Search This Blog

Tuesday, 14 June 2022

DOMO LA MAMBA - 1

 





    IMEANDIKWA NA : INNOCENT A. NDAYANSE (ZAGALLO)



    *********************************************************************************



    Simulizi : Domo La Mamba

    Sehemu Ya Kwanza (1)



    DAKIKA tano zilishapita tangu msichana huyo mrembo alipomaliza kuoga. Tayari alishajifuta maji kwa taulo zito jekundu. Sasa alikuwa akijitazama kupitia kioo kirefu kilichokuwa ndani ya bafu hilo. Akalishuhudia vyema umbo lake lililokuwa tupu kama alivyozaliwa. Akaridhika kwa kupata nywele nyingi na nyeusi tii, nywele zilizomwagika hadi mabegani, na hivyo kumfananisha na mrembo yeyote mwenye asili ya Uajemi.

    Alimshukuru Mungu kwa kumpatia umbo la wastani; si mnene si mwembamba. Rangi yake ya maji ya kunde alikiri kuwa ndiyo pekee iliyomfaa. Macho yake malegevu, pua yenye ukubwa wa wastani na mdomo wenye muundo uwavutiao wakware, ni viungo vilivyomfanya atabasamu peke yake bafuni humo kadri alivyozidi kujitazama kwenye kioo hicho kirefu, moyoni akijisifu kwa kujaaliwa uzuri huo.

    Alijipapasa kutoka kifuani hadi nyayoni, akivipitisha viganja vya mikono yake laini katika milima na mabonde ya mwili huo uliovutia. Akarudi nyuma hatua mbili, akijinyonganyonga mithili ya mlimbwende azungukaye jukwaani katika mchuano wa kumsaka kinara wa ulimbwende. Hakuishia hivyo; alivuta hatua tatu mbele, kwa maringo yaleyale, uso kauelekeza kwenye kioo, akitaka kushuhudia jinsi anavyoonekana mitaani pale atembeapo kwa mtindo huo.

    Akageuka na kuvuta hatua tatu kwa mtindo huohuo, lakini safari hii akiigeuza shingo yake na kulitazama umbo lake la nyuma kupitia kioo hichohicho. Tabasamu lake likakua, akifurahia usanii wa Mungu kwa jinsi alivyolifinyanga umbo hilo, na akajiweka katika kundi la wasichana walio katika daraja la kwanza au la pili kwa uzuri.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Mara tabasamu lake likageuka kicheko. Akacheka kwa sauti ya chini. Hakuwa na shaka kuwa wanaume wengi humtazama kwa matamanio kila anapopishananao, huku, kama wasioamini wakionacho, huzigeuza shingo zao na kulikodolea macho umbo lake la nyuma, macho yao yakivutwa na robota la kiuno chake.

    Mrembo huyo hakuwa mwingine, bali ni Fatma Mansour, ambaye asili ya uzawa wake ni katika kisiwa cha Unguja, Tanzania- Zanzibar.

    Historia ya Fatma inaanzia miaka ishirini na mitano iliyopita, wakati mama na baba yake walipoamua kuikimbia Unguja kufuatia tetesi zilizozagaa visiwani humo; kwamba, miaka michache ijayo, utawala wa Ki-sultani ungerejea.

    Wengi waliijua historia ya utawala wa Ki-sultani, utawala uliokuwepo kabla ya mapinduzi ya Zanzibar, baba yake Fatma, mzee Abdilatif Mansour akiwa ni miongoni mwa walioijua ladha ya shubiri ya utawala huo.

    Akiwa ni Mzanzibar mwenye akili timamu, hakuwa radhi utawala huo urejee baada ya kuutokomeza mnamo mwaka 1964. Kuzagaa kwa tetesi hizo kulimfanya mzee Abdilatif achukue uamuzi wa haraka wa kuikimbia Unguja.

    Baada ya siku tano za maandalizi na mawasiliano na nduguye aliyekuwa akiishi Tanzania Bara, wilayani Kibaha, kitongoji cha Maili Moja, siku ya sita aliondoka na mkewe kwa jahazi hadi bandarini Dar es Salaam.

    Kutoka hapo Dar, alitumia gari la nduguye hadi huko Kibaha ambako walipata makazi ya muda kwa huyo nduguye. Wakati huo mkewe Abdilatif alikuwa na mimba iliyopiga hodi kwenye miezi tisa. Ni miezi miwili tu aliyoishi hapo, iliyotosha kuleta sura mpya katika familia ya smzee Abdilatif Mansour. Alizaliwa mtoto, mtoto mzuri wa kike, mtoto ambaye siku chache baadaye akapewa jina la Fatma. Akawa ni Fatma Mansour.

    Mwaka mmoja baadaye, familia hiyo ilihamia jijini Dar es Salaam, kitongoji cha Tegeta ambako walipanga vyumba viwili. Waliishi hapo kwa takriban miaka sita kabla Mungu hajawakomboa kutoka katika maisha ya upangaji.

    Akiishi kwa malengo, Mzee Abdilatif alijitahidi kulimbikiza pesa kidogokidogo hadi akafanikiwa kununua nyumba hafifu katika kitongoji hichohicho. Sasa akatulia. Akawa na uhakika wa kujipatia riziki kupitia biashara ya kijiduka kichanga alichokifungua hapohapo nyumbani kwake.

    Miaka ikaenda, hatimaye mtoto Fatma akaanza masomo ya elimu ya msingi. Miaka saba baadaye akafikia tamati ya elimu hiyo na kujikuta akiwa miongoni mwa waliochaguliwa kujiunga na elimu ya sekondari. Shule aliyopangiwa ni Zanaki, hapohapo jijini Dar.

    Ni wakati akikaribia kufanya mtihani wa mwisho, akiwa kidato cha nne, ndipo balaa lilipozuka. Mzee Abdilatif alikumbwa na maradhi ya kifua, maradhi yaliyomwondoa duniani wiki mbili baadaye katika hali iliyowasononesha wengi; majirani, ndugu na jamaa huku mkewe akiwa ameathirika kisaikolojia kwa kiwango kisichokadirika.

    Kuanza mfumo mpya wa maisha, bila ya mwenzi wake, lilikuwa ni zoezi jipya na gumu kwa mama yake Fatma ambaye alijiona kama anayeelea hewani, ndani ya shimo lenye kina kirefu na chini akilakiwa na kiza cha kuogofya. Hakuwa na moyo wa ujasiri, hivyo, ile hali ya kusumbuliwa na mawazo kwa kipindi kirefu ilizidi kumsononesha kwa kiasi kikubwa. Afya yake ikadhoofika kwa kasi kila kukicha. Hatimaye ikatokea siku ambayo hakuamka asubuhi!

    Kilikuwa ni kifo cha ajabu na cha kistaarabu. Usiku wa jana yake alikuwa mzima wa afya, akizungumza kama kawaida na akala kama kawaida. Hata alipoingia kulala hakuonyesha kuwa alisumbuliwa na maradhi yoyote. Lakini siku ya pili ndipo yalipojiri hayo yaliyojiri!

    Fatma akabaki yatima!



    *****

    MSICHANA Fatma alijikuta katika hali ngumu zaidi. Wakati mama yake alipofariki, yeye alikuwa amebakiza mtihani wa mwisho wa kidato cha nne. Tukio la kifo cha mama yake lilimwathiri kiasi cha kushindwa kuendelea na mahudhurio shuleni. Kwa hali hiyo, hata mtihani hakufanya. Akaingia katika maisha mapya. Sasa akawa akiishi kwa hisani ya marafiki na vijana wa kiume waliomhonga vijisenti vya kula. Hatimaye akaamua kuzunguka huku na kule akisaka ajira. Fedha kidogo alizokuwanazo zikawa zikihamia kwa makondakta wa daladala na mama lishe. Takriban kila siku akawa akihangaika ofisi hii na ile akisaka ajira bila ya mafanikio.

    Kuna baadhi ya waajiri ambao walihitaji vyeti vyake vya shule; hakuwanavyo. Wengine walitaka kujua kama ana uwezo wa kutumia kompyuta; kikawa kikwazo kingine. Pia, kuna ambao walihitaji kujua kama ana fani yoyote aliyoimudu mathalani ukatibu muhtasi, uhudumu wa mapokezi, ukarani wa masijala, uhasibu na kadhalika na kadhalika; zote hizo zikamtupa.

    Nani angemwajiri?CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Hata hivyo, pamoja na kukosa vigezo hivyo vya kitaalamu, sura yake na umbo lake vilikuwa vivutio vikubwa machoni na akilini mwa hao waajiri. Hivyo, hawakumwacha hivihivi, walimtupia maneno mawili, matatu ya kumtaka kimwili. Matokeo yake alijikuta akimkubali meneja wa kampuni moja kwa makubaliano ya kupata ajira, lakini baada ya wiki moja ya kuchezewa, hatimaye alitemwa mithili ya kapi la muwa.

    Naye Mkurugenzi wa kampuni moja ya simu akamwahidi kazi nzuri, yenye mshahara mnono na marupurupu kibao. Lakini huyo naye, kama yule meneja, alistarehe naye katika hoteli moja maarufu kwa siku mbili tu kisha akamwepuka.

    Sasa Fatma Mansour akawa ni mtu wa kuhangaika, mahangaiko ambayo yalimfanya afikie hatua ya kuanza kukata tamaa. Kutupwa kitandani leo na meneja, kesho mkurugenzi, keshokutwa mhasibu, na siku nyingine kuli wa bandarini, kibaka, jambazi na kadhalika, yalikuwa ni maisha ambayo hakuyapendelea japo aliyaendesha kwa mfumo uliomridhisha kila aliyebahatika.

    Hakukosa kuzivaa kumbi mbalimbali za starehe, ambako mvuto wa sura na umbo lake ni vigezo vilivyompatia mwanamume wa kumpatia chochote. Ilikuwa ni kazi iliyomwingizia pesa, lakini pia ikiwa ni kazi ngumu, iliyomlazimu kuzifumbia macho kero zilizompata. Mstaarabu ‘alimkatia pochi’ baada ya starehe, mwungwana alimlipa kabla ya huduma, na, ‘chizi’ alimuaga kwa kejeli, matusi hata kwa kumtemea mate pindi tu alipohitimisha burudani yake.

    Ni Beka Bagambi aliyemtoa katika mfumo huo wa maisha. Walikutana kando ya Barabara ya Ufukoni, jirani na Jolly Club, saa 4 usiku. Fatma akiwa ndani ya T-shirt nyeupe na suruali nyeusi ya kitambaa chepesi, alikuwa akiangaza macho kutoka kwa mwanamume huyu hadi yule, akitarajia kuitwa na mmojawao ili wakastarehe kwa makubaliano maalumu.

    Ndiyo kwanza Beka Bagambi alikuwa akitoka ndani ya ukumbi wa Jolly, akilifuata gari lake la kifahari, Jeep Cherokee la Marekani ili arejee nyumbani kwake Masaki. Toti kadhaa za pombe kali alizogida huko ukumbini zilikwishaichangamsha akili; kilichobaki ni kwenda kulala. Ni wakati alipokwishaingia garini na kutumbukiza ufunguo kwenye swichi, ndipo alipomwona mrembo wa haja akimjia.

    “Habari yako, kaka,” alisalimiwa.

    “Poa tu. Vipi?” Beka Bagambi alimhoji huku akilitalii umbo lake ambalo tayari alikiri kuwa ni umbo linalovutia na kusisimua.

    “Shwari tu,” sauti laini ya mrembo huyo ilipenya masikioni mwake. “Unaonaje kama tutastarehe wote usiku huu?” mrembo aliongeza.

    Tayari Beka akamtambua vizuri mrembo huyo. Ni malaya! Anafanya biashara ya kuuza mwili wake! Akamtazama kwa makini; hakuwa ni mwanamke aliyestahili kuifanya kazi hiyo. Sura yake nzuri, macho yake yaliyobembeleza na kushawishi, na umbo lake lililojazia vyema, vilitoa taswira ya mama wa nyumbani, anayetunzwa na mwanamume anayejua jinsi ya kumtunza mke. Siyo kuja huku barabarani na kuunadi mwili wake mzuri, akidiriki kumchojolea nguo kila mwenye pesa huku akiwa tayari kutendwa vyovyote kulingana na thamani ya pesa alizolipwa.

    Ni mzuri, Beka alijisemea kimoyomoyo huku akiendelea kuutalii mwili wa mrembo huyo kwa macho yenye uchu wa matamanio.

    “Ingia twende,” hatimaye alimwambia.

    Mrembo Fatma alizungukia upande wa pili. Akafungua mlango na kuingia garini. Gari likasaga lami kuelekea Masaki, nyumbani kwa Beka ambako hadi kunapambazuka hawakuwa wameambua walao lepe la usingizi.

    Ndivyo uhusiano wao ulivyoanza.

    *****



    ALIPOTOSHEKA na zoezi la kujitazama kwenye kioo cha bafuni humo, akajifunga taulo hilo zito kiunoni kisha akatoka. Moja kwa moja hadi chumbani ambako alimkuta Beka kajilaza kitandani chali, mtupu kama alivyozaliwa, macho kayakodoa darini. Fatma alimfuata na kujilaza kando yake. Joto la mwili wake mwororo likamfikia Beka sawia kiasi cha kumfanya amkumbatie kwa nguvu. Nyuso zao zikasogeleana. Wakatazamana, macho ya kila mmoja yakiongea jambo fulani kwa namna ya ushawishi.

    Sasa mikono yao ikafanya kazi nyingine, zaidi ya kukumbatia. Ilishika, ikaminya na kutomasa hapa na pale, Fatma akiwa kinara wa zoezi hilo, akiwa ni mtaalamu anayejua wapi pashikwe vipi, wapi paminywe vipi na wapi patomaswe vipi. Hatimaye wakaikutanisha midomo yao, tendo lililompagawisha Beka kwa kiwango kikubwa, ilhali kwa Fatma lilikuwa ni tendo dogo tu, tendo la kawaida, ambalo kwa kipindi hicho halikumtia msisimko wowote.

    Ndiyo, kwa Fatma lilikuwa ni jambo la kawaida sana kwake. Alishakumbana na midomo mingi ya wanaume; mikubwa kwa midogo na michafu kwa misafi. Hivyo, alichokifanya hapo ni kumwehusha tu Beka na kuudhihirisha umahiri wake katika michezo ya mahaba.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Punde Beka akakurupuka na kumvaa, akionyesha dhahiri kuhitaji tena. Naye Fatma hakuwa na hiyana, alimpokea kwa namna iliyomfanya ajihisi yu katika sayari nyingine.

    Dakika kumi baadaye walitengana tena. Kwa mara nyingine wakatazamana, safari hii mboni za macho yao zikiwa na neno asante.

    Ni wakati huo, Beka alipojikuta akishangazwa na jambo moja. Tayari ilishakatika wiki moja tangu usiku ule wa kwanza alipomzoa Fatma kule Jolly Club.

    Hata hivyo, pamoja na kuvitesa viungo vyao kila usiku, na kila alfajiri, bado alikuwa akimwona Fatma kama mwanamke mgeni kwake. Ni hilo lililomshangaza. Sasa akajikuta akiingiwa na mapenzi ya dhati. Alihitaji kuwa naye kila wakati! Siyo kwamba alikuwa mchanga katika fani ya kustarehe na wanawake warembo, la hasha. Wengi walishaangukia kitandani kwake, na wengi kati ya hao walijitahidi kujionyesha walivyo wataalamu katika kumstarehesha mwanamume rijali.

    Huyu Fatma ni zaidi yao, Beka alikiri hivyo. Wala haikuwahi kumwingia akilini kuwa ipo siku atakayomwacha kama ilivyotokea kwa waliotangulia. Alitaka huyu awe ndiye mama wa nyumbani.





    Mara wakakumbatiana tena.

    “Beka…Beka…” Fatma aliita kwa mnong’ono.

    Beka hakuitika, badala yake alimbusu shavuni.

    “Beka…nakupenda Beka…”

    Ilikuwa ni kawaida ya Fatma kumtamkia hivyo mwanamume yeyote pindi wafikapo kileleni mwa starehe. Kwa Beka Bagambi, hilo lilikuwa ni tamko lililopenya moyoni na kuchipua mfereji wa furaha kiasi cha kumfanya na yeye aamue kuonyesha ni jinsi gani alivyojua kupenda.

    “Mpenzi, naona ile Chaser inakufaa,” alimwambia na kuongeza, “kuanzia sasa ni mali yako.”

    “Mmh! Ya kweli hayo?” Fatma alimtazama Beka kwa namna ya kutomwamini.

    “Ni vizuri pia wazazi wako wakawa na nyumba ya kisasa,” Beka akauendeleza umwamba wake. “Jaribu kuwasiliana nao, wakwambie wanapendelea kuishi wapi, kama ni huko Unguja au hapa Dar, uamuzi ni wao.”

    Ni hapo Fatma alipokumbuka kuwa kiasi cha wiki moja iliyopita Beka alimwuliza juu ya historia ya maisha yake; na kwa kuwa tayari alishakuwa na mazoea ya kuwalaghai wanaume, takriban kila alichomwambia Beka hakikukosa chembe ya uongo. Miongoni mwa kauli hizo zilizosheheni uongo ni kumwambia kuwa wazazi wake wako Unguja na hali zao siyo nzuri kimaisha.

    “Wanaishi kwenye kijumba kibovubovu kinachovuja kila mvua inaponyesha,” ndivyo alivyomwambia na kuongeza, “Hata kula yao inanitegemea mimi. Nisingependa kujiuza, lakini ningefanya nini ili wazazi wangu wapate walao mlo mmoja kwa siku?”

    Uongo wake huo ulikuwa ni ukweli akilini mwa Beka Bagambi. Hivyo, akaahidi kuwajengea nyumba ya kisasa, tamko lililomfanya Fatma aduwae kwa muda, asiamini akisikiacho Akajihisi yu ndotoni.

    “Nadhani pia itakuwa vizuri kama na wao watakuwa na gari lao,” Beka aliongeza.“Nitawatafutia dereva nitakayemlipa mshahara.”

    “Hak’ya nani?” Fatma aliropoka, macho kayatoa pima.

    “Na wewe nitakufungulia saluni ya kisasa pale Namanga, Msasani.”

    “Beka..!”

    “Itakuwa saluni ya nguvu. Haitatofautiana sana na saluni moja niliyoiona Karachi, Pakistan.”

    “Beka…Beka…nakupenda, Beka…” Fatma alibwata kwa mnong’ono kama aliyepagawa. Akamkumbatia Beka kwa nguvu zaidi.

    Kwa takriban dakika mbili walikuwa kimya, na ni wakati huo Fatma alipojiwa na picha nyingi kichwani mwake. Miongoni mwa picha hizo ni kujiona akiwa ndani ya gari la kisasa, Toyota Chaser akiliendesha huku akiwa na kadi inayomhalalisha umilikaji wa gari hilo, kuishi ndani ya jumba kubwa la kifahari ufukoni mwa bahari na hati za umilikaji wake zikiwa na jina lake, kumiliki shamba kubwa la minazi na mikorosho huko Bunju pembezoni mwa jiji, na kumiliki hoteli kubwa yenye hadhi ya juu ufukoni mwa bahari eneo la Kigamboni.

    Hakujua jinsi hayo yote yatakavyoweza kufanikishwa, lakini alijenga imani kuwa mawili au matatu kati ya hayo yatafanikishwa kwa mgongo wa Beka. Lini na kwa namna gani, hilo lilikuwa ni jambo jingine, jambo ambalo kwa wakati huo hakupenda kukisumbua kichwa chake kulifikiria.

    Hayo yalikuwa kichwani mwa Fatma. Hakujua yaliyokuwemo kichwani mwa Beka. Beka, ambaye katika ukimya huo, naye alikwishayapeleka mawazo yake mbali, akizirejesha kumbukumbu za mbinu zilizomfanya afanikiwe kupata fedha nyingi kwa kipindi kifupi kiasi cha kujiona yu miongoni mwa matajiri wadogo wa jiji la Dar es Salaam.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/



    ******



    MIAKA mitatu iliyopita, Beka aliondoka nchini Tanzania na kwenda Pakistan kwa kudandia meli kubwa ya mizigo, LINEA MESSINA, bandarini Dar es Salaam. Alibahatika kunusurika kutoswa baharini tofauti na vijana wengine wanne waliofumwa ndani ya vyumba vya meli hiyo. Huko, aliishi kwa baharia mmoja ambaye urafiki wao uliota mizizi tangu wakiwa safarini. Miezi miwili baadaye, baharia huyo akampa kazi ya roho mkononi; kusafirisha dawa za kulevya katika nchi kadhaa za Bara la Asia. Kwa muda wa miaka miwili akawa akifanya biashara hiyo ya kutisha. Kuzimeza pakiti kadhaa za dawa hizo na baadaye kuzitoa kwa njia ya haja kubwa, kwake likawa ni jambo la kawaida.

    Pamoja na kwamba yeye ndiye aliyekuwa mtendaji mkuu, pamoja na kwamba alifanya kazi hiyo kwa uadilifu mkubwa, hata hivyo ni yule baharia aliyenufaika huku Beka akiambulia vijisenti visivyomfikisha popote zaidi ya kula na kunywa.

    Ulikuwa ni mfumo wa maisha ambao Beka hakuutarajia wala kuupenda. Sasa picha moja ikamjia akilini, picha ya kufia huko Pakistan huku akiwa hohehahe au kukamatwa na kutupwa jela ambako ama angehukumiwa kifungo cha maisha au kifo. Hakuwa tayari kuyamalizia maisha yake kwa rekodi mbaya, hivyo, alipanga kuchukua uamuzi ambao aliamini kuwa ungemsaidia kumtoa katika minyororo ya ufukara ili na yeye awe mtu kati ya watu.

    Aliamini kuwa, kiwango chake cha elimu ya kidato cha sita kingeweza kumvusha katika mabonde na milima ya dhiki na umaskini uliomwelemea. Aliamini kuwa Kiingereza ndiyo lugha kuu duniani, hivyo popote ambako angekwenda asingekosa wa kuongea naye, wala asingeshindwa kuvuka vikwazo vyovyote.

    Wakati akijiwa na wazo hilo, baharia alikuwa safarini, na alitarajiwa kurejea baada ya mwezi mmoja. Hivyo, Beka aliona kuwa hicho kilikuwa kipindi mwafaka kwake katika kutekeleza lolote lile alilolidhamiria.

    Ndipo ikaja siku. Ilikuwa ni asubuhi, saa 4, alipotoka kuchukua dola 800,000 za Marekani kwa tajiri mmoja katikati ya jiji la Karachi, fedha hizo zikiwa ni sehemu tu ya malipo ya dawa za kulevya ambazo tajiri huyo alizichukua kiasi cha juma moja lililopita. Tofauti na safari zilizopita, safari hii pesa hizo hazikumfikia mke wa baharia na wala hakumtaarifu chochote kuhusu fedha hizo. Alizificha chumbani mwake na kuanza kufanya mkakati wa kutoroka.

    Siku ya tatu alikuwa angani, ndani ya ndege ya Shirika la Ndege la Uswisi, na baada ya kupita nchi kadhaa, hatimaye ndege hiyo ilitua jijini Nairobi. Hapo alijihifadhi kwa siku mbili kabla ya kuikwaa ndege nyingine iliyomshusha jijini Dar es Salaam. Alipozibadili zile dola, akajikuta akimiliki shilingi bilioni 1 na ushei za Tanzania. Kwa kiwango hicho cha pesa, hakupata shida kupata nyumba Masaki na kununua magari mapya matatu kwa mkupuo: Jeep Cherokee, Mercedes Benz 560 SEC na Toyota Chaser.

    Hakuwa na wasiwasi wa maisha. Tayari alishajiunga katika mtandao wa wafanyabiashara wengine waliokuwa wakijihusisha na ununuzi, uuzaji na hata usafirishaji wa dawa za kulevya baadhi yao wakiwa nchini Tanzania na wengine Uganda.

    Alichokuwa anataka kukikamilisha ni kusajili kampuni ya usafirishaji, kampuni ambayo itakuwa na ofisi kubwa yenye kila kinachohitajika ilhali ukweli ni kwamba itakuwa ni kampuni hewa ndani ya ofisi hewa. Hakutakuwa na chochote kitakachofanyika kuhusiana na usajili wa kampuni hiyo, zaidi ya kuiendekeza biashara yake ya dawa za kulevya.

    Wakati akijiandaa kuanza harakati zake na mtandao wake ilibidi aendelee na mambo mengine. Na miongoni mwa hayo mambo mengine ni kula bata. Kwa hali hiyo, ili aweze kuyafaidi maisha kwa jinsi atakavyo, hakukosa kuwachukua warembo wawili, watatu kwa siku tofauti na kuachana nao kila walipomkinai. Miongoni mwao ni huyu Fatma Mansour, mwanamke mrembo aliyenaye kitandani, wakifanya hili na lile katika kuzikonga nyoyo zao. Lakini, huyu bado anampenda na haikumwingia akilini kuwa ipo siku atakayomchoka.

    Mara akayarejesha mawazo yake pale kitandani na kumtupia macho Fatma. Akamshukuru Mungu kimoyomoyo kwa kumpatia zawadi hiyo ya aina yake; mwanamke mrembo, ajuaye ni kipi anachokihitaji mwanamume rijali pindi akutanapo na mwanamke mzuri.

    Akalipapasa paja kubwa, paja lililonona la Fatma. Hatimaye mkono huo ukatambaa hadi katikati ya miguu ambako ulikifanya kile kilichomfanya Fatma ashindwe kustahimili; akaguna na kuutoa kistaarabu huku akimtazama Beka kwa macho ambayo ni kama vile yalimwambia, Acha kunitesa, mwenzio.

    “Beka,” hatimaye Fatma aliita, sauti yake ikiwa na kijiuchovu cha mbali.

    Beka hakuitika, badala yake alimtazama kidogo huku akiachia tabasamu la mbali.

    “Beka,” Fatma alirudia, safari hii sauti yake ikiwa thabiti japo ilikuwa ya chini.

    “Vipi, mpenzi?”

    “Hivi kweli unanipenda, Beka?”CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Kwa nini unaniuliza hivyo?” Beka alimkazia macho.

    “Tafadhali, jibu kwanza swali langu,” Fatma alisisitiza.

    “Kwani vipi, huniamini?” Beka alishangaa.

    Akilini mwa Beka, aliamini kuwa, katika kumthibitishia mpenzio kuwa unampenda, yakupasa ufanye naye mapenzi kwa nguvu zako zote, ukitumia hata akiba ya ujuzi ulionao. Hivyo ndivyo alivyofanya yeye dakika chache zilizopita, lakini bado Fatma hakuonyesha kuridhika. Si ajabu kwa mtu kama huyo kutoridhika. Ni wanaume wangapi waliofanya naye mapenzi, wakitumia hata akiba ya nguvu na ujuzi wao hadi mijasho ikawatiririka lakini wasiwe hata na chembe ya mapenzi mioyoni mwao? Ni wengi. Na kuna wale ambao mara tu walipovaa nguo zao na kumtupia shilingi 5,000 au 10,000 hawakuwa na muda wa kumtazama tena!

    Huyu Beka Bagambi ni kati ya wanaume wachache walioonyesha kumpenda pendo la dhati kwa macho, kwa vitendo na kwa ahadi. Hata hivyo, yote hayo hayakuwa vigezo tosha vya kumfanya Fatma awe na imani nao. Walijituma kwa kila hali pindi walipojitupa kitandani, wakavitumia viungo vyao kikamilifu katika kumdhihirishia kuwa ni marijali, wakayatumia macho yao kubembeleza na kushawishi, na, walikuwa wepesi wa kutumia ndimi zao kuahidi zawadi hii na ile, ahadi zilizoendelea kuwa ahadi hadi leo, na labda hadi kesho.

    Beka alikuwa ni mtu wa kumi na tisa aliyeonyesha kumpenda kivitendo, kwa macho na kwa ahadi. Atamwamini vipi wakati hajampa chochote cha maana, zaidi ya shilingi 10,000 au 20,000 hadi 50,000 pindi alipodiriki kumpa mitindo fulani ya mapenzi, mitindo ambayo huitoa kwa nadra sana, tena kwa gharama kubwa?

    “Ni kipi kinifanye niamini kuwa unanipenda?” hatimaye alimuuliza. “Kunitupa kitandani kila mara ndiyo kigezo unachotegemea nikitumie kama kipimo cha kunipenda? Au kwa kuwa umenifundisha kuendesha gari? Au kwa kuwa nimekaa zaidi ya mwezi hapa kwako? Au kwa kuwa umekuwa ukinipa pesa kila ninapokuvulia nguo? Au kwa kuwa umekuwa ukinitoa auti kila jioni?”

    Akasita kidogo kisha akacheka. Hakikuwa kicheko chenye chembechembe zozote za upendo wala furaha. Hiki kilikuwa ni kicheko cha dhihaka, na alikikata ghafla, akaendelea, “Labda. Labda unanipenda. Lakini nafsi yangu bado inaamini kuwa yote hayo umeyatenda kama kunilipa ujira wa huduma ninayotoa kwako. Bado unanichukulia kama malaya tu! Na huenda unanichukulia hivyo kwa kuwa huwa nakuruhusu ukitumie kila kiungo cha mwili wangu kwa starehe yako.

    “Beka, kabla hujanitoa kwenye minyororo ya umalaya wa barabarani, nilikuwa nikikutana na wateja wa aina mbalimbali. Baadhi yao walikuwa wepesi wa kuhonga elfu thelathini hata hamsini kwa starehe kama hizi ninazokupa wewe. Walinipendea hicho tu; kufanya nao mapenzi, tena wengi wao wakipenda mapenzi kwa njia haramu. Nadhani wewe ni tofauti na wao. Naziona chembechembe chache za mapenzi katika macho yako, kauli zako na labda pia kwa huduma zako za ziada.

    “Lakini, hata hivyo, Beka, ukiwa ni tofauti na hao wengine waliokuwa wakinichukua leo, na kesho wananitazama kama malaya wengine, wewe unapaswa kunifanyia jambo lolote litakalokuweka katika daraja tofauti na hao wengine waliopita. Nipe zawadi itakayonifanya kuanzia sasa niamini kuwa hukunilazimisha nitoke barabarani ili tu uwe na wasaa mzuri wa kunitumia, bali ulikuwa na penzi la dhati kwangu, penzi la moyoni.”

    Beka alishangazwa na maneno hayo. Papohapo akamuuliza, “Lakini mbona nimeshakuahidi mengi sasa hivi tu?”

    “Ndiyo, umeniahidi. Ahadi hiyo siyo ya kutekelezwa leo. Nahitaji chochote kile unachoweza kunitekelezea sasa hivi.”

    “Ok,” Beka aliitika huku akijitoa kitandani. Akaifuata kabati na kuifungua saraka moja ambako alitoa kitabu cha hundi. Akakishika kwa sekunde chache kisha akakirudisha sarakani na badala yake akachomoa bunda moja la noti lililofungwa na mipira.

    Akamkabidhi Fatma huku akisema,”Ni shilingi milioni moja. Ningekuandikia cheki lakini nadhani bado utahisi nakuhadaa kwa kukupa cheki feki. Hizi ni zako, uzitumie upendavyo; hazihusiani na ahadi nilizokwishakupa; sawa mpenzi?”

    Fatma alizipokea pesa zile bila ya kutamka chochote. Kwa sekunde kadhaa akashindwa kuyaamini macho na masikio yake. Tabasamu hafifu likamtoka. Akajiona yu mwizi, tapeli au sifa yoyote ifananayo na hizo. Maishani mwake, tangu akumbane na mwanamume wa kwanza aliyemwonjesha dunia ya mapenzi, kisha wengine wengi wakafuatia, hadi huyu aliyenaye kitandani, hakuwahi kutokea mwanamume aliyempatia zaidi ya shilingi 50,000.

    Huyu Beka ni wa kwanza kumpatia kiasi kikubwa zaidi cha pesa, akidhihirisha ni kwa kiwango gani anampenda. Akamhurumia! Kwa ujumla, moyoni mwake hakuwa na upendo wowote kwake! Bado hakukijua kitu mapenzi. Mapenzi! Ni ndege wa aina gani? Ni mtu wa aina gani? Au, ni mdudu wa aina gani? Ukweli ni kwamba mapenzi hayakuwamo nafsini mwa Fatma bali alimthamini Beka kutokana na fadhila zake tu!





    “Fatma…nakupenda sana, Fatma,” Beka alinong’ona mithili ya alalamikaye. Akaongeza, “Amini…amini, tafadhali, kuanzia sasa, chochote kilicho ndani ya uwezo wangu nitakutimizia. Naomba uamini nikwambiayo. Siyo kwamba natamka hivyo kutoka kinywani tu; hapana, yanatoka moyoni.”

    *****



    UKUMBI wa DDC Kariakoo ulikuwa na watu wengi jioni hii ya Alhamisi. Takriban kila mmoja alionekana kujawa na furaha. Kila meza ilizungukwa na watu wanne au watano waliokuwa na vinywaji mbele yao. Ukiachilia mbali wale waliozijali bia zao, walikuwepo wengine, wanawake,waliojipitisha huku na kule, wakizijaribu bahati zao kwa wanaume wakware.

    Mijimama hiyo yenye maumbile makubwa hujitokeza zaidi ukumbini hapo siku kunapokuwa na burudani ya muziki wa taarabu. Usiku wa siku hiyo kulitarajiwa kuwa na muziki wa kundi moja maarufu la muziki huo wa taarabu, kundi lililotokea kujizolea mashabiki lukuki kutoka pembe zote za jiji la Dar es Salaam. Kwa ujumla ukumbi wote ulikuwa umechangamka; kila aliyeingia, kila aliyetoka wote walijawa na furaha.

    Katika meza moja kulikuwa na wanaume wawili waliokuwa wakinywa bia taratibu. Japo nyuso zao zilionekana kupambwa na tabasamu za mara kwa mara, hata hivyo alihitajika mtu mwenye upeo mkubwa kubaini kuwa watu hao hawakuwa na starehe kama wengine. Hata utaratibu wao wa unywaji ulidhihirisha kuwa, walikuwa hapo kwa lengo maalumu wala siyo kustarehe.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Mmoja alikuwa akililazimisha tu tabasamu lake, na pale alipojisahau, tayari mikunjo ilijiunda katika paji la uso wake. Zilishapita dakika kumi tangu alipoipeleka kinywani chupa yake ya bia na hakuonekana kuwa na haja ya kinywaji hicho. Zaidi, macho yake yalionyesha kuwa alikuwa na jambo zaidi ya jambo ambalo liliisokota akili yake. Kwa jina aliitwa Kessy Mnyamani.

    Mwingine naye hakutofautiana na Kessy. Yeye pia alikuwa amekunywa mafunda matatu tu ya bia tangu aketi hapo. Kama Kessy, naye macho yake yalionekana kutotulia huku sigara iliyokuwa mkono wa kulia ikipelekwa mdomoni kila baada ya muda mfupi. Aliitwa Matiko Kidilu.

    Wanaume hao hawakutofautiana sana kimaumbile. Kessy Mnyamani alikuwa mrefu na aliyejengeka misuli mithili ya mnyanyua vyuma vizito. Matiko alikuwa mfupi kidogo aliyejaa maungoni kama Kessy.

    Nusu saa ilishapita tangu waingie ukumbini humo na sasa walianza kuchoka kuendelea kuwemo.

    “Labda hatakuja,” Kessy alisema akionyesha kukata tamaa.

    “Sidhani,” Matiko alipinga. “Hana desturi ya kuvunja apointimenti. Labda kuna linalomchelewesha.”

    “Una namba yake ya simu?”

    “N’nayo, lakini simu yangu haina chaji.”

    “Hata mimi tatizo ni hilohilo.”

    Hazikutimu hata dakika tano, mara aliyesubiriwa akatokea. Ni Morris Maguru. Huyo naye kimaumbile alishabihiana na Kessy. Sasa timu ilikamilika. Mara baada ya raundi moja ya bia wakaamua kuondoka. Walipaona mahali hapo hapafai kwa kikao chao muhimu, kikao kilichohitaji utulivu mkubwa.

    “Kwa hapa Kariakoo hakuna baa yenye utulivu,” Kessy alisema. “Twendeni Kinondoni…”

    “Kote huko?!” Matiko alimdaka.

    “Nd’o maana’ake,” Kessy alisisitiza. “Tusijali umbali, tujali utulivu tunaouhitaji.”

    Ubishi ulikoma. Wakakodi teksi hadi katika Baa ya Meridian, Barabara ya Mwinjuma. Wakachagua viti katika kijighorofa, ambako hakukuwa na mteja hata mmoja.

    “Nadhani hapa patatufaa, au mnaonaje?” Kessy aliwauliza.

    “Yeah, pametulia,” Matiko aliitika.

    Mara tu vinywaji vilipotua mezani, kisha mhudumu kuwaacha peke yao, Kessy alimtazama Matiko na kumtupia swali: “Vipi, una pesa?”

    Lilikuwa ni swali ambalo Matiko hakulitarajia. Kwa sekunde chache aliduwaa kimya, macho kamkazia Kessy.

    “Nakuuliza wewe!” Kessy alikazia. “Nakuuliza, una pesa? Sio hizi pesa za kununulia bia. No! Nazungumzia pesa! Pesa! Pesa za kweli! Unazo?”

    Sasa Matiko aliielewa maana ya swali hilo. Akajibu, “Sina.”

    “Na Morris?”

    “Sina! We’ unazo?”

    Wote wakacheka. Mara Kessy akachomoa sigara moja, akaiwasha na kuvuta mikupuo miwili ya nguvu kisha akawatumbulia macho wenzie, akionyesha bayana kujitenga na masikhara.

    “Nafikiri sasa tunapaswa kusaka pesa za kutakata,” alisema kwa sauti nzito na ya chini. “ Pesa zitakazotuondoa kwenye maisha haya ya kubahatisha. Mnakumbuka mara ya mwisho tulipopata pesa nyingi ni lini, na zilikuwa kiasi gani?”

    “Mwaka jana,” Matiko alijibu.

    “Zilikuwa milioni tano,” Morris akaongeza.

    “Yeah, milioni tano,” Kessy aliafiki. “Lakini milioni tano za mbinde! Tena ni madafu ya kibongo! Isitoshe, tulilazimika kutoa roho za ‘mtu tatu’ na kujificha Kibaha kwa siku nyingi, tukizidi kupoteza pesa kwa matumizi yasiyo ya lazima. Upuuzi!

    “Wenzetu wamekuwa wakifanya dili linakuwa dili kweli, dili la nguvu! Ama watachukua milioni mia mbili au tatu, benki, ama watalivaa duka la kubadilisha fedha; hapo pia hawatatoka na chini ya milioni mia moja. Hayo ndiyo mapato. Lakini kwa kawaida, kama mnavyojua, mipango ya aina hiyo huhitaji mitaji. Ni lazima watu muwe na fungu zuri la pesa litakalosaidia katika kuwarubuni au kuwashawishi watu walio ndani ya taasisi hizo ili mambo yawanyookee.”

    Akatulia na kunywa mafunda machache ya bia yake. Kisha akaendelea, “Unasikia Matiko, unasikia Morris, nimeshachoka kufukuzanafukuzana na ma-defender ya Polisi, au kujifichaficha kila tupatapo vijisenti kidogo. Watu kama sisi, kwa marika yetu, tunapaswa kuwa na nyumba zetu. Saa hizi mtu uko ndani ukizungumza na mkeo, ukicheka na wanao, tiivii iko mbele yako, bia kando yako huku kiyoyozi kikikushushia ubaridi wa kukuburudisha.

    “Sasa sikilizeni,” aliendelea. “Kuna pesa mahala fulani. Wote si mnamfahamu Beka?”

    Matiko na Morris waliitika kwa kutikisa vichwa.

    “Ok, nadhani wenyewe mnamwona jinsi anavyotanua mshenzi yule,” Kessy aliendelea. “Ana magari mapya matatu! Tena yote ya bei! Ana mzinga wa jumba huko Masaki! Sijui katajirika vipi fala yule!”

    Matiko na Morris walicheka.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Kwani kuwa na magari na nyumba ndiyo utajiri?” Morris alihoji. “Tuseme kwamba ana pesa ya kula tu.”

    “Sawa, tunaweza kusema hivyo,” Kessy alikubali. “Lakini pesa yake ya kula, kwetu inaweza kutulisha miaka kibao, na tukayabadili maisha yetu kimaendeleo.” Akasita kidogo, akiwakodolea macho wenzake. Kisha akaendelea, “Tunatakiwa tupate pesa ambazo tukigawana, angalau kila mmoja anapata si chini ya milioni kumi.”

    Matiko aliguna. “Milioni kumi zitakufikisha wapi?”

    “Kwa kweli haziwezi kumfikisha mtu popote, lakini ni tofauti na watu watatu kugawana milioni tano,” Kessy alijibu. “Isitoshe, lazima tutambue kuwa kupata pesa benki lazima nguvu itumike, vinginevyo lazima tuwe na pesa, tena mamilioni ya kuwahonga wahusika wa ndani ili tufanikiwe. Pesa, hatuna. Na wenzetu waliozivaa benki mfululizo hivi karibuni walikuwa na mtandao mkubwa na silaha nzito. Lakini pia wamewazindua sana Polisi. Tusijidanganye kuwa kwa sasa kutakuwa na urahisi wowote wa kuivamia benki yoyote na kufanikiwa. Inabidi tuangalie upande mwingine kwanza. Na kwa upande wangu nimemwona Beka.

    “Siwabani, kila mtu yuko huru kutoa pendekezo lake. Kama kuna sehemu yoyote ambayo tunaweza kupata pesa zaidi, kulingana na nguvu ya mtandao wetu, semeni.”

    Ukimya ulitawala. Si Matiko wala Morris waliokuwa na pendekezo lolote jipya.

    “Ok, nimemchagua Beka kwa sababu moja; si mnajua kuwa kwa sasa yuko na yule malaya wangu, Fatma?”

    “Fatma?!” Matiko aliuliza kwa mshangao.

    “Huyohuyo!” Kessy alijibu. “Nataka tumtumie Fatma. Fatma hawezi kuniangusha, najua jinsi ya kumwingia.”

    Matiko aliafiki kwa kutikisa kichwa.

    “Sidhani kama ni vizuri kumvamia nyumbani kwake,” Kessy aliendelea. “Hatujui alivyojizatiti kiulinzi, na hatuna hakika kama anaweza kuwa na tabia ya kuweka pesa nyingi ndani. Kwa hali hiyo tutapaswa kutumia njia nyingine iliyo bora zaidi.”

    “Lakini nadhani itakuwa poa kama utamshirikisha Fatma kwa namna ambayo hatajua kwa undani kipi kinachoendelea,” Morris alisema.

    “Haitawezekana!” Matiko alipinga. “Fatma ni mtu mwenye akili timamu na ni mtoto wa mjini. Usimchukulie kama machangu wabwia unga. Hapana, yule yuko fiti, mwanangu. Hata kama utatumia misamiati migumu kiasi gani, bado atakushtukia tu. Kwa hilo tutakuwa tumechemsha. Tukitaka kufanikiwa, na kama kuna ulazima wa kumtumia, basi hatuna budi kuhakikisha pia kuwa hatumfichi kila jambo.”

    “Good!” Kessy aliafiki. “Hata akijua kila kitu hakuna noma. Huenda kwa kumtumia yeye tunaweza kupata njia nyingine nzuri zaidi ya kuwini. Kazi hiyo n’achieni mimi. Kesho kutwa tuonane saa kumi na mbili ili tujue kinachoendelea.”



    *****



    JAPO asubuhi hii ilitawaliwa na baridi kavu ya kiangazi, hata hivyo Kessy Mnyamani hakuchoka kusubiri. Mbele yake, hatua kama mia mbili hivi ndipo lilipokuwa jumba la kifahari la Beka Bagambi. Ukuta mrefu kiasi cha futi nane ulilizunguka jumba hilo huku kukiwa na vibao vyenye maandishi: NYUMBA HII INALINDWA NA MITAMBO MAALUMU YA KUZUIA WEZI. Vibao hivyo vilikuwa kwenye pande zote za kuta.

    Geti kubwa, jeusi, lililotosha kupitisha magari mawili kwa pamoja lilikuwa mbele mita kadhaa kutoka barabarani. Ndani ya ukuta huo, paa jekundu la jumba la Beka lilionekana vizuri ilhali sehemu ya chini haikuweza kuonekana kutokana na zuio la ukuta huo.

    Kessy alikuwa ameketi kando ya barabara, kwenye benchi lililokuwa chini ya mti wenye matawi mengi. Ni sehemu iliyoonekana kama itumiwayo na vijana au watu wa aina yoyote kwa mapumziko, hususan nyakati za mchana jua linaposhusha miali yake mikali na kuzua joto lisilovumilika.

    Watu wawili, watatu walimpita hapo na kumtupia jicho la kawaida, baadhi yao wakimsalimu bila ya kuonyesha kushangazwa kwa kuwepo kwake mahali hapo asubuhi hiyo. Hawakumjali, na yeye hakuwajali; alijali kulikodolea macho geti jeusi la jumba la kifahari la Beka Bagambi.

    Anga ilizidi kutakata. Alikuwa hapo tangu saa 12:30 alfajiri, na sasa ilikwishatimu saa 1:30, saa nzima bila ya kumwona yeyote akitoka ndani ya jumba hilo! Hakukata tamaa; aliwaahidi wenzake kuwa siku inayofuata angewapa matokeo ya maongezi kati yake na Fatma, maongezi aliyotarajia yawe asubuhi hii, mchana au jioni, lakini lazima iwe leo.

    Subira yavuta heri. Sigara moja hadi nyingine zikiteketea mdomoni mwake, hatimaye saa 2:10 ilitimu, muda ambao kile alichokuwa akikisubiri kilitimia. Beka Bagambi alitoka baada ya kufunguliwa geti na binti, mfanyakazi wa ndani. Alikuwa akiendesha gari jeusi, Jeep Cherokee ambalo aliliegesha mara tu alipovuka geti.

    Mara Fatma akatoka ndani kwa hatua za haraka. Akamfuata pale garini na kuongea naye maneno machache kisha akambusu shavuni na akarudi ndani huku akicheka. Beka akaling’oa gari kwa mwendo wa taratibu, tabasamu likichanua usoni pake. Akampita Kessy pale benchini na kumtupia jicho la kutomjali. Akatokomea.

    Kessy akashusha pumzi ndefu. Akanyanyuka na kuvinyoosha viungo vyake, kisha akaanza kuvuta hatua fupifupi akilifuata jumba la Beka. Alipofika getini aliangaza hapa na pale na kuiona swichi ya kubonyeza ili kengele ilie. Akaifuata na kuibonyeza. Muda mfupi baadaye geti likafunguliwa. Fatma Mansour alikuwa mbele yake!

    “Haa! Kessy!” Fatma alibwata, mshangao ukiwa bayana machoni pake. “Karibu! Karibu ndani,” aliongeza huku akimpisha lakini mshangao ukiendelea kumtawala.

    Fatma alikuwa na haki ya kushangaa. Tangu uhusiano wao uvunjike ilikwishapita miezi mitatu, na hakukuwa na dalili yoyote ya kuurejesha. Na aliifahamu vizuri kazi ya huyo hawara wake wa zamani, kazi iliyompatia pesa za kula na kunywa. Haikuwa vigumu kwa Kessy kutoa roho ya mtu, kama kwa kufanya hivyo atapata pesa. Hilo, Fatma alilitambua fika, na kwa namna moja au nyingine, alinufaika kwalo.

    Ni pale Kessy alipokamatwa kwa tuhuma ya uhalifu fulani, akaswekwa rumande kwa takriban miezi miwili, ndipo uhusiano wao ulipolegalega na hatimaye ukafa. Fatma akaendelea kusaka pesa katika kumbi za starehe, mwili wake ukiwa ni kitega uchumi tegemezi.

    Kuvunjika kwa uhusiano wao hakukumwathiri yeyote kati yao. Kessy alimpenda Fatma Mansour kwa kuwa kila siku usiku alimpa burdani, na pia alistahili hata kwa kutamba naye hadharani. Lakini pia alitambua kuwa ni malaya. Alimkuta kwenye kundi la malaya, akauendeleza umalaya hata walipokuwa na uhusiano, na alimwacha ili auendeleze umalaya wake.

    Leo ni Kessy huyohuyo yuko mlangoni pake! Kasimama bila hata ya wasiwasi, tabasamu la mbali likichanua usoni pake! Haonyeshi hata dalili ya hofu! Amefuata nini? Amepajuaje hapa? Maswali hayo yalijirudiarudia akilini mwake huku akimtazama Kessy kwa wasiwasi uliojificha.





    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Pita Kessy…pita ndani,” Fatma aliongeza, safari hii akilijibu tabasamu la Kessy kwa tabasamu jepesi ambalo halikudumu zaidi ya sekunde tano. Kwa ujumla hakuwa timamu kisaikolojia. Lakini aliamua kuwa mtulivu kutaka kujua sababu ya ujio wa Kessy.

    Kessy akapenya, geti likafungwa. Fatma mbele, Kessy nyuma walikwenda hadi ndani ya jumba lile la kifahari.

    Kwa takriban dakika tano ambazo Fatma alimwacha Kessy sebuleni na kutokomea chumbani, Kessy alizitumia kwa kuustaajabia umaridadi wa sebule ile. Ilikuwa ni sebule maridadi, iliyosheheni samani mbalimbali za kisasa. Akilini mwa Kessy hakuuona uhalali wa Fatma Mansour kuwa ‘mama mwenye nyumba’ hiyo. Fatma! Fatma! Mwanamke malaya! Leo ndiye mama wa jumba hili?! Kamroga Beka?

    Aliwaza hili na lile, akajiuliza hivi na vile, lakini mara wazo moja likamjia. Kwamba, huenda ni yale mateso kama aliyowahi kupewa yeye, ndiyo pia yaliyomvuruga akili Beka. Mateso ya faraghani, yenye kuliwaza, kuburudisha na kusisimua.

    Hatimaye Fatma alirejea. Akajipweteka katika sofa jingine kivivuvivu, tabasamu likichanua tena usoni.

    “Ndiyo, bibie, naona nd’o u’shanitupa jumla,” Kessy alimchokoza.

    “Kwa nini?”

    “Kila kitu kiko wazi. Umeamua kuishi na tajiri, sisi mahohehahe hatuna chetu tena.”

    Fatma akacheka. “Acha hizo, Kessy,” akasema kwa mzaha. “Kwanza leo imekuwaje ukanikumbuka?”

    “Unajua tena…” Kessy akaiacha sentensi hiyo ikielea.

    “Najua nini?”

    “Mavitu yako.”

    “Nini?” Fatma aliishusha zaidi sauti, akitaka yule mfanyakazi aliyekuwa jikoni asisikie.

    “Mavitu yako s’o mchezo, nd’o maana nimekufuata tena.”

    Fatma alisonya kisha akabibitua midomo. “Upuuzi wako bado hujauacha tu?”

    Wakacheka.

    “Ok,” Kessy alibadilika. Akakikata kicheko na kumtazama Fatma kwa macho makali, sura ya masikhara ikiwa imeshajitenga na uso wake. Akaongeza, “Tuyaache hayo mengine, Fatma. Sitaki ugeni wangu unichukulie zaidi ya robo saa humu ndani. Nataka tuzungumze. Ni maongezi nyeti, yanayotuhusu sisi wawili tu na yanapaswa kufanyika katika mazingira tofauti na hapa kwako.”

    Fatma aliguna. Akakunja uso akimtazama Kessy kwa macho makali. Kisha kwa sauti ya chini, alisema, “Nadhani sijakuelewa.”

    “Utanielewa tu. Panga muda leo hii, wapi tuonane na kuongea.”

    “Kwani maongezi yenyewe yanahusu nini?”

    “Ni ya kawaida tu,” Kessy alijibu huku akitabasamu kwa mbali. “Kumbuka kuwa mimi na wewe tumetoka mbali, Fatma…”

    “Lakini Kessy…”

    Hakuna cha lakini, Fatma,” Kessy alimkata kauli. “Angalia, usiwe mjinga. Fanya hima tuonane leo hii. We’ ni mtoto wa town, Fatma. Sasa fanya hivi, tukutane pale Palm Beach Hotel, saa kumi jioni, leo. Ni hapo utakapoweka lakini zako; sawa?”

    “We! Palm Beach?” Fatma alimtolea macho.

    “Yeah, kwan’vipi?”

    “Haiwezekani. Hoteli ile ni kubwa. Na Beka hakosi kuingia kwenye hoteli za aina hiyo. Ni’shakwenda naye pale mara mbili, tatu hivi karibuni.”

    “Ok, na lile jengo la Ubalozi wa Ufaransa, unalijua?”

    “Ndiyo.”

    “Chukulia kuwa nd’o unaelekea town,” Kessy aliendelea. “Ukifika pale kwenye kituo cha daladala cha ubalozi, cha kwenda Mwenge, nenda mbele kidogo. Mbele yako kuna barabara inayokwenda kulia. Barabara hiyo inapakana na ukuta wa jengo la ubalozi huo kwa upande wa kushoto. Ukifuata barabara hiyo, mbele kuna ki-baa kidogo lakini chenye hadhi. Unaonaje kama tutakutana hapo? Nadhani hapana noma. Beka hawezi kuingia kwenye vibaa vidogovidogo kama kile.”

    Fatma aliyatafakari maelezo ya Kessy kwa sekunde kadhaa. Kisha akaguna. Alipafahamu vizuri hapo palipotajwa na Kessy. Katika zungukazunguka yake ya kusaka wanaume, aliwahi kukesha katika maeneo ya Kinondoni mitaa ya Tunisia, Kinondoni Road na kwingineko ambako aliambulia pesa kidogo za kukidhi mahitaji yake.

    Hiyo baa ambayo Kessy kamtajia, aliitambua vizuri. Alishawahi kuizungukia. “Kwa hiyo, tufanye saa kumi, sio?” hatimaye alitaka uhakikisho.

    “Nd’o maana’ake.”

    “Lakini sio mambo ya zama zile?” Fatma alihoji huku kaukunja uso kidogo.

    “Hakuna kitu kama hicho.”

    “Hata hivyo bado kuna tatizo moja,” Fatma alisema kwa unyonge.

    “Lipi tena hilo?”

    “Muda.”

    “Muda?”

    “Ndiyo.”CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Kwani muda umekuwaje?”

    “Sina uhakika kama nitapata nafasi ya kutoka katika muda huo. Beka atakuwepo.”

    “Atakuwepo?” Kessy alimkazia macho.

    “Ndiyo. Ni kawaida yake kurudi kati ya saa tisa hadi saa kumi na moja.”

    Kessy alisonya kidogo, kisha akasema, “We’ ni mwanamke wa shoka, Fatma. Beka ni cha mtoto kwako. Tumia mbinu unazojua hadi alainike. Najua hukumbuki idadi ya wanaume uliowadanganya na wakadanganyika. Beka hawezi kuwa bwege wa kwanza kwako. Ataingia mkenge tu. Unasemaje? Zungumza kiutu uzima!”

    Fatma alifikiri kidogo kisha akajibu, “Nitajaribu.”

    Ok, nitakusubiri,” Kessy alisema huku akinyanyuka. Akaanza kutoka, lakini kabla hajaufikia mlango, akageuka. “Naomba namba yako ya mobile,” alimwambia.

    Fatma alimtazama huku akitabasamu, kisha akasema, “Haina haja. Muhimu ni kutimiza miadi. Kama itatokea tusionane, basi ujue leo haikuwa siku mwafaka; sawa?”

    “Poa, lakini ujitahidi.”

    “Nitajitahidi.”





    *****



    ALIJITAHIDI. Ilitokea kama aina fulani ya sinema ya mapenzi. Beka aliporejea saa kumi kasoro dakika chache jioni, alipokewa kwa namna aliyoizoea; kukumbatiwa, kupigwa busu hapa na pale, kutomaswa huku na kule na mengineyo mengi yaliyoviamsha viungo fulani mwilini mwake kiasi cha kujikuta wakikokotana chumbani ambako alitupwa chali kitandani.

    Kabla hajamudu kufanya lolote, akashangaa akipambuliwa nguo moja baada ya nyingine hadi akawa mtupu. Kipindi kilichofuata kiliihamisha akili yake hadi katika dunia nyingine, dunia yenye raha na msisimko wa kipekee. Na kama mara kadhaa zilizopita, safari hii pia alijikuta akiropokaropoka kwa faraja.

    Robo saa baadaye iliwakuta bafuni wakioga, na waliporejea chumbani ndipo Fatma alipomwomba ruhusa ya kwenda Kinondoni Moscow kumjulia hali rafiki yake.

    “Nikusindikize?”

    “Hakuna haja, mpenzi,” Fatma alipinga. “Si unajua tena maongezi ya wanawake…” akacheka huku akimpiga kijikofi cha mahaba katika shavu la kulia.

    Beka alikosa hoja ya kupingana naye. Mapokezi mazito aliyoyapata muda mfupi uliopita yalimfanya ajikute akikosa kauli mbele ya mrembo, Fatma Mansour.



    *****



    YALIKUWA ni maongezi mazito na marefu. Japo awali Fatma alikuwa na msimamo mkali wa kutoafikiana na Kessy, hata hivyo Kessy aliutumia kitaalamu ulimi wake kiasi cha kumlegeza na kumtepetesha Fatma mithili ya bamia iliyotokota mekoni. Msimamo wa Fatma ukayeyuka kama ambao haukuwahi kujikita katika mtima wake.

    “Hawezi kuwa na kitu kama milioni mia hivi, ndani?” katikati ya kikao hicho Kessy alimuuliza.

    “Kwa kweli siwezi kujua,” Fatma alijibu. “Lakini siku hizi watu wameelimika na kujanjaruka, Kessy. Mtu hawezi kulimbikiza mamilioni ya pesa ndani bila ya sababu ya maana. Ujambazi umewazindua wengi, kwa hiyo wanazikimbizia benki, wanabaki na vikadi vya ATM mifukoni mwao. Sanasana, tajiri nd’o anaweza kuhifadhi keshi, labda shilingi milioni moja au mbili tu, ndani.”

    Kessy alikunja uso kidogo, akaguna. Kisha akasema, “Lakini ni ukweli usiopingika kuwa huyo fala wako anazo. Na kama ziko benki, hazikosi milioni mia tano na zaidi; utakataa?”

    “Labda,” Fatma alijibu huku akinyanyua mabega na kuyashusha. Haikuwa bayana kama aliafiki au alipinga.

    “Ok, msuke, basi,” Kessy alisisitiza. “Msuke, asukike! Akikubali kudroo milioni hamsini, zako ishirini na tano na zinazobaki nagawana na wash’kaji zangu.”

    Fatma aliguna. Akamkazia macho Kessy. “Kwani hili dili ni la watu wangapi?”

    “Siki’za Fatma,” Kessy alisema kwa sauti ya chini. “Dili zuri la pesa huwezi kulifanya peke yako. Tuko watatu, wewe ni wa nne. Ni wazee wa kazi wa uhakika. Niko nao kabla hata hujanikimbia.”

    “Lakini mie huwa sipendi kufanya mipango inayoshirikisha watu zaidi ya wawili,” Fatma alisema kwa sauti ya unyonge, akimtazama Kessy kwa namna ya kutopendezwa na kauli yake.

    “Us’jali. Kwa hili ujue hakuna kitakachoharibika. Na n’na maana yangu katika kuwashirikisha hao wenzangu. Una jingine?”

    Fatma hakujibu, zaidi alionyesha kutafakari jambo. Hali hiyo ikamtia mashaka Kessy. Akahisi mdudu mbaya ameanza kuunyemelea mpango wao. “Vipi, mbona kimya?” hatimaye alimuuliza, na hakusubiri jibu, akaongeza, “Naisubiri kauli yako ya mwisho. Uwe mjanja, Fatma. Tumeanza kikao chetu vizuri, vipi doa liingie saa’izi?”

    Kwa mara nyingine hakusubiri jibu. Akaendelea, “Siki’za Fatma, pamoja na raha zote anazokupatia, sidhani kama ameshakukabidhi kitu kama milioni tano hivi na kukuruhusu uzitumie upendavyo…”

    “Lakini,” Fatma alizinduka. “Ni majuzi tu kanipa pesa nzuri ya matumizi yangu binafsi.”

    “Shi’ngapi?” Kessy alimkazia macho.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Milioni moja!”

    “Milioni moja! Milioni moja nd’o ukaona kakutajirisha!” Kessy akaachia tabasamu la dhihaka. “Milioni moja ni kitu gani kwako, Fatma? Anapaswa kukufungulia akaunti yenye kitu kama milioni ishirini hivi benki! Siyo kamilioni kamoja hako…”

    “Halafu ameniahidi kuwajengea wazazi wangu nyumba, kisha…”

    “Siki’za Fatma,” Kessy alimkata kauli. “Anaweza kukuahidi hata kukununulia Treni au Ndege. Si ahadi tu! Lakini je, atazitimiza ahadi hizo? Usiwe mbumbumbu, Fatma! Yaani bado tu hujatuelewa wanaume tulivyo? Wanaume tunatofautiana kitabia; wengine ni wakweli na waaminifu na wengine ni matapeli wa kutupa.”

    Kimya kifupi kikatawala huku wakitazamana. Kessy akahisi kuwa maneno yake yamemwingia vizuri Fatma, hivyo akawa na matumaini ya ushindi katika kampeni yake.

    “Usibabaishwe na jumba lile,” aliendelea. “Wala usipumbazwe na ahadi zake. Hujui kichwani mwake anawaza nini. Si ajabu kesho au keshokutwa akakutimua kama mbwa! Utakula hiyo milioni yako moja maisha yako yote?”

    Ulikuwa ni msumari wa mwisho kwa Fatma. Fikra za usaliti zikamtawala. Yakamtoka maneno mawili tu: “Poa, nitamwingia.”

    Yakawa ni maneno yaliyomsisimua Kessy zaidi ya kumfurahisha. “Hapo nimekuelewa,” alisema huku akijiwashia sigara. Akaongeza, “Naamini kila kitu kitakwenda kama n’navyofikiria. Keshokutwa unaweza kuwa unamiliki milioni ishirini na tano hivihivi! Mradi tu uwe ngangari wa kumlainisha adroo kiasi hicho cha pesa.”

    “Kazi hiyo n’achie mwenyewe,” Fatma alisema kwa majigambo. “Kesho, muda kama huu tukutane hapahapa nikupe jibu. Hakuna kitakachoshindikana. Beka hawezi kun’shinda mie mtoto wa Ki-zenji.”



    *****



    NI saa 5:30 usiku Beka na Fatma walipoamua kuizima televisheni na kwenda kulala. Kama kawaida yao walitaniana na kucheka, wakionekana ni watu walioridhika kimaisha, na kama vile hawatakufa wala kupatwa na misukosuko yoyote impatayo binadamu yeyote duniani.

    Lakini wakati huohuo, Fatma alikuwa makini, akilikumbuka jukumu zito lililokuwa mbele yake; kutimiza ahadi aliyoitoa kwa Kessy saa takriban nane zilizopita.

    “Beka,” hatimaye alimwita bila ya kujua ni kipi au ni vipi angeanza kuizungumzia hoja yake. Kwa mbali alihisi moyo ukidunda kwa mapigo ya kasi kidogo.

    Beka alimtazama na kumbusu shavuni bila ya kutamka chochote.

    “Nakupenda, Beka,” Fatma aliropoka.

    Kwa Beka Bagambi, huo ulikuwa ni wimbo aliozoea kuusikia kutoka kinywani mwa Fatma, lakini ulikuwa ni wimbo usiokinai masikioni mwake. Alipenda kuusikia tena na tena.

    “Hata mimi, mpenzi,” alijibu, naye hiyo ikiwa ni kawaida aliyokwishaigeuza sheria katika kujibu.

    “Hapana, Beka,” sasa ujasiri ulianza kumwingia Fatma. “Wewe hunipendi. N’na taarifa zako kuwa una wanawake kibao huko mitaani! Tena nasikia wengine u’shawageuza mabwege ka’miye; unawaahidi kuwatimizia hili na lile, lakini yote huyatimizi! Looh! Mwanaume wewe!”

    “Nini?!” Beka alishtuka. “Eti n’na wanawake wengine mitaani?”

    “Ndiyo! Kwani kipi cha ajabu?”

    “Sikia Fatma,” Beka alimgusa begani. Sasa, badala ya kulala, aliketi kitandani, akionekana kusawijika usoni. Alitaka kuongeza neno, sauti ikakwama. Akameza funda la mate kisha akashusha pumzi ndefu. “Fatma, utani huo s’o mzuri,” hatimaye aliipata sauti yake.

    “Utani?” Fatma alijitia mkali. “Unamaanisha kuwa nakutania? Tafadhali, Beka, mwenzio sipendi kutelekezwa kama hao wengine! Hapana! N’na mashaka kama kweli utanitimizia hayo mengine uliyoniahidi. Mwisho wako naona ni kwenye zile pesa ulizonipa siku ile; baass! Hilo gari si umenipa kwa mdomo tu! Kadi bado unayo, na ina jina lako! Cha ajabu ni kipi kama kesho utanifukuza ka’mbwa na gari ukabaki nalo?”

    Beka alichanganyikiwa. Hakutegemea kuambiwa maneno hayo. Kwa unyonge akasema, “Fatma, elewa kuwa nakupenda sana, na n’nakuapia kuwa sina mwanamke mwingine nje! Kama kuna watu wanaokwambia maneno hayo, basi kaa ukijua kuwa ni wachonganishi tu. Achana nao!”

    Bado Fatma alikaza uzi. Akaendelea kumshushia tuhuma nzito za ufuska, tuhuma ambazo hazikuwa hata na chembe ya ukweli ndani yake. Ukweli ni kwamba Beka hakuwa na hawara mwingine zaidi yake. Mwanamke wa mwisho aliachananaye kiasi cha miezi sita iliyopita baada ya mwanamke huyo kumwambukiza maradhi ya zinaa, maradhi yaliyomgharimu maelfu ya fedha kupambana nayo.

    Tuhuma hizi alizotupiwa zilimchoma moyo kiasi cha kudondokwa machozi bila ya kutarajia. Hii ilikuwa ni mara yake ya kwanza kumlilia mwanamke!

    “Fatma…Fatma…!”



    ***FATMA analisaliti penzi la kweli kutoka kwa BEKA……anatafunwa na kidudu aina ya tamaa….anaamua Kufuata maneno matamu ya KESSY…..sasa anaanza kumwingia BEKA….

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    JE atafanikiwa?????



    ITAENDELEA…….







0 comments:

Post a Comment

Blog