Simulizi : Ukweli Wenye Kuuma ( Painful Truth )
Sehemu Ya Tatu (3)
Bwana Wayne alikuwa ametulia kwenye kiti cha baiskeli yake huku macho yake yakiangalia televisheni. Pembeni alikuwepo mkewe, Bi Happy ambaye alikuwa amekilaza kichwa chake kochini. Katika kipindi chote ambacho walikuwa pamoja, maisha yao yalikuwa na furaha japokuwa Bwana Wayne hakuwa na uwezo wowote kitandani.
Uwepo wa mtoto wao, Andy ulikuwa ukiwapa furaha kila siku, mafanikio ya Andy yalikuwa yakimfurahisha kila mmoja. Walijivunia kuwa na mtoto kama Andy ambaye kadri siku zilivyokuwa zikizidi kwenda mbele alikuwa akizidi kusikika katika mafanikio ya watu na kuwa faraja katika mioyo ya wagonjwa.
Bwana Wayne akaonekana kushtuka, akajiweka vizuri na kuikazia macho televisheni. Mkewe, Bi Happy akaonekana kushtuka pia, akakiinua kichwa chake na kuanza kumwangalia mumewe usoni. Alipomuona anaiangalia televisheni ile na yeye akayapeleka macho yake katika kioo cha televisheni ile.
Tangazo la ibada kubwa ya kipekee lilikuwa likionekana katika televisheni ile. Bwana Wayne bado alikuwa akiendelea kuliangalia tangazo lile huku akiyasikiliza maneno ambayo yalikuwa yakitangazwa. Wenye shida na matatizo mbalimbali walitakiwa kuwepo katika ibada hiyo ambayo hufanyika kila Jumapili katika kanisa la Salvation from Christ lililokuwa hapo hapo jijini New York huku mchungaji Gibson Gabriel akitarajia kufanya maombezi siku hiyo.
“Ni lazima twende huko mke wangu” Bwana Wayne alimwambia mkewe, Bi Happy.
“Kwenye hiyo ibada?”
“Ndio. Ninaamini kwamba ugonjwa wangu utaponywa tu” Bwana Wayne alisema.
Moyoni mwake alikuwa na imani asilimia mia moja kwamba ni lazima ugonjwa wake ule ungekwenda kuponywa kama tu angekwenda kufanyia maombezi katika ibada hiyo. Kuanzia hapo siku ya Jumapili akaanza kuiona iko mbali.
Kiu kubwa ya kutaka kushiriki katika ibada hiyo ya maombezi ilikuwa imemkaba kooni, alitamani siku hiyo iwe siku ya maombezi ili aweze kwenda katika maombezi hayo ili nae apate uponyaji ambao angekwenda kuukumbuka katika maisha yake yote.
Ni kweli kwamba ilikuwa imepita miaka ishirini na tano wala hakuwahi kuingia kanisani lakini kwa kipindi hicho wala hakuwa na ujanja wowote ule ilimbidi kuingia kanisani kwani uponyaji ndicho kitu ambacho alikuwa akikihitaji sana.
Siku zikakatika mpaka kufikia siku ambayo alikuwa akiihitaji sana. Asubuhi na mapema akaanza kujiandaa na mkewe, Bi Happy na kisha kuanza kuelekea katika kanisa hilo. Bado imani kubwa ilikuwa moyoni mwake kwamba kama angefanyiwa maombezi basi alikuwa akienda kupokea uponyaji mkubwa maishani mwake.
Dereva akalipaki gari lake nje ya jengo la kanisa hilo, Bi Happy akateremka na kwenda kukitoa kibaiskeli katika boneti na kisha kuanza kumshusha mumewe na kumpakiza kwenye kibaiskeli kile na kisha kuanza kuelekea ndani ya kanisa lile.
Washirika wa kanisa hilo wakabaki wakiwa na mshangao, walikuwa wakimshangaa Bwana Wayne na mkewe. Kila mmoja alitambua kwamba Bwana Wayne alikuwa mtu maarufu sana kutokana na utajiri mkubwa ambao alikuwa nao.
Watu wengine wakachukua simu zao na kuanza kumpiga picha katika kipindi ambacho walikuwa wakiufuata mlango wa kuingia kanisani humo. Kwao ilionekana kuwa jambo gumu sana kukutana na mtu kama Bwana Wayne katika maisha yao, hivyo wakaichukua nafasi hiyo kuwa ya kipekee sana katika maisha yao.
Bwana Wayne na mkewe, Bi Happy wakaingia kanisani na kutulia. Ibada ilikuwa ikiendelea zaidi na mpaka mchungaji Gibson kusimama mbele ya kanisa na kuanza kuhubiri. Katika kila neno ambalo mchungaji Gibson alikuwa akiliongea, Bwana Wayne alikuwa akitikisa kichwa chake kutoka juu kwenda chini na chini kwenda juu.
Mwisho wa siku, Bwana Wayne akajikuta akilia, hakuamini kama kuna siku angesikia maneno matamu yaliyojaa faraja kama yale ambayo alikuwa akiyasikia kutoka kwa mchungaji Gibson. Mchungaji aliendelea kuhubiri mpaka katika kipindi ambacho aliwaita watu waliokuwa na magonjwa mbalimbali kwenda mbele ya kanisa hilo.
Bwana Wayne hakutaka kuchelewa, akaanza kukisukuma kibaiskeli kile na kuanza kuelekea mbele ya kanisa. Hakuwa peke yake mahali pale, zaidi ya watu mia tano walikuwa wamesimama. Mchungaji akawataka wagonjwa wale kushika sehemu ambazo zilikuwa na matatizo. Bwana Wayne akaupeleka mkono wake sehemu za siri.
Maombezi yakaanza hapo. Mchungaji Gibson akaanza kufanya maombezi, alichukua dakika tano, akawaruhusu wagonjwa wale kwenda kukaa katika sehemu zao huku akiwataka kuamini kwamba walikuwa wamepokea uponyaji.
Hiyo ndio ilikuwa siku ambayo ikayabadilisha maisha ya Bwana Wayne na mkewe, kila siku walikuwa watu wa kwenda kanisani huku mioyoni wakiamini kwamba Mungu alikuwa na mipango na maisha yao. Hali ya Bwana Wayne haikubadilika, iliendelea kuwa vile vile lakini moyoni alikuwa akiamini kwamba kuna siku agepokea uponyaji.
Bwana Wayne akaanza kujiingiza katika kumtumikia Mungu, alichokifanya ni kuanza kutoa kiasi kikubwa cha fedha kusaidia vituo mbalimbali vya uchungaji duniani. Kitu ambacho alikuwa amekipanga kwa wakati huo ni kumtumikia Mungu kwa njia tofauti tofauti kwani aliamini kwamba Mungu ameyabadilisha maisha yake kwa kumuokoa kutoka dhambini.
****
Andy hakutaka kuendelea kukaa nchini Tanzania, alichokifanya ni kuondoka kuelekea nchini Marekani huku moyo wake ukiwa katika maumivu makali kupita kawaida. Akatokea kumchukia Annastazia kuliko mtu yeyote katika dunia hii, hakutaka kumuona akiendelea kuvuta pumzi ya dunia hii tena.
Alitaka kujipanga na kummaliza msichana huyo ambaye alikuwa ameuumiza moyo wake kupita kawaida. Hakujali gharama ambazo angetumia katika kumuangamiza Annastazia, kitu ambacho alikuwa akikitaka ni kumuona Annastazia akifa mbele ya macho yake.
Nchini Marekani, akili yake wala haikutulia, kazi ambayo alikuwa amepewa na Dawson hakuwa amemkabidhi ingawa virusi vilikuwa vimekamilika. Alichokifanya katika kipindi hicho ni kuanza kutafuta dawa ya kuviua virusi hivyo.
Hiyo ndio ilikuwa kazi kubwa kuliko ile ya kutengeneza virusi. Alitumia kila njia katika kutengeneza dawa za virusi vile lakini hali ilionekana kuwa tofauti, dawa haikupatikana kabisa. Virusi ambavyo alikuwa amevitengeneza vilikuwa vikali sana kiasi ambacho dawa yake ilikuwa ni kazi kubwa sana kuitengeneza.
Tofauti na matarajio yake, Andy alichukua zaidi ya miezi miwili lakini bado hakupata dawa husika. Kichwani mwake hakuwa akimfikiria Annastazia tena, alikuwa akifikiria kuhusu kutengeneza dawa tu. Mara kwa mara Dawson alikuwa akiwasiliana nae lakini hakuweza kumgawia mzigo wa virusi wale mpaka pale ambapo angeweza kupata dawa yake.
Bwana Dawson aliendelea kusubiri zaidi na zaidi, miezi iliendelea kukatika huku Andy akiwa bize kutengeneza dawa mbalimbali lakini bado virusi wale hawakuweza kufa. Kazi ilionekana kuwa kubwa kuliko alivyofikiria kabla, Bwana Dawson hakukata tamaa bado alikuwa akiendelea kuamini kwamba dawa zingepatikana tu.
Mwaka ukakatika na ndipo Andy akawa amefanikiwa kupata dawa ambayo ilikuwa na uwezo mkubwa wa kuua virusi vile. Bwana Dawson akaonekana kuwa na furaha, hakuamini hata mara moja kama angefanikiwa kupata kile alichokuwa amekihitaji kwa muda mrefu.
Alichokifanya ni kuanza majaribio ya vile virusi. Alichokifanya ni kuanza kuelekea katika mitaa kadhaa jijini New York. Akawatuma vijana wake kuanza kuwateka watu na kisha kuwachoma sindano zile zilizokuwa na virisi. Alijua kwamba alikuwa akifanya dhambi ya uuaji lakini wala hakuonekana kujali, kitu ambacho alikuwa akikijali kwa wakati huo ni fedha tu.
Alichokifanya Dawson ni kuwaambia wasaidizi wake kuwatafutia watu ambao wangewachoma sindano ambazo zilikuwa na virusi vile. Walipowapata, wakawachoma na kuanza kuwafuatilia kujua hali zao zingeendelea vipi.
Kutokana na virusi vile vya Katerpilar kuwa na ukali mkubwa sana hata zaidi ya virusi vya UKIMWI, ni ndani ya wiki mbili tu, watu wale walikuwa wakikohoa kupita kawaida huku miili yao ikianza kukonda. Virusi wale walionekana kuwa na nguvu kubwa sana hata zaidi ya vurusi vya UKIMWI. Alichokifanya mara baada ya watu wale kuumwa kupita kawaida, akawateka tena na kisha kuwagawia dawa zile.
Dawa zile zikaonekana kuwapa nguvu, afya zao zikaanza kurudi kama zamani na kujikuta wakiwa na afya njema. Bwana Dawson akaonekana kuwa na furaha kupita kawaida kwani hakuamini kama kazi ingekuwa rahisi namna ile.
Kutokana na furaha kubwa ambayo alikuwa nayo, akampa Andy fedha zaidi kwani kwake ilionekana kuwa ushindi mkubwa ambao wala hakuutegemea hata siku moja. Mara baada ya kukamilisha kila kitu, akaanza kusubiri kuona ni kitu gani ambacho kingeendelea.
Katika kipindi ambacho alikuwa amewachoma wale watu sindano zile, wao wakafanya mapenzi na wapenzi wao pamoja na wake zao na kuwaambukiza ugonjwa ule. Kutokana na wake zao kutokuwa waaminifu wakajikuta wakianza kuusambaza ugonjwa ule.
Nchi ya Marekani ikaonekana kushtuka mara baada ya ugonjwa mpya kuanza kuingia katika nchi yao. Ugonjwa ule ukaanza kushambulia kwa kasi kubwa huku ukiwa na nguvu kushinda hata UKIMWI. Kazi kubwa ikaanza kwa madaktari katika kuitafuta tiba ya ugonjwa ule ambao ulionekana kuanza kuwa tishio kubwa.
“Kabla ya kutafuta dawa itatubidi kutafuta jinsi unavyoingia kwa binadamu” Dokta Huth aliwaambia waandishi wa habari.
Jopo la madaktari likawa limekusanyika katika ukumbi mkubwa ndani ya hospitali ya Caspean Care Centre. Dr Andy nae alikuwa pamoja nao huku akijifanya kutokuelewa kitu chochote ambacho kilikuwa kinaendelea, kwa kumwangalia, kamwe usingeweza kuhisi kama yeye ndiye ambaye alikuwa ameutengeneza ugonjwa ule ambao ulionekana kuongezeka kasi zaidi na zaidi.
Taarifa kwamba ugonjwa ulikuwa ukienezwa kwa njia ya kufanya ngono zembe ikatangazwa na hivyo watu kuambiwa kuwa makini kufanya ngono kwa kutumia mipira ya kondomu. Kwa walioelewa walielewa lakini wale ambao walijifanya kuwa wagumu kuelewa walikuwa wakiendelea kufanya ngono bila mipira ya kondomu kama kawaida.
Ugonjwa huo ukaanza kuenea zaidi na zaidi. Ukatoka katika jiji la New York na kuhamia jijini Washington. Bado uliendelea kuenea zaidi na zaidi huku ukiendelea kuua watu kama kawaida. Mwishowa dunia ukaonekana kuanza kukaribia.
Ni ndani ya mwezi mmoja tu, ugonjwa ule ukaenea katika bara lote la Marekani ya Kaskazini huku ukianza kuingia katika bara la Marekani ya Kusini. Kila mtu akaonekana kuwa na tahadhari, wasiwasi ukaonekana kuwa mkubwa katikati ya Wamarekani.
Madaktari waliangaika usiku na mchana lakini wala tiba haikupatikana, kila siku watu walikuwa wakizidi kuambukizwa ugonjwa huo. Dr Andy hakusema kitu chochote kile, kwa jinsi ilivyomchukua mwaka mzima mpaka kupata tiba ya dawa ile, hakuwa na uhakika kama kungekuwa na daktari ambaye angefanikiwa kuipata tiba ya ugonjwa ule mkali
Bwana Wayne alikuwa akiendelea kumtumikia Mungu kama kawaida, alikuwa ameamua kujitolea asilimia mia moja kumtumikia Mungu katika kipindi chote cha maisha yake. Bado alikuwa akiendelea kutoa misaada katika vyuo mbalimbali vya Biblia hasa vilivyokuwa barani Afrika.
Katika kila kitu ambacho alikuwa akikifanya, mkewe, Bi Happy alikuwa pamoja nae akimsaidia kwa kila kitu. Mapenzi kati yao yalikuwa yakiongezeka kila siku, walijiona kama kuanza upya. Mtoto wao, Andy hakuwa pamoja nae, alikuwa ameanza maisha yake kama mtu alikuwa akijitegemea. Hawakutaka kuyafuatilia maisha yake japokuwa walikuwa wakiendelea kuwasiliana nae kila siku.
“Mke wangu, ninajisikia tofauti fulani mwilini mwangu” Bwana Wayne alimwambia mkewe, Bi Happy.
“Tofauti gani?” Happy aliuliza.
“Nafiikiri Mungu Ametenda”
“Ametenda nini?” Bi Happy aliuliza.
Alichokifanya Bwana Wayne ni kuanza kukiendesha kibaiskeli chake kuelekea nae chumbani huku akimtaka mkewe kumfuata. Moyoni alikuwa na uhakika asilimia mia moja kwamba tayari Mungu alikuwa ametenda muujiza katika mwili wake. Mara baada ya kufika chumbani, akamtaka mkewe kukaa kitandani.
“Mungu Ametenda” Wayne alimwambia mkewe.
Alichokifanya akaivua suruali yake na nguo yake ya ndani, kitu ambacho kilionekana mbele ya macho ya Happy hakikuweza kuaminika hata kidogo. Ugonjwa ambao alikuwa nao miaka mingi iliyopita ukaonekana kupotea katika maisha yake, uume wake ulionekana kusimama.
Bwana Wayne akabaki akitoa machozi tu, alimwangalia mkewe pale kitandani lakini akashindwa kufanya kitu chochote kile, alibaki akilia tu. Akainama na kuushika mshipa ambao ulikuwa ukiufanya uume usimame, bado ulikuwa umekatika.
Ulikuwa ni muujiza mkubwa ambao hata kama angekuwa daktari gani angeweza kuushangaa. Halikuwa jambo ambalo liliwezekana kwa asilimia hata kumi kwa uume kusimama na wakati mshipa wake bado ulikuwa umekatika.
Bi Happy akasimama na kisha kuanza kumsogelea Bwana Wayne ambaye bado alikuwa akiendelea kulia kwa furaha. Akasimama pembeni yake na kisha kuanza kumbembeleza. Kwao ulionekana ni muujiza mkubwa ambao wala hawakuwa wameutarajia kabla.
“Hatimae Mungu Ametenda. Nitaendelea kumtumikia milele kama malipo yangu kwake” Bwana Wayne alisema huku akionekana kuwa na furaha.
Hiyo ndio ikawa siku ya kwanza kufanya mapenzi mara baada ya kupita miaka zaidi ya ishirini. Walifanya kwa zaidi ya dakika arobaini kitandani, kila mtu akajiona kuwa kama mtu ambaye alikuwa amezaliwa upya. Kama kuonyesha shukrani kwa Mungu wao, wakaahidi kumtumikia milele katika maisha yao yote.
Wakaanza upya kumtumikia Mungu kwa kuendelea kutoa misaada katika vyuo vya Biblia pamoja na katika vituo mbalimbali hasa vya watoto yatima vilivyokuwa barani Afrika. Kila siku maisha yao yalikuwa ya furaha, walikuwa na uhakika wa kufanya mapenzi muda wowote na sehemu yoyote ambayo walijisikia kuwa huru.
Japokuwa bado alikuwa mlemavu lakini Bwana Wayne hakuonekana kujali kitu chochote kile, bado alikuwa akiendelea kumtumikia Mungu. Kwake, Mungu alikuwa amefanya mambo mengi sana ambayo aliona kuyatoa maisha yake kwa ajili ya kumtumikia katika kipindi chote cha maisha yake.
“Nataka kuwa mchungaji. Najisikia kuitwa katika huduma hiyo” Bwana Wayne alimwambia mkewe ambaye kwa mbali akaonekana kushtuka.
“Unasemaje?”
“Najua umenisikia mpenzi. Tatizo lako moja tu, hautaki kuamini kile nilichokwambia” Bwana Wayne alimwambia Bi Happy.
“Nakuamini Mume wangu. Mungu amekuwa pamoja nasi katika kipindi chote. Namuamini Mungu kwa kila kitu, ila naomba ujue kwamba ninakuamini pia” Bi Happy alimwambia mumewe.
“Nitahubiri huku nikiwa katika kibaiskeli changu. Watu wengi wataponywa magonjwa yao” Bwana Wayne alimwambia Bi Happy.
“Naamini hilo”
“Naomba kukuuliza kitu mke wangu” Bwana Wayne alimwambia Bi Happy.
“Kitu gani?”
“Unajua kwamba sisi binadamu tunapotegeneza vitu huwa na spea? Yaani namaanisha vitu vya akiba?” Bwana Wayne aliuliza.
“Nafahamu”
“Basi amini kwamba hata miili yetu pia ina spea. Binadamu ametengeneza spea katika magari na vyombo vingine. Basi Mungu nae ana spea za miili yetu. Utakapotoboka jicho, kama ukimtumikia, atakupa spea ya jicho lako. Hata kwa sisi walemavu, najua Mungu ana spea za miguu yangu, na ninaamini kuna siku atanipa spea zangu kama nikiendelea kumtumikia katika maisha yangu” Bwana Wayne alimwambia mkewe.
Bi Happy hakuongea kitu, maneno ambayo aliyaongea mumewe yalionekana kumgusa, machozi yakaanza kumtoka. Hiyo ndio ilikuwa mara yake ya kwanza kugundua kwamba hata viungo vya binadamu huwa na spea za pembeni. Yalikuwa ni maneno ya kawaida lakini yaliyokuwa yamemgusa kupita kawaida.
Baada ya miezi miwili, Bwana Wayne akaanza kusomea uchungaji huku lengo lake kubwa likiwa ni kumtumikia Mungu katika maisha yake yote. Alitaka kuwahubiria wale ambao hawakuwa wameokoka waweze kuokoka na hata wale ambao katika maisha yao hawakuamini kwamba Mungu Yupo basi waamini.
“Natumaini hata watoto wetu wataokoka pia” Bwana Wayne alimwambia Bi Happy.
“Tuzidi kuwaombea Mungu” Bi Happy alijibu.
****
Watu walizidi kuteketea mwa kasi ya ajabu, ugonjwa wa kisasa ambao ulipewa jina la PENINA ulikuwa ukizidi kuua watu kadri siku zilivyokuwa zikizidi kwenda mbele. Madaktari hawakutaka kukata tamaa, bado walikuwa wakiendelea kutafuta tiba usiku na mchana. Mpaka miezi miwili inakatika, tayari watu zaidi ya milioni moja walikuwa wamekwishaambukizwa virusi hivyo nchini Marekani.
Watumishi wa Mungu wakaingia katika maombi ya kumuomba Mungu Aiepushe dunia na ugonjwa huo ambao ulikuwa ukitisha hata zaidi ya UKIMWI. Kila siku watu wa dini mbalimbali duniani walikuwa wakimuomba Mungu lakini hali bado ilionekana kuwa mbaya.
Tiba ilikuwa ngumu kupatikana huku watu wakizidi kuambukizana na kufa. Hakukuwa na kimbilio, ili kujikinga na ugonjwa wa PENINA basi ilikuwa ni lazima uache kufanya ngono au kama ulikuwa ukitaka kufanya basi utumie kinga maalumu.
Miezi mitano ikakatika na ndipo alipokuja kuibuka mtu ambaye akaonekana kuwa mkombozi wa dunia hii. Dunia nzima ikaonekana kukuamini kama mtu huyu aliyejiita jina la Martin Dowson alikuwa ameletwa na Mungu duniani kwa ajili ya kuwafuta machozi watu ambao walikuwa wakilia kila siku kwa sababu ya ugonjwa wa PENINA.
Dawson ndiye ambaye alikuwa ametangaza dawa ya kutibu ugonjwa huo ambao ulikuwa umeanza kuingia barani Ulaya na kuanza kusambaa kwa kasi ya ajabu. Kitu cha kwanza walichokifanya madaktari wakubwa ni kuipeleka dawa hiyo katika mahabara zao na kisha kuanza kuichunguza, ilionekana kufaa.
Wakatafutwa watu wanne ambao walikuwa wakiugua ugonjwa huo na kisha kuchomwa sindano iliyokuwa na dawa hiyo. Baada ya siku tatu kupita, afya zao zikaonekana kuwa nzuri na walipokuja kupimwa, hawakuwa na virusi vya Katapilar.
Madaktari wakuu wakaitangazia dunia kwamba tiba ilikuwa imepatikana na ilikuwa ikipatikana katika hospitali zote kubwa Marekani ya Kaskazini na Kusini pamoja na Ulaya. Katika wiki ya kwanza tu ambapo dawa hiyo ilikuwa imeuzwa, Bwana Dawson ambaye alijitangaza kuwa dokta aliingiza kiasi cha dola bilioni moja.
Kwake kilikuwa ni kiasi kikubwa cha fedha ambacho wala hakuwa amekitegemea kabla. Alichokifanya baada ya hapo ni kuanza kuwasiliana na Andy kwa ajili ya kutengeneza dawa zaidi. Kwa kuwa bado alikuwa akilipwa kiasi kikubwa cha fedha, Andy akatengeneza dawa hizo ambazo zilikuwa zikiendelea kusambazwa.
Bwana Dawson aliendelea kuingiza kiasi kikubwa cha fedha kiasi ambacho baada ya mwaka mmoja, akawa tajiri wa ishirini duniani. Matajiri wakubwa duniani wakaanza kuona mwanamapinduzi akiwa ameingia katika orodha yao. Kila siku walikuwa wakijitahidi kuweka vikwazo vya hapa na pale lakini bado Dawson alikuwa akija kwa kasi ya ajabu.
Kila kitu ambacho kilikuwa kikiendelea kilibaki kuwa siri ya watu wawili tu, Andy na Dawson mwenyewe. Hakutakiwa mtu yeyote afahamu ni kitu gani kilikuwa kinaendelea, na kama kungeuwa na mtu ambaye angefahamu ukweli, basi haikuwa budi kummaliza.
Ugonjwa ulikuwa ukizidi kusambaa lakini nazo dawa zilikuwa zikizidi kusambazwa. Serikali mbalimbali duniani zilikuwa zikiendelea kutoa kiasi kikubwa cha fedha kwa ajili ya kununua dawa hizo ambazo zilikuwa zikipekwa katika hospitali kubwa.
“Ni lazima nirudi tena Tanzania” Andy alisema.
Ulikuwa ni uamuzi wa haraka ambao wala haukuhitaji ushauri wowote ule. Kichwani kwake, jina la Annastazia lilikuwa limemjia tena kichwani mwake. Ingawa mwaka mmoja ulikuwa umepita tangu Annastazia afunge harusi na mwanaume mwingine mbele ya macho yake, lakini bado hasira zake zilikuwa juu ya mwanamke huyo.
Hakumpenda tena Annastazia, alitamani atengeneze virusi vingine na kisha kwenda kumchoma sindano mwanamke huyo na kuingiwa na virusi hivyo. Kwake, Annastazia alionekana kuwa adui namba moja katika maisha yake. Andy aliona ni afadhari kuwa na mapenzi ya dhati na shetani kuliko kuwa na mapenzi ya dhati na Annastazia.
“Kwanza nikiingia Tanzania. Kitu cha kwanza nitamlipua na bomu. Yaani sitaki hata mwili wake uonekane” Andy alisema katika kipindi ambacho alikuwa akiingia ndaniya ndege ya American Airlines tayari kwa kuanza safari ya kuelekea nchini Tanzania kwa ajili ya kumuua Annastazia ili airudishe furaha ambayo ilikuwa imepotea moyoni mwake.
Jua lilikuwa kali huku joto likiwa linaongezeka kadri dakika zilivyozidi kwenda mbele. Vijana ambao mara kwa mara walikuwa wakivaa kaoshi, muda huo ndio ulikuwa wakati wenyewe wa kuvaa vazi hilo ambalo lilikuwa likipendwa kuvaliwa na vijana waliokuwa wakiishi uswahilini.
Wauza maji ambao walikuwa wanabadilisha bishara zao mara kwa mara, kwa wakati huo walikuwa wakiingiza fedha kutokana na biashara yao ya maji yenye baridi kununuliwa kupita kiasi. Kila mtu ndani ya jiji la Dar es Salaam alikuwa akiilalamikia hali ya hewa ambayo haikuwa ikikuruhusu kujiachia chumbani bila kuwa na feni au kiyoyozi.
Ndege ya shirika la American Airlines ilikuwa ikikanyaga ardhi ya jiji la Dar es Salaam Na baada ya muda fulani abiria kuanza kuteremka. Andy alikuwa mtu wa kumi na nane kuteremka, macho yake akayapeleka juu na kisha kuyapeleka katika gari lililokuwa tayari kubeba mizigo ya wasafiri.
Hali ya hewa ikaanza kuonekana kuwa mbaya kwa upande wake, alichokifanya ni kuanza kuondoka kuelekea kule ambapo kulikuwa na mlango mkubwa wa kuingilia ndani ya jengo la uwanja ule wa ndege. Mara baada ya kuruhusiwa kuchukua begi lake, akaanza kuelekea katika sehemu iliyokuwa na teksi nyingi.
Akachukua teksi na kisha safari ya kuelekea katika hoteli ya Moven Pick kuanza. Kitu ambacho alikuwa akikifikiria kwa wakati huo ni namna ya kuweza kumuua Annastazia kama ambayo alikuwa amepanga katika kipindi ambacho alikuwa nchini Marekani.
Mbele yake kulionekana kuwa na kazi kubwa lakini kwa kutumia fedha, aliona kutokuwa na tatizo lolote lile. Alijiona kuwa na uwezo mkubwa wa kumpiga risasi Annastazia na kumuua ila wala hakutaka msichana huyo afe katika kifo hicho. Kumlipua kwa bomu ndicho kilikuwa kifo ambacho alikuwa amekipanga toka alipokuwa nchini Marekani.
Usiku hakulala kwa raha, bado alikuwa akifikiria namna ambayo angeitumia mpaka kupata bomu ambalo angelitega katika gari la Annastazia na kisha kulipuka. Hata kabla hajapata nini kilitakiwa kufanyika, usingizi ukampitia.
Asubuhi hakutaka kuchelewa, kitu ambacho alikuwa amekipanga ni kumtumia mwanajeshi yeyote kwani aliamini kupitia mtu huyo basi asingepata kazi yoyote kupata bomu. Alichokifanya kwa wakati huo ni kuelekea katika kituo cha daladala cha Mwenge ambako huko akabahatika kumpata mwanajeshi mmoja ambaye alikuwa na kitambaa kilichoandikwa MP mkononi.
“Kuna kitu ningependa unisaidie ila sidhani kama tunaweza kuongelea mahali hapa” Andy alimwambia mwanajeshi huyo ambaye alikuwa akitaka kupanda daladala kurudi nyumbani kwake.
Hata kabla mwanajeshi yule hajasema kitu chochote kile akaanza kumwangalia Andy usoni, uso wa wake wala haukuonyesha wasiwasi wowote ule japokuwa alikuwa na uhitaji wa kitu ambacho kilikuwa ni cha hatari.
“Kitu gani?” Mwanajeshi yule aliuliza huku akionyesha kuwa ‘serious’
“Naomba tukutane sehemu. Nitakulipa gharama zote za usumbufu” Andy alimwambia mwanajeshi yule.
Kwa muonekano wa Andy alikuwa akionekana kuwa ni mtu ambaye alitoka nje ya bara la Afrika. Ngozi yake ilikuwa iking’aa huku ikionekana kupata virutubisho vyote mwilini. Mwanajeshi yule tayari akaonekana kugundua kwamba kijana ambaye alisimama mbele yake alikuwa akitaka kufanya nae kazi ambayo ingemuingizia fedha nyingi na za kutosha.
Walichokifanya ni kupanga sehemu ya kukutania na kisha kila mtu kuondoka mahali hapo. Andy alibaki akijifikiria usiku mzima. Kwa kipindi hicho alikuwa na uhitaji mkubwa wa kupata bomu ambalo angelitega katika gari la Annastazia na kisha kulilipua katika kipindi ambacho mwanamke huyo angeingia garini.
Kadri muda ulivyokuwa zikizidi kwenda mbela na ndivyo ambavyo hasira zake juu ya Annastazia zilivyozidi kumpanda. Hakumpenda kabisa Annastazia, alikuwa akimchukia kupita kiasi. Kwake, ilikuwa ni rahisi sana kumpenda shetani kuliko hata kumpenda mtu kama Annastazia.
Tofauti na Annastazia, pia akaanza kuwachukia wanawake wote hasa wanaotoka nchini Tanzania, hakuwapenda kwa kuona kwamba wanawake wote wa Kitanzania walikuwa na tabia kama aliyokuwa nayo Annastazia, usaliti. Badala yakufikiria jinsi ya kumuua Annastazia, pia akaanza kufikiria jinsi ya kuwaua wanawake wote wa Kitanzania.
Siku iliyofuata, akaanza kuwasiliana na mwanajeshi yule na kuonana katika hoteli ya New Africa. Alichokifanya Andy kwa wakati huo ni kutumia fedha tu. Alijua kwamba asilimia kubwa ya Watanzania walikuwa wakiishi katika mazingira ya Kimasikini na hata wale ambao walikuwa wakifanya kazi hawakuwa wakilipwa katika kiwango ambacho kilikuwa kikiwatosha kuwakimu wao pamoja na familia zao.
Fedha kwake ndio ilikuwa silaha kubwa ya maangamizi ambayo angeweza kuitumia katika kila sehemu ambayo alitakiwa kuifanya. Mara baada ya kuonana, moja kwa moja wakaanza mazungumzo yao ambayo yalikuwa yamechukua muda mrefu.
“Unasema unahitaji bomu?” Mwanajeshi yule aliuliza huku akionekana kushtuka.
“Ndio” Andy alijibu huku akionekana kujiamini.
Mwanajeshi yule hakuongea kitu chochote kile, alibaki kimya kwa muda huku akionekana kufikiria kitu. Ombi la Andy kichwani mwake lilionekana kuwa ombi kubwa na zito ambalo wala halikutakiwa kuchukuliwa uamuzi kwa haraka haraka kama ambavyo Andy alikuwa akifikiria.
“Hicho ni kitu kisichowezekana hata kidogo” Mwanajeshi yule aliyejitambulisha kwa jina la Maulid alisema.
“Naomba unisaidie. Nina uhitaji nalo sana” Andy alisema lakini Maulidi hakuonekana kumuelewa hata kidogo.
Tayari Andy aliona mambo kuwa magumu kwa upande wake na hapo ndipo ambapo angeweza kuitumia silaha ambayo alikuwa akiiamini sana. Alichokifanya kwa wakati huo ni kutoa kiasi cha dola elfu tano na kuziweka mezani.
Kiasi hicho cha fedha kilikuwa ni kiasi kikubwa ambacho kingeweza kuwa ni mshara wa mwaka mzima wa Maulidi. Maulidi akabaki akiziangalia dola zile, kwa haraka haraka kichwa chake kikaanza kufanya kazi ya kuzigeuza zile dola kwa mfumo wa shilingi.
“Zaidi ya shilingi milioni sita na nusu” Maulidi alijisemea moyoni.
“Kama utakubali kunifanyia kazi hiyo. Nitakupa dola elfu kumi kama malipo. Kwa ujumla nitatoa kwako dola elfu kumi na tano kama malipo” Andy alimwambia Maulidi.
Hapo ndipo Maulidi alipoonekana kuchanganyikiwa zaidi, kiasi cha fedha ambacho alikuwa amekisema Andy kilikuwa ni kiasi kikubwa ambacho haikuwa rahisi kukataliwa na mtu yeyote ambaye alikuwa akiingiza mshahara wa kawaida. Alijiona kuwa kwa wakati huo Mungu alikuwa amemuona, kitendo cha kwenda katika ghala la silaha na kutoa bomu wala haikuwa kazi kubwa kwake.
“Unahitaji bomu la aina gani?” Maulidi aliuliza.
“La kutegwa. Yaani nataka kulitega kwenye gari fulani hivi. Liwe linaendana na uzito. Yaani uzito ukiongezeka garini basi nalo lilipue muda huo huo” Andy alisema.
“Hapo nimekupata ila bado kuna kitu inabidi kifanyike” Maulidi alisema.
“Kitu gani?”
“Nitakwenda kuongea na mkuu ila tatizo litakuwa moja”
“Tatizo gani?”
“Nae anaweza akahitaji fedha”
“Hilo si tatizo. Unafikiri atahitaji kiasi gani?”
“Kama dola elfu mbili hivi”
“Usijali” Andy alisema na kisha kuingiza mkono mfukoni, alipoutoa, akatoka na dola zilizokuwa na thamani ya Elfu tano na kisha kumkabidhi Maulidi.
“Kwa hiyo tukutane lini unipe mzigo wangu?”
“Tufanye kesho kutwa hapa hapa” Maulidi alisema.
Hapo ndipo ukawa mwisho wa maongezi yao, kila mmoja akaondoka zake. Siku nzima Andy alibaki chumbani akijifikiria, bado kichwa chake kilikuwa kikifikiria kuhusu kumuua Annastazia kwa bomu. Chuki kali bado ilikuwa ikiusukuma moyo wake kumuua Annastazia, tena kifo cha bomu ambacho kingeufanya mwili wake kutokuonekana kabisa.
Siku imbili zilizofuata wakakutana tena mahali hapo na kisha Maulidi kumkabidhi Andy bomu lile ambalo alikuwa ameliweka katika mfuko wa nailoni. Akampa namna ya kulitega huku akimwambia kwamba kama uzito ule ambao ulikuwepo garini ungeongezeka basi gari lingelipuka wakati huo huo na kila kitu kusambaratika.
Andy akaonekana kuridhika, alichokifanya ni kummalizia zile fedha ambazo zilikuwa zimebaki na kisha kuagana mahali hapo. Alichokifanya Andy mahali hapo ni kuanza kupatafuta mahali alipokuwa akiishi Annastazia.
“Unamzungumzia yule mwanamke ambaye anagomea ubunge mwaka ujao” Derava taksi aliuliza.
“Mmhh! Huyo yuko vipi?” Andy aliuliza.
“Maji ya kunde, mrefu na mwembamba kidogo. Aliolewa mwaka jana na jamaa anaitwa George” Dereva alijibu.
“Ndiye huyo huyo”
“Napafahamu anapokaa. Unataka nikupeleke?” Dereva taksi aliuliza.
“Hapana. Nataka unipeleke ofisini kwake” Andy alisema.
“Pia napafahamu. Anafanya kazi kama mkurugenzi wa kampuni ya UNIBEST ile inayouza magari. Ofisi yake ipo pale Ubungo Plaza ghorofa ya sita” Dereva alisema.
“Mmh! Unaelekea unafahamu mambo mengi kweli kuhusu yeye” Andy alimwambia dereva wa taksi huku akionekana kushangaa.
“Watanzania wengi wanaoishi Dar es Salaam wanamfahamu. Hiyo ni kwa sababu anatarajia kugombania ubunge mwaka ujao kwenye uchaguzi mkuu” Dereva alisema.
“Sawa. Unaweza kunipeleka hapo Ubungo Plaza?”
“Bila shaka” Dereva alisema.
Andy akapanda garini na kisha dereva kuwasha gari na safari ya kuelekea Ubungo Plaza kuanza. Wala haikuwa safari ndefu na yenye kuchosha wakawa wamekishafika katika jengo hilo. Alichokifanya ni kuteremka kutoka ndani ya gari lile.
“Nafikiri umemkuta. Gari lake lile pale” Dereva alimwambia Andy huku akiionyooshea kidole gari aina ya Range Rover nyeusi iliyokuwa imepakiwa pembeni.
“Sawa. Ngoja nikamuone. Nakuja sasa hivi” Andy alimwambia dereva na kisha kuondoka.
Alichokifanya ni kuanza kwenda ndani ya jengo lile ambalo lilikuwa likitoa huduma mbalimbali. Hakutaka kwenda kwenye ile ghorofa, ila alichokifanya ni kwenda mpaka juu ya ghorofa ile na kisha kuanza kuwaangalia watu ambao walikuwa wakiogelea katika bwawa ambalo lilikuwa limejengwa juu ya ghorfa lile.
Alikaa kwa muda wa dakika ishirini na ndipo alipochukua lifti na kisha kuanza kushuka chini. Akaanza kupiga hatua kuelekea katika teksi ile ambako akaingia na kisha kuondoka mahali hapo huku akijiahidi kwamba siku inayofuatia ndio ilikuwa siku ya kufanya kile alichokuwa amekikusudia, kulilipua gari la Annastazia na kumuua yeye mwenyewe.
****
Usiku mzima Andy alikuwa akionekana kuwa na mawazo, suala la kufanya mauaji ya kumuangamiza Annastazia lilikuwa likimsumbua kichwani mwake. Kamwe hakutaka kuona mwanamke yule akivuta pumzi ya dunia hii kwani aliona kutokustahili kabisa.
Akasimama kutoka katika kitanda na kisha kuufuata mfuko ambao ulikuwa na bomu lile ambalo alipewa na Maulidi na kisha kuanza kuliangalia. Uso wake ukaanza kuonyesha tabasamu kwani aliona kwamba alikuwa akielekea kufanikiwa juu ya kile ambacho alikuwa amekusudia kukifanya.
Kila alipokuwa akiangalia televisheni hasa vituo vya hapa Tanzania, sura ya Annastazia ilikuwa ikionekana kila wakati. Annastazia alionekana kuwa mwanamke ambaye alistahili moja kwa moja kuuchukua Ubunge wa Kinondoni ambao alikuwa akiugombania pamoja na watu wengine wa vyama pinzani.
Annastazia alikuwa akikubalika kuliko mgombea yeyote yule. Elimu yake ilikuwa kubwa kuliko hata ya wale wagombea wengine ambao walikuwa wakigombea pamoja nae. Annastazia alikuwa akijua kuongea kupita kawaida hali ambayo ilimfanya kukubalika kupita kiasi.
Kila mtu alikuwa akimpenda Annastazia na hata wale ambao walikuwa nje ya wilaya ya Kinondoni wakatamani kwenda katika wilaya hiyo ili mwaka kesho waweze kumpigia kura mwanamke huyo ambaye katika kizazi hicho alionekana kuwa lulu.
Chama tawala kilikuwa kikiendelea kumtangaza kila wakati kiasi ambacho akaanza kuwa maarufu kuliko mwanasiasa yeyote nchini. Kwenye magazeti, mara kwa mara picha yake ilikuwa ikionekana huku kwenye televisheni, mara kwa mara alikuwa akionekana akihojiwa.
Annastazia alikuwa akijua kujielezea na hata maswali ambayo alikuwa akiulizwa alikuwa akiyajibu kwa ufasaha kabisa hali ambayo ilimfurahisha kila mtu hata wanachama wa vyama pinzani.
Muda wote Andy alikuwa na hasira kali, kamwe hakutamani watu waendelee kumsifia Annastazia kwa kila kitu na wakati alikuwa mwanamke mbaya ambaye alikuwa ameuumiza moyo wake kupita kawaida. Sifa ambazo alikuwa akizipata kutoka kwa watu ndizo ambazo zilikuwa zikimfanya Andy kuendelea kumchukia kupita kawaida. Wala hazikupita dakika nyingi kitandani hapo, akapitiwa na usingizi.
Kitu cha kwanza alichokifakinya mara baada ya kuamka ni kunywa chai na kisha kujiandaa tayari kwa kwenda kuifanya kazi ambayo ilimfanya kulinunua lile bomu. Akavaa nguo zake na kutoka ndani ya chumba kile huku mfuko wake wa nailoni uliokuwa na bomu ukiwa mkononi mwake.
Akachukua teksi ambayo ilimpeleka mpaka Shekilango, akateremka na kuanza kutembea kwa mguu kuelekea kule lilipokuwa jengo la Ubungo Plaza. Mwendo wake ulikuwa ni wa taratibu sana, hakutaka kumtia wasiwasi mtu yeyote ambaye alikuwa akimwangalia.
Mara baada ya kufika getini, akaingia ndani ya eneo lile na kisha kuanza kulitafuta gari alilokuwa akilimiliki Annastazia. Akaangalia katika sehemu yote ya kupakia magari lakini hakuweza kuliona, alichokifanya ni kwenda katika floo kubwa ambayo ilikuwa ikitumika kupakia magari yale ambayo yalikuwa yakikaa kwa muda mrefu mahali hapo.
“P2” Andy alisema mara baada ya kuliona gari aina ya Range kwa mbali likiwa katika floo ya pili.
Akaanza kupandisha njia ile ya kuelekea katika floo ya pili. Alikuwa akiyapita magari kadhaa ambayo wala hakuwa na shida nayo. Alipolifikia gari la Annastazia, akaanza kuangalia katika kila upande ili kuona kama hakukuwa na mtu ambaye alikuwa akimwangalia.
Alipohakikisha kwamba kulikuwa na hali ya usalama, akainama na kuanza kulitoa bomu lile kutoka kwenye mfuko na kisha kulitega katika sehemu ambayo lilitakiwa kuwekwa. Hakukosea maelekezo ambayo alielekezwa na Maulidi, alitulia huku akifanya kila kitu ambacho kilitakiwa kufanywa.
Alipoona kwamba alikuwa amemaliza kazi yake, akatoka chini ya gari na kisha kuanza kuondoka mahali hapo akishuka chini huku akipishana na magari mengine ambayo yalikuwa yakielekea kule ambapo kulikuwa na eneo la kuegeshea magari.
Kidogo moyo wake ukaanza kufarijika kwa kujiona kwamba tayari alikuwa amemaliza kazi ambayo ilikuwa imemleta nchini Tanzania. Wala hakutaka kuondoka mahali hapo, kitu ambacho alikuwa akikisubiria ni kuusikia mlipuko wa bomu.
Ingawa alijua kwamba alitakiwa kukaa mahali hapo kwa muda wa masaa nane lakini wala hakuonekana kujali. Kitu ambacho alitamani kukisikia kwa masikio yake mwenyewe ni mlipuko wa gari ambao ungemfanya kujua kwamba tayari Annastazia alikuwa amelipuka kwa bomu.
Aliendelea kukaa mahali hapo zaid na zaidi, saa la kwanza likapita, hakukuwa na mlipuko wowote ambao ulisikika, masaa mawili yakapita lakini napo kukawa kimya, masaa matatu, manne, matano, sita mpaka saba lakini napo hali ilikuwa kimya.
Andy akaonekana kuwa na wasiwasi, hakuamini kama kweli muda wote huo Annastazia hakuwa ametoka ofisini kwake. Akaanza kushikwa na wasiwasi kwa kuona kwamba kulikuwa na mtu ambaye likuwa amemuona na hivyo kwenda kulitegua bomu lile. Tayari akajiona kufeli kile ambacho alikuwa amekifanya.
“Puuuuuuuu........” Ulikuwa ni mlipuko mkubwa wa bomu ambao ulisikika ghafla. Moshi mkubwa ukaanza kuonekana ukitoka kule kulipokuwa na maegesho ya magari, P2.
“Afadhali” Andy alisema kwa furaha na kuanza kuondoka.
****
Watu walikuwa wakikimbia ovyo mara baada ya mlipuko wa bomu kusikika masikioni mwao. Wakinamama na wasichana walikuwa wakipiga kelele za kuomba msaada kana kwamba bomu lilikuwa limelipuka hatua hatua tano kutoka walipokuwa wamesimama.
Abiria ambao walikuwa katika daladala ambazo zilikuwa katika foleni wakaanza kupiga kelele na kuteremka kutoka katika daladala zile na kisha kuanza kukimbia ovyo. Hakukuwa na mtu ambaye alikuwa amesimama, watu wote ambao walikuwa katika magari yao walikuwa wametoka na kukimbia kuokoa maisha yao.
Mlipuko wa bomu lile ulikuwa mkubwa sana na ulionyesha kwamba si gari moja ambalo lilikuwa limelipuka. Baada ya dakika tano kupita ndipo watu waliporudiwa na fahamu na kutaka kujua ni kitu gani ambacho kilikuwa kimetokea.
Moshi mwingi na mzito ulikuwa ukionekana kutoka katika sehemu ya kuegeshea magari ya P2 ambayo ilikuwa katika ghorofa ya pili karibu na jengo la Ubungo Plaza. Watu wakaanza kusogea katika sehemu ile huku kila mmoja akionekana kuwa na hamu ya kutaka kufahamu ni kitu gani ambacho kilikuwa kimetokea.
Magari zaidi ya saba yalikuwa yamelipuliwa na bomu ambalo lililipuka dakika chache zilizopita. Watu wote wakashika vichwa vyao mara baada ya kuona kwamba hata gari la Annastazia lilikuwa miongoni mwa magari ambayo yalikuwa yamelipuliwa na bomu lile.
Watu wakaonekana kuogopa zaidi mara baada ya kuangalia ndani ya gari lile na kukuta kwamba kulikuwa na mwili wa mtu ambaye bila shaka alikuwa mwanamke ukiwa umeungua kupita kawaida. Kila mtu akaonekana kuogopa, watu wakachukua simu zao na kuanza kupiga picha kila kitu kilichokuwa kikionekana mbele ya macho yao.
“Wamemlipua....” Mwanamke mmoja alisema kwa masikitiko huku machozi yakimlenga.
Hii ndio siku ambayo ilikuwa ya furaha kwa Andy. Sauti ya mlipuko ambayo alikuwa ameisikia ilionekana kumpa furaha ya ajabu ya kuona kwamba mtu ambaye alikuwa akimchukia kuliko mtu yeyote alikuwa ameripuka ndani ya gari lake.
Alirudi chumbani hotelini huku akifurahi kupita kawaida. Aliimba nyimbo zote ambazo alikuwa akizikumbuka. Moyo wake ulikuwa ukijisikia faraja kubwa, amani ikaonekana kuanza kurudi ndani ya moyo wake.
Akachukua mvinyo ambao ulikuwa pembeni yake na kisha kumiminika katika glasi ndogo aliyoichukua kutoka mezani na kuanza kunywa. Jina la Annastazia lilikuwa likiendelea kusikika kichwani mwake, alijiona kutotakiwa kumkumbuka mwanamke huyo kwani tayari alikuwa hayupo tena duniani.
Alichokifanya kwa wakati huo ni kupiga simu katika kampuni ya ndege ya Americans Airline na kutaka kuandaliwa tiketi ya kurudi kwani hakuwa na muda mrefu wa kukaa nchini Tanzania, alihitaji kuondoka haraka iwezekanavyo.
Hakutaka kuendelea kukaa nchini Tanzania kwani aliona kazi ambayo alikuwa amekuja kuifanya ilikuwa imekwishakamilika. Hakutaka kukamatwa kwa kile ambacho alikuwa amekifanya na hiyo ndio ilikuwa sababu ambayo ilimfanya kuondoka haraka iwezekanavyo kurudi nchini Marekani.
Siku iliyofuata, tiketi ilikuwa tayari, hivyo akaanza safari kurudi nchini Marekani huku moyo wake ukiwa na furaha kupita kawaida. Moyoni alijihisi kwamba yeye ndiye alikuwa binadamu ambaye alikuwa na furaha kuliko binadamu wote duniani.
Baada ya masaa ishirini na mbili, ndege ilikuwa ikitua ndani ya uwanja wa ndege wa John F. Kennedy nchini Marekani. Andy akateremka na kisha kuanza kuelekea nje ya uwanja ule ambapo akachukua teksi na kisha kuanza kumpeleka nyumbani kwake.
Nje kulikuwa na magari kadhaa ya kifahari, tayari kichwa chake kilikuwa kimekwishafahamu ni nani ambaye alikuwa amefika nyumbani pale. Akateremka na kisha kuanza kuelekea ndani. Macho yake yakatua usoni mwa Dawson ambaye alikuwa pamoja na wapambe wake.
Huku wote wakionekana kuwa na furaha wakakumbatiana. Wakaingia ndani huku wakiwaacha wale wasaidizi wa Dawson wakiwa nje wakiwasubiri. Wote wakajiona kuwa washindi katka maisha ambayo yalikuwa yakiendelea maishani mwao, walijiona kushinda kila kitu ambacho kilikuwa kimeshindikana.
“Nahitaji dawa zaidi” Bwana Dowson alimwambia Andy.
“Zile zimekwisha?”
“Ndio”
“Sawa. Nipe usiku wa leo. Kesho njoo kwani kila kitu kitakuwa tayari” Andy alimwambia Dawson.
Baada ya Dawson kuondoka, Andy akaelekea chumbani kwake, bado sherehe ya kujipongeza kwa kumuua Annastazi ilikuwa ikiendelea maishani mwake. Akachukua mvinyo kutoka katika jokofu lake na kisha kuanza kunywa.
Alijiona kuwa na kazi kubwa lakini alikuwa ameikamilisha kwa haraka kuliko alivyotegemea. Alijiona kuwa na kila sababu ya kujipongeza, alijiona kuwa mshindi hata zaidi ya washindi. Kwake, kifo cha kumlipua ndicho kilionekana kustahili kwa mtu kama Annastazia ambay alikuwa ameuumiza moyo wa kupita kawaida.
“Sasa nitaishi kwa amani. Hakuna mawazo tena wala kumfikiria mpumbavu huyu” Andy alisema na kisha kujilaza kitandani huku tabasamu pana likiwa usoni mwake.
****
Annastazia alikuwa akifanya kazi zake kwa haraka sana kwani siku hiyo alikuwa ameandaliwa chakula cha usiku na mheshimiwa rais kama heshima ya kukitangaza chama kile kwa nguvu zote. Moyo wake ulikuwa katika presha kubwa, ni kweli kwamba alikuwa akifanya mawasiliano na rais mara kwa mara lakini siku hiyo kwake ilionekana kuwa siku tofauti na nyingine.
Kwanza kuitwa ndani ya Ikulu huku akiwa pamoja na mumewe, George kulionekana kumfurahisha kupita kiasi. Muda wote macho yake yalikuwa yakiangalia saa kubwa ya ukutani, kwake, aliuona mshale wa dakika ukienda taratibu sana tofauti na siku nyingine. Alitamani asimame na kuifuata saa ile na kisha kuusogeza mshale wa saa na kisha kuona dunia nzima ikienda kama vile ambavyo alikuwa akitaka iwe.
Kila alipokuwa akiyaandaa mafaili yakea alikuwa akimuita sekretari wake ambaye alikuwa akiyaweka katika sehemu ambayo yalikuwa yakitakiwa kuwa. Muda ulizidi kwenda mbele mpaka kufikia muda ambao alitakiwa kutoka ndani ya ofisi yake. Akayakusanya mafaili yote ambayo yalitakiwa kuandikwa mambo fulani katika kipindi ambacho angekuwa nyumbani na kisha kumpa sekretari wake.
Sekretari akayachukua na kisha kupewa ufunguo wa gari ambapo akaanza kuondoka kuelekea katika sehemu ambayo ilikuwa na gari la kifahari lililokuwa na rangi nyeusi, Range na kisha kuufungua mlango.
Annastazia bado alikuwa ofisini huku akiendelea kukusanya vitu vingine. Mara sauti kubwa ya mlipuko ikasikika, Annasatazia akashtuka kupita kawaida kiasi ambacho alitamani kutoka nje ya ofisi ile na kukimbia. Kutokana na presha kubwa aliyokuwa nayo, akajikuta akiingia chini ya meza na kujilaza chini.
Katika maisha yake yote, hakuwahi kuusikia mlio wowote wa mlipuko kiasi ambacho alipousikia mlipuko ule alijikuta akitetemeka kwa hofu kubwa. Moshi mwingi ukaanza kuonekana nje ya ofisi ile kwa dirishani huku sauti za wakinamama zikisikika.
Annastazia hakutoka, aliendelea kubaki ndani ya ofisi ile tena chini ya meza kwa muda wa dakika thelathini na ndipo hapo alipotoka nje ya ofisi ile. Watu walikuwa wamejazana katika korido huku wakiongea yao, Annastazia alipotokea, wote wakayaamishia macho kwake na kuanza kumwangalia.
Annastazia hakuyaelewa macho ya watu wale yalikuwa yakimaanisha nini mbele yake, alitamani kuuliza lakini akajikuta akikaa kimya. Bado moyoni mwake hakuwa akijisikia amani kabisa, alikuwa akipiiga hatua za haraka haraka kuelekea kule ambapo kulikuwa na gari lake.
Watu walikuwa wamejazana kule P2 ambapo alikuwa amelipaki gari lake. Kwanza hakuelewa sababu iliyowafanya watu wale wajazane namna ile, akaanza kusogea karibu zaidi. Kila mtu ambaye alikuwa amemuona mahali hapo alimshangaa kwani watu wote waliokuwa mahali pale walifikiri kwamba mtu ambaye alikuwa akionekana garini alikuwa yeye.
Annastazia akajikuta akilia kama mtoto mdogo mara ya kuona ni kitu gani ambacho kilikuwa kimetokea. Hakulia kwa sababu ya thamani kubwa ya gari lake bali alikuwa akilia kwa sababu alikuwa amempoteza mtu ambaye alikuwa karibu nae kwa asilimia nyingi, Shannia, msichana ambaye alikuwa sekretari wake.
Annastazia hakuendelea kubaki mahali hapo, alichokifanya ni kuanza kupiga hatua kurudi ofisini mwake. Machozi yakaanza kumtoka na kilio kikaanza kusikika, Moyo wake ulikuwa unamuuma kupita kawaida, kumpoteza hannia kulionekana kumuumiza.
“Hawa watakuwa wapinzani wetu. Watakuwa viongozi wa vyama pinzani” Annastazia alijisemea huku akiwa hana habari kwamba kila kitu kilichokuwa kimetokea kilikuwa kimepangwa na Andy, mwanaume ambaye alikuwa amemsaliti miaka minne iliyopita.
****
Serikali ikaonekana kuchanganyikiwa mara baada ya kupata taarifa ya mlipuko ule ambao ulikuwa umetokea. Kila mtu alionekana kutokuelewa sababu ambayo ilimfanya mlipuaji kulilipua gari lile la mwanamke ambaye alionekana kuwa na nguvu sana katika mambo ya siasa nchini Tanzania, Annastazia Kapama.
Hakukuwa na sababu ya kupoteza muda, moja kwa moja uchunguzi ukaanza kufanyika kwa haraka sana. Tukio lile la kuripuliwa kwa gari la Annastazia Kapama likaonekana kuanza kuibua vita vya chama tawala na vyama pinzani kwa kuwaona kwamba walikuwa nyuma ya tukio lile.
Upelelezi ulikuwa ukifanyika chini chini lakini hakukuwa na mtu ambaye alipatikana kwa kulifanya tukio lile. Miezi ilienda zaidi na zaidi lakini hakukuwa na mtu yeyote ambaye alipatikana na hatia ya kufanya tukio lile.
Siku ziliendelea kukatika huku miezi nayo ikiendelea kukatika. Vuguvugu la uchaguzi likaanza kutokota nchini Tanzania. Wanachama mbalimbali wa vyama pinzani pamoja na wale wanachama wa chama tawala wakaanza kufanya kazi zao kama kawaida.
Kwa wale ambao walikuwa wakitumia khanga wakaanza kuzigawa kwa wanawake kama hatua mojawapo ya kuchaguliwa siku ya uchaguzi itakapofika. Wanaume nao wakaanza kupewa fulana pamoja na kofia kama harakati fulani za kuweza kuwateka na kuchukua kura zao.
Mwaka ukaisha na mwaka mwingine kuingia. Annastazia akaanza harakati zake za kusimama majukwaani na kuanza kuhutubia huku akiwaomba wananchi wa maeneo mbalimbali katika wilaya ya Kinondoni kumpigia kura katika uchaguzi mkuu ambao ulikuwa umebakia mwezi mmoja kabla ya kufanyika.
Kila mwananchi ambaye alikuwa akimsikiliza Annastazia alionekana kumkubali na kila mtu kuahidi kumpa kura yae mwanamke huyo ambaye alikuwa akitikisa sana jijini Dar es Salaam kwa wakati huo.
Annastazia alitembea maeneo mbalimbali wilayani Kinondoni huku akiendelea kuhutubia katika mikutano mbalimbali. Kila sehemu ambayo alikuwa akihutubia, watu walikuwa wakijaa kupita kawaida.
Kwa maneno ambayo alikuwa akiyaongea Annastazia, kila mtu alikuwa akimkubali kupita kawaida. Annastazia akaonekana kushinda uchaguzi hata kabla kura hazikuanza kupigwa. Watu zaidi ya asilimia sabini walikuwa wakimuunga mkono Annastazia ambaye alionekana kupania kuleta mabadiliko makubwa katika wilaya ya Kinondoni.
Kwa kuwa Annastazi alikuwa akikubalika huku amejikusanyia umaarufu mkubwa nchini Tanzania, wanasiasa wengine wakaanza kumtumia katika mikutano yao. Alionekana kukubalika kupita kiasi jambo ambalo kila aliposimama katika jukwaa lolote, alionekana kukubalika.
Katika kila mkutano ambao ulikuwa ukimhusu, mumewe, George alikuwa pembeni yake akimsikiliza. George alikuwa akijisikia amani na furaha moyoni, kuwa na mke kama Annastazia kulionekana kumfurahisha kupita kawaida.
Katika kila mkutano ambao alikuwa akiufanya, Annastazia alikuwa akimtambulisha mumewe, George kama mtu pekee ambaye alikuwa akimpenda na kumtia nguvu katika kila kitu ambacho kilikuwa kinaendelea katika maisha yake.
George alijisikia fahari, alijiona kuthaminiwa kupita kawaida, mapenzi juu ya mke wake yakaongezeka zaidi na zaidi. Waliishi kwa amani na upendo ndani ya ndoa yao, walithaminiana na kupeana mapenzi ya dhati.
Hatimae siku ambayo ilikuwa ikisubiriwa ikafikia, watu hawakutakiwa kuvaa aina yoyote ya nguo ambayo ilikuwa ikionekana kuwa ya chama fulani. Watu walitakiwa kuelekea katika sehemu maalumu ambazo zilikuwa zimetengwa kwa ajili ya kupiga kura na kumchagua kiongozi ambaye walimuona kufaa kuwawakilisha.
Saa tano asubuhi, Annastazia alikuwa akiingia katika viwanja vya shule ya Kambangwa kwa ajili ya kupiga kura huku akiwa ameongozana pamoja na mumewe, George. Watu wote ambao walikuwa wakimuona mahali hapo wakaanza kumshangilia huku wakianza kuimba nyimbo mbalimbali japokuwa walijua kufanya hivyo lilikuwa kosa kbwa sana hasa katika siku hiyo ya uchaguzi.
Annastazia na mumewe wakapiga kura na kisha kuanza kuongea na viongozi wengine ambao walikuwa mahali hapo na kisha kulifuata gari lao, wakaingia ndani na kuondoka katika uwanja wa shule hiyo.
Ingawa alikuwa na uhakika wa asilimia zote kushinda uchaguzi ule lakini moyo wake ulikuwa na wasiwasi mkubwa. Hali ya kujiamini ikaanza kuondoka moyoni mwake huku akianza kuamini kwamba kitu chochote kingeweza kutokea siku ya matokeo.
Aliwafahamu sana Watanzania ambao mara yingi walikuwa wakikukubali sana siku za kampeni lakini siku ya uchaguzi wakakugeuka. Alijiona kutakiwa kusubiria matokeo na kuona kama Watanzania walikuwa wamekifanya kile ambacho walikuwa wakimuonyeshea au walikuwa wamemgeuka.
“Nina wasiwasi mpenzi” Annastazia alimwambia mumewe, George.
“Hautakiwi kuwa na wasiwasi. Hebu jifikirie ni kwa jinsi gani unakubalika” George alimwambia Annastazia.
“Lakini si unawajua Watanzania walivyo?”
“Nawajua”
“Sasa kuna sababu itakayonifanya kujiamini mpenzi?”
“Wewe jiamini tu. Yaani kwa kura yangu na yako pekee zimekwishakupitisha hata kama wengine hawajapiga” George alimwambia Annastazia na kuanza kucheka.
Siku ambayo matokeo yalitakiwa kutangazwa ikawadia. Annastazia pamoja na mumewe wakaanza kuelekea katika ofisi za makao makuu ya chama chao cha Republic na kisha kuingia ndani ya jengo hilo huku wakisikiliza kutangazwa kwa matokeao yale kupitia redio ya Taifa.
Kila mtu ndani ya ofisi ile alibaki kimya huku akionekana kuwa makini kusikiliza matokeo ambayo yalikuwa yakiendelea kutangazwa edioni mule. Wagombea wengi wa chama tawala walikuwa wameshinda viti vya Ubunge katika sehemu mbalimbali nchini Tanzania.
Ghafla kama mtu alieyekuwa ameshtushwa na mlipuko fulani mkubwa, Annastazia akaruka juu, mikono yake akainyoosha juu mara baada ya kutangazwa kwamba alikuwa ameshinda kiti cha Ubunge wa Kinondoni.
Watu wote ambao walikuwa wakaanza kushangilia, ushindi wa Annastazia wa kuwa mbunge wa Kinondoni ukaonekana kuwafurahisha kupita kawaida. Annastazia akashindwa kuvumilia, akaanza kumfuata mumewe, George na kisha kumkumbatia huku machozi yakiomtoka.
Tayari watu ambao walikuwa mitaani wakatoka na kuelekea katika ofisi ya chama cha Republic huku wakishanglia kwa kupiga ngoma. Annastazia hakuweza kuvumilia kubaki ndani, akajikuta akitoka nje huku akianza kupunga mikono yake hewani.
Watu zaidi ya mia saba walikuwa wamekusanyika nje ya ofisi ya chama kile huku kadri muda ulivyozidi kwenda mbele wakizidi kuongezeka zaidi na zaidi. Mpaka saa moja kupita, watu zaidi ya elfu mbili walikuwa wamekwishakusanyika nje ya uwanja wa ofisi ile huku wengi wao wakiwa wamevaa khanga, fulana na kofia za chama cha Republic.
Safari ya kutembea mitaani huku wakishangilia ikaanza kufanyika mahali hapo. Watu wakajikusanya wengi mitaani huku Annastazia, mumewe pamoja na viongozi wa chama kile wakiwa pamoja na wananchi ambao walikuwa wakioekana kuwa na furaha kupita kawaida.
Kushinda kwa Annastazia kulionekana kuwapa nguvu na kuona kwamba mwisho wa matatizo yao ulikuwa umefikia tamati. Walikuwa wakimuamini sana Annastazia kwamba alikuwa mtetezi wa maisha yao magumu ambayo walikuwa wakiishi.
Maisha kwao yalionekana kuwa magumu, barabara zilikuwa mbovu sana huku maji yakiwa shida kupatikana katika sehemu kubwa ya wilaya ya Kinondoni. Annastazia ndiye ambaye alionekana kuwa na nguvu ya kupambana na matatizo hayo ambayo yalionekana kuwa sugu katika wilaya hiyo.
“Sasa nitafanya mabadiliko makubwa” Annastazia alimwambia mumewe, George.
“Hicho ndicho ambacho kinatakiwa kufanyika. Nitakuwa pamoja nawe mke wangu” George alimwambia Annastazia.
Je nini kitatokea mara baada ya Andy kujua Annastazia yupo hai?
Je huo ndio utakuwa mwisho wa kila kitu au atakuja kivingine?
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment