Simulizi : Dunia Rangi Rangire
Sehemu Ya Nne (4)
Kibe alipofika kijijini alimkuta mama yake akiwa na baba yake mdogo Mzee Kaborongo, Mzee Kaborongo alimuona Kibe kabla ya Mama yake, akamwambia Marina,
"Naona tumepata mgeni".
Marina alipoona kuwa mgeni ni mwanae, akasimama na kwenda kumpokea,
"Karibu mwanangu, karibu baba."
"Asante mama" Kibe akamshika mama yake mkono
"Makiwa mama."
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
"Yamepita baba, habari za huko utokako?"
"Nashukuru Mungu, shikamoo mama."
"Marahaba pole kwa safari."
"Asante."
Kibe akamfuata Mzee Kaborongo pale alipokuwa amekaa
"Makiwa baba." Mzee Kaborongo akamjibu,
"Yamepita, habari za mjini?"
"Siyo mbaya, shikamoo baba."
"Marahaba, dada yako ,Teresia hajambo?"
"Hajambo, anawasalimu sana."
"Tumezipokea, umeshazoea mji?"
"Si sana maana sehemu niliyokuwa nafanyia kazi ni mbali sana na mjini,"
Marina akaingiza mizigo ya Kibe ndani, alipotoka akatoka na mkeka na kuutandika karibu na alipokaa Kibe na Mzee Kaborongo. Kibe akaelezewa Mzee Sosongo alivougua hadi akafariki. Mzee Kaborongo akamwambia Kibe,
"Mzee Sosongo hatunae ila ametuachia msingi wakufanya ukoo wetu uendelee mbele, cha msingi ni ushirikiano kama utakuwa na jambo linakutatiza, mie nipo, usije ukasema baba yako mzazi amefariki kwahiyo huna tena wa kumkimbilia".
Kibe akamjibu,
"Sawa baba." Mzee Kaborongo akasimama akasema,
"Mama Kibe, ngoja nirudi nyumbani nikaangalie cha kufanya kabla giza halijaingia. Kibe akatoa bahasha na kumkabidhi Mzee Kaborongo,
"Baba barua yako hii nimepewa na dada nikuletee."
"Asante, ngoja niende, mengi zaidi tutaongea kesho, kwani si bado upo?"
"Ndiyo, nitakuwepo kwa muda hapa." Baada ya Mzee Kaborongo kuondoka, Kibe akamfuata mama yake ndani.
"Mama umeona zawadi nilizokuletea?"
"Sijaona maana hujaniambia kuwa kuna zawadi zangu."
"Kwa hiyo hujafungua hiyo mizigo kuona kuwa nimeleta nini?"
"Si heshima kufungua kitu ambacho hujaambiwa ufungue, kama umeniletea zawadi unatakiwa uniambie, mama zawadi yako hii nimekuletea."
"Basi mama nimekosa, nimekuletea vitenge, sijui kama utavipenda ama la maana sijui rangi uipendayo."
Mama Kibe akachukua vile vitenge na kujifunga kingine akajitanda, kasha akamuambia Kibe,
"Mbuzi wa kupewa, haangaliwi kama ana mapengo, nashukuru sana mwanangu, kuhusu rangi, rangi ile inayopendeza machoni ndiyo niipendayo nahii rangi hakika yapendeza macho, Mungu akazidishie mwanangu."
"Asante mama, nashukuru kama umevipenda, nimeleta sukari na unga wa ngano pia". Muda wa mifugo kurudi nyumbani ukawadia, Kibe akatoka kuiongoza ili iingie zizini.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Wakati Kibe anaiongoza mifugo iingie zizini, akasikia wimbo ukiimbwa redioni, baadhi ya maneno ya wimbo huo ni,
"Nyamaza kuliia, wanitia uchungu kwa kuondokewa na baba yetu...
"Baba alituasa yakuwa dunia ni rangi rangile, walimwengu ni wabaya, yapasa kuwabaini wema nawabaya...
"Baba alisema, maringo na majivuno yapasa tuyaepuke maana hapa duniani twapita, yatupasa kutenda mema na kumcha Rabana maana kwake tulitoka napia tutarejea."
Kibe aliposikia maneno yale toka redioni, machozi yakamtoka, alihisi kama anaimbiwa yeye. Aliporudi ndani Mama yake akaona Kibe amekuwa na huzuni sana na macho yake yamekuwa mekundu, akamuambia,
"Kibe mwanangu,baba yako hayupo nasi kimwili ila kiroho yupo nasi, unapohuzunika namna hiyo, huko alipo hapati pumziko la amani, atafurahi kama utakuwa unamwombea dua njema na kujibidiisha kimaisha, sote pua zetu zimeangalia chini, hiyo ina maana kuwa sote tutarudi mavumbini ambapo ndipo tulipotoka,"
Kibe hakusema kitu maana uchungu ulikuwa umemjaa rohoni, machozi yalimjaa machoni. Baada ya wiki mbili kupita toka Kibe alipofika kijijini, mama yake akamuuliza,
"Kibe, kama ni maombolezo, umeomboleza vya kutosha, je huko mjini warudi lini?" Kibe akatabasamu kisha akasema,
"Mama yaani umeshanichoka mara hii?"
"Siwezi kukuchoka mwanangu, kama ulikaa tumboni kwangu kwa muda wa miezi tisa yenye karaha na sikuchoka, sembuse wakati huu ambao unanisaidia? ninachofia ni kuhusu kibarua chako baba, hakuna laziada."
"nilikuwa nakutania tu mama, kujibu swali lako kwamba narudi lini mjini, jibu ni 'La' sitarudi tena mjini, nataka nikae hapa niangalie hii mifugo yetu".
"Kama mifugo ndiyo inayokufanya usiende, hilo lisikupe shida maana hata baba yako alikuwa haendi machungani kama alivyokuambia kipindi kile kabla hujaenda mjini kuwa kuna mtu anapewa mbuzi jike kil baada ya miezi minne."
"Huyo anaechunga, kwa mwaka atakuwa na mbuzi watatu, kama anachuka mifugo ya mabona manne, kwa mwaka atakuwa na mbuzi kumi na wawili, hivyo huo ni mtaji tosha kwake."
"Kwa hiyo unataka ubaki hapa ili ufanye hiyo kazi ya kuchunga mifugo ya watu?"
"Sina maana hiyo mama, ninachotaka mimi nikuangalia mifugo yetu nasio ya watu wengine".
"Kwani hiyo kazi uliyokuwa unafanya huko mjini, imekaje huitaki tena? au kuna mtu umemkosea huko sasa unataka ujifiche huku kijijini".
"Wala hakuna niliyekosana nae, kwanza wengi wao walinipa pesa za rambirambi walipojua kuwa nimefiwa, nimeamua tu kuwa sitaki tena kuajiriwa, nataka nijiajiri mwenyewe na ajira yangu ni hii mifugo yetu pamoja na kilimo, mjini kuna soko kubwa sana la bidhaa zitokanazo na mifugo pia mbogamboga zinaliwa kwa wingi huko."
"Haya baba, kama ndivyo ulivyoamua...
"Usihuzunike mama, chamsingi ni kuniombea heri ili nifanikiwe, kwanza hiyo kazi niliyokuwa nafanya sikuipenda, nilikuwa nasubiria tu nipate wasaa wa kutoka huko tulipokuwa."
"Ninachotaka na kukuombea ni mafanikio mwanangu, kuhusu kazi utakayofanya, mie sina kipingamizi bora iwe kazi halali mbele ya sheriana machoni pa Mungu."
"Inshaallah Mama Mungu asikie na ajibu maombi yako."
Kibe akaanza maisha rasmi ya kijijini, wakati huu akiwa na malengo ya kufanikiwa kimaisha kupitia kilimo na ufugaji. Alianza kuandaa shamba la kupanda mbogamboga, baada ya kulima kwa kukatua vizuri, akawa anapeleka mbolea ya samadi walau mifuko miwili kila asubuhi kabla ya kwenda kupeleka mifugo malishoni.
Alitengeneza vitalu, akamwaga mbegu za nyanya, vitunguu, pilipili mboga na karoti. Baada ya kuotesha, ikawa desturi yake kuamka alfajiri na mapema kwenda kunyweshea mimea yake aliyootesha,
kwakuwa kulikuwa na mto uliokuwa unapita karibu na bustani zake zilipo, hakupata shida ya kusomba maji. Teresia baada ya kupata habari kuwa Kibe hatorudi tena mjini, akaamua
kwenda kumtaarifu Bwana Kanjubai. Alipofika kwa Kanjubai, alimkuta akiongea katika simu, Kanjubai akamwonyeshea ishara yakuwa aingie na akae katika kochi. Kanjubai alipomaliza kuongea katika simu, akamsalimu Teresia na kasha kumuuliza nini kilichomleta. Teresia akamjibu,
"Aah Bwana Kanjubai, vibaya hivyo ndugu yangu, kwani siwezi kuja kukusalimia bila yakuwa na tatizo?"
"I didn’t say that, wajua I am a very busy man so niambie kama kuna tatizo au ni salamu tu because saa saba sharp natakiwa niwe nipo airpot naelekea Cape town."
"Sawa,nimekuja kukutaarifu kuwa Kibe,hatarudi tena huku kufanya kazi."
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
"Kwani yeye ameonaje hadi hataki tena kazi?"
"Nimeambiwa kuwa amesema hataki tena kazi ya kuajiriwa."
"Sasa atafanya nini huko kijijini? yeye hajui kuwa siku hizi kila kitu ni pesa?"
"Ameamua kuwa mkulima, baba yake amemuachia mifugo hivo ameona kuwa nijukumu lake kuiangalia hiyo mifugo, ukizingatia kuwa amezaliwa peke yake ni vizuri kukaa na mama yake ili amsaidie kazi maana mama yake ameshakuwa Mzee."
"Okay, nilifikiri pengine amegundua shughuli zetu so anataka kutuchomea utambi."
"Kwa hilo usihofu, Kibe hata hiyo cocain hajawahi kuisikia na hata kama ameisikia atamueleza nani? Toka azaliwe hajawahi kutoka kijijini, akienda mbali sana ni vijiji vya jirani, kusafiri kwake ni hivi nilipokuja nae huku."
Kanjubai akasimama na kwenda kusimama karibu na dirisha, akanyanyua pazia kidogo kuchungulia nje kama vile kuna anachoangalia. Alisimama pale dirishani kwa muda bila kusema kitu, kisha akageuka na kumwangalia Teresia, akasema,
"Mume wako umeongea naye mara ya mwisho lini?"
Teresia moyo ukamuenda mbio baada ya kuona Kanjubai alivyobadilika sura ghafula, akamjibu,
"Kwani hujaongea nae toka aende Lilongwe?".
"Damn it Teresia, stop beating around the bush, nimekuuliza umeongea na Samson mara ya mwisho lini, that's a simple question?"
Teresia akavuta pumzi ndefu kisha akasema,
"Toka niongee na Samson, wiki imekwisha."
Kanjubai akatoa kitambaa toka katika mfuko wa suruali yako, akasafisha miwani yake, alipoona imetakata akaivaa na kwenda kuegemeza mikono yake nyuma ya kochi alilokaa Teresia, akamwambia Teresia,
"Unaweza ukanifikiria kuwa pengine ninaover react but i'm not, kwani toka Samsom asafiri ni muda gani umepita?"
"Nafikiri ni wiki tatu na siku kadhaa, lakini nilipoongea nae aliniambia kuwa biashara si nzuri huko alipo," hayo yalikuwa maneno ya Teresia. Kanjubai akatoka pale alipokuwa ameegemeza mikono yake na kwenda kukaa kochi lililokuwa limegeukia alipokaa Teresia.
"Dont make me laugh, so anaclaim kuwa biashara siyo nzuri ndiyo maana hataki kuwasiliana na mimi? can you believe toka atoke hapa siku zote hizo hajawahi kunipigia simu? And he says biashara siyo nzuri, kwani nilimtuma akachuuze kama mchicha?"
Teresia akaanza kutokwa na kijasho chembamba, akamjibu Kanjubai,
"Kusema ukweli mimi sijui mapatano yenu kama ulimtuma akachuuze au la."
"Nilimwamini sana Samson hadi kufikia kumtuma kwenda kupeleka mzigo wa millions of shilings, sijui ni ibilisi gani aliyeingia kichwani mwake."
"Au pengine amepatwa na matatizo huku sie twamlaumu tu," Teresia alimwambia Kanjubai huku akikwepa kumwangalia machoni.
"Siku zote nikimtuma Lilongwe namwambia apeleke mzigo kwa mr Makuya, but Mr Makuya nimewasiliana nae anasema hajamuona, mwanzo nilifikiri kama ulivyosema kuwa pengine amepatwa na matatizo so nikaamua kutumia my souces kujua ukweli... Teresia akamkatisha Kanjubai.
"Kwa hiyo umegundua kuwa hana tatizo lolote?"
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
"listen to me Teresia and listen good, mimi naitwa Kanjubai, nobody and when i say nobody, i mean nobody can double cross Mr Kanjubai and get away with it, kama utawasiliana na Samson,
muambie kuwa kama anataka usalama wake apeleke mzigo wangu kama alivotoka nao huku bila kupungua hata chembe amkabidhi mr Makuya na haya yote tutayasahau kama yalitokea na maisha yataendelea kama ilivokuwa hapo awali, kama hatafanya hivyo, hahahaa tell him kuwa he will pay big time, and this is not a threat, it’s a fact, mwambie kuwa know nimeshajua alipo, infact hiyo simu uliyonikuta nikiongea nayo wakati unaingia hapa, ilikuwa inatoka kwa one of my man, so asifikiri kuwa anaweza kujificha na nisimpate."
"Sawa bwana Kanjubai, nitajitahidi kama nitampata nitampa ujumbe wako".
Kanjubai akasimama, akasema , "please do that,if you will excuse me nataka nijiandae kuelekea uwanja wa ndege, na mwambie Samson huwa nikisema kitu huwa sirudii mara mbili."
Teresia akanyanyuka na kuaga, bwana Kanjubai wala hakumjibu kuonyesha ni jinsi gani alivokasirika. Teresia alifika kwake bila kujua amefikafikaje kwakuwa alikuwa amejawa na mawazo kuhusu mambo aliyoelezwa na Kanjubai, 'Kweli tamaa mbele ni mauti, Sam my dear, ni sheitwan gani aliyekuingia hadi kufiria kutoweka na mzigo wa watu? Kwani ulikuwa hutosheki na pesa uliyokuwa unapata?' Hivo ndivyo Teresia alivyokuwa anawaza, hakujua la kufanya maana alijaribu kupiga namba ya simu, Samson aliyompigia mara ya mwisho lakini jibu alilopata ni kuwa namba hiyo haipatikani.
Teresia akaamua kuwa siku hiyo hataenda kufungua kibanda chake cha biashara, alijihisi kuwa hatoweza kuongea na wateja. Akaamua kutegesha saa kila baada ya nusu saa iwe inapiga kengele ili awe akijaribu kumpigia Samson simu.
Saa kumi jioni ilipofika akashtuka kuwa toka anywe kikombe kimoja cha uji asubuhi, hajatia kitu kingine tumboni, akaamua kwenda jikoni kuangalia kuwa ni kitu gani anachoweza kupika kwa haraka. Akakuta kuna viazi alikuwa amenunua na kuviweka katika jokofu,
akaamua avimenye apike na kipande cha samaki mkavu. Wakati anaendelea kumenya mawazo yake yote yakahamia kipindi
alipokutana na Samson, akakumbuka siku ile ambayo Samson alikuja kibandani kwake kula chakula, baada ya kuagiza wali na maharage na mboga za majani, akamuuliza Teresia,
"Hivi umeanza lini kuuza chakula hapa, maana mara ya mwisho niliposafiri hiki kibanda hakikuepo."
"Nina kama miezi mitatu toka nianze kufanya biashara hapa, kwani wewe unakaa maeneo haya?"
"Nakaa mtaa wapili toka hapa,mwanzo ulikuwa unafanyia wapi biashara? maana msosi wako mtamu sana."
"Asante na kama umegundua kuwa mapishi yangu ni mazuri basi wakaribishwa hapa 'LISHE BORA KIOSK', sijawahi kuuza chakula sehemu nyingine, hapa ndiyo pa kwanza." Samson huku akichota chakula na kukijaza mdoni, "Usinishangae kula yangu, nina haraka natakiwa saa nane niwe uwanja wa ndege."
"Hapana kuna mgeni wa boss wangu naenda kumpokea."
"Basi angalia usije ukapaliwa hadi ukashindwa kwenda huko uwanjani na mie sitaki kulaumiwa kuwa nimefanya uchelewe kwa kukuongelesha wakati unakula".
Samson akameza chakula kilichokuwa mdomoni kisha akamuangalia Teresia kitambo kidogo bila kusema kitu. Teresia alipogundua kuwa anaangaliwa,akamuambia Samson, "mbona wanikodolea hivo hadi najihisi kama vile sijavaa nguo? Maliza chakula uwahi huko ulikotumwa la sivyo kibarua kitaota nyasi."
Samson akatabasam kisha kaendelea kula bila kusema neno, alipomaliza kula akaomba maji ya kunywa, baada ya kunywa akasema,
"Na hayamaji, yamechemshwa kweli? Nisije nikaumwa na tumbo hapa nikashindwa kwenda kumpokea mgeni."
"Aka babu wewe, maji yangu nimechemsha kisha nikayachuja, ukiumwa tumbo usije ukasingizia maji, pengine ni umekula kiporo asubuhi."
"Hahaha,kwanza mimi siyo babu, usinizeeshe bure mtoto wa mwenzio, pili sijala kiporo, labda kama huu wali ulionipa ndiyo kiporo."
"Usijali hapa kila kitu ni fresh, sipiki chakula kingi sana hadi kibaki."
Baada ya Samson kulipa pesa ya chakula alichokula, akamuuliza Teresia,
"Hivi waitwa nani vile?"
"Unauliza kama vile unanifahamu, naitwa Teresia."
Samson akatabasamu, akasema huku akitingisha kichwa kwenda juu na chini,
"Teresia,Teresia,Teresia,jina zuri sana, mbona hujaenda kuwa mtawa?"
"Hahaha, jina langu na utawa vina uhusiano gani?"
"Unajua jina Teresia, au Teresa, watu wengi wenye jina hili ni
watawa,kwani hujawahi kusikia mother Teresa?"
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
"Nimewahi ila jina ni jina tu halihusiani na imani au kazi afanyayo mtu."
"Anyway, mie naitwa Samson, Samson Makereba."
"Hahahaa" Teresia aliangua kicheko.
Samson akamuangalia hadi alipotulia,"sasa wacheka nini?"
"Nacheka hilo jina 'MAKEREBA', jina la wapi hilo? limekaa kama jina la spare part, hahahaa."
"Jina la heshima hilo, watu wanalilia we unacheka."
"Kama kuna wanao litamani ni shauri yao."
"Haya bana,kama wacheka jina langu bora niondoke."
"Sema unachelewa na siyo vile nilivyo cheka ndiyo kuna kufanya uondoke."
"Ngoja niende ila nikipata muda nitakuja tena kula maana huu msosi unaopika, mmh si mchezo, sijui ulipoondoka huko kwenu ulipitia kwa bibi akakupa kandumba kidogo kakuchanganyia ili watu wakila tu wanogewe ili warudi tena?"
"Hapa hakuna cha ndumba wala nini, ni upishi wa mwanamke aliyefunzwa akafunzika namna yakuandaa maakuli".
"Kwa heri maana yaelekea wewe ni mwongeaji mzuri, ndiyo nimekuona leo tu lakini waongea kama twafahamiana kwa muda mrefu."
Teresia akatabasamu kwakukumbuka siku ile alipokutana na Samson. Baada ya kutayarisha chakula chake akala kisha akasafisha vyombo alivyotumia.
Saa moja usiku ilipofika, akajaribu tena kupiga simu ya Samson lakini jibu likawa ni lilelile, haipatikani. Akapata wazo kuwa awasiliane na Moris amuulize kama ana mawasiliano na Samson. Alipompigia simu, Moris akamjibu kuwa hajawahi kuwasiliana na Samson toka aondoke.
Teresia akaanza kukata tamaa ya kumpata Samson tena,' sijui wameshamuua? Na kama Kanjubai alivyonieleza kuwa anajua alipo ni kweli, ooh Samson,k wanini umeamua kucheza na maisha yako?', hayo yalikuwa mawazo ya Teresia. 'afadhali Kibe alivyoamua kutorudi kufanya hii kazi, kila wakati mtu unakuwa na wasiwasi kuwa utakamatwa,hata sijui nilikubali vipi kushiriki hii biashara, ama kweli majuto ni mjukuu'.
Teresia akaamua kuwasha tv, akaweka stesheni ya malawi kuangalia kama kuna habari zozote zinazoweza kumhusu Samson, lakini hakuona, akaamua kuangalia wanyama.
Je ni kweli Samson amekimbia na mzigo wa Bwana Kanjubai? je samson amekimbilia wapi? Je nini kitatokea akigundulika alipo?
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
ITAENDELEA
0 comments:
Post a Comment