Search This Blog

Tuesday, 14 June 2022

ULAANIWE - 1

 

        



    IMEANDIKWA NA : GEORGE IRON MOSENYA





    *********************************************************************************



    Simulizi : Ulaaniwe

    Sehemu Ya Kwanza (1)



    ULIKUWA usiku mnene, mapigo yangu ya moyo yalikuwa juu sana. Lile giza lilinitisha sana, mbaya zaidi kijiji kile palikuwa na tatizo ambalo hapo awali sikujua kama lipo.

    Hii ni kwa sababu ya kuishi mjini kwa siku nyingi na kuzoea kuwa lile tatizo haliwezi kuwa sehemu yoyote ile.

    Tatizo la mtandao!!

    Nisingeweza kumpigia simu baba yangu mdogo ili aweze kunifuata mahali nilipokuwa.

    Usalama wa mwili wangu nd’o ulikuwa kitu cha kwanza ambacho nilikuwa nakihofia lakini pia ndani ya begi nililokuwa nimebeba kulikuwa na vifaa vya ofisini. Kamera, barua kadha wa kadha ambazo nilitakiwa kuzifikisha ofisi iliponiagiza, nilikuwa na kifaa cha kunasia sauti na kamera ya kurekodi picha zinazotembea pia.

    Vile vifaa ukijumlisha na kompyuta yangu ndogo vilikuwa na thamani ya juu sana.

    Na ofisi isingenielewa kwa namna yoyote iwapo ningekabwa na kuibiwa vifaa vile. Maana mahali nilipokuwa si ofisi iliponiagiza.

    Bundi waliendelea kulia na wale ndege wengine wenye sauti za kukera mithiri ya bundi walizidi kukifanya kiza kile kiwe cha kutisha mno.

    Nikaikumbuka ikulu iliyopo jijini Dar es salaam inavyomeremeta na zile rangi zake nyeupe za kuvutia. Ikulu I’sokatika umeme wala maji.

    “Hivi raisi anapafahamu kweli huku? Ama hawa watu wanafahamu kama wana raisi kweli?” haya nd’o maswali pekee ya kujenga niliyojiuliza huku nikiwa bado ndani ya giza lile.

    Yaliyofuata baada ya hapo yalikuwa yaleyale maswali ya kuogofya.

    Nikakumbuka pia nyumbani kwa mjomba kuna mbwa wakali sana ambao ni kitambo sana lazima watakuwa wamenisahau.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Niliitoa simu yangu na kuitazama na kujaribu kurengesha hapa na pale ili niweze kupata mtandao walau niwasiliane na mjomba aweze kunitoa katika dhahama ile.

    Hakuna kitu!! Mtandao ukagoma kabisa na sit u kugoma hapakuwa na dalili ya mtandao.

    Nikakumbuka enzi zile, ni kampuni moja tu ya simu ambayo walau ilikuwa na haueni katika suala zima la mtandao. Ubaya kadi yangu ya simu ile ilikuwa ni mpaka niitafute ndani ya begi kisha niweze kubadilisha.

    Nikapiga moyo konde, liwalo na liwe.

    Nikachuchumaa kisha nikalifungua begi langu na kisha kwa kutumia mwanga wangu wa simu nikapekua huku nikiwa natetemeka.

    Simu ilinionyesha kuwa yapata saa tano usiku, nikaghafirika kwa sababu muda kama ule jijini Dar es salaam ni mchana kweupe.

    Lakini pale hapakuwa Dar!

    Nilikuwa kijijini kwa mjomba.

    Nilipekua na hatimaye nikaipata ile kadi ya simu!!

    Upesi nikaizima simu yangu na kisha nikaifungua ili niweze kubadilisha kadi niweke kadi nyingine ambayo walau ilikuwa inaweza kufanya kazi vyema katika kijiji kile.

    Shughuli ya kuweka kadi kwenye simu ilikuwa nyepesi kama tu kuna mwanga lakini ilikuwa tabu kufanyia gizani, mara niweke kadi ya simu vibaya mara nikosee kuweka betri.

    Akili ikachotwa na umakini wa kuweka kadi katika simu, nikasahau ile hatari niliyokuwa naiwaza mara kwa mara.

    Hatari ya kukumbwa na vibaka na kuibiwa kisha kujeruhiwa ama kuuwawa kabisa.

    Hilo lilikuwa kosa ambalo siwezi kulijutia kwa sababu ilibidi litokee tu ili lililotokea mbele yangu litokee.

    Niliona kama kivuli kikitikisika, niliponyanyua uso wangu nikakutana na kivuli kilichoveshwa nguo.

    Kivuli chenye mikono.

    Mkono ambao ulikuwa umebeba panga kubwa sana!!

    Macho yangu yalipolizoea giza nikagundua kuwa kile hakikuwa kivuli. Alikuwa ni mtu lakini alikuwa amevaa matambala kana kwamba ni kichaa.

    Moja kwa moja nikatambua mbele yangu kuna mtoa uhai na ntakuwa mpuuzi nikiendelea kutazama na mtoa uhai.

    “Shkamoo!” nilimsalimia.

    Yule mtu hakujibu kitu, nilichokisia kutoka kwake ni pumzi tu zikiwa zinapishana kwa kasi.

    Nikajiuliza nikikimbia nitakimbilia wapi. Sikuwa mwenyeji sana hasahasa kwa usiku, bora ingekuwa mchana basi ningeweza kuiona njia nikatimua mbio huku nikipiga makelele ya kuomba msaada!

    Begi langu lilikuwa wazi! Je nikimbie na kuliacha?

    Hapana!

    Mara ghafla Yule mtu mbele yangu akajikohoza. Kisha akatokwa na neno akiwa hana papara katika kuzungumza.

    “Wewe ni nani, na mbona unatembea katika mida isiyokuwa yako….”

    “Naitwa Jimmy… Jimmy mtangazaji wa Redio Adhuhuri….” Nilijitambulisha upesiupesi nikitumia nafasi hiyo kujitambulisha na dhamana niliyokuwanayo katika jamii, nilifanya vile kama pata potea na liwalo na liwe, kama ni nmtu mbaya angetumia fursa ile kunikamua kila nilichonacho kwa sababu tu ni mtangazaji ninayejulikana, na kama si mtu mbaya angeweza kunisaidia.

    Nilitaja jina langu basi tu! Huku nikitambua wazi redio yetu huko kijijini kwao haishiki kabisa.

    Ila uoga nadhani kila mtu anajua!!

    “Jimmy Elikael Sumo!”

    Ajabu! Mtu Yule mwenye matambala alilitaja jina langu kikamilifu kama ambavyo huwa najitambulisha nikiwa kazini.

    “Ni mimi.. naam ni mimi…”

    “Unajifanya kuyajua mapenzi sana eeh?” aliniuliza hatimaye. Swali lile lilinishangaza sana kwa sababu lilikuwa la ghafla mno.

    “Hapana mkuu.. ni kazi tu…” nilijitetea huku jasho likinitoka.

    Yule bwana alikaa kimya kwa sekunde kadhaa kisha akainama, na aliponyanyua uso wake alinikazia macho. Sasa alikuwa katika simanzi nzito!

    Nilitamani kumuuliza, lakini nililiogopa panga alilokuwa amelikamata vyema katika mkono wake.

    “Jimmy Elkael Sumo…” sijui kama alikuwa akiniita au alikuwa akilitaja tu jina langu. Nikatikisa kichwa kukubali kuwa ni mimi.

    Akainama tena bwana Yule, sasa alitumia muda mwingi zaidi.

    Alipounyanyua uso wake alikuwa akitokwa na machozi.

    “Kipi kimekuleta huku Jimmy, kipi kimekuleta katika ardhi hii mbaya. Ardhi yenye rutuba lakini ikikaliwa na watu wabaya. Usiku huu mkubwa unaenda wapi Jimmy.. niambie unaenda wapi Jimmy!” aliniuliza huku akipambana na kilio chake.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Naenda kwa mjomba wangu, mzee Mathias…”

    “Mathias Yule mwalimu mstaafu alikuwa akifundisha hapo shule ya msingi? Yule ni mjomba wako?”

    “Naam huyohuyo!”

    “Aah! Mathias mtu mwema sana, mtu mwema yeye na familia yake. Mungu ampe maisha marefu yeye na kizazi chake….. ila kuna familia haa zimezaa mashetani. Nami ni mtembea usiku, napambana na mashetani. Japokuwa hata mimi ni shetani, umewahi kukutana na shetani Jimmy Sumo?” Yule bwana alitoa kauli tata nisizozielewa. Na ile kauli ya kujiita yeye shetani ilinifanya niusikie mkojo ukizidi kusogea karibu.

    “Utaweza kufika mwenyewe usiku huu, maana kuna mashetani wengine kama mimi hawana mazungumzo marefu kama haya. Yanaua na kusahau!” aliniuliza, nikatamani kujibu kitu lakini mdomo ukawa mzito sana kwa sababu akili iliamini kuwa ninakabiliwa na shetani.

    “Najua huwezi kufika ukiwa mwenyewe!!” likaendelea kuzungumza jitu lile ambalo awali lilitokwa na machozi pasi nami kufahamu nini tatizo.

    “Sasa sikia, sogea.. sogea tufanye mpango mmoja… sogea Jimmy Sumo…” jitu lile lenye panga likanivuta karibu yake, mapigo yangu ya moyo yalikuwa juu sana. Lakini sikuweza kujua ni kipi ntafanya nikasogea.

    Jitu lile lilikuwa linanuka sana, lilinuka kinyesi cha ng’ombe na mbuzi. Na alipozungumza tena nikagundua kuwa hata mdomo wake ulikuwa unatoa harufu.

    “Sasa mimi ninakusundikiza hadi kwa mwalimu Mathias halafu mi sitakaa kabisa utaniruhusu mimi niende kuyasaka mashetani… si utaniruhusu Jimmy?” aliniuliza huku akinong’ona, kufikia hapo nikatambua kuwanilikuwa nazungumza na mtu ambaye akili zake hazijakaa mkao kichwani.

    Nikatikisa kichwa kukubali ilimradi tu!

    Tukaanza kuondoka, na tukiwa njiani akaanzisha mazungumzo.

    “Jimmy… haya mashetani ya kiume yanaua mwili unakufa na kusahaulika. Bora basi hayo yanakuua unaenda katika mbingu usizozijua kama zipo ama la… lakini kuna mashetani ya kike Jimmy. Kuna shetani moja hilo nd’o kuu kuliko yote linaitwa Maria. Jimmy haya mashetani ni hatari, yaani yanakuua moyo kisha unaendelea kubaki hai duniani. Jimmy wanawake ni mama zetu, dada zetu, rafiki zetu, bibi zetu, wake zetu, shangazi zetu lakini usisahau kabisa… unanisikia Jimmy usisahau kabisa nakusihi. Wanawake ukiwaamini sana wanakuletea majibu mawili tu…. Furaha ama majuto ya milele. Wasichana ni maadui zetu!!!

    Na msichana mpumbavu kupita wote ni Maria…. Maria ni mshenzi, muuaji, msaliti, mnafiki.. Maria kweli yaani…” lile jitu likashindwa kuendelea kuzungumza. Kilio kikamzidi akaanza kulia akalitupa panga lake chini…. Na akiwa bado vilevile katika kilio cha kwikwi akatokwa na kauli.

    “ULAANIWE MARIA…. Ulaaniwe wewe na kizazi chako. Na iwapo hautalaaniwa Maria nitakuonyesha kwa mkono wangu mwenyewe nini maana ya laana! Ntakulaani mwenyewe Maria.”

    Sasa nilipata kigugumizi cha akili kuhusiana na utimamu wa lile jitu. Kwa sababu kuna mambo ambayo liliyasema lakini yakiwa na ukweli mtupu ndani yake.

    Baadaye likasimama tena na kuendelea na safari hadi tukafika nyumbani kwa mjomba. Baada ya kugonga hodi, mjomba alipoamka mimi nilikuwa nangoja kwa hamu afungue mlango niweze kuzama ndani ikiwezekana hata nisiliage jitu lile japokuwa lilikuwa limenifanyia msaada mkubwa sana bila kunidhuru wala kuniibia chochote.

    Kweli mjomba akaufungua mlango baada ya mimi kujitambulisha, upesi baada ya kuufungua ule mlango nikakimbilia kuingia ndani kwa fujo huku nikimpiga kikumbo mjomba wangu!

    “Jimmy, namna gani bwana..” alinihoji. Hapo nikageuka nyuma nikapigwa bumbuwazi. Hapakuwa na lile jibu wala dalili yoyote ya jitu la kutisha.

    Nikamsimulia mjomba upesiupesi, akacheka sana na kuniambia kuwa nina mawenge na hakuna kitu kama kile pale.

    Ama! Nilichanganyikiwa kiasi Fulani!!

    Nikalala huku nikiliwaza lile jitu na kauli yake ya kumlaani Maria!

    Maria ni nani sasa? Mbaya zaidi lile jitu halikujitambulisha jina!!!

    Kizungumkuti kikaanzia hapa!!!



    NILICHUKUA muda mrefu sana kuupata usingizi, nikawa najiuliza kisha nakubaliana na hoja ya mjomba kuwa nilikuwa nina mawenge usiku ule, wala sikukutana na mtu yeyote yule na pale nyumbani nilienda nikiwa mimi mwenyewe.

    Lakini kila nilivyofumba macho nililiona lile jitu na panga lake, kisha nikayakumbuka na maneno yake ya ajabu ajabu.

    Kivipi sasa mjomba aseme eti sikuwa na mtu yeyote!

    Halafu!... lile jitu hadi mjomba linamjua vizuri kabisa.

    Hilo likawa wazo la mwisho kile kiubaridi cha usiku kikazidi kupuliza, nikajifunika gubigubi nikaanza kuusaka usingizi.



    Mjomba aliniamsha majira ya saa kumi na moja alfajiri wakati akiwa anafungulia ng’ombe kwa ajili ya kwenda kulima. Niliisikia miluzi yake ileile niliyoizoea tangu enzi zile. Alipiga miluzi huku akizungumza na ng’ombe wake ambao aliwapa majina kila mmoja.

    Sikuweza kuendelea kulala, nikaamka.

    Nikavaa suruali yangu na makubadhi yaliyoundwa kwa tairi la gari. Nikatoka nje!

    Nikasalimiana na mjomba, akanisihi niendelee kulala nikakataa katakata kuwa siwezi kulala tena. Tutaongozana wote shambani!

    Hakunipinga tukaondoka!

    Wakati tukiwa bado jirani na zizi tuliwasikia mbwa wakibweka kwa fujo sana. Mjomba hakujali sana badala yake alipaza sauti kuwaita.

    Ajabu! Hawakuja. Tofauti na alivyotarajia.

    Hapo ndipo akahisi kuna kitu, akawasha tochi yake tukaongozana na kuwakuta mbwa wakivutana huku na kule mjomba akamulika walichokuwa wanawania.

    “Whaat! Mjomba, nguo ya lile jitu, naikumbuka nd’o hiyo lile jitu mjomba….” Nilihamanika na kumweleza mjomba kile kitu alichokuwa akinibishia usiku uliopita.

    Na hapo hapo sauti ikitokea mbali kabisa ikaita katika namna ya kuacha mwangwi mkubwa.

    “Jimmy Elkael Sumo……. Jimmy Elkael Sumo… ntakutafuta kaka.”

    Kufikia hapo hapakuwa na ubishi tena, jitu lilikuwa linaishi!!

    Mjomba akataharuki, akawaamrisha mbwa wake wafuatilie ile sauti.

    Ila looh! Wale walikuwa mbwa mkali kwao, sio nje ya hapo. Wakafyata mkia na kuanza kumrukia rukia mjomba.

    Kwa hasira akaipiga teke mbwa moja ikabweka na kukimbia wenzake wakafuata.

    “Na siwapi chakula leo mbwa koko wakubwa nyie… “ kwa ghadhabu akabwatuka. Almanusura nicheke.

    Nikajikaza!

    “Je kama linguo lina sumu hili, mbwa koko hawa wanaweka midomoni tu…. Simbaaaa kujaa hapa!” akamalizia malalamiko yake kwa kumuita mbwa wake mmoja.

    Mbwa hakuja!

    Hali ilikuwa ya hatari.

    Mjomba akaniongoza hadi ndani na kisha akaanza kunieleza hisia zake juu ya kilichotokea.

    “Jimmy, uliwatembelea wataalamu kabla haujaanza safari!” aliniuliza.

    “Wataalamu gani anko?”

    “He! Na ukubwa wote huu hauwajui wataalamu… ulisafishwa?” akauliza kivingine sasa nikaelewa alichokuwa akimaanisha.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Hapana sijawani kuhudhuria huko….”

    “Basi hii ni ishara ya hatari, kuna watu wanakufuatilia. Ujue hakuna mchawi amewahi kugusa himaya yangu, tangu marehemu babu yako anirithishe hizi nyumba, hii nd’o mara ya kwanza. Hawa utakuwa umetoka nao Dar.. wajanja wajanja sana hawa…” mjomba alizungumza kauli ambazo hazikunitisha bali kunisikitisha kuwa imani za kishirikina bado zilikuwa tatizo kijijini.

    “Unamaanisha lile jitu …. Aaargh unamaanisha nilikutana na mchawi jana?”

    “Tena mchawi mwenye hatari sana..”

    “Mh! Mjomba mchawi anayelalamika kutendwa kimapenzi, anayejua kuwa ulifundisha shule ya msingi, mchawi analilia mapenzi na kumlaani msichana.. “ nikiwa nazungumza mjomba akanikatisha kwa swali.

    “Umewahi kumuona mchawi?” aliniuliza swali lililonifedhehesha ni kweli sikuwa nimewahi kuonana na mchawi.

    “Bado…”

    “Basi usijifanye unazijua sura za wachawi… usijifanye kabisaaa..” alinionya.

    Nikawa mpole. Akayatawala maongezi.

    Kisha akaingia ndani akarejea na bangili fulani la chuma na kuniambia nilivae.

    Mkubwa mkubwa tu! Nikalivaa!

    Ni vile hatukujua tu lijalo ama lililotokea nyuma ya visigo vyetu…

    Laiti kama tungejua……..



    ***



    SIKU mbili baadaye nilimuaga mjomba kuwa naelekea kazini, maana hata uwepo wangu pale ulikuwa wa kuibia ibia tu.

    Ofisi ilikuwa imetuagiza kutafuta vipindi maalumu hasahasa vya makala kwa ajili ya kuleta upinzani wa kweli kwa vituo vipya vya redio na runinga vilivyokuwa vimeanzishwa jijini Dar es salaam.

    Mimi na waandishi wengi watatu tulikuwa tumeuchagua mkoa wa Mara. Tuliamini huko pana mambo mengi sana ya kuandika.

    Lakini kabla sijaingia kazini nikajipenyeza na kwenda kumsalimia mjomba wangu katika kijiji kimoja kiitwacho Nyarukongo mkoani humo!!



    Ndani ya gari nilikuwa nimepakata begi langu huku ile bangili ikiwa mkononi mwangu.

    Awali niliwaza kuivua lakini nikajionya…

    Asiyesikia la mkuu……

    Basi nikaachana nayo!!

    Baada ya kuyatoa mawazo yangu katika lile bangili nikawa nafikiria juu ya makala ipi ambayo nitafanya na ikaleta changamoto hasahasa katika suala zima la mapenzi maana kipindi changu kilikuwa kikihusiana na mambo ya mapenzi.

    Kichwa kiliniuma sana na kisha nikahisi sijaenda mkoa sahihi, kama ningeyataka mapenzi ni heri kwenda Tanga!

    Sasa nilikuwa Mara!!

    Mawazo yangu yalikoma tena baada ya gari kusimama, kondakta akatuomba wanaume tushuke tusaidiane kusukuma.

    Kero nisizozipenda sasa!!! Nilighafirika.

    Lakini nililazimika kushuka.

    Katika kubanana mlangoni wakati wa kushuka kuna harufu niliihisi katika pua zangu ambayo nilikuwa naifahamu kabisa.

    Watafiti wa mambo ya kisayansi wanasema , kila mwanadamu hapa duniani ana harufu yake ya kipekee kabisa kasoro mapacha tu!! Hawa ndo wanafanana harufu!

    Naam! Kuna harufu niliifananisha, lakini kutambua ni nani anayenuka vile likawa tatizo. Nikafikiria zaidi ile harufu kama niliinusa Dar ama mkoa gani, jibu likachelewa sana kufika. Nikafikiri zaidi ubongo nao haukuwa na hiyana ukanipatia jibu!!

    Ilikuwa harufu ya jitu!!

    Mungu wangu!! Kidogo niangushe begi langu lenye vifaa vya kazini.

    Nikatazama ile bangili ilikuwa bado mkononi mwangu.

    Nini hiki kinanitokea sasa? Nilijiuliza.

    Inamaana jitu lipo katika basi ambalo nimepanda mimi?

    Hofu kuu ikatawala!CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Nilikuwa nasukuma gari huku nikimtazama kila mtu usoni kwa kuibiaibia huenda nitaiona sura ya jitu. Lakini sikuiona, watu walikuwa wamevaa nadhifu kasoro kondakta tu ambaye alikuwa amevaa nguo iliyochafuliwa na oili na uchafu mwingine kutokana na kuifanyia gari huduma.

    Gari likavuka kutoka katika lile tope.

    Tukarejea tena garini, nikaufuata msululu na kuingia garini.

    Kwa mara nyingine ile harufu ikanitoa mashaka ili nisijidanganye kwamba huenda pua zangu zilinusa vibaya.

    Nikainusa tena harufu ya jitu!

    Lakini sura ama walau mtu wa kufanania na jitu sikumuona.

    Zile imani za mjomba kuwa sikuandaliwa kabla ya safari nikaanza kuamini kuwa ni kweli tupu.

    Safari iliendelea bila matatizo, nilisubiri sana jitu athubutu kunigusa nipige kelele lakini sikuguswa na mtu yeyote yule, kila mtu aliendelea na shughuli zake.

    Hali ile ilinishangaza sana!

    Bora jitu angejionyesha hadharani kuliko kujificha na ninabaki kuinusa tu harufu yake.

    Hadi mwisho wa safari yetu hakuna kitu kibaya kilichonitokea.

    Ule mwangwi kuwa atanitafuta uliendelea kunisulubu.

    Nimemkosea nini kwani? Nilijiuliza.

    Au na hizi zilikuwa hisia zangu tu!!

    Nilijiuliza kabla ya kuungana na wenzangu hotelini.

    Nikawakuta wakiwa wanahariri makala zao kadhaa walizofanikiwa kuzipata.

    Mimi sikuwa na makala yoyote bado, ila hilo halikunisumbua kichwa! Muda tuliokuwa tumepewa wa mwezi mzima nje ya ofisi niliamini tu nitautumia vyema.

    Siku ya pili tukiwa tunapata kifungua kinywa, siku ambayo nilikuwa nimejipanga kuanza rasmi kusaka makala za kusisimua. Mezani nilipokuwa mara alifika muhudumu akiwa na bahasha, akamgusa begani mmoja kati ya wanahabari wenzangu. Kisha akampatia na kumweleza kuwa bahasha ile ililetwa mapokezi kwa ajili ya mmoja kati yetu. Kwa sababu yeye ndiye alikuwa mwenyekiti wa msafara aliipokea kisha akaifungua na kusoma palepale.

    “Duuh! Mwandiko huu ni zaidi ya daktari…”aliguna na kusema. Mimi nilikuwa nimejikita katika kunywa chai.

    “Natamani kufanyiwa kipindi cha redio au ataKama ni kwenye ViDEO, Hiro ndilo rengo langu hasaa naitwa JoSIA MWinYI. ASaNte”

    Kiongozi wa msafara akaisoma kama ilivyokuwa. Kwa pamoja tukajikuta tunacheka! Na hapo kila mmoja akatamani kuiona barua. Mimi sikuishika niliishia kuangalia tu…

    Mkuu wa msafara akaihifadhi katika pochi yake. Kisha akamuita yule muhudumu na kumuuliza huyo mtu hajaacha namba za simu wanampataje sasa ikiwa wamekubali ama wamekataa ombi?

    Älisema atakuja kati ya kesho ama keshokutwa.

    Mkuu wa msafara akacheka na kupuuzia!! Akaiacha ile barua katika pochi yake.

    Hakuna hata mmoja kati yetu aliyejua lijalo!!

    Laiti kama tungelijua!!

    Ama! Ya Mungu mengi kwakweli!!

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog