Search This Blog

Tuesday, 14 June 2022

DOMO LA MAMBA - 4

 





    Simulizi : Domo La Mamba

    Sehemu Ya Nne (4)





    Hatimaye mwezi mmoja ukakatika akiwa hapohapo kwa Chaupele. Sasa akiba yake ikawa imetetereka kwa kiasi kikubwa. Zile laki mbili zikawa zimeshuka hadi kubakia shilingi 50,000 tu! Lakini, kiafya alikuwa timamu. Lile jeraha la risasi aliyopigwa na Fatma likawa limepona. Zaidi, alinawiri na kunenepa, hali ambayo huenda ilitokana na kutoushughulisha mwili kwa muda mwingi.

    Japo alipata hifadhi nzuri hapo kwa Chaupele, hata hivyo nafsi yake ilimsuta, akihisi kila wakati sauti ikimwambia, Usiwe mjinga, Kessy. Malaya yule wa kike ana mamilioni ya pesa zako. Msake akupatie.

    Alijiona bado ana deni kubwa, deni la kumsaka Fatma ili ampatie mgawo wake, na aliamini kuwa lazima atampata, hata kama siyo leo au kesho. Alijiapiza kimoyomoyo kuwa kwa udi na uvumba lazima amsake na ampate!

    Hivyo, usiku mmoja akapanga kumtaarifu Chaupele kuhusu kuondoka, taarifa ambayo ilimshangaza Chaupele pindi ilipotua masikioni mwake.

    “Unataka kuondoka?” Chaupele alimuuliza. “Uende wapi mapema hivi?”

    “Popote,” Kessy alimjibu. “Hilo lisikusumbue, Chaupele. Nitakwenda popote tu. Umenitunza kwa mwezi mzima! Inatosha sana.”

    “Hapana, Kessy,” Chaupele alipinga. “Usidhani kuwa umekuwa mzigo kwangu. Ondoa wazo hilo kichwani mwako. Usichukulie eti kwa kuwa siku hizi sijihusishi tena na kazi zetu, nd’o basi na urafiki wetu hauna nguvu tena. Hapana! Siyo hivyo. Sisi ni kama ndugu; tuko pamoja.”

    Akasita kidogo kisha akaendelea, “Sipendi upate matatizo wakati kuna uwezekano wa kuyaepuka. Tambua kuwa hivi sasa Jeshi la Polisi limeimarishwa vilivyo. Askari wake wakiamua kula na wewe sahani moja, nakuapia, hata kwa miaka kumi watakusaka tu…”

    “Nimekuelewa,” Kessy alimkata kauli. “Lakini unataka nikae hapa kwako mpaka lini? Utanilea ka’ kinda hadi lini? Mtu nalazimika kushinda ndani kutwa nzima nikisoma magazeti, nikicheki tivii na kusikiliza redio. Hata bia nalazimika kunywea humuhumu ndani! Hayo ni maisha gani ndugu yangu? Yaani nakuwa sitofautiani na mhaini aliyeswekwa kizuizini! Hebu jaribu kufikiria, kama zingelikuwa zile enzi zako ungeweza kuishi hivi?”CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Chaupele hakujibu, badala yake aliinamisha kichwa kwa masikitiko. Aliuona dhahiri ugumu uliokuwa mbele yake katika kumshawishi Kessy akubaliane na ushauri wake.

    “Siki’za Chaupele,” Kessy aliendelea, “Kwa sasa wewe umeshastaafu kazi hii. Na umestaafu baada ya kujipatia donge nono kwa yule Mhindi wa Mtaa wa Libya, sio?”

    “Yeah.”

    “Sasa unadhani mimi sipendi kuwa na nyumba ka’hii yako? Sipendi kuwa na fenicha ka’ hizi zako? Sipendi kuwa na mke ka’ wewe? Sipendi… sipendi… sipendi kuwa na gari ka’wewe? Sema! Unadhani sihitaji kubadilika kimaisha niachane na mfumo huu wa maisha ya roho mkononi?”

    Ukimya mzito ukatanda. Wakabaki wamekodoleana macho. Kwa kiasi kikubwa Chaupele aliuona ukweli wa maneno ya Kessy. Nguvu zikamwishia. Akalazimika kumpa uhuru ingawa alimhurumia kwa kuona kuna dalili ya hatari mbele yake.

    “Jichunge sana, Kessy,” hatimaye alimwambia kwa unyonge. “Una kazi kubwa ya kuwakwepa askari. Kwa kweli naiona hatari kubwa mbele yako.”

    “Us’jali,” Kessy aliachia tabasamu kubwa. “Hata mwaka jana walifanya hivyohivyo. Achana nao. Kazi kubwa niliyonayo ni kumsaka yule malaya, nimchinje kama kuku na kuchukua masalia ya pesa za Beka.”

    “Una uhakika wa kumwona tena? Na hata kama utamwona, unadhani atakupatia pesa hizo?” Chaupele alimuuliza huku akimtazama kwa namna ya kukata tamaa.

    “Ndivyo ndoto zangu zinavyon’ambia,” Kessy alijibu kwa kujiamini. “Na kwa vyovyote hawezi kuwa kishamaliza milioni mia moja. Siyo rahisi!”

    “Kama katorokea nje?”

    “Yaani...”

    “N’na maana anaweza kuwa amepaa ughaibuni; si pesa anazo!”

    “Ni chizi tu anayeweza kufanya hivyo. Kwa miaka hii ukifanya ushenzi hapa bongo na ukajitia kuvuka mpaka tu, umeumia. Utadakwa kama kuku aliyelowa, mwanangu.”

    “Inategemeana, Kessy,” Chaupele alipinga. “Yule demu anaweza kuwa alijiandaa kabla ya dili hili kufanyika na nyie mkawa mabwege mkiamini kuwa ni mwenzenu. Kama aliweza kuwapinduka pale benki, atashindwa kuwa alishayaandaa mazingira mazuri ya kutokomea hata nje ya nchi?”

    Kessy alikunja uso, akamtazama Chaupele kwa macho makali. Kisha, kwa sauti ya chini isiyoashiria furaha yoyote, alisema, “Unasema kweli. Lakini maneno ya aina hiyo ni ya kunikatisha tamaa badala ya kunifariji na kunitia matumaini.” Akashusha pumzi ndefu kisha akaendelea, “Moyoni mwangu najisikia kuamini kuwa Fatma yupo. Tena yupo Dar hii-hii! Na zile pesa anazo; hakuzikimbizia benki. Anazo hapo alipojichimbia. Zinaweza kuwa zimepungua, lakini bado atakuwa na kitita cha kutosha. Nitampata, na kiasi chochote nitakachokipata kwake kitanitosha.”

    Mara akanyanyuka. Akamshika mkono Chaupele na kusema kwa msisitizo mkali: “Us’jali msh’kaji wangu. Yote maisha. Mungu akipenda tutaonana tena, na kama nitakufa, basi. Lakini kama itatokea tukaonana tena, naamini hatutatofautiana sana kimaisha.”



    *****





    Aliondoka asubuhi ya siku iliyofuata baada ya kuongezewa nguvu ya kiuchumi na Chaupele aliyempatia fedha taslimu shilingi 100,000. Akiwa na bastola mbili zenye risasi, pesa mfukoni na shibe ya chai nzito tumboni, alitembea kwa kujiamini, akikiacha kitongoji cha Kinondoni Moscow taratibu.

    Kwa mwonekano, huyu hakuwa yule Kessy wa kabla ya lile sakata la pale benki. La, huyu alikuwa tofauti sana. Awali, alikuwa na umbo la wastani, si mnene si mwembamba. Pia, alishajenga mazoea ya kunyoa upara kichwani na kutoziruhusu ndevu kuchomoza kidevuni. Kimavazi, alikuwa akipendelea kuvaa suruali za jeans na fulana, tukiachilia mbali ile siku ya mshikemshike pale benki, alipotinga suti nyeusi yenye thamani ya kutisha.

    Asubuhi hii alipotoka kwa Chaupele alikuwa amebadilika. Alikuwa ameongezeka umbo na alinawiri. Kidevuni kulifurika sharafa na kichwani alikuwa amevaa kofia pana. Mashati makubwa na suruali za kufungia mkanda tumboni ni mtindo alioamua uwe wa kudumu katika mabadiliko hayo. Isitoshe, miwani myeusi haikukosa machoni. Kwa ujumla alibadilika.

    Kituo chake cha kwanza baada ya kuondoka kwa Chaupele kilikuwa ni Tandale, kitongoji alichoamini kuwa isingekuwa rahisi kukamatwa na askari. Huko alikodi chumba Machungwa Guest House, moja ya nyumba za wageni za daraja la chini na iliyotoza kodi nafuu, shilingi 3000 tu kwa saa 24!

    Katika ukaguzi wake kwenye chumba alichoonyeshwa, aliugundua uduni wa kitanda ambacho kilibeba chaga zilizokwishalegea na godoro ambalo halikustahili kutazamwa mara mbili kutokana na uchakavu wake. Shuka pia zilichefua kwa kujaa madoadoa ya rangi tofauti.

    Kwa ujumla kilikuwa ni chumba ambacho kilidhihirisha kuwa gesti hiyo haikustahili kuwa na leseni hai ya biashara, na hata gharama hiyo ya chumba ilistahili kushuka. Hata hivyo Kessy hakuyajali mazingira hayo, alichojali ni usalama wake. Aliamini kuwa isingekuwa rahisi kwa askari kuja kumsaka katika gesti hiyo ya hadhi ya chini, gesti ambayo asilimia kubwa ya wateja wake ni makahaba wanaokodi vyumba kwa matumizi ya saa moja au mbili tu.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Juma la kwanza katika makazi yake hayo mapya hakuwa mtu wa kuonekana hadharani nyakati za mchana. Ni pale giza lilipoingia ndipo alipotoka na kwenda kwenye grosari ya jirani ambako alipata mlo na kunywa bia mbili, tatu. Aliiacha tabia hiyo mwanzoni mwa juma la pili. Bado alidhamiria kumsaka Fatma Mansour, hivyo, akawa akitoka asubuhi na kuzuru maeneo ya katikati ya jiji katika hiyo operesheni ambayo kwa kiasi kikubwa aliichukulia kama patapotea.

    Pamoja na hayo, hakuwa na moyo wa kukata tamaa. Dhana ya kuwa mwanamume ni mtu wa kuhangaika ilijikita kichwani mwake na kumpa matumaini ya mafanikio. Kwa hali hiyo, hakuacha kuikimbia Machungwa Guest House kila kukicha na kurejea zaidi ya saa mbili usiku.

    Kuna siku alishinda eneo la bustani ya Posta ya Zamani, siku nyingine Posta Mpya, Mnazi Mmoja, Stesheni, Kivukoni, Sokoni Kariakoo na kadhalika na kadhalika.

    Katika zoezi hilo alijaribu, na alikuwa makini katika kumchunguza kila msichana aliyefanana kimaumbile na Fatma, na akayatupia macho makali magari aina ya Toyota Chaser, Mercedes Benz na Jeep Cherokee yaliyofanana kwa rangi na umbo na yale magari ya aina hiyo yaliyomilikiwa na Beka Bagambi.

    Wiki moja baada ya kulianza zoezi hilo bado hakuwa ameambulia chochote. Magari mengi yalipita machoni pake na wanawake wengi walikatisha mbele yake, lakini Fatma hakuonekana. Sasa akaanza kuishiwa nguvu, hali iliyomjia pale alipobaini kuwa amesaliwa na shilingi 50,000 tu. Ndipo fikra za kulikimbia jiji hilo zikamjia. Alikimbie jiji la Dar es Salaam na kulivaa jiji la Arusha, jiji alilolizoea kuliko hata Dar na pia aliwafahamu vizuri matajiri wa huko. Ndiyo, aende huko na kuishi katika gesti, akifanya mikakati ya kumvamia tajiri yeyote na kujipatia pesa lukuki kisha avuke mpaka na kuingia nchini Kenya ambako angeishi hadi kufa kwake.

    Lilikuwa ni wazo lililokosa upinzani akilini mwake lakini hata hivyo hakutaka kulifanyia utekelezaji wa haraka. Aliamua kuvuta siku mbili zaidi za hii operesheni yake. Baada ya siku hizo, kama bado atakuwa hajapiga hatua yoyote, kitakachofuata ni kuivaa Arusha.

    *****





    *****

    Kelele zilizuka katika eneo la Kituo Kikuu cha mabasi cha Msamvu mjini Morogoro asubuhi moja. Askari walikuwa wakiwaandama wafanyabiashara ndogondogo. Vijana wengi walikimbia huku na kule katika kuyanusuru maisha yao.

    Kijana mmoja alikimbia hadi katika baa iliyokuwa jirani na kituo hicho. Akaingia ndani akitafuta namna ya kuwakwepa askari hao. Dhamira yake ilikuwa ni kupata upenyo wa kutokea upande wa pili.

    Hakuupata upenyo huo, badala yake akageuza njia na kurudi alikotoka. Ni hapo alipokumbana na askari mmoja. Machinga akamtazama mara mbili na kujenga imani kuwa anamweza. Akamvaa na kumtwisha konde zito la uso!

    Askari huyo akaangukia meza iliyokuwa na wateja tii! Chupa za vinywaji zikaanguka na vinywaji vikawamwagikia hao wateja. Machinga huyo hakujali, akatoka mkuku akielekea nje ya baa hiyo. Mbele yake kulikuwa na magari mawili; moja ni Range Rover jeupe na jingine ni Jeep Cherokee jeusi. Machinga alikimbia na kupita mbele ya lile Jeep kwa kasi kama kimbunga cha Madagascar kikielekea ukanda wa Pwani ya Kaskazini mwa Tanzania.

    Nyuma yake, jiwe kutoka kwa mtu asiyejulikana lilimkosa sentimeta chache. Jiwe jingine likarushwa! Hilo pia halikumpata, badala yake likatua juu ya boneti la Jeep na kutoa ukelele mkubwa!

    Chinga akanusurika na kutokomea!

    Watu wakabaki wakizungumza hivi na vile. Mlinzi wa baa ile akalisogelea lile Jeep na kupatazama pale jiwe lilipotua. Watu wengine pia wakasogelea hapo. Hatimaye mmiliki wa baa naye akaenda kwenye boneti hilo na kuungana na huyo mlinzi na watu wengine. Ni hapo mmiliki alipotaka kujua kuhusu uwepo wa gari hilo. Mlinzi akasubiriwa atoe maelezo.

    “Kwa kweli hata mimi sijui ni la nani,” mlinzi alijibu.

    “Hujui?!” mmiliki alimshangaa. “Mi’ naliona hapa kila siku. Lina siku nyingi hapa! Na linaonekana halijawahi kutoka tangu lilipoegeshwa kwa mara ya mwisho.”

    “Ni kweli,” mlinzi alisema. “Nilidhani ni la mteja. Sasa siku zimepita naliona tu hapa!”

    “Jeep Cherokee,” mwenye baa alisema kwa sauti ya chini akilikagua kwa kuchungulia hadi ndani. Akaongeza, “Kifaa cha Mmarekani. Uliza bei yake usikie! Utageuka ulikotoka!”

    Mlinzi na watu wachache walioyasikia maneno hayo wakacheka huku wakitikisa vichwa kuafikiana naye.

    Kisha, kama aliyeshtuliwa na kitu akamtazama mlinzi na kumuuliza kwa sauti kali, “Yaani huna kumbukumbu yoyote kuhusu gari hili na wakati wewe uko hapa kwa saa ishirini na nne? Hapana, jaribu kukumbuka vizuri!”

    Yule mlinzi alikuna kichwa, akakunja uso na kuzama katika fikra. Kisha akatikisa kichwa. Wote waliokuwa hapo wakamsogelea na kuonekana wamejawa na shauku ya kumsikiliza.

    “Vipi, umekumbuka?” mmiliki wa baa akamuuliza.

    Kwa mara nyingine alitikisa kichwa akionyesha ishara ya kukubali. Kisha akasema, “Yeah, nimekumbuka. Kuna mdada mmoja alikuja nalo, akapaki kisha akatoka. Nakumbuka alinisalimu, lakini hakuingia ndani. Alizunguka nyuma ya gari akawa kama analikaguakagua, akaja mpaka kwenye milango, akaishikashika…lakini jinsi alivyotokomea nd’o sijui!”CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Hakuwa mteja?” mfanyakazi mwingine wa baa hiyo alimuuliza.

    “Nakwambia hakuingia. Ni kama alikuja kupaki tu.”

    Mmiliki aliguna. “Unaweza kukumbuka ni siku ngapi zimepita?”

    “Nyingi tu!” mlinzi alijibu. “ Ni zaidi ya wiki mbili!”

    “Inaonyesha!” mmiliki naye aliafiki huku akiligusagusa boneti. “Hebu cheki vumbi lilivyoshona. Lakini lazima turipoti Polisi ili wachukue hatua. Hatuwezi kukaa na gari hapa ambalo hata mwenyewe hajulikani. Labda limeibwa mahala! Au limetumika kufanyia uhalifu halafu washenzi wakaja kulitelekeza hapa.”

    Wengi wakaonekana kukubaliana na kauli yake . Na mara mtu mmoja akasema, “Tucheki kadi ya bima hapo mbele, huenda tukamjua mmiliki.”

    Wote wakaelekea kwenye kioo cha mbele, lakini kwa mshangao hawakukuta karatasi yoyote iliyobandikwa kwenye kioo hicho, zaidi kulikuwa na alama za kubanduliwa kwa karatasi hizo. Nani kazibandua, hakuna aliyejua.

    Wakawa gizani. Hatimaye mmiliki wa baa akasonya na kumgeukia mlinzi. “ Hata hivyo uwe macho,” alimwambia kwa sauti ya amri, macho kamkazia, kidole cha shahada kikimtazama mlinzi huyo kuonyesha msisitizo. “Uwe makini, ucheki ni nani atakayekuja kulichukua. Akija, lazima alipe gharama za kumtunzia. Na usimruhusu alichukue mpaka uniarifu. Sawa?”



    “Ndiyo, bosi.”



    ****



    USAFIRI wa daladala kwa safari za mijini, na mabasi makubwa kwa safari ndefu ulikuwa umeanza kutokomea katika kumbukumbu za Fatma. Ilishapita miezi mitatu na kitu tangu alipotengana na usafiri wa aina hiyo. Kwa hali hiyo, wakati alipokuwa ndani ya basi la Abood akisubiri abiria wajae, kwake ilikuwa ni kero mojawapo. Na, ni wakati huo alipolikumbuka lile gari, Jeep Cherokee ambalo alilitelekeza hapo Msamvu siku alipoingia hapo Morogoro.

    Akaangaza macho na kuliona. Lilikuwa palepale, na huenda hakuna aliyejua kuwa limetelekezwa. Akalitamani, lakini akahisi pia kuwa huenda kuna mtego wa askari, mtego unaomsubiri yeyote atakayelifuata na kuliondoa hapo.

    Moyo ukamuuma alipoifikiria thamani ya gari hilo zuri la Kimarekani. Akakumbuka jinsi lilivyomtii siku ile alipoondoka Masaki katika jumba la Beka Bagambi huku akiwa ameliweka lile fuko la mamilioni ya pesa katika kiti cha pili.

    Lakini afanye nini?

    Hana budi kutumia usafiri mwingine, na hakutaka kukodi gari japo uwezo huo alikuwanao. Ndiyo maana alilazimika kutumia takriban saa nzima ndani ya basi hilo kabla halijajaa na kuondoka.

    Saa 4.30 alikuwa akiteremka katika kituo cha Kimara Mwisho. Hakutaka kufika kituo cha mwisho cha Ubungo kwa hisia kuwa anaweza kujikuta amejipeleka kwenye ‘domo la mamba,’ ama akakumbana na Kessy Mnyamani au akajikuta akibambwa na askari kama vile kumsukuma mlevi aliyechuchumaa.

    Mazingira ya pale Ubungo Terminal yalimfanya ajenge imani kuwa hapastahili kwa kushukia. Kuna mkusanyiko mkubwa wa watu tangu alfajiri hadi usiku wa manane. Kwa mtu wa aina ya Kessy, hatakosa kuzungukia eneo lile akijaribu kucheza bahati nasibu. Atazunguka hapa na pale, leo na kesho, na huenda Mungu akawa upande wake.

    Kessy Mnyamani!

    Akilini mwa Fatma aliamini kuwa kwa uchungu alionao Kessy, ikitokea wakaonana, uamuzi atakaochukua Kessy ni kwanza kumuua kisha afikirie kumdai pesa!

    Pia alitambua fika kuwa pale kuna kituo cha Polisi na askari wanaweza kuwa wanahaha, wakimsaka baada ya kupata taarifa zake. Kwa hali hiyo, huenda pale tu atakapoteremka kutoka ndani ya basi hilo, akakumbana na pingu. Na huo ndiyo utakaokuwa mwanzo wa kuozea jela.

    Hapana, Ubungo Terminal hapafai!

    Ndipo akaamua kuteremkia hapo Kimara Mwisho.

    Kutoka hapo alikodi teksi hadi Kinondoni ambako alikodi gesti akiamini kuwa siyo rahisi kwa askari kuyagundua maskani yake hayo mapya.

    Kwa siku tatu hivi za awali katika gesti hiyo, hakuwa mtu wa kuonekana hadharani mara kwa mara. Asubuhi alitoka na kwenda katika mgahawa ulio jirani, akapata stafutahi kisha akarejea chumbani. Mchana hakutoka, aliagiza viazi mbatata na nusu kuku, akala na kisha akalala. Usiku alikwenda Stereo Club, baa ambayo haikuzidi umbali wa hatua mia mbili kutoka katika gesti hiyo, na hapo akajipatia bia mbili, tatu na nyama choma kisha tena akarejea kujichimbia gesti.

    Hata hivyo, maisha hayo kwake hayakutofautiana na kifungo cha nje; Maisha ya kujifichaficha, akihofia hata kufika mtaa wa pili! Ni lini basi ataishi kama wengine? Na atayapataje maendeleo endapo atauendeleza mfumo huo wa maisha? Pesa anazo, tena ni pesa nyingi. Lakini atazifaidi vipi pesa hizo kama ataendelea kuishi katika gesti hiyo?CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Hapana, hakuwa radhi kuendelea kuishi hivyo. Alihitaji kuwa na nyumba yake ambayo angeijaza samani za kisasa kisha anunue gari la kuringia mitaani. Hisia za kukamatwa na askari hazikuwa na nguvu tena kichwani mwake. Alijenga imani kuwa askari wa Tanzania ni wepesi wa kuliweka kando suala la kumsaka mhalifu aliyepotea zaidi ya mwezi mmoja na hakuna fununu ya wapi alikokimbilia.

    Kwa jinsi alivyolizoea jiji la Dar es Salaam, aliamini kuwa asingekosa nyumba ya kununua eneo la Kigamboni au Mbagala, nyumba ambayo thamani yake haitazidi shilingi milioni 15 . Katu halikumjia wazo la kutafuta kiwanja au nyumba katika maeneo ya Mbezi, Kimara au Bunju. Alijua jinsi watu wengi wanavyoyathaminisha maeneo hayo. Kwa shilingi milioni 15, atakachoambulia labda ni kiwanja. Hivyo, alipanga siku inayofuata aende benki kuchukua kiasi fulani cha pesa kisha aanze mkakati wake kwa kuwasiliana na madalali.

    Alitulia gesti akimtumia mhudumu mmoja wa gesti hiyo, mhudumu ambaye naye alimuunganisha na dalali mmoja aliyefanya kazi chapchap na baada ya saa kadhaa jibu zuri likapatikana. Nyumba iliyouzwa ilikuwa katikati ya kitongoji cha Hananasif. Ilikuwa ni nyumba chakavu, ambayo ingemlazimu Fatma kuifanyia matengenezo makubwa. Haikuwa nyumba iliyojengwa kwa matofali ya saruji, la. Ilijengwa kwa miti na udongo huku paa lake likiwa la mabati yaliyochakaa. Kwa mtazamo mwingine ni kama vile ni kiwanja kilichouzwa, siyo nyumba. Zilihitajika fedha taslimu shilingi milioni 25 ili aweze kuimiliki nyumba hiyo. Kuhusu pesa, hilo halikuwa tatizo, ni kiasi tu cha kwenda benki kuzichukua.

    Isitoshe, kama alikuwa yuko tayari kununua nyumba Mbagala yenye thamani ya shilingi milioni 15, kwa nini asinunue hii ya hapo Hananasif kwa nyongeza ya milioni 10 tu japo ingemlazimu kutumia milioni kadhaa nyingine katika kuikarabati? Mbagala ni pembezoni mwa jiji, Hananasif ni ndani ya jiji. Wazo la kununua nyumba Mbagala likaota mbawa papohapo. Hivyo, siku iliyofuata aliondoka asubuhi kwenda benki kuchukua pesa kwa ajili ya kulikamilisha suala hilo.

    *****

    Hii ilikuwa ni siku pekee kichwani mwa Kessy, siku aliyoamua kuitumia kama kilele cha zoezi lake la kumsaka mbaya wake, Fatma Mansour. Hivyo, kama kawaida yake, baada ya stafutahi alitembea taratibu hadi katika kituo cha daladala cha Sweet Corner ambako alipata usafiri uliomfikisha kituo cha Fire.

    Pale, alisubiri usafiri mwingine uliomteremsha Posta Mpya. Sasa, kama alivyokuwa akifanya siku zote, alianza kuzungukazunguka katika eneo hilo ambalo kwa asubuhi hiyo lilikuwa na watu wengi ambao ama walishuka kutoka kwenye vyombo vya usafiri ama walisubiri usafiri wa kuwaondoa hapo.

    Takriban dakika ishirini zilikatika akiwa katika zoezi hilo huku akichukua tahadhari ya kutokugundulika na askari au Fatma. Hatimaye nafsi ilimtuma aachane na eneo hilo. Akaelekea Posta-baharini ambako alidhamiria kutulia katika bustani huku akiendelea na zoezi hilo. Huko akili ya kwenda kwenye kijiwe cha kahawa ikamjia. Aliwahi kufika katika kijiwe hicho siku za nyuma na kujiburudisha kwa kinywaji hicho huku akiyafaidi maongezi ya kisiasa yaliyovitawala vinywa vya walioketi hapo.

    Alijikuta akichekea moyoni pale alipowasikia baadhi ya watu wakijinadi kuwa wanafahamiana na kiongozi wa ngazi ya juu kitaifa wa chama fulani, mwingine akidai kuwa yeye na Rais wamekubaliana kufanya biashara fulani na kadhalika na kadhalika.

    Hakuyajali maongezi yao, alikunywa kahawa huku akiwaza mbali, akiifikiria hatima ya zoezi lililomkaabili.

    Saa yake ilimwonyesha kuwa ni saa 4:30. Bado ilikuwa ni mapema sana kwa upande wake. Aliamini kuwa hadi saa 10 au 11 jioni ndipo atakapojua kuwa maharage ni mboga au mbegu. Iwe Fatma amepatikana au hajapatikana ni hadi muda huo utakapotimu ndipo atakapojua nini cha kufanya.

    Kitu kimoja kilimsumbua kichwa wakati huo. Pesa. Hakuwa na pesa za kutosha kumsaka Fatma kwa umakini wa hali ya juu. Laiti kama angelikuwa na kiasi cha shilingi milioni tatu hivi, angejua ni wapi pa kumsakia mwanamke huyo. Angeweza kumkodi mtu yeyote kumsaidia kumsaka Fatma, na pia, angeweza kuingia mahali popote mathalan katika hoteli kubwa-kubwa au hata Ikulu kwa kutumia pesa zake.

    Akiwa katika bustani hiyo alichoma sigara moja hadi nyingine huku macho yake yakiendelea na zoezi lililomweka hapo. Zaidi ya saa nzima aliwaona watu wengi na magari mengi lakini kama ilivyokuwa katika siku zilizopita, bado hakuambulia chochote cha kumsaidia.

    Akaamua kubadili mazingira; akili ikamtuma atembee kidogo katika kunyoosha viungo. Mara tu aliposimama alitupa macho huku na kule, lakini akashtuka kidogo. Kwenye varanda ya jengo kubwa la NBC watu kadhaa wa jinsia tofauti walipita, hawa wakienda huku na wale wakienda kule. Baadhi yao walikuwa wakiingia ndani ya jengo hilo kupata huduma za kibenki.





    Kilichomshtua ni pale macho yake yalipotua kwa msichana mmoja mrefu aliyevaa miwani ya jua, fulana jeupe, suruali ya jeans na viatu vya mchuchumio akitembea kwa madaha. Kwa ujumla mwanamke huyo alivutia kwa tembea yake na vaa yake. Akiwa na mkoba begani, mwanamke huyo alitembea kwa hatua ndefu akilifuata jengo la benki. Hakuonekana kuwa na wasiwasi wowote! Alijiamini!

    Macho na hisia za Kessy ziliganda kwa mwanamke huyo. Akaitoa miwani na kumkodolea macho kwa makini zaidi. Kwa kiasi fulani alijiona yu ndotoni; eti yule amwonaye siye mtu halisi amfikiriaye wala kumtafuta. Lakini ni ndoto gani imjiayo mtu saa 5 adhuhuri wakati akiwa katikati ya jiji, kelele za magari zikivuma masikioni mwake huku akiwa na kumbukumbu sahihi ya kuzinduka usingizini mapema asubuhi na kutengana na kitanda hadi alipoiacha Tandale na kuja huku katikati ya jiji?

    Siyo ndoto, alijisemea kimoyomoyo huku akiendelea kumkodolea macho mwanamke huyo. Alianza kuamini kuwa huyo amwonaye siyo kwamba kamfananisha, la hasha. Ni mwenyewe! Ni yule aliyeisumbua akili yake hadi muda huo.

    “Ni yeye!” alinong’ona huku akizidi kumkazia macho.



    *****

    Akiwa timamu kiakili na kimaumbile, Fatma Mansour hakuiona sababu ya kumfanya ahofie chochote. Alijiamini, na hakuwa na sababu ya kutojiamini. Kiwango cha pesa alizozihifadhi katika benki hiyo ya NBC kilitosha kumtia kiburi cha kujiamini. Isitoshe, ndani ya huo mkoba wake mweusi kulikuwa na ile bastola yenye akiba ya risasi tano, bastola ambayo hakuwa radhi kuachana nayo isipokuwa pale tu atakapokuwa bafuni au chooni. Kwa hali hiyo, kwa nini asijiamini?

    Wasiwasi wa nini?

    Aogope nini?

    Amwogope nani?CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Tangu alipokifumua kichwa cha Matiko Kidilu pale benki tayari ubongo wake ulizibuka. Na kushuhudia Beka Bagambi akizamishiwa risasi za kifuani kulimwondolea ule moyo wa kibinadamu. Sasa alilichukulia suala la kuua mtu kama vile kuua mende au panya; ni tendo dogo, tendo la kawaida na lisilohitaji moyo wa ujasiri wala ukatili.

    Sasa huyu hakuwa yule Fatma Mansour aliyewahi kukigeuza kiuno chake kuwa kitegauchumi cha kumpatia pesa kutoka kwa mwanamume huyu na yule. La. Huyu alikuwa Fatma mwingine, Fatma ambaye tayari ana pesa ziitwazo PESA. Ndiyo, ni Fatma ambaye hata moyo wake umeshabadilika kwa kiasi kikubwa, na sasa, alilichukulia tendo la kuua mtu kuwa ni la kuburudisha nafsi mradi tu liwe katika dhamira ileile ya kulinda maisha na masilahi yake.

    Hata wakati huu alipokuwa akipanda ngazi za jengo hili la benki, hakujali nani anamtazama kwa matamanio, nani anamwangalia kwa wivu na nani anamkodolea macho ya chuki.

    Hakujali!

    *****

    Akili ya Kessy haikutulia. Aliendelea kumtazama msichana huyo mrembo kwa makini hadi alipotokomea ndani ya jengo la benki. Hata hivyo bado hakukubali, alijawa na shauku ya kumwona kwa mara nyingine, mara atakapotoka. Na ili afanikishe azma hiyo, alivuka barabara hadi kando ya jengo la TOYOTA lililopakana na jengo la benki. Pale alisimama akivizia kumwona tena mwanamke huyo, safari hii akitaka iwe ni kwa karibu zaidi.

    Katika kuleta picha ya kutoshtukiwa na mtu yeyote, aliisogelea meza moja ya magazeti na kujitia kuyatupia macho kama aliye makini. Dakika kadhaa zilipita akiwa anayatupia macho magazeti hayo huku pia kwa chati akipiga jicho kule benki. Ndipo, hatimaye baada ya dakika kadhaa alimwona mrembo huyo akitoka ndani ya jengo la benki, akasimama na kufungua mkoba wake kabla hajaingia garini.

    Taratibu, huku akiamini kuwa miwani yake ya jua na kofia pana kichwani vilitosha kuubadili mwonekano wake wa mwezi mzima uliopita, Kessy aliiacha meza ya magazeti na kumsogelea huyo mwanamke. Wakati huo mwanamke huyo alitoa miwani yake mieusi na kupangusa macho kwa leso yake.

    Ni hapo Kessy aliposhindwa kuyaamini macho yake! Akasimama na kuganda kama barafu, macho kayakodoa bila ya kupepesa. Akakipeleka kiganja cha mkono wa kulia kidevuni huku kinywa kakiachia wazi! Hatimaye, kwa mnong’ono wenye kitetemeshi cha mbali alibwata: “Fatma!”

    Ndiyo, hakuwa akibahatisha. Sasa aliamini akionacho. Ni Fatma Mansour, mwanamke mrembo ambaye siku moja, kiasi cha mwezi mmoja na nusu uliopita wakiwa katika mpango wa kujipatia mamilioni ya pesa pale kando ya benki ya CRDB Tawi la Azikiwe, aliwazidi ujanja na kutoweka na pesa zote!

    Leo yuko machoni pake! Kulitambua hilo kulimfanya Kessy ajikute kama aliyepigwa shoti ya umeme. Na akaendelea kuduwaa hata pale Fatma alipoirejesha miwani usoni na kisha akafungua mlango wa teksi na kuingia.

    Labda Kessy angeendelea kuduwaa vilevile na kujiona yu ndotoni kama asingezinduliwa na kitendo cha teksi ile kuondoka. Naye akakurupuka na kuikimbilia teksi nyingine iliyokuwa jirani yake. “Ifuate teksi ile!” alimwamuru dereva wakati kishaketi kitini.

    “Ipi, hiyo inayokata kushoto?”

    “Ndiyo! Lakini siyo kwamba tuifikie. Iache mbali kidogo lakini isikupotee.”

    Dereva alitia moto gari na kuliondoa huku akionekana kujawa na maswali mengi ambayo alisita kuyauliza. Walilifuata gari alilokuwemo Fatma hadi eneo la makaburi ya Kinondoni. Wakati huo gari alilokuwemo Kessy lilitengwa na gari moja kati huku lile alilokuwemo Fatma likiwa mbele. Pale makaburini teksi aliyokuwemo Fatma ilikata kushoto na kushika Barabara ya Wakulima.

    “Punguza mwendo kidogo halafu uwafuate,” Kessy alimwambia dereva.

    “Kwani vipi, unataka kufumania?” dereva aliamua kuuliza huku akijitahidi kuiweka sura yake katika hali ya kawaida na kimasikhara.

    “Nd’o maana’ake,” Kessy aliongopa. “Yule mwanamke ni waifu wangu. Nashangaa nimemwona town wakati aliniaga nyumbani kuwa anakwenda Vingunguti!”

    “I see. Mbona hii ni hatari msh’kaji wangu.”

    “Us’konde. Wewe hutapata tatizo lolote.”

    Teksi ya mbele iliiacha Barabara ya Wakulima na kushika Barabara ya Ngano. Magari hayo yakaendelea kufuatana huku waliokuwa gari la mbele wakiwa hawajui chochote kuhusu gari lililo nyuma yao. Hatimaye gari la mbele likasimama kando ya jengo moja katikati ya kitongoji cha Hananasif. Fatma akateremka na kutokomea ndani ya jengo hilo.

    “Pitiliza hadi pale mbele,” Kessy alimwambia dereva teksi.

    Wakati wakiipita ile teksi, Kessy alitupa macho kwenye gati la nyumba ile na kuona maandishi makubwa: KONGO GUEST HOUSE.

    Akashusha pumzi ndefu.





    *****



    KUTOKA Kituo Kikuu cha Polisi hadi kwenye mgahawa wa Meals, jirani na hoteli ya New Africa, Kitowela, askari ambaye hakuwa amevaa sare za jeshi hilo hakuhitaji kutumia usafiri. Alitembea taratibu, akifuata Barabara ya Sokoine huku akiburudishwa na kijiupepo cha wastani kilichopuliza asubuhi hiyo.

    Alipofika Posta ya Zamani alikuta watu waliokuwa wakisubiri usafiri wa daladala za kwenda Mwenge, Ubungo, Kimara, Mbagala, Gongo la Mboto na kwingineko. Akaendelea kuvuta hatua kwa mwendo wa asteaste huku akitupa macho huku na kule bila ya kuwa na dhamira maalumu.

    Ni katika kuangaza-angaza macho huko mara akajikuta akivutiwa na mtu mmoja, mwanamume aliyevaa kinadhifu. Awali alimtazama kwa kuvutiwa tu na uvaaji wake. Ndiyo, mtu huyo alipendeza kwa kiasi chake. Alivaa kofia pana kichwani huku akiwa ameyaziba macho kwa miwani mieusi na kufuatisha shati jeupe la mikono mifupi ambalo kwa kulitazama tu utabaini kuwa ni la bei kubwa, kisha suruali ya bluu iliyotakata na viatu vyeusi vilivyong’ara vikihitimisha utanashati wake. Wakati huo mtu huyo alikuwa ameketi kwenye kijiukuta kilichoizunguka bustani, akionekana kutokuwa tofauti na wengine waliokuwa hapo, ambao walikuwa wakiburudika kwa upepo murua kutoka baharini.CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    Sekunde ya tatu baada ya kumtazama kwa kuvutiwa na uvaaji wake, sasa akahisi kuvutiwa na jambo jingine lililomfanya hata amsogelee taratibu. Walitenganishwa na umbali wa hatua kama hamsini hivi, na wakati Kitowela alipoanza kumsogelea mtanashati huyo, mara akamwona akinyanyuka na kuvuta hatua akielekea kwenye kibaraza cha jengo la TOYOTA ambako pindi alipofika alisimama na kuonekana kama anayetega jambo fulani. Kadri alivyozidi kumtazama, picha fulani ikawa ikimjia kichwani. Japo alimtazama kwa chati sana kiasi cha mtu huyo kutobaini, hata hivyo alikuwa na hakika ya kuziamini hisia zilizomjia akilini.

    Aliamini kuwa huyu mtu ni yule ambaye mara kwa mara amekuwa akilisumbua Jeshi la Polisi. Hata jina lake lilikuwa kichwani mwake; Kessy Mnyamani. Siyo kwamba Jeshi la Polisi lilikuwa likimsaka Kessy kwa kuhusika na tukio la pale kando ya Benki ya CRDB, ambako watu wawili waliuawa na mwanamke mmoja kutoweka na fuko lenye fedha lukuki, la. Jeshi la Polisi halikuwa na uthibitisho wowote kuhusu hilo.

    Lakini kumbukumbu zilizoko Polisi ndizo zilizomfanya Kitowela amshuku Kessy kwa kila tukio la uhalifu linaloripotiwa. Mara kwa mara Kessy alitiwa mbaroni kwa tuhuma kadhaa za uhalifu. Kulikuwa na ushahidi wa kutosha kumtia hatiani, lakini mara zote alipofikishwa mahakamani na kesi yake kuunguruma kwa miezi kadhaa, hatimaye kwa mshangao wa wengi aliachiwa huru.

    Kuachiwa huru na mahakama hakukumfanya Kitowela na jeshi zima la Polisi liamini kuwa tuhuma zilizomfikisha huko mahakamani zilikuwa za uongo. Hapana. Walimjua vizuri Kessy, na hata Kessy mwenyewe alijua kuwa walimjua. Mbinu alizozitumia hadi akafanikiwa kushinda kesi hizo, si Kitowela si Mbunda wala yeyote katika jeshi hilo aliyezijua. Lakini siku walipokwenda Muhimbili kumtazama mmoja wa majeruhi wa ajali ya pale Fire, na kuambiwa na daktari kuwa majeruhi huyo aliondoka haraka bila hata ya kutibiwa, ukawa mwanzo wa kuhisi jambo.

    Isitoshe, baada ya kuambiwa kuwa mmoja wa waliouawa pale posta, kando ya Benki ya CRDB ni miongoni mwa wahalifu waliokuwa wakisakwa kwa muda mrefu sambamba na dereva wa gari lililopata ajali pale Fire, ambaye pia jina lake lilikuwa katika orodha ya majambazi sugu, imani kuwa Kessy ni mmoja wa tukio la Posta zilimwingia, na alikuwa na sababu ya kumfanya aamini hivyo.

    Katika tukio moja ambalo walimtia mbaroni Kessy, washiriki wenzake walikuwa ni Matiko Kidilu na Morris Maguru. Tukio hilo lilihusu uporaji wa pesa katika duka moja la kubadilisha pesa, jijini Arusha. Tukio jingine lilikuwa ni la utekaji wa basi lililokuwa likielekea Nairobi kutoka Dar es Salaam. Watekaji walikuwa na bahati mbaya kwani dakika chache tu baada ya kulisimamisha basi hilo huku wakiwa na mavazi ya askari wa Usalama Barabarani, eneo la Chalinze, mara gari dogo la doria lilifika eneo la tukio.

    Kilichofuata ni kundi la watekaji kusalimu amri na kutiwa mbaroni. Watu hao hawakuwa wengine bali ni Kessy Mnyamani, Matiko Kidilu na Morris Maguru. Na kama ilivyotokea katika tukio la Arusha, kwa tukio hili la utekaji Chalinze, watuhumiwa walipofikishwa mahakamani waliishia kuachiwa kwa kile kilichodaiwa na mahakama; tuhuma zisizokuwa na uthibitisho dhidi yao.

    Ni hapo alipojumlisha moja na moja na kupata mbili kwa tukio la majuzi lililomwacha mkazi mmoja wa Masaki, kijana aliyeaminika kuwa ni mfanyabiashara, Beka Bagambi akiuawa muda mfupi tu baada ya kutoka benki ambako kwa mujibu wa taarifa za wafanyakazi wa benki, marehemu alikuwa ametoka kuchota kiasi cha shilingi milioni 100 katika akaunti yake.

    Uchunguzi wa maiti ya yule mmoja wa waliouawa pale Posta uliishia kuibua taarifa kuwa ni jambazi aliyewahi kutuhumiwa kwa matukio kadhaa ya uhalifu, na jina lake halisi ni Matiko Kidilu. Pia, ilibainika kuwa yule marehemu aliyekutwa kwenye gari dogo, aliyesadikika kuwa ndiye aliyekuwa dereva, aliitwa Morris Maguru, ambaye pia kumbukumbu za Polisi zilionyesha kuwa naye alishawahi kutiwa nguvuni mara kadhaa kwa tuhuma mbalimbali za uhalifu.

    Kwamba hawa wawili waliokufa ni wa kundi moja, na kwamba kuna mmoja wa tatu anayesemekana kuwa aliepuka kutibiwa Muhimbili, ilikuwa ni hali iliyotoa taswira ya kumshuku Kessy kwa asilimia mia moja. Kwa nini? Umoja wao katika matukio kadhaa yaliyopita. Ndiyo, ni hilo lililowajengea imani Polisi kuhusu Kessy. Na ni hapo walipomweka kuwa mtuhumiwa wa kwanza katika msako wa wahusika wa tukio hilo la kando ya jengo la CRDB.

    “Ni mwenyewe,” alijikuta akinong’ona kwa msisitizo. Ndipo alipoamua kutwaa simu ya kiganjani na kuwasiliana na Mbunda ambaye wakati huo alikuwa kituoni.

    Ilikuwa ni taarifa iliyomshtua Mbunda kiasi cha kujikuta akinyanyuka kitini na kuanza kuzungumza huku akitembea huku na kule kama aliyerukwa akili.

    “Una uhakika ni mwenyewe?” Mbunda aliuliza kama asiyeamini alichoambiwa.

    “Nina uhakika, afande!” Kitowela alisisitiza. “Kwa kweli sikumfananisha. Naifahamu sura yake kama nilivyoikariri sura ya mwanangu.”

    “Na unasema uko Posta ya zamani?”

    “Yeah. Niko kando ya kituo cha daladala cha magari ya kwenda Mwenge.”

    “Na yeye anafanya nini?”

    “Aah…anaonekana kama vile anamsubiri mtu, maana’ake mara anakwenda huku mara huku. Sijui ana lengo gani.”

    “Sasa sikia.”CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    “Ndiyo, afande.”

    “Hakikisha hakupotei. Mfuatilie kwa makini. Usimwachie! Una silaha?”

    “Sina, afande!”

    Kimya kifupi kikatawala. Kisha Mbunda akawa hewani tena. “Hata hivyo, kula naye sahani moja. Umenielewa?”

    “Nakuelewa, afande.”

    Ok, kutokuwa na silaha siyo kikwazo. Hakikisha unamfuata kila aendako. Na tuwasiliane. Mimi nitakufuata sasa hivi.”



    ITAENDELEA

0 comments:

Post a Comment

Blog