Search This Blog

Tuesday, 14 June 2022

ULAANIWE - 3

 





    Simulizi : Ulaaniwe

    Sehemu Ya Tatu (3)



    “…. Sasa ninakaribia kuwa na furaha bwana Jimmy, furaha niliyoitafuta miaka kadhaa… kabla hujaendelea kusikiliza umepata nafasi ya kuangalia picha zangu nilizotuma. Kama bado tazama kisha uje hapa tena upoteze muda wako kunisikiliza rafiki yangu!!”

    Niliendelea kusikiliza na kukuta ujumbe mwingine juu, nikaufungua na kukutana na picha za mwanaume akiwa amekonda sana, nyingine akiwa kitandani na nyingine akiwa amesimama wima.

    Hakika! Alikuwa ni Japhet Sudi… lakini mbona sasa alikuwa amedhoofu kiasi kile, ni furaha gani hiyo ambayo anayo ilhali yu katika wakati ule mgumu!!

    Nikarejea tena ili niweze kusikiliza ni ujumbe gani kutoka katika ile sauti nilitakiwa kuupata.

    “Sina maneno mengi ya kukueleza Jimmy…. Ila ni kukupatia ujumbe mmoja tu. Mbona ukoo wako umejiingiza katika matatizo yasiyowahusu kabisa rafiki yangu eeh! Kwa nini Jimmy unataka nionekane mbaya sasa… wewe ni rafiki yangu kabisa lakini kwa mambo ambayo ndugu zako wamenifanyia naweka urafiki kando. Kama utaweza kuwahi kabla hayajawa mabaya itakuwa sala kwenu lakini vinginevyo…. Vinginevyo Jimmy. Hasira yangu na iwe juu yenu!! Siku tatu.. nakupa siku tatu… rekebishya palipoharibika.” Haikuendelea kuzungumza ile sauti badala yake ukaingia wimbo wa Parapanda italia parapanda!! Ulipoisha huo ukaja wimbo mwingine tena wa misibani uitwao tuonane paradise! Yaani ikawa nyimbo baada ya nyimbo…

    Ama kwa hakika nilipagawa!!

    Sijaonana na Jimmy miaka lukuki, sasa ananiambia kuwa kuna jambo ukoo wangu umemfanyia.

    Mbaya zaidi akanipatia siku tatu tu za kubadili ambacho anataka kukifanya!!

    Ni kitu gani sasa?? Swali hili likanifanya nishindwe kulala.

    Nikajaribu kumpigia mjomba Mathias simu lakini iliita tu bila kupokelewa! Bila shaka alikuwa amelala….

    Mkojo ukanibana ghafla na tumbo nalo likaanza kuuma... vipele vya baridi vikaniota kwa fujo!!

    ****

    Nikajitahidi kuusaka usingizi lakini haikuwezekana, nikajiweka katika tahadhari. Sikutaka kuamini kuwa Japhet Sudi ni kichaa ati yale maneno ameropoka tu!!CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Hapana yule jamaa ni mtu hatari kabisa.

    Kama aliweza kunifanya nionekane chizi kabisa mbele ya mjomba wangu miaka mitatu nyuma, na sasa bado ananiandama.

    Yule hakuwa mtu wa kawaida.

    Kumuwazia Japhet kuwa si mtu wa kawaida kukakifanya kichwa changu kianze kuuma huku macho yakinichonyota katika namna ya kujiandaa kutokwa na machozi, sekunde kadhaa mbele nikawa nalia kama mtoto peke yangu bila mtu wa kuniuliza ni kitu gani kinaniliza.

    Nikazikumbuka na zile nyimbo za parapanda italia, nyimbo ambazo huwa nazisikia msibani na kuziimba vyema. Sasa nilikuwa nimewekewa nizisikilize bila kujua ni kwa nini nimewekewa!!

    Nyimbo zile zikanipagawisha zaidi!!!

    Nikainusa harufu ya kifo!!

    Ni nani ameenda kulikorofisha jitu hili? Nilijiuliza huku nikikisugua kichwa changu ili walau kidogo niweze kukabiliana na maumivu yale.

    Masaa yalizidi kwenda na zile siku tatu nilizokuwa nimeahidiwa zilikuwa zinaanza kuyoyoma kwa kurudi nyuma masaa.

    Zilikuwa siku tatu sasa yakawa ni siku mbili na masaa ishirini!!

    Masaa manne yalikuwa yametoweka tayari!!

    Majira ya saa kumi na moja nilitoka kitandani, sikuwa nimeupata usingizi kabisa. Niliingiwa maliwatoni na kujisafisha kisha nikavaa nguo za ofisi na kuondoka nyumbani. Sikuweza hata kuendesha gari langu tena, nilikuwa nimepagawa!!

    Nikaabiri bajaji ikanifikisha ofisini. Nikamshangaza mlinzi, haikuwa kawaida yangu kuwahi kazini. Lakini siku hiyo nikawa mtu wa kwanza kufika hata wale watangazaji wanaokesha wakiwa hawajatoka!!

    Nilitia saini katika daftari kisha nikaenda na kuifungua ofisi yangu, nikategea hadi majira ya saa kumi na mbili na nusu nikamuwahi Joan.

    Mwanadada rafiki yangu wa karibu ambaye watu walikuwa wanatuchukulia kama wapenzi, na huenda maneno yao yalikuwa yanaelekea kuumba kweli.

    Tulikuwa tumezoeana sana!!

    Ni huyu pekee ambaye niliamini naweza kumshirikisha juu ya hili jambo.

    Alipotoka nikamzuaia na kumchukua hadi ofisini kwangu, nikamweleza kwa ufupi juu ya barua pepe niliyopokea usiku uliozaa asubuhi hiyo!!

    Alitumia muda mrefu sana kujaribu kunielewesha.

    Uzuri pale ofisini palikuwa na mtandao wa kuperuzi.

    Nikaifuangua kompyuta yangu na kisha nikaifungua anuani yangu ya barua pepe na kufungua jumbe kutoka kwa Japhet Sudi!

    Nikaweka sauti ya chini ili asikie yale ambayo niliyasikia. Tukazifikia hadi zile nyimbo, nikataka kuzima akanizuaia na kusihi tusikilize hadi mwisho!!

    Baada ya kuzisikiliza zile nyimbo. Joan alinitazama moja kwa moja machoni.

    “Jimmy! Uliwahi kugombania mwanamke na mtu yeyote?”

    Joan aliniuliza swali ambalo lilinikera kwa sababu nilikuwa nimeshajieleza kwake kila kitu juu ya kinachoendelea.

    Joan akauvuta mdomo wake kisha akaondoka ndani ya kile chumba!!

    Wivu ulikuwa ukimsumbua binti yule. Nikalitambua jambo hilo kwa mara ya kwanza kabisa, Joan alihisi kuwa kuna ugomvi wa kuwania wanawake nd’o chanzo cha mimi kutishiwa jambo lile.

    Nilisikitika sana alipoubamiza ule mlango, na hapo nikaamini kuwa maneno ya Japhet Sudi ‘jitu’ juu ya wanawake yalikuwa sahihi kabisa.

    Wanawake watu wa ajabu sana!!

    Tukio kubwa kama lile linalohusisha uhai, yeye analeta wivu wake.

    Nikatabasamu kisha nikaifunga kompyuta na kutoka nje, nikaenda kuketi na mlinzi walau akanipa stori mbili tatu zilizonisahaulisha kidogo juu ya jitu.

    Lakini nikakumbuka kuwa masaa yalikuwa yanazidi kuyoyoma na siku zinakatika.

    Hiyo siku nayo ikamalizika huku jambo kubwa nililokuwa nimefanya ni kuwapigia simu ndugu zangu na kuwauliza iwapo kuna mtu wamemkosea basi waombe radhi kwa sababu kuna hatari inakuja.

    Wengi walinicheka sana kuwa nimeingizwa mjini, kicheko na kejeli zao zikanifanya nami nilichukulie wepesi jambo lile.

    Nikaamua kumpuuzia Japhet hadi siku hizo zipite!!

    Siku tatu za ahadi!!

    siku ya pili ikaanza, nilipanga kumtafuta Joan ili walau nimwelezee kuwa alichofikiria hakikuwa kitu sahihi kabisa. Sikuwa kama anavyodhania!!

    Nilienda duka la nguo na kumnunulia nguo ya pinki, rangi aliyokuwa akiihusudu kupindukia!!

    Niliamini kuwa nguo ile itamfanya anisikilize na kisha kunielewa kabisa. Na nilipanga kumweleza kama ndugu zangu walivyokuwa wameniambia, kuwa Japhet Sudi ni mmoja kati ya watu waliokosa kazi mjini.

    Yupo kuwasumbua watu pasi na manufaa yoyote!!

    Jioni ya siku hiyo nilijiweka mahali nikiwa na zawadi yangu, nikampigia simu Joan ili tujumuike pamoja katika chakula cha usiku.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Simu iliita sana lakini haikupokelewa! Nikapiga mara ya pili ikaita tena pasi na majibu.

    “Joan akinuna anaboa kishenzi!!!” nilijisemea wakati simu inaita mara ya tatu.

    “Yaani Joan aargh!” niliendelea kughafirika huku nikitoa misonyo ya hapa na pale.

    Nilipopiga mara ya nne simu haikuita kabisa.

    Amenizimia simu sasa!! Nilishangaa!!

    Nikabaki kulitazama begi dogo ambalo nilikuwa nimebebea ile zawadi.

    Nikalitazama kama bomu ambalo linataka kulipuka ndani ya sekunde moja inayokuja, nikajikuta nachukia na kusimama ili niondoke.

    Mara simu yangu ikaita!!

    Yaani hapo amejifikiria weee ndo amepiga!!! Nikajisemea wakati naitoa simu mfukoni.

    “Mamii!!” nikaita bila kutazama vyema ikiwa ni yeye ama la!

    “Jimmy una taarifa zozote kuhusiana na Joan.. aam I mean mmeonana na Joan?” ilikuwa sauti na mwanamke nisiyemjua.

    “Samahani simu yangu haij…” kabla sijamaliza kumwelezea kuwa sijatambua yeye ni nani alijitambulisha.

    “Naitwa Modesta, mama mdogo wa Joan…” alijitambulisha mwanamke yule.

    “aah! Shkamoo mama, sijaonana na Joan… siku ya pili sasa.” Nilimjibu.

    Simu ikakatwa!!

    Na hapo ikaita tena ilikuwa namba nyingine.

    “Jimmy!! Unahitajika ofisini sasa hivi..” sauti ya mkuu wangu wa kitengo ikaunguruma!!

    Nikafadhaishwa na kitendo kile cha kuwa na mtu aitwaye bosi… sikuwa nimepanga kabisa kwenda kazini lakini nililazimika kwenda.

    “Ah! Bora kujiajiri yaani!!” nililalamika.

    Licha ya kulalamika bado nilitakiwa tu kwenda!!

    Nikalibeba begi dogo ambalo lilikuwa na nguo ndani yake!

    Nikakumbuka ile nguo ilikuwa ni maalum kwa ajili ya Joan.

    Joan ambaye mama yake mdogo ananipigia simu na kuniuliza kama nipo naye!!

    Hisia za wivu zikajichimbua kutoka katika moyo wangu. Joan yupo wapi hadi mama yake mdogo aniulize mimi.

    “Au nilivyomkera akaamua kwenda kwa bwana mwingine!!” nilijiuliza huku nikighafirika. Na hapo nikakumbuka kuwa simu yake iliita kisha ikakatwa!!

    Dah! Yupo na mtu!!

    Kughafirika kule kukanifanya nitambue wazi kuwa kuna hisia kali za mapenzi zilikuwa ndani ya chimbo la moyo wangu dhidi ya Joan!

    Nikajiapiza kuwa nikitoa ofisini nitafanya kila namna nitahakikisha kuwa nakutana na Joan, na baada ya kukutana itabidi anieleze alikuwa na nani!!

    Fikra hizo zikanifanya nitabasamu huku nikwa naendesha gari.

    “Mi fala kweli, nimuulize mimi kama nani yake sasa!!” nikajiuliza kisha nikaanza kucheka kwa sauti ya juu, kicheko kilichonitoa machozi.

    Sikujua kama kilikuwa kicheko cha mwisho mwisho!!

    Nilifika ofisini na kukuta bosi wangu akiwa anazunguka hapa na pale. Hakuwa yeye pekee hadi mmiliki wa redio niliyokuwa nafanyioa kazi alikuwa haeleweki.

    Waliponiona wakaniwahi na kunifungulia geti!

    Looh! Maajabu mabosi wananifungulia geti, au nimepandishwa cheo?? Nilijiuliza!!

    “Mwambie wewe…” mmoja alimrushia mwenzake mzigo wa kunieleza nini walichoniitia.

    Hapo moyo ukaanza kupiga kwa nguvu, wazo la kwanza likiwa kufukuzwa kazi. Nilipata uoga sana.

    “Jimmy… kuna mgeni wako alikuja sijui alikupigia simu kabla…” alinianza. Nikapinga kuwa sikuwa na ujio wowote kimiadi pale ofisini.

    “Ah! Ok kuna mgeni amekuja mwanaume mmoja hivi nadhifu tu, kuna mzigo wako ameuleta….”

    “Mzigo?” niliuliza.

    “Ndio kuna mzigo ameuleta na umefikishwa moja kwa moja mapokezi ili ukifika upewe. Lakini hata kabla wewe hujafika kuna tatizo limeibuka katika huo mzigo… kweli hakuna mgeni wako kwa siku ya leo?” alirudia kuniuliza.

    “Mkuu nimesema sikuwa na miadi na mtu!!” nilifoka huku nikanza kupagawa kidogo kidogo.

    “Ah! Sawa.. ila.. hebu twende twende labda utaelewa huo mzigo maana mhh!” hakusema akawa anamung’unya maneno…

    Nikaongozana nao hadi mapokezi. Dada wa mapokezi hakuwepo, na hata wao mwalipofika wakanipa maelekezo tu juu ya bahasha lakini hawakutaka kusogea.

    Na mimi nikagutuka nikagoma kusogea, kama mzigo wameupokea wao ni kipi kinawashinda.

    Baada ya kusukumana kwa sekunde kadhaa tukakubaliana kuwa mzigo ule hatuwezi kuugusa sisi bila uwepo wa jeshi la polisi.

    Simu ikapigwa polisi na baada ya nusu saa wakafika askari watatu.

    Na wao wakaanza kuogopa tulipowapa maelekezo bila kupiga hatua mbele!!

    Kwa kunyatia sana hatimaye wakaitoa ile bahasha!!

    Ama kweli ulikuwa mzigo wa maajabu!!

    Mzigo unaovuja damu!!

    Bahasha ilikuwa haitamaniki!!

    Askari kwa tahadhari kubwa wakaifungua…..

    Karatasi nyeupe ikatoka kwanza, hii ilikuwa imeandikwa kwa maandishi makubwa.

    “ULIMI NI SUMU!!”CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Na baada ya kuitoa ile karatasi, mara bahasha ikamyumba yule askari na kikatoka kitu kilichokuwa kimebakia ndani ya bahasha!!

    Ebwana! Eeh! Si askari na ukakamavu wao wala nani aliyebaki pale kila mtu akatafuta wapi pa kutokea.

    Bosi wangu mkubwa kabisa ninayemuheshimu akajichanganya badala ya kwenda mlangoni akataka kutokea sehemu isiyokuwa na mlango mara ana kwaana akakutana na kile tulichokuwa tunakikimbia!!!

    Alipiga yowe kisha akaanza kulia kama mtoto!!!



    ULE mtafaruku ukaendelea hadi mlangoni kila mmoja akawa anawania kupita wa kwanza mlangoni, yule bosi aliyekuwa analia kama mtoto baada ya kuchanganya njia ya kutokea baada ya kuona kuwa hakuna ambaye anajali kilio chake. Alikuja mbiombio na kutusukuma ili apite pale mlangoni.

    Ule unene wake akafanikiwa kututupa mbali, lakini bado hali ilikuwa mbaya kwake alibaki katika kile chumba ambacho sisi tulikuwa tunakikimbia!!!

    Baadaye sote tukawa nje huku kila mmoja akitweta katika namna ya kumpa nafuu.

    Binafsi nilikuwa nimechanganyikiwa sana nikiongezea na mghafiriko wa kitu nilichokuwa nimekishuhudia pale ndani miguu ikaniishia nguvu!!

    “Hivi ule ni ulimi wa mwanadamu au?”bosi wangu yule aliyekuwa analia hovyo aliuliza swali ambalo hakika lilinikwaza si mimi pekee bali hata wale maaskari.

    Swali lile alitakiwa ajiulize na kujipatia jibu yeye mwenyewe ama la angoje uthibitisho kutoka kwa daktari.

    Hali halisi aliiona pale ndani hakuna aliyetulia bali kutafuta usalama wake kana kwamba ule ulimi ulikuwa unatembea. Sasa hivi anaulizia kama ulikuwa wa mwanadamu ama la!!

    Askari mmoja akamjibu, “ule ni ulimi wa kondoo bosi!!”

    Jibu lile likanifanya nipate kicheko sehemu isiyotakiwa kucheka.

    Bosi wangu akapiga kite cha ghadhabu kisha akasimama na kujipukuta vumbi na sisi tukasimama!!

    “Yah! Utakuwa ulimi wa kondoo kweli…” bosi akazungumza peke yake.

    Wakati tuliwa hatujafahamu nini cha kufanya zaidi mara simu ya bosi wangu ikaita.

    Akaitazama kwa muda kisha akaipokea huku akisikiliza upande wa pili ni kitu gani kilikuwa kinasemwa.

    Mara akaruka kando kama aliyeona mdudu, na palepale bila kusema lolote akageuka nyuma kukitazama kile chumba ambacho kilikuwa na ulimi, na hapo akaanza kutimua mbio na unene wake kitamb kikiruka huku na kule.

    Nani abaki nyuma??

    Hilo ndó lilikuwa swali la msingi wakati kila mmoja akitimua mbio kumfuata bosi bila kujua ni kitu gani alikuwa anakikimbia!!

    Alipofika getini akasimama ghafla, nasi tukamfikia.

    “Jamani eeh! Sio ulimi wa kondoo ule kumbe…”alizungumza huku akihema juu juu.

    “Kuna kitu gani hapa kinaendelea jamani..” nililazimika kuuliza hatimaye.

    “Utakuwa ulimi wa Joan ule, Joan mfanyakazi wetu yule amekutwa huko sijui wapi… wapi vile sijui. Ahana ulimi.. utakuwa ule ni ulimi wa Jo… aaah” akashindwa kuendelea kuongea akajiinamia na kuanza kulia.

    Kilio kilekile kama mtoto mdogo!!

    Taarifa ile ikaupasua moyo wangu ghafla, kusikia kuwa yawezekana Joan ameuwawa na kukatwa ulimi. Niliishiwa nguvu kabisa. Nikamgusa bega bosi ili niulize zaidi!

    Wacha wee! Kuna watu waoga lakini bosi wangu alikuwa ameimarika katika kozi hiyo. Alipiga mayowe makubwa huku akitaka kukimbia. Nikamtuliza mzuka wake na kumuuliza taratibu.

    Akanipatia ile simu, nikatazama namba za mpigaji nikampigia.

    Wale maaskari wakaniamuru niweke loud speaker’nikafanya kama walivyotaka.

    Yule mtu wa upande wa pili alivyozungumza wakamtambua kuwa alikuwa ni askari mwenzao.

    Wakamuuliza maswali hapa na pale.

    Hakika alikuwa ni Joan! Alikutwa amekufa kando kando ya fukwe za ufukwe wa koko nje kidogo ya jiji la Dar es salaam

    Hakuwa na ulimi katika kinywa chake na walimkuta na kitambulisho ambacho kilielekeza kampuni ambayo alikuwa anafanyia kazi.

    Nilichoka!!

    Nikaaga na kuondoka huku kichwani nikijiuliza ni kitu gani kimemtokea Joan na ni kwa nini ule ulimi uletwe ofisini kwangu kama mzigo wangu.

    Mgeni gani wa kuleta vitu vya kutisha kiasi kile.

    Jitu!! Jina hilo likaniingia akilini mwangu na hapo nikamfikiria Japhet Sudi!!

    Lakini Japhet aliahidi kuwa atafanya mambo baada ya siku tatu na zilikuwa hazijafika bado.

    Ni nani huyu sasa? Au mwanaume wa Joan ambaye aligundua kuwa nammendea binti yule kimapenzi.

    Maswali yalikuwa lukuki nikakosa majibu!!

    Nikalazimika kuondoka kimyakimya eneo lile.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Halikuwa eneo salama hata kidogo.

    Nikajikongoja hadi nyumbani huku nikitambua kuwa kuanzia siku inayofuata nitakuwa mtu wa kuitwqa kituo cha polisi kila mara, ili kusaidia upelelezi.

    Mambo ya polisi nayajua! Na ikibidi wataniweka rumande ili niweze kumtaja aliyenitumia mzigo ule.

    Sawa wataniuliza… ina maana nimtaje Japhet Sudi au? Yaani mtu ambaye katika maisha yangu nimemuona mara mbili tu katika maisha yangu niende kumtaja kuwa ndiye muhusika.

    Haya nitamtaja, je wakiuliza kwanini ninamshuku…

    Eti hapo nipeleke ujumbe wa barua pepe….

    Yeah! Walau hapo ningepata cha kujitetea.

    Nikakaza mwendo hadi nikafika kituo cha daladala nikapanda gari na kutoweka, nikiwa ndani ya daladala ndo nikakumbuka kuwa nilienda ofisini na gari yangu binafsi siku ile ajabu nilikuwa nimeisahau.

    Nilipofika nyumbani kitu cha kwanza nikafungua kompyuta yangu na kuingia katika anuani yangu ya barua pepe.

    Lengo likiwa kuinukuu vyema anuani ambayo ilikuwa imenitumia ujumbe siku ile.

    Anuani ya jitu!!

    Nilipofungua nikakuta kuna barua pepe mpya mbili ambazo hazijafunguliwa!!

    Nikafungua upesiupesi.

    Nikakutana na kiambatanishi nikakifungua na hapo nikakutana na maandishi yakiwa na kichwa cha habari.

    “NAJIFUNZA KUANDIKA HADITHI”

    Nikataka kupuuzia ila nikaona nipitishe macho walau mistari miwili ingenitosha!!

    Haikuwa mistari miwili kama nilivyodhani!!

    MAANDISHI YAKASOMEKA HIVI!!

    Wasichana watu wa ajabu sana, yaani wao wanawaza mapenzi tu. Ukiwasiliana na mtu wao wanawaza mapenzi tu, yaani wa ajabu sana. Wanajifanya wana wivu halafu wanajivika vyeo vya upelelezi wakati hamna kitu kabisa.

    Najua kuandika sasa Jimmy na nitakuwa nakuandikia kila kitu, nayaandika haya wakati naulaumu ulimi wa mwanamke, na pia nayalaumu maiskio na akili zake za kupima.

    Yaani Jimmy nadhani ni mama yangu na mama yako na mama wa yule mwingine utakayempa asome haya maandishi ndó wanawake pekee waliokuwa na akili duniani! Ila hawa wasichana sijui akina Joan, akili zao kama Maria tu!!

    Nikisahau kuweka mikato na nukta nisamehe ndugu mwandishi, najifunza kuandika!!

    Hivi huyo Joan kwa mfano, angeamua tu kukaa kimya asinifuatilie kwani yangemkuta hayo kweli. Eti akanitafuta kwenye barua pepe yangu sijui ulimpa wewe sijui ni vipi, akaanza kunichimba hadi tukakutana. Tulipokutana anajifanya kunirembulia macho yake. Jimmy hawa wanawake wauaji tu!! Hamna kitu!!

    Mwishowe anaanza kunilaumu eti mimi kuna msichana nagombea na wewe, hivi Jimmy mimi na wasichana wapi na wapi rafiki yangu.

    Tangu ule ujinga wa Maria mimi na wasichana basi siwataki tena waliniua mara mbili sitaki waniue mara ya tatu.

    Ulimi wa Joan ukanikwaza sana nikaona si vibaya nikiuondoa Jimmy.

    Yaani ananikosea heshima kabisa mimi, yaani mimi nigombee msichana na umri huu kweli eeh!

    Najifunza kuandika kama haina mashiko usisite kuniambia.

    Zile siku zetu tatu za ahadi zipo palepale, utaamua mwenyewe sasa kwenda kuangalia maiti ya huyo hawara yako, ama kujitahidi hasira yangu isijekuwa juu ya ukoo wenu.

    Nakukumbusha kuwa iwapo Maria hatalaaniwa, basi nitamsaidia mtoa laana kulaani. Nitamlaani Maria na kizazi chake!!

    Nimemaliza kuandika nitoe kasoro!!

    Kwaheri!!

    Nilitetemeka, kama umewahi kutetemeka hutaniuliza kitu. Utaona ni jambo la kawaida!!

    Lakini nikusisitize kuwa nilitetemeka na kisha kupitiwa na haja ndogo bila kujua.

    Nilijikojolea!!

    Ama nilikuwa nimesoma simulizi za kutisha na kuangalia filamu za kutisha mno lakini ile barua ilikuwa inatisha kupita maelezo na mbaya zaidi ilikuwa ina harufu!!

    Harufu ya kifo!!

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog