Simulizi : Wivu
Sehemu Ya Nne (4)
Dina akamfahamisha John kuwa anaondoka kesho asubuhi kwenda Arusha kikazi itakayomchukua wiki moja huku akiilalamikia safari hiyo ilikuwa ni ya ghafla ambayo hakuitarajia.
Habari hizo zilimshitua John na kumchanganya baada ya kumkumbuka Richard! “Unakwenda na Richard?” aliuliza.
“Bado sijajua, lakini sidhani kama na yeye atakwenda!” Jibu hilo likashusha presha za John.
“Kwa hiyo unasafiri peke yako?” John aliuliza.
“Bado sijajua. Nilichoambiwa, kesho asubuhi niwahi kufika ofisini kuna safari ya kwenda Arusha!”
* * * * *
Dina aliwasili Uwanja wa Ndege wa Mwalimu Julius Nyerere akiwa kwenye teksi na alisindikizwa na mama yake. Walimkuta Richard akiwa amekwishafika kama alivyokuwa ameahidi.
Kitendo cha kuwepo kwa Richard mapema hapo uwanjani kwa ajili ya kumsubiri Dina kilionekana kumfurahisha mama yake Dina na kuamini Dina alikuwa kwenye mikono salama. Alimchukulia Richard kama mwanae na alimwona Dina kama yuko na kaka yake. Kwenye maamkizi kati ya mama huyo na Richard, mama yake Dina alionyesha upendo kwa kijana huyo. Dina na Richard wakamuaga, akawaombea heri kwenye safari yao. Baada ya mama huyo kuondoka, Dina na Richard wakajikuta kwenye muunganiko wa pamoja na wakawa karibu kama vile hawakuwa na tofauti zao.
“Ulishawahi kusafiri kwa ndege?” Richard alimwuliza Dina mara tu baada ya mizigo yao kukaguliwa kwenye mashine za usalama wakati walipoingia ndani ya jengo la Uwanja wa Ndege.
“Bado,” Dina alijibu na kucheka kicheko kidogo cha kuondoa aibu kutokana na swali aliloulizwa. Kilikuwa kicheko cha kwanza na cha wazi kumchekea Richard baada ya kipindi kirefu cha uhasama wao!
Richard akamfahamisha Dina kinachotakiwa kufanywa hatua inayofuata wakati walipokuwa wakikaribia kujiunga na moja ya foleni inayoelekea kaunta ambako kulikuwa na vitenganishi vya majina ya mashirika tofauti ya ndege yenye kuashiria utoaji huduma wa wasafiri wa ndege zao.
“Watakuwekea namba ya kiti, kwa hiyo unatakaje? Tuchague kukaa pamoja au tukae viti tofauti?” Richard aliuliza wakiwa wanaikaribia kaunta.
Dina akafumba macho na kujenga tabasamu.
“Mi sijui chochote, mambo yote nakuachia wewe!” alijibu na kumtazama Richard.
“Basi tukae pamoja au unasemaje?”
“Yaani bado unaniuliza mimi?” Dina alisema na kumwangalia Richard kwa ncha za macho yake.
“Poa, nitamwambia karani atuweke pamoja.”
Walipoingia ndani ya ndege kabla ya kukaa kwenye viti vyenye namba walizoandikiwa, Richard akamwuliza Dina, “Utapenda kukaa dirishani?”
“Mi naogopa kuangalia nje!” Dina alisema kwa sauti ndogo ambayo hakutaka asikiwe na abiria waliosimama jirani ambao walikuwa wakihangaikia kuiingiza mizigo yao kwenye majaluba ya kuhifadhi mizigo ya ndani ya ndege.
Richard akakaa sehemu ya dirishani, Dina akakaa kando yake.
Dina alikuwa mwepesi kuiangalia hali iliyomo kwenye ndege na kuwaangalia baadhi ya abiria waliokuwa wakiendelea kuhangaika kupandisha mizigo yao kwenye majaluba na wakati huo huo wahudumu wa ndani ya ndege wakiwasaidia kuwaonyesha abiria mahali vilipo viti vyao. Akakumbuka kujifunga mkanda. Akadhani angeufunga mkanda huo kama vile ajifungavyo kwenye gari. Akaukamata mkanda uliopo kwenye kiti chake na kutaka kujifunga, akagundua uko tofauti na ule wa kwenye gari, hali hiyo ikamfanya aanze kubabaika kujifunga.
“Niangalie mimi ninavyojifunga mkanda!” Richard alisema ghafla baada ya kumwona Dina akijaribu bila mafanikio kuufunga mkanda huo.
Dina akamwangalia Richard alivyokuwa akijifunga, kisha na yeye akajaribu kuiga. Akapatia!
Richard akatabasamu na kumwangalia Dina. Dina akalirudisha tabasamu na kumwangalia Richard kwa ncha za macho yake.
“Itabidi uzime simu yako, hawaruhusu matumizi ya simu kwenye ndege!” Richard alisema huku tabasamu likiwa bado lipo mdomoni mwake.
Dina akaizima simu yake!
* * * * *
Upweke uliosababishwa na kutokuwepo kwa Dina ofisini ulianza kumtesa Mohsein baada ya kuwasili kazini. Tokea Dina alivyoanza kazi, hii ilikuwa ni mara ya kwanza kutokuwepo pamoja. Kutokuwepo kwake kulikuwa kama kipimo kilichompa jawabu kuwa Dina alikuwa ni sehemu muhimu ya maisha yake ya kila siku hapo ofisini. Aligundua Dina alikuwa akimwongezea furaha ya kuipenda kazi yake kila alipokuwa naye.
Kutokuwepo kwa Dina kulimfanya ashindwe kuifanya kazi yake ipasavyo asubuhi hiyo na kujikuta mnyonge wakati wote. Ule uelewa wa kujua Dina hatokuja kazini kutokana na kusafiri kulimpa wakati mgumu na kuiona asubuhi iwe chungu kwake. Penzi lilikuwa likimuadhibu na wivu ulikuwa ukimwandama.
Kadri muda ulivyosogea kwenda mbele hali ya kujiona ni mgonjwa iliongezeka, kila kitu humo ofisini kikawa kinamkumbusha uwepo wa Dina. Tafakuri za mazoea ya kumwona Dina akifanya hiki au kile humo ofisini zilimwelemea. Alikikumbuka kicheko cha Dina chenye maringo, na uangaliaji wake wa kupenda kumtazama mtu kwa kutumia ncha za macho yake. Hali hiyo ilimfanya awe na hisia zilizomwumiza na kuhofu kama vile, Dina asingerudi tena! Akili yake haikuwepo kabisa ofisini, ilikuwa imetekwa na fikra za kumuwaza Dina na kumfanya atumie muda mwingi wa kuduwaa kuliko kufanya kazi. Dina alikuwa amemkaa akilini mwake kama muhuri wa moto ukaavyo kwenye nyaraka!
Siku hiyo pia, ilitumika kama mzani wa kugundua jinsi alivyotokea kumpenda msichana huyo kwa kasi ya ajabu. Alijishangaa kujiona akimlilia wivu hali akijua msichana huyo yuko njiani kuolewa! Lakini, alijishangaa zaidi kujiona akimwona Richard kuwa ndiye adui yake namba moja badala ya John ambaye ndiye mume mtarajiwa wa Dina!
Mohsein alijaribu mara kadhaa kujipa ujasiri wa kuachana na fikra za kumuwaza Dina na kumwonea wivu Richard, hasa akizingatia hata yeye ana rafiki yake wa kike wa muda mrefu wanaoheshimiana na kupendana na pengine wakaja kufunga ndoa! Alikiri huyo ndiye aliyestahili kupewa upendo wote badala ya kubabaishwa na Dina aliyejipenyeza ghafla kati kati ya penzi lao. Ushawishi wa kujipa ujasiri huo wa kumwondoa Dina mawazoni mwake aliuona ukikubalika akilini, lakini ukikataa moyoni.
Akiwa mwenye kujihurumia, Mohsein alijionya kuwa, upendaji aliojiachia nao wa kumpenda Dina kwa nguvu kiasi hicho unaweza ukaja kumzindua rafiki yake wa kike kugundua kuwa anamsaliti. Mawazo yake yakarudi nyuma na kukiri kuwa, siku ambayo moyo wake ulipenyezwa sumu ya kumpenda Dina na kumuingiza kwenye ufala wa kupenda kibwege uliomkuta hapo alipo, ni ile siku ambayo alifanya mapenzi na Dina wakiwa stoo. Kitendo hicho ndicho kiliingiza sumu kwenye mfumo mzima wa mzunguko wake wa damu na kuivuruga sehemu kubwa ya ubongo wake. Lakini pia, baada ya kitendo hicho ukawepo mwendelezo wa vitendo vya kuonyeshana kuwa wanapendana kila walipokuwa pamoja ofisini.
Siku ambayo Richard alirudi kutoka Morogoro ndio ikawa siku ya kuihitimisha fungate yao na furaha ya penzi lao kusambaratishwa baada ya Richard kumpa Dina taarifa ya safari!
Siku hizo ndizo ambazo zilikuwa na sumu iliyomwangamiza kiakili, sasa aliziona akizitumikia kwa kifungo cha mateso yanayomtesa huku akitawaliwa na donge la kumwonea wivu Richard kwa kuondoka na Dina. Akakiri kuwa, amezama kichwa kichwa kwenye penzi la Dina.
Nimekwisha! alijisikitikia peke yake!
* * * * *
Waliwasili Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro na Dina alishangaa pale alipokuwa kwenye gari lililowachukua kutoka uwanjani kugundua kuwa, uwanja huo wa Kimataifa ulikuwa mbugani na ukiwa mbali kabisa na jiji la Arusha ikiwa ni tofauti na Uwanja wa Ndege wa Dar es Salaam ambao haukuwa mbali kutoka katikati ya jiji.
Waliwasili Arusha, gari walilopanda likawapeleka moja kwa moja kwenye hoteli kubwa ya kimataifa na ya kifahari ya Masai Shield iliyokuwepo kando kidogo kwa kilomita chache kutoka katikati ya jiji la Arusha. Wakiwa mapokezi, Richard alijiandikisha, hali kadhalika kwa Dina naye ikawa ni hivyo hivyo, na walipokuwa wakijaza maelezo yao kwenye kadi ya hoteli ya kujisajili upangaji, kuna maeneo ambayo Richard alimwelekeza Dina namna ya kujaza kwenye kadi yake.
“Tungependa kwenda kustafutahi kabla hatujakwenda vyumbani kwetu,” Richard aliyeonekana sio mara yake ya kwanza kuwepo kwenye hoteli hiyo alimwambia mtumishi wa mapokezi.
“Mnakaribishwa. Restaurant yetu bado inahudumia kifungua kinywa,” mtu wa mapokezi alisema huku akiiangalia saa yake ya mkononi.
Waliruhusiwa kwenda kwenye mgahawa wa hoteli wakiwa na mizigo yao. Huko Richard alimsaidia Dina kuagiza kifungua kinywa kwa kumchagulia baadhi ya vitafunio kutokana na uzoefu wake. Wakati walipokuwa wakistafutahi, Richard aligundua Dina alikuwa na tatizo linalowakabili wasichana wengi warembo wa kutokuwa na uzoefu wa namna ya kukamata uma. Dina alikuwa akiikumbatia badala ya kuikamata wakati akikita kuchoma kitu anachotaka kula. Richard hakusema lolote! Baada ya kumaliza kustafutahi, walikwenda kwenye vyumba vyao na Richard akamwonyesha Dina chumba chake kilipo. Kilikuwa jirani na chake.
“Kesho ndio tutakwenda kuanza kazi, vipi baadaye utapenda kuuzunguka mji wa Arusha na kuujua?” Richard aliyekuwa amemsindikiza Dina hadi mlangoni mwa chumba alichopangiwa kukaa alimwuliza Dina kabla hajaingia chumbani humo.
“Mi nakusikiliza wewe!” Dina alijibu na kumwangalia Richard kwa ncha za macho yake.
“Basi pumzika, baada ya masaa mawili nitakuja kukugongea mlango ili ukatembee kuuona mji.”
“Sawa,” Dina alijibu kwa upole.
Richard akamsaidia Dina kumfungulia mlango wa chumbani kwake kwa kutumia kadi na kumwelekeza matumizi ya kadi hiyo ambayo hutumika badala ya funguo ya kawaida.
Akiwa chumbani peke yake na kushangazwa na uzuri wa chumba alichomo huku akijiona kama yuko ndotoni akiwa haamini yale yanayomtokea, Dina alikuwa tayari amechanganyikiwa! Hadhi ya kusafiri kwa ndege kikazi, kulala kwenye hoteli ya kifahari kama hiyo, kilikuwa ni kitu ambacho hakikuwahi kumtokea kwenye fikra zake. Alikiri huduma anayopewa haikuwa hadhi yake kikazi, ilikuwa ni hadhi ya mtu mwenye elimu inayoanzia na Shahada! Hakutaka kujidanganya kuwa alikuwa na bahati ya mtende kupewa hadhi hiyo kutokana na kazi aliyokuwa nayo. Hakuwa na elimu ya kazi wala ujuzi wa kazi hiyo! Alitambua yote hayo yalikuwa yakifanywa na Richard kwa sababu moja ya wazi; Richard alikuwa akimpenda na alikuwa akiuonyesha upendo wake kwake!
Aliwazia jinsi alivyokuwa akimkataa Richard kwa kipindi kirefu, kipindi ambacho Richard alikuwa akimbembeleza kwa kila hali ili warudiane. Akafikiria jinsi alivyomkatisha tamaa baada ya kumchagua John kuwa chaguo lake na kumteua kuwa mchumba wake! Alikuwa na uhakika maamuzi hayo yalimwumiza Richard, lakini yeye hakujali wakati huo; kwa sababu aliamini ni John pekee ndiye aliye moyoni mwake na ndiye mwenye haki ya kuutumia mwili wake. Lakini bila ya kutarajia, alijikuta akimsaliti John kwa kutembea na Mohsein, tena kwa hiari yake! Ulikuwa ni kama uamuzi wa ajabu kukubali kufanya kitendo hicho cha kumsaliti John, lakini aliukiri udhaifu uliomkuta wa kuvutwa na mvuto wa Mohsein, udhaifu ambao unaweza kumkuta yeyote! Sasa amejikuta akiwa na mabwana wawili, na kuwa tayari kila mmoja ampende kwa sababu yake. John kwa ajili ya ku-make love, na Mohsein kwa ajili ya ku-make sex!
Lakini sasa hapo alipo kwenye chumba cha hoteli ya kifahari, Dina alikiri yupo kwenye mtihani mwingine aliokuwa akipewa na Richard. Mtihani aliouona ukimchanganya kichwa, ulimchanganya kwa sababu ni mtihani ulioingia takrima ya mapenzi. Alikuwa na uhakika matendo aliyofanyiwa hadi sasa na Richard kama angeyaeleza kwa rafiki yake yeyote wa kike, rafiki yake huyo asingesita kumshauri kumkubali Richard! Na angemshawishi kuwa, takrima anayofanyiwa na Richard ni yenye upendo wa dhati kwa sababu Richard alishamuahidi kutaka kumuoa!
Aliyafikiria matendo yote aliyotendewa na Richard na kuamini hata ule mshahara aliopangiwa ulitokana na juhudi za Richard kumshawishi baba yake, na kwa mara ya kwanza alijikuta akiamini, hata kazi aliyoajiriwa ilitokana na Richard! Akaifikiria safari iliyofanyika asubuhi hiyo kutoka Dar es Salaam hadi hapo Arusha, matendo yaliyotokea kati yake na Richard katika safari nzima hakutaka kujidanganya nayo, alikiri yalikuwa ni matendo yaliyowezesha kuwaweka tena karibu na kujikuta wakiurudisha uhusiano wao kwa njia moja au nyingine. Alitakiwa airudishe fadhila hiyo ili kuonyesha uungwana wake!
Mtihani ulikuwa kwake!
****
SIMU yake ndio iliyomshitua, alijishangaa kujikuta kumbe alikuwa amepitiwa na usingizi akiwa amelala na suruali yake ya jeans iliyomshika vema mapajani. Awali kabla ya kupitiwa na usingizi alizungumza kwa simu na wazazi wake wote wawili, akawajulisha kuwa alikwishafika salama mjini Arusha. Pamoja na kuwakumbuka John na Mohsein lakini hakuwapigia simu kuwajulisha kuhusu kuwasili kwake jijini Arusha. Akiwa ameshituliwa na simu ambayo ilikuwa ikiendelea kuita akaiweka dhana ya kuwa huenda simu hiyo ilikuwa inapigwa na mmoja wapo kati ya John au Mohsein. Akaichomoa simu yake iliyojibana kutoka kwenye mfuko wa mbele wa jeans alikokuwa ameiweka. Akashangaa kuziona namba za mpigaji badala ya jina la mmoja wao kati ya John au Mohsein. Akashindwa kuijua simu hiyo ilikuwa ikipigwa na nani.
“Haloh,” alisema kivivu.
“Mimi Richard, nifungulie!” sauti kutoka kwenye simu ilisema. Akashituka baada ya kutambua ni Richard ndiye aliyekuwa akiipiga
simu hiyo, akakumbuka namba ya Richard alikwishaifuta muda mrefu kwenye simu yake, lakini pia akakumbuka siku chache zilizopita Richard aliiomba namba yake wakiwa ofisini na alimpa. Akakurupuka kutoka kitandani, akajifuta uso haraka haraka na kwenda kuufungua mlango. Akamkuta Richard amesimama mlangoni.
“Karibu,” Dina alisema.
“Siingii,” Richard alisema kwa upole.
“Nakusubiri Mapokezi, gari limeshafika.”
Dina akaikumbuka safari ya kwenda kuzunguka kuliangalia jiji la Arusha.
“Nakuja!” Dina alisema.
Walitumia muda mwingi kuzunguka mjini, Richard alimwonyesha Dina baadhi ya maeneo yenye umaarufu hapo Arusha, waliingia kwenye maduka tofauti na Richard akaitumia nafasi hiyo kumnunulia Dina zawadi mbalimbali, kisha alimuagiza dereva wa gari walilokuwemo ambalo ni mali ya kampuni yao kuwapitisha kwenye kituo cha mafuta kinachomilikiwa na kampuni ya baba yake. Walipofika hawakuteremka, Dina akaonyeshwa kituo hicho cha mafuta kuwa ni hapo ndipo ambapo kesho watakuja kufanya kazi. Dina akakiangalia kituo hicho ambacho kilikuwa kikubwa chenye Super Market pamoja na mgahawa wa Kimataifa.
Waliporudi hotelini, walikuwa wamechoka na njaa zilikuwa zikiwauma.
Richard alimsaidia Dina kubeba baadhi ya mizigo aliyomnunulia hadi chumbani kwa Dina.
“Richard,” Dina alisema wakiwa chumbani kwake baada ya kuiweka mizigo waliyoiingiza. “Mungu akubariki!”
“Amen,” Richard alijibu na kuunganisha alilokuwa anataka kulisema. “Unaonaje ukiagiza chakula kiletwe humu chumbani? Kuna kitu nataka kukuonyesha.”
Dina akamwangalia Richard kwa ncha za macho yake.
“Kuna kitu unataka kunionyesha?” aliuliza huku akionyesha kushangaa.
“Ndiyo. Nitakuonyesha wakati chakula kitakapoletwa,” Richard alisema na kuifuata kadi yenye orodha ya vyakula kwa ajili ya huduma maalumu ya chumbani huku akimuacha Dina akiwa bado yupo kwenye mshangao. Alirudi alipomuacha Dina, akamkabidhi kadi hiyo.
“Chagua, chakula gani utapenda uletewe?” alisema.
“Samaki,” Dina alisema alipokuwa akiitazama kadi hiyo.
“Naona kuna aina tofauti ya mapishi, unaweza ukanichagulia?”
“Nakuchagulia Poached fish, naamini utafurahia.”
“Wewe huagizi?”
“Kama utaniruhusu nile chumbani kwako, nitaagiza.”
Dina akamwangalia Richard. “Agiza!” alisema kwa sauti ya chini yenye maringo.
Richard akaagiza kwa kutumia simu ya humo humo chumbani, naye pia aliagizia samaki kama aliomchagulia Dina. “Itachukua sio chini ya dakika ishirini hadi kutuletea, wacha niende chumbani kwangu kuna kazi kidogo nakwenda kuifanya, nitarudi kabla ya chakula hakijaletwa,” Richard alimwambia Dina.
Wakaagana.
Ni kweli aliwahi kurudi kabla ya chakula kuletwa! Dakika tano baada ya kufika, chakula nacho kikaletwa. Richard akasaini kwenye stakabadhi ya malipo, kisha alitumbukiza mkono mfukoni na kutoa noti aliyompa mhudumu aliyeleta chakula ikiwa sehemu ya bakshishi. Mhudumu akashukuru na kutoka.
“Nionyeshe ulichotaka kunionyesha!” Dina alisema kabla ya kuanza kula.
“Kula kwanza…” Richard alisema huku akitabasamu.
Dina akagoma kula. “Sili mpaka unionyeshe hicho kitu!” alisema. Ikawa kama sehemu ya utani kwao ambao haukuwa rasmi. “Nitakuonyesha,” Richard alisema huku akiinuka kivivu kwa kujishika magoti wakati akisimama, akaenda kumsimamia Dina mgongoni.
“Nataka kukufundisha namna ya kukamata uma,” alisema huku akimuinamia Dina juu ya mabega yake.
“Khaa!” Dina alishituka.
“Yaani mimi sijui kushika uma?”
“Hujui kuushika wakati unapokula!”
“Haya makubwa!”
Richard akauchukua uma uliovingirishwa na kisu kwenye karatasi ya kujifuta mdomo iliyokuwa pembeni mwa sahani ya chakula, akaukamata kama alivyokuwa ameukamata Dina asubuhi walipokuwa wakistafutahi.
“Wewe unashika uma hivi,” akamwonyesha Dina.
“Uma haukamatwi hivi, unakamatwa hivi. Hebu jaribu,” akaurudisha kwa Dina.
Dina akasikitika kisha akafanya alivyoambiwa.
“Na kisu kikamate kama ulivyoukamata uma. Ukite uma juu ya samaki, kisha kata kwa kisu.”
Dina akafanya vile alivyoambiwa.
“Sasa endelea kula. Huo ndio ukamataji wa uma na kisu. Tatizo hili sio lako peke yako, nimeshuhudia vijana wengi, pamoja na kuupenda Uzungu, lakini wengi wanashindwa namna ya kukamata uma unavyotakiwa wakati wa kula.”
Walipokuwa wakiendelea kula, ghafla Richard alichukua kipande cha samaki alichokikata na kukiinua kwa uma.
“Nataka kukulisha,” Richard alisema huku akimwangalia Dina usoni. Dina akawa kama aliyeshangaa, akamwangalia Richard usoni bila ya kutoa jibu la haraka. Wakaangaliana kwa makini kama waliokuwa wakisomana akili zao. Hatimaye Dina akaufungua mdomo bila ya kutamka
lolote, akamruhusu Richard amlishe!
* * * * *
* * * * *
Jioni ya saa kumi na moja, Dina akiwa ameamka sekunde chache zilizopita na kabla hajakiweka vyema kichwa chake kutafakari, akausikia mlango wa chumbani kwake ukigongwa. Moja kwa moja akahisi ni Richard ndiye angekuwa anaugonga mlango huo. Akakumbuka wakati alipoachana naye mara tu baada ya kumaliza kula chakula cha mchana walichokula pamoja, Richard alimuaga na kumtaka apumzike, akisema wataonana baadaye. Ndipo naye alipoamua kulala na kupata usingizi mzuri hadi alipoamka na kusikia mlango ukigongwa.
Alipoufungua, akashangaa kumwona mhudumu wa vyakula akiwa amesimama na tray iliyobeba birika mbili, zote zilikuwa ndogo zenye ukubwa uliotofautiana, na kijaluba cha sukari, pembeni kukiwa na sahani iliyofunikwa na kitambaa.
“Sijaagiza!” Dina alisema, usoni akiwa na mshangao.
“Mzee Richard ameniagiza nikuletee,” mhudumu alisema.
Mzee Richard! Dina alishangaa na kutaka kujiuliza mtu huyo ni nani. Ghafla akapata jibu kuwa ni heshima aliyokuwa akipewa Richard. Akatabasamu na moyoni kukasuuzika baada ya kukiri, Richard alikuwa akimjali.
“Karibu,” alimwambia mhudumu na kumpa nafasi ya kuingia.
Mhudumu aliingia chumbani na kuangaliwa na Dina aliyekuwa amesimama mlangoni kwa ajili ya kumsubiri atoke.
“Nakwenda,” mhudumu aliaga baada ya kuviweka kwenye meza vitu alivyoingia nao.
“Yeye yuko wapi?” Dina aliuliza wakati mhudumu akiwa mlangoni anatoka.
“Yupo duka la kahawa akinywa chai,” mhudumu alijibu.
“Ahsante na karibu tena,” Dina alisema kisha akaufunga mlango nyuma ya mgongo wa mhudumu aliyetoka.
Dina aliiendea tray iliyoletwa na mhudumu na kuvipekua vitu vilivyoletwa. Birika kubwa ilikuwa na chai, birika ndogo ilikuwa na maziwa na alipokifunua kitambaa kilichofunika sahani, akaiona keki iliyomtamanisha, akatengeneza tabasamu dogo. Huduma ya V.I.P! aliwaza.
Akiwa anakaribia kumaliza kunywa chai aliyoletewa, simu ya chumbani kwake iliita. Alishituka na kuiangalia. Ilikuwa ni mara ya kwanza kuisikia ikiita tokea alivyoingia asubuhi. Hakuwa na uhakika kama alikuwa akipigiwa yeye au simu hiyo iliingia kwa makosa. Aliamini kama angekuwa ni Richard ndiye anayempigia basi angempigia kwa simu yake ya mkononi kama alivyofanya asubuhi.
Akaifuata simu hiyo na kusimama kando yake, badala ya kuiinua, akasita. Akaiangalia kama vile kilikuwa kitu cha ajabu kilichojenga uhai na kutoa mlio. Kisha kama vile anategua bomu, aliinua simu hiyo kwa uangalifu na polepole, akaiweka sikioni.
“Haloh,” alisema kivivu baada ya kuipokea huku akiamini sio yeye anayepigiwa.
“Umekwisha kunywa chai?” sauti ya kiume kutoka upande wa pili wa simu ilisema.
Dina akatabasamu kwenye simu baada ya kuigundua sauti ya Richard.
“Nimeshakunywa,” alisema.
“Nasikia uko duka la kahawa ukinywa chai?”
“Ni kweli. Utakuja?”
“Labda nikishaoga.”
“Basi nakuomba ufanye kitu kimoja,” Richard alisema kwa utulivu. “Ukishaoga uvae lile gauni jeusi katika zile nguo tulizozinunua leo.”
“Umelipenda?”
“Ni kati ya nguo zilizokupendeza mno wakati ulipokuwa ukizijaribu dukani, pia ni nguo ya jioni inayostahili kuingia nayo restaurant kwa chakula cha usiku.”
“Sawa mkubwa,” Dina alisema kiutani.
“Utanifuata nikishamaliza kuoga?”
“Utakapokuwa tayari njoo duka la kahawa.”
Akiwa bado hajamaliza kuzungumza na Richard kwenye simu, simu yake ya mkononi ikaita. Akaiangalia pale kitandani ilipokuwepo, lakini hakwenda kuipokea, alisubiri hadi alipomaliza kuzungumza na Richard ndipo alipoifuata. Ilikuwa imekwishaita zaidi ya mara mbili, na alipokuwa anaichukua ikaita tena. Alikuwa John!
“Mbona umechelewa kuipokea simu?” John alianza na lawama. “Bado nipo kazini!” Dina alidanganya.
“Vipi mzima?”
“Mimi mzima, nilitaka kukufahamisha kuwa nimekwisharudi Dar, vipi huko Arusha?”
“Ni kipindi cha baridi na ni kali.”
“Umefikia hoteli ipi?”
“Masai Shield.”
“Masai Shield?” John aliuliza kwa sauti iliyojaa mshangao kuonyesha alikuwa haamini Dina kufikia kwenye hoteli kubwa na ya kifahari kama hiyo.
“Aisey, hiyo hoteli ni ya kifahari sana! Richard uko naye?”
Wivu! Dina aliwaza.
“Tumemuacha huko huko Dar. Nasikia anaweza akaja baada ya siku mbili au tatu,” Dina alidanganya tena.
“John, nitakupigia baadaye nikipata mwanya, sasa hivi bado tuko bize sana.”
“Poa, Dina. Baadaye.”
“Baadaye John.”
“I miss you!”
“I miss you too!”
Zikawa ni simu zilizofuatana! Mara baada ya kumaliza kuongea na John, simu yake ikaita tena. Safari hii alikuwa Mohsein!
“Dina, vipi mambo?” Mohsein alisema kwenye simu.
“Poa. Vipi, za huko Dar?”
“Huku poa. Wangu hata kunipigia simu kunifahamisha kama umefika salama?”
“Tumefika na kuingia kazini moja kwa moja na jamaa bado nipo naye karibu.”
“Mmefikia hoteli gani?”
Dina akahisi na huyo naye atapigwa na mshangao kama aliopigwa nao John. “Masai Shield!” alisema.
“Eti wapi Dina?” Mohsein alipayuka kwenye simu kwa sauti iliyojaa mshangao.
“Masai Shield!”
“Unaona Dina? Huyo jamaa yupo kwenye kukupumbaza…” “Nitakupigia baadaye!” Dina alisema kwa mkato na kukata simu. Dina akakunja uso kwa hasira. Alitamani aizime simu yake ili asiwe na mawasiliano na watu hao wawili ambao wote alijua hoja zao zilianza kujikita kumjadili Richard, na yeye kwa wakati huo hakuwa tayari kulijadili hilo. Alihitaji amani, na kwa mara ya kwanza akakiri kuwa, Richard ndiye aliyekuwa akimpa amani aliyokuwa akiihitaji tokea alivyowasili hapo Arusha. Akatamani awe karibu naye kwa wakati huo, kuliko kuwa na mazungumzo na watu hao wawili yanayomjadili Richard!
Dina alikwenda kuoga huku akihisi watu hao wawili wakiwa kama mzigo kwake. Alipomaliza kuoga, aliiva nguo aliyoambiwa na Richard aivae.
Alipendezwa na nguo hiyo! Akaenda duka la kahawa kumfuata Richard. Alipokuwa akitoka kwenye lifti kuingia duka la kahawa, kila aliyekuwepo eneo hilo kuanzia wafanyakazi na wateja ambao wengi wao walikuwa ni Wazungu walimwangalia. Alionekana kama mlimbwende aliyekuwa akitembea juu ya jukwaa la mashindano ya urembo. Akamwona Richard, akatengeneza tabasamu dogo lililopokewa na Richard aliyekuwa amekaa peke yake mezani.
“Umependeza!” Richard alisema wakati akiwa amesimama na kumvutia kiti Dina.
“Ahsante,” Dina alisema wakati akikaa. “Utaongeza chai?”
“Hapana.” Mhudumu akafika.
“Hapana, sihitaji chochote,” Dina aliyekuwa akitabasamu alimwambia mhudumu kabla ya kuulizwa.
“Ningependa tuzunguke zunguke nje ya hoteli uiangalia mandhari iliyoizunguka hoteli, lakini baridi iliopo huko nje ni balaa!” Richard alisema baada ya mhudumu kuondoka.
“Mchana kulikuwa na baridi vile, sasa hivi kutakuwaje huko nje! Lakini hii hoteli ni nzuri nje hadi ndani Richard, utadhani upo kwenye pepo! Na yale mandhari ya nje yanatamanisha uzunguke zunguke kama ulivyosema.”
“Mwezi wa Novemba tutarudi tena, hali ya hewa itakuwa imebadilika na tutaweza kutembea tembea kwa miguu. Au unasemaje?”
Kikazi au kibinafsi? Dina alijiuliza. Mazingira halisi ya siku moja hiyo yalikwisha kuonyesha kuwa, wameurudisha uhusiano wao, kwa hiyo ujio mwingine wa kuja tena Arusha hakuujua ungekuwaje. “Sawa,” alijibu kwa sauti ya chini huku akiiangalia meza. Alikiri kwa hatua ambayo wameifikisha kwa siku hiyo, kamwe asingeweza kukataa chochote atakachoambiwa na Richard!
“Unaonaje tukienda baa kupata kinywaji cha kuvuta muda ili baadaye tukale chakula cha usiku?” Richard alisema.
“Sawa,” Dina alikubali.
Wakaenda! Wakati wakisubiri mhudumu aje awaulize na kuwahudumia vinywaji watakavyoagiza, Richard akakumbuka kinywaji alichomwona nacho John wakati akimpelekea Dina alipowakuta kwenye hoteli ya BBH eneo la bwawa la kuogelea. Richard akajiuliza kama Dina angekiagizia tena kinywaji kile alichopewa na John?
Crème de Menthe! alikikumbuka kinywaji hicho.
* * * * *
Usiku walikula chakula ghali na Richard aliagiza kinywaji cha Champagne. Mhudumu alipowahudumia kwa mara ya kwanza kuwatilia kinywaji hicho kwenye glasi zao na kisha kuondoka, Richard akawa wa kwanza kuinua glasi yake juu na kumwambia Dina, “Tunywe kwa furaha ya kuurudisha uhusiano wetu. Cheers!”
Kauli hiyo ya Richard ikawa imemwingiza Dina ili akiri kwa kauli yake mwenyewe kuwa, hatua ya kukubali kuigonganisha glasi yake na ya Richard na kutamka neno ‘cheers’ atakuwa tayari amekubali kuurudisha uhusiano huo!
Kwanza Dina alionekana kusita na kujikuta akimfikiria John, kisha akamfikiria Mohsein! Tuhuma ya kuongeza mwanamume wa tatu ilimtuhumu, akauona ni uhuni usiokubalika kwake. Akakiri moyoni lazima amteme mmoja wao. Mohsein akawa kafara, akalengwa kuachwa yeye!
“Cheers!” alisema na kuigonganisha glasi yake na ya Richard, akanywa funda moja kabla ya kuirudisha glasi mezani.
Richard naye akafanya hivyo hivyo.
Baada ya kumaliza kula, hawakuondoka mapema mezani. Waliendelea kuagiza Champagne na kuzungumza, walionekana kutulia na mazungumzo yao yalitawaliwa na sauti za chini huku wakiwa wanaangaliana ana kwa ana. Mwanga hafifu wa mshumaa uliokuwa ukiwaka kwenye meza yao, ulionyesha sura zao zikiwa kwenye masikilizano na kuzingirwa na mandhari ya mahaba kwa kila mmoja wao.
Usiku huo, Dina hakulala chumbani kwake, alikwenda kulala chumbani kwa Richard!
* * * * *
Dina alihamia rasmi chumbani kwa Richard ilipofika siku ya pili baada ya kukubaliana chumba alichokuwa akilala kirudishwe. Wakaanza kuishi kama bibi na bwana. Walilala, waliamka na kwenda kazini pamoja huku uchipuaji wa penzi jipya ukishamiri kwa kasi. Kila jioni baada ya kumaliza kazi, walichagua pa kwenda kama hawakuhitaji kurudi mapema hotelini. Ikawa kama vile huko Arusha walikokwenda, walikwenda zaidi kama fungate kuliko kikazi.
***
MOHSEIN alibaki na kinyongo tokea siku aliyokatiwa simu na Dina! Kitendo hicho alikichukulia ni dharau aliyofanyiwa! Hakuamini kama kulikuwa na dharura iliyomfanya Dina aikate simu hiyo ghafla, tena bila hata kuomba samahani au kutoa neno lolote la kumtafadhalisha kabla ya kuikata simu hiyo. Moja kwa moja Mohsein akakichukulia kitendo hicho alichofanyiwa na Dina kilikuwa ni kiburi kilichoonyesha kumthamini Richard na kumdharau yeye!
Tukio hilo likawa limemdhihirishia kuwa, tayari Dina ameanza kuwa karibu na Richard! Ni mazingira ambayo alikuwa ameyatabiri awali kuwa, uendaji wa pamoja wa safari hiyo, lengo lake lilikuwa ni hilo, lakini Mohsein hakutarajia kama lingefanyika kwa haraka hivyo. Hofu iliyoingia wivu ikaanza kumtafuna, wasiwasi wa kuwa huenda Richard na Dina wamekwishafanya mapenzi ikampandisha jazba. Dhana hiyo ikamgubika kwenye wingu kubwa la wivu. Donge likamkaa kooni, akatambua kuwa, Dina ndio basi tena kwake! Kitendo cha kuhisi Richard amekwishaingiliana kimwili na Dina huko Arusha waliko kilikoleza moto wa wivu uliokuwa ukiuteketeza moyo wake. Akatamani kupiga kelele, akajizuia. Akaanza kumlaumu Dina moyoni kwa kujirahisisha kwake kwa Richard!
Kwa mara ya kwanza aliilaumu nafsi yake kwa kukubali kujiingiza kwenye penzi la kumpenda Dina, alikiri alikuwa akimpenda na alikuwa akimhitaji awe karibu naye wakati wote. Lakini pia, akamwona Dina kuwa ndiye aliyemwingiza kwenye penzi na baada ya muda mfupi ameamua kumwumiza moyo! Aliiona ilikuwa ni aina ya dhihaka aliyofanyiwa. Mohsein akaapa na yeye lazima amwumize Dina kama vile alivyoumizwa yeye!
Akaanza kufikiria njia za kulipiza kisasi za kumkomoa Dina. Akamkumbuka John!
Alikuwa hajawahi kumwona, lakini alikuwa na habari zake zote! Ni Dina ndiye aliyemwambia wakati alivyomjulisha kuwa ana mchumba! Dina alizungumzia mengi yanayomhusu John na kumjulisha hadi anakofanyia kazi. Akapanga amfuate John kazini kwake! Akaenda! Akamwulizia kwa mlinzi, mlinzi akamwambia yupo, Mohsein akaomba aitiwe.
John alipotoka akashangaa kumwona mtu asiyemjua!
“Naitwa Mohsein, najua hunijui, lakini mimi nakujua,” Mohsein alisema huku akiangaliwa na John kwa makini. “Nadhani wewe ni mume mtarajiwa wa Dina? Au sivyo?”
Kwanza John alisita kujibu, akaonyesha wasiwasi wa kutojua kule anakopelekwa kimazungumzo. “Ni nani aliyekueleza kama mimi ni mume mtarajiwa wa Dina?” aliuliza.
“Dina!” Mohsein alijibu kiuhakika.
John akaganda na kuonekana kushitushwa na jibu alilopewa. “Ilikuwaje akakwambia wewe?”
“Tunafanya kazi pamoja. Alishanipa kadi ya mchango ya Send off ili nimchangie. Katika maongezi yetu ya kawaida alinitajia unapofanya kazi na ndio sababu nipo hapa kwa ajili yako. Swali langu liko palepale, wewe ndiye mume wake mtarajiwa?”
“Ndiyo ni mimi,” John alijibu akionekana bado yuko kwenye wasiwasi.
“Sasa sikiliza, mimi ni mwanamume mwenzio!” Mohsein alizungumza kwa sauti ya kishari iliyokaza. “Hawa wanawake unatakiwa uwajue kabla ya kuamua kuwaoa. Uzijue tabia zao na ujue uadilifu wao. Je, una kifua cha kuzijua habari zake?”
John alianza kuonekana kuchanganyikiwa baada ya kuambiwa hayo. “Nipo tayari,” alisema akijaribu kuifanya sauti yake imjengee taswira kuwa ni kweli alikuwa tayari. Hata hivyo uso wake ulijenga hofu ya kile alichokuwa akisubiri kuambiwa.
“Tatizo sio kuwa tayari,” Mohsein alisema kama vile Mwalimu anayemwelekeza kitu mwanafunzi wake. “Kifua chako kipo tayari kuhifadhi siri ninayotaka kukwambia? Sio tena uende ukapayuke kwake, Ooh, Mohsein ndiye aliyeniambia!”
“Niamini, sitomwambia!” John alijaribu kusema kwa utulivu. Mohsein akawa na uhakika kwa wakati huo mapigo ya moyo ya John yalikuwa yakipiga kwa nguvu kifuani pake, na hapo ndipo alipokuwa akipataka! “Nadhani unajua kama Dina yuko Arusha?” alisema.
“Ndio nafahamu,” John alijibu huku sura yake ikionekana kama aliyepigwa na msukule.
“Najua amekuaga kuwa anakwenda kikazi, lakini kwa taarifa yako hakwenda kikazi, bali amekwenda kustarehe na mtoto wa tajiri mwenye kampuni, anaitwa Richard!”
Kutajiwa jina la Richard, John akahisi aina ya kizunguzungu kikiwa kimemwandama. Mapigo ya moyo wake yakaanza kumwenda mbio, damu ikamchemka na uso wake ukawa mzito. Akajizuia ili asiyumbe au kuanguka.
“Najua amekwenda Arusha, lakini kikazi!” hatimaye John alipata nguvu ya kusema. “Unataka kuniambia hakwenda kikazi?”
“Kiofisi imetafsiriwa kikazi, lakini ni zaidi ya hivyo!”
John alijishika kiuno akauinamisha chini uso wake na kuviangalia viatu vyake, akaonekana kufikiri haraka haraka. “Namfahamu Richard, lakini sikujua kama wana mahusiano ya aina hiyo,” alisema. “Kwa hiyo waliondoka pamoja?”
“Walipanda ndege moja kwenda Arusha!”
Ilikuwa ni habari mpya kwake! Dina alikuwa hakumwambia kama angesafiri kwa ndege. “Safari hiyo Dina alikuwa akiijua kabla?” aliuliza.
“Mbona aliambiwa mapema tu, siku tano kabla!” “Na alijua kama angesafiri na Richard?”
“Richard ndiye aliyemuita kumfahamisha safari hiyo na kumuahidi kuwa wangeondoka pamoja kwa ndege. Haikuwa safari ya ghafla!”
Dina alinidanganya! John aliwaza baada ya kukumbuka kuambiwa na Dina kwenye simu kuwa, Richard alibaki Dar es Salaam. “Naomba kukuuliza swali moja la msingi…” alisema na kumwangalia Mohsein machoni.
“Niulize,” Mohsein alisema kwa kujiamini.
“Kwa nini umekuja kuniambia habari hizi?” John aliuliza na sura yake ikawa makini kumwangalia Mohsein usoni.
Swali hilo lilionekana dhahiri kumyumbisha Mohsein na akaonekana kukosa jibu sahihi. “Ina maana nimekosea kuja kukwambia?” alijikuta akiuliza badala ya kujibu.
“Sina maana hiyo! Nataka kukuuliza swali jingine…” Mohsein hakujibu!.
“Ulikuwa ukinijua?”
“Tatizo nilikuwa sijakuona, lakini nilikuwa nikijua kuna mtu kama wewe ambaye anataka kumuoa Dina! Kwani vipi?”
John alishusha pumzi kwa nguvu kama aliyechoka, kisha akasema, “Basi nimekusikia na nitazifanyia kazi habari ulizonipa.”
“Wewe ni mwanamume mwenzangu na mimi hili jambo limeniumiza. Kwa nini akufanyie upuuzi wa namna hii? Dina atakuwa na maana gani ya kukubali kuolewa na wewe halafu papohapo atembee na mwanamume mwingine? Wewe chunguza hizi habari na mwenyewe utajionea. Lakini utakuja kunipa mkono kama nilichokwambia ni kweli!”
“Sawa nimekusikia,” John alisema na kuonyesha hakuwa tayari tena kuendelea kuwepo hapo. “Nashukuru kwa taarifa yako!” akamuaga Mohsein na kabla ya Mohsein hajajibu, John akaondoka.
Mohsein akabaki ameduwaa huku akimwangalia John alivyokuwa akiondoka.
John alirudi kufanya kazi akiwa na mtafaruku wa mawazo, muda mwingi alijikuta akizubaa kuzifikiria tuhuma alizotuhumiwa nazo Dina. Moyo wake ulikuwa ukifukuta na mapigo ya moyo wake yalikuwa yakienda kasi. Wivu ulikuwa umetawala kila sehemu ya kiungo chake na hatimaye kujigundua kuwa, hata mikono yake ilikuwa ikitetemeka! Kila wakati alikuwa akisonya peke yake na kuna kipindi alitamani aipige ngumi meza yake ya ofisini!
Ingawa hakuwa na uhakika na sababu hasa zilizomfanya mtu aliyejitambulisha kwake kwa jina la Mohsein kumletea habari hizo, lakini alikuwa mwepesi wa kuziamini kutokana na ukweli kuwa, hata yeye mwenyewe kwa siku za hivi karibuni alijengwa na mashaka makubwa yaliyomtishia kuwa, huenda Dina na Richard wakaurejesha uhusiano wa mapenzi kati yao baada ya Dina kuajiriwa kwenye kampuni ya baba yake Richard ambako Richard anafanya kazi. Lakini, laiti asingekuwa na hofu hiyo tokea awali, kitendo cha Mohsein kumjia na kumpa habari hizo kingemuweka kwenye mashaka ya kutomuamini. Na pengine angemuwekea dhana kuwa, huenda Mohsein alimtaka Dina kimapenzi na baada ya kukataliwa ndipo akaamua kumfanyia fitina.
Lakini ni ile hofu aliyokuwa nayo awali dhidi ya ajira aliyopewa Dina kwenye kampuni ya baba yake Richard ndio iliyomfanya avutike na madai yaliyotolewa na Mohsein, ujio huo wa Mohsein akauona kama vile Mungu alimwelekeza aje amthibitishie mashaka aliyokuwa nayo dhidi ya ajira hiyo kuwa, yalikuwa ni ya kweli! Pamoja na kuziamini habari alizoambiwa na Mohsein, lakini mara kwa mara John alijikuta akiwa kama haamini kama ni kweli Dina angeweza kumfanyia usaliti wa aina hiyo.
Ni usaliti ambao awali walipeana viapo vya kutosalitiana. Mara kadhaa walikwisha kumjadili Richard, wakaapa kupambana naye kuhakikisha hafanikiwi kuwatenganisha huku Dina akichukua jukumu la kula kiapo kuwa, hata iweje, katu asingeweza kurudiana na Richard! Leo kusikia Dina amekiasi kiapo hicho na kukubali kumsaliti, John alijihisi akiteketea kwa maumivu aliyoshindwa kuyafananisha na mengine yoyote yaliyowahi kumtokea tangu ajitambue kuwa anaishi duniani!
* * * * *
* * * * *
Jioni baada ya kutoka kazini, John hakwenda moja kwa moja nyumbani kama ilivyo kawaida yake, badala yake alikwenda baa na kukaa kaunta. Aliamua kukaa kaunta kwa sababu ya kuepuka kupata ushirika wa mtu anayejuana naye. Alihitaji awe peke yake, asizungumze na mtu yeyote. Mzongo wa mawazo ulishakuwa mshirika tosha kwake! Akanywa vya kutosha na muda wote wa kunywa alikuwa amekipakata kichwa kilichojiinamia kwenye mkono wake.
Hatimaye aliamua aondoke hapo baa. Aliuhisi ulevi ukiwa tayari kichwani, lakini hakuwa na uhakika kama alilewa vya kutosha, pengine aliridhika na kiwango alichokunywa na kukubali kinatosha. Alitoka baa na kuiwasha pikipiki, akarudi nyumbani. Alifika nyumbani usiku uliozidi saa nne, alikuwa hajala chakula cha usiku na hakukihitaji kukila. Alichohitaji ilikuwa ni pombe aliyokwishainywa kwa ajili ya kukabiliana na maumivu yaliyoletwa na Dina.
Wakati alipokuwa akiufungua mlango alijihisi alikuwa akiyumba, lakini aliamini alikuwa akiyumba kistaarabu. Akaenda moja kwa moja chumbani kwake na kusimama kwenye kabati la kuvalia nguo. Akaichukua picha iliyosimamishwa ambayo ilijengewa fremu yenye nakshi ya kupendeza. Ilikuwa ni picha aliyoipiga akiwa pamoja na Dina, waliipigia ufukoni ikizionyesha nyuso na vifua vyao. John alikuwa kifua wazi kama alivyokuwa Dina, wote walikuwa na mikufu ya dhahabu shingoni mwao, lakini Dina aliongezeka kwa kuwa na sidiria ya kuogelea huku miili yao na nywele ndefu za Dina zikionyesha kulowa maji kuonyesha walitoka kuogelea. Dina alikuwa nyuma ya John akiwa amemuegemea kwa kumuinamia huku ameizungusha mikono yake shingoni mwa John, wote walikuwa wakicheka kwa furaha. Ilikuwa picha nzuri!
Akiwa ameishika picha hiyo kwa tahadhari kama vile alikuwa akiogopa isianguke, John alirudi taratibu kinyumenyume huku akiiangalia picha hiyo hadi alipofika kitandani na kukaa. Akaendelea kuiangalia. Mawazo yake yakaanza kuhama, ikawa kama vile picha hiyo ilikuwa ikimkumbusha vipindi vyote vya raha wakati akiwa na Dina. Aliyakumbuka maeneo mbalimbali yaliyowaletea furaha walipokuwa pamoja, lakini kwa wakati huo yalikuwa yakimletea mashambulizi yaliyokuwa yakimwumiza moyoni. Kumbukumbu za furaha na vicheko vilivyotawala vikamkumbusha jinsi walivyokuwa wakizienzi enzi zao za upendo huku kila mmoja akijiona amefika kwa mwenzake.
Hali hiyo ya kuyakumbuka matukio hayo ilimfanya John azubae hapo kitandani kama taahira aliyeudhiwa. Ghafla akayahisi machozi yakimtoka. Akaiweka picha kandoni mwake, kisha akajilaza chali kitandani huku kichwa akiwa amekipakata kwenye viganja vya mikono yake na kuiangalia dari ya chumbani kwake. Machozi yakiwa yanatiririkia kupitia kwenye ncha za macho yake, John akaijenga taswira ya kumwona Dina alipokuwa akijinadi kwa kula viapo tofauti huku akimhakikishia kuwa, mwili wake ni kwa ajili ya John na sio Richard au mwanamume mwingine yeyote!
“Ni wewe ndiye uliyechaguliwa John!” John aliisikia sauti ya Dina ikisema na kufanya mwangi uliojirudia. Ilikuwa ni kauli aliyokuwa akiambiwa na Dina mara kwa mara. Lakini kwa hapo alipo, John aliiona kauli hiyo kama iliyozungumzwa miongo kadhaa iliyopita!
Hasira zikaanza kushindwa kudhibiti uwezo wa akili yake kuweza kujizuia. Akajiinua ghafla, kikafuatia kitendo cha haraka cha kuichukua ile picha na kuitupa kwa kuibamiza ukutani. Fremu ikajiachia na vipande vya vioo vilivyovunjika kuangukia chini na vingine kubingiria hadi kwenye picha ilipoangukia! Kwa sekunde kadhaa akaiangalia ile picha ambayo ilikuwa imejifunika, akalitafsiri tukio la kujifunika kwa picha hiyo ni kama dalili za kumalizika kwa penzi lao! Akajikuta akilikataa wazo hilo na kujaribu kuliondoa mawazoni mwake. Akili yake haikuamini kama tukio la aina hiyo linaweza likawatokea wao! Ndipo alipotambua kuwa, ni yeye ndiye anayetakiwa kuliokoa penzi hilo lisipotee. Ni yeye ndiye aliyetakiwa kumrudisha Dina kwenye himaya yake!
Kumbukumbu za kuwepo kijijini kwao zikamrudia, akamkumbuka mganga aliyekuwa amemwendea! Akayakumbuka maagizo ya mganga na dawa alizopewa ambazo alihakikishiwa zingemfanya Dina awe kama Kondoo wake endapo atajipaka dawa hizo usoni muda mfupi kabla hajakutana naye ana kwa ana.
Namwendea huko huko Arusha! aliapa.
****
JOHN aliamka mapema asubuhi kabla hakujapambazuka vizuri akiwa amenyongea na kukosa amani ya moyoni. Mawazo yake yalielea kwenye bahari ya wivu kila alipoijenga taswira ya uwepo wa Dina na Richard peke yao jijini Arusha. Furaha ilikuwa mbali na yeye na kuhisi maumivu ya moyo huku akihofia huenda moyo wake umeathirika kiafya. Alikiri kuzidiwa kete na Richard, mpinzani wake wa muda mrefu ambaye leo anamshuhudia akitumia utawala wa fedha kumyang’anya Dina kwenye mikono yake.
John aliiwazia karata yake ya mwisho ambayo ingekuwa ni silaha pekee ya kupambana na Richard; karata ya ushirikina aliyopewa na mganga! Ilikuwa ndio tumaini pekee la kumrudisha Dina mikononi mwake. Aliamini ndio itakayommaliza Richard, ni karata itakayozifanya pesa na utajiri wa Richard visionekane vina umuhimu mbele ya Dina. Ni karata itakayomfanya Dina atekwe na penzi lake na kumwona yeye ndiye kila kitu kwake!
Akaanza kuijenga taswira ya jinsi atakavyomkabili Dina huko Arusha na nguvu ya dawa atakayokuwa amejipaka muda mfupi kabla ya kumkabili itakavyoweza kuifanya akili ya Dina itii kumsikiliza kila atakalomwambia. Aliipanga safari hiyo iwe na lengo moja la kufika na kumchukua Dina na kurudi naye Dar, huku akimuacha Richard akiwa haamini kile kilichotokea mbele yake!
Lakini kabla ya kuianza safari hiyo ya kwenda Arusha, John alijikuta akipanga kwenda kumwona mama yake Dina na kumshitakia kuhusu usaliti unaofanywa na Dina, lakini pia, akaamua kuifanya safari hiyo iwe ya siri, hata mama yake Dina asiijue.
Alimkuta mama Dina akiwa amekwisha kujiandaa kimavazi kwa ajili ya kwenda kazini. Alikuwa peke yake mezani akinywa chai tupu kama kichangamsha mwili kabla ya kupata kifungua kinywa kamili atakapokuwa yuko kazini. Ujio wa John asubuhi ya mapema hivyo ulimshitua mama huyo. Akamkaribisha John, John akakaa kwenye meza. Naye akaungana na mama mkwe wake kujimiminia kikombe cha chai tupu.
Nafasi hiyo ya kunywa chai pamoja, John akaitumia kuzijenga tuhuma zake dhidi ya Dina huku mama huyo akiwa makini kuzisikiliza.
“Ni nani aliyekwambia hizi habari?” mama Dina aliuliza baada ya John kumaliza tuhuma zake.
“Aliyeniambia ni mtu wa karibu sana na Dina, lakini sitokutajia jina kwa sababu nilimuahidi kuwa, sitomtaja.”
“Sawa,” mama Dina alisema kwa utulivu. “Siwezi kukulazimisha unitajie, lakini kwa mimi ninavyofahamu, huyo mtu amekudanganya mwanangu. Richard namchukulia kama mtoto wa hapa nyumbani kutokana na jinsi tunavyoishi na wazazi wake na yeye mwenyewe analielewa hilo. Na hata Dina naye analielewa hilo! Uwepo wa pamoja kwa Richard na Dina haukuanza juzi kwa sababu ya Dina kuanza kazi kwenye kampuni ya baba yake Richard, walijuana zamani na ukaribu wao ni wa muda mrefu na wako hivyo kama mtu na dada yake, na sivyo hivyo unavyofikiri mkwe. Aliyekwambia amekudanganya!”
John akatambua alikuwa akitwanga maji kwenye kinu! Hakumlaumu mama huyo, lakini alishindwa kumuelewa ni vipi alikuwa akiliangalia tukio la kukutana kwa Richard na Dina wakati huo anaouzungumzia, kuwa walikuwa na ukaribu wa dada na kaka kama majirani. Akaona asipoteze muda kuanza kumwelezea kwa kumthibitishia kuwa, Richard na Dina walikuwa kwenye urafiki wa mapenzi wakati huo na angeweza kuiwekea msisitizo hoja hiyo kwa kumthibitishia kuwa, ni Dina mwenyewe ndiye aliyeizungumza.
“Basi huyu mtu atakuwa hakunidanganya mimi, bali amejidanganya mwenyewe,” John alisema kwa kuhitimisha kauli ya ‘kubali yaishe!’
“Uwe mwangalifu na binaadamu mwanangu, ni watu wabaya!” “Kweli mama!” John alisema.
“Halafu mkwe, mwenzio aliniambia ulikuwa na mpango wa kuleta mahari hivi karibuni, unatarajia lini?”
John akazikumbuka pesa hizo za mahari alivyompa mganga aliyemfuata kijijini. “Ni kweli nina mpango huo mama, nitamtuma mshenga hivi karibuni,” John alisema na kuyakwepesha kumwangalia usoni mama mkwe wake kwa sababu alikuwa akidanganya.
“Mahari ni muhimu mwanangu ukitoa mapema, itatupa sisi wazazi nguvu ya kumsihi mwenzako awe mwangalifu na vitendo vinavyoweza kuashiria mashaka kama haya uliyokuja nayo asubuhi hii. Toa mahari haraka ili na sisi tuanze vikao vya harusi na hili la vikao litasaidia kuiweka akili ya mwenzako kumfanya ajione tayari ni mke wa mtu ili awe na nguvu ya kukabiliana kuepuka vishawishi vingine. Usidhani kama kila mtu anapenda nyie mfunge ndoa, wapo watakaojitokeza kuizuia ndoa yenu isifanyike kwa kutumia hila tofauti kama huyo mtu uliyemtaja. Jitahidi mwanangu ulete mahari mapema ili muwazibe midomo wabaya wenu!”
“Mama nimekusikia, naahidi nitalitekeleza hilo hivi karibuni,” John
alisema huku hatia ikiwa imemtawala. Akaaga.
Kauli ya mama yake Dina kuhusu mahari ilimuweka John kwenye angalizo la awali kuwa, kama angekuwa ameilipa mahari hiyo angekuwa na nafasi ya kumkabili moja kwa moja Richard huko Arusha anakokwenda na angeweza kumpa onyo la kutojihusisha kimapenzi na Dina! Lakini kwa kuwa bado hajailipa mahari hiyo, hakuwa na haki ya kumkabili Richard. Uamuzi wowote wa kumfanyia rabsha Richard, Richard angeweza kuuchukulia hatua ya kumpeleka polisi!
* * * * *
John alianzia kwenda kazini ambako alitoa udhuru na kupewa ruhusa ya siku tatu bila ya malipo. Huko kukamchelewesha kuwahi kwenda kituo cha mabasi. Alipofika aliyakuta mabasi yote yakiwa yamejaa kukawa hakuna nafasi ya kuongeza abiria. Akalazimika kupanda basi linaloishia mji mdogo wa Chalinze ambako aliteremka na kwenda kusimama njia panda ambako hupita mabasi yanayokwenda Tanga, Arusha, Mombasa na Nairobi. Huko akafanikiwa kupata nafasi kwenye basi litokalo Morogoro ambalo lilikuwa likienda Arusha.
Baada ya safari ndefu ya kilomita kadhaa, basi lao likalazimika kusimama kwa muda wa dakika kumi mjini Mombo kwa ajili ya chakula cha mchana. John aliteremka kutoka kwenye basi lakini hakwenda kula chakula, ilikuwa ni kawaida yake akisafiri huamua kutokula hadi ahitimishe safari yake. Akaagiza soda. Wakati akiinywa soda, simu yake iliita.
Alikuwa Dina!
Simu hiyo ikamchanganya, akasita kuipokea moja kwa moja. Alikuwa hajajiandaa kiakili kuzungumza naye. Akahisi kama vile Dina amemwona hapo mjini Mombo akiteremka kutoka kwenye basi. Akagundua alikuwa akipoteza muda kwa kujituhumu kipumbavu. Akaipokea simu. “Hai,” alisema.
“Mh, vipi mambo?” Dina alisema kwa kuchangamka.
“Huku poa ni kama ulivyokuacha,” John alisema kwa sauti tulivu, lakini akilini hakukuwa na utulivu.
“Vipi huko?”
“Huku mzigo tu.”
“Kuna jipya lolote?”
“Ah, litoke wapi?”
John akapata akili ya kuuliza. “Huwa mnapiga kazi kuanzia asubuhi mpaka saa ngapi?”
“Huwa tunapiga hadi saa kumi na moja, baada ya hapo tunarudi hotelini.”
John akawaza, kama atawahi kufika Arusha angalau kwenye saa kumi na mbili za jioni, basi kwenye muda wa saa mbili usiku angeweza kumfuata Dina hotelini. Na huko angemchukua na kwenda naye kwenye hoteli ambayo angefikia, labda vinginevyo, Dina amwombe walale pamoja kwenye hoteli ya Masai Shield alikofikia. Lakini wazo hili la pili kidogo alijikuta akilitia wasiwasi kutokana na kutojua kama Dina na Richard wanalala chumba kimoja au kila mmoja na chake.
“Lakini sio kazi za kukuchokesha sana?” John alisema baada ya kuridhika na hesabu zake.
“Kiasi,” Dina alijibu kwa sauti ya maringo.
“Jamaa vipi, kishatia timu?” John kwa mara ya kwanza aliuliza swali lililomlenga Richard kwa aina ya utani.
“Nani Richard?”
John akagundua swali la Dina lilikuwa la kuvutia pumzi kulijibu swali hilo. Aliamini hakukuwa na sababu yoyote ya kuuliza hivyo wakati alikuwa akijua ni nani anayeuliziwa. “Ndiyo,” alijibu.
“Nasikia ameingia leo,” Dina alisema.
Hasira ikachana kwenye moyo wa John! Ananidanganya! aliwaza na kulaani kwa kumalizia na tusi. Ilibaki alimanusura ashindwe kuidhibiti akili yake, na alikwishaanza kuinua ulimi wake kutaka kusema mbovu kupitia kwenye simu, lakini ghafla busara ilimjia, akajizuia. “Kwa hiyo hamjaonana?” alisema huku akiilazimisha akili yake itulie.
“Bado sijaonana naye, labda nitakaporudi hotelini huenda nikamwona kama na yeye atakuwa amefikia huko.”
Likawa eneo jingine la John kujizuia baada ya kuongopewa tena! “Aisii,” alisema kwa unyonge na kutamani kuaga ili akate mawasiliano, lakini akashindwa kufanya hivyo kwa kuogopa Dina asije akaingiwa na hisia za mashaka za kujiona ameshitukiwa. Isitoshe, ni Dina ndiye aliyekuwa amepiga simu, kwa hiyo atalazimika asubiri hadi Dina mwenyewe atakapoaga kwenye simu.
“Okay John, nilitaka kusikia sauti yako tu. Huenda baadaye usiku nikakupigia tena,” Dina alisema.
John akashukuru Dina alivyotamka hivyo. “Poa Dina, hata mimi nimefurahi kuisikia sauti yako,” alisema.
“Kwa hiyo baadaye.” “Poa.”
Wakakata mawasiliano. John akasikitika peke yake huku akiirudisha simu mfukoni.
* * * * *
Waliwasili mjini Arusha mwanga wa jioni ukiwa umeshapotea na John alipoiangalia saa yake ikaonyesha zilikuwa zimebaki dakika chache kufika saa kumi na mbili na nusu. Alipoteremka kwenye basi akakumbana na baridi kali, akakodi teksi haraka kabla baridi haijatawala mwilini mwake. Akapelekwa kwenye hoteli moja ndogo iliyokuwa mitaa kadhaa kutoka stendi.
Aliingia hotelini na kukaribishwa.
“Utakaa siku ngapi?” Mhudumu wa mapokezi alimwuliza John. “Usiku mmoja,” John alijibu. “Kesho asubuhi naondoka!” Akapewa chumba kilichopo ghorofa ya kwanza.
Huko chumbani, John alioga haraka haraka, yalikuwa maji ya moto na yaliweza kuurudisha uchangamfu uliokuwa umepotezwa kutokana na uchovu wa safari. Akabadili shati, akavaa fulana nzito ya baridi. Kingine alichokibadilisha ilikuwa chupi, lakini suruali aliirudia ile ile aliyokuwa amesafiri nayo ambayo ilikuwa ni jeans. Baada ya kubadili hizo nguo, John alifikiria kwenda kula, lakini akalipuuza wazo hilo baada ya kuwaza huenda atakapokutana na Dina, Dina anaweza akamkaribisha chakula cha usiku kwenye hoteli ya Masai Shield. Hakuwa na uhakika na hali ambayo angeikuta huko, lakini alikuwa na matumaini Dina asingeweza kumletea ubishi wowote wakati wa mazungumzo yao.
John alizitoa kutoka kwenye begi dawa alizopewa na mganga, akaziandaa juu ya meza. Akiwa amekaa kwenye kochi dogo la humo chumbani, alizitia pamoja dawa hizo kwenye mkebe mdogo wa plastiki na kuzichanganya, baadaye akachukua kichupa kidogo chenye mafuta na kuyachanganya mafuta hayo pamoja na zile dawa. Akaanza kuzichanganya tena na wakati huo huo akitia nia iliyokusudia kumfanya Dina pindi atakapokutana naye, akili ya Dina ipumbazike. Baada ya kuimaliza shughuli hiyo, akaingia hatua ya kujipaka dawa hizo usoni na mikononi hadi aliporidhika. Akaenda kujiangalia kwenye kioo kama kulikuwa na mwonekano wowote wa kuonekana zile dawa alizojipaka, baada ya kuridhika hakuna dalili zilizoonyesha kuwa amejipaka dawa, John akajiandaa kutoka.
Alitoka hotelini na kukodi teksi iliyokuwa imeegeshwa kwenye baa iliyokuwa jirani na hoteli aliyofikia. Hakuwa mgeni na mji wa Arusha, hivyo mara tu baada ya kuingia kwenye teksi akamwagiza dereva ampeleke kwenye hoteli ya Masai Shield.
* * * * *
Richard ndiye aliyekuwa wa mwisho kumaliza kuvaa. Alikuwa amesimama mbele ya kioo akijiangalia alipokuwa akijifunga tai huku Dina akiwa amekaa kitandani naye akimalizia kujivika hereni kwenye sikio lake. Ni muda mfupi uliopita watu hawa wawili walikuwa wametoka kufanya mapenzi na kisha kuoga na kujiandaa kwa ajili ya kwenda kula chakula cha usiku na baada ya kumaliza kula, walikubaliana waende kucheza kamari kwenye Casino iliyomo humo humo hotelini. Richard ndiye aliyemshawishi Dina ili akaijue kamari inavyochezwa. Dina alikuwa hajawahi kwenye maisha yake kuingia kwenye Casino yoyote.
Wote walionekana nadhifu na mwonekano wao ulidhihirisha walikuwa ni watu wenye kuogelea kwenye maisha ya kifahari. Dina alikuwa amevaa gauni la jioni lenye kitambaa chepesi, refu na lilifuata sambamba na mwonekano wa umbile lake kuanzia kifuani hadi chini. Kwa yeyote ambaye angemwona asingekuwa na hoja yoyote ya kupinga ughali wa gauni hilo dukani na ulimbwende uliopo kwa msichana huyo. Licha ya mwonekano aliokuwa akionekana Dina ndani ya gauni hilo, lakini Dina alizidi kurembeshwa na vito vya thamani vya dhahabu yenye kiwango bora inayomeremeta. Shingoni alikuwa na mkufu mwembamba na mrefu, wenye kito cha almasi iliyokuwa ikifanya miali inayong’aa kila kilipogeuka, masikioni mwake kulikuwa na hereni za mviringo mfano wa bangili huku vidole vyake viwili vya mkono wa kushoto vikivikwa pete, moja yenye kito cha almasi na nyingine iliyotengenezwa kwa mfano wa ua lichanualo. Kwenye maungio ya kiganja na mkono wa kushoto kulionekana bangili nne zilizolaliana huku mkono wake wa kulia ukarembeshwa na saa ndogo nyembamba ya kike yenye thamani kubwa. Vitu vyote hivyo vilivyokuwa mwilini mwake zilikuwa ni zawadi alizonunuliwa na Richard.
“Upo tayari?” Richard alimwuliza Dina na kukitingisha kidogo kitanzi cha tai kwa ajili ya kuiweka sawa.
Dina aliinuka moja kwa moja kutoka kitandani na kusema, “Twenzetu!”
Wakatoka.
Walikaribishwa na mkuu wa mgahawa ambaye alikwishaanza kumzoea Dina na akawa anamuita kwa jina la ‘Mrs. Richard!’ Walikaa kwenye meza ambayo ilikuwa imewekwa kibao chenye neno ‘Reserved’ na mara baada ya kukaa, mhudumu alikiondoa kibao hicho.
Wote waliagiza chakula kilichofanana, viazi vilivyokaangwa na kutiwa vitunguu vilivyokaangwa juu yake na kuku wa kukaanga wa kuchovywa na unga wa ngano uliochanganywa na mayai. Pamoja na kila mmoja kujaziwa maji baridi kwenye glasi ndefu mfano wa puto zilizokuwa zimejenga ukungu wa baridi, lakini pia Richard aliagiza mvinyo mweupe kwa ajili ya kusukumizia chakula chao.
Baada ya kumaliza kula, Richard na Dina hawakuwa na haraka ya kuondoka mezani, hawakutaka kuwa watu wa mwanzoni kuingia Casino. Waliamua kuagiza mvinyo mwingine na kuendelea kuzungumza kwa taratibu, yeyote ambaye angewaona asingesita kuwatabiri kuwa ni wapenzi wapendanao.
* * * * *
John aliteremka kutoka kwenye teksi iliyokuwa imesimama sawia kwenye mlango unaoingia moja kwa moja ndani ya jengo la hoteli ya Masai Shield. Teksi ikaondoka na yeye akageuka kuangalia mlangoni. Wahudumu wawili wenye sare za kazi wanaopokea wateja waingiao, walikuwa wamesimama ndani ya mlango wa kioo unaojifungua wenyewe pindi unapokaribiwa na mtu anayetaka kuingia au kutoka. Wote walimwona John alivyoteremka kwenye teksi na wakawa wanamwangalia.
Mara tu mlango ulipojifungua, John akaisikia harufu nzuri kutoka humo ndani; ni harufu ya aina moja ambayo duniani kote utakumbana nayo mara tu ukiingia kwenye hoteli za kifahari kama hizo. Alipokuwa akiingia aliwasalimia watu wale na wote waliitika kwa nidhamu na kumkaribisha.
Mteja ni Mfalme! John aliwaza baada ya wahudumu wale kumuinamishia vichwa wakati walipokuwa wakisalimiana. Ilikuwa ni mara yake ya kwanza kuingia kwenye hoteli hiyo ingawa alikuwa akiiona na kuipita kwa mbali wakati wa siku za nyuma alipokuwa akija Arusha. Aliingia ukumbini kulikokuwa na mandhari ya kupendeza iliyokuwa ikimulikwa kwa taa zenye nuru hafifu ambayo miali yake ilichomoza kutoka kwenye matundu madogo na membamba yaliyopo kwenye dari iliyonakshiwa kwa ujenzi wa kisanii.
***JOHN ameamua kumuibukia DINA huko huko Arusha.....kimya kimya....NII kitatokea?
**** MAMA DINA amekumbushia suala la mahali.....pagumu hapo!!!
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment