Simulizi : Dunia Rangi Rangire
Sehemu Ya Tano (5)
Wakati Teresia akiendelea kuwaza kuhusu mustakabali wa maisha yake, simu ikaita, akakurupuka toka pale alipokaa kwenda kuchukua simu akifikiri ni Samson anayempigia, alipoangalia jina la mpigaji akaona ni rafiki yake aitwae Jamila,
"Vipi shost, mbona leo haujafungua kibanda chako?" Jamila alimuuliza Teresia.
Teresia hakufurahi alipoona kuwa mpigaji hakuwa Samson hivo hakupenda kuwa na mazungumzo marefu na Jamila, akamjibu,
"Sijisikii vizuri leo, nahisi nitakuwa na malaria."
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
"Hata mie nilifikiri tu kuwa utakuwa unaumwa maana si kawaida yako kuacha kufungua, pole mwaya, nitakupigia kesho kuangalia kuwa unaendeleaje, ila kama hujaenda hospitali, kesho asubuhi na mapema uende ukachekiwe, sawa shosti?"
"Nashukuru, nitafanya hivo, usiku mwema," alipomaliza kumuaga Jamila, Teresia hakusubiri jibu maana anamfahamu vyema Jamila kuwa kama hata kata simu, Jamila ataanzisha stori za umbea alizo sikia mchana kutwa. Teresia alikuwa akitazama TV lakini akili yake na mawazo yote yalikua kwa Samson, alikumbuka jinsi walivoanza urafiki wao baada ya Samson kuwa mteja wake mzuri, karibia kila siku ambazo hakusafiri, alikuwa akienda kula chakula katika kibanda cha Teresia, siku hiyo Samson akamuambia Teresia,
"Leo usiku naomba nikutoe," Teresia akajifanya hajamwelewa,
"unitoe nini? Na kwanza sijakuambia kuwa nina kitu nataka nitolewe."
Samson akatabasamu kisha akasimama pale alipokuwa amekaa na kwenda alipokaa Teresia,akashika pua ya Teresia na kuitingisha tingisha,akamuambia,
"You are a naught girl."
"Wengine hatujui kidhungu,usije ukawa unanitukana."
"Hahaha, sijakutukana, nimesema kuwa umeumbwa ukaumbika."
Samson akakaa karibu na alipokuwa amekaa Teresia. Teresia alipoambiwa kuwa ameumbika, akahisi soni ikimuingia machoni, akashindwa kumuangalia Samson machoni, akaamua kutoka pale na kwenda kukusanya vyombo vilivyotumika. Kabla hajafikia vile vyombo, Samson akamshika mkono na kumzuia asiyondoke pale alipo, akamwambia,
"Mbona wataka kunitoroka kabla hatujafikia mwafaka?"
Kitendo cha Samson kumshika mkono, Teresia alihisi kama ameshika waya wa umeme,mwili wote ulimsisimka, akakosa jibu la kumuambia Samson. Samson alipoona Teresia hasemi lolote, akamkalisha mbele yake nakumuangalia machoni,
"Bibie, mbona umekuwa mpole ghafla, nimesema neno lolote lililo kukerehesha?" Teresia akatingisha kichwa kuonyesha ishara ya kuwa hakuna, bila kusema neno.
"Kwani umekuwa bubu? Teresia chiriku ameenda wapi?" Baada ya Samson kumuachia,Teresia alirudia hali yake ya kawaida, akamuambia Samson,
"Nilikuwa nakupima kama wewe ni jasiri au la."
Samson akasimama
"Wanipima kuwa mi ni jasiri kwa kigezo gani? kwanza hakuna kitu nilichoona hapa cha kunipima."
"Nilipokaa kimya, nilikuwa nakupima kama utakasirika na kuamua kuondoka ama utaonyesha kujali." Samson akacheka,
"Kama hilo ndiyo lilikuwa kusudio lako,umenipata maana nilijihisi mkosaji, sasa tuachane na hayo,je umekubali twende club?".
"Twende club kufanya nini?,mie sinywi pombe".
"Acha ushamba,siyo club za pombe,ni club za magoma kitakita,kwani hupendi muziki?"
"Napenda ila sijawahi kwenda disco toka nizaliwe."
"Basi ngoja iwe mara ya kwanza,twende ukasikie muziki kama ule usemao,"
Samson akarekebisha koo kisha akaanza kuimba,
"Nachungulia dirishani ooh, naona ni mvua yanyesha eeh, hakuna kilichobakia ooh, ila ni uchungu na huzuni eeh, mpenzi nauliza utarudi lini eeh, uje unitoe upwekwe na huzuni eeh, heri rudi mpenzi wa roho, sheri rudi mie nakufa kwa pendo, elewa dada nakupenda kwa uzuri wako, nakuomba utoroke eeh maana nakufa kwa upwekwe,njoo dada tuishi kwa upendo, ni wewe tu uliyeuteka moyo wangu,nakupenda kwa dhati."
Wakati wote huo Samson alipokuwa anaimba, alikuwa amefunga macho, Teresia akamuangalia jinsi alivojengeka kimaumbile, akahisi kumpenda Samson, alitamani awe wake peke yake.
Samson alipofungua macho, akaona jinsi Teresia alivokuwa anamuangalia kwa macho ya mahaba, moyo wake ukamuenda mbio, akatamani amkumbatie na kumbusu lakini aliona kuwa anaweza kuharibu kila kitu, akajiambia mwenyewe kichwani mwake, 'hawa watoto wa kutoka kijijini, hawatakiwi papara, mwendo wa kinyonga tu hadi tutafika', akatabasam. Teresia akamuuliza,
"Watabasamu nini?" Samsoni akamjibu,
"Unajua kama ukiamka asubuhi na kitu cha kwanza kukiona chapendeza machoni, shurti utabasam."
"Lakini sasa hivi si asubuhi, ni usiku."
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
"Nafahamu hivo, wakati naimba nilipofungua macho, macho yangu yakakutana na ua waridi lipendezalo kuliangalia wakati wote bila kuchoka."
"Eeeh! makubwa, haya hilo ua liko wapi?, maana mie silioni,isije ikawa upo ulimwenguni mwingine mie sijui."
"Nimimi peke yangu nilionae, sasa club tunaenda?"
"Sawa, ila sitaki nichelewe kurudi maana wajua shughuli zangu, saa kumi na moja alfajiri natakiwa niwe nimeshaamka."
"Usijali, tukiruka ngoma mbili tatu, tutarudi."
"Sawa, ila sikujua kuwa we ni mwimbaji."
"Kwani nimekuambia kuwa mimi ni mwimbaji?"
"Hujaniambia bali nimekuona ulivyokuwa unaimba huo wimbo kwa hisia kama vile wamwimbia mpenzi wako."
Samson akacheka kisha akamwambia ,
"Sasa katika waimbaji na mie nitasema nimo? si watu watanikimbia na kuniacha peke yangu wakisikia hili lisauti langu linalo fanana nala chura."
"Hamna, umeimba vizuri kweli, ningeweza ningekutunza."
"Kama hivo ndivo, basi kesho msosi utanipa bure, tena si kidogo kama huu unaonipimia? Msosi wa kushiba na kikombe cha chai au kahawa."
"Hehehee, uliona wapi mbuzi na kuku wakishirikishwa kupanga tarehe ya krisimasi?"
"Una maana gani?"
"Maana yangu nikuwa, mtu hajichagulii zawadi, we subiria na uwe mpole kama kondoo apelekwae mnadani."
Huo ndiyo ulikuwa mwanzo wa mapenzi kati ya Samson na Teresia,ambapo baadae waliamua kuishi pamoja kama mke na mume. Teresia aliendelea kukumbuka jinsi alivyokuwa akimuuliza mara kwa mara Samson kuwa ni aina gani ya kazi aliyokuwa akifanya, mara zote jibu lilikuwa,
"Vuta subira mama,ipo siku utamjua the really Samson."
Siku moja wakati Teresia anasafisha nyumba, akaamua atoe nguo zote kabatini ili azikung'ute vumbi la kabati, alipotoa nguo za Samson, pakiti iliyojaa unga kama wa ngano ikadondoka, Teresia akaichukua na kuichunguza kama imetoboka au la, alipoona hakuna sehemu iliyotoboka, akaamua kuirudisha sehemu alipo ikuta kisha akapanga nguo kama zilivokuwa. Samson aliporudi, Teresia akamuuliza kuhusu ile paketi ya unga. Samson akahamaki,
"Nani aliyekuambia uchakure nguo zangu?".
Teresia akamwambia,
"Sam, mbona umestuka hivo kama nimeua? nilikuwa napanga nguo vizuri kabatini na kwa bahati mbaya hiyo pakiti ikaanguka, kama nilifanya kosa kwa kupanga nguo zako vizuri, naomba
unisamehe na nakuahidi sitogusa tena nguo zako zikiwa kabatini."
Samson akaona kuwa huo ndiyo muda mwafaka wa kumueleza Teresia kazi anayofanya. Teresia alipotulia, Samson akamwambia,
"Hujafanya kosa kupanga nguo zangu, na pengine hii itanipunguzia wahaka niliokuwa nao". Teresia akashangaa maana hakuelewa Samson alichokuwa anaongea,
"Una maanisha nini unaposema nimekupunguzia wahaka?".
"Tere my dear, si unajua nikiasi gani ninavo kupenda?".
"Najua Sam hata mimi nakupenda sana ila sijaelewa nini unachomaanisha".
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Samson akamsogelea Teresia na kukaa, akashika viganja vyake, akamuambia,
"Kwanza nitakayo kueleza, usije ukamweleza mtu yoyoteyule, yote yaishie humu ndani, sawa?"
"Mbona wantisha Sam? yote haya yanahusiana na ile pakiti niliyoiona? au kuna jambo linguine."
"Inahusiana na hiyo pakiti, kwani unajua kuwa ni kitu gani kilichopomle ndani ya pakiti?"
"Sijui ila niliona imefanana kama unga wa ngano vile."
"Ule siyo unga wa ngano,inaitwa COCAIN," Samson aliposema hivo, akatulia ili kumpima Teresia kuwa amezichukuliaje hizo habari. Teresia aliposikia neno COCAIN, midomo ikaanza kumcheza, asijue la kusema, akabaki akiwa ameachama mdomo kwa mshangao. Samson alipoona kuwa Teresia ameshtuka sana, akamwambia,
"Tere darling, mbona umestuka hivo? ile siyo sumu ni kilevi tu kama vile pombe."
"Sikutegemea kitu kama hicho, si unajua kuwa cocain ni haramu?"
"Niharamu kama unataka iwe haramu, nisikilize kwa makini Tere, umekuwa unaniuliza mara kwa mara kuwa kazi nafanyia wapi na mara zote nimekuwa nakuambia uvute subira."
"Ndivyo ila siyoni kufanya kwako kazi kunahusiana vipi na cocain".
TERESIA alipoona hakuna cha kufanya, akaamua kwenda kulala, alihangaika kitandani bila kupata usingizi, ilipofika saa saba usiku, akaamka na kupiga magoti, akasema,
"Mungu wangu, najua mimi ni mkosaji mbele yako baba, nimefanya yale yasiyostahili machoni pako na jamii pia, lakini kwani mtoto akinyea kiganja kinakatwa? Nakuomba ewe Rabana, uliyetuumba sisi wana waadamu kwa pande la damu, uliyeumba majini kutoka katika ndimi za moto, ulituumba ili tukuabudu, baba, pia tukukimbilie pale tulemewapo na mizigo, nakuomba unifungulie njia na kunionyesha nini cha kufanya eeh baba, Samson ni mume wangu japo hatuja halalisha mbele yako baba, najua nimkosaji mbele yako ila ninachokuomba, umpatie ulinzi huko alipo, mwepushe na maadui wanaomtakia mabaya, kama atarudi salama, nakuahidi kuwa tutaenda kanisani ili tufungiwe ndoa na majina yetu uyaandike huko mbinguni, usituache sisi waja wako japo tuwakosaji, AMINA."
Alipomaliza maombi, akarudi kitandani na alijihisi kuwa amepata msaidizi wakumsaidia kupata suluhu ya shida zake. Akiwa pale kitandani, alikumbuka jinsi Samson alivyomwingiza katika biashara ya cocain, akakumbuka kuwa ilikuwa siku ya jumamosi jioni, Samson alimfuata pale kibandani kwake, alipofika alikuta vijana watatu wakila chakula, Samson akawasalimu kisha akamfuata Teresia kule jikoni, akamuambia ,
"Leo nataka na mimi nile hiki chakula unachouza maana toka tuanze kuishi pamoja sijawahi kuja kula hapa." Teresia akamuambia,
"Lakini utalipa maana katika biashara hakuna mchezo."
"Usijali mama, and speaking about biashara, nataka uwe msaidizi wangu wa ile ishu yangu niliyokueleza."
"Ishu gani hiyo?,kama ni ile ya ile inayohusu co. . . .
Kabla hajamalizia, Samson akamziba mdomo na kumuambia,"shhhh,unataka uanike mchele kwenye kuku wengi?, si tulishayaongea na ukakubali kuwa niendelee tu, na kama nilivo kuambia, jamaa wameshajua kuwa unafahamu kuhusu hii biashara na hii biashara inahusisha watu ambao kuua kwao ni
sawa na kumchinja kuku, sasa ninachotaka kufanya,unawaona wale vijana pale?".
Teresia akachungulia na kuwaona wale vijana watatu wakila, akamjibu, "Ndiyo nimewaona".
"Sasa wale vijana ni watumiaji wa white sugar,” Teresia akashangaa,
"White sugar ndiyo nini tena?"
Samson akamjibu kwa kunong'ona, "White sugar ni cocain, sasa nataka niwatambulishe kwako ili wakitaka bidhaa waje hapa wakuone."
"Sam, mbona unataka kuniingiza katika matatizo? tulikubaliana kuwa we uendelee ila usinihusishe."
"Siyo mimi nilie amua kuwa uingizwe kwenye huu mtandao, mkuu ndie aliyesema uingizwe, hii ni kutokana na uchunguzi wa kina waliokufanyia baada ya kugundua kuwa tunaishi pamoja."
"Wamegundua au umewaambia?"
"Sijawahi kumwambia mtu kuwa nina mke ninaye ishi naye, huu mtandao ni mpana sana, kuna watu kazi yao ni kupeleleza mienendo ya watu wengine, hivo wamenichunguza na wakampa mkuu habari kuwa nina mke ninaye ishi naye."
Baada ya Teresia kuelezewa kuwa kazi yake itakuwa kuchukua cocain ambazo zimeshafungwa katika kipimo kinachouzwa na kukaa nazo hapo kibandani kwake, wateja wataelezwa kuwa wakitaka waje pale kibandani na kujipatia hashishi.
Samson akamtambulisha Teresia kwa wale vijana na huo ndiyo ukawa mwanzo wa Teresia kujiingiza katika biashara ya kuuza dawa za kulevya. Teresia akakumbuka pia siku alipoanza kutumia cocain, alikumbuka kuwa ilikuwa jioni wakiwa wamejipumzisha katika makochi huku wakitazama TV, Samson akaleta unga kidogo katika karatasi akawa anaunusa, Teresia alipomwona akamuuliza,
"Sasa huo unga una raha gani? si kama tu ugoro aliokuwa ananusa bibi yangu?" Samson akamwambia,
"Huu si kama ugoro, ukipata hii kitu dunia yoote inakuwa yako, hakuna kitu inayokufanya uwe na raha katika huu ulimwengu kama hii kitu, hebu jaribu kidogo halafu utanieleza."
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Teresia akachukua kidogo akaweka puani na kuvuta, baada ya muda mfupi, akaanza kucheka hovyo na kuanza kuimba nyimbo zisizoeleweka. Wakati anaendelea kuwaza jinsi alivoingia katika mtandao wa dawa za kulevya, Teresia akapitiwa na usingizi, aliposhtuka ilikuwa saa mbili asubuhi.
Samson akiwa anaelekea katika fukwa za Maputo, alihisi kuwa kama vile kuna mtu anaye mfuatilia lakini hakuwahi kumwona huyo mtu. Akajisemea, "Kanjubai wakati huu, umekula huu na hasara juu, umesahau kuwa kuti mgema alilozoea kukalia ndiyo lililomwangusha, nimechoka kutumwa kila siku, huku ukinufaika wewe, wakati mimi maisha yangu bado hayajaimarika.”
Alipofika katika fukwe, akanunua dafu na kwenda kukaa katika gogo la mnazi lililokuwa karibu na maji ya bahari yanapoishia kugonga yanapoletwa na mawimbi. Wakati anendelea kunywa maji ya dafu, akawa anafikiria jinsi atakavozitumia pesa alizo pata baada ya kuuza mzigo aliopewa na Kanjubai, akatabasamu alipokumbuka jinsi alivyogeuza njia badala ya kwenda Lilongwe kama alivyoagizwa, akaenda Maputo ambapo alikuwa ameshapatana na jamaa mmoja toka Duban, baada ya kukutana nae na kumkabidhi nusu kilo ya cocain, alikabidhiwa mkoba uliojaa pesa, Dola milioni mbili. Samson akapanga kuwa, kwa sababu ana pesa za kutosha kuanzisha biashara tofauti na cocain, akapanga kuelekea Namibia.
Alipanga kuwa akifika kule, atasoma masoko ya bidhaa mbalimbali na atakapotambua biashara itakayompa faida nzuri, basi ataanza maisha mapya huko na hatorudi tena nyumbani kwao.
“Sijui Teresia ameshapata habari kuwa nimetoweka na mzigo wa Kanjubai?” hayo yalikuwa mawazo ya Samson. 'akigundua kuwa nimetoweka,atafikiria kuwa nilikuwa simpendi, japo kiuhakika nampenda sana, ooh Teresia my dear, ningetamani sana kama tungekuwa wote huku, twende tukaanze maisha yetu upya na tufunge ndoa kanisani ili Mungu atupe uzao wenye baraka'.
Kanjubai baada ya kugundua kuwa Samson yupo Maputo, alimwagiza mpelelezi wake aliyejulikana kama Cosmo kwa jina la utani, kuwa amchunguze kama bado yupo na mzigo wake au ameshauza. Cosmas au Cosmo kama alivyojulikana, alimfatilia Samson hadi akagundua hoteli anayo kaa. Alifanya jitihada hadi akaweza kuingia chumba alichokuwa analala Samson, akatafuta kila sehemu kuwa pengine ataona mzigo alio agizwa na Kanjubai.
Alipokosa kuona sehemu zote zile alizohisi kuwa anaweza kuweka, akaamua kufungua mkoba aina ya brifcase, alitumia ujuzi wake kufungua, alipo ufungua, akakutana na mabunda ya pesa yaliyokuwa yamejaa, akachukua bunda moja ili kuhakikisha kuwa ni halali au si halali.
Alipogundua kuwa zote ni halali, akarudisha zile pesa na kufunga ile brifcase kama alivyoikuta. Akatoka pale na kurudi sehemu ile ya ufukwe aliyomwona Samson. Hakumwona pale alipomuacha, akamtafuta lakini hakumuona, akaamua kumpigia Kanjubai simu na kumweleza kuwa, Samson alikuwa ameshauza ule mzigo. Kanjubai akakasika, "are you sure na unachoeleza mimi?"
"Am very sure boss, infact nimekuta brifcase imejaa American dollar na hesabu yangu ya haraka haraka ni kama Dola milion moja unusu kwenda juu."
Kanjubai kuambiwa vile, akalegeza tai yake shingoni, akavua miwani akaenda kuiweka mezani, akamwambia Cosmas,
"Sasa kwa nini hujachukua hiyo pesa na kuniletea?"
"Hujaniambia kuwa kama nitaona pesa za huo mzigo nizichukue, so unataka nifanye nini kwa sasa?"
Kanjubai akasimama kutoka katika kiti alichokuwa amekaa na kukaa juu ya meza iliyokuwa pale ofisini kwake, akamwambia Cosmas, "Kama utaweza kuchua hizo pesa, zichukue uniletee kisha nitajua nini cha kumfanya huyu paka mweusi."
"Sawa boss, nitakupigia kukueleza kitakacho endelea hapo kesho," Cosmas alipokata simu akaamua kutafuta chakula ale maana jua karibia lilikuwa linatua nayeye hakula chochote toka alipokunywa chai asubuhi. Alienda katika mgahawa uliokuwa unaitwa MAKONDE REUSTAURANT, akaagiza atengenezewe samaki mbichi kwa ugali. Baada ya nusu saa akaletewa samaki aina ya sato na ugali kama alivyoagiza. Wakati anaendelea kula, akamwona Samson akitoka katika ule mgahawa, 'kumbe huyu jamaa alikuwa humu ndani na nilipoingia humu sikumwona, ila sidhani kama ananijua', hayo yalikuwa mawazo ya Cosmas, mara baada ya kumwona Samson akitoka.
'we nenda tu ukajipumzishe au sijui waenda kujirusha, lakini mwisho wako unakaribia', Cosmas aliwaza huku akikata mnofu wa samaki na kuubugua, akamwita muhudumu aliyekuwa akipita karibu ya meza aliyokuwa
amekaa, "Mhudumu, naomba pilipili tafadhali." Baada ya kumaliza kula, akaagiza aletewe kikombe kimoja cha kahawa.
Samson alipokuwa katika mgahawa wa Makonde, alimwona mtu akiingia, lakini alikuwa hakumbuki vyema kuwa alimwona wapi, alipomaliza kula na kulipa, akamkumbuka yule mtu aliyemwona akiingia pale mgahawani, roho ikamwenda mbio alipokumbuka kuwa yule jamaa anaitwa Cosmo, na alikuwa mtu mwenye roho ya ukatili sana,
"Huyu jamaa najua tu ametumwa na Kanjubai, kilichopo hapa ni kuhama usiku huu huu, maana kama ameshajua nilipofikia, anaweza akanidhuru au apotee na pesa zangu", hivyo ndivo Samson alivokuwa akiwaza.
Alipofika hoteli aliyofikia, akachukua mizigo yake na kwakuwa alikuwa hadaiwi, akarudisha funguo na kuondoka. Akakodisha teksi yakumpeleka kituo cha mabasi,
alipofika kituoni akakuta kuna basi moja ambalo lilikuwa halijajaa na lilikuwa linaelekea Harare. Akatabasam, huku akijisemea, 'kwa heri Cosmo, sijui utamwambia nini Kanjubai utakapogundua kuwa nimetoweka?' akakata tiketi na kwenda kukaa kiti cha nyuma kabisa, dirishani. Kibe alianza kuona matunda ya kazi yake baada ya kuanza kuuza, karoti, nyanya na vitunguu.
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
Watu wengi wakawa wanakwenda kununua mbogamboga kwa Kibe, maana hakutumia kemikali za kuulia wadudu bali alitumia aina ya majani ya miti aliyokuwa ameonyeshwa na marehemu baba yake, haya majani aliyatwanga na kuweka mimea yake na mazao yakawa mazuri.
Kibe alipoona amepata pesa nzuri, akaamua auze baadhi ya mifugo ili apate pesa ya kutosha kununua ng'ombe wa kisasa wa maziwa. Akajenga vizuri sehemu atakayo muweka ng'ombe wake wa maziwa, juu akaezeka kwa makuti.
Alipokamilisha banda la ng'ombe, kama alivoelekezwa na mtaalamu wa mifugo, akaenda katika ranchi ya kituo cha mifugo kuangalia aina ya ng'ombe atakayo weza kununua. Alionyeshwa aina tofauti ya ng'ombe, akaelezewa kila aina ya ng'ombe na kiasi cha maziwa anachotoa kwa siku. Kibe akachagua ng'ombe aina ya Freshan, ambaye alikuwa na mimba ya miezi mitano.
Siku moja Kibe alipokuwa amejipumzisha baada ya shughuli zake za mchana kutwa kumalizika, alikuja mjumbe wa nyumba kumi kumuelezea kuwa kuna mtaalamu atakuja pale kijijini kwao kesho yake ili awaelimishe wanakijiji kuhusu matumizi ya bio gas. Kibe akashangaa na kumuuliza yule mjumbe,
"Hii baio gesi, ni gesi ya namna gani? isije ikawa ni hizi gesi zinazo choma nyumba huko mijini?" Mjumbe akamwambia,
"Kwa uelewa wangu mdogo ni kuwa, hii ni aina ya gesi itokanayo na kinyesi cha wanyama."
"Basi kama ni hivyo, nitakuja ila baada ya kupunguza kazi zangu"
"Sawa ila usichelewe maana unaweza ukakosa yale ya muhimu."
Kibe alipoenda katika ule mkutano, alijifunza mambo mengi mazuri ya maendeleo, akaahidi kuwa lazima abadilishe maisha ya pale nyumbani kwao. Walielekezwa namna ya kutengeneza mashimo ya kuweka kinyesi cha ng'ombe na mashimo ya kuhifadhia gesi ile itakayotokana na kil kinyesi cha ng'ombe.
Ilikuwa imepita miaka miwili toka Kibe aanze kuona mafanikio ya kazi zake, alikuwa amejenga nyumba nzuri ya matofali ya kuchoma, hakuwa anaenda tena machungani maana akifuga ng'ombe wa kisasa wa maziwa na mbuzi watatu wa maziwa, ambao alikuwa akiwamudu kuwalelea majani pale nyumbani, pia alianza kutumia bio gas, na alikuwa amenunu tv yake ndogo maana alikuwa anapata umeme wakutosha uliotokana na bio gas, mama yake alikuwa ameshaanza kusahau matumizi ya kuni maana alikuwa akipika na gesi itokanayo na kinyesi cha wanyama.
Ilikuwa siku ya Jumamosi jioni, Kibe akiwa anatazama taarifa ya habari, akaona habari iliyomustua, akamwita mama yake ili nae aione, habari yenyewe ilikuwa hivi,
"Jeshi la Polisi limefanikiwa kuwatia mbaroni watu kadhaa kwa kujihusisha na biashara ya madawa ya kulevya, kukamatwa kwao kumefanyika kutokana na upelelezi wa muda mrefu uliofanya na kachero ajulikanae kwa jina la fedinand, kachero huyu baada ya kugundua kuwa kuna shamba la mmea aina ya coca eneo lijulikano kama tambaeni, mmea huu ndiyo unaotumika kutengenezea dawa aina ya cocain", taarifa ikaendelea kuelezea,
"Jeshi la polisi lilipovamia eneo hilo kulitokea majibizano ya risasi ambapo watu watatu waliuawa, akiwemo mtu msaidizi wa kanjubai aitwae Lio", msoma habari pia akataja majina ya watu waliokamatwa ambao walikuwa wakishirikiana na bwana Kanjubai, miongoni mwao ni,
"Teresia Kaboronga, Moris Tendawema, Twalibe Ibrahim." Kibe akafunga macho na kuziba uso wake kwa viganja vyake, mama yake akamuuliza,
"Nimesikia jina la Teresia likitajwa hapo, ina maana na yeye alikuwa anauza dawa za kulevya?"
"Sijui mama, ila pengine alikuwa anauza maana alikuwa anafahamiana vyema na hao watu na hapo walipotaja kuwa hizo dawa zilikuwa zinatengenezewa, ndiyo nilipokuwa nafanyia kazi,"
Marina kusikia vile akahamaki,
"Mbona tuliambiwa na Teresia kuwa ulikuwa ukifanya kazi kwa muhindi?"
"Ndiyo nilikuwa nikifanya kazi kwa Muhindi ambaye ni huyo bwana Kanjubai ambae polisi wamesema kuwa hawajui alipotorokea."
"Kwahiyo nawewe ulikuwa ukiuza hayo madawa?"
"Hapana, kwanza mimi hata nilikuwa sielewi kilichokuwa kikiendelea"
"Una maana gani ukisema ulikuwa hujui kilichokuwa kikiendelea?"
"Mimi kazi yangu ilikuwa kutwanga hayo majani na kila nilipo wauliza wenzangu kuwa yale majani tuliyokuwa tukitwanga kila siku yalikuwa na kazi gani? Walikuwa wananijibu kuwa nisitake kujua, eti mie nilichofata pale ni pesa tu.
"Marina aliposikia kuwa mwanaye hakujua kuwa anafanya kazi ihusiyo dawa za kulevia, roho ikamtulia, akamuliza Kibe,
"Sasa ulijuaje kuwa hayo majani yalikuwa ya hayo madawa?"
"Kuna rafiki yangu mmoja, anaitwa Fabian, yeye alikuwa kitengo kingine tofauti na kitengo chetu,huyu ndiye alinielezea yanapopelekwa yale majani baada ya kutwangwa na kitu ambacho kinatengenezwa huko ambayo ndiyo hiyo cocain waliyoitaja,niliambiwa hivo nilijiapia kuwa kama nitapata nafasi ya kuondoka pale, sitorudi tena."
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
"Sasa nimeelewa kuwa kwanini ulikuwa hutaki kurudi, ila kwanini hukuniambia?, ulinifanya niwe na mawazo kuwa pengine umeharibu vitu au umeiba pesa za watu ndiyo maana hukuwa unataka kurudi huko."
"Nisamehe mama maana nilimuahidi huyo rafiki yangu kuwa sitomwambia mtu yeyote, maana siri ingetoka halafu waseme ni mimi niliyeitoa, wasingesita kunisaka na kuniua." Marina akarudi jikoni kuendelea kutayarisha chakula cha usiku.
Kibe alifuatilia ile habari lakini hakusikia Fabian akitajwa kuwa amekamatwa, pia hakusikia jina la mumewe Teresia likitajwa, akawa anawaza, 'pengine Fabi aliamua kuacha na Samson, sijui alikuwa anajua kuwa Teresia anauza cocain?
Au na yeye alikuwa muuzaji na wakati wenzake wanakamatwa hakuwepo maana anasafiri kila wakati'. Kibe alipoona hakuna kitu cha kumfurahisha katika tv, akaamua kuizima na kufungulia redio, akatafuta stesheni yenye muziki, akawekea stesheni yenye muziki uliokuwa ukiimba hivi,
"Hata uwe mzuri wakupindukia aah, tabia yako ikiwa mbaya ni bure kabisa... "Hata ujipambe kwa vito ung'ae kama nyota aah, tabia yako ikiwa mbaya ni bure kabisa...
"Hata uwe na maringo, utembee kama twiga, tabia yako ikiwa mbaya ni bure kabisa, tabia njema utakwenda popote, heshima kijana, tanguliza kwanza mbele ujeuri m'baya ooh.
"Kibe wakati anaendelea kusikiliza muziki, akasikia mama yake akimwita aende kula. Kibe alipofika jikoni akakuta mama yake amepika chapati za kusukuma na kuku wa kienyeji aliyeungwa kwa kweme, pia alikuwa amepika chai nzito ya maziwa. Kibe akatabasamu, akatamani kama baba yakeangekuwepo, akamwambia mama yake,
"Mama, kweli dunia ni rangi rangile, leo hii sisi ndiyo tunakula chapati kama chakula cha usiku? Mtu angesema miaka mitano iliyopita kuwa ipo siku ambayo tutakula hivi na kuishi katika nyumba kama hii yenye umeme, nisingekubali hata kwa mtutu wa bunduki." Marina akatabasamu, huku akiweka mboga kitika bakuli la kibe, akamwambia,
"Hakuna lenye mwanzo lisilo na mwisho na maisha ni kupanda na kushuka." "Kweli mama, kilichobaki sasa nitafute mchumba nioe, nataka hii nyumba ijae kelele za watoto."
"Nafurahi kama umelitambua hilo mwanangu,na nakuombea kwa Mungu akupe mke mwema."
"Amin, amin mama, Inshaallah Mungu apokee dua zako."
CHANZO: https://deusdeditmahunda.blogspot.com/
MWISHO
0 comments:
Post a Comment