Search This Blog

Sunday, 19 June 2022

WIVU - 3

 





    Simulizi : Wivu

    Sehemu Ya Tatu (3)





    “Nimekupa uisome ili ujue haitawezekana kufunga ndoa, hadi miezi mitatu ipite! Hukuyaona masharti niliyoandikiwa? Si umeona siruhusiwi kuchukua ruhusa zaidi ya siku moja? Ndoa inahitaji uwe huru, ikibidi uwe na ruhusa ya zaidi ya wiki moja, wengine huchukua hadi likizo. Kwa hiyo tarehe uliyoitaja haitowezekana. Itabidi tusubiri hadi baada ya miezi mitatu ndio tufunge ndoa!”



    Kauli hiyo ikamnyong’onyesha John, ikamchanganya kwa muda huku akiuona mpango wake ukielekea kushindwa.



    Hakukubali!



    “Tunaweza tukaoana bila sherehe!” John alisema kama aliyekurupuka huku akionekana kukosa umakini.



    “Usinichekeshe John! Tuoane bila ya sherehe kisa nini?” Dina aliuliza katika hali inayomshushua John.



    John akaanza kuueleza uwongo wake, Dina akausikiliza mwanzo hadi mwisho.



    “Muda wa wewe kwenda kusoma na muda niliopewa kazini hautatofautiana sana,” Dina alisema kwa utulivu baada ya kumsikiliza John.

    “Mimi nitakuwa tayari kukusubiri hadi urudi! Kwani kuna haraka gani mpaka tufunge ndoa kwenye mazingira kama hayo yasiyo na sherehe? Nitasubiri hadi utakaporudi ili tuweze kufanya kitu cha uhakika. Hata hivyo, unadhani upande wetu utalikubali wazo lako? Eti tuoane kwanza halafu sherehe baadaye? Najua nao watakujibu kama hivi ninavyojibu. Mimi nakuomba usisumbuke kuwapa ushauri huo upande wa kwetu. Nakushauri kitu kimoja,” Dina akanyamaza na kumwangalia John aliyekuwa amesimama kama aliyeumbuliwa huku akionekana kukosa hoja.

    “Fanya hiyo mahari iletwe kama ulivyopanga. Itakuwa vizuri ukiilipa kabla hujaondoka nchini ili uonekane kweli una dhamira ya kunioa!”



    Pigano la kwanza dhidi ya Richard, John akakiri amekwishalipoteza!



    ***



    RICHARD akiwa amekiegesha kidevu juu ya vidole alivyovifumbata pamoja huku mikono yake ikiwa imeegemea juu ya meza ya ofisini kwake, alikuwa ametulia katika hali hiyo kwa muda mrefu na kuonekana kutekwa mawazo na kitu alichokuwa akikifikiri. Ilikuwa kama fumbo mfumbie mjinga! Alikuwa akikifikiria kitendo cha kuajiriwa Dina hapo ofisini kilivyokuwa kimemshitua, kilimshitua kutokana na kitendo hicho kufanyika siku chache baada ya kutoka kuzungumza na baba yake kuhusu msichana huyo huyo ambaye alikiri anampenda na yupo tayari kumuoa.



    Kuajiriwa kwa Dina katika mazingira aliyoyachukulia kuwa ni ya kumshitukizia ambayo yalifanyika kimya kimya kisha akakabidhiwa awe chini ya uongozi wake, Richard aliwaza jinsi baba yake alivyokuwa hakufanya tena rejea ya mazungumzo yaliyomhusu msichana huyo tokea pale mara ya mwisho walivyolizungumzia suala lake na matokeo yake ni kumleta hapo akiwa amekwisha ajiriwa.



    Richard alidhani kuajiriwa kwa Dina hapo ofisini kungekuwa ni sababu tosha ya kumfanya baba yake alirejeshe tena suala la msichana huyo kwenye mjadala wao uliokuwa haujamalizika kuhusu kumuoa, lakini alishangaa kumwona baba yake hakufanya hivyo! Ukimya huo wa baba yake ulimshangaza, lakini pia, alishangaa na kujiuliza kwa nini baba yake hakutaka kumshauri au kumdokeza kama alikuwa na mipango ya kumwajiri Dina?



    Awali katika siku za mwanzoni, ajira hiyo ya Dina ilimsumbua kichwa kutokana na kumchukulia Dina kuwa ni adui yake baada ya kumkataa na kisha kukubali kuposwa na John. Tukio hilo la Dina kuajiriwa na kisha kuletwa kwenye idara yake kufanya kazi; tena bila ya barua ya ujulisho, lilimfanya apigwe na butwaa na kutomwelewa baba yake kwa uamuzi huo. Akawa anajiuliza mara kwa mara, ni nini kilichomfanya baba yake amwajiri msichana huyo wakati alikwishamfahamisha kuwa, alikataa kuolewa naye?



    Lakini wingu la uteguzi wa kitendawili hicho kilichokuwa kimemuweka kwa siku kadhaa kwenye sintofahamu iliyokuwepo kati yake na baba yake kuhusu ajira hiyo ya Dina, Richard alianza kukitegua kitendawili hicho baada ya baba yake kumwandikia barua ya kiofisi zikiwa zimepita takribani siku tano tokea Dina kuajiriwa. Aliikumbuka barua hiyo iliyomjulisha kuwa, Dina atakuwa chini ya uongozi wake na ikamjulisha kiwango cha mshahara ambacho angelipwa.



    Kiwango cha mshahara ndicho kilichokuwa chachu ya kumzindua akili! Mara ya kwanza alipokuwa akikisoma kiwango hicho alijikuta akiamini kuna makosa ya kisarufi yaliyofanyika kwenye barua hiyo, lakini baada ya kuona kiwango hicho kilikuwa kimeenda sambamba kwa kurudiwa kimaandishi, akawa amepigwa na butwaa baada ya kuona hakukuwa na maantiki yoyote iliyostahilisha Dina alipwe mshahara mkubwa kama huo wakati hana ujuzi wowote wa kazi!



    Richard alikumbuka jinsi alivyoingiwa na ushawishi wa kwenda kumkabili baba yake mara baada ya kuletewa barua hiyo ili amwulize ni kwa nini alimwajiri Dina bila ya kushauriana na yeye hali akijua kuwa yeye na Dina hawaelewani? Isitoshe, pia alikusudia kumwuliza ni kwa nini ameamua kumlipa mshahara mkubwa kama huo wakati wapo wafanyakazi walioajiriwa wakiwa na ujuzi wao ambao hawapati mshahara kama huo? Akakumbuka kabla ya kuuchukua uamuzi huo wa kumkabili baba yake, alijiwa na wazo lililomfanya asite kuuchukua uamuzi huo baada ya kujiuliza kuwa, huenda kuna sababu iliyomlazimisha baba yake kumwajiri Dina na kuamua kumlipa mshahara wa aina hiyo. Wazo hilo ndilo lililompa nafasi ya kuufikiria uamuzi huo wa baba yake na kabla hajaenda mbali kifikra ndipo alipoweza kukitegua kitendawili hicho alichotegwa na baba yake!



    Chachu ya kukitegua kitendawili hicho ilimjia Richard baada ya kuuwazia mshahara ambao angepewa Dina na kuyawekea mashaka maamuzi hayo. Akahisi lazima kungekuwa na sababu nyuma ya maamuzi hayo yaliyolazimisha Dina aanze kazi na mshahara kama huo. Ndipo alipogundua kuwa kiwango hicho cha mshahara kilikuwa ni aina ya chambo kilichovikwa kwenye ndoana alichotegeshewa Dina ili kumlainisha na aione familia ya mzee Ken ipo karibu naye. Ulikuwa mtego! Richard aliwaza. Mtego ambao ulikusudiwa kwa Dina ili aulegeze msimamo wake wa kukataa kuolewa na familia hiyo! Richard alitabasamu peke yake baada ya kugundua kuwa, Dina amechezwa shere kwa kutengenezewa wigo asioweza kuutoka; wigo utakaomfanya amkubali ili asiupoteze mshahara huo!



    Richard akakiri kwa mtaji huo, isingekuwa ajabu kumwona Dina akiurudisha uhusiano uliokuwa umetoweka kati yao!



    Ghafla akamkumbuka John! Akakumbuka kuwa, Dina yupo karibu kuolewa na John! Badala ya wazo hilo kumwingiza kwenye unyonge kama ilivyokuwa awali kila alipokuwa akikumbuka jambo hilo, safari hii Richard alijikuta akiliwazia jambo hilo kwa mtazamo tofauti. Kilichomfanya awe na mtazamo huo tofauti ni kule kuajiriwa kwa Dina hapo ofisini. Aliamini kuletwa kwa Dina na kuwekwa karibu yake kungemwezesha kuua Tembo kwa ubua. Richard alitengeneza tabasamu la ushari baada ya kujiona safari hii ana nafasi kubwa ya kumpata Dina hata kama ataolewa na John! Aliamini bado angekuwa na nafasi ya kumchukua na kutembea naye kwa siri akiwa ameolewa!



    Wazo hilo la kuja kutembea na Dina akiwa ameolewa na John lilimfariji mno na kujisikia burudiko kwenye moyo wake. Aliuona huo ndio ungekuwa wakati mwafaka wa kulipiza kisasi kwa John! Na kwake ingekuwa ni furaha ilioje kama angefanikiwa kukifanya kitendo hicho katika mazingira hayo Dina akiwa ameolewa! Kitendo hicho kingemfurahisha zaidi moyo wake kwani angejiona angekuwa analipiza kisasi katika njia inayostahili, na ingekuwa ni nafasi yake ya kumdhihirishia John kuwa alifanya makosa kumpora Dina akiwa mikononi mwake! Alitaka liwe fundisho kwa John ili mara nyingine asivamie maeneo yanayomilikiwa na watu wenye pesa kama yeye!



    Kisasi chake alitaka kisiishie kwa kumchukulia John mke wake halafu iwe basi; lakini pia, alitaka John aje atambue kuwa yeye anatembea na mke wake! Na sio tu John ajue kuwa mkewe anatembea na yeye, lakini pia, aliapa kuitumia nafasi hiyo kuhakikisha anamdhibiti Dina kimapenzi hadi awe chizi kwa ajili yake na John alifahamu hilo! Alipenda amwone John akitesekea penzi kama alivyoteseka yeye wakati alipokuwa akimbembeleza Dina warudiane. Alitaka kusiwepo maelewano kati ya John na Dina kwenye ndoa yao. Alipania kuisambaratisha ndoa hiyo, alitaka amshuhudie John akihangaika kwenda kuomba msaada kwa Padri ili kuiokoa ndoa yake bila ya mafanikio! Alitaka Kanisa lifikie mahali likubali kuvunjwa kwa ndoa hiyo, kisha yeye ndiye aje kumuoa Dina!



    Lakini wakati akiifikiria mikakati hiyo ya kumsulubisha John na kumrudisha Dina kwenye himaya yake ya mapenzi, Richard alikiri bado kulikuwa na tatizo mbele yake ambalo alikiri kuwa ni kubwa na linalohitaji aina nyingine ya maamuzi! Tatizo hilo aliliangalia kama vile Mwanasayansi anavyokiangalia kirusi cha hatari kinachotaka kujipenyeza kwenye mfumo mzima wa mawasiliano ya chombo muhimu.

    Alikuwa Mohsein!



    Alimwona Mohsein kama mtu aliyekuwa akihatarisha harakati zake ziingie kwenye ugumu usio wa lazima. Na tatizo halikuwa kwa Mohsein mwenyewe, bali lilikuwa ni Dina! Aligundua Dina alikuwa akimpenda Mohsein. Kulikuwa na dalili za wazi zilizokuwa zikionyeshwa na Dina kuwa amekwisha kimahaba kwa Mohsein na akalikumbuka tukio la kuwafumania wakiwa wamevigusisha pamoja vichwa vyao kwa aina fulani ya mahaba wakati alipokuwa amewaingilia ghafla ofisini.



    Tukio hilo lilikuwa likimtafuna Richard, wivu na chuki ya kumchukia Mohsein ikawa imejijenga, na hakutaka kujidanganya; kwa sababu dalili zote zilikuwa ziko wazi zikionyesha kuwa, kama kuna mtu anayeweza kumpata Dina kirahisi bila ya kujali kikwazo cha uchumba uliopo kwa John basi Mohsein ndiye mwenye nafasi hiyo! Richard akajionya endapo hatochukua hatua za haraka, uwezekano wa Mohsein kumchukua Dina mbele ya macho yake usingezuilika!



    Richard alikiri hilo ni tatizo na akaliona ni kubwa na la hatari! Asingekubali litokee huku akiliona! Afanye nini? alijiuliza. Amfanyie fitna Mohsein afukuzwe kazi? Aliiona hiyo ndio njia pekee itakayomuweka kwenye amani, lakini pia, aliogopa kitendo hicho kingeweza kigandulika na Mohsein kuwa, amefukuzwa kazi kwa ajili ya kuonewa wivu dhidi ya Dina! Hilo lingeweza kumchochea Mohsein kufanya juhudi za ziada kuhakikisha anatembea na Dina kama sehemu ya kulipiza kisasi! Richard alipolifikiria hilo, mchomo wa wivu ukapenya moyoni mwake! Akajionya kuwa, maamuzi yoyote ya kumfukuza kazi Mohsein yangeleta janga badala ya suluhisho.



    Akajaribu kujituliza na kufikiri kwa kutumia uwezo wa akili badala ya akili za nguvu. Akajiuliza, ni njia ipi ya kuitumia ili Mohsein aachane na fikra za kumtaka Dina kimapenzi? Njia pekee aliyoiona kuwa inaweza ikamsaidia, ni kufanya kila njia ili Mohsein ajue kuwa, yeye ndiye aliyemwajiri Dina na Dina yuko hapo kwa ajili yake. Alikuwa na uhakika endapo Mohsein atalifahamu hilo, basi angeogopa kujihusisha kimapenzi na Dina kwani angeelewa, Dina ni mali za bosi wake!



    Kwa kuwa alikuwa na safari ya kikazi ya kwenda Morogoro, Richard akapanga mara atakaporudi kutoka Morogoro ndipo angeyaonyesha makucha yake kuwa yeye ndiye bosi na mmoja wa wamiliki wa kampuni hiyo. Akaamini, mwelekeo wa uelewa huo ungemtisha Mohsein!



    Laiti angelijua kosa analolifanya, kamwe Richard asingeenda safari hiyo ya Morogoro!







    * * * * *



    Ilikuwa siku ya pili tokea Richard alivyokuwa amekwenda Mkoa wa Morogoro kwa ajili ya kufanya ukaguzi wa ndani wa mahesabu kwenye kituo chao cha mafuta ambacho ni kikubwa kuliko vingine vyote mkoani humo. Mohsein akawa amekaimu nafasi yake kiofisi.



    Ilikuwa ni kawaida kwa kila inapokuwa Richard hayupo ofisini kikazi, Mohsein ndiye anayekaimu madaraka yake, labda itokee wote wasafiri safari moja ya kikazi. Siku ambayo Richard aliondoka kwenda Morogoro aliacha maagizo kwa Mohsein kuwa, kukahesabiwe vifaa alivyokuwa ameviorodhesha kwenye nyaraka aliyomkabidhi Mohsein ili vikahesabiwe upya baada ya kutokea utata wa orodha kamili ya mahesabu kuhusu vifaa hivyo vilivyokuwa vimehifadhiwa stoo na alitaka shughuli hiyo ifanyike siku hiyo hiyo aliyokuwa akisafiri ili akirudi akute majibu.



    Lakini baada ya Richard kuondoka, Mohsein akazembea kuianza kazi siku hiyo kama alivyokuwa ameagizwa, akasubiri hadi siku ya pili asubuhi ndipo alipoikabidhi kazi hiyo kwa kumpa Dina akaifanye badala ya kuifanya yeye.



    Ilikuwa ni kazi ya siku moja, lakini Dina akaingia nayo siku ya pili akiwa bado hajaimaliza!



    Ikiwa ndani ya siku ya pili kazi hiyo haijamalizwa, na ikiwa ni siku ya tatu tokea Richard alivyoondoka kwenda Morogoro, ilipofika saa tano asubuhi, Mohsein akaanza kuingiwa na mashaka kuwa, huenda Richard angerudi siku hiyo na kuikuta kazi ikiwa haijamalizika. Kwa kumhofia Richard asije akaja kumbwatukia atakapoikuta kazi hiyo haijamalizika na wakati jukumu hilo alipewa yeye, Mohsein aliamua kumfuatilia Dina ili ajue amefikia wapi na endapo ikibidi amsaidie.



    Alimfuata Dina aliyekuwa peke yake kwenye hiyo stoo ambayo haikuwa kubwa ya kutosha na iliyozungukwa na makabati ya chuma yaliyokuwa wazi ambayo yalibeba vifaa mbalimbali vya kampuni, akamkuta yupo katikati ya kuhesabu.



    “Bado hujamaliza?” Mohsein alimwuliza Dina.



    “Ungenikuta nimekwishamaliza,” Dina alijitetea.

    “Lakini kulikuwa na baadhi ya maboksi ilibidi niyapangue kwanza kisha ndio nikaendelea kuhesabu.”

    “Kwani bado sana?”



    “Kama utanisaidia, tutamaliza mapema.”

    “Umebakiza upande upi?”



    Dina akamwonyesha Mohsein upande wa makabati yaliyokuwa na vifaa hivyo. Mohsein akaenda kuhesabu. Iliwachukua dakika arobaini na tano hadi kuimaliza kazi hiyo.



    “Chukua hesabu nilizozipata ili uingize kwenye mahesabu yako,” Mohsein alisema huku akimpa Dina karatasi aliyokuwa akiingizia nukuu za hesabu zake alizozipata.



    Dina aliichukua karatasi hiyo na kusogea kwenye mwanga zaidi ambako alikwenda kuegemea kwenye kabati lililokuwa na uwazi na kuutumia uwazi huo kama meza ya kurekebishia hesabu zake huku akiwa amesimama. Mohsein akajiunga naye. Wakasaidiana kuzifanya pamoja hesabu hizo.



    Wakati walipokuwa wakiendelea kuzifanya hesabu hizo, mabega yao yalikuwa yakigusana mara kwa mara na hali hiyo kuonekana ni ya kawaida kwao hadi walipomaliza na kupata uhakika wa hesabu walizozirekebisha.



    “Nakushukuru kwa msaada wako,” Dina alisema, akiwa amegeuka kumwangalia Mohsein.



    Mohsein akamwangalia Dina. “Usijali,” alisema.



    “Lazima nijali bwana…” Dina alisema na kutabasamu huku akiendelea kumwangalia Mohsein.

    “Ningekuwa sijaimaliza hii kazi kama sio wewe kuja na kunisaidia!”



    Mohsein naye akatengeneza tabasamu na kusema, “Poa.”



    Ghafla kukajenga ukimya kati yao ulioleta faragha humo ndani huku kila mmoja akishindwa kujisogeza alipokuwa amesimama. Wakatekwa na ukimya, kisaikolojia wakajiona wapo kwenye faragha iliyojitokeza huku kila mmoja akikiri nafsini mwake kuwa ilikuwa na jambo mbele yao linalohitaji kufanywa kati yao. Wakaangaliana, wakawa mabubu kwenye vinywa vyao, lakini macho yao yakawa yanazungumza lugha ya ukimya ambayo kila mmoja aliielewa maana yake. Mapigo ya mioyo yao ikaanza kwenda kasi. Mohsein akawa wa kwanza kuonyesha kusudio lake kwa kuuangalia mdomo wa Dina, akauinamisha uso wake na kuusogeza usoni kwa Dina na mdomo wake kuulengasha mdomoni mwa Dina!



    Mohsein akasita kuupeleka moja kwa moja mdomo wake kinywani kwa Dina, akasikilizia marejesho ya Dina yatakuwaje. Dina akawa ameganda kama aliyepigwa na shoti ya umeme, naye akajikuta akiuangalia mdomo wa Mohsein kwa macho yaliyoonyesha haiba ya kukubali kitendo kinachofuatia, kisha akafumba macho. Mohsein akaupeleka mdomo wake kinywani kwa Dina na papi zao za midomo kugusana. Mohsein akaupitisha ulimi wake..!



    Dina akaupokea!



    Kila mmoja alilihisi joto la ulimi wa mwenzake wakati ndimi zao zikinyonyana. Dina akauhisi mkono wa Mohsein ukianza kumpapasa kwenye paja lake ukiwa umeipandisha juu nguo yake, akawahi kuuzuia alipouhisi ukitaka kuingia ndani zaidi. Akaendelea kukaza msuli wake wa mkono kuuzuia mkono wa Mohsein uliokuwa ukitaka uende zaidi ya hapo.



    Vita ya kuzuiana mikono iliendelea huku ndimi zao zikiendelea kunyonyana!



    *****



    HAIKUWA wiki njema kwa John tokea alivyojibiwa na Dina kuwa hakukuwa na uwezekano wa wao kuoana mapema kama alivyokuwa amekusudia. Sababu iliyokuwa imetolewa na Dina, John aliiafiki kuwa ni ya msingi, lakini alilaani kipengele kilichotumika kwenye barua ile kilichomnyima Dina kupata ruhusa ya kupumzika kikazi hadi miezi mitatu ikatike! Kipengele hicho alikiona kama vile kilikusudiwa kuingia kwenye dhamira yake ya kumuoa Dina isifanikiwe.



    Hofu dhidi ya Richard iliendelea kujikita kila alipoifikiria miezi hiyo mitatu ipite bure bila ya kufunga ndoa na Dina, lakini wakati huo huo miezi hiyo ikitumika akimwona Dina akiwa karibu na Richard! Kihoro hicho ndicho kilichokuwa kikimtesa kwa wivu! Hakuamini kama Dina angekuwa na ubavu wa kuendelea kuhimili vishawishi vitakavyofanywa na Richard kwa wakati wote huo, hali hiyo ilimfanya awe na wingi wa hisia kuwa, Dina atamsaliti!



    Hofu ilikuwa ikimtawala na kumuweka kwenye hali ngumu kila alivyokumbuka kuwashuhudia wanawake wengi wakiwaacha wanaume waliokuwa wakiwapenda na kuwafuata wanaume wenye pesa! John alizidi kuumia moyoni jinsi wanawake hao walivyokuwa hawajali maumivu yaliyowakuta wanaume waliokuwa nao baada ya kuwaacha, na wakati mwingine walidiriki hata kuwatolea maneno ya kebehi wakati wanaume hao walipokuwa wakiwabembeleza warudiane.



    Fedha! John alinyong’onyea baada ya kuikiri nguvu ya chombo hicho. Awali kabla ya Dina kuajiriwa na kampuni ya mzee Ken, John aliwahi kujisifia kuwa ni mwenye bahati ya kumpata msichana aliyeumbika kama Dina aliyekuwa tayari kumkataa mwanamume mwenye pesa kwa ajili yake na kukichukulia kitendo cha Dina kumkataa Richard kama kigezo chake cha kupendwa. Alikuwa akijiona ni shujaa na kuhisi burudiko moyoni mwake kila alipokuwa akionana na Richard na kumcheka moyoni. Na wakati Richard alipokuwa akijaribu kumbembeleza Dina ili warudiane, John alifikia hali ya kumshangaa na kumwona kama aliyepungukiwa na akili!

    Hakutaka kuamini Dina angeweza kumsaliti kupitia kwa mtu aliyekwisha kumkataa tokea awali. Lakini kwa upande wa pili hisia zilikuwa zikiendelea kumuonya mara kwa mara kuwa, ukaribu wa kikazi kati ya Dina na Richard ungewalazimisha watu hao wawili wajenge maelewano kati yao ambayo Richard angeyatumia kurejesha tena uhusiano wa mapenzi uliotoweka! John aliuhisi moyo wake ukienda mbio na dalili za kupandwa na shinikizo la damu zilikuwa zikimwashiria kutokana na wivu ulioitawala akili yake. Akakiri moyoni kuwa, kitendo cha kurudiana kwa Dina na Richard kama kitafanyika kingemwumiza mno!



    Akaingiwa na akili ya kutaka kumshawishi Dina aache kazi, lakini alijikuta akijijibu mwenyewe kuwa hilo lisingewezekana! Aliamini hilo lisingewezekana kutokana na ukweli alioukiri mwenyewe kuwa, nyota yake ya mapenzi ilikuwa imefunikwa na nyota ya Dina! Dina alikuwa na sauti dhidi yake, alilolitaka ndilo litakalofanyika na aliamini Dina angelikataa wazo lake hilo na asingekuwa na ubavu wa kumlazimisha!



    Ndani ya nafsi yake alikuwa akiandamwa na hatia iliyokuwa ikimsuta kutokana na ukweli kuwa alikuwa akimpenda mno Dina. Hatia hiyo ikawa inamuingiza kwenye hofu ya kuachwa na hata kudiriki kutawaliwa na mawazo ya kijinga kuwa kusingekuwa na mbadala wa maisha mengine bila ya Dina! Akauhisi ule unyonge wa kutokuwa na ushawishi wa kumuweka Dina chini ya himaya ya amri yake ukimzomea.



    Mawazo yake yakarudi kule kule kwenye kuwahi kumuoa Dina mapema kabla ya Richard hajafanikiwa kurudisha uhusiano na Dina, aliamini hatua hiyo angalau ingemuweka kwenye haki ya kummiliki Dina kuwa mkewe, haki ambayo angeitumia kukabiliana na Richard kama angediriki au hata kujihusisha na Dina kimapenzi. Lakini ukweli huo ulikuwa mbali!



    Alijua asingeweza kumshawishi Dina aache kazi kwa sababu Dina asingemsikiliza. Lakini pia asingeweza kumkabili Richard na kumuonya dhidi ya Dina kwa sababu Dina bado hajawa mkewe, na asingeweza kumvaa Richard kwa mkwara wowote kwa sababu mwenzake ana pesa inayoweza kutumika kwenye vyombo vya sheria na vyombo hivyo kumgeukia yeye na akajikuta akiswekwa mahabusu au pengine hata gerezani!



    Akili yake ikajiwa na wazo la kimbilio la wanyonge; kwenda kwa waganga kwa ajili ya ushirikina! Angalau kwa kiasi fulani wazo hilo lilianza kumfariji baada ya kuifikiria hatua hiyo. Hakuwa ni mtu aliyependa kujihusisha na vitendo vya ushirikina, lakini aliamini ushirikina upo. Alishawahi kuzisikia sifa za mara kwa mara walizokuwa wakisifiwa waganga waliopo kijijini kwao, sifa ambazo zilikuwa zikitolewa na watu wa mkoa wao. Hatua ya kuwafuata waganga kama hao aliamini kama ataichukua ingemsaidia kupambana na Richard. Fikra za kujipa matumaini kuwa dawa ya mtu mwenye pesa ni kupambana naye kwa kutumia njia za kishirikina ikaanza kumtawala kichwani.



    Kwa upande huo aliamini angemwendea fundi wa shughuli hizo na kumtaka afanye uchawi wake ili Dina anapomwona Richard aingiwe na hisia kama vile ameona kinyesi! Pili, angemtaka fundi huyo afanye utaalamu wake wa kuifanya nyota yake iitawale nyota ya Dina ili aweze kumdhibiti kimapenzi. Aliamini kitendo hicho kingemfanya awe na sauti mbele ya Dina na Dina angegeuzwa kuwa kama Kondoo kwa kutii kila ambalo angelizungumza. Fikra hizo zikamrudisha John kwenye Ukamanda wa kujiona yupo tayari kurudi tena kwenye uwanja wa vita kupambana na Richard! Kwa mtazamo huo, John akaisifia akili yake kupata wazo la kishirikina!



    Akaipanga siku maalumu ya kwenda kumwona mganga kijijini kwao!



    * * * * *





    Usiku, Dina alichelewa kupata usingizi kutokana na fikra zilizokuwa zimemtawala karibu kutwa nzima ya siku hiyo; fikra za kumfikiria Mohsein na tukio lilitokea siku hiyo kati yao kwenye stoo ya kazini kwao! Ni tukio lililomlazimisha awafikirie watu wawili kwa wakati mmoja, Mohsein na John! Alikiri tukio la kufanya mapenzi na Mohsein siku hiyo lilikuwa limedhihirisha jinsi lilivyoishinda ile dhamira yake aliyojipa awali ya kuchukua hadhari na maamuzi yake pindi anapokuwa na Mohsein. Alikuwa ameshindwa kuitekeleza! Alikiri kushindwa huko kulitokana na ukweli kuwa, akiwa mbele ya Mohsein alikuwa akijisikia raha wakati wote kama vile alirogwa naye!



    Kumruhusu Mohsein afanya naye mapenzi kulimdhirishia ni namna gani moyo wake ulivyotekwa na jamaa huyo. Hakutaka kuamini kama ametokea kumpenda, kwa sababu aliamini ni John pekee ndiye aliyetokea kumpenda. Alikubali kuwepo kwa hisia fulani zilizokuwa zikimfanya afarijike kila anapokuwa yuko na Mohsein, lakini alipingana na nafsi yake kuwa amempenda Mohsein. Aliamini mapenzi yake yapo kwa John na kukiri John ndiye kila kitu kwake. Lakini hata hivyo, nafsi yake iliendelea kumsuta kwa kukataa kuungama kuwa, kitendo cha kufanya mapenzi na Mohsein kilishatia ufa kwenye msimamo wake huo wa kuwa, John ni kila kitu kwake!



    Ufa huo ulioutikisa msimamo wake ulimfanya akiri kwa mara ya kwanza kuwa, binadamu ana udhaifu ndani ya nafsi yake. Ni udhaifu wenye msukumo mkubwa wa ushawishi pale unapojikuta umezungukwa kwa ukaribu na ushawishi huo. Alikiri njia pekee ya kuepusha kuingia kwenye majaribu ni kukaa mbali na ushawishi wa aina hiyo; vinginevyo ni kushawishika kama alivyojikuta akishawishika kwa Mohsein! Yeye na Mohsein walikuwa na ukaribu, ukaribu uliokuja baada ya nafsi yake kukiri mapema kuwa Mohsein ni mwenye haiba ya kupendeza, jamali wa sura na umbile! Kukiri huko kukawa kama aliyeiruhusu sumu imwingie kwenye mishipa yake ya damu! Huo ndio ukawa udhaifu wa kwanza uliomwingiza kwenye ushawishi ambao ulikuja kuchochewa na ukaribu wao wa kila siku. Sumu ikaanza kumtafuna!



    Akamruhusu Mohsein afanye naye mapenzi katika mazingira ambayo mwenyewe alikiri kuwa, alikubali mwenyewe kwa hiari yake. Kukubali kuwa alikifanya kitendo hicho kwa hiari yake kuna kipindi akawa anakijutia kiaina, lakini pia majuto hayo yakawa hayamwumizi sana kichwa kwa sababu alichokifanya ulikuwa ni uamuzi wake mwenyewe! Kuyumba huko kimawazo kukamdhihirishia jinsi alivyomkubali Mohsein kwenye nafsi yake na hakutaka kujidanganya kwa hilo, kwa kuwa alishakiri alikuwa akiufurahia ukaribu uliopo kati yake na Mohsein!



    Kukiri huko kulimfanya kila alipokuwa akimfikiria Mohsein na kile kitendo kilichofanyika stoo kulimletea msisimko fulani, lakini pamoja na kuwaza hivyo, fikra za kumfikiria John nazo zikawa zinajipenyeza muda huo huo. Alimfikiria John kwa sababu aliamini ndiye anayempenda na aliamini pia, hata ndoa yao nayo ingefanyika kama walivyopanga. Lakini pia akakiri moyoni kuwa, bado angeendelea kumruhusu Mohsein kuwa mtu wake wa karibu kuiba kufanya naye ngono!



    Katika hali ya kujipanga kisaikolojia, Dina alikiri upo uwezekano wa kuiratibu mihimili yenye uzito tofauti ya kupenda watu wawili kwa wakati mmoja. Alijua mambo hayo huwa yanafanyika na huendelea kufanyika kila kukicha kwa wanandoa kufanya mapenzi nje ya ndoa. Dina aliamini matendo hayo huwa yanajulikana ndani ya jamii na wakati mwingine huchukuliwa kama ni matukio ya kawaida, lakini hugeuka kutokuwa ya kawaida, pale fumanizi linapotokea.



    Ni matukio yanaohusisha kada tofauti, wake na waume. Wapo waheshimiwa wenye heshima zao, wapo wenye elimu zao, wapo wenye madaraka makubwa na wakati mwingine hata kwa viongozi wa kidini, wote hao hujihusisha na vitendo hivyo. Udhaifu wa mwanadamu! Dina aliwaza. Lakini kwa upande mwingine hisia za kupingana na mawazo hayo zilimjia. Akazitazama katika mtazamo wa Kishetani, lakini akakiri ni mtazamo uliokaa kifalsafa zaidi kuliko Kibaolojia. Akakubali kuwa, inapotokea binadamu akatawaliwa na udhaifu huo huwa ni vigumu kuuondoa kirahisi kama mahubiri ya dini yalivyo. Akakiri kuwa, hata yaliyomtokea kati yake na Mohsein yalitokana na udhaifu wa kibinadamu na sio Ushetani!



    Jambo pekee ambalo aliliona lingemuweka kwenye utulivu na amani katika kukabiliana na hali hiyo ni kujipanga kuitunza siri hiyo isijulikane na John! Siri ndio ingetumika kuliendesha zoezi hilo la kumtumikia John na Mohsein, kwa sababu kwa upande wa John ni kuwa alimpenda, na kwa upande wa Mohsein ni kwamba nafsi yake ilitaka awe naye. Hata hivyo, ili kuitunza siri hiyo alikiri mmoja alipaswa amjue mwingine na sio wote kutojuana! Alimwona Mohsein ndiye mwenye haki ya kutakiwa kumjua John, ili ajue ni mchumba wake na anahitaji kuheshimiwa.



    Hisia za Shetani! alijiambia wakati akiyawaza hayo. Lakini akazipuuza kwa kujiweka kibaolojia zaidi kuwa yeye ni binadamu wakati mwingine huendeshwa na nafsi yake inavyomshawishi! Akauona huo ndio ukweli wenyewe na anapaswa akabiliane nao!



    Richard! Tukio la kumkumbuka lilikuja kama onyo asilolitarajia, onyo lililomkumbusha kuwa kuna mtu muhimu aliyekuwa amesahauliwa. Dina aliiona hatari iliyopo mbele yake endapo Richard atagundua mahusiano ya mapenzi yaliyopo kati yake na Mohsein! Alijua ugunduzi huo ungemletea Richard wivu wa mapenzi ambao aliamini ungeweza kuleta kizaaza cha kumpotezea kazi mmoja wao, ama yeye au Mohsein! Au wote kwa pamoja! Dina alikuwa na uhakika Richard alikuwa bado hajaachana na nia yake ya kutaka kumuoa, na alijua lazima angekuja kumwomba ili warudiane. Dalili zilikuwa za wazi zilizokuwa zikimuashiria kuwa Richard alikuwa bado akimuhitaji, kuanzia uangaliaji wake hadi uzungumzaji. Kila kitu kilijidhihirisha kwa Dina kuwa, Richard alikuwa bado akiendelea kuteseka na penzi lake!



    Tokea awali, baada ya kuajiriwa na kufahamu kumbe Richard naye anafanya kazi kampuni hiyo hiyo, Dina alijipanga mapema kuwa, endapo Richard atamwomba waurudishe uhusiano wao, asingemkubalia! Na alijiandaa kuitumia sababu ya kuchumbiwa na John kuwa ni kigezo cha kumkatalia. Alijua uamuzi huo ungeendeleza uadui kati yao, lakini aliamini Richard asingeweza kumfukuza kazi kwa sababu sio yeye aliyemwajiri, bali ni baba yake!



    Lakini ni hili tatizo jipya lililojitokeza ndilo lililokuwa likiichachafya akili yake. Mahusiano yake na Mohsein! Hakutaka kujidanganya na tatizo hilo. Alijua ni tatizo kubwa na lingeleta balaa endapo Richard atagundua kuwa yeye na Mohsein wana uhusiano wa mapenzi. Alikuwa na uhakika tatizo hilo litawasha moto wa kutisha hapo ofisini kati ya watu hao wawili; Richard na Mohsein! Pengine hata kufikia kupigana au kufanyiana visa vya kuudhi. Hofu ikaanza kumuumiza Dina na kichwa kikamuuma, mashaka yakamwingia kuwa anaweza akasababisha mtafaruku utakaoivuruga ofisi nzima na kusambaa hadi kwa mzee Ken na mzee Ken angemwambia mama Richard na mama Richard angemwambia mama Dina, na mama Dina angemwambia baba Dina na baadaye taarifa hizo zingemfikia John!



    Wote hao wangemwona yeye ndiye chanzo cha matatizo na mzigo wote wa lawama ungemwangukia. Uamuzi wa kufukuzwa kazi alikuwa na uhakika ungefanyika, na aliamini kusingetokea mtu yeyote kati ya hao ambaye angemwonea huruma, isitoshe hata wazazi wake wasingesita kumlaani kwa kupoteza kazi iliyokuwa ikimpatia kipato kizuri ambacho kingekuwa msaada mkubwa kwa wazazi wake hao.



    Akiwa amechanganyikiwa na kuzinduka kwake huko, Dina alikurupuka kitandani na kuichukua simu iliyokuwa pembeni yake, akampigia Mohsein.



    “Sema Dina,” sauti ya Mohsein ilisikika baada ya kuipokea simu. Ilikuwa nzito yenye kujiamini na iliyotulia, ikionekana kama aliyekuwa ametoka usingizini.



    “Ulikuwa umelala?” Dina aliuliza kwa tahadhari, hakutaka kuingia moja kwa moja kwenye hoja.



    “Siwezi nikasema hivyo, lakini nilikuwa nimepitiwa na usingizi nikiwa kwenye kochi.”



    “Ulikuwa ukifanya nini hapo kwenye kochi?”



    “Nilikuwa naangalia runinga nikapitiwa na usingizi. Vipi?” “Mohsein, kuna jambo muhimu nataka nikwambie,” Dina alisema kwa sauti iliyokuwa na umakini.



    “Niambie mpenzi,” Mohsein alisema kwa kujiamini na kiburi cha ujivuni kikawepo ndani yake huku sauti yake ikiendelea kujenga kujiamini.

    “Nakuomba uhusiano wetu asiujue mtu yeyote pale ofisini!”



    Kimya kidogo kikapita, kisha Mohsein akasema, “Kwa nini unasema hivyo? Au unadhani mimi ni mropokaji?”

    “Sina maana hiyo, lakini sitaki watu wajue!”



    “Ni hilo tu?” Mohsein aliuliza kiwepesi.

    “Hofu ondoa, labda uje utamke wewe mwenyewe kwa watu!”



    Dina akagundua jinsi Mohsein alivyoijibu hoja hiyo kiwepesi. Akaingiwa na wasiwasi.

    “Mohsein please, niko serious!” alisema kwa sauti yenye kusisitiza.



    “Mbona unaonekana kama una hofu fulani?”



    “Ni kweli nina hofu Mohsein…stori yake ni ndefu, lakini nataka ujue kuwa, yeyote atakayeufahamu uhusiano wetu na habari hizo zikamfikia Richard, ujue ama sote kwa pamoja au mmoja wetu, kibarua kitaota nyasi!”



    “Mbona sikuelewi Dina?” Mohsein aliuliza na safari hii sauti yake iliondoka kwenye kujiamini na kutwaliwa na wasiwasi.



    “Ni stori ndefu kama nilivyokwambia, kesho asubuhi tutakapokutana ofisini nitakuelezea.”



    Siku ya pili walipokutana, Dina alimpa ukweli wote Mohsein!



    Ikawa ni mara ya kwanza Mohsein kutambua kuwa, Dina ana mchumba na harusi ingefanyika baada ya miezi mitatu ijayo. Akatajiwa jina la mchumbiaji na kukiri alikuwa hamjui. Lakini kibaya zaidi ni pale alipoupata mshituko uliomwogopesha, aliposikia kuwa, hata Richard ni mmoja kati ya watu wanaowania kumuoa Dina!



    * * * * *



    Richard alirudi kutoka Morogoro baada ya siku tatu akaenda ofisini moja kwa moja. Alifika ofisini saa sita mchana, akawasalimu baadhi ya wafanyakazi aliojisikia kusalimiana nao. Aliwakuta Mohsein na Dina wakijiandaa kutaka kwenda kula chakula cha mchana. Tukio hilo la kuwaona Mohsein na Dina wakitaka kutoka pamoja likapenyeza mchomo mkali wa wivu moyoni mwake.



    “Dina nisubiri!” Richard alimwambia Dina kwa sauti iliyoonyesha ana jambo muhimu analotaka kulizungumza kwake. Kisha akatoka ofisini humo bila ya kusubiri jibu.



    Dina na Mohsein wakaangaliana kwa macho yaliyoingiwa na wasiwasi, hofu ikaingia kwenye mioyo yao na kila mmoja akaingiwa na sintofahamu ya agizo hilo.



    “Kwani vipi?” Mohsein aliuliza kwa sauti ya chini kama vile alikuwa akiogopa Richard asisikie huko alipo.



    Dina akayainua na kuyashusha mabega yake. “Sijui!” alijibu. Mohsein akauangalia mlango wa ofisi yao kama vile alitarajia Richar angerudi tena. Kila mmoja akawa ameingiwa na hofu kuwa, Richard amekwishapata habari ya mahusiano yao, lakini kila mmoja akashindwa kumwuliza mwenzake swali hilo.



    “Kwa hiyo nikusubiri?” Mohsein aliuliza huku sauti yake ikionyesha kujiamini kwake kulishaondoka.



    “Sio vizuri akituona tukiondoka pamoja!” Dina alisema kwa sauti ya kuonya.

    “Wewe nenda kale!”



    Mohsein akawa kama aliyepigwa butwaa na jibu la Dina.

    “Kwa hiyo hutokuja?” aliuliza huku akionyesha kutoridhishwa na uamuzi wa Dina.



    Dina akaonekana kidogo kama amechanganyikiwa.

    “Agh, Mohsein we nenda!” alisema huku sauti yake ikiwa na hasira. Hakutaka Richard awakute wakiwa bado wako pamoja humo ofisini ingawa ni ofisi yao kikazi. Hatia ilikuwa imemjenga. Kwa mara ya kwanza alijitambua kuwa, alianza kumwogopa Richard!



    Mohsein akamwangalia Dina kwa uso uliohamanika, akasema kwa unyonge, “Poa.” Kisha akatoka na hali ile ile ya unyonge.



    Kila mmoja alikiri moyoni kuwa, ujio wa Richard umekuja kutibua fungate yao ya siku mbili iliyokuwa imewapa uhuru humo ofisini kwa kuonyeshana kuwa ni wapenzi wapendanao huku wakifanyiana dalili zote za kimahaba na wakati mwingine walifikia hadi kujiamini kwa kuitumia nafasi ya kuwepo kwao wawili ofisini kunyonyana ndimi zao.



    Ilikuwa kama vile Paka akiondoka… Ndivyo ilivyokuwa kwao!



    Dina akiwa amebaki peke yake humo ofisini baada ya Mohsein kutoka, alijikuta akishindwa kuendelea na kazi. Akili ilikuwa imekwama kuwaza jambo lolote, agizo alilopewa na Richard lilikuwa kama lililoitia akili yake ugonjwa wa kiharusi.



    Laiti isingekuwa mahusiano ya mapenzi aliyoyaanzisha na Mohsein, kamwe agizo hilo lisingemshitua! alijiambia moyoni. Angejiamini kama alivyokuwa akijiamini siku za nyuma wakati alivyokuwa akiitwa na Richard ofisini na alikuwa hamwogopi hata pale walivyokuwa wakizungumza ana kwa ana. Lakini tukio hilo la kuanzisha mahusiano ya mapenzi na Mohsein, ghafla kukawa kumeibadilisha hali hiyo. Sasa alianza kumwogopa Richard tena kwa kasi kubwa kuliko alivyotarajia. Ikawa kama vile alikuwa amejitengenezea mwenyewe Shetani wa kuja kumtisha!



    Maswali yaliyotawaliwa na hofu kuwa huenda taarifa za mahusiano yake na Mohsein zimekwisha kumfikia Richard yalikuwa yakirindima kichwani mwake na kuhisi hicho ndicho alichokuwa akiitiwa. Akajiuliza, ni kipi hasa alichokuwa akikihofia? Ni ile hofu ya kugundulika mahusiano yake na Mohsein? Au ni kufukuzwa kazi baada ya kugundulika mahusiano hayo? Dina akakosa utulivu wa akili wa kuchanganua mchanganuo huo!



    Richard akaufungua mlango wa humo ofisini bila kupiga hodi. Hakuingia moja kwa moja, alisimama mlangoni na kuuzuia mlango usijifunge. Kitendo hicho kikamshitua Dina, lakini kibaya zaidi ni pale alipoonyesha dalili zote za kumwogopa Richard! Bahati iliyoje, Richard akawa hakuuona woga uliokuwepo usoni mwa Dina.



    “Njoo ofisini!” Richard alisema kwa sauti kavu, kisha bila ya kupoteza muda wala kuhangaika kumchanganya machoni Dina, akatoka.



    Dina akashusha pumzi, akajizoa kitini na kusimama, kisha akatoka ofisini. Alimkuta Richard amekaa nyuma ya meza akiandika, Dina akaenda kukaa kwenye kiti kilichopo mbele ya meza ya Richard kwa nidhamu ambayo hajawahi kuifanya tokea siku aliyoanza kuingia kwenye ofisi hiyo.



    Uingiaji wa Dina humo ofisini haukumfanya Richard auinue uso wake kumwangalia ingawa alijua kuwa ni Dina ndiye aliyeingia. Aliendelea kuandika kama vile hakuna mtu aliyeingia. Dina akaenda kukaa kwenye kiti cha wageni kilichopo mbele ya meza ya Richard. Kitendo hicho nacho hakikumshitua Richard kuinua macho yake kumwangalia mtu aliyekaa. Dakika kadhaa zilipita huku akiendelea kuandika na bila ya kumsemesha Dina. Hali hiyo ikawa inamtesa Dina Kisaikolojia na kujikuta akihofia hata kujikohoza. Ilikuwa ni kama vile ni zamu ya Richard kumtesa Dina!



    Hatimaye Richard aliacha kuandika, akauegemea mgongo wa kiti kwa aina fulani ya ujivuni na kumtazama Dina kwa mara ya kwanza tokea alivyokuwa ameingia.



    “Dina,” Richard aliita kwa sauti ya kuonyesha yeye ni bosi. Dina aliitikia kwa sauti iliyokwama kusikika vizuri.



    Kabla ya kuendelea kuzungumza, Richard akaonekana kama vile ameigundua hali aliyokuwa nayo Dina, akaonyesha dalili ya kutaka kumwuliza kama alikuwa anaumwa.



    “Jumatatu tunakwenda Arusha kikazi!” Richard alisema ghafla. Ule mwonekano aliouonyesha kutaka kuiulizia afya ya Dina ukawa umetoweka usoni mwake. “Tunakwenda kufanya ukaguzi wa ndani wa mahesabu. Huenda ikatuchukua wiki moja au zaidi,” akanyamaza na kumwangalia Dina machoni.



    Dina akayakwepesha macho yake. Kauli ya Richard ilikuwa shambulio alilokuwa hakujiandaa nalo.



    “Ni moja ya utaratibu wa kazi zetu ulivyo,” Richard akaendelea bila ya kusubiri jibu la Dina. “Huwa ni kawaida kwenda mikoani kufanya ukaguzi wa ndani wa mahesabu kila baada ya muda fulani, hutegemea na mkoa wenyewe. Juzi na jana nilikuwa Mororgoro kwa shughuli kama hiyo. Kwa hiyo mkoa unaofuata ni Arusha. Jiandae kwa safari hiyo!”

    “Tunakwenda wangapi?” Dina aliuliza.



    “Wawili, mimi na wewe!” Richard alijibu kisha akamwangalia Dina kwa macho ya kuuliza kama ana swali jingine.



    Dina akabaki kimya.



    “Sawa?” Richard aliuliza na kumwangalia Dina kwa mtazamo wa kumsanifu.



    Dina alionyesha kusita, kisha akajibu kwa sauti ndogo yenye unyonge kwa kusema, “Sawa.”



    * * * * *



    Mohsein alirudi ofisini baada ya kuutumia muda wa kula mchana kwa kunywa soda na keki, hamu ya kula ilikuwa imemtoka! Alimkuta Dina akiwa amejiinamia ofisini. Kumwona Dina akiwa kwenye hali hiyo, moja kwa moja akajua Dina amepata tatizo na bila ya kujiuliza, akahisi tatizo hilo litakuwa limesababishwa na Richard!



    “Vipi?” Mohsein aliuliza akiwa ameinama huku akijaribu kukiinua kichwa cha Dina aliyekuwa amekilalisha juu ya meza.



    Dina akakitikisa kichwa chake kumtaka Mohsein amuachie. Mohsein akahisi kuna tatizo kubwa kuliko alivyolichukulia awali.



    “Dina!” Mohsein aliita akiwa ameuondoa mkono wake kichwani kwa Dina na kuufanya mhimili wake wa kuegemea kwa kuukita juu ya meza.

    “Mhh,” Dina aliitikia bila ya kuuinua uso wake.



    Mohsein akahisi Dina alikuwa akilia. Hali hiyo ikamchanganya! Akapatwa na kihere, “Kwani vipi?” aliuliza.

    Badala ya kujibu, Dina akashusha pumzi kwa nguvu huku akijiinua na kukaa vizuri. Hakuwa alikuwa akilia, lakini alionekana kuikaribia hali hiyo. Akaangalia juu ya meza kisha asiseme lolote.



    “Richard amekwambiaje?” Mohsein aliuliza huku akiwa na uhakika ni Richard ndiye aliyemfikisha Dina kwenye hali hiyo.



    “Amenitaka niende naye Arusha kikazi!” Dina alisema bila kuondoa macho yake mezani. Sauti yake ilikuwa imenyongea na uso wake kuonekana kuzidiwa na mawazo.



    “Ahh!” Mohsein aliguna kwa sauti iliyotaharuki.

    “Lini?” aliuliza.

    “Jumatatu!”



    “Amekwambia mnaenda wangapi?” Mohsein aliuliza kwa kihoro cha kuogopa jibu atakalopewa.



    “Mimi na yeye!”



    Mohsein akatoa tusi la kumtukana mzazi wa Richard!



    Mchomo wa wivu ulikuwa umepenya moyoni mwa Mohsein, akaonekana kuchoka kama aliyeibuliwa kutoka kwenye msukule, akaongoza taratibu hadi kwenye meza yake na kukaa. Nguvu zilikuwa zimemuishia!



    “Jamaa amepania!” Mohsein alisema kwa sauti ndogo na kuonekana kama aliyekuwa akiongea peke yake.

    “Umemjibu nini?” safari hii aliipandisha juu sauti yake kutaka Dina asikie.



    Dina akamwangalia Mohsein kwa mara ya kwanza tokea alivyokuwa ameingia.

    “Ulitaka nimwambieje?” naye aliuliza kwa sauti ya taratibu huku akionekana hana cha kujitetea.



    “Mwambie unaumwa huwezi ukaenda!” Mohsein alibwata na kuonyesha wivu ulikuwa ukichukua nafasi yake kumchanganya.



    Dina hakujibu. Kimya kikapita kati yao.



    Kwa mara ya kwanza, Mohsein akagundua ni kwa kiasi gani alikuwa akimpenda Dina na kwa wigo gani aliokuwa akimhitaji awe naye karibu. Wivu ulikuwa ukirindima na kumtafuna. Alihofu safari hiyo Richard aliipanga kwa kuikusudia kwa lengo la kupata faragha atakayoitumia kumbembeleza Dina ili atembee naye kimwili.



    “Kwa hiyo?” Mohsein aliuliza kama mpumbavu aliyechanganyikiwa huku akimwangalia Dina.



    “Kwa hiyo?” Dina alirudishia swali kwa sauti ile ile ya taratibu huku akionyesha kushangaa kwa kutomwelewa Mohsein.



    “Nenda kamfahamishe kuwa unaumwa na hutoweza kwenda safari hiyo!” Mohsein alisema kwa msisitizo.



    “Wacha tu, niende!” Dina alisema kwa mkato.



    “Uende naye Arusha?” Mohsein aliuliza kama vile hakuamini alichokisia.



    “Ghafla nimwambie kuwa naumwa?” Dina alisema.

    “Atanishangaa kumlalamikia hivyo baada ya kutajiwa safari!”



    “Yeye si alikuwa Morogoro! Utamwambia una karibu siku mbili ulikuwa unaumwa!”



    “Atataka kujua kwa nini sikumwambia palepale? Na atataka kujua kama kazini nilikuwa nakuja siku zote. Akijua kama nilikuwa nakuja siku zote, atajua siumwi bali nasingizia ugonjwa kwa kuikataa safari!”



    Mohsein akanywea! Akaonekana kushindwa kuendelea kumshawishi Dina aikatae safari hiyo.



    “Kwanza wewe kazi yenyewe hujaijua vizuri, kwa nini asinichukue mimi?” Mohsein alilalamika na kuuonyesha dhahiri kuumizwa na wivu aliokuwa nao. “Kwani wewe Arusha huna ndugu?”



    Uso wa Dina ukaonyesha mshangao kutokana na swali aliloulizwa. Akatingisha kichwa kukataa.

    “Sina!” alisema.

    “Kwa nini unaniuliza hivyo?”



    “Kama ungekuwa na ndugu yeyote ningekushauri ukalale kwake baada ya kufika Arusha.”



    Dina akatingisha tena kichwa na kusema, “Sina!”



    “Mimi ninaye dada yangu, anaishi Kaloleni. Unaonaje nikiongea naye?”



    “Ili nifikie kwake?” Dina aliuliza, akaonekana kumshangaa Mohsein. “Bila ya kufanya hivyo huyu mshamba atakusumbua mkifika Arusha!



    Atataka mfikie hoteli moja na pengine hata kukodi chumba kimoja!”

    “Hilo halitawezekana!” Dina alisema na sauti yake ilijenga ubishi. “Eti nini, achukue chumba kimoja? Hawezi akaniburuza kirahisi hivyo! Si bora niache hiyo kazi yenyewe!”



    Kauli hiyo ikamfanya Mohsein kutaka kuiteka nyara hoja hiyo ili amshawishi Dina bora aache kazi kuliko kwenda Arusha! Mtazamo wa wivu ndio uliokuwa ukimtesa, kwa sababu alihofu endapo Dina atakubali kwenda Arusha, ni wazi kuwa Richard atakuwa na nafasi kubwa ya kumpata Dina! Lakini moyo wake haukumpa ushujaa wa kuyatamka hayo. Alijua ungekuwa ni ushauri wa kijinga uliotokana na wivu, alihofu Dina angemdharau. Badala yake akaongea kwa kujitetea huku sauti yake ikinyongea. “Nina hakika mkifika Arusha atakuletea upuuzi wa kukutaka kimapenzi, ukimchekea shauri yako!”



    Dina akafanya tabasamu dogo kumwonyesha Mohsein kuwa amemuelewa. “Mimi sio mtoto mdogo, hawezi akanilazimisha!”



    “Hata hivyo, bado ukifika unayo haki ya kukataa kukaa naye hoteli moja! Hakuna sheria itakayokulazimisha kukaa naye hoteli moja!”



    “Mohsein,” Dina aliita kwa utulivu, kisha akaendelea, “Pamoja na kwamba mimi na Richard tuna uadui wetu, lakini bado ni bosi wangu. Kuna mambo ambayo naweza kumkatalia, lakini sio ya kikazi! Safari tunayokwenda ni ya kikazi na hata kama tutakaa hoteli moja bado litakuwa ni suala la kikazi. Lakini pale atakapotaka kunilazimisha kukaa chumba kimoja na yeye, hilo litakuwa sio suala la kikazi tena na nitakuwa na haki ya kumkatalia!”







    Kauli hiyo angalau ikampa matumaini Mohsein, wivu wake ukashuka kwa asilimia fulani, lakini kitendo hicho cha Richard kutaka kusafiri na Dina bado kilikuwa kikimteketeza! Akatamani achukue ruhusa ya dharura ili naye aende Arusha kivyake vyake, akiamini kuwa karibu na Dina ndio njia pekee ya kumlinda.



    Hadhari aliyopewa na Dina kuwa amechumbiwa, ikaonekana kusahaliwa na Mohsein, akajiona yeye ndiye mwenye haki ya kummiliki Dina kuliko mtu mwingine yeyote!







    ***





    JOHN aliwasiliana na baba yake na kumtaarifu kuwa, lile kusudio lake la awali la kutaka ndoa yake na Dina ifungwe mapema, sasa halipo tena. Sababu ile ile ya barua ambayo Dina alimwonyesha kama kikwazo kinachozuia kufunga ndoa mapema, ndio aliyoitumia kumwambia baba yake.

    “Kwa hiyo mmekubaliana?” baba yake alimwuliza.



    “Alikuwa tayari tufunge ndoa mapema, lakini ni sababu hiyo ya barua ndio imeleta kikwazo,” John alijitetea.

    “Kwa hiyo sikumwambia tena kama ulikuwa ukimhitaji.”



    “Hakukuwa tena na ulazima, hata mimi nilitaka kuzungumza naye kwa suala hilo hilo. Lakini vipi kuhusu suala la upelekaji mahari, si bado liko pale pale?”

    Kuulizwa swali hilo kukamkumbusha John kusudio lake la kutaka kwenda kijijini kwao kwa ajili ya kumfanyia ushirikina Dina. Akahofu pesa ambazo angekwenda nazo zisingetosha baada ya kuambiwa mganga atakayekwenda kumwona huwa anatoza gharama kubwa kutokana na sifa kuwa, wateja wake wengi ni vigogo wa Serikali. Taarifa hizo zikamuweka kwenye hitaji la kuongeza pesa ili aweze kuikabili gharama atakayotajiwa. Kwa kuwa hakuwa na pesa nyingine za ziada ya akiba zaidi ya zile za mahari zilizokuwa zikisubiri kupelekwa kwa wazazi wake Dina, John akaamua alisimamishe kwanza zoezi la kupeleka mahari na pesa hizo zikafanye kazi ya ushirikina!



    “Kwa kuwa ndoa yenyewe itafanyika baada ya miezi mitatu, nadhani hakuna haraka ya kupeleka mahari mapema,” John alimwambia baba yake.



    “Ni wewe tu, hata ukisema zipelekwe leo au kesho ni wewe mwenyewe na maamuzi yako!” baba yake alimjibu.



    Safari ya kupelekwa mahari ikaahirishwa! Umuhimu wa kutaka kumdhibiti Dina kwa kumfanyia ushirikina ukachukua nafasi.



    Kuchelewa kuyapeleka mahari hayo hakukuisumbua akili yake kwani aliamini, endapo Dina atatengenezwa na kuinamishwa kwa imani za kishirikina, basi kutampa uwezo wa kumwambia Dina waanze maisha ya kuishi pamoja kama mtu na kimada wake kisha ndoa ingefuata baadaye.



    Aliamini hilo lingewezekana kwa sababu madawa yangemdhibiti Dina na atakuwa akizipokea amri zake kwa kila atakachomwambia.

    Huo ungekuwa ni ushindi mkubwa kwake wa kumsambaratisha Richard!



    Siku ya pili, John alionana na Dina, akamuaga kwa kumwongopea kuwa anatarajia kusafiri kwenda kijijini mwishoni mwa juma kwa ajili kuwapelekea taarifa za harusi wazee wake wengine walioko huko na kuahidi angerudi Jumatatu.



    Jumatatu hiyo ikamkumbusha Dina kuwa ndio siku ambayo yeye na Richard watasafiri kwenda Arusha!



    Awali, Dina alikuwa amepanga amtaarifu John safari yake hiyo ya kwenda Arusha. Alipanga amwambie siku ya Jumapili asubuhi, siku ambayo ni kawaida yake kuitumia akiwa nyumbani kwa John hadi jioni kabla ya kurudi nyumbani kwao. Lakini hakupanga kumwambia kuwa angesafiri na Richard, alijua kauli hiyo ingemchanganya John. Badala yake angemwambia kuwa anasafiri kwenda Arusha kikazi kwa muda wa wiki moja. Lakini baada ya John naye kumwambia alikuwa akitarajia kusafiri, Dina akabadili azma yake ya kutaka kuaga. Akaamua asubiri hadi John atakaposafiri, kisha ampigie simu huko kijijini atakakokuwa amekwenda amfahamishe kuwa na yeye amepata safari ya ghafla ya kikazi kwenda Arusha! Alijua kwa kufanya hivyo angekuwa ameondoa bugudha ambayo ingempata kutoka kwa John kama angemuaga wakiwa Dar es Salaam, aliamini John angeleta ligi ya kuuliza maswali lukuki yenye mrengo wa wivu ambayo yangemhusisha Richard na kutaka kujua kama naye angesafiri, lakini kwa kupitia kwenye simu aliyaona maswali hayo yasingempa wakati mgumu kuliko kama ingekuwa ni ana kwa ana!



    Alikwishaanza kukerwa na tabia za wivu zilizoanza kuonyeshwa na John alizokuwa akizielekeza kwa Richard dhidi yake tokea aanze kazi kwenye kampuni ya mzee Ken!



    * * * * *



    Hadi ilipofika siku ya Ijumaa mchana, Dina alikuwa hajaambiwa lolote kuhusu kujiandaa na safari aliyoambiwa. Alitarajia kuambiwa mapema mipango ya kujiandaa na safari itakavyokuwa, lakini hadi kufika siku hiyo hakukuwa na dalili zozote kutoka kwa Richard zilizoonyesha kuwa angelizungumzia jambo hilo.



    Alishangaa kuona, tangu Richard alipomzungumzia kuhusu safari hiyo, hajawahi tena kulizungumza jambo hilo japo kwa kumdokeza muda wa kuondoka au safari hiyo itaanzia kituo gani. Ukimya wa kutoambiwa ulimuweka njia panda kwa sababu siku hiyo ya Ijumaa ndio siku ya mwisho ya wiki kufanya kazi, siku zinazofuata za Jumamosi na Jumapili ni siku za mapumziko. Aliamini hata kama wangeondoka siku hiyo ya Jumatatu kama alivyokuwa ameambiwa na Richard, pengine kwa kuondokea ofisini kwa gari la ofisi au la Richard mwenyewe, bado alistahili kuarifiwa mapema ili hiyo Jumatatu aweze kuja kisafari.



    Ukimya huo wa Richard haukuwa ukimsumbua Dina peke yake, lakini hata Mohsein ulikuwa ukimgusa, tena kwa kiasi kikubwa kutokana na kuteswa na wivu. Safari ya Dina kuondoka akiwa na Richard ilikuwa ikimuuma kila alipokuwa akiifikiria. Mawazo ya wivu yalikuwa yakimteketeza kila alipokuwa akiijenga picha ya uwepo wa peke yao kwa watu hao wawili watakapokuwa Arusha. Sononeko la kuchukuliwa kwa Dina kwenye mikono yake na kutenganishwa naye lilikuwa likimwadhibu. Bila ya kujijua, hali hiyo ikamfanya Mohsein apoteze uzito ndani ya siku hizo chache za kusubiri Dina na Richard waondoke kwenda Arusha.



    Safari hiyo ya Dina na Richard kwenda Arusha ilikuwa kama chachu iliyomzindua Mohsein kuujua uzito wa penzi lake lilivyozama kwa Dina. Awali alivyokuwa ameambiwa na Dina kuwa awe mwangalifu ili Richard asiyajue mahusiano yao kutokana na sababu zilizoelezwa, fikra za Mohsein zikamuweka kujiona kama shujaa aliyebahatika kumpata Dina na kuhisi burudiko la kumuwazia bosi wake anavyohangaika kupapata mahali alipopata yeye kiulaini na kumwona Richard kama fala fulani aliyekuwa hatakiwi kimapenzi na Dina!



    Lakini tokea Richard alivyorudi kutoka Morogoro na kumjulisha Dina kuwa atasafiri naye kikazi kwenda Arusha, upepo wa kumwona Richard kuwa ni ‘fala fulani’ ukawa umegeuka! Wivu ukajitengeneza, ufala ukamgeukia yeye! Akaanza kumlalamikia Dina kwa kumtuhumu Richard kuwa anatumia madaraka yake kumlazimisha kusafiri naye kama njia ya kwenda kumlazimisha kufanya naye mapenzi! Ingawa Dina alimpa moyo na kumhakikishia kitu kama hicho hakiwezi kutokea kwake, bado Mohsein alikosa imani.

    Lolote linaweza likatokea kati yao! Fikra hizo zikaendelea kumtafuna Mohsein.



    Lakini ukimya uliokuwa ukiendelea kujitokeza kuhusu safari hiyo huku Dina akidai kuwa, Richard hajamwambia lolote jingine linalohusiana na maandalizi ya safari hiyo huku wiki ikiishia kukatika, Mohsein akaanza kupata aina fulani ya faraja kuwa huenda safari hiyo haipo tena. Yeye kwa upande wake na kama ilivyokuwa kwa Dina, wote kwa pamoja walitaka safari hiyo ivunjike, na ukimya huo ulivyokuwa ukiendelea wakaanza kupata matumaini kuwa, pengine upo uwezekano wa safari hiyo kutokuwepo tena na huenda ikawa ndio chanzo cha ukimya huo!



    Wivu, chuki na husda, Mohsein alikuwa amemuwekea Richard, akawa anaomba Richard afikwe na mabaya, kama vile kuumwa ghafla au kutokee jambo lolote litakalomzuia asiweze kusafiri safari hiyo na badala yake safari hiyo imwangukie yeye! Wakati akiwa na mtafaruku wa msongo mkali wa mawazo na kukiri kumpenda Dina kwa kasi ya ajabu na kujiona ndiye mwenye uhalali wa kummiliki, Mohsein akawaza kuwa, endapo safari hiyo itakuwepo kama Richard alivyopanga, basi ni vyema akafanya mpango kati ya Jumamosi au Jumapili amwombe Dina aje nyumbani kwake ili awahi kufanya naye mapenzi angalau kuondoa usongo aliokuwa nao kabla ya Dina hajasafiri. Aliamini kufanya mapenzi na Dina kungekuwa ni aina ya faraja ambayo ingempunguzia kukabiliana na machungu wakati Dina atakapokuwa hayupo, na angeitumia nafasi hiyo wakati wa kufanya naye mapenzi kumsisitiza Dina asikubali kabisa kumpa penzi Richard watakavyokuwa wapo Arusha!



    Wakiwa ofisini mchana huo katika hali ile ya sintofahamu ya uwepo wa safari hiyo ya Arusha, Mohsein akaona bora autumie wakati huo kumshawishi Dina aje nyumbani kwake siku inayofuata kwa kusudio alilokuwa amelipanga la kufanya naye mapenzi.



    “Dina,” John aliita kwa kujiamini.

    “Unaonaje kesho…” akasita kuendelea baada ya kuusikia mlango wa ofisini kwao ukigongwa. Akaonekana kuchukizwa, “Karibu!” alisema kwa hasira.



    Akaingia msichana ambaye ni mfanya usafi na mpika chai wa ofisini. Akasimama na kumwangalia Dina.

    “Dada Dina,” alisema. “Bosi Richard anakuita ofisini kwake!”



    Mohsein akahisi mfano wa kisu kikali kikichana katikati ya moyo wake! Akashindwa hata kumwangalia Dina wakati Dina alipoinuka. Dina akaiona hali iliyomkuta Mohsein, akaamua kuondoka bila ya kusema lolote kwa Mohsein. Mohsein akamwangalia Dina alipokuwa anauvuta mlango wa ofisini kwa ajili ya kuufunga wakati akitoka, akatamani kumuita na kumwambia asiende!



    Dina akaufunga mlango nyuma yake baada ya kutoka, Mohsein akabaki anasaga meno huku akiuangalia mlango huo ukimsuta!

    Dina alimkuta Richard akizungumza kwenye simu wakati alipokuwa akiingia ofisini kwake. Safari hii Richard aliupunga mkono wake kumkaribisha kwenye kiti huku akiendelea kuzungumza na simu. Dina akaenda kukaa na kubaki kimya huku akijiangalia kucha zake za mikono na wakati mwingine kuyazungusha macho yake kuziangalia kuta za ofisi hiyo kama kwamba ilikuwa ni mara yake ya kwanza kuingia ofisini humo.



    Richard alimaliza kuzungumza kwenye simu na kumwangalia Dina huku akiirudisha simu juu ya meza. Akafanya tabasamu dogo. “Nilikwambia safari ni Jumatatu vile?” alisema.

    Dina aliitikia.



    “Ulishawahi kufika Arusha?”



    “Bado,” Dina alijibu kwa sauti ya chini. Ghafla alijiona anazungumza na mtu aliyemzoea.



    “Tiketi yako,” Richard alisema huku akimpa Dina bahasha yenye rangi mchanganyiko buluu na nyeupe iliyokuwa na nembo ya kampuni yao.

    Dina aliipokea na kuiweka mapajani mwake bila ya kuifungua.



    “Na hizi pesa ni za teksi,” Richard alisema tena na kumpa Dina bahasha nyingine iliyofanana na ile ya kwanza.

    Bahasha hiyo nayo, Dina aliipokea na kuiunganisha na ile ya kwanza kwa kuiweka pale pale mapajani mwake, nayo hakuifungua.



    “Hakikisha unawasili Uwanja wa Ndege saa kumi na mbili na nusu asubuhi, utanikuta nikikusubiri.”

    Lilikuwea ni shambulio jingine ambalo Dina alikuwa hakujiandaa nalo!



    Alikuwa hajawahi kupanda ndege! Uelewa wa kuwa atasafiri kwa ndege ulimyumbisha akili yake. Kila kitu alikiona ni kigeni kwake, alikuwa hajui teksi itakayompeleka Uwanja wa Ndege itamgharimu kiasi gani na atakapofika uwanjani hangejua angeanzia wapi. Akili yake ikawa tegemezi kwa wazazi wake ambao walikuwa na uzoefu wa kusafiri kwa ndege miaka ya nyuma kabla ya kustaafu kazi kwa baba yake aliyekuwa akisafiri kikazi kwa usafiri huo ambapo wakati mwingine alikuwa akisafiri na mama yake.



    Lakini pia kuwepo kwa Richard katika safari hiyo na uwepo wake wa kutangulia kufika Uwanja wa Ndege kwa ajili ya kumsubiri yeye nako kulimpa matumaini ya kuwa atakuwa na mtu mzoefu kwenye safari hiyo.

    Wazo la kumuwazia Richard kuwa ni sehemu ya msaada atakaokuwa akiuhitaji wakati wa kuingia na kuwepo kwake kisafari ndani ya ndege, likamfanya akiri kuwa lingeuleta tena ukaribu wa mahusiano yao binafsi yaliyoasiana kwa muda mrefu.

    Wazo hilo likamfanya alikumbuke onyo la Mohsein!



    * * * * *



    Kujua kuwa Dina atasafiri kwa ndege kulimtia wazimu Mohsein! Bao la kisigino! Alikiri kufungwa bao hilo. Aliiona kete iliyotumiwa na Richard ilikuwa ni ya aina yake, kete yenye ushawishi kwa mtu kama mwanamke, au mwingine yeyote mwenye kupatiwa huduma kama hiyo! Yeye mwenyewe alishawahi kusafiri na Richard kwa safari za kikazi kama hizo na kwa mikoa tofauti, lakini hakuna hata safari moja aliyowahi kusafiri kwa ndege. Safari zote Richard alizowahi kusafiri kwa ndege za ndani au nje ya nchi, alisafiri peke yake.



    Kwa mara ya kwanza uelewa ukaanza kumjia kuwa, vita aliyokuwa akijaribu kupigana ilianza kumuelemea mapema. Mwanzo huo uliofanywa na Richard kwa kumkabidhi Dina tiketi ya ndege, zilikuwa dalili za wazi zinazomthibitishia kuwa, alikuwa anashindana na mtu mwenye fedha na aliyepania kuitumia kuhakikisha anaununua ushindi kwa hali yoyote ile! Hali hiyo ilimchanganya na kujikuta akishindwa kujizuia.



    “Unaona!” Mohsein alibwata mbele ya Dina na kuonekana kupoteza kabisa mhimili wa akili kichwani mwake na kujikuta akisimama. “Mimi nimeshasafiri naye mara kibao, hakuna hata siku moja aliyowahi kunisafirisha kwa ndege! Mi nakwambia hii safari sio ya kikazi, ina lengo lake! We utaniambia!” akamwangalia Dina kwa sura iliyojenga wasiwasi. “Kwa nyie wanawake..!” akasita, kisha akasema. “Sijui!”



    “Nakuomba uondoe presha Mohsein,” Dina alisema kwa utulivu. “Unajipa presha za bure, mimi nimekwishakwambia atakuwa anajisumbua! Au huniamini?”



    “Kukuamini nakuamini,” Mohsein alisema kwa sauti yenye kujitilia mashaka na kauli yake mwenyewe. Alikuwa hamwangalii Dina usoni, hasira ilikuwa bado ikitawala usoni mwake na alikuwa amenuna!



    “Sasa kwa nini unapandisha presha?”



    Mohsein akasikitika. “Inauma, Dina!” alisema kwa sauti iliyomwonyesha ni kweli alikuwa akiumizwa na maumivu aliyokuwa akiyasikia. Kisha akakiangalia kiambaza cha ukuta wa ofisini, akaganda kama aliyezubaa, na kubaki hivyo.



    Dina akakosa la kuzungumza, alikwisha kumwona Mohsein akiwa kwenye kiwango cha juu cha wivu.



    “Nataka kesho uje nyumbani!” Mohsein alisema ghafla huku akimwangalia Dina. “Saa ngapi utakuja?”



    Dina akaonyesha mshangao usoni mwake.

    “Kuna nini?” aliuliza.

    “Uje tuagane!”



    Dina akawa mwepesi kukijua kilichomo kichwani mwa Mohsein. “Kesho sitokuja!” alisema bila ya kumwangalia usoni Mohsein.



    “Basi fanya Jumapili!”



    “Nayo pia itakuwa ngumu kuja!”



    Mohsein akajenga ndita kwenye paji lake la uso.

    “Kwa nini?” aliuliza akionekana kuwa na aina ya kisirani.



    “Nitakuwa bize na kujiandaa kwa safari!”



    Jibu hilo likamrudisha Mohsein kwenye kiti, akakaa kwa unyonge na kujiinamia. Akapiga kite huku akitingisha miguu yake. Akauinua uso wake na kumwangalia Dina usoni.

    “Unajua kuwa nakupenda?” alisema.

    “Najua,” Dina alijibu kwa sauti ya chini.



    “Sidhani!” Mohsein alisema kulikana jibu la Dina. Nadhani unahisi kama nakupenda, lakini hujui ni kwa kiasi gani nakupenda Dina, labda pengine sijawahi kukutamkia neno hilo na ndio sababu ya kutoujua uzito wa mapenzi yangu kwako. Lakini, laiti ungeingia kwenye moyo wangu na kuujua uzito wa kukupenda kwangu, usingenifanyia hivi!”



    Dina akaonyesha aina ya mshangao huku akimwangalia Mohsein. “Kwani nimekufanyia nini?”



    “Usingenikatalia!”



    Dina akafumba macho. Akataka kutamka neno, lakini akaishia kutanua papi za mdomo bila ya kuongea lolote.



    Mohsein akaonekana kuwa mnyonge ghafla na mwenye kukata tamaa. “Ungekuwa unanipenda, ungekuja nyumbani tukaagana. Lakini huoni umuhimu huo kwa sababu bado hujanikubali!”



    Imeshakuwa kero! Dina aliwaza. Ghafla akamfikiria John na safari yake ya kwenda kijijini kwao kwa ajili ya kutoa taarifa za harusi yao. Akapanga jioni baada ya kutoka kazini, aende kwake kwa ajili ya kuagana naye na mengine yatakayofuatia!



    ****



    JOHN alikuwa amekaa upande wenye dirisha kwenye basi alilopanda asubuhi hiyo ya siku ya Jumamosi akielekea kwao kijijini. Upepo uliokuwa ukiingia kupitia dirisha alilokuwepo ulimfanya alirudishe kwa kulifunga kidogo kwa lengo la kuupunguza upepo unaoingia. Akatulia kwa kujiegemeza kwenye kiti na kufumba macho kama aliyekuwa akihitaji kulala. Akaanza kuyakumbuka mapenzi aliyofanya na Dina jana jioni baada ya Dina kuja nyumbani kuagana naye. Kisha akaifikiria hiyo safari yake…



    Alijikuta akimlaani Richard na kumwona ndio chanzo cha safari hiyo, lakini pia akaamini safari hiyo ndio ya kukata mzizi wa fitina wa vita iliyopo kati yao. Kuifikiria vita hiyo kukamfanya amuwazie mganga anayemfuata huko kijijini ambaye kwake alikuwa kama silaha ya maangamizi anayoiendea. Akajenga matumaini jinsi mganga huyo atakavyolishughulikia tatizo lake kwa ukamilifu, na aliamini matunda ya safari hiyo ni kurudi na ushindi wa kuja kumdhibiti Dina kwa kumuweka kwenye kiganja chake! Aliyawazia madawa yenye nguvu za ajabu atakayopewa na mganga jinsi yatakavyoweza kumdhibiti Dina na kumfanya asiwe anavutiwa na mwanamume mwingine yeyote zaidi yake yeye!



    Alikuwa na uhakika baada ya kurudi kutoka huko anakokwenda, juhudi za Richard za kutaka kurejeana na Dina zitakuwa zimefikia ukingoni! Dina angekuwa haoni wala kusikia la mtu; wa kuonekana angekuwa ni yeye na wa kusikilizwa angekuwa ni yeye! Wengine wote wangeonekana ni wajinga fulani, mmoja wao akiwa ni Richard! Richard asingekuwa tena mwiba wa kuwa tishio la ndoa yake, na utajiri wake usingekuwa mali kitu kwa Dina!



    Akalikumbuka tukio la kusindikizwa na Dina asubuhi ya siku hiyo hadi Kituo cha Mabasi yaendayo Mikoani cha Ubungo. Akaamini alikuwa akipendwa na Dina kwa dhati, lakini pia akakiri Richard alikuwa kidudu mtu anayetaka kuliharibu penzi hilo!



    Aliiona safari hiyo ilikuwa na umuhimu kuliko hata ile ndoa aliyotaka kuiwahisha. Uamuzi wa kwenda kumwona mganga kwa lengo la kujihami ulikuwa wa maana na wenye manufaa kwake, kwa sababu lengo ni kumdhibiti na kummiliki Dina. Alitaka awe mmiliki pekee wa kummiliki, hakuhitaji mshirika kwenye umiliki huo. Hiyo ndio ilikuwa dhamira yake ambayo endapo itafanikiwa, suala la kufunga ndoa na Dina lisingekuwa na haraka tena. Angeweza kuichelewesha kidogo ili ajipange upya endapo pesa aliyokuwanayo mfukoni itaishia kwa mganga anayemwendea. Alikuwa na uhakika Dina asingeulalamikia uamuzi huo wa kuichelewesha ndoa kwa sababu angekuwa hana kauli ya kuipinga kauli yake!



    Matumaini hayo yalimpa furaha wakati akiwa ndani ya basi, akaihisi furaha ya ushindi wa kumdhibiti msichana mzuri kama Dina ikielekea kwake!



    John alijikuta akitabasamu peke yake; tabasamu la ushindi!



    * * * * *



    John baada ya kuwapa taarifa baadhi ya wazee wake wanaoishi kijijini kuwa anatarajia kufunga ndoa, akawaomba siku inayofuata wampeleke kwa mganga aliyewatajia jina ambalo alipewa na jamaa zake wa Dar es Salaam. Aliwadanganya wazee hao kuwa anataka akafanyiwe tiba ya kuimarisha mwili wake kwa kuogeshwa na kufukizwa madawa kabla ya kufunga ndoa. Wazee hao wakamhadharisha kuwa, mganga anayemtaka ana gharama kubwa kwa sababu haishi kwa kutegemea uganga kama waganga wengine walivyo, mganga huyu ni mfanyabiashara mwenye biashara zake. Wakamshauri wampeleke kwa mganga mwingine ambaye hayupo mbali na eneo wanaloishi.



    “Lakini huyu niliyemtaja si ndio yule anayewashughulikia hadi Mawaziri waliopo Serikalini?” John aliuliza kwa lengo la kutaka kuupinga ushauri aliopewa.



    “Hizo ni habari tunazosikia juu juu kuwa, anapokwenda Dar es Salaam huwa anakwenda kuwafanyia Mawaziri, lakini kwa hapa kijijini hatujawahi kumwona Waziri yeyote aliyewahi kuja kwa ajili yake. Labda ndio sababu inayomfanya atoze gharama kubwa kwa wateja wanaomwendea. Lakini kwa sisi wakazi wa hapa kijijini huwa hatumtumii, wote tunakwenda kwa mganga tuliyekwambia,” ulikuwa moja ya ushauri alioambiwa.



    John hakukubaliana na ushauri aliopewa, akamg’ang’ania mganga aliyesifiwa na watu wa Dar es Salaam. Akapelekwa!



    Gharama alizoambiwa zikawa kubwa mara mbili ya vile alivyofikiria baada ya kuelezea shida yake. Akahakikishiwa kazi atakayofanyiwa ni ya uhakika na yeye mwenyewe atarudi hapo kijijini kuja kutoa mkono wa pongezi kwa mganga huyo. Ikamlazimu John alitumie fungu la mahari alilokuwa amelichukua kama akiba endapo pesa alizokwenda nazo zisingetosha. Akafanyiwa shughuli aliyoihitaji ambayo ilichukua siku mbili, akapewa masharti ya kufanya, mengine aliyaanzia hapo hapo kijijini na mengine akatakiwa aende akayamalizie akifika Dar es Salaam.



    Ilipofika usiku wa Jumapili akijiandaa kutaka kulala ili asubuhi asafiri kurudi Dar es Salaam, akamfikiria Dina, akaona ni vyema amjulishe kuhusu safari yake hiyo ya kurudi Dar es Salaam, lakini badala ya kupiga, John akawahiwa kupigiwa na Dina!



    Dina akamfahamisha John kuwa anaondoka kesho asubuhi kwenda Arusha kikazi itakayomchukua wiki moja huku akiilalamikia safari hiyo ilikuwa ni ya ghafla ambayo hakuitarajia.



    Habari hizo zilimshitua John na kumchanganya baada ya kumkumbuka Richard!

    “Unakwenda na Richard?” aliuliza.



    “Bado sijajua, lakini sidhani kama na yeye atakwenda!” Jibu hilo likashusha presha za John.



    “Kwa hiyo unasafiri peke yako?” John aliuliza.



    “Bado sijajua. Nilichoambiwa, kesho asubuhi niwahi kufika ofisini kuna safari ya kwenda Arusha!”



    * * * * *



    ***MOHSEIN amechomolewa na DINA kuhusu kuagana....RICHARD anamchanganya DINA kwa kumweleza kuwa atasafiri na ndege...je atamnasa???

    *** JOHN ameenda kwa mganga ....vipi atafanikiwa shida zake??





    ITAENDELEA





0 comments:

Post a Comment

Blog