Simulizi : Wivu
Sehemu Ya Tano (5)
John aliteremka kutoka kwenye teksi iliyokuwa imesimama sawia kwenye mlango unaoingia moja kwa moja ndani ya jengo la hoteli ya Masai Shield. Teksi ikaondoka na yeye akageuka kuangalia mlangoni. Wahudumu wawili wenye sare za kazi wanaopokea wateja waingiao, walikuwa wamesimama ndani ya mlango wa kioo unaojifungua wenyewe pindi unapokaribiwa na mtu anayetaka kuingia au kutoka. Wote walimwona John alivyoteremka kwenye teksi na wakawa wanamwangalia.
Mara tu mlango ulipojifungua, John akaisikia harufu nzuri kutoka humo ndani; ni harufu ya aina moja ambayo duniani kote utakumbana nayo mara tu ukiingia kwenye hoteli za kifahari kama hizo. Alipokuwa akiingia aliwasalimia watu wale na wote waliitika kwa nidhamu na kumkaribisha.
Mteja ni Mfalme! John aliwaza baada ya wahudumu wale kumuinamishia vichwa wakati walipokuwa wakisalimiana. Ilikuwa ni mara yake ya kwanza kuingia kwenye hoteli hiyo ingawa alikuwa akiiona na kuipita kwa mbali wakati wa siku za nyuma alipokuwa akija Arusha. Aliingia ukumbini kulikokuwa na mandhari ya kupendeza iliyokuwa ikimulikwa kwa taa zenye nuru hafifu ambayo miali yake ilichomoza kutoka kwenye matundu madogo na membamba yaliyopo kwenye dari iliyonakshiwa kwa ujenzi wa kisanii.
Kwenye ukumbi huo ambako kulikuwa na ukimya uliovunjwa na mziki mororo wa ala tupu uliosikika kwa sauti ndogo, eneo hilo lilikuwa na sofa za kupendeza ambazo baadhi zilikuwa zimekaliwa na wateja; wengi wao wakiwa ni Wazungu. Pia kulikuwa na matangazo ya huduma mbali mbali yaliyokuwa yakiwaka kwa kunakshiwa na taa za rangi kwenye baadhi ya kuta zilizomo humo ndani. John akaliona eneo alilokuwa akilihitaji; eneo la mapokezi ambalo lilikuwa lipo mbele yake. Kwenye meza ndefu iliyojengwa kwa muundo wa upinde kulionekana baadhi ya wateja waliokuwa wakihudumiwa na wafanyakazi watatu wa idara hiyo mapokezi. Wafanyakazi wote watatu walikuwa ni wasichana warembo wenye sare za kazi zilizofanana.
John alikwenda kusimama kwenye meza hiyo na kusubiri mmoja wa wafanyakazi hao amaliziane na baadhi ya wateja waliokuwepo hapo. Akapatikana mmoja aliyemwendea John.
“Karibu; nikusaidie nini?” msichana huyo wa mapokezi alimwambia John kwa lugha ya Kiingereza.
“Nataka kuonana na mgeni wangu, kati ya Richard Ken au Dina,” John alisema kwa kujiamini kwa kutumia lugha ya Kiingereza ambayo hakuwa na umahiri nayo sana.
Msichana akainua simu na kupiga, akaonekana kusikilizia kwa makini. Akairudisha.
“Hawapo chumbani, nadhani watakuwa restaurant wakila chakula cha jioni,” msichana alisema.
Hawapo chumbani! John alishangaa.
“Naweza kwenda kuwaona? Mimi ni mfanyakazi mwenzao,” alisema na kujaribu kuificha taharuki aliyoipata.
“Unaweza kwenda kuwaona,” msichana alisema na kuonyesha kumalizana na John, akataka kuondoka kwenda kuhudumia mteja mwingine aliyefika hapo ambaye alikuwa ni Mzungu.
“Unaweza ukanielekeza? Siijui restaurant yenu ilipo,” John aliwahi kusema kabla msichana yule hajaondoka.
Msichana akamwelekeza. “Ahsante,” John alisema.
“Unakaribishwa!” msichana alisema na kuonyesha tabasamu bandia la kikazi kisha akamfuata yule mgeni akiyekuwa amewasili.
Pamoja na kuwa alitarajia kitu kama hicho kingeweza kutokea, lakini ule ukweli uliojitokeza kutokana na kauli ya yule msichana wa mapokezi kutoa kauli iliyoonyesha kuwa, Richard na Dina hawakuwepo chumbani, ilimdhihirishia John kwamba, Richard na Dina walikuwa wakikaa kwenye chumba kimoja, ikawa kama vile jambo hilo hakuwahi kulifikiria kabla!
Udhihirisho huo uliomdhihirishia kuwa Richard na Dina walikuwa wakitumia chumba kimoja ulimchanganya. Hasira na wivu vilimjia kwa wakati mmoja na alijishangaa jinsi alivyoweza kujizuia mbele ya yule msichana kutoonyesha kuchanganyikiwa alikokupata. Mapigo ya moyo wake yalikuwa yakimwenda mbio wakati alipokuwa akielekea katika lifti itakayompeleka kwenye ghorofa ulipo mgahawa ambako ndiko alikoelekezwa waliko Richard na Dina. Mkanganyiko uliokuwa kichwani mwake ulimfanya alijihisi kutamani kumuua yeyote kati ya Dina au Richard! Akili yake ilimtuma kutoukubali uzoba aliokuwa akifanyiwa na watu hao.
Akiwa amesimama nje ya mlango kuisubiri lifti iwasili, John alirudia kama mara mbili au zaidi kushusha pumzi za hasira kama vile afanyavyo mtoto mwenye hasira aliyetoka kulia kwa ghadhabu. Alijaribu kuituliza akili yake na kujihisi kama anayeshindwa kuidhibiti. Subira yake ya kuisubiri lifti ilimfanya asitulie sehemu moja, alizunguka huku na kule na kuiona lifti hiyo ikichukua masaa kadhaa kuwasili. Lifti ikawasili, akaingia.
Lifti ilimchukua na kwenda kusimama kwenye ghorofa yenye mgahawa. John alitoka akiwa na baadhi ya wateja wengine waliokuwa wakienda kula kwenye mgahawa aliokuwa akielekea. Yeye na wale wateja kwa pamoja walikaribishwa na msimamizi wa huduma za mgahawani.
“Nataka kuonana na Richard Ken, nimeambiwa yuko huku anakula,” John alimwambia mkuu wa mgahawa aliyekuwa ameanza kumwonyesha meza ya kwenda kukaa.
* * * * *
“Yesu wangu!” Dina alisema na papohapo kuonyesha kushituka wakati uso wake akiwa ameuelekeza mlangoni ambako wateja walikuwa wakiingia.
“Kitu gani?” Richard aliuliza na kuangalia alikokuwa akiangalia Dina. Akaonekana kutokigundua kilichokuwa kimemshitua Dina. “Vipi?” aliuliza tena huku akiurudisha uso wake kumwangalia Dina.
Dina alikuwa bado akiangalia mlangoni, kisha kwa sauti ndogo kama vile alikuwa anaongea peke yake akasema kwa kifupi, “John!”
Ndipo Richard akapata mshituko ulioungana na kitendo cha kuangalia tena mlangoni. Kauli yake ikapotea baada ya kumwona mkuu wa mgahawa akimwonyesha John mahali walipo!
John akawa kama aliyezubaa huku akiangalia upande walipo Richard na Dina.
“Wacha nimfuate kule kule!” Dina alisema ghafla na kuinuka. “Mwache aje hapa hapa!” Richard alisema na kumzuia Dina kwa
kumshika mkono. Richard alishaingiwa na wasiwasi kunaweza kukatokea patashika kati ya Dina na John endapo wangebaki peke yao na ndio sababu ya kumzuia Dina. Lakini pia alikifanya kitendo hicho kwa sababu alikuwa akijiamini kupigana, aliwahi kuchukua mafunzo ya karate wakati alipokuwa akisoma Uingereza. Hata hivyo alishakuwa na zaidi ya miaka miwili tokea aliposimama kuendelea na mafunzo hayo na hakuwa na mazoezi ya aina nyingine yoyote tokea alivyorudi nchini, hata hivyo aliamini angeweza kumdhibiti John asimfanyie fujo yoyote Dina kama angewafuata hapo.
“Niache nikazungumze naye,” Dina alisisitiza kwa kujiamini. Richard akamuachia! Dina akaondoka na kuharakisha kwenda
kumkabili John kabla hajaingia eneo la ndani zaidi la mgahawa lenye wateja waliokuwa wakila chakula.
Akiwa amesimama huku akimwangalia Dina aliyekuwa akimjia, John alishindwa kuamini kama anayemwona hapo alikuwa ni Dina yule yule aliyekuwa akimlia viapo vya uaminifu. Alijiona kama aliyekuwa akimwangalia Dina mpya mwenye uzuri ulioongezeka ghafla kiasi kwamba hata baadhi ya wateja waliokuwemo humo mgahawani walikuwa wamegeuka kumwangalia.
Dina alipokuwa akielekea kule alikosimama John, hatua zake ziliufanya ule mkufu wa dhahabu wenye kito cha thamani aliouvaa shingoni, kidani chake kichezecheze na kutoa miali ya kung’ara kila kilipokuwa kikitikisika kifuani kwake, na wakati huo huo hereni za dhahabu zilizokuwa mfano wa bangili kubwa nazo zilikuwa zikiyumba masikioni mwake wakati akitembea. Mwonekano wa Dina ulimfanya John apigwe na ganzi huku akishindwa kuamini kama yeye ndiye mmiliki wa mapenzi wa msichana huyo anayekuja mbele yake. Akili yake ilikuwa imepumbazwa na uzuri wa binti huyo aliyeonekana kuwa kwenye daraja la juu la kimaisha. Hasira iliyokuwa imemvaa wakati akiwasili hapo ikaanza kunywea taratibu!
Ghafla akaiona fahari ya kummiliki msichana mzuri wa aina hiyo, tukio hilo likamfanya akumbuke kuwa ni msichana huyo ndiye anayemfanya aingie kwenye ushindani wa kumgombania kati yake na Richard! Na ndiye aliyekuwa akimhangaisha kwenda kwa waganga kwa ajili yake ili afanikiwe kumrudisha kwenye himaya yake!
Siwezi kumuachia Richard! aliapa ghafla. Akayakumbuka madawa aliyojipaka usoni kuwa yalikuwa na uwezo wa kuipumbaza akili ya Dina pindi atakapoangaliana naye machoni! Na hicho ndicho kilichomleta hapo Arusha; aje amchukue na kurudi naye Dar es Salaam!
“Vipi?” Dina aliuliza alipomkaribia John huku sura yake ikiwa kwenye mshangao na nusu kwenye kuchanganyikiwa.
Kitendo cha Dina kumwangalia sawia John kwenye macho yake wakati alipomwuliza swali hilo, ndicho John alichokuwa akikihitaji. Alihitaji Dina ayaangalie macho yake kwa kuamini madawa aliyojipaka ndipo yatakapofanya vyema kazi yake. Na yeye akayatuliza macho yake machoni mwa Dina na kupoteza sekunde kadhaa kama sehemu ya kukoleza ufanyaji kazi wa dawa hizo kabla ya kulijibu swali la aliloulizwa.
“Nimekufuata turudi Dar es Salaam!” John alisema baada ya kujitosheleza na muda alioutumia kuangaliana na Dina, na hata aliposema hivyo, alisema kwa kujiamini. Akatarajia Dina angegwaya.
Lakini badala ya kugwaya, Dina akashangaa!
“Hebu njoo huku!” alimwambia John kwa sauti ya upole lakini yenye amri. Alikuwa akijielewa jinsi anavyoweza kumdhibiti John na alikuwa na uhakika John angefuata alichosema.
John akamfuata! Wakaenda ulipo ukumbi wa baa, wakakaa kwenye sofa. Mhudumu akafika muda huo huo na kuwauliza wanachohitaji kunywa.
“Utakunywa nini?” Dina alimwuliza John.
John akazitambua fikra za Dina kuwa zipo kwenye kumwongoza kama alivyokuwa amezoea siku zote. Kwa kuwa na yeye alikuja hapo kwa imani ya kuleta mapinduzi ya kuyageuza mazoea hayo kwa kuamini dawa alizojipaka, akaona sasa ilikuwa zamu yake kuchukua utawala wa kumtawala Dina kimapenzi.
“Sihitaji kinywaji chochote Dina!” John alisema kwa sauti aliyotaka Dina aione ni amri.
“Nimekuja kukuchukua turudi zetu Dar! Kwa hiyo tuondoke!”
Dina akatengeneza tena mshangao usoni na kumwangalia John. “John umelewa?” aliuliza kwa kujiamini na kuonyesha kiburi kidogo kwenye sauti yake ili kuonyesha ni yeye ndiye mwenye turufu ya utawala wa kumtawala John.
“Ni mzima na akili yangu!” John alijibu kifedhuli huku mikono akiwa ameituliza juu ya magoti yake. Ghafla akajiona ana nguvu za kupambana na Dina kimazungumzo, akaamini dawa alizopewa na mganga zilikuwa zikimpa nguvu hizo!
Jibu la John likamfanya Dina amwangalie mhudumu aliyekuwa bado amesimama akisubiri maagizo.
“Nikikuhitaji nitakuita,” alimwambia mhudumu kwa lengo la kumwondoa.
Mhudumu akaondoka.
“Umekuja kunichukua wakati unajua nimekuja huku kikazi?” Dina alimwuliza John kwa utulivu baada ya mhudumu kuondoka.
“Nimeamua! Kwa hiyo tunaondoka pamoja hadi hotelini nilikofikia!” John alisema kwa sauti yenye ushari.
“Na kesho asubuhi tunarudi Dar es Salaam!”
Dina hakujibu haraka. Alitulia kwa sekunde chache huku akimwangalia John kwa dalili zile zile za mtu aliyemzoea huku akionekana kama anayetaka kuisoma akili ya John.
“Unajua John sikuelewi!” alisema na safari hii sauti yake ilikuwa na ukali fulani.
“Hunielewi kwa sababu lugha niliyoizungumza huijui? Au hunielewi kwa lipi?” John aliuliza.
Hata hivyo, John alikuwa ameanza kushangazwa kumwona Dina akiwa bado anaonyesha aina fulani ya ubishi. Alitarajia Dina hadi muda huo angekuwa tayari amekwishapumbazwa na dawa alizojipaka na angekuwa anatii kila analoelezwa. Alitarajia endapo Dina kama angetokea kuhoji, basi angehoji maswali madogo madogo yasiyoashiria aina yoyote ya kuleta ubishi; lakini mwonekano uliokuwepo hapo ulianza kuwa tofauti na matarajio hayo. Dina alikuwa bado akionyesha kuwa na akili zile zile za utawala dhidi yake! John akaanza kuuhoji uwezo wa dawa alizojipaka kama zilikuwa na uwezo wa kumbadilisha Dina.
“Utakujaje ghafla bila ya kuniarifu?” Dina aliuliza kwa sauti iliyoonyesha kukerwa na kuonekana joho la utawala wa kumtawala John likiwa bado maungoni mwake.
“Halafu kufika tu unaniambia umekuja kunichukua unipeleke hotelini kwako! Hakuna kunisalimia, hakuna kuulizana! John umechanganyikiwa?”
“Nadhani nina haki ya kukwambia hivyo! Dina, mimi ni mchumba wako!” John naye alisema kwa ukali wa kujibu mapigo.
Dina akatoa kicheko kidogo cha dharau.
“Haki ya kunikokota unavyotaka? Bado hujawa na haki hiyo John!’ alisema kwa utulivu huku akitingisha kichwa chake kuonyesha kusikitika. “Hata mahari yenyewe hujanilipia unaanza kusema hivyo! Je, ukinioa itakuwaje?”
John akamkumbuka mama yake Dina na kauli hiyo ya mahari. Akanywea kiaina, lakini akajipa matumaini ya kuyatawala mazungumzo hayo. Bado alikuwa akiamini dawa zake zingefanya kazi.
“Lakini mimi bado ni mchumba wako Dina!” alisema kwa ajili ya kuendeleza ligi ya ubishi. “Kuna makosa gani kukwambia hivyo?”
“Najua kuwa ni mchumba wako, lakini ndio uamue kunifuata huku Arusha bila ya kunifahamisha kama unakuja?” Dina alisema, kisha ghafla akaonyesha kukerwa na kitendo hicho.
“Kwa nini hukuniambia kama unakuja wakati mchana wa leo tulizungumza kwenye simu? Ulikuwa na mawazo gani kichwani mwako? Huniamini? Lengo lilikuwa ni kunifumania?”
John akapigwa na butwaa! Lakini halikuwa butwaa lililoletwa na kauli hiyo kali ya Dina; bali lilitokana na kule kutomwona Dina kutokuwa na dalili za kulainika! Alijiona bado akizungumza na Dina yule yule ambaye siku zote yuko juu yake.
“Kwa hiyo hatutakwenda hotelini nilikofikia?” John aliuliza swali ambalo alikuwa na uhakika sio jibu la swali aliloulizwa.
“Nakuomba kitu kimoja John!” Dina alisema kiukomavu na kumwangalia John machoni. “Naomba urudi Dar! Kama unalo lolote la kuniambia hata kama nimekuudhi, basi unisubiri hadi nitakapokuja Dar. Samahani kwa kukwambia hivyo, lakini sikudanganyi John; kweli umeniudhi!”
John akapoteza mhimili wa kujizuia, akaonyesha kuanza kuchanganyikiwa. Alizirudisha nyuma nywele zake kwa kuzisukuma na vidole vyake vya mkono. “Dina, bado unanipenda?” aliuliza huku akiwa amekiegesha upande kichwa chake. Swali lake halikuulizwa kimahaba, lilikuwa na aina ya ushari.
“John bwana! Maswali gani hayo unayoniuliza?”
John akagundua alikuwa akipoteza muda kusubiri nguvu za dawa alizojipaka zifanye kazi. Yule mshenzi amenitapeli! aliwaza. Akaachana na mawazo hayo ya kishirikina ambayo yalikuwa yamemjengea subira kwa wakati wote. Akairudisha akili yake kwenye uhalisia wa jambo analokabiliana nalo kuwa, Dina na Richard walikuwa wanalala chumba kimoja humo hotelini! Na isitoshe pia, amewafumania wakiwa kwenye meza moja wakila chakula wakionekana dhahiri ni wapenzi!
Wivu ukarudi upya na subira ikamtoka!
“Mimi najua kila kitu Dina! Usifikiri miye zoba!” John alibwata huku akionekana kuchachamaa ghafla. “Nina habari zenu zote kuhusu wewe na yule mshenzi wako uliyekuwa naye pale mezani!” alisema na kunyoosha mkono kuelekeza upande uliko mgahawa ambako yuko Richard.
“Kwa taarifa yako, najua kama ulisafiri naye kwenye ndege moja! Isitoshe vilevile, najua kama unalala naye chumba kimoja!” alinyamaza na kutweta huku macho yake yakitambaa mwilini mwa Dina.
“Ni nini kilichokubabaisha Dina? Au ni hiki kijiguo pamoja na hizi dhahabu alizoanza kukununulia? Hukuwanavyo hivi wakati ulipoondoka Dar! Uwongo? Kwa muda huu mfupi wa kuja hapa Arusha tayari umeamua kunisaliti? Umeisahau ahadi uliyoniahidi kuhusu huyu jamaa? Umesahau kama uliapa Miungu yote kunihakikishia kuwa hutotembea naye? Umesahau yote niliyokutendea? Umesahau tulikotoka? Unanifanyia haya ukiwa na pete yangu ya uchumba kidoleni mwako Dina?”
Dina aliganda. Akaonekana kama mlemavu asiyeweza kuzungumza. Alikuwa amenywea kama aliyenyeshewa. Akaonekana kama sanamu lenye kupepesa macho. Kiburi na kule kujiamini kukatoweka. Aligwaya!
John alikuwa tayari ameghadhibika!
“Tunaondoka pamoja kwenda hoteli nilikofikia!” alisema na kuukamata mkono wa Dina.
Dina akaufyetua mkono wake kutoka mkononi mwa John.
“Bwana tutakuja kuongea Dar!” Dina alisema na kuonekana kurejewa na fahamu. Akasimama kutaka kuondoka.
John akawahi kumzuia Dina kwa kumshika tena mkono.
“Huwezi ukazungumza na mimi halafu ukataka kuondoka kienyeji, rudi kwenye kiti!” alisema kwa sauti ndogo kujaribu kuwafanya watu wasifuatilie kinachoendelea hapo.
Dina akanywea tena, safari hii macho yake yakawa yameingia woga! Na yeye naye akazungukwa na kiwingu cha hofu kama ya mwenzake ya kuogopa watu wasilifuatilie tukio lao. Akarudi kwenye sofa.
“Mimi nazungumza na wewe halafu unaondoka!” John alisema,
munkari ulikwishaanza kumpanda. “Sasa mimi nakwambia, kwa yule mshenzi wako hurudi! Na utaondoka na mimi!”
“John mimi nipo kazini! Sasa mambo gani haya unayonifanyia? Utaniharibia kazi…” Dina alilalamika kwa sauti ya kujitetea, alikuwa hajawahi kumwona John akiwa katika hali ya hasira kama anayomwona nayo hapo na hali hiyo ilianza kumwogopesha.
“Kazi ya kuja..!” John alitaka kutukana, lakini na yeye akashindwa kumalizia alilotaka kulitamka. “Nitakutukana Dina!” alisema kwa hasira. “Sijawahi kukutukana hata mara moja! Tafadhali Dina!”
Dina hakujibu!
John akasimama.
“Twende!” alisema kwa jazba. Dina hakujibu wala hakuinuka!
Hasira na wivu vikampagawisha John! Akamuinamia Dina na kuukamata mkono wake karibu na kwapa, akaanza kumuinua kwa nguvu. “Nadhani ulikuwa hunijui!” alisema na kuanza purukushani ya kumvuta Dina ambaye alikuwa akigoma kuinuka.
Tukio hilo likaanza kuwavutia wateja na wafanyakazi waliokuwepo eneo hilo. Wahudumu wawili wa kiume wakaenda eneo walilokuwepo Dina na John, wote kwa pamoja wakamvaa John ili amwachie Dina huku wakimsihi aache vurugu. Kitendo hicho kikamfanya Dina apate upenyo wa kuchomoka. Akafyetuka kama mtego ulioteguka, akakimbia kurudi mgahawani alikomuacha Richard!
John alikuwa mtu wa kufanya mazoezi mara kwa mara hasa ya kuogelea na kukimbia, akatumia nguvu za kushitukiza kuwasukuma wahudumu wale wawili waliokuwa wamemzuia na kuwabwaga chini. Akaitumia nafasi hiyo kumkimbiza Dina aliyekuwa nusu anakimbia nusu anatembea!
* * * * *
Richard alikuwa amekosa amani muda wote tokea Dina alivyokuwa ameondoka. Aliwaona Dina na John wakiongozana kuelekea ulipo ukumbi wa baa na kupotea machoni kwake, tokea wakati huo kukawa na ukimya! Alikuwa na uhakika, John alikuja hapo Arusha ghafla kwa kushitukiza na alikusudia kumshitukiza Dina. Hakujua ni nini kilichomleta ghafla, lakini alihisi huenda kuna kidudu mtu aliyemvujishia mahusiano yake na Dina yalivyo hapo Arusha.
Hakutaka Dina akakabiliane na John kama Dina alivyokuwa amesisitiza wakati John alipokuwa ameingia hapo mgahawani. Alikuwa na wasiwasi Dina asingekuwa salama kuwa peke yake na John. Kitendo hicho cha kuondoka pamoja na kwenda kuzungumzia baa na ukimya uliokuwa unazidi kuendelea kukamfanya akose amani. Kuna kipindi alijikuta alishawishika kutaka kumtuma mhudumu wa humo hotelini ili afuatilie nyendo za watu hao wawili, kisha aje kumripotia. Lakini alijikuta akikwama kuutekeleza uamuzi huo kwa hofu ya kuruhusu watu wengine waingilie mambo yasiyowahusu.
Wasiwasi aliokuwa nao kuhusu Dina aliyekuwa mikononi mwa John akiwa peke yake, ulimfanya ajikute akiinywa pombe ya mvinyo kwa kasi iliyomshitua hata yeye mwenyewe. Aliliona jukumu la kumtetea na kumlinda Dina lilikuwa ni lake endapo John ataamua kufanya lolote la kumdhuru. Kwa hiyo, kitendo cha kuendelea kuwepo hapo akiendelea kumsubiri Dina arudi kikawa kinamtia kwenye hali hiyo ya kupoteza umakini wa unywaji wake. Ghafla akawaona wateja waliokuwa wakiendelea kula chakula humo mgahawani walioko upande ambao wanaliona eneo la ukumbi wa baa, wakigeuza sura zao kwa mpigo na kuliangalia eneo hilo.
Richard akatambua kuna walakini unaotokea kati ya John na Dina!
* * * * *
Hakusubiri! Richard aliinuka na kuanza kujitoa katikati ya meza na kiti alichokuwa amekalia. Akawaona wahudumu wakitaharuki, kisha wote kwa pamoja akawaona wakielekea eneo la baa. Tukio hilo likamfanya Richard afanye papara ya kutoka, na alipokuwa akitoka miguu yake ikakisukuma kiti kilichokuwa nyuma yake, kikapiga mwereka na kutoa sauti ya kuanguka. Akiwa hajali tukio la kuangusha kiti kutokana na akili yake kutekwa na kule watu wanakoangalia ambako ndiko waliko Dina na John, ghafla akamwona Dina akitokeza huku akikimbia kumfuata kule aliko! Baadaye akafuatia John aliyekuwa akimkimbiza Dina! Richard hakufikiri mara mbili, alijua Dina yuko hatarini na lilikuwa jukumu lake kumtetea. Akachomoka, lakini hakumfuata Dina!
Alimkabili John!
Wakavaana katikati kama fahali wawili wenye hasira. Wakashikana na kuzoana kimzobemzobe, wakaangushana kwa kishindo kwenye meza iliyokuwa jirani yao ambayo ilikuwa haina wateja. Nyenzo za kulia chakula zilizokuwa zimepangwa kwenye meza hiyo zikaanguka kwa kishindo cha kelele na kutawanyika chini. Hali ya vurugu ikawa imetawala kwa watu hao wawili. Wote walikuwa wameangukia sakafuni na kila mmoja akitaka kuwahi kuinuka kabla ya mwenzake. Wakakikirishana huku kila mmoja akionyesha misuli yake, lakini akawa ni Richard ndiye aliyewahi kutupa ngumi iliyompata John kwenye paji la uso. John alisukumwa chini na nguvu ya ngumi hiyo, Richard akawahi kupanda juu ya mwili wa John ambaye alianza kutoka damu sehemu aliyopigwa ngumi na kuanza kuikaba shingo ya John kwa mikono yake huku akitumia nguvu zote, kama vile alipania kumuua!
Wahudumu ambao walikuwa wakipiga kelele ya kutaka walinzi wa hoteli waitwe, walikwenda kwa pamoja kwenye ugomvi uliokuwa ukiendelea huku Richard akionekana amemdhibiti vyema John katika ile hali ya kumkaba koo. John akaonekana anapoteza nguvu!
“Mtoeni anamuua mwenzake!” kelele za wahudumu na wateja hasa wanawake zilisikika zikihimizana. Baadhi ya wahudumu wa kiume wakamvamia Richard na kuanza kumvuta kumwondoa kutoka mwilini mwa John na kufanikiwa kuwaachanisha. Kitendo hicho cha kuwaachanisha kikampa nafasi John ya kuokota kisu kabla ya Richard hajapata mhimili mzuri wa kujiinua. Kilikuwa kisu cha kulia chakula kati ya nyenzo zilizokuwa zimeeanguka chini, John akazitumia nguvu zake zote kumchoma kisu hicho Richard sehemu ya ubavuni!
Richard alipiga ukelele na kuangukia ubavu uliochomwa kisu na kukishikilia kisu hicho kilichojikita ubavuni mwake. Wakati huohuo damu ikachukua nafasi yake kutoka! Tukio hilo liliwachanganya watu wote waliokuwepo eneo hilo, sura zilizohamanika kwa hofu na taharuki iliyowatawala mioyoni mwao wakaonekana kuanza kuhaha kutafuta eneo la kukimbilia. Baadhi yao wakakimbilia kwenda kusubiri lifti.
Wakati vurugu za kila mmoja aliyekuwepo hapo akisema lake, John aliinuka na kuokota kisu kingine. Uso wake uliopigwa ngumi ukiendelea kuchirizika damu kwenye sehemu iliyopigwa, alianza kutamba kwa kuzunguka kama Sokwe na kuonekana kupagawa. Sura yake iliogofya, macho yake yaliyotapakaa damu aliyokuwa akijaribu kuifuta mara kwa mara kwa kutumia eneo la mkono karibu na bega lake yalionekana kuingiwa na woga. Akaanza mkwara wa kuwatisha kuwachoma kisu wateja wa hoteli waliokuwa wamesimama mbele yake. Wateja hao wakaanza kurudi nyuma huku wakitoa nafasi ya kumpisha John apite.
Kelele za kushakiziana zikaanza, “Jamani mkamateni anakimbia huyo!”
John alikuwa bado akitamba na kisu chake mkononi, aliupindisha mgongo wake kama anayepigana miereka. Alikuwa na mwonekano wa kutisha, alikuwa kama mwendawazimu aliyepandwa na kichaa, aliyazungusha macho yake yaliyoonekana kuwa makubwa ghafla, akawa kama aliyekuwa akitafuta kimbilio. Akawaona baadhi ya wateja waliokuwa wakiwahi kuingia kwenye lifti kulikimbia eneo hilo. Naye akatimua mbio kuelekea huko huko kwenye lifti!
Kelele za taharuki zikasikika! “Huyo anakuja!”
Watu waliokuwa wamekwishaingia ndani ya lifti ambayo ilikuwa haijafunga mlango wakapagawa walipomwona John akikimbilia kwenye lifti walipo wao!
“Jamani huyo anakuja!” kelele za kutaharuki zilisikika kutoka ndani ya lifti.
Lifti ikaonekana sio tena sehemu ya kujiokoa! Vurugu mechi za kila mmoja kutaka kuwahi kutoka kwenye lifti zikaanza kuleta tafrani. Wengine waliowahi kutoka wakajikuta wakiangukia mlangoni kutokana na kihere cha kumkwepa mtu waliyekwishamhesabia kuwa ni mwendawazimu. Baadhi yao walioshindwa kujiinua kwa haraka waliamua kutambaa kwa magoti kumkwepa John aliyekuwa akielekea kwenye lifti. Ndani ya sekunde zisizozidi tatu, lifti ikawa haina mtu hata mmoja!
Mlango wa lifti ukaanza kujifunga, John akawahi kuuzuia kwa kutanguliza mguu na mkono wake. Akaingia! Lifti ikajifunga mlango, watu waliokuwepo kwenye ukumbi huo wote kwa pamoja wakajikuta wakiuangalia mshale uliopo juu ya mlango wa lifti ukionyesha lifti ilikuwa ikishuka chini!
Eneo la mapokezi lililopo chini nako kukawa na sintofahamu ya habari za kutatanisha zilizowafikia kuhusu rabsha inayoendelea mgahawani, habari zikapokewa kwa mitazamo tofauti na kuwaletea mkanganyiko watu waliokuwepo huko. Kila mmoja alisema lake baada ya mwito wa haraka wa kutakiwa walinzi wa hoteli wawahi kwenda eneo hilo. Taarifa hizo zikawakurupua baadhi ya walinzi waliokuwepo kuwahi kwenda mgahawani kwa kutumia ngazi badala ya lifti ambayo ilionekana kuchelewa kufika chini.
Lifti aliyokuwemo John ilifika chini na kupishana na wale walinzi walioamua kutumia ngazi. Mlango ulifunguka na watu waliopo pale wakamwona John akitoka akiwa ameshika kisu mkononi huku akiwa na damu usoni na mkononi. Taharuki ikawafika, kila mmoja akatoa njia kumpisha John aliyekuwa akikimbia kuelekea mlangoni huku akitishia kumchoma kisu yeyote aliyekuwa mbele yake!
Mlango wa kioo ukajifungua wenyewe baada ya John kuukaribia, akatoka nje huku wafanyakazi na baadhi ya wateja wakishangaa kumwangalia akitokomea!
***
DINA alikuwa amechanganyikiwa! Hali hiyo ikawa inamzidia kila alivyokuwa akimwangalia Richard aliyekuwa amelala sakafuni huku akiwa amezungukwa na watu. Wakati huo huo mtu mmoja aliyekuwa amepiga magoti kando ya mwili wa Richard alionekana akitoa huduma ya kwanza kujaribu kuizuia damu kwa kumuwekea nguo sehemu yenye jeraha la kisu.
Meneja wa hoteli ambaye aliwasili muda mfupi baada ya John kufanikiwa kutoroka bila ya kukamatwa, aliwahakikishia baadhi ya wateja na wafanyakazi waliokuwepo eneo hilo kuwa, gari la wagonjwa lilikuwa lipo njiani baada ya kulipigia simu kulihitaji. Walinzi wachache wa hoteli waliowahi kufika kabla ya John hajawahi kutoroka na lifti, nao walikuwa wakishutumiwa kwa kushindwa kumzuia John alipokuwa akitoroka kwa kutumia lifti. Lakini wao walikuwa wakijitetea kuwa, mazingira yaliyokuwepo hayakuwawezesha kuweza kumkabili John, dai lao kubwa likiwa; hali aliyokuwa nayo John ilikuwa sio hali ya kumvamia bila ya kuwa na silaha, vinginevyo angeweza kumjeruhi mtu mwingine au pengine hata kuua!
Gari la wagonjwa liliwasili pamoja na gari la Polisi. Wahudumu wa gari hilo waliingia na machela, moja kwa moja walimchukua Richard na kumwingiza kwenye gari la wagonjwa ambako walichukua kifaa cha hewa ya oksijen na kukipachika eneo la usoni mwa Richard na kuondoka naye kumwahisha hospitali. Polisi waliowasili walipewa maelezo ya haraka kutoka kwa mashuhuda, hususan wafanyakazi wa hoteli waliokuwepo eneo hilo wakati wa mtafaruku huo ulipotokea.
Dina akawa mlengwa namba moja wa kuisadia polisi, wakaondoka naye kumpeleka kituoni!
* * * * *
Mara tu baada ya kufanikiwa kutoroka kutoka hoteli ya Masai Shield, John aliitumia nafasi hiyo kujipa huduma ya kwanza ya kuizuia damu iliyokuwa ikimtoka usoni kwa kuikandamiza kwa nguvu sehemu yenye jeraha kwa kuitumia leso yake hadi damu hiyo ilipoacha kutoka. Akajifuta baadhi ya sehemu zilizoingia damu na kufanikiwa kwa kiasi kidogo kuiondoa damu yote, kisha aliivua saa yake ya mkononi na viatu alivyokuwa navyo, vyote akavitupa kwenye kichaka cha eneo la kichochoro alichokuwepo. Baada ya kujiridhisha na hali aliyokuwa nayo, akajitokeza barabarani na kukodi teksi iliyomrudisha hotelini kwake.
Alipoingia hotelini, mwonekano aliokuwa nao ulimwogopesha mfanyakazi wa mapokezi aliyekuwa zamu.
“Vipi?” mfanyakazi huyo aliuliza huku akionyesha dhahiri alikuwa ameshituka.
“Nimevamiwa na wahuni!” John alimlalamikia mhudumu huyo. “Wapi?”
“Maeneo ya huko mitaani,” John alisema na kuzuga kuelekeza mkono wake upande hewa anakokuzungumzia. “Walinivamia kwa nyuma, wamenipiga na kuninyang’anya pesa na vitu vingine!”
Mfanyakazi wa mapokezi akaiangalia miguu ya mteja wake na kumwona hana viatu.
“Wamekupora na viatu?” aliuliza kama vile viatu ndio vilikuwa muhimu kwake.
“Na saa pia wamechukua!”
“Walikuwa wangapi?”
“Siikumbuki idadi yao, nadhani hawakupungua watano. Walinivamia kama mbwa mwitu!”
“Simu yako nayo?”
“Hawakufanikiwa kuichukua, nilipata upenyo nikawachomoka na kukimbia!”
“Itabidi tuliripoti tukio hili polisi!”
“Halafu iweje?” John aliuliza kwa mshangao.
“Sidhani kama polisi watanisaidia kunirudishia pesa na vitu nilivyoibiwa! Isitoshe wanaweza kunipotezea muda wangu kwa ajili ya kwenda mahakamani wakati sikumbuki hata sura ya mmoja wa vibaka hao. Ninachoshukuru wameniachia uhai wangu. Sihitaji kufanya kesi na mtu yeyote! Nipe funguo yangu ya chumbani nikapumzike!”
“Pole sana!” mtumishi wa mapokezi alisema kisha alitoa funguo na kumpa John.
Huko chumbani, John akiwa amechanganyikiwa alivichukua vitu vyake alivyokuwa amevitoa kwenye begi saa chache zilizopita wakati alipokuwa amewasili kwenye hoteli hiyo akitokea Dar es Salaam na kuanza kuvirudisha tena ndani ya begi. Alikuwa ameamua kutoroka usiku huo kurudi Dar es Salaam haraka iwezekanavyo! Alikuwa na uhakika polisi watakuwa wanamtafuta kwa udi na uvumba kutokana na tukio la kumchoma kisu Richard!
Akafanikiwa kuvirejesha vitu vyote kwenye begi na kuamua kuondoka, lakini alijikuta akisimama ghafla na begi lake mkononi kabla ya kuufungua mlango wa chumbani. Kilichomfanya asimame hapo mlangoni ni baada ya kujiuliza angeelekea wapi akishatoka hapo hotelini? Alikuwa na uhakika muda huo kusingekuwa na uwezakano wa kupata usafiri wa haraka utakaomtoa nje ya Arusha! Usafiri pekee ambao ungeweza kumwondoa haraka na kumfikisha angalau mji wa Moshi ungekuwa ni wa teksi, lakini hakuwa na fedha ya kukodi teksi ya kuweza kulipia kwa umbali mrefu kama huo. Isitoshe, bado angehitajika kuwa na pesa nyingine za kulipa gharama za usafiri za kumfikisha Dar es Salaam.
Akaukumbuka usafiri wa malori ambayo mengi huanza safari nyakati za jioni hadi usiku. Akaamini usafiri huo ungemsaidia kumwondoa hapo Arusha, lakini kikwazo kikawa, alikuwa hajui wapi angeyapata malori hayo usiku huo. Kwanza alikuwa halijui eneo linaloegeshwa malori hayo, pili, woga wa kukamatwa na polisi ulikwisha kumwingia. Hofu hiyo ikamjengea hadhari endapo atahangaika kwenye mitaa kuyatafuta malori ya kumuwezesha kusafiri usiku huo kungeweza kuchangia kumkamatisha kirahisi kwa polisi. Hali ya kuchanganyikiwa ikaanza kumtesa!
Aliondoka taratibu pale mlangoni alipokuwa amesimama na begi lake, akarudi kitandani na kukaa huku akionekana kuchoka ghafla. Majuto ya tukio alilolifanya la kumchoma kisu Richard yalikuwa yakimtafuna wakati wote na wakati huo huo akinung’unikia moyoni kuwa yote hayo yasingetokea kama sio Dina kumsaliti! Lakini pia kwa upande mwingine alijilaumu mwenyewe kwa hatua aliyoifanya ya kumchoma kisu Richard. Alijua ulikuwa ni wivu na hasira vilivyomfanya atende hayo. Nafsini alijirai mara kwa mara kuwa, alichotakiwa kufanya baada ya kugundua ukweli kuwa Dina alikuwa amemsaliti, ilikuwa ni kuondoka pale hotelini, kisha angefanya maamuzi mengine dhidi ya Dina mbele ya safari.
Maji yalishamwagika!
Hata hivyo kuna wakati alikuwa akijiridhisha kwa kujipa moyo kuwa kitendo alichokifanya kilistahili kwa Richard kwa sababu alitaka kumfanya bwege! Alimwona Richard ndiye aliyepaswa kulaumiwa kwa sababu alikuwa akiyajua mahusiano yake na Dina, na pia, alikuwa akifahamu kuwa, walikuwa wakikaribia kufunga ndoa! Kwa nini Richard anifanyie ushenzi kama huu? alijiuliza. Alitaka kunifanya zoba? Alinidharau kuwa nisingeweza kumfanya lolote? John akapiga kite cha hasira humo chumbani, akajiinamia na kukipakata mikononi kichwa chake. Alikiri alikuwa amejiingiza kwenye matatizo mazito ambayo hakuyatarajia, na kwa mara ya kwanza alijikuta akiilani siku ambayo yeye na Dina walionana kwa mara ya kwanza! Yasingenifika yote haya! aliwaza.
Akiwa bado amejiinamia, mawazo yake yalirudi hotelini Masai Shield na kulifikiria tena tukio lililotokea. Alijikuta akitaka kufahamu hali ya kiafya aliyonayo Richard baada ya kumchoma kisu. Hofu ilikuwa imemtawala kwa kitendo hicho, lakini alijipa matumaini kuwa, kisu alichokitumia kumchoma nacho Richard kilikuwa ni kisu cha mezani cha kulia chakula na aliamini hakikuwa na urefu mkubwa wa kuweza kuingia kwenye mwili wa binadamu na kuleta madhara ya kutishia uhai wa mtu. Hakitakuwa kimemsababishia madhara makubwa! alijipa imani. Sidhani kama anaweza akafa! Wazo hilo likamfanya auinue juu uso wake na kufumba macho. Akasali kimya kimya yasitokee maafa kama hayo.
Kuingiwa na wazo la kuwa anaweza akawa ameua, alijikuta akiingiwa na hofu nyingine ya aina yake! Wazo la kutoroka usiku huohuo likarudi kwa kasi mpya, lakini pia akapata mashaka na uamuzi huo. Alikiri kuwa, hata kama angeweza kuutekeleza uamuzi wa kutoroka usiku huo, bado lingekuwa sio suluhisho, angeendelea kutafutwa na polisi bila kujali kama ameua au hakuua, kwani kosa alilokuwa amelifanya bado ni la jinai na lazima angetafutwa kwa ajili kushitakiwa.
Kwa mzunguko huo, John alikiri kukimbia sio dawa ya tatizo hilo, labda angekimbilia nje ya nchi kama vile Kenya. Ingekuwa ni rahisi kwa kutokea hapo Arusha kuweza kukimbilia Nairobi, lakini angekimbilia kwa nani huko Nairobi? Kwanza katika maisha yake alikuwa hajawahi hata kulikanyaga jiji hilo! Pili, alikuwa hamjui mtu wake yeyote anayeishi huko!
Lakini pia, tatizo jingine aliloliona mbele yake ni familia aliyoingia nayo kwenye ugomvi. Familia ya mzee Ken Korogwe! Familia tajiri yenye uwezo wa kuapa kupania kumtafuta na wakampata! Ni familia yenye nyenzo zote za uwezeshaji wa kurahisisha kutafutwa kwake popote atakapokimbilia na angepatikana! Ni familia ambayo kwao dunia ni kama kijiji pindi wakianza msako wa kumtafuta. Kwa hiyo hata kama angekimbilia maeneo ya Alaska au Australia ambako ni mbali kwa kutokea ukanda wa Afrika ya Mashariki, bado angekamatwa! Hapo pakamvunja nguvu! Akakiri hana pa kukimbilia!
Kukiri huko kuwa hana pa kukimbilia, John akaanza kufikiria kujipeleka mwenyewe polisi! Aliuona uamuzi huo ndio wa busara, angejipeleka na angelielezea tukio zima linalohusisha mahusiano ya mapenzi kati yake na Dina na wale wote waliojihusisha na Dina kwa njia moja au nyingine na angemtaja Mohsein kuwa ndio chachu ya kuyajua yote hayo.
Akauafiki uamuzi huo wa kujipeleka mwenyewe kituo cha polisi!
* * * * *
Mtumishi wa Idara ya Mapokezi wa hoteli aliyofikia John hakuridhika na maamuzi yaliyofanywa na John kwa kuliacha tukio la kuvamiwa na wahuni kisha kuporwa liishie kimya kimya. Matukio ya aina hiyo yaliwahi kutokea siku za nyuma kwa wateja wao ambao walidai kama alivyodai John kuwa matukio yaliyowakuta yasiripotiwe polisi kwa ajili ya kukataa usumbufu. Awali walikuwa wakizikubali hoja za namna hiyo zilizotolewa na wageni wao wa hoteli, matokeo yake hoteli hiyo ikaingia lawamani kuwa ni hoteli inayoshirikiana na vijana wa kihuni kuwaibia wateja wa hotelini hapo.
Lakini baada ya kuathirika kibiashara kutokana na sifa mbaya iliyowakuta, utawala wa hoteli hiyo ulichukua hatua za makusudi kurudisha heshima ya hoteli hiyo kwa kujiweka karibu na polisi kwa matukio yote ya kihalifu ambayo yangewatokea wateja wao. Lakini licha ya kujiweka karibu na polisi, pia wakaamua kuandika waraka kwa wafanyakazi wote kuwa watoe taarifa kwa uongozi wa hoteli pindi linapotokea tukio la kihalifu kwa mteja wao. Waraka huo ukasisitiza, yeyote atakayeshindwa kufanya hivyo, hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yake.
Sheria hiyo mpya ndio iliyomlazimisha mtumishi huyo wa mapokezi kutolipuuzia tukio la vibaka kumvamia John lisiishie kimya kimya. Akaenda kuliripoti kwa meneja wake wa zamu usiku huohuo.
“Anaitwaje huyo mteja?” meneja wa zamu alimwuliza mtumishi wake baada ya kupokea taarifa hizo.
“John Sailas, anatokea Dar es Salaam na aliwasili jioni ya leo. Amepanga chumba namba 112, kwenye fomu ya maelezo amejaza kukaa kwa usiku mmoja. Maelezo yake yanaeleza ni mwajiriwa wa cheo cha karani wa stoo na anatarajia kurudi Dar es Salaam baada ya kuondoka Arusha.”
“Alikuaga anakwenda wapi wakati alipotoka kabla ya kuvamiwa na vibaka?”
“Alikuja na kuacha funguo kwangu na kusema anatoka. Hakuniambia wapi anapoelekea na sikumwuliza. Aliporudi ndio akanieleza kuwa alivamiwa na vibaka.”
“Ulimwuliza ni wapi alikovamiwa na vibaka?”
“Aliniambia alivamiwa maeneo ya katikati ya mji, hakunitajia sehemu rasmi. Tatizo ni kuwa, hakuonyesha kutaka kulizungumzia sana tukio hilo na sijui ni kwa nini. Hata nilipomshauri tuliripoti tukio hili polisi, alikataa.”
“Itabidi tuwaarifu polisi, wao ndio watakaoamua kama waje kumhoji au waliache kama mhusika anavyotaka. Huwezi kujua matokeo ya aina hii yana athari za aina gani. Je, kama ni jambazi ametoka kufanya uhalifu na kupata misukosuko kisha akasingizia kuwa ni vibaka ndio waliomvamia? Hili suala ni la kuliripoti polisi na wao watajua cha kufanya!”
Muda mfupi uliofuata, madai yaliyotolewa na John ya kuvamiwa na vibaka, meneja wa zamu wa hoteli hiyo akayaripoti polisi!
***
DINA Nzasa akiwa Kituo cha Polisi cha Mkoa wa Arusha alifanyiwa mahojiano na kachero Mussa kuhusu tukio lililotokea hoteli ya Masai Shield. Kabla ya kuruhusiwa kuondoka, alikiri kumfahamu John na akaelezea kuwa ni mchumba wake, lakini pia, alikiri kitendo kilichofanywa na John kilitokana na wivu wa kumtuhumu kuwa anatembea na Richard.
“Ni kweli unatembea naye?” kachero Mussa aliyekuwa akimhoji alimwuliza.
“Siwezi kukujibu swali hilo!” Dina alijibu.
Mussa akajikuna kichwani kwa kutumia kalamu aliyoishika. “John alikuja kufanya nini Arusha?”
“Sijui.”
“Uliujua ujio wake?”
“Sikuujua. Nilimwona akiingia ghafla hotelini!”
“Alikuwa akijua kama upo Arusha?”
“Ndiyo, isitoshe nilimuaga.”
“Alikuwa akijua kama ulifikia hoteli ya Masai Shield?”
“Awali hakujua ningefikia hoteli ipi kwa sababu hata mwenyewe nilikuwa sijui ningefikia wapi. Lakini baada ya kuwasili hapa Arusha ndipo nikawasiliana naye kwa simu nikamwambia kuwa nimefikia hoteli ya Masai Shield.”
“Unasema John anakutuhumu kuwa unatembea na Richard, ni mahusiano gani yaliyopo kati yako na Richard mpaka John afikirie kitu kama hicho?”
“Kama nilivyokwambia awali, Richard ni bosi wangu. Hakuna zaidi ya hilo.”
“John aliwahi kuziweka wazi hisia za tuhuma hizo kwako?”
“Kwa kipindi chote cha uhusiano wetu amekuwa na hisia hizo na alikuwa akizizungumza kwangu.”
“Unayo sababu yoyote unayoijua ya kumfanya awe na hisia hizo?” “Kwa sababu nilianza mahusiano naye baada ya uhusiano wangu na Richard kuvunjika. Hilo ndilo linalomfanya John asiwe na imani kuwa uhusiano wangu na Richard umekufa.”
“Lakini si anajua kama mko pamoja kikazi?”
“Anajua.”
“Kabla ya tukio hili, kuliwahi kutokea tukio la wao kukutana na kutupiana maneno kwa ajili yako?”
“Sidhani, kwa sababu hakuna yeyote kati yao aliyewahi kunilalamikia.”
“Ulisema John alipofika pale hotelini alikukuta ukiwa umekaa meza moja na Richard?”
“Ndiyo.”
“Alisema nini baada ya kuwakuteni?”
“Kabla ya kutukaribia pale mezani, niliwahi kuinuka nikamfuata na tukazungumza pembeni.”
“Alikwambia nini baada ya kuwa naye?”
“Tatizo alikuja kiushari, aliponiona tu, akadai kutaka kuondoka na mimi ili twende kwenye hoteli aliyofikia yeye. Nikamkatalia!”
“Alikupa sababu ya uamuzi wake huo?”
“Sababu ni kuwa mimi ni mchumba wake.”
“Sio kwa sababu amegundua kuwa una mahusiano ya mapenzi na Richard?”
Dina hakujibu.
“Alikutajia hiyo hoteli aliyofikia?”
“Tulikosa kuelewana kabla hata ya kunitajia hoteli yenyewe. Akataka kunichukua kwa nguvu, ndipo nilipoamua kukimbia, akanifukuza. Richard akamzuia na matokeo ndio hayo yaliyotokea.”
“Unaweza ukatabiri endapo kama hatorudi hotelini ni wapi muda huu anaweza akawepo? Nakuuliza hivyo kwa sababu hatutarajii kumkuta hotelini akiwa amejificha baada ya kufanya tukio kama lile ingawa bado hatujajua ni hoteli ipi aliyofikia.”
“Mimi ni mara yangu ya kwanza kuja Arusha na hajawahi kuniambia kama ana jamaa yake yoyote hapa Arusha.”
“Unayo picha yake?”
“Unamaanisha kwa kule hotelini nilipo?”
“Kama ni hotelini au kwenye simu yako, nikiwa na maana kama nitaihitaji leo ninaweza nikaipata?”
“Sina kawaida ya kutembea na picha yake.”
Baada ya hapo, Mussa akaonekana kutokuwa na maswali zaidi ya kuhoji. Akalazimisha kuhoji maswali mengine ya hapa na pale lakini yakakosa msaada wa kumsaidia kuweza kujua John angepatikana vipi.
“Richard amepelekwa hospitali gani? Nataka kwenda kumwona!” Dina alisema baada ya kuhisi askari huyo hana maswali mengine zaidi.
“Bado sijajua. Itanibidi nifanye mawasiliano na wenzangu walioondoka naye. Huenda tukaenda pamoja hospitali.”
Kachero Mussa alimsindikiza Dina hadi nje ya Kituo cha Polisi na kumpeleka kwenye gari la polisi, akamwomba amsubiri humo kwenye gari. Kisha Mussa alirudi ndani kituoni na kufanya mawasiliano ya simu na polisi waliokuwa wameongozana na Richard alipokuwa akipelekwa hospitali.
Dina akiwa peke yake kwenye gari la polisi kwa takribani dakika zisizopungua kumi, alikuwa kwenye shinikizo lililokuwa likimchanganya. Tukio la kupigana kati ya Richard na John lilimkosesha amani wakati wote na kujikuta akipata wakati mgumu wa kupata jibu baada ya kujiuliza, ilikuwaje John akajua kuwa yeye na Richard walisafiri pamoja kwenye ndege? Na alijuaje yeye na Richard walikuwa wakiishi chumba kimoja?
Dina akakumbuka jinsi alivyokuwa amemdanganya John kwa kumwambia alikuwa hakusafiri na Richard kwenye safari hiyo ya kuja Arusha. Au ni mama ndiye aliyemwambia John kuwa, yeye na Richard walisafiri pamoja kwenye ndege? alijiuliza. Swali hilo likayafanya mapigo yake ya moyo yafanye mshituko baada ya kutambua upo uwezekano wa mama yake kumwambia John ukweli huo! Dina alijikuta akitamani kujitafuna vidole vyake baada ya kugundua alifanya kosa kutomhadharisha mama yake kuhusu siri hiyo!
Ujio wa kurudi kachero Mussa hapo garini ukamwondoa Dina kwenye jinamizi lililokuwa likimwandama baada ya kushituliwa na mlango wa gari uliofunguliwa na kumwona Mussa akiingia na kukaa nyuma ya usukani.
“Wenzangu walioshiriki kumpeleka Richard hospitali, wanasema Richard yuko chumba cha upasuaji akifanyiwa upasuaji. Nadhani suala la kwenda kumwona ni mpaka kesho atakapokuwa amepelekwa wodini,” kachero Mussa alisema na papohapo akaliwasha gari.
“Ni vyema nikurudishe hotelini na kesho asubuhi nitakufuata kukupa taarifa za hospitali.”
“Wanasemaje kuhusu hali yake?” Dina aliuliza huku akijaribu kuituliza akili yake.
“Wanasema, aliingizwa chumba cha upasuaji akiwa anaongea. Inaonyesha hayuko kwenye hali mbaya inayohatarisha maisha yake.”
“Mungu atamsaidia!” Dina alisema.
“Amen,” Mussa alijibu na kuliondoa gari.
* * * * *
Kwa mara ya kwanza tokea awasili hapo Arusha na kuyafurahia maisha ya kifahari kwa kunywa mivinyo mitamu, vyakula vya bei ghali vyenye ladha inayokufanya ujisikie kula, kulala kwenye chumba cha kifahari cha hoteli yenye hadhi ya nyota tano, Dina kwa mara ya kwanza alijikuta akiiangalia hoteli hiyo kwa mtazamo tofauti. Sasa hoteli hiyo alivyokuwa akiteremka kutoka kwenye gari la polisi alikuwa akiiona kama ngome fulani ya Kishetani! Wakati akiingia hotelini humo eneo la mapokezi aliyahisi macho ya wafanyakazi yakimwangalia tokea mlangoni na baadhi yao walidiriki kumpa pole na yeye alizipokea kwa kujibu kwa sauti hafifu.
Chumbani ambako mara baada ya kufika alijitupa kitandani kama mzigo akiwa na nguo zake. Macho yake yaliangalia juu kwenye dari iliyonakshiwa na kujikuta akiirudisha kumbukumbu ya kuwaona Richard na John walivyokuwa wakipigana. Tukio hilo lilikuwa limenasa kwenye ubongo wake na kuwa kama gurudumu la sinema lililokuwa likijizungusha kichwani mwake kwa wakati wote. Ni tukio lililomfedhehesha kila alipolifikiria.
Ghafla akaanza kulia! Majuto yalikuwa yamemwinamia na kila kitu kikaanza kujitokeza kinyume. Alijiona ni mgeni hotelini hapo, hakuwa na mtu yeyote ambaye angeweza kumshirikisha kwa kumweleza matatizo yaliyomfika! Lakini pia, hata hapo Arusha alikuwa ni mgeni napo, hakuwa na mtu ambaye pengine angesema amfuate nyumbani kwake au amuite hapo hotelini angalau amshirikishe kulijua jinamizi linalomwandama usiku huo!
Alikuwa peke yake!
Baada ya kulia kwa dakika kadhaa akiwa peke yake humo chumbani, hatimaye akili ikamjia kuwa kulikuwepo na mtu hapo Arusha ambaye angeweza kuzungumza naye! Aliamini huyo angeweza kushirikiana naye kulizungumza tatizo hilo pengine kwa mapana zaidi ingawa aliamini kusingekuwa na maelewano kati yao.
Alikuwa amemkumbuka John!
Alitaka kuzungumza naye angalau amfahamishe kuwa polisi walikuwa wakimtafuta na alikuwa tayari hata kumpa msaada wa kifedha usiku huo ili atoroke. Alikiri nafsini mwake kuwa ni yeye ndiye aliyehusika kumwingiza John kwenye wakati huo mgumu. Fikra hizo za kumwona John ameingia ndani ya matatizo kwa ajili yake zilimwumiza moyo, akamwonea huruma kijana huyo na kutambua ni jinsi gani anavyompenda!
Nafsi yake ikawa ikimsuta jinsi alivyomsaliti mchumba wake huyo, akaulaani moyo wake jinsi ulivyoshindwa kukabiliana na vishawishi vilivyomkabili. Lakini bado alijiona anayo nafasi ya kumwomba msamaha John na angeweza kuitumia nafasi ya kumpigia simu kuzungumza naye, pia angeitumia nafasi hiyo kumshawishi aondoke haraka hapo Arusha kwa kumtahadharisha kuwa polisi wanamtafuta na angemwahidi kumsaidia kwa kumpa pesa za kutosha alizopewa na Richard! Angeweza kumtumia pesa hizo kwa njia ya simu kwa kuzituma kupitia moja ya ofisi ya kampuni ya simu ambayo ina tawi lake hapo hotelini ambalo linafanya kazi kwa saa ishirini na nne.
Dina alijifuta machozi kwa kutumia kiganja chake, kisha akajifuta kamasi nyembamba kwa kutumia nguo aliyoivaa. Uamuzi wa kumpigia simu John ndio ungefuata, lakini alijikuta akipata kigugumizi cha kuufa
nya uamuzi huo. Alikuwa akiogopa kuzikabili lawama atakazopewa na John, hakuwa na uhakika angezijibu vipi shutuma hizo. Akapiga moyo konde, akaichukua simu yake na kumpigia John.
John hakupatikana!
Nguvu zikamwishia, kilio kikawa faraja yake!
MLIO wa simu ndio uliomshitua kutoka usingizi! Alichukuliwa na usingizi bila ya kujitambua alipokuwa amejilaza wakati akilia. Alishangaa kuiona asubuhi imeshafika na ndipo alipojitambua alikuwa amelala na lile gauni alilokuwa amepanga aende nalo Casino akiwa na Richard usiku uliopita. Kujiona ameamka akiwa na gauni hilo kukamtonesa kulikumbuka zogo la usiku lililotokea hapo hotelini. Simu iliyokuwa ikiita ilinyamaza, lakini sekunde chache baadaye ilianza kuita tena.
“Haloh,” Dina alisema baada ya kuipokea simu ya chumbani kwake, kisha akapiga mwayo.
“Samahani,” sauti ya kike ilisema kwenye simu. “Una mgeni wako hapa mapokezi. Amejitambulisha kwa jina la kachero Mussa.”
Ndipo fahamu kamili zilipomrudia kuwa alikuwa na ahadi na kachero huyo asubuhi hiyo.
“Naomba anipe dakika kumi za kujiandaa,” Dina alisema kwenye simu. Kisha akamsikia msichana aliyepo kwenye simu akizungumza na mtu, akajua alikuwa akizungumza na kachero Mussa.
“Anasema utamkuta akikusubiri hapa mapokezi,” hatimaye msichana wa mapokezi alisema.
“Mwambie anisubiri mgahawani, anaweza akaagiza kifungua kinywa kwa bili yangu,” Dina alisema na kisha kukata simu.
Alitumia muda zaidi kuliko ule aliouahidi. Alikoga, kisha alijikwatua kwa vipodozi akiwa amekaa kwenye stuli iliyopo mbele ya kioo cha kujiangalia wakati wa kuvaa. Moyo wake ulikuwa bado mzito kutokana na sintofahamu iliyokuwepo kati ya John na Richard. Wote alitaka kujua taarifa zao zikoje. Kwa John ni kwa ajili ya kujua kama amekwishakamatwa na polisi, na kwa Richard ni kuhusu afya yake inavyoendelea baada ya upasuaji aliyofanyiwa.
Kwa upande wa Richard angalau alikuwa na matumaini ya kuonana naye pindi atakapokwenda kumwona hospitali atakapoongozana na kachero Mussa. Alikuwa na uhakika asingemkuta kwenye hali ya kuruhusiwa kuzungumza na wageni kwa kuwa hali yake ya kiafya ingekuwa bado haijatengemaa. Akaijenga taswira ya atakavyomwona Richard akiwa kitandani. Taswira hiyo akaijenga kwa kumwona Richard akiwa hajarudiwa na fahamu kikamilifu kutoka kwenye madawa ambayo angekuwa amepewa kwa ajili ya kufanyiwa upasuaji. Alijua asingeweza kuzungumza naye zaidi ya kumwangalia na kisha angeondoka, lakini akajenga matumaini ya kuzungumza naye wakati wa jioni atakavyorudi tena hospitali. Alikuwa na uhakika muda huo John angekuwa amerudiwa na fahamu kikamilifu.
Akapanga jioni atakapokuwa anarudi tena hospitali itamlazimu anunue maua na kadi ya kumtakia Richard uponaji wa haraka.
Akiliona tatizo la Richard likiwa halimwumizi sana kichwa, Dina alikiri tatizo la John ndilo lililokuwa likimpa wakati mgumu. Alijiuliza kwa muda huo wa asubuhi John angekuwa wapi? Alijua John asingekuwa mpumbavu wa kuendelea kuwepo hotelini wakati akijua amefanya tukio ambalo limemwingiza kutafutwa na polisi, lakini pia akajengwa na wasiwasi zaidi huenda John hakulala kabisa huko hotelini. Fikra hizo zikamfanya ayahisi machozi yakimlengalenga machoni baada ya kuifikiria hali ambayo angekuwa nayo John. Akaijenga taswira ya kumwona John akiwa kwenye wakati mgumu akiishi kwenye hali ya kukosa amani kutokana na woga wa kukamatwa na polisi! Kwa mara nyingine, Dina alijisikia vibaya baada ya kujiona ndiye aliyeisababisha hali hiyo kwa John!
Wazo la kumpigia tena simu John likamrudia. Shinikizo la kutaka kumsaidia kwa kumpatia pesa za kumsaidia kutoroka likaanza tena kuisumbua nafsi yake, aliamini kitendo hicho kingeweza kumwonyesha John kuwa yuko pamoja naye kwenye tatizo hilo. Kwa upande mwingine, aliuona msaada huo ungekuwa ni sehemu ya kumwomba John msamaha kwa kile kilichotokea!
Aliifuata simu yake iliyokuwa bado ipo kitandani na kumpigia John. Alipokuwa akisubiri simu hiyo ianze kuita upande wa pili anakopiga, kimya hicho cha kusubiri pamoja na kwamba kilikuwa ni cha muda mfupi, lakini kilimuweka kwenye wakati mgumu. Kilimjengea woga wa kukabiliana na jibu kutoka kwenye simu kuwa, mteja anayempigia hapatikani. Akaomba hilo lisitokee.
“Samahani, mteja unayempigia hapatikani, jaribu tena baadaye!” sauti kutoka kwenye simu ilisikika.
Dina aliishiwa nguvu! Akaushusha chini mkono wake uliokamata simu, kisha akauinua juu uso wake uliokata tamaa. Alikuwa na uhakika John alikuwa amezima simu yake na asingeweza kumpata! Hakuhitaji kujiuliza ni kwa nini, yeyote angekuwa kwenye mazingira kama aliyonayo John, angefanya hivyo. Akatamani John apate akili ya kuiwasha simu yake kisha ambipu japo mara moja. Alitamani iwe hivyo, lakini kwa hali halisi, ilikuwa sawa na mtu mwenye kiu anayetamani kukiona kidimbwi cha maji jangwani!
Ghafla akamkumbuka kachero Mussa, alikwisha kumsahau!
Kitendo cha kumkumbuka kachero huyo kuwa alikuwa akimsubiri kikamtoa chumbani haraka. Akamkuta akiwa anamalizia kifungua kinywa alichokiagiza. Kilikuwa ni kifungua kinywa kilichokamilika, kinachojulikana kwa jina la English Breakfast.
“Samahani kwa kukuweka sana,” Dina alisema huku akivuta kiti na kukaa kwenye meza aliyokuwepo Mussa.
“Usijali,” Mussa alisema huku akijifuta mdomo kwa kitambaa cha mezani.
“Nashukuru kwa kifungua kinywa.”
“Usijali,” Dina alisema. Kisha aliagizia chai na vipande vya mikate ya kuokwa.
Dina alianza kunywa juisi na kusubiri chai aliyoiagiza.
“Hali ya Richard inaendeleaje?” aliuliza baada ya kumeza funda la juisi.
“Bado sijapata habari zake,” Mussa alisema huku akijaribu kutoyatuliza macho yake.
“Nilipitia kituoni kujua kama kungekuwa na ripoti yoyote iliyoletwa na askari aliyekuwa akimlinda hospitali, hata hivyo alikuwa bado hajaiwasilisha. Nadhani askari mwenzake wa kuchukua nafasi yake atakuwa amechelewa kwenda kumtoa.”
“Na vipi kuhusu John?”
“Kuna mtu mwenye jina lake amekamatwa jana usiku na polisi,” Mussa alisema.
“Tutaanza kwenda huko ili ukamthibitishe kama ndiye yeye, kisha ndipo tutakapokwenda kumwangalia Richard.”
Taarifa ya kukamatwa kwa John ikampotezea Dina hamu ya chai aliyoiagiza!
“Nitakunywa chai nitakaporudi!” Dina alisema huku akivuta nyuma kiti alichokalia na kusimama. Alijua asingeweza kuinywa chai ambayo angeletewa na hakutaka kachero Mussa alibaini hilo. “Twenzetu!” alimalizia kwa kusema hivyo akiwa amekwishajitoa kwenye meza.
“Kwa nini usingekunywa kabisa,” Mussa alishauri.
“Huwezi kujua, unaweza ukajikuta umechaelewa kurudi, ukarudi hapa mchana baada ya shughuli ya huku na kule. Unajua mambo yetu ya kipolisi hayana dogo.”
“Mara nyingi sipendi kunywa chai asubuhi,” Dina alidanganya.
“Nimekwishazoea kufanya kazi wakati wa asubuhi bila ya kunywa chai.”
Mussa akataka kuongeza neno, lakini alisita baada ya kumwona Dina akiwa amekwishaupachika mkoba wake begani na kutangulia kuondoka. Akaamua kuongozana naye. Wakapita kwa mtunza fedha ambako Dina alilipa gharama za kifungua kinywa alichokula Mussa.
Wakati wakiwa wamekwishatoka nje ya hoteli, Dina alijikuta akiwa kwenye wakati mgumu kimawazo. Alikuwa tayari amechanganyikiwa na habari za kukamatwa kwa John, lakini alipata ugumu pale alipokuwa akijitahidi kuificha hali hiyo isionekane na kachero huyo anayeandamana naye.
Wakiwa kwenye gari, kachero Mussa hakuonyesha kuwa kwenye mdadi wa kuzungumza, sehemu kubwa ya mwonekano wake alipokuwa akiliendesha gari, alionekana kuwa kwenye tafakuri iliyomtuliza. Ukimya ukajitokeza kati yao, Dina akaomba hali hiyo iendelee kuwa hivyo, kwani naye alihitaji utulivu utakaomuweka kwenye kujiandaa jinsi atakavyokabiliana na John. Hakujua angeongea naye nini wakati akiwa amesimamiwa na polisi, lakini kilichokuwa kikimsumbua zaidi ni pale atakavyolijibu swali la kachero huyo litakalomtaka athibitishe mbele ya John kama huyo aliyekamatwa ni John! Alikuwa na uhakika jibu la kukubali kumthibitisha John lingekuwa kama usaliti atakaokuwa amemfanyia John!
Siku mbili, tatu za nyuma alipokuwa kwenye gari akienda ofisini akiwa na Richard, Dina alikuwa akifurahia kuiangalia mandhari ya jiji hilo la Arusha kila alivyokuwa akipita, lakini asubuhi hiyo, kwa mara ya kwanza tokea afike kwenye mji huo, Dina aliuona mji huo kama eneo asilotaka kuliona kwenye maisha yake! Hali hiyo ilimfanya kukitumia kimya kilichowekwa na kachero Mussa kufumba macho yake wakati wote huku akiusikilizia myumbo unaofanywa na gari wakati likipita kwenye miinuko ya barabara au wakati likikata kona. Kibaya zaidi, hakutaka hata kushuhudia kule anakopelekwa!
Alijikuta akifumbua macho baada ya kulisikia gari hilo limesimama na kisha likazimwa injini. Akajua wamefika! Lakini alipoyaangaza macho yake akashangaa kuliona gari hilo likiwa limesimama nje ya hospitali ya Mount Meru. Akamwangalia kachero Mussa kama vile uangaliaji wake ungemfanya Mussa aujibu mshangao wake. Hata hivyo, Mussa hakuonekana kukijua kilichokuwa kinafanyika kwa Dina, yeye alikuwa ameinama akihangaika kuufungua mkanda wa kiti cha gari.
“Umeamua tuanze kwa kumwangalia Richard?” Dina aliamua kuuliza. Mussa alishusha pumzi kwa nguvu na kuangalia mbele ya kioo cha gari, akaonekana kama vile alikuwa akiwaangalia watu waliokuwa wakikatisha
mbele ya gari hilo.
“Hapana!” alijibu bila ya kuacha kutazama mbele. Jibu hilo likamtia hofu Dina. Akawa na wasiwasi kuwa, maadam kama siye Richard aliyewafanya waje hapo, basi atakuwa ni John! Dhana ikamjenga kuwa John atakuwa alikumbana na kipigo cha polisi baada ya kukamatwa na majeruhi aliyoyapata ndio yatakuwa yamemfanya alazwe hospitalini hapo.
“John amelazwa?” Dina aliuliza na sauti yake ilishindwa kuificha hofu aliyokuwa nayo huku akiwa bado hajayabandua macho yake kumwangalia kachero Mussa.
“Amefariki!” Mussa alijibu kama vile alikuwa akizungumza peke yake. Akageuka na kumwangalia Dina aliyekuwa tayari amepigwa na mshangao usoni. Akaendelea, “Alipatikana kwenye chumba chake cha hoteli aliyofikia akiwa amejinyonga!”
Shingo ya Dina ikalegea ghafla, mboni za macho yake zikajibinua kuelekea juu!
* * * * *
Kitendo cha Dina kuzirai mle ndani ya gari kulimfanya kachero Mussa achanganyikiwe baada ya kujaribu kuutingisha mwili wa Dina kwa lengo la kumuamsha bila ya mafanikio. Akatambua kulihitajika huduma ya kihospitali ili kuweza kukabiliana na tatizo hilo. Akaufungua mlango wa gari na kuchomoka kwa kasi, akakimbilia idara ya mapokezi ambako alijitambulisha cheo chake kwa mfanyakazi wa hospitali mwenye beji iliyomwonyesha ni mtumishi wa mapokezi aliyekuwa anataka kuingia chumba cha mapokezi akitokea nje na kumweleza kilichomsibu.
“Kwa hiyo huyo dada yuko kwenye gari yako?” mtumishi huyo aliuliza kwa utulivu kama vile tatizo aliloambiwa halikuhitaji huduma ya dharura.
“Ndiyo yupo kwenye gari yangu!” Mussa alisema na kuonekana akikosa utulivu.
“Subiri nikutafutie watu wa kwenda kumchukua,” mfanyakazi yule wa mapokezi alisema. Akaanza kurudi alikotoka, lakini kabla hajachanganya hatua akatokea mtu, mtu huyo akamfanya asimame, wakaanza kusalimiana na kitendo hicho kiliwachukua takribani dakika moja kama vile hakukuwa na jambo la dharura alilotakiwa mtumishi huyo wa hospitali alishughulikie.
Kitendo hicho kikamchafua Mussa. Hasira iliyompanda kichwani ikamsukuma kutaka kumfokea mtumishi huyo wa hospitali, lakini kabla hajafanya hivyo, akatokea mhudumu wa wagonjwa ambaye ni mwanamke, akaitwa na yule mtumishi.
“Omba msaada wa mwenzako ili mfuatane na huyu bwana, ana mgonjwa wake yuko kwenye gari amezidiwa,” alisema yule mtumishi wa mapokezi.
Kitendo hicho kikamfanya kachero Mussa azishushe hasira zake. “Utaandamana na huyu dada kwenda kumchukua mgonjwa wako,”
mtumishi wa mapokezi alimwambia Mussa, kisha akaendelea kuzungumza na mtu wake na kuonekana amelimaliza tatizo hilo.
Muuguzi wa kike na wa kiume walikisukuma kitanda cha magurudumu hadi kwenye gari alilokujanalo Mussa, wakamtoa Dina na kumpakia kwenye kitanda na kumuwahisha kwenye chumba cha daktari huku Mussa akifuata nyuma yao.
* * * * *
Dina alihifadhiwa kwenye chumba maalumu hadi aliporejewa na fahamu. Alirejewa na fahamu akiwa peke yake baada ya muuguzi wa kike anayemwangalia akiwa ametoka nje. Dina hakutambua yuko wapi, lakini akahisi kama yuko hospitali. Akafumba macho kujaribu kuvuta kumbukumbu ya kutaka kujua ilikuwaje akawepo hapo. Harufu ya madawa ya binadamu ikamhakikishia kuwa yuko hospitali, lakini akawa bado hajaelewa alifikaje hapo. Akavuta tena kumbukumbu kutaka kujua mara ya mwisho alikuwa wapi kabla ya kufika hapo. Akaikumbuka hoteli ya Masai Shield!
Kuikumbuka hoteli hiyo ikawa kama vile imemfungulia rejesho la kumbukumbu zilizokuwa zimepotea. Akaanza kukumbuka kimoja baada ya kingine…
Amefariki! hatimaye akaikumbuka kauli ya kachero Mussa alivyokuwa naye kwa mara ya mwisho kwenye gari akimzungumzia John!
Muuguzi akaingia!
“Umeamka?” muuguzi aliuliza huku akionyesha tabasamu dogo akiwa amesimama kando ya kitanda alicholalia Dina.
Dina hakujibu, kumbukumbu iliyomrejea ikaanza kumtoa machozi. Muuguzi akaingia kwenye kazi ya kubembeleza. Juhudi zake zikafanikiwa kumtuliza Dina asilie kwa sauti, lakini aliendelea kutokwa na machozi. Ghafla akataka kijiinua, akajilazimisha kujizoa zoa huku akionekana kukosa nguvu.
“Unataka kwenda wapi?” muuguzi alimwuliza.
“Nataka kukaa,” Dina alijibu.
Muuguzi akamsaidia kumuinua, Dina akakaa kitandani na miguu yake ikaning’inia bila ya kukanyaga sakafuni. Baada ya kukaa, akabaki kimya.
“Unajisikiaje?” muuguzi aliuliza baada ya kumwona Dina yuko kimya. “Naomba unipeleke nikamwone!” Dina alisema bila ya kufafanua. Muuguzi akajua alichokimaanisha Dina.
Taarifa za kujinyonga kwa John zilikuwa zikijulikana na baadhi ya wauguzi, mmoja wa wauguzi hao alikuwa ni huyo anayemuuguza Dina kwenye chumba cha mapumziko ambaye pia alishiriki kumtoa Dina kutoka kwenye gari alipokuwa amezirai. Muuguzi huyo pia, alikuwa na taarifa zilizomjulisha kuwa, Dina ana mahusiano na John ingawa hakuujua kwa undani uhusiano wao ulikuwa ni wa aina gani. Hivyo, kauli hiyo ya Dina kutaka kwenda kumwona anayetaka kumwona akawa ameielewa vizuri kuwa, Dina alikuwa akitaka apelekwe chumba cha maiti kumwona John!
“Mimi sina mamlaka ya kukupeleka,” muuguzi alimwambia Dina. “Msubiri daktari akija umfahamishe, yeye ndiye mwenye mamlaka ya kukupeleka.”
Dina hakujibu. Alizubaa na kutulia bila ya kutikisika sehemu yoyote ya mwili wake, hakuonekana hata kupepesa macho yake. Muuguzi akabaki ameshangaa.
“Hivi ni kweli John amekufa?” Dina aliuliza na kuonekana kama amerudi ghafla kwenye uhai.
Swali hilo likamuweka muuguzi kwenye wakati mgumu. Akasita kujibu baada ya kukiri swali hilo lilikuwa limemchanganya. Lilikuwa gumu kulitolea jibu la haraka. “Kwani wewe wamekwambiaje?” naye aliuliza.
“Nasikia amejinyo…” Dina hakuimaliza kauli yake, shingo yake ikalegea na macho yake kujipindua tena. Akaangukia ubavu!
Muuguzi akawahi kumdaka Dina kabla hajaangukia chini kutoka kitandani. Akamlaza vizuri na kuirudisha miguu yake kitandani. Akajaribu kumtingisha huku akimuita. Baada ya kuona hakuna dalili yoyote ya kuitikiwa, akaamua kutoka mle chumbani kwa mwendo wa kasi, akaenda kumuita daktari!
* * * * *
Mohsen aliwasili ofisini asubuhi, alikuwa bado akiendelea na majonzi ya kumkosa Dina tokea alivyoondoka kwenda Arusha na alikuwa akiendelea kuumizwa na wivu kwa kujua yuko na Richard. Lile Jinamizi la kumkumbusha vitendo vya kimapenzi alivyokuwa akifanya na Dina wakiwa humo ofisini lilikuwa likiendelea kumtesa. Alikuwa bado akimwona Dina kama vile yuko naye humo ofisini. Alijihisi kama anayechanganyikiwa kadri siku zilivyokuwa zikienda. Mazoea ya uwepo wao wa pamoja kwenye mapenzi ya muda mfupi yalimtesa kana kwamba alikuwa kwenye mapenzi ya muda mrefu na msichana huyo.
Pamoja na kuwa kwenye hali hiyo, lakini kila alipokuwa akimfikiria Dina ndivyo alivyokuwa akijilaumu kwa hatua aliyoichukua ya kumfuata John na kumbwagia mambo ambayo alikiri hayakupaswa kujulikana na John kupitia kwake. Tukio hilo lilikuwa likimkosesha amani baada ya kujiona alikuwa amekosea kuchukua hatua kama hiyo. Kitendo hicho kikamuweka kwenye mashaka kuwa, yote aliyokuwa amemweleza John yangeweza kumfikia Dina. Uwezekano wa John kwenda kumweleza Dina na kisha kulitaja jina lake kuwa ndiye aliyemwambia, aliuona upo. Fikra hizo zikawa eneo jipya lililomkosesha amani kwa muda wote, hasa pale alipojiona angeonekana mshamba wa mapenzi na mwanamume mmbeya!
Hofu hiyo ilimtia kwenye kiwingu kizito, iliyomwingizia majuto na kukiri upuuzi huo aliufanya kwa sababu ya wivu wa kijinga! Fikra hizo za kukiri uhayawani wake zilimuweka kwenye wakati mgumu, ugumu ambao ulimjengea uhakika wa kuja kumgharimu kwa gharama kubwa siku chache zijazo. Kwanza alikuwa na hakika ya kumpoteza Dina kama mpenzi wake ambaye tayari alikwishajikita moyoni mwake. Akakiri hilo litakuwa ni pigo kubwa kwake na kumfanya aanze kuhisi kama vile hakutakuwa na maisha mengine ikiwa atamkosa Dina. Lakini pia, kitendo hicho cha kupeleka umbeya kwa John alikiri kinaweza kumgharimu kwenye kazi yake! Alikuwa na uhakika Dina angeshikwa na hasira na angemshukia kama Mwewe na hatimaye angemshitaki kwa Richard! Richard angekuwa amepata sababu ya kumfukuza kazi!
Akiwa kwenye lindi la mawazo asubuhi hiyo humo ofisini kwake huku akiwaza jinsi atakavyompoteza Dina na kuipoteza kazi yake, Mohsein alijikuta akipata wazo jipya. Wazo la kutaka kurudi tena kwa John, safari hii kwa ajili ya kumpigia magoti! Alipanga aende kumsihi na kumrai asije akamtaja kwa Dina kuwa ni yeye ndiye aliyeyazungumza maneno hayo. Hiyo ndio aliiona njia pekee ya kuweza kumuokoa asikumbane na adhabu hizo mbili.
Akapanga muda wa kumfuata John kazini kwake. Akaona ni vyema kuitumia nafasi ya ruhusa ya mchana inayotumika kwa ajili ya wafanyakazi kwenda kula, aitumie kwenda kumwona John! Akajiandaa kujipanga namna ya kumkabili kwa mara nyingine ya pili.
Ikiwa imebaki saa moja na ushee muda wa mapumziko kwa ajili ya chakula cha mchana ufike, taarifa za msiba zikaja hapo kazini, taarifa zilizowashitua wafanyakazi wote wa kampuni hiyo.
Lilikuwa tangazo la kufariki kwa Richard!
* * * * *
Kifo cha Richard kilileta hisia tofauti kwa wafanyakazi wa kampuni hiyo. Wapo waliofurahia kifo hicho kutokana na ujivuni aliokuwa nao kijana huyo wakati wa uhai wake, wakazificha furaha zao na kuunganika kwenye majonzi. Lakini pia walikuwepo walioguswa na kifo hicho kwa kukiri kuwa walikuwa wamempoteza mtu wanayemjua ambaye ni mfanyakazi mwenzao na huzuni ziliwagusa zaidi kwa kumwona Richard amefariki akiwa bado ni kinda.
Mohsein yeye alikifurahia kwa sababu Richard alishakuwa adui yake, akakichukulia kifo hicho kwamba kitakuwa kimeondoa moja ya adhabu mbili alizokuwa akizifikiria. Adhabu ya kufukuzwa kazi na Richard! Pamoja na kufurahia kwa upande huo, lakini upande wa pili ndio uliomfurahisha zaidi. Kifo cha Richard kingemuwezesha kulifaidi penzi la Dina kwa wakati mwafaka, na ili kuliwezesha hilo, alitakiwa kumkabili John hata kama ni kwa kutumia vitisho, kuhakikisha hathubutu kumwambia Dina kwamba yeye aliupeleka umbeya kwake!
Taarifa endelevu za kifo cha Richard ziliendelea kuwasili kwa namna tofauti hapo kazini. Taarifa nyingine zikaletwa kuwa, mzee Ken na mama yake Richard wanaondoka kwa ndege kuelekea Arusha asubuhi hiyo.
Baadaye zikaja taarifa za kipolisi kuwa, Richard aliuawa kwa kupigwa kisu kwenye ugomvi unaosadikika ulitokana na wivu wa mapenzi wa kumgombania mwanamke, lakini hazikumtaja mwanamke mwenyewe. Hatimaye zikaja taarifa zenye mshituko zilizoeleza, polisi walikuwa wamethibitisha ugomvi uliosababisha kifo cha Richard ulimhusisha mume mtarajiwa wa mfanyakazi mwenzake Richard anayeitwa Dina Nzasa, aliyetambulika kwa jina la John Sailas ambaye baada ya tukio la kumpiga kisu Richard aliamua kuchukua uamuzi wa kujinyonga akiwa kwenye chumba cha hoteli aliyokuwa amefikia. Inasemekana John kabla ya kujinyonga aliacha barua yenye maelezo yake na polisi wamelithibitisha hilo kwa kusema kuwa, wanamtafuta mtu mmoja aliyetajwa kwenye barua hiyo kuwa ndiye anayeaminika ni chanzo cha ugomvi huo. Polisi imekataa kulitaja jina la mtuhumiwa huyo kwa sababu za kiusalama.
Taarifa hizo zikawa si njema kwa Mohsein! Kwanza hakuamini kama John alikwenda Arusha na moja kwa moja akatambua kilichompeleka John Arusha ni zile taarifa alizokuwa amempelekea. Msala! aliwaza. Akajua mambo yamekwisha kuharibika na hofu yake ikawa ni barua iliyoachwa na John ambayo iko mikononi mwa polisi. Akawa na uhakika polisi watakuwa wakimtafuta yeye kwa kuamini barua hiyo itakuwa imelitaja jina lake! Mohsein akawa amechanganyikiwa. Akapata wazo la kutoroka kabla ya polisi hawajafika hapo ofisini kumkamata!
Akatoka ofisini kwake, akawaaga wafanyakazi wenzake aliokutana nao kwenye korido kuwa anakwenda kula chakula cha mchana.
Hakurudi tena kazini!
Siku ya pili asubuhi wakati wafanyakazi wakiwa kazini na wengine wakifuatilia mipango ya kuwasili kwa mwili wa Richard ambao taarifa za awali zilisema ungewasili kwa ndege siku inayofuata, ilipofika alasiri ya siku hiyo, taarifa nyingine za msiba zikawasili.
Alikuwa Mohsein!
Taarifa hizo zilipokewa kama mchezo wa kuigiza usiokubalika, hakuwepo aliyekuwa tayari kuziamini, hasa baada ya taarifa hizo kudai, Mohsein alikutwa chumbani kwake akiwa amejinyonga na kuacha ujumbe mfupi kwenye barua iliyoandikwa:
Wivu umeniponza!
Mohsein.
MISA
MISA ya kumwombea John Sailas ilifanyika kwenye Kanisa Katoliki la Kimara Baruti baada ya siku ya arobaini tokea alipozikwa kwenye makaburi ya Kimara. Baada ya misa hiyo, wafiwa walikwenda makaburini kwa ajili ya kupanda Msalaba na kuweka mashada ya maua kwenye kaburi lake. Mmoja wa walioweka mashada hayo alikuwa ni Dina ambaye baada ya kuweka, akahisi hatia kwenye nafsi yake. Machozi yakaanza kumtoka na kilio cha kimya kimya kikafuata.
Ikabidi apewe msaada wa kuondolewa!
* * * * *
Misa ya Richard ilifanyika siku nne tokea misa ya John ilipofanyika. Misa yake ilifanyika kwenye Kanisa la Mtakatifu Peter lililopo Oysterbay. Dina alihudhuria misa hiyo akiongozana na wazazi wake, na wakati walipokuwa wakitoka Kanisani ili kujiandaa kwenda kwenye makaburi ya Kinondoni alipozikwa Richard kwa ajili ya kupanda Msalaba, Dina akasikia akiitwa. Ilikuwa sauti ya kike iliyotoka nyuma yake ikimuita kwa jina lake. Alipogeuka akamwona Judi aliyekuwa ameandamana na kijana mmoja wa kiume.
“Hai Judi!” Dina alisema na kusimama.
Ilikuwa ni mara yao ya pili kuonana tokea walivyoonana kwa mara ya mwisho walipokutana kwenye msiba wa Richard.
“Kutana na mchumba wangu,” Judi alimwambia Dina.
“Anaitwa Martin,”
“Nafurahi kukufahamu,” Dina alisema huku akimpa mkono Martin. Kisha Judi akamtambulisha Martin kwa Dina.
“Martin, kutana na Dina, tulisoma pamoja kuanzia kidato cha kwanza hadi cha nne kwenye shule ya Sekondari ya Jangwani.”
Martin aliyekuwa bado akiliendeleza tabasamu lake akasema, “Nami nafurahi kukufahamu.”
Baada ya Dina na Martin kusalimiana, Judi aliufungua mkoba wake na kutoa bahasha, akampa Dina.
“Nilihisi tungeonana huku Kanisani,” Judi alisema.
“Nikapata wazo la kuja nayo hii kadi ili nikikuona nikupe. Mungu naye ametuwezesha tumeonana.”
Dina aliipokea kadi aliyopewa ambayo ilikuwa ndani ya bahasha na kusema, “Ahsante.” Hakuhoji ni ya nini kwa sababu angeifungua na kuisoma baadaye.
Wakaagana.
Akiwa kwenye gari ndogo amekaa nyuma pamoja na mama yake huku baba yake akiwa amekaa mbele na dereva, Dina aliifungua bahasha aliyopewa na Judi, akaichomoa kadi na kuisoma. Akagundua ilikuwa ni kadi ya mwaliko inayomwalika ahudhurie sherehe ya kufunga ndoa kati ya Judi na Martin!
Mchomo mkali ukapita na kuuchana moyo wa Dina, akaacha kuendelea kuisoma kadi hiyo, akaamua kuangalia nje ambako watu wachache walikuwa wakitembea kando ya barabara ya Ali Hassan Mwinyi na wakati huohuo magari waliyokuwa wakipishana nayo yalisikika yakitoa mivumo ya kasi ya mwendo. Macho ya Dina yalikuwa yamegubikwa na machozi yaliyomnyima nafasi ya kukiangalia kinachotokea barabarani.
Upepo uliokuwa ukiingia kupitia dirisha lililokuwa upande aliokaa Dina uliyapeperusha machozi na kuyasambaza kwenye ncha za macho yake wakati gari hilo likiwa kwenye mwendo.
Akajifuta machozi ya upande mmoja wa jicho lake kwa kutumia kiganja cha mkono wake.
****UMEJIFUNZA NINI????
***KAMA UMEJIFUNZA MFUNDISHE NA MWENZAKO!!!!
***
MWISHO
Simulizi hii imenipa mafunzo mengi sanaa...lakn kwnz tuwe na mioyo yenye uvumiliv hasa ktk mambo ya mahusiano kingine pia tuwe waaminifu ktk ahadi tunazowapa wenza wetu.pia tusiwe ni watu wa kuyumbishwa yum bisha katk maamuzi tunayofany kila siku
ReplyDelete