi mimi niko macho, nimekwisha toka ndani ya ndoto yangu, la kufanya ni lile jambo ambalo ninahisi sio ndoto. Nalo ni la mimi kurudi kwetu nikaolewe na yule mchumba wangu niliyewekewa na baba yangu, kwani ndio muafaka. Ni kweli ndoa huandikwa mbinguni.”



    Halfani alimuangalia Lulu kwa macho ya Huruma, lakini Lulu alionekana kuamini alilokuwa akisema. Mara alimtazama tena Halfani na kumuambia,



    “Kaka Halfani, nina ombi moja tu kwako tafadhali.”



    “Sema tu Lulu hata kumi na moja, tena bila ya tafadhali.”



    “Ninarudi nyumbani, baba yangu atafurahi mno nitakapomuambia nimekubali niolewe na yule mchumba niliyepangiwa. Na nina hakika harusi itaanza kuandaliwa mara moja. Sasa ninaloliomba kwako, siku ya harusi yangu, uje unipige picha nikiwa nina mume wangu halafu picha hizo umpelekee Edo, wasemaje?!”



    “Kwa hilo halina shaka Lulu, sasa niambie nitajuaje shughuli hiyo itakuwa lini?!”



    “Uwe unawasiliana na dada Flora hapa nyumbani mara kwa mara, muachie namba yako ya simu nawe chukua yake.” Halfani alifurahia sana wazo hilo, na aliongezea kusema “Hilo ni wazo zuri mno ambalo litanitoa mimi katika hisia za uhalifu. Pia kwa kuongezea nitampigia Edo simu, kama harusi yake itakuwa bado basi siku hiyo ikifika niende, ambayo nina hakika itakuwa hivi karibuni, ili nikampige na yeye picha akiwa na mke wake, wakati nikija kwenye harusi yako nikuletee, hii itanifanya nijikomboe na niwe huru tena au unaonaje?”



    “Sawa sawa kabisa kaka Halfani, fanya hivyo ili niweze kuona picha ya ndoto yangu.”



    * * *



    Baada ya harusi yao kubwa na ya kufana Onespot na Vicky walionekana kuwa watulivu na waliochoka, wakiwa bado wamo ndani ya kitanda kikubwa majira ya saa tatu asubuhi ya siku ya jumapili, Vicky alilaza kichwa chake juu ya kifua cha Onespot kilichokuwa wazi. Sehemu ya tumbo mpaka miguuni ilifunikwa na shuka kubwa ambayo pia shuka hiyo hiyo ilifunikiwa mwili wa Vicky kuanzia miguuni hadi kwenye matiti. Mkono wa kushoto wa Onespot uliegeshwa juu ya bega la kushoto la Vicky. Walikuwa katika hali hiyo kwa dakika kadhaa huku macho ya Onespot yaliyokuwa wazi kabisa yakikodolea dari ya chumba hicho walichokuwemo. Kimya hicho cha muda kilivunjwa na sauti ya Onespot iliyoita,



    “Vicky?!”



    “Mmh!”



    “You are my wife now, u mke wangu sasa.”



    “Ndiyo,na wewe ni mume wangu sasa.”



    “Kabisaa…totally yours”



    “Do you really love me Onespot?, unanipenda kweli?!Nataka kuondoa shaka iliyo moyoni mwangu.”



    “Shaka gani Vicky?!” Vicky alinyanyua kichwa chake na kumuangalia Onespot.



    “Hisia zako juu ya Lulu!”



    “Oh! Come on Vicky, let us not talk about her, tusizungumzie habari zake, niliyemuoa ndiye niliyempenda kushinda wote. Leo ni siku yetu ya kupanga tuende wapi fungate?!” Vicky alitoa tabasamu kubwa, kisha akambusu Onespot shavuni na kusema,



    “Samahani mpenzi, wewe unafikiri tuende wapi kwa ajili ya fungate yetu?!”



    “Unanirudishia swali Vicky, haya basi, twende London, Paris, New York, Nairobi, Kampala, Harare au Johannesburg, sema wapi? Popote upendapo tutakwenda na hii ni zawadi ya pendo langu kwako.” Vicky alijihisi kufanikiwa mno, aliona sasa kweli Onespot ni wake yeye kabisa, ndipo alipojibu,



    “Tuna haja gani ya kwenda kwenye fungate yetu ugenini?! Kama uwezo tunao, kwa nini tusiende kwenye mbuga za wanyama Serengeti na Ngorongoro na kurudi kupumzika Arusha?!”



    “Good idea! Ni wazo zuri sana Vicky, tutapata nafasi ya kuona wanyama na kupumzika vile vile. Sasa nitafanya mpango wiki ijayo tuende safari yetu kwenye fungate ili tusipoteze muda, wiki mbili zitatosha.”



    * * *



    Furaha kubwa walikuwa nayo wazazi wake Lulu baada ya kumuona binti wao amewasili nyumbani kwao. Ilizidi maradufu pale alipowaeleza kwamba ameamua kurejea nyumbani na yupo tayari kuolewa na huyo mchumba aliyewekewa na wazazi wake hao.



    “Ah! Mwanangu Lulu! Hebu nikuuulize, je, vipi hukuweza kupata huyo mchumba wa kumchagua mwenyewe?!” Baba yake Lulu alimuuliza mwanawe kwa taratibu. Lulu alitulia kidogo kabla hajajibu swali aliloulizwa na baba yake, kisha akarudisha pumzo polepole na kusema,



    “Baba, kusema kweli mchumba nilimpata, niliyempenda sana, au ninayempenda sana kuliko nilivyofikiria, lakini kumbe ilikuwa ni ndoto baba, ndoto ambayo sitaweza kuisahau maisha yangu yote yaliyobakia.” Aliishiliza kusema kwa sauti ndogo na ya chini. Mzee Frank alimuangalia binti yake kwa masikitiko kidogo, kisha akajaribu kumfariji kwa maneno,



    “Sikiliza Lulu binti yangu, ndoa hupangwa na Mungu, usidhani wote waliooana walitaka kuoana na hao waliooana nao, hata, sio wote. Mimi baba yako binafsi, nilipokuwa bado mvulana na msela, nilipendana na msichana ambae si mama yako. Niliahidi kumuoa, lakini kabla sijafanya hivyo, nilipata safari ambayo ilinichukua muda mrefu, na niliporudi nilikuta yule msichana amekwisha olewa na mtu mwingine aliyejitokeza kwanza kwa wazazi wake. Nilisikitika lakini sikuwa na la kufanya, bali niliwaomba wazazi wangu wanitafutie msichana mwingine wa kumuoa. Ndipo nilipotafutiwa huyu mama yako. Tulioana na mapenzi yetu yalianza ndani ya ndoa. Leo hii hata nikifa halafu nirudishwe tena mwanzo wa maisha yangu na niulizwe ninataka kumuoa nani, nitamchagua mama yako. Nisingetaka kuoa mwanamke mwingine yeyote zaidi ya mama yako. Mume tunayetaka kukuoza mwanangu tunaamini ni mwema, na amezaliwa na watu wema wanaotoka katika familia nzuri, yenye adabu, huruma, upendo na heshima. Nasi tuna hakika utafurahia maisha yako ya ndoa, mwanangu, nina imani utampenda mume wako.” Baada ya mahubiri haya marefu, Mzee Frank alimuangalia mwanawe Lulu usoni na kuongeza kwa kumuuliza,



    “Je, mwanangu Lulu, upo tayari kuolewa na huyu mchumba tuliyekuchagulia?!”



    “Ndiyo baba, nipo tayari.”



    “Vema, mama mwanangu, sasa leo pumzika ili ujiandae kwa kesho kukutana na wakwe zako na mchumba wako, kwani bado yupo anakusubiri.”



    * * *



    “Haloo!”



    “Haloo, ni nani mwenzangu?!”



    “Mimi ni Halfani Matai ninayezungumza.”



    “Ah, haa! Bwana Halfani ni Edo Oloi anaongea vipi habari za huko Dar?!”



    “Za huku nzuri tu Edo, sijui za huku Arusha?!”



    “Safi tu”



    “Mambo yanaendeleaje, harusi yako tayari?”



    “Hapana, bado, kwani vipi huko?”



    “Huku salama tu, Onespot na Vicky wamekwisha funga ndoa, sasa nilikuwa nina taka kujitolea niwe mpiga picha katika harusi yako…kwa gharama zangu mwenyewe…kama itawezekana!”



    “Ahsante sana kwa kujitolea kwako Halfani, lakini nasikitika kukueleza kuwa kumetokea tatizo kidogo ambalo limefanya harusi ichelewe kidogo. Lakini kama itakuwa tayari nitakujulisha, ninapenda uwe mpiga picha katika harusi yangu.”



    “Tatizo gani tena hilo Edo?!”

    “Ah! Bwana wee, its my destiny, ni maajaliwa yangu!”

    “Yapi tena! Mbona unanipa wasiwasi?!”CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Huyo mchumba niliyewekewa.. naye..pia..” Twi, twi, twi,twiii…Simu ilikatika ghafla! “Halloo! Halloo!” Sauti ya Halfani ilikauka, lakini hakupata jawabu. Alipokagua simu yake ya kiganjani ambayo alikuwa anatumia kwa mazungumzo, alikuta pesa zimekwisha. Alijuta kwa nini asingeikagua na kuona zimebaki shilingi ngapi katika simu yake kabla hajampigia Edo. Alitamani kisimu chake hicho cha kiganjani akitupe, lakini akaona kuwa sio uamuzi mzuri ni bora akanunue vocha nyingine aongeze. Wakati Halfani anatafuta wapi pa kupata vocha ya simu, alionelea kwanza apite kwa akina Lulu kujua habari zake, alipofika alimkuta Flora yupo nyumbani.

    “Vipi Flora, habari za hapa.”

    “Za hapa nzuri tu bwana Halfani karibu.”

    “ Ahsante sana da’Flora, nimeona nipite tu mara moja kuulizia, labda kuna jambo jipya kuhusu Lulu.” Flora alitabasamu kidogo na kuzidi kumkaribisha Halfani.

    “Sawa, lakini basi karibu upite ndani Halfani, habari hizo za Lulu, unataka uelezwe juu juu umesimama?!”

    “Hapana da’Flora ni kuwa nina haraka kidogo.”

    “Hata hivyo, lakini hebu pita ukae japo kidogo tu!”

    “Ahsante dada.” Halfani alipita sebuleni akaketi juu ya kochi, mara aliletewa soda, sprite.

    “Da’Flora umeanza kujipa tabu nami nakuambia ni mgeni wa kupita tu.”

    “Kwa hiyo chupa moja ya soda?! … Hebu tafadhali kunywa wakati ninakueleza habari za Lulu.”

    “Ahsante, kwa yote pamoja na soda ya sprite, inaelekea Da’Flora kichwa chako kizuri hakisahau, umeweza kukumbuka kuwa ninapenda soda aina ya sprite.”

    “Ahsante, sasa Bw. Halfani, habari nilizozipata kuhusu Lulu, ni kuwa asingeamua kurejea nyumbani mwenyewe, sijui ingekuwaje! Sababu kulikuwa kuna mtafaruku mkubwa huko nyumbani. Baba alichachamaa mno kwa ajili ya huyo mchumba aliyewekewa Lulu. Imekuwa bahati Lulu amekwenda huko nyumbani, kwa hivyo sasa wameelewana na leo asubuhi nimezungumza na mama ameniambia

    habari zaidi atanieleza keshokutwa kwa kunipigia simu.” Flora alionekana amemaliza alilotaka kumueleza Halfani ambaye alikuwa na machache ya kuuliza.

    “Ndio tuseme mipango yote inaenda vizuri?!”

    “Inaenda vizuri kwa upande wetu, yaani wa baba na Lulu, lakini mama amenidokezea kwamba kulikuwa na tatizo kidogo, huko, upande wa mume. Nasikia huyo mchumba alichoka kusubiri na alipata habari kuwa Lulu ana mvulana huku Dar. Kwa hiyo wazazi wake sijui walichukuliaje swali hilo. Lakini kwa alivyonieleza mama, amesema kwa vyovyote vile mbivu na mbichi zitajulikana ndani ya siku hizi mbili.” Halfani alitulia, akiangalia sehemu ya juu ya kiwambaza cha sebule kilichokuwa kimepewa mgongo na Flora, bila kusema neno. Alikuwa akiwaza, Flora alimuuliza,

    “Halfani mbona unaonekana upo mbali kidogo kimawazo?!”

    “Da’Flora! Ninafikiria hatima ya mambo ya watu wawili hawa yaani Lulu na Edo kama walivyonieleza wao wenyewe ni kuwa tangu mwanzoni walipokutana mambo yao yanafanana sana. Sasa hivi wapo mbalimbali lakini bado yanafanana.” Flora alijiweka sawa na kumuuliza Halfani,

    “Kwa vipi Bw. Halfani?!”

    “Ni muda mfupi tu uliopita nilikuwa ninaongea na Edo kwa njia ya simu, mwisho wa mazungumzo yetu, Edo alikuwa ananiambia kuwa mipango yake ina matatizo kidogo. Wakati anasikitika kuwa ndio maajaliwa yake na anataka kunielezea ni nini hasa tatizo na inaonekana linahusu huyo mchumba wake, simu ikakatika. Sikuweza kupata maelezo yake kamili, hivi unionavyo nilikuwa ninakwenda kutafuta vocha kwa ajili ya simu yangu ya kiganjani.” Flora alisikitika na kusema kwa sauti ya chini,

    “Hivi unafikiri Halfani, na huyo Edo nae atakuwa na matatizo gani yahusuyo mchumba wake na wazazi wake?!”

    “Ndilo hilo ambalo silijui, lakini picha kamili ni kuwa tatizo lipo kwa Edo na tatizo lipo vile vile kwa Lulu, na tusubiri tuone wakati tunawaombea watu wawili hawa wasio hatia kila mmoja wao apate mwisho mwema.”



    * * *



    Halfani baada ya kununua kadi kwa dola za kutosha, aliamua asimpigie simu Edo kwa wakati ule wa mchana, bali asubiri jioni ndipo ampigie ili waendelee na mazungumzo yao. Kwenye majira ya saa kumi na mbili na robo hivi, Halfani alichukuwa simu yake ya kiganja, ikiwa yupo nyumbani kwake ametulia na kuanza kubonyeza bonyeza nambari za Edo aliyepo Arusha.

    “Haloo?!”

    “Halloo, ni Edo hapa anazungumza!”

    “Halloo, hapa ni Dar, ni Halfani tena.”

    “Ohoo, Bw. Halfani samahani simu ilikata mawasiliano wakati ule, na bahati mbaya nikawa sina credit na mimi!”

    “Bila samahani Edo, ni kosa langu, simu iliishiwa. Sasa hebu nielezee ulilotaka kunieleza wakati ule.” “

    “Halloo!”

    “Halloo, ninakusikia!” “

    “Nililotaka kukueleza ni kuwa, huyo mchumba niliyewekewa, kulionekana kuna pingamizi ya yeye kutoafiki mipango ya wazee wake. Pia ilisemekana anaye mvulana wake tayari, lakini hata hivyo, mambo yamesawazishwa. Hivi ninavyokuambia…haloo…unanisikia lakini?!”

    “Halloo, halloo, ninakusika Bw. Edo endelea.”

    “Hivi sasa ninajitayarisha pamoja na wazazi wangu na wazee wachache wengine, tunakwenda hukoo… ukweni huko kwa mchumba…halloo…” Halfani

    alikigeuzia kisimu kutumia mkono mwinigne kukizuilia hapo sikioni,

    “Halloo, Bw. Edo, sasa tuwasiliane lini tena ili unipe habari kamili?!”

    “Nitakupigia mimi.”



    * * *



    Moyo wa Lulu ulikuwa ukimwenda mbio ijapokuwa akili zake zilikuwa shwari kabisa hazikuwa tupu kwa wakati huo ambao alibaki peke yake chumbani akisubiri kuitwa au kuja kuchukuliwa. Alirembeshwa vipasavyo, ingawa si kwa urembo wa kiasili halisi wa kabila lao la kimasai, lakini ni kwa urembo na vazi la kisasa lakini linaloashiria ni la kabila hilo. Alikuwa anasubiri kuja kuchukuliwa na kupelekwa sebuleni ambako kulijaa wanachama wa familia mbili ya kwake yeye Lulu na ya mume mtarajiwa anayetaka kumuoa, wakiwemo wazazi wa pande zote mbili. Wakati huo familia ya mchumba wa Lulu na ujumbe mzima uliopo walikwishakaribishwa na tayari wamemaliza kula chakula cha jioni, pamoja na bwana harusi mtarajiwa. Wakati ulifika wa kuletwa Bi. Harusi mtarajiwa nae aje aonekane kwa wote waliokuwepo. Waliondoka wanawake watatu toka kundi hilo la watu waliokuwepo hapo kwenye sebule ya nyumba ya baba yake Lulu, kwa ajili ya kumleta aje aonekane na kumuona mchumba wake. Walimkuta Lulu yuko tayari, mmoja katika wanawake watatu hao, alikuwa ni mama yake mzazi Lulu ambae alitamka kumwambia binti yake,

    “Mwanangu Lulu, sina mengi ya kukueleza kwani yote amekwisha kukueleza baba yako, isipokuwa nakuomba umkubali mume huyu kwa moyo mmoja kabisa, na naamini utampenda. Maadamu sisi wazazi wenu wa pande zote mbili tumekwisha afikiana katika suala hili, basi ndoa yenu ndio Muafaka kwetu sisi na itakuwa hivyo kwenu nyinyi pia, umesikia mama mwanangu?!” Lulu alijiamini kabisa mpaka hapa mambo yalipofikia ni kuwa hana wasiwasi wala kipingamizi tena. Alimjibu mama yake kwa sauti ya chini, “

    “Sawa mama, nimesikia, na msiwe na wasiwasi na mimi, nimekubali na nimeridhika kabisa.”

    “Vizuri mwanangu, haya sasa nyanyuka twende ukakutane na wakwezo pamoja na mchumba wako.” Lulu aliingia ndani ya sebule taratibu akiongozwa na kina mama wale watatu. Katika makochi mengi yaliyokuwepo kwenye sebule hiyo pamoja na viti, vilikuwa vimekaliwa na watu wake kwa waume, ambao wote walielekeza macho yao upande ambao Lulu alikuwa anaingilia. Mmoja wa watu hao alikuwa ni bwana harusi mtarajiwa. Yeye alikuwa ameketi juu ya kochi la mtu mmoja, peke yake. Kochi hilo lilikuwa limeelekea upande ule ule aliotokea Lulu, kiasi cha kumfanya bwana harusi huyo mtarajiwa asiwe na tabu ya kugeuza shingo kama baadhi ya waliokuwepo hapo walivyofanya katika kumuangalia Lulu akiingia. Alitoa macho yake kumuangalia Lulu, alimtulizia macho pasipo kupepesa. Lulu nae alipofika karibu na kuelekezwa kuketi juu ya kochi lililokuwa karibu kabisa na la mchumba wake, ndipo aliponyanyua mboni za macho yake na kujaribu kuwaangalia watu wakiokuwepo. Hakutaka kuanza kwa kumuangalia mchumba wake, la hapana, aliyatembeza macho yake na kujaribu kuwaangalia watu waliokuwepo hapo, na mwisho kabisa ndipo alipoyafunua zaidi macho hayo kumuangalia mvulana aliyekaa naye karibu kwa vizuri na makini. Macho ya mvulana ambayo kwa sasa alikuwa ameyakodoa kabisa na kuyatuliza usoni kwa Lulu, yalikutana sawa sawa na ya Lulu. Moyo wa Lulu ulisita kwa nukta chache, alijihisi yupo kwenye ndoto, mchumba na mvulana yule, alikuwa ni Edo!!. Walibaki kutoleana macho kwa kuangaliana, huku wote wawili vinywa vyao wameviacha wazi!



    Mlio wa simu ulioita humo kwa humo bila kuacha ulimuamsha Halfani aliyekuwa usingizini. Alikaa kitako juu ya kitanda na kuenda miayo kabla hajaipokea simu hiyo, alitupa jicho juu ya kiwambaza na kuangalia saa, ilikuwa ni saa saba na nusu za usiku. Aliwaza. “Ni nani huyo anayenipigia saa hizi?! Isije ikawa amekosea namba!” Alinyoosha mkono wake na kunyanyua kisimu chake kilichokuwa karibu na kitanda. Kwa sauti ya uchovu aliipokea simu hiyo.

    “Haloo! Mie ni Halfani hapa, ni nani mwenzangu?!”

    “Halloo, ni mimi Edward Oloi…Edo.”CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Ohoo! Edo!” Halfani alijiweka vizuri na kujipekua shuka alilokuwa amejifunika na kuliweka kando, aliketi wima kitandani.

    “Rafiki yangu Halfani, sikuweza kusubiri kupambazuke, samahani kwa kukuamsha.”

    “Lakini kwema?!”

    “Sana, tena siwezi kusubiri kujumuika nawe katika furaha niliyonayo Halfani, oo! God is great, Mungu mkubwa ndugu yangu!”

    “Kulikoni Edo?!”

    “Lakini kwanza kabisa niambie simu yako ina chaji ya kutosha?!”

    “Nimechaji hii leo mchana, tunaweza tuzungumze mpaka asubuhi, wee endelea tu, iwapo na wewe hutaishiwa dola.”

    “Hapana siishiwi, nimejizatiti Halfani! Huwezi kuamini, kama vile ambavyo sikuamini mimi.” Halfani alitoa tabasamu la peke yake kwa kuhisi kama anayemuona Edo.

    “Hebu basi nieleze Edo, kuna nini?!”

    “Kuna nini, na mimi ninaoa jumamosi ijayo!”

    “Lakini hilo jambo lilikuwa tangu mwanzo linategemewa kuwepo, sasa cha kuamini na kutokuamini ni nini?!”

    “Ni mke nitakae muoa Halfani, huwezi kuamini?!”

    “Ni bomba sana enhee?!”

    “Ile mbaya rafiki yangu, oh! Mungu na asifiwe.”

    “Hongera Edo, hongera sana, haya nipe mpangilio mzima wa harusi yako itakavyokuwa.”

    “Vyovyote itakavyokuwa, harusi yangu Muafaka.” Halfani alianza kujaribu kutafakari vipi huyu Edo?! Ni furaha tupu tupu tu?! Au kuna kitu kingine?!”

    “Niko macho nakusikiliza wewe tu.”

    “Mbona huniulizi nitamuoa nani?!”

    “Hata ukimtaja mimi nitakuwa simjui, bora umesema ni mzuri sana, basi wacha nisubiri mpaka hapo nitakapokuja , nitajionea mwenyewe.’’ Halfani alisema kwa sauti ya kukata tamaa.

    “Haloo, humjui?! We nadhani ningekuamsha usiku wote huu kama siamini jambo lenyewe ninalokuamshia nawe litakufurahisha?!”

    “Haya niambie basi Edo, unaniweka na wasiwasi na shauku.”

    “Na hivyo ndivyo nilivyokuwa mimi kabla sijamjua mchumba wangu yukoje! Halfani, siku ya jumamosi ijayo, mimi Edo Oloi, ninamuoa Lulu Frank!” Halfani kidogo aiponyoshe simu ya kiganja.

    “Eti nini?”

    “Ehee! Ndiyo, mimi na Lulu tunaoana Jumamosi.”

    “Unajua Edo rafiki yangu, utani namna hii ni mbaya, kwangu mimi ni kama unanisimanga! Unaelewa dhahiri kuwa ningependa iwe hivyo, nina maana wewe utaoa, na Lulu ataolewa. Yaliyopita si ndwele tugange yaliyopo na yajayo.” Kulikuwa kimya upande wa pili wa simu inapozungumza mara.

    “Halloo, halloo!” Halfani aliita.

    “Halloo Halfani, nimekusikia yote uliyosema, let us be serious, mimi nitamuoa

    Lulu na Lulu ataolewa na mimi Edo. Sikiliza rafiki yangu, amini Lulu ndiye mchumba niliyewekewa au kuchaguliwa na wazazi wangu. Na Lulu nae ni mimi ndiye mchumba wake aliyechaguliwa na wazazi wake. Tumefikia Muafaka wa kikweli kweli wa wazazi wetu wa pande zote mbili na wa pendo letu.” Edo alimueleza Halfani mambo yote yalivyokwenda kati ya familia yake na familia ya Lulu, na namna walivyokuwa siku walipokutana mbele ya wazee wote.

    “Halloo! Sijui nisema nini Edo, sidhani kama utaweza kuhisi furaha niliyonayo. Mweny-Ezi-Mungu na ashukuriwe, baraka ziwe kwenu wewe na Lulu.”

    “Aamin!”

    “Sasa rafiki yangu niambie nifungashe sasa hivi nije huko Arusha?!”

    “Hapana, lala kwanza!’

    “Nilale nini na hivi sasa tayari majogoo yanawika?!” Edo aliangua kicheko cha dhati na kucheka kiasi cha kuifanya simu ya Halfani ivume kidogo.

    “Sawa sawa Halfani, sasa fungasha kamera za kawaida, za video…nadhani kila kitu unajua wewe, fika hapa siku tatu kabla ya siku ya harusi.”



    * * *



    Baada ya wiki nzima na siku kidogo zilizowachukuwa Onespot na Vicky kutembelea mbuga za wanyama Seregeti na Ngorongoro, waliamua siku chache zilizobaki za fungate yao waje wazimalizie Arusha kabla hawajarejea Dar es salaam. Walitafuta hoteli kubwa ya kifahari na kupangisha sehemu kubwa yenye vyumba na sebule (suite) ya hoteli hiyo. Walikuwa wakitembelea sehemu mbalimbali za mji wa Arusha kwa wakati wa jioni na usiku, kisha wanarudi na kupumzika. Jumamosi ya harusi ya Edo na Lulu ilifika, Onespot na Vicky walikuwa bado wamo ndani ya fungate yao hapo hapo mjini Arusha. Harusi ya Edo na Lulu ilisherehekewa kinamna tatu! Kwanza iliozwa kimila za kimasai, pili iliozwa kanisani, na tatu ilikuwa ni tafrija kubwa iliyoandaliwa na mzee Oloi, ambayo aliikodishia ukumbi mkubwa wa hoteli waliyofikizia Onespot na Vicky.

    Mzee Oloi licha ya kukodi ukumbi pia aliwaalika kwa kadi maalum wageni wote waliokuwa wakipanga hoteli hiyo kuhudhuria tafrija ya harusi ikiandamana na chakula cha jioni itakayofanyika jioni ya Jumamosi hiyo. Bahati mbaya au nzuri kadi hizo maalum hazikuandikwa majina ya maharusi hao, yaani Edo na Lulu. Zilitaja tu kuwa wageni wote mnaalikwa na kuombwa kuhudhuria karamu maalum ya harusi itakayofanyika ukumbi wa hoteli jioni hiyo, ni mualiko toka kwa wazazi wa harusi hao. Hali ya uharusi harusi walikuwa bado wanayo Onespot na Vicky isitoshe walikwishatembea na kuzurura vya kutosha, waliamua mara moja kuhudhuria. Jambo la kwanza walipoingia ukumbini hapo ni kutafuta sehemu nzuri ya kukaa na wakaketi, waliona mtu kwa mbali ambaye walimfananisha na Halfani.

    “Onespot, yule sie Halfani yule?!” Vicky alimuuliza mumewe.

    “Yuko wapi?!”

    “Yulee pale aliyesimama karibu na meza ile yenye wanawake wawili, tena ana kamera mkononi.”

    “Ndiye yeye yule, wala habadiliki!” Alijibu Onespot.”

    “Siku hizi amehamia Arusha?!”

    “Sifahamu, lakini tusubiri tu inavyoonekana ni mpiga picha wa shughuli hii, kwa hiyo ni lazima atakuja na upande huu wa kwetu!” Muziki mwanana wa bendi mbalimbali ulioongozwa na Dj. mmoja kijana ulikuwa unaburudisha, huku Mc wa tafrija hiyo akibwabwaja kila tukio linalohitajika kufanywa. Baada ya muda kidogo kupita, alichokuwa anakitaraji Onespot kilitokea, Halfani alikuja mpaka karibu na walipokuwa wamekaa Vicky na Onespot, lakini hakuwa amewaona. Onespot alitamka,

    “Bw. Halfani, ndiye wewe au macho yangu?!” Halfani aligeuka ghafla.

    “Siamini macho yangu Onespot! Vicky! Mmekuja hapa?!”

    “Sisi tumo ndani ya fungate, tukuulize wewe?!”

    “Mimi nimo kazini, kama mnavyojua, kwa hiyo mumealikwa katika harusi hii?!” Aliuliza kwa mshangao.

    “Ndiyo tumealikwa, tumefikia hoteli hii hii, kwa hiyo tumepata mualiko maalum wa ujumla wa wageni.” Halfani alitulia kidogo na kuwaangalia, kisha akauliza.

    “Kwa hiyo hamkualikwa na bwana harusi au bibi harusi?!”

    “We don’t even know who’s wedding it is, kwa kweli hatujui hata hii harusi ni ya nani?! Tumekuja kujifurahisha tu.” Halfani alitoa tabasamu kubwa la faraja na kusema,

    “Ni matumaini yangu mtafurahi kuliko mlivyokusudia. Mimi hii ni harusi ya marafiki zangu, nimejitolea kuja kuwapiga picha…burudikeni tutaonana baadae.” Halfani aliondoka akiwa na furaha moyoni mwake. Mc alisema hili na lile na baada ya muda kupita, aliwafahamisha waalikwa kuwa sasa bwana na bibi harusi wanaingia. Waliombwa watu wote wasimame kwa heshima yao na kuwakaribisha kwa kupiga makofi na kuimba kwa pamoja, ‘huyoo bwana harusi anaingia, huyoo bibi harusi anaingia!’ kwa furaha na bashasha Onespot na Vicky walisimama huku wakimfuatisha Mc anavyoimbisha. Ghafla walisita kupiga kofi na kugeuza nyuso zao kuangaliana, baada ya kuwaona na kuwatambua maharusi hao kuwa walikuwa ni Lulu na Edo. Kwa bahati mahali walipokuwa wamesimama ndipo palipokuwa na njia ya kuendea jukwaani. Maharusi hao walipofika karibu na waliposimama Onespot na Vicky, Lulu alikuwa wa kwanza kuwaona, alimgusa Edo kwa kumshitua, naye alipoangalia alikutana uso kwa uso na Onespot. Waliangaliana kwa dakika chache kisha Edo alinyoosha mkono na kumpa Onespot ambaye nae kwa unyonge alipeana viganja na Edo.

    “Karibu kwenye harusi yangu Onespot na kutana na mke wangu Mrs. Lulu Oloi!”

    “Ahsante Edo.” Onespot alisema kwa sauti ya chini. Edo alimgeukia Vicky na kumuambia,

    “Hongera Vicky…Mrs. Pato.”

    “Ahsante Edo, kuanzia leo amini usiamini ndoa yangu itakuwa na amani, tusamehe kwa yote tuliyotenda Lulu.”

    “Bila samahani.” Lulu alimjibu Vicky na akamvuta karibu yake na kumkumbatia. Onespot alionekana kama vile amelowa kwa mvua. Edo alimuangalia kisha alimuita,

    “Onespot, unakumbuka maneno yako?! Kuwa aliyepata na aliyeshinda ni aliyekwishaoa?! Kwa hiyo ikiwa vita yetu ni Lulu, basi leo nimekushinda!”

    “Ni kweli kabisa Edo, tufikie Muafaka kuwa mambo yote hupangwa na Mungu.” Wakati Edo na Onespot wanakumbatiana, Halfani alipiga picha, picha ya ukweli, picha ya MUAFAKA!

    Ujumbe: LOVECHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/



    L – Lulu

    O – Onespot

    V – Vicky

    E - Edo



    TOA MAONI YAKO!!!



    ~ MWISHO ~

    yanayofanana, kuanzia begi zao za nguo, ajira yao,



0 comments:

Post a Comment

Blog