Simulizi : Wivu
Sehemu Ya Pili (2)
Mapenzi ya kumpenda Dina yalikwisha kumuingiza kichwa kichwa kiasi cha kujiona hawezi akajitoa! Ukawa ni mshituko ambao hakuutarajia, likawa ni pigo kwake kukataliwa baada ya kupenda! Akajaribu kuomba aina yote ya misamaha, lakini Dina hakuonyesha dalili ya kurudi nyuma kwenye uamuzi wake!
Wakati akiwa kwenye jitihada zote za kutaka kulirudisha tena penzi kwa Dina, likizo nayo iliyokuwa ikimuweka nchini ikaisha. Richard akarudi Uingereza bila ya mafanikio ya kuurudisha tena uhusiano wake na Dina!
* * * * *
Kurudi kwake Uingereza kukaonyesha ni namna gani alivyokuwa amechanganyikiwa na penzi lililovurugika. Tukio la kunyonyana ndimi na Dina likaendelea kuleta jinamizi lisiloisha kwake. Richard akaanza kupiga simu za mara kwa mara hasa usiku kutoka Uingereza kumpigia Dina. Alibembeleza na kulalamika huku akimsihi Dina amweleze sababu ya kumgeuzia kibao.
Dina hakuonyesha hasira wala kinyongo wakati wote alipokuwa akizipokea simu za Richard, alimsikiliza Richard alivyokuwa akihangaika na maneno, na mwisho wa mazungumzo yao Dina aling’ang’ania msimamo wake wa kutomwambia Richard sababu ya kumkataa, zaidi ya kumwambia, “Niliamua tu iwe basi!”
Ikawa ni kauli iliyomtesa Richard wakati wote. Umbali uliokuwepo kati yake na Dina ukawa ni kikwazo kingine, akawa anatamani arudi nchini angalau kungemuwezesha kuonana na Dina na kuyaweka mambo sawa na pengine fursa hiyo ingempa nafasi ya kukijua kile kilichomfanya Dina amkatae ghafla. Hata hivyo mawazo yake hayo yakabaki kuwa ni jambo lisilowezekana kutekelezeka kwa ukweli kuwa, asingeweza kurudi Tanzania na kuacha masomo.
Baada ya kukiri asingeweza kurudi nchini, ndipo Richard alipojaribu kuicheza karata yake ya mwisho kwa kumuahidi Dina pindi atakapomaliza masomo yake nchini Uingereza na kurudi nyumbani, jambo la kwanza ambalo angelifanya ni kumuoa!
Karata hiyo nayo, Dina akaitolea nje!
Richard akanyoosha mikono kusalimu amri akiwa London!
* * * * *
Baada ya kukaa Uingereza na kumaliza masomo yake, Richard alirudi nchini akiwa na Shahada yake. Ujio wake wa kurudi nchini, haukumshitua Dina. Richard akalielewa hilo, likamwumiza moyoni. Hata hivyo, akajaribu tena bahati yake kwa kuonana na Dina na kumlia kiapo kuwa ahadi ya kumuoa aliyoiahidi ilikuwa ni ya dhati na angekuwa tayari hata kwenda kujieleza kwa wazazi wake Dina kuhusu kusudio lake hilo.
Dina akapangua tena!
Ndipo Richard alipoamua kuanzisha urafiki na Judi!
Aliuanzisha uhusiano na Judi kwa sababu alikuwa akijua Judi na Dina walikuwa wakifahamiana! Wasichana hao wawili walikuwa na historia iliyokuwa ikifanana kidogo na ile ya Richard na John. Hao nao waliwahi kusoma shule moja kama ilivyokuwa kwa John na Richard. Tofauti iliyokuwepo kati yao ni kuwa Judi na Dina wao walisoma pamoja kuanzia kidato cha kwanza hadi cha nne kabla ya kuachana huku kila mmoja akienda kumalizia masomo ya kidato cha tano na cha sita kwenye shule tofauti. Kwa fikra za Richard alizokuwanazo, alifikiri urafiki aliouanzisha na Judi ungeweza kumwumiza Dina na aliamini ingekuwa ni sehemu ya kulipiza kisasi chake kwa yale ambayo Dina alimfanyia!
Kwa upande wa Judi, pamoja na kukubali kuwa rafiki wa kike wa Richard, lakini yeye alikuwa haijui nasaba yoyote iliyokuwepo kati ya Richard na Dina. Hata hivyo, Dina alikuja kujua baadaye kuwa Richard ameanzisha uhusiano wa mapenzi na Judi. Ingawa taarifa hizo hazikumwumiza lakini kwa kiasi fulani zilimkera.
Kwa kuwa lengo lilikuwa ni kumwumiza Dina, Richard alipokuja kujua kuwa Dina alikuwa akiufahamu uhusiano uliopo kati yake na Judi, kinadharia akajiona tayari ni mshindi! Jambo hilo likamfanya Richard kuuimarisha uhusiano wake na Judi kwa kwenda naye kila mahali na kumtambulisha kwa kila mtu aliyekuwa akimfahamu huku akiamini uhusiano wao huo ungeleta gumzo jijini Dar na wangekuwa mfano wa watu wapendanao. Akawa na hakika sifa hizo zingemfikia Dina, na aliamini zingemchoma na kumwumiza kama alivyoumizwa yeye na Dina! Uamuzi wake huo wa kujenga uhusiano na Judi akategemea ingekuwa ni fimbo pekee ya kumwadhibu nayo Dina ili ajutie nafasi aliyoichezea!
Richard akaanza kuamini ushindi ulikuwa ukienda upande wake baada ya kubaini habari za uhusiano wake na Judi zilikuwa zipo kwenye kilele cha kuzungumzwa na watu tofauti na hasa wale wa daraja lao. Isitoshe, wengine wakawa wanazizidisha kwa kutia chumvi kwa kutangaza kuwa, wawili hao wangeoana!
Richard akaridhika kuwa amemkomoa Dina, lakini pia, akafanikiwa kumuondoa Dina kwenye fikra zake huku nafsi yake ikiridhika kuwa ameweza kulipiza kisasi. Pamoja na kuamini kuwa ameweza kuitimiza nadhiri ya kumwumiza Dina na yeye mwenyewe kuanza kuusahau ule ulazima wa kumwona Dina ni sehemu muhimu ya maisha yake, lakini bado alikiri kwenye moyo wake kuwa, adhabu aliyoipata na kuitumikia kutoka kwa msichana huyo ilikuwa kubwa na iliyomwumiza mno. Akajionya kuwa, mara nyingine asifikie kumpenda mwanamke mwingine kama alivyompenda Dina ambaye amemuachia kovu kwenye moyo wake lililosababishwa na jeraha la kupenda!
Lakini akiwa ndani ya imani hiyo ya kuwa ameweza kuitekeleza nadhiri yake, ghafla pasipo mategemeo Richard akajikuta akiingia kwenye mshituko mwingine asioutarajia pale alipobaini kuwa, kovu hilo lililoachwa na Dina moyoni mwake, kumbe kidonda chake kilikuwa bado kibichi na kilikuwa mbali na unafuu wa kupona.
Utambuzi huo ulikuja kama siku mbaya kwake, siku ya mwishoni mwa wiki aliyokuwa akiifurahia akiwa na Judi. Ilikuwa siku ya Jumapili!
Siku hiyo alikuwa akiisheherekea mapumziko ya juma la mwisho akiwa na Judi wakiwa kwenye hoteli ya BBH iliyopo nje ya jiji kandoni mwa fukwe ya bahari. Ilianzia wakati Richard akiwa anatoka chooni akimrudia Judi aliyekuwa amemuacha ufukoni akipunga upepo. Choo alichokuwa ametoka kukitumia kilikuwa karibu na bwawa la kuogelea, na alipokuwa akirudi aliamua kuitumia njia nyingine tofauti na ile aliyoitumia awali kuendea chooni. Njia hii aliyoamua kurudi nayo ilipita karibu na hilo bwawa, tofauti na ile ya mwanzo ambayo ilipita mbali na bwawa na pia ilikuwa ya mzunguko hadi kufika chooni.
Ghafla wakati alipokuwa akirudi kutoka chooni, Richard akamwona John Sailas! John alikuwa amevaa bukta pekee mwilini iliyolowa maji kuonyesha muda mfupi uliopita alikuwa akiogelea, alikuwa akitokea kwenye baa akiwa amezibeba glasi mbili za vinywaji vya aina moja vyenye rangi ya kijani ambavyo alihisi ni kinywaji aina ya Crème de Menthe vilivyotumbukizwa barafu iliyosagwa. Kitendo cha kumwona John kikamfanya kutaka kumuita, na sababu ya kutaka kumuita ni kwamba walikuwa hawajaonana kwa kipindi kirefu kidogo. Akasita kuitekeleza dhamira yake hiyo ya kumuita baada ya kumwona msichana aliyekuwa hatua kadhaa mbele huku mgongo wa msichana huyo ukiwa umeelekea kwake akiwa amekaa kwenye kingo za bwawa la kuogelea na nywele zake zikiwa zimelowa huku miguu yake ameitumbukiza kwenye maji. Msichana huyo alikuwa amevaa bikini ya kuogelea ambayo ni chupi na sidiria akiwa amegeuka kuangalia nyuma na kutabasamu baada ya kumwona John.
Richard alisimama ghafla baada ya kugundua msichana aliyekuwa akimwangalia alikuwa ni Dina! Bila ya kukusudia kuufanya uamuzi huo, Richard alijikuta akirudi kinyume nyume kama aliyekuwa ameona jambo la hatari. Akabadili njia huku akiendelea kumwangalia Dina alivyokuwa akimpokea John glasi yenye kinywaji, kisha John akajiunga kukaa pembeni mwa alipokaa Dina, naye miguu yake akaitumbukiza majini kuwakabili kuwaangalia watu waliokuwa wakiogelea. Kitendo cha John kukaa karibu na Dina kukayafanya mabega yao yagusane, Dina akatumia bega lake kuligonga bega la John kiushikaji. Kitendo hicho hakikuwa na nguvu iliyotumika, lakini John akafanya igizo kama aliyekuwa amesukumwa kwa nguvu. Akayumba kidogo kuonyesha ameyumbishwa na msukumo wa bega la Dina, kisha akamwangalia Dina aliyekuwa akimwangalia kwa ncha za macho yake huku akitabasamu. John naye akatabasamu, kisha wote wawili wakazikutanisha papi za midomo yao na kubusana kwa mara moja.
Tukio hilo likamuacha Richard kwenye maumivu yaliyomchanganya kichwa. Ilikuwa ni vigumu kwake kusadikisha yanayotokea ni sehemu ya mkanganyiko wa mawazo yanayomjengea taswira zisizokuwepo kutokana na jinamizi la kuachwa na Dina, au yupo ndotoni akiiota ndoto hiyo!
Yote aliyoyaona aliyapinga kwa kuamini hayakuwa kwenye ithibati ya matukio ya kweli. Hakukubali kukiri kama aliyemwona ni John Sailas na yule aliyekuwa naye ni Dina. Pili, hakukiamini kile kilichokuwa kinamdhihirishia kichwani mwake kuwa, endapo ni kweli hao aliowaona ni John Sailas na Dina, basi kinachomdhihirishia hapo ni kwamba watu hao ni wapenzi, tena ni wapenzi wa muda mrefu!
Akakubali kujiondoa kwenye uhayawani wa kuukataa ukweli unaotokea mbele yake, akakiri hayuko ndotoni na anayoyaona ni ya kweli! Lakini pia hakujua kilichokuwa kikimwumiza. Ni kule kumwona Dina akiwa na bwana mwingine? Au ni kumwona Dina akiwa na John Sailas? Akagundua kilichokuwa kikimwumiza ni kugundua John Sailas ni bwana wake Dina! Awali alitarajia kitendo chake cha kumchukua Judi na kumfanya rafiki yake wa kike kingemfanya Dina alipize kisasi kwa kumtafuta bwana wa uhakika na mwenye uwezo kama aliokuwa nao yeye. Kamwe hakutarajia Dina na uzuri aliokuwa nao angeweza kumkubali mtu kama John Sailas mwenye maisha ya kawaida yanayoendeshwa kwa kutegemea ajira yenye kipato cha wastani! Richard aliishiwa nguvu, akashusha pumzi na kusikitika
peke yake. Akarudi alipokuwa amemuacha Judi.
Kero la aina ya maisha aliyonayo John bado liliendelea kumsulubu Richard. Alimshangaa Dina kumkubali mtu mwenye kumiliki usafiri wa pikipiki. Akailinganisha tofauti iliyokuwepo kati yake na John. Yeye alikuwa ni mtoto wa tajiri mwenye kuuchezea utajiri wa baba yake unaompa umiliki wa kubadilisha magari ya kifahari muda wowote anaotaka. Isitoshe pia, ni mrithi mtarajiwa wa mali za baba yake pindi akifariki. Alikwisha kuonana na John Sailas barabarani zaidi ya mara tatu wakati yeye akiwa anaendesha gari lake la kifahari na John akiwa na pikipiki yake akiwa amekifunika kichwa chake kwa kofia ngumu ya helmeti. Utofauti huo wa kimaisha, Richard aliuona ungempa moja kwa moja turufu ya ushindi kwenye vita hiyo ya mapenzi, lakini haikuwa hivyo! Ni John Sailas ndiye aliyeonekana ni mshindi!
Lilikuwa pigo kwa Richard, pigo lililomuanzishia kumchukia John na kumwona ni adui yake namba moja. Hakuamini mtu mwenye maisha aina ya John Sailas anaweza akamshinda. Fikra hizo zikamuweka kwenye ubishi wa kutokubali kushindwa. Akaamini, endapo safari hii kama ataianzisha tena vita ya kumrudisha Dina mikononi mwake angeweza akafanikiwa nayo. Alihisi kulikuwa na dosari ndogo aliyokuwa ameifanya kwenye kumwongoza Dina wakati mtafaruku wao ulipotokea. Hakuijua dosari hiyo, lakini aliamini ilikuwa ni ndogo ambayo anaweza akaisawazisha. Vinginevyo, Dina asingeweza amuache yeye aliyezungukwa na utajiri, kisha akamfuata mtu kama John Sailas ambaye alimwona kama mbabaishaji wa maisha!
Tukio hilo la kumwona John Sailas akiwa na Dina, Richard alilichukulia kama tusi na fedheha kwake, lakini pia akalifanya ni changamoto kwake. Hakutaka kuamini mtu kama John anaweza akawa na ubavu wa kumnyang’anya msichana kama Dina! Akajiapiza lazima arudi kwenye vita ya kumrudisha Dina mikononi mwake! Tukio hilo likaendelea kumtesa, akakosa amani. Kwa mara ya kwanza alijikuta akikiri kuwa, uamuzi wake wa kumchukua Judi kama njia ya kumkomoa Dina ilikuwa sawa na hakuna alichokifanya!
Richard akaapa, piga ua lazima amrudishe tena Dina mikononi mwake kwa gharama yoyote!
Siku chache baada ya tukio hilo kutokea, ndipo Judi alipomwuliza Richard kuhusu kufunga ndoa kwao. Likawa ombi lililokwishachelewa kutolewa! Akili ya Richard ilikuwa imetekwa upya na penzi la Dina huku akijitangazia vita dhidi ya John Sailas!
* * * * *
Richard akaingia rasmi vitani kumsaka Dina, lakini haikuwa rahisi kwa kumvizia barabarani. Kwa mara ya kwanza alijikuta akijilaumu kwa uamuzi wake wa awali wa kuifuta namba ya simu ya Dina siku chache baada ya kuanzisha urafiki na Judi. Kukosekana kwa namba ya simu ya Dina kukawa ni tatizo jipya kwake. Richard akawa hana mtu wa karibu ambaye angemwezesha kuipata namba hiyo kwa urahisi.
Uwezekano pekee ambao ungemwezesha kuonana na Dina kirahisi ni kwenda nyumbani kwao Dina. Wazo hilo alilipinga moja kwa moja, aliuona ni uamuzi wa kujirahisisha na ungetoa nafasi kwa Dina kujiweka kwenye ujivuni usio na lazima pale ambapo angemwona amekuja nyumbani kwao kwa ajili ya kubembeleza penzi. Kikwazo hicho kikamuweka Richard kwenye wakati mgumu wa kuweza kuonana na Dina. Siku zikaanza kupotea huku kila siku Richard akihaha kutafuta njia ya kuonana na Dina.
Mara nyingi ukiomba kwa dhati huwa unapewa. Mungu akampa Richard bahati hiyo ya kuonana na Dina. Walionana bila ya kutarajiana. Ilikuwa wakati Richard akikatiza kwa nje kwenye duka linalouzwa simu lililopo katikati ya jiji. Akiwa anaukaribia mlango wa duka hilo kwa nia ya kuupita ili aendelee na safari yake, ndipo Dina akawa anatoka kutoka kwenye duka hilo. Wote wawili wakashituka.
“Dina!” Richard aliita kwa uchangamfu uliokuwa hauna nguvu sana. Aliogopa kujiamini moja kwa moja.
Dina alitabasamu na kusema, “Hai, Richard!”
“Za siku nyingi?”
“Poa. Zako?”
“Zangu mbaya.”
“Kwa nini?”
“Sikutarajia kunikataa kwako kukufanye unichukie hivi Dina. Umekuwa sio mtu wa kunitafuta kwa simu japo kwa kusema heloh?”
“Unanilaumu mimi wakati wewe mwenyewe unafanya kitu hicho hicho?”
“Mimi nataka sana kukupigia Dina, lakini naogopa kutonesha jeraha uliloniachia moyoni. Ukweli ni kwamba bado nakupenda Dina.”
“Sio vizuri Judi akikusikia ukisema kauli kama hiyo kwangu.”
“Judi siko naye tena!”
“Eti unasemaje Richard?”
“Tumeachana!”
“Kwa nini?
“Ukweli ni kwamba bado hajapatikana mtu wa kuiziba nafasi yako. Bado nakupenda Dina!”
Kauli hiyo ikamfanya Dina atoe kicheko cha kama aliyeguna.
“Ina maana huna habari?” alisema.
Richard akaonyesha kushangaa kidogo.
“Habari ipi?” aliuliza.
Ndipo Dina alipomweleza Richard kuwa, anatarajiwa kuolewa na John Sailas siku chache zijazo! Taarifa hizo zikawa zimemmaliza Richard!
Akiwa bado hajayaponya majeraha yaliyotoneshwa upya, wiki mbili baadaye Richard anashangaa kumwona Dina akiwasili kwenye ofisi za kampuni ya baba yake!.......
*
Akiwa bado hajayaponya majeraha yaliyotoneshwa upya, wiki mbili baadaye Richard anashangaa kumwona Dina akiwasili kwenye ofisi za kampuni ya baba yake!
LILIKUWA kama shambulizi la ghafla walilofanyiana. Wote wawili, Dina na Richard walitumia takriban sekunde mbili au tatu kushangaana huku wakitazamana bila yeyote kati yao kutamka neno.
“Dada karibu,” msichana wa mapokezi alisema huku akimwangalia Dina na wakati huo huo akiiba kumwangalia Richard aliyekuwa bado ameduwaa akimwangalia Dina.
“Ahsante,” Dina alisema na kuonyesha kuondoka kwenye mshangao uliompata.
“Nadhani ni mgeni wangu!” Richard alimwambia msichana wa mapokezi kabla ya msichana huyo hajaanza kumhoji Dina.
“Karibu Dina.”
“Nimekuja kumwona mzee Ken,” Dina alisema huku akimwangalia Richard.
Richard akaonyesha kidogo kupigwa na butwaaa.
“Karibu yupo,” alisema kabla hajatekwa na butwaa lake.
“Anajua kama utakuja?”
“Anajua,” Dina alijibu.
“Twende nikupeleke ofisini kwake,” Richard alisema na kuuweka mkono wake mgongoni mwa Dina na kuondoka naye.
Walifika ofisini kwa Katibu Muhtasi na Richard alimtambulisha Dina kuwa ni mgeni wa Mzee Ken, kisha akamwongoza Dina hadi mlangoni mwa ofisi ya mzee Ken. Aliugonga mlango na kuufungua, akamwingiza Dina na kusema huku akimwangalia mzee Ken, “Mgeni wako!” kisha baada ya kusema hivyo alitoka na kuufunga mlango.
Mazungumzo kati ya mzee Ken na Dina yalichukua takribani dakika kumi na tano hadi ishirini. Dina akafahamishwa kazi ambayo angeajiriwa, akaikubali.
“Nitakulipa mshahara wa shilingi laki nane na nusu ukiwa chini ya uangalizi wa miezi mitatu, na ikifika miezi sita, nitakupandishia mshahara wako na kufikia shilingi milioni moja na elfu sabini na tano,” mzee Ken alisema.
Dina hakuamini alichokuwa akiambiwa, alihisi kulikuwa na makosa kwenye matamshi ya mzee Ken. Akatamani amwambie mzee huyo arudie kauli yake, lakini hakuweza.
“Upo tayari kwa mshahara huo?” mzee Ken aliuliza huku akili yake
ikicheza na akili ya Dina na kugundua binti huyo alikuwa tayari amekimeza chambo.
“Nipo tayari,” Dina alisema kwa sauti hafifu ambayo ilibaki kidogo ikatae kutoka kutokana na kutoamini bahati iliyomwangukia ya kuajiriwa kwa kulipwa mshahara mkubwa.
“Subiri hapo nje,” mzee Ken alisema.
“Ukitoka niitie huyo mama.” Dina alisimama kwa nidhamu kabla hajaondoka, na hatua zake
alivyoanza kutoka alikuwa akitembea kwa woga na miguu yake alihisi kama iliyokuwa ikitetemeka na kutembea kwa tahadhari kama vile alionywa sakafu ya humo ofisini ingevunjika kama angeikanyaga kwa nguvu. Alitoka na kuyapeleka maagizo aliyotumwa kumpelekea Katibu Muhtasi.
Baada ya Katibu Muhtasi kuingia ofisini kwa mzee Ken alikokuwa ameitwa, ikamchukua muda mfupi akatoka. Alipotoka alimchukua Dina hadi kwenye ofisi iliyokuwa jirani na ilipo ofisi ya Richard. Huko walimkuta kijana aliyeonekana kuwa na umri wa takribani miaka thelathini anayeitwa Mohamed Hussein, lakini alikuwa akiitwa kwa jina la mkato, Mohsein.
“Mohsein,” Katibu Muhtasi alimuita kijana huyo.
“Huyu binti ni mfanyakazi wetu mpya, anaitwa Dina. Utamfundisha kazi unazozifanya ili akusaidie na muwe pamoja,” baada ya kusema hivyo, akamgeukia Dina na kusema, “Dina, huyu anaitwa Mohamed Hussein, wengi tunamuita Mohsein. Utakuwa naye pamoja na atakufundisha kazi zote unazotakiwa kuzijua,” baada ya kusema hivyo akamgeukia tena Mohsein.
“Mohsein, utamwonyesha Dina bosi wenu ni nani.”
Baada ya kumtambulisha Dina, Katibu Muhtasi alitoka, akaenda ofisini kwa Richard ambako alimhabarisha Richard kuhusu ujio wa Dina.
Siku hiyo hiyo Dina akaanza kazi rasmi!
* * * * *
“Eti nini?” John Sailasi aling’aka akiwa na butwaa usoni mwake kuonyesha kutokiamini kile alichokisikia kutoka kwa Dina. Akazunguka chumbani mwake kama mnyama mkali aliyejeruhiwa. Akiwa amejikamata kiuno, John alimwangalia Dina huku uso wake ukionekana kama anayetatizwa na kitu. Akacheka kicheko kilichoonyesha kumwumiza. “Usiniambie barua uliipeleka leo, na kazi ukaianza leo hii!” alisema.
“Isitoshe, umeahidiwa kulipwa shilingi laki nane na nusu kama mshahara wako na baada ya miezi sita utaongezewa hadi kufikia milioni na ushee!
Huoni kama kuna sintofahamu katikati yake? Hujiulizi inakuwaje huna ujuzi wowote, lakini bado utalipwa shilingi laki nane na nusu kama mshahara wako wa kuanzia? Za nini zote hizo wakati hauna umaalumu wowote kwenye kazi hiyo? Halafu kitu cha ajabu ni kuwa umetakiwa uripoti kazi zako kwa Richard, huu ni mzaha, Dina!”
“Mzaha ki-vipi?” Dina aliuliza kwa utulivu.
“Wakati ulivyoambiwa uandike barua, ulijua ni kazi gani unayokwenda kuifanya?”
“Sikuijua!” Dina alisema na kuinua juu mabega yake kama mtu asiye na hatia. “Nilichotakiwa niandike ni barua ya kuomba kazi na niambatanishe na vyeti vyangu vya shule.”
“Uliwahi kumwambia mama yako akutafutie kazi kwenye kampuni ya baba yake Richard?”
“Sikuwahi kuongea naye. Lakini hiyo sio sababu ya kutonitafutia kazi.”
“Ninavyoshangaa hivi, sina maana sitaki ufanye kazi! Lakini huwa najiuliza, imekuwaje ukapata kazi ghafla na kirahisi hivyo? Hiyo barua uliyoiandika, ulikuwa umeomba nafasi kazi gani? Au walikuwa wakimuhitaji mtu kwa haraka sana kwenye nafasi hiyo waliyokupa?”
“Niliandika kazi yoyote, nadhani elimu yangu ya kidato cha sita labda ndio iliyonifanya wakubali kunipa mshahara huo.”
John akacheka kicheko cha dhihaka na kusikitika.
“Mshahara huo waliokuahidi kukupa haupishani sana na wa mhitimu wa Chuo Kikuu aliyeondoka na shahada yake! Sembuse kidato chako cha sita ukiwa umekosa hata alama za kukupeleka chuoni? Tuachane na hilo, lakini pia bado huna ujuzi wowote wa kazi unayoijua zaidi ya kuhitimu na kupata cheti cha kidato cha sita, halafu ulipwe mshahara huo? Huo ni mzaha Dina, lazima hapa kuna namna!”
Uso wa Dina ukiwa kama uliogwaya, alimwangalia John na kusema kwa sauti ya utetezi, “Labda ni kwa vile mama yangu na mke wa mzee Ken ni marafiki.”
“Nina muda gani tokea nianze na wewe Dina?” John aliuliza kwa aina ya kusuta. “Kipindi chote hicho hujawahi kuniambia kama mama yako na mama yake Richard..,” hapa alisita, kisha akasema kwa mkazo, “Mimi simuiti mke wa mzee Ken…namuita mama yake Richard! Sioni sababu ya kuzunguka! Hujawahi hata siku moja kunitamkia kama wao ni marafiki! Nakumbuka uliwahi kuniambia kuna wakati mama yako aliwasaidia wao kupata hati ya kiwanja kutoka Wizara ya Ardhi, basi! Leo unaniambia wao ni marafiki? Dina! Au kwa sababu ya kupata hiyo kazi?”
“Kwa hiyo unafikiri hii kazi nimeipata kwa sababu ya Richard?” “Kuna sababu nyingine?”
Dina akacheka kicheko cha karaha, kifupi na kilichoudhi.
“Yaani John unamaanisha nini?” Dina alisema kwa sauti iliyokereka.
“Yaani mimi kukubali kufanya kazi kwenye kampuni ya mzee Ken maana yake kazi hiyo kanifanyia mipango Richard? Au kufanya kazi chini yake ndio nitakuwa demu wake?”
“Nakijua unachokiwaza wewe! Unahisi mimi nalia wivu, lakini wacha ionekane hivyo..!” John akasita, akacheka kicheko kidogo kilichoonyesha kumwumiza ndani kwa ndani.
“Sitaki kusema zaidi, lakini nakwambia kitu kimoja, mimi siridhiki wewe ufanye kazi pale!”
“Kwa hiyo ina maana huniamini? Umekwishaniona kuwa nakusaliti?” Dina alisema kwa sauti ya kulalamika na iliyoonyesha lawama ndani yake.
“Wewe umepelekwa pale kama chambo, nakwambia Dina!”
“Kwa hiyo mama yangu ameshiriki kwenye njama za kuniuza?”
“Sina maana hiyo!”
“Sasa una maana gani ukisema nimepelekwa pale kama chambo wakati ni mama yangu ndiye aliyenifanyia mipango hii ya kazi?”
“Tuyaache hayo Dina,” John alisema na kuonyesha kukata tamaa. “Fanya nikusindikize nyumbani!”
Dina alishusha pumzi kwa nguvu, kisha akaunamisha chini uso wake na kuubana mdomo wake. Akazama kwenye fikra.
Ilikuwa ni siku ya kwanza Dina akiwa ameanza kazi, lakini pia ikawa siku ya kwanza kazi hiyo kumwingiza kwenye mgogoro na John!
* * * * *
Ajira hiyo ya Dina ilimkosesha amani John Sailas. Taarifa alizopewa na Dina kuwa ameanza kazi kwenye kampuni ya mzee Ken na kazi hiyo akiwa anaifanya chini ya usimamizi wa Richard, hali kadhalika na kiwango cha mshahara alichoahidiwa kupewa, ulimkamilishia jawabu kuwa, kuna zengwe lililosukwa dhidi ya Dina!
John alikuwa akijua Richard na Dina waliwahi kuwa na mahusiano
kabla ya kufarakana, na pia alikuwa akizijua juhudi alizozifanya Richard kumwomba Dina waurudishe uhusiano huo na Dina alikataa. Taarifa hizo, John alikuwa ameambiwa na Dina mwenyewe kwenye mazungumzo yao ya kawaida huku Dina akiapa kuwa hajawahi kutembea na Richard, lakini alikiri uhusiano wao ulikuwa ni wa aina ya mapenzi. Tukio la kuambiwa taarifa hizo lilitokea siku za mwanzoni za urafiki wao baada ya John kujua pahali ilipo nyumba ya akina Dina ni jirani na anapoishi Richard. John akamwambia Dina kuwa, yeye na Richard waliwahi kusoma shule moja na darasa moja walipokuwa kidato cha kwanza kabla ya Richard kuhamia nchini Kenya kwa masomo, ndipo Dina naye alipomweleza John uhusiano uliokuwepo kati yake na Richard kabla hawajafarakana.
Kwa kipindi chote hicho, ingawa John baadhi ya wakati alikuwa akionana na Richard hususan baada ya Richard kurudi kutoka Uingereza, lakini John hakudiriki kumtamkia Richard kuwa ana mahusiano na Dina. Na sababu iliyomfanya John asimwambie Richard ni kutokana na kutokuwa watu wa karibu kiurafiki zaidi ya kule kujuana kuwa waliwahi kusoma shule moja, kidato kimoja, na kwa mwaka mmoja! Pamoja na kutomwambia kutokana na sababu hiyo, lakini sababu nyingine iliyomfanya asimgusie lolote linalohusu uhusiano wake na Dina, ni kwamba John hakutaka Richard aujue uhusiano huo kati yake na Dina kwa kuhofia endapo Richard angejua, angeweza kuianzisha vita ya kumgombea Dina na yeye John alihisi angeshindwa vita hiyo kutokana na kuwa Richard ni mtoto wa tajiri mwenye uwezo wa vishawishi vyote ambavyo vingemfanya Dina arudi tena kwake!
Tokea wakati huo, John alipokuwa akimsikia Dina akilalamika kuwa Richard alikuwa bado akimsumbua kwa kumfuata fuata, alijikuta akiingiwa na homa ya wasiwasi huenda siku moja Richard angeweza kufanikiwa kumgeuza mawazo Dina na Dina angeurudisha tena uhusiano wake na Richard na yeye akitoswa!
Mawazo hayo yalikuwa yakimtesa na kumkosesha amani. Faraja pekee aliyokuwa akiipata ambayo hakuiwekea asilimia mia moja ni kule kupewa moyo na Dina kuwa aondoe wasiwasi, huku Dina akimhakikishia kuwa kamwe asingeweza kurudisha uhusiano wake na Richard hata ingetokea wakiachana yeye na John! Huo ulikuwa upande mmoja wa faraja.
Lakini upande wa pili wa faraja aliyokuwa akiipata John ni kule kusoma kwa Richard Uingereza. Akawa anajaribu kuitumia nafasi ya kutokuwepo kwa Richard nchini kuuimarisha uhusiano wake na Dina.
Akahisi amefanikiwa kulitimiza hilo! Lakini wakati akifikiri hivyo, siku chache baadaye akapata habari kuwa Richard amerudi nchini, tena moja kwa moja!
Habari hizo zilimsumbua kwa sababu ya kumpenda sana Dina. Usumbufu huo ukamfanya ajikute akifanya mambo ya kibwege yaliyotawaliwa na wivu, akaanza kuzifuatilia nyendo za Dina kwa siri kuchunguza kama angeziona dalili za watu hao wawili kuurudisha uhusiano. Lakini kabla ya matokeo ya upelelezi wake hayajampa picha yoyote, ndipo alipojikuta akipata faraja baada ya kusikia Richard ameanzisha mahusiano na Judi!
Unjema wa habari hizo ulikuja pale Dina alipomhabarisha kuwa, msichana aliyeingia kwenye mahusiano na Richard ni msichana aliyesoma naye pamoja sekondari na walikuwa wakifahamiana vizuri ingawa hawakuwa na urafiki wa karibu sana, lakini walikuwa na aina ya urafiki. Tukio hilo likampa John imani kuwa, isingekuwa rahisi kwa Dina kumkubali tena Richard wakati akijua ana mahusiano na Judi ambaye alisoma naye shule moja kwa miaka minne huku wakiwa na urafiki fulani.
Hatimaye John akaja kuzisikia habari zilizokuwa zimeanza kuenea kuwa, Richard na Judi wanataka kuoana! Taarifa hizo zikamchanganya akili kutokana na furaha aliyoipata na iliyomhakikishia kuwa, ndoa hiyo kati ya Richard na Judi itasababisha kutokuwepo tena na uwezekano wa Richard na Dina kurudiana! Furaha yake hiyo ikamlazimisha na yeye ajibu mapigo kwa haraka kama jibu la kumfurahisha Dina; akaamua kupeleka posa kwa wazazi wake Dina! Aliamini hilo lilikuwa jibu kwa Dina asije akajisikia unyonge atakapomwona mwenzake anaolewa!
Lakini siku chache baada ya kujibiwa posa yake kuwa imekubaliwa, John akaambiwa na Dina kuwa, mahusiano kati ya Richard na Judi yamefikia tamati! Ni taarifa ambazo kidogo zilimshitua, lakini hazikumuweka roho juu hasa kutokana na kule kukubaliwa posa yake, akaamini ndoa atakayoifunga na Dina itamfanya ammiliki msichana huyo anayempenda kuliko kitu kingine chochote kile, kwa haki zote. Hata hivyo faraja hiyo haikudumu, kabla ya ndoa yake kufanyika mashaka mapya yakapandikizwa moyoni mwake, baada ya Dina kumfahamisha kuwa amepata ajira kwenye kampuni ya baba yake Richard!
Akiwa ametoka kumsindikiza Dina na kumfikisha nyumbani kwao huku kiza kikiwa kimeishaingia, alipokuwa anarudi nyumbani kwake akiwa ndani ya daladala na akiwa ameiacha pikipiki yake nyumbani kutokana na Dina kuapa kuwa hapandi pikipiki, John alikuwa amejawa na hofu ya wazi iliyomkosesha amani kufuatia kitendo cha Dina kukubali kuajiriwa kwenye kampuni ya baba yake Richard! Zilikuwa ni habari zilizomjia kama shambulizi la ghafla ambalo hakujiandaa nalo, na laiti angekuwa anazifahamu kabla, angeweza kuweka pingamizi kwa kumshawishi Dina asikubali.
Aliamini Richard alikuwa amepania kutaka kumrudisha Dina kwenye himaya yake ya mapenzi baada ya harusi yake na Judi kuvunjika, na akawa na dhana kuwa Richard ameamua kufanya hivyo kama eneo la kumlipizia kisasi Judi. John akakiri kuwa, endapo Richard atafanikiwa kuurudisha uhusiano wake na Dina ni wazi kitendo hicho kitakuwa kinaitishia ndoa yake isifanyike! Hakuwa na uhakika ni mbinu za aina gani zilizotumiwa na Richard hadi kufanikisha Dina aajiriwe kwenye kampuni ya baba yake, lakini aliamini, ama Richard alimtumia mama yake kwenda kumwambia mama yake Dina kumwambia kuna nafasi ya kazi inayomfaa Dina, au Richard mwenyewe alimkabili mama yake Dina na kumwambia kuna kazi anayotaka kumwajiri Dina huku akijua mama yake Dina asingeweza kuilaani bahati hiyo kutokana na binti yake kutokuwa na ajira.
Mzunguko wa ajira hiyo ulivyopatikana bado uliendelea kumtia mashaka baada ya kukifikiria kiwango cha mshahara atakacholipwa Dina, ni kiwango kilichoonyesha mazingira aliyoyaamini yana ushawishi wa kumshawishi Dina aikubali ajira hiyo na kisha pia, aione familia hiyo ya mzee Ken kuwa ni wakarimu. Alizikumbuka tuhuma alizowahi kuzisikia kuwa, Richard hudekezwa sana na wazazi wake. Alijikuta akizipa nguvu tuhuma hizo kwa kuihusisha familia hiyo kujiingiza kikamilifu kwenye kuitengeneza njama ya kumsaidia Richard ili afanikiwe kumpata Dina! John alihisi Richard atakuwa amewaambia wazazi wake jinsi anavyomuhitaji Dina na huenda baba yake alimpa hakikisho la kumsaidia kuliondoa tatizo hilo kwa kukubali kumpa ajira Dina kwenye kampuni hiyo, vinginevyo, mzee huyo asingekuwa tayari kumwajiri Dina kwa kupoteza pesa nyingi kumlipa mshahara mkubwa wa aina hiyo!
John hakuona mantiki nyingine yoyote iliyotumika kumfanya Dina alipwe mshahara mkubwa kama huo wakati ni mbumbumbu asiyekuwa na ujuzi wowote wa kazi anayoijua. Aliamini hakuna mwajiri yeyote duniani anayeweza kumwaga pesa kwa ajili kulipa mshahara mkubwa bila ya kuwepo faida. Aliamini Dina hakuwa na faida yoyote kwa mzee huyo kibiashara na wala hakuwa na thamani ya kulipwa mshahara kama huo, isipokuwa amelifanya hilo kwa ajili ya kumsaidia mwanae!
Kumfanya Dina awe chini ya uongozi wa Richard kikazi, John aliamini ni sehemu ya mkakati utakaoimarisha kuurudisha uhusiano uliopotea kati ya Richard na Dina. Hali hiyo ikamfanya John ajiulize kama taarifa za kuolewa kwa Dina zilikuwa zikifahamika na familia ya mzee Ken? Na kama zitakuwa zinafahamika, inakuwaje wafanye maamuzi ya kuhatarisha kuivunja ndoa ya Dina? Na kama watakuwa hawana habari hizo je, urafiki wa mama Dina na mama Richard unaodaiwa na Dina, inakuwaje mama yake asimfahamishe mama Richard kuwa Dina anatarajiwa kuolewa hivi karibuni?
John akaanza kuingiwa na wasiwasi kuwa huenda Dina alimdanganya alipodai kuwa, hakuwa aliijua mipango hiyo ya kazi tokea mapema! Lakini hata kama ni kweli alikuwa haijui, John aliwaza, ina maana ajira ile ya kuwekwa karibu na Richard haikumshitua? Akaifikiria kauli ya Dina ya kujiamini aliposema, asingeweza kukubali kuwa demu wa Richard hata kama wangeshirikiana na Richard ofisi moja! John alishindwa kujipanga auegemee upande upi kati ya kuiamini kauli ya Dina au Dina alisema vile kumwondoa njiani?
Katika kufikiri huko, John alikiri kitu kimoja kuwa, yeye na Richard wapo kwenye mpambano wa kumgombea Dina! Ingawa aliingiwa tena na ile hofu ya kuwa anapambana na mtu mwenye uwezo wa kipesa, lakini kulijua hilo hakukumkatisha tamaa, aliamini Dina angekuwa upande wake kwenye vita hivyo. John akaiona njia pekee ya kupambana na Richard ni kuhakikisha anaharakisha ulipaji wa mahari aliyotakiwa atoe na kisha afanye haraka ya kutangaza siku ya kufunga ndoa.
John akajikuta akiwa na ari mpya iliyompatia nguvu mpya ya kuhakikisha anafanikiwa kuikamilisha mahari hiyo ndani ya wiki mbili zijazo!
MOHSEIN, kijana mtanashati mwenye kutumia manukato ya kiume ya bei ghali anayezungumza lugha ya Kiingereza kwa ufasaha, mtulivu na mcheshi wa tabia, jamali wa sura na umbo, mrefu wa futi tano na inchi kadhaa zilizokwenda mbele. Alikwisha anza kumzoea Dina kutokana na ukaribu uliokuwepo kati yao kutokana na kumfundisha kazi ambazo wakati mwingine walijikuta mabega yao yakigusana kwa muda mrefu kutokana na kuelekezana kazi. Hali hiyo ikamfanya kadri siku zilivyokuwa zikisogea, ndivyo Mohsein alivyokuwa akitamani siku inayofuata iwadie haraka ili akaonane tena na Dina.
Mohsein alijizuia asimwonyeshe Dina dalili yoyote itakayoleta sura ya kumtaka kimapenzi, ingawa mwenyewe alikiri alikuwa amempenda Dina tokea siku ya kwanza alipomwona. Hakuwa na uhakika kama Dina alikwisha kuziona dalili hizo, lakini aliamini wanawake ni wepesi wa kuzijua fikra za mwanamume hususan jambo lenyewe likihusu penzi. Alitaka sana kumhoji Dina kuhusu maisha yake binafsi kama ana rafiki wa kiume na mengineyo, lakini hakutaka kuharakia kwa sababu alihisi Dina naye alikuwa yupo katika kutarajia kuhojiwa mambo kama hayo. Hakutaka aonekane ana papara!
Dina alifurahia jinsi alivyokuwa akielekezwa kuzifanya kazi alizokuwa akifundishwa na Mohsein. Mohsein alikuwa mpole kwake na hakuonyesha hasira wakati pale Dina alipokuwa akizivurunda kazi alizokuwa akielekezwa. Dina alianza kuzielewa baadhi ya kazi na kuziwakilisha kwa Richard kwa kuzipeleka ofisini kwake na wakati mwingine ilibidi azitolee maelezo ya kujieleza kwa mdomo kazi alizozipeleka pale Richard alipokuwa akitaka maelezo ya ziada.
“Umeanza kuijua kazi kwa haraka Dina,” Richard alisema huku uso wake ukiiangalia kazi iliyoletwa na Dina.
Dina alitengeneza tabasamu na kusema, “Ahsante.”
Dina akatoka ofisini kwa Richard, lakini kichwani mwake akawa anazifikiria sifa alizitoka kupewa na Richard. Kipindi chote tokea alivyoanza kazi, walikuwa hawaonani mara kwa mara na Richard, na pale walipokuwa wakionana, walikuwa wakisalimiana na kuulizana la hapa na pale bila ya kuulizana lolote linalohusiana na uhusiano wao. Lakini pale alipoanza kuijua kazi, ndipo mawasiliano ya kuonana na Richard angalau mara moja kwa siku yakaanza. Mwanzoni alipoanza kuzipeleka ripoti zake za kazi ofisini kwa Richard kulimpa wasiwasi kutokana na kuhofia Richard angeitumia nafasi hiyo ya kumfuata ofisini kungeanzisha mazungumzo ya kuurejesha tena uhusiano wao. Wakati alipokuwa akizifikiria sifa alizotoka kupewa na Richard, Dina aliona ni kama dalili za Richard kuutafuta upenyo wa kuyaanzisha mazungumzo yatakayogusia tena uhusiano wao uliovunjika.
Alijua Richard alikuwa akisubiri muda mwafaka wa kuianzisha hoja hiyo, na yeye alikuwa amejiandaa kwa kuikataa. Hofu yake ilikuwa ni kuwepo kwa mahusiano mabaya kati yao baada ya kuueleza msimamo wake huo kwa Richard. Hata hivyo alijipanga aende kwa mama yake kulilalamikia tatizo hilo kama litajitokeza, kwa kuamini mama yake ana uwezo wa kumkabili mama Richard na kuliwakilisha lalamiko hilo. Akaamini tatizo hilo lingeweza kumalizwa kupitia kwa wazazi wao na Richard angetakiwa amuheshimu hasa kwa kuzingatia kuwa yeye Dina ni mke mtarajiwa.
Kwa upande wa mahusiano yake na Mohsein alikuwa akiyafurahia, hata pale walipokuwa wakigusana mabega yao wakati alipokuwa akifundishwa kazi, kulikuwa na kitu kilichokuwa kinamjia na kumfanya ajihisi kuifurahia hali hiyo na kujikuta akijiachia huru ili iendelee kuwepo. Hali hiyo ilimsababisha apate mazoea ya kuinusa hewa inayotawaliwa na manukato anayojipaka Mohsein ambayo ilikuwa ni sehemu inayomfanya aufurahie ukaribu uliokuwepo kati yao.
“Manukato yako ni mazuri,” Dina alimwambia Mohsein wakati Mohsein alipokuwa amemuinamia akimwelekeza jambo kwenye kompyuta huku nyuso zao zikikaribiana kugusana.
Mohsein alitengeneza tabasamu fupi na kumwangalia Dina huku akiwa bado amemuinamia.
“Yaani siku zote ulikuwa huyasikii, ila leo umeyasikia?” alisema.
Dina aliyekuwa ameuinua uso wake alimwangalia Mohsein kwa kutumia ncha za macho yake na kupendeza alipokuwa akifanya hivyo.
“Labda leo ndio nimeamua nikueleze,” alisema.
“Ahsante,” Mohsein alisema na sura zao zikagusana, lakini hakuna yeyote kati yao aliyefanya juhudi ya kuuondoa uso wake kwa mwenzake.
Richard akaingia ghafla ofisini mwao, akawakuta katika hali hiyo. Mohsein na Dina wakashituka kwa pamoja, Mohsein akasimama wima kuuondoa ukaribu uliokuwepo kati yake na Dina na Dina naye akajiweka sawa kwenye kiti alichokalia. Richard akazuga kama vile hakulitilia maanani jambo hilo, lakini Dina akawa mwepesi kutambua kuwa Richard aliumizwa na mwonekano alioukuta kwao.
“Vipi?” Richard alisema kama kuiondoa hali ya sintofahamu iliyojitwika ghafla humo ofisini.
“Kuna kazi nilikuwa namwelekeza Dina kwenye kompyuta,” Mohsein alisema huku akionyesha kama aliyekuwa akijitetea zaidi.
“Nyaraka inayojumuisha uuzwaji wa mafuta ya vituo vya Dar es Salaam ulikwisha kuiweka kwenye uwiano kama nilivyokuwa nimekuagiza?” Richard aliuliza huku akionekana kujitahidi aonekane yupo kawaida.
“Ndio nilikuwa naimalizia bosi,” Mohsein alisema.
“Ndio unaimalizia wakati umesimama hapa..?” Richard aliyeonyesha kupandwa na jazba la ghafla alisema na kusita, akamwangalia Dina kwa uso aliojitahidi usionekane kuwa umechukia.
“Dina, hapa ni kazini!” alisema na sauti yake ilikuwa ikimtuhumu Dina bila ya kufafanua. Kisha akatoka humo ofisini bila ya kuongeza neno lolote.
“Imemchoma!” Mohsein alisema.
“Anaweza akakuletea matatizo!” Dina alisema huku uso wake ukionyesha hofu.
“Kwani ametukuta tukifanya nini?” Mohsein aliuliza na sauti yake ilionyesha ubishi.
“Si umemwona alivyobadilika?”
“Kwani ametukuta tukifanya nini? Si ametukuta tukielekezana kazi?”
“Hayo unayasema wewe, mwenzako kishaenda mbali!”
“Shauri yake!”
* * * * *
Tukio hilo lilimfanya Dina akose amani, alihisi ni tukio ambalo lingeweza kumwingiza Mohsein kwenye matatizo ya kikazi kwa kuamini Richard angelilifanyia wivu. Lakini kwa mshangao, Richard hakuonekana kufanya hivyo.
Siku zilizofuata Richard akionekana kuwa shwari aliendelea na shughuli za kikazi kama kawaida na hakuligusia tukio hilo kwa aina yoyote ya mazungumzo wakati Dina alipokuwa akiziwakilishwa ofisini kwake kazi alizokuwa akizifanya. Dina alipomwuliza Mohsein kama Richard katika siku hizo amemwonyesha tabia tofauti, Mohsein alijibu, “Walaa! Yupo kawaida tu!”
Dina alikiri tukio lilitokea kati yake na Mohsein halikuwa tukio lililoonyesha wapo kwenye mapenzi, lakini aliungama kuwa lilikuwa kwenye unasaba na jambo hilo. Alikuwa na uhakika Richard aliuona unasaba huo wakati alipoingia ghafla na ndio sababu ya kumpa onyo kuwa eneo hilo ni eneo la kazi.
Kauli hiyo ya Richard iliyomwonya ilimfanya Dina ajisikie vibaya na akajishitumu huku akikiri ni kweli alikuwa amejisahau na kujiachia huru mno kwa Mohsein. Hofu yake ikamhadharisha kuwa, Richard amepata picha iliyomwonyesha kuna ukaribu wa suala la mapenzi kati yake na Mohsein. Tukio hilo likazidi kumpa fadhaa pale alipofikiria kuwa, Richard atapata picha gani hususan pale atakapomletea hoja ya kutaka kurudiana naye na yeye atakapoitumia hoja ya kuchumbiwa na John kama kikwazo cha kuurudisha uhusiano huo, lakini wakati huo huo akishuhudiwa kujirahisi kwa Mohsein!
Kwa mara ya kwanza Dina aliyagundua mapungufu yake kwa Mohsein na kujionya awe mwangalifu na maamuzi yake pale anapokuwa naye, vinginevyo ataumbuka!
* * * * *
Harakati za John Sailas za kutafuta mahari na vikorombwezo vingine alivyotakiwa avipeleke, zilifanikiwa kwa muda aliokuwa ameupanga. Aliwasiliana na wazazi wake kuwaatarifu upatikanaji wa vitu hivyo, nao waliitisha kikao, wakazungumzia namna mahari hiyo itakavyopelekwa na watu watakaoandamana na mshenga wakati wa kupeleka. Ndipo kwenye kikao hicho, John akaitaja rasmi tarehe ya kufunga ndoa ambayo alitaka ikatangazwe siku ya kupeleka mahari.
Uamuzi wa tarehe hiyo aliyokuwa ameitaja, John aliufanya akiwa amemshirikisha rafiki yake Muddy pekee. Ilikuwa tarehe ya mapema sana na waliipanga kutokana na shinikizo la John aliyekuwa akitaka awahi kumuoa Dina kabla ya Richard hajamzidi kete!
“Najua sasa hivi Richard anafanya kila aina ya njama za kutaka kulazimisha penzi kwa Dina, yaani jamaa haridhiki mpaka ampate!” John alimlalamikia Muddy wakati alipokuwa akimweleza kuhusu tukio la Dina kuajiriwa kwenye kampuni ya mzee Ken.
“Jamaa sasa anaharibu!” Muddy alisema kuichangia hoja hiyo. “Agh,” John alipiga kite cha hasira wakati alipokuwa akiendelea
kulalamika. “Dina mwenyewe hamtaki! Lakini yeye analazimisha kumwajiri kwa sababu kaupata upenyo wa kumwona Dina hana kazi, basi na yeye kajiona apige bao hapohapo!”
“Dina mwenyewe anasemaje?” Muddy aliuliza kwa sauti kama iliyokuwa na ushari kidogo.
“Dina atasema nini?” John alisema kwa kunyongea na kuonekana yupo kwenye kumtetea Dina.
“Wazazi wake nao ndio hivyo, nao wamemshinikiza akaifanye hiyo kazi!”
“Lakini umekwisha kumhadharisha Dina kuwa Richard yupo kwenye njama hizo?”
“Nisubiri nini? Lakini Dina mwenyewe naye hataki kunielewa!” John alisema kwa hasira.
“Yeye kakazania tu…” hapa akasema kwa kuigiza sauti ya kike. “Ooh, Richard hawezi kunipata kwa sababu sio yeye aliyeniajiri kazi!” kisha akamalizia kwa hasira, “Mademu bwana!”
“Lakini kama Dina mwenyewe anajiamini na ana hakika na analosema, sasa wewe una wasiwasi gani? Mwanamke kama hataki, hataki! Mimi naamini Dina hawezi kumkubali Richard.”
“Mimi ninavyoona, ili kukata mzizi wa fitina ni kuwahi kumuoa Dina! Nikishamuoa, jamaa ataogopa kumvaa. Si unajua mke wa mtu anavyouma? Jamaa lazima ataogopa. Na kama akiendelea kumsumbua, nitamkabili na kumpa onyo. Mimi mtoto wa kihuni bwana, sio mtoto wa mama kama yeye!”
Mjadala wao ukaishia kwa ufumbuzi kuwa, dawa ni kuwahi kumuoa Dina kama njia ya kumkomoa Richard!
Akiwa kwenye kikao kilichoitishwa na wazazi wake, baada ya kuitaja tarehe ya kufunga ndoa, baadhi ya wazee walionyesha kuipinga tarehe hiyo kwa madai kuwa ipo karibu sana.
“Tarehe hiyo haitupi muda wa kutosha kuiandaa sherehe ya harusi kwa mpangilio. Michango yenyewe siku hizi ni ya kubembelezana, tunatakiwa angalau tutoe muda kidogo kwa wachangiaji waweze kujiandaa,” mjomba wake John alisema.
“Sihitaji sherehe kubwa!” John alijibu huku akihofia kama atalegeza msimamo basi hoja ya tarehe itatekwa na wazee hao.
“Kwani una haraka gani mpaka unataka kuiharakisha ndoa?” baba yake alimwuliza.
“Wenyewe tumeamua!” “Wewe na Dina?”
“Ndio!” John alidanganya. Asingeweza kuieleza sababu ya kuiharakisha ndoa hiyo kuwa ni kwa ajili ya kumwogopa Richard. Angedharauliwa na angeonekana ana wivu mkali mno!
“Wenye harusi ni sisi na sisi ndio tutakaokupangia!” shangazi yake alisema kwa sauti ya amri.
John akaonekana kupigwa na butwaa, lakini akili yake ikiwa inawaza haraka haraka huku akijionya kuwa, akifanya mzaha wa kukubali ndoa hiyo icheleweshwe, Richard atamzidi akili!
“Basi sisi tutaoana kwanza,” John alikurupuka. “Halafu nyie mtapanga hiyo sherehe yenu!”
Kila mtu kwenye kikao hicho akaonekana kumshangaa John na kauli yake.
“Kwani unachokiharakisha ni nini hasa?” mjomba wake alimwuliza. “Kuoana!” John alijibu kimkato.
“Tunajua mnataka kuoana, lakini kwa nini mnaharakisha?” John akakosa jibu la haraka, akayagwaya gwaya macho yake.
“Enhe?” mjomba aliguna kwa msisitizo wa kumwuliza John.
“Wenyewe tumeamua tu!” John alisema huku akiwa na uhakika alikuwa hana hoja yenye nguvu ya kuyalinda maamuzi yake.
“Ina maana mkishatoka Kanisani kufunga ndoa mnarudi nyumbani na mkeo? Hakuna kingine kitakachofuatia baada ya hapo?”
“Sihitaji watu wengi wa kutusindikiza Kanisani, tunaweza tukawa watu wachache wasiozidi kumi, hao wanatosha. Sherehe ndogo ya nyumbani inatosha.” John alijibu huku akijaribu kuyakwepa macho yaliyokuwa yakimwangalia.
“Hayo ndio maamuzi mliyokubaliana na mwenzako?” baba yake alimwuliza.
“Yeye hana matatizo, najua atanikubalia!” John aliitamka kauli hiyo, ikawa sawa na mtu aliyejikwaa ulimi kutamka neno ambalo hakutarajia kulitamka.
“Kwa hiyo hujazungumza naye?”
“Tuliwahi kulizungumza hilo!” John alidanganya ili kuweka mambo sawa.
“Mkaafikiana vipi?”
John hakujibu, badala yake alijikuna kichwani.
Dhana ya kuwa John alikuwa akidanganya ikaanza kutanda humo ndani.
“Nataka kukutuma John, unasemaje?” baba yake aliuliza swali la ghafla kwa John.
John akamwangalia baba yake. “Niulize,” alisema.
“Nataka kuonana na Dina, mwambie namuita! Kesho unaweza ukaja naye?”
John akaonekana kusita tena, lakini safari hii hakukawia kutoa jibu. “Sawa!” alisema kwa sauti iliyoonyesha kutoridhika na agizo hilo.
Kikao kikaahirishwa, ikasubiriwa kwanza Dina awasiliane na baba yake John.
Hofu ya dhahiri ilikuwa imemtawala John na wivu ulikuwa ukimtafuna. Alikuwa na uhakika endapo atakubali matakwa ya wazee wake wanavyotaka ya kucheleweshwa kufanyika kwa ndoa hiyo ili waweze kujipanga, basi kipindi hicho kitatoa nafasi kwa Richard kufanikiwa kumpata Dina! Imani yake iliendelea kumshinikiza kuwa, kuwahi kumuoa Dina mapema ndio ufumbuzi pekee wa kumsaidia Dina awe na staha itakayomjenga ajione yeye ni mke wa mtu. Aliliona hilo lingemuongezea Dina ujasiri wa kuendelea kumkataa Richard kwa ajili ya kuilinda ndoa yake, kuliko kama angekuwa bado hajaolewa.
John aliamini, fikra za mwanamke aliyeolewa ni tofauti na mwanamke aliyekuwa hajaolewa. Alimwona mwanamke ambaye hajaolewa ni rahisi kushawishika kimawazo kutokana na kule kujiona kuwa yuko huru. Nafsi yake ilizidi kuumia pale alipokuwa akijenga taswira kumwona Dina akishawishika dhidi ya ushawishi wa Richard, taswira hiyo ikampeleka kwenye fikra za kuwaona wawili hao wakifanya mapenzi kwa siri huku yeye akishikishwa bango la kuwa, Dina ni mchumba wake!
Huku ni kuhanithiwa! John alilaani na kusaga meno kwa hasira. Kitendo cha baba yake kutaka kumwona Dina kilimdhihirishia kuwa,
baba yake alikuwa akitaka kumwuliza Dina kama amekubaliana na wazo la kufungwa ndoa bila sherehe yoyote. Aliujua huo ungekuwa ni mtego kwa Dina, na Dina angetaka kuijua sababu ya kufanyika hayo. John akatambua kuwa angeumbuka!
Utatuzi pekee wa kuiokoa hali hiyo ili iwe shwari kabla ya Dina hajaupokea mwito wa kuitwa na baba yake, aliona ni kuwahi kumshawishi Dina akubali wazo la ndoa yao ifanyike mapema kisha sherehe iwe siku nyingine. Alijua makubaliano hayo yangehitaji ushawishi mkubwa kutoka kwake kumshawishi Dina hadi akubaliane nayo.
Ushawishi huo lazima uandamane na uwongo utakaomridhisha Dina hadi akubaliane nao. Akapanga autengeneze uwongo atakaodanganyia kuwa, kazini kwake kuna mpango wa kumpeleka nje ya nchi kwa ajili ya kwenda kusoma kwa miezi mitatu, hivyo ni muhimu kwao wakifunga ndoa mapema kabla hajaondoka, kisha sherehe ije kufanywa baada ya kurudi kutoka masomoni. Akaufikiria uwongo huo kwa sekunde kadhaa, akauona unakubalika, akaupitisha kuwa unafaa autumie. Lakini pia, bado aliona kuna kizingiti kingine kinachotakiwa kuondolewa; ni lazima autumie uwongo huo huo kuwaeleza wazazi wake kabla ya Dina hajaonana na baba yake. Angeanza kwa kuwaomba msamaha wa kwa nini hakuwa mkweli kwanza, angejitetea kuwa, mara ya kwanza alishindwa kuwaambia jambo hilo kwa sababu alitaka mambo yenyewe kwanza yakamilike huko kazini, baada ya hapo ndio angewaeleza. Akaamini uwongo huo nao ungekubalika kwa wazazi wake tena kirahisi zaidi kuliko hata utakavyokuwa kwa Dina.
Usiku wa siku hiyo iliyofanyika kikao na John kutakiwa aupeleke mwito wa kuitwa Dina kwenda kumwona baba yake, John akaamua kwenda nyumbani kwa kina Dina. Wakakutana kwenye eneo la nje la nyumbani kwa kina Dina, eneo ambalo lilitumika kama sehemu yao maalumu ya kukutana kwao.
Awali Dina alivyoanza kazi kwenye kampuni ya mzee Ken, mazungumzo ya watu hao wawili kila walipokuwa wakikutana yalikuwa yakitawaliwa na Dina. Mara nyingi Dina alipenda kumwelezea John mambo mbali mbali ya kazini na kila alivyokuwa akiyaelezea, John alilazimika kuulizia habari za Richard japo kwa ufupi, lakini Dina akawa anamhakikishia kuwa, hakuna kinachoendelea kati yao na wakati mwingine alikuwa akijibu kwa kusema, “Achana na yule bwege!” Jibu lililokuwa likimfurahisha John. Lakini katika siku zote hizo, Dina hakuwahi kudiriki kulitaja jina la Mohsein au kumzungumzia kama kuna mtu kama huyo anayefanya naye kazi!
Majibu yaliyokuwa yakimponda Richard kutoka kinywani kwa Dina yalikuwa yakimpa faraja John, lakini bado moyoni alikuwa hana amani. Alikuwa akiamini Richard alikuwa bado na dhamira ya kutaka kurudiana na Dina na alikuwa akimtafutia Dina wasaa mwafaka wa kumkabili kimazungumzo! Hapo ndipo palipokuwa pakimwumiza John. Palikuwa pakimwumiza kwa sababu nafsi yake ilikuwa ikitoa nafasi kubwa kwa Richard kushinda vita hiyo ya kumgombea Dina kwa imani ileile kuwa, Richard ni mtoto wa tajiri na ana nafasi kubwa ya kuja kumshawishi Dina hadi angelainika endapo yeye atazembea kuchukua hatua za haraka za kumuoa Dina!
Kwenye mazungumzo yao ya usiku huo, John alionekana kuwa mtaratibu sana kiasi kwamba Dina akagundua John ana mabadiliko kwa siku hiyo. John alikuwa akizungumza kwa nadra na kuonekana kuwa mbali kimawazo. Wakati mwingi alimuacha Dina azungumze, hali hiyo ikamlazimisha Dina alazimike kutaka kujua kilichomo kichwani mwa John.
“Mbona uko hivyo?” Dina alimwuliza John.
“Ki-vipi?” John naye aliuliza.
“Nakuona kama haupo haupo?”
“Agh, kuna kitu kinaniumiza kichwa!” John alijibu na kuuinamisha chini uso wake kuonyesha bado yuko kwenye fikra zinazomwumiza.
“Kitu gani?” Dina aliuliza na kuonyesha kuwa makini kumwangalia John.
John akazuga kama anayezivuta fikra, kisha akasema, “Wakati wowote kuanzia sasa mshenga atawaarifu wazee wako siku ya kuleta mahari, lakini pia kuna kitu kipya kimejichomoza, Dina.”
“Kitu gani?”
“Nataka ndoa yetu tuifunge mapema!”
“Mapema kama lini?” Dina aliuliza kama vile swali alilokuwa akiliuliza halikuwa na ulazima sana.
John akamtajia tarehe.
Dina akaonekana akizipigia hesabu siku zilizobaki hadi kuifikia tarehe iliyotajwa na John. Ghafla akaonekana kubadilika sura. “Yaani wiki tatu zijazo?” aliuliza huku akishangaa kama vile lilikuwa jambo la ajabu.
Mshangao ulioonyeshwa na Dina ukaonekana kama unaotaka kumpa wakati mgumu John kujieleza. Lakini John alijikuta kwenye faraja baada ya kujiamini kuwa, uwongo alioupanga kumweleza Dina kama ataueleza vizuri kama alivyokuwa amejiandaa, ungefanikiwa kumshawishi Dina aikubali hoja yake.
“Najua jambo hili limekuja kama kukushitukiza..,” John alianza kusema.
“Subiri kwanza!” Dina alimkatisha John. “Kuna kitu nimekumbuka!”
alisema na kugeuka kuiangalia nyumba yao kama vile kitu anachotaka kukizungumza kitahusisha na nyumba hiyo. Akaurudisha uso wake na kumwangalia tena John. Akasema, “Kila siku nilikuwa nasema, nitakapoonana na wewe nikueleze, lakini kila ukija huwa nasahau. Afadhali leo umenikumbusha! Naomba unisubiri kidogo,” Dina alisema kwa haraka, kisha aligeuka na kuondoka, akarudi nyumbani kwao.
John akabaki ameshangaa kwa sababu Dina hakumpa nafasi ya kumaliza alichokuwa anataka kukizungumzia. Hakuwa na uhakika wa kukielewa kilichokuwa kimezungumzwa na Dina, akabaki kwenye kutoelewa kama kilichozungumzwa na Dina kilihusisha na hoja aliyokuwa ameianzisha.
Ilimchukua dakika chache Dina kurudi. Alikuwa ameshika barua mkononi, alipofika akampa John. “Kwanza isome kabla hatujazungumza lolote,” alisema.
Ilikuwa ni barua yenye nembo maalumu kutoka kwenye kampuni anayofanyia kazi Dina. John aliisoma barua hiyo huku akiangaliwa na Dina. Alipomaliza kuisoma, akaonyesha kuielewa, lakini hakuonyesha kuelewa sababu iliyomfanya Dina ampe kwa msisitizo kama vile kulikuwa na umuhimu maalumu aliotakiwa aujue kutoka kwenye barua hiyo.
“Mbona ni jambo la kawaida kuwa chini ya uangalizi wa miezi mitatu unapoajiriwa kazi,” John alisema kwa sauti ya kutaka kumwonyesha Dina kuwa vitu vya aina hiyo ni kawaida kwenye ajira.
“Wengine hupewa hadi miezi sita, itategemea na sehemu aliyoajiriwa.”
“Tatizo silo hilo!” Dina alisema kwa sauti ya juu kidogo, uso wake ukionyesha aina fulani ya kukerwa kutokana na John kutoielewa azma ya kumpa barua hiyo.
“Nadhani hujaelewa kwa nini nimekupa uisome!”
John akamshangaa Dina, akaamua kuwa kimya kumsubiri Dina amalizie hicho alichotaka kumuelewesha.
“Nimekupa uisome ili ujue haitawezekana kufunga ndoa, hadi miezi mitatu ipite! Hukuyaona masharti niliyoandikiwa? Si umeona siruhusiwi kuchukua ruhusa zaidi ya siku moja? Ndoa inahitaji uwe huru, ikibidi uwe na ruhusa ya zaidi ya wiki moja, wengine huchukua hadi likizo. Kwa hiyo tarehe uliyoitaja haitowezekana. Itabidi tusubiri hadi baada ya miezi mitatu ndio tufunge ndoa!”
Kauli hiyo ikamnyong’onyesha John, ikamchanganya kwa muda huku akiuona mpango wake ukielekea kushindwa.
Hakukubali!
“Tunaweza tukaoana bila sherehe!” John alisema kama aliyekurupuka huku akionekana kukosa umakini.
JOHN katika mtihani mgumu sana……..je? atachukua maamuzi gani. Hiyo ndoa anayolazimisha ITAWEZEKANA????
DINA ameanza kuhisi kitu Fulani kwa MOHSEIN ..je nini hatma yao??
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment