IMEANDIKWA NA : HASSAN S. KAJIA
*********************************************************************************
Sehemu Ya Kwanza (1)
*******
BAADA YA KUIACHA FAMILIA YAKE NYUMBANI TANZANIA NA KWENDA KUISHI NCHINI UHOLANZI KWA KIPINDI CHA MWAKA MMOJA AKIFANYA KAZI NCHINI HUKO. MZEE AMIGOLAS ANAMALIZA SHUGHULI ZAKE NA KUAMUA KURUDI TANZANIA.
ANARUDI KWA FURAHA MOJA TU. KWENDA KUUNGANA TENA NA FAMILIA YAKE HIYO AMBAYO WALITENGANA KWA MUDA HUO.
MISUKOSOKO NA VITIMBWI VYA MAPENZI, TAHARUKI NA MTAFUTANO PAMOJA NA VISASI, NI MAMBO AMBAYO YANAPAMBA SIMULIZI HII KALI…..
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
ENDELEA
*****
BAADA ya chakula cha jioni mzee Ambrose Seduke alikuwa tayari ameshaweka mambo safi kwa ajili ya safari yake ya kurejea Tanzania. Suti nyeusi na shati la blue bahari lililonakshiwa na tai ndefu vilimfanya aonekane nadhifu sana. Alichungulia tena kwenye kioo na kuona kila kitu tayari. Sasa aligeukia upande wa pili na kukutana na picha ya familia yake iliyokuwa katika fremu. Ndiyo kitu cha mwisho kukipakia katika begi lake. Aliichukua na kuingalia vizuri kabla ya kuiweka ndani ya begi. Alikumbuka siku ambayo mpigapicha aliwatoa wote wakiwa katika tabasamu lililomfanya atabasamu peke yake. Alimwangalia mke wake Mercy pamoja na watoto wake Chris, Hancy, Naomi na Marry. Alitamani angekuwa nao pamoja siku hiyo.
Aligeukia tena kioo kilichokuwa pembeni ya kabati la nguo na kurekebisha tena tai yake. Sasa ilikuwa imekaa sawa sawa. Alitembea hatua tatu kisha akaikumbuka pakiti yake ya sigara aliyokuwa ameiweka mezani. Aliishika na kuanza kuifungua taratibu pakiti ile.
Hofu kubwa kwake ilikuwa ni juu ya safari. Safari ya kwenda kuonana na familia yake. Safari ambayo aliifikiria kwa mwezi mzima. Alitoa sigara moja baada ya nyingine huku akizunguka katika chumba chake akitafakari hili na lile kuhusu familia yake ambayo ilikuwa ikimsubiri kwa hamu kubwa sana. Aliwakumbuka wanawe na mke wake. Aliangalia tena begi lake. Alitazama sehemu alipoiweka ile picha na kufungua begi. Aliitazama tena na tena bila kuchoka huku akiendelea kuiteketeza sigara yake. Ni mwaka sasa tangu aondoke nyumbani, na sasa safari imewiva. Alitabasamu, alijua tu atafika salama.
Amsterdam Uholanzi ndiyo nchi iliyomtenga na familia yake kwa kipindi chote hicho. Shughuli aliyoifanya huko ni ya kuhakiki ubora wa madini ya dhahabu na Tanzanite ambayo yalitokea Tanzania. Madini hayo yalisafirishwa kwa ajili ya kuuzwa nchini huko. Ni taaluma ambayo alipata kuisomea na kuwa mtaalamu wa masuala ya madini.
Alilipwa fedha nyingi sana zilizomfanya kuwa moja kati ya mamilionea. Matajiri wa kutupwa nchini Tanzania. Alihakikisha familia yake inaishi vizuri hata kama akiwa mbali. Hakujionea ufahari. Alinunua nyumba kubwa sana maeneo ya Tabata ambayo watu tayari walishaitungia jina la hekalu. Ilikuwa na ulinzi ambao haukuthubutu yeyote aweze kuingia ndani ya hekalu hilo bila ya ridhaa ya wenyeji wa hapo. Ni nyumba ya kisasa yenye kila aina yap ambo lililostahili kuwa kwenye nyumba ya kifahari kama ya kwake.
*****
Sigara tano tayari ziliteketea. Chumba kilijaa moshi mithili ya nyumba ya msonge inayotumia jiko la kuni. Kwake ilikuwa ni burudani tosha kumwondolea mawazo na baridi kali iliyokuwa ikitesa watu ambao hawakuizoea kama yeye. Hoteli aliyokuwa akiishi haikuwa mbali na kiwanja cha ndege cha Amsterdam.
Alikuwa akisubiria simu kutoka kwa rafiki yake Peter kumtaarifu atoke kwa ajili ya kuelekea uwanja wa ndege. Asingeweza kusubiria nje kwani baridi ilikuwa ni kali sana. Sigara na kuni ambazo zilikuwa zikiteketea kwa moto chini ya dohani kwa ajili ya kupasha chumba joto. Hakukaa kwenye kiti. Muda wote alikuwa amesimama.
Akiwa amesimama dirishani akiuangalia mji kwa mara ya mwisho taa kubwa zilizoashiria eneo fulani kuna klabu zilimvutia kwa jinsi zilivyokuwa zikipishana. Ndege nyingine zilizokuwa zikienda nchi nyingine zilipishana angani. Nyingine zilitua zikirudisha na kuwaleta abiriwa wengine kutoka mataifa mengine. Alitamani angekuwa na familia yake huko alipo lakini muda wa kazi ulishakwisha na saini ya mkataba ilionyesha ni mwaka mmoja tu ndiyo angefanya hiyo kazi na kurejea nyumbani. Alitabasamu na kurudi mbele ya dohani kujituliza kupata joto tena. Mara simu yake iliita aliifuata kwenye meza na kuipokea.
“Ndiyo bosi, nadhani dereva atakuwa amefika hapo hotelini,” sauti ya Peter ilimhakikishia kwamba safari tayari.
“Nashukuru sana, tutakutana uwanja wa ndege tafadhali.”
“Sawa mkuu, ndiyo niko njiani kuelekea huko.”
Mlango wa chumba cha mzee Ambrose uligongwa na jamaa mmoja akiwa amevalia suti ya rangi ya damu ya mzee alikuwa amesimama akisubiri afunguliwe. Mzee ambrose alishangaa kumwona mtu mwenye asili ya Afrika akiwa amesimama mlangoni.
Mimi ni Mtanzania,” mzee Ambrose alijitambuliusha kwa mtu yule ambaye hawakufahamiana.
Ooh, nafurahi kusikia hivyo, mimi natokea Nigeria, ni dereva Taxi. Peter kaniagiza nikupeleke Uwanja waNdege wa Amsterdam.
Ndiyo niko tayari. Nilikuwa nikisubiria simu yake kama alivyoniambia kuna mtu atakuja kunichukua mpaka uwanja wa ndege.”
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Yule dereva alijitambulisha kwa jina la Odoyo kisha akachukua moja ya mabegi mawili yamzee Ambrose na kulipeleka hadi katika buti ya gari lake. Alirejea na kuchukua sanduku lingine kubwa na kulipeleka huku mzee Ambrose akifunga chumba na kukabidhi funguo kwa wahudumu wa hoteli. Aliaga na kuelekea kwenye gari la Odoyo tayari kwa safari ya kuelekea uwanja wa ndege.
*****
Akiwa ndani ya gari la Odoyo waliongea machache kuhusu watu weusi wanavyoishi katika nchi za wazungu. Odoyo alikiri kwamba bado hali ni mbaya hata wakiwa huko. “Kama hujaajiriwa ofisini kwa taaluma muhimu ujue ni tabu sana utakabiliana nazo,” Odoyo alimsimulia mzee Ambrose kwa kimombo mambo yanayoendelea huko kwa wazungu.
“Nimejionea Odoyo, bora Afrika, na ni kwa nini msirudi nyumbani kamma hali ni hii?” alihoji mzee Ambrose. Odoyo alimwangalia kupitia katika kioo cha gari mzee Ambrose na kumfananisha na mtu aliyemtakia kifo siku yoyote. Hakujua ni kwa nini alikimbia Afrika.
“Hapana mzee, hapa afadhali kidogo tofauti na nchi yetu, kote tabu lakini zinatofautiana. Nyumbani kuna machafuko sana na ndicho kilichotukimbiza wengi huko. Wengine wapo Italia, Ujerumani, Uingereza na Amerika. Ukiokoteza kazi kama hizi ni afadhali na kama tajiri yako atakuwa anakujali pia. Mi nashukuru naelewana na mkuu wangu na nafanya kazi ya kumwendesha yeye na familia yake.”
“Na Peter mlijuana naye vipi bwana Odoyo?”
“Peter ni rafiki wa mkuu wangu. Alimsaidia kupata mawasiliano na Ubalozi wa Nigeria Uholanzi ili aweze kunitambulisha kama mgeni huku. Alimsaidia sana na ndo maana leo akaniagiza nije kukuchukua na mkuu wangu asingeweza kukataa kwa sababu ya Peter.”
“Ahaa, Peter anafahamika sana huku eeh?”
“Kweli, anafahamika sana, hata hivyo ni kwa sababu ya kazi yake, unafanya kazi katika kampuni ya mawasiliano. Na wageni wengi humtumia katika kuwafikisha katika balozi za nchi zao.”
“Kweli Odoyo, hata mimi nilifahamiana na Peter kwa njia hiyohiyo, sikujua kama ni Mtanzania mwenzangu. Ila alivyoniona naongea na simu kabla sijamweleza natafuta Ubalozi wa Tanzania aligundua mimi ni Mtanzania kwani nilikuwa nikizungumza lugha ya Kiswahili na familia yangu. Amekuwa na mimi kwa kipindi chote nilichokaa hapa Uholanzi na leo tunasafiri pamoja kuelekea Tanzania.”
Odoyo aliegesha gari karibu na bango kubwa lenye picha ya wachezaji wa timu ya taifa ya Uholanzi. Mmoja ya wachezaji aliowafahamu mzee Odoyo ni mshambuliaji mahiri na mfungaji hodari wa klabu ya Manchester United ya Uingereza, Robin Van Persie. Aliteremka huku akiliangalia lile bango huku akitikisa kichwa chake kuonyesha kuvutiwa na ile picha katika lile bango kisha akamwonyesha Odoyo.
“Navutiwa sana na huyu mchezaji awapo uwanjani,” alikuwa akimwonyesha picha ya Van persie. “Mimi ni shabiki wa Manchester United ya Uingereza,” Odoyo alicheka sana na kumwambia mzee Ambrose kwamba hata yeye aliipenda sana klabu hiyo na kwamba akiwa hapo Uholanzi alivutiwa sana na klabu ya Ajax Amsterdam.
Waliteremsha mizigo na kupakia katika vitoroli ambavyo wangevisukuma mpaka katika eneo la abiria wanaotarajia kusafiri kwa ajili ya kukaguliwa.
Mzee Ambrose alikuwa akiangaza huku na kule akiliangalia Jiji la Amsterdam kwa mara ya mwisho kabla ya kupanda ndege.
“Bwana Ambrose,” alishtuliwa na sauti ya Peter ambaye aliwaona wakati mzee Ambrose analinyooshea kidole bango lenye picha ya timu ya taifa ya Uholanzi na kuwafuata kwa ajili ya kumwelekeza Mzee Ambrose sehemu za kupita hadi kufikia ndege. Ndege yao ilikuwa ianze safari saa sita na nusu usiku. Uwanja ulikuwa umejaa ndege na abiria walikuwa wengi sana.
“Inaelekea wasafiri ni wengi kweli,” alisema mzee Ambrose.
“Kweli, ujue kipindi kama hiki cha likizo watu wengi hurudi makwo. Ni kama tufanyavyo sisi. Sidhani kama ungependa kuendelea kukaa huku hata kipindi kama hiki japo kwako si likizo,” Peter alisema huku akiburuta begi lake kubwa kuelekea palipo sehemu ya kusubiria usafiri.
“Haswaa, siwezi kweli, hata ingekuwa ni likizo ya siku tatu, ningependa kwenda nyumbani kuiona familia yangu.’ Alisema mzee Ambrose.
*****
Saa sita na dakika 35 ndege ilianza kulitafuta anga la Amsterdam, abiria wote walikuwa kimya huku wengine wakionekana wakifungua mikanda yao baada kuelezwa na mmoja wa wahudumu wa ndege baada ya ndege kukaa sawa.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Mzee Ambrose alikaa sawa na kuchukua moja wa magazeti yaliyokuwa yakipitishwa na mhudumu na kuanza kujisomea. Peter ambaye alikuwa pembeni yake alikuwa akijiburudisha na kahawa kuondoa baridi iliyokuwa ikipuliza kwa wakati huo kutokana na viyoyozi vilivyokuwa vimewashwa katika ndege pamoja na hali ya hewa ya mji huo kabla ya kuanza kwa safari.
“Bwana Peter, ona kitu nilichokuwa namwonyesha Odoyo. Kumbe Van Persie alifunga magoli yote peke yake na kuifanya timu yake kutangazwa mabingwa wa Uingereza. Alifunga magoli matatu. Ona hapa anashangilia. Nilimwambia Odoyo nampenda sana huyu mchezaji na hasa kwa sababu anacheza kwenye timu ninayoipenda.”
“Aah, ni mchezaji mzuri sana huyu, hata timu yake ya taifa anafanya vizuri pia.” Peter alikubaliana na mzee Ambrose kwa kuunga mkono kauli yake.
Muda ulizidi kwenda huku wakibadili ndege pamoja na anga za nchi mbalimbali. Mzee Ambrose alijisikia yuko nyumbani baada ya kuona yuko katika anga la Afrika. Safari hii ndege ilikuwa inatua katika Uwanja wa Ndege wa Jomo Kenyatta wa nchini Kenya. Alihisi yupo Tanzania kwani alijua saa mbili haziishi atakuwa ameshawasili Uwanja wa Ndege wa Mwalimu Nyerere.
*****
Mlima Kilimanjaro ulioonekana kwa mbali wakati ndege ikiwa juu ulimfanya mzee Ambrose atabasamu kila mara. Peter alimwona akichungulia nje kupitia kioo cha ndege huku nakitabasamu. Lijua kuwa mzee Ambrose alikuwa ana hamu sana ya kufika nyumbani. hakumsemesha bali aliegemea na kujipumzisha kwa muda mfupi uliobakia kabla ya ndege kufika uwanja.
Saa tatu asubuhi ndege ilikuwa Uwanja wa Ndege wa Mwalimu Julius Nyerere. Mhudumu aliwatangazia abiria wote kwamba walikuwa wamefika salama na hivyo wanaweza kuteremka. Watu walikuwa wengi sana sehemu ya mapokezi wakiwasubiri ndugu zao waliowasili hapo.
Mercy akiwa mwenye furaha kubwa alikuwa amesimama pamoja na watoto wake wakimsubiri mzee Ambrose, mume wake. Hancy mtoto wa Ambrose pamoja na kuwa mdogo, ndiye aliyekuwa wa kwanza kumwona baba yake ambaye alikuwa amebeba mabegi mawili madogo huku mabegi mengine yakiletwa na toroli lililokuwa likisukumwa na mhudumu wa uwanjani hapo.
“Mamy, Baba yuleee,” mama yake alimshangaa sana Hancy kwani wote hawakuwa wamemwona kutokana na wingi wa watu waliokuwa wakiwalaki ndugu zao. Aliwaza pengine amemfananisha, Hancy alichoropoka na kupita katikati ya watu hadi kumfikia mzee Ambrose huku akimwita kwa sauti kubwa, babaa! babaa!
“Hancy mwanangu,” mzee Ambrose aliweka mabegi yake chini na kumnyanyua Hancy juu. “Umenionaje mwanangu,… mama yuko wapi?” ghafla alishangaa wote wamefika na kumzunguka. Kwa furaha aliwakumbatia kila mmoja. Walifurahi sana.
Magari mawili ya kifahari yalikuwa yamepaki yakimsubiri mzee Ambrose na familia yake. Chriss ambaye ndiye mtoto wa kwanza wa mzee Ambrose aliendesha Hummer gari la familia yao na Richard, dereva wa nyumbani aliendesha Range Rover nyeusi iliyowabeba ndugu wengine wa mzee Ambrose kama dada yake na wadogo zake wengine pamoja na ndugu wa upande wa mama.
Mzee Ambrose aliangana na Peter ambaye naye alikuwa amefuatwa na gari. Yeye hakulakiwa sana kama ilivyo kwa mzee Ambrose kwani mara nyingi alikuwa akirudi nchini wakati mzee Ambrose akiwa Uholanzi. Hivyo alishazoea kwenda na kurudi mara kwa mara.
Walianza kuondoka na kuelekea nyumbani maeneo ya Tabata Makuburi. Watu wengi walishangaa magari hayo ambayo yalikuwa yamepambwa vizuri na yaliyokuwa masafi. Baadhi ya watu walijua ni harusi iliyokuwa ikisindikizwa na magari mengine ambayo yalikuwa yakifuatana na msafara huo.
Kila mmoja alikuwa na furaha ndani ya gari. Furaha ya kumpokea mzee Ambrose. Mzee Ambrose alikuwa mwenye furaha sana huku akiwa amempakata Hancy.
Magari yaliingia ndani na watu kuteremka. Ilikuwa ni kama mshangao mkubwa sana kwa mzee Ambrose ambaye hakuamini macho yake kwa alichokiona katika nyumba yake. Alimwangalia kila mtu pasipo kuamini kile kinachoendelea siku hiyo katika jumba lake la kifahari.
Sherehe kubwa ilikuwa imeandaliwa siku hiyo. Wageni wengi walikuwa wamealikwa kwa ajili ya kumkaribisha tena nyumbani mzee Ambrose. Meza zilichafuka kila aina ya vinywaji ambapo wahudumu wa hoteli kubwa walipewa tenda kwa ajili ya kuhudumia katika sherehe hiyo. Zilitolewa zawadi mbalimbali kwa mzee Ambrose pamoja na yeye kuwapa watu zawadi alizokuja nazo kutoka Uholanzi.
Ilikuwa ni siku ambayo kwake hakuitarajia baada ya kuwa na hamu kubwa sana ya kuiona familia yake baada ya kutengana nayo kwa kipindi cha mwaka mmoja.
Peter alijumuika jioni yake baada yam zee Ambrose kumwalika pamoja na familia yake.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Ni vizuri tukajumuika pamoja Peter kwenye hii sherehe niliyoikuta hapa. Nadhani ni yakwetu sote. Njoo na familia yako.”
“Bila shaka,” alijibu Peter kabla yam zee Ambrose kuata simu na kuendelea na sherehe huku akiwasubiri.
Sasa alikuwa akiiteremsha miwani yake sawa sawa ili aweze kuona vizuri sura yam zee Ambrose. Akiwa ameegemea gari lake aina ya Toyota Harrier, alionekana akitamani kucheka kicheko cha kejeli na dharau.
Siku hiyo aliiona ni siku ya kupendeza sana kwake. Aliwaangalia ndugu zake mzee Ambrose ambao walikuwa na furaha sana wakimkaribisha mtu wao ndani. Aliangaza kila mahali kuahakikisha hakuna aliyemwona.
Akiwa ni mwenye furaha tele huku akijipulizia taratibu moshi wa sigara toka kinywani alikuwa akifuatilia kwa karibu zaidi moja baada ya lingine lililokuwa likiendele kuanzia mapokezi mpaka sherehe iliyokuwa ndiyo kwanza imeanza katika jumba la mzee Ambrose.
Midomo yake ilipatwa na hamu. Siyo hamu ya chakula bali hamu ya utajiri. Aliitoa sigara yake mdomoni na kuiwasha na kuilamba midomo yake na kisha kuingia ndani ya gari lake na kuondoka.
Njiani aliwapigia watu wake simu ili wakutane mara moja wito ambao uliitikiwa na kila mmoja John, Chacha, Baltazar, Bwigire na Shebby. Ni katika ukumbi wa starehe wa Maisha ambapo mara nyingi walikuwa wakikutana kwa ajili ya mipango yao.
“Nadhani tumejionea wenyewe, hizo ni baadhi ya picha ambazo niliweza kuzipiga kuanzia wakitoka uwanja wa ndege hadi nyumbani. hakuna aliyeniona nikifanya kazi yangu na wala sikupenda niwasumbue mje kwani najua kila mtu alihitaji kupumzika na ndio maana mmeweza kufika hapa mara moja.
Safi sana. Mambo yatakuwa mazuri, hakuna ubishi, kila mmoja ana hamu na utajiri, au siyo washkaji zangu?” alihoji Deo huku asikilizwa kwa makini sana.
“Kweli mkuu, hatushindwi kitu pale, labda tuwe wajinga.”
“Alright, hapo ndipo nnapokupendea kamanda wangu,” Deo alimjibu Chacha ambaye alionyesha kuwa na hamu kweli na utajiri kwa kauli alizosema Deo huku wenzake wakitikisa vichwa kuonyesha kwamba wapo pamoja na yaliyosemwa.
“Ndiyo wakati huu mkuu.”
“Sasa, pale kwake leo kuna sherehe. Sherehe kubwa tu tena hadi sasa inaendelea nadhani wanakesha,” alisisitiza huku akinyanyua glasi yake ya mvinyo na kuiweka tayari kuimimina mdomoni. Miwani yake meusi ilimfanya asionekane macho kwani tofauti na siku nyingine, siku hiyo walikuwa wamekutana jioni saa kumi na moja mara tu baada ya kuondoka nyumbani kwa mzee Ambrose.
Aliwaangalia wote. Akakumbuka maneno ya Chacha aliyoyasema muda mfupi uliopita, ‘Kweli mkuu, hatushindwi kitu pale, labda tuwe wajinga’.
“Chacha, itabidi uhudhurie hiyo sherehe hadi ujue ni nini kitaendelea maana najua ni lazima wataongelea maendeleo yake pamoja na nyumbani.tuchangamkeni jamani,” alisema Deo huku akitabasamu.
“Ndiyo, bosi Deo,” aliitikia Chacha kwa furaha akiijibu ile furaha aliyoionyesha Deo baada ya kumteua yeye kwenda kufatilia. Alijua hiyo ni njia ya kuonyesha uaminifu kwa bosi wake huyo ambaye kwa kpindi chote walichokuwa naye alikuwa akiwatajirisha kwa kuhakikisha anawagawia vizuri mali watakazofanikiwa kuzipata.
“Basi we ungetangulia kujua alafu utatujulisha ukifanikisha na tutapanga tukutane tena ili tujue tunaanzaje, Sidhani kama pesa alizokuja nazo atakuwa ameziweka benki maana mpaka akazibadilishe ndipo aweze kuziweka.”
“siyo wazee wote wajanja mkuu, hizo bado amezishikilia mwenyewe…. Inaonekana bado hajaiamini benki. Wazee wanapenda makuu hata kama wamezoea hela… hizo ni zetu,” alisema John ambaye aliongea huku akipuliza nje moshi wa sigara aliyokuwa akiivuta.
“Nitahakikisha najua yote bosi. Nitatumia mbinu zangu zote kufanikisha hilo,” Chacha alisema huku akimwangalia Deo kuashiria yuko tayari kwa kazi. Na ambaye hakuonyuesha dalili zozote za utani ndani yake.
“Sawa, wewe nenda, nadhani unakiasi cha kutosha kufanikisha kazi yako.”
“Ndiyo mkuu, niko tayari. Nawaacha kwa muda,” Chacha alisema huku akisimama kutoka juu ya meza aliyokuwa ameikalia na kulifuata gari lake.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Kazi njema…. Sisi wakati tunamsubiri Chacha nadhani ni muda wa kwenda kujinoa na kuwa tayari kwa lolote, kila mmoja akafikirie juu ya hizo Dola za wazungu. Maisha yanakuja,” Deo alisema huku akionekana mwenye furaha na aliyecheka wakati wote.
“Kweli Bosi Deo,” wote waliitikia na kumalizia vinywaji vyao.
*****
Nyumbani kwa mzee Ambrose mambo yalikuwa yakienda vizuri, watu waliendelea kula na kunywa. Ni katika hatua za mwisho za kutoa maneno machache ndipo Chacha alikuwa amefika ndani ya uzio wa nyumba ya mzee Ambrose. Alibahatika kuyasikia.
Baada ya kumaliza kuongea mzee Ambrose alimnyanyua Hancyna kumrusharusha juu kisha alimwachia na kumwelekeza akamfuate paka wake ambaye alikuwa amejilaza juu ya ubao pembeni ya ukuta wa nyumba ile. Hancy alikuwa na umri wa miaka minne. Alimkimbilia paka wake. Ghafla alirudi alipo baba yake na kutulia.
“Paka yuko wapi Hancy,” alihoji baba yake huku akimnyanyua kwa lengo la kumbeba tena.
“Amekimbia.” Watu walicheka kwa kauli aliyoitoa Hancy ambaye alikuwa akihema kama vile alihofia kitu fulani.
Chacha alikuwa ameshatoka nyumbani kwa mzee Ambrose. Alihofia kama atakuwa ameonwa na mtu yeyote. Alitembea haraka na kuingia ndani ya gari lake alilolipaki mbali kidogo na nyumba ya mzee Ambrose. Alipiga gari lake moto na kutokomea. Akiwa maeneo ya River Side, Chacha alitoa simu yake na kuzungumza na Deo.
“Haloo, Bosi Deo, huku mambo nmekamilisha.”
“Sawa Chacha, unaweza kwenda kulala, tutakutana kesho asubuhi.”
“Sawa bosi.”
Chacha alikuwa anakaa maeneo ya Magomeni. Alikata na kuianza barabara ya Morogoro hadi alipofika Magomeni nyumbani kwake na kujipumzisha.
Huku kwa Deo, aliwasiliana na wenzake na kupanga kesho yake wakutane mapema asubuhi. Ilikuwa ni ili kupanga namna watakavyoivamia nyumba ya mzee Ambrose. Alimweleza kila mmoja na kukubaliana wakutane jioni wakiwa tayari tayari.
*****
Asubuhi baada ya sherehe kuisha jana yake. Nyumbani kwa mzee Ambrose palikuwa pametuli. Watu walikuwa bado hawajaamka kutokana na uchovu wa kusakata rumba na kusherehekea ujio wa mzee Ambrose ambaye yeye hakuchoka sana kwani alikuwa mtulivu wakati wote akizungumza na mmoja baada ya wengine waliopenda kumhoji maswali juu ya safari yake.
Baada ya wengine kuondoka usiku huo wengine walibaki na kulala hapo hadi kesho yake. Ukubwa wa jumba la mzee Ambrose ulimeza watu wengi waliofika siku hiyo.
Asubuhi hiyo Hancy alikuwa wa kwanza kuamka. Alitoka na kwenda hadi sehemu ambayo alimwacha paka wake usiku wa jana ambao huwa anamwacha hapo kila siku ikiwa ni sehemu ya paka wake huyo pa kulalia.. Ni sehemu hiyo hiyo katika geti dogo la kutokea nje alimwona mtu akipita kwa kasi hali iliyomwogopesha sana Hancy hadi akakimbia kwa baba yake.
Mzee Ambrose alitoka na kumkuta Hancy kwa mwenyewe nje ya geti. Alimfuata na kumchukua na kurudi naye ndani huku akiwa amembeba na kumrusharusha juu huku wakicheka. Wakati wote mzee Ambrose alikuwa na furaha kwa kuwa na familia yake karibu.
Maisha yaliendelea kama kawaida, kila siku jioni mzee Ambrose alikaa na familia yake na kuzungumza juu ya maendeleo yao, walifurahia sana kuwa pamoja kila wakati. Walikaa na kunywa pamoja na kula.Wageni mbalimbali walifika kwake kumpongeza nakuisalimia familia yake.
Peter ambaye alikuwa ameungana na mzee Ambrose na kumsapoti kwa kila jambo. Alifurahia sana kuona urafiki wao unavyomarika kila siku. Hasa ni kwa mwaliko ambao aliupata jana yake kutoka kwa mzee Ambrose. Alikumbuka mengi.
Alikumbuka walivyokuwa Uholanzi na mambo mengine waliyoyafanya huko. Walizunguka sehemu nyingi pamoja. Akimwonyesha mzee Ambrose sehemu muhimu za kihistoria ambazo alijua zitamvutia sana.
Hata familia zao ziliungana wakiwa Tanzania na kuishi kwa upendo na ushirikiano. Chris na Justin nao walikuwa wakitembeleana. Yote hiyo ni kwa sababu ya urafiki wa wazee wao. Walitoka pamoja mwisho wa wiki na kurudi pamoja. Wengi wa marafiki zao walijua ni ndugu hata kama si wa kuzaliwa pamoja.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Naomi na Marry pamoja na mama yao Mercy nao walikuwa wakishinda nyumbani kwa Peter siku za mwisho wa wiki au watoto wa kike wa Peter, Juliana na Michelle pamoja na mama yao Vicy wangeenda kushinda nyumbani kwa mzee Ambrose hata kama wazee wangekuwa mbali na nyumbani. Haikuwa rahisi kwa watoto wao kugombana zaidi ya kutaniana.
Hancy ambaye alikuwa mdogo, mtoto wa mwisho wa mzee Ambrose yeye alikuwa akipenda kucheza na dada zake na wakati mwingine mama yake. Watoto wote wa Peter walikuwa wakubwa tofaut na Hancy ambaye ndiye pekee aliyekuwa na umri mdogo katika familia ya mzee Ambrose.
Ni familia zilizolandana namna ya maisha. Kila kitu wangefanya pamoja ambacho kilihitajika kushirikiana.
*****
Woga ulimwingia kila mmoja usiku huo. Hakuna aliyeamini juu ya kilichotokea. Mwanga wa tochi kubwa ndiyo uliangaza huku kukisikika sauti za watu wakilia kwa maumivu makali yaliyopelekea kimya kingine kilichotawala nyumba ya mzee Ambrose.
Alirudi nyuma na kukimbilia chumbani kwao ambako napo alikuta yaleyale aliyoyaacha sebuleni. Ghafla, Hancy alikuwa katika uvungu wa kitanda. Hakuweza kutoka mle ndani tena. Alipatwa na hofu. Aliogopa sana. Alishuhudia damu ikitiririka kuelekea uvunguni mwa kitanda. Aliogopa sana. Hakuweza kupiga kelele wala hakuweza tena kuhema kwa hofu iliyomkamata. Ghafla tena alisikia sauti za watu wakikimbia. Hakutoka kwenda kuangalia.
Baada ya muda wa dakika 15, kimya kilikuwa kikubwa, Hancy alitoka ufunguni mwa kitanda na kusimama, alipapasa na kushika damu ambayo ilikuwa ikielekea sehemu aliyokuwa amejificha. Ni giza tu ndilo lililokuwa limetanda chumbani kwake. Alilia kwa woga. Hakujua afanye nini. Alitembea huku akipapasa ukutani hadi alipofanikiwa kushika kitasa cha mlango. Alifika katika sebule yao kubwa, nako kulikuwa na kiza kikubwa kama alipopaacha mwanzo. Hakuweza kutoa mapazia kwani yalikuwa ni makubwa na hivyo asingeyaweza na yeye alikuwa ni mdogo. Kazi hiyo ilikuwa ni ya wafanyakazi wa ndani wa familia yao. Ambao nao hawakusikika wakimpa amri Hancy ya kuleta tochi kama ilivyo kawaida yake.
Alikimbilia tochi iliyokuwa juu ya kabati na kuiwasha. Mara nyingi umeme ukikatika kwao, yeye ndiye angekuwa wa kwanza kukimbilia tochi na kuiwasha kisha amkabidhi yeyote aliye karibu. Walimwacha kwani alikuwa ni mtoto na wasingeweza kumzuia kuiwasha. Hiyo ikawa kama kazi yake pindi umeme unapokatika.
Alimulika. Alikutana na miili iliyolala chini. Aliona damu ikiwa imetapakaa kila mahali, aliita ‘baba…mama, aliita tena na tena.
Hakujibiwa. Aliita dada Naomi….dada Marry….hakuna aliyeitikia. Aliita kaka Chris, kaka Chris…lakini hata yeye hakuitika, alimulika pasipo kumwona. Alijua alimuacha chumbani kwao ambako walikuwa wakilala pamoja. Alielekea chumbani, alimulika na kumwona Chris amelala chini kifudifudi, alijaribu kumgeuza lakini hakuitikia pindi alipomwita.
Alikosa msaada kwa wote ambao jana walikuwa wakifurahia na kukimbizana pamoja na baba yake mzee Ambrose. Usiku huo palikuwa kimya kama siku nyingine akishtuka wakati wenzake wakiwa wamelala.
Hancy alilia kwa kwikwi, alijua watu walioingia ndani usiku ndiyo
waliowakata ndugu zake. Alitoka nje ili kuwaita walinzi. Alikuta ni vilevile kama alivyoacha ndani. Walinzi wote watatu walikuwa wamelala chini.Walikuwa wamekufa. Mbwa na paka wake pia walikuwa wamelala. Hancy aliogopa sana. alirudi ndani na kujaribu kuita tena kila aliyemmulika na tochi. Alimfuata mzee Ambrose na kuita tena na tena. Hakuitika. Usingizi ulimpitia Hancy akiwa juu ya mwili wa mama yake.
*****
Mamaaa, mamaa…. Hancy alipiga kelele huku akiita. Hakujua alipokuwa. Hancy alikuwa amebebwa na askari polisi wa kike. Alijua amebebwa na mama yake. Ndoto ya ajabu ndiyo iliyomfanya apige kelele. Aliweweseka kifuani kwa yule askari polisi. Yule askari alimwonea huruma sana Hancy.
“Mtoto pekee yake ndo amebaki?” aliwaza huku akijiuliza.
“Mchukue mpeleke kwenye gari,” yule askari alimwambia mwenzake huku akimkabidhi Hancy ili ampeleke kwenye gari.
Watu walikuwa wengi sana asubuhi hiyo, polisi na viongozi mbalimbali walifika baada ya kupata taarifa za mauaji nyumbani kwa mzee Ambrose.
Hakuna aliyeamini. Wengi walijua ni njama zimepangwa kwani
ilisikika taarifa ya kuuliwa na kuibiwa kwa kiasi kikubwa cha fedha za mzee Ambrose. Walifanya njama hizo hawakujulikana huku polisi wakisema ya kwamba uchunguzi utafanyika ili kuwabaini wahusika na kuwachukulia hatua za kisheria.
Jiji zima lilipooza kutokana na taarifa hizo huku vikundi mbalimbali vikiwa vinajadili juu ya kiasi hicho kikubwa cha pesa ambacho kiliibwa.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Wengine walikuwa wakimjadili Hancy, mtoto pekee wa mzee Ambrose ambaye alikuwa amepona wakati wa mauaji hayo.
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment