IMEANDIKWA NA : BEKA MFAUME
*********************************************************************************
Simulizi
: Wivu
Sehemu Ya Kwanza (1)
Sehemu Ya Kwanza (1)
JUDI
alimalizia kujifunga mkufu shingoni baada ya kukamilisha
kujikwatua
kwa vipodozi tofauti vya gharama huku akiwa amevaa vazi lililompendeza mwilini.
Alikuwa ameamkia nyumbani kwa Richard ambako alikuja usiku uliopita na kulala
hadi asubuhi hiyo. Yeye ndiye aliyekuwa wa kwanza kumaliza kuoga na alikuwa
akimsubiri Richard amalize kuoga kisha watoke pamoja kwenye gari la Richard.
Kituo chao cha kwanza kingekuwa kwenye mgahawa wa Monde uliopo katikati ya
jiji
kwa ajili ya kifungua kinywa, kisha baada ya hapo, Richard
angempeleka kazini kwake.
Akiwa amekaa kitandani baada ya kutoka
kujiangalia kwenye kioo
kilichopo kwenye kabati la kuvalia, Judi
alianza kujiuliza kama ulikuwa ni wakati mwafaka wa kumuuliza Richard kuhusu
matumaini yake ya kuolewa naye. Walikuwa ndani ya uhusiano wa mapenzi kwa muda
mrefu na alikuwa akijisikia fahari mbele ya wanawake wenzake kuwa na
uhusiano
huo na Richard ambaye ni mtoto wa mfanyabiashara tajiri na
maarufu jijini Dar es Salaam. Pamoja na kuwepo na uhusiano huo wa muda mrefu,
lakini haikuwahi kutokea hata siku moja kujikuta wakizungumzia suala la
kuoana.
Haikuwa ni mara yake ya kwanza kulala nyumbani kwa
Richard.
Alishakuwa mwenyeji wa nyumba hiyo tokea uhusiano wao
ulivyoanza na kumfikisha hadi siku hiyo. Mara nyingi, husan siku za mwishoni mwa
wiki kuanzia Ijumaa hadi Jumatatu alikuwa na mazoea ya kuhamia nyumbani kwa
Richard na kuumiliki umama wa mwenye nyumba kuanzia usafi hadi mapishi na
mengineyo, kiasi kwamba hata nguo zake zikawa zimegawanyika sehemu mbili; baadhi
zikiwa nyumbani kwao ambako aliishi na wazazi wake na nyingine zikiwa nyumbani
kwa Richard.
Uhusiano wao ulifahamika hadi kwa wazazi wao na kila
mmoja alikuwa amejenga uhusiano mzuri kwa upande wa wazazi wa mwenzake. Richard
alikuwa na uwezo wa kwenda nyumbani kwa akina Judi na kuomba kuondoka naye kwa
muda wowote. Hali kadhalika, Judi aliweza kwenda nyumbani kwa Richard kwa muda
wowote alioamua. Ingawa wote walikuwa huru kuyafanya mambo hayo, lakini walikuwa
wakitofautiana kimawazo. Kwa upande wa Judi, yeye alikuwa hajiamini kama alikuwa
peke yake kwenye penzi la Richard. Hakujua ni kwa nini alikuwa akipatwa
na
hisia hizo mara kwa mara, kuna wakati alikiri huenda ni kwa vile
Richard alikuwa ni mtoto aliyezungukwa na utajiri wa baba yake na mwonekano wake
kumvutia msichana mwingine yeyote kutaka awe naye!
Wivu! Hilo ndilo
lililokuwa likimsumbua na kumwingiza kwenye
wasiwasi huo. Alikiri
dhana hiyo ya wivu ndio iliyokuwa ikiisumbua
nafsi yake na kumjengea
woga kuwa, Robert alikuwa na wanawake wa nje! Pamoja na kuwa na hisia za aina
hizo, lakini hakuwahi kumfumania na mwanamke mwingine japo mara
moja!
Kwa upande wa Richard, yeye mawazo yake
yalikuwa yakikinzana
kimkabala na mawazo ya Judi. Yeye alikuwa
akiamini Judi alikuwa
hana mwanamume mwingine zaidi yake kutokana na
uaminifu aliokuwa nao Judi. Pamoja na kuwa na mitazamo tofauti kati yao, ajabu
ni kwamba, hakuna hata mmoja aliyediriki kuzizungumza hisia hizo kwa
mwenzake.
Mahusiano yao ya muda mrefu yaliwawezesha kuwajengea mazoea
ya kuzoeana, wakawa na uhuru kwa kila mmoja kwenda kwa mwenzake kwa muda wowote
na wakati mwingine bila hata ya kutaarifiana. Uhuru huo ulimfanya Judi na wazazi
wa pande zote mbili kuamini kuwa, suala la ufungaji wa ndoa kati yao lilikuwa
lipo njiani na lingetangazwa wakati wowote. Lakini kama ilivyo ada kwa tamaduni
za Kiafrika, mwanamume ndiye aliyepewa jukumu la kutamka dhamira hiyo, Judi
akaamini, ipo siku Richard angekuja kulitamka jambo hilo
kwake.
Richard hakufanya hivyo! Na Judi naye akashindwa
kuvumilia!
Ndipo asubuhi hiyo, Judi alipoamua iwe siku ya kuuvunja
ukimya
huo!
* * * *
*
Richard alitoka kuoga na kuingia chumbani.
Kitendo cha kufunguliwa kwa mlango wa maliwatoni ambayo ilikuwa imo humo humo
chumbani, ile hali ya kutoka kuoga aliyokuwa nayo Richard na kufunguliwa kwa
mlango huo kulisababisha harufu ya sabuni ya kuogea iingie chumbani humo, lakini
ilichukua sekunde chache harufu hiyo kumezwa na manukato yenye harufu ya nuni
yaliyokuwa yamepulizwa mwilini na kwenye nguo alizovaa Judi.
Judi
akaanza kumpigia mahesabu Richard aliyekuwa ameanza kuvaa nguo ya ndani na kisha
akamwona akivaa suruali aliyoitoa kwenye kining’inizo cha kuwekea nguo kwa
kutumbukiza mguu mmoja baada ya mwingine kwenye suruali hiyo. Judi akashusha
pumzi kwa nguvu bila ya kutarajia. Hali hiyo ilimjia baada ya kugundua jambo
alilokuwa anataka kulizungumza kwa Richard lilikuwa na uzito mkubwa kwenye
mustakabali wa maisha yake ya baadaye.
Hali ya utambuzi wa mustakabali
huo ilimuweka kwenye unyonge, hata kule kujiamini kuwa yeye ndiye mwenye nafasi
ya kuolewa na Richard, ghafla kukaanza kumuweka kwenye njia panda. Hofu hiyo
ikamuweka kwenye mizani kwa kuzivuta kumbukumbu za matukio kwa kipindi chote
alichokuwa na Richard, ikawa kama vile anajifanyia usaili utakaomwezesha kumpa
moyo wa kuendelea na dhamira yake aliyoidhamiria; dhamira ya kulizungumza suala
la ndoa kwa Richard!
Aliyakumbuka matukio mengi mazuri yaliyoonyesha
upenzi kati yao; kama vile kununuliwa vito na nguo za thamani kwenye maduka
yanaouza bidhaa hizo kwa bei ghali; kutoka pamoja kwa ajili ya kula chakula cha
usiku kwenye hoteli za kifahari au migahawa ya Kimataifa;
kuhudhuria
kwa pamoja mialiko tofauti ya sherehe walizokuwa wakialikwa
au wakati mwingine kufurahisha nyoyo zao kwa kwenda kwenye mahoteli yaliyopo nje
ya jiji la Dar es Salaam au kwenye majumba tofauti ya starehe.
Ujumla
wa kuyakumbuka matukio hayo ulimfanya ajione ni nembo
maalumu ya
Richard na kuamini kuwa, ni yeye ndiye aliyechaguliwa!
Lakini pia,
pamoja na kuyakumbuka mazuri yote yaliyofanyika kati yao, pia aliikumbuka mizozo
waliyokuwa wakizozana kwa mambo madogo. Kama vile kukasirikiana kutokana na
maudhi yaliyokuwa yakisababishwa na vijijambo vya kipuuzi, wakati mwingine
kuwafikisha kununiana kwa saa kadhaa au zaidi ya hivyo.
Baadhi ya
matukio waliyoudhiana waliweza kuombana misamaha,
lakini pia kuna
baadhi yaliyowafanya wasiombane misamaha kwa sababu kila mmoja alijiona ana haki
ya kuvuta kamba upande wake. Mizozo ambayo hakuwakuombana misamaha iliweza
kumalizika kimya kimya na kuwa kama vile hakukuwepo na mtafaruku uliotokea kati
yao.
Alipoyaweka kwenye mizani matukio hayo, mengi yakawa ni mazuri na
zile kasoro chache zilizokuwa zikijitokeza, akazichukulia ni sehemu ya kawaida
kwa binadamu wanaoishi kwa karibu. Ukweli huo ukamuweka Judi kwenye imani
aliyoikubali kuwa, walikuwa wakipendana kwa
dhati.
Akajiona yupo kwenye nafasi kubwa ya
kuolewa na Richard!
Hali hiyo ikamrejeshea nguvu ya kuitupa karata
yake juu ya meza!
“Richie,” Judi aliita. Alikuwa amezoea kumwita
Richard kwa jina hilo.
Richard aliyekuwa amesimama mkabala na kioo
kilichopo kwenye
kabati la kuvalia akiwa anazichana nywele zake,
aligeuka na kuitikia huku akimwangalia Judi aliyekuwa bado amekaa
kitandani.
“Kuna jambo nataka nikuulize,” Judi alisema huku
akijaribu
kuyatuliza macho yake kumwangalia Richard usoni na wakati
mwingine kuyakwepesha.
Richard alishitushwa na kauli hiyo baada ya
kugundua Judi alikuwa
amekosa utulivu usoni mwake wakati akiitamka.
Akahisi kulikuwa na tatizo!
“Jambo gani?” Richard aliuliza huku akiwa
ameganda na kitana chake mkononi.
“Una mpango wowote wa
kunioa?”
Richard alionekana kama aliyesukumiwa ngumi ya ghafla
iliyotua
usoni mwake! Akiwa ameishiwa nguvu ghafla baada ya kupigwa
swali hilo, alijikokota kwa kujisogeza taratibu hadi kwenye kabati la kuvalia,
akaliegemea. Uso wake ulikuwa umepigwa na tahayari iliyomwonyesha kuwa, alikuwa
akihaha kulitafuta jibu. Macho yake yalishindwa kuyakabili macho ya Judi
yaliyokuwa yakimwangalia. Akaiangalia sakafu iliyojengwa kwa marumaru kama vile
eneo hilo ndilo lingetoa majibu ya swali alilokuwa ameulizwa.
Ukimya
uliofanywa na Richard ukaanza kumchanganya Judi. Akili
yake ilianza
kukataa kuamini kile anachokishuhudia kutoka kwa Richard.
Richard
alikuwa akionekana kupata kigugumizi kulijibu swali ambalo lingehitimisha ndoto
ya Judi; ndoto ya kuolewa!
“Mbona hunijibu?” Judi aliuliza huku sauti
yake ikionyesha
ukakamavu wa kutaka ajibiwe, lakini moyo wake
ukisambaratika kwa maumivu yaliyoanza kumkatisha tamaa. Woga na hofu ya kupewa
jibu litakalomwumiza vikawa vinaitafuna nafsi yake, hali hiyo ikauweka moyo wake
kwenye mapigo ya kasi yaliyotishia uhai wake!
Richard alianza kwa
kupiga kite na kushusha pumzi huku uso wake
ukiwa bado unaangalia
sakafuni.
“Hapana Judi!” Richard alijibu kama vile alikuwa akiongea na
sakafu aliyokuwa akiitazama. Kisha akauinua uso wake kumwangalia Judi. “Sina
mpango wowote wa kukuoa!” alimalizia.
“Yesu wangu!” Judi alinong’ona
peke yake na kuishiwa nguvu huku
akiwa amefumba
macho.
“Najua haitokuwa rahisi…” Richard alianza kuutetea uamuzi
wake.
Judi akawahi kumnyooshea mkono Richard kumzuia
asiendelee
kuzungumza.
Kimya kikapita kati
yao.
Judi akashusha pumzi kwa nguvu akiwa bado amefumba macho. “Uko
serious na jibu lako?” aliuliza.
Richard akaonekana kuwa kwenye wakati
mgumu, lakini pamoja na kuwa kwenye hali hiyo, bado alikusudia kuwa kwenye
msitari wa ukweli.
“Ndiyo! Niko serious!” Richard
alisema.
Judi akanywea, kila kiungo chake cha mwili kikaonekana
kama
kimekataa kufanya kazi! Akatulia pale kitandani alipokuwa.
Ghafla
akalikumbuka tukio la kufanya mapenzi na Richard saa chache
zilizopita baada ya kurudi kutoka disko kabla hawajalala na kuamka asubuhi
hiyo.
Halikuwa tukio geni kwao, lakini tukio hilo la saa chache
zilizopita likawa kama tukio pekee katika maisha yake na Richard lililompa picha
halisi jinsi Richard alivyokuwa akimchezea katika maisha ya ngono walizokuwa
wakizifanya huku yeye akiamini kwa imani zote kuwa, ilikuwa ni njia ya kuelekea
kwenye kufunga ndoa!
Lilikuwa pigo kwenye maisha yake! Aliusikia moyo
wake ukikatika
pande mbili kwa maumivu makali aliyokuwa hajawahi
kukumbana
nayo. Alihisi kama anayeelekea kuzirai, akajaribu kupambana
na hali hiyo isimtokee akiwa ndani ya nyumba hiyo ambayo sasa ilishakuwa ni
nyumba asiyotaka aendelee kuwemo tena. Akamudu kuizuia hali hiyo, lakini
akashitukizwa na tukio jingine ambalo laiti angepatwa na hisia za mapema kuwa
lilikuwa njiani kumtokea, kamwe asingeweza kuliruhusu limtokee mbele ya Richard;
Richard alishakuwa Shetani mbele yake!
Yalikuwa machozi aliyoshindwa
kuyazuia!
Kitu kikaja kumbana kooni na kumwanzishia kilio chenye
kwikwi
iliyomuweka kwenye kilele cha majuto! Richard akamsogelea na
kumshika maungoni ili ambembeleze, Judi akaupangua kwa nguvu mkono wa Richard
usimshike!
“Tafadhali usinishike!” Judi alisema kwa sauti yenye chuki
iliyotawaliwa na hasira zilizokuwa katikati ya kilio.
Kuanzia siku
hiyo uhusiano wao ukawa umeingia
doa!
*****
JOHN
Sailas akiwa varandani mwa nyumba anayoishi yenye chumba kimoja cha kulalia,
varanda moja, jiko na choo ambayo alipanga, alitengeneza tabasamu dogo mdomoni
mwake wakati akiisoma barua iliyoletwa na mshenga wake iliyokuwa imejibu barua
yake ya uchumba aliomchumbia rafiki yake wa kike anayeitwa Dina siku kadhaa
zilizopita.
Barua aliyokuwa akiisoma ilikuwa ikielezea jinsi
alivyokubaliwa uchumba wake na tabasamu alilokuwa amelijenga lilikuja baada ya
kusoma masharti yaliyokuwa yanahitaji yatimizwe siku itakayopelekwa mahari.
Baadhi ya masharti aliyaona kama aina ya mzaha
unaochekesha.
Kukubaliwa kwake kumuoa Dina alikutarajia kwa sababu
alikwisha
kuizungumza nia yake hiyo kwa mwenyewe Dina, wakakubaliana
na ndipo alipomtuma mshenga kuipeleka posa hiyo. Lakini pia, hata kabla ya
kulizungumza hilo, uhusiano wao wa mapenzi uliokwishadumu kwa zaidi ya mwaka
mmoja, nao ulikuwa ukifahamika na wazazi wa Dina, hali kadhalika na wazazi wake
mwenyewe. Pamoja ya kuwa mila za Kiafrika huwa zinawaweka mbali mtu na mkwewe,
lakini uhusiano wake na Dina
uliweza kumuweka karibu na mama mkwe wake
kiasi kwamba kukawa na urafiki fulani ulioongezea aina ya utani wa hapa na
pale.
Ukaribu huo na mama mkwe wake ndio uliompa John uelewa kuwa,
posa yake hiyo isingekumbana na vikwazo vyovyote. Alikuwa akijua mama yake Dina
ndiye aliyekuwa na sauti ndani ya nyumba huku baba yake Dina ambaye ni mstaafu
akiwa hana kauli ya kumpinga mama huyo. Mama yake Dina ambaye bado ni mwajiriwa,
ndiye aliyekuwa mwendeshaji wa nyumba kwa karibu kila kitu.
John
aliikunja barua aliyokuwa akiisoma na kuirudisha kwenye
bahasha, kisha
akaiweka juu ya meza na yeye mwenyewe kujilaza kivivu kwenye sofa aliyoikalia.
Uso wake aliuelekeza juu na kuliangalia pangaboi lililokuwa likizunguka kwa kasi
ndogo. Uzungukaji wa pangaboi aliokuwa akiuangalia ilikuwa ni kama vile alikuwa
akizirudisha nyuma tafakuri zake kwa kipindi cha zaidi ya mwaka mmoja uliopita
kwa kuikumbuka siku ambayo yeye na Dina walionana kwa mara ya kwanza. Ilikuwa
siku ya Jumamosi!
Aliikumbuka vizuri siku hiyo. Siku hiyo alikwenda
eneo la Ndege Beach akiwa na pikipiki yake. Hakuwa mgeni na eneo hilo, alikuwa
na mazoea ya kwenda mara kwa mara kwa ajili ya kuogelea kutokana na fukwe ya
eneo hilo kuwa ya kupendeza ukilinganisha na fukwe nyingine zilizopo Dar es
Salaam kama ukiziondoa zile za eneo la Kigamboni.
Akiwa na begi lake
lililobeba nguo yake ya kuogelea baada ya kufika kwenye fukwe hiyo, alilitua
begi juu ya mchanga mweupe hatua chache
kutoka baharini. Aliwaangalia
kwa sekunde chache watu waliokuwa
wakiogelea kwenye bahari ambayo
haikuwa na mawimbi makubwa kwa siku hiyo. Kisha aliinama tena, akalifungua begi
lake na kutoa bukta aliyoiandaa kuogelea nayo. Kabla ya kuivaa bukta hiyo,
alijifunga taulo kubwa iliyoziba maungo yake ya kati hadi miguuni, akaivua
suruali yake ya jeans kwa kuiunganishia na chupi aliyokuwa ameivaa na kuzikunja
vizuri nguo hizo kisha akaivaa bukta ya kuogelea. Baada ya kuwa kamilifu kwenye
hali ya kwenda kuogelea, alizichukua nguo zake alizozivua na
kuzitia
kwenye begi pamoja na ile taulo.
Badala ya kwenda kuogelea, John
alikaa kwenye mchanga kando na lilipo begi lake na kuanza kuwatizama waliokuwa
wakiogelea baharini.
Akavutiwa na kundi dogo la wasichana watatu,
wawili wakionekana
angalau wanaweza kujaribu kuogelea na yule watatu
akiwa hajui kabisa kuogelea. Msichana huyo wa tatu ndiye aliyemvutia; na si
kwamba kwa vile alikuwa hajui kuogela, lakini pia alikuwa na mvuto kuliko
wenzake aliokuwa nao. Msichana huyo mwenye umbo la kupendeza lenye urefu wa
wastani, alipendezwa na nguo za kuogelea aina ya bikini ambayo ilimfanya John
apate ushawishi wa kumkaribia msichana huyo ili amwone
vizuri!
Aliendelea kumwangalia msichana huyo alivyokuwa akijilaza
kwenye maji kama anayetaka kuogelea, lakini kwa kukosa ustadi wa kujua kuogelea,
akawa anaishia kwenye mwelekeo wa kuzama kila alipokuwa akijaribu kuogelea.
Wakati wote alipokuwa akijaribu alijikuta akiishia kupiga magoti na sura yake
kuangukia majini. Kitendo hicho kilimfanya ajiinue kwa haraka kila tukio hilo
lilivyofanyika na kuonyesha woga wa kuogopa kuzama huku akijifuta maji ya usoni
na kuhema kwa kuacha
mdomo wazi na kuzitafuta pumzi kwa kuruka ruka
kwenye maji huku akipenua macho yake. Hali hiyo ilimfanya John atabasamu peke
yake.
John aliondoka alipokuwa amekaa na kuelekea kwenye maji, akaenda
upande walipokuwepo wasichana hao na kumfuata yule aliyekuwa hajui
kuogelea.
“Samahani,” John alimwambia yule msichana. “Una nia ya
kujua
kuogelea?”
Uso wa msichana yule ukajengwa na aibu kwa
kugundulika kuwa hajui kuogelea, hata hivyo aibu hiyo akaiziba kwa tabasamu
lenye haya.
“Kwa jinsi unavyojaribu kuogelea, katu hutojua kuogelea,”
John
aliendelea bila ya kusubiri jibu la msichana huyo. “Kwanza ni
mwoga. Pili, maji hayawezi yakakuinua kwa sababu tu, unataka kuelea. Kuna mbinu
za uogeleaji ambazo lazima ufundishwe ndipo utakapoweza kuogelea,” John alisema.
Akakumbuka kujitambulisha. “Jina langu ni John, John
Sailas.
Unaitwa..?”
Moja kwa moja macho ya msichana yule
yakawaangalia wenzake
walioacha kuogelea, nao wakawa wanakuja pale
aliposimama na John.
“Vipi?” mmoja wa wale wenzake wawili alimwuliza
huku akijaribu
kumwangalia John kwa kutaka kujua
kinachoendelea.
“Nataka kumfundisha mwenzenu namna ya kuogelea,” John
alijibu
ingawa swali lililoulizwa lilikuwa halikulenga
kwake.
Nyuso za mshangao zikajengwa na wasichana hao wawili na
kuonyesha dhahiri hawakulitarajia jibu hilo. Wakajikuta wakimwangalia mwenzao
kama kutaka kujua ameliafiki vipi wazo hilo. Mwenzao hakujibu chochote, ukimya
wake ukawajumuisha wote watatu kupigwa na ganzi ya kutojua wajibu nini kwa mtu
huyo au wawili hao wamshauri vipi mwenzao.
“Nitarudi baadaye nijue
mmeamuaje!” John alisema kisha alijilaza
kwenye uso wa maji na kuanza
kuogelea kwa ustadi wa kukusudia
kuwaonyesha wasichana hao namna gani
jinsi anavyojua kuyakata maji.
John aliogelea kwa umbali mrefu kama
njia ya ushawishi kumfanya
msichana huyo endapo atakubali kufundishwa
naye basi ajione atakuwa salama mikononi mwake.
John aliporudi tena
kwa wale wasichana, wakakubali amfundishe
mwenzao, lakini kwa sharti
kuwa hata nao walihitaji kufundishwa.
“Basi nitaanza na huyu ambaye
hajui kabisa,” John alisema.
Wazo la John
likakubaliwa.
Wakiwa wawili peke yao kabla ya kuanza kufundishana
kuogelea, John akakumbuka kujitambulisha tena, “Jina langu ni John
Sailas…”
Macho ya John na yule msichana yakaangaliana. John akauhisi
moyo wake ukipiga kwa kasi. Akakijua kilichopo moyoni mwake dhidi ya msichana
huyo.
“Naitwa Dina,” msichana alisema huku akionyesha tabasamu
dogo
lililojificha kwa dhamira.
Ni siku ambayo John
hakuisahau kamwe!
* * * *
*
Aliacha kuliangalia pangaboi lililokuwa
likizunguka na kukiangalia kiambaza cha varandani mwake. Akiwa hajaondoka
kimawazo kuzikumbuka siku za mwanzo alivyoonana na Dina, John alizikumbuka siku
hizo jinsi walivyokuwa wakipanga na wasichana hao siku za kuendelea
kuwafundisha.
Akiwa ameanza kwa kumfundisha Dina kama makubaliano yao
yalivyo, John alijikuta akipata wakati mgumu wa kutoonyesha hisia zake jinsi
alivyokuwa akiteketea kimapenzi kwa msichana huyo hasa pale alipokuwa akiuzuia
mwili wa Dina kwa mikono yake ambayo ilikuwa ikilaliwa na Dina aliyekuwa
akijilaza juu ili asizame wakati akimfundisha mbinu za kutumia mikono na miguu
wakati wa kuogelea. Kitendo hicho ambacho kilifanya mgusano wa mara kwa mara
kwenye matiti ya Dina na ulaini wa tumbo la msichana huyo kukawa kunampelekea
John kwenye hisia za matamanio zaidi, isitoshe wakati mwingine Dina alikuwa
akionyesha woga wa kuzama na kujikuta akimkumbatia John. Kitendo cha mgusano wa
miili yao kwa kukumbatiwa na Dina kilimfanya John awe anajihisi
kama
anayepigwa na shoti ya umeme!
Kadri walivyokuwa wakizoeana, macho yao
yakaanza kuonyesha ukweli wa mambo kila walipokuwa wakitazamana. Ujumbe wa
kuonyeshana kuwa wote wawili wanahitajiana ukawa dhahiri kati
yao!
Siku moja John akauvunja ukimya!
“Dina,” John aliita
wakati wakiwa ndani ya maji yaliyowafika kwenye vifua vyao wakiangaliana ana kwa
ana. “Nataka uwe girl friend wangu!” Ajabu ni kwamba, Dina hakuonyesha mshituko
na kauli hiyo, ikiwa ni kinyume na John alivyotarajia kuwa ingeleta ubishano
kati yao.
“Nilijua ipo siku ungeniambia hivi,” Dina alisema na
kuikunja miguu yake ndani ya maji na kuanza kuelea na kichwa chake kuwa juu na
hapo hapo akayapuliza nje maji yaliyoingia kinywani mwake.
“Nataka
upajue ninapoishi,” John aliendelea.
“Tutapanga!” Dina alisema
kirahisi kama vile jambo hilo halikuwa na umuhimu kwake, kasha alianza kuogelea
na kumuacha John akiwa amesimama palepale alipokuwa.
Hawakupanga! John
alisita kulikumbushia, alihofia angeonekana anaharakisha mambo. Dina naye akawa
anaonyesha kama vile hakukuzungumzwa jambo la mapenzi kati yao! John akaendelea
kuwafundisha kuogelea wasichana hao huku Dina akiwa kwenye hatua kubwa ya kujua
kuogelea.
John akaona subira yake inaweza ikamwangamiza. Akamvaa tena
Dina!
“Dina nataka Jumapili uje nyumbani kwangu!” John alimwambia
Dina
kwenye simu, safari hii likawa sio ombi tena, bali ni mwendelezo
wa kile alichokianza!
“Si tutaonana Jumapili beach? Tutakapoonana
tutalizungumza hilo,” Dina alijibu kwa utulivu.
John akatambua yupo
kwenye kuyeyushwa na Dina. Akakaza buti!
“Jumapili sitokwenda beach,”
alisema. “Nitaitumia siku hiyo kwa ajili ya kukusubiri wewe uje
nyumbani.”
“Huoni kama utakapokuja beach utaweza kunielekeza vizuri
nyumbani kwako na tutakapoipanga siku itakuwa ni suala la mimi kuja moja kwa
moja?”
“Naishi Kimara Baruti, niambie ni saa ngapi utakuja hiyo
Jumapili ili nikusubiri kituoni?” John aliingiza karata ya
ubishani.
“John mbona hivyo?” Dina alilalamika. “Nimekwambia
tutakapoonana beach tutayazungumza yote hayo. Kwani una wasiwasi
gani?”
“Kwa hiyo unanikatalia?”
Kimya kikajiunda kwenye
simu.
“Dina,” John aliita.
“Bee,” Dina
aliitika.
“Kwa hiyo nijue hutaki?” John aliuliza.
John
akamsikia Dina kwenye simu akishusha pumzi.
“Basi nitakuja saa nne,”
hatimaye Dina alikubali.
“Nisubiri kituoni.”
Saa nne! John
aliwaza. Akaufikiria muda huo jinsi unavyotumiwa kwa siku za Jumapili kwa watu
mbali mbali kupeana ahadi. Hakujua ni kwa nini ulionekana ni muda bora kuliko
muda mwingine!
“Utanikuta nikikusubiri,” John alisema.
Baada
ya kukata mawasiliano, John akatambua zilikuwa zimebaki siku mbili kuiwezesha
Jumapili ifike! Akaomba ahadi ya Dina iwe ya kweli na akamwomba Mungu siku hiyo
kusitokee tatizo lolote litakaloingiza doa ahadi hiyo.
Jumapili
ikafika, John akawa kituoni kabla ya saa nne. Akatarajia kumwona Dina akiwasili
kwa daladala, akashangaa alipomwona akiteremka kutoka kwenye
teksi!
Ukawa mwanzo wa penzi lao, sasa wanataka
kuoana!
* * * *
*
John aliinuka kutoka pale
varandani alipokuwa amekaa, akaichukua barua yake ya majibu na kuingia nayo
chumbani kwake. Aliyafikiria mahari aliyotajiwa, kidogo yalikuwa juu lakini
hayakumwumiza kichwa.
Akafikiria namna ya kuzipeleka habari hizo kwa
wazazi wake. Alijua angelaumiwa kwa kiasi fulani kwa kuyafanya mambo kipeke yake
hadi kufikia hatua hiyo bila ya kuwahusisha wao. Hilo nalo halikumsumbua kichwa,
wazazi wake hawakuwa wakiendekeza lawama zisizokuwa na tija. Walikuwa waelewa na
wenye ufahamu wa kuyajua mazingira tofauti. Simu yake ikaita.
Alikuwa
Muddy, rafiki yake wa karibu sana.
“Sema Muddy,” John alisema baada ya
kuipokea simu.
“Nakuja kwako, upo nyumbani?”
“Wewe uko
wapi?” John aliuliza.
“Nina kama dakika tatu au mbili nitakuwa
nimeshatia timu hapo
kwako.”
“Utanikuta,” John
alisema.
Muddy alimkuta John akilifunga jokofu lake baada ya
kujimiminia maji ya kunywa kwenye glasi na kuirudisha chupa.
“Na mimi
nahitaji hayo maji,” Muddy alisema na kwenda kuchukua glasi iliyokuwa ndani ya
kabati la vyombo la kisasa.
John aliyekuwa ameitoa tena nje ya jokofu
chupa ya maji aliyoitumia awali, alimmininia kwenye glasi maji aliyokuwa
akiyahitaji Muddy. Muddy akayanywa maji akiwa amesimama.
“Posa
imejibu,” John alisema.
“Usiniambie!” Muddy alisema huku akijifuta
mdomo kwa kiganja chake na kuiweka glasi juu ya meza.
“Subiri
nikuletee barua yenyewe,” John alisema akiwa na furaha huku akielekea chumbani
kwake.
Muddy aliisoma barua hiyo na kadri alivyokuwa akiendelea
kuisoma, uso wake ulizidisha tabasamu hadi alipoimaliza.
“Mwanangu
unaoa!” alisema huku akiirudisha barua hiyo kwa John.
“Ndio
manaake!”
“Lakini mahari wamegonga!”
“Kitu chenyewe kile
ghali.”
“Kweli mwanangu, Dina mgogoro!”
Wote wakacheka na
kugongesheana mikono.
“Umeshamwambia mwenyewe?” Muddy
aliuliza.
“Nani, Dina?”
“Yeah.”
“Sijamwambia,
lakini si atakuwa anajua?”
“Hata kama anajua, kumwambia nako kuna raha
yake.”
“Jioni atakuja, nitamwambia. Isitoshe nina mpango wa kumnunulia
na kumvisha pete ya uchumba, lakini hatutafanya sherehe yoyote.”
“Ahh,
hebu mtwangie umpe news.”
“Unajua hata wazee bado sijawaambia!” John
alisema.
“Eti?” Muddy aliuliza huku uso wake ukionyesha kutoamini kile
alichokisikia.
“Sijawaambia!”
“Lakini si wanajua kuwa
umechumbia?”
“Hilo nalo sijawaambia!”
“Hayo masihara
John?”
“Kweli sikuwaambia!”
Muddy akaonekana kuchoka ghafla,
akakaa kwenye sofa. “Yaani wewe siku zote hizi za mchakato wa kutaka kumchumbia
Dina, ina maana wazazi walikuwa hawajui?” aliuliza.
John akionekana
kama aliyekosa amani, naye alijikuta akikaa kwenye sofa.
“Leo
nitakwenda kuwafahamisha,” alisema.
“Duu!” Muddy aliguna, kisha
hakuendelea.
“Lakini wazazi ni waelewa, watanielewa tu.” John alisema
na sauti yake ilionyesha wazi alikuwa akijitetea.
“Hivyo ulivyofanya
kama dharau ya kiaina mwanangu,” Muddy alilalamika.
“Wao ndio
watakaokuwa kila kitu kwenye harusi yako, halafu hawajui kama umechumbia na
wakati wanamjua Dina. Hiyo noma na haipendezi!”
“Nitakwenda kuyaweka
sawa, usiwe na presha.”
“Tatizo lako John unajiamini sana. Shauri
yako!”
John akaamua kuyabadilisha
mazungumzo.
*****
MZEE
Ken Richard Korogwe, tajiri maarufu jijini Dar es Salaam mwenye kumiliki meli
mbili ndogo za mizigo zinazoitwa vidigidigi zinazosafirisha mizigo kwenye
mwambao wa Afrika ya Mashariki kama vile Mombasa, Zanzibar na Comoro na ambaye
pia ni mmiliki wa malori ya mafuta na vituo vya mafuta kwenye maeneo tofauti
jijini na vingine vikiwa mikoani, ndiye baba mzazi wa Richard, mtoto pekee
aliyezaa na mkewe kwa miaka thelathini na mitano wanayoishi ndani ya ndoa yao.
Baada ya kuzaliwa Richard, miaka michache baadaye mkewe aligundulika kuwa na
matatizo
ya tumbo na kufanyiwa operesheni ya kuondolewa kizazi, hali
iliyowafanya wabaki na mtoto mmoja tu. Kubaki kuwa na mtoto mmoja kukawafanya
yeye na mkewe wamwone Richard kama jicho lao, nembo na tunda la ndoa
yao.
Mzee Ken na mkewe walihakikisha wanampa Richard elimu iliyo bora
na kumfanya Richard afanikiwe kupata Shahada yake nchini
Uingereza.
Mzee Ken kitaaluma ni Mhasibu, awali aliwahi kuajiriwa kuwa
Mhasibu Mkuu kwenye Kampuni ya Mafuta kwa miaka kadhaa kabla ya kuteuliwakuwa
Mkurugenzi wa Fedha na Utawala kabla ya kuacha kazi na kufungua biashara
zake.
Mafanikio ya Richard kupata Shahada yalitokana na umahiri
wake
kwenye somo la hisabati na kulidhihirisha kurithi kipaji cha baba
yake. Richard baada ya kupata Shahada yake alirudi nchini na kujiunga na
biashara za baba yake na kuwa mmoja wa viongozi kwenye kampuni inayomilikiwa na
baba yake.
Malezi yalimfanya Richard awe na jeuri na kiburi cha
kudharau watu.
Ujio wa Richard kwenye kampuni hiyo ya baba yake
kukazua malalamiko ya kuwanyanyasa wafanyakazi na malalamiko hayo yakamfikia
mzee Ken. Lakini mzee huyo kutokana na shinikizo kutoka kwa mkewe ambaye
ni
mama yake Richard, akawa anashindwa kumchukulia hatua kali mwanae,
badala yake akawa anamsihi asiwe anawanyanyasa wafanyakazi hasa wa ngazi ya
chini. Usia wake ukasaidia kupunguza kwa kiasi fulani manyanyaso hayo, lakini
haukumaliza dharau za kijana huyo aliyekuwa akiringia utajiri wa baba yake na
elimu aliyokuwa nayo. Baadhi ya wafanyakazi walilazimika kuacha kazi kwa ajili
yake, ikawa inamlazimu mzee Ken apate kazi ya kuziba nafasi zinazoachwa kwa
kuajiri wafanyakazi wengine
kila matukio hayo
yalipojileta!
Richard alikuwa haiishi na wazazi wake, alikuwa akiishi
kwenye moja ya nyumba nzuri zilizokuwa zikimilikiwa na baba yake iliyopo eneo la
Mlalakuwa. Huko ndiko alikokuwa akiutumia muda wake na rafiki yake wa kike Judi,
hadi walipokorofishana kuhusiana na masuala ya
ndoa!
* * * *
*
Kitendo cha Richard kukataa kumuoa
kilimdhihirishia Judi kuwa alikuwa ahitajiki tena na Richard! Jambo hilo lilimpa
wakati mgumu, likakatisha tamaa mustakabali wa hatima ya maisha yake ya ndoa
kuishi na Richard.
Alimpenda Richard, alimpenda si kwa sababu ni mtoto
wa tajiri, lakini pia alimpenda kwa sababu ni kweli alikuwa akimpenda!
Alimheshimu kwa kila hali. Alimfanya aikatae mialiko ya kumtaka kimapenzi
aliyokuwa akipewa na wanaume tofauti wenye uwezo wa juu wa kimaisha. Kamwe
hakutarajia kama ingetokea siku Richard angemtamkia kauli kama
hiyo!
Lilikuwa pigo kwake!
Ingawa Richard alijaribu
kumbembeleza waendelee kuwa wapenzi, lakini kwa kutoa sharti la kutofunga ndoa
wakati alipokuwa akijaribu kumfafanulia uamuzi wake huo wa kutomuoa, hata hivyo
Judi hakuliridhia ombi hilo ingawa alijua kama angelikubali lingetoa nafasi
nyingine ya kuendelea kufaidika kupata huduma za Richard. Judi alikiri kama
angekubaliana na ombi hilo angekuwa sawa na kukubali kutumika kingono huku
akijua haolewi! Ingawa alikiri, endapo angekubaliana na ombi hilo la Richard
ingekuwa ni nafasi yake ya kuweza kuificha siri ya kukataliwa kwake kuolewa,
lakini pia, kungewezesha kuendelea kuwakomoa kwa kuwaumiza wanawake wenzake
waliokuwa wakimwonea wivu. Hata hivyo aliuona uamuzi wa kukubali kuendelea kuwa
hawara wa Richard usingemsaidia.
Hakuwa tayari kuchezewa kisa tu,
aonekane na wanawake wenzake kuwa amemdhibiti Richard! Alichokihitaji ni ndoa na
sio kuchezewa!
Uamuzi huo wa Richard wa kukataa kumuoa ulimwumiza
kila
alipoikumbuka kauli hiyo iliyokana kumuoa na wakati mwingine
ilifanya aina ya mwangi uliomtesa kichwani mwake. Aliiona ni aina ya dharau
aliyofanyiwa na alikuwa hakujiandaa na tukio la aina hiyo kutokana na kujiamini
kwa asilimia zote kuwa, alikuwa ni chaguo la Richard! Judi alijijua kuwa ni
mmoja kati ya wanawake wenye sifa za uzuri na mwenye mvuto kiasi cha kujiona
alikuwa ni chaguo maridhawa kwa mtu aina ya Richard. Alikumbuka jinsi alivyokuwa
hakusita kuonyesha dalili za kumkubalia wakati Richard alipokuwa akimzengea siku
za nyuma kabla hawajafikia kuwa na mahusiano ya kimapenzi. Na baada ya kuwa
wapenzi, urafiki wao ukawa wa wazi, popote walipokwenda walikuwa pamoja.
Uhusiano wao ukawa sehemu ya mazungumzo kwa vijana wenye
umri wao
hususan wasichana ambao wengine hawakuzificha hisia zao za kumwonea
wivu.
Viongozi wenye vyeo tofauti, Serikalini, Mashirika binafsi na
Taasisi
nyinginezo walikuwa wakimjua Richard kuwa ni mtoto wa mzee
Ken, mfanyabiashara tajiri. Na kila walipokuwa wakikutana naye wakati akiwa na
Judi, Richard hakusita kutoa ujulisho kuwa, Judi ni rafiki yake wa
kike!
Ujulisho huo ukampa Judi umaarufu wa kujulikana kama mchumba wa
Richard. Ukamzidishia kupata marafiki waliojikomba kwake na wakaibuka vile vile
waliokuwa wakimwonea donge!
Umaarufu wa kujulikana kwake ulimfanya
apewe kipaumbele kwa
kuletewa kadi kadhaa za mialiko kutoka kwa watu
mbalimbali wenye daraja la juu kimaisha, zilizokuwa zikimtaka ahudhurie vikao
vya harusi, michango ya sherehe na Harambee nyingine tofauti. Na mahudhurio yake
katika shughuli kama hizo yalikuwa yakitukuzwa kwa kupokewa kama mtu maalumu.
Judi alikiri heshima zote alizokuwa akizipata zilitokana na uhusiano wake wa
kuwa na Richard ubavuni mwake! Akajiuliza, kwa nini Richard alitumia nguvu zote
za kumtambulisha kwa watu mbalimbali
kisha aje kumtosa kirahisi
hivyo?
Ilimuuma!
Ilimuuma kwa sababu hakuijua sababu
iliyomfanya Richard akatae
kumuoa. Moyo wake ulipata tabu ya kuamini
labda kuna mwanamke mwingine ambaye Richard alipanga kumuoa. Alishindwa
kuliamini hilo kutokana na ukweli wa mzunguko wa maisha aliyoishi akiwa na
Richard.
Richard alikuwa akimtimizia kila alichokuwa akikihitaji,
lakini pia,
aliweza hata kumfungulia benki akaunti yenye kiwango
kizuri cha pesa huku akaunti yake ya zamani ikiendelea kuwepo.
Judi
alizidi kutatizwa na tukio la kukataliwa kuolewa na Richard ilhali Richard tokea
awali alikuwa akimwonyesha dalili zote kuwa alikuwa akimpenda na hakuwahi
kumfanyia visa vya aina yoyote pamoja na kuzungukwa na hisia za kumhisi kuwa ana
wanawake wengine.
Kwa nini Richard amekataa kunioa? Swali hilo
likabaki kuwa mwiba
uliomwumiza moyoni kila
alipojiuliza!
Judi hakuwa mtoto wa maskini, lakini pia hakuwa mtoto wa
tajiri. Wazazi wake wote wawili walikuwa wasomi na wenye uwezo wa pesa wa
kawaida uliotokana na ajira zao wakiwa ni watawala makazini wanakofanyia
kazi.
Maisha hayo ya wazazi wake ambao anaishi nao kwenye nyumba nzuri
waliyoijenga eneo la Makongo na yeye mwenyewe kupewa elimu ya kutosha
iliyompatia kazi nzuri, aliamini yangeweza kumsaidia kumuweka kwenye uamuzi wa
kuachana na Richard, kisha angejenga subira kwa kutoa nafasi kwa mwanamume
mwingine msomi mwenye kazi nzuri na maisha mazuri
kujitokeza ambaye
atakuwa na mapenzi ya dhati na hatimaye kufunga naye ndoa.
Kwa
kuupitisha uamuzi huo, Judi akajiandaa kupambana na wakati
mgumu
wakati uhusiano wake na Richard utakapojulikana kuwa
umevunjika.
Alijua wapo watu ambao wangemkabili bila ya aibu na
kumwuliza ukweli
wa jambo hilo. Na wengine wangetaka kuijua hata sababu ya uhusiano wao
kuvunjika, wengi wao wakiwa ni wanawake!
Wanawake! Judi aliwaza. Kweli
tuna matatizo!
* * * *
*
Ofisi za kampuni ya mzee Ken zipo kwenye jengo
moja maarufu jijini Dar es Salaam lililokuwa na maofisi mengine ya makampuni
tofauti lililoko katikati ya jiji. Ofisi za kampuni yake zilikuwa kwenye ghorofa
ya nne ndani ya jengo hilo lenye ghorofa zaidi ya kumi na mbili. Mzee Ken
mwenyewe alishikilia vyeo vya Mkurugenzi Mtendaji na Mhasibu Mkuu huku mwanae
Richard akiwa ni Mkaguzi wa Ndani wa Mahesabu.
Asubuhi ya siku hiyo
Richard aliingia ofisini na kumkuta karani wake wa kike akiwa shughulini na
kompyuta.
“Niitie Rama!” Richard alimwambia karani wake bila ya
kutanguliza salamu yoyote, alionyesha kisirani asubuhi hiyo na sauti yake
ilifanya amri.
Karani huyo aliyeitwa Rehema alimwangalia Richard na
kugundua bosi wake yupo kwenye kisirani asubuhi hiyo. Alikuwa akizijua vizuri
tabia za Richard na alikwishazizoea na kumzoea Richard mwenyewe. Aliubinua mdomo
wake kwa aina ya dharau wakati Richard akiingia ofisini kwake.
Rama
ambaye ni dereva anayetumiwa mara kwa mara kuliendesha gari la Richard pale
anapohitajika dereva wa kuliendesha, umri wake ulikuwa wa mtu mzima aliyevuka
miaka hamsini. Wafanyakazi wote kasoro Richard, walikuwa wakimuita kwa jina la
‘mzee Rama.’ Mara zote alikuwa akivaa kofia ya baragashea na suti ya Kaunda
yenye rangi ya ugoro ambayo ni sare yake ya kazini. Alifika ofisini kwa Rehema
kuitikia mwito, akasimama mbele ya meza aliyokuwepo Rehema.
“Umesema
bosi ananiita?” mzee Rama aliuliza.
“Yuko ndani!” Rehema alisema kwa
sauti iliyoonyesha kumchukia Richard.
“Na leo uangalie, naona jamaa
hakuamka vizuri!”
Macho yaliyoonyesha woga yakajitokeza usoni kwa mzee
Rama, akajikuta akiuangalia mlango wa ofisi ya Richard kama vile Richard
angejitokeza muda huo huo. Akaurudisha uso wake kwa Rehema kasha akaiinamia meza
na kujizuia kwa mhimili wa mikono yake.
“Kwani anasemaje?” alinong’ona
huku akiwa ametengeneza kibyongo mgongoni
mwake. Sauti yake haikufanya
mzaha, alionyesha dhahiri alikuwa akimwogopa Richard.
“Mi, ntajuaje?”
Rehema alimshushua mzee Rama kwa kumpa jibu la mkato. Kisha akaendelea, “Na wewe
mzee acha woga! Unamwogopa huyo Richard utadhani ni Mungu wako!”
Mzee
Rama akajaribu kutengeneza tabasamu lililokataa usoni kwake.
“Huyu
kijana ni mkorofi sana!” alisema.
“Hee! Unaanza kuogopa kabla hujajua
anachotaka kukwambia? Huyu si kama mwanao tu! Naona siku atakayokwambia kibarua
kimeisha, utarudishwa nyumbani ukiwa maiti!”
Mzee Rama akajichekesha.
“Wewe mtoto acha maneno ya uchuro!” alisema huku akiendelea
kujichekesha.
Mlango wa ofisi ya Richard ukafunguliwa, Richard
akatokeza! Mzee Rama akashituka, akaganda pale alipokuwa, akabadilika kama siye
yeye aliyekuwa akizungumza. Kujichekesha kukayeyuka, akauchuna uso kama samaki
aliyekaushwa! Rehema akawa anaumia mbavuni kwa kujizuia kucheka huku akijitahidi
kuendelea na kazi kwenye kompyuta kama vile hajui
kinachoendelea.
Richard alikuwa amekamata funguo za gari mkononi,
akamwangalia mzee Rama, kisha bila ya kusimama akamtupia funguo hizo, zikampiga
mzee Rama maungoni na kuangukia miguuni mwake huku akihangaika kutaka
kuzidaka.
“Kalikoshe gari langu!” Richard alisema bila ya kugeuka
nyuma, akatokahuku akimuacha mzee Rama ameinama akiziokota funguo
alizotupiwa.
Baada ya Richard kutoka nje ya ofisi, Rehema alisikitika
peke yake na kulalamika kwa hasira, “Huyu baba huyu!” kisha
asiendelee.
Uso wa mzee Rama ulikuwa bado umejengwa na hofu ya nidhamu
ya woga, akamwangalia Rehema na kusema, “Wacha nitoke, asije akarudi na
kunikuta!”
Rehema alimwangalia mzee Rama alivyokuwa akitoka kisha
akaendelea tena kusikitika peke yake. Akajisemea moyoni: Laiti ningetupiwa mimi
funguo zile, nami ningeziokota na kumrudishia kwa kumtupia nazo na kazi leo hii
ningeacha!
* * * *
*
Mzee Ken alimaliza kifungua kinywa akiwa na
mkewe kwenye meza ya chakula, wote wawili wakiwa wamejiandaa kutoka, kila mmoja
na safari yake na usafiri wake.
“Unakumbuka leo kuna kikao kingine cha
harusi?” mkewe alisema.
“Nakumbuka lakini sitokwenda!” mzee Ken
alijibu.
“Kikao kilichopita hukwenda na hiki pia
huendi?”
“Leo mchana nitakuwa kwenye mkutano
utakaokutanisha
wafanyabiashara wa hapa nchini na ujumbe maalumu wa
kibiashara kutoka Uturuki unaoongozwa na Waziri wao wa biashara aliyewasili hapa
nchini jana. Ukienda wewe inatosha, sio lazima wote tufike.”
“Sawa,
basi nitamfahamisha Adam kuwa na leo hutofika.”
“Na mimi baadaye
nitampigia simu kumjulisha kuwa sitofika,” mzee
Ken alisema huku
akionyesha kutaka kuondoka.
Mkewe akamwangalia kwa sura yenye jambo.
“Una haraka sana?”
aliuliza.
“Kwani vipi?”
“Kuna
kitu nataka kuzungumza na wewe!”
Kauli hiyo ikamfanya mzee Ken atulie
na kumwangalia mkewe kwa
utulivu. “Kinahusiana na hicho kikao cha
harusi?” aliuliza.
“Hapana. Kinamhusu Richard!”
“Ana
nini?”
“Hivi Richard anataka mpaka mmoja wetu afe ndio
aoe?”
Swali hilo kidogo lilionyesha kama kumchanganya mzee
Ken,
akaonyesha uso wenye mshangao. “Kwa nini unasema hivyo?”
aliuliza.
“Ulishawahi kumshauri lolote kuhusu suala la kuoa?” mkewe
aliuliza swali badala ya kujibu swali.
“Mbona sijakuelewa unachotaka
kukizungumza?”
“Nataka kujua ni lini Richard atapata wazo la
kuoa?”
“Nadhani hilo ni suala lake binafsi. Kwa nini
usimwulize?”
“Najua ni suala lake binafsi, lakini sisi wazazi wake ni
jukumu letu
kumshauri au kujua mawazo yake kuhusu jambo hilo. Unadhani
yeye na Judi wataishi maisha ya uhawara mpaka lini? Wamekwishakaa hivyo kwa muda
mrefu, nadhani sasa umefika wakati wa kumshauri afunge ndoa na
mwenzake.”
Mzee Ken hakufanya haraka ya kujibu. Alionekana kutafakari
huku
akivigonga vidole vyake juu ya meza.
“Ni vyema
tukamshauri hivyo,” mkewe akawahi kusema kabla ya
mzee Ken hajajibu na
kuichukua nafasi hiyo kulieleza alilotaka kulieleza.
“Ukaaji wao wa
uhawara kwa muda mrefu unaweza ukawafikisha
kwenye vishawishi vingine
vinavyoweza kuwaingiza kwenye migogoro itakayowafikisha kuachana. Matokeo yake,
Richard anaweza akadakwa na shangingi. Akapungwa vilivyo na hatimaye kudai
kumuoa. Si unawajua wanawake wa mijini walivyo werevu hasa wakishanusa harufu ya
fedha.
Wakijua Richard ni mwanao unadhani watamwachia? Watahakikisha
wanamdhibiti hata kama ikibidi kwenda kwa waganga ili mradi wamuinamishe, kama
wenyewe wanayosema kulishwa limbwata. Usije ukashangaa ukamwona mwanao
akatuletea mwanamke ambaye siye na akadai kutaka kumuoa!”
“Unayoongea
ni kweli, lakini pia tunatakiwa tuangalie na upande wa pili. Inawezekana wenyewe
wakawa hawajapanga hivyo.”
“Kuna ubaya gani tukiwashauri hivyo?
Utajuaje ikiwa hujakaa na
mwanao na kuzungumza naye?”
“Kwa
hiyo, unachokitaka nikae na Richard ili nimwulize kama ana
mpango
wowote wa kuoana na Judi? Au nimwulize kama ana mpango wowote wa
kuoa?”
“Sasa ni yupi mwingine wa kumuoa zaidi ya Judi? Judi
ndiye
tunayemfahamu na hata wewe mwenyewe umekwisha kumsifia kuhusu
tabia zake. Kwanza ana elimu nzuri, kazi nzuri na tabia yake ni nzuri. Ni yupi
mwingine zaidi yake? Richard atakaponiletea kiruka njia unafikiri nitakubaliana
naye?”
“Sawa,” mzee Ken alisema kwa sauti ndogo.
“Usiitikie
kama vile nakulazimisha!” mkewe alisema huku akionyesha kuugundua unyonge
ulioonyeshwa kwenye sauti ya mumewe. “We huoni fahari endapo Richard ataoa sisi
tukiwa hai? Au hujisikii vibaya kila baada ya muda tunaletewa kadi za kuhudhuria
vikao vya harusi za wenzetu wanaotaka kuozesha watoto wao? Sisi kazi yetu
itakuwa ni kuwachangia hadi lini? Na sisi tutachangiwa lini? Au unataka
tuchangiwe michango ya sanda badala ya harusi? Aaa bwana, lazima ifikie mahali
na sisi tuchangiwe, na sisi tusikie fahari kumwona mtoto wetu anaoa.
Nimeshachoka kuwapigia watoto wa wenzangu vigelegele, nataka na mimi mtoto wangu
apigiwe vigelegele!”
“Sasa lawama za nini tena mke wangu? Umeongea
nimekukubalia!
Nimekwishakwambia nitakwenda kuzungumza na Richard
asubuhi hii ili tumsikilize na yeye ana maoni
gani!”
RICHARD
baada ya kumtupia funguo mzee Rama na kutoka ofisini,alielekea moja kwa moja
hadi ilipo ofisi ya baba yake. Aliingia na kumkuta Katibu Muhtasi wa baba yake
ambaye ni mama wa makamo, akamsalimia kwa Kiingereza kwa dhamira ya kukwepa
kutoa shikamoo.
“Baba yupo?” Richard aliuliza baada ya kusalimia,
wakati huo huo akauangalia mlango wa ofisi ya mzee Ken.
“Bado
hajafika,” mama huyo alijibu huku akimwangalia Richard usoni.
Richard
akashukuru na kutoka. Akaelekea kwenye korido inayoelekea kwenye lifti,
akaisikia kengele ya lifti inayoashiria kuwasili kwa lifti kwenye ghorofa hiyo
na kuusikia mlango wake ukijifungua. Wakatoka watu wawili, mzee Ken na dereva
wake aliyekuwa amebeba mkoba wa ofisini. Richard akasimama.
“Nimetokea
kukuulizia sasa hivi,” Richard alisema na kumsalimia baba yake baada ya
kukaribiana huku dereva wa baba yake akisalimiana naye bila ya
kusimama.
“Vipi una tatizo?” mzee Ken aliuliza.
“Nilikuja
kuhusu masuala yale ya TRA.”
“Bado sijayamaliza, nitakujulisha yakiwa
tayari.”
“Halafu pia, nilitaka kutoka na huenda nikachelewa kidogo
kurudi,”
Richard alisema kwa kujiamini, akauparaza mkono wake kwenye
mgongo wa tai iliyompendeza.
“Kabla hujatoka, kwanza nataka
tuzungumze,” mzee Ken alisema na kuondoka.
Kauli hiyo ikamlazimisha
Richard amfuate baba yake.
Wakati wakianza kuingia kwenye ofisi ya
Katibu Muhtasi, wakapishana na dereva wa mzee Ken aliyekuwa akitoka. Richard
akatangulia kuingia ofisini kwa baba yake wakati mzee Ken akiwa amesimama
akisalimiana na Katibu Muhtasi wake.
Wakiwa ofisini, mzee Ken akiwa
amekaa nyuma ya meza yake ya thamani na Richard akiwa amekaa mbele kwenye sofa
ya wageni, mzee Ken alianza kwa kusema, “Mama yako..,” akasita ghafla.
Akabadilisha kauli, “Kuna jambo tumelijadili mimi na mama yako, na tumeona ni
wajibu wetu kukushauri, hata kama jambo hilo litakuwa linaingiliana na maisha
yako binafsi,” hapa alinyamaza na kumwangalia kwa utulivu Richard. Kisha
akasema, “Richard, mna mpango wowote wa kuoana,
wewe na
Judi?”
Swali hilo likaonekana ni la ghafla kwa Richard aliyeonyesha
dhahiri kutolitarajia. Kwa sekunde kadhaa alionekana akiwa kwenye wakati mgumu
wa kuweza kulijibu. Akakumbuka kuulizwa swali kama hilo na Judi siku chache
zilizopita.
“Hatuna mpango wowote,” hatimaye Richard
alijibu.
“Kwa hiyo mtaishi kwenye uhawara mpaka lini? Au hamna mpango
hata wa kutangaziana kuwa ni wachumba?”
Richard akajenga ukimya
mwingine. Kisha aliinua kichwa chake kumwangalia baba yake. “Nitakapokuwa tayari
kuhusu suala hilo nitawaelezeni,” alisema.
“Sipingani na kauli yako,
lakini napata shida kuamini kama kwa kipindi chote mlivyoishi pamoja mkiwa
marafiki mtakuwa hamjawahi kujadiliana jambo hilo?”
Swali hilo
likaonyesha kumpa tena wakati mgumu Richard.
Akakitengeneza kimya
kingine.
“Tulishawahi kulijadili,” hatimaye Richard
alisema.
Safari hii mzee Ken hakuingiza neno. Akamwonyesha Richard
kuwa anasubiri maelezo zaidi ya jambo alilolizungumza.
“Lakini
hatukuelewana!” Richard alisema huku akiiangalia sakafu ya vigae
ing’aayo.
“Kwa nini?”
“Nilimkatalia!”
“Nadhani
sijakuelewa vizuri! Ulimkatalia…?” mzee Ken alisema huku akionyesha kutokiamini
alichokisikia.
“Nilimwambia sina mpango wa kumuoa!”
Kauli
hiyo ikakamilisha mshituko wa mzee Ken, hata hivyo utulivu wake aliouonyesha
uliweza kuuficha mshituko wake.
“Judi alisemaje baada ya kumtamkia
hivyo?” mzee Ken aliuliza na alijaribu kujiweka kwenye utulivu
zaidi.
Safari hii Richard aliuinua uso wake na
kumwangalia baba yake, kisha aliinama tena kuiangalia sakafu. “Hatukuwa na
maelewano tena!” alisema na kunyamaza. Ghafla akaendelea, “Sasa hivi hatuko
pamoja!”
Bila ya kutarajia, mzee Ken alijikuta akishusha pumzi kwa
nguvu. Akaikumbuka kauli ya mkewe iliyoonya hatari ya Richard kuangukia kwenye
mikono ya shangingi. “Kama ulijiona huna mpango wa kumuoa karibuni, kwa nini
usingemweleza ukweli kuwa, kwa sasa hivi huna mpango huo, lakini ungempa
matumaini ya baadaye!” mzee Ken alisema huku akionyesha wazi kutoridhika na
maamuzi hayo ya mwanae na hata sauti yake ilifanya mkwaruzo. “Kwa nini umweleze
kuwa huna mpango wa kumuoa?”
“Nilimweleza hivyo kwa sababu sio chaguo
langu!”
“Jesus!” mzee Ken alihamanika na kushindwa kuamini kuisikia
kauli hiyo ikitoka kwa mwanae. “Kwa hiyo chaguo lako ni nani?”
“Dina!”
Richard alisema bila ya kutafuna maneno.
“Dina?” mzee Ken aliuliza
huku akiwa amepigwa na butwaa na hofu ya kuwa analetewa shangingi aliyetabiriwa
na mkewe ikiwa imekwisha kumvaa. “Ni nani huyo Dina?” safari hii sauti yake
aliipandisha kidogo.
“Sisi tunamjua?” aliuliza kwa lugha ya
Kiingereza.
“Dina Nzasa. Mama
anamjua!”
* * * *
*
Usiku baada ya mkewe kurudi kutoka kwenye kikao
cha harusi na yeye kurudi kutoka kwenye mkutano, wakiwa tena kwenye meza ya
chakula, baada ya kumaliza kula ndipo mzee Ken alipomwelezea mkewe yaliyojiri
kwenye mazungumzo kati yake na Richard.
“Na anasema unamjua huyo
Dina!” mzee Ken alimalizia.
“Dina Nzasa…Dina Nzasa…” mkewe alijaribu
kuvuta kumbukumbu.
“Ah, nimekwishamfahamu!” alisema na uso wake kujaa
nuru. “Si yule binti wa Bwana Nzasa anayeishi karibu na duka la vinywaji hapa
mtaa wa nyuma yetu?”
“Nzasa yupi?” mzee Ken aliuliza huku akionyesha
bado hajamtambua mtu anayefahamishwa.
“Nzasa huyu aliyekuwa Mwenyekiti
wa Bodi ya Utalii, sasa hivi amestaafu. Ana kama miaka miwili tokea astaafu.
Mkewe ni huyu dada anayefanya kazi Ardhi ambaye alitusaidia kupata hati ya
umiliki wa kiwanja chetu kilichopo Boko. Mara hii umekwisha
kumsahau?”
“Nimekwisha kumkumbuka!” mzee Ken alisema. “Si huyu
aliyekuwa
akimtuma binti yake hapa nyumbani kutuletea zile
nyaraka…”
“Haswaa!” mkewe alidakia. “Basi ndiye huyo anayeitwa Dina!”
kisha sauti yake ikatulia na kuendelea, “Dina anavyoonekana ni msichana
aliyetulia na miye nilikuwa sijui kama wana uhusiano wowote na Richard. Au
Richard alikwambia kama nilikuwa naujua uhusiano wao?”
“Yeye alisema,
wewe unamjua Dina.”
“Ni kweli namjua! Richard jamani!” mkewe mzee Ken
akapiga kite cha kuhamanika. Kisha akasema kwa sauti ya kuhuzunisha, “Hili la
Richard kusema eti Judi sio chaguo lake, kwa kweli limeniumiza mno. Unajua
nashindwa kumwelewa mwanao! Alimtongozaje kama sio chaguo lake? Inahuzunisha
kumwona mwanangu amempotezea muda wake yule msichana, kwa kweli siamini! Maskini
Judi, nilikuwa nampenda huyu binti wa watu na yeye mwenyewe alikuwa anampenda
sana Richard. Hivi nitamwangaliaje siku tutakapokutana?” mke wa mzee Ken
akaonyesha kukata tamaa. “Ndio hivyo, hatuwezi tukayaingilia maamuzi ya Richard.
Yeye ndiye anayemjua vizuri Judi kuliko tunavyomjua sisi na hatujui kwa nini
amemchagua Dina, labda ndiye aliyemwona anamfaa. Pengine amependezwa na tabia
zake!”
“Lakini kuna tatizo jingine linaloumiza kichwa kuliko hilo,”
mzee Ken alisema, kisha kabla ya kuendelea aliinamisha kichwa na
kusikitika.
“Ni mtafaruku juu ya mtafaruku,” alisema. Mkewe mzee Ken
akaingiwa na mshangao, akasubiri kusikia mumewe atasema nini.
“Dina
hamtaki Richard!” mzee Ken alisema kwa msisitizo.
Mkewe mzee Ken
akaishiwa nguvu! “Amekwambia Richard mwenyewe?” aliuliza kama asiyeamini
alichokisikia.
“Yeye mwenyewe Richard ameniambia, tena bila ya
wasiwasi wowote!
Anasema amejitahidi sana kumbembeleza Dina kwa
kutumia mbinu tofauti lakini anadai Dina alikataa katakata kukubali kuolewa
naye. Cha ajabu mwanao bado anasisitiza kuwa, Dina ndiye chaguo
lake!”
“Huyu mtoto ana wazimu?” mke wa mzee Ken aling’aka. “Mwanamke
amemkataa si basi!”
“Labda ana sababu ya
kumng’ang’ania.”
“Hawa watoto wetu wa siku hizi watatuua kwa presha.
Kama mwanamke amekukataa si unatafuta mchumba mwingine wa kuja
kumuoa?”
“Naona unayazungumza mambo yaliyopitwa na wakati mke wangu.
Hayo unayoyazungumza ni ya enzi zetu, enzi zetu unatafutiwa mchumba halafu
unaonyeshwa, baadaye unaulizwa kama umemkubali au umemkataa. Ukisema humtaki,
basi unatafutiwa mchumba mwingine. Leo hakuna hilo. Wenyewe kwa wenyewe
wanatafutana huko huko wanapoonana na wakishakubaliana kuoana ndipo wanapokuja
kwetu na kutufahamisha na mara nyingine hata kama wazazi wakikataa, wao
wanalazimisha kuoana.
Lakini hili la mwanao limekuja kiaina yake,
mwanao hatakiwi, yeye analazimisha! Utaliingiliaje jambo kama
hilo?”
“Tena umenikumbusha baba Richard!” mkewe mzee Ken
alisema.
“Nakumbuka mama yake huyu msichana aliwahi kuniambia yuko
mbioni kutaka kumwozesha binti yake…ndio nakumbuka! Aliniambia angeniletea na
kadi ya mchango!”
“Binti yake yupi?”
“Nadhani atakuwa ni
huyu huyu Dina.”
“Anataka kuolewa na
nani?”
“Sijui.”
Uso wa mzee Ken ukaangukia kwenye mshangao.
“Ina maana Richard
hajui kama huyo anayetaka kumuoa kuwa anaolewa na
mtu mwingine?” aliuliza.
“Sijui. Naona huyu mtoto anataka
kutuchanganya!”
“Wacha niongee naye sasa hivi!” mzee Ken alisema na
kuichukua simu yake ya mkononi iliyokuwa mezani. Akampigia
Richard.
Kimya kilipita kati yao wakati mzee Ken akisubiri kujibiwa
kwenye simu aliyoipiga. Hatimaye mzee Ken alijitikisa mwili na kusema, “Richard!
Mbona huyu msichana uliyemzungumza kumbe naye anataka
kuolewa?”
“Najua!” Richard alijibu kutoka upande wa pili wa
simu.
“Lakini ni yeye ndiye niliyempenda na moyo wangu unaniuma kuona
anaolewa na
mtu mwingine!” Richard alisema.
“Nitakupigia
baadaye!” mzee Ken alisema na papohapo alikata simu. Akamwangalia mkewe, “Unajua
huyu mtoto hovyo sana!” aling’aka.
“Kwani
anasemaje?”
“Anasema analijua jambo hilo!”
“Jambo
gani?”
“La Dina kuolewa!”
“Ebo!” mkewe mzee Ken alisema kwa
mshangao.
“Ndivyo anavyodai! Halafu anaendelea kusema, eti huyo ndiye
aliyempenda na moyo wake unamuuma sana kuona anaolewa na mtu mwingine! Huyu
mtoto ana wazimu?”
“Ama kweli moyo ukipenda..!” mkewe alisema bila ya
kumalizia.
Akasikitika peke yake.
“Sasa ana maana gani
kusema hivi?” mzee Ken aling’aka tena.
Mkewe akafikiri, kisha akasema,
“Hawa watoto wetu wa siku hizi si ajabu ukasikia amefanya jambo la ajabu kwa
vitu vya kipuuzi kama hivi!”
Mzee Ken akamwangalia mkewe kwa
kushituka. “Una maana gani?” aliuliza.
“Lakini sidhani kwa Richard
kama anaweza akafanya upuuzi wa aina hiyo,” mkewe alisema huku akijaribu
kuituliza sauti yake.
“Upuuzi gani?” mzee Ken aliuliza huku akionyesha
kama vile alikuwa akikijua kinachotaka kutamkwa na mkewe.
“Anaweza
akajiua!”
“Ohoo, sasa mke wangu unaongea nini!” mzee Ken
alihamanika.
“Khee! Unashangaa hilo? Kwa nini asiweze? Hawa watoto
wetu wa leo wana akili? Au unafikiri huko kusoma nje ndio kutamfanya asiweze
kufanya upuuzi wa aina hiyo?”
“Sasa kwa mfano akiung’ang’ania huo
upuuzi wa kutaka kumuoa
tutafanyaje?”
“Itabidi tukaingize
fitna ili Dina asiolewe na huyo anayetaka
kumuoa!”
“Halafu?”
“Aolewe na Richard!”
“Wakati
huyo Dina kishamwambia wazi mwanao kuwa hamtaki?”
“Yeye Dina ni nani
hadi awe na jeuri hiyo?” mke wa mzee Ken alisema kwa sauti ya
dharau.
“Sasa utafanyaje?”
“Sijajua, lakini naweza
nikaivuruga ndoa yake asiolewe na huyo anayetaka kumuoa, kisha nikakigeuza kibao
mwanangu Richard akageuka kuwa mume wa kuja kumuoa Dina. Babu, mwanamke mwenzake
ni
mwanamke, asikwambie mtu!”
“Utakwenda kumwambia nini huyo
Dina ili akuelewe unachokizungumza?”
“Sina muda wa kuongea naye!” mke
wa mzee Ken alisema kijeuri na kubenua mdomo wake.
“Kumbe utakwenda
kuongea na nani?” mzee Ken aliuliza kwa kauli iliyoonekana kama kitu
anachokizungumzia ni kigumu kufanyika.
“Mama
yake!”
“Tutakuwa tumefanya dhambi!” mzee Ken alisema bila ya
kumwangalia mkewe machoni.
“Kwa hiyo upo tayari mwanao
ajiue?”
Mzee Ken akaduwaa na kumwangalia mkewe.
“Lakini hajasema kama atajiua!” alisema.
“Anayetaka kujiua anasema?
Naomba hili jambo uniachie mimi!”
Mzee Ken alishusha pumzi, akakosa la
kusema.
“Hivi, kama Richard anataka kumuoa Dina, kwa nini ishindikane
kumuoa?” mkewe mzee Ken alisema kwa sauti ya kiburi. “Marafiki zetu
watatuelewaje wakisikia kuwa tumeshindwa kutumia uwezo wetu wa utajiri
kuishawishi familia tuliyoizidi kipato kukubali binti yao aolewe na mtoto wetu?
Mumewe yule mama sasa hivi hana kitu! Mafao yake ya kustaafu alikwenda
kuyanunulia shamba, shamba limewashinda na nasikia wameliuza au wanataka
kuliuza. Sasa hivi yule mama ndiye mlishaji wa nyumba kwa kutegemea hicho
kibarua chake cha huko Ardhi, sijui ana kicheo gani! We si umeona baada ya
kutufanikishia kuipata hati ya kiwanja cha Boko, mbona zile laki tatu tulizompa
kama ahsante hakuzikataa?
Azikatae ana jeuri hiyo?”
Mzee Ken
akabaki kuwa bubu.
“Na sitaki umwambie Richard lolote!” mkewe alionya.
“Niwachie mimi mambo yote nitayaweka
sawa.”
******
ILIKUWA
usiku muda mfupi baada ya taarifa habari kutoka kwenye runinga kumalizika, mama
yake Dina aliusikia mngurumo wa gari inayosimama nje ya nyumba yao, kisha
akasikia mlio wa mlango wa gari uliofungwa. Akajua ni mgeni wa hapo
nyumbani.
“Nadhani kuna mgeni,” mzee Nzasa alisema akiwa amekaa
sebuleni kwenye sofa akiangalia runinga.
Mama yake Dina aliinuka
kutoka kwenye sofa akaenda mlangoni.
“Hodi!” sauti ya mwanamke
ilisikika kutoka nje akiwa amekwishaingia ndani ya uzio wa nyumba hiyo kupitia
kwenye geti dogo lililokuwa wazi.
“Karibu,” mama yake Dina aliitikia
akiwa ndani, akaufungua mlango wa mbele. “Oh, karibu mama Richard,”
alisema.
“Ahsante mama Dina,” mke wa mzee Ken alisema na kuingia
ndani.
“Karibu mama, karibu!” mzee Nzasa alisema alipomwona mke wa
mzee Ken.
“Ahsante shemeji,” mama Richard alisema na kumpa mkono mzee
Nzasa na kusalimiana naye kabla ya kukaa kwenye sofa.
“Gari umeiacha
na mtu nje?” mama Dina aliuliza.
“Hapana.”
“Hakuna haja ya
kutia wasiwasi, vibaka hawapitipiti kwenye mtaa huu,” mzee Nzasa alisema. “Wacha
niwapisheni.”
“Ah, hapana shemeji, mbona nimekuja kwa mazungumzo ya
kawaida
tu,” mama Richard alisema.
“Lakini si umekuja kwa
ajili ya kumwona mwenzako?”
“Ni kweli, lakini sio
faragha.”
“Usijali, nitaangalia TV ya chumbani, nyie endeleeni,” mzee
Nzasa alisema na kuondoka.
“Ehee, za siku mbili, tatu mama Richard?”
mama Dina aliuliza baada ya mzee Nzasa kuondoka.
“Nzuri tu, za
kwenu?”
“Sisi hatujambo, karibu.”
“Dina yupo?” mama Richard
aliuliza na kuangalia upande wenye korido ambako kuna vyumba.
“Yupo
chumbani kwake anaangalia TV.”
“Kilichonileta kwako mama Dina,” mama
Richard alisema.
“Nakumbuka uliwahi kuniambia unataka kumwozesha binti
yako na ungeniletea kadi ya mchango. Nimeifuata hiyo kadi.”
“Kadi za
mchango bado sijaanza kutoa mama Richard, nikitoa nitakupitishia. Wala usitie
shaka.”
“Ukweli ni kwamba nilianza kutia shaka, nikasema mhh, huyu
mama Dina si aliniambia anataka kumwozesha binti yake na angenipitishia kadi ya
mchango? Mbona kimya? Ndio nimeamua kuja mwenzangu, pengine
umenisahau.”
“Sijakusahau mama Richard, nasubiri tu mambo yaive ndio
nikufuate.”
“Basi kumbe wasiwasi wangu ulikuwa wa
bure.”
“Sijui nisemeje mama Richard, nakushukuru kwa kuyafuatilia haya
mambo, si unajua yanavyochanganya kichwa?”
“Hayo ni ya kuyasema? Mhh,
we haya mambo yaangalie kwa mwenzako tu, lakini yakija kwako lazima
yakuchanganye!” mama Richard alisema, akanyamza na kujenga ukimya mfupi. Kisha
akajiweka vizuri kuuliza swali lililomleta kwenye nyumba hiyo. “Kwani ni binti
yako yupi anayeolewa?” aliuliza.
“Anayeolewa ni Dina!” mama Dina
akajinasisha.
Mama Richard akamudu kuutengeneza mshangao wa bandia
usoni kwake. “Haa! Dina ndiye anayeolewa?” alisema huku sauti yake ikionyesha
kufanikiwa kushangaa.
“Dina mwenzangu!” mama Dina akazidi kujiingiza
kichwa kichwa.
“Anaye rafiki yake, wenyewe wamekubaliana waoane, basi
ndio ameleta
barua ya kumchumbia.”
“Kwa hiyo tayari
mmemjibu?”
“Tumemjibu, sasa tunasubiri alete hayo mahari kisha nasi
tuanze vikao.”
Mama Richard akaitumbukiza karata aliyoipanga kuanza
kuicheza.
“Nakumbuka Dina aliwahi kuniambia kitu kama vile alikuwa
akisubiri majibu yake ya kidato cha sita? Na majibu si tayari yametoka? Kwani
hakuchaguliwa kwenda Chuo Kikuu?”
“Hakubahatika mwenzangu!” mama Dina
alisema na kuguna.
“Imeniuma sana kutochaguliwa kwake!”
Hapo
ndipo mama Richard alipoukamata usukani wa kumwongoza mama
Dina!
“Sasa kwa nini mnakimbilia kumwozesha? Si mngemtafutia kwanza
Chuo cha kusoma? Au hata awe na ajira yake kisha ndio aolewe?”
“Kuna
mipango ya kazi tunayomfanyia.”
“Sasa kwa nini msisubiri kwanza aanze
kazi kisha aolewe?”
“Hata wajomba zake walilizungumza hilo, na sisi
tulimshauri hilo na hajakataa, lakini anauliza hiyo kazi itapatikana lini? Ili
kama kuiahirisha harusi basi ijulikane itaahirishwa kwa muda
gani.”
Mama Richard akajiona yupo karibu ya kumuua Tembo kwa
ubua.
“Akipata kazi sehemu nyingine yoyote si anaweza akafanya? Au
lazima apate huko mnakomtafutia?” alisema.
“Mwenzangu kokote kule! Je,
huko tunakotegemea ikikosekana?”
Mama Richard akaitumbukiza karata
yake ya mwisho.
“Basi mimi nitazungumza na baba Richard ili ampatie
kazi kwenye kampuni yake. Nadhani sio vyema mkafanya haraka ya kumwozesha, bora
aende kwa mumewe akiwa na kazi yake, maisha yenyewe haya ni ya kusaidiana. Tena
nitamwambia baba Richard ampe mshahara mzuri.”
Kitanzi kikawa
kimening’inizwa usoni kwa mama Dina, naye bila ya kusita akakitumbukiza kichwa
chake. “Mbona nitakushukuru mama Richard kama ukiweza kunifanyia hilo!”
alisema.
“Kama mimi mwenyewe nimekuahidi, basi hilo usilitie shaka
nalo. Nitahakikisha baba Richard anampatia Dina kazi yenye mshahara
mzuri!”
Hali ikabadilika ghafla. Mama Dina alijikuta akiwa
ananyenyekea kama kijakazi mbele ya nokoa na hata pale mama Richard alipoaga,
ilibidi mama Dina kutaka kwenda kumuita Dina ili aje
kumsalimia.
“Hapana usimsumbue mtoto, mwache apumzike. Lakini kitu
kimoja mama Dina,” mama Richard alisema kwa utulivu. “Habari hizi za kazi
usimgusie kabisa Dina, usimwambie kama kuna kazi ninayomtafutia.
Na
sitaki ajue kama ni mimi ndiye ninayemtafutia. Na endapo kama
atajua, ama kwa kumwambia wewe mwenyewe au kuambiwa na mtu mwingine yeyote, mama
Dina itabidi unisamehe, ujue sitohangaika kumtafutia kazi mwanao! Naomba hilo
ulizingatie. Please usimwambie!”
“Kwa jina la Yesu Kristo Msalabani,
sitamwambia!”
“Nitafurahi ukilizingatia hilo!”
“Sitomwambia,
hilo nakuahidi!”
Kabla ya mama Richard hajatoka
nje, aliombwa asubiri kidogo ili aitwe mzee Nzasa ambaye alitoka na kumsindikiza
pamoja hadi nje. Huko nje mama yake Dina alionyesha unyenyekevu uliopitiliza kwa
mama Richard na kumwombea kwa kumtaja Yesu kila baada ya muda kabla ya
mama
Richard hajaingia kwenye gari.
Mama Richard alipokuwa
akiondoka na gari lake, mama Dina aliipunga mikono yake yote miwili kwa furaha
yenye unyenyekevu.
* * * *
*
“Nimekwisha kummaliza!” mama
Richard alimwambia mzee Ken wakati alipokuwa akimwelezea kuhusu mazungumzo yake
na mama Dina yalivyokwenda. “Kwa hiyo, kinachotakiwa ni kumwajiri na kumpa kazi
itakayomuweka karibu na Richard na Richard ataitumia nafasi hiyo kumshawishi
Dina asiolewe na badala yake amuoe
yeye!”
“Usitegemee jambo hilo litafanyika kwa
haraka kama unavyozungumza!” mzee Ken alionya huku akiwa ndani ya vazi la pajama
akiwa amelala kitandani kama ilivyokuwa kwa
mkewe.
“Lipi? La kumwajiri? Au la kumshawishi?”
mama Richard aliuliza kwa sauti iliyoonyesha kushituliwa na kauli ya mzee
Ken.
“La kumshawishi Dina hadi akubali,” mzee Ken
alijibu akiwa amelala chali. “Lazima litachukua muda hadi kufanikiwa. Na endapo
itakuwa hivyo, ujue uwezekano wa Dina kuolewa na huyo mchumba wake mara tu baada
ya kupata kazi utakuwepo. Utakuwepo kwa sababu kikwazo kilichokuwa
kimeisimamisha ndoa yao kitakuwa hakipo tena! Kwa hiyo, ipo hatari ya ndoa hiyo
kufanyika wakati Richard akiwa bado hajafanikiwa kumshawishi Dina kuizuia ndoa
hiyo!”
“Ken, lazima itumike mbinu kumzuia Dina asiolewe na huyo
mchumba wake!” mama Richard alisema kwa sauti kavu.
“Kivipi?” mzee Ken
aliuliza kwa sauti ya upole.
“Mbinu ni hii Ken; utakapomwajiri Dina,
umpe barua itakayomuweka chini ya uangalizi wa miezi mitatu hadi ajira yake
itakapothibitishwa,” mama Richard alisema. “Barua hiyo itatoa masharti
atakayoyasaini, na moja ya masharti hayo ni kuwa, kwa kipindi hicho cha miezi
mitatu atakachokuwa anaangaliwa utendaji wake, hakutakuwa na ruhusa ya dharura
atakayopewa itakayozidi siku moja labda itokee kuwe na msiba wa kifo cha mmoja
wa wazazi wake, kaka au dada wa kuzaliwa naye! Sharti hilo litambana ashindwe
kuomba ruhusa kwa ajili ya kwenda kufunga
ndoa!”
“Usisahau kuwa, umekwisha kujenga ukaribu
na mama yake na anaweza akautumia ukaribu huo kuja kumwombea mwanae apatiwe
ruhusa ya kwenda kuolewa!”
“Hapo ndipo
atakapokosea! Nitaitumia nafasi hiyo kumweleza umuhimu wa kazi ya mwanae
kimaisha, na nitamshawishi na lazima atashawishika kukubali kuliahirisha suala
la ndoa hadi baada ya miezi mitatu aliyopewa mwanae imalizike. Nina hakika kwa
mshahara utakaokuwa unampa Dina, kamwe hatokubali kuilaani bahati
hiyo.”
“Kuna umuhimu wa Richard kuambiwa kusudio
hilo?”
“Hapana, kwa sasa asiambiwe! Ataambiwa
baada ya Dina kuajiriwa.” “Na ikimalizika miezi hiyo mitatu huku Dina akiendelea
na msimamo wake wa kukataa kuolewa na Richard, hapo itakuwaje?” “Ikatishe ajira
yake!”
* * *
* *
Mawasiliano kati ya mama Richard na mama Dina
yakaendelea bila ya watoto wao kufahamu, huku mmoja akiijua njama anayoifanya
dhidi ya mwenzake, mwingine akiwa haijui njama anayofanyiwa na
mwenzake!
Baada ya wiki moja, zengwe la mama
Richard likawa limekamilika, na ulipofika usiku akampigia simu mama
Dina!
“Mwambie Dina, kesho asubuhi saa nne awe ofisini kwa mzee Ken,”
mama Richard alimwambia mama Dina kwenye simu na kumwelekeza ilipo ofisi
yenyewe. “Aende na vyeti vyake vya shule. Akifika mapokezi aseme ameitwa na mzee
Ken.”
“Nitamwambia usiku huu aanze kuvitafuta vyeti vyake!” mama Dina
alisema kwa sauti iliyonyenyekea.
“Yeye akifika mwambie ajitambulishe
kwa mzee Ken kuwa ni mtoto wa mzee Nzasa.”
“Nitamwambia dada, kwa
kweli nakushukuru sana.” “Haina tabu. Haya usiku mwema.”
“Nawe pia.
Yesu akubariki mama
Richard!”
“Amen.”
****
RICHARD
alikuwa amesimama, mgongo wake ukiwa umeelekezwa mlangoni wakati alipokuwa
akizungumza na msichana mfanyakazi anayefanya kazi idara ya mapokezi kwenye
kampuni ya mzee Ken. Richard aliyekuwa amemsindikiza mgeni wake aliyemtoa hadi
hapo mapokezi na kuagana naye sekunde chache zilizopita, lakini kabla hajarudi
tena ofisini kwake, akakumbuka kuwa, asubuhi hiyo magazeti aliyokuwa ameletewa
ofisini kwake yalikuwa pungufu.
“Leo sijaliona
gazeti la Flames likiletwa ofisini kwangu, wewe unalo hapo kwako?” Richard
alimwuliza msichana huyo wa mapokezi.
“Mtu wa magazeti leo kaleta hilo
moja tu la Flames, na limepelekwa kwa Mkurugenzi,” msichana wa mapokezi
alijibu.
Wakati msichana yule alipokuwa akijibu, mlango wa kuingilia
hapo mapokezi uliotengenezwa kwa kioo ukasikika ukifunguliwa. Macho ya yule
msichana yakavutika kuuangalia mlango huo, kitendo hicho nacho kikamvuta Richard
aangalie mlangoni.
Wakamwona Dina
akiingia!
Kitendo cha kuonana kati ya Dina na
Richard kikawa kimewaletea mshituko wote wawili na kuonyesha dhahiri hakuna
yeyote aliyetarajia kukutana na mwenzake eneo hilo huku Dina akionyesha wazi
kabla ya hapo alikuwa hajui kama Richard alikuwa akifanya kazi kwenye kampuni
hiyo!
Tukio la kumwona Dina akiingia kulimfanya
Richard agande kwa sekunde chache huku akiwa hayaamini macho yake kama aliyekuwa
akimwangalia alikuwa kweli ni Dina. Akili yake kwa sekunde hizo chache ilikuwa
kama iliyokuwa imepooza, ikashindwa kuwaza kwa haraka. Akabaki akiwa ameduwaa
huku akimwangalia Dina ambaye naye alikuwa akimwangalia. Ndipo Richard
akakumbuka tukio lililoufanya moyo wake uzidi kupata
pigo…
Aliikumbuka kauli aliyoambiwa na Dina mara
ya mwisho walipokutana nje ya duka linalouzwa simu, kauli iliyomtaarifu kuwa,
Dina na John Sailas wanatarajia kufunga ndoa wakati
wowote!
* * * *
*
Richard alikuwa akimfahamu John Sailas, wote
waliwahi kusoma shule moja ya Azania, walikutana wakiwa kidato cha kwanza na
wakawa darasa moja. Hawakuwa na ukaribu wa kuitwa marafiki, lakini walikuwa na
ukaribu wa kuwa wanafunzi waliosoma darasa moja. Walisoma wakiwa pamoja kwa
muhula mmoja pekee. Muhula wa pili, Richard alihamishiwa shule nyingine nchini
Kenya.
Kwa upande mwingine ujuano wa kujuana kati
ya Richard na Dina ulikuwa ni wa muda mrefu. Walijuana tokea wakiwa wadogo
kutokana na kuishi eneo moja na mitaa yao ilikuwa jirani. Wakati Richard
alipokuwa kidato cha kwanza, Dina alikuwa darasa la sita. Mwanzo wa Richard
kuanza kumtongoza Dina kilikuwa ni kipindi Richard alichokuwa amerudi likizo
kutoka nchini Kenya wakati huo akiwa kidato cha tatu na Dina akiwa ameingia
kidato cha kwanza.
Kupoteana kwao kulikosababishwa
na Richard kusoma nchini Kenya, kulimfanya Richard ayashangae mabadiliko ya
ghafla ya kimwili yaliyomtokea Dina baada ya yeye Richard kurudi nchini kwa
ajili ya likizo. Richard alimwona Dina kama aliyekua haraka kimaumbile. Umbile
zuri la kike lililokuwa limejichomoza kwa kuvigawa viungo vya Dina kwenye hesabu
sahihi, kulimfanya Richard aingiwe na hisia za matamanio ya mapenzi dhidi ya
jirani yake huyo.
Uzuri wa Dina na umbile lake
hilo lililoanza kutatanisha wanaume wengine lilimfanya Richard awe na wakati
mgumu wa kushindwa kuzificha hisia zake na kujikuta kama mtu anayepigwa na
shambulizi la ghafla kila alipokuwa akikutana na Dina njiani. Akashindwa
kujizuia, akaamua kumkabili Dina na kumpa yake
kauli.
Dina
akamkataa!
Richard hakukata tamaa. Akabuni mbinu
mpya ambayo kwa upande mwingine ilikuwa kama ya kitoto; mbinu ya kulitumia jina
la baba yake. Akawa anamwomba Dina aende naye nyumbani kwao na kumwambia kuwa,
baba yake angefurahi sana kama angemwona naye. Richard alikuwa akiamini kama
Dina angeukubali mwito huo wa kwenda nyumbani kwao, ule ufahari wa kimaisha
ulioenea kila sehemu ya nyumba yao ungekuwa ni chachu kuu ya kumfanya Dina
amkubali kirahisi. Hata hivyo, Dina hakulikubali karibisho
hilo!
Si kwamba Dina alikuwa hamjui baba yake
Richard, alikuwa akimjua vizuri sana mzee Ken kuwa ndiye baba yake Richard, na
utajiri wa mzee huyo ulikuwa ukijulikana na kila mtu kwenye kila kona ya maeneo
hayo wanayoishi. Hata hivyo, sababu iliyomfanya Dina kumkataa Richard ilitokana
na Dina kujiona ndio kwanza ameanza masomo ya Sekondari na alikuwa amepania
afike mbali kimasomo, hivyo hakuwa tayari kujiingiza katika mapenzi na mwanamume
yeyote.
Hatimaye Richard aliondoka na kwenda
masomoni Uingereza baada ya kufanikiwa kupata chuo, lakini aliondoka akijijua
ana deni la kuja kuhitimisha dhamira yake aliyoiwekea nadhiri kuwa lazima aje
kumpata Dina kimapenzi wakati atakaporudi
likizo.
Likizo yake ya kwanza ilipowadia, Richard
alirudi nchini akiwa na matumaini tele ya kumpata Dina. Alirudi akiwa
amebadilika tabia. Akawa mtu wa kunata na kujisikia huku akionyesha kuuhusudu
Uzungu kupitiliza. Katika siku za mwanzoni mwa likizo yake alidhani kule kusoma
kwake nchini Uingereza kungemfanya Dina ampapatikie na angeweza kumpata
kirahisi. Lakini Dina hakuwa hivyo! Dina aliendeleza msimamo wake uleule wa
kuhakikisha Richard hampati!
Kengele ya hadhari
ikalia kichwani mwa Richard, akagundua kumbe ujivuni ungemharibia mambo.
Akajibadili kutoka kwenye tabia ya ujivuni na kuingia kwenye tabia ya kuwa
mpole, akawa mnyenyekevu mbele ya Dina. Akaepuka kuzungumza stori za mapenzi
kila alivyokuwa akikutana naye. Akaanza kuzungumza stori za matukio ya kusisimua
yaliyopo na yaliyotokea nchini Uingereza. Stori hizo zenye mchanganyiko wa
kutoka kwenye matukio halisi na historia nyingine za kuvutia alizokuwa
akiziangalia kutoka kwenye dokumentari tofauti za vipindi vya kwenye runinga
huku akimudu kuvielezea kwa ufasaha, vikaonekana kumwingia na kumvuta
Dina.
Hali ikabadilika ghafla, Dina akaanza
kuyafurahia mazungumzo hayo kila alipoonana na Richard. Ukaribu wao ukazidi, na
Richard akajaribu kuitumia tena nafasi hiyo kumtaka Dina afike nyumbani kwao,
lakini Dina hakuwa tayari kwa hilo. Hata hivyo, mkaa pamoja na waridi hunukia
waridi. Ukaribu huo ukaanza kuleta mabadiliko, mwelekeo wa kuelekea kwenye
mapenzi ukaanza kimya kimya. Ikafikia mahali ikawa halahala mti na macho!
Richard akakaribia kidogo afanikiwe kumpata Dina
kimapenzi.
Tukio hilo lilianzia usiku wakiwa
pamoja nje ya nyumba ya akina Dina, walikuwa peke yao kwenye eneo hilo
walilokuwa wakipenda kuonana na kuzungumza stori zao. Richard akazungumza neno
lililomfurahisha Dina, Dina akajikuta akicheka na kukiegemeza kichwa chake
kwenye bega la Richard. Ghafla Richard akapata akili ya kujaribu bahati yake,
akauzungusha mkono wake kwenye shingo ya Dina na kumkumbatia. Akaunamia uso wa
Dina na kuonyesha dhahiri alikuwa na lengo la kuubusu mdomo wa Dina. Mungu si
Adam, akaishikia siku ya Richard kwa Richard kujikuta akinyonyana ndimi na Dina
bila ya bishano la aina yoyote.
Siku hiyo Richard
hakuiamini bahati hiyo! Hata alivyokwenda kulala, usingizi ulikataa kuja mapema,
muda mrefu alijikuta akilifikiria tendo hilo na kuwa kama gurudumu la santuri ya
video iliyokuwa ikijirudia wakati wote!
Lakini
bahati hiyo ikaja kuharibiwa na marafiki zake ambao ni watoto wa matajiri kama
alivyo yeye. Badala ya kuendelea na mkakati wa kutulia uliomletea matunda kwa
Dina, Richard akaanza kukosa utulivu. Marafiki zake wakaanza kumyumbisha kwa
kumfuata nyumbani kwao na kwenda naye kwenye madisko. Ikawa leo huko, kesho
kule. Mara kwenye fukwe za bahari, mara wako na wasichana hawa, kesho wale. Dina
akazishitukia tabia za Richard za kubadilisha wasichana, hata hivyo akaamua
asimlalamikie Richard jambo hilo.
Aliamua
asimlalamikie kwa sababu hakuuona ulazima huo! Ukaribu wao haukuwa mzito hivyo,
hata kile kitendo cha faragha kilichofanyika kati yao cha kunyonyana ndimi zao
hakikuwa kimemwumiza kutokana na kuwa, kilifanyika mara
moja!
Dina hakukubali tena kukirudia kitendo hicho
kila walipokuwa pamoja. Akawa amembadilikia ghafla Richard! Akaanza kumkwepa
Richard kila Richard alivyokuwa akiomba kuonana naye na hata wakati walivyokuwa
wakionana, Dina hakuwa tayari tena kukubali kusimama eneo lolote la faragha.
Akawa anampa picha ya wazi Richard kumwonyesha kuwa, sasa ule ukaribu uliokuwa
ukihitajiwa kati yao haukuwa na umuhimu tena! Richard akaanza kumlalamikia Dina
kuwa amebadilika ghafla, hata hivyo Dina aliamua kutompa sababu ya kwa nini
alikuwa akifanya hivyo!
Kugundua kuwa alikuwa
hatakiwi na Dina kulianza kumchanganya Richard, lakini kilichomchanganya zaidi
ni kule kutoijua sababu iliyomfanya Dina auchukue uamuzi huo wa ghafla wa
kumkataa pasipo kumtamkia. Matumaini ya uhusiano wao baada ya tukio la
kuzikutanisha ndimi zao akayaona yakiteleza mikononi mwake huku juhudi za kuzuia
zikipoteza dalili zote.Hapo ukawa mwanzo wa Richard kugundua kile alichokuwa
hakijui mwanzoni kuwa, kitendo cha kukataliwa na Dina kilikuwa ni jambo
lisilokubalika kwake!
Mapenzi ya kumpenda Dina
yalikwisha kumuingiza kichwa kichwa kiasi cha kujiona hawezi akajitoa! Ukawa ni
mshituko ambao hakuutarajia, likawa ni pigo kwake kukataliwa baada ya kupenda!
Akajaribu kuomba aina yote ya misamaha, lakini Dina hakuonyesha dalili ya kurudi
nyuma kwenye uamuzi wake!
Wakati akiwa kwenye
jitihada zote za kutaka kulirudisha tena penzi kwa Dina, likizo nayo iliyokuwa
ikimuweka nchini ikaisha. Richard akarudi Uingereza bila ya mafanikio ya
kuurudisha tena uhusiano wake na
Dina!
* * * * *
****DINA
ndani ya ofisi moja na RICHARD..mpenzi wake wa utotoni…nini
kitaendelea??
****Je? Ile mbinu ya Mama Richard
itazaa matunda.
***Ndoa ya John na Dina…na vipi hatma ya
Judy???
**NI VITA KATI YA PESA, MAPENZI NA
WIVU!!!
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment