Simulizi : Domo La Mamba
Sehemu Ya Pili (2)
Beka alichanganyikiwa. Hakutegemea kuambiwa maneno hayo. Kwa unyonge akasema, “Fatma, elewa kuwa nakupenda sana, na n’nakuapia kuwa sina mwanamke mwingine nje! Kama kuna watu wanaokwambia maneno hayo, basi kaa ukijua kuwa ni wachonganishi tu. Achana nao!”
Bado Fatma alikaza uzi. Akaendelea kumshushia tuhuma nzito za ufuska, tuhuma ambazo hazikuwa hata na chembe ya ukweli ndani yake. Ukweli ni kwamba Beka hakuwa na hawara mwingine zaidi yake. Mwanamke wa mwisho aliachananaye kiasi cha miezi sita iliyopita baada ya mwanamke huyo kumwambukiza maradhi ya zinaa, maradhi yaliyomgharimu maelfu ya fedha kupambana nayo.
Tuhuma hizi alizotupiwa zilimchoma moyo kiasi cha kudondokwa machozi bila ya kutarajia. Hii ilikuwa ni mara yake ya kwanza kumlilia mwanamke!
“Fatma…Fatma…!”
Fatma hakuitika, badala yake alimtazama kwa macho malegevu, huruma ikianza kumwingia kwa mbali, huruma ambayo hata hivyo ilidumu kwa sekunde chache na kutoweka pale fikra juu ya shilingi milioni 25 zilipomrudia kichwani.
“Fat…Fatma…” sauti ya Beka ilisikika tena, sauti iliyosihi, kigugumizi kikiwa bayana kooni mwake.
Ni hilo ambalo Fatma alilihitaji. Sasa, moyoni akajenga imani ya ushindi. Na katika kuikamilisha kazi yake, alilala na kuzianzisha tena zile fujo zake, usiku huu akitumia utaalamu maradufu. Baada ya muda mfupi Beka alikuwa akitapatapa, kisha akalia tena, lakini hiki kikiwa ni kilio tofauti na kile cha awali. Hiki kilikuwa ni kilio cha faraja. Dakika nyingi baadaye walitengana, wakatazamana kwa macho ya mahaba huku Fatma akisemea moyoni: Nimekuumbua…bado una deni moja…pesa…kunipa pesa. Upende usipende, utanitajirisha…bwege wee!CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Kwa sauti alisema, “Beka, kama unanipenda, kesho anza kutimiza ahadi zako.”
“Sawa, bibie. Kesho nitakukabidhi kadi ya Toyota Chaser, halafu nitadroo pesa za kukufungulia saluni.”
“Na pesa za kuwatumia wazazi kwa ajili ya ununuzi au ujenzi wa nyumba yao?” bado Fatma alimbana.
“Zote nitadroo kesho hiyohiyo.”
“Hapana,” Fatma alipinga haraka. “Mambo ya benki fanya keshokutwa. Kesho shughulikia suala la gari; sawa, mpenzi?”
“Poa tu.”
Fatma alikuwa na sababu ya kupinga uchukuzi wa pesa benki siku iliyofuata. Ilikuwa ni siku aliyopanga na Kessy kukutana ili ampe taarifa kuhusu mpango wao.
Lakini akiwa na tashwishi ya kujua kiwango cha kitita kitakachochukuliwa benki, hakusita kumuuliza, “Kwani unatarajia kudroo kiasi gani, mpenzi?”
“Sabini si zitatosha?”
“Sabini? Yaani milioni sabini?”
“Yeah.”
Fatma alifikiri kidogo kisha akasema, “Nadhani zitatosha. Lakini..” akasita.
“Lakini nini?”
“Kwa nini usidroo kitu kizima ili hesabu yake ikae vizuri? Tena huenda ikasaidia kwa balansi kama kutatokea upungufu wowote.”
“Kwa hiyo nichukue mia kamili!”
“Itakuwa vizuri kwa jinsi ninavyoona mimi. Sijui, wewe.”
“Us’konde.”
*****
HII ilikuwa ni siku iliyofuata, baada ya ule usiku ambao Fatma alitumia hila zote kumghilibu akili Beka hadi wakafikia makubaliano ya Beka kwenda benki kuchukua fedha taslimu, shilingi milioni 100. Saa 10:30 jioni, Fatma alitwaa simu yake ya mkononi na kumpigia Beka.
“Hallow, dear,” Beka aliitika.
“Vipi, uko wapi beibe?”
“Niko eneo la TAZARA kwenye foleni. Kwan’vipi?”
“Nd’o unarudi au?”
“Yeah. Lakini napitia PPF Tower kwa ishu f’lani. Kuna tatizo lolote?”
“Hakuna; nilitaka kukutaarifu tu kuwa natoka kidogo.”
“Wapi tena?”
“Mwenge… ah! No! Ni kule maeneo ya Mbezi.”
“Kufanya nini?”
“Kuchukua yale maua ya kupandikiza mbele ya nyumba.”
“Ok, lakini si unajua taimu hizi kuna foleni kubwa?”
“Hainibabaishi. Foleni kubwa iko kati ya Morocco na Mwenge. Mi’ n’tapitia Kawe na kwenda kuzukia kule mbele. Isitoshe, bado mapema. Foleni mbaya inaanza saa kumi na moja.”
Dakika iliyofuata Fatma alikuwa akitabasamu. Mara akamwita Debora, binti aliyekuwa akifanya kazi hapo nyumbani. Debora alipokuja alimwambia, “Natoka kidogo. Baba yako hajarudi. Ukisikia mlio ka’ wa kengele ya baiskeli, usifungue geti. Ukisikia mlio kama wa kinanda, nd’o ufungue; atakuwa ni yeye. Umenisikia?”
“Ndiyo, mama.”
Fatma alikuwa na sababu ya kutoa hadhari hiyo. Tangu alipoongea na Kessy kuhusu mpango wa kujipatia mamilioni ya shilingi, hakuwa na imani na mtu yeyote zaidi ya Beka. Lolote lingeweza kutokea kabla ya mpango wao kutekelezwa. Hakuwa na sababu ya kumfanya ajisikie kumwamini Kessy walao kwa asilimia ishirini.
“Binadamu wa leo wana tabia ya kugeukana dakika yoyote,” alinong’ona wakati akiingia ndani ya gari dogo, jeupe, Toyota Chaser na kuling’oa taratibu.
Robo saa baadaye alikanyaga breki katika baa ileile aliyokuwa na Kessy jana. Akateremka huku akiangaza macho katika meza chache zilizokuwa na wateja. Akamwona Kessy katika meza iliyokuwa peke yake, pembezoni mwa ukumbi. Kama kawaida yake, Kessy alikuwa na bia mbele yake, sigara mkononi. Zaidi, safari hii gazeti moja la burudani lilikuwa mezani, macho juu yake, akifunua kurasa hadi kurasa huku yote ayasomayo yakielea tu kichwani. Hakuwa pale kwa ajili ya kunywa bia au kusoma gazeti, hapana. Alikuwa pale kutokana na miadi baina yake na Fatma. Haya mengine yalikuwa ni ya ziada tu.
Kwa sekunde kadhaa Fatma alisimama akimtazama, ilhali yeye akiwa bado kaliinamia gazeti lake. Fatma akahisi nywele zikimsimama ghafla. Na papohapo akajiwa na wazo jipya, wazo ambalo kwa kipindi hichohicho pia alihisi kuwa kapewa na Mungu. Lilikuwa ni wazo ambalo tangu alipoanza kuzungumza na Kessy kuhusu mpango wa kujipatia mamilioni ya shilingi, halikuwahi kumjia akilini hata kwa mbali, wazo la kutoziachia pesa hizo zipite katika mikono ya mtu mwingine.
Angeweza kumwamini baba na, au, mama yake mzazi kama bado wangelikuwa hai. Ndiyo, kwa suala la kumsaliti Beka, na suala hilo likiwa linayagusa maisha ya Beka kwa asilimia mia moja, zaidi ya hao wazazi wake hakukuwa na kiumbe mwingine aliyezaliwa chini ya jua ambaye angeweza kumwamini japo kwa asilimia moja.
Mpango huu ulikuwa mzito na uliohitaji umakini wa hali ya juu. Ulikuwa ni mpango uliohitaji mtu mwenye uchu wa maendeleo, kiu ya utajiri, moyo wa kijasiri, na ikibidi, mtu huyo awe tayari kutenda ukatili wa aina yoyote. Yeye alikuwa na uchu mkubwa wa maendeleo, alikuwa na kiu kali ya utajiri, lakini alijaaliwa kiwango cha wastani cha ujasiri katika moyo wake, huku, ukatili, hususan ukatili uwezao kuhatarisha maisha ya mtu likiwa ni jambo zito sana kwake kulitekeleza.
Hiyo ni kwa upande wake, siyo kwa Kessy na wenzake. Wao walihitaji maendeleo, walitaka kutajirika, na, ukatili kwao ulikuwa ni miongoni mwa burudani mikononi na mawazoni mwao, wakifurahia kuvunja shingo ya mtu au kumshindilia risasi za kichwani.
Akilini mwa Fatma, Kessy na wenzake hawakuwa binadamu wa kawaida japo walikuwa na viungo vya kawaida na walizungumza na binadamu wengine kama kawaida. Wanaweza kufurahi na wewe dakika ya kwanza na wakakuua dakika ya pili. Ni hilo lililomfanya asiwaamini. Hakuwa na hakika ya kupata haki yake kwa jinsi inavyostahili. Au, huenda baada ya mafanikio ya mpango wao, wakampa mgawo wake halafu muda mfupi baadaye wakamchinja kama kuku na kujitwalia pesa zote!
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Jambo jingine lililomtia shaka ni kuhisi kuwa baada ya kugawana pato lao kwa haki, kisha wakaagana kwa amani, kungekuwa na uwezekano wa siri kuvuja saa au siku chache baadaye. Hakuwajua hao wenzake Kessy lakini alizijua fika tabia za Kessy pindi pesa zinapomtembelea. Alikuwa ni mtu wa matumizi makubwa na majigambo yanayokera. Aliwahi kudiriki kufunga mauzo kwenye baa moja huko Manzese, akiwaruhusu wateja wanywe tani yao. “Ninazoo! Ninazooo…! kunyweni..kunyweniii! Ni’shalipa!” Ndivyo alivyotamba.
Kwa Fatma, tabia hiyo haikuwa ya ufahari wa kujivunia hata kidogo. Ni ujinga! Ni ushamba! Ni ulimbukeni! Je, kama Kessy yuko hivyo, hao wenzake wakoje? Hawawezi kuwa walevi-mbwa wenye vichwa vya panzi, ambao pindi pombe zinapovitawala vichwa vyao huropoka chochote, mathalan kutoboa siri ya mafanikio yao? Je, mmojawao, kama siyo wote, hawezi kuwa mbumbumbu au limbukeni wa mapenzi, ambaye atadiriki kumtamkia mpenziwe jinsi alivyofanikiwa kujipatia mamilioni ya shilingi?
Fatma aliamini kuwa, matukio hayo, na mengine yafananayo na hayo, huenda yangekuwa kiini cha uvujaji wa siri. Na hapo ndipo na yeye angetiwa mbaroni na kuozea jela. Ni mawazo hayo yaliyomfanya apange jinsi ya kuwageuka wenzake. Ndiyo, awageuke na kutwaa milioni 100 zote!
Yeye peke yake!
Wazo hili likamfanya ajilaumu kwa kumkubalia Kessy kuwa angeweza kumlainisha Beka. Aliamini kuwa kusingekuwa na kikwazo chochote kama yeye peke yake angeamua kumzidi ujanja Beka Bagambi. Asingeshindwa. Lakini tayari alishachelewa. Hata kama hatampa ukweli Kessy kuhusu uchukuzi pesa benki kesho yake, bado hilo lisingemzuia Kessy asiwafanyie ushenzi mwingine, mathalan kuwapora gari au kuwavamia nyumbani usiku.
Maji yamekwishamwagika, alinong’ona kwa hasira, mnong’ono ambao haukuweza kuyafikia hata masikio yake mwenyewe. Hivyo, ni uamuzi mmoja tu uliopitishwa akilini mwake; kuwageuka wakati, au muda mfupi kabla ya mgawo wa pato. Kwa hali hiyo, alipomfikia Kessy tayari alikuwa ameshapitisha uamuzi wa kushirikiana naye hadi dakika ya mwisho; hadi milioni 100 zitakapopatikana!
*****
“AMEKUBALI,” Fatma alimwambia Kessy muda mfupi baada ya kuketi.
“Yes! Hayo nd’o maneno, bibie,” Kessy alisema huku akimpa mkono Fatma. “Sikutegemea kuwa ungeshindwa kumghilibu akili mshamba yule. Enhe, kwa hiyo itakuwaje?”
“Ni kesho!” Fatma aliishusha sauti. Akageuka kushoto, kulia na nyuma, akihofia masikio yasiyohusika kuweza kuyanasa mazungumzo yao. Hakukuwa na mtu yeyote. Akamrudia Kessy na kuongeza, “Kesho asubuhi atakwenda benki kudroo. Ni CRDB Azikiwe Branch.”
“Yap!” Kessy alizidi kuifurahia taarifa hiyo. Akanyanyua chupa ya bia na kunywa mafunda kadhaa kwa pupa. Alipoirejesha mezani, akatwaa sigara nyingine na kuiwasha kisha akaanza kuivuta kwa madaha. “ Nadhani sasa tutaagana na umaskini, si nd’o maana’ake?” aliongeza, safari hii akimshika kiganja Fatma na kumtomasa kimahaba.
Fatma aliunyofoa mkono huku akicheka. Akamwita mhudumu na kumwagiza soda aina ya Sprite. Wakati mhudumu akiondoka, papohapo Kessy akahoji, “Enhe, sema Fatma, atadroo kiasi gani?”
“Kwani ni kiwango kipi kingefaa kwa mgawo wa watu wanne?” Fatma naye akamtupia swali.
“Fifty ingekuwa poa, au zaidi ya hapo.”
“Siku ile, kwa pendekezo lako ulizungumzia milioni hamsini; nusu yangu, nusu yenu, sawa?”
“Ndiyo,” Kessy alijibu huku kakunja uso, macho yake mekundu yakimtazama Fatma bila ya kupepesa.
“Hilo lilikuwa ni pendekezo lako,” Fatma alisema kwa kujiamini. “Mimi nilikuwa na pendekezo langu wakati nilipokuwa naye jana usiku. Na ukae ukijua kuwa wewe ulinikuta najiuza barabarani, ukaniteka. Tulipoachana, nilirudi barabarani kuuendeleza umalaya wangu. Beka naye alinikuta kwenye mazingira kama uliyonikuta wewe, akaniteka. Na hadi leo niko naye. Sina uhakika, lakini nadhani kanogewa. Na jana nimetumia mbinu zangu za umalaya katika kumlainisha ili asituwekee usiku.”
Kufikia hapo akasita kidogo. Akaitwaa chupa yake ya soda na kuipeleka kinywani. Akanywa funda dogo na kuirejesha haraka mezani. Akamkazia tena macho Kessy. Akashusha pumzi ndefu na kuendelea, “Inabidi unisikilize vizuri, na unielewe. Kinyume cha hivyo, dili linakufa sasa hivi!”
Ukimya ukatawala kwa sekunde kadhaa. Kisha, Fatma akaendelea, “Nimemwambia adroo milioni mia moja.” Hakuficha, na hakuiona haja ya kuuficha ukweli huo.
“Nini?” Kessy aliuliza kwa mnong’ono, sauti yake ikiwa imefurika tani kadhaa za mshangao.
“Hujanisikia au hujanielewa?” Fatma alimtolea macho.
“Nadhani sijakuelewa.”
Fatma akairudia kauli yake.
“Milioni mia moja!” mshangao ulikuwa bayana katika sauti na macho ya Kessy baada ya kumsikia vizuri Fatma akikitamka kiwango cha pesa.
“Nd’o maana’ake,” Fatma alimdaka. “Lakini usizitolee udenda buree! Makubaliano yetu ni milioni hamsini. Upo mpaka hapo?”
“Nakusoma, endelea.”
“Akilini mwako hakukuwa na uwezekano wa Beka kudroo shilingi milioni mia moja. Hiyo ni kazi ya kiuno changu; kubali, usikubali! Sasa hebu sema, uko tayari niendelee kuzungumza au u’shaingiwa na mtimanyongo?”
“Zungumza tu,” Kessy alijibu huku akililazimisha tabasamu kuchanua usoni pake.
“Milioni hamsini za ziada ni zangu; sawa?” sauti na macho ya Fatma vilionyesha ujasiri na msimamo usiotenguliwa hata kwa mtutu wa bunduki. “Milioni hamsini nyingine, nd’o kama tulivyoongea. Tuko pamoja?”
“Tuko pamoja. Wala us’konde.”
Hapo tena kimya kifupi kikatawala. Vinywa vikawa na zoezi la kupokea vinywaji vyao. Muda mfupi baadaye, kimya hicho kikavunjwa na Kessy.
“Halafu kuna jambo jingine unalopaswa kujua.”
“Lipi tena?”
“Upo uwezekano wa kutokea maafa.”
“Nini?”
“N’na maana kuwa,” Kessy alianza kufafanua. “Katika kuhakikisha mpango hauharibiki, kuna uwezekano wa risasi kutumika.”CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Fatma aliguna, akamtazama Kessy kwa macho makali zaidi. Kisha akauliza, “Kwani hamwezi kumaliza mchezo bila ya kutokea kashkash?”
“Inawezekana,” Kessy alijibu kwa sauti ya chini zaidi. “Lakini, lazima uelewe kuwa mpango huu ni mzito, na hatutaki ukwame kwa sababu za kijinga. Milioni nane nitakazozimiliki mimi, siyo pesa ndogo. Tangu nianze dili hizi sijawahi kushika milioni tano, zangu peke yangu. Sanasana nilishashika milioni mbili kushuka chini. Na hiyo milioni mbili ni’shaishika mara moja tu! Zaidi huwa napata laki mbili, tatu tu.
“Sasa nataka kubadilika. Umri unakwenda. Sitegemei kuyamaliza maisha yangu kwa kazi hizi za roho mkononi. Hapana. Nataka niwe na pesa nzuri nitakayoizungusha kwa biashara halali; nioe, nipate watoto, nizeeke hata kufa nikiwa na heshima yangu.” Akatulia kidogo. Akaitwaa chupa yake na kuipeleka kinywani. Akaimaliza bia iliyokuwemo. Alipoirejesha chupa mezani, akaendelea, “Kwa hiyo, Fatma, ukae ukijua kuwa kama italazimika kumuua huyo bwana’ko ili tupate hizo pesa, hatutasita kufanya hivyo.”
“Ayiii! Wewe!” Fatma alitokwa macho pima. “Yamekuwa hayo tena?”
“Ndiyo!” Kessy alijibu kwa msisitizo mkali. Akaongeza, “Beka siyo bwege kama unavyoweza kumfikiria. Haujui jinsi alivyotajirika kiajabuajabu kiasi kile. Kwa vyovyote lazima atakuwa na silaha ya kumlinda. Kwa hiyo hawezi kwenda benki kinyoronyoro ka’ mdebwedo, kudroo milioni mia moja bila ya chuma mfukoni. Haiwezekani, Fatma!
“Hebu n’ambie, unadhani kukitokea mshikemshike ataachia tu pesa zichukuliwe huku anaangalia?” Hakusubiri jibu, papohapo akajazia, “Siyo rahisi! Siyo rahisi kabisa! Lazima atajibu. Na hapo huenda mimi au yeyote kati ya wenzangu akarudisha namba. Sijali kwa wenzangu kufa, lakini kwa kweli mimi siko tayari kufa, kifo cha kijinga…”
“Hapana, Kessy,” Fatma alimkata kauli. “Hujazianza leo dili hizi. Huoni wenzio wanavyochota pesa mahala bila hata ya kusikika mlio wa risasi? Siku hizi mambo yanafanywa kisayansi! Siyo lazima kuwe na kukurukakara. Mkifanya hivyo, mnaweza kujikuta mkipambana hata na askari wa benki. Unadhani matokeo yake yatakuwa ni nini?”
“Acha woga we’ mwanamke,” Kessy alikaza uzi. “Sisi tunafanya kazi kwa uhakika na kwa kujiamini. Hatubahatishi, wala hatutishwi na yale magwanda ya FFU wa benki. Labda tu unihakikishie jambo moja; unampenda sana bwana’ko?”
“Aah! Wapi! Sina maana hiyo.”
“Basi, tulia,” Kessy alinong’ona. Akamkazia zaidi macho Fatma. Kisha, kwa sauti hiyohiyo ya chini, lakini safari hii ikiwa ni sauti yenye msisitizo mkali, aliongeza,“Huwezi kujua; labda yeye anakupendea kiuno chako tu. Siku akikuchoka atakutema kama kapi la muwa. Zaidi, atakupa vijisenti vingine vichache vya kuanzia maisha huko mbele ya safari. Hii ndiyo nafasi yako ya mwisho; cheza kwa akili yako yote!”
Walizungumza kwa kirefu, na hatimaye wakafikia mwafaka. Walipoachana, kila mmoja alikuwa na mkakati wake kichwani. Kessy alizihitaji sana pesa hizo! Alitegemea upatikanaji wa shilingi milioni 50, lakini tayari Fatma kaweka bayana kuwa zitakuwa shilingi milioni 100!
Hakutarajia!
Kiwango hicho kilikuwa ni maradufu! Zilikuwa ni pesa ambazo aliamini kuwa kama angeziweka katika milki yake, basi tayari angekuwa ameutokomeza umaskini. Na hakukiona kikwazo chochote kitakachomfanya azikose pesa hizo. Kuvifumua vichwa vya marafiki zake, Matiko Kidilu na Morris Maguru, kisha akausambaratisha uso mzuri wa mrembo Fatma Mansour ilikuwa ni kazi ndogo sana kwake, kazi nyepesi kupindukia!
Fatma Mansour, kwa upande wake yeye aliwaza jinsi atakavyofanikiwa kuzipata shilingi milioni 100 zote bila ya kugawana na mtu yeyote. Akakumbuka kuwa, Beka Bagambi alihifadhi bastola nyumbani kwake. Siku moja, kiasi cha majuma mawili yaliyopita, walikwenda ufukoni mwa bahari majira ya jioni. Ni huko ambako Beka alimpa mazoezi ya kuitumia silaha hiyo kwa kulenga shabaha. Kwa siku mbili mfululizo walifanya hivyo, na Fatma alikuwa mwepesi wa kushika mafunzo. Siku ya tatu alionyesha umahiri kwa kufumua vizibo vya chupa kumi za soda kati ya chupa kumi na tano.
“Una kipaji cha kipekee, mtoto wa kike!” Beka alimwambia.
“Kwa nini?”
“Uwezo wako wa shabaha siyo wa kawaida! Wallahi nakuapia!”
“Asante,” Fatma alijibu.
Bastola hiyo ilikuwa ndani ya moja ya saraka za kabati kubwa iliyokuwa chumbani. Na Beka hakuwa na mazoea ya kutembea nayo au kuikagua. Ni juzi tu alipoifungua na kuisafisha kisha akaijaribu kwa kufyatua risasi tatu hewani. Baada ya hapo alizipachika risasi kumi ndani yake kisha akairejesha sarakani.
“Kesho nitaichukua,” alinong’ona wakati akiiacha Barabara ya Ali Hassan Mwinyi na kushika ile ya Haile Selassie Avenue, akirejea Masaki.
*****
KUKUA kwa teknolojia ya mawasiliano nchini Tanzania kumekuwa msaada mkubwa kwa wananchi tofauti na karne zilizopita hadi mwishoni mwa karne ya ishirini.
Siyo ajabu kukutana na mtoto wa miaka kumi na mitano akimiliki simu ya mkononi. Kuna simu lukuki madukani, baadhi ni zenye bei ya kutisha kwa ughali wake huku nyingine zikiwa za bei ya kuokota au kama wanavyodai wenyewe: “bei karibu na bure.”
Mwanafunzi anamiliki simu, tena mwanafunzi ambaye hata hajalinusa darasa la tano; mzururaji anamiliki simu, kibaka ana simu, mfanyabiashara, ofisa wa serikali, tapeli na kadhalika, wana simu!
Simu kila kona! Simu kwa kila mtu! Simu za aina zote!
Ni simu hizi pia ambazo zimesaidia sana katika kufanikisha mipango ya watu wengi, iwe ni mipango mikubwa kwa midogo, mizuri kwa mibaya. Kwa njia ya simu, watu wamefanikiwa kuiba mamilioni ya shilingi benki au popote. Kwa njia ya simu, wahalifu kadhaa wametiwa mbaroni kabla au baada ya kutenda uhalifu. Na, ni kwa njia ya simu hizohizo, wale wasio waaminifu katika ndoa wamefanikiwa kutimiza miadi na wapenzi wao wa pembeni kwa urahisi bila ya siri zao kuvuja.
Ndiyo, na ni simu hizo ndizo zilizowaunganisha Kessy, Matiko na Morris, dakika arobaini na tano tu baada ya Kessy kuachana na Fatma. Haikuwa kazi kubwa. Alichofanya Kessy ni kuandika ujumbe mfupi: Tukutane garden posta ya zamani baada ya nusu saa. Akautuma kwa Matiko na Morris kwa zamu. Kisha akakodi teksi akielekea huko katikati ya jiji. Nusu saa baadaye walikuwa miongoni mwa watu wachache walioketi katika bustani hiyo, wao wakiwa wamechagua sehemu ya pembeni, sehemu ambayo walihakikisha kuwa maongezi yao hayatayafikia masikio yasiyohusika.
“Mpaka dakika hii mambo yanakwenda vizuri,” Kessy aliwaambia wenzie. “Tumekubaliana kesho asubuhi mchezo uchezwe.”CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Kilichofuata ni mlolongo wa hadithi nzima kuhusu maongezi baina yake na Fatma.
“Umemaliza?” hatimaye Matiko alimuuliza baada ya kumwona katulia.
“Nimemaliza.”
“Ok, lakini bado kuna jambo ambalo haliko wazi,” Matiko aliongeza.
“Lipi?”
“Muda. Umesema tu kwamba ni kesho asubuhi. Ni asubuhi ya saa ngapi?”
“Kwa kweli hilo hatukulizungumzia,” Kessy alijibu. “Lakini haliwezi kuwa kikwazo kwetu. Cha muhimu ni kufika kwenye eneo lile tangu saa mbili asubuhi tukiwa kamili kikazi.”
Ukimya ukatawala tena kwa kitambo kifupi. “Tunachopaswa kujadili hapa ni kuhusu usafiri. Tunatakiwa kuwa na gari, tena gari lisilokuwa na hitilafu yoyote. Tutalipata wapi?” Kessy aliwatazama wenzake kwa zamu.
Kwa mara nyingine ukimya ukapita. Matiko na Morris walionekana kuzama mawazoni. Hatimaye Morris aliibuka, “Zinahitajika pesa.”
“Pesa?” Matiko alimtazama.
“Nd’o maana’ake,” Morris alisisitiza. “Kwa kuwa tunatakiwa kuwa na gari tutakalolimiliki peke yetu kwa ishu ya kesho, ni lazima tulikodi kwa pesa nyingi kidogo.”
“Gari lenyewe lipo?” Kessy alimdaka.
“Lipo. Tena ni kifaa cha uhakika.”
“Aina gani?” Matiko alihoji.
“Mark 11 ya nguvu.”
“La nani?”
“La mzee mmoja wa Magomeni Mapipa,” Morris alijibu. “Ni mtu wa madili mzee huyo. Muhimu ni kumweleza ukweli tu kwamba mnalitumia gari lake kwa dili la aina f’lani. Hapo ndipo atakapotoa chaji yake.”
“Unadhani anaweza kuchaji kiasi gani?” Kessy aliuliza.
“Siwezi kujua, lakini kwa ishu ka’ hii yetu sidhani kama itakuwa chini ya milioni.”
“S’o mbaya,” Kessy alisema. “Tuchange kiasi hicho halafu tukamwone. Keshi zikiwa mkononi hawezi kuziacha hata kama alikuwa na mpango wa kutuchaji zaidi ya hizo. Huo ndiyo uchawi wa pesa.”
Wakaafikiana hivyo.
*****
MIAKA kadhaa iliyopita, Seif Suleiman alifunga safari kutoka kwao Kigoma, katika kitongoji cha Ujiji na kulivaa Jiji la Dar es Salaam kwa minajili ya kusaka maendeleo ya kimaisha. Jijini Dar maisha hayakumwendea vizuri katika miaka miwili ya awali japo alipata hifadhi kwa rafiki yake, Robert ambaye aliishi kwa kufanya vibarua hapa na pale.
Seif naye ilimlazimu kuingia mitaani kila kukicha akisaka ajira, zoezi ambalo ni kama vile lilikuwa la kubahatisha kwani kuna wakati alifanikiwa kupata vibarua lakini vikiwa ni vile ambavyo havikudumu zaidi ya wiki tatu, nne hivi. Siku zilikwenda, miezi ikapita, hatimaye miaka miwili ikakatika.
Ndipo ikaja siku ambayo hakutarajia kuwa yangetokea hayo yaliyotukia. Siku hiyo, akiwa eneo la Masaki akihaha kusaka hivyo vibarua, mara akakutana na Salum, fundi maarufu wa ujenzi ambaye aliwahi kufanya naye kazi kiasi cha miezi mitatu iliyopita huko Oysterbay kwenye ujenzi wa jumba la mfanyabiashara maarufu nchini.
“Vipi, Seif ?” Salum alimchangamkia.
“Poa tu,” Seif alijibu kwa unyonge, macho na mavazi yake yakitangaza bayana makali ya maisha yaliyomwandama.
Haikumlazimu Salum kuchukua hata dakika moja kubaini kuwa Seif ana hali mbaya kimaisha hivyo wakiwa pembezoni mwa barabara, Salum aliamua kumvuta kando zaidi kuwapisha watembea kwa miguu. Wakasimama chini ya mti uliokuwa na kivuli kizito.
Dakika tano baadaye walikuwa wamekwishaongea kwa kirefu na ndipo Salum alipoigundua shida iliyomkaabili Seif. “Us’konde,” alimpoza. Akaingiza mkono mfukoni na kutoa bulungutu la noti. Zilikuwa ni mchanganyiko wa 10,000/-, 5,000/- na 1,000/-. Kwa makisio ya karibu Seif alihisi ni shilingi 400,000.
Salum alichomoa noti tano za 1,000 na kumpatia. Kisha akamgusa bega na kusema, “Kuna kazi mahala f’lani. Siyo ya ujenzi kama ulivyozoea, lakini malipo yake siyo mabaya.”
“Kazi gani?” Seif alimdaka.
“Kusafisha banda la ng’ombe na kuwalisha.”
“Siyo kazi ngumu. Malipo yake?”
Salum alionekana kufikiri kidogo kisha akajibu, “Nasikia ni elfu tatu kwa siku, chai na chakula cha mchana hapohapo.”
“Poa tu, nipeleke sasa hivi!”
“Sikupeleki. Nitakupa ramani. Najua huwezi kupotea.”
Alimwelekeza.
Dakika kumi baadaye Seif alikuwa nje ya jumba jingine kubwa na zuri, mali ya tajiri Yohana. Pale getini alimkuta mlinzi aliyevaa kinadhifu- sare ya kazi iliyokuwa na utambulisho wa kampuni moja ya ulinzi. Na baada ya kujieleza kwa kifupi kwamba anatafuta ajira yoyote, mlinzi huyo akamtaka asubiri wakati yeye akiingia ndani.
Dakika chache baadaye akarejea na kusema, “Ingia ndani. Utauona mlango mkubwa uko wazi. Humo utamkuta bosi mwenyewe. Ni mtu mzima bongebonge hivi.”
Seif akajitosa ndani ambako alimkuta mzee Yohana Ntuzule akiwa ameketi sofani huku kikombe cha kahawa ya moto kikiwa juu ya stuli iliyokuwa kando yake.
Baada ya kujuliana hali, kisha Seif kuzungumzia dhamira ya ujio wake, mzee Yohana alimweleza ni kazi gani iliyopo. Kisha, huku akimtazama kwa makini, alimuuliza, “Utaiweza?”
“Nitaiweza, mzee wangu,” Seif alijibu haraka.
“Malipo ni shilingi alfu tatu kwa siku; chai na chakula cha mchana juu yangu,” mzee Yohana aliongeza. “Kama uko tayari, uingie kazini sasa hivi.”
“Niko tayari, mzee.”
Mzee Yohana akanyanyuka na kumwambia: “Twende nikakuonyeshe kazi yenyewe.”
Wakaandamana hadi uani ambako Seif alionyeshwa mabanda mawili yaliyokuwa na ng’ombe wanne; wawili kila banda. Mzee Yohana akaanza kutoa maelekezo jinsi ya kuyasafisha. Katikati ya maelezo yake, mara mlio wa simu ukasikika kutoka ndani.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Mzee Yohana akashtuka. “Oh! Kaniletee simu yangu!”alimwagiza Seif. “Wahi! Iko juu ya stuli!”
Seif akatii, akiondoka kwa mwendo wa haraka kuelekea ndani. Alipoifikia stuli, akaiona simu juu yake huku kando ya stuli hiyo kukiwa na fuko la Rambo. Akaitwaa simu lakini moyo ukasita kumruhusu aondoke, akairudisha kwenye stuli. Akatupa macho kulia ambako mlango wa chumba ulikuwa wazi.Udadisi ukamjia. Akaendelea kukodoa macho huko chumbani na kuuona mfuko mdogo uliotuna ukiwa juu ya kitanda kipana na cha kifahari.
Akahisi sauti ikimwambia kuwa aingie humo chumbani. Mapigo ya moyo wake yakaongeza kasi huku ushawishi wa kuingia chumbani humo ukizidi kumbana. Hatimaye, kama aliyesukumwa na jitu lisiloonekana, akavuta hatua ndefu akiingia chumbani humo lakini kwa kunyata. Hatua tano tu akawa mbele ya kitanda kile na mara akaupeleka mkono kwenye ule mfuko. Akaufunua na kuangalia kilichomo. Alichokiona kilimshtua na kumzulia mshangao mkubwa.
Pesa!
Ndiyo, ndani ya mfuko ule kulikuwa na nyaraka chache na mrundikano wa mabunda ya noti! Moyo ukazidi kumdunda kwa nguvu. Akageuka kutazama kule sebuleni. Mara akayahamishia macho kwenye simu iliyoendelea kuita. Hakuijali simu hiyo, tayari alishajiwa na wazo jipya, wazo la kuondoka na mfuko ule!
Lakini alihisi kuna vikwazo mbele yake. Apitie wapi? Mlango wa mbele atakutana na yule mlinzi; atamwambia nini? Na, je, kama mlinzi huyo atamshtukia na kumzuia? Wazo la kupita huko mbele akalifuta papohapo. Akapiga moyo konde na kuamua kupita kulekule uani, yatakayofuata atayajulia hukohuko.
Akautwaa ule mfuko na kuondoka humo sebuleni taratibu. Muda mfupi baadaye alikuwa kule uani. Akaangaza macho kwa ukaguzi wa eneo zima lililomzunguka. Akauona mlango mdogo kwenye uzio wa ukuta. Ukuta huo ulikuwa wapata urefu wa futi tano hivi.
Kuutazama mlango kisha ukuta na halafu kuyapeleka macho kwa mzee Yohana, lilikuwa ni zoezi lililomchukua chini ya sekunde tano. Mzee Yohana alikuwa amempa mgongo, akiwatazama ng’ombe wake mabandani.
Akili ya Seif ikafanya kazi haraka. Kutoka pale aliposimama hadi kwenye ule mlango mdogo wa kutoka nje, alipaswa kutembea kati ya hatua thelathini na hamsini. Ulikuwa ni umbali ambao kwa vyovyote ungemzindua mzee Yohana. Na hapo ndipo mambo yangeharibika.
Akamtazama tena mzee Yohana, ambaye umbo lake kubwa na teketeke lilitoa taswira kuwa hawezi kuhimili kashkash zozote zitakazohitaji wepesi na nguvu. Lakini hicho hakiwezi kuwa kigezo cha kumfanya ashindwe kukitumia kinywa chake kupiga kelele zitakazomleta yule mlinzi au hata watu wengine wa mbali. Na, ni kelele hizo zitakazokuwa kikwazo kingine. Seif aliamini hivyo.
Kwa hali hiyo, aliamua kumfuata mzee Yohana ili aumalize mchezo kistaarabu. Hata hivyo, wakati akimwendea, vishindo vya miguu yake viliyafikia masikio ya mzee Yohana ambaye aligeuka kumtazama, mshangao ukijidhihirisha machoni pake kwa kumwona Seif na lile fuko la Rambo. Lakini kama alidhamiria kuhoji lolote kuhusu fuko lile, hakuipata nafasi hiyo. Teke zito lilitua shingoni mwake! Sekunde mbili baadaye mateke mengine mawili yakawa yameshatua kifuani na kumpeleka chini sawia.
Vilikuwa ni vipigo vikali, vipigo ambavyo mzee Yohana hakuvitarajia wala hakuwa na uwezo wa kuvimudu. Akiwa pale chini, alihema kwa shida, macho kayatoa pima na kuonesha dhahiri kurufaika kiakili.
Seif hakuhitaji kumtazama zaidi. Akilini mwake alimwona kuwa tayari yu mahututi na hawezi hata kutumia kinywa chake kuomba msaada. Hivyo, hakumjali, aliondoka kwa hatua ndefu, fuko la Rambo mkononi, akiufuata ule mlango ambao ulimtii mara tu alipojaribu kuufungua.
Masaki likiwa ni eneo tofauti na maeneo mengine kama vile Kariakoo, Buguruni, Magomeni, Sinza, Kigogo, Manzese na kwingineko, Seif alichekelea kimoyomoyo baada ya kutomwona mtu yeyote jirani na eneo hilo la nyumba ya mzee Yohana. Akaondoka taratibu, kwa mwendo wa kujiamini na hatimaye akatokomea.
Ni fuko hilo lililoyabadili maisha yake. Shilingi milioni 14 alizozikuta humo ndizo zilizomtoa kwenye ufukara. Mwaka mmoja baadaye hakuwa yule Seif mwenye kusaka nauli ya daladala au kumwomba bia rafikiye. La. Huyu alikuwa Seif mwingine, Seif aliyenazo, Seif ambaye mtaani aliheshimika, alithaminika na kutukuzwa.
Miaka mingi baadaye alikuwa akimiliki nyumba mbili; moja, Magomeni Mapipa na nyingine, Mbagala Kizuiani, wakati huo kazi yake kuu ikiwa ni kuwavamia wenye pesa na kuwapora akishirikiana na kundi lake. Hatimaye akanunua magari mawili madogo ya kifahari, magari ambayo upatikanaji wake ulitokana na kazi moja aliyoifanya akishirikiana na wenzake wawili kwa kuvamia duka la kubadilisha fedha mjini Morogoro na kupora fedha lukuki zikiwa ni shilingi za Tanzania, Pauni za Uingereza, Yen za Japan na Dola za Marekani.
Baada ya hapo hakuwa tena mtu wa kujitosa moja kwa moja katika ulingo wa kashkash pindi azisakapo pesa. Sasa akawa mkodishaji magari. Kila aliyemfahamu, hususan wale majambazi wakongwe, walikodi magari yake kwa minajili ya kutenda uhalifu. Morris alimfahamu mzee Seif kiasi cha mwaka mmoja uliopita, siku alipokwenda na mwenzake, Bob Kijicho kukodi gari. Walimpa shilingi laki saba kwa kutumia gari lake kwa muda usiozidi saa 24 huku wakiwa wamemweleza ukweli kuwa walidhamiria kwenda kupora fedha Oysterbay kwenye duka la kubadilisha fedha.
*****
ILIKUWA ni kawaida iliyokwishageuzwa sheria na mzee Seif kuketi kibarazani, nje ya nyumba yake akisikiliza redio. Akiwa hapo, siyo kwamba fikra zake zilizama katika matangazo ya redio, la hasha. Alikuwa na lake jambo. Mtaa huo wa Idrissa, kama ilivyo mitaa mingine ya Magomeni, nyakati za jioni watu wengi huonekana wakipita, hawa wakielekea upande mmoja na wale upande mwingine. Baadhi yao huwa ni wanawake warembo, ambao mavazi yao huwa vivutio vikubwa kulingana na maumbile yao.
Akiwa amekwishatimiza umri wa miaka 59, bado mzee Seif alikuwa ni ‘kijana.’ Hakukosa kuwakodolea macho yenye kila dalili ya matamanio mabinti hata wanawake wakubwa waliopendelea kuvaa suruali zilizowabana vilivyo maungoni au vijisketi vilivyoyaanika mapaja yao hadharani.
Japo alikuwa na mke na watoto watatu, hata hivyo mzee Seif hakutulia. Akimtamani mwanamke, na akamhitaji, pesa zitazungumza. Na mitego yake aliiweka hapo nje takriban kila siku jioni, akimkagua kwa macho kila mwanamke aliyepita hapo barabarani. Jioni hii pia alikuwa katika mitego hiyo, akimtazama kwa makini kila mwanamke aliyepita na kumkonyezea jicho yule waliyekutanisha macho.
Ni wakati akiwa katika zoezi hilo, mara akawaona watu wakimjia. Walikuwa ni wanaume wenye miili ya kikakamavu, warefu na watanashati. Aliwatazama kwa makini na kuhisi kumkumbuka mmojawao japo kwa mbali. Wakati akiendelea kuwatazama hisia za kutembelewa na askari, ugeni ambao kutokana na rekodi ya kazi zake hauwezi kuwa ni ugeni wa heri, zikamjia akilini. Hata hivyo hakubabaika.
Alijiamini; alijua jinsi ya kuzungumza nao. Hatimaye wageni hao walimfikia, na hawakuwa wengine, bali ni Kessy Mnyamani, Morris Maguru na Matiko Kidilu. Akijawa na udadisi juu ya wageni hao, mzee Seif aliamua kutowakaribishia hapo nje tofauti na anavyofanya kwa wageni wengine ambao kwake huwa ni wageni wa kawaida. Hawa watakaribishwa ndani, na kama ni watoto wa Said Mwema watajuana hukohuko ndani. Kwa ujumla alijenga hisia kuwa ugeni huo una jambo. Ndiyo, ni jambo zito, jambo ambalo ama ni la kumwingizia pesa ama ni la hatari, liwezalo kumfikisha mbele ya mkono wa sheria.
Aliwakaribisha huku akitangulia sebuleni.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Akiwa bado na tashwishi moyoni mwake, baada ya kuketi so
fani alichokoza, “Ndiyo, nadhani ujio wenu una dhamira maalum. Karibuni sana.”
“Asante, mzee,” Morris alijibu huku Kessy na Matiko wakitikisa vichwa kuashiria kukubali.
“Tumekuja kikazi, mzee,” Morris aliongeza. “Nadhani unaweza kukumbuka kuwa tulionana kiasi cha mwaka mzima uliopita.”
“Wewe au nyie wote?” mzee Seif alimkazia macho Morris.
“Mimi na wewe.”
Mzee Seif aliachia tabasamu dhaifu, tabasamu alilolikata muda mfupi baadaye na kumkazia tena macho Morris. “Ni hilo lililokuwa likinisumbua kichwani tangu nilipowaona,” hatimaye alisema kwa utulivu. “Tukiacha hawa wengine, wewe sura yako siyo ngeni machoni pangu.”
“Ni kweli, hujakosea.”
“Mara ya mwisho tulionana wapi na lini?” mzee Seif aliendelea kumdadisi.
“Hapahapa.”
Mzee Morris aliguna. “Hapa?!”
“Ndiyo.”
“Kwa dili gani?”
“Ilikuwa ni kuhusu usafiri,” Morris alijibu. “Tulikuwa tukihitaji gari kwa ajili ya kazi f’lani.”
“Gari…” mzee Seif alitamka kwa sauti ya chini kama anayezungumza peke yake, macho kayakaza juu ya zulia.
“Ndiyo. Nilikuwa na Bob Kijicho….”
“Ahaaa! Basi, tosha. Nimekumbuka.” Sasa uso wa mzee Seif ukang’ara mwonekano wa kujiamini. “Enhe, sema basi, kuna kazi?”
Nyuso za Kessy na Matiko zikapambwa na tabasamu. Wakajenga imani ya mafanikio. Wakamtazama Morris kwa namna ya kumwambia, wewe ndiye dereva…
Morris alielewa. Papohapo akajibu, “Hatukuja kupiga stori, mzee. Tunataka gari.”
“Gari, sio?” hatimaye alisema kwa sauti ya chini, macho yakiwa yameganda kwa Morris.
“Nd’o maana’ake.”
“Kwa kazi gani?”
“Kama kawaida.”
“Sijakuelewa,” uso wa Mzee Seif ulibadilika ghafla, lile tabasamu likayeyuka mithili ya donge la barafu lililotupwa motoni. Akamtazama Morris kwa macho makali. Kisha akaongeza, “Sitaki mambo ya riwaya za vitabuni au magazetini hapa. Zungumza kwa kifupi, kitu kinachoeleweka. We’ vipi?”
Ndipo Morris alipoamua kupasua jipu, akamweleza kwa uwazi dhamira ya ujio wao.
Kilikuwa ni kikao kilichodumu kwa takriban nusu saa na mwafaka ukapatikana. Mzee Seif akapewa shilingi milioni moja na kuahidiwa kurejeshewa gari lake saa 8 mchana, akikabidhiwa katika eneo la Tegeta.
Gari hilo, Toyota Mark 11 lenye mvuto mkali, lilibadilishwa vibao vya nambari za usajili na kubanduliwa vielelezo vyote vilivyokuwa kwenye kioo, vielelezo ambavyo vingeweza kumtia matatizoni mzee Seif mbele ya vyombo vya dola kama kutatokea uchunguzi wowote. Rangi yake nyeupe iliachwa vilevile.
“Mimi huwa siyo mtu wa kuzidiwa akili,” mzee Seif aliwaambia wakati wa kuhitimisha makabidhiano. “Najua mnafukuzia mamilioni ya pesa, lakini hayo hayanihusu, n’nachotaka ni gari langu tu, likiwa salama na kwa wakati tuliokubaliana. Hila yoyote dhidi ya gari langu haitawafikisha popote. Naomba mtambue hivyo. Mkisikia kuna mtu anaitwa SEIF basi ndiye mimi! Seif, mzaliwa wa Tongwe! Kigoma!”
**MCHEZO unaelekea pazuri……..gari imepatikana….aliyewaazima naye ni yuleyule ‘misheni tauni’…..nini kitaendelea katika sakata hili……….FATMA naye hajatulia yupo katika harakati za kuzibeba milioni mia zote…..NANI KUIBUKA KINARA.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
ITAENDELEA…
0 comments:
Post a Comment