Search This Blog

Tuesday, 14 June 2022

ULAANIWE - 4

 





    Simulizi : Ulaaniwe

    Sehemu Ya Nne(4)



    ILIPOISHIA!!



    Jimmy ametumiwa barua pepe na Japhet Sudi, barua hii ina utata ndani yake. Japhet anasisitiza kuwa ana kisasi na ukoo wa Jimmy…….

    Jimmy hajui lolote!!! Na masaa yanazidi kukatika!!!



    ENDELEA!!



    Zile siku zetu tatu za ahadi zipo palepale, utaamua mwenyewe sasa kwenda kuangalia maiti ya huyo hawara yako, ama kujitahidi hasira yangu isijekuwa juu ya ukoo wenu.

    Nakukumbusha kuwa iwapo Maria hatalaaniwa, basi nitamsaidia mtoa laana kulaani. Nitamlaani Maria na kizazi chake!!

    Nimemaliza kuandika nitoe kasoro!!

    Kwaheri!!



    Nilitetemeka, kama umewahi kutetemeka hutaniuliza kitu. Utaona ni jambo la kawaida!!

    Lakini nikusisitize kuwa nilitetemeka na kisha kupitiwa na haja ndogo bila kujua.

    Nilijikojolea!!

    Ama nilikuwa nimesoma simulizi za kutisha na kuangalia filamu za kutisha mno lakini ile barua ilikuwa inatisha kupita maelezo na mbaya zaidi ilikuwa ina harufu!!

    Harufu ya kifo!!



    Nilifadhaika sana baada ya kugundua kuwa nilikuwa nimejikojolea pale nilipokuwa. Lakini sikukumbuka kujilaumu.

    Sasa ulikuwa wakati wa kutafuta mtu wa kumpunguzia limbikizo lile la mawazo.”

    Nikaukumbuka mstari huu wa kusisitiza!!

    “Zile siku zetu tatu za ahadi zipo palepale, utaamua mwenyewe sasa kwenda kuangalia maiti ya huyo hawara yako, ama kujitahidi hasira yangu isijekuwa juu ya ukoo wenu.”

    Nikanyanyua simu yangu na kumpigia kaka yangu ambaye aliongoza msafara wa kunitania kuwa nimechezewa akili na mtu mjinga hapo mjini na mimi nimetetereka.

    Aliyepokea saimu alikuwa mkewe, hata sikukumbuka kumsalimia. Nikaomba kuongea na mumewe akasema yupo bafuni nikamlazimisha aipeleke simu bafuni.

    Alitoa mguno wa kushangaa lakini nilimfokea sasa na kumwamuru!!

    Ama! Nilikuwa nimepagawa maana sekunde zilizidi kwenda mbele na kumaanisha kuwa ule muda wa ahadi ulikuwa unakaribia.

    Baada ya dakika moja nikaisikia sauti ya kaka yangu upande wa pili.

    “We Jimmy.. mambo gani haya sasa inamaana hau…”

    “Kaka ndio sikuweza kusubiri hata sekunde moja...”

    “Üsinambie kuwa ni habari za jitu…” akasema kisha nikamsikia mkewe akicheka kisha kaka naye akacheka.

    “Bro.. si masihara tena ujue si masihara hata kidogo, Japhet Sudi hana masihara…”

    “Japhet Sudi ndó nani” bakaniuliza.

    “Ndó huyo jitu bro… ndo jitu mwenyewe. Kaka mmemfanyaje Japhe eeh! Mmemfanya nini nataka majibu sasa hivi maana bado dakika chache tu… nataka majibu” nilimlazimisha kaka.

    Kimya kikatanda nikatambua kuwa alikuwa katika mshangao.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Dogo umeanza kuvutia bangi ukubwani au?” aliniuliza swali ambalo lilinikera. Nikajikuta natokwa na tusi zito la nguoni.

    Sikuwahi kumtukana kaka yangu hata siku moja, hii ikawa mara ya kwanza.

    Palepale simu ikakatwa na nilipojaribu kupiga simu haikupokelewa. Nilituma ujumbe mfupi, si kwa ajili ya kumwomba msamaha bali kwa ajili ya kumsisitiza awe makini kwa sababu Japhet hana masihara.

    Usiku huohuo nikapokea simu kutoka kwa baba yangu. Alinikaripia sana kisha kunisihi siku inayofuata nifunge safari kwenda Moshi kijijini.

    Nilitambua kuwa kaka yangu alikuwa amenishtakia tayari. Lakini ule haukuwa muda wa kujitetea, nikamuuliza mzee kama alikuwa anamfahamu Japhet Sudi.

    Akanitukana kikabila na kuniambia kuwa nisipoenda kesho yake atanilaani yeye akishirikiana na kaburi la marehemu mama yangu.

    Doh! Nilipagawa kusikia lile neno laana, na hapo nikakumbuka kuwa Japhet Sudi ‘jitu’naye aliapa kunilaani mimi na ukoo wangu ikiwa sitaitafuta suluhu kabla ya siku tatu ambazo sasa zilikuwa zimesalia kwenye masaa tu!!

    Iwapo sitalaaniwa na mzee Elkael Sumo basi laana ya Jitu ilikuwa inanihusu, kitu kibaya ni kwamba hakuna aliyetaka kuniamini.

    Wakaishi na imani yao kuwa nilikuwa nimeanza kuvuta bangi.

    Nikiwa katika mawazo yale mara simu yangu ikaita. Alikuwa ni dada yangu, huyu tulikuwa tunaelewana sana tangu utotoni. Nikajifariji kuwa walau nimepata mtu wa kumfikishia ujumbe naye akanielewa vyema na kuwashawishi hao wasiotaka kunisikiliza hasahasa kaka yangu ambaye tangu kukua kwetu alikuwa na tabia za kitemi. Kisa tu ni kaka.

    Nikapokea simu!!

    “Jimmy, Jimmy mdogo wangu. Yaani unamtukana Martin kweli, unamjibu baba Jimmy, yaani siamini… Jimmy nini kimekuvuruga mdogo wangu. Maana kabla ya kukupigia wewe nimejaribu kuzungumza na Joan ili anieleze una matatizo gani. Simu yake naye haipatikani, ni nani amekuudhi kwani…” alinihoji kwa upole.

    Ile kutaja jina Joan akawa amenikumbusha ule ulimi ofisini, ulimi ambao kwa namna moja ama nyingine ulikuwa wa Joan. Marehemu Joan!

    “Dada, nilikueleza juu ya jitu… na hapo umemtaja Joan naomba usiku huu huu wafikishie taarifa ndugu zetu wote waambie jitu limeung’oa ulimi wa Joan na limemuulia mbali.

    Jitu lina kisasi na ukoo wetu na sijui ni kisasi gani. Dada wewe ndiye pekee unayeweza kunielewa nikizungumza katika utulivu huu. Sijachanganyikiwa ila nimepagawa, dada kuna jambo baya sana linakuja nyuma yetu. Na lipo hatua chache sana liweze kutufikia.

    Tusipokuwa makini na kuendelea kuamini kuwa Jimmy kachanganyikiwa. Tutalia na kusaga meno.

    Japhet Sudi ni nani dada?” mwishowe nilimuuliza.

    “Joan amefanya nini umesema? Joan ameuwawa….” Alianza kulia dada yangu na baada ya hapo hapakuwqa na mazunghumzo tena.

    Hakuna siku ambayo simu yangu ilikuwa ‘bize’kama siku hiyo.

    Ni dakika tano tu baada ya kuzungumza na dada yangu. Sasa simu zikaanza kuingia kwa fujo, mara kaka Martin, ikikatika inaingia ya mkewe, mara baba yangu, mara wajomba, mara mashemeji…. Nikashindwa kupata uchaguzi.

    Na hapo yalikuwa yamebaki masaa manne tu ili siku tatu ziweze kutimia baada ya ujumbe ule kutumwa katika anuani yangu ya barua pepe.

    Zile nyimbo za parapanda italia parapanda zikaanza kujirudia masikioni mwangu!!!

    Nilipoona sina uuchaguzi wa simu gani nipokee, nikaamua kuizima kabisa maana simu zile zilikuwa zinanipotezea muda kwa sababu sikuwa na maamuzi ya nini nifanye.

    Nikaamua kuzima kabisa!!

    Baada ya kuzima simu ile nikaiendea simu ya mezani na kumpigia rafiki yangu ambaye alikuwepo katika kisanga cha mzigo wa damu ofisini, nikamuuliza iwapo anaweza kumtambua mtu aliyeleta mzigo ule.

    Akamuelezea muonekano wake.

    Ajabu akasema ni mwanaume mwenye afya yake nzuri tu, na pia ni nadhifu sema anakosa kitu kimoja tu.

    Hana tabasamu hata kidogo!!!

    Na hapo nikaamua kuingia katika anuani yangu ya barua pepe ili walau nimsihi jitu anisamehe mimi na ukoo wangu japokuwa sikuwa najua lolote ambalo nimemkosea. Pia nikapanga kuichukua ile picha aliyonitumia akiwa amekondea ili niweze kufananisha na muonekano alionielezea yule bwana!!!

    Nilipofungua nikakutana na ujumbe wake. Tatizo moja tu alikuwa akitumia anuani mpya kila siku.

    Ilikuwa kama ile ya awali japokuwa hii haikuwa na salamu za utangulizi.



    IKASOMEKA!!



    Nipo safarini Jimmy na sikuona kama ni vibaya nikiendelea kujifunza kuandika, maana wanasema juhudi huongeza maarifa.

    Jimmy, natambua riwaya zangu hazitasomwa sana… ooh! Bado sijajua kama ni riwaya katika mfumo huu. Tafadhali utanijibu kama huu mfumo natumia ni wa riwaya kweli ama ninakosea.

    Ni usiku Jimmy nawe umelala, lakini mimi ninasafiri. Nasafiri huku naandika, naandika kwa sababu sina namna nyingine ya kuuliwaza moyo wangu zaidi ya haya maandishi.

    Nina hasira sana Jimmy, hasira ambayo kuua kwangu ni jambo la kawaida tu. Na hasira hizi zote amezisababisha Mungu!!

    Hah! Unashangaa, amezisababisha yeye, yaani mimi nilimuomba mke mwema akanipatia Maria. Nikamuamini kupita maelezo Jmmy sikuwahi kumsaliti msichana yule hata siku moja. Natamani siku zirudi nyuma walau uingie katika kile chumba changu kule kijijini kwa mwalimu Mathias. Chumba changu kilijaa picha za Maria kila kona, si kwamba alikuwa mrembo sana lakini niliamua kumuamini tu. Kwani urembo wa m,sichana ungenifikisha wapi mimi Jimmy. Sikumpima kwa urembo bali nikamkubali kwa sababu alikuwa mwema kwangu.

    Sasa alipoingia huko Dar kwenu sijui aliingiliwa na mdudu gani, halafu sasa Mungu hakuniambia kuwa Maria ameharibika tayari akaniacha tu, akaniacha niendelee kumuamini yule shetani. Haya hayo yote nikavumilia, nikamuomba basi Mungu anisaidie kumwaibisha Maria.. nikaishia kuabika mimi mjini. Nimelala kituo cha basi Jimmy, nimekula majalalani mimi, nimeteseka sana Jimmy. Halafu mimi niliyetendwa nateseka ghafla nasiki yule Malaya amefaulu na serikali inaenda kumsomesha nje ya nchi… haya hapo nisimlaumu Mungu kweli au nimlaumu nani sasa.

    Halafu baadaye akaolewa!

    Nikamuomba tena Mungu amlaani walau ndoa yake iyumbeyumbe lakini bado ikawa imara, sasa namlaani mimi mwenyewe. Yeye na wote walioshiriki kuua moyo wangu na kunifanya niwe mpagani nisiyeamini lolote kuhusu mambo ya kiroho!!

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Jimmy laiti kama hili lingekuwa karatasi sidhani kama ungeweza kusoma walau neno moja kati ya haya, nalia Jimmy nalia kama mtoto mdogo. Kuna abiria mwenzangu hapa ni mwanamke ananiuliza eti kwa nini ninalia, we ngoja nikimaliza kuandika hapa nitamjibu kwa vitendo mwanaharamu mkubwa huyu.

    Anajifanya kununua tuma tunda gani sijui ananipa mara ananunua keki ananipa, shenzi kabisa!! Mpumbavu huyu.

    Jimmy kabla ya kukichapisha kitabu changu naomba uondoe sehemu zenye lugha kali za matusi, nayaandika haya huyku nikiwa mwenye hasira kali.

    Na kinachonisikitisha hii safari ninayoenda nitafika wakati muafaka kabisa. Yale masaa ya urafiki baina yangu mimi na wewe yatakuwa yamekwisha.

    Nitakuwa katika upande wangu wa maisha nawe utakuwa upande wako.

    Ujue Jimmy mfano hii ingekuwa filamu ingeuza sana, yaani wewe na mimi tulikuwa marafiki lakini ghafla tunakuwa maadui. Ona Joan keshakufa, hivi kama ingekuwa filamu Joan angefaa nani kucheza nafasi yake labda.

    Halafu kuna hao ninaoenda kuanza nao, yaani hawanijui kabisa kwa sura halafu hawajui kama mimi ni adui yao. Sasa naingia pale kama jambazi kuu nimevaa koti kubwa naanza na yule mwanamke nanyonga halafu mwanaume namuacha amzike mkewe kwanza. Baada ya hapo napotea tena naenda mkoa mwingine.

    Halafu hii vita mwisho kabisa Jimmy na Japhet Sudi, aisee itapendeza sana. Hapo ndo anapatikana steringi.

    Jimmy! Hii itauza sana niamini mimi.

    Halafu wabongo kwa uongo hawajambo yaani wakati nanunua hii kompyuta wakasema eti inatunza chaji masaa nane, sasa hivi hapa inasema bado dakika tano izime….

    Kama vipi ngoja niizime tu!

    Sema nashukuru sana japokuwa haunipi maksi zangu naamini nazidi kuwa bora katika uandishi.

    Ila naamini riwaya hii haitauza kabisa kwa sababu imeegemea upande wa wanawake!!

    Ngoja nikichaji kompyuta hii nitajaribu kuhamia upande wa pili!!!



    Ndugu msomaji, umewahi kuona kilio cha mtu mzima tena hadharani!

    Nililia, nililia kwa sauti ya juu sana, mbaya zaidi nani angenipooza.

    Nikawasha simu yangu na kuitazama nikaona zinaingia meseji nyingi sana kwa fujo. Nikajiuliza zitanisaidia nini nikisoma.

    Nikafikiria kwenda polisi nikatoe taarifa ile mara moja. Lakini jeshi letu nililitambua wazi kamwe wasingetilia maanani jambo lile.

    Nikafungua zile meseji nisome upesiupesi nione kama ipo hata moja ambayo inaweza kunipatia mwangaza.

    Tatu za kwanza zilikuwa zimejaa malalamiko kuwa sipokei simu na nimezima kabisa.

    Ule ujumbe wa nne ulikuwa umeandikwa kwa herufi kubwa.

    “JIMMY KAMA UPO KWAKO ONDOKA MARA MOJA ASKARI WANAKUJA KUKUKAMATA. USIJIBU MESEJI HII KAKA!!”

    Ujumbe huu ukanipagawisha zaidi, nikataka kutoka nje vilevile, nikausikia ubaridi katika suruali yangu.

    Nikakumbuka kuwa kumbe nilikuwa nimejikojolea!!!

    Sikujali kuhusu hilo nikataka kutoka vilevile.

    Na hapo nikausikia mlango wangu ukigongwa kwa nguvu sana!!!

    Ule ubaridi ukatoweka likawa joto tena.

    Nilikuwa najikojolea upya!!!





    Ile hodi ilinipagawisha hasahasa nilipofananisha na ule ujumbe ambao nilikuwa nimetumiwa. Ujumbe kuwa polisi walikuwa wananitafuta.

    Licha ya utu uzima wangu ule na hekaheka za hapa na pale za uandishi wangu nilikuwa muoga sana wa kupelekwa mahabusu.

    Si kwamba sikuwahi kupelekwa hapo kabla la! Nimewahi lakini sikukaa kwa muda mrefu nikaachwa huru.

    Nilikuwa nimekamatwa kimakosa!

    Hii ya wakati huu haikufanana na ile ya bahati mbaya, hakika nilikuwa matatani sana.

    Kuhusushwa na kifo cha Joan!!

    Nilishindwa kujibu ile hodi nikaanza kuhaha pale ndani nisijue nitajificha wapi.

    Ile hodi iliendelea kwa fujo sana na kunifanya nizidi kupagawa. Na mara ghafla ikakoma.

    Nikasikia hatua za mtu zikipotelea mbali na mlango haukuguswa tena.

    Niliufikia mlango na kuchungulia nje sikuona mtu yeyote.

    Mara simu yangu ikaita na kunishtua sana, sasa sikupuuzia tena kupokea nikapokea upesi upesi.

    Mpigaji alikuwa anacheka badala ya kuzungumza kitu chochote, nilimuuliza nini kinatokea hakujibu akaendelea kucheka.

    “Bastard!!” nilisema wakati nataka kukata simu. Kisha nikamsindikiza na tusi jingine zito.

    Kicheko chake kikakomea pale.

    “Heh! Jimmy na wewe naye unakuwa kama Maria ndugu yangu, unanitukana Bastard sijui na maneno gani hayo mengine. Hivi mnakuwaje wanadamu lakini, kwa hiyo umenufaika nini kunitukana labda ndugu yangu Jimmy!”

    Ilikuwa sauti ya Japhet Sudi! Jitu!! Na sikuwa nimekosea.

    “Japhet ni kitu gani unakitaka katika maisha yangu, tafadhali kama ni uhai wangu nitakuelekeza uje nyumbani kwangu uuchukue, Japhe sitaki kuishi maisha ya mashaka. Niambie nini unataka….” Nilimkaripia na nikajihisi kuwa simuogopi tena kiumbe yule.

    “Jimmy, umesema kama ni uhai nifanyeje?” akaniuliza kisha hakunipa nafasi ya kujibu chochote akaanza kucheka sana. Nikamvumilia hadi akamaliza kucheka kisha akaendelea.

    “Yaani nimekuja hapo muda si mrefu umehangaika wee chumbani kwako, sasa hivi wajifanya jasiri eti kama ni uhai nije niuchukue. Haya rudia kauli yako na nije hapo sasa hivi kuuchukua uhai wako ili uache kuishi kwa mashaka…. Rudia kauli yako mpuuzi wewe unayependa kutukana…”

    Kauli zile za Japhet zikanifanya moyo wangu upige tofauti na kawaida… nilitumbua macho haswa.

    Yaani Japhet alikuwa amefika nyumbani kwangu usiku ule. Akili ikanipa jawabu kuwa yule jamaa hakuwa mtu wa kawaida hata kidogo.

    “Jimmy! Hivi wewe ni mwandishi gani wewe, au haukusomea taaluma yako, yaani hata mimi niliyeamua kuisoma juu juu tu bila mwalimu natambua wazi kuwa fasihi simulizi katika upande wa hadithi ni kitu ambacho si cha ukweli moja kwa moja bali ni uongo unaofanana na ukweli unaofikishwa kwa jamii husika ili jamii ielimike, iburudike na kuliwazika. Sasa wewe mpumbavu nakueleza kuwa nipo garini ninaenda mkoani unaamini tu kibwegebwege. Utakuja kufa kipuuzi wewe. Mimi nipo hapa mjini bado kuna mambo nakamilisha kwa hayo masaa kadhaa ambayo yamebaki ili tuanze rasmi makubaliano yetu.

    Jimmy! Umenisikitisha sana, lala salama ndugu yangu wa dhati!!”

    Simu ikakatwa palepale na haikupatikana tena!!

    Sihitaji kuelezea namna ambavyo nilipagawa mpenzi msomaji. Nilijiona kama mtu ambaye shingo yangu ipo katika kitanzi cha kunyongewa na sina msaada wowote ule.

    Jitu lilikuwa linanitambua kuliko kawaida!!CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    *****

    KIJIJINI NYARUKONGO.

    Mjomba wangu bwana Thomas, mtu wa kwanza kabisa kumwelezea juu ya Jitu alikuwa katika harakati kubwa sana. Ukoo mzima ulikuwa unamtazama yeye. Ni yeye ndiye alionekana anaweza kutukomboa. Kasoro mimi tu nd’o sikuwa na imani naye hata chembe. Niliamini kuwa jitu ni kiumbe hatari sana ambaye hatabiriki wala hakabiriki.

    Naam! Ilikuwa kama nilivyoamini.

    Baada ya siku mbili kupita tangu zile siku tatu za ahadi kukatika. Hatimaye nilipokea ujumbe tena kutoka kwa jitu ambaye wakati huu alijitambulisha kama mwanafunzi anayejifunza kuandika hadithi za kusisimua na kutisha. Kwenye mabano akaandika simulizi za kutungwa!!

    Nikajiuliza kutungwa gani wakati anaandika mambo ambayo anayafanya!!

    Ujumbe wa wakati huu ulikuja katika namna ya kitofauti sana.

    Nilikuwa nimeacha mazoea kabisa ya kuendesha gari langu badala yake nilikuwa mtu wa kupanda daladala, niliamini kabisa kuwa kwa kujichanganya na watu naweza kusaidiwa hata nitakapokutana na jitu ana kwa ana tena. Lakini nikiwa katika gari langu binafsi uwezekano wa kukamatwa ulikuwa mkubwa sana kisha kuuwawa.

    Nilipofikiria juu ya kuuwawa nikaamini kuwa yale maneno yangu ya kumweleza jitu aje kuuchukua uhai wangu niliyasema ilimradi tu.

    Siku hii nikiwa natoka polisi kuandika maelezo juu ya tukio la kuuwawa kwa Joan. Nilipanda daladala kama kawaida yangu, nilikuwa namtazama kila mtu kwa makini sana ili nitambue iwapo nipo karibu na jitu ama la!

    Nikatambua kuwa hakuwepo mazingira yale!

    Nikapanda na kuketi katika kiti kimoja na kukiacha kiti kingine katika upweke, punde dada mmoja akakiondoa upweke kiti kile.

    Hakunisalimia! Akajikita katika mambo yake, alikuwa anatumia simu yake!

    Namimi sikuihitaji salama yake hata kidogo!

    Nilikuwa nawaza mambo yangu mengi zaidi.

    Vituo kadhaa mbele yule dada akashuka, aliposhuka kwenye kile kiti akahamia mwanaume mwingine mtu mzima sana. Hakuchukua muda akaanza kusinzia mara aniangukie nikawa nafanya kazi ya ziada kumweka sawa.

    Anajirekebisha kisha dakika inayofuata anarudia yaleyale.

    Hadi nafikia kituo changu alikuwa amenichosha haswa!

    Niliposhuka na yeye akashuka!!

    Akabaki pale kituoni wakati mimi naondoka zangu!!

    Nilipofika mbele nikasikia simu ikiita katika mfuko wa koti langu!!

    Mlio ule ulikuwa mpya sana masikioni mwangu.

    Nikaitoa simu ile na kuitazama, haikuwa ngeni sana machoni mwangu!

    Lakini ni wapi niliwahi kuiona.

    Nikaipokea huku nikibabaika kidogo, ile simu imeingia vipi katika mfuko wa koti langu.

    “Samahani naweza kuongea na dada Suzi….” Sauti ya kiume iliniuliza.

    “We nani?” nilimuuliza.

    “Rafiki yake kipenzi sana…. Kwani wewe nani yake..”

    “Na hii simu imekuwaje sasa mimi ninayo jamani eeh! Mbona mnanifanyia hivi lakini.” Nililalamika.

    “Alisema wewe nd’o ubaki na hiyo simu. Si unamjua lakini… sikia usinimalizie salio wewe kijana. Nenda nyumbani kwake ukamuulize hiyo simu alimpa nani sawa?” alifoka na nikaitambua sauti halisia ya Japhet Sudi.

    Ghafla nikaiachia ile simu ikaanguka chini.

    Nikamsikia Japhet akiendelea kuzungumza nikaiokota upesi na kumuuliza ni kitu gani amemfanyia dada yule.

    “Sijamfanyia jambo lolote, ila mwambie kuwa uchungu wa mapenzi haufananishwi na uchungu wa kitu chochote kile. Sawa watu wanasema uchungu wa kufiwa na mtu umpendaye inauma sana lakini kwani ni nani hajui kuwa wewe Jimmy ipo siku utakufa, nani hajui kama mimi nitakufa pia. Lakini je kuna ambaye anazaliwa ili aumizwe katika mapenzi. Kamuulize huyo Suzi ni fahari gani aliipata kwa kumlaghai Maria wangu akamtafutia mabwana akamwambia eti hana hadhi ya kuwa na mimi.

    Niliumia sana Jimmy wakati huyu Malaya ananicheka, nazikumbuka sura nyingi sana lakini ya huyo dada Suzi sitaisahau kamwe.

    Nd’o maana nakutuma umweleze kuwa achezee vitu vyote lakini sio mapenzi.

    Sijui tu hata nikuelezeje Jimmy ujue kuwa naumia sana.

    Yaani mama yangu mzazi akafa kipuuzi tu kisa hawa Malaya wawili. Nasikia walimpigia simu na kumweleza kuwa nimerukwa na akili na nipo mjini nazurura. Mama yangu mjomba wako mzee Mathias anamjua vyema. Nikikosea matumizi ya nyakati usisahau kunikumbusha ndugu mwandishi.

    Mama yangu alikuwa na matatizo ya moyo, akafa!

    Kisa uongo wa hawa mabinti ambao walijiona wao ni wa mjini sana, eti leo hii Malaya waolewe halafu mimi nipo tu nachekelea. Hapana Jimmy hata ungekuwa wewe, mbaya zaidi nimewaombea laana na hata hawajalaaniwa badala yake wamebarikiwa.

    Hebu Jimmy naomba na mimi uniombee laana naweza nikabarikiwa.

    Mimi ni shetani Jimmy, ninavyozungumza na wewe hapa mimi ni mtu mbaya kupindukia!

    Ukoo wako sikutaka kuugusa hata kidogo, mmenichokoza na uzuri ni kwamba zile siku za ahadi zimekwisha na hakuna lolote ulilofanya zaidi ya kujifungia ndani na kulialia kama mtoto wa kike.

    Salio linaniishia Jimmy!!CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Kumbuka kumpelekea dada Suzi simu yake!

    Na umsalimie sana!!

    Simu ikakatwa!

    Sasa sikutaka kuendelea mbele zaidi, nikatimua mbio kumsaka yule mzee ambaye alikuwa ananibughudhi kwenye daladala, mashaka yangu yote yalikuwa kwake kuwa ndiye muhusika.

    Nilimsaka kila kona nab ado sikufanikiwa kuambulia kitu chochote.

    Nikaamua kwenda polisi ili tuongozane kwenda kwa dada Suzi maana niliamini kabisa kuwa hapatakuwa na amani nyumbani kwa dada yule ambaye alikuwa mtoto wa baba yangu mkubwa!!

    Nilitamani sana tumkute akiwa hai ilimradi tu nimfahamu huyo Maria na kutambua ni kitu gani kibaya alimfanyia Japhet maana alikuwa amenieleza mengi sana lakini bado sikuwa nimepata jambo kubwa sana hadi kumfanya aanze kuua!!

    Nilifika kituo cha polisi na ile simu mkononi, nikatoa taarifa nikapewa askari wawili tukaandamana nao hadi nyumbani kwa dada Suzi.

    Nyumba ilikuwa kimya sana.

    Tukamkuta mlinzi akiwa amesinzia, akakurupuka baada ya kushtuliwa.

    “Suzi yupo?” nilimuuliza.

    “Hapana ametoka lakini aliacha maagizo ikiwa utakuja nikupatie makaratasi yake uyapeleke kwenye lile shindano sijui la uandishi wa hadithi….” Alizungumza huku akitoa bahasha kubwa!

    Maaskari wakaniuliza juu ya hilo shindano la uandishi wa hadithi kama Suzi alikuwa mwandishi nikapinga. Wakaichukua ile bahasha!

    Asalaale!! PAKAKUCHA!!!

    Kauli ikatokea nyuma yetu!

    “Hivi Jimmy utakuwa mpuuzi mpaka lini, mambo yako unafanya kitoto toto sana”

    Sote kwa pamoja tukageuka, jicho langu likakutana na lile bisu lenye mpini wa aina yake. Na aliyekuwa pale hakuwa mwingine.

    Alikuwa ni jitu!!

    Maaskari wakafanya kosa kubwa kupita yote kati ya ambayo waliwahi kuyafanya!!

    Hawakujua kuwa yule hakuwa mtu bali jitu!!!

    Haukupatikana muda wa kurekebisha makosa yao!

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog