Search This Blog

Sunday, 19 June 2022

DUNIA RANGI RANGIRE - 3

 





    Simulizi : Dunia Rangi Rangire

    Sehemu Ya Tatu (3)



    WEWE hapana wasiwasi, mimi kwisha ongea na bana Abdilah, amesema utakuta kijana wake akikusubiria kaskazini mwa ufukwe."

    Teresia alipofika kijijini kwao, baada ya kusalimiana na mama yake na baba yake, akawauliza,

    "Ba mkubwa na ma mkubwa, hawajambo?" Mama yake akamjibu,

    "Mzee Sosongo hali yake siyo nzuri ila mkewe ye hajambo."

    "Kwani hali yake, ikoje? anaumwa?"

    "Ndiyo, anaumwa sana, kama ungejua, ungekuja na Kibe ili amuone baba yake."

    Kesho yake asubuhi,Teresia alikwenda kwa Mzee Sosongo kumjulia hali. Alipofika alimfikia mama Kibe akifagia uwanja.

    "Hodi mama",alisema Teresia.

    "Teresia huyo, karibu mwanangu."

    "Shikamoo mama."

    "Marahaba mwanangu, habari huko mjini kwenu?"

    "Huko twashukuru, maisha yanaendelea, sijui nyie hapa."

    "Hapa ni hivo hivo, hauchi hauchi, unakucha."

    "Poleni sana, nimeambiwa baba anaumwa."

    "hatujapoa maana kadiri siku zinavosonga hali inazidi kuwa mbaya, nikupokee ulivyobeba kama nivya kwetu."CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    "Nivyakwenu, zawadi toka kwa Kibe."

    "Alifanikiwa kupata kazi?, na anaendeleaje na maisha ya mjini?"

    "Kazi alipata na ameshazoea japo yupo mbali kidogo na ninapoishi."

    "Kuwa mbali au karibu na wewe si tatizo, muhimu ni kuwa amepata kazi, nisamehe mwanangu tumekuwa tu tunaongelea hapa bila kukukarisha ndani, karibu ndani mwanangu."

    "Asante, baba yupo wapi nikamsalimu?"

    "Yupo hapo chumbani, ingia tu maana sidhani kama amelala,” Teresia akaenda chumba alichokuwepo Mzee Sosongo, akabisha hodi lakini hakujibiwa. Alikuwa akimsikia Mzee akikohoa, akaamua asukume mlango na kuingia. Mzee Sosongo alikuwa amejifunika blanketi, Teresia alipomuona Mzee Sosongo alivyo dhoofu, machozi yakaanza kumtoka, akamsogelea pale alipokuwa amejilaza.

    Huku machozi yakimtoka akamuita,

    "baba, baba, baba," Mzee Sosongo akakohoa kitambo kidogo kisha akasema kwa sauti ya uchovu,

    "we - we ,u - na i - twa na - ni?"

    Huku akilia kwa kwikwi, akapenga kisha akasema,

    “Naitwa Teresia baba, umenisahau?"

    "Te-re-si-a,m-to-to wa-na-ni?"

    "Mtoto wa Kaborongo, mdogo wako."

    "Te-re-si-a ma-ma,hu-ja-mbo?"

    "Sijambo, shikamoo baba."

    "Ma-ra-ha-ba ma-ma, u-me-kuja ku-ni-ona?"

    "Ndiyo baba,unaendeleaje?"

    "Ba-do na-u-mwa ma-ma, koh koh koh koooh koh,ha-ba-ri za hu-ko u-to-ka-ko?"

    "Huko hatujambo,Kibe anawasalimu sana."

    Wakati wote huo Teresia alikuwa akitiririkwa na machozi, alimwonea huruma Mzee Sosongo alivyokuwa anaongea kwa tabu na jinsi alivyokuwa amedhoofu. Mzee Sosongo akamwambia Teresia,

    "Ki-be ha-ja-mbo?, a-li-pa-ta- ka-zi?"

    "Ndiyo baba, hajambo na kazi alipata, amenipatia pesa kidogo na sukari niwaletee."

    “Tu-na-shu-ku-ru, je mu-me-o na-ye ha-ja-mbo?"

    "Hajambo anawasalimu sana," Wakati Teresia na Mzee Sosongo wanaendelea na maongezi, mama Kibe akaingia mle chumbani, akamwambia Teresia,

    "Mwanangu, njoo huku walau upate kikombe cha chai," Teresia akanyanyuka pale alipokuwa ameketi na kumfuata mama Kibe hadi jikoni. Wakati anaendelea kunywa chai, akamuuliza mama Kibe,

    "Baba toka ameanza kuumwa, mulishawahi kumpeleka hospitali?"

    "Baba yako mbishi sana, hataki kwenda hospitali na hata hizo dawa za kizungu hazitaki, anasema eti zina sumu."

    "Kwani ni nini hasa kinachomsumbua?"

    "Miguu inavimba,anasumbuliwa na kifua na kuna wakati tumbo lilikuwa limevimba."

    "Sasa anatumia dawa gani?"

    "Anatumia dawa za mitishamba."

    "hizo dawa zimamsaidia? kwani bado anavuta kiko?"

    "tunaweza tukasema zinamsaidia maana tumbo halijavimba tena toka azianze, kiko havuti tena."

    "Je anakula vizuri?"

    "Hapana mwanangu, chakula chake ni uji na supu, chakula kigumu akila anatapika."

    "Je akipewa ndizi zilizopondwa na kuwa kama uji anatapika pia?"

    "Hicho sijawahi kumpa, labda nijaribu."

    "Hicho niachie, naomba unitayarishie ndizi na kama kuna nyama naomba uinjike jikoni."

    "Nilifikiri una haraka, unataka urudi nyumbani."

    "Leo nimekuja kushinda hapa,nitaondaoka jioni ila kama hutaki usaidizi wangu.....

    Marina akamkatisha Teresia,

    "Hapa ni kwenu na nitafurahi sana ukishinda hapa maana kila wakati ukija hapa una haraka."

    "Baasi kama ni hivyo hata kulala nitalala huku, naomba unitayarishie

    hizo ndizi nianze kuzimenya."

    "Nyama nilishainjika nilikuwa nataka nimuandalie supu,kuhusu kumenya ndizi hizo niachie maana zina utomvu."

    "Mama! mbona wataka kunifanya kama sijawahi kumenya ndizi?, sinimekulia hapa, tafadhali nakuomba uniletee hizo ndizi na kisu na wewe ukaendelee na shughuli nyingine."

    Baada ya ndizi kuiva Teresia akaziponda hadi zikawa laini kasha akachua supu na kuchanganya. Marina alipomfata jikoni akamuuliza,CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    "Haya mwanangu, niambie mapishi yanavoendelea."

    "Hebu kiangalie kama hiki akila, atatapika?"

    Marina akaweka kidogo katika bakuli na kuonja,

    "Kitamu sana, hiki atameza bila shida na hatatapika, ngoja nikuletee bakuli uweke ili nikamlishe maana hawezi kula mwenyewe."

    "Kama hawezi kula mwenyewe leo itakuwa zamu yangu ya kumlisha."

    "Utamuweza? Japo anaumwa nimbishi kweli,kwasababu wewe umepika, ngoja namie nikamlishe."

    "Hapana mama,nimekuambia leo ni zamu yangu,nipe hiyo bakuli," wakati Teresia anaendelea kumlisha Mzee Sosongo,Mzee Sosongo akamuambia,

    “Te-re-si-a ma-ma.”

    “Labeka baba."

    "ka-wa-i-da mtu a-ki-wa m-ze-e kama mi-mi,ya-bi-di ku-wa-na-si-hi

    wa-pe-ndwa wao,maana ha-tu-ju-i siku wa-la saa ma-u-ti yata-ka-po tu-kumba....

    Teresia akamkatisha Mzee Sosongo.

    "Baba mbona waongelea tena mambo ya kifo? usikate tamaa Mungu ndiyo muweza na bila shaka atakuafu."

    "Acha ni-o-ngee kwa-nza,upe-ndo na kusuluhisha pale mna-po ko-sana, ndiyo msi-ngi wa ndoa, wa-o-na mimi na ma-ma yako, japo tu-li-che-lewa kupata mto-to hatukuwahi ku-ja-ri-bu kutengana, na-ku-ambia hi-vo mana nyie vi-ja-na wa siku hizi hamkawii kuachana, mkikorofishana kido-go huo ndiyo mwisho wa ndoa, Kibe ni ndu-guyo, hu-ko alipo we-we ndiyo mle-zi wake, akipotoka mwonye na mreke-bishe, koh koh koooh kooh koh...

    Wakati Mzee Sosongo anaendelea kuongea, akapaliwa na kuanza kukohoa, akakohoa hadi akatapika kile chakula alichokuwa amekula. Marina akamwambia Teresia amwache apumzike kwanza, wakamletea maji akanywa kidogo huku akihema kwa tabu sana.

    "Mama, mi nilikuwa naona tumpeleke hospitali."

    "Mwanangu, baba yake alisema, kama kuna anaetaka amwachile laana basi ampeleke hospitali."

    "Lakini jinsi anavyoumwa hivi, angeweza kupatiwa matibabu nakupata afueni".

    "Labda ukaonge nae pengine wewe anaweza kukusikiliza."

    Teresia akarudi kule chumbani, akakuta Mzee Sosongo ametulia, akafikiri amelala, akarudi kumweleza mama Kibe.

    "Nafikiri amelala maana ametulia."

    Marina kusikia vile akastuka, akatoka pale jikoni na kwenda kumtazama Mzee Sosongo maana haikuwa kawaida yake kulala mchana. Alipofika akamuita,

    "Baba Kibe, baba Kibe", hakujibiwa, akaamua amshike mkono. Aliposhika mkono wake ulikuwa wa baridi, akawekea mkono kifuani kwake ili kuangalia mapigo ya moyo, akagundua kuwa Mzee Sosongo alikuwa amefariki. Baada ya kugundua kuwa Mzee Sosongo amefariki, akapiga kelele,

    "Uuuuwii…uuuwii, baba Kibe umeniacha mpenzi, ulikuwa rafiki, mpenzi na mume mwema kwangu, nitaishi vipi bila wewe jamani mume wangu, kwani umeniacha Sosongoo uuuwiii."

    Teresia aliposikia Marina akipiga kelele akakimbilia kule chumbani kumfuata,

    "Mama kwani imekuaje?, mbona walia? Jamani baba amefanyaje mama?"

    Marina akamjibu huku akilia.

    "Teresia mama, baba yako hatunae tena, baba amefariki Teresia."

    Teresia naye akaangua kilio na kwenda kumkumbatia Mzee Sosongo,

    "Baba, baaaba, baba kwa nini baba, kwa nini umetuacha baba, ulikuwa kiongozi wetu wa familia, tulikuwa twahitaji sana hekima zako baba, sasa umetuacha," hayo yalikuwa maneno ya Teresia, huku akilia kwa sauti ya juu. Teresia alilia hadi akaishiwa nguvu, Marina alipoona Teresia anaishiwa nguvu akamshika mkono na kumtoa pale alipokuwa amemkumbatia Mzee Sosongo na kumpeleka chumba kingine kisha akamkorogea sukari katika maji na kumpa anywe,

    "Kunywa haya maji ili upate nguvu na ujikaze maana kifo ni wajibu, tumwombee tu kwa Mungu ili ampe pumziko la amani huko aendako." Majirani waliposikia vilio, wakafika pale kwa Mzee Sosongo kujua nikipi kilichojiri. Walipotambua kuwa Mzee Sosongo amefariki, mmoja wa wazee aitwaye Njuguna akaombwa aende kwa mdogo wake Sosongo, Kaborongo akamweleze kuhusu kifo cha nduguye.





    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    BAADA ya mazishi ya Mzee Sosongo, Teresia alirudi mjini kuendele na shughuli zake. Baada ya wiki kuisha akaenda kwa bwana Kanjubai kumpa taarifa za msiba wa baba yake Kibe.

    "Sasa wewe nataka hii kijana irudi kijijini, yeye ilishaanza zoea kazi," hayo yalikuwa maneno ya Kanjubai akimueleza Teresia. Teresia akamjibu,

    "Nimekuambia kuwa baba yake mzazi amefariki hivyo lazima aende nyumbani akamwone mama yake na pia aone alipozikwa baba yake, baada ya hapo si atarudi aendelee na kazi yake?"

    "Hapo sasa mimi iko elewa wewe, kesho Moris atakwenda chukua yeye alete hapa, kwani siataweza kwenda menyewe huko kijijini?".

    "Akipakizwa katika gari la kuelekea huko kijijini atafika bila shida, sasa si utampa pesa za rambirambi?"

    "Teresia! Teresia! wewe nafikiri pesa iko okotwa? yeye anapata mshahara hiyo inatosha yeye."

    "Nafahamu kuwa anapata mshahara,lakini hii ni shida iliyompata mfanyakazi wako bwana Kanjubai, ni kiasi gani unachopata kutokana na kazi anayokufanyia? ukijali masilahi ya mfanyakazi wako nayeye atajali na kujituma kwa bidii kazini."

    "Wewe iko maneno mengi sana, basi nitaangalia chakufanya but this because of you otherwise i wouldn't give him a dime,”

    "Nashukuru kama umenielewa, sasa nataka mzigo mwingine maana ule wa mwisho haukukaa sana".

    "Hii ni kazi ya Moris, subiria yeye arudi toka huko alipoenda then atakupa".

    "Sitamsubiri nina haraka, kama wewe huwezi kunipa basi akija mweleze aniletee pale kijiweni kwangu".

    "Unataka akuletee kete ngapi?".

    "Mwambie aniletee kete tano".

    "No problem, kwa heri".

    "kwa heri Kanjubai". Kibe baada ya kujifanya uchunguzi kwa muda mrefu hakuna jibu alilopata, siku moja baada ya kazi akaambiwa kuwa ni zamu yake ya kusubiria watakao chukua malighafi ya siku hiyo.

    Akiwa amekaa katika gogo huku akiwaza jinsi wazazi wake wanaendelea, Fabian akamfata pale alipokuwa,

    "Inakuaje mtu wangu, mbona waonekana kama umehamia ulimwengu mwingine?"

    "Ooh bwana Fabi, niko poa mtu wangu na nafikiria kuhusu haya maisha."

    "Wanasema kuwa maisha ni kama kitabu kila siku unafungua ukurasa mpya."

    "Kweli mtu wangu, vipi huko juu kazi inaendaje?"

    "Huko shwari, unajua toka siku ile uniulize lile swali lako nimekuwa nakuchunguza ili nione kama we ni mtu wa siri au la."

    "Sikiliza nikuambie Fabian, mimi nilikwenda jando na jambo muhimu tuliyofunzwa ni kuwa msiri, yale yote tuliyoelezwa yaliishia kulekule porini, hivyo kama hilo ndiyo lililokuwa linakupa hofu, shaka ondoa."

    "Shaka sina tena, ndiyo maana leo nataka nikueleze ujue kinachoendelea hapa, kama utataka kuendelea kufanya kazi hapa hiyo itakuwa juu yako."

    "Sawa, nitegulie kitendawili na unieleze yote."

    "Poa, siku ile uliniuliza kuhusu haya majani munayotwanga kila siku yana kazi gani, au sivyo?"

    Kibe alipoambiwa hivyo, akamsogelea Fabian hadi wakawa wanagusana

    mabega,akamjibu,

    "Haswaa." Fabian akatabasamu kisha akaendelea,

    "Umeshawahi kusikia mmea uitwao coca?".

    "Sijawahi ila najua soda iitwayo coca".

    "Basi kuanzia leo ujue kuna mmea uitwao coca na yale majani munayotwanga ni majani ya huo mmea".

    "Kwa hiyo soda ya coca hutengenezwa na haya majani tunayotwanga kila siku?"

    "Acha papara, umeuliza swali sasa tulia kama unanyolewa ili upate majibu.”

    "Ni ile shauku ya kutaka kujua maana nimesumbua kichwa hadi nimechoka, endelea kaka."

    "Sasa yale majani yanatengenezea cocain,si unajua cocain kuwa ni nini?"

    "Sijui na sijawahi kusikia hilo neno, kwani ndiyo nini hiyo?".

    "Umewahi kusikia madawa ya kulevya?"

    "Ndiyo si wanaita unga au hashishi?".

    "Baasi huo unga ndiyo cocain au mandrax, sasa yale majani mukitwanga hapa yanachukuliwa na kupelekwa kuchemshwa hadi yatoe nta, hii nta huchanganywa na dawa nyingine pamoja na mafuta ya taa hadi mwisho unapatikana unga mweupe pee kama poda, hiyo sasa ndiyo cocain,"

    Baada Fabian kumaliza kumuelezea Kibe, Kibe hakusema kitu, alihisi mwili kumtetemeka.

    Fabian alipoona kuwa Kibe ameingiwa na woga, akamuambia,

    "Oyaa mbona umekuwa mpole ghafla kama umemwagiwa maji ya baridi?"

    "Siyo hivyo kaka hizi habari ulizonipa zimeniogofya, kusema ukweli sikutegemea kuwa kazi nifanyao ni haramu."CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    "Haya sasa umejua, na usije ukamuambia yeyote nilichokueleza maana hiyo ni siri kubwa ukiitoa ujue unakaribisha mauti yako."

    "Usijali kaka, nilishasikia sana habari za wauza unga, sasa hata hamu ya kufanya kazi tena imeisha."

    "Kazi lazima ufanye maana huumwi, we fanya kazi huku ukitafakari niliyokuambia kasha uamue kama utataka kuendelea ama la na kama ukiwaambia kuwa hutaki tena kazi yaweza ikakuletea madhila maana watakuuliza kwanini unaacha kazi."

    "Ngoja nifikirie kwanza maana hizi ni habari nzito sana kwangu, nikuulize swali?"

    "Uliza tu"

    "Hii cocain wanauzia wapi? na ushawahi kuionja kuwa ni tamu ama la?"

    "Unataka uionje?"

    "Siwezi na sitowahi kutumia hiyo kitu,nijibu basi swali langu."

    "kuhusu sehemu inapouziwa sijui ila soko lipo tena kubwa sana na kuonja niliwahi kuionja, siyo tamu, ladha yake niya uchachu."

    "Sasa kama ni chachu, wanapata raha gani kuitumia?"

    "Kile ni kilevi ndugu yangu, unanusa au unalamba kidogo baada ya muda unajihisi kuwa upo ulimwengu mwingine wenye raha zote za dunia hii."

    "Kwahiyo bado unatumia, maana unavyoielezea yaelekea umzoefu."

    "Hahaha,nimekuambia nilionja nikifikiri ni tamu kama glucose lakini sijawahi kuitumia, najua madhara yaletwayo na hizo dawa hivyo siwezi kutumia."

    "Kumbe ina madhara? mie nilifikiri ni ulevi pekeyake."

    "Ile kitu ukianza kuitumia kuiacha itakuwa shida, na usipoipata wakati itakapokuwa imekuzoea, utakuwa hoi kwa ugonjwa, kila kiungo kitakuwa kinauma".

    "Duuh! sitaki hata kuiona, nashukuru sana Fabi, kwa kunifumbulia fumbo lililokuwa linanitatiza toka nifike hapa."

    "Hakuna shida mtu wangu chamsingi haya niliyokueleza yaishie hapahapa, kama utataka upigwe risasi ya kichwa basi utoe hii siri, usije ukasema sijakuonya."

    "Shaka ondoa kaka, ngoja mie nirudi kwenye makazi yetu nikaoge maana nimechoka sana"

    "Poa, kwaheri Kibe."

    "Kwa heri kaka."

    Kibe alipofika katika makazi yao, akamkuta Moris akimsubiria. Moris akamwambia kuwa amekuja kumchukua maana Teresia amerudi toka kijijini na Mzee Sosongo anaumwa sana hivo Kibe anatakiwa aende. Kibe akajitayarisha kisha wakaondoka na Moris. Alipofika mjini akapelekwa kwa Teresia.

    Teresia alipomwona machozi yakaanza kumtoka, akamkumbatia Kibe kwa muda bila kusema lolote huku akilia kwa kwikwi. Kutokana na hali ile Teresia aliyoionyesha, Kibe moyo ukamwenda mbio, wazo likamjia kuwa baba yake atakuwa hayupo tena duniani, akajikaza kiume na kumwambia dada yake,

    "Dada mie ni mtoto wa kiume kama kuna lolote baya we nieleze tu maana mabaya na mazuri tumeumbiwa siye wanaadamu," Teresia akatulia kisha akaenda kukaa katika kochi, Kibe akamfata pale alipokaa, akakaa pembeni yake na kushika viganja vyake akamwambia,

    "Kwanza shemeji yupo wapi?" Teresia akavuta pumzi ndeefu,

    "Shemeji yako amesafiri jana atarudi baada ya wiki mbili."

    "Sawa dada nipe hali halisi uliyoikuta huko kijijini na usinifiche maana mie siyo mtoto mdogo."

    Kibe akatabasam na kumwangalia machoni,

    "Oooh Kibe mdogo wangu, kifupi nikuwa baba hatunae tena, Mzee Sosongo ametutoka." Kibe alipoambiwa hivyo alihisi kama amekatwa maini, alikuwa anahisi kulia, lakini machozi hayakutoka, akabaki kuangalia tu dari, Teresia akamkumbatia na kumwambia,

    "Usiogope kulia mdogo wangu, lia maana itakusaidia kutoa uchungu rohoni."

    Teresia alimalizia tu maneno yake, akaanza kulia tena kwa sauti. Kibe hakutokwa na machozi ila alihisi kuishiwa nguvu, wakati Teresia anaendelea kulia huku akiwa amemkumbatia Kibe, alihisi kuwa Kibe

    amekuwa mzito ghafla, akamsukuma ili amwangalie machoni lakini alikuwa amelegea.

    Teresia kuona vile akamlaza katika kochi kisha akafungua vifungo vya shati na kuanza kumpepea, baada ya muda Kibe akafungua macho, Teresia akampa maji yenye glucose akanywa.

    Baada ya muda akarudia hali yake ya kawaida na akamuuliza Teresia,

    "Baba amefariki lini?"

    "Hii ni wiki ya pili toka afariki, nilipoenda kipindi kile nilipokutumia taarifa kuwa naenda kijijini,hali yake haikuwa nzuri."

    "Sasa mbona sijapewa taarifa pindi tu alipofariki?"

    "Kibe mdogoangu, wafahamu vema mazingira ya kijiji chetu, na hupo unapofanyia kazi hakuna simu hadi mtu atoke huku aende huko kutoa taarifa."

    "Sawa dada,kesho asubuhi nataka niende nyumbani".

    "Sawa mdogo wangu."

    CHANZO:  https://deusdeditmahunda.blogspot.com/

    ITAENDELEA



0 comments:

Post a Comment

Blog