Simulizi : Akirudi Tumuue
Sehemu Ya Tano (5)
*** *** *** *** *** ***
NDANI ya dakika tano Kasha alikuwa ameshatazama saa mara tano. Ilikuwa ni jioni, saa 12:20. Sarah alikuwa amemwambia kuwa Ndege itatua uwanjani saa 12:00. “Muda huu wako njiani,” alinong'ona huku akijitoa sofani.
Akaifuata kabati kubwa ya vyombo. Alikumbuka kuwa majuzi alimwona Sarah akipanga vyombo kabatini humo. Miongoni mwa vitu vilivyomvutia na kumsisimua ni kisu.
Aliifungua kabati na kuangaza hapa na pale, hatimaye akakiona. Naam, kilikuwa ni kisu kizuri, kirefu, chenye mpini mzuri na makali ya kuridhisha.
“Yap! Sasa mambo supa!” kwa mara nyingine alinong'ona huku akipenyeza mkono na kukitwaa kisu hicho.
Mara akajikuta akiachia tabasamu zito huku akikiangalia kwa makini kisu hicho. Na katika kuthibitisha makali yake, akakijaribu kwa kukipitisha juu ya sofa. Kilifanya kazi vizuri; sofa lilichanika!
Naam, yakawa ni matokeo ya kumwongezea matumaini ya kufanikisha lolote lile alilodhamiria kulitekeleza kwa kutumia kisu hicho. Kwa ujumla aliamini kuwa ni kisu chenye uwezo wa kutumbua utumbo wa mtu bila ya kutumia nguvu nyingi.
Akakiweka mezani na kisha akalifuata jokofu ambako alitoa chupa moja ya whisky. Akatwaa glasi kabatini na kumimina kinywaji hicho nusu ya glasi. Akanywa kwa pupa na kuitua glasi mezani.
Dakika moja baadaye akahisi joto kali mwilini. Akasimama na kunyoosha viungo. Kisha, kwa mara nyingine akaitupia macho saa ya ukutani. “Kumi na mbili na nusu!” alinong'ona kwa mshangao.
Akilini mwake aliiweka ramani ya barabara watakazopitia Machibya na Sarah kutoka Uwanja wa Ndege hadi hapo Ada Estate. Watapita Barabara ya Nyerere, Bibi Titi, Ali Hassan Mwinyi hatimaye watakapofika eneo la Namanga Msasani, watashika Barabara ya Ruhinde na kuuingia 'msitu' wa Ada Estate.
Ilikuwa ni Jumamosi, siku ambayo haikuwa na foleni ya magari iwezayo kuwafanya wachukue zaidi ya nusu saa njiani. Hivyo Kasha alihisi kuwa hawatakuwa mbali.
Akapiga ngumi kiganjani kwa kujiamini, sasa akijihisi kutokwa na uchovu na badala yake ni ujasiri mkubwa uliomvaa, ujasiri uliomwondolea ule moyo wa huruma ambao humtawala na kumfanya asite kuitekeleza azma yake yoyote kabla ya kupata kinywaji cha kutosha.
Haraka alikitwaa kisu kile na kuelekea chumba cha kulala. Huko aliwasha taa, macho yakivinjari hapa na pale kisha akatoka bila ya kuzima taa hiyo. Akaingia stoo ambako hakuchukua hata sekunde tano, akatoka. Muda wote huo alikuwa akitafuta chumba au sehemu ambayo alidhamiria kujificha kabla ya kufanya kazi yake.
Hatimaye aliamua kutumia chumba kilekile cha malazi, chumba maalumu kwa malazi ya Machibya na Sarah. Aliporidhika na uamuzi huo, alizima taa ya chumbani na kujilaza kitandani.
Hazikuzidi hata dakika mbili, akashtuka. Masikio yake yalinasa ngurumo ya gari nje ya nyumba. Papohapo akakurupuka kitandani na kulifuata dirisha. Pale aliweza kuliona geti la kuingilia, sawia.
Nyumba hiyo ilikuwa na taa kila kona kwa nje. Isitoshe, pia kulikuwa na taa kubwa yenye mwanga mkali mlangoni, taa ambayo ilipeleka mwangaza wake getini kwa nguvu kubwa. Yeyote ambaye angeingia getini ni lazima angemulikwa na taa hiyo kubwa ya mlango wa sebuleni.
Ni taa hiyo kubwa iliyomrahisishia kazi Kasha; alimwona Sarah akilisukuma geti na kuiacha nafasi kubwa ya kutosha kupitisha watu watano kwa pamoja au gari. Pia, muda mfupi baadaye alifanikiwa kumwona mtu, mwanamume ambaye alikuwa ameketi kiti cha mbele, kushoto ndani ya gari. Sarah alirudi garini na kuliendesha taratibu hadi kwenye egesho lake.
Sasa Kasha aliishughulisha vilivyo akili yake. Hakutaka kosa lolote litendeke, kosa litakalosababisha mkakati alioupanga utibuke, tena utibuke dakika ya mwisho. Hilo lingekuwa ni kosa ambalo angelijutia hata mbele ya Mungu. Na kwa kuwa alijiamini kwa kiwango kikubwa, hakuiona sababu ya kumfanya ashindwe kuitimiza azma yake.
Ashindwe!
Yeye Kasha!
Yeye, ambaye aliogopwa na watu kuliko aogopwavyo Simba au Nyoka? Yeye, ambaye alijiamini kuwa ana akili zaidi ya kumbe yeyote duniani? Yeye, ambaye haogopi silaha yoyote atishiwayo?
Yeye!
Naam, alijiamini. Na alikuwa na sifa moja iliyomfanya ajione yu 'Mungu-mtu.' Alijaaliwa uwezo wa kuwa na shabaha kali pale atumiapo bastola. Lakini alikuwa na shabaha kali zaidi akitumia kisu. Simama hatua kumi au kumi na tano tu mbele yake. Akikurushia kisu kitagota palepale alipopakusudia! Hakukosi!
Kutoka katika mlango wa chumba hicho hadi kwenye mlango mkubwa wa sebule, hazikufika hatua ishirini, japo zilizidi kumi. Kwa umbali huo, Kasha hakuwa na shaka yoyote kuhusu shabaha. Kujiamini kulikuwa palepale!
Akaufungua mlango taratibu na kuacha upenyo mdogo tu wa kutosha kuwaona Sarah na Machibya wakati wakiingia. Kisha akakiangalia tena kisu alichokishika katika kono lake la kulia.
Akatulia!
**********
“ULIACHA taa zikiwaka?” Machibya alimuuliza Sarah mara tu waliposhuka garini. Wakati huo Machibya alikuwa akiangalia sebuleni kupitia madirisha mawili makubwa ambayo wakati huo hayakuwa yamezibwa na pazia.
Ikamlazimu Sarah kulitafuta jibu la haraka. “Umeme. Umeme ulikatika tangu asubuhi, na sikukumbuka kuzima main-switch.”
Likawa ni jibu lililomkata kilimilimi Machibya.
Wakaufuata mlango wa sebule, Sarah mbele, Machibya nyuma. Huku mapigo ya moyo wa Sarah yakienda kasi, kijasho chembamba kikimvuja, mikono ikimtetemeka kwa mbali, tumbo likimuunguruma, aliupachika ufunguo ndani ya kitasa na kujitia kuuzungusha ilhali alitambua fika kuwa haukuwa umefungwa.
Machibya alikuwa gizani. Hakugundua chochote kilichokuwa ndani ya moyo wa Sarah. Hatimaye Sarah akausukuma mlango na kutangulia kuingia.
**********
GARI dogo lililokuwa na askari watatu wakiongozwa na Sajini Kajia lililipita gari la Nissan Laurel lililoegeshwa nje ya geti likaenda kuegeshwa kando ya nyumuba moja iliyokuwa katika duka la bidhaa za rejareja. Kajia akasema, “Nazuga kidogo hapo dukani. Ichungeni gari hiyo.”
Solomon naye akateremka na kuvinyoosha viungo kisha akatoa sigara mfukoni na kuiwasha, macho yake makali yakiliganda lile Nissan Laurel.
Hatimaye Kajia akarudi, soda mkononi, soda ambayo aliinywa kwa pupa, funda hadi funda.
“Vipi, kipi kilichojiri?” aliuliza, macho kamkazia Solomon.
“Wameteremka,” Solomon alijibu. “Lakini, afande, kati yao Kasha hayupo...”
Jicho kali la Kajia lilimnyamazisha Solomon.
“Zibua ubongo wako, Solomon,” hatimaye Kajia alisema. “Ni kweli Kasha hayupo kati yao, lakini kumbuka kuwa ni huyo mwanamke...au tuseme ni hilo gari ndilo lililombeba Kasha kule Maktaba Road! Vinginevyo, unataka niichukulie kauli ya Inspekta kuwa ni kauli ya mwendawazimu.....!”
“Hapana, afande, sina maana hiyo...”
“Ok, rejesha akili yako kwenye mafunzo yako wakati uko CCP.”
Kimya kifupi kikatawala, Kajia akiigugumia soda yake hadi ilipokwisha chupani. Kisha akaitupa chini chupa hiyo. Akawaashiria wenzake wamfuate. Wakati huo alikuwa akiipapasa bastola iliyokuwa mfuko wa kulia wa suruali, na simu, mfuko wa kushoto.
Alifikiria kumpigia simu Inspekta Dismas lakini akasita. Bado alihitaji kuthibitisha kauli ya Dismas, kuwa huyo mwanamke anaweza kuwa msaada mkubwa wa suala wanalolifuatilia. Hivyo, alidhamiria kukutana na mwanamke huyo ana kwa ana, aongee naye kwa kina ili aweze kuchambua na hatimaye kubaini zipi ni pumba na upi ni mchele.
Walipolikaribia geti, Kajia akashtuka, akalitazama geti hilo kwa makini kisha akaangaza macho kwenye ukuta mrefu uliolizunguka jumba hilo, ukuta ambao juu yake kulitandazwa safu tatu za seng'enge sanjari na kibao chenye maandishi: ENEO HILI LINALINDWA NA MITAMBO MAALUMU.
Kajia alishusha pumzi ndefu, akaachia tabasamu la kukata tamaa.
Akawatazama wenzake, kisha akasema, “Jamaa kajiweka sawa kiulinzi. Katandaza umeme. Lakini tusikate tamaa. Twendeni huku.”
Wakaanza kulizunguka eneo hilo. Zaidi ya robo tatu ilijengwa ukuta huo, lakini, nyuma kabisa, sehemu lilipojengwa banda la kuku, ukuta haukuzingira.
Kajia alitoa kifaa kidogo mfukoni na kugusa hapa na pale kisha akanong'ona, “Huku ni shwari. Hajatega umeme, na nadhani hata king'ora hakijategwa. Hata hivyo tuwe makini.”
Akamtazama zaidi Solomon na kuongeza, “Tumia upenyo huo kuingia. Kisha sogea mbele kwa hadhari, ukague kama kuna chochote kibaya. Kama ni shwari, utushtue, tuje.”
Solomon alifuata maagizo hayo, na baada ya dakika kama moja au mbili hivi, alirejea.
“Shwari,”aliwaambia.
Sasa Kajia na dereva waliingia. Kijigiza kilizidi kukomaa, hivyo wakachukua hadhari kufuatia taa zilizokita katika kila pembe ya ukuta wa jumba hilo. Kwa uchunguzi wa haraka na wa uhakika walibaini kuwa hakukuwa na mlinzi yeyote ndani ya eneo hilo.
Taratibu waliufuata mlango wa sebule, hatua zao zikiwa ni za kunyata zaidi ya unyataji wa kawaida.
**********
AKIWA makini, kando ya mlango wa chumba cha malazi, kisu mkononi, Kasha hakutaka kuichelewesha kazi yake. Aliwaacha Sarah na Machibya wavute hatua chache tu, kiasi cha kuweza kumwona Machibya kwa usahihi kutoka kichwani hadi miguuni.
Sarah alipovuta hatua zaidi, Kasha akaamua kutekeleza lengo lake. Kwa wepesi wa ajabu alikirusha kisu kile kwa shabaha kali, akitumia zaidi ya robo tatu ya nguvu za kono lake la kulia! Kilichotokea ni kile kilichokuwa matarajio yake. Kisu kiligota shingoni mwa Machibya na kumpeleka sakafuni huku akitokwa na macho ya mshangao!
Lilikuwa ni tendo lililochukua sekunde chache sana, na halikutofautiana na sinema machoni mwa Sarah. Naam, machoni na akilini mwa Sarah, lilikuwa ni tukio la kushtua, kutisha na kustaajabisha.
“Mamaa! Mamaaa...! Kasha umeua!” Yowe kali lilimtoka Sarah. Angeupata wapi ujasiri wa kustahimili kukaa kimya wakati akishuhudia mwenzi wake akizamishiwa kisu cha shingo, kisu kilichotoa picha ya kuuondoa uhai wake?
Hata hakukumbuka yale maongezi na mapatano yake na Kasha! Kilichotwaa nafasi nafsini mwake ni woga usio kipimo. Akabaki akitetemeka mwili mzima, akimtazama Kasha mithili ya amtazamaye ibilisi mtoa roho za watu!
**********
NDIYO, yowe alilolitoa Sarah lilikuwa kubwa. Halikuishia humo sebuleni, lilipenya kuta na kuyafikia masikio ya Sajini Kajia na wenzake waliokuwa hatua chache kutoka mlangoni.
“Afande!” Solomon alibwata kwa mnong'ono huku akimtazama Kajia kwa macho makali.
Kajia hakuitika, tayari alishaichomoa bastola yake na kuishika kwa mkono wa kulia. Sekunde ya pili alikwishausukuma mlango kwa teke la nguvu, na kwa kasi ya ajabu akaivaa sebule hiyo huku akifuatwa na wenzake.
Papohapo macho yao yakaufikia mwili wa Machibya uliokuwa sakafuni ukitokwa damu nyingi, kisu kikiwa kimezama shingoni kwa namna ya kutisha. Haraka Kajia akayahamisha macho kutoka kwenye mwili wa Machibya.
Akamwona Kasha ambaye tayari alishaanza kurudi chumbani. Kwa kasi ileile ya kutisha akauinua mkono na kufyatua risasi mbili kwa shabaha kali, risasi zilizotua kwenye paji la uso wa Kasha, zikamrusha juu na kumtupa chini chali huku ubongo wake ukichuruzika sakafuni mithili ya uji wa moto!
**********
TANGU Inspekta Dismas alipotaarifiwa kuwa gari lililokuwa likisakwa limeonekana katikati ya jiji, akili yake haikutulia. Sofa halikukalika wala soda haikunyweka tena. Alikuwa akizunguka hapa na pale sebuleni mwake, shauku ya matokeo ya maagizo aliyotoa ikiwa imemjaa.
Alitamani kumpigia simu Kajia baada ya kuona imepita zaidi ya nusu saa bila ya kutaarifiwa chochote kingine. Lakini alisita, akaamua kuvuta subira huku moyo ukiwa juu. Naam, hatimaye simu yake iliita. Akaitazama kwenye kioo na kuliona jina: KAJIA likielea.
Haraka akabonyeza kitufe fulani na kuitega sikioni. “Sema!” alitamka kwa sauti iliyofurika udadisi.
“Tumempata!”
“Nini?!”
“Tumempata, afande!” Kajia alirudia, safari hii kwa msisitizo.
“Ni Kasha?!”
“Yeah, ni mwenyewe.”
“Yaap!” Inspekta aliachia tabasamu la dhati, usowe ukionyesha matumaini makubwa ya kulikamilisha lengo lake. Akaongeza, “Sajini, hapo mmefanya la maana. Ni kazi nzuri....”
“Lakini...”
“Enhe, vipi tena?”
“Hatukumpata akiwa hai.”
“Unasema?”
“Nasema, hatukumpata akiwa hai!” Kajia alisisitiza.
“Kwa nini, alileta kujua?”
“Nd'o maana'ake, afande! Tulimkuta nd'o kwanza ameua mtu kwa kisu! Ikatulazimu tumwashe za uso!”
Kimya kifupi kikatawala. Kisha Inspekta akasema, “Aah, s'o mbaya. Kifo cha jambazi mmoja ni nafuu kwa mamilioni ya Watanzania wapenda amani.”
Ukimya mwingine ukapita, kisha Inspekta Dismas akaibuka tena. “Enhe, na yule mwanamke?”
“Tuko naye. Yuko chini ya ulinzi. Tunakwenda naye kituoni.”
“Good.”
***MWISHO***
*****RIWAYA HII IMEISHIA HAPA. HUENDA ITAULIZWA HUYO SARAH AMEISHIA VIPI BAADA YA KUCHUKULIWA NA POLISI? JIBU LIKO WAZI SANA…NAAMINI HATA WEWE MSOMAJI UNAWEZA KUJUA NI KIPI KITAKACHOFUATA. TUNAWASHUKURU SANA.*****
0 comments:
Post a Comment