Simulizi : Akirudi Tumuue
Sehemu Ya Nne (4)
**** **** **** **** **** ****
KAJIA aliguna, akashusha pumzi ndefu. Akamtazama kwa makini bosi wake, akionyesha kuhitaji maelezo zaidi ya hayo.
“Amepanda gari jeusi aina ya Nissan Laurel pale kwenye makutano ya barabara za Bibi Titi na Maktaba.”
“Hukumfuatilia angalau ujue alikoshia?”
“Ingewezekana. Lakini kaa ukijua kuwa kumfuatilia mtu wa aina ya Kasha hakutofautiani na kumfuatilia chatu mwenye njaa. Inatakiwa umfuate huku ukiwa kamili.”
“Na hukuzinoti hata namba za gari alilopanda?”
“Hilo ndilo nililofanikwa kulipata,” Inspekta alisema huku akimpatia Kajia namba hizo. “Shughulikia suala hilo; tumjue mwenye gari hilo na mengine yote yanayostahili katika kufanikisha kazi yetu. Haikuwa teksi, labda kama ilikuwa ni teksi bubu.”
**********
ILIKUWA ni kazi nyepesi kwa Sajini Kajia. Dakika thelathini baadaye, tayari alikuwa na jina la mmiliki wa gari lenye nambari alizopewa na Inspekta Dismas. Lakini kikwazo kilikuwa ni jinsi ya kumpata mmiliki huyo au kuyajua makazi yake halisi.
Siku tano zilipita bila ya gari hilo kuonekana mitaani licha ya mitego mingi na mikali kuwekwa katika jiji zima kwa saa 24. Siku ya sita, Kajia aliingia ofisini kwa Inspekta huku akiwa na hisia tofauti.
“Labda mshenzi kishalihama jiji,” alimwambia.
“Siyo rahisi,” Inspekta alipinga. “Njia zote za kutoka nje ya jiji zina ulinzi madhubuti. Vituo vyote vina picha yake na maelezo yanayomhusu. Ambacho hatukufanya ni kuisambaza picha yake magazetini na kwenye vituo vya televisheni. Huu ni msako wa kimya-kimya; huwezi kujua, huenda hatua ya kumtangaza kwenye vyombo vya habari inaweza kumpa mwanya au mbinu ya kufanya chochote, hususan kutokomea zaidi.”
Kajia aliridhika na maneno ya bosi wake. Sakata lilikuwa ni jinsi ya kumtia mbaroni Kasha. Bado walikuwa katika kiza kinene!
**********
JOTO kali la Jiji la Dar es Salaam lilimlaki Machibya mara tu alipoikanyaga ardhi ya Tanzania kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere saa 12.00 jioni siku ya Jumamosi. Akalivua jaketi lake na kulipachika begani. Kisha akaitoa simu mfukoni na kumpigia Sarah.
Hawakuzungumza kwa muda mrefu, Machibya alihitaji kujua tu kama Sarah amekuja uwanjani kumpokea.
“Yeah, nina zaidi ya nusu saa tangu nifike,” Sarah alimjibu.
Machibya alitoka na mizigo yake baada ya kukamilisha taratibu nyingine za uwanjani hapo. Alipotokeza nje ya jengo, akaangaza macho huku na kule akimtafuta Sarah. Akajitoa kwenye mkusanyiko wa watu waliofika hapo kuwapokea jamaa zao. Akaelekea kwenye maegesho ya magari.
Huko kulikuwa na magari mengi ya aina mbalimbali. Kati ya hayo, ni manne tu yaliyofanana na Nissan Laurel la Sarah kwa muundo na rangi. Nje ya gari mojawapo alimwona Sarah kwa usahihi mkubwa akiwa ameliegemea gari lake.
Akamfuata.
**********
INSPEKTA Dismas alikuwa nyumbani kwake jioni hiyo. Tofauti na siku nyingine, siku hiyo kwa mbali alihisi uchovu na maumivu viungoni. Hisia kuwa ananyemelewa na malaria zilimjia lakini akapanga kwenda kupimwa hospitali kama hali hiyo itashamiri.
Alikuwa sebuleni, kaketi sofani, chupa ya Cocacola ikiwa kando yake. Labda siku ingeisha bila ya kuisumbua akili yake katika kutafuta ufumbuzi wa tatizo lolote kubwa au kuvihangaisha viungo vyake kwa kuvishughulisha kwa jambo hili na lile, kama lisingetokea hili lililotokea.
Simu yake ya mkononi iliita!
“Afande! Ile Nissan Laurel imeonekana sasa hivi ikipita Barabara ya Bibi Titi Mohammed, eneo la Mnazi Mmoja,” sauti ilipenya masikioni mwake mara tu alipoiegesha simu hiyo kando ya sikio.
“Nini?!” alibwata kwa mshtuko.
Kauli ile ikarudiwa, safari hii kwa msisitizo mkali.
Ilikuwa ni taarifa ambayo Inspekta Dismas hakuitarajia. Kutoonekana kwa Kasha kwa siku zaidi ya saba tangu alipoonwa pale kwenye makutano ya barabara za Maktaba na Bibi Titi, na kutoonekana tena kwa lile gari lililomchukua, ilikuwa ni hali iliyoanza kumkatisha tamaa askari huyo mkongwe. Taarifa hii iliyomjia kwa wakati asiotarajia, ilimshtua, ikamsisimua na kumfariji. Kwa kiasi fulani sasa alianza kuiona taa ya ushindi mbele yake.
“Ipi, ile iliyomchukua mtu wetu tunayemtafuta?”
“Hiyohiyo!”
“Una hakika?”
“Sibahatishi, afande! Hivi n'navyoongea na wewe huenda ikawa imefika kwenye taa za makutano ya Bibi Titi Road na Nkurumah Road. Cha kushangaza dereva ni mwanamke na yuko peke yake!”
“Hilo ndilo linalokushangaza?” Inspekta alibwata. “ We' vipi? Cha muhimu ni kuifuatilia haraka sana. Hakikisheni haiwapotei. Huyo mwanamke anaweza kuwa msaada mkubwa kwetu! Isitoshe, wanawake wa siku hizi hawaaminiki sana. Baadhi yao ni majambazi hatari!”
Amri hiyo ilitekelezwa.
Gari dogo aina ya Toyota Mark 11 lililokuwa likimilikiwa na Jeshi la Polisi, lakini namba zake za usajili zikiwa hazitofautiani na za magari ya raia wa kawaida, lilikuwa na zoezi la kuivinjari mitaa mbalimbali ya kitongoji cha Kariakoo hadi Mnazi Mmoja.
Ilipotimu saa 11:00 jioni, askari watatu wasiovaa sare, ambao ndio waliokuwa wakizunguka na gari hilo, waliamua kuegesha katika kituo cha Mnazi Mmoja, kando ya Hoteli ya Star Light.
Barabara hiyo ya Bibi Titi Mohammed ilikuwa tulivu kwa kiasi fulani. Zile hekaheka za wafanyakazi wanaokwenda majumbani, kwa siku hiyo hazikuwapo. Na ule wingi wa magari unaozua msongamano takriban kila siku jioni, kwa Jumamosi hiyo haukuwapo.
Idadi kubwa ya watu ilikuwa majumbani, ikiwa ni siku ya mapumziko kwa asilimia kubwa ya waajiriwa. Hivyo, wakati askari hao walipokuwa wameegesha gari lao hapo, ziliweza kukatika hata dakika mbili kabla ya gari jingine kupita. Zaidi, ni daladala za Mwananyamala-Stesheni ndizo zilizoibua uhai pale zilipopaki na makondakta kuanza kuuza biashara kwa sauti kubwa: “Mwananyamala! Mwananyamala inageuka...!”
Ni utulivu huo, na upungufu wa magari yanayotamba barabarani uliowasaidia askari hao pale walipoliona gari dogo, jeusi aina ya Nissan Laurel likija kwa mwendo wa wastani likitokea kwenye makutano ya barabara hiyo na Barabara ya Morogoro.
Solomon, mmoja wa askari hao aliliona wakati liko mbali. Akalikodolea macho kwa makini zaidi. Mara gari hilo likawafikia na kuwapita kwa mwendo wa wastani.
Kitu fulani kikamgonga kichwani Solomon. Akazikodolea macho nambari za usajili za gari hilo. Akaguna huku akiharakisha kuchomoa karatasi moja mfukoni mwake na kuisoma. Akashtuka na papohapo akaitwaa simu yake na kupiga, akidhamiria kumtaarifu Inspekta Dismas.
“Hakikisheni hamfanyi uzembe wowote utakaosababisha mwanamke huyo awapotee!” Inspekta alisisitiza simuni, wakati gari hilo la doria lilipokuwa limeshaanza kuliandama lile Nissan Laurel.
Kajia ambaye alikuwa mkuu wa msafara huo, alikuwa kaketi mbele, kiti cha kushoto, akiwa makini, akimhimiza dereva kuhakikisha anayaweka magari mawili kati kabla ya lile waliloliandama. Japo walilazimika kuitii amri ya Inspekta Dismas, hata hivyo akilini mwa Sajini Kajia hakuamini kuwa hatua hiyo inaweza kuwa na manufaa yoyote kwa upande wao.
Alihisi kuwa wanacheza kamari. Alijiuliza, kama mlengwa wao ni Kasha, ya nini kumfuata huyu mwanamke? Na kama kweli huyu mwanamke ana uhusiano wowote na Kasha, na anatambua fika kuwa Kasha anatafutwa na Polisi, je, hata watakapomtia chini ya ulinzi, hawezi kuwa 'ngangari' na kuficha chochote anachokijua kuhusu Kasha?
Isitoshe, huenda wakawa wanamfuata bila ya kujua kuwa wanapoteza muda wao. Inspekta Dismas aliliona gari hilo likiondoka na Kasha pale kwenye makutano ya Barabara za Bibi Titi Mohammed na Maktaba. Alimwona Kasha, na aliliona gari hilo ambalo sasa kundi la Kajia limethibitisha kuwa ndilo lililombeba Kasha siku ile jioni, kufuatia nambari zake za usajili walizopewa na Inspekta Dismas.
Lakini huyu mwanamke ambaye Inspekta Dismas anadai kuwa atakuwa 'msaada mkubwa' ndiye aliyekuwa garini siku Kasha alipolipanda gari hilo pale jirani na Maktaba? Ichukuliwe kuwa siye aliyekuwa akiendesha gari hilo. Je, wakimsumbua kwa maswali yao kwa taaluma yao, hiyo itakuwa njia mwafaka ya kusaidia kumpata Kasha?
Na, kama siku hiyo aliazima gari hilo kwa mmiliki, na akawatajia mmiliki mwenyewe, je, wakimsaka mmiliki huyo na kumpata, atawasaidia kumpata Kasha ambaye hulala jicho moja kalifumba huku jingine likiwa wazi?
Haya, ichukuliwe kuwa huyu mwanamke wanayemfuata, ndiye aliyeondoka na Kasha pale kwenye makutano ya barabara za Bibi Titi na Maktaba. Je, sababu hiyo itatosha kuwafanya wamchukulie kama mhusika mkuu wa kumhifadhi Kasha katika kipindi chochote walipokuwa wakimtafuta kwa udi na uvumba?
Huenda wakaonekana ni watu wa ajabu pale atakapowashangaa, akidiriki hata kuwabwatukia kuwa huwa hana tabia ya kutotoa msaada wa usafiri kwa yeyote.
“Kwani cha ajabu ni kipi hapo? Kwani kutoa lifti nd'o limekuwa kosa? Mtu mwenyewe mbona nilimwacha pale kwenye kituo cha daladala cha Agakhan!”
“Halafu akaelekea wapi?” labda ndilo swali litakalowastahili kumuuliza.
“Haikunihusu!” huenda ndivyo angewajibu. Na labda ataongeza, “Kwani kuna tatizo gani?” Hapo, huenda akawa na taswira ya kujiamini kwa kiwango cha juu.
*** *** *** *** ***
HUENDA wakaonekana ni watu wa ajabu pale atakapowashangaa, akidiriki hata kuwabwatukia kuwa huwa hana tabia ya kutotoa msaada wa usafiri kwa yeyote.
“Kwani cha ajabu ni kipi hapo? Kwani kutoa lifti nd'o limekuwa kosa? Mtu mwenyewe mbona nilimwacha pale kwenye kituo cha daladala cha Agakhan!”
“Halafu akaelekea wapi?” labda ndilo swali lililowastahili kumuuliza.
“Haikunihusu!” huenda ndivyo angewajibu. Na labda ataongeza, “Kwani kuna tatizo gani” Hapo, huenda akawa na taswira ya kujiamini kwa kiwango cha juu.
Wakiwa ni askari wanaojua kutoa majibu yoyote kwa maswali ya aina yoyote, hatashindwa kumpa majibu ya kitaalamu kwa kuzingatia viwango vya elimu yao katika taaluma hiyo. Lakini, je, huyo mwanamke ni nani? Hawezi kuwa askari mwenzao au aliyewahi kuwa askari kama wao, na labda akapata elimu ya juu ya taaluma hiyo zaidi yao?
Kama ni askari, au aliwahi kuwa askari, ni dhahiri watakuwa na kipindi kigumu cha kutatua tatizo lao pale watakapomweka kati. Wazo hilo lilichukua nafasi kubwa kichwani mwa Kajia.
Hakutaka yeye na askari wenzake waonekane 'wajinga' pale mwanamke huyo atakapowabana kwa kauli hii na ile, na maswali haya na yale.
Hivyo alilazimika kuitii amri ya Inspekta Dismas kwa shingo upande huku akihakikisha kuwa anapata picha halisi ya nyendo za mwanamke huyo kabla ya kumtaarifu chochote bosi, Dismas.
Walilifuata gari lile kwa namna ambayo dereva alielekezwa na Kajia hadi Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere.
Sajini Kajia alizidi kushangaa. Akamtazama dereva wao. “Anasafiri?” hatimaye aliuliza.
Dereva hakujibu, alikuwa akitafuta eneo la kuegesha gari.
“Au kaja kumpokea mtu!” Kajia aliongeza, safari hii akiyahamisha macho kutoka kwa dereva hadi kwa askari mwingine aliyeketi kiti cha nyuma.
Katika kuonyesha kuwa yuko pamoja naye kimawazo, askari huyo naye alimtazama kidogo Kajia, kisha akayarejesha macho kule kwenye Nissan Laurel kabla hajatamka neno moja tu: “Labda.”
“Ok, tusubiri tumwone atafanya nini,” Kajia alitamka.
Walibaki garini humo bila ya kuyabandua macho yao kwenye lile gari dogo, jeusi, Nissan Laurel wakifuatilia kila hatua atakayochukua mwanamke huyo. Kulikuwa na magari mawili tu yaliyowatenganisha na wao, hivyo hawakuwa na wasiwasi wowote.
Waliendelea kusubiri, na muda mfupi baadaye wakajenga imani kuwa mwanamke huyo atakuwa amekuja kumpokea mtu. Hilo lilitokana na kutomwona akitoka garini humo, badala yake, pale dereva alipoteremka na kutembea-tembea kama mzururaji hadi akalifikia hilo Nissan, alimkuta kajiegemeza kitini, gazeti mkononi, macho yakiwa yameganda katika ukurasa fulani wa gazeti hilo.
Kama dakika ishirini au thelathini hivi baadaye, pilikapilika zilijitokeza miongoni mwa watu waliofika katika eneo hilo. Wengi wao walilisogelea lango kuu kuwaangalia jamaa zao waliotarajia kutua jioni hiyo.
Kajia na wenzake waliendelea kutulia garini. Muda mfupi baadaye macho yao yakatua kwa kijana mmoja mrefu, aliyevaa suti nyeusi akilifuata lile Nissan Laurel, begi kubwa jeusi likiwa katika mkono wake wa kulia. Askari hao wakashuhudia mwanamume huyo na mwanamke yule wakikumbatiana na kupigana busu. Kisha taratibu gari lile likaondoka.
“Huenda yule nd'o bwana wa huyo mwanamke,” Kajia alisema.
“Na labda ndiye mwenye gari,” askari mwingine aliongeza.
Kajia aliafiki kwa kutikisa kichwa.
**********
“VIPI kuna tatizo lolote?” Machibya alimuuliza Sarah wakati walipokwishaliacha eneo la Uwanja wa Ndege, sasa walikuwa wakitaka kuingia Barabara ya Nyerere.
Machibya alimfahamu vizuri Sarah, kwamba ni mwanamke aliyejaaliwa ucheshi pale anapokuwa na furaha au anapokuwa na majonzi. Tangu alipolifikia gari hilo pale Uwanja wa Ndege, na Sarah akashuka haraka na kumkumbatia kisha kumbusu kabla hajampokea lile begi, furaha ya dhati haikusomeka usoni pake.
Ndiyo, aliachia tabasamu lile la kawaida, na kumtazama kwa mtindo uleule uvutiao, macho yake yakiwa yamelegea na kubembeleza, lakini akilini mwa Machibya tabasamu hilo lilificha siri kubwa moyoni mwa Sarah, siri iliyoipeperusha ile furaha yake ya dhati anayokuwa nayo kila ajapo kumpokea.
Wakati huo, tangu walipoondoka kule uwanjani Sarah alikuwa kimya tu, jambo ambalo halikuwa la kawaida kwake. Kwa jumla, japo alimudu kuendesha gari hilo bila ya matatizo yoyote, hata hivyo mawazo yake yalikuwa mbali na hapo.
Alimkumbuka Kasha, aliyemwacha nyumbani akiwa tayari kwa kazi muhimu. Akayakumbuka maneno ambayo Kasha alimwambia saa chache zilizopita kule nyumbani, Kinondoni Ada Estate, eti: “Yatakayojiri baada ya nyie kufika, n'achie mimi....”
Kwa mbali Sarah alihisi hali ya hatari. Akakumbuka pia siku ile Kasha alipotoa pendekezo la kumuua Machibya pindi tu atakaporejea. Sasa woga ukamwingia Sarah, woga ambao hakuuruhusu ujidhihirishe usoni pake. Japo aliyakaza macho barabarani katika kuonyesha kuwa yuko makini katika uendeshaji wa gari, hata hivyo hakushindwa kumtupia jicho la chati Machibya ambaye alikuwa akimtazama kwa makini akisubiri jibu.
Kichwani mwa Sarah hakujali kutazamwa na Machibya, alijali tukio lililotarajiwa kutekelezwa na Kasha dakika kadhaa baadaye. Japo alitambua fika kuwa Kasha hakuwa na silaha nzito mathalani bastola, hata hivyo, hiyo haikuwa sababu ya kumfanya ajenge imani ya kunusurika kwa Machibya. La hasha.
Alimtambua Kasha kuwa siyo mtu wa kawaida, anaweza kuitekeleza azma yake kwa kutumia mbinu yoyote. Hilo halikuwa na ubishi ubongoni mwake. Historia ya Kasha ilitosha kumfanya Sarah aamini hivyo, ni historia iliyomweka Kasha katika kundi la watu wenye vitendo vya ajabu, vyenye kusikitisha na kutisha.
“Sarah,” kwa mara ya pili sauti ya Machibya ilipenya masikioni mwa Sarah, na ndipo Sarah alipozinduka, akakumbuka kuwa kuna swali ambalo alikuwa hajalijibu.
Na katika kuonyesha kuwa hakuwa mbali kifikra, alikenua meno kidogo, akiachia tabasamu bandia, tabasamu ambalo kwa mwenye upeo mkubwa wa 'kumsoma' mtu asingelaghaika na kulichukulia kuwa ni tabasamu halisi kutoka moyoni.
Machibya alikuwa na upeo mkubwa wa kutambua kuwa mtu amchunguzaye anatabasamu kutoka moyoni au anaachia tabasamu la kinafiki, tabasamu la usoni tu huku moyoni kukiwa na jambo jingine kinyume na tabasamu hilo. Hata hivyo hakupenda kukiumiza kichwa chake kumchokonoa zaidi Sarah, alichohitaji ni kufika nyumbani na kujipumzisha.
Sarah aliongeza mwendo, ukimya ukitawala ndani ya gari hilo. Walifika kituo cha Tazara, wakakipita. Hatimaye walifika mwisho wa Barabara ya Nyerere pale ilipokutana na Barabara za Nkurumah, Lumumba na Bibi Titi. Hadi walipofika hapo, walishanusurika kupata ajali mara mbili kutokana na makosa ya Sarah, matukio yaliyozidi kumfanya Machibya aziamini hisia zake; kwamba siku hiyo Sarah hakuwa timamu kiakili.
**********
NDANI ya dakika tano Kasha alikuwa ameshatazama saa mara tano. Ilikuwa ni jioni, saa 12:20. Sarah alikuwa amemwambia kuwa Ndege itatua uwanjani saa 12:00. “Muda huu wako njiani,” alinong'ona huku akijitoa sofani.
Akaifuata kabati kubwa ya vyombo. Alikumbuka kuwa majuzi alimwona Sarah akipanga vyombo kabatini humo. Miongoni mwa vitu vilivyomvutia na kumsisimua ni kisu.
Aliifungua kabati na kuangaza hapa na pale, hatimaye akakiona. Naam, kilikuwa ni kisu kizuri, kirefu, chenye mpini mzuri na makali ya kuridhisha. “Yap! Sasa mambo supa!” kwa mara nyingine alinong'ona huku akipenyeza mkono na kukitwaa kisu hicho.
Mara akajikuta akiachia tabasamu zito huku akikiangalia kwa makini kisu hicho. Na katika kuthibitisha makali yake, akakijaribu kwa kukipitisha juu ya sofa. Kilifanya kazi vizuri; sofa lilichanika!
******SARAHA NA MACHIBYA WAKO NJIANI WAKIREJEA NYUMBANI. MACHIBYA KISHAMWONA SARAH KUWA HAYUKO TIMAMU KISAIKOLOJIA LAKINI ANAUCHUNA. KULE NYUMBANI KASHA NAYE KISHAJENGA IMANI KUWA WATU WAKE WAKO NJIANI. AMAJIWEKA SAWA. JE, NI KIPI KITATOKEA? TUONANE
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment