IMEANDIKWA NA : NYEMO CHILONGANI
*********************************************************************************
Simulizi : A Sex Video Scandle
Sehemu
Ya Kwanza (1)
“YOU ARE THE BEST IN THE WORLD......MARRY ME FILBERT.....BE MY VALENTINE TONIGHT....WE ARE GOING TO BE CHAMPION THIS SEASON.....” Hayo yalikuwa baadhi ya mabango kadhaa ambayo yalikuwa yameshikwa na mashabiki wa timu ya Newcastle United, mashabiki wa kiume na mashabiki wa kike.
Kelele zilikuwa zikizidi kuongezeka, zilikuwa zimebaki dakika ishirini kabla ya timu hizo kuingia uwanjani na kisha mechi hiyo kuanza. Kila shabiki wa timu ya Newcastle bado alikuwa na hamu kubwa ya kumuona mchezaji huyo ambaye alijulikana zaidi katika kuzifumania nyavu za timu pinzani.
Filbert Martin, hilo ndio lilikuwa jina la mchezaji huyo ambaye katika siku hiyo ndio ilikuwa siku yake ya kwanza kuichezea timu ya mpira wa miguu ya Newcastle United hapo nchini Uingereza. Filbert alikuwa kijana kutoka nchini Tanzania, kijana ambaye alikuwa na shauku kubwa ya kucheza mpira wa kulipwa katika moja ya nchi ya Ulaya, katika miaka hiyo, ndoto zake zilikuwa zimekwishakamilika.
Katika miaka ya nyuma Filbert alikuwa kijana wa kawaida sana ambaye alikuwa na ndoto ya kuwa mwanasheria nchini Tanzania. Alipokuwa akisoma kidato cha kwanza katika shule ya sekondari ya Makurumla, kila siku ndoto yake ilikuwa ni kuwa mwanasheria mkuu nchini Tanzania. Kila alipokuwa akisoma, ndoto yake bado iliendelea kukua maishani mwake, alikuwa akijitahidi sana kusoma, hakuona kama angeweza kukamilisha ndoto ya kuwa mwanasheria mkuu nchini Tanzania bila kusoma.
Nyumbani kwao hawakuwa na uwezo mkubwa, wazazi wake walifanikiwa kujenga nyumba lakini nyumba hiyo wala haikuwa kubwa, ilikuwa ni nyumba ya kawaida sana na alikuwa akiishi na wazazi wake pamoja na kaka yake mmoja, Denis na dada yake, Rachel. Maisha hayakuwa mazuri sana, mzee Martin hakuwa na fedha za kumfanya kufanya mambo makubwa kwa ajili ya familia yake au kuanzisha biashara kubwa, kitu ambacho kila siku alikuwa akiwasisitizia watoto wake ni kuhusu elimu tu.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Ndoto za mzee Martin zilikuwa ni kuwaona watoto wake wakisoma kama alivyokuwa amesoma. Japokuwa hakuwa na fedha nyingi lakini kila siku alikuwa akiamini kwamba endapo mtu ukasoma basi kwa asilimia kadhaa maisha yako yangeweza kubadilika huko mbele kutokana na elimu uliyokuwa nayo kuweza kukubalisha katika mazingira unayoishi. Kila siku kilio chake kilikuwa hicho hicho, watoto wake wasome ili waweze kukamilisha ndoto zao ambazo walikuwa wamejiwekea katika maisha yao.
Maneno ya baba yao ndio ambayo yaliwafanya kusoma sana, kila siku Filbert alipokuwa akilala mawazo yake yalikuwa yakifikiria kitu kimoja tu, kuwa mwanasheria mkuu nchini Tanzania. Ndoto yake iliendelea kukaa ndani ya moyo wake mpaka pale ilipokuja kufa na kuanza kujiwekea ndoto nyingine kabisa, ndoto ambayo wala haikuhitaji usome sana, alitamani kuwa mwanasoka mkubwa duniani.
Hiyo ndio ndoto nyingine ambayo ilikuwa imekuja moyoni mwake. Ndoto hiyo ilianza kuja mara baada ya kuchaguliwa katika timu ya darasa la kidato cha kwanza shuleni hapo, japokuwa ilikuwa mara yake ya kwanza kucheza mpira katika uwanja mkubwa, Filebrt akaanza kusikia kitu cha tofauti moyoni mwake kuhusiana na mchezo wa mpira wa miguu. Uwezo wake katika ufungaji ulikuwa mkubwa sana, wanafunzi wenzake walionekana kumshangaa kwani uwezo ule ulikuwa umepanda kwa haraka sana.
Akatamani kuwa mchezaji mkubwa wa kulipwa duniani, hakutaka kucheza soka nchini Tanzania, kitu alichokuwa akikitaka ni kucheza soka katika moja ya nchi za Ulaya. Kitendo cha kuwa na ndoto hiyo kikamfanya hata uwezo wake wa darasani kupungua, hakuona kuwa na sababu ya kusoma sana na wakati wachezaji wengi wa mpira duniani hawakuwa wamesoma sana.
Hakujua ni kwa jinsi gani angeweza kukamilisha kile ambacho alikuwa amejiwekea moyoni mwake. Familia haikuwa na fedha za kutosha za kuweza kumsafirisha kumpeleka katika moja ya nchi za Ulaya kwa ajili ya kucheza soka la kulipwa jambo ambalo lilimfanya kubaki kimya kwani hata kama angemwambia baba yake bado asingeweza kumsafirisha kuelekea barani Ulaya kwa ajili ya kucheza soka.
Bado kila siku alikuwa na ndoto ya kucheza mpira katika nchi mojawapo Ulaya. Japokuwa alikuwa na umri mdogo wa miaka kumi na tano, alijitahidi sana kufanya mazoezi huku akiamini kwamba kungekuwa na siku ambayo angepanda ndege na kuelekea Ulaya kwa ajili ya kucheza mpira wa kulipwa.
Uwezo wake bado ulikuwa ukimshangaza kila mtu, kila alipokuwa uwanjani alionekana kuwa makini sana. Alikuwa hodari katika kufunga magoli ya kila aina. Alikuwa na uwezo mkubwa wa kutumia miguu yake yote miwili, alikuwa na uwezo mkubwa wa kutumia hata kichwa chake, pamoja na hayo yote, Filbert alikuwa hodari katika kupiga chenga.
“Huyu dogo atakuja kuwa mchezaji mzuri sana hapo baadae” Jamaa mmoja ambaye alikuwa akiitazama mechi katik ya timu ya kidato cha kwanza na kidato cha tatu katika uwanja wa shule ya Makurumla alimwambia mwenzake.
“Dogo anajitahidi sana. Sasa katika umri kama huu ndio anatakiwa kwenda Ulaya kucheza ila kwa hapa Tanzania, utakuta mpaka anakuwa babu bado yupo humu humu kwenye mechi za mchangani” Kijana mwingine alimwambia mwenzake.
Uwezo wake ulikuwa ukiridhisha sana uwanjani kwa kila aliyekuwa akimwangalia. Umakini wake mbele ya goli ulikuwa mkubwa sana, ulimvutia kila mtu ambaye alikuwa akimwangalia. Bado ndoto yake ya kucheza mpira wa kulipwa Ulaya ilikuwa ikiendelea moyoni mwake. Alipoona kwamba bado muda unazidi kwenda na hakukuwa na kitu kilichobadilika, akaamua kumwambia baba yake.
“Unajua kucheza mpira kweli?” Mzee Martin alimuuliza Filbert.
“Najua sana”
“Wewe unajua vipi kama unajua?” Mzee Martin alimuuliza Filbert.
“Wengi wanaoniangalia wanasema ninajua” Filbert alijibu.
“Sawa. Ila soma, nataka utimize ndoto yako ya kuwa mwanasheria mkuu hapa Tanzania” Mzee Martin alimwambia Filbert.
“Sasa hivi nimebadilisha wazo baba”
“Wazo gani?”
“Nataka kuwa mwanasoka mkubwa duniani. Nataka niende nikacheze Ulaya” Filbert alimwambia baba yake ambaye alibaki akiwa amepigwa na mshangao.
“Oooopppssss....!” Mzee Martin alijikuta akishusha pumzi ndefu.
“Vipi tena baba? Haiwezekani?”
“Inawezekana sana. Kama umeamua inawezekana sana” Mzee Martin alimwambia Filbert.
“Nataka kukamilisha ndoto yangu baba”
“Usijali. Nitajitahidi kadri ya uwezo wangu kukufanya kuwa mwanasoka mkubwa duniani” Mzee Martin alimwambia Filbert.
Kitu cha kwanza alichokifanya mzee Martin ni kumtafutia uhamisho Filbert kutoka katika shule ya sekondari ya Makurumla na kumpeleka katika shule ya sekondari ya Makongo. Hapo ndipo ambapo Filbert alitakiwa kufanya kile ambacho alikuwa akitaka kukifanya kila siku katika maisha yake. Kutokana na uwezo wake wa kucheza mpira kuwa mkubwa, katika mechi ya kwanza tu shuleni hapo akajikuta akiitwa katika timu ya shule.
Mwaka huo alikuwa kidato cha pili. Timu ya shule ilikuwa imejaza wachezaji wa kidato cha tatu na cha nne na ni Filbert tu ndiye ambaye alikuwa mchezaji kutoka katika kidato cha chini. Uwezo wake wa kucheza mpira uliendelea kuonekana kila siku, akafanikiwa kufunga magoli mengi kitu ambacho walimu walionekana kuvutiwa nae.
“Nimewaona wanafunzi wengi wakiwa wamepita hapa na kuwa wanasoka, ila kwako, umekuwa mtu wa tofauti sana” Mwalimu Kessy alimwambia Filbert katika kipindi ambacho alikuwa akijiandaa kwa ajili ya kucheza mechi katika mashindano ya Umitashumta.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Asante. Ninataka kutimiza ndoto yangu ya kuwa mwanasoka mkubwa duniani” Filbert alimwambia mwalimu Kessy.
“Inawezekana sana. Cha msingi wewe jitume tu, hiyo ndio siri ya mafanikio” Mwalimu Kessy alimwambia Filbert ambaye alizidi kujituma zaidi na zaidi.
Kadri muda ulivyozidi kwenda mbele na ndivyo ambavyo uwezo wake wa kufunga magoli ulivyozidi kuongezeka zaidi na zaidi. Wanafunzi kwa walimu wakatokea kumpenda, wasichana kama kawaida yao wakaanza kumletea shobo lakini Filbert hakuonekana kupenda wanawake, alichokuwa akikitaka ni kuwa mchezaji mkubwa.
Japokuwa kila siku alikuwa akiwakataa wanawake lakini mwisho wa siku uvumilivu ukaonekana kumshinda kabisa mara baada ya kujikuta akiingia katika mikono ya mtoto wa kitajiri, Amanda Frank ambaye alikuwa akisoma katika shule ya Kenton iliyokuwa Sinza. Siku ambayo alikutana na msichana huyo ilikuwa ni siku ambayo shule ya Makongo ilipoomba kucheza mechi na shule ya Kenton maombi ambayo yalikubaliwa na wachezaji pamoja na mashabiki wa timu hiyo ya shule kuelekea huko.
Wanafunzi wa shule ya Makongo hawakuonekana kuhofia, walikuwa wakijiamini sana, uwepo wa Filbert katika kikosi chao kuliwafanya kujiona kuwa washindi katika kila mechi ambayo walikuwa wakienda kucheza. Siku hiyo ndio ambayo Filbert akaonyesha uwezo wa juu, sauti za wakinadada ambazo zilikuwa zikisikika kwa kusema ‘USINIUMIZIE’ zilikuwa zikimchanganya sana na kujikuta akicheza kwa moyo mmoja.
Filbert alionyesha uwezo mkubwa kitu ambacho kilimpelekea kufunga magoli matatu peke yake. Uwezo ule ukawafanya wasichana wengi wa shule ya Kenton kuvutiwa nae. Kila mmoja alikuwa akitaka kumfuata japo kumuomba namba ya simu ila hakukuwa na msichana ambaye alikuwa akijiamini, ni msichana Amanda ndiye ambaye alimfuata Filbert na kisha kuanza kuongea nae.
“Hongera” Amanda alimwambia Filbert ambaye akauinua uso wake na kumwangalia msichana huyo, alikuwa Amanda, msichana ambaye alikuwa miongoni mwa wasichana wazuri shuleni hapo.
“Asante” Filebrt alijibu na kisha kuyarudisha macho yake chini na kuendelea kufunga kamba za viatu vyake.
“Unajua sana kucheza mpira, nani kakufundisha kucheza mpira?” Amanda alimuuliza Filbert ambaye akaachana na kazi ya kufunga kamba za viatu na kumwangalia Amanda usoni.
“Sikufundishwa, nimejikuta tu nikijua kucheza mpira” Filbert alimjibu Amanda.
“Sawa. Baba yako alikuwa ni mchezaji mpira?”
“Hapana”
“Au babu yako?”
“Mmmh! Sijui”
“Sawa. Nimefurahi kuongea nawe”
“Usijali”
“Ninaitwa Amanda Frank”
“Mimi ninaitwa Filbert Martin”
“Nimefurahi kukufahamu. Chukua hiki kikaratasi” Amanda alimwambia Filbert na kisha kumkabidhi kikaratasi.
“Kina nini?”
“Utaona tu kina nini. Utakachokikuta naomba ukifanyie kazi” Amanda alimwambia Filbert.
“Naruhusiwa kukifungua hapa?”
“Hapana. Kifungue nitakapoondoka” Amanda alimwambia Filbert.
Katika kipindi chote ambacho Amanda alikuwa akiongea na Filbert wasichana wengine shuleni hapo walikuwa wakimwangalia kwa macho ya wivu. Nafasi aliyoipata Amanda ilionekana kuwa nafasi adimu sana ambayo kila mmoja alikuwa akiitamani kuipata. Baada ya dakika kadhaa, wanafunzi wa shule ya Makongo wakatakiwa kuingia ndani ya mabasi yao na kuanza kuondoka mahali hapo kupelekwa majumbani kwao.
Filebrt alitulia katika kiti chake, kila mmoja katika kipindi hicho alikuwa akiizungumzia mechi hiyo pamoja na uwezo ambao Filbert alikuwa ameuonyesha uwanjani. Uwezo wake ule ndio ambao uliifanya timu ya shule ya Makongo kuibuka na ushindi mnene. Filbert hakuwa mtu wa makuu, hakuringa, alijiona kuwa sawa na wengine.
Kile kikaratasi alichopewa na Amanda kilikuwa mkononi mwake, hakuonekana kuwa na habari nacho, stori za mechi ile zilikuwa zimeshika kasi na hivyo kusahau kabisa kukisoma. Gari lilipofika Kijitonyama, Filbert akateremka, akaagana na wenzake na kisha kuelekea nyumbani. Huku akiwa njiani, akakumbuka kwamba alikuwa amepewa kikaratasi na msichana Amanda, alipojiangalia mkononi, kilikuwepo, alichokifanya ni kukifungua na kisha kukiangalia kilikuwa na nini, kilikuwa na namba ya simu ambayo ilikuwa imeandikwa huku chini kukiwa na alama ya kopa, unajua alama hiyo ilimaanisha nini? Ilimaanisha MAPENZI.
Kitendo cha kuiona namba ile ya simu ya Amanda kilionekana kumshtua kupita kawaida, hakutegemea kama kungekuwa na msichana ambaye angeweza kumfanyia kitu kama kile. Katika maisha yake hakutaka kabisa kuwa na msichana yeyote yule lakini kwa jinsi Amanda alivyokuwa alionekana kuwa tofauti sana.
Ni kweli alikuwa amewaona wasichana wengi warembo ambao walikuwa na mvuto kupita kawaida, wasichana ambao kila walipokuwa wakitabasamu basi ni lazima moyo wako ungesisimka sana. Kwa msichana kama Amanda, alionekana kuwa tofauti sana, kitendo cha Amanda kuja na kuongea nae na kisha kumgawia kikaratasi kile kilimfanya kufurahi japokuwa hakutaka kukitilia maanani.
Hakutaka kumpa nafasi msichana katika maisha yake, aliwakumbuka wachezaji soka wengi ambao walishuka kiwango kwa asilimia kubwa kisa wanawake. Alimkumbuka Gerard Pique, Ronaldinho na watu wengine, kwa wanamichezo kama yeye, wanawake walionekana kuwa chanzo namba moja kwa mchezaji kushuka kiwango.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Hakutaka kuwa na msichana kabisa, alijiona kuwa na safari ndefu mbele ya maisha yake, safari ambayo ilihitaji nguvu ya ziada mpaka kufika pale alipotaka kufika. Kitendo cha kuwa na msichana kilimaanisha kwamba angetumia muda mrefu kuwa na msichana kuliko kufanya mazoezi kitu ambacho hakutaka kabisa kitokee.
Filbert alibaki akiziangalia namba zile, moyoni mwake taswira ya msichana Amanada ikaanza kumkaa kichwani na kuanza kujiona hali ya tofauti kabisa. Moyo wake ukaanza kujisikia kitu cha tofauti sana, kitu ambacho hakuwahi kukisikia katika maisha yake yote. Mchoro wa kopa ambao ulikuwa ukionekana katika kikaratasi kile ukaonekana kumchanganya kupita kawaida, akawa anauangalia mara mbili mbili huku akionekana kutokuamini kama msichana mrembo kama Amanda angeweza kumwandikia kitu kama kile.
Filbert akainuka kutoka kitandani, akaifuata simu yake ambayo alikuwa ameiweka kwenye socketi ya umeme akiichaji na kisha kuichukua na kuiwasha. Katika kipindi hicho lengo lake kubwa lilikuwa ni kumpigia simu Amanda, alijiona kuwa na umuhimu wa kumpigia simu msichana huyo. Akaanza kubonyeza vitufe vya simu ile. Hata kabla hajabonyeza kitufe cha kijani kwa ajili ya simu kuita, Filbert akatulia kwanza na kuanza kufikiria mambo mengi katika maisha yake.
Alikuwa akiupenda sana mpira, hakutaka kujihusisha na wanawake kabisa kwa kuamini kwamba uwezo wake wa kucheza mpira ni lazima ungeshuka. Orodha ya wachezaji wa mpira wa miguu ambao walikuwa wameshuka kiwango ikazidi kuongezeka kichwani mwake na mwisho wa siku akajikuta akiitoa namba ile na kuipotezea, kikaratasi akakiweka kabatini.
Huo ndio ulikuwa uamuzi wake wa mwisho kujiwekea katika maisha yake, hakutaka kabisa kujihusisha na wanawake kwa kuona kwamba Amanda angeweza kumfanya kushuka kiwango chake na hatimae kuzima ndoto zake za kuwa mchezaji mkubwa wa kulipwa katika moja ya klabu barani Ulaya.
“Haiwezekani. Nisije nikawa kama Ronaldinho” Filbert alijisemea.
Akaachana kabisa na suala la Amanda na kuanza kufanya mambo yake. Kila siku akawa mtu wa kuamka asubuhi na mapema na kisha kuanza kufanya mazoezi kabla ya kwenda shuleni, Mwili wake ukajengeka sana na kujiona kufaa kabisa kuchezea katika moja ya klabu kubwa hasa za watoto walio chini ya miaka kumi na saba.
Makali yake hayakupungua, kila siku yalikuwa yakizidi. Watu wa timu pinzani walikuwa wakimhofia sana Filbert, uwezo wake ulikuwa mkubwa sana kila alipokuwa akikutana na walinzi wa timu pinzani. Filbert hakuonekana kuwa mtu mwenye huruma kila alipokuwa akigusa mpira, mawazo yake katika kipindi chote kilikuwa ni kufunga magoli na kamwe hakuonekana kuridhika hata kama angefunga magoli zaidi ya kumi.
Siku ziliendelea kukatika zaidi na zaidi mpaka kufikia simu ambayo wachezaji walio chini ya umri wa miaka kumi na saba ndani ya jiji la Dar es Salaam walikuwa wakihitajika kwa ajili ya kutengeneza timu ya mkoa ambayo ingeshiriki katika mashindano ya Copa Coca Cola. Kwa sababu shule ya Makongo ndio ambayo ilipewa kibali cha kuandaa kikosi cha timu hiyo itakayowakilisha jiji la Dar es Salaam, Filbert alikuwa mtu wa kwanza kujumuishwa katika kikosi hicho.
“Kama kweli unajua kucheza mpira, hapo ndipo pa kuonyesha makali yako. Kila siku nitakuwa nakuja kuangalia mechi mnayocheza, ila lengo zaidi ni kukuangalia wewe” Mzee Martin alimwambia mtoto wake, Filbert.
“Nitacheza kwa juhudi zote baba” Filbert alimwambia baba yake.
“Nataka kila goli utakalofunga liwe zawadi kwa ajili yangu na mama yako” Mzee Martin alimwambia Filbert.
“Nitafanya hivyo baba. Ninawapenda sana, hata kama nitafanikiwa kutimiza ndoto yangu, hakika nitakuwa nikiwakumbuka sana na kuwa nanyi bega kwa bega” Filbert alimwambia baba yake.
Baada ya wiki tatu mashindano hayo yalianza rasmi. Kama alivyokuwa ameahidi mzee Martin ndivyo alivyofanya. Katika kila mechi ambayo timu ya vijana kutoka jijini Dar es Salaam ilipokuwa ikicheza amzee Martin alikuwepo uwanjani. Uwezo wa Filbert ulionekana kuwa mkubwa kupita washambuliaji wote ambao walikuwa wakicheza katika mashindano yale.
Mpaka mashindano yale yanamalizika, Filbert akawa mfungaji bora pamoja na mchezaji bora wa mashindano yale. Hiyo ikaonekana kuwa furaha ndani ya jiji la Dar es Salaam kwa kutoa timu bingwa, mchezaji bora na mfungaji bora. Sherehe ikaandaliwa ndani ya hoteli ya Kilimanjaro ambapo huko rais akaamua kujumuika nao na kisha kuwaahidi watanzania kwamba ingetafutwa timu moja ya taifa ya vijana ambayo ingejumuisha wachezaji kutoka katika timu zote zilizoshiriki na kisha kuelekea nchini Ubelgiji kwa ajili ya kufanya majaribio na timu za huko.
“Ni lazima tuwape changamoto wachezaji wetu, natumaini hii itakuwa timu bora ambayo haijawahi kutokea nchini Tanzania” Rais aliwaambia waandishi wa habari.
“Wachezaji ambao watateuliwa watapelekwa nchini Ubelgiji, majina yataandaliwa na mchakato mzima utaanza kufanyika kwa ajili ya safari hiyo” Rais aliwaambia waandishi wa habari.
Baada ya wiki moja majina ya wachezaji ambao walitakiwa kuunda timu ya taifa ya vijana ya Tanzania ikatangazwa na Filbert kuwa mmoja wa wachezaji hao. Hiyo ikaonekana kuwa furaha kwake na kwa familia kwa ujumla, hakuamini kwamba katika kipindi hicho nae alitakiwa kupanda ndege na kuelekea nchini Ubelgiji kwa ajili ya kwenda kucheza na timu za vijana za nchini humo.
“Hapo ndipo pa kujitangaza Filbert” Mzee Martin alimwambia mtoto wake, Filbert.
“Nitajitahidi baba. Nitacheza kadri niwezavyo” Filbert alimwambia baba yake.
Filbert alijiona kuwa njiani kukamilisha kile alichokuwa akikitamani siku zote katika maisha yake, kuwa mchezaji mkubwa duniani. Kila siku alikuwa mtu wa kufanya mazoezi lakini bado kulikuwa na kitu ambacho kilimsumbua sana kichwani mwake, taswira ya msichana Amanda.
Kila alipokuwa akifanya mazoezi, taswira ya msichana huyo ilikuwa ikimjia sana kichwani mwake. Hakuwa amemtafuta simu japokuwa ilikuwa imepita miezi miwili. Hakutaka kumtafuta kwa sababu moyo wake haukuwa tayari kujihusisha na msichana yeyote katika kipindi hicho mpaka pale ambapo angekuja kuwa mchezaji wa kulipwa barani Ulaya.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Amanda....subiri kwanza Amanda mpaka nikamilishe ndoto yangu” Filbert alikuwa akijisemea kila alipokuwa akiiangalia namba ya simu ya Amanda.
Hayo yalikuwa ni maamuzi binafsi ambayo alikuwa amejiwekea katika maisha yake, hakutaka kuwa na msichana yeyote pale mpaka pale ambapo angefanikiwa kuwa mchezaji wa kulipwa barani Ulaya. Maisha yaliendelea kila siku mpaka kufikia wiki moja kabla ya wachezaji kuanza safari ya kuelekea nchini Ubelgiji.
Filbert alikuwa na imani kubwa moyoni mwake kwamba asingeweza kurudi nchini Tanzania pamoja na wachezaji wenzake, aliamini kwamba kwa jinsi uwezo wake ulivyokuwa mkubwa basi ilikuwa ni lazima kuchukuliwa na timu yoyote ile nchini Ubelgiji. Kila siku alikuwa akiliamini jambo hilo kitu ambacho kilimpelekea kuwa na uhitaji wa kuwasiliana na Amanda hata kabla hajaondoka kuelekea Ubelgiji.
*****
Amanda alionekana kuwa mwenye furaha katika kipindi chote hasa mara baada ya kumpa namba ya simu Filbert. Kila siku uso wake ulikuwa na tabasamu pana kwa kuamini kwamba Filbert angeweza kumpigia simu siku yoyote ile kuanzia siku ile ambayo alimkabidhi namba yake ya simu. Kila siku Amanda alikuwa makini na simu yake, kila alipokuwa akiiona namba ngeni ikiingia simuni mwake alikuwa akiipokea kwa mapozi yote lakini mpigaji wala hakuwa Filbert.
Zoezi lake la kupokea namba ngeni kwa furaha liliendelea kwa takribani wiki mbili lakini hakukuwa na mafanikio yoyote yale, Filbert hakuweza kumpigia simu. Hilo likaonekana kuwa pigo kubwa moyoni mwa Amanda, moyo wake ukaanza kusononeka sana kwa kujiona kutokuthaminiwa na kusikilizwa. Kitendo kile cha kutokupigiwa simu ndicho ambacho kilimpelekea mara kwa mara kusimama mbele ya kioo na kisha kuanza kujiangalia.
Kila siku alikuwa akiitwa msichana mrembo, alikuwaje mrembo na wakati mvulana ambaye alikuwa amempa namba yake ya simu hakuwa amemtafuta kama alivyotaka? Angejiita vipi mrembo na wakati mvulana ambaye alikuwa ametokea kumpenda hakuwa ameonyesha nia ya kuwa nae kama alivyokuwa ameionyesha yake?
Amanda akaumia kupita kawaida, upweke ukaanza kumuingia moyoni mwake, hakujiona kuwa na thamani, japokuwa alikuwa mrembo lakini katika kipindi hicho akaanza kuupuzia urembo wake. Kitendo cha Filbert kutokumpigia simu kilikuwa kimemnyong’onyeza kupita kawaida. Amanda hakujua afanye nini, kwenda shuleni Makongo hakuweza kwa sababu kila siku shuleni alikuwa akipelekwa na gari la baba yake na kurudishwa na gari huku kila alipokuwa akiingia nyumbani hakuwa akitoka.
“Filbert....Filbert mbona unanifanyia hivi?” Amanda aliuliza huku akilengwa na machozi. Mbele yake aliiona taswira ya Filbert, kila slichokuwa akikiongea aliamini kwamba Filbert alikuwa akimsikia.
Siku zikaendelea kukatika kama kawaida, namba ya Filbert haikuingia ndani ya simu yake. Mwezi wa kwanza ukakatika na mwezi wa pili kuingia. Hapo ndipo ambapo aliliona tangazo kwenye gazeti kwamba mashindano ya Copa Coca Cola yalitarajiwa kufanyika ndani ya jiji la Dar es Salaam na hivyo jiji la Dar es Salaam kutoa kikosi chao.
Hakujua ni kwa nini alivutiwa na kuliangalia tangazo hilo. Japokuwa hakuwa mfuatiliaji wa mpira kwa sana lakini akajikuta akianza kuliangalia tangazo lile, alipofika katika vikosi vya wachezaji ambao wangeliwakilisha jiji la Dar es Salaam, akapigwa na mshtuko mara baada ya kuliona jina la mtu ambaye alikuwa akimpenda sana, Filber.
“Filbert mpenzi wangu....” Amanda alijikuta akiita huku akilitolea macho jina la Filbert ambalo lilikuwa katika gazeti lile.
Amanda akaonekana kupewa kazi ya kuanza kufuatilia mashindano ya Copa Coca Cola ambayo yalitarajiwa kuanza baada ya wiki moja. Toka siku ya kwanza mashindano yalianza rasmi, Amanda alikuwa akikaa kitandani kwake chumbani na kisha kuanza kuangalia mpira. Hakupenda mpira na lengo lake halikuwa ni kuangalia mpira bali alikuwa akitaka kumuona mvulana ambaye alikuwa akimpenda kwa moyo wake wote.
Kitendo cha kumuona Filbert kwenye luninga akicheza mpira kilimfariji sana, moyoni mwake alikuwa akijisikia amani kupita kawaida, hakuamini kwamba mwisho wa siku alikuwa amemuona mwanaume ambaye alikuwa akimpenda kwa moyo wake wote.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Filbert....Filbert kipenzi naomba unipigie simu mpenzi. Ninaumia moyoni, unaniumiza moyoni kipenzi” Amanda aliita kila alipokuwa akimuona Filbert kwa karibu.
Maisha ndivyo yalivyokuwa. Kila siku Amanda alikuwa mtu wa mawazo tu, alimfikiria sana Filbert kiasi ambacho wakati mwingine alijiona akianza kukonda. Moyo wake ulikuwa katika mapenzi juu ya Filbert kwa asilimia moa moja, hakumtaka mwanaume mwingine, kwake, Filbert alionekana kuwa namba moja ambaye wala hakuwa na mpinzani yeyote.
Siku ziliendelea kukatika na mashindano yake kumalizika. Zawadi alizozipokea Filbert zilimfurahisha sana Amanda kwa kuona kwamba hatimae mpenzi wake alikuwa amejinyakulia sifa kubwa nchini Tanzania. Moyo haukupoa, tena katika kipindi hicho ndio uliumia zaidi kwa sababu mashindano ya Copa Coca Cola yalikuwa yamemalizika na hivyo asingeweza kumuona tena Filbert.
Kama kuumia alikuwa ameumia sana moyoni mwake na kama kuwa na mawazo alikuwa nayo mengi sana juu ya Filbert lakini hali haikuonekana kubadilika kabisa, bado Filbert hakuwa amepiga simu jambo ambalo lilikuwa likimuumiza sana Amanda. Siku zikaendelea kukatika mpaka kufikia siku ambayo Amanda aliisikia simu yake ikianza kuita, alipoichukua na kisha kuangalia kioo cha simu yake, ilikuwa namba ngeni.
Kwanza akaonekana kukasirika kupita kawaida. Katika kipindi hicho ambacho alikuwa amechoka hakutaka kupokea simu ya mtu yeyote yule, kitendo cha kusumbuliwa na mtu ambaye namba yake haikuwa ndani ya simu yake kilionekana kumkasirisha kupita kawaida. Alichokifanya ni kubonyeza kitufe cha kijani na kisha kuanza kuita huku sauti ikisikika kuwa na uchovu.
“Hallow” Amanda aliita mara baada ya kupokea simu ile.
“Hallow! Habari yako Amanda” Sauti ya upande wa pili ilisikika.
“Salama. Naongea na nani?” Ambanda aliitikia na kuuliza swali.
“Unahisi unaongea na nani?” Sauti ya upande wa pili iliuliza.
“Kuna wengi wananipigia siwezi kufahamu naongea na nani” Amanda alijibu.
“Unaongea na Martin”
“Martin! Martin ndiye nani?”
“Filbert Martin” Sauti ya upande wa pili ilisikika.
Amanda akauhisi moyo wake ukipiga kwa mshtuko mkubwa, hakuamini kile ambacho alikuwa amekisikia simu mwake. Mara baada ya kukaa kwa muda wa miezi mitatu kwa maumivu makali na majonzi yasiyokwisha moyoni leo hii alikuwa akiisikia sauti ya mtu ambaye aliamini kwamba alikuwa ndiye furaha yake na tumaini lake. Moyo wake ulioshtuka ukaanza kuingiwa na furaha kubwa moyoni mwake, hakuamini kwamba mwisho wa siku mtu ambaye alikuwa akitaka kuisikia sauti yake ndiye ambaye alikuwa amempigia simu.
“Filbert....!! Filbert ni wewe?” Amanda aliita na kuuliza, tayari macho yake yakaanza kulengwa na machozi, furaha ikaonekana kumzidi uzito.
“Ni mimi....”
“Siamini”
“Huamini nini?”
“Miezi mitatu imepita, kwa nini haukunipigia simu jamani?” Amanda alimuuliza Filbert.
“Nilikuwa bize Amanda”
“Bize kiasi ambacho ulishindwa hata kuniandikia meseji?”
“Naomba unisamehe”
“Umeniumiza sana Filbert, nimekaa nikikufikiria wewe kila siku. Kwa nini umekuwa ukinifanyia hivi jamani?” Amanda aliuliza, machozi yakaanza kutiririka mashavuni mwake.
“Naomba unisamehe” Filebrt alisikika simuni.
“Usijali. Nimekusamehe” Amanda alimwambia Filbert.
“Asante sana. Ninatarajia kusaifiri wiki ijayo ila kabla sijasafiri ningependa kuonana nawe” Filbert alimwambia Amanda.
”Hakuna tatizo. Tuonane wapi na lini?”
“Nataka tuonane popote utakapo na muda wowote utakao” Filbert alimwambia Amanda.
“Tuonane kesho saa tisa alasiri” Amanda alimwambia Filbert.
“Hakuna tatizo. Utaweza kutoka nyumbani kwenu?”
“Kwa ajili yako tu nitaweza” Amanda alimwambia Filbert.
“Sawa. Tuonane sehemu gani sasa?”
“Nitakwambia” Amanda alimjibu Filbert.
Siku hiyo ikaonekana kuwa siku ya furaha kuliko siku zote katika maisha yake. Amanda hakuamini kama alikuwa ameongea na mtu ambaye alikuwa akimpenda sana, Filbert. Siku hiyo hakutaka kulala mapema, kitu ambacho alikifanya ni kuanza kuchati na Filbert tu. Tayari namba alikuwa nayo kwa wakati huo, tena hakuonekana kuridhika, kila alipokuwa akiiangalia alijiona kama angeweza kuipoteza, alichokifanya ni kuihifadhi katika kitabu chake cha kumbukumbu, kwenye kompyuta yake, akaiandika ndani ya kabati lake, akaandika kwenye email na kisha kujitumia, kwa kifupi ni kwamba hakutaka kuipoteza kabisa.
Siku iliyofuatiwa ambayo walitakiwa kuonana, Amanda hakusoma kwa raha darasani, kila wakati alikuwa na mawazo juu ya Filbert tu. Masaa kwake yalionekana kutokwenda kabisa, kila wakati alikuwa akimfikiria Filbert tu. Kila mwalimu ambaye alikuwa akiingia darasani alionekana kutumia muda mwingi kufundisha, kitu ambacho alikuwa akikitaka ni kuona akiondoka shuleni na kwenda kuonana na mtu ambaye alikuwa akitamani sana awe mpenzi wake, Filbert.
Dakika ziliendelea kwenda mbele, kila wakati macho yake yalikuwa katika saa yake ya mkononi, siku hiyo mshale wa dakika ulionekana ukisogea taratibu sana, alitamani kuushika na kuupeleka haraka haraka ili masaa yakatike na hatimae kuweza kutoka darasani na kwenda kuonana na Filbert. Dakika zikasonga zaidi na zaidi, vipindi vilipokwisha, akachukua simu yake na kisha kuanza kumpigia baba yake ambaye alikuwa na kawaida ya kumpigia dereva kwa ajili ya kwenda kumchukua Amanda shuleni.
“Leo tutatoka saa kumi na mbili” Amanda alimwambia baba yake.
“Kuna nini tena?” Sauti ya mzee Frank ilisikika simuni.
“Kuna kazi tumepewa tuifanye kama kundi kwa sababu mitihani inakaribia” Amanda alidanganya.
“Sawa. Kwa hiyo nimwambie aje saa ngapi?”
“Saa kumi na mbili”CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Sawa binti yangu. Soma sana utafanikiwa tu”
“Usijali baba. Nakupenda”
“Nakupenda pia”
Hapo Amanda akawa na furaha, kitendo cha kumdanganya baba yake kwamba alitakiwa kufanya kazi pamoja na kundi mpaka saa kumi na mbili kilionekana kumfurahisha kwa kuona kwamba siku hiyo angekaa na Filbert kwa muda mrefu na kuongea bila kusahau kumwambia kile alichokuwa akijisikia juu yake.
“Kwa hiyo tuonane wapi?” Sauti ya Filbert ilisikika simuni.
“Mlimani City kwenye ukumbi wa Cinema” Amanda alijibu.
“Kwa nini iwe huko?”
“Nina nguo za shule Filbert”
“Sawa. Hakuna tatizo” Filbert alimjibu Amanda na kisha kukata simu.
“Oooopppsss...!!” Amanda alishusha pumzi ndefu.
Saa nane na nusu kengele ya kuondoka nyumbani ikagongwa na wanafunzi kutoka na moja kwa moja kuanza kwenda kwenye mabasi kwa ajili ya kupelekwa nyumbani. Amanda hakutaka kutoka darasani, alibaki darasani huku akitaka wanafunzi wapungue na kisha yeye kutoka na kuelekea katika jengo la Mlimani City.
Wanafunzi walipopungua vya kutosha, Amanda akatoka darasani na kisha kuanza kuelekea nje ya shule. Moja kwa moja akaisimamisha bajaji ambayo ilikuwa ikipita mahali hapo na kumtaka dereva kumfikisha Mlimani City.
“Elfu tano” Dereva alimwambia Amanda.
“Usijali. Wewe twende tu” Amanda alimwambia dereva.
Safari ya kuelekea Mlimani City ikaanza, muda wote Amanda alikuwa akimfikiria Filbert. Hakuamini kama siku hiyo alikuwa akienda kuonana na mwanaume ambaye alikuwa akitamani sana japo kukaa nae kwa dakika kadhaa, Filbert. Kama kummisi moyoni mwake alikuwa amemmisi vya kutosha na katika kipindi hicho alikuwa akitaka kumwambia ukweli kuhusiana na hali iliyokuwepo moyoni mwake.
Mapenzi yalikuwa yamemlevya, alijihisi kuwa tofauti sana moyoni mwake, Filbert alionekana kuwa mwanaume maalumu ambaye aliletwa katika maisha yake na kuwa nae katika kipindi chote. Mzigo mzito wa mapenzi juu ya Filbert ulikuwa umemuelemea na alimhitaji mtu huyo kwa ajili ya kuushusha mzigo huo mzito.
Mara baada ya kufika karibu na eneo la jengp la Mlimani City, Amanda akateremka, akamlipa dereva kiasi cha fedha alichokuwa akikihitaji na kisha kuanza kuelekea ndani ya eneo la jengo hilo. Muda wote Amanda alionekana kuwa na furaha, kitendo cha kutaka kuonana na Filbert siku hiyo kilionekana kumuwekea furaha moyoni mwake, furaha ambayo hakuwahi kuwa nayo kabla.
Alichokifanya ni kuelekea katika sehemu ya kukata tiketi na kisha kukata tiketi za watu wawili kwa ajili ya kuangalia filamu mpya ambayo ilikuwa imetoka katika kipindi hicho, MY LATE MOM iliyokuwa imeigizwa na muigiza Matt Damon. Hakuishia hapo, alipokata tiketi zile, akanunua na bisi kwa ajili ya kula ndani ya ukumbi huo wakati wanatazama filamu.
“Upo wapi?” Amanda alimuuliza Filbert katika kipindi ambacho aliamua kumpigia simu kwa kuwa aliona muda ukienda bila kuonekana mahali hapo.
“Ndio nimeshuka kutoka katika daradala katika kituo cha Remmy, hapa ninatembea kuja huko” Filbert alimwambia Amanda.
“Sawa. Wahi, filamu ishaanza”
“Kuna filamu gani hapo?”
“My Late Mom”
“Mmmh! Hiyo sijawahi kuiona. Ina ngumi?”
“Sidhani. Ni kama filamu fulani ambayo inahusu sana maisha” Amanda alimjibu Filbert.
“Sawa nakuja. Ila ingekuwa in ina ngumi ingekuwa raha sana”
“Usijali, siku nyingine tutakuja kuangalia filamu ya ngumi” Amanda alimwambia Filbert na baada ya maongezi ya hapa na pale kukata simu.
Wakati huo Filbert alionekana kuwa kila kitu moyoni mwake, kitendo cha kuisikia sauti yake tu kiliuridhisha moyo wake. Amanda akaanza kuelekea katika sehemu iliyokuwa na mabenchi ya kisasa na kisha kukaa huku akimsubiria Filbert. Wala haukupita muda mrefu, Filbert akafika mahali hapo, kitu cha kwanza walichokifanya ni kukumbatiana japokuwa kwa Filbert alionekana kujishtukia.
“Unanukia vizuri” Filbert alimwambia Amanda.
“Asante Filbert. Umependeza”
“Hahaha! Acha kunitania. Yaani kuvaa jezi ya Arsenal ndio nimependeza?”
“Kweli tena. Halafu umebadilika sana”
“Nimekuwaje?”
“Mzuri. Mzuri zaidi ya kipindi cha nyuma” Amanda alimwambia Filbert ambaye hakuongea kitu chochote zaidi ya kubaki kimya.
Wakaanza kupiga hatua kuelekea katika mlango wa kuingia ndani ya jumba la Cinema na kisha kutulia katika sehemu moja mpaka pale ambapo filamu hiyo ilipoanza kuonyeshwa. Katika kipindi chote cha kuangalia filamu hiyo, mawazo ya Amanda yalikuwa kwa Filbert tu, alikuwa akijifikiria ni kitu gani ambacho alitakiwa kuongea mahali hapo. Mtu ambaye alikuwa amemsubiria kwa kipindi kirefu tayari alikuwa amefika na kuwa karibu nae na ni yeye tu ndiye ambaye alikuwa akisubiriwa kuongea kile ambacho kilikuwa kikimsumbua moyo wake katika kipindi kirefu.
“Sina hamu ya kuangalia filamu” Amanda alimwambia Filbert, filamu ndio kwanza ilikuwa imefika katikati.
“Kwa nini? Mbona ni filamu nzuri tu?”
“Natamani sana kuongea na wewe” Amanda alimwambia Filbert.
“Ok! Hakuna tatizo”
“Uliniambia kwamba unataka kusafiri, unataka kwenda wapi?” Amanda alimuuliza Filbert.
“Nataka kwenda Ubelgiji”
“Ubelgiji?”CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Ndio”
“Kufanya nini?”
“Kucheza soka” Filbert alimwambia Amanda.
“Na utarudi lini?”
“Sijajua”
“Mmmh!”
“Nini tena Amanda”
“Umepata timu huko au kuna ndugu yako?” Amanda alimuuliza Filbert.
“Sina ndugu Ulaya”
“Sasa nani atakupokea?”
“Nitakwenda na timu ya taifa ya vijana wa Copa Coca Cola” Filbert alimwambia Amanda.
“Ndio ile aliyoizungumzia rais?”
“Ndio hiyo hiyo”
“Sasa si wiki mbili tu jamani, au unataka kuzamia?”
“Hapana. Ninaishi katika imani” Filbert alimwambia Amanda.
“Kivipi?”
“Kwamba nitapata timu”
Amanda akanyamaza, maneno aliyoyaongea Filbert yalionekana kuwa mazuri kwa kila mtu ambaye angeyasikia lakini kwa Amanda yalionekana kuwa kama mwiba mkali moyoni mwake. Alikuwa akimpenda sana Filbert, hakutaka mwanaume huyo aondoke mikononi mwake, alikuwa akihitaji kuwa nae zaidi na zaidi na ikiwezekana hata kufunga ndoa kanisani na kuwa mume na mke.
“Kwa hiyo ukipata timu ndio hatutoonana tena?” Amanda alimuuliza Filbert huku akionekana kuwa mpole.
“Tutaonana. Kutakuwa na vile vipindi ambavyo msimu wa mechi unakwisha, nitakuwa nakuja na kuonana nawe Amanda” Filbert alimwambia Amanda.
“Sawa” Amanda aliitikia kinyonge.
Tayari furaha aliyokuwa nayo kipindi kifupi cha nyuma ikayeyuka moyoni mwake, alikwishajua kwamba hicho ndicho kilikuwa kipindi cha mwisho mwisho kuonana na Filbert na hivyo hakutakiwa kuifanyia mzaha kila nafasi ambayo alikuwa ameipata. Bila kutarajia na bila uoga wowote ule Amanda akaanza kumshikashika upaja Filbert hali ambayo ikamfanya kushtuka.
“Vipi tena Amanda?” Filbert aliuliza huku akionekana kushtuka, akautoa mkono wa Amanda pajani kwake.
“Ninakupenda Filbert” Amanda alimwambia Filbert.
“Unanipenda? Nashukuru Amanda” Filbert alimwambia Amanda.
“Filbert naomba uwe mpenzi wangu” Amanda alimwambia Filbert kwa sauti ya chini.
“Amanda! Upo sawa kweli?” Filbert alimuuliza Amanda, yaani alijifanya kama kushtukizwa na wakati alikuwa akifahamu kila kitu ambacho kingeweza kutokea au kuambiwa na Amanda.
“Nipo sawa Filbert. Ninakupenda sana na ninataka uwe mpenzi wangu” Amanda alimwambia Filbert kwa sauti ya chini iliyojaa mahaba.
“Hapana Amanda. Hivi unajua kwamba mimi ni mcheza soka?” Filbert alimuuliza Amanda.
“Najua”
“Unajua matatizo wanayokutana nayo wanasoka mara wanapokuwa na wanawake?” Filbert alimuuliza Amanda.
“Hapana”
“Mwanasoka unapokuwa na mwanamke, kwanza uwezo wako uwanjani unashuka sana, magoti yatakuwa yakilegea sana” Filbert alimwambia Amanda.
“Kwa hiyo mchezaji wa mpira hatakiwi kuwa na mwanamke?” Amanda alimuuliza Filbert.
“Hiyo ndio maana yangu”
“Mbona huko Ulaya wanaoa sasa?”
“Wale wamekuwa professional Amanda ila si kwa mtu kama mimi ninayechipukia” Filbert alimwambia Amanda.
“Nimekuelewa. Nikuulize swali?”
“Uliza tu”
“Unanipenda?”
“Unamaanisha nini?”
“Hivyo hivyo ulivyofikiria kichwani mwako. Unanipenda?”
“Amanda....Amanda mbona unakuwa na haraka hivyo?”
“Lazima niwe na haraka Filbert. Unaondoka kuelekea Ubelgiji na umesema kurudi huku mpaka msimu uishe, hauoni kwamba hii ndio nafasi yangu ya kukwambia kila kitu ninachojisikia kukwambia kuhusiana na mapenzi?” Amanda alimwambia Filbert.
“Najua Amanda. Najua huu ni wakati wako”
“Basi naomba uniambie”
“Ila naona kama bado mapema sana”
“Kivipi?”
“Tuna nafasi ya kuendelea kuwa marafiki wa kawaida kabla ya kuingia katika mahusiano ya kimapenzi” Filbert alimwambia Amanda.
“Tatizo lipo pale pale Fulbert. Unaondoka wewe na hautegemei kurudi karibuni, hivi unadhani utaniacha katika hali gani?” Amanda alimuuliza Filbert, wakati huo wote wawili walikuwa wakiongea kama watu wazima.
“Amanda....!!”
“Unataka kwenda kuoa mzungu?”
“Hapana”
“Labda ndicho unachokitaka na ndio maana unakataa kuwa nami Filbert” Amanda alimwambia Filbert, katika kipindi hicho alikuwa amekwishabadilika, macho yake yalikuwa yamekwishaanza kulengwa na machozi.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Umenielewa vibaya Amanda”
“Nakuomba uwe mpenzi wangu Filbert”
“Amanda....mbona unakuwa na haraka”
“Nilikwishakwambia sababu zinazonifanya kuwa na haraka. Kwanza naomba unijibu swali langu, unanipenda?” Amanda alimuuliza Filbert.
“Ooopppsss...!! Unaonekana kutokunielewa Amanda” Filbert alimwambia Amanda.
“Naomba unijibu kwanza”
“Nilikwishakujibu kabla”
“Hapana, haukunijibu na hata kama ulinijibu sikusikia. Unanipenda?” Amanda alimwambia Filbert na kumuuliza.
“Ninakupenda”
“Asante. Naomba uwe mpenzi wangu”
“Utavumilia?”
“Kuvumilia nini?”
“Nitakuwa mbali na Afrika. Utavumilia kuwa peke yako mpaka nitakaporudi?” Filbert alimuuliza Amanda.
“Kama utachaguliwa na timu yoyote ile nitavumilia. Ukichelewa nitakuja huko huko Ubelgiji” Amanda alimwambia Filbert.
“Kuja kufanya nini?”
“Kukuona mpenzi wangu na pia kusoma chuo”
“Mmmh! Aya”
“Umemaanisha nini kusema aya?”
“Nimeridhika na maneno yako”
“Kwa hiyo umekubaliana nami?”
“Sina jinsi. Kama umeridhika, nimekubaliana nawe Amanda”
“Kwa hiyo leo hii ndio tumeufungua ukurasa wa kimapenzi pamoja?”
“Bila shaka”
Hiyo ikaonekana kuwa nafuu kwa Amanda, akashusha pumzi ndefu, hakuamini kwamba kile ambacho alikuwa akikitamani kwa muda mrefu leo hiyo ndio kilikuwa kimetimia. Kuanza mahusiano na Filbert kilikuwa ni kitu ambacho kilimfanya kuwa na furaha sana, bila kuogopa macho ya watu ambao walikuwa bize wakiangalia filamu, Amanda akambusu Filbert mdomoni.
Huo ndio ukawa mwanzo wa mahusiano yao ya kimapenzi, huo ndio ukawa mwanzo wa mahusiano ambayo yalikuwa yenye kuumiza na kukera, yalikuwa ni mahusiano ambayo yalikuwa ni mwanzo wa moja ya filamu ya ngono ambayo ilirekodiwa na kutaka kusambazwa Tanzania nzima ili watu waone uchafu wa mtu ambaye alikuwa akiaminika na kukubalika sana nchini Tanzania. Yalikuwa ni mahusiano ambayo yalisababisha mambo mengi yenye kutisha. Hawakuonekana kujali, katika kipindi hicho kitu ambacho walikuwa wakikijali ni kuwa katika mahusiano ya kimapenzi tu, hawakujua kabisa kuhusiana na skendo ya video ya ngono ambayo ingeweza kurekodiwa kutokana na mahusiano hayo kuanzishwa siku hiyo ndani ya ukumbi huo wa Cinema ndani ya jengo la Mlimani City.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Je nini kitaendelea?
Je mahusiano hayo yataweza kudumu?
Je mahusiano haya yalisababishaje hii skendo ya filamu ya ngono?
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment