Simulizi : Ukweli Wenye Kuuma ( Painful Truth )
Sehemu Ya Pili (2)
Bwana Brown alionekana kuchanganyikiwa mara baada ya kuyasikia maneno yale ambayo alikuwa ameambiwa na kijana wake, Wayne. Kitu cha kwanza akazirudisha kumbukumbu nyuma na kuanza kukumbuka kama kuna siku yoyote Wayne alikuwa ametembea na msichana na kumpa mimba lakini hakupata jibu.
Hakuelewa ni mtoto gani ambaye Wayne alikuwa amemzungumzia mahali hapo. Akakiinua kichwa chake kutoka karibu na Wayne na kisha kuyapeleka macho yake usoni kwa mke wake, Bi Lydia. Uso wa Bwana Brown ulionyesha waziwazi kwamba ulikuwa umetawaliwa na maswali mengi, akaanza kupiga hatua na kumfuata mke wake.
“Vipi?” Bi Lydia aliuliza huku akionekana kuwa na hamu ya kutaka kufahamu kitu.
“Anamtaka mtoto wake” Bwana Brown alimjibu.
“Mtoto gani?”
“Sijui”
“Kwani katika kipindi ambacho alipata ajali, Kristen alikuwa mjauzito?” Bi Lydia aliuliza.
“Hapana”
“Sasa mtoto gani anayemtaka?”
“Hata mimi mwenyewe nashangaa. Ila nafikiri atakuwa hajakaa sawa, si unajua mishipa yake ya fahamu ndio inaanza kurudi katika hali yake”
“Inawezekana”
Hakukuwa na mtu ambaye alijisumbua kufuatilia maneno ambayo alikuwa ameyaongea Wayne kwani walijua kwamba akili yake wala haikuwa imekaa sawa. Daktari mmoja na manesi wawili wakaingia ndani ya chumba kile na kisha kuwataka Bwana Brown na Bi Lydia kutoka ndani ya chumba kile kwa ajili ya kuanza kazi yao.
Kila siku Wayne alikuwa akiwaambia maneno yale yale kwamba alikuwa akitaka kumuona mtoto wake. Maneno yale yakaendelea kuwashtua kupita kawaida kitu kilichowapelekea kuanza kufuatilia. Walifuatilia kwa muda wa mwezi mmoja lakini hawakufanikiwa kujua mtoto ambaye Wayne alikuwa akimzungumzia.
Hali ya Wayne ilikuwa ikizidi kutengemaa kadri siku zilivyokuwa zikizidi kwenda mbele. Kutokana na fedha nyingi ambazo alikuwa nazo Bwana Brown, madaktari kutoka katika hospitali kubwa wakaanza kuingia ndani ya hospitali ile kwa ajili ya kumtibia Wayne.
Miezi tisa ikakatika na ndipo hali ya Wayne ikarudi kabisa ila mwili wake ulikuwa na tofauti kubwa sana. Alichokifanya daktari ni kuwaita wazazi wake ndani ya ofisi yake na kisha kuanza kuongea nao huku kila mmoja akionekana kuyafurahia maendeleo ya Wayne.
“Tunamshukuru Mungu kwa kuwa Wayne anaendelea vizuri” Dokta aliwaambia huku akiyaweka vizuri miwani yake pamoja na kulichukua faili kubwa ambalo lilikuwa juu ya meza yake.
“Hata sisi tunashukuru” Bwana Brown alimwambia daktari huku akiwa amemshika mkono mkewe pale vitini walipokuwa wamekaa.
“Kuna mambo mawili ambayo yametokea katika mwili wake. Kwanza ninasikitika kuwaambia kwamba mtoto wenu Wayne hatoweza kutembea tena. Miguu yake pale ilipo ilikuwa imesagika kidogo. Katika kipindi chote tulikuwa tukiangaika nayo. Namshukuru Mungu kwamba tulifanikiwa kwa asilimia themanini kwani kama tungeshindwa kabisa, haina budi tungeikata miguu yake” Daktari aliwaambia.
Kila mmoja akaonekana kushtuka, maneno ambayo alikuwa ameyaongea daktari yalionekana kuwagusa kupita kawaida, walimwangalia daktari mara mbili mbili kana kwamba yeye ndeye ambaye alikuwa amesababisha yale yote.
“Ila tunashuru kwamba ni mzima” Bi Lydia alimwambia daktari.
“Jambo la pili ni kwamba tuligundua kwamba mtoto wenu amekatika mshipa mkubwa ambao unawezesha uume wake kusimama. Mshipa ule haufanyi kazi tena, kwa maana hiyo mtoto wenu hatoweza kusimamisha uume wake tena jambo ambalo halitoweza kumpa mtoto katika maisha yake yaliyobakia” Daktari aliwaambia.
Taarifa hiyo ndio ambayo ilionekana kumshtua zaidi kila mmoja. Wakamwangalia daktari kwa macho yaliyojawa na mshtuko, hawakuonekana kukiamini kile ambacho daktari alikuwa amekiongea mbele yao. Kwa mtoto wao Wayne kukosa uwezo wa kuwa na mtoto kulionekana kuwakosesha raha, waliyaona maisha yake kujaa giza huko mbeleni.
Hawakujua Wayne angeishi katika maisha gani, kutokutembea na kutokuwa na uwezo wa kusimamisha uume wake yalionekana kuwa matatizo makubwa ambayo yalikuwa yameupata mwili wake. Bi Lydia akashindwa kujizuia, akainamisha kichwa chake chini, alipokiinua, machozi yalikuwa yakimtoka.
Ni kweli kwamba walikuwa na mtoto mwingine, huyu alikuwa akiitwa Esther, lakini kwa upande wao walikuwa na mapenzi ya kweli kwa Wayne. Hata kama Esther angepata watoto kumi lakini furaha yao isingekamilika bila Wayne kutokuwa na mtoto.
Hawakujua ni kitu gani ambacho walitakiwa kukifanya, kukubaliana na matokeo yale ikaonekana kuwa kazi kubwa sana mioyoni mwao. Walichokifanya mara baada ya kutoka ndani ya hospitali ile ni kuanza kuwasiliana na madaktari waliokuwa wakubwa zaidi kutoka katika nchi mbalimbali.
Wayne akaanza kusafirishwa na kupelekwa katika nchi mbalimbali duniani kwa ajili ya kuangalia uwezekano wa kulitatua tatizo lile ambalo alikuwa nalo mwilini. Walitembea zaidi ya nchi kumi duniani tena kwa madktari mabingwa ambao walikuwa na uwezo mkubwa lakini kote huko hawakufanikiwa kabisa jambo lililowafanya kurudi nchini Marekani.
Wote wakakubaliana na matokeo. Wayne akaanza maisha mapya ya kuwa mlemavu wa miguu yake. Kila siku waandishi wa habari walikuwa wakielekea ndani ya nyumba hiyo na kuanza kuongea na Wayne ambaye siku zote hakuonekana kuwa na furaha.
Kitu ambacho alikuwa akitaka kuwaambia wazazi wake ni kuhusu Happy, msichana wa Kitanzania ambaye alimuacha akiwa mjauzito. Hakutaka kufanya haraka katika kuwaaambia hilo kwani aliamini kwamba ni lazima apate muda wa kutulia kabla ya kuongea kitu chochote kile.
Siku ziliendelea kukatika lakini Wayne hakuongea kitu chochote kile kwa wazazi wake. Kila siku alikuwa akijitahidi kutafuta njia mbalimbali za kumuwezesha kuwasiliana na Happy lakini ilishindikana kabisa. Miezi miwili ikakatika na ndipo hapo Wayne alipoamua kuwaita wazazi wake na kuanza kuongea nao.
“Nahitaji kwenda Tanzania” Wayne aliwaambia.
“Kuna nini?”
“Hapana. Ninahitaji tu kwenda Tanzania” Wayne aliwaambia.
“Hali yako si nzuri kusafiri masafa marefu. Tuambie kitu chochote kijana wetu tutakufanyia ila si kukuruhusu kuelekea nchini Tanzania” Bwana Brown alimwambia Wayne.
“Maisha yangu yametawaliwa na majonzi, kila siku nilikuwa nikikaa nikimfikiria msichana mmoja ambaye nilikutana nae katika mazingira ya kutatanisha na kumfanyia kitu ambacho kimekaa na kuniumiza moyoni” Wayne alisema huku akianza kulengwa na machozi.
Kila mmoja alikuwa kimya akimwangalia Wayne, maneno ambayo aliyaongea yalikuwa yamewagusa mioyoni mwao lakini pia yalikuwa yamewachanganya kupita kiasi. Wayne akaonekana kuwa na kitu kizito ambacho alikuwa akitaka kuwaambia kwa wakati huo.
“Unatuchanganya” Bwana Brown alimwambia.
“Nafahamu kama mmechanganyikwa na maneno yangu ila ninahitaji kwenda nchini Tanzania kuonana na Happy” Wayne aliwaambia. Wote wakaonekana kushtuka zaidi.
“Happy! Ndiye nani huyo?” Bi Lydia aliuliza kwa mshtuko.
“Msichana niliyemuacha akiwa na ujauzito wangu” Wayne alijibu.
Kwa mshtuko ambao walikuwa wameupata mioyoni mwao, walijihisi kwamba muda wowote ule wangeweza kuzimia. Maneno yale yaliwachanganya zaidi kuliko hata maneno mengine ambayo walikuwa wameyasikia kutoka kwa Wayne.
Wakamwangalia Wayne na kuanza kumsoma saikolojia yake kuona kwamba alikuwa akitania au alikuwa akimaanisha kile ambacho alikuwa akikiongea. Wayne alionekana kumaanisha. Jina la Happy ndilo ambalo lilizua mjadala mkubwa vichwani mwao, wakatamani kumfahamu huyo Happy, mbali na huyo, pia walitaka kufahamu kuhusu huo ujauzito.
“Umesemaje?” Bwana Brown aliuliza huku akionekana kuwa na mshtuko uliojaa furaha.
Hapo ndipo Wayne akaanza kuwaadithia kila kitu ambacho kilikuwa kimetokea katika safari yake ya kwanza ya kitalii kuelekea nchini Tanzania miaka sita iliyopita. Hakuficha kitu chochote kile, alikuwa wazi kwa kila kitu ambacho alikuwa amekifanya kipindi kile.
Bwana Brown na mkewe, Bi Lydia wakaonekana kushtuka kwa furaha, hawakuamini kama kijana wao alikuwa na uwezekano wa kuwa na mtoto ambaye alikuwa nchini Tanzania. Wakajikuta wakisimama na kukumbatiana, machozi ya furaha yakaanza kuwatoka.
“Msifurahi kwa sasa mpaka pale ambapo mtakapomuona mtoto wangu mbele ya macho yenu. Hamuwezi kujua kwamba labda Happy alipata matatizo na mimba kutoka au hata mtoto kufariki” Wayne aliwaambia.
“Ni lazima nisafiri kuelekea huko Tanzania. Ni lazima nikamchukue mjukuu wangu” Bwana Brown alisema huku akionekana kuwa na furaha.
“Nami pia ninataka kwenda huko. Ninataka kumuona mjukuu wangu” Wayne aliwaambia.
“Wewe pumzika nyumbani. Tutakwambia kila kitu kitakachojili” Bwana Brown alimwambia Wayne.
Hakukuwa na cha kuchelewa, kwa haraka haraka viza zikaandaliwa na baada ya siku mbili safari ikaanza. Ndani ya ndege, Bwana Brown na mkewe, Bi Lydia walikuwa wakizungumzia kuhusu mtoto huyo ambaye walikuwa wakielekea kumuona nchini Tanzania.
Sala zao bado zilikuwa zikiendelea mioyo mwao kwa kumuomba Mungu awe Amemlinda mtoto yule mpaka katika kipindi ambacho watamchukua na kumpeleka kwa baba yake. Waliiona ndege ikienda kwa mwendo wa taratibu sana, walitamani wapotee kama wachawi na kujikuta ndani ya nyumba hiyo ambayo walikuwa wameelekezwa.
Mara baada ya ndege kutua katika uwanja wa Mwl Julius Nyerere, wakatoka nje ambako wakaomba kupelekwa katika ofisi za shirika la ndege la Precious Airlines na kukata tiketi ya ndege tayari kwa ajili ya kuelekea jijini Arusha.
Kutokana na kutokuwa na wasafiri wengi siku hiyo, wakapata ndege na saa tisa jioni safari ikaanza. Walichukua dakika arobaini na tano mpaka ndege kuanza kutua katika uwanja wa KIA ambapo wakaanza kuelekea katika moja ya hoteli ya nyota tano ya Jupiter iliyokuwa hapo Arusha.
Wakapata chumba na kutulia. Wakatoa ramani ambayo walikuwa wamechorewa na Wayne na kisha kuanza kuiangalia vizuri. Kila mmoja akaonekana kuridhika, ramani ya kuelekea nyumbani kwa Bi Selina ilionekana kueleweka vichwani mwao.
Siku iliyofuata asubuhi na mapema safari ya kuelekea nyumbani kwa shangazi yake Happy, Bi Selina ikaanza. Walikuwa wakiifuatilia ramani ile kama jinsi ilivyokuwa imeelekeza. Walipata tabu sana kutokana na nyumba nyingi kujengwa na hata mazingira kuwa tofauti sana, mwisho wa siku wakafanikiwa kuiona nyumba hiyo.
Wakaanza kuugonga mlango na baada ya muda fulani, mwanamke mmoja aliyekuwa na nywele zilizoanza kupatwa na mvi akafungua mlango, alikuwa Bi Selina. Wakajitambulisha kwake, wakaonekana kueleweka.
“Mmmhh!”
“Mbona umeguna?” Bwana Brown aliliza.
“Sidhani kama Happy atakubali kuonana nanyi” Bi Selina aliwaambia.
Hapo ndipo walipoanza safari ya kuelekea Machame. Njia nzima Bwana Brown na mkewe walikuwa wakijitahidi kuuliza maswali mengi kuhusu mjukuu wao lakini Bi Selina hakutaka kujibu chochote kile. Wakaingia ndani ya daladala, Bwana Brown hakujali kama alikuwa tajiri mkubwa, kitu ambacho alikuwa akikijali kwa wakati huo ni kumuona mjukuu wake tu.
Wakaanza kuingia katika eneo la nyumba ya mzee Lyimo. Bi Selina akaanza kuufuata mlango na kisha kuugonga, baada ya muda, Bi Vanessa akaufungua mlango ule. Wazungu ambao walikuwa wakionekana mbele yake hakuwa akiwafahamu lakini akaonekana kuhisi kitu fulani. Baada ya salamu, akawakaribisha ndani.
Maongezi yakaanzia hapo huku nae mzee Lyimo akiwa pembeni. Bwana Brown alijitahidi kujielezea kwamba alikuwa nani na alikuwa amefuata kitu gani mahali hapo. Hakukuwa na mtu ambaye alikuwa amemuelewa, walionekana kupinga kupita kawaida.
Kila walipokuwa wakikumbuka siku ambayo Wayne alikuwa amekuja hapo na kisha kuondoka kwa hasira mara baada ya kuambiwa kwamba Happy alikuwa mjauzito waliona hakukuwa na sababu za kuwakubalia ombi lao.
“Amechukua miaka sita na huu unakwenda kuwa mwaka wa saba, hajawahi kumjulia hali mtoto wake, mbaya zaidi alikataa mimba na kusema kwamba si ya kwake, iweje leo anakuja kudai mtoto? Hata kama ni mahakamani tutakwenda lakini Andy atabaki kuwa kwetu” Mzee Lyimo aliwaambia huku akionekana kukasirika.
Hapo ndipo Bwana Brown alipoanza kuelezea kila kitu ambacho kilikuwa kimtokea katika maisha ya Wayne toka katika kipindi kile alichokuwa amepata ajali na kulazwa kitandani kwa muda wa miaka sita. Wote wakaonekana kushtuka, hasira ambazo walikuwa nazo zikaonekana kupotea.
“Hapo alipo hawezi hata kutembea. Na kamwe hatoweza kutembea katika maisha yake” Bwana Brown aliwaambia.
“Furaha pekee ambayo imebaki kwake ni kumuona mtoto wake tu. Nafikiri ataweza kufanya jambo lolote baya kama tu hatutarudi na kile ambacho amekitarajia” Bi Lydia aliwaambia.
Habari za kupata ajali kwa Wayne zikaonekana kuwa mpya kwao, ni kweli kwamba Wayne alikuwa ameikataa mimba ile lakini katika upande wao mwingine wa moyo walijua kwamba kama asingepata ajali basi angekuwa amekwishafika nyumbani hapo siku nyingi.
Alichokifanya Bi Vanessa ni kuinuka na kuelekea chumbani kwa Happy ambaye alikuwa amelala. Ile kuufungua mlango, Andy akatoka huku akikimbilia pale sebuleni na kumfuata mzee Lyimo na kuishika miguu yake.
“Babu atata mma” Andy alisema katika lafudhi ya kitoto.
Bwana Brown na mkewe hawakuamini mara macho yao yalipotua kwa Andy. Andy alikuwa amefanana kwa kila kitu na mtoto wao, Wayne. Wote wakaonekana kufarijika, wakajikuta wakitokwa na machozi ya furaha.
“Ndiye yeye. Mwangalie alivyofanana na baba yake” Bi Lydia alisema huku akitamani kumfuata Andy na kumkumbatia.
Wala hazikupita dakika nyingi, Happy akatokea sebuleni hapo akiongozana na mama yake. Macho yake yakatua kwa Bwana Brown na Bi Lydia ambao macho yao bado yalikuwa yakimwangalia Andy. Alichokifanya Happy ni kumfuata mtoto wake, Andy kumchukua na kumpakata.
Mazungumzo yakaanza upya, walielezea kila kitu ambacho kilikuwa kimetokea katika maisha ya Andy mara baada ya kuondoka nchini Tanzania na kuelekea nchini Marekani. Tofauti na matarajio yao, Happy alikuwa akitabasamu muda wote ambao alikuwa akielezewa kuhusu Wayne.
“Hayo ndio malipo. Hivyo ndivyo Mungu alivyotaka iwe. Andy ni mtoto asiyekuwa na baba. Nafikiri huyo Wayne ambaye amewatuma mje kumchukua si yule Wayne ambaye nini baba yake. Kama mlivyokuja na ndivyo ninavyotaka muondoke. Mtakapomuona, naomba mmwambie kwamba baba yake Andy alikwishafariki hata kabla Andy hajazaliwa. Mtakapoona haelewi naomba mmwambie kwamba Andy alifariki kwa ugonjwa wa Tete kuwanga ambao ulikuwa umemsumbua sana utotoni” Happy alisema.
Bila kutarajia, Happy akajikuta akianza kutokwa na machozi, uwepo wa Bwana Brown na mkewe ulionekana kumkumbusha mbali sana tangu kipindi cha kwanza ambacho alikutana na Andy. Kamwe hakutaka kumuona mwanaume huyo, alikuwa akimchukia kupita kiasi. Ilikuwa ni afadhali kukutana na shetani angempenda kuliko kukutana na mwanaume ambaye alikuwa ameikimbia mimba yake.
“SITAKI KUONANA NAE WALA MTOTO WANGU KWENDA POPOTE” Happy alisema na kisha kuingia chumbani kwake pamoja na mtoto wake, Andy.
Walijaribu kuugonga mlango lakini wala mlango haukufunguliwa. Bwana Brown na mkewe wakakaa mahali hapo huku wakimtaka mzee Lyimo na Bi Vanessa waongee na Happy lakini hilo nalo halikuwezekana kwani Happy alikuwa amejifungia mlango na wala hakukuwa na dalili za kuufungua.
“NIMESEMA SITAKI....SITAKI....SITAKI......SITAKI...”Sauti ya Happy ilisikika kwa nguvu masikioni mwao.
Hakukuwa na mtu ambaye aliamini kama kweli Happy alikuwa amemaanisha kile ambacho alikuwa amekisema. Waliendelea kuugonga mlango lakini wala Happy hakuufungua, bado aliendelea kujifungia. Bwana Brown na mkewe bado walikuwa wamesimama mlangoni huku wakimtaka Happy kufungua mlango lakini bado Happy alikuwa king’ang’anizi, hakufungua mlango.
Walisimama mlangoni kwa zaidi ya nusu saa lakini hali haikuonekana kubadilika. Walichokifanya mara baada ya kuona Happy amekataa katakata kuufungua mlango ni kuaga mahali hapo na kurudi hotelini. Usiku hawakulala, vichwa vyao vilikuwa vikifikiria kuhusu mjukuu wao, Andy Ryn. Huyo ndiye alikuwa mtu pekee ambaye walikuwa wakimhitaji na kwenda nae nchini Marekani mpaka kwa baba yake.
Kutokuondoka na Andy kwenda nae Marekani waliona ingeweza kuleta tatizo fulani katika maisha ya baba yake, Wayne. Iliwabidi kupigana mpaka kufanikiwa, hata ikiwezekana kwa njia zisizokuwa za uhalali ili mladi tu Andy awe mikononi mwao.
Vichwa vyao vilikuwa vikisumbuka usiku kucha lakini hawakupata jibu juu ya kile ambacho walitakiwa kukifanya. Kwa wakati huo mioyo yao ilikuwa na furaha kumuona Andy lakini waliona furaha yao isingekamilika kama tu wasingerudi nchini Marekani pamoja na Andy.
“So what should we do? (Kwa hiyo tufanye nini?)” Bi Lydia aliuliza.
“Lets kidnap him (Tumteke)” Bwana Brown alijibu huku akionekana kumaanisha kile ambacho alikuwa amekisema.
“Do you think this is good idea? (Unafikiri hili ni wazo zuri?)”
“Things are not like we expected before. Everything goes wrong (Mambo hayapo kama tulivyotegemea. Kila kitu kinakwenda sivyo)” Bwana Brown alisema.
“I dont think if this is good idea. How can you kindnap your grandchild? (Sidhani kama hili ni wazo zuri. Utamteka vipi mjukuu wako?)” Bi Lydia alisema.
Wazo ambalo alikuwa amelitoa Bwana Brown lilionekana kutokumuingia akilini kabisa Bi Lydia, hakuona kama ilistahili Andy atekwe na kupelekwa nchini Marekani. Kitu ambacho alikuwa akikifikiria yeye ni maisha ya baadae hasa mara baada ya Andy kuja kuujua ukweli na kuambiwa kwamba alitekwa.
“Hapana mume wangu. Tutumie fedha” Bi Lydia alitoa wazo.
“Kivipi?”
“Kazi rahisi sana. Ninachoamini ni kwamba Happy anawasikiliza sana wazazi wake hata kama wakisema kitu gani. Kwa jinsi hali nilivyoiona, wazazi wale hawatotusaidia kwa nguvu zote, cha msingi tutumie fedha” Bi Lydia alielezea wazo lake.
Ingawa mara ya kwanza lilionekana kuwa si wazo zuri kichwani mwa Bwana Brown lakini baadae akaliona kufaa sana. Walichokifanya siku iliyofuata ni kwenda nyumbani kwa mzee Lyimo, siku hiyo hawakutaka kabisa kuzungumzia kuhusu kumchukua Andy, siku hiyo walikuwa wakizungumzia namna ya kupatengeneza eneo hilo.
“Tumejifikiria sana, tena usiku kucha. Mjukuu wetu tumeamua kumuacha hapa hapa ili aendelee kupata malezi ya mama yake. Ila tunachokitaka ni kumtengenezea maeneo mazuri ya kukaa, kamwe hatutoweza kuacha eneo hili namna hii” Bwana Brown alisema maneno ambayo yalionekana kumfurahisha kila mtu, hata Happy mwenyewe.
Kiasi cha shilingi milioni hamsini kikatolewa na kisha ujenzi wa nyumba kubwa kuanza. Mafundi wakubwa waliokuwa na uwezo mkubwa wakaitwa mahai hapo na kisha kazi ya ujenzi kuanza. Kazi haikuwa ndogo hata mara moja, nyumba kubwa na ya kisasa ikaanza kutengenezwa.
Kwa mwaka huo wa 1996, kiasi cha shilingi milioni hamsini kilikuwa ni kiasi kikubwa sana cha fedha. Huku ujenz wa nyumba ile ukiendelea, Bwana Brown na mkewe, Bi Lydia wakaaga na kurudi nchini Marekani huku kila kitu kuhusu nyumba kikiwa kimetolewa na huku wakiwa wameacha kiasi cha shilingi milioni mia moja kwa ajili ya matumizi.
Mzee Lyimo na familia yake walionekana kushukuru kupita kawaida, kwao Andy alionekana kuwa na faida kubwa kiasi ambacho wakabaki wakimshukuru Mungu kwa hatua aliyoichukua Happy kuzaa na Wayne.
Kuanzia hapo, kazi kubwa ya mzee Lyimo na mkewe, Bi Vanessa ilikuwa ni kumbembeleza Happy akubali lile ambalo Bwana Brown na Bi Lydia walikuwa wakilitaka, kuondoka na Andy. Happy alikataa katakata, ila mwisho wa siku akajikuta akikubali ila kwa sharti na yeye kusafiri ili asikae mbali na mtoto wake.
Nchini Marekani, Wayne hakuwa na furaha hata kidogo, kitendo cha wazazi wake kurudi pasipo kuwa na mtoto wake, Andy kilimkosesha amani kabisa. Wayne hakutaka kukubali hata mara moja, moyoni aliamini kama angekwenda yeye mwenye nchini Tanzania basi kazi isingekuwa kubwa, ni lazima angerudi na mtoto wake.
Baada ya wiki mbili, Wayne akaanza safari pamoja na wazazi wake kwenda nchini Tanzania. Ndani ya ndege kiu yake ilikuwa ni kumuona mtoto wake ambaye alikuwa damu yake yeye mwenyewe. Walipofika jijini Dar es Salaam wakachukua ndege na kuelekea jijini Arusha.
Muda wote huo Wayne alikuwa na kiu kubwa ya kumuona mtoto wake ambaye alimuona kuwa wa thamani kuliko kitu chochote kile katika maisha yake. Wakafika Arusha na kuchukua vyumba hotelini huku Wayne akiendelea kuwa katika kibaiskeli chake cha walemavu.
Siku iliyofuata safari ya kuelekea Machame ikaanza. Nyumba kubwa na ya thamani ilikuwa imejengwa kiasi ambacho ilionekana kutokuwa na hadhi kubwa ya kujengwa nchini Tanzania. Magari mawili yalikuwa katika eneo hilo huku trekta kubwa likiwa limepaki pembeni kabisa, fedha zile zilizokuwa zimeachwa zilionekana kuyabadilisha maisha yao.
Wakati Bwana Brown na familia yake wanaingia ndani ya eneo la nyumba ile, walipokelewa kwa mapokezi makubwa. Happy hakuamini macho mara baada ya kumuona Wayne. Japokuwa mwanaume huyo alikuwa amemfanyia mambo mengi mabaya lakini akaonekana kuanza kuyasahau yote.
Akaanza kupiga hatua na kumfuata Wayne, alipomfikia, akamkumbatia. Wayne akashindwa kujizuia, akaanza kumuomba msamaha Happy huku akilia kama mtoto kiasi ambacho kilionyesha kwamba alikuwa akijutia kile ambacho alikuwa amekifanya maishani mwake miaka sita iliyopita.
“Nimekusamehe” Happy alisema huku akijifuta machozi yake.
Andy akaletwa mahali hapo, Wayne akatamani kusimama, akaanza kukisukuma kibaiskeli chake na kumkumbatia Andy. Hakuamini kama tayari alikuwa ameiona damu yake, machozi yalizidi kuongezeka machoni mwake, kumuona Andy kulimpa faraja kuu maishani mwake.
Siku hiyo ilionekana kuwa siku ya furaha kuliko zote katika maisha ya Wayne, muda wote Andy alikuwa pembeni yake. Hakutaka kumuachia kwani aliona kama angemwacha aende kwa mtu mwingine basi asingerudi tena mikononi mwake.
Happy hakutaka kukumbuka maisha ambayo yalikuwa yamepita, alipanga maisha yajayo pamoja na mwanaume ambaye alikuwa aemkimbia miaka ya nyuma, Wayne. Kila kitu kilichokuwa kimepita kilionekana kuwa kama historia, alitakiwa kukisahau na kuanza kuandika historia nyingine.
Baada ya wiki mbili, safari ya kurudi nchini Marekani ikaanza, japokuwa walikuwa wamekuja watatu lakini kurudi walikuwa wakirudi watano, yaani Happy pamoja na Andy.
“Nitatumia fedha zangu zote, uwezo wangu wote mpaka mtoto wangu anafanikiwa” Wayne aliwaambia wazazi wake.
“Usijali. Tutakuwa pamoja nawe katika kila hatua utakayopitia” Bwana Brown alisema na kisha wote kukumbatiana.
****
Maisha mapya yakaanza nchini Marekani huku Wayne na Happy wakiishi kama mume na mke. Mapenzi yao yakarudi, wawili hao walionekana kupendana na kujaliana katika kila hali. Happy hakuangalia matatizo aliyokuwa nayo Wayne ya ulemavu au ya kutokusimamisha, ila kitu ambacho alikuwa akikiangalia ni mapenzi ya kweli.
Kila siku walikuwa na furaha kupita kawaida mpaka katika kipindi ambacho Andy alipoanzishwa katika shule ya St’ Augustine iliyokuwa Woodmere hapo hapo jijini New York. Shule hii ndio ambayo ilikuwa ikiongoza kusomwa na watoto waliotoka katika familia ya kitajiri jijini New York.
Wanafunzi wengi ambao walikuwa wakisoma katika shule hiyo walikuwa wazungu kitu ambacho kilisababisha wengi kumshangaa Andy ambaye alikuwa na mchanganyiko wa rangi. Ingawa wanafunzi weusi hawakuwa wengi katika shule hiyo lakini Andy alionekana kuwa tofauti kwao.
Masomo yakaanza kama kawaida, katika kipindi cha kwanza Andy alikuwa mgumu kuelewa kutokana na lugha ambayo ilikuwa ikitumika ila baada ya kukaa kwa miezi sita, akaanza kuelekewa kila kitu. Hapo ndipo ukali wake ulipoanza kuonekana.
Andy alionekana kuwa na uwezo mkubwa sana, alikuwa ni mtoto mwepesi kuelewa na alikuwa mtoto mgumu sana kusahau. Uwezo huo ndio ambao uliwafanya walimu kuanza kuona kitu cha tofauti, Andy alionekana kuwa mtoto wa ajabu.
Muda mwingi ambao alikuwa shuleni hapo, Andy alikuwa akipendelea kukaa karibu na wadudu. Wadudu ndio walikuwa sehemu ya maisha yake na kama ikatokea siku akamuona mdudu akiwa amekufa, siku hiyo haikuwa ya amani katika maisha yake.
Uwezo wake mkubwa ndio ambao uliwapelekea walimu kumpandisha darasa, alionekana kuwa mbele ya darasa lile ambalo alikuwa akilisoma. Huko alipopelekwa napo alikuwa moto mkali. Kila siku alikuwa akiongoza darasani, haikujalisha kama ilikuwa jaribio la kawaida au mtihani.
Andy hakuwa msomaji kabisa na wala haikuwahi kutokea hata siku moja kushika daftari kusoma. Muda mwingi shuleni alikuwa akishinda akiwaangalia wadudu. Hakujali alikuwa sehemu gani, hata kama alikuwa darasani, alikuwa akienda na kichupa ambacho kilikuwa na wadudu ndani yake.
Mara kwa mara Happy na Wayne walikuwa wakiitwa shuleni na kuambiwa kuhusu mtoto wao, wote walikuwa wakijivunia kupata mtoto ambaye alikuwa na uwezo mkubwa kama Andy. Miaka ikaendelea kukatika na ndipo Happy na Wayne wakaamua kufunga ndoa katika kanisa la St’Thabita lililokuwa Marrtson nje kidogo mwa jiji la New York.
Mapenzi yao yalikuwa makubwa, walikuwa wakiheshimiana kama mke na mume japokuwa Wayne hakuwa na uwezo wowote wa kufanya kazi kitandani. Happy hakutaka kuliangalia tatizo hilo, kitu ambacho alikuwa akikiangalia ni mapenzi ya kweli kwake.
Hali ile ikaanza kumuweka Wayne katika wakati mbaya, muda mwingi alikuwa akionekana kuwa na mawazo. Moyoni alitamani sana kufanya mapenzi na mke wake ila hakuwa na uwezo huo. Wayne alionekana kuwa kama kwenye msiba, alikuwa na kila kitu ambacho alikuwa akikihitaji katika maisha yake.
“Inatubidi tutumie uume wa bandia” Wayne alitoa wazo.
“Wa nini?”
“Kukusaidia mke wangu. Unajua hali hii inaniumiza sana, wakati mwingine najiona kama sitakiwi kuwa pamoja nawe, yaani najiona kutokuwa mwanaume mwenye sifa za kuwa na mwanamke mzuri kama wewe” Wayne alimwambia Happy.
“Haiwezekani. Siwezi kufanya mapenzi na uume wa bandia. Kama hali yako itaendelea milele, acha nami niwe hivi milele” Happy alimwambia Wayne.
Hivyo ndivyo walivyokuwa wakiishi. Kila siku walikuwa wakiangalia mikanda ya ngono huku Wayne akitaka kuona kama alikuwa na mabadiliko yoyote lakini bado hali ilikuwa vile vile. Kila kitu ambacho walikuwa wakikifanya hakikuwa kikiwasaidia.
Bado walikuwa wakiendelea kwenda katika mahospitali makubwa duniani kutafuta tiba lakini bado hali iliendelea kuwa vile vile. Ikafika kipindi wote wakaonekana kukata tamaa jambo ambalo liliwafanya kutulia na kusubiri muujiza wa Mungu.
Miaka ikakatika mpaka kufika kipindi ambacho Andy akaingia High School. Kwa sababu alikuwa akipenda sana wadudu, akaamua kuchagua somo la Bailojia liwe kama kichwa katika masomo yake aliyokuwa ameyachagua.
Kadri siku zilivyozidi kwenda mbele na ndivyo ambavyo uwezo wake darasani ulivyozidi kuongezeka. Alikuwa akifahamu mambo mengi kuhusu wadudu na hata sumu ambazo zilikuwa zikiwaua wadudu kwa muda mchache sana.
Andy akaona hiyo haitoshi, hapo ndipo alipoamua kuanza kuufuatilia mwili wa mwanadamu na jinsi damu ilivyokuwa ikifanya kazi kubwa mwilini. Hakuishia hapo bali vile vile akaanza kutafuta sababu ambazo zilikuwa zikimfanya binadamu kufa katika kipindi ambacho mwili wake ulikuwa ukiwekewa sumu fulani.
Katika kila kitu ambacho Andy alikuwa akijiuliza akaanza kupata jibu hali iliyoifanya akili yake kukua zaidi na zaidi. Ubora wake katika masomo ukaongezeka zaidi. Wanafunzi shileni hapo walikuwa wakizidi kumuogopa Andy ambaye toka ameanza masomo shuleni hapo hakuwa kushika namba zaidi ya namba moja.
Mwaka huu ndio ambao ulikuwa wa mwisho kabla kumaliza elimu ya juu kabla ya kuanza chuo. Katika maisha yake yote yote, Andy alikuwa akihofia sana kujiingiza katika mahusiano. Shuleni kulikuwa na wasichana wengi ambao walikuwa wakitamani sana kuwa na uhusiano na Andy lakini jambo hilo lilionekana kuwa gumu.
Maishani mwake alijifunza mengi kuhusiana na mahusiano ya kimapenzi, alikwishawahi kuwaona watu wakilia usiku na mchana huku wengine wakianza kuzichukia jinsia ambayo ilikuwa imemsababishia maumivu makali moyoni mwake, aliyachukia mapenzi na kamwe hakutaka kujiingiza katika mahusiano.
“Kamwe siwezi kupenda” Andy aliwaambia marafiki zake.
“Kwa nini?” Bruce aliuliza.
“Naogopa nitaua. Yaani sitaki kupenda kwa sababu nitaua” Andy alimwambia.
“Utaua! Kivipi?”
“Unafikiri nikipenda halafu nikasalitiwa, nitamuacha hai mtu aliyeuumiza moyo wangu?”
“Lakini si unajua kuna usahaulifu. Unachokifanya ni kuachana nae na kisha kutafuta mwingine” Bruce alimwambia.
“Hapana. Bado haitosaidia. Nitaua tu. Hiyo ndio sababu ambayo inanifanya kutokuingia katika mahusiano” Andy alisema.
Moyoni alipanga kabisa tena kwa moyo mmoja kutokujiingiza katika mahusiano lakini kila alipokuwa akiwangalia msichana Annastazia Kapama alionekana kuanza kuusaliti moyo wake. Hakuona kama angeendelea kuwa katika msimamo ambao alikuwa amejiwekea.
Annastazia Kapama alikuwa ni msichana aliyetoka nchini Tanzania ambaye baba yake alikuwa Waziri wa Mambo ya Ndani na Nje, Bwana Simon Kapama. Ingawa walikuwa wamezaliwa watatu katika familia yao lakini Annastazia ndiye ambaye alikuwa akipendwa zaidi.
Bwana Kapama hakutaka watoto wake wasome nchini Tanzania jambo ambalo lilimpelekea kuanza kuwasomesha nje ya nchini katika nchi za Marekani, Uingereza na India. Kapama alikuwa msichana mwenye mvuto mkubwa shuleni hapo kiasi ambacho wavulana wengi walikuwa wakitamani sana kuwa nae.
Umbo lake lilikuwa la kimisi huku uso wake wa upole ndio ulikuwa chachu kubwa ya uzuri wake. Mashavuni mwake, vishimo viliwili vilikuwa vikionekana lakini kila alipokuwa akicheka au kutabasamu, vishimo vile vilionekana vizuri zaidi.
Muda wote Annastazia alikuwa mcheshi hali ambayo ilimfanya kupata marafiki wengi shuleni hapo. Japokuwa wanafunzi wengi walikuwa wakijaribu bahati zao kwa Annastazia lakini kamwe hakuonekana kuwa msichana mwepesi kabisa.
Katika kipindi chote cha maisha yake, Annastazia alitamani sana kuwa mwanasiasa kama alivyokuwa baba yake. Kila siku alikuwa akisoma vitabu vilivyokuwa vimeandikwa na wanasiasa wengi ili kujua walianzia wapi mpaka kuwa wanasiasa wakubwa.
Kama ilivyokuwa kwa Andy na ndivyo ilivyokuwa kwa Annastazia, kamwe hakutaka kujiingiza katika mahusiano ya kimapenzi, kwake aliyachukia mapenzi kama alivyokuwa akimchukia adui yake aliyemtishia kumuua.
Katika kila kona, alikuwa akiyaepuka mapenzi. Ilikuwa ni kawaida kuongea na Annastazia kuhusu mambo mengine na kuondoka huku akiwa amekasirika mara tu utakapoanza kuzungumzia mapenzi. Hakujiona kuwa tayari kuingia katika mapenzi, alijiapiza kuitunza bikira yake mpaka kwa mwanaume ambaye angetokeza kumuoa.
Kadri siku zilivyozidi kwenda mbele na kuzidi kuangaliana, kuna vitu ambavyo vikaanza kujitokeza ndani ya mioyo yao. Mara ya kwanza hawakuwa wakivifahamu vitu hivyo mpaka pale ambapo walianza kukaa pamoja na kuanza kuzungumza. Kila mmoja akaanza kujisikia furaha kila alipokuwa akiongea na mwenzake kiasi ambacho kama walikuwa mbali hawakujisikia kuwa na furaha kabisa.
Mara ya kwanza walionekana kutokujua ni kitu gani kilikuwa kikiendelea lakini mara walipoanza kugusana, miili yao ikaanza kujisikia hali ya tofauti. Ukaribu wao ukaanza kuongeeka kiasi ambacho wanafunzi wakaanza kujua ni kitu gani kilikuwa kinaendelea katika maisha yao. Andy akawa haambiwi kitu chochote juu ya Annastazia lakini nae Annastazia akawa haambiwi chochote juu ya Andy.
Kwa mara ya kwanza katika maisha yao wakajikuta wako ndani ya gari peke yao na kuanza kugusanagusana mpaka pale tamaa ya mwili ilipowashika. Hakukuwa na kilichoendelea zaidi ya kuanza kufanya ngono.
Andy akawa ameitoa bikira ya Annastazia lakini nae Annastazia akawa amemkaribisha Andy katika ulimwengu wa ngono. Kuanzia siku hiyo ndipo ukaribu wao ulipozidi zaidi na zaidi, walipendana na kuthaminiana kupita kawaida.
“Utanioa?” Annastazia alimuuliza Andy.
“Unaniuliza au unaniambia?”
“Nakuuliza”
“Hapana. Hapo umeniambia” Andy alimwambia Annastazia na kisha wote kukumbatiana.
Katika kipindi hicho hakukuwa na mtu aliyekuwa akifikiria kama watu walikuwa wakilia katika mahusiano, hawakukumbuka kama kuna watu walikuwa radhi kuua mara tu wanaposalitiwa, wao kwao waliona mahusiano kuwa ni furaha ambayo ingedumu katika maisha yao yote. Wakajisahau kama kulikuwa na maumivu makali katika mahusiano ya kimapenzi.
Kama ni jeuri ya fedha basi kijana George alikuwa akiongoza nchini Tanzania. Yeye alikuwa mtoto wa tajiri wa Bwana Mtimbi ambaye alikuwa akimiliki kiasi kikubwa cha fedha. Ukiachilia mbali utajiri huo mkubwa aliokuwa akimiliki baba yake, pia alikuwa akijivunia sana kutokana na baba yake kuwa Waziri wa Nishati na Madini nchini Tanzania.
Maisha ya starehe ndio ambayo alikuwa amezoea kuishi toka katika kipindi ambacho alikuwa amepata ufahamu wa kujitambua. Alikuwa akimshawishi sana baba yake amnunulie magari ya kifahari na kutokana na mapenzi makubwa ambayo alikuwa nayo baba yake, alikuwa akimnunulia.
Mitaani watu hawakuwa na amani hata kidogo, George na marafiki zake walikuwa wakileta fujo na magari yao ya kifahari ambayo yalionekana kuwa kero kwa Watanzania ambao asilimia themanini walikuwa wakiishi katika maisha ya dhiki.
Alizaliwa huku akiwa amezikuta fedha na hata wakati huo alikuwa akikua huku akiziona fedha, kwake hakuwahi kuzitafuta fedha hizo zaidi ya kuzitumia kadri ya uwezo wake. George alikuwa miongoni mwa watoto wa viongozi ambao walikuwa wakipenda sana starehe, ilikuwa ni bora umnyime kitu chochote lakini si kumnyima kwenda klabu nyakati za usiku au kulala na wasichana watatu kila ifikapo mwisho wa wiki.
Mtanzania gani ambaye alikuwa akiishi Dar es Salaam hakuwa akimfahamu George? Kila mtu alikuwa akimfahamu kijana huyo ambaye sifa zake chafu zilikuwa zikiendelea kutapakaa katika kila kona jijini Dar es Salaam.
George akajikuta akiwa ameanza kuyanufaisha magazeti na vyombo vingine vya habari. Kuonekana kwa picha yake katika magazeti na kuandikwa maneno yaliyojaa kashfa kuliyafanya magazeti hayo kununuliwa kupita kawaida.
Baba yake, Bwana Mtimbi alijitahidi kumuita George mara kwa mara na kuongea nae lakini wala hakuonyesha mabadiliko yoyote zaidi ya kuendelea kuwa vile vile huku wakati mwingine akionekana kuzidisha. Ingawa baba yake alikuwa na hasira juu ya tabia zake lakini hakuwa na la kufanya zaidi ya kumuacha afanye kile ambacho alikuwa akijisikia kufanya.
Fedha zikamtia wazimu George, akaonekana kuchanganyikiwa, kila siku alikuwa akipamba vichwa vya habari katika magazeti mengi jijini Dar es Salaam. George akaonekana kuishusha heshima ya baba yake, watu wakaonekana kumdharau kwa kuwa tu alishindwa kabisa kumdhibiti kijana wake ambaye kadri siku zilivyozidi kwenda mbele na ndivyo ambavyo aliendelea kuvuma kwa kashfa.
“Unafikiri nisipofanya haya sasa hivi nitayafanya kipindi gani? Umri unaenda, na ujana ni maji ya moto, acha nihangaike nayo” Hayo yalikuwa maneno ambayo mara kwa mara yalikuwa yakitoka kinywani mwa George.
Ingawa kila siku alikuwa akifanya mambo mengi ya starehe pamoja na kutembea na wasichana wengi lakini kila siku moyo wake ulikuwa kwa msichana mmoja tu, Annastazia Kapama. Akili yake ilikuwa imechanganyikiwa juu ya binti huyo, kwake, lengo lake halikuwa kumchezea na kisha kumuacha kama wasichana wengine, kwa Annastazia, alitaka kumuoa kabisa na kuachana na mambo mengine.
Kwa mara ya kwanza alikutana na Annastazia katika kipindi ambacho watoto wa Mawaziri walikuwa wamekutana katika sherehe ya kumpongeza mtoto wa Waziri Stefano, Anania. Siku hiyo ndio alikuwa amemuona Annastazia, akauhisi moyo wake ukimpenda kwa moyo wa dhati.
George hakutaka kuchelewesha muda, alichokifanya ni kumfuata Annastazia na kumuelezea kile ambacho alikuwa akikihisi moyoni mwake. Annastazia hakuonekana kuwa mwepesi hata mara moja, akamkataa George.
George akaonekana kuumia hali ambayo ilimfanya kukosa raha kila siku. Unyonge ukaanza kumtawala moyoni, mapenzi yakaonekana kuanza kumtesa. Alishindwa kulala vizuri wala kula vizuri kwani kila alipokuwa akiufikiria uzuri wa Annastazia halafu akifikiria kwa jinsi alivyokataliwa, hakuona sababu yoyote ya kumfanya kuwa na furaha.
Kila siku alikuwa akimfuata shuleni St’ Marys lakini napo haikuonekana kumsaidia. Annastazia aliendelea kumkataa George, hakuvutiwa nae hata siku moja. George hakuonekana kukata tamaa, kwake aliamini kwamba asilimia kubwa ya wasichana hukaza siku ya kwanza na hatimae kuulegeza msimamo wao.
Kila siku aliendelea kumfuatilia Annastazia lakini bado msimamo wake ulikuwa vilevile. Hapo ndipo George alipoamua kubadilika, skendo mbalimbali ambazo alikuwa nazo aliziona kuanza kumharibia. Alichokifanya kwa wakati huo ni kutoa kiasi fulani kwa waandishi wa habari kwa ajili ya kuandika mambo mengi juu yake kwa ajili ya kumsafisha.
Wiki nzima magazeti ya udaku yalikuwa yakiandika kuhusu mabadiliko ambayo alikuwa ameamua kuyafanya George juu ya maisha yake. Kwa mara ya kwanza wananchi walionekana kutokuamini lakini ya mwezi mzima wakaonekana kuamini kutokana na magazeti yale kuendelea kumsafisha zaidi na zaidi.
“Nimeamua kubadilika. Nimekubali kwamba yale niliyokuwa nikiyafanya yalikuwa ni ujinga mbele zenu na hata mbele ya jamii” George aliwaambia wazazi wake.
Bado harakati zake za kumtafuta Annastazia na kumuweka katika himaya zilikuwa zikiendelea kila siku lakini Annastazia hakuonekana kukubaliana nae hata mara moja japokuwa alikuwa akijua kwamba George alikuwa amebadilika.
Moyo wa George ukaonekana kupatwa na pigo kubwa mara baada ya kufahamu kwamba Annastazia alikuwa akikaribia kuelekea nchini Marekani masomoni. Akaongeza nguvu zaidi za kumwambia kuwa nae lakini bado Annastazia alikuwa akikataa.
“Nakuomba Annastazia. Nitakuwa tayari kuwa mwaminifu juu yako mpaka utakaporudi” George alimwambia Annastazia kwa sauti ya chini iliyokuwa ikimaanisha.
“Sikutaki George. Muda wangu wa kuwa na mwanaume haujafika” Annastazia alimwambia George.
“Ninakupenda Annastazia, ninakupenda sana” George alimwambia Annastazia.
“Sikutaki” Annastazia alimwambia George na kisha kuwasha gari lake na kuondoka.
Siku hiyo ilikuwa pigo kubwa kwa George, alipata muda mwingi wa kuongea na Annastazia lakini bado alionekana kuwa mgumu kukubaliana nae. Usiku hakulala, alikesha kama popo huku akimfikiria Annastazia ambaye alikuwa ameuteka moyo wake kupita kawaida.
Kuanzia siku hiyo hakuweza kumuona tena Annastazia mpaka pale aliposikia kwamba alikuwa amesafiri kuelekea nchini Marekani kuanza masomo. George akakosa amani, alichokifanya kwa wakati huo ni kuwaleza wazazi wake juu ya kile ambacho kilikuwa kimetokea.
“Unampenda kweli?” Mzee Mtimbi aliuliza.
“Ninampenda. Niko tayari kumuoa hata atakaporudi” George alimjibu baba yake.
Kwa hali ambayo alikuwa akionekana nayo George ilikuwa ni vigumu sana kwa Bwana Mtimbi kuvumilia, alichokifanya ni kuanza safari kuelekea nyumbani kwa Bwana Kapama na kuwaelezea vyote ambavyo George alikuwa amemwambia.
Bwana Kapama na mkewe wakaonekana kufurahia kwani kutokana na wao kuwa marafiki, waliona urafiki ungeongezeka zaidi kama watoto wao wangeungana na kuwa kitu kimoja. Wote wakakubaliana, kilichotakiwa mahali hapo ni kumsubiria Annastazia arudi kutoka masomoni na kisha kumwambia kile ambacho kilikuwa kimeendelea.
“Utaweza kumsubiri mpaka miaka miwili ipite?” Bwana Kapama aliuliza.
“Ni michache sana. Hata ukisema mitano, niko tayari” George alisema.
“Kwa hiyo tumpe taarifa juu ya kinachoendelea?”
“Hapana. Nataka tumfanyie ‘suprise’”
“Ila si mpaka ninyi mkubaliane?”
“Ndio. Ila naona kama ninyi wazazi mkihusika, hakutokuwa na tatizo halafu mtakuwa mmenipa urahisi” George aliwaambia.
Hapo ndipo uvumilivu wa George ulipoanza. Mwezi wa kwanza ukakatika, wa pili ukakatika na wa tatu nao ukakatika. Uvumilivu bado ulikuwa ukiendelea moyoni mwake. Hatimae mwaka ukakatika. George hakutaka kuwa na uhusiano na msichana yeyote, alikuwa akimsubiria Annastazia.
Miezi bado iliendelea kukatika na hatimae miezi tisa kukatika. Ni miezi mitatu tu ndio ambayo ilikuwa imebaki hata kabla Annastazia hajarudi nchini Tanzania na kuanza maisha mapya huku lengo lake likiwa ni kujifundisha kuhusu siasa na miaka mitano ijayo agombee ubunge katika uchaguzi mkuu.
“Kama nimeweza kuvumilia kwa muda wa mwaka mmoja na miezi tisa, hakika miezi mitatu haitonishinda, nitaendelea kumsubiria” George alijisemea.
Kuhusika kwa wazazi wa pande zote mbili ndio ilikuwa sababu ambayo ilimpa nguvu kwa kuona kwamba kwa vyovyote vile ni lazima Annastazia angekubali na kuwa nae kabla ya kumuoa na kuwa mume na mke.
****
Mapenzi kati ya Andy na Annastazia yalikuwa yakiendelea kama kawaida, kwao mapezi yalionekana kuwa na furaha na kamwe hawakuipa mioyo yao kufikiria kama kuna watu walikuwa wakiumizwa katika mahusiano.
Walipendana na kuthaminiana huku wakipeana ahadi za kuishi milele huku wakiwa pamoja. Maneno yale ambayo yalikuwa yakitoka mara kwa mara vinywani mwao yalikuwa yakionekana kuendana sana na matendo ambayo walikuwa wakiyaonyesha. Mitihani ya mwisho ikafika na hatimae kumaliza. Andy hakuwa na jinsi, alichokifanya ni kumpeleka Annastazia nyumbani kwao na kumtambulisha kwa wazazi wake.
“Umeamua kumchukua Mtanzania kama mama yako?” Bwana Wayne aliuliza.
“Ndio. Nimefuata kile ambacho baba alikifuata nchini Tanzania” Andy alijibu na kuwafanya wote kuanza kucheka sebuleni pale.
“Tuna mapenzi ya kweli sana. Ninauunga mkono uamuzi wako mtoto wangu” Bi Happy alimwambia Andy.
Annastazia alionekana kuwa na furaha, kutambulisha ndani ya nyumba ya tajiri Wayne ilionekana kuwa furaha kwake na kuwa kitu ambacho hakuwahi kukitarajia katika maisha yake. Kitu ambacho alikiahidi mbele ya uwepo wa watu hao ni kumpenda Andy kwa moyo wa dhati katika maisha yake yote.
Wote wakajiona kuwa huru, wakawa radhi kuyaonyesha mapenzi yao mbele ya mtu yeyote, kitendo cha wazazi wa Andy kukubali kilionekana kuwapa faraja kupita kawaida. Kazi ilikuwa imebaki moja tu, kuwaelezea wazazi wa Annastazia kile ambacho kilikuwa kimetokea katika maisha yake katika kipindi ambacho alikuwa nchini Marekani.
“Itanibidi kuelekea nchini Uingereza, kuna vitu inabidi niende kuviangalia. Waambie wazazi wako kila kitu na kunipa taarifa ya kilichoendelea” Andy alimwambia Annastazia.
Baada ya siku tatu, Andy akasafiri kuelekea nchini Uingereza kama moja ya matembezi yake kabla ya kujiunga na chuo cha Oxford ambacho kila siku kilikuwa kichwani mwake. Hakuwa na wasiwasi na mpenzi wake, kitu ambacho alikuwa akikiamini ni kwamba wangekubaliwa na hatimae kufunga ndoa katika kipindi ambacho watakuwa wakiendelea na masomo ya chuo.
Siku nne baadae, Annastazia akaanza safari kuelekea nchini Tanzania. Moyo wake ulikuwa ukimfikiria mpenzi wake na namna ambayo angewaambia wazazi wake. Hakufikiria kama wazazi wake wangekataa kutokana na baba yake Andy kuwa maarufu na tajiri mkubwa duniani.
Kitu ambacho alikuwa akikitaka kwa wakati huo ni kuwaeleza juu ya moyo wake. Katika kipindi chote ambacho aikuwa chuoni, kamwe hakuwahi kumfikiria George ambaye alikuwa akimsumbua sana, moyo wake ulikuwa ukimfikiria mtu mmoja tu, Andy.
Mara baada ya kumaliza kila kitu alichokifuatilia nchini Uingereza, Andy akaamua kuanza safari kuelekea nchini Tanzania huku lengo lake likiwa moja tu. Katika maisha yake yote, alichagua kuwa raia wa Tanzania, aliamua kuchukua uraia wa mama yake kwa kuwa alitaka kuwa karibu sana na Annastazia.
Kila kitu alikuwa akikifanya kwa siri kubwa sana. Kwa sababu alikuwa na vyeti vya kuzaliwa wala hakuwa na pingamizi lolote, alihesabika na kuwa mmoja wa Watanzania kama ilivyokuwa kwa Watanzania wengine.
Hakutaka kuwasiliana na Annastazia katika kipindi ambacho alikuja nchini Tanzania kisiri, alichokifanya mara baada ya kumaliza taratibu zote ni kurudi nchini Marekani na kuamua kuwaambia wazazi wake. Bwana Wayne akaonekana kukasirika lakini hasira zake hakutaka kuzionyesha waziwazi kwa sababu alijua kwamba mtoto wake alikuwa amefanya uamuzi ambao aliuona kufaa katika maisha yake.
“Maisha yangu yatakuwa nchini Tanzania tu. Nitahitaji kuwa karibu na mpenzi wangu” Andy aliwaambia wazazi wake ambao wala hawakuwa na kipingamizi zaidi ya kumtaka kuanza masomo ya chuoni huku kiu yake ikiwa ni kutaka kuwa dokta wa viumbe hai, yaani wanyama na binadamu kwa ujumla.
“Nadhani hapa ndipo Annastazia atajua ni kwa jinsi gani ninampenda’ Andy alijisemea huku akiziangalia picha za Annastazia katika kompyuta yake.
Annastazia akawa na kiu kubwa ya kutaka kuwaona wazazi wake, kilikuwa kimepita kipindi kirefu sana pasipo kuwaona zaidi ya kuongea nao simuni tu. Ndani ya ndege alionekana kuwa na presha kubwa, aliiona ndege ikienda kwa mwendo wa taratibu sana.
Kwanza alikuwa na kiu kubwa ya kuwaambia wazazi wake juu Andy ambaye alionekana kuwa kila kitu kwake. Alikuwa na uhakika wa asilimia mia moja kwamba wazazi wake wangekuwa pamoja nae bila kipingamizi chochote.
Ndege ilichukua masaa kadhaa na ndipo ikaanza kutua katika uwanja wa ndege wa Mwl Julius Kambarage Nyerere ndani ya jiji la Dar es Salaam. Annastazia akaanza kuchungulia kwa nje kupitia kidirisha kidogo ambacho kilikuwa katika upande wake.
Ndege ikasimama na hatimae abiria kuruhusiwa kutoka ndani ya ndege hiyo. Annastazia aliuona mwili wake ukimtetemeka huku kwa mbali kijasho kikionekana kumtoka. Katika kipindi hicho, alikuwa na kiu kubwa sana ya kuwaona wazazi wake kwa mara nyingine tena.
Abiria wakaanza kuteremka katika ngazi za ndege ile huku wakitakiwa kutotoka nje ya jengo la uwanja wa ndege kabla ya mizigo yao kuchunguzwa. Wakatoka mikono mitupu ndani ya ndege ile huku gari maalumu likifika mahali hapo na kuchukua mizigo yao.
Akaanza kupiga hatua za haraka haraka, ingawa alikuwa amebakiza hatua chache kuwaona wazazi wake lakini kwake zikaonekana kuwa hatua nyingi. Alimuona abiria aliyekuwa akitembea mbele yake kutembea kwa mwendo wa taratibu kupita kawaida, alitamani kumpita na kuwa wa kwanza.
Mara baada ya mizigo kuchunguzwa, abiria wakaichukua mizigo yao na kuelekea sehemu ambayo ndugu zao na marafiki walikuwa wamekaa wakiwasubiri. Ghafla, Annastazia akaanza kukimbia kuwafuata wazazi wake na kisha kuwakumbatia kwa furaha.
Kuwaona wazazi wake kwa mara nyingine lilionekana kuwa tukio kubwa na la kipekee katika maisha yake, furaha ikaonekana kumzidi, akajikuta akianza kutokwa na machozi. Wakakumbatiana kwa sekunde kadhaa na kisha kuachiana.
Hapo ndipo alipogundua kwamba wazazi wake walikuwa wamekuja na mtu mwingine mahali hapo, huyu alikuwa George. Annastazia akaonekana kushtuka, hakuamini kumuona George mahali hapo. Huku akionekana kushangaa, akayapeleka macho yake kwa wazazi wake, tabasamu pana yalikuwa yakionekana nyusoni mwao.
“Karibu Annastazia...” George alimkaribisha Annastazia.
“Asante” Annastazia alisema na kisha kulichukua begi lake.
Furaha yote ambayo alikuwa nayo katika kipindi kichache kilichopita ikatoweka moyoni mwake, uwepo wa George mahali pale ulionekana kumkasirisha. Kwa kipindi hicho alikuwa akikumbuka mbali sana toka katika kipindi ambacho George alikuwa akimfuatilia na kumkataa.
Wakaingia ndani ya gari, Annastazia hakutaka kuongea tena, muda wote macho yake yalikuwa yakiangalia nje kupitia dirishani. Alionekana kukasirika, uwepo wa George mahali pale ulionekana kumkasirisha kupita kawaida.
Gari likafunga breki nje ya nyumba kubwa ya kifahari, geti likafunguliwa na gari kuingizwa ndani. Annastazia akateremka na moja kwa moja kuelekea chumbani kwake. Bado alionekana kutokuwa katika hali ya kawaida, mama yake akaanza kupiga hatua kumfuata kule chumbani alipokuwa.
Annastazia alikuwa amelala kifudi fudi huku uso wake ukiangalia pembeni, mama yake akaingia na kukaa karibu nae pale kitandani. Bado ukimya ulikuwa umemtawala Annastazia, hakuongea kitu chochote kile zaidi ya kumwangalia mama yake kana kwamba hakuwa akimfahamu.
“Mbona umebadilika hivyo?” Bi Sara aliuliza.
“Nahitaji muda wa kupumzika mama” Annastazia alimwambia mama yake.
Ingawa Bi Sara alionekana kufahamu kile ambacho kilikuwa kimememsababisha binti yake kuwa katika hali hiyo, akaamua kutoka ndani ya chumba kile na kuelekea sebuleni. Uso wake ulikuwa ukionyesha tabasamu pana, kwake aliona kwamba kazi wala haikuwa kubwa kama ambavyo walikuwa wakifikiria kabla.
“Kidogo uwepo wako umeonyesha mafanikio” Bi Sara alimwambia George.
“Mmh!”
“Mbona unaguna?”
“Inawezekana kweli? Hali yake haikuwa ya kawaida kabisa” George alisema.
“Hiyo niachie mimi. Unajua imekuwa kama suprise kwake, hata kama ningekuwa mimi ningekuwa katika hali kama yake” Bi Sara alimwambia George.
Siku hiyo Annastazia hakutoka chumbani kwake, alijifungia muda wote. Moyo wake bado haukuwa na furaha hata kidogo, kadri picha ya George ilivyokuwa ikimjia kichwani mwake ilionekana kumkasirisha. Moyo wake haukutokea kumpenda George wala kuvutiwa nae.
Wazazi wake hawakutaka kuvumilia kumuona akiwa kwenye hali hiyo, walichokifanya ni kumuita na kuongea nae sebuleni. Annastazia hakutaka kuwaambia ukweli wazazi wake japokuwa alikuwa akifahamu fika kwamba wazazi wake walikuwa wakifahamu kila kitu.
“Ni mchoko tu” Annastazia aliwaambia.
Huo ndio ukawa mwanzo wa maisha yaliyokuwa na karaha, Annastazia hakuwa na raha tena, uwepo wa George ambaye alikuwa akifika nyumbani hapo mara kwa mara ulionekana kumkasirisha kupita kawaida. Hakumpenda kabisa George ingawa wazazi wake walikuwa wakiulazimisha ukaribu kuwepo miongoni mwao.
Kila alipokuwa akija George nyumbani hapo, Annastazia alikuwa akiitwa na kuachwa sebuleni pamoja na George. Muda wote wa kukaa hapo sebuleni Annastazia hakuwa akiongea kitu chochote kile zaidi ya kuangalia televisheni.
Mapaka kufikia hatua hiyo tayari akaona kulikuwa na kila dalili za pingamizi kutoka kwa wazazi wake kama tu angewaambia kuhusu Andy, alichoamua ni kukaa kimya. Kamwe George hakuchoka kuja nyumbani hapo, kila siku alikuwa akifikia nyumbani hapo.
Bwana Kapama na mkewe, Bi Sara walikuwa wakihakikisha kwamba ukaribu huo unazidi zaidi na zaidi. Baada ya miezi miwilili, Annastazia akajikuta akianza kuongea na George bila kupenda. Wazazi wake wakaona jambo hilo kutokutosha, wakazidi kuwafanya watu hao kuwa karibu zaidi na zaidi hasa mara walipokuwa wakiwapa safari za kwenda katika mikoa ya jirani kama Morogoro na Dodoma huku wakati mwingine wakiwataka kwenda Zanzibar kwa ajili ya matembezi.
Ingawa mara kwa mara alikuwa akiwasiliana na Andy lakini katika hali ambayo hakuweza kuitegemea, akaanza kumsahau Andy. Andy akaanza kuanza kupiga hatua kutoka nje ya moyo wake huku George akianza kuingia ndani.
Baada ya mwezi moja akaanza masomo chuo kikuu huku akisomea sheria. Wazazi wake hawamkutaka kwenda kusoma mbali na Tanzania kwa kuhofia kwamba angeweza kumsahau George hali ambayo ingewasababisha kuanza upya kazi yao.
Mara kwa mara Annastazia alikuwa pamoja na George ambaye alikuwa akimng’ang’ania kama ruba, hakutaka kumpa nafasi ya kupumzika kwani alihofia kumpoteza kwa mmoja wa watoto wa Kitanzania waliokuwa wakiishi Dar es Salaam ambao walikuwa wakisifika kwa tabia za kuchukua wasichana wa watu bila kujali utajiri au elimu.
Kwa mara ya kwanza Annastazia akaruhusu kinywa chake kunyonyana na kinywa cha George. Hapo ndipo alipochanganyikiwa zaidi mpaka kufikia hatua ya kumsahau Andy huku akionekana kusahau kama alikwishawahi kukutana na mtu ambaye alikuwa na jina hilo katika dunia hii.
“Nataka kukuoa haraka iwezekanavyo” George alimwambia Annastazia.
“Hapana. Ni lazima nisome kwanza hata kabla ya harusi” Annastazia alimwambia.
“Kusoma si umekwishasoma mpenzi. Au unataka usome mpaka wapi?” George aliuliza.
“Nitakapoanza kuchukua degrii” Annastazia alijibu.
George hakuwa na jinsi, alichokifanya ni kuwa mvumilivu. Miezi ikakatika huku akionekana kuwa na kiu ya kutaka kumuoa Annastazia na hatimae kumuita mke wake halali wa ndoa. Mwaka wa kwanza ukakatika, mwaka wa pili nao ukakatika, bado George alikuwa na kiu kubwa ya kumuoa Annastazia.
Hatimae mwaka wa tatu ukatimia na kukatika, Annastazia hakuwa na jinsi, kama ambavyo alikuwa ameahidi na ndivyo ambavyo ilitakiwa kuwa. Wakawaambia wazazi wao juu ya hatua ambayo walikuwa wamefikia. Kila mmoja akaonekana kufurahishwa na hatua ile.
“Sisi kama wazazi tunawapa Abdul zote” Wazazi wa pande zote mbili walisema.
Harakati za harusi zikaanza kwa haraka sana. Magazeti yakaanza kuandika hatua kwa hatua jambo ambalo liliwafanya watanzania kuwa na hamu kubwa ya kutaka kuiona harusi hiyo ikifanyika. Fedha zilimwagwa na viongozi mbalimbali wa nchi hii huku harusi ikitarajiwa kuwa ya kifahari kuliko zote ambazo ziliwahi kufanyika katika ardhi ya Tanzania.
Annastazia akaonekana kupata jina kubwa nchini Tanzania mara baada ya kutangaza nia yake ya kuwania kiti cha ubunge wa Kinondoni. Kila mtu alionekana kumkubali Annastazia kutokana na kuwa na changamoto kubwa na elimu aliyokuwa nayo. Ukiachilia hayo yote, jina la baba yake lilikuwa likizidi kumbeba zaidi na kumuweka juu.
Kila kitu ambacho kilitakiwa kufanyika kilifanyika kwa haraka haraka. Mpaka mwezi unakatika kila kitu kilikuwa tayari. Tarehe ya harusi ikapangwa na wasimamizi wa harusi ile wakaandaliwa kabisa. Wapambaji wa ukumbi na wanaharusi walikuwa wameitwa kutoka nchini Afrika Kusini, hakukuwa na sababu ya kuwatumia wapambaji wa hapa na wakati kiasi kikubwa cha fedha kilikuwa kimeandaliwa.
“Siamini kama wiki ijayo tunakwenda kuwa mume na mke” George alimwambia Annastazia.
“Ninataka kuwa na familia yangu sasa” Annastazia alimwambia George.
Wiki moja ikaonekana kuwa kubwa kwa wachumba hao, kila mmoja alionekana kuwa na oresha ya kuona wanafunga ndoa na kuwa mume na mke. Walijua kwamba walikuwa wamepitia mambo mengi katika maisha yao ya nyuma lakini kwa wakati huo walitakiwa kusahau kila kitu.
Siku ambayo ilikuwa ikisubiriwa na Watanzania ikawaida. Watu zaidi ya elfu mbili walikuwa wamekusanyika ndani ya kanisa la Praise And Worship lililokuwa Mwenge jijini Dar es Salaam. Watu zaidi ya elfu saba walikuwa wamebaki nje huku wakifuatilia kile ambacho kilikuwa kinaendelea kupitia televisheni ambazo zlikuwa zimewekwa nje ya kanisa hilo.
Kama kawaida yao, waandishi wa habari hawakuwa nyuma, walikuwa wakiendelea kuchukua na kupiga picha kila tukio ambalo lilikuwa likiendelea mahali hapo. Kila mtu kanisani alionekana kuwa na furaha, kitendo cha kupata nafasi ya kuhudhuria harusi hiyo kilimpa furaha kila mmoja.
Bwana Kapama, Bwana Mtimbi na wake zao walikuwa katika viti vya mbele kabisa huku wakifuatilia kila kitu ambacho kilikuwa kikifanyika kanisani hapo. Viongozi mbalimbali walikuwa wamekusanyika kanisani hapo huku rais wa nchi akiwa mmojawapo. Harusi ilionekana kujaza viongozi wengi wa nchi.
Wanakwaya bado walikuwa wakiendelea kuimba huku wakivuta subira kuwasubiri maharusi. Zilipita dakika thelathini, vigele gele vikaanza kusikika kutoka nje ya kanisa. Hakukuwa na cha kujiuliza kwani kila mtu alijua fika kwamba maharusi walikuwa wamekwishafika mahali hapo.
Kwa haraka bila kupoteza muda, mchungaji Samuel akachukua kipaza sauti na kuwataa maharusi kuingia kanisani hapo. Muziki ukaanza kupigwa na maharusi kuanza kuingia huku wakisindikizwa na watoto waliokuwa na maua. Hatua zao zilikuwa za taratibu sana, flashi za kamera zilikuwa zikiendelea kuwamulika.
Nyuso zao zilikuwa zimetawaliwa na furaha, tukio ambalo lilikuwa linatokea kwa wakati huo lilionekana kuwa tukio moja kubwa na la kukumbukwa kutokea katika maisha yao. Walitumia dakika kadhaa mpaka kufika mbele ya kanisa lile.
Mchungaji akasimama mbele yao. Kitu cha kwanza alichokifanya kabla ya kufungisha ndoa ile ni kuanza kusoma Neno la Mungu. Wanaharusi walikuwa na hamu ya kufungishwa ndoa jambo ambalo waliona kama mchungaji akichelewa kuwafungisha ndoa.
Mchungaji alihubiri Neno la Mungu kuhusu ndoa, ni ndani ya dakika tano tu akawa amekwishamaliza na kutaka pete ziletwe mahali hapo. Mchungaji akazichukua zile pete na kuanza kuziangalia, aliporidhika, akakipeleka kipaza sauti karibu na kinywa chake.
“Kabla sijafungisha ndoa hii, kuna mtu mwenye kuweka kipingamizi ndoa hii isifungwe mchana wa leo?” Mchungaji aliuliza.
Kila mtu kanisani hapo akaanza kuangalia huku na kule kuona kama kulikuwa na mtu ambaye alikuwa amesimama. Kanisa zima lilikuwa kimya, hakukuwa na mtu ambaye alikuwa amesimama. Mchungaji akarudia kwa mara ya pili napo hakukuwa na mtu ambaye alisimama. Mchungaji akaona kutokutosha, akarudia kwa mara ya tatu.
Hakukuwa na mwanaharusi yeyote ambaye alionekana kuwa na wasiwasi mahali hapo ingawa macho yao yalikuwa yakiangalia kila upande huku nyuso zao zikiwa zimetawaliwa na tabasamu. Annastazia hakuonekana kuamini mara baada ya macho yake kutua usoni mwa mtu ambaye alikuwa akimfahamu vilivyo japokuwa alikuwa katikati ya umati wa watu huku akiwa amevaa miwani, alikuwa ANDY.
Andy hakutaka kupoteza muda, akaanza masomo katika chuo kikuu cha Oxford kilichokuwa nchini Uingereza huku akisomea udaktari juu ya viumbe hai wakiwemo binadamu na wanyama. Kila mwanachuo ambaye alikuwa akichukua masomo ambayo alikuwa akichukua alionekana kumuogopa Andy ambaye sifa zake zilikuwa zikivuma kwamba alikuwa hatari.
Kila siku alikuwa akiwasiliana na Annastazia huku akiendelea kumwambia ni kiasi gani alikuwa akimpenda na wala hakutaka uhusiano wao uishie hapo, alitaka awe nae katika maisha yake yote. Baada ya ukali wake darasani kukubalika na kila mwanachuo, wasichana wakaanza kumpenda Andy, wakaanza kujaribu bahati zao.
Msichana wa kwanza ambaye alikuwa akitamani sana kuwa pamoja na Andy alikuwa Marie. Kila siku Marie alikuwa akifanya vitu vingi kama kumpigia simu usiku, kumtumia meseji za mapenzi na hata kumpelekea zawadi za mapenzi lakini Andy hakuonekana kukubaliana nae kwani bado moyo wake ulikuwa ukimpenda sana Annastazia na kamwe hakutaka kumsaliti kama alivyomuahidi.
Marie hakukata tamaa, kila siku alikuwa akijaribu kumfuatailia Andy lakini juhudi zake zote zikagonga mwamba. Mpaka mwaka wa kwanza unaisha bado Marie alikuwa akiendelea kumfuatilia Andy ambaye alionekana kuwa mgumu kujiingiza katika mahusiano ya kimapenzi pamoja nae.
Hapo ndipo Andy alipoanza kuyaona mabadiliko makubwa katika mahusiano yake ya kimapenzi na Annastazia. Kuwasiliana kwa simu kukaanza kupungua na si kama zamani. Alijitahidi sana kumpigia simu lakini wala simu haikuwa ikipatikana.
Alichokifanya yeye ni kuanza kuwasiliana nae kwa kutumia mtandao wa Facebook. Aliwasiliana nae zaidi na zaidi, akakuta mawasiliano yakiwa yamekatika ghafla. Alichokifanya ni kuanza kulitafuta jina la Annastazia Kapama lakini wala hakupatikana hali iliyomaanisha kwamba alikuwa amekwishamblock katika mtandao huo.
Andy akaonekana kukasirika, hakuamini kile ambacho kilikuwa kimetokea, alichokifanya ni kuhamia katika mtandao wa Skype lakini napo huko hali ilikuwa ile ile, katika kila kona ambazo alikuwa akimtafuta Annastazia, hakumuona.
Picha zake alizokuwa nazo katika laptop yake ndio zilikuwa kumbukumbu ambazo alibaki nazo. Kila apokuwa akiziangalia picha zile usiku alijikuta akilia. Hakuamini kama angeweza kumpoteza Annastazia katika hali kama ile ambayo ilitokea.
Maisha yake akayaona yakibadilika, mbele yake akaanza kuona giza. Alitamani sana asafiri na kuelekea nchini Tanzania ambako huko angeweza kuonana na Annastazia na kuanza kuongea nae lakini jambo hilo likaonekana kuwa gumu sana kwake kutokana na masomo ambayo yalikuwa yakimtaka kutokupoteza muda.
Msichana wa pili ambaye alikuwa akimhitaji sana Andy chuoni pale alikuwa Patricia, msichana ambaye alikuwa miss wa vyuo vikuu nchini hapo. Andy bado aliendelea kuwa na msimamo ule ule, kamwe hakutaka kumkaribisha msichana yeyote moyoni mwake na wakati bado alikuwa na Annastazia.
Moyoni alijua fika kwamba bado Annastazia alikuwa kwake na kamwe hakutakiwa kumsaliti hata mara moja, kwake aliona lisingekuwa jambo jepesi lenye kuvumilika kama Annastazia angesikia kwamba amemsaliti.
Kila mwanachuo alimuona Andy kuwa mjinga, uzuri ambao alikuwa nao Patricia ilionekana kuwa ni zaidi ya uzuri, kila mvulana chuoni hapo alikuwa akimhitaji msichana huyo ambaye halikuwa hasikii chochote kwa Andy.
Kama kawaida yao wasichana, Patricia akaanza vituko, kila siku alikuwa akileta vituko vya mahaba kwa Andy lakini wala Andy hakuonekana kujali, kitu ambacho alikuwa akikijali ni masomo na uhusiano wake kwa Annastazia tu.
Uwezo wake mkubwa wa darasani na kufahamu mambo mengi ndio ambao uliwasababisha Waingereza kuanza kumwangalia kwa jicho la tatu. Wakaamua kumuajiri katika hospitali yao huku wakimlipa mshahara mkubwa sana.
Andy alionekana kuwa mtu wa ajabu katika kufahamu mambo mengi kuhusiana na mwili wa binadamu. Wagonjwa mbalimbali ambao walikuwa na magonjwa sugu walionekana kupata suruhisho hasa pale ambapo Andy alipoanzisha dawa yake aliyoiita Androone ambayo ilikuwa ikitibu magonjwa mengi katika mwili wa binadamu.
Dawa hiyo ikaanza kutangazwa katika kila kona duniani, watu wakaanza kuinunua kwa gharama kubwa ambapo Andy akaanza kuingiza kiasi kikubwa katika akaunti yake. Japokuwa Andy alikuwa ameanza kiutani lakini baadae akajikuta akianza kuingiza fedha nyingi sana.
Ni ndani ya miezi sita tayari alikuwa ameingiza zaidi ya paundi milioni mia tano. Maisha kwake yakaanza kubadilika, akaanza kujituma zaidi na zaidi kwani hakutaka kuridhika hata mara moja. Alijua fika kwamba alizaliwa katika ukoo uliokuwa na fedha lakini kamwe hakutaka kufikiria kuhusu fedha hizo, alihitaji kuwa na fedha zake mwenyewe.
Wamarekani wakaonekana kushtuka, kitendo cha Andy kuwa nchini Uingereza na wakati baba yake alikuwa Mmarekani kikaonekana kuwakasirisha, walichokifanya ni kuongea na Bwana Wayne ambaye akaongea na mtoto wake na kisha kurudi nchini Marekani.
Ugomvi ukaanza kutokota kati ya mataifa haya mawili, Uingereza ikaanza kuichukia Marekani kwa kuwa walikuwa wamepokonywa kitu ambacho kilikuwa na uhakika wa kuingiza kiasi kikubwa cha fedha nchini mwao. Andy akawa amerudi nchini Marekani na kuanza kufanya kazi katika hospitali ya Midtown Care ambao ilikuwa ikimlipa kiasi kikubwa cha mshahara mara tatu ya kile alichokuwa akilipwa nchini Uingereza.
“Kuna kazi tunataka kufanya” Mwanaume mmoja alimwambia Andy mara baada ya kuonana nae nyumbani kwake.
“Kazi gani?” Andy aliuliza huku akionekana kuwa na wasiwasi.
“Ninataka kuingiza fedha, kwa hiyo kuna kitu ninahitaji kukifanya” Mwanaume huyo, Dawson alimwambia Andy.
“Bado haujawa muwazi. Kitu gani?” Andy aliuliza.
“Nataka unitengenezee virusi fulani ambavyo vitakuwa vikiingia katika mwili wa mwanadamu kwa njia ya ngono. Tena viwe virusi hatari zaidi ya hivi vya UKIMWI” Dawson alisema.
“Mmmh!” Andy aliguna.
“Usijali. Nitakupa malipo mazuri sana” Dawason alimwambia Andy.
“Umenichanganya. Sasa faida yako hapo itapatikana vipi?” Andy aliuliza.
“Nataka pia unitengenezee dawa yake ya kuua virusi hivyo. Hiyo dawa niwe naimiliki mimi. Kwa kila mtu ambaye atakuwa akiingiwa na virusi hao, dawa nitakuwa nayo mimi, kwa hiyo mimi ndiye nitakayeingiza fedha” Dawson alimwambia Andy.
“Nipe muda nijifikirie” Andy alimwambia Dawson.
“Lakini itawezekana?”
“Asilimia mia moja” Andy alijibu na Dawson kuondoka.
****
Andy bado alikuwa akihitaji fedha za kutosha, japokuwa alikuwa akiingiza kiasi kikubwa cha fedha lakini hakuonekana kuridhika hali ambayo ilimfanya kukubali kuvitengeneza virusi ambvyo alikuwa akivihitaji Bwana Dawson.
Kwanza akalipwa nusu ya malipo na kisha kazi kuanza mara moja. Andy alichukua muda mrefu katika kutegeneza virusi ambavyo baadae vilitakiwa kusambazwa dunia nzima hata kabla ya dawa yake kutangazwa, hivyo ndivyo ilivyotakiwa na Bwana Dawson.
Andy akaanza kushinda katika maabara yake iliyokuwa ndani nyumba yake, masaa yote alikuwa bize akitengeneza virusi hivyo ambavyo vilitakiwa kusambazwa kwa njia ya ngono. Kazi haikuwa ndogo hata mara moja, kila virusi ambavyo alikuwa akivitengeneza vilionekana kuwa si imara, hivyo vilikufa mapema.
Andy akaona kazi kubwa kubwa sana jambo ambalo lilimhitaji kuwa na utulivu zaidi. Wakati mwingine alikuwa akikataa kula mpaka pale ambapo kila kitu kitakapokamilika lakini mwisho wa siku alijikuta akila kutokana na kutumia masaa mengi sana bila mafanikio yoyote yale.
Andy alitamani kuomba ushauri kutoka kwa madaktari wengine lakini jambo hilo lilionekana kuwa gumu kutokana na usiri mkubwa uliokuwepo katika kutengeneza virusi vile. Andy alishinda maabara huku wakati mwingine hata akikatisha kazi zake za kuelekea kazini.
Fedha ambazo alikuwa ameahidiwa kilikuwa kiasi kikubwa cha fedha, alijua fika kwamba alikuwa akienda kuiteketeza dunia lakini kwake hakuonekana kujutia jambo lolote lile, kiasi cha fedha ndicho ambacho kilikuwa kikihitajika kuongeza fedha katika akaunti yake.
Bado kazi ile ilionekana kuwa ngumu kupita kawaida lakini bado alikuwa akiendelea kukomaa kila siku. Kuanzia saa mbili usiku mpaka saa tano usiku ndio ulikuwa muda wake wa mapumziko ambao alikuwa akiutumia katika kupekuapekua mambo mbalimbali katika kompyuta yake.
Andy alitumia kipindi cha wiki tatu na nusu na ndipo alipofanikiwa kuvitengeneza virusi hivyo ambavyo vilionekana kuwa na nguvu kubwa kuliko hata virusi vya UKIMWI. Virusi hivi ambavyo alikuwa amevitengeneza vilionekana kumshangaza hata yeye mwenyewe kwa jinsi vilivyokuwa, vilikuwa vimeambatana ambatana hali iliyomfanya kuvipa jina la Katerpilar.
Furaha ikaonekana kurudi kwa Andy, kidogo akaanza kujisikia amani moyoni mwake, kitendo cha kutengeneza virusi vile kilionekana kuwa kitendo ambacho kilimpa mafanikio makubwa katika kazi yake. Alishinda ndani akila na kunywa huku virusi vile akivihifadhi vizuri hata kabla hajamkabidhi Bwana Dawson kazi yake.
Siku hiyo alishinda akipekua pekua mambo mbalimbali katika mtandao wa Internet. Hapo ndipo alipofikiria kuanza kumtafuta Annastazia katika sehemu mbalimbali hasa katika mitandao ya nchini Tanzania. Hakuwa na uhakika kama angeweza kumuona au kusoma tetesi zozote kuhusiana na msichana huyo ila kitu ambacho alikitaka kukifanya na kuridhika nacho ni kumtafuta tu.
Katika kila website ambayo alikuwa akifungua, hakweza kumuona Annastazia kabisa jambo ambalo lilimfanya kukata tamaa. Hakujua ni kwa jinsi gani angemuona msichana huyo na kumwambia kuhusiana na jinsi alivyokuwa akimhitaji katika maisha yake.
Katika kupekua pekua ndipo alipokutana na tangazo kubwa ambalo lilikuwa likihusu harusi kubwa ya watoto wa Mawaziri ambayo ilitakiwa kufanyika nchini Tanzania. Ingawa alionekana tangazo hilo kutokumhusu lakini akaonekana kuvutiwa nalo hali iliyomfanya kuanza kulisoma.
Andy akaonekana kushtuka kupita kawaida mara baada ya macho yake kutua katika jina ambalo alikuwa akilifahamu vizuri kabisa, lilikuwa jina la ANNASTAZIA KAPAMA. Andy hakutaka kuishia hapo, tayari akaonekana kuwa na mashaka na jina lile hali iliyomfanya kuanza kulibofya jina lile na picha ya Annastazia kutokea.
Andy akaonekana kushtuka, moyo ukaonekana kumuuma kupita kawaida. Alilirudia tangazo lile mara mbili mbili huku akionekana kutokuyaamini macho yake. Hakuamini kama Annstazia ambaye alikuwa akimpenda kwa moyo wake wote alikuwa ameamua kufunga ndoa na mwanaume mwingine na kumuacha peke yake.
Andy akajikuta akiifunika laptop yake na kisha kuinamisha kichwa chini. Mawazo juu ya Annastazia yakaanza kujirudia kichwani mwake, akaanza kukumbuka mambo mengi ambayo alikuwa amefanya na Annastazia toka siku ya kwanza ambayo alikutana nae shuleni mpaka siku ya mwisho kuachana nae, hakuonekana kuamini kama Annastazia alikuwa amemsaliti na kuamua kwenda kwa mwanaume mwingine.
Andy akajikuta akianza kutokwa na machozi, na baada ya sekunde kadhaa akaanza kulia kwa sauti kama mtoto mdogo. Alijuta kwa nini aliamua kuingia katika mahusiano na msichana yule ambaye alimuonyeshea mapenzi na baadae kumletea maumivu makali. Andy hakutaka kukubali, hakutaka kuona harusi ikifungwa na yeye kuwa nchini Marekani, alichokifanya ni kusafiri kuelekea nchini Tanzania.
Ndege ilipotua katika uwanja wa Mwl Julius Kambarage Nyerere, akachukua teksi ambayo ilimpeleka mpaka katika hoteli ya kimataifa ya Serena. Alichukua chumba kimoja na kutulia ndani. Kutokana na harusi ile kuwa kubwa na ya kifahari, ilikuwa ikitangazwa mara kwa mara katika vyombo vya habari ambapo kila wakati Andy alipokuwa akiziona taarifa zile alikuwa akilia kama mtoto.
Maisha yake akayaona yakianza kubadilika, ‘Mauaji’ ndio neno ambalo lilikuwa limeanza kumtawala moyoni mwake, isingewezekana hata mara moja kumuacha msichana yule hai na wakati alikuwa amemuumiza kupita kawaida. Alichotaka kukifanya kwa wakati huo ni kushiriki katika harusi hiyo kwa kuamini kwamba angeweza kumuona Annastazia japo kwa mara moja.
Siku zikakatika na hatimae siku ile kufika. Andy akachukua teksi na kisha kuanza kuelekea katika kanisa lile. Uwepo wa watu wengi ulionekana kumuumiza kwa kuona kwamba kama angekuwa yeye basi watu wangekuwa wengi zaidi ya wale ambao walikuwa wamekusanyika kanisani mule.
Alichokifanya ni kutafuta kiti kimoja kilichokuwa katikati ya viti vingine na kutulia. Muda ulizidi kwenda mbele mpaka katika wakati ambao maharusi wakaanza kuingia ndani ya kanisa lile. Andy akayapeleka macho yake kwa maharusi wale, hasira zikamkaba zaidi mara baada ya kumuona Annastazia akiwa ndani ya shela huku George akiwa pembeni yake.
Andy akainamisha kichwa chake chini na machozi kuanza kumtoka tena, hakuamini kama kweli katika maisha yake alikuwa amesalitiwa. Hakuamini hata kidogo kama Annastazia alikuwa ameamua kumuacha na kumchukua mwanaume mwingine.
Andy akaanza kulia kwa sauti ya chini, moyo wake ulikuwa katika maumivu makali kupita kawaida. Kumuona Annastazia akiolewa na mwanaume mwingine kulimuumiza kupita kawaida. Maharusi wakafika mbele na mchungaji kuanza kuhubiri.
Muda wote Andy alikuwa akimwangalia Annastazia huku akilia, hakuamini kile ambacho alikuwa akikiona mbele yake. Akajiona kutokuwa na kosa lolote kama itatokea siku akimuua Annastazia ambaye alikuwa ameuumiza moyo wake kupita kawaida.
“Kabla sijafungisha ndoa hii, kuna mtu mwenye kuweka kipingamizi ndoa hii isifungwe mchana wa leo?” Mchungaji aliuliza.
Kila mtu kanisani hapo akaanza kuangalia huku na kule kuona kama kulikuwa na mtu ambaye alikuwa amesimama. Kanisa zima lilikuwa kimya, hakukuwa na mtu ambaye alikuwa amesimama. Mchungaji akarudia kwa mara ya pili napo hakukuwa na mtu ambaye alisimama. Mchungaji akaona kutokutosha, akarudia kwa mara ya tatu.
Andy hakutaka kusimama, aliendelea kubaki pale kitini huku akiendelea kumwangaia Annastazia ambaye alikuwa akiangalia huku na kule. Macho yake yakagongana na Annastazia ambaye wasiwasi ukaongezeka zaidi. Mara baada ya mchungaji kuona kwamba hakukuwa na mtu yeyote mwenye kipingamizi, akaifungisha ndoa ile.
Annastazia akajikuta akipoteza furaha yote ambayo alikuwa nayo, kitendo cha Andy kuwa ndani ya kanisa lile akiangalia harusi ile hata yeye kilionekana kumuumiza na kumkumbusha mbali sana. Annastazia alitamani kumfuata Andy na kumuelezea hali ambayo alikutana nayo Tanzania aliporudi lakini hakuwa na nafasi ile tena.
Andy akasimama na kuanza kuondoka. Mikono yake alikuwa amekunja ngumi kwa hasira. Moyo wake ulikuwa na maumivu makali ambayo aliamini kwamba hakuweza kuyapata kabla. Alimchukia Annastazia kuliko wanadamu yeyote katika dunia hii, alikuwa tayari kumuua muda wowote ule.
Akaingia katika teksi ambayo alikuja nayo na kisha kuanza kupelekwa hotelini. Muda wote alikuwa katika hasira kali, alionekana kuvimba kupita kawaida. Mauaji ndiyo ambayo alikuwa akitaka kuyafanya kwa wakati huo. Alipofika hotelini akaingia chumbani na kutulia kitandani.
Bado moyo wake ulikuwa katika maumivu makali, akasimama na kuanza kutembea tembea huku na kule huku akikipiga ngumi kiganja chake kila wakati. Muda wote huo, machozi yalikuwa yakimtoka na baada ya muda kuanza kulia kama mtoto mdogo.
Kifo ndicho kitu ambacho kilistahili kumkuta Annastazia, alipanga kumuua katika kifo cha aina yake kwa kutumia mikonoyake mwenyewe, hakuona sababu ya kumuacha msichana huyo hai, alitaka kumuua kwa gharama yoyote ile.
“Nitakuua...nitakuua...NI LAZIMA NITAKUUA ANASTAZIA....” Andy alisema huku akiendelea kulia kwa maumivu makali moyoni mwake.
Je nini kitaendelea?
Je Andy ataweza kumuua Annastazia kama alivyojiapiza?
Je Andy ataweza kutengeneza virusi hao kwa lengo la kuiteketeza dunia?
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment