Simulizi : Ulaaniwe
Sehemu Ya Tano (5)
Nyumba ilikuwa kimya sana.
Tukamkuta mlinzi akiwa amesinzia, akakurupuka baada ya kushtuliwa.
“Suzi yupo?” nilimuuliza.
“Hapana ametoka lakini aliacha maagizo ikiwa utakuja nikupatie makaratasi yake uyapeleke kwenye lile shindano sijui la uandishi wa hadithi….” Alizungumza huku akitoa bahasha kubwa!
Maaskari wakaniuliza juu ya hilo shindano la uandishi wa hadithi kama Suzi alikuwa mwandishi nikapinga. Wakaichukua ile bahasha!
Asalaale!! PAKAKUCHA!!!
Kauli ikatokea nyuma yetu!
“Hivi Jimmy utakuwa mpuuzi mpaka lini, mambo yako unafanya kitoto toto sana”
Sote kwa pamoja tukageuka, jicho langu likakutana na lile bisu lenye mpini wa aina yake. Na aliyekuwa pale hakuwa mwingine.
Alikuwa ni jitu!!
Maaskari wakafanya kosa kubwa kupita yote kati ya ambayo waliwahi kuyafanya!!
Hawakujua kuwa yule hakuwa mtu bali jitu!!!
Haukupatikana muda wa kurekebisha makosa yao!
ASKARI wakamuonya Japhet kuwa asimame palepale na kutua kisu chake chini. Kisha anyanyue mikono yake juu la si hiovyo watamfyatua risasi.
Moyoni nilitabasamu na kuamini kuwa hatimaye Japhet alikuwa amekamatika kwa sababu askari mmoja tayari alikuwa ameipakata kiganjani bastola yake tayari kwa shambulizi.
Niliamini kuwa ‘jitu’hakuwa na namna nyingine ya kujitetea.
Lakini wakati anakishusha kisu chake chini alifanya kitendo ambacho hata siwezi kukusimulia ukaelewa lakini tambua kuwa hakikuwa kitendo kilichotarajiwa na mtu yeyote kati yetu.
Ninachoweka kukusimulia ni kwamba, katika sekunde ya kwanza askari aliyeshika bunduki alipiga yowe na kuachia bunguki yake kisha sekunde iliyofuata Japhet Sudi ‘jitu’alikuwa amemtia kabali kali kabisa yule askari ambaye bado alikuwa wima!!CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Na hapo nikashuhudia damu zikivuja kutoka katika paja la yule askari.
“Dah! Hebu ngoja tuone kama kweli ni dakika tano kama walivyosema…”hatimaye Japhet alizungumza huku akinitazama usoni, sikujua ni kitu gani anamaanisha.
Zilipopita hizo dakika tano Japhet akaanza kucheka sana kisha akaendelea kuzungumza nami kama kwamba mimi ni rafiki yake na tunashirikia katika mpango huo.
“Yaani Jimmy, nilipouziwa hiki kisu waliniambia hii sumu inachukua dakika si zaidi ya tano kuondoa uhai wa mwanadamu, aisee hata dakika tatu hazijapita jamaa keshakuwa mzoga.
Sasa hawa ulikuja nao huku kufanya nini Jimmy…” ahanitupia swali.
Nilitamani kukimbia lakini si mimi tu hata yule mlinzi wote tulikuwa tumepagawa na utaanza vipi kumkimbia mtu ambaye ndani ya sekunde mbili tu ameweza kukabilia na watu wawili tena mmoja akipoteza uhai na mwingine akiwa akigumia katika kabali matata.
Hakika ilikuwa ngumu sana.
Nikatulia nisiwe na cha kujibu.
“Jimmy..”akaniita.
“Eeh!” nikaitika kama bwege.
Ghafla akamwachia yule askari na hapohapo nikapokea kibao kikali usoni.
“Pumbavu wewe mimi sijakuita halafu unaitika….”alinikaripia. nikashangaa yaani huyu jamaa ananiita yeye mwenyewe halafu hapohapo anakana kuwa hajaniita kisha ananipiga.
Askari aliyeachiwa kutoka kwenye ile kabali alikuwa akikohoa kwa fujo huku akisaka hewa kwa nguvu.
“Liangalie jamaa lako, yaani basi we ukaona umekuja na bonge moja la steringi kwenye muvi eeh! Haya mwangalie steringi wako, we Jimmy umewahi kuwasikia waasi wa nchi ya Kongo.?”aliniuliza. nikaogopa kujibu huenda angeweza kunichabanga kibao tena.
“Waasi hawana utu hata kidogo, nimeishi na watu wasiokuwa na utu. Muasi anaweza kukuua hata kama ni rafiki yake kiasi gani, lakini si bora basi muasi hata jina lenyewe tu linatisha, vipi kuhusu mwanamke. Mwanamke ni jina jema sana mama yangu na mama yako wote si ni wanawake. Lakini mwanamke wa kuja kukuua moyo wako na kukupa mateso makali nje na ndani ya mwili ni zaidi ya muasi.
Jimmy unashangaa kuniona nikiwa na afya njema sana rafiki yangu!! Mimi sina afya na ni mtu wa kufa tu, lakini naona nimepewa uhai na siku hizi za kuishi ilimradi tu nifanye kitu ambacho moyo wangu unataka na sitaki ushauri wowote ule katika hili. Au wewe unaona nakosea kufanya hivi, hebu tuzungumze kirafiki na unishauri kama rafiki yako tu sahau kuhusu Joan na huyu steringi wako aliyekufa…”
Dah! Nilipagawa ndugu msomaji, mtu amesema hataki ushauri wowote hapohapo ananiomba mimi nimshauri, ama kwa hakika sikuwa nazungumza na mtu mwenye timamu zake.
“Haya basi tufanye kuwa wewe ni mimi. Yaani wewe Jimmy uwe Japhet. Ni miaka kadhaa nyuma sasa, ushakubaliana na hali kuwa Maria hakutaki tena na ataolewa na mtu mwingine, ukaamua kuendelea na maisha yako ukamsahau Maria.
Lakini kumbe huyo Maria bado anafuatilia maisha yako, kila unachokigusa anaingiza mkono wake ili kukuharibia kisa tu hataki yule bwana yake apate fursa ya kuonana na wewe. Unaamua kuwa mzoa taka unashangaa unaitwa mwizi, unaamua kuokota chupa tupu za maji ukauze unakumbwa na kesi ya ubakaji ghafla, unafungwa miaka miwilki hapoo gereza gani hilo, hilo mbele ya Kinyerezi. Yah! Segerea! Unafungwa Segerea, kesi hauielewi mara ubakaji mara sijui kitu gani na hapo mama yako amekufa tayari huna wa kukutetea.
Huko gerezani Jimmy wanatokea wanaume , nikisema wanaume si unanielewa Jimmy acha hivi vivulana ulivyovileta hapa na kujifanya ndo mastering kwenye muvi. Wanaume hao wanakulazimisha eti uwe mke wao, Jimmy yaani hili sakata lingekukuta wewe ungekuwa umeolewa sasa hivi na unaishi vizuri tu na mumeo kwenye ndoa yenu.
Nikapambana Jimmy, ule ukakamavu wa kijijini ukanifanya niepuke mtego huu. Askari mmoja akatokea kuwa rafiki yangu na mwishowe akanieleza kuwa kuna shetani anaitwa Marian ameamua kunipoteza kwenye uso wa dunia.
Jimmy nililia kama mtoto nakwambia, kwa hiyo Maria alikuwa tayari mimi niolewe si ndo maana yake sasa. Alitaka niolewe kabisa niwe mwanamke.
Jimmy, hadi hapa ninapozungumza na wewe silijui umbo la Maria akiwa uchi wa mnyama, sijui lolote kuhusu yeye sasa kwanini anifanyie vile.
Au kisa alikuwa na pesa na ana mwanaume mwenye pesa.!!
Lakini mimi hata wazo la kumuharibia mahusiano yake sikuwa nalo kabisa.
Ile picha niliyokutumia ile hapo nilikuwa nimetoka gerezani sasa.
Nilipotoka nikagundulika sasa kwa mara ya kwanza kuwa nilikuwa nimeathirika na virusi vya UKIMWI.” Japhet akakoma kusimulia hapa, akainama chini na kujifuta machozi!!
Japhet alikuwa analia, kilio cha mtu mzima!!
Ajabu sasa yule askari aliyenusurika kufa kwa kupigwa kabali, mlinzi pamoja na mimi wote tulikuwa tunasikiliza simulizi hii ya kusikitisha na kutia hasira.
“Jimmy sasa hapa sielewi ilikuwaje yaani hadi sasa hivi, maana kabla ya kwenda jela kiukweli Maria aliponitenda nilifanya ngono kama starehe, leo navuta msichana huyu kesho yule. Akinikinai namwacha kwa dharau nachukua mwingine. Si unajmua nilikuwa na pesa zile ambazo nilipata baada ya kulipwa na serikali kuna nyumba yetu ilipitiwa na barabara!!
Ilibidi tu iwe ngono na si kitu kingine, maana sinywi pombe mimi yaani unavyoniona hapa nadhani nitapewa tuzo siku ya mwisho. Mh! Hivi ni Tuzo ama Tunzo maana hili neno linanivuruga kweli?”
“Ni tunzo lakini hata tuzo ni sawa tu!!” nilimjibu huku nikiwa natetemeka.
“We mwehu nini..” akanibadilikia.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Yaani hii ni tunzo nah ii tuzo unasema zote sawa. Elimu yako inakusaidia nini Jimmy, au nd’o unaishia kufikiri kuwa yupo mwanadamu wa kuweza kukusaidia katika kuulinda uhai wako. Akili yako inaishia hapa pa kutembea na masteringi.
Sikiliza kaka Jimmy, hayupo mwanmadamu wa kuutoa uhai wake kwa ajili ya mtu mwingine labda iwe katika filamu mbovu. Nilipokuwa huko Ndola Zambia katika kambi ya hao waasi niliokwambia…. (nikashangaa waasi gani hao alioniambia)… sasa huko kuna jamaa mmoja alikuwa ni mlinzi wa raisi. We! Siku moja ikapigwa risasi likiwa shambulizi la kumuua raisi aisee si unajua hawa mabodigadi eti raisi akipigwa risasi inabidi wewe nd’o ujirushe ufe. Jamaa yeye akakimbia tena mbio kali sana.
“ Jitu akakoma na kutokwa na kile kicheko chake cha dhihaka!!
“….sasa wewe unakuja na hivi vijamaa hata mafunzo ya ukomandoo havijui. Unataka wautetee uhai wako. Kuwa mwanaume Jimmy simama wewe kama wewe. Mimi ni mwanaume Jimmy, nilipambana jela na sikufanywa mwanamke, mimi ni mwanaume sana tu lakini udhaifu mmoja tu ambao nimeshindwa kabisa kukabiliana nao, siwezi kusamehe Jimmy. Siwezi kumsamehe Maria pamoja na kizazi chake ukiwemo ukoo wako Jimmy yaani nitawatesa sana. Mpaka nilaaniwe ndo ntaacha. Halafu nilisimulia pale tukio la gerezani halafu ghafla nikahamia tukio la kule kambi ya waasi halafu ghafla tena nikahamia kwa yule mlinzi wa raisi. Hivi huo mtindo unaitwaje maana kuna kipengelea kwenye ile simulizi ninayoandika nimetumia mtindo huo lakini siujui jina lake.. unaitwaje kwani?” akanitupia swali lile.
Nikababaika kidogo katika kumjibu. Nilihisi lugha yangu inaweza kumchanganya kiasi fulani.
“Huo ni mtindo rukia….” Nilimjibu!!
“Hapo kidogo umenikosha Jimmy, kwa hiyo kuna ule mtindo wa moja kwa moja, mtindo rejea na huo ni mtindo rukia.” Akanisifu kisha akacheka kidogo.
“Halafu sijakwambia… lakini hapa hapafai mimi kukweleza mambo yangu juu ya ile simulizi. Hawa jamaa hawatakiwi kusikiliza kabisa. Wapi patafaa kwa ajili ya mazungumzo kama saa moja hivi ama lisaa na nusu!!” aliniuliza kana kwamba hakuna maiti pembeni yetu, yaani ni kama tupo mtaani tu.
“Chukua hiyo bahasha twende zetu!” akanionyesha ile bahasha iliyokuwa chini, bahasha ambayo alikuwa amempa mlinzi atukabidhi.
Nikaiokota huku natetemeka.
“Wewe kuruta!! Kamsaalimie afande Rajabu wa kule Chang’ombe mwambie Sululu Jembe anamsalimia. Ukimwambia hivyo tu atanikumbuka. We mlinzi kazi nd’o hauna tena nisamehe bure.” Akanishika mkono tukaanza kuondoka.
Mara sauti ikakaripia!!
“Mpo chini ya ulinzi nafyatua vichwa vyenu mkipiga japo hatua moja mbele.” Ilikuwa sauti ya yule askari.
“Dah! Sasa afande Rajabu nani atamfikishia salamu zangu, au kama vipi nitakuagiza wewe si itakuwa sawa pia.” Japhet alinieleza pasi na chembe ya wasiwasi. Kisha hapohapo akageuka na kumwendea yule askari.
Ebwana wee! Askari alikuwa haamini macho yake wakati Japhet anamrushia usoni risasi zote zilizokuwa katika ile bunduki.”
“Yaani wewe kuficha hako kabunduki kwenyea gwanda ukadhani sitaiona, sikia wewe lofa watu tumeficha bunduki hadi katika nyama za paja nab ado kuna wahuni wakagundua. Ulishawahi kumeza bunduki wewe?” akamuuliza na hapo akawa amemfikia.
Japhet akanionyesha kitukisichotoka katika akili yangu hadi leo hii!
Akanionyesaha kuwa yeye ni zaidi ya mnyama.
Kwanza aliikata sikio ya yule askari, akainyonya damu kisha akaitema.
“Hili ni sikio lako dogo, kule kongo nyama za watu kwetu chakula.”
Kisha akaushika mkono wake na kuukunja katika namna isiyotakikana, hadi ukatoka mlio ‘ka!’ mkono ukakatika, nasisitiza haukuvunjika mkono ule. Ulikatika.
Askari akapoteza fahamu!!
Jitu akaendelea kutumia kisu chake!!
Ni kama alikuwa akimchuna mbuzi tu kikawaida!!
Dakika chache zilitosha kumpoteza kabisa duniani!
Japhet hakuwa mtu wa kawaida. Nilikiri hilo jambo huku nikijiuliza, ilikuwaje hadi akawa hivi.
Akamaliza pale na kunishika mkono, tukatoweka eneo lile huku tukiwa njiani akaanza kunisimulia juu ya ile hadithi yake ilivyokuwa inaendelea!!
Nilichanganyikiwa, alikuwa amefika mbali sana!!
Mipango yake haikuwa ya kawaida!!
#Naam! Ni JITU na JIMMY!!!.....
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
MWISHO
0 comments:
Post a Comment