Simulizi : Usiku Wa Manane
Sehemu Ya Tano (5)
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Hancy…. Najua utafanikiwa kwa hilo bila ya mimi,” aliuliza Fina baada ya kuona kimya kidogo kilichosababishwa na fikra za Hancy aliyeonekana akifikiria jambo.
“Usijali mpenzi,” ngoja niwafuate hukohuko.
“Hapana Hancy… sikuruhusu kwa leo. Nenda kesho. Hii safari nimekuja kwa ajili yako na nlikuambia leo nalala kwako.”
“Okey Baby,” Hancy alisema huku akitabasamu. Alimbeba juu juu Fina na kuingia naye ndani. Zoezi zima la kulienzi penzi lao likashika hatamu baada ya wote kuwa na hamu ya mwenzake kwa muda mrefu. Fina hakujionyesha kuogopa kufanya lolote ambalo alijua litrampoza hasira na kumrudisha Hancy katika dunia ya huba na iliyojaa asali ya upendo. Alijitutumua kila awezavyo hali iliyomfanya Hancy akiri uzuri wa Fina kipenzi chake cha moyo.
*****
Jioni ya siku inayofuata Hancy alimuacha Fina nyumbani kwake na kuondoka. Alimuacha ndani ya mikono salama ya mlinzi wake. Hancy aliendesha gari lake kuelekea Ukumbi wa Klabu ya Maisha. Watu walikuwa wengi na magari yalikuwa yamepakiwa karibu karibu.
Alipata nafasi ya kuegesha gari lake. Alipaki gari lake na kuingia ndani ya ukumbi. Hakuwa anapenda kuingia klabu lakini siku hiyo alifanya hivyo. Lengo lake lilikuwa ni kuwatafuta wale wauaji. Aliishia kuzunguka huko ndani bila ya kuona mafanikio yoyote. Alitoa simu yake akitaka kumpigia Van Brussel kama alivyoelekezwa na Fina.
Ghafla alishtuliwa na mtu ambaye alimvuta na kumwingiza katikati ya wanawake aliokuwa amekaa nao.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Van Brussel,” aliita Hancy kwa furaha baada ya kumwona rafiki yake Hancy. Hancy aliona kama ndoto alimwonyesha simu yake Van Brussel kwa lengo la kumwonyesha ile namba aliyopewa na Fina. Van Brussel hakujua kama Fina na Hancy walikuwa wapenzi.
“Unaona hii namba?” Hancy alimwonyesha Van Brussel ile namba aliyotaka kuipiga.
“Namba yangu… nani amekupa?” Van Brussel alishangaa kuona Hancy akiwa na namba yake. Alithibitisha kweli ilikuwa yake.
“Nitakuambia Van, naomba tuongee kwanza. Ndiyo maana nikakutafuta hadi huku japo mimi sio mpenzi wa kuingia katika kumbi za starehe.”
Hancy alimtoa Van Brussel nje kwa lengo la kuongea naye. Waliwaacha wale warembo wakiendelea kuserebuka huku wakinywa taratibu vinywaji vyao na wao kutoka nje ya ukumbi. Waliangalia sehemu nzuri lakini zote watu walikuwa wamesimama wakizungumza. Waliamua kwenda moja kwa moja hadi kwenye gari la Hancy.
“Habari yako Hancy, nimekutafuta sana bila mafanikio. Nilijua siku moja nitakuona nikija Tanzania na sasa imekuwa hivyo,” Hancy alikuwa akimwangalia Van Brussel alikumbuka zile picha zake alizomwonyesha na wale watu aliowachora kipindi alivyokuwa mdogo na kwenda nazo Uholanzi.
“Napenda tuzungumze kidogo Van…” Hancy alimwita kwa ufupi kama alivyokuwa akifanya hivyo wakati wakiwa Uholanzi.
“Tuingie hapa kwenye gari langu. Ni jambo la maana sana ningependa tuzungumze na baada ya kusikia upo huku na nikapewa namba zako nilifurahi kwa sababu najua utanisaidia sana.”
“Gari lako zuri zana. Hongera sana,” Van Brussel alilipenda gari alilokuja nalo Hancy. Lilikuwa ni Range Rover nyeusi.
Hancy na Van Brussel waliingia ndani ya gari na kuanza kuzungumza. Alifungulia kidogo music ili kufanya sauti zao zisisikike nje. Vioo vya gari lake vilikuwa ni vyeusi na hivyo isingekuwa rahisi kwa mtu yeyote kuwaona wakiwa ndani.
Hancy alimhadithia Van Brussel kila kitu alichokijua. Kuanzia alivyokuwa mdogo hadi anachokikumbuka. Alijua kwamba kwa utaalamu wake wa kuchora na kwa kuwa yeye ndiye aliyewachora wale watu weusi huenda angepata msaada wake.
“Unakumbuka ile picha ya wale watu weusi ulionionyesha kipindi kile tukiwa shuleni.”
“Ndiyo nakumbuka, kuna nini Hancy?”
“Ukiwaona wale watu unaweza kuwakumbuka kweli?”
“Aaah! Mbona walikuwa ndani na wote wamekuja pale wakanisalimia. Unataka kuniambia wale watu ndo wabaya kama ulivyonihadithia. Ina maana wale watu ndiyo walioua wazazi wako na ndugu zako?” Van Brussel aliuliza kwa mshangao. Hancy alibaki ameinamisha kichwa chini huku akibubujikwa na machozi. Alijihisi mshindi kwani alijua tayari ameshawapata.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Wale ni rafiki zangu, nimejuana nao muda mrefu sasa. Kobra wale.”
“Hancy alimwangalia Van Brussel na kubaki kimya. Hakujua ni namna gani Hancy alivyokuwa na hasira juu yao.
“Sioni ulazima wa wao kuishi,” alisema Hancy huku akiunyanyua uso wake na kumwangalia Van Brussel. Wamekwisha.”
“Unataka kufanya nini Hancy?”
“Kama nilivyokuambia. Waliua ndugu zangu na sasa wanapeta. Sasa ni zamu yao.” Alisema Hancy huku akimwonyesha Van Brussel panga ambalo alilitoa nyuma ya kiti cha gari lake.
“Hili ndilo waliolitumia kuwaulia ndugu zangu. Sasa litawamaliza wote.” Hancy alitoa picha ya ndugu zake na kumwonyesha Van Brussel. Alimwangalia Van Brussel na kuhisi Van Brussel aliogopa.
“Unataka kuwavamia wote sasa hivi Hancy?” Van Brussel alisema kwa woga.
“Nimewapata,” alisema Hancy ka sauti ya upole iliyomfanya Van Brussel abaki akimwangalia kwa mshangao.
Van Brussel alikuwa amemwelewa Hancy. Alimwonea huruma akawa hasemi chochote. Waliingia klabu na kuanza kuzunguka pamoja kule ndani. Alianza kumwonyesha mmoja mmoja.
Deo alikuwa amezungukwa na kundi la wadada waliokuwa wakicheza muziki karibu yake. Alikuwa amelewa.
“We mzungu wetuu,” aliita kwa sauti ya kilevi wakati Van Brussel na Hancy walivyokuwa wakipita. Watu walicheka kwa dhihaka aliyoionyesha Deo kwa Van Brussel. Hakujali.
Alimfuata pamoja na Hancy na kuongea naye.
“Leo uko na mweusi.. mwenzetu huyo.” Watu walicheka baada ya kusikia utani huo. Hancy alikuwa akimwangalia kwa hasira. Alitamani amvamie na kumuulia palepale.
Alitoka na kumwacha Van Brussel akiwa na Deo pamoja na watu wake. Aliingia ndani ya gari lake. Simu yake iliita. Alikuwa ni Fina aliyempigia na kuanza kuongea naye.
“Mpenzi,” alisema Fina.
“Fina.”
“Niambie, bado hujarudi nyumbani?”
“Hapana. Ila nimeshaonana na Van Brussel. Tumeongea naye na sasa nimetoka nje nimewaacha wakizungumza na Deo.”
“Nadhani kila kitu kitakuwa poa Hancy.”
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Kweli, tuanze kazi yetu.”
“Sawa Hancy, nimekuelewa. Take care. Nakupenda sana.”
“Nakupenda pia.”
Hancy alimaliza kuongea na Fina. Alifungua gari lake na kuingia. Van Brussel alikuja na kuagana naye na Hancy alielekea nyumbani kwake.
*****
Ni na mapema Hancy anaamka. Analifuata panga na kulinoa kila wakati. Anaufuata mgomba uliokuwa karibu yake na kuanza kuushambulia kwa hasira hadi unaisha wote. Analiangalia lile panga lake. Anayaangalia kwa umakini makali yaliyonolewa kwa takriban wiki nzima. Anaridhika.
Siku nzima anaimaliza kwa kufikiria mbinu gani aitumie kuwamaliza wote.
“Nimewajua wote. Nimewatambua wote. Fina atanipeleka kwa kila mmoja wao,” aliwaza huku akimalizia kuvaa viatu.
Alichukua simu yake na kumpigia Fina ili wajue wanakutana wapi.
“Natumai utanionyesha kwa kila kiumbe ninayemtafuta,” alisema Hancy.
“Kote napajua usiwe na wasiwasi mpenzi,” Fina alijibu huku akiingia ndani ya gari lake hali iliyomfanya Hancy asikie mngurumo wa gari na kuhoji.
“Unakuja na gari lako?”
“Ndiyo mpenzi.”
"Kwani si tunatumia la kwangu kwenda huko?”
“Ndio…we tukutane tu ntakuonyesha.”
“Tunakutana wapi kwani?”
“Shekilango, nitaacha gari langu kwa rafiki angu. anakaa hapo hapo Shekilango.”
“Sawa mpenzi, nitakukuta hapo?”
“Ok.”
*****
Hancy alitoka nyumbani na kumfuata Fina. Hakutaka kupoteza muda wake. Aliwasiliana na Fina na kumfuata Shekilango walipoahidiana wakutane. Fina alikuwa akimsubiri Hancy ambaye alikuwa ameshamwona na kumfuata pale alipokuwa amesimama.
Wakiwa kwenye gari, Fina alionekana bado mwenye uchovu lakini kama walivyopanga alijitahidi kutii wito na mipango yao. Hakutaka kuharibu mipango hasa akimfikiria Hancy.
“Unaonekana umechoka sana.”
“Kweli, leo nilishinda nafanya tu usafi nyumbani.”
“Tunaanzia wapi?”
“Magomeni kwa Chacha,” aliitikia Fina.
“Una uhakika tutamkuta leo?”
“Ndiyo, hawezi kutoka usiku na leo nadhani atakuwepo maana sio siku ya kwenda klabu.”
“ Sawa,” Hancy alikubali na kuanza kuondoka kuelekea Magomeni. Mwendo wa dakika kumi walikuwa wamefika.
“Mbona mapema hivi lakini?”
“Usijali, hatuendi sehemu nyingi, tutakaa kwanza mahali kisha muda ukienda ndo twende kwake.” Hancy alisema huku akimwangalia Fina aliyeonekan kuchoka. Hakujali kwani kazi yake ilikuwa ni kuonyesha tu mlango na kuelekeza njia. Alimwacha bila kumsemesha hadi alipoanza kusinzia na kulala. Alimwacha alale hadi muda wake utakapofika. Aliamua apaki gari maeneo ya Magomeni Mwembe Chai ili asije akapitiliza walikotaka kwenda.
Fina alishtuki. Alishtuka kuona gari limesimama. Alimshika Hancy began a kukaa vizuri.
“Samahani mpenzi,” alimsemesha Hancy ambaye alikuwa ameegemea kiti chake huku ameshika panga. Fina alimwona Hancy asiye na utani. Ghafla alianza kuelekeza ili kufika nyumbani kwa Chacha.
Kulikuwa hakuna magari barabarani kwa kuwa ulikuwa ni usiku sana. dakika chache ziliwatosha Hancy na Fina kufika maeneo ya Magomeni Mapipa. Giza lilikuwa kali. Hadi kufika nyumbani kwa Chacha, Hancy aliendesha gari taratibu ili majirani na watu wengine wasiweze kusikia. Mtaa alioishi Chacha ulikuwa kimya wakati huo.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Saa nane kasoro moja Hancy alikuwa amesimama nje ya mlango wa Chacha. Aliliangalia gari lake. Alimwangalia Fina aliyekuwa ndani ya gari. Panga lake alikuwa ameliweka ndani ya koti kubwa alilokuwa amelivaa.. kisha aligonga mlango wa Chacha ambaye alikuwa ameshalala. Chacha alishtuka. Hakutegemea ugeni wa muda huo. Aliangalia saa. Hakuiona vizuri kwa sababu ya usingizi.
“Nani tena usiku huu?” alihoji Chacha huku akienda kufungua mlango.
“Hancy… karibu, vipi mbona mida hii, kulikoni?” Chacha alihoji kwa mshangao huku akiangalia saa yake iliyokuwa ukutani. Ilikuwa ni saa nane na dakika tatu.
“Samahani sana ndugu Chacha. Najua hukutegemea ujio wangu wakati huu.”
“Umepatwa na nini. Kwema?” Chacha aliuliza kwa mshangao huku akimkaribisha Hancy ndani.
“Nimepatwa na tatizo, n’takuwa hapa kwako kwa usiku huu, nimevamiwa njiani leo sikuwa na gari, nimewatoroka hao vibaka nkakumbuka uliniambia unakaa hapa Magomeni.”
“Sasa na nyumba nani kakuonyesha….”
“Oooh!!!.... usijali, sitapita tena hii mita yenu bila gari,” Hancy aliingia huku akiangalia vizuri chumba cha Hancy. Chumba kilichokuwa nje kilichojitegeme. Kilionyesha wazi aliyeishi pale ni kapera.
“Karibu uake kwanza. Pumzika hapo.”
“Nashukuru,” Hancy alichomoa ile picha ya ndugu zake na kuiweka mezani. Hakutaka kuupoteza muda wake kuongea na moja ya makatili anaowatafuta. Aliangalia maisha yake na utu wake ambavyo havikuendana. Alimwona mtumwa aliyefanya kazi ya kikatili ili kumfurahisha bosi wake, Deo.
Alitoa panga na kumwonyesha Chacha ambaye alikuwa amepigwa na butwaa asijue la kufanya. Alimsukuma kwa nguvu na kuangukia kwenye sofa. Hasira ziilimpanda kwa kadri alivyokuwa akimwangalia. Hancy alimwekea mguu juu ya kifua chake huku akilishika panga bara’bara.
“Kaa chini na usijiguse mpumbavu wewe,” Hancy alitoa amri ambayo ilitekelezwa na Chacha mara moja. Alikuwa akihema kwa nguvu baada ya kuona kwamba ule haukuwa utani wala ndoto bali ulikuwa ni ukweli. Panga tayari lilikuwa likikaribia kumkabili. Hakuweza hata kupiga kelele. Sasa alijua anakufa.
“Unawajua hawa watu kwenye hii picha?
“Ndiyo, nawajua.” Aliiangalia ile picha kwa makini kwa amri moja tu ya kutaka kuwatambua na kuelezea anavyowajua huku akiliangalia lile panga kwa woga.
“ Ni mzee mmoja hivi alifariki kitambo anaitwa Ambrose.” Aliongea huku akitetemeka midomo kwa woga.
“Shhhh! Nyamaza,” Hancy alivuta panga na kumkata nalo mkono wa kushoto. Damu ziliruka nyingi. Hancy hakujali. Haikuwa nyingi kama ile aliyoishuhudia wakati akiwa mdogo nyumbani kwao. Aliutenganisha mkono na mwili wa Chacha.
“Shhh!! Sitaki kelele.” Hancy alimziba mdomo Chacha ili asiweze kupiga kelele. Haraka alimfuata na kumwonyesha mkono wake huku akimfunga na kipande cha kitambaa mdomoni asiweze kupiga kelele. Alimpiga kwa kutumia ule mkono wake.
“Hii ndo alama mliyonidhihirishia nyie ndo mliomuua baba yangu na ndugu zangu. Hatabaki hata mmoja na nimeanza na wewe, nimewatafuta kwa miaka mingi na sasa nimewapata. Wenzako wanajitayarisha huko waliko. Nadhani hutaweza kuwajulisha huko walipo. Ntawafuata mwenyewe.” Hancy alinyanyua tena panga juu na kumtwisha la kichwa lililomaliza uhai wa Chacha. Kitambaa alichomfunga mdomoni kilimnyima uwezo wa kupiga kelele.Alimpiga picha na haraka alitoka na kuelekea kwenye gari. Alikuwa amechafuka kwa damu.
“Vipi Hancy,” alihoji Fina.
“Tayari,” Hancy aliwasha gari na kutokomea nyumbani kwake.
Alifika kwake saa tisa za usiku. Aliliosha panga lake huku akihema kwa nguvu kabla ya kuingia ndani. Fina alimwangalia kwa huruma sana.
“Lazima waishe wote,” alisema kwa hasira na kuliweka juu ya kabati panga lile.
*****CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Habari zilizagaa kila mahali. Habari juu ya mauaji ya kutisha pasipo muuaji kukamatwa wala kujulikana. Hakuna aliyemdhani mwenzake wala aliyekuwa hata na hisia kwamba ni Fulani ama Fulani anaweza akawa ametekeleza mauaji yale. Kila mmoja katika kundi la Kobra aliingiwa na woga.
Baada ya siku tano, Hancy alionekana akiwa na Fina katika ukumbi wa Maisha. Huko waliwakuta wahalifu wao. Waliamua kufanya hivyo ili wasigundue kwamba ni wao wanaohusika.
Van Brussel alikuwa nao pamoja baada ya kuwaona wakisakata musiki. Haikuwa kawaida ya Hancy. Aliamua kuwaaga ili aondoke. Fina naye alimuaga Van Brussel.
“Subirini,” Van Brussel alitaka watoke wote. Alitaka akajue maendeleo ya Hancy ambaye hawakuonana kwa siku kadhaa. Alikuwa bado hajamwona Fina hadi pale Fina alipomsemesha.
“Kumbe mnafahamiana?” alihoji Fina huku akiwa amemshika Hancy mkono.
“Haah….Fina…. Hancy… Nafurahi kuwaona hivi…. Sasa nimejua ni nani aliyekupa namba zangu,” Hancy na Fina walikuwa wakitoka.
“Hancy,” aliita Van Brussel. Hancy naye aligeuka ili kumsikiliza Van Brussel. Walikuwa wameshafika katika gari la Hancy.
“Sema ndugu yangu,” Hancy alisimama imara kumsikiliza Van Brussel.
“Sitaki kujiuliza ni nani aliyefanya yale niliyoyasikia. Hongera. Unachofanya ni haki yako,” Van Brussel alisema huku akimpigapiga Hancy begani kumpongeza.
“Usijali…. Hatabaki mtu,” Hancy alisema huku akitabasamu.
“Hatojua mtu…ntaendelea kuwahadaa sana,” alisema Van Brussel.
“Ntashukuru sana ndugu,” Hancy alisema huku akifungua mlango wa gari na kuingia. Waliondoka na kumwacha Van Brussel akiwa bado klabu.
“Kazi itaendelea kesho tena.”
“Usijali mpenzi.”
Saa saba na nusu usiki, Hancy na Fina walikuwa Ubungo. Safari yao ya kwenda Kimara safari hii ilikuwa nyepesi kwani Fina alikuwa tofauti na alivyoonekana mwanzo. Alikuwa tayari kufanya kazi baada ya siku kadhaa za kupumzika ili kuwasahaulisha watu tukio la kwanza. Hata kikundi cha Kobra hakuna aliyekuwa na wazo la kukumbana na tukio kama lile alilokumbana nalo Chacha siku chache zilizopita.
Mbele ya mlango wa John Kaputa. Hancy alikuwa amesimama. Alichungulia kwa dirishani. Hakuna aliyemwona. Sasa alielekea mlangoni.
“John,” sauti hiyo ilimshtua sana John aliyekuwa amelala. Hakutegemea kama angepata ugeni usiku wa siku hiyo. Alichokisikia siku mbili zilizopita baada ya kifo cha Chacha kilimwogopesha sana.
“Nani saa hizi….saa nane usiku,” John alishangaa huku akiiangalia saa yake huku akiteremka kitandani. Saa ilikuwa ikionyesha ni saa nane na dakika mbili ikielekea tatu.
“Ni mimi John, tafadhali fungua. Wanaweza wakanikuta hapa, wataniua,” Hancy aligongagonga mlango kama mtu aliyekuwa akifukuzwa na kutaka kujificha huku akiita kwa sauti ya chini ili asisikike na majirani wakatoka na kumwona. Alijua kelele zingezuia mpango wake.
“Aaah, Hancy, kumbe ni wewe, vipi kuna nini?”
“Kuna watu wananikimbiza nahisi wanahisi nina pesa wanataka wanikabe,” Hancy alijitetea na kuingia ndani.
“Pole sana Hancy,” John hakuamini kumwona Hancy wakati ule nyumbani kwake. Alijua labda Hancy naye anajihusisha na ujambazi na hivyo alifanya tukio moja na sasa anakimbizwa au amekoswakoswa huko alikotoka.
“Asante John,” Hancy alimsukuma John hadi kwenye sofa lililokuwa karibu, John alishtuka baada ya kujikuta yuko kwenye kochi baada ya kusukumwa.
“Nataka uniambie juu ya hawa watu,” Hancy aliitoa ile picha na panga huku akilibinuabinua juu kumtishia John. John jasho lilikuwa likimtiririka. Alitamani asingefungua mlango, alijua wazi mhusika wa kifo cha Chacha ndiye huyuhuyu.
“Tafadhali usiniue Hancy, ntakuelezea.”
“Ndiyo ninachokitaka, hawa ni kina nani?” Kwa hofu aliyokuwa nayo John hakuanza hata kuongea Hancy alimcharaza panga la shingo na kutenganisha kichwa na kiwiliwili. Alimpiga picha kama alivyofanya kwa chacha. Alitoka na kuelekea kwenye gari.
“Vipi Hancy, fresh?”Fina alihoji baada ya Hancy kuingia kwenye gari.”
“Tayari mpenzi,” Hancy aliangalia saa yake ambayo ilikuwa ikionyesha ni saa nane na dakika kumi. Aliwasha gari na kuondoka.
*****
Asubuhi maeneo yote ya Dar es Salaam kuanzia Kimara ambapo tukio hilo la mauaji lilitokea na mikoani habari kama zile za Chacha zilianza kutawala kila mahali. Polisi waliwajua watu hao baada ya kufa. Magazeti, redio na runinga vilitawala kuhusu mauaji hayo. Kikubwa ni baada ya wote kugundulika ni wa kikundi kimoja ambacho kimekuwa kikitafutwa kwa muda mrefu. Hiyo ni baada ya wachunguzi kubaini alama yao ya Kobra katika mikono yao.
“Inaelekea huu mtandao ni mkubwa, wenye mitandao mikubwa huwa wanajiwekea alama.” Polisi mmoja ambaye alikuwa akiutazama mwili wa John baada ya kutolewa baada ya kutambuliwa na ndugu alikuwa akimnong’oneza mwenzake aliyekuwa akilinda naye eneo hilo kwa wakati huo.
****
Ni siku mbili tu zilipita ndipo polisi wakajikuta tena nyumbani kwa Baltazari na siku inayofuata kwa Shebby ambao walibainika kuwa ni moja ya watu wa kundi lililokuwa likitafutwa.
Wote waliuliwa muda mmoja katika siku tofauti.Muuaji hakujulikana wala hakuna aliyehisiwa kwamba ndiye muuaji.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Ni nani atakayekuwa anafanya haya mauaji.Na inaonyesha kwamba analipiza kisasi. Kwa nini watu wote ni wa kikundi kimoja. Nadhani itabidi tuulizane polisi kama kuna mmoja wetu anayefanya haya,” alihoji mmoja wa polisi waliokuwa nyumbani kwa Baltazar.
“Hakuna aliyeuliwa na risasi, wote inaonyesha wameuliwa kwa kukatwa, inaelekea ni watu wengi na si mmoja aliyewavamia,” Deo alikuwa nyumbani kwa Baltazar siku hiyo, alihesabu taratibu idadi ya watu wake waliokufa. Hofu ilimtawala sana. Alijua wamekwisha wote.
“John, Chacha, Shebby, Baltazar wote wameuliwa, Bwigire sijamsikia hadi sasa, nahisi labda polisi hawajasikia habari zake, huenda nimebaki peke yangu,” Deo alikosa raha, alifungua chupa yake ya mvinyo na kunywa kidogo na kuiweka tena kwenye siti ya pembeni katika gari lake. Hakutaka kushuka kwani polisi walikuwa wameingia nyumbani kwa Baltazar. Aligeuza gari na kuondoka.
*****
Bwigire aliondoka nyumbani kwake saa tano usiku. Alizima simu na kuiweka mfukoni. Hakutaka kusikia sauti ya yeyote yule. Aliingia kwenye gari na kuondoka, taswira mbalimbali zilimwandama, alijiona amekuwa mwoga kitu ambacho hakuwahi kuhisi kabla. Aliendesha gari hadi ufukweni mwa Bahari ya Hindi. Alilipaki karibu na mti mkubwa wa mnazi. Alijihisi sasa yuko salama.
Hancy na Fina waliliona gari la Bwigire kuanzia maeneo ya Posta.
“Ndio yeye, nyumba yake iko Kigamboni. Nadhani leo hatalala huko atakuwa hukuhuku,” Fina alimweleza Hancy juu ya Bwigire ambaye muda mfupi tu alipita karibu na jengo la Benjamin Mkapa.
“Atakuwa anaelekea Mwenge au?” Hancy alihoji.
“Sidhani, tumfatilie asije akatupotea,” Fina aliongea hayo huku akinyanyuka na kuchukua mkebe wake, alitoka nje ya jengo lile na kuchungulia uelekeo wa gari la Bwigire.
Hancy aliwasha gari na kumfuata Bwigire. Alimfatilia hadi alipopaki gari chini ya mti kule ufukweni.
“Amekuja kufanya nini huku?”
“Sijui Hancy, tusubiri tujue anataka kufanya nini,” Fina alimsihi Hancy.
Saa saba na nusu usiku bado waiendelea kusubiri. Hawakujua anataka kufanya nini.Bwigire alikuwa amelala, amelala usingizi mzito. Lengo lake lilikuwa kukwepa kadhia na kuhofia maisha yake. Kila alipofikiria mauaji ya rafiki zake aliogopa kukaa nyumbani. Simu alizima na hakutaka kutafutwa.
“Sitaki kupoteza muda wangu Fina, ikifika saa nane naenda kummaliza, haiwezekani saa mbili tunamsubiri hatujui anafanya nini kwenye gari.”
“Lakini alipita na gari mwenyewe, sidhani kama atakuwa na msichana ndani ya gari.
“Asituchoshe,” Hancy alitoka kwenye gari na kumfuata. Bwigire alikuwa katikati ya usingizi mzito.Alijua atakuwa amefunga kila mahali. Alijua pia atakuwa na silaha kama bastola. Aliingia chini ya gari. Alitafuta waya wa betri ya gari na kuuchomoa. Hapo sasa ilikuwa rahisi kwa Bwigire kufungua kwani aliwasha kiyoyozi na kulala. Sasa hakupata hewa ya kutosha.Alianza kuhisi vibaya.Aliamka.Cha kwanza alifungua vioo vya gari.Alipata afueni.
Saa nane kamili, Hancy alikuwa amesimama pembeni ya mlango wa gari la Bwigire. Bwigire alishtuka sana baada ya kumwona.
“Teremka chini,” amri ilitolewa na Hancy na bila ajizi Bwigire alimjibu. Fina alisogeza gari karibu ili kumulika na ajionee kinachoendelea. Ilikuwa pia ni njia ya kusaidia mwanga kumfikia Hancy.
“Unawafahamu hawa watu?” Hancy alimwonyesha Bwigire ile picha ya familia yao. Bwigire alikuwa akitetemeka sana. Alijua huo ndiyo mwisho wake.
“Ndiyo nawajua ila siyo wote, huyu hapa ni mzee Ambrose na mke wake, watoto siwajui wote.”
Bwigire alitaka kumshambulia Hancy ili atoroke lakin Hancy tayari alikuwa ameshamuwahi. Alimkata kwa panga mguuni na kumfanya ashindwe kufanya lolote.
“Tafadhali niache usiniue,” kauli hiyo haikuingia akilini mwa Hancy, haikumsaidia Bwigire kwani tayari alikuwa ameshamtenganisha kichwa. Haraka Hancy alimpiga picha na kuondoka.
*****
Deo tayari alikuwa amesikia habari juu ya kifo cha Bwigire, mmoja kati ya watu wake. Alijua ndiyo mwisho wake sasa, hakutamani kufa ila alijua lazima atakufa. Hakuwa na ajizi zaidi ya kutoroka nchi au kujisalimisha polisi.
“Siwezi kuwaruhusu polisi wanikamate,” aliwaza.
*****
Ulikuwa ni usiku wenye ladha ya kipekee kwa wakazi wengi wa Dar es Salaam. Usiku ambao si kila mmoja aliuonja kwani Ufukwe wa Coco ulioko Bahari ya Hindi ulikuwa umejaa. Hancy na Fina walikuwa wamekaa pembeni ya gari lao wakisubiria shamrashamra za Mwaka Mpya zilipuke itakapofika saa 6:00 usiku. Kelele za spika zilizokuwa zikiteremsha muziki wa nguvu ziliuteka ufukwe mzima.
Deo alifika siku hiyo, kabla ya safari yake ambayo alijua ataianza mara tu baada ya shamrashamra zile kuisha. Alijisimamia kando ya mti huku akiwa ameishikilia sigara yake iliyokuwa ikiteketea taratibu huku akiivuta mara chache sana. Mawazo ndiyo yalimfanya hadi awaze sana. Amani ilimtoweka.Hamu iliishia kwenye sigara pekee.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Saa sita kamili tayari shamrashamra zililipuka. Deo alinogewa na ufukwe. Aliona ni bora aondoke alfajiri kwani Doreen alitamani sana kuendelea kuselebuka naye.
“Usiondoke muda huu, ni usiku sana. Halafu ntashindwa kuwa na furaha peke yangu. Naomba uondoke hata alfajiri sana. Najua una maweazo lakini tuendelee kwanza.” Doreen alijitahidi kumbembeleza Deo ili aendelee kuwa naye, Deo hali ilirudi kama kawaida na kuendeleza burudani. Hakujali tena alichokiwaza juu ya muuaji.
“Hancy,” aliita Fina ambaye alisimama ghafla baada ya kumwona Deo.
“Nini Fina?”
“Yule pale Deo, ndiyo yeye.”
Hancy haraka alirudi sehemu alikokuwa amepaki gari.
“Unataka ufanye nini Hancy?” Fina aliuliza kwa mshangao.
“Hujui nataka kufanya nini?” Hancy alimuuliza Fina kwa sauti ya chini. Alitoa panga na kulishikilia barabara. Mwanga hafifu uliokuwa pale ufukweni ulimfanya asionekane.
“Siwezi kumwacha hapa, lazima nimuue.Isitoshe atakuwa ameshajua taarifa za wenzake. Nataka niwaonyeshe watu wote kwamba yote yaliyotokea ni kwa sababu yangu. Watu hawawafahamu na isitoshe waliua ndugu zangu tena kwa hili panga nikishuhudia. Leo sitakubali hata mmoja abaki. Nashukuru sana niliwafahamu wote na sasa ni kisasi juu ya ndugu zangu. Fina liwalo na liwe, hapahapa nammaliza.” Fina hakuwa na la kusema, alibaki kimya akiangalia jambo ambalo Hancy alikuwa akienda kulitekeleza.
Hancy alimfata Deo.Alimkuta akisakata rumba katikati ya watu. Ghafla Deo alijikuta akivutwa na kukutana na ngumi moja ya uso iliyompeleka hadi chini. Watu waliokuwa wakicheza karibu na Deo walirudi nyuma baada ya kuona panga, wengine walikimbia wakihofia maisha yao. Deo alikuwa chini. Hakuwa na ujanja zaidi ya yeye mwenyewe kujiokoa kwa namna ambayo angeweza.
Hancy alisukumwa ghafla na Deo. Deo akaokota chupa na kuigonga juu ya chupa nyingine na kuvunjika, alitumia kipande kile kumtisha nacho Hancy. Hancy hakutetereka zaidi ya kuendelea kumsogelea Deo. Deo alirusha chupa ile na kufanikiwa kumjeruhi nayo Hancy kifuani. Hancy hakutetereka tena. Alimsogelea Deo. Alifanikiwa kumshika mkono na kumkata mkono aliokuwa ameshikilia chupa na chupa kudondoka. Deo hakuwa na ujanja tena, Hancy alimkata tena mguu kumfanya asiweze kukimbia.
“Utauaaaa!Mwachee, Mwachee!” sauti za baadhi ya watu zilikuwa zikimsihi Hancy asiendelee kumkata Deo. Hancy aliacha na kutoa ile picha ya ndugu zake pamoja nay a rafiki zake Deo aliowaua. Alianza kumwonyesha zile picha moja baada ya nyingine.Watu wote walikuwa kimya wakiangalia kilichokuwa kikiendelea. Muziki ulikuwa umesimama ghafla na shamrashamra zikawa hazipo tena. Watu wote walihamishia macho kwa Hancy na Deo.
“Hawa ndiyo wahuni wenzako mmaojiita Kobra?” watu walisogea karibu kuziona zile picha. Alitoa picha ya ndugu zake na kumwonyesha.
“Kwa kujiona nyie ndo kila kitu hapa mjini, mliamua kuua ndugu zangu kwa tama zenu za pesa,” zimewafikisha wapi hadi sasa. Sihitaji hizo pesa mlizochukua kwa mzee Ambrose. Nlichokihitaji ni na nyie mfuate njia na namna mlivyowafupishia maisha yao.” Deo alijitutumua kujaribu kutoka lakini hakuweza.
“Haa, ni unyama waliomfanyia mzee wa watu na familia yake.”
“Huyu ndiye yule mtoto wake wa mwisho ambaye alinusurika kifo.”
“Kumbe ndiyo hili kundi lililofanya ule unyama.”
Kila mmoja aliongea lake. Polisi walikuwa wanakaribia kufika eleo walilokuwepo Hancy na Deo. Hancy hakutaka Deo aendelee kuishi kwa kuchukuliwa na polisi. Alimkata na panga hadi kuhakikisha amekufa. Sasa alijiona mshindi. Hata polisi walivyofika waliishia kuuchukua mwili tu. Hancy alishikiliwa kwa ajili ya mahojiano na polisi.
*****
Van Brussel alikuwa nje ya kituo cha polisi cha Buguruni. Alikuwa amefika kwa ajili ya kumwekea dhamana Hancy. Hakujua kama Hancy alikuwa ameshaachiwa huru ila alikuwa bado ndani ya jengo akichukua baadhi ya vitu vyake ambavyo alikuwa navyo wakati akipelekwa kituoni hapo. Alifurahi sana kumkuta Van Brussel nje akimsubiri.
“Wewe ni shujaa,” Van Brussel alimwambia Hancy kwa lafudhi ya kizungu. Hancy alicheka. Nyuma yake alikuwa Fina ambaye alikuwa amebeba begi liliokuwa na vitu vya Hancy.
“Tutayaongelea nymbani,” alimalizia Hancy huku akiingia ndani ya gari.
“Sasa Hancy, nipishe mimi niendeshe,” alisema Van Brussel huku akimfungulia Hancy mlango wa abiria na yeye kuingia mlango wa dereva. Hancy alifanya kama alivyosema Van Brussel na baada ya dakika kumi walikuwa nyumbani kwa Hancy.
Walipumzika baada ya kuoga na kula. Wakiwa wamepumzika sebuleni, Hancy aliwasha Tv na kuanza kuangalia. Ghafla aliona picha yake ikiwa katika TV, aliwahi na kuongeza sauti.
“Hancy ambaye alinusurika kufa kipindi akiwa mtoto mdogo wa miaka minne, alifanikiwa kulipa kisasi cha mauaji ya ndugu zake, alitaka kuliangamiza kundi hilo lililojiita Kobra na pia kuwaonyesha wananchi juu ya watu hao. Aliamua kufanya mauaji hayo usiku wa saa nane kama ilivyotokea kwa ndugu zake ambao waliuliwa mnamo saa nane Usiku. Pia alisema kwamba asingeweza kuona watu wale wakiendelea kuishi kwani kila mara alikuwa akiona sura zao usoni na kumkumbusha siku walivyofanya mauaji nyumbani kwao…” CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Pole Hancy, wewe ni shujaa, umekamilisha ndoto zako,” Hancy alitabasamu baada ya kusikia taarifa zile jambo ambalo lilimfanya Fina amkumbatie na kumbusu kwa furaha huku Van Brussel akichungulia taarifa iliyokuwa bila kuelewa lililosemwa.
MWISHO
0 comments:
Post a Comment