Search This Blog

Tuesday, 14 June 2022

AKIRUDI TUMUUE - 3

 





    Simulizi : Akirudi Tumuue

    Sehemu Ya Tatu (3)



    *** *** *** *** *** *** ***

    KUNA wakati yowe dogo jembamba lilisikika, likiambatana na sauti ya kike ikimwaga sifa kwa kukitaja mfululizo kiungo fulani huku miguno mizito na uropokaji wa kimahaba uliotoka kwa sauti ya kiume nao ukipokea mara chache.



    Hata hivyo, pamoja na kufanyiana hayo yote, bado kichwani mwa Kasha kulikuwa na jambo lililomsumbua, jambo ambalo hakutaka ifike asubuhi nyingine bila ya kuliweka bayana kwa Sarah. Alitaka autumie usiku huohuo kumdokeza Sarah kisha kumshawishi akubaliane nalo.



    Taa ya rangi ya bluu ikiwaangazia nuru hafifu, nuru waliyoipenda, Kasha na Sarah waliendelea kulala kitandani hapo huku wakitazamana kwa macho yaliyoridhika kwa kile walichokifanya muda mfupi uliopita. Wakati huo pia mikono yao haikutulia, Sarah alikuwa akimpapasa Kasha katika paji la uso huku Kasha akiutelezesha mkono wake katika milima na mabonde ya mwili ule mwororo wa Sarah.



    Hatimaye: “Sarah,” Kasha aliita kwa upole, macho yake yakimtazama Sarah, sawia. Tazama yake ilionyesha kulikuwa na jambo zito alilotarajia kumweleza Sarah.



    Sarah hakuitika, badala yake aliyatua macho yake usoni pa Kasha. Hiyo ilitosha kumdhihirishia Kasha kuwa Sarah alikuwa tayari kumsikiliza.



    “Sarah, si unajua kuwa kitendo cha kunihifadhi hapa ni cha hatari kwako na kwa mumeo?”



    “Kwa nini unauliza hivyo?” Sarah alimkazia macho.



    “Jibu swali langu kwanza.”



    Sekunde chache za ukimya zilipita. Kisha kwa sauti ya chini, sauti ya unyonge, Sarah akajibu, “Ni kweli.”



    “Bwana'ako anaweza kurudi baada ya siku mbili, tatu hivi zijazo, siyo?” Kasha aliendelea kuhoji.



    Sarah alishtuka. Ni hapo alipokumbuka kuwa baada ya siku saba, Machibya atarejea. Hakujibu kwa sauti, alitikisa kichwa kama ishara ya kukubali.



    “Kwa hali ilivyo, utalazimika kunitimua kabla hajatia timu hapa,” Kasha aliendelea. “Unadhani nitaishije? Elewa kuwa sina kitu; sina pesa. Na hapa Dar sina mtu mwingine anayeweza kuwa na moyo wa ukarimu kama wako. Wapo watu wengi ninaowafahamu na wananifahamu. Kwa bahati mbaya sina imani nao. Kama nitajipeleka kwa mtu asiyekuwa na moyo mgumu kama wako, zitawachukua saa chache sana askari kunitia mbaroni. Unaweza kunisaidiaje kwa hilo?”



    Sarah alizama katika fikra nzito. Kasha alikuwa amezungumza maneno mazito, maneno yenye ukweli mtupu. Lakini pia, ulikuwa ni ukweli usiopingika kuwa Sarah alimpenda Kasha. Alimpenda kwa sababu tu alikuwa ni mwanamume aliyejua kuutumia uwanaume wake sirini pale kitanda kilipowalaki.



    Hivyo, huruma ilimwingia mtoto wa kike. Akajitolea kumpa msaada. Kwa jinsi hali ya maisha ilivyokuwa imemnyookea, hakukiona kikwazo chochote cha kutomsaidia Kasha. “Tafuta gesti yoyote ya bei nafuu,” alimwambia.



    “Gesti?”



    “Ndiyo. Nitakulipia kwa wiki moja, na nitakupa pesa kidogo za chakula.”



    Kasha aliuona ukungu mzito wa kikwazo mbele yake. Hata hivyo hakuamini kuwa ukungu huo unaweza kumfanya asitekeleze lolote lile alilodhamiria kulitekeleza.



    Kwa ujumla alijiamini, hivyo akaamua kupasua jipu. “Sarah, naomba unieleze jambo moja,” alisema.



    “Jambo gani?”



    “Kama kweli unampenda huyo bwana'ako.”



    Sarah alikunja uso kidogo kisha akatabasamu kwa mbali. “Kwa nini unauliza hivyo?”



    “N'na sababu.”



    “Sababu gani?”



    “N'ambie kwanza, unampenda kutoka moyoni? Au kwa kuwa tu mambo yake si mabaya?”



    Sarah alicheka. “Ameyabadili maisha yangu, kwa nini nisimpende?”



    “Kwa hiyo una maana pesa zake zimekuwa chachu ya kulikoleza penzi lenu, sio?”



    “Nd'o maana'ake.”



    “Hebu,” Kasha alisema na kusita. Akakohoa kidogo kisha akaendelea, “Kama angekuwa na hali duni kama yangu, yupi angekuwa na uzito moyoni mwako?”



    “Wewe!” Sarah alijibu kwa mkazo.



    Kasha alimtazama Sarah kwa makini, na akauona ukweli wa jibu hilo katika macho yake. Hapo, akaanza kuiona nuru ya ushindi mbele yake, na kwa kujiamini, alisema, “Ok, sasa tufanye kitu muhimu kwa faida yetu.”



    “Kitu gani?”



    “Tutengeneze maisha yetu binafsi, mimi na wewe.”



    Kimya kifupi kilizuka, Sarah akiyatafakari maneno hayo.





    “Umenielewa?” Kasha alimshtua.



    “Bado.”



    “Kwa kifupi, tumgeuzie kibao.”



    Sarah alishtuka. Akaguna. “Tumgeuzie kibao?!”



    “Nd'o maana'ake,” Kasha alijibu haraka, sauti yake ikiwa ya kujiamini huku macho yake yaking'ara. “Kumbuka kuwa yule ni hawara yako tu, sio mumeo. Isitoshe hauna kinga yoyote ya kukufanya awe wako wa kufa na kuzikana. Umezaa naye? Hapana. Au una mimba yake?” hapo akamkazia macho zaidi, akionekana kusubiri jibu.



    “Sina mimba,” Sarah alijibu.



    “Unaona! Kwa hiyo ukae ukijua kuwa anaweza kukutimua dakika yoyote, ukamwacha na jumba lake, mipesa yake na magari yake. Utaondoka kama ulivyoingia!”



    Kwa mara nyingine Sarah aliguna.



    “Unabisha?” Kasha alimdaka.



    Sarah hakujibu, badala yake alishusha pumzi ndefu, hali iliyomfanya Kasha ajenge imani kuwa maneno yake yamemwingia vilivyo. Hapo akapata ujasiri wa kutoboa kila kitu.



    “Sikia, akirudi tumuue!” alitamka kwa sauti ya chini, sauti nzito na yenye msisitizo mkali.



    Maneno hayo yalipenya kwa usahihi mkubwa masikioni mwa Sarah, lakini ilikuwa vigumu kwake kuyaelewa. Na kwa jumla yalikuwa ni maneno yenye uzito mkubwa ambayo hakutaka kuchukulia pupa katika kuyaelewa.



    Kwa sauti ya chini zaidi, alisema, “Sijakuelewa. Umesema?”



    Kasha hakuona haja ya kutumia mzunguko katika maelezo yake. Akaamua kupasua zaidi: “Ni hivi, akitia timu tu, tumzimishe!”



    “Nini?!” Sarah alibwata, akakurupuka kitandani na kumtazama Kasha kwa macho makali. Akasimama katikati ya chumba hicho, uchi kama alivyozaliwa, mikono kiunoni, akihema kwa nguvu. “Kasha una wazimu?” aliongeza.



    Kasha hakuwa mtu wa kutishwa na tazama ya Sarah, wala hakuwa ni kiumbe wa kubabaishwa au kushangazwa na swali hilo. Tangu alipoubuni mpango huo alitarajia mambo mawili; kudhaniwa kuwa kakumbwa na kichaa au kupongezwa kwa ubunifu wa jambo lenye manufaa. Lililotokea ni moja kati ya hayo.



    Naam, hakubabaika. Alichofanya ni kuachia tabasamu kubwa, tabasamu la kujiamini, kisha kwa upole akasema, “Tulia. Keti tuzungumze kwa utulivu.”



    “Tuzungumze! Tuzungumze kuhusu upuuzi huo?”



    “Ndiyo,” Kasha alisema kwa upole na kwa sauti ya chini. “Hata kama ni upuuzi, keti tufikie tamati yake.”



    Sarah alishusha pumzi ndefu, akarudi kitandani huku akionekana kutokuwa na furaha yoyote.



    “Sarah,” Kasha alimwita kwa upole.



    Hakuitika.



    “Sarah,” Kasha alirudia.



    “Nakusikiliza,” Sarah alisema bila hata ya kumtazama. Alikodoa macho darini, uso ukiwa umekunjamana.



    “Usiwe mjinga, Sarah,” Kasha aliendelea. “Uwe makini maishani mwako, Sarah. Jaribu kuona mbele. Ringa na mali yako, usiringie vya hawara, mwanaume asiye mumeo...”



    Kasha alizungumza kwa kirefu, akamsuka Sarah, na akasukika, akalainika. Akawa ndembendembe!



    Sasa badala ya kuketi, alijilaza kabisa kitandani hapo, kando ya Kasha. Akautupa mkono kifuani pa Kasha na kuanza kupapasa kwa namna ivutiayo.



    Wakatazamana.



    “Lakini hatutagundulika?” hatimaye Sarah alihoji huku akiendelea kumpapasa kifuani.



    “Haiwezekani!” Kasha alijibu kwa sauti thabiti.



    Kwa jumla Kasha hakuwa na wasiwasi kuhusu mpango huo. Alijiamini na aliamini kuwa hakuna litakaloshindikana. Akaongeza, “Jambo muhimu ni kuhakikisha suala hilo linakamilika, au tuseme linapaswa kutekelezwa siku hiyohiyo atakayorudi! N'na maana kuwa hapaswi kupata usingizi ndani ya nyumba hii, labda ilale maiti yake!”



    Ukimya mfupi ukapita, kisha akaendelea, “Cha muhimu tena, na hiki kikiwa cha uzito wa juu zaidi, ni utunzaji wa siri. Kwa kipindi hiki ambacho atakuwa hajarudi, jitahidi sana kuuchunga ulimi wako. Sawa?”



    “Kwa hilo hata usitie shaka,” Sarah alisema kwa kujiamini.



    **********





    SIKU zilikuja, siku zikaenda, hatimaye siku iliyosubiriwa na Kasha kwa shauku kubwa ikawadia. Ilikuwa ni mwishoni mwa wiki, siku ya Jumamosi. Kama kawaida, siku hiyo pia Sarah aliondoka asubuhi, akaenda kwenye shughuli zake, lakini akawahi kurejea. Saa 7:00 mchana ilimkuta nyumbani ambako aliandaa maakuli.



    Baada ya saa nzima waliifuata meza kubwa na kujipatia mlo. Kisha wakarudi sofani na kuwasha televisheni. Sarah aliseti kituo fulani ambacho kilikuwa kikirusha muziki wa Kikongo mfululizo.



    Wakati Sarah aliyagandisha macho kwenye screen ya televisheni, Kasha alikuwa mbali kimawazo kiasi cha kutoiangalia televisheni hiyo mara kwa mara. Akili yote ilikuwa juu ya utekelezaji wa kazi muhimu iliyomkaabili saa chache zijazo.



    Mara aliigeuza shingo taratibu na kumtazama Sarah. “Una hakika atakuja leo?”



    Sarah aliyahamisha macho na akaziondoa akili katika televisheni hadi usoni pa Kasha. “Kwa nini unauliza ivo?” hatimaye alihoji.



    “Huwezi kujua. Anaweza kuahirisha makusudi tu na kuamua kuja baada ya wiki moja nyingine.”



    “Aaah, wapi, siyo kawaida yake. Kama kuna mabadiliko yoyote kwa vyovyote vile angenipigia simu. Tena angenipigia tangu jana.”



    “Na alikwambia ataingia saa ngapi?”



    “Ndege itatua airport saa kumi na mbili jioni.”







    *** *** *** *** *** ***



    WAKATI Sarah aliyagandisha macho kwenye screen ya televisheni, Kasha alikuwa mbali kimawazo kiasi cha kutoiangalia televisheni hiyo mara kwa mara. Akili yote ilikuwa juu ya utekelezaji wa kazi muhimu iliyomkaabili saa chache zijazo.



    Mara aliigeuza shingo taratibu na kumtazama Sarah. “Una hakika atakuja leo?”



    Sarah aliyahamisha macho na akaziondoa akili katika televisheni hadi usoni pa Kasha. “Kwa nini unauliza ivo?” hatimaye alihoji.



    “Huwezi kujua. Anaweza kuahirisha makusudi tu na kuamua kuja baada ya wiki moja nyingine.”



    “Aaah, wapi, siyo kawaida yake. Kama kuna mabadiliko yoyote kwa vyovyote vile angenipigia simu. Tena angenipigia tangu jana.”



    “Na alikwambia ataingia saa ngapi?”



    “Ndege itatua airport saa kumi na mbili jioni.”



    Kasha alikunja uso kidogo. “Nusu saa itakayofuata itatosha kumfikisha hapa, si nd'o maana'ake?”



    “Itakuwa hivyo kama hakutakuwa na kikwazo chochote njiani.”



    “Yaani kama magaidi wa Kisomali hawataiteka ndege?”



    Sarah alicheka. “Magaidi wa Kisomali hawana ubavu wa kuteka ndege,” alisema na kuporomosha tusi zito la nguoni akiwalenga hao magaidi wa Kisomali.



    “Hawawezi?!”



    “Ndiyo, hawawezi!”Sarah alikazia. “Hawana ubavu huo, nakwambia kweli. Kazi yao ni kushinda baharini na kuvizia meli tu,” akaporomosha tusi jingine zito, walengwa wakiwa ni walewale, magaidi wa Kisomali.



    Tabasamu la mbali lilichanua usoni pa Kasha. Kisha katika kuonyesha kuwa masikhara hayo hayana nafasi katika maongezi yao, aliuliza, “Si utakwenda kumpokea?”



    “Yeah. Nadhani ni lazima iwe hivyo, kinyume chake hatanielewa.”



    “Hapo, shwari.”



    Kwa mara nyingine ukimya ukatawala kabla Kasha hajahitimisha kwa kusema, “ Yatakayojiri baada ya nyie kuwasili n'achie mimi; sawa?”



    “Poa tu.”



    **********





    INSPEKTA Dismas alikuwa na mazoea ya kuvinjari mitaa ya katikati ya jiji hususan siku za wikiendi au siku yoyote anapokuwa mapumzikoni.



    Jioni moja, alitoka nyumbani kwake, Kurasini, akapanda daladala lililomshusha Posta Mpya. Siku hiyo aliazimia kwenda Mtaa wa Alykhan eneo la Upanga ambako alikuwa na miadi ya kuonana na rafikiye wakanywe bia katika baa fulani mtaani hapo.



    Mara tu alipoteremka kituoni, alirudi alikotokea kwa mwendo wa taratibu. Akaiacha Barabara ya Azikiwe na kuifuata Barabara ya Maktaba. Akaendelea kuvuta hatua kwa mwendo wake uleule wa kinyonga. Hatimaye akalikaribia jengo la CMC AUTOMOBILE LTD. Akasitisha kutembea, sasa akawa akiyatupia macho magari na wakati mwingine, majengo ya SOPHIA na MORANI yaliyokuwa upande wa pili wa barabara.



    Alipotosheka, akaendelea kutembea. Lakini mara tena akasimama ghafla. Alikuwa na sababu ya kufanya hivyo. Mbele yake, hatua kama thelathini hivi, alimwona mtu, mwanamume aliyesimama kando ya barabara akiyatupia macho magari yaliyosongamana barabarani.



    Sura ya mtu huyo haikuwa ngeni machoni mwa Inspekta Dismas. Alimtambua vizuri. Sekunde tano za awali alitulia akimtazama, sekunde ya sita alikuwa ameshaunyanyua mguu wa kushoto na kuendelea kutembea. Alipomfikia, alimpita kwa mbele huku akimtupia jicho mara moja tu, jicho la siri ambalo mtu huyo hakulibaini.



    Baada ya kumpita kwa hatua kumi hivi, alielekea barabarani kwa mwendo wa taratibu zaidi, kisha akasimama tena. Hazikupita hata dakika mbili mara akamwona mtu huyo akilifuata gari moja dogo na kuingia, kisha gari hilo likaondoka baada ya ruhusa ya taa za Usalama Barabarani.



    Inspekta akachanganyikiwa! Mtu huyo aliyepanda gari na kutokomea alikuwa muhimu sana. Ni yule aliyetoroka Mahakama Kuu muda mfupi baada ya kesi dhidi yake kuahirishwa!



    Akili ya Dismas ilifanya kazi haraka. Alitambua fika kuwa asingeweza kulizuia gari hilo ambalo lilikuwa katikati ya magari mengine mengi. Isitoshe, msururu huo wa magari ulishaanza kutambaa. Angefikiriwa yu kichaa kama angediriki kulizuia gari hilo huku akiwa hana utambulisho wowote wa kuwafanya madereva wamchukulie kuwa ni askari. Zaidi, wangemhisi kuwa ni jambazi.



    Hivyo, alichokifanya ni kuzikariri nambari za gari hilo na muda mfupi baadaye alikuwa ametoa kijitabu kidogo mfukoni mwake na kuziandika nambari hizo.



    Tukio hilo liliivuruga ratiba yake ya matembezi. Papohapo akaifuata teksi iliyompeleka ofisini. Huko alichakurachakura katika majalada yake yenye rekodi za majambazi sugu na kukipata alichokuwa akikitafuta.



    Jalada mojawapo lilikuwa na picha ya pasipoti ya mwanamume. Inspekta hakuhitaji kutumia hata sekunde tano kubaini kuwa ni picha ya nani. Alimtambua vizuri! Ni yule jambazi hatari ambaye vyombo vya dola vimehaha kwa muda mrefu vikimsaka bila ya mafanikio.



    Aliitazama picha ile kwa makini, akivuta kumbukumbu zake kwa utulivu, akiilinganisha picha hiyo na yule mtu aliyemwona nje ya jengo la CMC. Hii picha ya ndani ya jalada ni ya mtu mwenye nywele nyingi na sharafa kibao, tofauti kabisa na yule aliyemwona kando ya Barabara ya Maktaba.



    Hata hivyo, tofauti hiyo haikumfanya ajenge imani kuwa sura hizo ni za watu wawili tofauti. Hapana, hilo halikupata nafasi yoyote akilini mwake. Aliamini kuwa mtu huyu ni yuleyule aliyemfahamu na ambaye Jeshi la Polisi lilikuwa likimsaka kwa udi na uvumba.



    Mara akaachia tabasamu dogo, tabasamu lisilokuwa na chembe yoyote ya furaha, tabasamu lililofuatiwa na mnong'ono: “Kazi anayo. Safari hii labda anywe sumu mapemaaa! Afe kabla hatujamtia mbaroni. Vinginevyo...” akaiacha sentensi hiyo ikielea.



    Na ni wakati huo pia ndipo alipomkumbuka Sajini Kajia, askari shupavu anayeshirikiana naye katika mikasa mbalimbali. Simu haikuwa mbali, aliitwaa na kumpigia Kajia, akimtaka afike ofisini hapo haraka sana.



    “Kuna nini afande? Mbona leo niko off ?” Kajia ambaye wakati huo alikuwa nyumbani kwake, alihoji simuni.



    “Uko off. Hata mimi niko off. Lakini idara yetu haina mapumziko ya uhakika. Si unalijua hilo?”



    “Najua, afande.”



    “Ok, nakusubiri.”



    Kauli hii ya mwisho ya Dismas, masikioni na akilini mwa Kajia ilikuwa ni amri iliyo dhahiri. Kwa hali hiyo hakuwa na budi kuitekeleza amri hiyo. Zikamchukua dakika ishirini tu kutoka kwake, Kurasini hadi Kituo cha Polisi Kati.



    “Ndiyo, afande,” alisema mara tu alipoingia ofisini mwa Inspekta Dismas. Akaketi kitini na kuongeza, “Wito wako umenishtua sana. Naamini kuna jipya lisilopaswa kuwa kiporo.”



    “Hakuna jipya,” Inspekta Dismas alisema kwa utulivu, macho akiwa ameyazamisha kwenuye jalada lililokuwa na picha ya mtuhumiwa wao. Akaongeza, “Ni suala la kawaida, tulilokwishaanza kulifanyia kazi, lakini tukalisitisha kwa kipindi kirefu.”



    “Ni lipi hilo?”



    Inspekta Dismas hakujibu, badala yake alimsogezea jalada lile.



    “Si Kasha huyu?” Kajia alishangaa.



    “Ndiye.”



    “Sasa?”



    “Si unaikumbuka ishu yake?”



    “Ndiyo,” Kajia alijibu haraka. “Alitoroka mahakamani!”



    “Na aliua mahakamani!” Dismas aliongeza.



    Kimya kikatanda ghafla.



    Kisha Dismas akamtazama Kajia kwa macho makali. “Yupo mji huu,” alisema kwa msisitizo mkali. Akaongeza, “Nimemwona kwa macho yangu leo hii.”



    Kajia aliguna, akashusha pumzi ndefu. Akamtazama kwa makini bosi wake, akionyehsa kuhitaji maelezo zaidi ya hayo.

    “Amepanda gari jeusi aina ya Nissan Laurel pale kwenye makutano ya barabara za Bibi Titi na Maktaba.”



    “Hukumfuatilia angalau ujue alikoshia?”



    “Ingewezekana. Lakini kaa ukijua kuwa kumfuatilia mtu wa aina ya Kasha hakutofautiani na kumfuatilia chatu mwenye njaa. Inatakiwa umfuate huku ukiwa kamili.”



    “Na hukuzinoti hata namba za gari alilopanda?”



    “Hilo ndilo nililofanikwa kulipata,” Inspekta alisema huku akimpatia Kajia namba hizo. “Shughulikia suala hilo; tumjue mwenye gari hilo na mengine yote yanayostahili katika kufanikisha kazi yetu. Haikuwa teksi, labda kama ilikuwa ni teksi bubu.”



    **********



    ILIKUWA ni kazi nyepesi kwa Sajini Kajia. Dakika thelathini baadaye, tayari alikuwa na jina la mmiliki wa gari lenye nambari alizopewa na Inspekta Dismas. Lakini kikwazo kilikuwa ni jinsi ya kumpata mmiliki huyo au kuyajua makazi yake halisi.



    *****VYOMBO VYA DOLA VINA MACHO MAKALI. TAYARI INSPEKTA DAMAS KAMWONA MTU ANAYEMSHUKU KUWA NDIYE ALIYETOROKA MAHAKAMANI. SUALA LA KUMFUATILIA LINAANZA. WAKATI HUOHUO, KASHA NA SARAH WAMEFIKIA MWAFAKA KUHUSU MPANGO ALIOUBUNI KASHA. NINI HATIMA YA MCHANGANYIKO HUU WA MAMBO?





    ITAENDELEA





0 comments:

Post a Comment

Blog