Simulizi : Usiku Wa Manane
Sehemu Ya Pili (2)
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Watu walikuwa wengi sana asubuhi hiyo, polisi na viongozi mbalimbali walifika baada ya kupata taarifa za mauaji nyumbani kwa mzee Ambrose.
Hakuna aliyeamini. Wengi walijua ni njama zimepangwa kwani
ilisikika taarifa ya kuuliwa na kuibiwa kwa kiasi kikubwa cha fedha za mzee Ambrose. Walifanya njama hizo hawakujulikana huku polisi wakisema ya kwamba uchunguzi utafanyika ili kuwabaini wahusika na kuwachukulia hatua za kisheria.
Jiji zima lilipooza kutokana na taarifa hizo huku vikundi mbalimbali vikiwa vinajadili juu ya kiasi hicho kikubwa cha pesa ambacho kiliibwa.
Wengine walikuwa wakimjadili Hancy, mtoto pekee wa mzee Ambrose ambaye alikuwa amepona wakati wa mauaji hayo.
*****
Peter wazo la kufanya makubwa na mzee Ambrose ni moja ya mambo ambayo aliyapa kipaumbele katika kichwa chake. Alitabasamu kila alipogundua ya kwamba mzee Ambrose anaheshimika sana na kwamba amekuwa rafiki yake mkubwa sana.
Ni siku ambayo, Peter rafiki yake mzee Ambrose alikuwa amepanga kufika nyumbani kwa mzee Ambrose. Hakutaka kuliacha suala hilo la biashara lichukue muda kwani likizo yake ya wiki mbili ingeisha bila ya kufanya chochote. Hivyo aliamka mapema kwa ajili kwanza ya mazoezi kabla ya kuoga na kupata chochote.
Alipenda sana kusikiliza redio yake asubuhi pindi aamkapo. Na siku zote hakupitwa na taarifa ya habari ya saa moja kamili asubuhi. Siku hiyo taarifa ya habari ilikuwa tofauti sana na zile alizozisikiliza kwa vipindi vyote ambavyoamekuwa msikilizaji wa redio hasa kipindi cha taarifa ya habari. Habari ambayo hakuitambua na wala hakuamini masikio yake ambapo alikuwa amesimama akiduwa bila ya kujua afanye nini wakati huo. Taarifa hiyo iliingia katikati ya habari zikitokea eneo la tukio.
“...Habari za kusikitisha zilizotufikia hivi punde….. mtoto wa miaka minne amenusurka kufa na wengine kumi na moja wanaripotiwa kufa baada ya kuvamiwa na watu wasiofahamika nyumbani kwao Tabata Makuburi. Watu hao ni wa familia moja ya mfanyabiashara maarufu mzee Ambrose Seduke. Mzee Ambrose pamoja na familia yake walikutwa wakiwa wamekufa mnamo asubuhi baada ya raia mmoja kukuta miili ya walinzi wawili waliokuwa wakilinda nyumba hiyo ikiwa imejaa damu na kutoa taarifa polisi. Miili ya maiti hao imepelekwa katika Hospitali ya Muhimbili kuhifadhiwa kwa ajili ya kupisha uchunguzi. Mtoto aliyenusurika kufa ni mtoto wa mwisho wa mzee Ambrose. Inasemekana kuwa mauaji hayo yalitokea saa nane kamili Usiku.”
Habari hizo hazikumwingia kabisa Peter. Hakuamini tenba na tena. Alizunguka huku na huko akizitafakari. Aliiangalia redeio yake kubwa aina ya SONY WEGA pasipo kuamini. Chai haikunyweka tena.
“Justin,” aliita kwa nguvu. Kisha akamfata katika chumba alichukua amelala. Haraka alimwamsha Justin ili ampeleke Hospitali ya Muhimbili kuhakikisha alichokisikia kwenye taarifa ya habari.
“Justin…amka…n’taka kwenda Muhimbili Hospital sasa hivi…vaa haraka unipeleke..” Peter aliongea kwa sauti ya juu kumwamsha Justin. Sauti hiyo iliwaamsha wote waliokuwa wamella nyumbani kwake. “Haraka hata usioge,” alifoka tena Peter huku Justin akilitoa shuka alilokuwa amejifunika.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Justin hakumwelewa baba yake kwa nini siku hiyo amekuwa hivyo. Aliteremka haraka na kuvaa shati lake pamoja na suruali. Siku zote baba yake huwa hawai kutoka nyumbani. Justin baada ya kusikia hospitali alifanya upesi na kutoa gari nje na kuanza safari ya kuelekea Muhimbili.
Baada ya nusu saa, Peter na Justin walikuwa Muhimbili. Wingi wa watu katika hospitali hiyo ulimwogopesha Justin.
“Baba kuna nini hapa leo?” aliuliza Justin. Lakini Peter hakumjibu lolote. Walielekea moja kwa moja hadi katika chumba cha kuhifadhia maiti na kujitambulisha. Hakukuwa na pingamizi lolote kwani hata baadhi ya watu walikuwa wakiruhusiwa kuingia kuwaangalia kwani kabla ya Peter hakukuwa na ndugu yeyote aliyefika hapo. Msimamizi aliwaruhusu kuingia na kujionea miili ya marehemu ikiwa ndani ya jokofu. Peter aliinamisha kichwa chini.
“Baba Ambrose!” Justin alishtuka baada ya kuuona mwili wa mzee Ambrose baada ya Peter kuufunua ili kuuangalia. Hakuamini macho yake.
“Baba, wameuliwa wote?”
“Hapana, Hancy kabaki,” alisema Peter huku machozi yakimtoka.
Watu walikuwa wengi nje.hakuna aliyeamini juu ya tukio lile. Kila mmoja alizungumza lake hapo hospitali.
*****
Ndugu wa marehemu wakisaidiana na Peter walifanikisha mazishi ya marehemu wote kumi na moja. Wote kwa pamoja walizikwa katika shamba kubwa lililokuwa nyumbani kwa mzee Ambrose. Hancy alichukuliwa na mjomba wake aliyekuwa akiishi Magomeni Mapipa.
Huku akiwa kwa mjomba wake, Peter aliahidi kumlea na kumwendeleza kimasomo kama alivyokuwa akifanya baba yake. Suala hilo liliafikiwa a mjomba wake Hancy ambaye kwa kipato chake asingewza mwenyewe kufanikisha hayo huku akiwa na familia kubwa nyumbani kwake.
Aligundua ya kwamba Mzee Ambrose mbaye pia alikuwa akimtegemea alikuwa karibu sana na Peter na hivyo kwa Peter kumchukua Hancy itakuwa ni sahihi kwani familia hizo mbili zilikuwqa kitu kimoja.
Ndugu wa familia walikubaliana na Peter na hivyo wakati mwingine Hancy alikuwa akiishi nyumbani kwa Peter kabla ya kuhamia moja kwa moja na kupazoea. Justin alikuwa akimpeleka shule na kumrudisha kila siku na hivyo mjomba wake alionelea Hancy akae tu nyumbani kwa Peter hata pale Peter alipokuwa akisafiri kurudi katika shughuli zake nchini Uholanzi. Hancy akahamia kabisa.
Wakati mwingine Peter alimpeleka Hancy Uholanzi kipindi cha likizo ya shule ili kumfanya asahau kwani mara nyingi alikumbuka na kulia. Peter alishangaa kuona mtoto mdogo akilia kila siku kwa kuwakumbuka wazazi wake na ndugu zake.
“Baba Justin, bora ukakae naye huko huko Uholanzi ukija uje naye ili asahau mazingira ya huku kwani yanampa tabu sana. kila siku ye ni kulia tu,” Vicky mke wa Peter alisema huku Justin akitikisa kichwa kuonyesha kukubaliana na wazo la mama yake ambaye likuwa amembeba Hancy aliyekuwa akilia.
“Kweli,” aliitikia Peter. Nitakwenda naye. Najua akipata kupazoea kule na akikutana na watoto wa kule atasahau. Basi wiki ijayo nitaondoka naye.
Hancy hakuelewa chochote. Akiwa amesimama karibu na geti, alimwona mtoto mdogo wa kike akiwa anakuja karibu na geti lile. Alikuwa akimwangalia sana Hancy. Alifika na kumsemesa Hancy ambaye alikuwa akizidi kumwangalia.
“Njoo tukacheze,” alisema yule mtoto. Hancy alirudi nyuma na kumkimbilia Justin ambaye alikuwa akifuta gari.
“Nini Hancy,” alisema Justin huku akimbeba Hancy. Alimwona yule mtoto akiwa amesimama kwenye geti.
“Fina!” aliita Justin huku akielekea katika geti kumfungulia Fina geti huku akiwa amembeba Hncy.
“Twende tukamfungulie mchumba! Alisema Justin akimwambia Hancy ambaye alikuwa hajui lolote.
“Karibu Fina. Umemwona mchumba… haya Hancy shuka chini ucheze na mchumba ako,” Justin alisema huku akimshusha Hancy chini na kumuunganisha na Fina ili wacheze pamoja. Haikuwachukua muda Hancy na Fina wakaanza kuzoeana na kucheza pamoja. Walikimbizana na kuchezea vitu mbalimbali huku wakifurahia.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Hancy akawa na furaha kila alipokuja Fina nyumbani kwao na kucheza naye. Ikawa furaha pia kwa Fina ambaye alipenda sana kucheza na Hancy pindi aliporudi kutoka shule ya awali aliyokuwa akisoma hata baada ya Hancy kuhamia Uholanzi alikopelekwa na Peter.
Akiwa huko nchini Uholanzi, Hancy alijifunza kuchora. Alipenda sana kuchukua karatasi za Peter na kujichorea chochote alichokipenda. Alipenda sana kuchora picha za watu. Aliwachora wazungu kwa mwonekano wa pua ndefu. Picha hizo zilimfanya Peter acheke sana alipoziona. Alimsifia sana Hancy kwa usanii wake huo akiwa bado na umri mdogo.
“Wewe ni mchoraji mzuri sana,” alisema Peter akimsifia Hancy baada ya kuziona picha alizozichora.
Usiku Hancy akiwa amelala, aliota ndoto ambayo ilimkumbusha siku alivyoshuhudia ndugu zake wakikatwakatwa na mapanga na kuchomwa kwa visu. Alishtuka sana kutoka usingizini na kuita kwa nguvu….’maaamaaa, baaaabaa’. Peter alikimbilia chumba alichukuwa amelala Hancy na kumwangalia. Alimkuta akilia sana na kumuuliza.
“Mwanangu Hancy, kuna nini?” Hancy alizidi kulia huku akiendelea kuita baabaa…maamaa…. Peter alimchukua na kuelekea naye katika chumba alichokuwa amelala yeye.
Asubuhi alimuamsha. Hancy alikuwa amepoa. Hakuwa na wasiwasi wowote. Peter alimwona akiwa na furaha, alifurahi baada ya kumwona akivaa viatu vyake huku kawek picha zake pembeni.
Baada ya matayarisho ypte asubuhi hiyo, kama kawaida alikwenda naye ofisini kwake. Hakukuwa na mtu ambaye angebaki na Hancy nyumbani na hivyo Peter alikuwa akienda kushinda naye ofisini kwake. Hancy alikuwa ameshasahau juu ya alichokiota wakati akiwa ofisini kwa Peter. Peter alimwona akiwa anataka kuanza kuchora akamsemesha.
“Hancy, leo napenda uchore picha ya watu wa kule nyumbani… kila siku we unachora tu wazungu. Leo wachore na watu wa kule nyumbani.” hancy alicheka huku akimuata Peter na kumwangalia usoni huku akimsikiliza.
“Leo uchore vizuuuri afu nitakupa zawadi.”
“Sawa baba,” Hancy aliitikia na hapohapo alianza kujichorea watu wake mbalimbali ili amwonyeshe Peter. Hakuwa na uwezo wa kuchanganya rangi hivyo alichora tu kwa kutumia penseli ambayo alipewa na Peter.
“Hujamaliza tu, nataka nione jinsi unavyojua kuchora.”
“Tayari baba,” Hancy alinyanyuka na kwenda kumwonyesha Peter picha alizokuwa amezichora kama alivyoagizwa. Alitumia dakika kama thelathini kukamilisha michoro yake. Jambo hilo lilimshangaza sana Peter kuona kawachora watu wengi katika karatasi moja na wakionekana ni watu kweli. Peter alivutika kwa kipaji alichonacho Hancy.
“Mmh, Safi sana, mtoto unajua sana kuchora. Hawa watu kama vile wa kule nyumbani… mimi nilijua unajua kuchora tu wazungu…. Hapa sasa unatakiwa uende shule ukajifunze zaidi.”
Peter alifikiria kwa kipindi hicho angempeleka Hancy katika shule za awali za nchini Uholanzi. Alijua Hancy anacho kipaji na hivyo ingekuwa ni vizuri kama angemwendeleza ili asije akapoteza kipaji chake. Huko Uholanzi Peter alikuwa anaishi katika kitongoji cha De Wallen.
*****
Hancy alianza shule ya awali. Alikutana na wanafunzi wenzake ambao nao walikuwa wanapenda sana kuchora. Alikutana na Van Brussel. Mwanafunzi ambaye alikuwa mdogo lakini alikuwa na kipaji cha kuchora cha hali ya juu. Hancy alimshangaa sana hasa baada ya kuona baadhi ya picha zake alizokuwa amezichora. Van Brussel alichora picha ya ramani ya nchi yao pamoja na wazazi wake na ndugu zake.
Pia alichora picha za wadudu na wanyama mbalimbali. Hancy alitamani sana awe kama yeye. Alipenda sana kukaa karibu naye ili wawe marafiki wakubwa. Aliweza kumchora mtu kwa kumwangalia tu sura yake na kumtoa kama alivyo.
“Nani aliyekufundisha kuchora hivi?” Hancy alimuuliza Van Brussel ambaye alikuwa akiangalia picha za Hancy huku akimwangalia Hancy. Hakuona utofauti mkubwa kati ya picha zake na picha za Hancy. Alizitamani sana picha za Hancy hasa bada ya kuangalia picha alizowachora watu weusi.
Alitamani Hancy na yeye azione picha zake ambazo alichora kama yeye. Aliikumbuka picha ambayo aliwachora watu weusi ambao wanafanana na wa kwenye picha ya Hancy.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Nimejifunza mwenyewe Hancy, twende ukaone na mimi nimechora watu weusi.” Hancy aliongozana naye hadi katika begi la Van Brussel. Alilifungua na kutoa picha ambayo Hancy baada ya kuiona alishtuka kidogo. Alikosa raha.
Taswira ya kitu cha kutisha ikaja mbele yake. Aliogopa. lakini alijikaza na kuendelea kuongea na Van Brussel. Kwanza alijiuliza juu ya kufanana kwa sura zilizokuwa katika picha yake na picha ya Van Brussel. Alisitasita kuongea na mwishowe akamwambia Van Brussel.
“Unajua kuchora sana Brussel. Napenda kuwa kama wewe. Hao ni kina nani?” alimhoji Hancy juu ya watu wale kwani hakuona watu weusi wengi katika nchi hiyo zaidi ya baadhi ya rafiki zake Peter wawili ambao amewazoea.
“Nilikuwa Tanzania na mama yangu, tulikuwa tunakunywa juice sehemu nikawa nawaangalia hawa watu nikawachora. Nimechora vizuri Hancy?”
“Tanzania?” Hancy alishtuka aliposikia Van Brussel alikuwa Tanzania.
“Ndiyo Hancy, wewe unatokea Tanzania?” Van Brussel alimhoji Hancy ambaye alikuwa ameduwaa akizitazama zile picha. Sura taswira ilimjia kichwani na kuanza kulia. Alikumbuka picha alizozichora. Alizitazama tena akizilinganisha na picha za Van Brussel. Aliona kama ni ile ndoto inamjia tena siku aliyoiota na kuchukuliwa na Peter kwenda kulala naye.
“Ndiyo, mimi natokea Tanzania na huku niko na baba angu, anaitwa Peter.” Hancy aliondoka na kuelekea kwenye gari tayari kuelekea nyumbani. Alisahau kumrejeshea Van Brussel picha za wale watu.
“Hancy, picha yangu,” Van Brussel alikimbilia gari haraka kwa ajili ya kuchukua picha yake.
“Van…. naiomba. Nitakupa na mimi moja.”
“Haya ichukue, na wewe nipe ya kwako.” Hancy alitoa picha nzuri aliyomchora Peter na kumkabidhi.
“Nzuri sana,” Van Brussel alimwambia Hancy. Akafurahi na kukimbia kuelekea kwa wenzake ambao walikuwa wakielekea katika basi lingine lililokuwa likielekea kitongoji kingine cha Amsterdam.
Sasa alikuwa na picha mbili ambazo alizifananisha. Aliziangalia kila wakati na kuwaona watu wale wakiwa wanafanana sana. moja ikiwa kaichora yeye mwenyewe na nyingine ameichora Van Brussel.
Alifika nyumbani na kuziweka zote katika begi lake. Mara kwa mara alihisi wale ndiyo wahusika wa vifo vya wazazi wake na ndugu zake. Alliwachukia. Aliwaona ndotoni. Kila sura iliyomtokea asubuhi alizifuata zile picha na kuziangalia. Aliiona sura ile ikiwa pale.
*****
Jiji la Amsterdam lilikuwa katika kipindi cha baridi sana. Jua halikuonekana kwa siku hiyo. Watu hawakuonekana mitaani wakitembea na badala yake walikaa nyumbani kwao na kuwasha moto na kukaa karibu na moto huo kwa ajili ya kuondoa baridi. Theluji ilikuwa ikiteremka nyingi huku maduka baadhi yakiwa yamefunikwa na theluji hiyo. Magari pia yaliyokuwa yameegeshwa kandokando ya barabara yalikuwa yamejaa theluji na mengine kuzibwa kabisa.
Akiwa amesimama nje ya duka kubwa la vifaa vya muziki pamoja na santuri za filamu tofauti tofauti. Hancy aliyekuwa amevalia koti kubwa lililomkinga na baridi alikumbuka filamu ambayo aliipenda ya ‘Before i self destruct’ ya msanii 50 Cent. Filamu hiyo ilimpa ujasiri kila alipoiangalia na kila alipokumbuka yaliyomtokea.
Ni katika kujilinda. Kujua mbinu na kujua mambo mengine yahusuyo maisha. Alipenda kuzitazama filamu mbalimbali zilizochezwa na watu wakionyesha ujasiri katika mapambano dhidi ya wadhalimu. Alisoma pia vitabu mbalimbali wakati akiwa chuo na hivyo kujua mengi.
Huko Uholanzi, aliogopewa kutokana na hasira zake za ghafla ambapo mara kwa mara alikuwa akipelekwa vituo vya polisi kutokana na kumjeruhi mtu. Ni mara mojha tu aliyokwenda katika klabu za usiku ambako huko zilitokea vurugu na kusababisha majeruhi wengi. Baadhi ya watu waliokuwepo huko walimsingizia ya kwamba yeye ndiye aliyeanzisha ugomvi na hivyo kupelekwa kituo cha polisi. Baada ya kujitetea aliachiwa huru.
Ni siku hiyo hiyo Hancy alicha kwenda klabu za usiku. Hakutoka tena hata pale marafiki zake walipomfuata waende.
Mpaka kipindi hiki ambacho amekuwa akielewa mambo mengi juu ya maisha na nini cha kufanya ndipo alifikiria kuishi mwenyewe. Hakutaka tena kumtegemea Peter ambaye alimwona kama baba yake mzazi licha ya kujua ukweli juu ya wazazi wake na ndugu zake.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Ni miaka kumi na tisa ilikuwa imepita. Hancy alimaliza masomo yake ya fani ya uchoraji na kompyuta. Alirudi Tanzania na kumwacha Peter akiwa bado anaendelea na kazi zake huko nchini Uholanzi. Sasa alikuwa na miaka ishirinu na mitano wakati Peter akionekana mzee zaidi ambaye alikuwa anakaribia hata kustaafu kazi yake ambayo amekuwa akiifanya kwa kipindi kirefu cha maisha yake.
Miaka mingi aliyoitumia kusoma nchini Uholanzi ilimfundisha mengi. Ujasiri na mbinu za kimaisha vilikuwa ni vitu ambavyo alivizingatia ikiwa ni pamoja na kufanya mazoezi ya kujiweka sawa kimwili na kiafya. Hilo lilimwongezea kujiamini.
Baada ya kuhamishia makazi yake nyumbani Tanzania, Hancy alikuwa na jambo moja tu la kufanya. Jambo ambalo alikaa nalo kichwani kwa kipindi chote hicho alichokuwa Uholanzi. Kupata sehemu na kuweza kufungua kmpuni yake ya masuala ya uchoraji. Japokuwa aliahidiwa na Peter lakini dhamira yake ya kuanza mwenyewe ilikuwa palepale.
Alikutana na wasanii wengine wa nchini na kubadilishana nao ujuzi. Aliangalia kazi zao na kufananisha na za kwake ili kuona ubora wa uchoraji wake.
Mmoja kati ya wasanii wa kuchora aliyekutana naye likuwa ni Athuman ‘Soo’. Alifahamika sana kwa kuchora katika mabango, makaratasi na hata miili ya watu ‘Tattoo’. Kama ilivyokuwa kwa Van Brussel kule Uholanzi. Rafiki yake Hancy waliyekuwa pamoja Uholanzi. Hancy alipenda kuona kazi za Athuman. Alizipenda sana na hivyo alikuwa akipita katika jengo lake na kuzikagua moja baada ya nyingine.
Alishtuka mara baada ya kuona karatasi nyingi nyeusi. Zilikuwa ni zenye michoro ya Tattoo. Alizichukua na kuanza kuziangalia. Tasiwra ya ajabu ilimjia usoni. Alibaki ameduwaa hadi Soo alipoingia na kumkuta akiziangalia zile picha. Ilikuwa kama kafanya kosa kwani hakuruhusu watu kuona michoro ya Tattoo kwani mengine ilikuwa ni siri za watu. Hancy alikuwa akiutazama sana mchoro mmoja wa tattoo iliyokuwa na alama ya nyoka aina ya Cobra ambao ni nyoka hatari sana.
Kumbukumbu ya alama Fulani ilimjia kichwani.Aliwaza kuhusu ilea lama.
"Hapana, sijakosea.Ndiyo hii hii,” Soo alimsikia, aliichukua ile karatasi huku Hancy akiwa bado ameduwaa.Alishtuka alipomwona Soo.
"Kaka, vipi…alafu siruhusu mtu kuingia katika hiki chumba, njoo huku,” Soo alimwambia Hancy. Hakumwelewa kwa hali aliyokuwa nayo.
“Samahani kaka,” Hancy alimwomba samahani Soo.
Inaelekea una kitu unawasa kaka, vipi.
“Hapana kaka, niko sawa. Naomba nikuache nitarudi wakati mwingine, ila kazi zako nzuri. Zimenivutia nan do maana nikawa na hamu ya kuziangalia zote. Kazi nzuri sana, safi sana,” Hancy alisifia kazi za Soo na kisha alimuaga na kuondoka.
Aliingia kwenye gari lake haraka ili arudi nyumbani. Foleni ya Buguruni kwenye taa za kuongozea magari zilimfanya ahisi kichwa kinamuua. Alitafuta njia ya uchochoroni na kuibukia kwa mbele. Aligeuza shingo na kuona ile foleni bado iko vilevile magari hayajaruhusiwa, aliongeza mwendo ili kuwahi lakini akiwa njiani taswira ya ile picha ilimjia tena. Aliikumbuka michoro yote aliyoikuta mule bandani mwa Soo.
Huko aliona picha za watu mbalimbali kama vile viongozi na wapiganaji na wanamapinduzi maarufu kama Che Guevara, Bob Marley na Hugho chavez. Iliziangalia kabla ya kuhamia kwenye picha zinazoonyesha matukio kama ya picha za watumwa, Wamasai wakichunga ng’ombe na wanyama wakiwinda na kula majani.
Aliona pia picha ya Wamasai wakichinja ng’omne kwa ajili ya sherehe huku damu ikiwa inatiririka nyingi kutoka kwa yule ng’ombe. Aliogopa na kusimamisha gari lake kando ya barabara ya Mandela akielekea nyumbani kwake Tabata Makuburi. Aliteremka kwa lengo la kununua gazeti. Alikuwa amefika katika kituo cha Relini ambapo pia ipo kampuni ya kuchapisha magazeti ya Mwananchi.
Watu walikuwa wengi katika kituo hicho kilichokuwa kikiuza magazeti. Kila mmoja alitaka kununua gazeti hilo kwa kuwa liliandika habari za kina kuhusiana na matukio mbalimbali yaliyotokea nchini na sehemu nyingine duniani.
Habari zilizokuwemo ndani ya gazeti hazikumfurahisha kabisa Hancy. Alishalilipia na hivyo alisimama kando na kuiangalia ile habari vizuri. Aliona kwanza kichwa cha habari ambacho kilisema, ‘MAJAMBAZI WAUANA’. Aliendelea kusoma habari hiyo ambayo ilikuwa ikiendelea katika ukurasa mwingine wa gazeti hilo.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
‘Moja ya majambazi waliokuwa wakitafutwa kwa udi na ufumba akutwa amekufa nyumbani kwake Tandika. Alikuwa katika ugomvi wa kugombea pesa. Inasemekana kwamba aliyemuua ni moja ya majambazi wenzake wanaotafutwa. Majambazi hao walikimbia baada ya mauaji hayo’.
Hasira zilimpanda sana Hancy. Hakuendelea tena na safari ya kurudi kwake. Aliamua kumtafuta Fina ili azungumze naye mambo yao. Hakutaka Fina ajue mipango yake kwa wakati huo kwani tangu arudi kutoka Uholanzi, Hancy amekuwa akimwonyesha mapenzi Fina ili asigundue njama zake.
Alikumbuka mambo mengi aliyoahidiana na Fina kila walipoonana alipokuwa akirudi nchini. Mawazo yake hayakuwa ka mwingine zaidi yake.
Safari ya kwenda nyumbani ikafa na sasa ilikuwa kwenda kumwona Fina kipenzi chake.
****
Mawazo na fikra juu ya Hancy ni vitu ambavyo vilikuwa vimemtawala Fina kwa kipindi ambacho Hancy alikuwa nchini Uholanzi. Maisha yake hakuhisi yapo sawa kutokana na kutokuwepo kwa Hancy ambaye mara kwa mara aliporudi Fina hakuzificha hisia zake. Siku hiyo kila aliyemfahamu Fina angejua tu ya kwamba Hancy amerudi nchini.
Hata Hancy alijua juu ya furaha ya Fina na hivyo alimletea kila alichoona kitamfurahisha siku akionana naye.
Siku hiyo fina alikuwa ameongozana na Justin wakielekea katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Alimwomba Justin waongozane naye kwani alijua ujio huo wa Hancy ni muhimu kuliko awali alivyokuwa akirudi. Safari hii Hancy ilikuwa asirudi tena Uholanzi kwani alikuwa ameshamaliza masomo yake na hivyo alirudi nchini ili kutafuta kazi ya kufanya pamoja na kusimamia baadhi ya biashara ambazo zilikuwa ni za baba yake ambazo Peter alizisimamia vizuri na kuhakikisha Hancy anafaidika nazo ikiwa ni pamoja na kusoma na kufanyia mambo mengine. Alimfungulia akaunti ya benki na kumwekea kiasi kikubwa cha pesa ambazo zingemsaidia wakati akirudi nchini.
Fina alifurahi sana kumwona mpenzi wake. Kama kila siku alivyokuwa akitamaniHancy arudi sasa ilikuwa ni kweli.
Uwanja wa ndege ulikuwa na watu wengi mno. Ni kipindi hiki ambapo watu wengi walikuwa wakirudi nyumbani kwa ajili ya likizo ndefu japokuwa kwa Hancy yeye ilikuwa ni zaidi ya ndefu kwani hakutarajia kurudi tena Uholanzi. Fina ndiye aliyekuwa wa kwanza kumwona Hancy kabla ya Justin ambaye alikuwa amesimama karibu na sehemu ya wageni kupita.
“Oooh… My Hancy,” alisema Fina huku akiwa ameibana mikono pamoja na kuhisi ameshamkumbatia Hancy.
“Fina!.. kaka Justin!” aliita Hancy kwa mshangao baada ya kuwaona.
“Hancy,” aliita Fina huku akimkumbatia Hancy kwa nguvu. Alishindwa kujizuia na kumpiga busu ambalo liliacha tabasamu kubwa sana kwa Hancy.
“Karibu mpenzi, nilikumiss sana,” alisema Fina aliyekuwa akiteremkwa na machozi. Hali hiyo ilimfanya Hancy ahisi huruma kwa Fina kutokana na umbali ambao walikuwa wameachana kwa kipindi kirefu.
“Usijali Fina, nimerudi kabisa, hutonikosa tena pindi utakaponihitaji.”
“Kaka Justin,” Hancy alimwita Justin ambaye wakati wote alikuwa anatabasamu huku akiwaangalia Hancy na Fina ambao walikuwa wamekumbatiana.
“Hancy…. Umekuwa mkaka sana,” alisema Justin.
“Kweli kaka, hata mi naona nimebadilika sana. si kma kipindi kile nilivyorudi tena. Nashukuru kwa kunipokea kaka Justin,” Hancy alisema huku akimshika Fina mkono na kuelekea kwenye gari tayari kwa kurudi nyumbani. Justin aliendesha gari huku Hancy na Fina wakiwa siti ya nyuma. Fina alikuwa amemlalia Hancy begani huku wakiendelea na mazungumzo taratibu.
Uwili wao uliendelea kama zamani wa kukaa pamoja na kufanya mambo kwa kila mmoja kumfikiria mwenzake.
Walitoka pamoja mara nyingi. Hancy hakupenda kwenda klabu. Ni mara nyingi Fina alikuwa akimhimiza Hancy aende laini hakuweza. Alikubali tu kutoka lakini siyo kwenda klabu bali kustarehe Ufukwe wa Coco hadi jioni na kurudi nyumbani.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Ni kwa muda huo wa kuwa pamoja ndipo Hancy alipomsimulia Fina kuhusu mkasa mzima alioujua alivyokuwa mdogo. Japo Hancy alikuwa mdogo lakini Peter alimsimulia juu ya wazazi wake na familia yake. Ni siku ambayo Hancy alipatwa na mshtuko mkubwa uliomsababisha aumie.
“Aaaah, tokaaa, toka. Niache ntakuuaaa,” Hancy alipiga kelele huku akikimbia kuelekea mlangoni. Alijigonga ukutani na kuumia sehemu ya kichwani. Peter alimfata na kumwangalia. Alikuwa akilia sana. Alimchukua na kumpeleka hospitali.
Daktari alimsaidia na kumpa dawa. Pia alimshauri Peter kwamba kutokana na hali hiyo inayomtokea mara kwa mara ni vyema akawa analala naye kila siku kwa sababu kutokana na kujigonga huko anaweza akapata madhara makubwa.
Peter aliafiki ushauri wa daktari na hivyo alianza kulala na Hancy kila siku hadi alipomtafuta mtu mwingine ambaye alikuwa akilala na Hancy.
Baada ya kupona kabisa Hancy alimsimulia Peter kilichomtokea na kuhusu watu aliowaona wakimtokea.
“Kweli baba, ni mara nyingi naona watu wamenshikia panga wanataa kuniua. Wanasema ni lazima niwafuate wazazi wangu na ndugu zangu. Kwani kuna nini? Na mimi nipo huku na sijawahi kukutana na mtu huku iweje wanitokee.”
Hancy alimweleza Peter na kumweleza namna sura zilivyo. Peter alikumbuka picha aliyoichora Hancy alipokuwa mdogo.
“Hilo tatizo limekuanza lini Hancy?”
“Ni siku nyingi sana baba. Sikumbuki lini. Hata nlivyokuwa mdogo nakumbuka nilipatwa na matatizo kama haya, naogopa baba.”
Peter alikumbuka pia siku Hancy alivyopatwa na tatizo na kulia na kumfuata. Ni miezi michache baada ya wazazi wake kuuliwa pamoja na ndugu zake. Alijua alichokiota Hancy ni kile alichokishuhudia siku majambazi walivyovamia nyumbani kwao na kuwaua ndugu zake.
*****
Hancy alimwonyesha ile picha Fina. Picha ambayo aliichora kwa kufikiria tu. Picha ambayo aliambiwa na Peter aichore wakati alivyokuwa Uholanzi.
“unajua kuchora Hancy.”
“Nashukuru sana Fina.”
Fina alipatwa na mshangao alipoiangalia ile picha. Alijiona kama amewafananisha wale watu. Alifikiria sifa zao na urafiki wake na wao. Alijua wazi itakuwa ni wao. Lakini hakujua kama Hancy alikuwa akiwatafuta watu wale. Hakutaka kwanza kumwambia chochote Hancy. Badala yake alimwonea sana huruma na kumpa pole.
“Fina nawatafuta sana hawa watu. Nadhani ni wakati mzuri huu wakati nkisubiria majibu ya sehemu nilizoomba kazi nianze kuwatafuta… Ona pia, hii alama niliikumbuka nikaichora, na siku nmeenda kwa rafiki angu anayechora n’kaiuta. Ni mchoro wa Tattoo,” Hancy alimwonyesha Fina karatasi nyingine yenye mchoro wa Tattoo.
Mchoro huo Fina aliufahamu sana. Aliwajua wote waliokuwa wakiutumia mchoro huo. Walikuwa ni kama rafiki zake kwani mara nyingi walikutana klabu wakinywa na kucheza muziki. Alikuwa na uhakika kwamba ndio wao kutokana na picha ya mchoro huo. Alimwangalia Hancy mbaye alikuwa na nia ya kufanya jambo kweli. Nafsi ya Fina iliwaza la kufanya.
“Lazima nimsaidia Hancy wangu,” Fina aliwaza huku akimwangalia Hancy kwa huruma.
Hancy alimwomba Fina waondoke na kurejea nyumbani. Fina hakukataa ombi la Hancy ambaye alionekana kuwa na hasira ambazo Fina alikuwa anazielewa.
Hancy hakwenda kwa pita. Alihamia Tabata Makuburi nyumbani kwao. Alimwomba Peter akakae Tabata katika nyumba yao ambayo kwa muda mrefu imekuwa ikipangishwa. Ni baada ya Hancy kuomba ndipo wapangaji waliokuwa wamepangisha hapo kumaliza mkataba wao na kuondoka.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Hancy alimpeleka kwanza Fina nyumbani kwao kisha akaelekea nyumbani kwake Tabata Makuburi.
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment