Simulizi : Ukweli Wenye Kuuma ( Painful Truth )
Sehemu Ya Nne (4)
Utengezaji wa dawa ukaanza tena. Watu walikuwa wakizidi kuambukizwa huku wengine nao wakizidi kupatiwa tiba. Ugonjwa ule ulionekana kutisha kupita kawaida. Maambukizi yalikuwa makubwa kuliko hata magonjwa mengine.
Amani ikaonekana kutoweka duniani hasa nchini Marekani. Watu ambao walikuwa wakiondoka barani Marekani pamoja na Ulaya kuelekea Afrika ndio ambao waliufanya ugonjwa huo kuingia barani Afrika.
Dawa zilikuwa zimecheleweshwa kuletwa barani Afrika kiasi ambacho kiliwafanya watu wengi kupoteza maisha. Ugonjwa ule ulionekana kuwa na nguvu kubwa sana barani Afrika huku maambukizi yakiwa ya hali ya juu. Kila siku watu walikuwa wakifa na wengine wakizidi kuambukizwa.
Mpaka zile dawa zinaingia barani Afrika, zaidi ya watu milioni mbili walikuwa wamekufa na kuzikwa huku milioni kumi na mbili wakiwa wamekwishaambukizwa ugonjwa huo ambao ulionekana kuwa wa kihistoria.
Hapo ndipo wale watu ambao walikuwa hawamuabudu Mungu wakaanza kumuabudu Mungu kwani kwao waliona kuwa kama laana ambayo ilishushwa katika kizazi hiki ambcho kinaonekana kujawa na maovu mengi.
Ingawa Andy alikuwa akijitahidi kutengeneza dawa nyingi kwa siku lakini maambukizi yakaonekana kuwa makubwa hata zaidi ya utengenezaji wa dawa zile. Zaidi ya aslimia saba walikuwa wakiambukizwa ugonjwa ule kila mwezi.
Ingawa watu walikuwa wakitakiwa kutumia kinga lakini wengi wao hawakutaka kutumia kinga hizo kwa kuona kwamba zilikuwa zikiondoa ladha fulani hasa wakati wa kufanya tendo la ndoa na wapenzi wao au wake zao.
Bado kiasi kikubwa cha fedha kilikuwa kikiendelea kumiminika katika akaunti yake ikiwa sehemu ya malipo ambayo alikuwa akilipwa na Dawson. Utajiri wake ulikuwa ukizidi kuongezeka kila siku lakini kamwe hakutaka kuridhika.
Miezi iliendelea kukatika na hatimae kukutana na msichana ambaye moyo wake ukaanza kuangukia katika penzi zito, msichana huyu alikuwa Sofia aliyekuwa na asili ya Venezuela. Lengo lake kubwa kwa Sofia lilikuwa ni kuanzisha mahusiano ya mapenzi na hatimae kufunga ndoa hapo baadae.
Andy hakuwa radhi kumwambia Sofia ingawa mara kwa mara alikuwa akikutana nae hasa alipokuwa akielekea katika katika benki ya Atlantic. Sofia alikuwa akifanya kazi hapo kama mwanamahesabu katika benki hiyo.
Tayari moyo wake ulikuwa katika mapenzi mazito, ni kweli kwamba alikwishawahi kupenda sana kipindi cha nyuma lakini kwa sasa alikuwa akipenda zaidi ya mara ya kwanza. Alimhesabia Sofia kuwa sehemu katika maisha yake, alijiona kuanza kumthamini binti huyo hata kabla hajamwambia kitu chochote kuhusiana na mahusiano.
Mara kwa mara alikuwa akimtaka akutane nae katika mghahawa kwa ajili ya chakula cha usiku lakini kidogo Sofia hakuonekana kumuelewa kabisa. Alijifanya yuko bize sana na kazi mbalimbali za nyumbani.
Sofia alikwishajua kwamba Andy alikuwa akimpenda sana lakini kwake alijiona kutokuwa tayari kuanza mahusiano na mwanaume yeyote kwa kipindi hicho. Kumbukumbu za maisha yake ya nyuma ya kusalitiwa ndizo ambazo zilikuwa zimeuharibu kabisa moyo wake na kuuacha ukiwa na matundu matundu.
Ingawa alikuwa akiletewa mapozi lakini Andy hakukata tamaa, Sofia akakubali kutoka na Andy kwa ajili ya chakula cha usiku. Kila mmoja alionekana kuwa na furaha siku hiyo huku uhusiano wa kimapenzi ukianzia hapo mghahawani.
“Nitakupenda katika maisha yangu yote” Andy alimwambia Sofia.
“Usije kuumiza moyo wangu Andy. Nilikuwa nahofia sana kuwa na uhusiano na mtu maarufu au tajiri” Sofia alimwambia Andy.
“Naomba uniamini. Kamwe sitoweza kukuumiza” Andy alimwambia Sofia.
Hiyo ndio ilikuwa siku ya kwanza kuingia katika mahusiano tangu asalitiwe na Annastazia. Kwake hakumkumbuka kabisa Annastazia kwani alijua kwamba tayari katika kipindi hicho alikuwa marehemu mara baada ya kumlipua na bomu garini.
Andy hakutaka kupoteza muda, alichokifanya ni kwenda kumtambulisha Sofia nyumbani kwao. Bwana Wayne na mkewe, Happy walionekana kuwa na furaha, kumuona kijana wao akiwa katika mahusiano huku akijiandaa kuoa kuliwapa furaha sana.
“Nimeamua kusahau kila kitu” Andy aliwaambia wazazi wake.
“Umefanya jambo la maana sana” Bwana Wayne alimwambia Andy.
Baada ya miezi miwili, Andy akafunga ndoa na Sofia na kuanza maisha ya ndoa. Maisha yake yalikuwa yametawaliwa na furaha kubwa, Sofia ndiye alikuwa mtu wa karibu katika maisha yake lakini kamwe hakutaka kumuambia kitu chochote kuhusiana na virusi vya katapilar ambavyo alivitengeneza.
****
Hakukuwa na mtu ambaye aliamini kama Annastazia angeweza kushinda nafasi ya kuwa spika wa Bunge la Jamhuri wa Muuungano wa Tanzania. Umri wake ulikuwa mdogo sana lakini alionekana kukubalika kupita kawaida.
Ndoto zake ambazo alikuwa amejiwekea miaka mingi iliyopita tayari zilikuwa zimekamilika. Kuchaguliwa kwake na kuwa Spika wa Bunge kulimuonyeshea ni kwa jinsi gani alikuwa akikubalika sana hata Bungeni.
Watanzania walishtuka kutokana na uchaguzi wa kumchagua kama spika wa Bunge lakini hakukuwa na mtu yeyote ambaye alilaumu. Kwao, Annastazi alionekana kustahili kuchukua nafasi yoyote ile hata kama ulikuwa uraisi wa nchi.
Alionekana kuwa mwanamke aliyekuwa na kiu kubwa ya maendeleo, alionekana kuwa mwanamke ambaye kamwe hakutaka kuwaona Watanzania wakiishi katika maisha ambayo walikuwa wakiishi, maisha yaliyojaa umasikini mkubwa.
Magazeti mbalimbali na vyombo vingine vya habari vilikuwa vikimwaga sifa mbalimbali kwa Annastazia. Kura amabazo zilikuwa zimempigia zilionekana kuwa nyingi sana hali iliyoonyesha kwamba hata baadhi ya wabunge wa vyama pinzani walikuwa wamempigia kura.
Siku ya kwanza bungeni, Annastazi hakuweza kuamini kama kweli alikuwa amevaa jozi kubwa ambalo lilikuwa likivaliwa na spika wa Bunge. Moyoni mwake alikuwa akijisikia furaha sana kiasi ambacho wakati mwingine alikuwa akilengwa na machozi ya furaha.
Hiyo ndio ilikuwa siku ya kwanza ambayo ilikuwa imebaki kuwa kama kumbukumbu katika maisha yake. Katika kila kitu ambacho kilikuwa kikitokea katika maisha yake, alikuwa akimshukuru Mungu pamoja na mume wake, George ambaye alionekana kuwa mfariji mkubwa katika maisha yake.
****
Maisha yake ya ndoa pamoja na mke wake yalikuwa yakiendelea kama kawaida, alimpenda Sofia kuliko msichana yeyote yule. Alimthamini na kumpa kila kitu ambacho alikuwa amekistahili kukipata kutoka kwake.
Miezi ikaatika na hatimae mwaka wa kwanza kupita, Sofia akawa mjauzito. Hiyo ilikuwa ni furaha kubwa kwa Andy ambaye alikuwa ameongeza mapenzi maradufu kwa mke wake. Miezi tisa ikapita na hatimae mtoto wa kiume kuzaliwa na kumpa jina la Brian.
Familia ikaonekana kuongezeka, mapenzi makubwa yakaongezeka maradufu katika maisha yao. Kwa sababu Andy alikuwa akijulikana sana nchini Marekani, taarifa ile ilikuwa ikitangazwa sana. Magazeti mbalimbali, majarida pamoja na vyombo vingine vya habari vilikuwa vikitangaza mambo mengi ambayo yalikuwa yakitokea katika familia hiyo.
Miezi iliendelea kukatika na mwaka mwingine kuingia. Andy alionekana kupatwa na mshtuko mkubwa. Sura ya mtu ambaye alikuwa akiiangalia katika kompyuta yake hakuwa akiamini hata mara moja, ilikuwa picha ya Annastazia ambaye alikuwa Spika wa Bunge la Tanzania.
Andy akaivuta vizuri laptop yake na kisha kuiangalia vizuri picha ile, alikuwa Annastazia. Kumbukumbu za maisha yake ya nyuma zikaanza kurudi tena, chuki ambayo alikuwa nayo juu ya msichana huyo ikarudi tena.
Hakuelewa ni kwa nini Annastazia hakuwa amekufa katika ule mlipuko ambao alikuwa amemlipua mwaka uliopia. Alichokifanya Andy ni kuichukua ile picha na kuihifadhi sehemu huku kila wakati akiwa akiiangalia.
Bado alikuwa na hasira na Annastazia, hakuona sababu yoyote ambayo ilimpelekea Annastazia kuendelea kuvuta pumzi ndani ya dunia hii, alikuwa akitaka kumuua kabisa na kumpoteza katika dunia hii.
Hapo ndipo alipopanga safari ya kurudi tena nchini Tanzania na kisha kumuua Annastazia. Wala hakutaka kuchelewa, alichokifanya ni kumuaga mke wake, Sofia na kisha safari ye kuelekea nchini Tanzania kuana huku akiwa na hasira kali na Annastazia.
Kwa sasa hivi hakutaka kumuua kwa kitu chochote zaidi ya kumchoma kisu tumboni mara kadhaa na ndipo amuache huku akimwangalia mpaka katika kipindi ambacho atakata roho. Baada ya siku mbili, Andy akaanza safari ya kuelekea nchini Tanzania huku akitumia ndege yake.
Kila wakati alikuwa akijifikiria ni kwa njia gani ambayo angeitumia kuonana na Anastazia na kisha kumuua kwa kumchoma kisu zaidi ya mara tano tumboni. Mawazo mbalimbali yalikuja kichwani mwake, hivyo akaona kwamba kazi haikuwa kubwa sana.
Nchini Tanzania, akaamua kuanza kufuatilia Annastazia alikuwa mbunge wa wapi. Wala hakupata shida ya kulifahamu hilo, akapata jibu kwamba alikuwa mbunge wa Kinondoni. Alichokifanya ni kuchukua ndevu za bandia ambazo alikuwa amekuja nazo na kisha kuzivaa.
Alichokifanya hapo ni kwenda katika ofisi ya mbunge huyo na kisha kuongea na wasaidizi wake ambao alikuwa amewakuta mapokezini. Akajiwekea lengo la kutaka kuisaidia wilaya ya Kinondoni kwa kuitengenezea barabara kadhaa ambazo zitahesabika kwamba Bi Annastazia ndiye ambaye alikuwa amefanya hilo.
Hiyo ilikuwa ni taaarifa ya furaha sana kwa upande wao, mfadhiri ambaye alikuwa amejitokeza kwa kutaka kuisaidia wilaya ya Kinondoni alionekana kuwa muhimu kwao. Walichokifanya ni kumpigia simu Annastazia na kisha kumwambia kuhusiana na mtu huyo ambaye alionekana kuwa mfadhiri ambaye alikuwa na fedha za kutosha.
“Anaitwa nani” Annastazia aliuliza huku akionekana kuwa na furaha.
“Ben Killerandy” Msaidizi wake alisema.
Japokuwa Annastazia alikuwa mkoani Dodoma ambapo Bunge lilikuwa likiendelea, akaamua kuanza safari ya kuja jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kuonana na mfadhiri huyo ambaye alionekana kuja katika muda muafaka.
Alipofika ndani ya jiji la Dar es Salaam moja kwa moja akaanza kuelekea katika ofisi yake ambako huko akaanza kupata mambo mengi kuhusiana na mtu huyo ambaye alikuwa amejitolea kuitengeneza wilaya ya Kinondoni.
Annastazia akapewa namba ya simu na kisha kuanza kufanya nae mawasiliano. Sauti ya Andy ilikuwa imebadilika kabisa na isingewezekana hata kidogo kujulikana na Annastazia. Wakapanga sehemu ya kuonana na bila hiyana yoyote Andy akataka waonane nyumbani kwa Annastazia ambako huko ndipo angemuua.
Siku iliyofuata, Andy akajiandaa vilivyo huku akiziweka ndevu za bandia ambazo alikuwa amekuja nazo kutoka nchini Marekani na kisha kukodi teksi. Huku safari ikiwa inaendelea, Andy alikuwa na kiu ya kumuona Annastazia na kumuua kama ahadi ambayo alikuwa ameiweka katika maisha yake.
Gari likafunga breki nje ya geti la jumba kubwa la kifahari na kisha kuruhusiwa. Andy akateremka na kuanza kuingia ndani ya eneo la nyumba hiyo ambako alikaribishwa mpaka ndani. Macho yake yakatua kwa Annastazia ambaye alifika sebuleni hapo.
Mshipa wa hasira ukamsimama, chuki kubwa na hasira ikaanza kumpanda moyoni mwake. Alitamani kumrukia Annastazia na kisha kuvizamisha visu vile tumboni mwake. Uso wa Annastazi ulikuwa na tabasamu kubwa, ingawa Andy alikuwa akirudisha tabasamu lile lakini moyo wake ulikuwa umejawa na hasira kali.
“Karibu” Annastazia alimkaribisha.
“Asante”
Hapo ndipo mangezi yalipoanza. Andy alikuwa akimwambia mipango ambayo alikuwa ameipanga kuhusiana na kuboresha miundombinu mbalimbali nchini Tanzania hasa katika wilaya ya Kinondoni. Alichokifanya yeye kwa wakati huo ni kuzitoa karatasi kadhaa ambazo alikuwa amekuja nazo kutoka nchini Marekani na kisha kuanza kumuonyeshea. Ilionekana kuwa karatasi ambayo iliandikwa mipango mikubwa ya kuibadilisha kabisa wilaya ya Kindondoni ambako baada ya kila kitu kukamilika basi Annastazia ndiye ambaye angeonekana kwamba alikuwa amefanya yote hayo.
“Sawa” Ngoja nijiandae tuelekee ofisini kuonana na wenzangu ambao moja kwa moja kazi hiyo itafanyika” Annastazia alisema na kisha kuondoka kuelekea chumbani.
Andy hakutaka kubaki mahali hapo, alichokifanya ni kusimama na kisha kuanza kuelekea chumba mule. Lengo lake kubwa lilikuwa ni kumuua huko huko chumbani kwa kumchoma visu kadhaa. Huku akiendelea kujiandaa, ghafla Annastazia akashtukia mlango ukifunguliwa na Andy kuingia ndani.
Annastazia alionekana kushtuka sana, hakuamini kama mgeni huyo angeweza kuingia chumbani kwake kirahisi namna ile. Alibaki akimwangalia Andy huku macho yake yakionyesha mshtuko.
“Unafanya nini chumbani humu?” Annastazia alimuuliza Andy pasipo kumfahamu.
“Nimekuja kukuua tu” Andy alijibu huku hasira zikianza tena kumpanda.
“Nimekufanya nini Killerandy?” Annastazia aliuliza huku akionekana kuwa na wasiwasi.
Alichokifanya Andy ni kuzivua zile ndevu za bandia. Annastazia bado hakuwa amemfahamu Andy kwani ilikuwa imepita mika mingi sana bila kumtia machoni. Hata zile ndevu ziipotolewa, bado hakuweza kumfahamu.
“Nimekufanya nini?”
“Ulinisaliti. Uliuumiza sana moyo wangu” Andy alisema lakini bado Annastazia hakuonekana kuamini.
“Kukusaliti! Mbona sikufahamu na wala sikuwahi kukuona kabla!” Annastazia alisema huku akianza kutetemeka kwa woga.
“Ninaitwa nani?”
“Killerandy”
“Hayo ni majina mawili. Hebu yaweke yawe kwenye majina mawili ndio utatambua mimi ni nani” Andy alimwambia Annastazia.
“Mungu wangu!” Annastazia alisema kwa mshtuko.
“Najua umenifahamu mimi ni nani” Andy alimwambia Annastazia.
Alichokifanya Andy ni kukitoa kisu chake na kisha kuanza kumsogelea Annastazia. Alipotaka kupiga kelele tu, akashtukia akifunikwa mdomo wake na viganja vikubwa vya Andy. Akalazwa kitandani na kisha kufungwa mdomo kwa kanga zilizokuwa kitandani.
“Nitakuua baada ya kukubaka. Sikubaki kwa sababu nina tamaa ila ninakubaka kama hatua ya kukudhalilisha” Andy alimwambia Annastazia na kisha kuanza kumbaka.
Yalikuwa ni maumivu makali kwa Annastazia kwa kuwa Andy hakutaka kutumia uume wake tu, wakati mwingine alikuwa akitumia hadi mkono wake na mpini wa kisu chake. Annastazia alibaki akilia lakini sauti yake haikutoka kabisa.
Andy hakutaka kutoka kifuani kwa Annastazia, kadri alivyokuwa akifikiria namna ambavyo mwanamke yule alivyokuwa ameeuumiza moyo wake kipindi cha nyuma, alizidi kumbaka zaidi na zaidi. Kutoka na mpini wa kisu kile kuchunika chunika, sehemu ya ukeni ya Annastazia ikaanza kutoka damu.
“Ni lazima nikuue” Andy alimwambia Anastazia.
Machozi yalikuwa yakimtoka Andy, kadri alivyokuwa akimwangalia Annastazia na ndivyo ambavyo alikuwa na hasira zaidi na zaidi. Akanyanyua kisu juu na kisha kukizamisha kifuani mwa Annastazia. Anastazia akakipeleka kifua chake juu na kukileta chini, damu zikaanza kutapakaa kitandani. Andy hakuridhika, akakinyanyua kisu tena na kisha kukizamisha tena kifuani mwa Annastazia, alifanya hivyo mara sita, Annastazia akatulia kitandani, alikuwa amekwishakufa hapo hapo.
Andy hakutaka kubaki mahali hapo, alichokifanya ni kutoka chumbani mule na kuondoka zake. Hakukuwa na mtu yeyote ambaye alifahamu kitu chochote kilichokuwa kimetokea ndani, wakairuhusu ile teksi kuondoka.
“Nina amani sasa” Andy alijisemea.
“Unasemaje?” Dereva aliuliza.
“Hapana. Hakuna kitu”
“Sawa. Ila unatoka damu”
“Damu! Ziko wapi?”
“Shingoni” Dereva alimwambia Andy ambaye alionekana kuwa na wasiwasi mkubwa.
Andy akamtaka dereva asimamisha gari nje ya baa moja ambako akateremka na kuanza kuelekea chooni huku lengo lake likiwa ni kujifuta damu zile hata kabla hajashtukiwa na mtu yeyote yule. Akaingia chooni, maji yalikuwa mengi, alichokifanya ni kuzivua nguo zake na kisha kuanza kujifuta.
Alitumia muda wa dakika thelathini chooni na ndipo akatoka kuelekea katika sehemu ilipokuwa teksi ile. Andy akapigwa na mshtuko mara baada ya kuona gari la mapolisi likiwa limesimama pembeni ya teksi ile huku mapolisi wakiongea na dereva yule ambaye alionekana kuwa na wasiwasi mwingi.
Mara macho ya dereva yakagongana na macho yake, dereva akanyoosha mkono wake kumuelekezea yeye. Andy akaonekana kushtuka, hakujua ni kitu gani ambacho kilikuwa kinaendelea, akili yake ikamtuma kuona kwamba tayari hali ya amani ilikuwa imechafuka. Alichokifanya mahali hapo ni kukimbia na mapolisi wale waliokuwa na bunduki kuanza kumkimbiza huku wakipiga risasi hewani kama ishara ya kumtaka kusimama na kujisalimisha ila Andy hakufanya hivyo zaidi ya kuendelea kukimbia tena kwa kasi kubwa kama mwanariadha wa mbio fupi.
Chakula kilikuwa kimekwishaiva na ni Annastazia ndiye ambaye alikuwa akihitajika kwenda katika sehemu ya kulia chakula na kula chakula hicho cha mchana. Kama kawaida yake mfanyakazi wake wa ndani, Glory akaanza kuugonga mlango wa chumbani kwa Annastazia lakini hakukuwa na dalili za mtu kwenda kuufungua mlango ule.
Glory hakuonekana kuwa na wasiwasi, alichokifanya ni kulekea sebuleni huku akidhani kwamba Annastazia alikuwa nje ya jengo lile akiongea na walinzi au wafanyakazi wengine wa nyumba hiyo. Annastazia hakuonekana mbele ya macho yake.
Ingawa alikuwa amekifunika vizuri chakula kile katika hotpot lakini bado alihitaji bosi wake ale katika muda muafaka na hata kama alikuwa amelala, kila siku alikuwa amemwambia amuamshe mara tu chakula kinapokuwa tayari.
Glory hakuonekana kuelewa kitu chochote kile, kwa jinsi alivyokuwa ameita nje ya chumba kile hakuwa na uhakika kwamba Annastazia hakuwa amemsikia hata kama alikuwa katika usingizi mzito namna gani. Alichokifanya kwa wakati huo baada ya kuita kwa muda mrefu ni kuufungua mlango ule.
Moyoni alikuwa akihofia kwani toka aanze kufanya kazi ndani ya nyumba ile hakuwahi hata kukiona chumba kile, si kwamba alikuwa akizuiliwa bali hakuwa amejiwekea mazoea ya kuingia ndani ya chumba kile.
Mlango haukuwa umefungwa, aliufungua na kisha kuingia ndani. Moyo wake ukamlipuka, damu mwilini mwake ikaanza kuzunguka kwa kasi kubwa huku hofu ikiwa imemwingia moyoni. Hakuamini kile ambacho alikuwa akikiangalia mbele yake, maiti ya Annastazia.
Glory akaanza kupiga uyowe ambao uliwafanya walinzi pamoja na wafanyakazi wengine kufika chumbani mule. Kila mtu ambaye alikuwa ameuona mwili wa Annastazia alibaki kuwa na mshtuko, hawauamini kile ambacho walichokuwa wakikiona kwa wakati ule.
“Msiuguse mwili huu” Mlinzi mmoja aliyekuwa na nguo za kiaskari aliwaambia na kisha kutoka nje ya chumba kile.
Moja kwa moja akaanza kuelekea mpaka katika kijumba kidogo ambacho kilikuwa kikitumiwa na mlinzi wa pale mlangoni na kisha kuchukua daftari lililokuwa mezani na kisha kuanza kulifungua kwa kasi ya ajabu.
Macho yake yakatua katika jina la Killerandy. Alichokifanya ni kuanza kuangalia namba za gari ambalo lilikuwa limeingia ndani ya eneo la nyumba ile. Kwa haraka haraka akaanza kuandika pembeni na kisha kuondoka mahali hapo.
Kitu cha kwanza ni kwenda katika kituo cha polisi ambacho wala hakikuwa mbali kutoka katika nyumba ile na kisha kuanza kuelekezea kile ambacho kilikuwa kimetoke. Kila polisi alionekana kuwa na mshtuko, walichokifanya ni kuingia katika defender yao na kisha kuondoka mahali hapo.
“Unasema namba za gari unazikumbuka?” Polisi aliuliza.
“Si kuzikumbuka tu, hadi kuzinadika nimeziandika. Hizi hapa”
“Hebu zitaje”
“T113 NYC”
“Na njia ambayo gari hiyo imeelekea unaifahamu?”
“Yeah! Tena wameelekea kule kunapokuwa na foleni kubwa”
Dereva alikuwa akiendesha gari kwa mwendo wa kasi sana kiasi ambaco watu wengi ambao walikuwa wakiliangalia gari lile walifikiri kwamba lilikuwa katika mashindano fulani. Mapolisi walikuwa wamejiandaa na bunduki zao kama walikuwa katika muvi fulani iliyotungwa na Ubunifu Wetu.
Foleni kubwa ilikuwa ikionekana mbele yao, magari ambayo mengi yao yalikuwa ya watu binafsi yalikuwa yakisogea taratibu sana kuingia katika barabara ya Ally Hassan Mwinyi. Walichokifanya ni kuanza kuvunja sheria kwa kupita katika njia ya watembea kwa miguu huku watu wakiwashangaa.
“Ilikuwa ni gari aina gani?” Polisi mmoja aliuliza.
“Teksi”
“Mstari wa rangi gani?”
“Njano”
“Sio ile iliyosimama nje ya ile bar?”
“Yeah! Ndio ile ile” Mlinzi yule alijibu hasa mara baada ya kuona namba za gari.
Mapolisi wale wakazidi kulisogelea gari lile huku wakiweka bunduki zao vizuri. Kila akaonekana kuwa na hamu ya kuingia kwa ajili ya mapambano tu, mikono yao ikaanza kuwasha, kiu ya kumpiga mtu makofi ikaanza kuwakamata.
Wakaruka kutoka garini na kisha kuanza kulifuata teksi ile. Dereva alikuwa akipiga mluzi huku sauti ya muziki ikisikika kwa mbali. Ghafla akashtukia mlango ukifunguliwa na kushikwa fulana na kutolewa nje bila kufahamu ni mtu gani alikuwa amemtoa nje ya gari kinguvu.
“Yuko wapi?”
“Nani?”
“Paaaaa” Alipigwa kibao cha nguvu shavuni.
“Yuko wapi?” Lilikuwa swali la pili kutoka kwa polisi, hata kabla hajatoa jibu lolote lile, Andy akatokea mahali hapo jambo lililomfanya kumnyooshea kidole na mapolisi wale kuanza kumfukuza huku wakijaribu kumfyatuulia risasi ambazo zilimkosa ila hawakuataka kumuacha.
****
Andy alikuwa akikimbia kwa kasi kuelekea katika upande ambao ulikuwa na fremu nyingi. Milio ya risasi bado ilikuwa ikisikika kutoka katika bunduki walizozishika maaskari wale ambao walionekana kutokuwa na shabaha kabisa.
Watu waliokuwa karibu na eneo lile walikuwa wakikimbia ovyo, milio ya risasi ambayo ilikuwa ikisikika ilikuwa ikiwatisha kupita kawaida. Andy hakutaka kusimama, kukamatwa kwa kusalimu amri kungemaanisha kwamba alikuwa ameshindwa kabisa kujinasua kutoka kwa mapolisi wale.
Aliendelea kukimbia mpaka kufika katika uwanja wa Don Bosco, hapo hakutaka kusimama, akaendelea kukimbia zaidi na zaidi kuelekea ilipokuwa barabara ya kuingilia Orysterbay. Alipoifikia barabara ile, hakutaka kuiingia, akaendelea kwenda mbele kule kulipokuwa na sheli iliyokuwa karibu na jengo la Mult Choice.
Watu bado walikuwa wakiendelea kukimbia kila milio ya risasi ilipokuwa ikiendelea kusikika. Andy alionekana kuwa kama mtu ambaye alikuwa amekimbia riadha kwa kipindi cha nyuma kutokana na kasi yake ilivyokuwa kubwa.
Mapolisi ambao walikuwa walinzi katika geti la kuingilia katika jengo la Multi Choice walionekana kutokuwa na ushirikiano na mapolisi wale ambao walikuwa wakimkimbiza Andy. Walimuona kabisa Andy akielekea katika upande ule waliokuwa lakini hawakufanya kitu chochote zaidi ya kupigwa na butwaa tu.
Andy hakuwa akifahamu sehemu yoyote ile, yeye alikuwa akikimbia huku lengo lake likiwa ni kuwapotea mapolisi tu. Bila kuangalia kama kulikuwa na magari yalikuwa yakipita, Andy akavuka barabara na kuelekea kule kulipokuwa kukitengenezwa masofa.
Wauza masofa wote walikuwa wamekwishakimbia kutokana na milio ya risasi ambayo ilikuwa ikiendelea kusikika mahali pale. Andy hakuonekana kuwa radhi kusimama, akaendelea kukimbia mpaka karibu na viwanja vya Leaders.
Milio ya risasi wala haikusikika tena hali iliyoonyesha kwamba bunduki zile za mapolisi zilikuwa zimeishiwa risasi. Andy akapandisha njia ya juu mpaka karibu na jengo la T.H.T na kulipita kwa kasi ya ajabu. Andy akayapeleka macho yake nyuma, mapolisi hawakuonekana kabisa hali iliyomuonyesha kwamba alikuwa amewaacha umbali mrefu.
Hakusimama, aliendelea kukimbia mpaka alipotokea katika shule ya Sekondari ya Kinondoni Muslim ambako hapo akachukua teksi na kumtaka dereva kuendesha kuelekea Posta. Mpaka teksi inaondoka mahali hapo, Andy hakuwa akiamini kama alikuwa amefanikiwa kuwatoka mapolisi wale ambao walionekana kuwa na uchu wa kumpiga japo risasi moja.
“Mbona hivyo?” Dereva alimuuliza Andy huku akionekana kumshangaa.
“Nimepigiwa simu ya dharura. Ofisi yetu inateketea kwa moto. Nawahi kwenda kuokoa mafaili yangu ya muhimu” Andy alijibu.
“Ofisi gani?”
“Ofisi yetu”
“Ipi?”
“Augh! Acha maswali bwana. Endelea kuendesha gari” Andy alimwambia dereva mara baada ya kuona maswali yakizidi kuongezeka.
Mpaka wanafika katika hoteli ya Serena, dakika theathini zilikuwa zimekatika. Andy akateremka na kisha kumgawia dereva kiasi cha fedha ambacho kilitakiwa na kisha kuanza kuelekea ndani ya hoteli ile.
Akaingia chumbani na kisha kujilaza kitandani. Moyo wake ulionekana kuwa na furaha kupita kawaida mara alipokumbuka kwamba kile kitu ambacho kilimfanya kuja nchini Tanzania kilikuwa kimekwishakamilika.
Alichokifanya kwa wakati huo ni kuinuka na kuanza kuelekea sehemu ilipokuwa televisheni na kisha kuiwasha. Hakutaka kuangalia vituo vya nje, akafungua kituo cha TBC na kisha kuanza kuangalia kuona kipi kilikuwa kimeendelea.
Macho yake yakatua katika picha ya Annastazia, taarifa za kifo chake zilikuwa zimekwishatangazwa. Moyo wake ukafarijika kupita kiasi, kumuua Annastazia kulionekana kumfurahisha kupita kiasi.
Akainuka na kwenda kuchukua kikopo cha Red Bull na kupiga pafu moja. Uso wake ulikuwa umejawa na tabasamu kila alipokuwa akiangalia televisheni na kukutana na picha ya Annastazia ambapo taarifa juu ya kifo chake zikiwa zinatangazwa.
“Hayo ndio malipo ya usaliti” Andy alisema huku akiichukua glasi yake ya soda na kuunyoosha mkono wake juu kama ishara ya ushindi.
Ghafla Andy akapigwa na mshtuko mara baada ya kuyarudisha macho yake katika kioo cha televisheni na kukutana na picha yake. Huku akionekana kuwa na mshtuko na macho yake yakionekana kutokuamini, akaanza kuiangalia vizuri picha yake.
Jina lake halisi lilikuwa likitangazwa hadharani huku picha yake ikionekana vizuri. Bado Andy alikuwa amepigwa na mshtuko mkubwa huku akionekana kutokuamini macho yake. Kwa haraka haraka, akabadilisha kituo cha televisheni na kuhamia katika vituo vya kimataifa hasa katika kituo cha CNN. Hapo ndipo wasiwasi ulipozidi kumkamata hasa mara baada ya kuona kwamba hata CNN walikuwa wamepata taarifa ile kutokana na mtandao wao kuwa mkubwa.
Walichokifanya CNN ni kuanza kuielezea historia fupi ya maisha yake huku baba yake akiwa mchungaji mkubwa wa Kimataifa huku akiwa mlemavu. Andy alionekana kuumia kupita kawaida kwani aliamini kwamba alikuwa amelichafua jina la baba yake kupita kawaida.
Akajikuta akipiga magoti chini, machozi yakaanza kumtoka na kuanza kulia kwa uchungu. Moyo wake ulikuwa katika maumivu makali kupita kawaida, kulichafua jina la baba yake kulionekana kumuumiza sana.
“Nisamehe baba” Andy alijisemea.
Hapo ndipo alipojiona kuanza kuishi maisha ya kujificha, hakuwa radhi kukamatwa kabisa, alihitaji kuanza kujificha mpaka atakapoanza safari ya kuelekea nchini Marekani kwa kutumia njia za panya, hasa meli kubwa za mizigo.
Tayari Andy hakujisikia kuwa na amani hata mara moja kama tu angeendelea kukaa katika hoteli hiyo. Alichokifanya ni kulala kitandani huku akisubiri usiku uingie na hivyo kuondoka hotelini hapo kwani kukaa hapo kwake kulimaanisha kwamba angkamatwa muda wowote ule.
Usingizi haukupatikana kabisa ila alikuja kushtuka kutoka katika lindi la mawazo ilipotimia saa moja na nusu usiku. Alichokifanya ni kuchukua kila kitu kilichokuwa chake na kisha kuanza kuelekea nje ya chumba kile.
Akaingia katika lifti ambayo ilimchukua mpaka chini na kuanza kuondoka huku akionekana kuwa na wasiwasi mkubwa. Lifti ilipofika chini, kwa haraka haraka akateremka na kuanza kuelekea sehemu ambayo ilikuwa na mlango wa kutokea katika eneo la hoteli ile huku saa yake ikimuonyesha kwama tayaari ilikuwa imetimia saa mbili kasoro.
Huku akiwa ametoka nje ya hoteli ile, ghafla akageuka nyuma, macho yake yakatua kwa wanaume watatu ambao nao walionekana kumfuatilia huku kadri muda ulivyozidi kwenda mbele walikuwa wakiongeza kasi.
Tayari Andy akaona kuwa kulikuwa na hatari na wala hakutaka kujiuliza wale walikuwa ni wakina nani, akaanza kukimbia kwa kasi. Nao wale wanaume watatu wakaanza kumkimbiza. Tayari swali lake ambal alikuwa nalo kichwani kuhusiana na wale watu alikuwa amekwishapata jibu, walikuwa askari kanzu.
Kama kawaida yake, kwa sababu yeye ndiye alikuwa kwenye hali ya hatari, aliweza kukimbia kwa mwendo wa kasi hata zaidi ya wale mapolisi ambao walikuwa wakimkimbiza. Akafika kwenye eneo lililokuwa na makaburi ya wahindi, akayapita na kuzidi kuelekea mbele zaidi huku akiifuata barabara ile ya Ally Hassan Mwinyi.
Alipofika mbele karibu na daraja la Sarender, akakata kona kushoto na kuanza kuifuata barabara ile. Andy akaanza kuchoka jambo ambalo hata kasi yake ikaonekana kuanza kupungua. Mapolisi wale walionekana kuwa kama walikunywa dawa za kuongeza nguvu, walizidi kumsogelea zaidi na zaidi.
Akakata kona nyingine na kutokea katika sehemu ambayo ilikuwa na baadhi ya watu ambao walikuwa wamelala chini, walikuwa watoto yatima. Kwa kuwa alikuwa amechoka na alishindwa kuendelea kukimbia, akaanza kumfuata mwanamke mmoja ambaye alikuwa pembeni kwenye giza pamoja na mtoto wake huku akiwa na shuka kubwa, alichokifanya ni kuingia ndani ya shuka hilo.
“Naomba unifiche....” Andy alimwambia mama yule huku akijifunika shuka lile.
Masikio yake yote yalikuwa yakisikiliza ni kitu gani ambacho kingeendelea mahali hapo. Ghafla akaanza kusikia vishindo vya watu wakija, walipofika karibu na lile eneo alilokuwa yule mama wakasimama na kuanza kumwangalia mama yule huku wakionekana kuwa na wasiwasi.
“Sisi ni mapolisi” Mwanaume mmoja alimwambia mama yule ambaye tayari woga ulianza kumshika.
Alijiona kutokuwa na jinsi, kama angeulizwa kuhusiana na Andy, mwanaume ambaye alikuwa amemficha basi ni lazima angemtaja kwani katika maisha yake alikuwa akiwaogopa sana mapolisi. Kitu cha pili ambacho alikiona kwamba ni lazima angemfichua Andy kule alipokuwa ni kwa sababu alikuwa hamfahamu hata kidogo. Asingekuwa tayari kuingia katika matatizo na wakati mtu ambaye alikuwa amemficha hakuwa akimfahamu.
Maswali mengi yakaanza kujikusanya kichwani mwake, kwa nini yule mwanaume alikuwa akikimbizwa na mapolisi? Kwa nini aliamua kumfuata yeye pale alipokuwa na kuhitaji hifadhi? Je alikuwa raia mwema au si raia mwema? Na kama alikuwa raia mwema kwa nini alikuwa akikimbizwa na mapolisi? Kila swali ambalo alikuwa akijiuliza kichwani lilimpa jibu kwamba ilikuwa ni lazima amtaje Andy ambaye alikuwa amejificha katika shuka lake.
“Kuna mtu tulikuwa tunamkimbiza, umemuona mahali hapa?” Polisi mmoja aliuliza.
“Ndio” Mwanamke yule alitoa jibu ambao lilimfanya Andy ndani ya shuka lile kupigwa na mshtuko mkubwa.
Mapolisi walionekana kuchanganyikiwa mara baada ya kufika katika barabara ya lami karibu kabisa na shule ya Sekondari ya Kiislamu ya Kinondoni na kutokumuona Andy, mtu ambaye walikuwa wakimkimbiza. Wakajaribu kuangaia huku na kule lakini wala hakuonekana machoni mwao.
Hawakujua kama Andy alikuwa amechukua daladala na kuondoka katika eneo hilo au alikuwa amevuka barabara na kuelekea upande wa pili. Kila kitu ambacho walikuwa wakijaribu kujiuliza kwa wakati huo wakakosa jibu kabisa hali iliyowafanya kukata tamaa kabisa.
Walitaka kuondoka mahali hapo ila kabla ya kuondoka wakaamua kwenda kuwauliza madereva taksi ambao walikuwa karibu na eneo lile, walijua fika kwamba madereva wale ni lazima wangejua mahali ambapo Andy alikuwa ameelekea kwa wakati huo.
“Mnamaanisha jamaa aliyekuwa na mchanganyiko wa rangi?” Dereva mmoja aliuliza.
“Ndiye huyo huyo”
“Musa alimchukua hapa kwenda nae upande ule wa Kaskazini. Sasa sijui walikuwa wakielekea mjini, Oysterbay au Coco Beach, ila Musa alimchukua” Dereva mmoja alijibu.
“Musa ndiye nani?” Polisi aliuliza.
“Dereva teksi mwenzetu wa kitengo hiki”
“Tunaweza kumpata muda gani?”
“Mmh! Labda mumsubiri mpaka atakaporudi”
“Hamna namba yake ya simu?”
“Aliibiwa wiki iliyopita. Hana hata hamu ya simu. Unacheza na Manzese nini” Dereva alijibu.
Mapolisi hawakutaka kuendelea kuongea nao, walichokifanya ni kuacha ujumbe kwamba walikuwa wakimhitaji Musa. Wakaacha namba zao za simu ili wapigiwe mara moja katika kipindi ambacho Musa atakuwa amerudi kutoka kule alipokuwa amempeleka Andy.
Saa moja usiku mapolisi walikuwa wakipigiwa simu na kuambiwa kwamba Musa alikuwa mahali pale ambapo alikuwa akipaki gari lake. Musa alipewa taarifa kwamba alikuwa akitafutwa na mapolisi ambao walikuwa wakitaka awe mahali hapo.
Ni ndani ya dakika kumi mapolisi wakafika mahali hapo na kisha kuonana na Musa ambaye muda wote alikuwa akionekana kukosa amani kabisa, kitendo cha kufuatwa na mapolisi kilionekana kumtia wasiwasi sana.
Akaanza kuulizwa maswali kadhaa kuhusu kazi ile ambayo alikuwa akiifanya huku lengo kubwa la mapolisi wale wakitafuta kuzoeana nae hata kabla hawajamuuliza kuhusiana na Andy ambaye alikuwa amemsafirisha mchana. Walichukua dakika tano kuuliza kuhusu kazi yake na ndipo walipoanza kumuuliza kuhusiana na Andy.
“Yule jamaa mwenye mchanganyiko wa rangi?”
“Ndio”
“Alikuja hapa huku akionekana kuwa na haraka na mwingi wa wasiwasi. Nilipomuuliza kuhusiana na hali yake, aliniambia kwamba moto ulikuwa ukiteketeza ofisi yake na hivyo alikuwa akielekea kule kuokoa mafaili yake muhimu” Musa alijibu.
“Kwa hiyo ulimchukua na kumpeleka wapi?”
“Hotelini?”
“Hoteli gani?”
“Serena”
Mapolisi hawakutaka maswali zaidi, walichokifanya kwa wakati huo ni kuondoka na Musa kuelekea katika hoteli hiyo ambapo baada ya kufika wakaagiza viywaji huku macho yao yakiwa yanaangalia kila kona mahali hapo.
Kila mmoja alikuwa na uhakika kwamba usiku huo wangeweza kumuona Andy na hivyo kumkamata na kumfikisha katika vyombo vya sheria kwa tuhuma za kumuua Annastazia, spika wa Bunge ambaye alikuwa akikubalika sana.
Wala hawakukaa zaidi ya dakika kumi mara mbele yao akaonekana mwanaume mmoja ambaye kwa kumuangalia tu waliweza kumgundua kwamba alikuwa Andy, walichokifanya kwa wakati huo ni kuinuka na kuanza kumfuata.
Andy alikuwa akionekana kuwa na wasiwasi, muda wote alikuwa akiangalia huku na kule huku akionekana kuwa na wasiwasi mwingi. Mapolisi wale walikuwa wakimfuata, kadri Andy alivyokuwa akipiga hatua na ndivyo ambavyo alikuwa akizidi kuongeza kasi mpaka kufikia hatua ya kuanza kukimbia.
****
Ulikuwa ni msiba mkubwa ambao ulikuwa umeikumba nchi masikini ya Tanzania. Kila mwananchi ambaye alisikia kifo cha mwanamke ambaye alionekana shupavu, Spika wa Bunge, Annastazia Kapama akashindwa kuamini kile ambacho alikuwa amekisikia.
Watu wengi wakaonekana kuwa katika nyuso zilizojaa majonzi, kifo cha Annastazia kikaonekana kushtua kila mtu. Mitaani hakukukalika hata kidogo, watu walikuwa wakikizungumzia kifo cha Annastazia ambacho kilikuwa kimetangazwa masaa mawili yaliyopita.
Gazeti la Mlalahoi ambalo lilikuwa likitoka kila jioni likawa limeandika taarifa zile ambzo zilionekana kumshtua kila mtu siku hiyo. Gazeti hilo liliuza kopi nyingi sana nchini Tanzania kutokana na wananchi kulinunua kwa wingi sana siku hiyo.
Kila mtu alitaka kufahamu chanzo cha mauaji hayo ambayo yalikuwa yametokea chumbani kwake. Taarifa juu ya mtu ambaye alikuwa ametoka nchini Canada, Killerandy zikapatikana na hapo ndipo watu wakafahamu kwamba huyo mtu ndiye ambaye alikuwa amefanya mauaji yale.
Taarifa hazikuishia hapo, zilielezea kila kitu kwamba mtu huyo ambaye alijifanya kuwa mfadhiri alikuwa amedanganya jina, jina lake halisi alikuwa akiitwa Andy Wayne ambaye alikuwa dokta mkubwa sana nchini Marekani. Alikuwa amezaliwa na mwanamke wa Kitanzania huku baba yake akiwa mzungu kutoka nchini Marekani.
Gazeti lile likaonekana kuendelea kumvutia kila mtu. Likaeleza taarifa zaidi kwamba mwanaume huyo alikuwa amesoma shule moja na Annastazia huku wakiwa katika uhusiano wa kimapenzi. Kila mtu alionekana kuwa na hamu ya kutaka kufahamu kile ambacho kiliendelea baada ya kumaliza shule. Hakukuwa na kitu chochote ambacho kiliendelea zaidi ya watu hao kutokuonekana tena.
Hiyo ndio taarifa ambayo ilikuwa imechapwa katika gazeti hilo ambalo lilikuwa limepata habari hiyo kupitia mtandao mkubwa wa CNN ambao walionekana kufuatilia mambo mengi ya nyuma ambayo yalitokea katika maisha ya Andy.
Taarifa ile haikuwashtua Watanzania tu bali hata Wamarekani walionekana kushtuka kutokana na kile ambacho walikuwa wamekisikia na kukiona katika televisheni. Andy alikuwa ni daktari mkubwa sana ambaye alikuwa msaada mkubwa katika jamii yote ya Wamarekani, kamwe hawakutaka kumuonamtu wao akipata tatizo lolote lile, bado walikuwa wakimhitaji zaidi ya dokta yeyote yule kutokana na utaalamu wake ambao alikuwa nao juu ya magonjwa mbalimbali ya wanawake.
Watanzania wakaanza kuandamana huku wakiwa na mabango ambayo yalikuwa yakimtaka Andy akamatwe na kusfikishwa mbele ya mkono wa sheria ambako huko angeukumiwa kunyongwa au kufungwa kifungo cha maisha na kazi nzito.
“Ameuawa. Yaani mtu mzuri anauawa halafu mbaya anaachwa” Mwananchi mmoja ambaye alionekana kuwa na hasira alimwambia mwenzake.
Maandamanobado yalikuwa yakiendelea kama kawaida huku yakianza kuenea kila siku. Watu wa Morogoro wakaanza kuandamana na hata wa mikoa mingine nao wakifanya vile vile. Ndani ya masaa kumi tu, Watanzania waliokuwa katika mikoa yote nchini Tanzania wakaanza kuanamana kumtaka Andy atafutwe, akamatwe na hatimae kuhukumiwa kifo.
George alionekana kuchanganyikiwa, mara ya kwanza alipokuwa akipewa taarifa cha kifo cha mke wake alijiona kuwa kama ndondoni ambapo baada ya muda mfupi angeamka na kujikuta yupo kitandani. Masikio yake hayakuamini kile ambacho alikuwa amekisikia kutoka kwa mfanyakazi wa ndani, alichokifanya kwa wakati huo ni kuanza safari ya kuelekea nyumbani kwake.
Garini hakuonekana kutulia hata kidogo, alionekana kuchanganyikiwa kabisa huku kila wakati akiupiga piga usukani wa gari lake. Hakujua afanye nini mara atakapofika nyumbani na kukuta kwamba kile alichokuwa ameambiwa kilikuwa ni ukweli mtupu.
Akafika nyumbani na kuanza kupiga honi. Mlinzi akaufungua mlango, kwa jinsi hali ilivyokuwa ndani ilimfanya kuona kwamba kile ambacho alikuwa ameambiwa simu kilikuwa na ukweli asilimia mia moja. Mapolisi walikuwa wamejazana nyumbani kwake huku gari la wagonjwa likiwa katika eneo la nyumba ile.
Kwa haraka George akateremka kutoka garini na kisha kuanza kwenda ndani. Alitembea kwa haraka haraka, machozi yalikuwa yameanza kumlenga huku kadri alivyozidi kusogea mbele na ndivyo ambavyo machozi yale yalivyoanza kumtoka na kutiririka mashavuni mwake.
Mwili wa mkewe ulikuwa kitandani huku damu zikiwa zimetapakaa kitandani, George akaanza kulia kama mtoto huku akiliita jina la mke wake ambaye alikuwa akimpenda sana. Hilo lilikuwa pigo kubwa moyoni mwake, moyo wake ulimuuma kupita kiasi, hakuamini kama kweli huo ndio ulikuwa mwisho wa kumuona mkewe ambaye alikuwa akimpenda sana.
****
Mwanamke yule bado alikuwa akionekana kuwa na wasiwasi sana, kwake mapolisi walionekana kuwa watu wa hatari kabisa ambao kila siku katika maisha yake alikuwa akiwaogopa sana. Ila pamoja na hilo, akaanza kumfikiria Andy ambaye alikuwa amemficha, kama angesema ukweli kuwa alikuwa amemfunika na shuka lake na kisha mwanaume huyo kukaatwa, angepata nini? Tena isitoshe hata wale mapolisi wasingeweza kumshtukuru.
“Mama unatuchelewesha. Umemuona wapi?” Polisi mmoja aliuliza huku akionekana kuanza kupatwa na hasira.
“Alipita hapa akiwa anakimbia. Ameelekea kule kwenye giza” Mwanamke yule aliwaambia mapolisi wale.
Hakukuwa na cha kuuliza zaidi au kusubiri kitu chochote kile, walichokifanya mapolisi wale ni kuanza kukimbia kuelekea kule ambapo walikuwa wameambiwa kwamba Andy alikuwa amekimbilia, hakukuwa na polisi yeyote ambaye alikuwa na mashaka na shuka lile ambalo lilionekana kumfunika mtu, mapolisi wote walijua kuwa mtu ambaye alikuwa amefunikwa alikuwa mtoto wa mwanamke yule.
“Wewe baba amka undoke” Mwanamke yule yule alimwambia Andy ambaye akalitoa shuka lile na kuanza kuangalia huku na kule.
“Nashukuru sana” Andy alimwambia mwanamke yule na kisha kuondoka kwa kasi mahali hapo.
Mwanamke yule akaonekana kukasirika kupita kawaida, kitu ambacho alikuwa amekifikiria kabla kilionekana kuwa tofauti. Alichokitegemea kutoka kwa Andy ni shukrani ya kiasi fulani cha fedha kutokana na kile ambacho alikuwa amemfanyia.
Kuondoka kwa Andy bila kumpatia kiasi chochote kulionekana kumkasirisha sana. Moyo wake ukaanza kujuta kwa kuamua kumficha Andy ambaye wala hakuwa msaada wowote kwake. Alikuwa akiishi katika maisha ya kimasikini, kumsaidia Andy kulionekana kumpa matumaini ya kupata japo shlingi elfu moja kwa ajili ya kunywa chai asubuhi.
Andy bado alikuwa akikimbia, moyo wake ulikuwa ukimshukuru sana mwanamke yule ambaye alikuwa amemficha na kumfanya kutokuonekana kwa mapolisi wale ambao walionekana kuwa na hasira nae. Mbio zake ziliishia barabarani ambapo akachukua teksi na kutaka kupelekwa katika hoteli yoyote ndogo.
Dereva wa teksi ile akaanza kumpeleka katika hoteli ya Jumanji ambayo ilikuwa Magomeni Mapipa. Ni mwendo wa dakika saba tu wakawa wamekwishafika. Andy akateremka na kumlipa fedha dereva teksi yule na kisha kuelekea katika hoteli ile.
Maisha yake yakaanza katika hoteli hiyo huku akianza kufuatilia kila kitu ambacho kilikuwa kinaendelea kupitia televisheni. Picha zake zilikuwa zimebandikwa kila sehemu, alitafutwa kila sehemu lakini wala hakupatiikana. Kila gari ambalo lilikuwa likitoka nje ya jiji la Dar es Salaam lilikuwa likichunguzwa huku ulinzi mkubwa ukiwa katika uwanja wa ndege lakini napo huko wala Andy hakuonekana hata mara moja.
Mitaani bado msako ulikuwa ukiendelea, wapelelezi walikuwa wamemwagwa katika kila kona ndani ya jji la Dar es Salaam lakini wala Andy hakuweza kuonekana wala tetesi kusikika mitaani mwamba alikuwa sehemu fulani.
Mwezi wa kwanza ukapita, muda mwingi Andy alikuwa akikaa ndani tu na kama alikuwa akitoka nje basi ilikuwa ni usiku tu, tena katika muda ambao hakukuwa na watu wengi. Andy hakuwa akifanya mawasiliano ya simu na mtu yeyote yule, alikuwa akihofia sana kukamatwa.
Baada ya miezi miwili kupita, hapo ndipo alipojifikiria kuanza safari ya kurudi nchini Marekani bila kuonekana. Kwake kazi ilionekana kuwa kubwa lakini kwa kutumia fedha alijiona kufanikiwa kwa urahisi sana.
Kwa jinsi alivyokuwa akitafutwa ingekuwa ngumu sana kama angetumia ndege, usafiri ambao alikuwa akiufikiria kichwani mwake ilikuwa ni usafiri wa meli za mizigo. Hapo ndipo alipoanza harakati za kutafuta msaada huo hata kabla mambo hayajawa makubwa zaidi.
Alichokifanya ni kutoka chumbani mule hotelini na kuanza kuelekea barabarani ambapo akanunua kofia kubwa na kuivaa kichwani. Akasimamisha teksi ambayo ikaanza kumpeleka kule alipokuwa akitaka kwenda. Kusafiri salama kuelekea nchini Marekani haikuwa rahisi hata mara moja lakini kwake aliona kutokuwa na tatizo kubwa kwa sababu tu alikuwa ameishi sana nchini Marekani.
Meli ambayo alikuwa akiitaka kwa wakati huo ni meli ya mizigo ambayo ilikuwa ikielekea nchini Uingereza au nchi yoyote Ulaya. Alitaka kwanza kuelekea nchini Afrika Kusini ambapo huko angejua ni kwa jinsi gani angeunganisha safari kwani hakutaka kutumia meli moja kwa kuogopa kukamatwa.
Kwa kutumia kiasi cha fedha ambacho alikuwa nacho wala hakupata tabu kuingia bandarini. Moja kwa moja akaanza kuelekea katika sehemu ambayo ilikuwa ikihusika na mizigo ambayo ilikuwa ikiletwa kutoka nchini Ugiriki na kuanza kuongea na wahusika. Benedict hakuonekana kupata tabu sana kwani alionekana kuwa mtu kutoka nje na wala si mzamiaji.
“Sasa kwa nini unataka kutumia meli?” Kolatov, Mgiriki mwenye asili ya Urusi aliuliza.
“Najisikia tu” Andy alijibu.
“Una kiasi gani?”
“Dola elfu nne”
“Sawa. Kajiandae, safari itaanza kesho kutwa baada ya kumalizia hii mizigo iliyobakia” Kolatov alimwambia.
Benedict akaanza kurdi tena garini. Moyoni mwake alijiona kuwa mshindi kwani aliona ni lazima safari yake ya kurudi nchini Marekani ingefanikiwa. Alichokifanya ni kumtaka dereva wa taksi ampeleke daraja la Salenda huku lengo lake likiwa ni kutaka kuonana na mwanamke yule ambaye alikuwa amemsaidia kumficha na shuka katika kipindi kile alichokuwa anakimbizwa na polisi.
“Siamini kama ni wewe” Mwanamke yule alimwambia Andy.
“Ni mimi mama”
“Nilifikiri usingerudi. Karibu” Mwanamke yule alimwambia Andy na kumkaribisha katika kibanda kidogo ambacho alikuwa akikitumia kama chumba chake.
Hapo ndipo maongezi yalipoanza. Alichokifanya Andy ni kuchukua kiasi cha shilingi laki tano na kumgawia mwanamke yule ambaye alionekana kuchanganyikiwa kwani kiasi kile cha fedha kilionekana kuwa kikubwa sana kwake.
Kwa kuwa mwanamke yule alikuwa amekabidhiwa kiasi kikubwa cha fedha, moyoni mwake akaonekana kuwa radhi mbele ya Andy kuongea kitu chochote kile, fedha zilionekana kuubadilisha kabisa moyo wake.
Muda wote wa maongezi Andy alikuwa akijitahidi kumsoma mwanamke yule aliyejitambulisha kwa jina la Sikitu huku akitaka kujua mambo mengi kuhusu maisha yake. Bi Sikitu akaonekana kuwa muwazi, hakujali kama mwanaume yule aliyekuwa mbele yake hakuwa akimfahamu au la, alichokifanya hapo ni kutaka kuhadithia historia yake ambayo ilionekana kujaa matukio mengi.
“Una moyo?” Mwanamke yule alimuuliza Andy.
“Wa nini tena?”
“Kuisikiliza hiyo stori yangu”
“Ninao”
“Sawa. Nitakapoimaliza naomba uniambie kama sisi wa wanawake wa Kitanzania tunastahili kupendwa” Mwanamke yule alisema maneno ambayo yalionekana kumshtua Andy.
“Mmmh!” Andy alijikuta akiguna.
“Mbona umeguna?”
“Subiri kwanza. Una mtoto?”
“Ninae”
“Yupo wapi?”
“Barabarani”
“Anafanya nini?”
“Ananisadia kuombaomba. Unajua nimekwishakuwa mzee sasa. Huwa sijisikii vizuri kila ninapokwenda kuomba kwenye madaladala na ndio maana ninamuachia yeye kwenda kuombaomba” Bi Sikitu alimwambia Andy.
“Sawa. Unaweza kuniambia historia ya maisha yako?” Andy alimuuliza mwanamke yule.
“Naweza. Ila sitaki kuchukua muda wako mwingi baba yangu. Historia yangu imegawanyika sehemu tatu, sehemu ya kwanza kuanzia utotoni, sehemu ya pili kuanzia ujanani na sehemu ya tatu kuanzia miaka thelathini na tano. Wapi unapotaka nianzie?” Bi Sikitu alimuuliza Andy.
“Kutokana na muda. Anzia miaka thelathini na tano” Andy alimwambia Bi Sikitu huku akionekana kutaka kufahamu kile ambacho kilitokea katika maisha ya mwanamke huyo.
Macho yangu yalikuwa wazi japokuwa kwa wakati huo nilikuwa kitandani na usiku ukiwa mkubwa sana. Mtoto wangu, Abdul alikuwa amekwishalala kutokana na kutakiwa kuamka asubuhi na mapema kuelekea shuleni.
Kwa mbali kelele za kaka yangu, Rahman na mkewe Fatuma zilikuwa zikisikika. Kelele zao za kugombana hazikuwa siku ya kwanza kusikika, mara kwa mara walikuwa wakigombana hasa Fatuma alipokuwa akirudi usiku huku akiwa amelewa.
Rahman alikuwa mwanaume mpole sana, siku zote alikuwa akiipenda familia yake. Alimpenda sana mke wake, Fatuma ambaye alikuwa akimpa kila kitu alichokuwa akikitaka katika maisha yake. Fatuma alionekana kuwa mwanamke mjinga sana, kiburi na majivuno ndio yalikuwa sehemu ya maisha yake. Alijua fika kwamba mumewe, Rahman alikuwa akimpenda sana na ndio maana alikuwa akifanya ambo ya kijinga sana kwa kuona kwamba hasingeweza kuachwa.
Rahman alikuwa mwanaume mvumilivu sana, aliona mkewe akifanya mambo ya kijinga lakini kamwe hakuwahi kumkaripia au kumpiga. Kwangu nilimuona Rahman kuwa mwanaume mjinga sana kwani hakukuwa na mwanaume ambaye angevumilia mambo yale ambayo alikuwa akiyafanya Fatuma.
Mimi na Rahman tulikuwa ndugu ambao tulizaliwa na wazazi wawili na tulikuwa watoto pekee katika familia yetu. Wazazi wetu walifariki kipindi kirefu kilichopita. Nilifanikiwa kupata mume, Abdallah ambaye nilizaa nae mtoto mmoja ambaye ndiye huyu niliye nae, Abdul.
Mume wangu alikuwa kila kitu katika maisha yangu, alinifanyia mambo mengi sana huku akinionyeshea upendo mkubwa na ndio maana nilizimia mara nyingi sana mara nilipopewa taarifa kwamba alikuwa amefariki mara baada ya kugongwa na gari katika kipindi ambacho alikuwa akitoka kazini.
Ndugu zake wakaonekana kuwa na ukali katika mali za ndugu yao. Kwa sababu nilikuwa na mawazo mengi sana juu ya marehemu mume wangu, wala sikuonekana kujali kuhusu mali. Ndugu zake wakafanikiwa kuchukua mali zote ambazo zilikuwa zangu na za marehemu mume wangu.
Hapo ndipo kaka yangu, Rahman alipoamua niende kuishi nyumbani kwake pamoja na mtoto wangu. Fatuma hakuonekana kuufurahia ujio wetu ndani ya nyumba ile, alituonyeshea chuki za waziwazi kabisa lakini wala sikuonekana kujali kitu chochote kile.
Maisha ambayo alikuwa akiishi Rahman na mkewe, Fatuma ndio ambayo yalikuwa yakinikasirisha sana. Nilikuwa nikiyakumbuka sana maisha ya Rahman katika kipindi cha nyuma, alikuwa mwanaume mpole sana ambaye hata wazazi wetu walikuwa wakimshangaa sana.
Fatuma ndiye ambaye alijiona kuwa kichwa cha familia, alifanya kitu chochote ambacho alikuwa akitaka pasipo kuambiwa kitu chochote kile, Katika maisha yangu nikatokea kumchukia sana Fatuma, mbaya zaidi nikatokea kuwachukia wanawake wote kwani kwangu kuyaona maisha kama yale haikuwa mara ya kwanza.
Wanawake walionekana kuwa viumbe vya ajabu sana ambavyo wala havikustahili kuonyeshewa mapenzi ya dhati, huwa tunakuwa wasumbufu sana kwa mawanaume mara tu wanapoamua kutuonyeshea mapenzi ya dhati.
Mara nyingi sana nimekuwa nikimkufuru Mungu kwa kuamua kuniumba nikiwa mwanamke, sikustahili kabisa kuwa mwanamke katika maisha yangu. Nilijiona kuwa tofauti na wanawake wengine, nilikuwa nikiishi maisha tofauti na wanawake.
Siku za kwanza hata kabla sijawa mkubwa nilikuwa nikisikia mauaji mengi tu waliyokuwa wakiyafanya wanaume juu ya wanawake, moyoni nilikuwa nikiumia sana kwani sikuwa nikitegemea kuona au kusikia mambo kama hayo lakini baada ya kukua nikaja kuona kwamba walistahili kufanyiwa mambo kama yale.
Mioyo yetu ni mioyo mikatili sana, huwa tunaweza kubadilisha hali ya mchezo muda wowote ule. Kumsaliti mtu fulani kwa sababu ya fedha wala si jambo kubwa kwetu, huwa hatuyajali maumivu ambayo watakuja kuyasikia mara baada ya kuwasaliti. Fedha ndio kitu ambacho tunakitafuta sana katika maisha yetu.
Kilipita kipindi kirefu sana hatimae Rahman akafariki katika mghahawa mmoja huko Shinyanga alipokuwa amekwenda kikazi. Kifo chake kilikuwa na utata mkubwa sana kwani alikuwa amewekewa sumu katika kinywaji chake.
Nilikuwa nimeshikwa sana na wasiwasi moyoni kwani tangu Rahman aondoke kuelekea Shinyanga nae mkewe, Fatuma alikuwa haonekani nyumbani na hivyo kumtilia mashaka kwamba alikuwa amehusika katika kifo hicho.
Moyo uliniuma sana na kuanza kujuta kwa nini Rahman hakuwa amemuua Fatuma tangu zamani mpaka kuja kuuawa yeye. Kifo cha Rahman ndicho ambacho kilisababisha mambo mengi katika maisha yangu na mwanangu.
Baada ya mwezi Fatuma akatufukuza katika nyumba yake. Sikuwa na ndugu yeyote ndani ya jiji la Dar es Salaam hali iliyonifanya nianze maisha ya mitaani pamoja na mwanangu. Shuleni akafukuzwa kwa kukosa ada, moyoni niliumia sana.
Japokuwa mimi ni mwanamke lakini milele nitaendelea kuichukia jinsia hii. Mwanamke ameonekana kutokuwa na mapenzi ya dhati, na hata kama atakuonyeshea mapenzi ya dhati katika kipindi hiki, baadae anaweza kubadilika na kuwa na roho mbaya hata zaidi ya shetani.
****
Bi Sikitu akashindwa kuvumilia, machozi yalikuwa yakimtoka. Alikuwa ameelezea kwa kifupi sana historia fupi ya maisha yake lakini bado ilionekana kumgusa sana. Andy alibaki akimwangalia kwa masikitiko, akapata jukumu la kuanza kumbembeleza.
Hapo ndipo Andy alipoanza kumfikiria Annastazia na kuona kwamba alistahili kumuua kutokana na kile ambacho alikuwa amemfanyia. Usaliti ukaonekana kuwa sehemu ya maisha ya wanawake wengi ambao walikuwa wakiishi nchini Tanzania. Moyo wake ukazidi kuwachukia wanawake wa Kitanzania.
Andy akainuka na kisha kuaga. Moyoni mwake kukaanza kujengeka kitu kingine, sasa akatamani kuwaua wanawake wote wa Kitanzania. Hakutaka kuwaacha wakibaki hai, alijiona kuwa na sababu ya kuua mamilioni ili aokoe mabilioni.
Chuki yake juu ya wanawake wa Kitanzania ikawa kubwa moyoni mwake. Alipofika barabarani akasimamisha teksi akapanda na kisha safari ya kuelekea hotelini kuanza. Kila mwanamke ambaye alikuwa akimuona njiani kwake alionekana kuwa mbaya na msaliti mkubwa, kiu ya kutaka kuwaua wanawake wa Kitanzania ikamkaba moyoni, hakuona sababu ya kuwaacha watu na wakati mara kwa mara walikuwa wakiwasaliti wanaume zao na kuwasababishia maumivu makali mioyoni mwao.
Alipofika hotelini, akateremka na kuanza kuelekea ndani ya jengo la hoteli ile. Kadri alivyozidi kuwaona wanawake na ndivyo ambavyo hasira zake zilipokuwa zikiongezeka zaidi na zaidi, wanawake kwake walionekana kuwa kama mashetaki ambayo hayakuwa yakistahili huruma yoyote ile maishani mwao.
Aliingia chumbani na kujipumzisha huku akipanga safari ya kuelekea Bandarini kesho kutwa na kuanza safari ya kuelekea Marekani. Akili yake haikutulia usiku huo, alikuwa akiwaza juu ya kuondoka nchini Tanzania pasipo kugundulika na mtu yeyote yule.
Alikuwa akiziona televisheni mbalimbali zikiendelea kutangaza kwamba alikuwa akitafutwa, kwa mtu yeyote ambaye angefanikisha kupatikana kwake akiwa hai au amekufa atakabidhiwa kiasi cha shilingi milioni hamsini.
Muda wote Andy alikuwa akicheka kwa kujiona mshindi kati ya washindi, kwake, kukamatwa kulionekana kuwa vigumu sana kutokana na mipango yake ya safari ambayo ilikuwa ikiendelea kufanyika.
****
Baharia, Kolarov alikuwa ameshtuka sana mara baada ya kumuona Andy mbele ya macho yake. Kiasi cha fedha ambacho kilikuwa kimetangazwa kwake kilionekana kuwa kikubwa japokuwa alikuwa akihitaji kiasi kikubwa zaidi.
Kadri alipokuwa akiongea na Andy, alitamani sana kuwapigia simu mapolisi na kuwaita mahali hapo wamkamate na kisha kumgawia kiasi cha fedha ambacho kilikuwa kimeahidi na kutangazwa mara kwa mara katika vyombo vya habari.
Juhudi za kumkamata Andy zilionekana kufifia machoni mwa Watanzania kutokana na Andy kuonekana kuwa mjanja sana. Serikali haikukata tamaa, bado ilikuwa ikiendelea kumtafuta Andy kwa mategemeo ya kumkamata.
“Una uhakika ni yeye?” Lilikuwa ni swali lililotoka kinywani mwa polisi mmoja ambaye alikuwa akiongea simu na Kolarov.
“Asilimia mia tatu”
“Upo wapi?”
“Mbona unakuwa na haraka hivyo? Sikiliza, nionganishe na wakubwa zako kwanza” Kolarov alimwambia polisi yule ambaye bila ubishi aliiunganisha simu ile na makao makuu ya polisi.
“Unasemaje?” Kamanda mkuu, Bwana Pawasa aliuliza kwa mshtuko.
“Ndio hivyo. Nipo nae na anataka kuondoka kuelekea nchini Marekani kwa njia za panya” Kolarov alimwambia.
“Kwa njia gani?”
“Za panya”
“Zipi?”
“Hebu acha kuuliza maswali ya kitoto. Mna milioni mia moja niwaonyeshe pa kumkamata?” Kolarov aliuliza.
“Ni kiasi kikubwa sana cha fedha. Kiasi kilichowekwa ni milioni hamsini tu” Kamanda Pawasa alimwambia Kolarov.
“Kama hamna basi poa. Mwacheni tu aondoke zake” Kolarov alisema na kukata simu.
Kolarov alibaki akitabasamu tu, alijua fika kwamba ni lazima angepigiwa simu na kuanza kubembelezwa juu ya kiasi kile cha fedha ambacho alikuwa akikihitaji. Hakuwa na wasiwasi wa mawasiliano ya simu yake kwani alikuwa akitumia mtandao wa simu wa Kimataifa ambao ulikuwa ukitumika sana na wageni wa kimataifa hasa wakubwa. Hata kama wangejaribu kusoma signal ya mahali simu hiyo ilipokuwa imepigwa, kusingekuwa na mtu yeyote ambaye angefanikiwa kupata signal.
Alichofikiria ndicho kilichotokea, baada ya dakika kadhaa simu yake ikaanza kuita, akaipokea huku tabasamu pana likiendelea kuonekana usoni mwake.
“Mmefikiria nini?” Aliuliza.
“Nimeongea na wakuu, wamekubali kukupa kiasi hicho cha fedha” Kamanda Pawasa alijibu.
“Sawa. Mnachotakiwa kufanya ni kuja na hicho kiasi cha fedha nami nitawapeni mtu huyo mnayemhitaji. Mmesikia?” Kolarov alisema.
“Sawa”
****
Alichokifanya Andy ni kuanza kuwasiliana na Dawson na kumueleza kila kitu ambacho kilikuwa kimeendelea. Dawson alionekana kushtuka sana kwani kwa mara ya kwanza ambapo aliziona taarifa zile katika magazeti na vyombo vingine vya habari alikuwa akipuuzia kwa kuona kwamba alikuwa mtu mwingine ambaye walikuwa wamefanana majina tu.
Kwa kuwa Andy alikuwa mtu muhimu sana katika maisha yake huku dawa zaidi zikiwa zinahitajika, Dawson akaamua kufanya kila linalowezekana kuhakikisha kwamba Andy anafika salama nchini Marekani na kuendelea na utengenezaji wa dawa za virusi aina vya Katapillar ambavyo vilikuwa vikisambaza ugonjwa wa PENINA.
“Nataka kuwaandaa vijana wangu wakufuate huko” Bwana Dawson alimwambia.
“Hapana. Wasije Tanzania. Kama itawezekana waje Afrika Kusini” Andy alimjibu.
“Hilo linawezekana. Kuna kingine?”
“Ndio. Nitahitaji sura ya bandia ambayo itakuwa imetengenezewa passport pamoja na hati zote za kusafiria” Andy alimwambia.
“Usijali. Ni ndani ya masaa mawili. Usiku huu vijana wangu watapanda ndege na kuja Afrika Kusini ambako huko utakutana nao na kisha kuanza safari ya kuja huku. Sisi ndio wazungu bwana, mtu mweusi hawezi kutusumbua” Bwana Dawason alimwambia Andy.
Mara baada ya siku ya safari kufika haraka haraka Andy akaanza kujiandaa tayari kwa kutoroka kuelekea nchini Marekani kwa kutumia meli ya mizigo iliyokuwa bandarini. Lengo lake kwa wakati huo lilikuwa ni kutaka kufika Afrika Kusini ambako angekutana na vijana wa Dawson na kisha harakati za safari kuanza huku akiwa na sura ya bandia. Kichwani mwake, mawazo yake yalikuwa juu ya safari hiyo huku mara kwa mara akimuomba Mungu Aweze kumlinda mpaka kufika salama nchini humo.
Alipofika getini, macho yake yakatua kwa Kolarov ambaye alikuwa akimsubiri na kisha kuanza kuondoka nae kuelekea katika meli ile. Kwa kuwa Kolarov alikuwa akijulikana na watu wengi hasa wafanyakazi katika bandari ile wala hakukuwa na mtu yeyote ambaye alimuuliza swali lolote lile kuhusiana na mgeni wake.
Wakafika katika meli ile na kumpeleka Andy katika chumba kimoja kilichokuwa na mizigo kadhaa huku akisingizia kisa cha kumuingiza mule ilikuwa ni sababu ya ulinzi wake. Andy hakuonekana kumtilia mashaka Kolarov, japokuwa walikuwa wamekutana kwa kipindi kichache sana lakini akajikuta akianza kumuamini.
Muda wote ule Andy alikuwa akifurahia, alijiona kuwa mshindi zaidi ya washindi, kwake, kumuua Annastazia na kisha kurudi nchini Marekani bila kuonekana ilionekana kuwa ushindi mkubwa sana. Alibaki ndani ya chumba kile kikubwa huku akiwa amewekewa magazeti mbalimbali ambayo akaanza kuyasoma.
Ni picha zake ndizo ambazo zilikuwa zimeenea kwa sana katika kila gazeti ambalo alikuwa akilisoma, watu walikuwa wakihitaji kumuona akifikishwa mbele ya sheria na kushtakiwa kwa tuhuma za kumbaka Annastazia na kisha kumuua kinyama.
Aliendelea kubaki mule chumbani kwa takribani dakika thelathini na ndipo akaanza kusikia mlango ukigongwa. Mara ya kwanza hakutaka kuufungua kwa kujua kwamba hakukuwa na mtu yeyote ambaye alikuwa akiufahamu uwepo wake ndami ya meli ile lakini aliposikia kwamba alikuwa Kolarov, akaufuata mlango na kuufungua.
Andy alibaki kuwa na mshtuko mkubwa, mwili wake ukapigwa ganzi. Macho yake yalikuwa yakiangalia midomo ya bunduki tano ambazo zilikuwa zimemuelekezea kutoka kwa mapolisi walioonekana kuwa na hasira kali.
Andy alijiona kukamatwa kirahisi sana, kichwa chake wala hakikupata kazi ya kujiuliza ni nani alikuwa amewaelekeza mapolisi kwamba alikuwa ndani ya meli ile kutokana na Kolarov kuwa pembeni yao akimwangalia huku uso wake ukiwa na tabasamu pana na mfuko mkubwa wa kaki ulioonekana kuwa na fedha ukiwa mkononi mwake.
“Uko chini ya ulinzi” Polisi mmoja alimwambia na kisha kumsogelea na kumfunga pingu kwa nyuma.
****
Mapolisi walikuwa wakitamani kumfahamu mtu ambaye alikuwa akiwapa taarifa njema kwa wakati huo, kumkamata Andy ndicho kitu ambacho kila Mtanzania alikuwa akikitaka sana kukisikia. Kuhusu fedha wala halikuwa tatizo kubwa.
Mara baada ya Kolarov kuwapa maelekezo ya mahali alipokuwa, mapolisi wakaanza kujiandaa huku mikononi wakiwa na kiasi hicho cha fedha. Ni mwendo wa dakika kumi tu wakawa wamekwishafika katika bandari hiyo ambapo wakaingia bila kizuizi chochote kile.
Kitu cha kwanza ambacho walikuwa wakikitaka ni kuonana na mwanaume ambaye alijitambulisha kwao kwa jina la Kolarov aliyekuwa katika meli ya mizigo ya Caspian. Wakapelekwa mahali ilipokuwa meli ile na kisha kutaka kuonana na Kolarov.
“Una uhakika ni yeye?” Polisi mmoja ambaye alionekana kuwa mkuu wao alimuuliza.
“Asilimia 600”
“Sawa. Tumfuate”
“Subirini kwanza. Fedha zenyewe ziko wapi?” Kolarov aliuliza.
“Fedha kabla ya mzigo?”
“Mzigo kabla ya fedha? Nipeni kwanza. Huyu mtu yupo na wala hakimbii” Kolarov aliwaambia.
Hapo hapo polisi ambaye alikuwa na bahasha kubwa ya kaki akaitwa na kisha kumpa mkuu yule wa mapolisi bahasha ile ambayo ilikuwa na kiasi kikubwa cha fedha. Kolarov hakutaka kuhesabu kwani alikuwa na uhakika kwamba hakufanyiwa mchezo wowote mchafu.
“Bora mlivyoziweka kwenye dola kwani mmenipa urahisi mkubwa” Kolarov aliwaambia huku uso wake ukiwa kwenye tabasamu pana.
Hapo ndipo ambapo akaanza kuingia ndani ya meli ile pamoja na wale mapolisi ambao walikuwa wamekuja mahali pale. Wala hakujisikia uchungu moyoni, kumkamatisha Andy kwa mapolisi kulionekana kuwa jambo zuri sana kutokana na fedha ambazo alikuwa amelipwa.
Hakumjua Andy kwa sana zaidi ya kumuona ona kwenye vyombo vya habari tu na ndio maana hata kama alikuwa akikamatwa, kwake wala halikuwa tatizo kubwa kutokana na akili yake kwa wakati huo kufikiria zaidi fedha.
Akaanza kuugonga mlango ule na kisha baada ya muda fulani Andy kuufungua na mapolisi kumuweka chini ya ulinzi.
Je nini kitaendelea?
Je Andy atapewa hukumu gani?
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment