IMEANDIKWA NA : INNOCENT A. NDAYANSE (ZAGALLO)
*********************************************************************************
Sehemu Ya Kwanza (1)
NI katikati ya jiji la Dar es Salaam. Hii ilikuwa ni saa 11 jioni. Barabara ya Maktaba ilikuwa imefurika magari. Upande mmoja wa barabara hiyo ulikuwa na foleni kubwa ya magari yaliyokuwa yakitoka eneo la Posta Mpya yakielekea katika vitongoji vingine vya jiji la Dar es Salaam hususan Kinondoni, Masaki, Oysterbay, Mwenge, Kawe, Tegeta hata Bunju.
Sarah alikuwa ndani ya gari, akiwa ni miongoni mwa walioiunda foleni hiyo. Akiwa ndiyo kwanza ametoka katika duka maarufu la Imalaseko alikofuata mahitaji yake, Sarah, mwanamke mrembo, mwenye umbo zuri na sura inayovutia aliingia ndani ya gari lake na kuondoka. Dakika kadhaa baadaye alikuwa Barabara ya Azikiwe halafu Barabara ya Maktaba.
Ni wakati alipoingia katika barabara hiyo ndipo kero ya foleni ilipoanza. Magari yakawa yakisogea kwa mwendo wa kusuasua. Wakati huo Sarah alikuwa akiangaza macho huku na kule. Kulia kwake akashuhudia majengo yaliyokamilika na ambayo bado ujenzi wake ulikuwa ukiendelea.
Jengo moja, KAZI HOUSE ndilo lililokuwa limekamilika na lilionyesha kupendezesha zaidi eneo hilo. Hakujua majengo hayo yalimilikwa na nani au na kampuni gani, na wala hakuwa na haja ya kujua.
Foleni ikaendelea kusogea kwa mwendo wake wa kusuasua. Labda angeendelea kuangalia huku kisha kule, kama macho yake yasingegota kwa mtu mmoja mara tu foleni iliposimama tena, gari lake likiwa hatua chache kutoka kwenye taa za Usalama Barabarani.
Mtu huyo alikuwa ni mwanamume, akiwa amesimama kando ya jengo la CMC. Alionekana kama anayemsubiri mtu. Hakuwa na taswira ya mtu wa 'njaa-njaa.' Utanashati wake ulimweka katika daraja la watu wanaostahili kuchukuliwa kuwa wao walikwishaistaafisha dhiki maishani mwao.
“Ni mwenyewe,” Sarah alijikuta akinong'ona, macho yake yaliyorembuka yakiendelea kumtazama mtu huyo.
Mara wazo likamjia, wazo aliloamua kulifanyia utekelezaji wa haraka. Alibonyeza kitufe fulani mara vioo vya gari vikashuka. Papo hapo akapiga honi kali mara mbili.Yule mwanamume aliyesimama kando ya barabara akayapeleka macho kwenye gari hilo.
Naye Sarah hakuchelewa, alishahisi taa ya kijani ingewaka muda ufupi ujao na hivyo kumshinikiza aliondoe gari hilo kabla hajaonana na mtu huyo. Haraka akamwita kwa ishara ya mkono.
Mtu yule akashangaa na kuvuta hatua akifuata gari hilo.
“Hee! Sarah!” alibwata kwa sauti ya chini, macho yake yakionyesha bayana mshangao uliomkumba.
Sarah hakutamka chochote. Alibonyeza kitufe kingine, mara milango ikafunguka. Mwanamume huyo akaingia katika mlango wa mbele.
Taa ya kijani ikawaka. Gari la Sarah na magari mengine yakasaga lami. Wakashika Barabara ya Bibi Titi Mohammed kisha Barabara ya Ali Hassan Mwinyi, Sarah akionyesha jinsi alivyomudu kukiongoza chombo hicho cha moto.
“Kasha, za siku?” hatimaye Sarah aliuvunja ukimya wakati walipokuwa wakivuka jirani na Nyumba ya Sanaa.
“Siyo mbaya sana,” mwanamume huyo alijibu kwa sauti ya chini, sauti nzito, yenye kijimkwaruzo cha mbali, macho yake yakimwangalia Sarah kipembepembe. Akaongeza, “Vipi, we' mwenzangu, naona mambo yako ni supa siku hizi.”
Sarah aliguna. Kisha akasema, “Ni hadithi ndefu.” Akasita kidogo na kama aliyezinduliwa, akahoji, “Pale ulikuwa unamsubiri nani?”
“Nimsubiri nani Sarah? Nilikuwa nashangaa-shangaa tu katika kuvuta muda.”
“Ok, unaonaje, twende kwangu tukazungumze vizuri?”
“Kwako?”
“Nd'o maana'ake. Ni huko nitakapokupa hadithi yote kwa kina, na wewe unipe hadithi yako; sawa?”
“Poa. Mradi tu unihakikishie usalama wangu.”
“Usihofu, hakuna tatizo lolote.”
**********
KASHA halikuwa jina geni vichwani mwa maofisa wa Jeshi la Polisi. Isitoshe, sura yake haikuwa ngeni machoni mwa wanausalama hao ambao mara kadhaa kwa miaka kadha wa kadha walikuwa wakisumbuana naye.
Ndiyo, lilikuwa ni jina maarufu, jina ambalo pia lilizoeleka kwa wasomaji wa magazeti, watazamaji wa televisheni na wasikilizaji redio. Hawakuwa hao pekee, bali pia hata matajiri kadhaa wa Jiji la Dar es Salaam, matajiri ambao tayari baadhi yao walishapoteza roho zao pale walipojaribu kumdhibiti asitekeleze maazimio yake, nao walimtambua vizuri.
Miaka kadhaa iliyopita, Kasha alifanikiwa kujipatia donge nono, fedha taslimu shilingi milioni 20 kutoka kwa tajiri mmoja mwenye asili ya Kiasia katikati ya jiji na kuondoka baada ya kumtoa roho tajiri huyo kwa kumzamishia risasi tatu kifuani.
Pesa zile zilikuwa ni pato kubwa kwake, pato ambalo hakuwahi kulipata tangu alipoamua kutumia mfumo huo wa maisha katika kujipatia pesa. Hivyo, kwa kiasi fulani alijiona kishajitenga na kundi la 'wenye njaa.' Akawa ni mtu wa matumizi makubwa ya starehe. Wanawake na bia wakawa ni wapenzi wake wakuu.
Hatimaye, alipobaini kuwa akiba hiyo ilizidi kuporomoka, akaamua kumtafuta mtu wa kutulia naye. Ndipo akamsaka mwanamke mrembo, mwanamke ambaye atawakosha watu kwa sura, umbo, vaa yake na tembea yake. Na alimpata.
Mrembo huyo aliitwa Sarah. Kutokana na hali njema ya kiuchumi aliyokuwa nayo Shaka, hakupata kipingamizi pale alipomshawishi mtoto huyo wa kike kwenda naye gesti ambako waliupitisha usiku bila ya kuambua lepe la usingizi.
Ni usiku huo uliozaa uhusiano wao. Sasa ikawa ni kawaida kwao kukutana kila baada ya siku mbili, tatu na kuistarehesha miili yao kadri walivyotaka.
Naam, penzi lao likamea huku Sarah akitambua fika kuwa Kasha alikuwa akipata pesa kwa njia za haramu, njia za kutisha na za hatari. Ndiyo, alitambua hivyo, lakini hakujali; alichojali ni huduma bora, hususan pesa.
Hivyo hata kama hakuonana na Kasha kwa wiki nzima, na ikatokea wakaonana, na Kasha akampatia pesa nzuri, hicho kilikuwa ni kigezo cha kumfanya Sarah amchukulie kuwa ni mwanamume zaidi ya wanaume.
Lakini, siku moja Kasha akiwa huko 'kazini' kwake, usiku saa 7 hivi, mambo yalitibuka. Walinzi wa tajiri mmoja wa Mtaa wa Nkurumah katikati ya jiji, hawakuwa usingizini. Walimwona Kasha na wenzake wawili wakiwafuata huku kila mmoja akiwa na bunduki. Walinzi wakawa makini, wakajiandaa kikamilifu.
Dakika chache baadaye patashika ikaibuka! Lakini wale walinzi walikuwa na maarifa zaidi, wakazitumia silaha zao kwa ufundi mkubwa na kufanikiwa kuokoa maisha yao, mali na maisha ya bosi wao.
Kwa upande wa pili, ni Kasha peke yake aliyenusurika huku wenzake wakilala kando ya jengo hilo, maiti.
Lilikuwa ni pigo zito kwa Kasha, pigo lililomfanya ajikute akichukua wiki mbili bila ya kufanya chochote cha kumwingizia pesa. Akiba pekee iliyosalia zilikuwa ni shilingi laki tatu tu! Alipozilinganisha pesa hizo na zile milioni 20 alizozipata awali, alijiona kama vile hana kitu.
Hatimaye asubuhi moja akashtuka alipoamka na kujikuta ana shilingi 30,000 tu. “Elfu thelathini!” alinong'ona kwa fadhaa. Lakini akajipa matumaini. Aliikumbuka bastola yake yenye risasi tatu, silaha aliyoamini kuwa ingeweza kumtatulia matatizo yote yatokanayo na ukosefu wa pesa.
Hivyo, akaamua kufanya kazi usiku wa siku hiyo. Naam, saa 5 usiku alitoka nyumbani kwake, Sinza akapitia mtaa huu hadi ule hatimaye akatokea sehemu iliyokuwa na baa iliyokuwa mafichoni kidogo. Kulikuwa na wateja wachache, wasiozidi kumi, hali aliyotarajia kuikuta.
Alitulia kwa mbali kidogo akiyasoma mazingira kisha taratibu akalisogelea eneo hilo. Kisha: “Wote laleni chini!” aliamuru kwa sauti kali.
**** **** **** **** ****
HATIMAYE asubuhi moja akashtuka alipoamka na kujikuta ana shingi 30,000 tu.
“Elfu thelathini!” alinong'ona kwa fadhaa. Lakini akajipa matumaini. Aliikumbuka bastola yake yenye risasi tatu, silaha aliyoamini kuwa ingeweza kumtatulia matatizo yote yatokanayo na ukosefu wa pesa.
Hivyo, akaamua kufanya kazi usiku wa siku hiyo. Naam, saa 5 usiku alitoka nyumbani kwake, Sinza akapitia mtaa huu hadi ule hatimaye akatokea sehemu iliyokuwa na baa iliyokuwa mafichoni kidogo. Kulikuwa na wateja wachache, wasiozidi kumi, hali aliyotegemea kuikuta.
Alitulia kwa mbali kidogo akiyasoma mazingira kisha taratibu akalisogelea eneo hilo. Kisha: “Wote laleni chini!” aliamuru kwa sauti kali.
Kilichofuata ni risasi moja aliyofyatua na kuisambaratisha globu moja. Lilikuwa ni tukio lililowaogofya wateja wote ambao asilimia kubwa yao walikuwa ni wenye umri usiopungua miaka 50.
Wote walitii amri hiyo. Kasha akawa makini, akimchunguza kila mmoja. Alihofia isije ikawa kuna mmojawao ni askari na ana bastola, akatumia ujanja na wepesi wa aina yake kujibu mapigo.
“Atakayejitia kutikisika tu, namlisha ya kichwa!” alifoka.
Wakafyata.
Ni hapo alipoamua kumpitia mmoja, mmoja kwa kasi ya ajabu, akiwapekua mifukoni, na kwa wanawake, mikoba yao ikivurugwavurugwa hadi alipohitimisha zoezi lake.
Haikuwa kazi ya bure! Alikusanya simu kumi na pesa lukuki. Kisha akatoka taratibu akiwaacha wateja hao wamelala vilevile, kifudifudi, roho zikikaribia kuwatoka, wasijue kuwa mbaya wao kishatokomea.
Nusu saa baadaye alikuwa akichekelea.Tayari alishajua kuwa kafanya kazi ya maana. Ilikuwa ni baada ya kupita ujia mmoja hadi mwingine hadi alipotokeza Barabara ya Shekilango, jirani na Baa ya Afrika Sana.
Hapo alikodi teksi iliyompeleka umbali wa mita 500 tu na kuiacha, hadhari ya kutogundulika kapita wapi na wapi akiwa ameipa kipaumbele.
Kutoka hapo aliposhuka kwenye teksi, alitembea kwa hatua za kawaida, pesa na simu zikiwa ndani ya fuko dogo la Rambo, bastola mkononi. Hakubabaishwa na milio ya simu hizo ambazo wapigaji ama walijua kuwa kazipora ama hawakujua chochote.
Haikupita hata dakika moja bila ya simu moja kuita au hata simu mbili, tatu kwa mpigo. Hilo hakulijali, wala hakuwa na wasiwasi wowote; bastola yake ilikuwa ni sawa na Mungu wake wa pili. Asingesita kuitumia kama angetokea yeyote wa kuletea fyoko!
Alipofika kwake, Tandale Uzuri, na kujifungia chumbani mwake, ndipo kile kicheko cha chinichini kilipomtoka.
Hakuwa mbumbumbu wa simu; alizijua zile simu za bei kubwa na za bei ya chini. Katika simu alizozitoa ndani ya fuko lake, sita zilikuwa za bei ya kutisha madukani; simu moja iliuzwa si chini ya shilingi laki saba! Nyingine zilikuwa za shilingi laki tatu hadi mbili. Alijua wapi pa kuziuza simu hizo na nani wa kuzinunua.
Kwake, hilo lilikuwa ni jambo dogo sana. Kwa makadirio ya haraka, alitarajia kumiliki shilingi milioni mbili au tatu baada ya 'tajiri' wake kuzinunua simu zote, na hapo akiwa ameuza kwa ile bei ya 'kutupa.'
Alipozihesabu pesa, tabasamu la kifahari likamtoka. Saa chache zilizopita alikuwa na shilingi 5,000 tu! Sasa kuna laki sita mbele yake! Mungu ampe nini?
Naam, mambo yalimwendea kama alivyotaka, na hakukamatwa!
Kesho yake jioni hakuwa akimiliki hizo laki sita pekee, la hasha. Baada ya kuziuza simu kwa yule 'mtu wake' akawa na pesa taslimu shilingi 3,500,000.
Ni hapo lilipomjia wazo la kuondokana na ukapera. Aoe! Na aliyeutawala ubongo wake kuhusu hilo hakuwa mwingine zaidi ya Sarah. Ndiyo, Sarah, mwanamke aliyejaaliwa sura nzuri, mwanamke aliyebahatika kupewa umbo livutialo, na akiwa ni mwanamke ambaye kichwani mwa Kasha ndiye aliyejua nini cha kumfanyia mwanamume pindi wazichojoapo nguo zao na kujitupa kitandani au popote pale panapowastahili. Na alitaka ndoa kati yake na Sarah iwe ni ya kipekee, ndoa ambayo itabaki ni simulizi vinywani mwa watu siku zijazo ikibidi, hata kwa vizazi vijavyo.
Lakini alizijua gharama za ndoa za kifahari. Hivyo aliamua kusaka pesa zaidi. Akilini mwake aliamini kuwa shilingi milioni 20 hata 50 ndizo zingetosha kuifanya sherehe yake iwe SHEREHE kweli. Watu wanywe, watu wale na kusaza. Iwe ni sherehe ambayo vituo vya redio vitaizungumzia, magazeti yataandika, televisheni zitaonyesha na watu mitaani watakesha wakiisifia.
Ndipo alipopanga mpango mzito utakaomwingizia kitita kizito cha pesa. Naam, ulikuwa ni mpango wa kumwingizia shilingi milioni 30 au zaidi na baada ya hapo aachane na shughuli hiyo, badala yake aanzishe mradi utakaomwingizia pesa za kuyaendesha maisha siku hadi siku.
Hakufanikiwa!
Ilikuwa ni baada ya kumuua mlinzi wa tajiri mmoja katika Mtaa wa Zaramo katikati ya jiji na kuondoka na fedha taslimu, shilingi milioni 50, alijikuta akitazamana na bunduki nne za askari polisi mita kama 50 tu kutoka kwa tajiri huyo. Alitiwa mbaroni na kesho yake akasimama kizimbani akikabiliwa na mashtaka ya wizi wa kutumia silaha na mauaji.
Alisota rumande kwa mwaka mmoja bila ya dhamana, na kipindi chote hicho hakukuwa na mtu yeyote aliyekwenda kumjulia hali. Hata Sarah!
Alikuwa katika ulimwengu mwingine wa maisha, ulimwengu wa kukosa uhuru wa kufanya kile akipendacho na kula chakula akitakacho. Na kwa kuwa alitambua fika kuwa kesi yake ilikuwa kubwa na mbaya, na ingeisha vibaya kwa upande wake, aliamua kutumia njia yoyote ili ajiokoe.
Siku moja, ikiwa ni miongoni mwa siku alizopelekwa mahakamani, alifanikiwa kuwatoroka askari chini ya ulinzi muda mfupi tu baada ya kuahirishwa tena kwa kesi hiyo. Aliponyoka huku akiacha maiti watatu, askari aliowaua kwa kutumia misuli yake.
Alipozuka Barabara ya Kivukoni, kando ya Mahakama Kuu alimkuta mzee mmoja wa Kihindi akishuka kutoka garini mwake. Hakumpa hata dakika moja, alimtwisha konde la shingo na kumpokonya ufunguo wa gari. Sekunde chache baadaye Kasha alikuwa akiondoka katika eneo hilo kwa kasi ya kutisha na kuwaacha watu wakistaajabu, baadhi yao wakihisi kuwa huenda ni utayarishaji wa miongoni mwa sinema nyingi zinazotayarishwa nchini.
Hakuhitaji kulitumia sana gari hilo. Alikwenda nalo hadi Magomeni ambako alilitelekeza na kupanda daladala hadi Kimara ambako pia alichukua usafiri wa basi kubwa lililokuwa likienda Morogoro.
Hakufika Morogoro. Aliishia Kongowe. Huko Kongowe alikwenda kwa Mama Sikujua, mwanamke aliyewahi kuwa na uhusiano naye wa kimapenzi miaka kadhaa iliyopita. Lakini, licha ya kupata hifadhi hapo kwa Mama Sikujua bado hakuridhika. Hivyo, siku moja ikiwa ni miezi miwili baadaye, aliondoka, akapanda basi dogo hadi Kariakoo, mtaa wa Msimbazi jijini Dar-es-Salaam, jiji alilolizoea na kulipenda.
Akiwa katika mavazi ya heshima; suti nyeusi iliyoshonwa vizuri, alionekana kama mtu yeyote mstaarabu na asiyekuwa na doa lolote katika mienendo yake. Ni mwonekano huo uliomfanya apishane na askari watatu walioshindwa kumtambua japo walikutanisha macho. Siku hiyo akarandaranda katika mitaa ya Kariakoo hadi akachoka.
Alipoitazama saa akagundua kuwa ilitimu saa 10 jioni. Mfukoni alikuwa na shilingi 7,000 tu, yakiwa ni masalia ya shilingi 10,000 alizomwibia Mama Sikujua asubuhi.
Sasa akaamua kuiacha Kariakoo. Akaivaa mitaa ya katikati ya jiji, Uhindini, na baada ya kupita huku na kule, hatimaye akatokea Barabara ya Maktaba ambako bila ya dhamira maalumu alisimama na kuukodolea macho msururu wa magari kwenye makutano ya Barabara za Bibi Titi Mohammed na Maktaba.
Akiwa hapo, mara akamwona mwanamke aliyekuwa ndani ya gari dogo, akimwita kwa ishara ya mkono.
**********
DAKIKA ishirini baadaye, Sarah alikanyaga breki nje ya nyumba kubwa, ya kisasa, Ada Estate, Kinondoni. Muda mfupi baadaye yeye na Kasha walikuwa sebuleni. Ilikuwa ni sebule pana na iliyopendeza kutokana na kufurika samani zenye thamani kubwa. Kwa sekunde au dakika kadhaa Kasha alikuwa akijiuliza ni vipi Sarah ameweza kuyamudu maisha kwa kiwango hicho.
Huku akiendelea kuduwazwa na ubora wa sebule hiyo, mara Sarah alimzindua: “Unatumia kinywaji gani?”
Kasha alifikiri kidogo kisha akajibu, “Nikipata bia baridi nadhani roho itasuuzika.”
“Bia gani?”
“Tusker.”
Sarah alitokomea chumbani na kurejea baada ya muda mfupi, mikononi akiwa na sinia ambalo juu yake zililala chupa nne za bia.
*****KASHA KAKARIBISHWA NYUMBANI KWA SARAH. ANASTAAJABU KUWA NI VIPI MAMBO YAMEMYOOKEA SARAH. NI KIPI KITAFUATA? TUONANE
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment