Simulizi : Domo La Mamba
Sehemu Ya Tatu (3)
Ndipo Morris alipoamua kupasua jipu, akamweleza kwa uwazi dhamira ya ujio wao.
Kilikuwa ni kikao kilichodumu kwa takriban nusu saa na mwafaka ukapatikana. Mzee Seif akapewa shilingi milioni moja na kuahidiwa kurejeshewa gari lake saa 8 mchana, akikabidhiwa katika eneo la Tegeta.
Gari hilo, Toyota Mark 11 lenye mvuto mkali, lilibadilishwa vibao vya nambari za usajili na kubanduliwa vielelezo vyote vilivyokuwa kwenye kioo, vielelezo ambavyo vingeweza kumtia matatizoni mzee Seif mbele ya vyombo vya dola kama kutatokea uchunguzi wowote. Rangi yake nyeupe iliachwa vilevile.
“Mimi huwa siyo mtu wa kuzidiwa akili,” mzee Seif aliwaambia wakati wa kuhitimisha makabidhiano. “Najua mnafukuzia mamilioni ya pesa, lakini hayo hayanihusu, n’nachotaka ni gari langu tu, likiwa salama na kwa wakati tuliokubaliana. Hila yoyote dhidi ya gari langu haitawafikisha popote. Naomba mtambue hivyo. Mkisikia kuna mtu anaitwa SEIF basi ndiye mimi! Seif, mzaliwa wa Tongwe! Kigoma!”
“Tunaomba utuamini, mzee,” Kessy alisema. “ Shida yetu siyo gari, ni hiyo kazi tunayoifukuzia kesho. Usiwe na hofu yoyote.”
“Ok, nawatakia kazi njema. Kama mnavyoiona na mlivyoitesti, iko fiti. Haina hitilafu yoyote. Wekeni mafuta full tank ili mfanye kazi yenu vizuri. Sawa?”
“Tumekuelewa, mzee,” Morris alijibu huku akiingia garini, Kessy na Matiko wakifuatia.
Wanaume wa shoka wakaondoka. Gari likasaga lami hadi Kinondoni Mkwajuni ambako walililaza na kuahidiana kukutana asubuhi ya siku inayofuata kwa ajili ya utekelezaji wa hatua nyingine muhimu.
“Saa mbili kamili, sawa?” Kessy aliwauliza wenzie, sauti yake ikiashiria amri.
“Yeah, ni muda mzuri,” Matiko alijibu.
“Cha muhimu,” Kessy aliendelea, “Tuwe makini na ndimi zetu. S’o mtu uende kunywa bia zako huko mitaani halafu unaanza kubwabwaja ovyo, ‘Oh, kesho nitakuwa milionea; ooh, kesho nitaufukuza umaskini; ooh, s’jui hivi s’jui vile…’ tuwe makini! Starehe zilikuwepo, zipo na zitaendelea kuwepo hadi siku ya kiama. Tafa….”
“Inatosha,” Matiko alimkata kauli. “Kati yetu hakuna mtoto mdogo wala chizi. Wote ni watu wazima, na tuna akili timamu. Tuko hapa tukijua nini tunafanya na kipi tutakachokifanya kesho.”
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
*****
SAA 2 asubuhi Mtaa wa Azikiwe ulikuwa na pilikapilika nyingi. Watu walipita upande huu na ule huku msururu wa magari ukitawala pande zote mbili za barabara. Hali hiyo ni ya kawaida kwa mitaa mingi ya katikati ya jiji la Dar, hususan kule kulikobatizwa majina ya ‘Uhindini’ au ‘Posta’ na kadhalika.
Mrundikano wa watu na kelele za jenereta kwa kipindi hicho ambacho makali ya mgawo wa umeme yalishamiri jijini, kwa mtaa huo maarufu ilikuwa ni adha tupu na hasa kwa mgeni yeyote ambaye hajaizoea hali hiyo. Hata hivyo, hayo yalijiri zaidi siku za Jumatatu hadi Ijumaa na ahueni kujitokeza siku za Jumamosi, Jumapili na siku za sikukuu.
Hii ilikuwa ni Jumanne, siku kama zilivyo siku nyingine ambazo ofisi huwa wazi. Daladala zilimiminika kituoni hapo, abiria wakipanda, abiria wakishuka jirani na jengo la Posta. Upande wa pili wa kituo hicho kuna majengo mawili makubwa ambayo ni utambulisho mkubwa wa eneo hilo; Benjamin William Mkapa Tower na jingine ni lile linalomilikiwa na Benki ya CRDB.
Gari dogo aina ya Toyota Mark 11, jeupe lilipita mbele ya benki hiyo na kwenda kuegeshwa mbele kidogo likichanganyika na teksi chache zilizokuwa hapo. Ndani ya gari hilo kulikuwa na watu watatu, wanaume ambao vioo vya giza vya gari hilo viliwahifadhi wasionwe na mtu wa nje.
Aliyekuwa nyuma ya usukani ni Morris Maguru wakati kushoto kwake aliketi Kessy Mnyamani na Matiko Kidilu. Wote walikuwa wamevaa suti nyeusi za gharama kubwa. Macho yao yalifichwa na miwani myeusi huku kofia pana zikiwa vichwani.
Morris alikuwa na bastola yenye risasi sita wakati Kessy alikuwa na silaha mbili za aina hiyo huku Matiko akimiliki bunduki ya SMG.
Mara tu Morris alipozima injini, walitulia humohumo garini wakiangaza macho kwa makini kule benki na kuyavinjari maeneo ya jirani.
“Isije ikawa tumewahi sana,” Morris alisema.
“Ni afadhali kuwahi kuliko kuchelewa,” Kessy alimdaka. “Hatutaki kupoteza chochote! Milioni moja i’shaingia mifukoni mwa mzee Seif. Hawezi kurudisha tukijitia kwenda kumwambia eti dili limefeli.”
“Lakini,” Matiko naye aliingilia. “Siku hizi wanoko wengi. Tukiendelea kujichimbia humu garini, hao madereva teksi hawatatuelewa. Wanaweza kutuchoma kwa maafande.”
“Ni kweli,” Kessy aliafiki. “Lakini kwa kuwa wewe una SMG, iweke mahala pazuri kisha utoke. Tunatakiwa tuonekane ni watu wa kawaida...”
“Hata hivyo bado tunatakiwa tuwe na hakika ya muda atakaokuja yule fala,” Matiko alimkata kauli.
“Itakuwa ngumu,” Kessy alisema kwa sauti yenye uthabiti. “Uwezo huo hatuna. Lakini kuja, lazima waje. Unadhani yule malaya wa kike ataachia donge nono hilo limpite? Lazima watakuja!”
Mara Kessy akafungua mlango na kutoka. Morris akafuatia na baada ya muda kidogo, Matiko naye alitoka. Morris alivuka barabara na kwenda upande wa pili ambako alinunua sigara na kurudi. Kessy na Matiko, wao kila mmoja alinunua gazeti na kujitia kusoma ilhali akili zao hazikuwepo kabisa katika magazeti hayo. Katika kipindi hicho, kwa macho ya wizi kila mmoja wao alikuwa akiangalia kule benki ambako waliyasubiri mawindo yao. Na wakati huohuo, kila mmoja alikuwa akiuota ‘utajiri’ uliokuwa mbele yake.
Matiko Kidilu, yeye alizipangia matumizi makubwa milioni zake nane ambazo zilikuwa mgawo wake. Alitarajia kununua kiwanja huko Mbagala Majimatitu. Alipanga kutumia shilingi milioni tatu au tatu na nusu kwa zoezi hilo na masalia ayatumie kwa kuanzisha mradi wa kumwingizia pato la kutosha kuyaendesha maisha. Jambo jingine alilolipa uzito kichwani mwake ni kuoa. Amtafute mwanamke mwenye mvuto mkali hadharani na mtundu sana kitandani. Huyo ndiye aliyestahili kuwa mkewe.
Kwa upande wa Morris Maguru, yeye hakufikiri chochote cha ziada, zaidi ya kutafuta vyumba viwili vya kupanga, vyumba vya hadhi ya juu eneo la Makumbusho ambako atavijaza samani mpya na za kisasa. Hatakosa kununua gari dogo lililokwishatumika na mabaki ya pesa ayatumie kwa kustarehe na wanawake; Dar es Salaam imtambue!
Mawazo ya Kessy Mnyamani yalikuwa tofauti na wenzake. Yeye alifikiria jinsi atakavyozinyambulisha hesabu zake kwa umakini wa hali ya juu, awazidi maarifa na kutwaa pesa zote kabla au baada ya kuwaua. Aliamini kuwa, bila ya kuwatoa roho hao wenzake, pamoja na mrembo Fatma Mansour, katu hataweza kuzimiliki kwa uhuru pesa hizo sanjari na kuzitumia kwa jinsi apendavyo.
Hata hivyo, chochote alichotarajia kukitekeleza katika kufanikisha azma yake, ni lazima kingesubiri wakati wa kugawana pato lenyewe. Aliamini hivyo, na hakuwa na wasiwasi wowote kuhusu kufanikiwa. Wala hakutaka kujenga imani kuwa kazi iliyowakabili mbele yao, dakika au saa chache zijazo itakuwa ni ya kubahatisha. Eti ni pata potea! Hapana, hilo halikumwingia akilini hata chembe.
Alijiamini!
*****
FATMA Mansour alikanyaga breki za Toyota Chaser mbele kidogo ya gari la akina Kessy. Muda mfupi baadaye Beka Bagambi aliteremka na kuanza kuelekea benki, mkononi akiwa na mkoba mweusi.
“Mshenzi kaingia,” Kessy aliwanong’oneza wenzake. Akaongeza, “Tumwache mpaka atoke na kulisogelea gari lake.”CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Akasita na kumkazia macho Matiko. “Nadhani itafaa urudi garini na uwe tayari na makini muda wote. Ukimwona analisogelea gari lake tu, toka nje haraka na umwashe. Halafu, mwaga mvua zaidi angani kuhakikisha wanoko wanapagawa. Mimi nitakuwa makini muda wote kufuatilia mzigo.”
Hapo sasa akamgeukia Morris: “Kazi itabaki kwako. Leo ndiyo nitajua kama kweli wewe ni dereva au zilikuwa ni hadithi zako tu za vijiweni.”
Baada ya kusema hivyo, alianza kutembea taratibu, akilisogelea gari la Beka Bagambi. Haikuwa rahisi kwa mtu yeyote kumtilia mashaka; utanashati wake ulimlinda. Pia haikuwa rahisi kwa mtu mwingine kumtambua, isipokuwa Fatma Mansour ambaye alimtambua pindi tu alipomtia machoni.
Hisia kuwa kundi la Kessy lilijiandaa kikamilifu zikamjia Fatma baada ya kumwona Kessy akimtupia jicho la wizi wakati akipita kando ya gari lake kwa hatua fupifupi, mikono mifukoni, akionekana kujiamini kwa kiwango cha juu.
Fatma alishusha pumzi ndefu, akapandisha vioo vya gari kisha akautwaa mkoba wake na kuufungua. Kwa kuwa hakutaka kosa lolote litendeke, kosa litakalosababisha milioni 100 zipeperuke kabla hajazitia mkononi, aliitoa bastola mkobani, akaifungua ili tu kuthibitisha kuwa risasi zilikuwemo. Kulikuwa na risasi kumi!
Hakuirejesha mkobani, alibaki akiigeuzageuza mikononi huku kila baada ya sekunde chache akitupa macho benki kisha kwa Kessy na wenzake. Kwa kiasi fulani mashaka yalimwingia moyoni, hali iliyotokana na kuwaza kuwa hii ilikuwa ni mara yake ya kwanza kujihusisha na kazi hiyo, ilhali kundi la Kessy liliishi kwa mfumo huo wa maisha.
*****
BEKA Bagambi alitoka ndani ya Benki ya CRDB, Mtaa wa Azikiwe kwa mwendo wa kawaida, mkoba wake mweusi ukiwa mkono wa kushoto. Hakuwa na wasiwasi lakini alitupa macho kulia na kushoto akiwatazama watu aliopishana nao bila ya dhamira yoyote ya kufanya hivyo. Alikuwa amebakiza hatua kama kumi tu alifikie gari ndipo lilipotokea tukio la kushtukiza.
Matiko alitoka garini haraka huku akiwa na bunduki mkononi, akamweka Beka katika shabaha nzuri kisha akafyatua risasi tatu mfululizo zilizokwenda kuzama kifuani mwake sawia! Kama anayejiuliza ni kipi kilichotokea, Beka aliduwaa, macho kayakodoa, kisha taratibu akaanguka chini chali!
Hakuvuta pumzi zaidi ya sekunde mbili!
Utulivu ulitoweka! SMG ya Matiko iliendelea kumwaga risasi ovyo angani! Watu waliokuwa katika kituo cha daladala wakaanza kuhaha wakikimbia huku na kule katika kuyanusuru maisha yao. Wakati huo Fatma alishatoka garini. Akamshuhudia Matiko akihaha na bunduki yake kwa hali ya kujiamini. Alipotupa macho upande mwingine, akamwona Kessy akiukimbilia mkoba uliokuwa kando ya mwili wa Beka. Akili ya Fatma ikafanya kazi ya ziada; tayari alishaiona dalili ya kutokomea kwa pesa zile.
Hakuduwaa, akaamua kukikwamua kikwazo cha kwanza; Matiko. Ndiyo, alimwona Matiko kuwa ni kikwazo kikubwa kwa wakati huo, hivyo risasi ya kwanza ilikifumua kichwa chake kwa shabaha kamili! Risasi hiyo ikamrusha juu Matiko na kumtupa kwenye mlingoti wa umeme, bunduki nayo ikaanguka juu ya bodi la teksi moja kati ya nne zilizokuwa zimeegeshwa hapo. Papohapo akamgeukia Kessy na kufyatua risasi mbili kwa pupa. Risasi hizo zikamkosa Kessy sentimita chache sana, zikivuma kando ya sikio lake la kulia.
Lilikuwa ni tukio ambalo Kessy hakulitarajia. Ndiyo kwanza alikuwa ameufikia ule mkoba, na wala haikumwingia akilini kuwa kungeweza kuzuka upinzani wowote dhidi yake. Hakuutwaa tena mkoba ule, badala yake kwa mshtuko mkubwa aligeuka, bastola ikiwa mkono wa kulia tayari kwa mapambano.
Macho yake yakakutana na ya Fatma. Akashangaa. Kando ya barabara hiyo kulikuwa na teksi zisizopungua tano zikisubiri abiria. Akarukia nyuma ya teksi moja na kujikinga. Sasa wakawa wakiwindana na kurushiana risasi za kushtukiza. Takriban dakika nzima ikapita wakiwa katika hali hiyo. Hatimaye, katika hekaheka hiyo risasi moja ikamparuza Kessy katika bega la kulia. Maumivu makali yakamwingia. Akasonya kwa hasira huku akiufuata tena ule mkoba.
Kasi yake katika kuufuata mkoba haikuwa ya kuridhisha. Fatma alikuwa mwepesi zaidi. Tayari alishaukimbilia mkoba na kuutwaa, kisha akakimbilia garini. Dakika iliyofuata gari hilo lilikuwa limeshaliacha eneo hilo kwa kasi ya kutisha.
Akiwa hatofautiani na mwendawazimu, Fatma alikuwa mwepesi wa kufikiri, kupanga na kutekeleza maazimio yake kwa kujiamini. Mara tu alipoling’oa gari, hakwenda mbali, alipita kwenye kituo cha mafuta kilicho jirani kisha akaishika Barabara ya Kisutu kabla hajaiacha huko mbele na kuifuata Barabara ya Zanaki. Muda mfupi baadaye alikuwa Barabara ya Bibi Titi ambako alikumbana na foleni.
Hata hivyo, foleni hiyo haikuwa kero iliyodumu kwake kwani muda mfupi baadaye magari yalianza kuserereka barabarani. Fatma alipoanza kuufuata msururu huo, kwa kutumia kioo cha ndani ya gari, akayachunguza magari yaliyokuwa nyuma yake. Moyo ukampiga paa!
Gari la akina Kessy lilikuwa limetanguliwa na gari moja tu kabla ya kumfikia. “Wananifuata!” alinong’ona, hofu ikianza kumjia tena. Akayatupa macho kushoto kwake, kitini ambako mkoba mweusi ulilala juu yake. Akashusha pumzi ndefu huku akiyarejesha macho barabarani.
Hatimaye akaingia Barabara ya Morogoro ambayo haikuwa na msongamano wa magari. Akakanyaga kibati cha mwendo kwa nguvu zaidi. Mara akachunguza kama bado gari la akina Kessy lilimwandama. Akashtuka! Walikuwa nyuma yake!
Sasa akawa amefika kwenye makutano ya barabara za Morogoro, Msimbazi na Mazengo. Wakati huo askari wa Usalama Barabarani alikuwa anasitisha magari yanayotoka katikati ya jiji yakielekea Magomeni na badala yake akayaashiria kutembea yale yaliyotoka Barabara ya Morogoro kuingia Barabara ya Msimbazi.
Gari la Fatma lilikuwa mbele. Kusimama aliona kuwa kungemvurugia mpango wake wote, hivyo, aliamua kuutumia mwanya uliokuwa mbele yake kukiuka amri ya askari; akavuka kwa kasi zaidi. Gari lililotumiwa na Kessy na Morris nalo lilimwandama lakini wakati huohuo lori tani 10 nalo lilikwishaingia Barabara ya Msimbazi kwa makeke. Likalikosakosa gari la Fatma lakini dereva hakumudu kuliepuka gari la akina Kessy; lililivaa ubavuni na kuzua kishindo kikubwa kilichoitawala anga na kuwafanya watu waliokuwa eneo hilo kukumbwa na taharuki. Toyota Mark 11 ‘mayai’ ikakunjwa, ikakunjika!
Haikutamanika!
Morris alikufa papohapo huku Kessy aliyekuwa kiti cha nyuma akipata michubuko michache usoni na katika mguu wa kulia.
Kwa Fatma aliyeishuhudia ajali hiyo kupitia kioo cha gari lake, haikumwingia akilini kuwa kuna uwezekano wa wabaya wake kunusurika. Akatabasamu kwa furaha, akijifariji kuwa wakati askari watakapoanza operesheni ya tangu kule benki hadi kiini cha ajali hiyo, yeye atakuwa kilomita nyingi nje ya Dar es Salaam akizifaidi milioni 100 peke yake!CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Aliiacha Barabara ya Morogoro na kuifuata Barabara ya Umoja wa Mataifa hadi Ali Hassan Mwinyi, moyoni mwake akiamini kuwa tayari kishamhadaa yeyote aliyedhamiria kumwandama. Akaendelea kuugandisha mguu wa kulia katika kibati cha mwendo. Toyota Chaser ikamtii!
Muda mfupi baadaye akawa nje ya geti la nyumba ya Beka. Alipotupa macho kushoto moyo ukamlipuka! Simu aliyokuwa akiitumia Beka Bagambi ilikuwa imelala kitini. Aliiacha makusudi au ilitoka mfukoni bila ya mwenyewe kujua? Vyovyote vile, lakini kitendo cha kuiona simu hiyo kulimfikirisha haraka na kumpa matumaini zaidi. Alijua kuwa kifo cha Beka Bagambi kitawafanya askari waingie kazini. Kama wataipata simu hiyo, kwa vyovyote ingekuwa ni hatua mojawapo katika kumfikisha na yeye mikononi mwao. Akaizima na kuiweka mkobani.
Haraka akateremka na kwenda kubonyeza kengele ambayo alijua kuwa Debora angetambua kuwa ni yeye au Beka. Hata dakika moja haikutimu, geti likafunguliwa. Debora alikuwa mbele yake.
“Nifuate,” Fatma alimwamuru huku akitangulia ndani, mwendo wake ukiwa ni wa haraka tofauti na ambavyo Debora alizoea kumwona.
Walipokwishafika ndani, bila hata ya kuketi Fatma akamhoji, “Kwenu wapi?”
“Kwetu?” Debora alimtazama kwa mshangao.
“Jibu swali. Sina muda wa kupoteza!”
“Makambako.”
“Umetoka Makambako ukaja hapa, au ulikutana na Beka hapahapa Dar?”
“Alimtuma mtu kuja Makambako kutafuta msichana wa kazi.”
Fatma akashusha pumzi ndefu. Hakuwa katika hali ya kawaida, hata Debora alimshuku. Aliangaza macho huku na kule bila kuutua ule mkoba. Kisha tena akamgeukia Debora. “Unakwenda kwenu; sawa?” alimwambia kwa msisitizo.
“Bee?” Debora hakuyaamini masikio yake.
“Jiandae, unakwenda kwenu!”
“Kwani…”
“ Hakuna maswali! Unakwenda kwenu!”
Hakukuwa na mjadala. Msichana alitii amri.
Wakati msichana huyo akikusanya vijiguo vyake na vikorokoro vingine vilivyomhusu, Fatma alikuwa chumbani ambako alifungua saraka moja ya kabati na kutoa funguo za gari jingine la Beka; Jeep Cherokee. Akaziweka katika himaya yake. Kisha akafungua saraka nyingine ambako alitoa mafurushi ya noti na kuzipachika katika mkoba uleule uliozua sokomoko kule mjini.
Akaendelea kuangaza macho huku na kule chumbani humo. Mara akaikumbuka albamu ya picha. Ndani ya saraka nyingine kulikuwa na albamu kubwa ya picha alizopiga akiwa na marehemu Beka Bagambi enzi za uhai wake. Hakuiacha, aliitwaa na kuiweka ndani ya sanduku la nguo alizotarajia kuondoka nazo. Kadi ya benki hakuiacha, hiyo aliisokomeza ndani ya kijimfuko cha siri kwenye suruali yake ya jeans.
Kwenye mkoba wake wa kujidai nako hakukuwa haba, kulihifadhi shilingi 150,000. Hazikubaki, alizitoa na kuzifutika katika mfuko wa nyuma wa suruali. Cha mwisho, ambacho aliona ni muhimu kwake ni kitambulisho cha kupiga kura, ambacho aliamini kuwa kukiacha kungewapa mwanga askari na kuwarahisishia kazi ya kumsaka. Kitambulisho hicho kilitaja jina lake, la baba yake, la babu, kituo alichoandikishwa, na tarehe aliyoandikishwa japo hiyo haikumtia jakamoyo.
Pia, kulikuwa na picha yake, wilaya aliyozaliwa na anwani ya makazi aishiko yaani, kata, mtaa na mkoa. Hivyo, kukiacha lingekuwa ni tendo litakalomsogeza jirani zaidi na mlango wa jela. Alikitwaa na kukiweka ndani ya pochi yake.
Nini kingine? alijiuliza akitupa macho huku na kule kwa mara ya mwisho. Jaketi. Ndiyo, aliliona jaketi lake likiwa ukutani. Nalo akalitwaa na kulivaa.
Nini kingine? Hakuna. Akatoka chumbani humo, begi la nguo mkono wa kulia, mkoba wa pesa, kushoto. Alipotokeza sebuleni akamkuta msichana yule katulia sofani na mfuko wake wa nguo.
Fatma akamtazama jinsi alivyochanganyikiwa. Akamhurumia; hakujua ni kwa nini anatimuliwa ghafla kiasi kile. Hakutambua kuwa tajiri wake tayari ni marehemu, na kwamba hatua aliyochukua Fatma, ya kumrudisha kwao, ni mbinu tu ya kuuepuka mkono wa sheria.
Angemwacha hapo, ambacho kingefuata kingetoa matokeo mabaya kwake, Fatma. Kwa vyovyote vile askari wangemkuta na wangemsumbua kwa maswali ya msingi na mengine yasiyo na maana kiasi cha kuwapa mwanga wa kutosha na wakapata pa kuanzia katika kumsaka aliyesadikiwa kuwa ni mkewe marehemu Beka, mwanamke mrembo aitwaye Fatma Mansour.
Isitoshe, kitendo cha kumwacha hapo si tu kwamba kingewasaidia askari pekee, la. Huenda pia kingemfanya msichana huyo wa watu ajikute akiingia katika dunia ya misukosuko na kero zisizostahimilika. Angebebwa hadi kituo cha polisi ambako huenda asingetoka kwa kile kilichoundiwa msamiati wa Anaisaidia Polisi.
“Tayari?” alimuuliza.
“Ndiyo, mama.”
Fatma akatabasamu kidogo. “Sikia, Debora,” alimwambia. “Usishangae kuona unatakiwa kwenda kwenu ghafla hivi. Ni jambo la kawaida tu.” Akaingiza mkono mfukoni na kuzitoa zile pesa alizozikuta kwenye mkoba wake wa kujidai muda mfupi uliopita, shilingi 150,000. Akampatia Debora huku akimwambia, “Zitakusaidia huko nyumbani.”CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Debora hakuyaamini macho yake. Alizipokea pesa zile huku mikono ikimtetemeka. Pamoja na kutimiziwa mahitaji yake madogomadogo huku pia akilipwa mshahara wa shilingi 30,000, hata hivyo haikuwahi kumjia ndoto ya kuja siku atakayokabidhiwa kiasi hicho cha fedha. Kwake zilikuwa ni fedha nyingi.
“Ok, twende,” aliambiwa.
Wakafuatana hadi kwenye gari la Jeep. Mara tu walipokwishaingia akalitia moto, swichi ikaitika. Akakanyaga kibati cha mwendo taratibu, na taratibu vilevile akiiachia klachi. Jeep ikamtii. Akaanza kuiacha nyumba hiyo taratibu huka picha ya Beka akilishwa risasi za kifuani, akaduwaa kama asiyeamini, macho kayatoa pima- ikamjia kichwani.
Akatikisa kichwa kwa masikitiko huku akizidi kuongeza mwendo. Robo saa baadaye alikuwa Mbezi Mwisho akiitoka Dar es Salaam kwa kasi ya kutisha baada ya kumwacha Debora kando ya kituo cha mabasi ya mikoani, Ubungo.
Jeep Cherokee likasaga lami!
*****
Ajali ya lori aina ya Scania tani 10 lililoligonga gari dogo aina ya Toyota Mark 11 kwenye makutano ya barabara za Morogoro, Msimbazi na Mazengo ilizua mkusanyiko mkubwa wa watu. Idadi kubwa ya waliokuwa wakisubiri usafiri katika kituo cha daladala cha Fire walikimbilia eneo hilo la tukio.
“Mamaa!” mwanamke mmoja alisikitika pindi alipomwona dereva wa gari dogo alivyobanwa na bodi.
“Duh! Babaa’ake, atapona mtu hapo?” kijana mmoja alikuwa kama aombolezaye.
Kwa ujumla eneo hilo lilikuwa na hekaheka tupu. Takriban kila aliyefika hapo ama alishangaa ama alisikitika. Ni mtu mmoja tu ambaye ajali hiyo haikumwathiri kisaikolojia. Mtu huyo ni Kessy Mnyamani, mmoja wa waliokuwa ndani ya gari dogo. Yeye, muda mfupi tu baada ya ajali, japo kwa kiasi fulani alibanwa na bodi la gari hilo, hata hivyo alijitahidi kuvumilia. Hata pale wasamaria wema walipofanikiwa kumtoa nje, hakutaka kuonekana kuwa kaumia japo kidogo.
“Unajisikiaje, anko?” mtu mmoja alimuuliza.
“Sijaumia sana,” alijibu. “Ni michubuko tu. Labda kero nyingine ni kuchafuka.”
“Hapana, usiseme hivyo, bradha,” mtu mwingine alimwambia. “Ajali s’o kitu cha mchezo. Subiri upelekwe hospitali kuchekiwa.”
Kessy aliwatazama wanaume hao wawili waliomshika mikono. Akaziona nyuso zao zilivyodhamiria kumpeleka hospitali, jambo ambalo hakuwa tayari kulitekeleza. Lakini atawashawishi vipi hadi wakubali kumwachia? Japo alihisi maumivu ya mbali sana kwenye paji la uso, katika mguu wa kulia na kwenye jeraha la risasi mkononi, hata hivyo bado aliuona ugumu wa kuwashawishi hawa wasamaria wema wamwachie. Kwa vyovyote wasingekubaliana naye, na wangemchukulia kuwa kachanganyikiwa kutokana na ajali hiyo.
Mara teksi iliegeshwa kando yao.
“Gari hilo hapo, anko,” mmoja wa waliomshika Kessy alimwambia huku akimfunga Kessy kitambaa kwenye jeraha la risasi iliyomparuza. Jeraha hilo lilisababisha damu itoke. Akaongeza: “Jitahidi twende Muhimbili ukachekiwe.”
Kwa shingo upande Kessy aliingia garini. Safari ya Hospitali ya Muhimbili ikaanza.
FATMA aliliegesha Jeep Cherokee kando ya baa moja katika kituo cha mabasi cha Msamvu, pembezoni kidogo mwa Manispaa ya Morogoro. Kutoka hapo alikodi teksi iliyokwenda kumwacha katikati ya mji ambako alikodi teksi nyingine hadi kwa rafiki yake, Sharifa aliyeishi eneo la Mji Mpya.
Alikuwa makini hivyo hata hakudiriki kumpa ukweli halisi Sharifa kuhusu kiwango cha pesa alichonacho. “Ni milioni kumi shosti,” ndivyo alivyomdanganya.
“Milioni kumi! Umeuchinja mwenzangu!” Sharifa alisema kaachia domo wazi.
“Si pesa ya kujidaia, ni ya kula tu. Lakini kiasi fulani nataka nikiweke benki, huenda kikanisaidia siku za usoni.”
“Benki! Kwenye akaunti yako! Watakunasa ka’ mlevi…”
“Hawawezi! Kule nyumbani sikuacha hata kadi ya benki ambayo huenda ikawasaidia kwa namna moja au nyingine.”
Asubuhi ya siku iliyofuata, Fatma alipeleka benki kiasi cha robo tatu ya pesa alizokuwanazo na kuzihifadhi. Kwa ujumla mambo yalikuwa shwari kwa upande wake. Hakupata msukosuko wowote. Mwezi mmoja ukakatika akiwa hapo kwa Sharifa. Lakini yalikuwa ni maisha ambayo hakuyapenda hata kidogo, maisha ambayo hayakutofautiana na mtu aliye mahabusu. Alihitaji uhuru; akutane na yeyote, aende atakako na astarehe atakavyo. Awe huru na autumie uhuru huo kwa raha zake.
Hapo kwa Sharifa alikula akitakacho lakini muda mwingi alilazimika kushinda ndani tu akihofia kukutana na watu mbalimbali ambao huenda miongoni mwao wakawa ni askari. Kama si ufungwa ni nini? Huko siyo kuyafaidi maisha, ni kuteseka. Sasa alitaka kuyafaidi maisha. Alitaka kurejea Dar, ‘atese’ na zile pesa ambazo zaidi ya robo tatu alizihifadhi katika benki moja siku ileile alipouvaa mji wa Morogoro. Hata hivyo alipoliwasilisha wazo hilo kwa Sharifa, akakumbana na pingamizi kali.
“Fatma!” Sharifa alimshangaa. “Unataka kurudi Dar?”
“Ndiyo.”CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Msonyo mkali ukamtoka Sharifa. Akabibitua mdomo kabla ya kuongeza, “Acha upuuzi, Fatma. Futa wazo hilo la kitoto kichwani mwako. Tambua kuwa kiasi cha pesa ulizochukua kitawafanya askari wakusake kwa udi na uvumba! Na katika msako wao wanaweza kuwa na dhamira mbili; ama wakutie mbaroni na kukufungulia mashtaka ama wakushinikize uwakatie mshiko.
“Pesa unazo. Unaweza kuamua kuwakatia pochi ili tu kuua soo. Lakini wale siyo watu! Siyo watu, Fatma! Hawaridhiki! Leo ukiwapa, kesho watataka tena. Sasa utawapa hadi lini? Na ukiishiwa tu, unao! Wanakutia pingu. Mchezo unahamia mahakamani. Na huko nako kama huna kitu nd’o umeumia. Utaozea jela. Hebu fikiri vizuri mdogo wangu. Usilichukulie suala hili kijuujuu.”
Yalikuwa maneno mazito akilini mwa Fatma, lakini hayakuweza kuubadili msimamo wake. Alishajenga utaratibu wa kujiamini na kuyaamini mawazo yake. Asingeweza kuitengua kanuni hiyo hata kwa mtutu wa bunduki.
Baada ya lile sakata la pale benki, vyombo mbalimbali vya habari vilitangaza, vikinukuu taarifa za Jeshi la Polisi. Taarifa hiyo ilidai kuwa mmoja wa watu wawili waliouawa nje ya Benki ya CRDB alijulikana kwa jina la Beka Bagambi mkazi wa Masaki. Mtu wa pili hakutambulika, na tukio hilo likahusishwa na ujambazi huku pia likiwa limewajumuisha watu wengine watatu, mmoja wao akiwa ni mwanamke. Kilichomfariji Fatma ni kwa kuwa taarifa hiyo haikumtaja mwanamke huyo. Hakujulikana! Kuna wanawake wangapi Dar? Ni wengi sana, na baadhi yao wameshajihusisha na matukio ya aina hiyo kama ambavyo pia ni wengi vilevile wanaomiliki au kuendesha magari.
Ni hilo lililomfanya asihofie kurejea Dar. Na pia, kuhusu ile ajali ya gari lililotumiwa na Kessy na Morris, alisikia kupitia vyombo hivyohivyo vya habari kuwa, mtu mmoja alifariki dunia na mwingine kujeruhiwa. Aliishuhudia ajali hiyo kupitia kioo cha gari lake lakini hakujua ni nani aliyeripotiwa kufa ingawa alipenda mtu huyo awe Kessy.
Hata hivyo, kuhusu Kessy, hakupenda kukisumbua kichwa kumfikiria. Alichojali yeye ni kurudi Dar es Salaam. Baas! Na msimamo huo aliuweka bayana kwa Sharifa.
“Nitacheza ninavyojua,” alimwambia. “Ninawajua askari wa siku hizi walivyo. Cha kwanza kwao ni pesa, ndipo wajibu wa kazi zao unafuata. Wangekuwa wanajua pa kuanzia katika kunitafuta, hapo sawa, ningejua kuwa nachezea moto. Lakini wako gizani. Nilikuwa nikiishi Tegeta na wazazi wangu. Si unajua?”
Sharifa alitikisa kichwa akiashiria kukubali.
“Walipofariki nikabaki peke yangu,” Fatma aliendelea. “Nilikuwa sina kitu. Shule ilishanishinda. Nilipokuwa nikienda kwenye maofisi ya watu kuomba kazi, mabosi wakawa wakinishikashika na kuniomba penzi. Ikawa kila ninayemkubalia hanipi kazi! Nd’o nikaamua kuingia viwanja ambako nilikukuta wewe mwenzangu ukiwa tayari mwenyeji. Nikazoea maisha ya viwanja. Mwenzangu ulipowini ukasepa. Mimi nilikutana na huyo Beka kiajaliajali tu pale Jolly Club. Viuno vyangu vikamchanganya, akanihamishia kwake. Hakujua sina wazazi wala hakujua kuwa nilikuwa naishi Tegeta.
“Hebu sasa n’ambie, hao wazee wa krauni watanipatia wapi? Na kwani mimi ni mhaini au gaidi ambaye serikali nzima inaweza kusimamisha shughuli nyingine na kuamua kunisaka? Usihofu. Acha n’ende, usinitie nuksi kwa hofu yako mwanamke.”
Sharifa akacheka kimbea, Fatma akampokea huku wakigongesha mikono.
Kisha Fatma akasema, “Lakini sitakuacha iviivi shosti! We ni Mungu wa pili kwangu, lazima nikupooze.”
“Yes! Hayo mambo!” Sharifa alisema kwa sauti ya deko.
Muda mfupi baadaye Fatma alimkabidhi Sharifa shilingi milioni mbili za kumfumba mdomo.
Siku iliyofuata alikwenda kituo cha Msamvu kwa ajili ya kupata usafiri wa kumrejesha Dar es Salaam, jiji alilodhamiria kulitumia katika kumwendeleza kimaisha bila ya kuwakwepa askari. Zaidi ya shilingi milioni tisini bado zilikuwa benki, na aliamini kuwa zingetosha kuanzishia biashara kubwa itakayomwingizia faida ya kuonekana, na hasa kama biashara hiyo ataifungua katika jiji hilo.
*****
Kessy hakuwa mjinga. Alitambua jinsi mkono wa serikali ulivyo mrefu na macho yake yalivyo makali. Hivyo, wakati teksi iliyombeba ikilikaribia geti la Muhimbili, yeye alikuwa akiwaza jinsi atakavyotoroka. Jeraha la risasi aliyopigwa na Fatma lilikuwa dogo sana, ni kama vile mchubuko tu, na kwa kuwa hakukuwa na mfupa ulioathirika, hakuiona sababu ya kuliwazia.
Ndiyo, alipanga kutoroka, lakini aliepuka kutumia pupa kwa kuamini kuwa hawa wasamaria watamshangaa na kumshuku kuwa ama kachanganyikiwa ama siyo raia mwema.
Hatimaye akafikishwa mbele ya daktari. Baada ya uchunguzi mdogo, daktari akamwanbia kuwa itabidi apumzishwe wodini, jambo alilolihisi mapema na ambalo hakuwa tayari kulitii. Na kwa kuwa mara tu wale wasamaria walipomfikisha mbele ya daktari waliondoka, kwake aliona nuru ya mafanikio ikianza kumwakia.
“Lakini dokta,” hatimaye alisema. “Kuna umuhimu gani wa kulazwa? Isitoshe sina pesa za kugharimia matibabu.”
Haikuwa kweli kuwa hana uwezo wa kugharimia matibabu, bali zaidi, alijiona hana tatizo lolote mwilini. Pia alikuwa na sababu ya msingi iliyomfanya apingane na kauli ya daktari. Kwa kipindi kirefu amekuwa akisakwa na Polisi kwa tuhuma mbalimbali zilizohusiana na uhalifu. Kutiwa mbaroni ni jambo aliloliepuka kwa nguvu zote. Kwa leo, kukubaliana na pendekezo hili la daktari ilikuwa ni sawa na kujipeleka mahabusu. Angekutwa wodini na kuendelea kutibiwa akiwa chini ya ulinzi.
“Kwani huna ndugu?” daktari alimuuliza.
“Sina.”CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Na hawa waliokuleta?”
“Hao ni watu waliojitolea tu baada ya ajali.”
“Kwa hiyo huna ndugu au jamaa yeyote hapa Dar, ambaye akipewa taarifa anaweza kuja kukusaidia?”
“Dokta, kwa kweli sina mtu wa kuweza kunisaidia,” Kessy alisisitiza. “Ndugu zangu wote wako nyumbani huko Handeni.”
Daktari alimtazama kwa huruma na kuonekana akifikiri jambo fulani. Hata hivyo Kessy hakumpa nafasi zaidi ya kufikiri, akanyanyuka na kusema, “Sikiliza, dokta. Usipate taabu. Acha n’ende zangu. Nikipata pesa nitakuja.”
“Lakini…”
Kessy hakuendelea kumsikiliza. Tayari alishafungua mlango na kutoka. Wanaume wawili aliopishana nao hatua chache nje ya ofisi hiyo hawakuonyesha kumjali lakini aliwatilia mashaka. Japo walivaa mavazi ya kawaida, hata hivyo sura zao zilitangaza kazi zao.
Askari!
Papohapo, kwa siri akaipapasa mifuko ya suruali na kubaini kuwa bastola zake mbili zilikuwemo. Aogope nini tena? Akaongeza kasi ya kutembea hadi nje ya eneo hilo ambako alikodi teksi iliyompeleka kwake, Mtaa wa Chemchem, Magomeni Mapipa.
****
KACHERO Mbunda alikuwa ofisini kwake wakati simu ya mezani ilipoita. Akanyanyua kiwiko na kukitega kando ya sikio.
“Afande, kuna mauaji yametokea eneo la Posta,” sauti ya upande wa pili ilimtaarifu.
“Mauaji?” kachero Mbunda alihoji kwa mshangao.
“Ndiyo, afande.”
“Saa ngapi?”
“Siyo muda mrefu, afande.”
“Ni mauaji ya aina gani?”
“Ni risasi, afande. Inaonekana majambazi wamemuua mtu aliyetoka CRDB. Wamemuua na kutoroka na fedha.”
Mbunda aliiangalia saa ya ukutani kisha akaguna. “Muda gani umepita tangu tukio lifanyike?” hatimaye alimuuliza.
“Kama…kama dakika mbili, tatu hivi zilizopita.”
Mbunda alisonya kisha akauliza, “Kwani wewe ni nani?”
“Koplo Sanga, afande.”
“Hao majambazi wameelekea upande upi?”
“Wameshika Kisutu Road.”
“Umezichukua namba za gari wanalotumia?”
“Afande, kwa kweli sikuwahi kufanya hivyo. Lilikuwa ni tukio lililokwenda haraka haraka sana!”
“Ok.”
Kachero Mbunda alikata simu haraka na kuwasiliana na Mkuu wa Kitengo cha Usalama Barabarani. “Kuna majambazi wamempora mtu eneo la Posta na kutokomea kwa gari wakipita Kisutu road. Kazi kwako, hakikisha hawatokomei!”
Alipoirejesha simu mezani akanyanyuka kitini na kutoka ofisini. Alihisi kukereka kwa taarifa hizi za mara kwa mara kuhusu ujambazi. Akatoka nje ya jengo na kusimama akiyakodolea macho magari yaliyopita kwa wingi Barabara ya Sokoine. Kijiupepo cha wastani kilichopuliza kutoka baharini kikamtia faraja ya wastani. Lakini, kama alitarajia kuendelea kuburudika kwa upepo huo, haikuwa hivyo. Sajini Kitowela, mmoja wa askari wa Kitengo cha Upelelezi alimfuata pale mtini na kumgusa bega. “Kuna ishu,”alimwambia.
“Nini tena?”
“Kuna ajali imetokea Faya.”
“Kwa hiyo?” Mbunda alimtazama huku kakunja uso. “Kwani sisi ni trafiki?”
“N’na maana’angu kukwambia hivyo. Ajali hiyo siyo ya kawaida.”
“Ni ya vipi?”
“Inadaiwa ni magari yaliyokuwa yakifukuzana, gari moja linaloendeshwa na mwanamke likifukuzwa na lililoendeshwa na mwanaume.”
Mbunda hakutaka kusikiliza zaidi. Papohapo alilifuata gari, Land Rover 110 defender lililokuwa hatua chache kutoka walipo. “Haraka sana , Faya.”
Dereva alikanyaga moto kwa mwendo wa kasi hadi kituo cha daladala cha Fire, Mbunda na Kitowela wakiwa garini. Walipofika katika eneo la ajali, walimfuata askari wa Usalama Barabarani ambaye naye alikuta tayari majeruhi kishapelekwa hospitali.
“Lakini tukio lenyewe lilikuwaje?” Mbunda alimuuliza askari huyo.
“Inasemekana gari hili lilikuwa katika mwendo mkali likilifuata gari jingine dogo ambalo liliendeshwa na mwanamke,” trafiki huyo alieleza.
“Enhe?”
“Lile gari la mbele limepotea lakini hili ndilo lililokumbwa na gari hili la Scania.”
“Umeshawasiliana na wenzio wa Magomeni na kwingineko?” Kitowela alimuuliza.
“Yeah. Nimefanya hivyo japo sidhani kama itasaidia sana.”
Mbunda akamuuliza yule trafiki, “Huyo aliyejeruhiwa kapelekwa hospitali gani?”
Trafiki alisita kidogo kisha akajibu, “Nadhani itakuwa ni Muhimbili, maana’ake hata waliompeleka nasikia ni wasamaria wema walioishuhudia ajali hiyo. Mtu ambaye hakufahamu hawezi kukupeleka hospitali ya pesa. Kwa vyovyote itakuwa ni Muhimbili.”
“Twende,” Mbunda alimwambia Kitowela.
Haoo! wakaelekea Muhimbili. Moja kwa moja hadi kwa daktari. Kwa jinsi walivyokuwa na haraka, hawakujali kumtazama yeyote ambaye walikutana naye. Na wakati wakikaribia mlangoni kwa daktari wakapishana na mtu ambaye naye alionyesha kuwa na haraka akitoka ofisini kwa daktari.
Hawakumjali. Waliingia ofisini kwa daktari bila ya kubisha hodi, Mbunda akiusukuma mlango na kutangulia kuingia. “Ndio, dokta, samahani kwa kukuvamia,” Mbunda alisema huku akimtazama daktari kwa macho makavu. Daktari alibaki kaduwaa, akiwatazama. Mbunda akaendelea, “Sisi ni askari kutoka kituo kikuu. Tunahitaji kujua kama umeshampokea mtu yeyote aliyejeruhiwa katika ajali ya gari muda mfupi uliopita.”
Daktari alivua miwani na kuyafikicha macho kisha akawakodolea askari hao mithili ya atazamaye kitu cha kustaajabisha.CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
“Tunakuuliza wewe dokta!” Mbunda alimsisitizia.
“Yeah, ni kweli kuna mtu ametoka hapa muda huuhuu. Tena yawezekana mmepishana naye hapo mlangoni.”
“Sasa hivi?” Kitowela alihoji.
“Sasa hivi!” daktari alijibu kwa mkazo. “Amekataa hata kupumzika. Anadai hana pesa na tena eti hajaumia sana. Kwa kweli alionekana kutotulia. Ametoka haraka sana!”
“Ulimuuliza jina lake?” Mbunda alimuuliza.
“Kwa kweli sikuwahi kufanya hivyo. Kama nilivyowaambia, mtu mwenyewe alikuwa macho juujuu!”
Mbunda hakuiona sababu ya kuendelea kuwa humo ndani ya ofisi ya daktari. Wakatoka haraka bila hata ya kuaga.
“Sasa hii ni biashara kichaa,” Mbunda alimwambia Kitowela wakati wakirudi garini. “Nadhani la kufanya sasa ni kumjua marehemu yule aliyeporwa pesa. Tutakapopata taarifa za kumhusu nadhani ndipo tutakapokuwa na la kufanya.”
Wakarudi ofisini.
****
KICHWANI mwa Kessy, hakupaona pale Magomeni alikopanga chumba kuwa palistahili kuendelea kuishi baada ya sekeseke hilo la benki. Alishahisi mdudu mbaya kishaivamia biashara yao. Hivyo alichukua nguo zake chache na akiba ya pesa zake, shilingi laki mbili, akaondoka kimyakimya bila hata ya kumuaga mwenye nyumba wala yeyote kati ya wapangaji wenzake. Haukuwa muda wa kumwamini yeyote.
Safari yake ilikomea kwa Chaupele Kandile, rafikiye, jambazi mstaafu aliyeishi Kinondoni Moscow. Pesa zake zilikuwa nyenzo ya kumfanya apate hifadhi ya siri na kutafutiwa muuguzi aliyempatia matibabu ya siri hapohapo kwa Chaupele.
Katika hifadhi hiyo mpya, Kessy hakuwa mtu wa kutembea mitaani. Asubuhi aliagiza magazeti na kushinda ndani akiyasoma. Na kwa siku mbili mfululizo, baada ya lile sakata la pale benki, aliziona habari hizo katika magazeti manne tofauti, lakini hazikumtisha wala kumfadhaisha. Kwake, zilikuwa ni habari za kawaida, habari zisizokuwa na uzito wowote.
Siku ya tatu magazeti hayo yakawa na habari mpya. Tukio hilo likawa limepitwa na wakati kwa vyombo vya habari na akaamini kuwa pia litakuwa limepitwa na wakati hata kwa Jeshi la Polisi.
Hatimaye mwezi mmoja ukakatika akiwa hapohapo kwa Chaupele. Sasa akiba yake ikawa imetetereka kwa kiasi kikubwa. Zile laki mbili zikawa zimeshuka hadi kubakia shilingi 50,000 tu! Lakini, kiafya alikuwa timamu. Lile jeraha la risasi aliyopigwa na Fatma likawa limepona. Zaidi, alinawiri na kunenepa, hali ambayo huenda ilitokana na kutoushughulisha mwili kwa muda mwingi.
Japo alipata hifadhi nzuri hapo kwa Chaupele, hata hivyo nafsi yake ilimsuta, akihisi kila wakati sauti ikimwambia, Usiwe mjinga, Kessy. Malaya yule wa kike ana mamilioni ya pesa zako. Msake akupatie.
Alijiona bado ana deni kubwa, deni la kumsaka Fatma ili ampatie mgawo wake, na aliamini kuwa lazima atampata, hata kama siyo leo au kesho. Alijiapiza kimoyomoyo kuwa kwa udi na uvumba lazima amsake na ampate!
Hivyo, usiku mmoja akapanga kumtaarifu Chaupele kuhusu kuondoka, taarifa ambayo ilimshangaza Chaupele pindi ilipotua masikioni mwake.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/***KESSY amepona majeraha yake, sasa yu timamu kiafya…..amekusudia kumsaka FATMA ili aweze kumchojoa pesa….kumbuka sasa hakuna urafiki kati yao bali uadui mkubwa……
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment